Simulizi : Dili La Dola Bilioni Nne
Sehemu Ya Nne (4)
Hilo ndilo lililotakiwa kufanyika, codes za kuingilia kwenye database ya benki zilitakiwa kupatikana haraka iwezekanavyo. Akampigia simu Richard na kumwambia kwamba kulikuwa na kazi kubwa hivyo alitakiwa kupanda ndege haraka sana na kuelekea nchini Kenya katika Jiji la Nairobi.
Ili aaminike, naye Upendo akapewa simu na kuzungumza na Robert na kuambiwa kuhusu Richard kwamba kulikuwa na kazi ilitakiwa kufanyika haraka sana. Akakubaliana naye na siku iliyofuata tu mwanaume huyo akasafiri mpaka nchini Kenya.
Alipofika huko, akakutana na wenzake wawili na kuanza kuongea. Kwanza akaambiwa kuhusu pesa zilizokuwa zimeingizwa kwenye akaunti, zilikuwa nyingi mno kiasi kwamba hata Richard mwenyewe alionekana kushangaa.
“Kwa hiyo?” aliuliza.
Wakamwambia kuhusu msichana aliyekuwa na cheo cha Umeneja Masoko, alikuwa msichana mrembo na mwenye msimamo hivyo walimpigia simu yeye na kumuhitaji kwa sababu walihitaji kwa udi na uvumba kuchukua pesa zile.
Walimpa maelekezo yote na hivyo siku iliyofuata Richard akaondoka na kuelekea huko benki huku akiwa amevalia shati jeupe, tai nyeusi na suruali nyeusi huku miwani ikiwa machoni mwake.
Alipoingia benki tu, wasichana wote wakageuka na kumwangalia. Walichokiona, hawakuamini, uzuri wake ulinogeshwa na miwani aliyovaa, kila aliyemuona alidiriki kusema kwamba Mungu alijua kuumba, walihisi siku ambayo Mungu alimuumba Richard alisema kwamba alihitaji kutengeneza mwanaume mwenye sura nzuri kuliko wote katika dunia hii.
Richard alitembea na kwenda kukaa kwenye kiti na wateja wengine. Wasichana hawakuyatoa macho kwake, walibaki wakiduwaa kwa kumwangalia, wale waliokuwa mapokezi walitamani kumfuata na kumuhudumia, wasichana wengine waliokuwa wakifanya kazi hapo wakawaita wenzao kwa lengo la kumwangalia Richard tu.
Msichana mmoja wa hapo alishindwa kuvumilia, kila alipomwagalia Richard alihisi moyo wake ukiwa na kimuemue cha kutaka kuzungumza na Richard, akaanza kumsogelea na kuongea naye.
“Samahani! Sijui unahitaji huduma gani ya kibenki?” aliuliza msichana huyo huku akimwangalia Richard aliyekuwa akitabasamu tu.
“Nahitaji kuonana na Meneja Masoko!” alijibu.
“Oh! Njoo huku,” alisema msichana huyo.
Richard akasimama na kuanza kumfuata msichana huyo, kwa jinsi alivyokuwa akitembea, kila mmoja alitamani sana kuongozana naye, wafanyakazi wengine wakamuonea wivu mwenzao kwa kuona kwamba alifanikiwa kumchukua Richard, hata kama hakufanikiwa siku hiyo basi angepewa hata namba ya simu.
Walipofika kwenye mlango wa ofisi ya Rachel, kwanza akaingia na kuanza kuongea naye, alimwambia kuwa kulikuwa na mgeni mlangoni, alikuwa mzuri wa sura kupita kawaida, alimtaka hivyo Rachel alitakiwa kutulia asilete mapepe hata kidogo.
“Ni mzuri! Ana uzuri gani?” aliuliza Rachel.
“Wewe acha tu bosi! Huko chini nimeacha balaa, kila msichana anamtaka!” alisema msichana huyo.
“Mmh! Hebu mwambie aingie,” alisema Rachel.
Msichana huyo akatoka na kumwambia Richard aingie. Mwanaume huyo akafanya hivyo, alivyoufungua mlango tu na macho ya Rachel kugongana naye, hapohapo akahisi kama moyo wake ukilegea, akaanza kutetemeka kwa hofu huku kijasho chembamba kikianza kumtoka, mwanaume aliyekuwa akimwangalia alikuwa kama vile alivyoambiwa kwamba ni mmoja wa watu waliokuwa na sura nzuri mno.
“Karibu sana,” alisema Rachel huku akimpa mkono.
Walipogusana tu, Rachel akahisi akipigwa shoti iliyosambaa mwili mzima na kumpa hali ambayo hakuwahi kuihisi hapo kabla.
“Asante sana!” aliitikia Richard na kukaa, alichompagawisha zaidi msichana huyo ni pale alipoanza kumwangalia kwa jicho la mahaba ambalo lilianza kueleza hisia zake kwa msichana huyo.
“Siwezi kuvumilia...” alijisemea Rachel.
***
Rais Kimoni alikuwa kimya, alihitaji kujua kile kilichokuwa kikiendelea. Aliwaambia watu wa benki wazizuie pesa zile kwa kuamini kwamba mtu ambaye alimwambia kuwa alikuwa na picha hizo amtumie na yeye mwenyewe kuzifuta katika simu yake.
Aliambiwa kazi ingefanyika kikamilifu hivyo kitu alichokisubiria kilikuwa ni picha hizo kutumiwa tu. Ilichukua zaidi ya saa moja, hakukuwa na kitu kilichofanyika na alipojaribu kumpigia simu Robinson, haukuwa ikipatikana.
Hakutaka kuwa na hofu, aliamini kwamba picha angetumiwa tu kwa kuwa tayari alimtumia mwanaume huyo pesa na asingeweza kutoa kiasi chote hicho, na kama kweli alihitaji kuzitoa zote alitakiwa kwenda benki ambapo huko angetuma watu na kwenda kumkamata.
Siku hiyo alisikilizia, siku ya pili ilipoingia, alipoona kimya ndipo akajaribu kumpigia simu Robinson kwa lengo la kuzungumza naye lakini simu haikuwa ikipatikana.
Alijua kulikuwa na kitu, akawasiliana na benki, wakamwambia kwamba pesa zilikuwepo kwenye akaunti na haikuchukuliwa hata shilingi moja.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alichokifanya ni kumtumia ujumbe mfupi Robinson na kumwambia kwamba kila kitu alikamilisha hivyo alitakiwa kumtumia picha hizo na kuzifuta kwa kuwa tu aliheshimu kile alichomwambia.
Baada ya kutuma ujumbe huo, alisubiri mpaka saa moja jingine ndipo akaona ujumbe ukiwa umepokelewa kitu kilichoonyesha kwamba mwanaume huyo aliwasha simu, hapohapo simu yake ikaanza kuita.
Aliyekuwa akipiga alikuwa Robinson, moyo wake ukashtuka, alianza kumuogopa mtu huyo kwani aliamini kwamba angemfanyia jambo moja baya sana kama tu angeruhusu picha zile zibaki kwa wapinzani. Akaipokea harakaharaka.
“Niambie! Umeziona hizo pesa?” aliuliza rais.
“Niliziona tangu jana! Nashukuru sana! Nimeshazichukua, nakutumia picha sasa hivi,” alisema Robinson kutoka upande wa pili.
“Umezkwishazichukua?” alijikuta akiuliza rais huku akipigwa na mshtuko.
“Kwani si zangu! Sasa kwa nini nisizichukue?”
“Basi naomba nitumie hizo picha na uzifute kabisa kwako!” alisema rais.
“Usijali! Nipe dakika kadhaa!”
Rais Kimoni alichanganyikiwa, hakuamini kilichokuwa kikiendelea, Robinson alimwambia kwamba pesa hizo alizichukua, sasa ilikuwaje watu wa benki kumwambia kwamba pesa hizo bado zilikuwa kwenye akaunti hiyo.
Haraka sana akawapigia na kuanza kuongea nao. Walichomwambia ni kwamba pesa hizo bado zilikuwepo kwenye akaunti ile na kile alichoambiwa kwamba zilitolewa ulikuwa ni uongo mtupu.
“Kwa hiyo walionidanganya ni nyie au yeye?” aliuliza.
“Yeye!”
“Basi zirudisheni kwenye akaunti yangu,” alisema rais na kukata simu.
Kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, hakujua ni kitu gani hasa kilichokuwa kikiendelea. Alikaa kwa dakika kadhaa, ujumbe wa WhatsApp ukaingia kumaanisha kulikuwa na picha alizokuwa ametumiwa, alipozifungua, zilikuwa picha za Kimeta alizokuwa na msichana Jesca.
Moyo wake ukatulia japokuwa hakuwa na uhakika kama mtu huyo hakubaki na picha, alichokuwa akikisikilizia kilikuwa ni kutoka kule benki na kuambiwa kuhusu pesa hizo.
Baada ya kuona kuna ukimya sana kwa zaidi ya nusu saa, akaamua kupiga simu na kuwauliza. Meneja ambaye alikuwa akizungumza naye alionekana kutetemeka, aliogopa, ni kama alikuwa na kitu alichotaka kumwambia rais lakini aliogopa kufanya hivyo.
“Kuna nini?’ aliuliza rais kwa sauti ya kibabe.
“Mkuu, ni kwamba....”
“Pesa hazipo au?”
“Mkuu! Yaani hatujui nini kimetokea,” alisema mwanaume huyo wa upande wa pili.
