Search This Blog

Tuesday 20 December 2022

MIFEREJI YA DHAHABU: PASIPO SILAHA, CHUKI WALA UKATILI - 5

    


http://pseudepigraphas.blogspot.com/2020/06/mifereji-ya-dhahabu-pasipo-silaha-chuki_10.html


Simulizi : Mifereji Ya Dhahabu:  Pasipo Silaha, Chuki Wala Ukatili 

Sehemu Ya Tano (5)


Baada ya muhunzi kugundua kuwa mlango huo hautaweza kufunguka kwa nje akapendekeza kuwa watoboe ukuta ili kuingia ndani. Viongozi wa benki wakakubali na kazi kutoboa ukuta ikaanza. Kutokana na unene wa ukuta na kutoboa kwa makini ili wasisababishe hasara nyingine, ilichukua takribani masaa matatu kutoboa tundu kubwa kiasi la kumuwezesha mtu kupita. Yule muhunzi ndiye alikuwa mtu wa kwanza kuchungulia ndani na alipochungulia alipatwa na mshangao kana kwamba amepoteza fahamu kwa sekunde kadhaa. Hakuamini alichokuwa anakiona ndani ya vault. Huku bado akiwa na mshangao alimgeukia Meneja wa Benki aliyekuwa amesimama nyuma yake na kumwambia kwa mshangao, "Merde de putain" ("you have been robbed" ("Mmeibiwa")).


Baada ya wote bumbuwazi kuwaisha kutokana na kutoamini macho yao walichokuwa wanakiona mbele ya macho yao, hatimae wakapiga simu polisi na haraka sana polisi wakawasili. Baada ya Polisi kuwasili na kuingia ndani ya vault nao pia hawakuamini kile walichokuwa wanakiona mbele ya macho yao. Wote kwa pamoja macho yao yaliganda kwenye Ujumbe ulioandikwa kwenye ukuta, "sans armes, ni haine, ni violence" (Pasipo silaha, chuki wala ukatili).




KUKAMATWA, KUSHTAKIWA NA KUWA 'HURU' TENA


Ndani ya miezi miwili polisi walifanikiwa kugundua kuwa Spaggiari ndiye muhusika mkuu wa tukio lile. Haijulikana hasa ni namna gani polisi walifanikiwa kugundua kuwa Spaggiari ndiye alikuwa 'mastermind' wa tukio lile, kwani kumekuwa na maelezo mengi sana yanayokinzana lakini angalau ufafanuzi unaoonyesha uhalisia kidogo ni kwamba mmoja wapo wa watu walioshiriki tukio lile alipopewa mgao wake wa fedha pia alipewa na miche kadhaa ya dhahabu (gold bars) na bila kutumia akili au kuwa na subira akauza mche mmoja ndani ya wiki chache baada ya tukio. Baada ya siku kadhaa mtu aliyeununua mche huo aliripoti polisi kuwa ameuziwa mche wa dhahabu unaofanana kabisa na moja ya miche inayoripotiwa kuwa imeibiwa kwenye vault ya benki ya Société Générale.

Polisi wakamfatilia huyo mtu na wakafanikiwa kumtia nguvuni na baada ya kumuhoji kwa siku kadhaa akawataja wenzake wote akiwemo Albert Spaggiari.


Polisi waliposikia kuwa Spaggiari ndiye alikuwa kiongozi wa tukio hilo, walishikwa na butwaa kwani Spaggiari alikuwa ni moja ya watu mashuhuri na anayeheshimika zaidi jijini Nice. Na kipindi wanapata taarifa hii alikuwa yuko safarini mashariki ya mbali akiwa amemsindikiza rafiki yake Meya wa jiji Bw. Jacques Médecin, katika ziara ya kiserikali.


Siku ambayo Meya na Spaggiari wanarejea Nice kutoka mashariki ya mbali, Spaggiari alikamatwa hapo hapo uwanja wa ndege na kufunguliwa mashtaka ya kuhusika kupanga na kushiriki tukio la ujambazi katika benki ya Société Générale.


Kesi hii ilitikisa vyombo vya habati ulimwengu mzima na umaarufu wa Spaggiari ukaongezeka maradufu na mwenyewe alionekana kufurahia haswa jinsi alivyokuwa anazungumziwa kila kona ya Dunia.


Wakati kesi ikiwa inaendelea Spaggiari akatunga hadithi ambayo kwa bahati mbaya Jaji aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo aliiamini na akawa anatamani kujua kiundani. Spaggiari aliwaeleza kuwa alifanya tukio hilo ili kukiwezesha kiuchumi kikundi cha siri cha wazalendo kilichoitwa 'Catena' (neno la kifaransa linalomaanisha 'Chain' (mnyororo)).


