Search This Blog

Saturday 5 November 2022

JUDITH...JUDITH - 5

 







    Simulizi : Judith....Judith

    Sehemu Ya Tano (5)









    Alikuwa akiwaza jinsi atakavyomudu kuishi katika nchi hiyo ngeni ilhali hana hata ndugu huku pia ubalozi wa Rwanda ukiwa hauna taarifa yake. Akaendelea kuwaza na kuwazua, jibu asilipate. Hatimaye akaamua kufumba macho na kuulazimisha usingizi.



    Dakika kumi baadaye alipitiwa na usingizi bila ya kujitambua, akazinduka asubuhi. Sasa akapiga moyo konde na kuamua kutoka, aukague mji huo mkubwa wa Dar es Salaam, labda huenda akapiga hatua moja nzuri katika kuhangaika huko.



    Na sasa hakutaka kumshirikisha mtu yeyote hususan yule Swaumu ambaye jana walikubaliana kuwa leo watakwenda wote kwenye maduka ya kubadilisha pesa. Hata huyu mhudumu wa mapokezi naye hakupaswa kujua ni kipi kinachoendelea.



    Hivyo, mara tu baada ya kuoga, alivaa nguo nyingine kisha akaondoka kimya-kimya, machoni mwa wapita njia wenzake akionekana kuwa ni mwanamke wa kuvutia. Ndani ya pochi ambayo nayo aliinunua jana kule sokoni, kulikuwa na pesa kidogo za Tanzania, shilingi 9,000 zikiwa ni masalia ya zile 30,000/- alizoachiwa jana na Baraki.



    Alitembea huku akiwafuata watu wengine walioonekana kuwa na haraka, wengi wao wakiwa wamevalia kinadhifu, hali iliyompa hisia kuwa huenda walikuwa wakielekea kule ambako watu hupaita ‘mjini.’ Na wengi kati ya watu hao walikuwa ni wanawake. Akaendelea kuwafuata.



    Alikumbuka kuwa jana, wakati akiwa na Swaumu wakienda sokoni, aliyaona mabasi madogo ya abiria yenye maandishi ubavuni: CITY BUS. Alitaka ayatumie magari hayo kumfikisha huko panapoitwa ‘mjini.’ Akaendelea kuwafuata hao watu wengi ambao baadhi yao walikuwa na mabegi madogo mikononi.



    Robo saa baada ya kuianza safari hiyo, akajikuta akitokea Barabara ya Rashid Kawawa. Akaivuka na kushika Barabara ya Chemchemi. Hatimaye alijikuta akiibukia katika kituo cha daladala cha Magomeni Mapipa ambako alikuta idadi kubwa ya watu wanaosubiri usafiri.



    Daladala zilikuja, daladala zikaondoka. Yeye hakukurupuka kupanda. Hakujua ni wapi alikopaswa kwenda na pia hakuwa na haraka. Akaendelea kuwatazama abiria wakikimbilia kila daladala iliyoingia. Kuna zilizokwenda Posta, nyingine Kariakoo, Muhimbili na hata Kivukoni.



    Hatimaye aliamua kupanda daladala lililokwenda Posta, bila ya kupajua huko Posta na kama atafanikiwa kutimiza malengo yake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Aliteremkia Posta Mpya. Akavuka barabara bila ya kumuuliza mtu yeyote, jambo lolote. Moyoni mwake alipanga kutafuta duka la kubadilisha pesa, lakini aliamua kuwa makini kwa kuwa alijua fika kuwa thamani ya pesa alizonazo ni kubwa hivyo kama watu wengine wangefahamu huenda ingekuwa hatari kwa upande wake. Kuna vibaka, matapeli na majambazi. Yeyote kati ya hao anaweza kumfanyia unyama kwa kujitwalia pesa hizo kwa njia moja au nyingine.



    Akaifuata Barabara ya Jamhuri, akitembea kwa kujiamini kama vile ni mwenyeji wa eneo hilo . Huko mbele akajikuta akikumbana na Mtaa wa Zanaki. Hapo akasita. Sasa akajiwa na wazo la kuachana na Mtaa wa Jamhuri.