“Niambie chochote kile,” alisema.
Jamaa huyo akaanza kumwambia kwamba pesa zilionekana kwenye akaunti hiyo lakini walipoingia kwa lengo la kuzihamisha, hazikuwepo, kulikuwa na mtu aliyezichukua na kuwaachia kivuli cha pesa hizo.
Rais hakujua chochote kile, kwake, taarifa hiyo ilimchanganya kupita kawaida. Ilikuwaje pesa aitume humo, ikae halafu wamwambie kwamba kulikuwa na kivuli, pesa hiyo haikuwepo.
Hakutaka kukubali, ikulu hakukukalika, akaondoka na kuelekea huko benki yeye mwenyewe. Wafanyakazi walijua kilichokuwa kikiendelea, kitendo cha kumuona rais huyo mahali hapo wakajua tu nini kilikuwa kikienda kutokea.
Hakuonana na meneja, alionana na mkurugenzi na kuanza kuongea naye. Kila alichoambiwa, hakikuingia akilini, ilikuwaje pesa hizo ziwe humo na baada ya muda zisionekane? Kwake, lilikuwa jambo lisilowezekana kabisa.
“Atakuwa ni yule mwanaume, yaani amechukua hizo pesa bila benki kujua, kivipi? Alizihamishaje?” alijiuliza rais huku pale kitini alipokuwa akionekana kuchoka mno.
***
Rachel alibaki akimwangalia Richard, hakuamini kama angeweza kukutana na mwanaume aliyekuwa na sura nzuri kama huyo ambaye alikaa mbele yake.
Aliambiwa kwamba alikuwa na shida, kwake, alikuwa tayari kumsaidia kwa kila kitu kwa kuamini kwamba shukrani kubwa na ya kipekee ambayo angempa ingekuwa ni kulala naye.
Kwa jinsi Richard alivyokuwa akiongea, alijiamini kupita kawaida, alimwangalia msichana huyo huku akijifanya kuwa na pesa ya kumiliki kampuni ya Google, alizungumza naye na kitu pekee alichomwambia ni kutaka kufanya biashara na beki hiyo.
Alimwambia mipango yake, japokuwa haikuwa imekamilika lakini Rachel aliona kama imekamilika na kuamini kwamba benki hiyo ingekwenda kufanikiwa sana kama tu wangeungana na biashara ya mwanaume huyo aliyekuwa mbele yake.
“Yaani mtatengeneza mamilioni! Ningependa nionane na mkuu wa kitengo cha IT, manake kwenye biashara hii lazima na wao wahusike,” alisema Richard.
Haraka sana Rachel akanyanyua mkonga wa simu na kupiga upande wa pili ambapo baada ya sekunde kadhaa alikuwa akiongea na mwanamke mmoja, alimuhitaji kwenda ofisini kwake ambapo baada ya kumuona Richard, naye akashtuka.
“Rebecca...karibu sana!” alisema Rachel.
Huyo mkuu wa kitengo cha IT alikuwa msichana mrembo mweupe, mfupi, mwenye wowowo la kuwaiba wanaume za watu, aliyenona miguu na kiuno kilichomegeka.
Alikuwa msichana mzuri ambaye naye aliwatingisha sana wanaume waliokuwa wakifanya kazi humo. Aliitwa ofisini humo, kitendo cha kumuona Richard alishindwa kuamini kama kungekuwa na mwanaume mzuri kama alivyokuwa.
Akaambiwa kuhusu Richard na mwanaume huyo kuanza kumwambia kuhusu biashara yake. Alikubaliwa kwa haraka sana kwa kuwa alikuwa na sura nzuri na ya kuwavutia wanawake.
Walizungumza mengi na baada ya hapo akamuaga Rachel na kuomba kwenda katika chumba cha IT kwa lengo la kuzungumza na wengine.
Kila alichokisema, kilikubaliwa na hivyo kwenda huko. Lengo lake halikuwa kwenda kweli ila alihitaji muda wa kukaa chemba na Rebecca ili azungumze naye.
“Yaani nimeona wanawake wengi katika dunia hii, ila sijaona msichana mrembo kama wewe,” alisema Richard huku akimwangalia msichana huyo usoni.
“Jamani! Kweli?”
“Ndiyo! Unaonekana kuwa msichana wa kipekee sana, mwerevu, mwenye mafanikio makubwa mno. Nimeamua kuja kufanya biashara na nyie ila kuna kitu nataka sana unisaidie, kama ukinisaidia, nakupa elfu hamsini,” alisema Richard huku akimwangalia msichana huyo.
“Kitu gani?”
“Namba ya siri ya database ya hapa kwenu,” alisema Richard maneno yaliyoonekana kumshtua mno Rebecca.
“Namba ya siri ya database?”
“Ndiyo!”
Rebecca akakaa kimya, alimwangalia mwanaume huyo huku akionekana kutokuamini kile alichokisikia. Aliijua namba ya siri ila kila alipojaribu kufikiria kazi ambayo ingefanyika kupitia namba hiyo hakupata jibu zaidi ya kuhisi kulikuwa na mchezo mbaya.
Hakutaka kumwambia, alimkatalia katakata. Alichokifanya Richard ni kukatisha mazungumzo kuhusu database na kumwambia kwamba alihitaji kuonana naye chemba na kuzungumza.
Rebecca alivyoambiwa hivyo akachanganyikiwa, kutoka na mwanaume kama Richard kwake ingekuwa bahati ya mtende kwa marafiki zake na wakatu wengine. Akakubaliana naye na hatimaye wakatoka na kwenda kwenye Mgahawa wa Oswardo ambao ulikuwa maarufu hapo Nairobi na kuanza kuzungumza huko.
Richard akajifanya kumpenda mno Rebecca, alimsifia vya kutosha, alimpamba kwa maneno matamu mno kiasi kwamba msichana huyo akajiona yeye ndiye mwanamke mrembo kuliko wote katika dunia hii.
Walizungumza kwa dakika arobaini na tano huku wakinywa juisi, wasichana mbalimbali waliokuwa wakiingia katika mgahawa huo walipomuona Richard, walichanganyikiwa mno kwani uzuri wake ulionekana kwa kila aliyekuwa akimwangalia.
“Ningefurahi kama ningepata nafasi ya kuwa nawe chumbani leo hii,” alisema Richard kwa kuamini msichana huyo asingeweza kukataa hata kidogo.
Ni kama Rebecca alisikia vibaya, akauliza kile alichoambiwa huku akionekana kutokuamini. Richard alimwambia zaidi kwamba alihitaji kuwa naye usiku wa siku hiyo kwa kuwa alimpenda sana.
Kumkataa mtu kama Richard ulionekana kuwa ujinga wa hali ya juu, kwa kutumia pesa zake mwenyewe, akakubali na kuchukua chumba.
Hicho ndicho alichokitaka Richard, alifanikiwa kulala naye, alimuonyeshea mapenzi ya usiku mmoja kiasi kwamba msichana huyo alichanganyikiwa. Hakuishia hapo, akaahidi kumuoa kama tu angekuwa tayari kumwambia kila kitu alichotaka kuambiwa na kumuonyeshea uaminifu wote.
Rebecca alikubali kwa asilimia mia moja na hata alipoulizwa kuhusu namba ya siri, hakuwa na jinsi, akakubaliana na mwanaume huyo kwamba iwe siri na asimwambie mtu yeyote yule kama alimwambia kuhusu jambo hilo la siri.
Alichokiamini Rebecca ni kwamba mwanaume huyo angemuoa na kuishi naye kwa raha kabisa kumbe mwenzake alimfuata kwa sababu tu kulikuwa na namba za siri alizokuwa akizihitaji.
Usiku huo wakaonyesheana mapenzi motomoto na walipoachana tu, Richard akamtumia namba Robinson ambaye akaanza kufanya kazi ya kuingia katika database ya benki hiyo.
“Hureeeeee....” Robinson alipiga uyowe mkubwa.
Hakukuwa na muda wa kuchelewa, haraka sana Robinson akaingiza codes zake na kufanikiwa kuingia ndani ya database hiyo kwa kutumia namba za siri alizokuwa amepewa na Richard. Kazi hiyo ndiyo ilikuwa ngumu kuliko zote, kitendo cha kupata namba hizo zilimaanisha kwamba alikuwa na uwezo wa kufanya kitu chochote kile.
Kwenye database hiyo akatafuta akaunti yao, alipoiona, akaziona pesa hizo ila hazikuwa na uwezo wa kutoka hata kidogo. Hiyo ilikuwa kazi ndogo, alikuwa mtundu kupitiliza hivyo alichokifanya kilikuwa ni kuweka virusi vyake kwa ajili ya kuuharibu mfumo mzima kwa dakika kadhaa, azitoe pesa hizo na kuziweka katika akaunti yao iliyokuwa nchini Tanzania.
Hicho ndicho alichokifanya, haraka sana wakati virusi wakiwa wameanza kushambulia mfumo huo, huku akawa anafanya kazi yake ya kuhamisha pesa hizo.
Robert alikuwa pembeni yake, alibaki akishangaa tu, aliiangalia kompyuta ya Robinson na kazi iliyokuwa ikifanyika lakini hakuweza kupata kitu chochote kile, kwake vilionekana vitu ambavyo havikueleweka hata kidogo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alifanikiw akuhamisha pesa hizo ila hakutaka kuondoa kivuli, alihitaji watu wa benki watakapoangalia waone kuna pesa lakini baada ya kuingia kwa ndani wakute kukiwa na shilini 0.00.
