IMEANDIKWA NA THE BOLD
************************************************************************
Simulizi : Geranimo E.k.i.a Kutoka Makao Makuu Ya Cia Langley, Oparesheni Ya Kukamatwa Osama Bin Laden
Sehemu Ya Kwanza (1)
Mwaka 2001, mwezi Desemba katika milima ya Tora Bora baada ya mapambano ya siku kumi na moja toka tarehe 6 hadi 17 na mabomu kadhaa kudondoshwa katika milima hiyo hatimaye askari wa miguu walianza zoezi la kuikagua milima hiyo kuangalia kama kuna masalia yoyote muhimu yanayoweza kuwapa fununu ya kuielewa vita waliyoianzisha kati yao Majeshi ya Marekani na Wanamgambo wa Taliban.
Katika mchakato huo wa ukaguzi wanajeshi wa marekani walifanikiwa kumuokota kijana mmoja wa umri wa mika 21 akiwa hai. Baada ya kumuokota wanajeshi kadhaa wakampakia katika chopa ya kivita na kurudi nae katika kambi ya kijeshi ya Bagram Air Base iliyo nchini Afghanistan.
Baada ya kufika katika kambi ya Bagram wanajeshi wakaanza kumuhoji kijana huyo ajieleze yeye ni nani na alikuwa anafanya nini katika milima ya Tora Bora.
Baada ya kujitambulisha kijana huyo akawaeleza kuwa alikuwa anawinda katika milima hiyo ya Tora Bora na kwa bahati mbaya akajikuta ameingia kwenye eneo ambalo hakujua kuwa kulikuwa na mapigano ya kijeshi.
Maafisa wote wa kijeshi hawakuamini maelezo haya na waliendelea kumuhoji kwa siku kadhaa lakini yule kijana alishikilia maelezo yake yale yale kuwa alikuwa anawinda milimani.
Baada ya kutokuwepo kwa mafanikio yoyote ya kumuhoji kijana huyu Maafisa wa ngazi za juu wa kijeshi katika kituo cha Bagram wakawasiliana na maafisa wa CIA waliopo nchini Afghanistan na kuwaeleza juu ya tukio hilo. Maafisa hao wakawashauri kuwa kijana huyo wakabidhiwe wao ili wamuhoji wao kwa kina.
Siku tatu baadae kijana huyo akakabidhiwa kwa maafisa wa CIA na wao wiki moja baadae wakamsafirisha kutoka Afghanistan mpaka kwenye jela za siri (Black Sites) za CIA zilizopo ulaya katika nchi ya Romania na baadae akaamishiwa jela za siri nchini Poland.
Baada ya kijana huyo kufikishwa huko mahojiano yakaendelea na akaendelea kushikilia msimamo wake kuwa alikuwa anawinda kwenye milima ya Tora Bora. CIA ikaamua kupanua wigo wake zaidi ili wamtambue. Wakachukua alama zake za vidole na kuziingiza katika mfumo wa alama za vidole wa nchi karibia zote za kiarabu lakini wakapata matokeo sifuri, hakukuwa na taarifa zozote zinazoshabihiana alama za vidole za kijana huyo.
Hii ilikuwa na maana nyingi lakini maana moja kubwa ni kwamba kijana huyu hakuwa na rekodi yoyote ya uhalifu katika maisha yake, alikuwa ni 'raia mwema'!
CIA wakaanza kuhisi labda kijana huyu kweli hakuwa na hatia yoyote. Lakini kabla hawajalipa nafasi wazo hilo kukua kwenye vichwa vyao, wakaakua wafanye kitu cha kubahatisha, wakaingiza alama za vidole za kijana huyo katika mfumo wa kiusalama wa nchini kwao marekani na matokea ambayo waliyapata hakuna ambaye aliweza kuamini.
Kumbukumbu za mifumo ya kiusalama ya nchi za marekani zilionyesha kuwa mtu mwenye alama hizo za vidole zinafanana kabisa na mtu ambaye alijaribu kuingia nchini marekani siku ya tarehe 3 Agosti 2001 katika uwanja wa ndege wa Orlando, Florida akitokea Dubai.
Maafisa wa uhamiaji wa uwanja wa ndege wakamkataa kuingia nchini marekani kutokana na sababu kadhaa. Kwanza kijana huyo alikuwa na fedha dola 2,800 pekee na hii iliwapa shida maafisa wa uhamiaji kuelewa angewezaje kuishi nchini marekani? Pili kijana huyu alikuwa amekata tiketi ta kwenda pekee (one way ticket).
Sababu hizi mbili zilipelekea maafisa wa uhamiaji wa uwanja wa ndege kuhisi kijana huyu alikuwa na mpango wa kuwa muhamiaji haramu kwani dalili hizo zilionesha kuwa hakuwa na mpango wa kurudi tena kwao. Hivyo basi maafisa hao wa uhamiaji wa uwanja wa ndege wa Orlando wakamkataa kijana huyo juingia nchini marekani na wakamrudisha alikotokea.