    Akapinda kushoto na kufuata Mtaa wa Zanaki. Hakufika mbali, mara akaliona duka lenye bango kubwa ukutani: SAKA BUREAU DE CHANGE. Akasimama na kulitazama kwa sekunde chache kisha akalifuata. Dakika ishirini baadaye alikuwa akitoka ndani ya duka hilo huku akiwa na pesa za Tanzania, shilingi 2,000,000 na ushei. Akasimama kando ya barabara akiwa hajui ni wapi alikopaswa kwenda na kipi alichopaswa kufanya.



    Akatulia kando ya barabara hiyo, nje ya duka hilo huku akiwa ameduwaa. Dakika mbili baadaye akapata uamuzi wa kukodi teksi. Japo alikuwa mgeni, lakini hakuwa mtu wa kushindwa kuzitambua teksi za jijini Dar, ambazo zilikuwa na utambulisho rasmi. Akaipungia mkono teksi ambayo ilimtii.



    “Magomeni,” alimwambia dereva teksi akiwa ameshaingia garini.



    “Magomeni ipi?”



    Lilikuwa ni swali ambalo Judith hakulitarajia. Hakuijua vizuri Magomeni na vitongoji vyake. Amwambie ni Magomeni ipi? Hata hivyo hakutaka kuudhihirisha ugeni wake kwa huyu dereva. Akamjibu, “Nitakuelekeza mbele ya safari.”



    Walipofika jirani na Bondeni Hotel, Judith akakikumbuka kile kituo cha daladala alichopandia wakati anakuja Posta. Akamwambia dereva akate kulia. Dereva akatii. Walipofika jirani na kituo hicho, akamwamuru asimame.



    “Ni kiasi gani?”



    “Elfu kumi.”



    Dakika iliyofuata Judith alikuwa ameshaachana na teksi hiyo. Akatembea taratibu akiifuata barabara ileile aliyoitumia asubuhi kuja hapo kituoni. Ni wakati huo ndipo alipoihisi njaa, na akakumbuka kuwa tangu asubuhi alikuwa hajatia kitu tumboni.



    Akaangaza hapa na pale na kuona baa moja nyuma ya kituo cha daladala. Watu walikuwa wengi katika eneo hilo, baadhi wakinywa soda, baadhi wakinywa supu na wengine wakinywa bia.



    Alikwenda na kuagiza supu, chapati mbili na soda. Wakati akisubiri huduma hiyo, mara akamwona mtu mwingine akija katika meza hiyo. Alikuwa ni mwanamume, kijana mwenye umri kati ya miaka ishirini na mitano na thelathini na mitano. Kijana huyo alipofika alimtazama Judith huku akiachia tabasamu la mbali na kisha akasema, “Samahani, sista, naweza kuketi hapa au mwenyewe katoka?”



    Judith akaunyanyua uso na kumtazama mtu huyo. Akavutiwa na utanashati wake; shati jeupe la mikono mirefu, suruali nyeusi na viatu vyeusi vilivyonakshiwa vizuri. Macho ya kijana huyo yalikuwa kitu kingine kilichomvutia kiasi cha kuhisi mshtuko kila walipotazamana.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Au kuna mtu, sista?” kijana huyo alirudia kumuuliza huku akimtazama kwa makini zaidi, tabasamu likizidi kuchanua.



    “Keti tu,” Judith alijibu. “Sidhani kama kuna mtu aliyekuwa hapa. Mie nimekuta meza nyeupe.”



    Dakika chache baadaye mtu huyo alikuwa akinywa soda huku Judith akifakamia supu.



    “Samahani, anti, tunaweza kufahamiana zaidi?” kijana huyo aliamua kuuvunja ukimya uliokuwa umeitawala meza hiyo.



    Judith alimtazama kidogo kisha akayarejesha macho kwenye bakuli la supu. Akachota mchuzi kwa kijiko na kunywa. Akafanya hivyo mara mbili zaidi, kisha akaachia tabasamu la mbali. “Inategemeana ni kufahamiana ki-vipi,” hatimaye alisema.