“Huu ulikuwa mchezo mdogo sana,” alisema Robinson.
Kwa kuwa aliamini kwamba pesa hizo zingeweza kuonekana mahali zilipokwenda, akapata kazi nyingine ya kuharibu mawasiliano na baadaye kuufanya mfumo mzima wa kuhamisha pesa usomeke kwamba pesa zilitumwa kuelekea kwenye akaunti ya chama tawala cha nchi hiyo.
“Nimemaliza. Pesa zimekwishaingia,” alisema Robinson huku akionekana kuwa na furaha.
“Zimekwenda wapi sasa?” aliuliza Robert.
“Kwenye akaunti yetu!”
Hiyo haikutosha, kiasi ambacho alikituma huko kilikuwa kikubwa sana, watu wa benki wangeweza kuhoji kuhusu pesa hizo kitu ambacho alihisi kingewaweka matatani.
Mchezo alioucheza ulikuwa mdogo tu, akaziacha pesa hizo lakini akaweka loki kwamba watu wa benki kama wangeingia kwenye akaunti yao, kiasi cha pesa ambacho wangekikuta kingekuwa kilekile kumbe kulikuwa na pesa nyingine ambazo hazikuweza kuonekana mpaka pale ambapo wangeanza kufanya yao.
“Kwa hiyo hizo tuzifanyaje?” aliuliza Robert.
“Tutatakiwa kusafiri kuelekea nchini Marekani, huko tutafungua akaunti na tutaziingiza hizi pesa, hata tukizutuma huku kutakuwa hakuna maswali yoyote yale, tena kule kuna mambo mengi tutayafanya nitawaambia tukifika huko,” alisema Robinson.
Robert akabaki kimya akimwangalia rafiki yake huyo, alimshangaa lakini alimshukuru Mungu kwa kumkutanisha na mtu kama huyo. Alikuwa na akili kubwa mno, kitendo cha kuhamisha pesa hizo na kwenda kwenye akaunti yao huku akiwaambia kwamba hata benki wenyewe wasingejua kilimshangaza sana.
Baada ya saa moja, Richard akarudi na kuuliza kuhusu kilichoendelea. Akaambiwa kila kitu kwamba mchezo ulikamilika na pesa hizo zilikuwa mahali salama kabisa.
“Kwa hiyo mkwanja wote umeingia?” aliuliza Richard huku akionekana kushangaa.
“Ndiyo! Naomba simu nimpigie Oyoyo,” alisema Robinson na kupewa simu yake.
Hawakwenda nchini Kenya kuuza sura bali walikwenda huko kwa ajili ya kutengeneza pesa na kurudi nchini Tanzania. Robinson akawasiliana na Oyoyo na kumwambia kwamba picha walizokuwa wakizihitaji walikuwanazo hivyo kama walitaka basi walitakiwa kuwapa dola laki mbili kwa ajili ya kuwaachia picha hizo.
Kilikuwa kiasi kikubwa sana, si kwamba asingekipata, alikuwa na uhakika wa kukipata kwa muda mfupi lakini kiasi chote hicho kukitoa kwa mtu mmoja lilionekana kuwa jambo gumu.
Hakumficha, alimwambia ukweli, naye Robinson akamwambia kwamba kama suala hilo lilikuwa gumu basi wangekwenda kwenye kesi hiyo bila kuwa na ushahidi na hivyo Bwana Kimeta angeachwa huru kwa kuwa ushahidi ulikosekana.
“I will call you,” (nitakupigia) alisema Oyoyo na kukata simu.
Kichwa chake kilichanganyikiwa, mwanaume aliyeongea naye alionekana kuwa mtu hatari ambaye hakuonekana kuwa na masihara hata kidogo. Alichokigundua ni kwamba mwanaume huyo alikuwa Mtanzania kutokana na lafudhi yake ilivyokuwa katika kutamka baadhi ya maneno ya Kiswahili vizuri kabisa.
Akawaambia wenzake, nao walichanganyikiwa kama alivyochanganyikiwa. Walijadili suala hilo huku wakimshirikisha Jesca na mwisho wa siku kukubaliana kwamba wamtumie pesa mwanaume huyo kwa ajili ya kutumiwa picha hizo.
“Lakini kweli hatuwezi kuzipata pasipo kumtumia pesa?” aliuliza mwanaume mmoja.
Walikaa na kujadili kwa kipindi kirefu mno na mwisho wa siku wakakubaliana kwamba wachukue begi lililokuwa na pesa hivyo na kuondoka nalo kuelekea katika maduka ya Westgate Shoppig Mall yaliyokuwa hapo Nairobi.
Maduka hayo yalikuwa ni kama Mlimani City, ndiyo ambayo Jumamosi ya tarehe 21 mwaka 2013 yalivamiwa na wanamgambo wa kigaidi wa Al Shabaab na kuwaua baadhi ya watu na kutoroka.
Humo ndipo ambapo Oyoyo na wenzake walijadiliana kwamba ni lazima makabidhiano yafanyike huko ili kama itawezekana basi waweze kumkamata mtu huyo na kumfungulia mashtaka.
Baada ya kukubaliana, Oyoyo akampigia simu Robinson na kumwambia kuhusu jambo hilo. Kwanza akashtuka, kitendo cha kuambiwa kwamba makabidhiano yakafanyie huko Westgate Shoppig Mall kukamtia hofu kwa kuhisi kulikuwa na jambo moja kubwa lilitakiwa kutokea huko.
Alimwambia Oyoyo kuhusu jambo hilo, hofu aliyokuwanayo kwamba inawezekana mwanaume huyo alipanga mikakati ya kuhakikisha wanamkamata lakini Oyoyo alimwambia kwa sababu kiasi alichokihitaji kilikuwa ni kikubwa mno basi ilikuwa ni lazima waende huko na kukabidhiana.
“Mkileta polisi?”
“Hatuwezi kufanya hivyo kwa sababu mna picha za ushahidi! Naomba tuonane huko, sisi wenyewe hatukuamini, tukionana sehemu ambayo ni tofauti na huko unaweza kutuma watu wamteke mletaji halafu useme hukuzipata,” alijitetea Oyoyo.
“Sawa. Iwe kesho, majira ya saa kumi jioni, nitakwambia mahali pa kuziweka humo ndani,” alisema Robinson na kukata simu.
Aliwaambia wenzake kile alichoambiwa, wote wakacheka, waliambiwa jambo la kitoto sana, walihisi kwamba kulikuwa na mtego mkubwa ambao mwanaume huyo alitaka kuutumia lakini kwa sababu waliamini kwamba wao walikuwa na akili kubwa, wakakubali na hivyo kujipanga tayari kwa kwenda kuchukua pesa huko.
Walitakiwa kwenda Westgate, wakaone jinsi mazingira yalivyokuwa. Kwa kuwa ilikuwa ni mchana, wakaelekea huko na kuanza kuangalia huku na kule jinsi mambo yalivyokuwa humo ndani. Watu walikuwa wengi humo, ilikuwa ni Ijumaa ambayo kulikuwa na watu ambao waliamua kufanya manunuzi ili wikiendi wasitokea.
Walizunguka huku na kule na kuona sehemu ambayo waliamini kwamba kama pesa zingewekwa hapo na wao kwenda kuzichukua, basi ilikuwa ni lazima waonekane na kukamatwa.
“Nadhani pesa ziwekwe pale karibu na ule mlango ulioandikwa emergency,” alisema Robert.
“Halafu?”
“Nina wazo moja, kama kuna mwingine mwenye wazo jingine aseme tuone lipi zuri,” alisema Robert.
Akaanza kuwaambia kuhusu mpango wake. Alichokifikiria ni kwamba wafanye kila liwezekanalo kuhakikisha wanamtafuta mtu anayehusika na umeme ndani ya jengo hilo, kwa maana ya kwamba walitakiwa kuzima umeme wa jengo zima na kwa sababu humo hakukuwa na madirisha, kulikuwa na milango tu kama Mlimani City basi ingekuwa rahisi kuwa na giza kubwa na hivyo kuchukua pesa hizo na kuondoka nazo,” alisema Robert huku akiwaangalia wenzake.
“Ila napo kuna tatizo katika hilo,” alisema Robinson.
“Lipi?”
“Nje kuna mwanga. Huoni kama mtu ukiondoka na hilo begi utaonekana ukifika kwenye mwanga hata kama ndani kuna giza?” aliuliza.
“Atakayechukua begi hilo hatopitia mlango wa mbele, atapitia ule wa emergence,” alijibu Robert.
“Napo huko kuna mwanga. Nahisi tuangalieni jingine, yaani nataka hizi pesa zichukuliwe kitaalamu mpaka washangae,” alisema Robinson.
“Mimi nina wazo!” alisema Richard.
“Lipi?”
“Tufanyeni kila liwezekanalo tukarekodi milio ya risasi halafu tuje na flashi ambapo kwa ndani kutakuwa na sauti hizo za risasi,” alisema Richard huku wenzake wakimwangalia.
“Halafu!”
“Tukifika humu, kwa sababu kuna sauti ya muziki inasikika, bila shaka kuna sehemu ambapo hii miziki inabadilishwa, tujue ni sehemu gani, humo ndipo ambapo mmoja wetu atakwenda na kuweka hii flashi na kuanza kusikika hiyo milio ya risasi,” alisema Richard.
“Mh!”
“Ni wazo langu.”
“Halafu watu wakisikia milio ya risasi inakuwaje?” aliuliza Robinson.