Spaggiari akawaeleza kuwa hayuko tayari kuwapa taarifa za kikundi hicho Polisi kwani hawaamini bali yuko tayari kutoa taarifa kwa Jaji huyo peke yake. Hivyo basi ikawekwa ratiba maalumu ambayo Spaggiari alikuwa anapelekwa ofisini kwa Jaji na kila walipokutana alikuwa anampa kikaratasi alichokiandika kwa mafumbo (coded message) na ilikuwa inamlazimu Jaji akune kichwa haswa ili kung'amua kilichoandikwa na Spaggiari kuhusu siri za hicho kikundi cha 'Catena'.


Katika moja ya vikao vyao na Jaji, Jaji akiwa 'bize' kung'amua Ujumbe huo wa mafumbo Spaggiari aliinuka kutoka kwenye kiti kana kwamba anataka kumkaribia Jaji ili ampe ufafanuzi. Lakini jambo la ajabu alikimbia kwa spidi ya ajabu mpaka dirishani na kujirusha nje kwa uhodari wa hali ya juu (kumbuka aliwahi kuwa mwanajeshi kitengo cha Parashuti). Ofisi ya Jaji ilikuwa juu ghorofa ya Tatu katika hilo Jengo la mahakama, lakini kutokana na Spaggiari kujirusha kwa uhodari alitua chini juu ya paa la gari bila kudhurika. Kisha akakimbia kuvuka barabara na kulikuwa na piki piki inamsubiri.


Baada ya kukwea juu pikipiki akageuka kuwaangalia juu dirishani maaskari pamoja na Jaji waliokuwa wanachungulia wakiwa hawaamini kilichotokea ndani ya sekunde chache. Spaggiari akapayuka kwa nguvu "Au revoir" (kwaherini). Kisha akatabasamu kwa dharau na inasemekana akawaonesha kidole cha kati. Kisha kwa mwendo wa kasi na uhodari pikipiki ikapotea mbele ya upeo wa macho yao. Hiyo ndio ilikuwa mara ya mwisho kwa mamlaka za serikali za ufaransa kumuona Spaggiari.


Wiki mbili baadae mtu mwenye gari ambalo Spaggiari alitua alipo ruka kutoka ghorofani alipokea cheki ya thamani ya faranga 5,000 pamoja na kikaratasi kikisema ni kwaajili ya matengenezo ya paa la gari lake.

Pia kuna tetesi ambazo zimeenea mno toka kipindi hicho mpaka sasa kuwa mtu aliyempakia Spaggiari kwenye pikipiki na kumtorosha alikuwa Christian Estrosi bingwa wa Dunia wa mbio za pikipiki ambaye baadae alikuja kuwa waziri katika serikali ya Ufaransa.


Baada ya kutoroka Spaggiari alielekea nchini Argentina na kuishi huko na kufanyiwa upasuaji wa kubadilisha muonekano (plastic surgery). Inasemekana Spaggiari alikuwa anarudi mara kwa mara nchini Ufaransa kumuona mkewe Audi na Mama yake.


Akiwa nchini Argentia inasemekana kuwa alikuwa karibu sana na CIA akiwasaidia kufanikisha shughuli ambazo CIA hawakutaka kujihusisha nazo moja kwa moja kwa kuhofia jina la idara yao kuchafuka ikitokea siri kuvuja.

Mfano mzuri ni jinsi ambavyo Spaggiari (au daniel jina walilotumia CIA kumtambua (code name)) alishirikiana na Michael Townley afisa wa DINA (kitengo cha ushushushu cha nchi ya Chile) kuchora mchoro na kulipua gari la balozi wa Chile nchini Marekani.


Skandali hii ilichangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha mahusiano ya kidiplomasia kati ya marekani na Chile na hakuna aliyejua uhusika wa CIA mpaka pale mwaka 2000 ambapo CIA waliweka hadharani nyaraka kadhaa za siri baada mda wake wa usiri kupita.


Albert Spaggiari alifariki June 8, 1989 kwa kansa ya koo kutokana na matumizi ya sigara.

Fedha, Vito vya thamani, hati fungani na nyaraka nyingine za siri zilizoibwa na Albert Spagiari na Genge lake havijapatika mpaka leo hii. Tukio hili limebakia katika vichwa vya Wafaransa kama tukio kubwa pekee la wizi wa vitu vya thamani ya juu zaidi na lililotekelezwa kwa umaridadi na akili nyingi au kama Spaggiari mwenyewe alivyolielezea; "Sans armes, ni haine, ni violence" (Pasipo silaha, chuki wala ukatili").




Jiunge na Group langu la WhatsApp kusoma simulizi mpya kila siku. Kuna malipo ya 5,000/- kwa mwezi. Wasiliana nami 0759 181 457





Mwisho.



The Bold


    0 comments:

    Post a Comment

    Blog