    Kijana yule alilikuza tabasamu lake na kusema, “Ni kwa utaratibu wa kawaida tu.”



    “Sijakuelewa,” Judith alisema, safari hii akiunyanyua uso na kumtazama kijana huyo kwa makini, paji la uso wake likiunda mikunjo ya mbali.









    “Yaani kwa mfano,” mtu huyo alisema, “Mimi naitwa Edson. Ni jina langu halisi. Ni mzaliwa wa Kigoma. Nadhani mpaka hapo inatosha. Sijui wewe. Au nitakuwa nimegeuka Ofisa Uhamiaji au askari polisi?”



    Kicheko cha mbali kilimtoka Judith. Akamtazama tena Edson na kuyasoma macho yake, akitaka kuthibitisha kama kuna uwiano wowote kati ya macho hayo na maneno yake. Akakumbana na macho yaliyong’ara sanjari na tabasamu dhaifu lililolandana na utazamaji wake.



    Sasa Judith akajiona ameondokana na upweke. Japo huyu mtu alikuwa mgeni kabisa machoni pake, tofauti na Baraki aliyemwokoa kutoka Rwanda, hata hivyo alijiona kuwa kampata mkombozi halisi.



    “Naitwa Judith,” hatimaye alisema. Hakuendelea kutoa utambulisho zaidi, alijiuliza kama ilikuwa sahihi kutoboa undani wa asili yake. Jibu lililomjia akilini ni HAPANA.



    Alitambua fika kuwa uraia wa mtu ni jambo linalotiliwa umuhimu katika mataifa mengi duniani. Siyo kwamba raia au mzaliwa wa nchi moja haruhusiwi kuishi nchi nyingine, la hasha. Anaweza kuishi, lakini kwa utaratibu unaokubalika kisheria. Raia wa nchi nyingine, kama yeye Judith, anaruhusiwa kuishi Tanzania ama nchi nyingine yoyote endapo tu atakuwa amefuata kanuni husika ambazo zinatambulika kitaifa na kimataifa.



    Kwa hali hiyo, yeye alipaswa kuwa hapo Dar es Salaam huku Idara ya Uhamiaji ikiwa na taarifa yake. Isingewezekana amtamkie bayana huyu mtu kuwa yeye ni mzaliwa wa taifa la Rwanda . Hilo halikumwingia akilini wakati huo. Akaendelea kufikiria jinsi atakavyojieleza kama ataulizwa swali jingine hususan kuhusu uraia wake.



    “Ni jina zuri,” Edson alimkatisha mawazo yake. Akatamka tena kwa sauti ya chini, “Judith…Judith, jina zuri kama ulivyo.”



    Tabasamu jingine likamtoka Judith. Akaunyanyua uso na kumtazama kidogo Edson kisha akayaepuka macho na kuyarejesha mezani. Kwa sauti yenye taswira ya aibu, akasema, “Asante.”



    “Unaishi maeneo hayahaya ya Magomeni?” Edson alirusha tena swali.



    “Ndiyo.”



    “I see. Ni mpweke kama mimi au…?”



    Judith akamtazama tena, safari hii kwa chati sana . Akakohoa kidogo na kunywa tena soda yake, kama vile hajalisikia swali hilo .



    “Eti Judi,” Edson alimbana. “Umeolewa?”



    “Kwa nini unauliza ivo?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Edson alicheka kidogo kisha akasema, “Wengine ni waoga wa kupigwa risasi au kuchomwa visu na wenye mali.”



    Judith naye akacheka.



    Wakatazamana, macho ya kila mmoja yakiwa na kitu fulani kilichozungumza neno moja tu: MAPENZI. Judith akabibitua midomo na kuendelea kunywa supu yake. Kwa mara nyingine ukimya ukapita katika eneo hilo.



    Wakatazamana tena, safari hii Judith akaachia tabasamu la kirafiki,

    zaidi ya urafiki wa kawaida.



    “Judith,” Edson alimwita kwa sauti ya chini.