“Yaani cha kwanza tutazima taa, kutakuwa na giza, watu si watajua ni kawaida umeme umekatika, halafu ghafla tunapiga kelele kwamba kuna mtu ana bunduki, watu wakitaharuki, yule aliyekuwa kwenye chumba cha kubadilishia muziki ataweka flashi na kuanza kupiga kelele za risasi. Hebu fikiria, mtu anasema kuna watu wa bunduki, ghafla umeme unazima na milio ya risasi kusikika huku kukiwa na giza, kuna mtu atabaki kweli ndani?” aliuliza Richard.
“Mh! Hakuna!”
“Na kwa sababu bado Wakenya wanaogopa uvamizi wa Al Shabaab ni lazima watakimbia kuelekea nje. Wakati watu wakikimbia, tunachukua begi letu, tunapita mlango huo wa dharura na kuondoka huku ndani kukiwa na varangati,” alisema Richard.
“Mh! Hilo wazo lako kiboko,” alisema Robert.
“Naomba tufanye hivyo! Tukifanikiwa katika hilo, basi pesa tumechukua na kusepa zetu,” alisema Richard.
“Sawa.”
Wakati hayo yote yakiendelea kupangwa, walikuwa wamekaa kwenye viti vyao wakiendelea kuyajenga. Kila mtu aliyekuwa akipita hapo aliwaangalia, kitu kilichowafanya watu kuangalia sana ni uzuri aliokuwanao Richard.
Wasichana wengine hawakutaka kupita, walisimama pembeni na kuanza kumwangalia Richard, alikuwa mzuri wa sura kiasi kwamba walihisi kuchanganyikiwa. Walitamani japo mwanaume huyo awasalimie tu lakini hakutaka kujirahisisha namna hiyo.
Baada ya kukubaliana, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuonana na mtu ambaye alihusika katika kubadilisha nyimbo zilizokuwa zikisikika humo na kuongea naye. Waliulizia na kuambiwa mahali alipokuwa. Wakaondoka na kumfuata, walipoonana naye wakamuita pembeni na kuzungumza naye.
Walijua jinsi Waafrika tulivyokuwa, kwenye mambo ya pesa walikuwa tayari kufanya jambo lolote lile. Walimwambia kuhusu kubadilisha sauti za muziki kwa sekunde kumi tu, yaani wanabadilisha muziki na kurudisha kama zamani.
Hawakutaka kumwambia ukweli kwa kuhisi kwamba angekataa. Walimdanganya kwa kumwambia kwamba mmoja kati yao mpenzi wake alikuwa akitimiza miaka ishirini na walitaka kumfanyia sapraizi mahali hapo, yaani watoe sauti za muziki wa kawaida na waupige muziki wa siku ya kuzaliwa ambao ulikuwa kwenye flashi yao.
Hilo halikuonekana kuwa tatizo hata kidogo, lilikuwa jambo dogo mno kwani haikuwa mara ya kwanza, Wakenya walikuwa wakifanya mambo hayo mara kwa mara humo hivyo akakubaliana nao na hivyo kumlipa kiasi cha shilingi elfu ishirini na kuondoka zao huku wakimwambia kwamba kesho wangerudi. “Hakuna tatizo!” alisema.
“Sawa. Nitakuja kesho,” alisema Robonson.
Baada ya kumaliza hilo, wakaondoka na kuanza kutafuta sehemu ya kuzima umeme jengo zima. Kwanza walitaka kujua kama jengo lingezimika, jenereta lingechukua muda gani mpaka kujiwasha.
Hilo walitakiwa kulifanya wenyewe, walimuuliza dada mmoja aliyekuwa na duka humo na kumwambia kwamba walikuwa mafundi umeme na hivyo walitaka kuona swichi ya kuzima jengo zima ilikuwa wapi, kwa kuwa alijua ilipokuwa, akawaonyeshea na hivyo kwenda huko.
Ilikuwa katika njia ya kuelekea chooni, kwa pembeni karibu kabisa na ofisi ya meneja mkuu wa hilo jengo. Walichokifanya, pasipo kuogopa kitu chochote kile, Robinson akaizima na kukimbia kuelekea chooni huku wakiangalia saa zao.
Ni ndani ya sekunde kumi tu, jenereta likawaka na hivyo kujua kwamba mara umeme unapokatika, huchukua sekunde kuanzia tano mpaka saba kwa jenereta kujiwasha, hivyo walitakiwa kufanya haraka sana.
“Tuna sekunde tano za kurekebisha kila kitu, twendeni tukajipange na kesho turudi kikazi. Ni lazima hizi pesa tuondoke nazo, cha msingi tuwaambie wazipeleke karibu na duka la Tecno, umeme ukizimika na milio ya risasi kusikika, mmoja anakwenda kulichukua, anatokea mlango wa dharura na kuondoka nalo, sawa?” alisema Robinson na kuuliza.
“Sawa.”
Walipofika hotelini, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuanza kurekodi sauti za milio ya risasi, hilo halikuwa tatizo, ilikuwepo nyingi sana kwenye mitandao na hivyo kuichukua na kuiweka kwenye flashi na hivyo kupanga mikakati ya kukamilisha jambo lao siku ya kesho ambayo ilikuwa ni Jumamosi iliyokuwa na watu wengi mno hapo Westgate Shopping Mall.
Asubuhi ya siku hiyo ilipofika, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuzungumza na Oyoyo, Robinson alimwambia mahali pesa hizo zilipotakiwa kuwekwa, hilo halikuwa na tatizo, mwanaume huyo akawapanga watu wake na kuwaambia kila kitu na hivyo ilivyofika majira ya saa tisa kuanza kuelekea huko.
Robinson na wenzake walikwishafika humo. Walikaa kwa kutengana huku macho yao yakiwa mahali pale walipotaka pesa hizo ziwekwe. Walimuona mwanaume mmoja akielekea pale, akaangalia huku na kule na kuziweka pesa zile zilizokuwa kwenye begi na kuondoka.
Waliangalia huku na kule, waliwaona baadhi ya vijana wakisogea karibu na kule, walijua kabisa kwamba hao walikuwa miongoni mwa watu waliotaka kuona ni nani ambaye angekwenda kuchukua lile begi, wamkamate na kuondoka naye.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ulikuwa ni mchezo wa kitoto sana, wakaacha na Robinson kuanza kuelekea kule kwa jamaa anayebadilisha nyimbo huku akiwa na flashi yake. Alitembea kwa kujiamini huku akiwa na kofia yake kichwani kwa ajili ya kujizuia na kamera za CCTV zilizokuwa mahali hapo.
Alipofika huko katika chumba cha kubadilishia miziki, akakutana na kijana yule aliyeonana naye jana na kuanza kuzungumza. Alimchangamkia kana kwamba walifahamiana miaka mingi iliyopita.
Wakaanza kuongea na Robinson kuchukua simu yake na kumwambia kijana yule alihitaji kuzungumza na mtu ambaye alikuwa humo na mpenzi wake ili ajiandae kumfanyia sapraizi hiyo.
Simu ikapokelewa na Robert na kuanza kuzungumza naye. Iliunganishwa mpaka katika simu ya Richard na hivyo watatu kuanza kuwasiliana.
Robinson alikwenda pembeni kidogo ili mazungumzo yake naye yasisikike na jamaa huyo. Alimwambia Robert kuwa alitakiwa kusogea kule kulipokuwa na begi lakini pia Richard alitakiwa kujifanya akienda chooni, yeye ndiye ambaye alitakiwa kuzima taa baada ya kusikia Robert akipiga kelele kwamba kulikuwa na mtu aliyekuwa na bunduki humo ndani.
“Haina shida! Weka flashi kabisa,” alisema Robert.
Baada ya kumaliza, hakukata simu, alimwambia jamaa kwamba alihitaji kuweka hiyo flashi, baada ya kuruhusiwa na kuiweka, akamwambia Robert aanze kupiga kelele kwa kudai kwamba kulikuwa na mtu aliyekuwa na bunduki ndani ya jengo hilo.
“Somebody got gun....somebody got gun....” (kuna mtu ana bunduki...kuna mtu ana bunduki...) alipiga kelele Robert, sauti ambayo ilisikika na kila mtu mahali hapo.
Watu wakaogopa, kumbukumbu za mwaka 2013 zikaanza kuwajia vichwani mwao, walichohisi ni kwamba wanamgambo wa Al Shabaab walivamia tena hivyo kujianza kukimbia.
Wakati wakiwa wametajaruki huku wakiangalia kila upande na Robert akiendelea kupiga kelele, mara ghafla milio ya risasi ikaanza kusikika kutoka kwenye spika zilizokuwa humo, hakukuwa na mtu aliyejua mahali zilipotoka, kwa kuwa hilo lilikuwa duka kubwa watu wakaanza kukimbia hovyo.
Wakati wakikimbia kuokoa maisha yao, ghafla umeme ukazimika kitu kilichowachanganya zaidi watu na kuhisi kwamba kweli kulikuwa na ugaidi humo na ndiyo maana baada ya milio ya risasi kusikika kwa wingi, umeme ukakatika.
Hakukuwa na mtu aliyegundua kwamba zilikuwa ni spika, Robert aliposema kwamba alimuona mtu akiwa na bunduki, na milio ya risasi kusikika na ghafla umeme kukatika, hakukuwa na mtu aliyebaki, kila mmoja akaanza kukimbia huku kukiwa na giza.