Maafisa wa CIA walishitushwa na jambo hili na wakawasiliana na vyombo vingine vya usalama nchini Marekani na pasipo kupoteza muda maafisa kutoka shirika la upelelezi la FBI wakafika katika uwanja wa ndege wa Orlando, Florida ili wapate taarifa zaidi kuhusu nini hasa kilitokea siku ya Agosti 3 2001 siku ambayo kijana huyo alikataliwa kuingia nchini marekani.
Baada ya FBI kufika uwanja wa ndege waliomba kuzungumza na maafisa uhamiaji waliokuwepo siku ya tarehe 3 Agosti pia waliomba wapatiwe mikanda ya video ya kamera za ulinzi za uwanja wa ndege.
Baada ya kuangalia mikanda hiyo ya video, FBI waligundua jambo kubwa zaidi ambalo hawakulitegemea kabisa. Kamera za ulinzi zilizo nje ya uwanja zilirekodi gari inayomilikiwa na Mohamed Atta likiwa limepaki nje ya uwanja wa ndege.
Kwa wasiomfahamu Mohammed Atta ndiye alikuwa mtekaji kiongozi wa watu walioteka ndege za kimarekani na kwenda kuzigongesha katika magorofa ya WTC siku ya tarehe 11, Septemba 2001. Pia ndiye aliyeendesha moja wapo ya ndege hizo zilizotekwa.
Kwahiyo FBI wakang'amua kuwa siku hiyo Mohammed Atta alifika uwanja wa ndege kumpokea kijana huyo lakini kwa bahati mbaya maafisa uhamiaji walimkataa asiingie Marekani.
Hii ilikuwa na maana kwamba kama kijana huyu asingelitiliwa shaka na maafisa wa uhamiaji basi alitakiwa kuwa mojawapo ya washiriki walioteka ndege na kuzilipua katika majengo ya WTC siku ya Septemba 11, 2001.
Taarifa hizi ziliishitua FBI na pasipo kuchelewa wakawataarifu maafisa wa CIA katika jela ya siri nchini Poland ambako kijana huyu alikuwa anashikiliwa, na baada ya maafisa hawa kupata taarifa hii mara moja wakawasiliana na Makao Makuu ya CIA Langley, Virginia nchini Marekani.
Mara baada ya taarifa hizi kufika Makao Makuu ya CIA, Mkurugenzi wa CIA Bw. Leon Panetta akaamuru kijana huyo awekwe 'mahali salama' kwa ajili ya 'mahojiano' zaidi.
Ndege ikaandaliwa na safari ya kuelekea gereza la Guantanamo Bay ikaanza.
Jina halisi la kijana huyu anaitwa Mohammed al-Qahtani kipindi anakatwa alikuwa na umri wa miaka 21 na kwa sasa ana miaka 36 na ni mfungwa namba 63 (ISN 10063) katika gereza la Guantanamo Bay.
NDANI YA GUANTANAMO: 'MAHOJIANO' ZAIDI
Baada ya kijana al-qahtani kufikishwa katika gereza Guantanamo ambapo aliwekwa selo katika jengo lililoitwa Camp Delta 'mahojiano' zaidi yakaendelea. Licha ya mambo yote ambayo vyombo vya usalama viligundua juu yake lakini kijana yule aliendelea Kushikilia msimamo wake kuwa alikuwa anawinda kwenye milima ya Tora Bora.
Ilifikia hatua mpaka Katibu mkuu kiongozi wa makamu wa rais wa kipindi hicho Bw. David Addington pamoja na mshauri wa ikulu Bw. Alberto Gonzales walifika binafsi katika jengo la Camp Delta ndani ya gereza la Guantanamo mahsusi kwaajili ya kuongea na kijana al-qatani ili aeleze ukweli lakini kijana huyo akashikilia msimamo kuwa yeye ni muwindaji.
Ndipo hapa ilipofikia hatua hii Waziri wa Ulinzi wa Marekani wa wakati huo akaidhinisha 'Mbinu za Mahojiano Zilizoboreshwa' (Enhanced Interrogation Techniques) zitumike kumuhoji kijana huyo.
Mbinu hizi zilizoboreshwa zilikuwa zinajumuisha kwa mfano kutesa mfungwa kwa kumnyima pumzi kimateso kwa kumiminia maji (waterboarding), mikao ya msongo (stress positions), kumnyima usingizi n.k.
Uamuzi huu ulikuja kuleta mushkeli na watu wa haki za binadamu miaka iliyofuata.
Baada ya maafisa waliokuwa wanamuhoji kupewa idhini ya kutumia 'mbinu zilizoboreshwa' inasemekana kwamba kijana al-Qahtani ndiye mmoja wa wafungwa wa Guantanamo waliovunja rekodi kwa kuhojiwa muda mrefu zaidi kwa 'mbinu zilizo boreshwa'. Inasemekana kijana al-Qahtani alihojiwa kwa siku 48 mfululizo!
0 comments:
Post a Comment