    Judith hakuitika kwa sauti, alimtazama kidogo Edson kisha akauinamisha tena uso.



    “Judith,” Edson aliita tena na safari hii alionekana kutojali kuitikiwa. Akaendelea, “Samahani kwa hili nililokuuliza kama nitakuwa nimefanya kosa.”



    “Hapana, hujafanya kosa,” Judith alijibu huku akiyaepuka macho ya Edson.



    “Asante. Kwa hiyo?”



    “Sijaolewa,” jibu la Judith lilikuwa fupi.



    Lilikuwa ni jibu lililomtia ujasiri Edson. Sasa akapata nguvu ya kuendelea kuzungumza.







    **********



    EDSON alikuwa akifanya kazi Wizara ya Viwanda na Biashara. Tangu ahitimu masomo na kuanza rasmi ajira, ilishatimu miaka miwili, na kituo chake cha kwanza katika ajira hiyo kilikuwa jijini Dar es Salaam , makao makuu ya wizara hiyo.



    Tangu alipobalehe Edson hakuwa mpenzi wa wanawake. Kwa ujumla hakulipa kipaumbele suala la kuwa na uhusiano wa mapenzi na wanawake. Lakini siyo kwamba aliishi vivihivi, la hasha. Kabla hajahitimu darasa la saba alidiriki kufanya mapenzi na mwanamke mmoja katika mazingira ambayo hata yeye hakuyatarajia. Baada ya siku hiyo, ilipita miaka takriban mitatu hadi alipodiriki kufanya tena tendo hilo na wasichana wawili kwa nyakati tofauti wakati akiwa kidato cha nne.



    Ndiyo, ngono ilikuwa ni burudani kwake lakini hakuichukulia kama sheria badala ya kawaida katika utekelezaji. Sasa alikuwa na miaka mitatu akiwa hajafanya tendo hilo kiuhalisia, zaidi aliziweka hisia zake kwa mmoja wa wale wasichana aliowahi kufanya nao tendo hilo, akiweweseka bafuni au popote alipopaona panastahili kwa faragha, sabuni ikiwa ndiyo nyenzo madhubuti katika kumtatulia matatizo yake faraghani.



    Tangu alipoanza kazi hapo Wizara ya Viwanda na Biashara alikumbana na vishawishi vingi kutoka kwa wanawake warembo, lakini alikuwa makini, maradhi ya Ukimwi yakiwa ni tishio kubwa kwake. Nasaha zilizotolewa katika vyombo mbalimbali vya habari sanjari na kuwakumbuka baadhi ya watu aliowajua, ambao waliumwa na hatimaye kufariki akiwaona, ilikuwa ni taswira halisi ya kumfanya afikiri mara mbili-mbili kabla ya kuchukua hatua ya kumchojolea nguo mwanamke yeyote.



    Ndiyo, alikuwa makini, lakini pia alitambua kuwa alipaswa kuoa. Ataishi peke yake hadi lini? Ni kwa wazo hilo la kumpata mwenzi ndipo alipoamua kutulia, akimwomba Mungu ampatie huyo atakayestahili kuwa mkewe.



    Asubuhi hii akiwa na Judith kando yake, alihisi kuwa Mungu kampatia mchumba. Alimwona Judith kama mwanamke wa kipekee, ambaye hajapata kumwona tangu azaliwe.



    Japo Judith hakutofautiana na wafanyakazi wenzake ambao hawajaolewa na ambao pia walionyesha dhahiri kumhitaji, wakiwa wazuri kwa sura na maumbile yao , hata hivyo akilini mwa Edson hawakustahili kuwa katika himaya yake. Japo mtaani alipoishi aliwaona mabinti kadhaa ambao ilikuwa ni kiasi tu cha kuwaambia wazazi wao, “nataka kumuoa mwanenu…” wakakubali haraka, au yeye mwenyewe kumvaa moja kwa moja binti na kumtamkia, bado hakuwa tayari kufanya hivyo.