Wale waliokuwa kwenye maduka ya bidhaa wakatoka na kuanza kukimbia, wengi waliumia kwa kujigonga, watoto walianza kulia na hakukuwa na mtu aliyebaki mahali hapo, mpaka wauzaji wenyewe walianza kukimbia hovyo.
Hiyo ndiyo ilikuwa nafasi yenyewe, kulikuwa na giza lakini macho ya Robert yalikuwa makini mno, haraka sana akalisogelea lile begi, akalichukua, akaufungua mlango wa dharura na kutoka huku akiwa na begi lile.
Wanaume wale ambao walikuwa ndani humo kwa lengo la kumuona mtu ambaye angechukua begi hilo nao walitimua mbio, waliogopa kufa, walichanganyikiwa, walijua ni kweli kwamba kulikuwa na mtu aliyekuwa na bunduki ambaye alianza kushambulia.
Haraka sana kwa kutumia mwanga wa simu yake Robinson akatoka katika kile chumba na kukimbia, akaungana na Richard na kutoka nje ambapo wakaunganisha mpaka nyuma, wakakutana na Robert aliyekuwa na begi lenye pesa, wakachukua teksi moja na kuondoka huku wakiwa wamefanikiwa kwa kile walichokitaka.
Polisi walikusanyika nje ya maduka hayo huku wakiwa na bunduki, nao wenyewe waliogopa kuingia ndani, waliambiwa kulikuwa na magaidi humo ndani, walijua wanamgambo wa Al Shabaab walivamia tena na kufanya mashambulizi.
Hakukuwa na mtu aliyeingia, kila mmoja alibaki nje huku akiogopa, walisimama mbali kabisa kwa kuamini kwamba kweli mule ndani kulikuwa na magaidi kumbe hakukuwa na kitu.
Hapo nje walikuwa wakisikilizia, hawakutaka kuingia, walihitaji wanajeshi wafike kwani wao ndiyo waliokuwa wazoefu zaidi, baada ya dakika ishirini, wakafika makomandoo ambao wakaanza kuingia ndani kikomandoo huku wakiwa na magwanda yao na bunduki nzito na kali mikononi mwao.
Walitembea kwa machale huku wakiangalia kila upande, hawakufanikiwa kuona mtu yeyote wala maganda ya risasi, kama kweli risasi zilipigwa mfululizo ilimaanisha kwamba wangekutana na maganda lakini kitu cha ajabu kabisa kulikuwa peupe.
“Mbona hakuna mtu, hata damu?” aliuliza mwanajeshi mmoja huku akiangalia kila upande.
“Hata mimi nashangaa! Walisema kwamba kulisikika milio ya risasi, mbona hata maganda hakuna?” aliuliza mwingine.
Siku hiyo ilikuwa ni habari kuhusu uvamizi huo tu, kwenye vyombo vya habari kulikuwa na taarifa kuhusu tukio hilo kiasi kwamba hata Al Shabaab wenyewe waliposikia, walitoa taarifa na kusema kwamba hawakuhusika katika shambulio hilo.
Wakati hayo yote yakiendelea, Oyoyo alijaribu kuzungumza na vijana wale waliokwenda huko Westgate Shopping Mall na kuwauliza kuhusu kile kilichotokea. Vijana hao walimwambia kila kitu kwamba walikwenda kuweka begi lile lililokuwa na pesa na baada ya dakika kadhaa wakaanza kumsikia mwanaume mmoja akipiga kelele kwamba kulikuwa na mtu aliyekuwa na risasi, ghafla umeme ukakatika na milio ya risasi kuanza kusikika.
“Kwa hiyo?” aliuliza Oyoyo.
“Tukakimbia.”
“Mlirudi?”
“Ndiyo! Ila begi halikuwepo,” alisema Oyoyo.
Huko alipokuwa akashika kichwa, tayari akili yake ilimwambia kwamba pesa hizo zilichukuliwa na mwanaume huyo na iliwezekana kabisa kuhusu suala la uvamizi, hakukuwa na uvamizi wowote ule.
Akafuatilia taarifa ya habari, alihitaji kujua kila kitu kilichotokea kama kulikuwa na maganda ya risasi yalipatikana, alipouliza, aliambiwa hakukuwa na kitu chochote kile, yaani hakukuwa na dalili zozote zile za uvamizi ndani ya jengo hilo.
Akawapigia simu wenzake na kukutana, wakaanza kuzungumza suala hilo, hakuwaficha, aliwaambia ukweli kwamba hawakufanikiwa kumkamata kijana huyo kwa sababu alisababisha vurumai ndani ya jengo hilo na kuchukua pesa hizo.
“Mmh! Sijaelewa, yaani kivipi?” aliuliza mwanaume mmoja.
“Humo hakukuwa na uvamizi wowote ule.”
“Lakini wanasema kwamba milio ya risasi ilisikika!”
“Hakuna kitu!”
“Sasa hiyo milio ni ya nini?”
“Hebu subiri! Nahisi kuna kitu.”
Kichwa cha Oyoyo kilichanganyikiwa, alifikiria mambo mengi mno, akawachukua watu wake na kuelekea kwenye duka hilo, walisema kwamba kulisikika milio ya risasi, kama kweli hakukuwa na maganda ya risasi yaliyopatikana inamaana kulikuwa na njia nyingine ambayo ilitumika.
Akili yake ilimwambia mtu aliyekuwa akihusika na kubadilisha miziki ndani ya jengo hilo alikuwa akihusika hivyo kuonana naye na kuanza kuzungumza.
Kijana huyo alimwambia ukweli kwamba kulikuwa na mtu alimfuata akiwa na wenzake, alimwambia kwamba kulikuwa na msichana alikuwa na sherehe ya siku ya kuzaliwa hivyo walitaka kumfanyia sapraizi.
Alimwambia kila kitu, hakutaka kumficha. Oyoyo na wenzake walibaki wakimsikiliza tu na mwisho wa siku wakakubaliana kwamba walishindwa kumpata kijana huyo kwa kuwa aliwatoka katika hatua ya mwisho kabisa.
“Watanzania! Watanzania! Watanzania!” alisema Oyoyo huku akionekana kuchanganyikiwa. Pesa nyingi ambazo hakutaka kabisa kuona zikiondoka, zilichukuliwa katika mazingira ya kutatanisha na kubaki mikono mitupu.
***
Vijana watatu hatari, wazee wa mipango, vijana wasioshindwa na kitu chochote kile walikuwa ndani ya teksi wakirudi hotelini. Hawakuzungumza kitu chochote kile, walikuwa kimya huku wakiangalia nje ya gari hiyo.
Ilikwenda mpaka walipofika hotelini ambapo wakateremka na kumlipa pesa yake dereva teksi na kuingia ndani. Kila mmoja alikuwa na furaha, hakukuwa na mtu ambaye aliamini kwamba wangeweza kupata kiasi kikubwa cha pesa.
Hizo dola laki tano zilikuwa pesa nyingi mno, ni zaidi ya bilioni moja kwa pesa za Kitanzania. Walitakiwa kuondoka na kuiweka pesa ile kwenye benki, lakini haikutakiwa kuwa ya Tanzania, walitakiwa kuzibadilisha kwa mfumo wa dola na kuziweka katika akaunti yao.
Chumbani, begi likafunguliwa, walikuwa na mpango wa kuzibadilisha kuwa kwenye pesa ya Kimarekani lakini kitu kizuri kabisa tayari pesa hizo zilibadilishwa na hivyo kuwa na kazi nyepesi mno kwao.
Wakakumbatiana na kupongezana kwamba kazi kubwa waliyotakiwa kuifanya nchini Kenya ilikamilika na hivyo walitakiwa kuondoka kurudi Tanzania.
“Ila bado Kimeta!”
“Achana naye. Kwa hizi pesa tulizozipata, nadhani tumefanikiwa. Tuondokeni. Ngoja niwatumie hizi picha, kwa ishu ya Kimeta kumbaka yule msichana, acha apelekwe jela tu, sisi hatutoshughulika na ishu yake,” alisema Robinson na kumtumia Oyoyo zile picha huku akimshukuru sana kwa pesa alizoziweka kwenye begi kwani zilifika mikononi mwao salama kabisa.
“Ni kweli nyie ndiyo mliosababisha vurumai ndani ya Westgate?” aliuliza Oyoyo.
“Inawezekana! Ila pesa tamu sana. Siku nyingine kukitokea tatizo, usisite kuwasiliana nami,” alisema Robinson na kukata simu. Siku hiyohiyo wakaanza safari ya kurudi nchini Tanzania huku wakiwa wamepiga pesa za kutosha huko Kenya.
Upendo aliridhika, kitendo cha kuwa na Richard kilimpa moyo kwamba hatimaye alifanikiwa kupata alichokipata. Chuo kizima kilijua kwamba wawili hao walikuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi, alimpenda mwanaume huyo kiasi kwamba hakutaka kuona mtu yeyote yule akienda na kulivunja penzi lao.
Alikuwa radhi kufanya kitu chochote kile lakini si kuona akimkosa mwanaume huyo. Kulikuwa na wanawake wengi waliomfuata Richard na alijua kupambana naye, si kwa kuwafuata bali hata kuwatumia watu waliokwenda na kuwapiga mikwara mingi.
Kwa penzi la Richard alikuwa radhi kufanya chochote kile, kuua kwake halikuwa jambo gumu, ilimradi alijua kwamba alipambana kuhakikisha penzi lake na Richard linadumu, hakujali kitu chochote kile.
Aliagwa na Richard kwamba alikuwa akienda nchini kenya, aliambiwa na Robinson kuhusu kuhitaji kwa mwanaume huyo lakini moyo wake haukuwa na amani hata kidogo, alihisi kabisa kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea katika maisha ya watu hao.
Iliwezekana kabisa kwamba walikuwa wakimtumia mpenzi wake kwa ajili ya mambo ya kipumbavu na ndiyo maana alitamani kuwaambia ukweli kuhusu kumuacha mpenzi huyo ili aendelee kumfaidia.
Siku zikakatika mpaka ile ambayo Richard na wenzake wakarudi nchini tanzania na kuomba kukutana naye. Alijua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea kutokea huko, alikuwa na uhakika kwamba watu hao walipata pesa zake hivyo alitakiwa kuachana na Richard.
Hakukubali hata kidogo, ilikuwa ni lazima apambane kuhakikisha jambo hilo halikubaliki hata kidogo. Kwake, pesa hazikuwa na umuhimu wowote ule, alichokuwa akitaka kuwa nacho maisha yake yote ni Richard tu na si mtu mwingine.
Vijana hao walitaka kukutana na Upendo kwa kuwa Richard alichoka, hakuwa huru, Upendo alikuwa king’ang’anizi mno, kila wakati alitamani kuona akiwa na mwanaume huyo lakini si kuona akiondoka mikononi mwake.
“Najua mnajua jinsi yule demu alivyokuwa mbaya,” alisema Richard huku akiwaangalia wenzake.
“Ndiyo maana tukasema tukamlipe pesa zake ili akuache kwa sababu hatuna muda wa kuendelea kubaki nchini Tanzania, ni lazima tuondoke kuelekea Marekani mwezi huu,” alisema Robinson.
“Naomba kitu cha kwanza tumuite, tumlipe pesa zake na mimi niendelee na maisha yangu,” alisema Richard.
Hiyo ndiyo ilikuwa sababu ya kuwasiliana na Upendo kwa lengo la kuonana naye. Hilo halikuwa tatizo, wakaonana katika Mgahawa wa Samaki Samaki na kuanza kuzungumza naye.
Walimwambia ukweli, maneno yao yalikuwa kama msumali wa moto moyoni mwa Upendo, hakuamini alichokisikia, wakati mwingine alitamani sana kuona kila kitu kilichokuwa kikiendelea kuwa kama ndoto.
Moyo wake uliuma mno, alimwangalia Richard, hakutaka kumuacha, alitamani kuona akiendelea kuwa naye. Aliamini kwamba kiasi cha pesa ambacho aliwaazima watu hao kilikuwa kikubwa kiasi kwamba wasingeweza kukipata ndani ya muda mfupi namna ile.
Hilo lilimpa maswali mengi kichwani mwake, kama kweli watu hao walipata kiasi hicho kikubwa ndani ya mwezi tu, je, walikuwa wakifanya biashara gani ya siri kiasi cha kuwaingizia pesa hizo.
“Kwa hiyo sasa tunataka uachane na Richard, tunakulipa pesa yako sasa hivi,” alisema Robinson huku akimwangalia Upendo aliyeonekana kutia huruma mno.
“Ila mbona mnanikatili hivi?”
“Tunakukatili? Kivipi?”
“Kwa sababu tulikubaliana ni baada ya miaka mitano,” alisema Upendo.
“Hapana! Tulikubaliana ndani ya miaka mitano. Hata mwezi huu mmoja pia upo ndani ya miaka hiyo mitano,” alisema Robinson.
Kwa Upendo lilikuwa sula gumu kumuingia kichwani, katika vitu ambavyo hakutaka kabisa kuona vikitokea ni kuachana na mwanaume huyo.
Alizungumza nao lakini hawakutaka kumuelewa, walimwambia kuhusu mpango wao wa kusafiri na kuelekea nje ya nchi, hawakutaka kubaki nchini Tanzania kwa sababu kulikuwa na mambo walihitaji kuyafanya kwa ajili ya kuingiza pesa zaidi.
Japokuwa hakupenda lakini hakuwa na jinsi, mwisho kabisa Upendo akakubaliana nao lakini alihitaji kuzungumza na Richard kwa sababu kulikuwa na kitu muhimu sana alihitaji kumwambia.
Richard hakujua kilikuwa kitu gani, akakubali na hivyo kwenda pembeni na kuanza kuzungumza. Alichomwambia ni kwamba alikuwa na mimba yake, alihisi dalili zote na alifurahi sana kuona akiwa amepata mimba hiyo kwa kuwa yeye ndiye alikuwa mwanaume aliyempenda kuliko wote katika dunia hii.
“Una mimba yangu?” aliuliza Richard huku akimwangalia Upendo.
“Ndiyo!”
“Unamaanisha nini? Yaani unajua sijaelewa?” aliuliza Richard huku akimwangalia msichana huyo.
“Kwani mtu akiwa na mimba yako huwa anamaanisha nini?” aliuliza Upendo,
“Kwa sababu tulikuwa tunatumia kinga kila siku!”
“Lakini unakumbuka siku ambayo kinga ilipasukia ndani?” aliuliza Upendo.
“Nakumbuka! Lakini pia....”
“Richard! Nina mimba yako,” alisema Upendo na kuondoka mahali hapo.
Richard alibaki akiwa amesimama, hakuamini kilichokuwa kikiendelea, alikumbuka kabisa kwamba siku ambayo kinga ilipasukia ndani hakumwaga mbegu zake ndani ya mwanamke huyo, sasa ilikuwaje amwambie kwamba alikuwa na mimba?
Alijifikiria mengi, alijiuliza maswali ambayo hayakuwa na majibu yoyote yale. Upendo akawaambia wamtumie pesa hizo hivyo Robinson kumwambia kwamba siku inayofuata angekwenda benki na kumuhamishia kiasi hicho cha pesa, hivyo akaondoka zake.
Robinson na Robert walimwangalia Richard, kwa jinsi alivyoonekana ilionyesha kulikuwa na tatizo lililotokea, wakamuuliza na yeye kuwaambia kila kitu alichoambiwa na msichana huyo kwamba alikuwa na mimba yake.
Hakuwaficha kitu chochote kile, aliwaambia kuhusu kinga, kama alivyoshangaa yeye hata watu hao nao walishangaa, ilikuwa ni vigumu kwa msichana kupata mimba na wakati hakukuwa na mbegu zilizoingia katika mfumo wake wa uzazi.
Walichomwambia ni kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea, iliwezekana kabisa msichana huyo alikuwa akimdanganya kwa kuwa aliamini kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wao baada ya kulipwa pesa hizo.
“Kwa hiyo ananidanganya?” aliuliza Richard.
“Nadhani! Hebu kwanza wasiliana naye na umwambie ishu ya kwenda kupima,” alisema Robert.
Hilo ndilo alilolifanya, haraka sana akawasiliana na Upendo na kumwambia suala la kwenda kupima ili kujua kama alikuwa na mimba kweli ama la.
Upendo hakutaka kuona hilo likitokea ila alichokifanya ni kuanza kumzungusha kwa kumwambia wangekwenda lakini hilo halikutokea kabisa.
Richard akapata uhakika kwamba huo ulikuwa mpango uliochezwa na msichana huyo na ukweli ni kwamba hakuwa na mimba kama alivyokuwa amemwambia hivyo kuachana naye na kuendelea kufanya mambo yake mengine.
Siku zilikatika, baada ya siku mbili, Richard akaja kushtuka akiwa nje ya nyumba yake aliyopanga akiwa amelala kibarazani. Hakujua ni kitu gani kilitokea, alishangaa mno kwani kitu alichokikumbuka ni kwamba mara ya mwisho alikuwa klabu akinywa na marafiki zake na baada ya hapo, hakukumbuka ni kitu gani kilikuwa kimetokea.
Haraka sana akampigia simu Robinson na kuanza kuongea naye, alihitaji kukumbushwa mahali alipokuwa, ni kitu gani kilitokea mpaka asubuhi kujikuta akiwa kibarazani nyumbani kwake.
“Jana ulilewa sana, ulikunywa mpaka tukashangaa,” alisema Robinson kwenye simu.
“Nililewa sana?”
“Ndiyo! Wanawake walikufuata kutaka kuondoka nawe, ukakataa, yaani hukumbuki lolote lile?” aliuliza Robinson kwenye simu kitu kilichomfanya Richard kuanza kukumbuka.
“Halafu ikawaje?”
“Uliondoka mapema sana kwenda nyumbani. Nadhani ulipofika, hata kuingia ndani ukashindwa ndiyo maana ukalala kibarazani. Kichwa chako cha panzi, acha pombe chalii angu,” alisema Robinson na kuanza kucheka.
Richard akakata simu, hakutaka kuishia hapo tu, akampigia simu Robert na kuanza kumuuliza kilichokuwa kimetokea usiku wa jana. Kama alivyoambiwa na Robinson ndivyo alivyoambiwa na Robert pia kwamba alilewa sana na kuondoka kurudi nyumbani, hakukumbuka kilichotokea njiani mpaka asubuhi hiyo ambapo alijikuta akiwa amelala kibarazani.
“Mh! Pombe siyo ishu kabisa,” alisema Richard na kuingia ndani.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hakutaka kuwasiliana na Upendo, bado alikuwa na mambo mengi ya kufanya, kulikuwa na mipango mingi mbele yao ambayo walitakiwa kuhakikisha mpaka wanaipatia muafaka na kufanikiwa zaidi.