    Alihitaji kuoa, lakini alihitaji kumuoa yule atakayempenda kutoka moyoni. Hakuhitaji kuijua historia ya huyo mke mtarajiwa, jambo hilo aliamini kuwa lingemfanya asite kuchagua yule amfaaye. Huyu Judith alimvutia kwa sura na umbo lake. Kwake, hizo zilikuwa ni sifa tosha. Hakupenda kuijua historia yake. Isitoshe, moyo wake ulimkubali. Nini zaidi?



    Kwa hali hiyo, pale alipomuuliza Judith kama ameolewa, naye akamjibu, “Sijaolewa,” kwake lilikuwa ni jibu lililomtia faraja kubwa. Na ndipo alipoamua kufungua ukurasa mpya. Akajieleza, akajieleza, akituma rasmi ombi la kuwa karibu zaidi kiuhusiano.



    **********http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    MJINI KIGALI



    SIKU ya pili baada ya Makella kukimbiwa na Judith hakutoka nyumbani. Alijihisi kuchanganyikiwa. Hakuwa timamu. Kila alipofikiria kufanya hiki, akajikuta akiona kuwa haifai kufanya.

    Tangu alipoingia chumbani mwake jana hadi saa 4 asubuhi hii hakuwa ametoka, alijikuta akimchukia kila mtu na hata kujichukia mwenyewe.



    Alijilaza kitandani huku akisonya kila wakati na tayari alikuwa amekwishavuta sigara tano kwa hasira. Akijihisi kuwa timamu kidogo kila alipovuta. Akafungua kabati na kutoa chupa kubwa ya whisky, akaifungua na kunywa funda kadhaa kisha akarudisha kabatini.



    Akajiwa na wazo la kutoka ili akazimalizie hasira zake kwa Jamillah, mwanamke ambaye alikuwa na uhusiano naye wa kimapenzi ilhali akitambua fika kuwa ni mke wa askari mwenzake.



    Akaiacha bunduki ndani na kutoka. Hapakuwa mbali hapo kwa Jamillah. Ni nyumba ya nne tu kutoka hapo alipoishi Makella. Na Makella alikwenda kwa kujiamini kwa kuwa alitambua kuwa Ramadhani ambaye ndiye mume wa Jamillah bado alikuwa hospitali alikolazwa kwa maradhi ya homa.



    Pombe zikichangia kumpa ujasiri, Makella alitembea kwa kujiamini na kuufikia mlango wa nyumba hiyo. Taa zilikuwa zikiwaka. Akagonga mara mbili. Muda mfupi baadaye mlango ukafunguliwa. Jamillah alikuwa mbele yake!





    Wakatazamana, Jamillah akiwa anaonekana kutokuwa na furaha lakini Makella akashindwa kuitambua hali hiyo. Akaingia ndani kama kwake. Akarudisha mlango na kumvuta Jamillah kisha akamkumbatia kwa nguvu.



    Jamillah akajitahidi kujing’atua bila ya kutamka chochote. Makella akaendelea kumng’ang’ania na kumbusu shavuni. Hakutambua kuwa kutoka chumbani, masikio ya Ramadhani ambaye siku hiyo daktari alikuwa amemruhusu kurudi nyumbani yalinasa purukushani hiyo.









    Taratibu Ramadhani alitoka kitandani na kuchungulia. Akamwona Makella akimkumbatia Jamillah. Hasira zikampanda kwa kiwango kisichokadirika. Akakumbuka tetesi alizowahi kuzisikia kuwa Makella alikuwa na uhusiano wa mapenzi na Jamillah. Hasira zikampanda. Akageuka na kurudi kwenye kabati ambako alifungua saraka moja na kutoa bastola. Papohapo akatokeza sebuleni na kufoka, “Makella…Makella….kumbe ndiyo tabia yako!”



    Makella akashtuka na kumwachia Jamillah. Akageuka na kukutana uso kwa uso na Ramadhani aliyekuwa amemlenga kwa bastola. Makella akaduwaa. Akatamani kutamka neno asiweze.

    Akayashuhudia macho ya Ramadhani yakimtazama bila ya kupepesa na yakitangaza jambo moja tu; NITAKUUA.