Walipanga kwa pamoja kwamba ni lazima wasafiri waelekee nchini Marekani ambapo huko waliamini wangepata pesa nyingi na kufanikiwa kuliko walivyokuwa barani Afrika.
Hawakuacha kukutana, kila siku walionana na kuzungumza mambo mengi mno. Walikumbuka kwamba walipanga kwenda nchini Misri baada ya kutoka Kenya lakini huko waliona kama wangejichelewesha, kwenda Marekani kungewafanya wapate mabilioni ya pesa.
Wakati wenzake wakiendelea kufikiria kuhusu kuelekea nchini Marekani kichwa cha Richard kilimfikiria zaidi Upendo. Alihisi kulikuwa na kitu kilitokea na ndiyo maana aliambiwa na msichana huyo kwamba alikuwa na mimba.
Alifikiria mambo mengi lakini kubwa zaidi ni kitendo cha kumpa mimba msichana huyo. Alikuwa mbaya wa sura, alichukiwa na wanaume wote chuoni lakini jambo la ajabu kabisa, eti mwisho wa siku alimpa mimba na kutarajia kupata mtoto pamoja naye.
“Hivi nizae na msichana mbaya namna ile! Mungu kwa nini umenipiga kwa pigo hili?” aliuliza Richard alipokuwa chumbani akifikiria kuhusu msichana huyo.
Kwa kuwa Upendo alijua Richard kuwa na mimba yake basi muda mwingi akawa anampigia, aliendelea kumwambia kwamba alimpenda kuliko mtu yeyote yule na ndiyo maana aliamua kupata ujauzito wake kama njia mojawapo ya kumuonyeshea ni kwa jinsi gani alimthamini.
Kwa Richard moyo wake ulikuwa na hasira mno, wakati mwingine alitamani kumwambia ukweli kwamba hakumpenda lakini kitendo cha kubeba mimba yake tu kikamfanya kuogopa na kuhisi kwamba angeharibu kila kitu.
“Ila simpendi! Huo ndiyo ukweli, yaani simpendi mno,” alisema Richard kila alipokuwa akimfikiria msichana huyo.
Siku ziliendelea kukatika, bado Richard aliendelea kuwaza kama kweli Upendo alikuwa na mimba au alikuwa akimtega. Moyo wake ukagawanyika, alihisi kabisa kwamba inawezekana msichana huyo alimdanganya ili tu baadaye afanye juu chini na azae hata mtoto kwa mwanaume mwingine ili ionekane kama yeye ndiye aliyekuwa baba wa mtoto huyo.
Hilo likampa hofu na hatimaye kuamua kumpigia simu na kuzungumza naye. Kwanza walizungumza mambo mengine kabisa na mwisho kabisa Richard akaingizia suala lake kwamba alihitaji kuamini kama msichana huyo alikuwa na mimba kweli au alimdanganya kwani kipindi cha nyuma kila alipokuwa akimwambia waende hospitali msichana huyo alikataa kwa kuleta visingizo vingi.
“Basi twende hospitali tukapime,” alise aRichard.
“Hakuna shida. Twende.”
Hilo ndilo lililotokea, siku iliyofuata wawili hao wakaondoka na kuelekea hospitalini. Huko, kila mtu aliyekuwa akiwaona alishangaa. Kilichowashangaza ni uzuri wa Richard na ubaya wa Upendo.
Walikuwa watu wawili wasioendana, wasichana wengi walitokea kuvutiwa na Richard lakini kwa jinsi alivyoamua kuwa na msichana mbaya kama Upendo, wengi walishangaa.
“Jamani yule kaka mzuriiiiiii....kama malaika,” alisema msichana mmoja aliyekuwa amekaa na wenzake kwenye benchi hospitalini hapo.
“Kweli shoga’angu...ila yule msichana aliyekuwa naye! Mh! Mbona anatisha hivyo?” aliuliza msichana mwingine huku naye akionekana kushangaa.
Muda wote Richard alikuwa akijishtukia, hakuamini kama kweli yeye leo hii alikuwa akitembea na Upendo ambaye alikuwa na mimba yake. Walikwenda moja kwa moja mpaka kwa daktari ambapo akampima Upendo na kukuta akiwa na mimba ya wiki mbili.
“Ni kweli una mimba ya wiki mbili,” alisema daktari huku akiwaangalia wawili hao walioonekana kuwa tofauti, kwa Upendo alikuwa na tabasamu pana ulioufanya ubaya wake uongezeka lakini kwa Richard alikuwa na hasira kali zilizomfanya kuonekana mzuri zaidi.
Ni kama Upendo alijua kila kitu kilichokuwa kikienda kutokea, kitendo cha Richard kutokuwa na furaha baada ya kuwa naye aliamini kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wao na hivyo kuachana. Hakutaka kuona hilo likitokea katika vitu ambavyo hakutamani kabisa kuona vikitokea basi kilikuwa ni kuachana na mwanaume huyo.
Alimpenda, tena kutoka moyoni mwake, alijua kabisa kila kitu kati yake na Richard kilikuwa kikienda mwisho kwa kuwa tu mwanaume huyo hakuonekana kumpenda hata kidogo.
Alihitaji sana kuwa na mtoto na Richard, hakujua angefanya nini kwani mwanaume huyo naye alikuwa makini sana kila walipokuwa wakifanya mapenzi. Hilo lilimsumbua sana kichwani mwake, hakutaka kuona akiendelea kusononeka, aliamua kuanza kuulizia kama kungekuwa na uwezekano wowote wa kufanya ili ashike mimba yake.
Akampigia simu rafiki yake aliyekuwa nchini Marekani na kumuuliza kuhusu jambo hilo. Rafiki yake huyo akamwambia kama kweli alihitaji kushika mimba kutoka kwa Richard ilikuwa ni lazima azichukue mbegu zake na kuzipandikiza kwenye mayai yake.
“Kivipi?” aliuliza Upendo.
Rafiki yake huyo aliyeitwa kwa jina la Manka akaanza kumwambia kuhusu vitu hivyo ambavyo alitakiwa kufanya. Kulikuwa na mambo mawili ambapo yeye alitakiwa kuchagua mojawapo kwa ajili ya kulifanya kushika mimba ya mwanaume huyo.
Kitu cha kwanza kiliitwa IVF yaani In Vitro Fertilization. Hii ni njia inayotumika kwa wanawake ambao wanakuwa na mirija iliyoziba, wanaume wenye mbegu chache, wanawake waliokuwa na uvimbe katika ovari na matatizo mengine mengi.
Hii hufanyika kwa kuchukua mbegu za mwanaume na mwanamke na kuziweka katika chupa maalumu iliyokuwa na hali ya joto ambapo pale hukaa kwa kipindi kirefu na mtoto kuanza kutengenezwa.
Hatua ya kutengeneza mtoto kwa kutumia mbegu za mwanaume na mwanamke ilianza mwaka 1978 katika Mji wa Oldham nchini Uingereza ambapo Louise Joy Brown alitengenezwa katika chupa na kuwa mkubwa kabisa huko maabara.
Yalikuwa ni mafanikio makubwa mno kufanyika na hivyo watoto kuendelea kutengenezwa kwenye chupa mpaka leo hii.
Ukiachana na IVF pia kulikuwa na ile ya kufanya Surrogation. Hiyo ni ile hatua ambayo mwanaume anatolewa mbegu zake na kupandikizwa kwa mwanamke pasipo kufanya mapenzi.
Mbegu za mwanaume zinapokutana na yai la mwanamke, hupata mimba na kuanza kukua mpaka kufikia hatua ya kujifungua.
Hii njia hutumika zaidi kwa matajiri ambao wanakuwa hawana watoto hivyo huchukua wanawake wengine na kuwapandikizia mbegu na kujifungua.
Hii ilionekana kuwa njia sahihi kwa Upendo, alihitaji kuwa na mbegu za Richard ili azichukue na kuzipandikiza katika mfuko wake wa uzazi ili ashike ujauzito wa mwanaume huyo na mwisho wa siku kujifungua.
“Hiyo njia ya pili nimeipenda. Ninaweza kuonana na watalaamu hao?” aliuliza Upendo.
“Si tatizo!”
Haraka sana akaunganishwa na madaktari hao na kuanza kuwasiliana nao kwa barua pepe. Aliwaambia ukweli kwamba kulikuwa na mwanaume ambaye alihitaji sana kuchukua mbegu zake na kuzipandikiza katika mayai yake.
Hilo halikuwa tatizo hata kidogo, madaktari hao wakakubaliana naye na kumwambia alipie kiasi cha dola laki mbili kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.
Kwake, pesa hazikuwa na tatizo lolote lile, kitu pekee alichokuwa akikitaka wakati huo ni kupata mtoto ambaye angezaa kutokana na mbegu za Richard.
Upendo aliwaambia kuhusu Richard, aliwaambia kila kitu na hivyo madaktari hao kumwambia kwamba wangefanya kila liwezekanalo kumsaidia kwa hali na mali.
Baada ya siku kadhaa, madaktari hao wakasafiri mpaka nchini Tanzania ambapo wakaonana na Upendo huku wakiwa na vifaa vyote na hivyo kuanza kumsubiri Richard aliyekuwa amekwenda nchini Kenya.
Baada ya kurudi ndipo akamwambia kuhusu suala la mimba. Alihitaji kumtengeneza kwanza, ajue kwamba alikuwa na mimba yake. Richard alipoambiwa na hivyo kutaka kwenda kupima na msichana huyo alikataa katakata na alifanya hivyo kwa sababu bado mbegu hazikuwa zimepandikizwa.