    Mara Makella akahisi kitu kikipenya kifuani, kikamzulia joto kali kisha maumivu yakaanza kumwingia kwa mbali. Nguvu zikaanza kumomonyoka maungoni, Uwezo wa macho kuona ukawa ukimkimbia kwa kasi ya kutisha. Miguu ikashindwa kuubeba mwili. Akamwona Ramadhani akigeuka na kurudi chumbani na bastola yake.



    Cha mwisho alichoambulia ni yowe kali la Jamillah na alipoanguka sakafuni hata maumivu hakuyasikia!





    **********



    MSHTUKO alioupata Judith pindi alipokutanisha macho na Edson haukuwa wa kawaida. Na alikumbuka mara ya mwisho alipoupata mshtuko wa aina hiyo ni siku alipokumbana na Zalidi, kijana ambaye alitokea kumvutia kwa kiasi kikubwa. Zalidi naye alikuwa Mtutsi na waliishi wote mjini Kigali, Rwanda lakini wakiwa mbalimbali kwa makazi.



    Zalidi aliporusha ndoano, Judith alikosa uwezo wa kuikwepa. Akanaswa. Wakawa wapenzi. Lakini kabla hawajafikia ile hatua ambayo Zalidi aliihitaji sana, hatua ya kustarehe kimwili, mauaji yalitokea mtaani alikoishi Zalidi. Wazazi wake Zalidi pamoja na Zalidi mwenyewe, waliuawa kikatili na askari wa Kihutu.



    Tangu hapo Judith hakujua kupenda wala kutamani hadi siku hii alipopata tena mshtuko huu, mshtuko ulioifanya akili yake ivurugike kiasi cha kujikuta akiwa mwepesi wa kujibu kuwa hajaolewa. Na ndipo maongezi kati yao yaliponoga, Edson akiwa kinara.



    Waliachana baada ya saa tatu, maongezi baina yao yakiwa yamewaweka karibu zaidi.



    Sasa Judith alijikuta akifungua ukurasa mpya. Akatamani kila wakati awe na Edson. Hata aliporudi kule gesti, mawazo yake yote yalikuwa kwa Edson. Alikuwa na hamu wawe pamoja, wakumbatiane na hatimaye kufanya kila kitu ambacho mioyo yao ingewashawishi. Kwa ujumla alimpenda na kumhitaji Edson kwa kiwango kikubwa. Ndipo akajiwa na wazo la kumtoroka Baraki, mfadhili wake tangu Rwanda.



    Alitambua fika kuwa, haitakuwa busara kumtoroka Baraki, lakini afanye nini? Huyo Baraki mwenyewe ana mke. Vipi amtegemee mtu wa aina hiyo katika maisha yake? Na pia, kiwango cha pesa alizokuwa nazo kilikuwa kichocheo kingine katika kumfanya amtoroke Baraki.



    Si tu kwamba kwa kuwa amekutana na Edson na kuvutiwa naye ndiyo maana akaamua kumkimbia Baraki. La hasha. Alijua kuwa mapenzi ya Baraki hayatadumu, ni mapenzi ya muda tu, mapenzi ambayo siku yatakapoyeyuka ndipo atakapojikuta katika dunia mpya, katika maisha mapya.



    Hivyo, hakutaka kupoteza muda. Jambo la kwanza aliloamua kulifanya ni kuondoka katika gesti hiyo. Ndiyo, aondoke na kwenda kuishi popote. Kama ni suala la pesa, hilo halikuwa tatizo. Pesa anazo, tena za kuweza kumlinda kwa siku nyingi. Ni kipi kitakachoharibika? Hakuna.



    Alipofika gesti tu, alitwaa kila kilicho chake na kuondoka huku akimwambia yule mhudumu kuwa Baraki amemwagiza wakutane mtaa wa pili kwenye baa moja anakopata bia.



    “Ndiyo uondoke na mizigo?” mhudumu alimhoji kwa mshangao.



    “Ameniagiza kuwa niende nayo,” Judith alijibu kisha akaongeza, “Kwani kuna tatizo gani? Anadaiwa?”



    “Hapana, nauliza tu shemeji yangu.”



    Ni hapo mtoto wa kike, msichana mrembo, msichana wa Kitutsi, Judith Ndayishimiye alipotokomea kisayansi. Usiku wa siku hiyo ukawa ni yeye na Edson, Edson na yeye. Siku mbili baadaye walikutana tena, hatimaye ikawa haipiti siku bila ya kuonana. Uhusiano wao ukazaa uchumba kamili. Na ni katika muungano huo ndipo Judith alipoamua kumtobolea ukweli kuhusu historia ya maisha yake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Ilikuwa ni hadithi iliyomsononesha sana Edson. Na akaahidi kuitunza siri hiyo.



    “Usihofu, Judith,” alimwambia. “Lakini nakuahidi kuwa hutapata shida yoyote. Cha muhimu, ni wewe kujitahidi kutomropokea mtu yeyote kuhusu mkasa huo. Pole sana, mpenzi. Hayo ni mapito tu. Huenda Mungu alipanga wewe usiuawe na uje kuishi huku Tanzania. Uje kumwondolea upweke Edson.”



    Mwaka mmoja baadaye, ndoa kati ya Judith na Edson ilifanyika. Sherehe kubwa ikafuata. Watu wakala, watu wakanywa na kusaza.







    **********







    SIKU moja, ikiwa ni miaka mitatu baada ya Edson na Judith kufunga ndoa, Judith alikuwa eneo la Kariakoo na mwanaye, Jerome ambaye wakati huo alikuwa na umri wa mwaka mmoja na nusu. Alikwenda huko kutafuta nguo zake na za mwanaye kwa ajili ya sikukuu ya Krismasi. Alipita mtaa huu na ule, akiingia duka hili na lile, akiangalia nguo hii na ile.



    Hatimaye, katika pitapita yake hiyo, aliingia katika duka moja Mtaa wa Kongo. Duka hilo lilisheheni watu. Humo alitulia akiangalia kwa makini nguo nyingi zilizokuwa katika mauzo. Kulikuwa na wahudumu wawili ambao waliwasikiliza wateja huku mmiliki wa duka, mzee wa Kihindi akiwa ameketi kitini, meza iliyosheheni makabrasha ikiwa mbele yake.



    Judith alijisogezasogeza hadi mbele na kumgusa mhudumu mmoja huku akimwambia, “Kaka, nipatie ile blauzi nyekundu.”



    Yule mhudumu alimtazama kidogo Judith kisha akageukia kwenye rundo la nguo zilizotundikwa mbele ya wateja. Akaisogelea blauzi moja na kuigusa huku akimuuliza, “Hii hapa?”



    “Hiyohiyo. Ni bei gani?”



    Mhudumu hakujibu, aliitoa blauzi hiyo na kumletea Judith huku akisema, “Itazame kwanza, dada.”



    Ni wakati mhudumu huyo akimpatia blauzi hiyo ndipo macho yao yalipogongana. Mhudumu yule alishtuka kidogo na kumkodolea macho zaidi Judith. Judith naye akamtazama kwa mshangao huku akiipokea blauzi.



    “Ni bei gani?” Judith aliuliza tena.



    “Shilingi elfu kumi tu.”



    Judith alilipa na kuamua kuondoka. Tazama ya mhudumu huyo ilimshangaza, na zaidi, ilimkera. Akaamua kwenda duka jingine. Ilikuwa ni wakati amevuka maduka mengine mawili tu mara akasikia akiguswa bega. Akageuka na kukutana na yule mhudumu wa duka la kwanza.



    “Samahani dada, sijui kama nimekufananisha au sijakufananisha,” kijana yule alisema kwa sauti ya upole. Kisha akaongeza, “Naomba kukuuliza.”



    Judith alisimama na kumtazama kwa makini kijana huyo ambaye macho yake yalionyesha ujasiri uliofichika moyoni. “Unasemaje?” hatimaye alimuuliza.



    “Naitwa Rwagasore. Je, wewe ni Judith mtoto wa marehemu mzee Ndayishimiye?”



    Moyo wa Judith ulipiga paa! Katika nchi hii ya Tanzania, yeye akiwa ni mgeni, hakutarajia kuwa kuna mtu ambaye angeweza kumfahamu. Akashusha pumzi ndefu na kumkodolea macho zaidi kijana huyo. Kisha, badala ya kujibu, naye akauliza, “ Kwani vipi?”



    “Sina nia mbaya, dadangu. Nauliza tu.”



    “Na kama ndiye au siye wewe unataka nini?”



    “Basi, dada kama nimekuudhi niwie radhi,” Rwagasore alisema huku akionyesha kuanza kuondoka.



    “Subiri,” Judith alimzuia kwa kumshika mkono.



    Rwagasore akatii.



    “Mimi ndiye Judith, mtoto wa marehemu mzee Ndayishimiye, enhe, unasemaje?” Judith aliamua kutoboa ukweli huo akiwa ameamua kuwa liwalo na liwe.



    “Ni kweli dada?” kijana yule alionekana kutomwamini Judith.



    “Ni kweli! Enhe, kwani vipi? Unasemaje?”



    “Pole sana, dada,” Rwagasore alisema kwa unyonge huku akimtazama kutoka juu hadi chini. “Pole kwa matatizo yaliyokukuta. Mimi nilikuwa mtoto wa mzee Nsanze, nyumba ya tatu toka kwenu. Hata mimi wazazi wangu waliuawa. Mimi nilijificha kwenye migomba nje ya nyumba, ndiyo maana nilinusurika. Lakini nilisikia kuwa wewe ulitekwa na Makella. Habari hizo zilienea sana baada ya vurugu ile. Tukasikia kuwa Makella alipania kukuoa kwa nguvu. Baadaye tukasikia kuwa ulimtoroka. Ni kweli dada?”



    Judith hakujibu, akaendelea kumtazama Rwagasore kwa namna ya kumpa nafasi ya kuendelea kuongea.



    “Tukasikia kuwa Makella alikuwa akikusaka, na alidai kuwa akikupata lazima akuue, eti ulimwibia pesa zake!” Rwagasore aliendelea. “Lakini Mungu mkubwa, dada Judith. Siku chache tu baada ya wewe kupotea, Makella alifumwa kwa mke wa askari mwenzake. Akauawa kwa kupigwa risasi kifuani!”



    “Nini? Makella kauawa?!” Judith alibwata huku macho kayatoa pima.



    “Ndiyo dada! Alikufa kifo kibaya sana! Baada ya kupigwa risasi, yule askari mwenye mke alimkata sehemu za siri na kumchinja shingo, kichwa kule kiwiliwili kule! Akamtumbua tumbo lote, maini, utumbo na kila kitu nje! Nakwambia, Makella alibaki ni maiti isiyotazamwa mara mbili!”



    Judith alitwaa leso ndani ya mkoba na kufuta jasho usoni. Kisha akainua mikono juu na kusema, “Ee, Mungu, ushukuriwe. Nikulipe nini Mungu wangu?”



    Mara akahisi machozi yakimlengalenga. Hakujua kama yalikuwa machozi ya furaha au majonzi. Taarifa hii njema ya kifo cha Makella ilizirejesha kumbukumbu kichwani mwake, kumbukumbu ya siku baba, mama na wadogo zake watatu walipouawa mbele yake na kundi la watu watatu wenye silaha, Makella akiwa miongoni mwao.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa kutumia leso ileile aliyafuta machozi hayo kisha akamshika mkono Rwagasore na kusema, “Asante kaka’ngu kwa taarifa hiyo.” Akafungua pochi na kuchomoa noti moja ya shilingi 10,000. Akampatia.



    Kisha akaondoka huku akimtupia tabasamu hafifu, moyoni akijisikia kujawa na faraja ya aina yake. Kwa sauti ya chini sana ambayo haikuweza kuyafikia masikio ya mtu mwingine, alitamka, “Mungu uhimidiwe! Jina lako litukuzwe!”



    MWISHO


0 comments:

Post a Comment

Blog