“Hivi tutaweza kuzipata mbegu zake kweli pasipo kufahamu?” aliuliza Upendo.
“Zitapatikana!”
Alichomwambia daktari ni kumnywesha dawa ya usingizi mwanaume huyo na kisha apelekwe sehemu ambapo huko angetolewa mbegu zake kitaalamu na kupandikizwa kwenye mayai yake.
Hilo likamfanya Upendo kuwashirikisha wasichana wawili ambao walitakiwa kumfuatilia Richard kila kona na siku ile ambayo alikwenda klabu na wenzake na kunywa, miongoni mwa wasichana waliokuwa wamekaa nao walikuwa hao wawili.
Wakamuwekea dawa ya usingizi mzito kwenye kinywaji chake na alipokunywa tu, akahisi uchovu mwingi, akaaga n kuondoka humo ila alipofika ndani ya gari tu, akapitiwa na usingizi mzito.
Wasichana hao wakaingia ndani ya gari hilo na kuondoka naye ambapo wakaonana na Upendo aliyekuwa amewaandaa madaktari wake hivyo kumchukua Richard na kumpeleka kwenye chumba fulani walichokuwa wameandaa.
Macho yao yalipotua kwa mwanaume huyo, wakapata sababu ya Upendo kutamani mno kuzaa naye, alikuwa mwanaume mzuri wa sura, alivutia kiasi kwamba ingekuwa ni vigumu kwa msichana yeyote yule kukataa kuzaa naye.
Humo ndani wakaanza kuushtua mwili wake, kuifanya damu yake izunguke kwa kasi kubwa. Walimshika sehemu muhimu, hasa kwenye nyonga na magotini kwa nyuma na kuanza kuzitekenya sehemu hizo.
Ulikuwa ni utaalamu mkubwa, mambo hayo yote yalifanyika huku akiwa amepitiwa na usingizi mzito. Madaktari hao walikuwa wazoefu na kazi zao, mara kiungo cha Richard kikasimama na kuendelea kufanya kazi yao kwa kutumia mafuta maalumu laini waliyokuwanayo.
Walifanikiwa kwa asilimia mia moja, mbegu zake zikatolewa, zikawekwa kwenye chombo maalumu na kisha Upendo kuchomwa sindano ya usingizi, kifaa kingine kikachukuliwa na kuanza kuingizwa kwenye mayai yake kupitia sehemu za siri.
Mbegu hizo ziliingizwa, walizifuatilia kwa kutumia mashine maalumu, zikaenda katika yao la uzazi la Upendo na hivyo kuanza kutengeneza mtoto taratibu pasipo wawili hao kukutana kimwili.
Baada ya kumaliza hatua hiyo iliyochukua saa mbili, Richard akachukuliwa na kupelekwa ndni ya gari ambapo liliendeshwa, na alipofikishwa kwake, akatolewa na kulazwa kibarazani huku akiwa hajui ni kitu gani kilitokea.
***
Vijana hao watatu hawakutaka kuendelea kubaki nchini Tanzania, ili wapate pesa zaidi ilikuwa ni lazima kuondoka na kuelekea nchini Marekani. Huko walikuwa na uhakika wa kuingiza pesa nyingi sana kama tu wangekuwa na uwezo wa kufanya madili makubwa na mengi.
Njiani, wakiwa ndani ya ndege vichwa vyao havikutulia hata kidogo, walikuwa wakifuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea wakati huo nchini humo. Kulikuwa na mambo mengi mno kiasi kwamba walichanganyikiwa ni lipi ambalo walitakiwa kuanza nalo.
Walitaka kudili na watu wakubwa kiasi cha serikali kushtuka lakini pia wakahisi kitendo cha kutafutwa na serikali ya Marekani ingekuwa kitu kikubwa na kibaya mno kiasi kwamba ingewafanya kutokuishi kwa raha kama walivyotakiwa kuishi na wakati walikuwa na pesa.
“Kuna taarifa nimeiona hapa,” alisema Robert huku akiwaoyeshea wenzake simu iliyokuwa imeunganishwa na huduma ya intaneti.
“Habari ipi?”
“Mshawahi kumsikia mtu anaitwa Kamacho?” aliuliza.
“Hapana! Ndiye nani?”
Robert akaanza kuwaelezea kuhusu mtu huyo. Alikuwa ni mmoja wa watu waliokuwa wakitafutwa sana na serikali ya Marekani. Alikuwa mtu wa Mexico ambaye alisafirisha sana madawa ya kulevya kuelekea nchini humo.
Katika orodha ndefu ya CIA, mtu wa kwanza kabisa ambaye alikuwa juu ni huyo mwanaume. Kazi yake kubwa ilikuwa ni kusafirisha madawa ya kulevya kutoka Mexico na kuingia Marekani.
CIA walipambana naye, walijitahidi kuizuia biashara hiyo lakini walishindwa kabisa kitu kilichowafanya kumteka kaka yake aliyeitwa kwa jina la Hernandez na kumfunga gerezani kwa kumsingizia kuhusika na uuzaji wa madawa ya kulevya kama ilivyokuwa kwa ndugu yake.
Walichomwambia ambacho kilikuwa cha siri sana ni kutakiwa kujisalimisha, kama kweli alihitaji ndugu yake atoke gerezani, na kama alimpenda basi alitakiwa kuelekea nchini Marekani na kujipeleka mwenyewe katika kituo cha polisi.
“Oh! Sasa hapo kuna nini? Yaani kuna uhusiano upi wa sisi na huyo Kamacho?” aliuliza Richard huku akimwangalia Robert.
“Yaap! Hivi hatuwezi kumtorosha jela huyo Hernandez halafu tukapiga pesa ndefu kwa Kamacho?” aliuliza Robert.
Swali lake hilo likamfanya Richard kuanza kuangaliana na Robinson, kwao lilikuwa jambo moja gumu sana ambalo walihisi kabisa wasingeliweza hata kama wangetumia ujanja gani.
“Haiwezekani!” alisema Robinson.
“Hahah! Hakuna kitu kama hicho. Unakumbuka kwamba hakuna kisichowezekana chini ya jua? Basi hili nalo linawezekana kabisa kufanyika, tumtorosheni huyu mtu,” alisema Robert huku akiwaangalia wenzake.
“Tutafanya vipi? Yaani itakuwaje mpaka tumtoroshe mwanaume huyu?” aliuliza Robinson.
Robert akaanza kuwaambia mipango yake, kile alichokuwa amekifikiria ambacho aliamini kwamba kama wangekifanya basi ingekuwa kazi nyepesi kwao kumtoa gerezani Hernandez.
Kwa jinsi alivyokuwa akiielezea mipango yake, ule ugumu ambao ulikuwa vichwani mwa marafiki zake ukaanza kutoweka na hatimaye hata nao kuhisi kwamba kitu hicho kilikuwa chepesi sana kama tu wangethubutu kufanya hivyo.
Aliwaambia mipango yote na baada ya hapo akawaambia kuwa kama wangefanikiwa basi wangechukua kiasi cha dola milioni mia moja kutoka kwa Kamacho.
“Atatoa hizo pesa?” aliuliza Richard.
“Atatoa tu. Damu nzito kuliko maji, hizo pesa atatoa. Kama kweli mtu ana utajiri wa dola bilioni kumi, tena kila siku anaingia mamilioni ya pesa, atashindwaje kutoa pesa hizi, cha msingi ni kuonana naye kwanza,” alisema Robert huku akiwaangalia wenzake.
Dola milioni mia moja zilikuwa ni zaidi shilingi bilioni mia mbili, walitakiwa kupambana mpaka wanazipata pesa hizo kutoka kwa Kamacho.
Ndege ilichukua saa ishirini na mbili ndipo ikaanza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JFK jijini New York.
Kabla ya kuteremka wakaanza kuangalia mandhari ya jiji hilo. Walikumbuka kwamba waliambiwa mengi kuhusu Marekani na siku hiyo walikuwa ndani ya ndege wakiteremka tayari kwa kukanyaga ardhi ya nchi hiyo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kipindi cha nyuma, miezi michache iliyopita hawakuwa na uhakika wa kufika nchini humo kwa haraka kipindi hicho lakini siku hiyo, ni ndani ya miezi michache tu walikuwa wakikanyaga huku wakiwa matajiri wakubwa.
Walipoikanyaga tu, kila mtu akashusha pumzi kwa nguvu, moja ya ndoto zao zilikuwa zimekamilika kitu kilichowafurahisha mno.
Wao na abiria wengine wakaanza kutembea kuelekea lilipokuwa jengo la uwanja huo. Walipofika, wakachukua mabegi yao na kutoka nje ambapo walikuta gari la Hoteli ya King Lear likiwasubiri nje, wakaingia na kuanza kuelekea katika hoteli hiyo huku kila mmoja akiwa na uhakika wa kufanikiwa.
“Jamani kama tutafanikiwa, tutakuwa tumepiga bonge moja la bao,” alisema Robinson huku akiwaangalia wenzake.
“Kweli kabisa. Ila tutafanikiwa, hata kama CIA watatutafuta, bado tutafanikiwa tu,” alisema Richard huku akiwa na uhakika kufanikiwa kwa mipango yao yote waliyokuwa wameipanga ndani ya ndege. Kitu cha kwanza kilikuwa ni kumtafuta huyo Kamacho.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment