Simulizi : Judith....Judith
Sehemu Ya Nne (4)
KICHWA cha Judith kilikuwa kizito. Aliuhisi uzito huo kutokana na mambo yaliyoisumbua akili yake. Kumbukumbu ya mauaji yaliyotokea usiku huo, saa chache zilizopita zilimganda akilini. Hakujisikia kuwa yu binadamu wa kawaida, wala hakuwa na hamu ya kuendelea kuishi. Kuuawa kwa wazazi wake na wadogo zake kulimwathiri kisaikolojia kwa kiwango kisichokadirika.
Isitoshe, ni muda mfupi tu uliopita alipomtoroka Makella huku akiwa amemwibia dola 2,000 za Marekani, tendo aliloamini kuwa lingeweza kumletea matatizo zaidi, hata kuyahatarisha maisha yake.
Kwa hali hiyo, alihitaji usalama, na usalama huo uwe wa uhakika. Hapo alipo, bado hakujiona kuwa yu katika sehemu nzuri kwa usalama wake. Lakini afanye nini? Hakuwa na la kufanya. Akalazimika kusubiri muda ambao Baraki ataamua waondoke huku kimoyomoyo akiomba Mungu, Makella asitokee.
Alikunywa bia huku akiilazimisha nafsi yake kutii utomasaji wa Baraki katika chuchu za matiti yake na wakati mwingine mkono ukivuka hadi mapajani ambako ulitulia na kuyapapasa-papasa.
Japo eneo waliloketi halikuwa na mwanga, hata hivyo halikuwa likistahili kuchukuliwa kuwa ni maficho kamili, eneo ambalo mtu yeyote mwingine ambaye angefika hapo angeshindwa kuwaona. Kwa vyovyote vile, mtu ambaye angelisogelea eneo hilo kwa umbali wa hatua tano kutoka kwenye meza hiyo, kama anamfahamu Judith, angeweza kumtambua. Ni taswira hiyo ambayo Judith hakuipenda, na hakuipenda kwa kuwa alihofia kukutwa hapo na Makella.
Mara Baraki aliacha kumpapasa. Akaitazama saa yake na kusema, “Nadhani huu ni muda mwafaka. Saa nne! Twende na bia zetu garini, na nyingine ziko hukohuko. Sidhani kama tutazimaliza.”
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Yalikuwa ni maneno ambayo Judith aliyahitaji, zaidi ya hizo bia au jambo jingine lolote. Hakuhitaji bia, alihitaji kuwa mbali na Makella. Hakumhitaji Baraki, alihitaji kuwa mbali na Makella! Aliyahitaji maficho!
Kwa furaha ambayo ilifurika moyoni na kufanikiwa kutoiweka hadharani, aliitwaa chupa na kuipeleka kinywani. Safari hii hakunywa, alimimina! Alipoitua chupa hiyo mezani, ilikuwa tupu. Sasa akamtazama Baraki kwa namna nyingine kabisa, macho yake yakitoa shukrani za dhati.
Baraki akiwa hayajui yaliyomo moyoni mwa Judith, alivutiwa na macho hayo, akamvuta na kumbusu shavuni. Hakuishia hapo, akajaribu kupenyeza ulimi kinywani mwa Judith, jaribio ambalo safari hii Judith hakulizuia, akafuata ule usemi wa ‘mtaka cha uvunguni.’ Wakakutanisha midomo yao na kudumu katika busu hilo kwa sekunde kadhaa, Baraki akipata burudani halisi ilhali Judith akiwa katika starehe bandia.
Dakika tano baadaye walikuwa wameshaagana na wahusika wakuu wa mpaka wa Rwanda na Tanzania. Lori aina ya Fuso lilikuwa barabarani, ndani ya ardhi ya Tanzania, Baraki akiwa nyuma ya usukani, kando yake kaketi Judith na kushoto, alikuwa ni msaidizi wake, Livingstone.
Kama kuna jambo ambalo Judith alilihitaji, na likiwa ni jambo ambalo lingemfariji kwa kiasi kikubwa, ni hilo la kuvuka mpaka na kuingia Tanzania.
“Mungu anipe nini?” alinong’ona kwa sauti ambayo haikuyafikia hata masikio yake mwenyewe.
Akiwa na ujasiri uliosababishwa na bia alizokunywa sanjari na bangi aliyovuta, Baraki alitumbua macho barabarani huku mwendo wa gari ukiwa mkali. Na kila alipohisi usingizi unamnyemelea, aliegesha gari pembezoni mwa barabara, akateremka na kwenda nyuma ya gari ambako aliwasha msokoto wake na kuvuta kidogo. Kisha alirudi garini na kukanyaga tena mafuta.
**********
MAKELLA aliteremka ndani ya teksi, dakika ishirini tu baada ya kuikodi. Kimoyomoyo Makella alimsifu dereva huyo kwa umahiri wake. Akalisogelea eneo hilo la mpakani kwa hadhari kubwa. Lilikuwa ni eneo lililochangamka kwa kiasi kikubwa. Baa mbili maarufu zilikuwa zimefurika watu. Magari manne makubwa ya mizigo yalikuwa kando ya baa hizo.
Makella hakujiunga na wateja hao. Alimfuata askari mmoja aliyekuwa akizunguka-zunguka hapa na pale. Akamsalimu na kumuuliza kama ameiona teksi yoyote katika eneo hilo.
“Teksi?” askari yule aliuliza huku akionyesha mshangao wa mbali.
“Ndiyo.”
“Saa ngapi?”
Makella alifikiri kidogo kisha akajibu, “Siyo zaidi ya nusu saa iliyopita.”
Ukimya mfupi ukapita. Kisha yule askari akasema, “Yeah. Nadhani nimeiona. Ilipaki hapo,” akaonyesha kwa kidole. Kisha akaongeza, “Haikukaa sana . Ilimleta mtu na kugeuza.”
Makella akashtuka. “Ulimwona mtu mwenyewe?”
“ Kama sikosei, alikuwa ni mwanamke.”
Haraka Makella akaingia katikati ya mkusanyiko wa watu katika baa mojawapo. Humo alihaha akiangaza macho huku na kule, kwa huyu na yule hadi akakata tamaa. Mlengwa wake hakuwemo. Akaivaa baa ya pili ambako pia alifanya zoezi kama la awali.
Patupu!
Akazidi kuchanganyikiwa. Akaamua kumrudia yule askari.
“Vipi, umemwona?” askari yule alimuuliza huku akimtazama kwa mshangao.
Makella akakataa kwa kutikisa kichwa. Kisha naye akarusha swali, “Unaweza kukumbuka yule mwanamke alikuwa amevaaje?”
Yule askari wa baa aliguna kidogo, kisha akasema, “Sikujali kuhusu kuvaa kwake. Lakini alikuwa ni mrefu. Ni Mtutsi. Vipi, kuna tatizo?”
Makella alikunja uso na kuonyesha kufikiri. Kisha, badala ya kujibu kwa mara nyingine akaibuka na swali: “Una hakika kuwa umewaona wateja wote walioingia?”
“Ndiyo!” askari alisisitiza.
“Na waliotoka?”
“Nimewaona!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sasa huyo mtu atakuwa wapi, maana’ake humo ndani ya baa zote mbili hayumo!”
Askari alishangaa. “Umeangalia vizuri?”
“Hadi vyooni!”
Askari yule aliguna na kuonekana akifikiri jambo. Kisha ghafla akaonekana kukumbuka kitu. Akasema, “Lakini kuna watu kama wawili, watatu hivi wameondoka muda si mrefu kwa Fuso. Mmoja wao alikuwa ni mwanamke.”
“Aaah!” Makella alitamka kwa namna ya kukata tamaa. Kisha akauliza, “Wamekwenda wapi?”
“Lile gari ni la Watanzania. Huwa linakuja huku mara kwa mara. Na hufanya safari zake usiku tu. Kwa vyovyote vile leo walikuwa wakirudi Tanzania .”
“Wana muda gani tangu wameondoka?!” sauti ya Makella ilijaa kitetemeshi cha hasira.
“ Kama nusu saa hivi.”
Makella alitikisa kichwa kwa masikitiko. Kisha ghafla akasema, “Mambo yanazidi kuwa magumu…” akasita na kuondoka kwa hatua ndefu akizifuata ofisi za mpakani. Jibu alilolipata huko likazidi kumchanganya.
“Wamepita hapa muda mrefu kidogo,” mhusika mkuu alimwambia.
“Unaweza kukumbuka yule mwanamke alikuwaje?”
“Ki-vipi?”
“Yaani kimavazi na mwonekano wake kwa jumla.”
“Kwani kuna tatizo gani?” mkuu yule alimbana Makella.
Ilimbidi Makella abuni uongo wa haraka alioamini kuwa ungemsaidia. “Ni mhusika katika tukio la utunguaji wa ndege iliyomuua Rais,” alisema.
“Khaa! Kumbe…” mkuu wa ofisi hiyo alizidi kushangaa. Kisha akasema, “Haonyeshi kuwa ni mhusika katika mpango huo mchafu. Vaa yake na sura yake ni tofauti kabisa na hilo unalosema! Na anaonekana bado ni binti mbichi kabisa!”
“Kwa kifupi unaweza kukumbuka alivyovaa?” Makella alimkata kauli.
“ Sana tu. Alikuwa amevaa T-shirt ya bluu na sketi nyeusi. Macho yake yamerembuka. Nywele ni nyingi, zimeshuka hadi mabegani.”
Makella alitikisa kichwa akionyesha ishara ya kukubali. Kisha akasema, “ Ni mwenyewe.”
“I see,” yule mkuu wa ofisi alitamka kwa masikitiko. Akaongeza, “Saa hizi watakuwa mbali.”
“Najua, lakini ipo siku atapatikana tu,” Makella alisema huku akiondoka. “Itabidi tuwasiliane na Serikali ya Tanzania haraka iwezekanavyo. Na kwa Tanzania atakamatwa tu. Hana ujanja!”
Ilikuwa imetimu saa 6 usiku. Kwa Makella, ulikuwa ni usiku mbaya zaidi. Kwa namna nyingine alihisi Mungu hayuko upande wake. Hata hivyo, wakati akiirudia teksi ili arudi mjini, moyoni alikuwa akiamini kuwa ipo siku atakayomtia mkononi mbaya wake.
“Judith…! Judith…!” alitamka kwa hasira wakati akifungua mlango wa teksi na kuingia.
**********
SIKU iliyofuata, wakati jua linakaribia kuzama, lori aina ya Fuso lilikuwa likiingia katika mji wa Biharamulo, mkoani Kagera, nchini Tanzania .
“Itabidi tulale hapa,” Baraki aliwaambia Livingstone na Judith. Kisha akamgeukia Judith: “Unaionaje Tanzania? Kuna vurugu kama kule kwenu?”
Badala ya kujibu, Judith alitabasamu kidogo na kuyaepuka macho ya Baraki ambayo yalikuwa yamemganda, akisubiri jibu.
“Naamini utaipenda Tanzania,” Baraki aliendelea. “Kama nilivyokwambia jana, huku hakuna mauaji ya kikabila kama kule kwenu. Tuna makabila zaidi ya mia moja na ishirini, na makabila kati ya matano au sita ni makubwa sana kama ilivyo huko kwenu kwa makabila ya Kihutu na Kitutsi. Lakini huku Tanzania ukabila hauna nguvu. Mtu wa kabila moja anaweza kuoa au kuolewa na wa kabila jingine. Kule kwenu inawezekena hiyo?”
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Judith alikataa kwa kutikisa kichwa.
“Inasikitisha,” Baraki alisema kwa sauti ya chini.
Yalikuwa ni maneno yaliyomwingia vizuri Judith. Alielewa na akashangaa. Kwake, haikumwingia akilini kuwa anaweza kumchojolea nguo Mhutu, iweje aolewe naye?! Eti Watanzania wao hawana utamaduni wa kujali ukabila. Mmakonde anaweza kuolewa na Msukuma, Muha akamwoa Mchaga, na kadhalika na kadhalika.
Hata hivyo, mawazo hayo yalipeperuka haraka kichwani mwake pale Makella alipomjia tena akilini. Hakuhofia kuwa huenda akavuka mpaka na kuingia Tanzania katika harakati zake za kumsaka, bali alizidi kuumia moyoni pale kumbukumbu ya jinsi Makella na wenzake walivyodiriki kunyanyua bunduki na kuwamiminia risasi baba, mama na wadogo zake watatu usiku wa siku iliyopita.
Kwa mbali alihisi machozi yakilenga machoni. Akaharakisha kuyafuta kwa namna ambayo Baraki hakutambua. Kwa ujumla hakuiona haja ya kila mtu kuyajua masaibu yaliyompata. Kila mtu, hata huyu Baraki! Ajue ili iweje? Na kwani akijua atamsaidiaje?
Akiwa ni msichana mwenye umri wa miaka 22, tayari alikuwa na uwezo wa kupambanua baya na zuri. Alikuwa na uwezo kuamua chochote kwa hiari yake, mradi aijue faida au madhara yake.
Alihitaji kumtoroka Makella, na kwa hilo amefanikiwa. Suala kuwa hawa wasamaria wema walistahili kujua yaliyomsibu, hakuona kuwa lilistahili. Dola 2,000 zilizokuwa ndani ya bukta aliyoivaa ndani ya sketi zilimtia matumaini ya kutotetereka kimaisha japo yuko ugenini.
Saa 2 usiku Baraki alikuwa akiegesha gari kando ya nyumba ya wageni ambayo walikuwa na mazoea ya kufikia kila walipofika mjini humo. Ni Kyaka Guest House.
Usiku huo ukawa ni mtihani mwingine kwa Judith, mtihani ambao hakujua kama ataushinda ilhali yuko ugenini na yuko na watu ambao kwake ni wageni kabisa. Kilichomtorosha kule Kiyovu Hotel ni kutokubali kufanya mapenzi na Makella. Lakini huyu mfadhili wake, Baraki ameonyesha bayana tangu kule mpakani kuwa anamhitaji kwa ajili ya kustarehe naye kimwili.
Akatae? Na akikataa Baraki atachukua hatua gani? Kwa vyovyote uhusiano utavunjika. Na matokeo ya kuvunjika kwa uhusiano huenda pia kukamfanya Baraki atoe taarifa katika Idara ya Uhamiaji kuwa kuna Mnyarwanda mmoja aliyeingia nchini kinyume cha sheria.
Hadi wakati Baraki alipokuwa akifunga mlango wa gari na kumshika mkono Judith wakielekea ndani ya gesti hiyo, bado Judith hakuwa akijua uamuzi aliostahli kuchukua kama ataombwa penzi na Baraki.
Baraki alichukua vyumba viwili; kimoja kwa ajili ya Livingstone, na kingine kwa ajili yake na Judith.
Moyo wa Judith ulikuwa mzito pale alipokaribishwa chumbani na Baraki. “Tutakuwa pamoja, mpenzi,” Baraki alimwambia huku akimtazama kwa macho yaliyozungumza bayana uchu dhidi yake. Akaongeza, “Naamini utakuwa usiku mzuri kwako na kwangu, usiku utakaoiliwaza mioyo yetu kwa kiwango kikubwa, eti?”
Yaleyale! Judith aliwaza kwa uchungu. Afanye nini? Akahisi kitu kikimshawishi kutoleta ukaidi wowote kama Baraki atataka penzi. Jambo moja tu lilimtia faraja; kufanikiwa kumtoroka Makella. Kufanya mapenzi leo na Baraki haitakuwa mara ya kwanza kwake maishani. Tayari alishafanya tendo hilo na kijana mmoja huko Gisenyi, kijana ambaye alimwondolea usichana wake na wakaendelea kufanya hivyo mara kadhaa kabla kijana huyo hajakumbwa na mauti ya ghafla katika sekeseke lilelile la ukabila miezi takriban sita iliyopita.
Lakini kwa kijana yule, Judith alifanya mapenzi kwa kuridhia. Na ni kwa itikadi hiyo ya kufanya mapenzi na mtu ampendaye, ndiyo maana aliamua kumtoroka Makella. Pamoja na hayo, kumtoroka Makella akiepuka kumvulia nguo, na kumkatalia Baraki, ni mambo mawili tofauti.
Makella alikuwa ni muuaji; aliwaua baba, mama na wadogo zake na pia alikuwa ni wa kabila la Wahutu. Huyu Baraki siyo Mhutu, ni Mtanzania. Isitoshe, Baraki amemfadhili kwa kiwango kikubwa, ufadhili ambao hata yeye mwenyewe haujui uzito wake. Kumvulia nguo Baraki hakuona kuwa ni kosa, zaidi atakuwa naye amelipa fadhila. Kwa ujumla bado aliuhitaji ufadhili wa Baraki, na aliuhitaji ufadhili wa Watanzania. Dola 2000 alizokuwanazo, hakuona kuwa ni kinga madhubuti katika nchi hii ngeni. Bado aliihitaji roho yake!
Kwa hali hiyo aliamua jambo moja kwa faida yake; kumfurahisha Baraki usiku huo. Na ndivyo ilivyokuwa; Baraki aliuona usiku huo kuwa ni mzuri kupindukia, viungo vyake vikiburudika huku nafsi ikiliwazika. Kwa upande wa Judith, yeye kwake ulikuwa ni usiku wenye adha aliyolazimika kuivumilia japo pia alilazimika kumridhisha Baraki kwa kila hali, akitoa ushirikiano wote uliohitajika.
Waliingia jijini Dar es Salaam saa 4 asubuhi, siku ya sita baada ya usiku huo. Mara tu gari lilipoegeshwa kwa tajiri wa Baraki eneo la Tabata Dampo, Baraki na Judith waliondoka pamoja hadi Magomeni Kondoa ambako Judith alipatiwa chumba katika gesti moja ya hadhi ya kati.
“Usihofu, utaishi hapa kwa muda bila matatizo yoyote,” Baraki alimwambia. “Mimi naishi mbali kidogo, na nina mke. Lakini hilo lisikutishe. Hutapata shida yoyote. Tuko pamoja baby.”
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alipokwishasema hayo, alimpatia shilingi 30,000 huku akiongeza, “Za chakula cha mchana. Kama unasikia njaa, hapo nje kuna chipsi na kuku. Nikuchukulie?”
Judith alikataa kwa kutikisa kichwa. Kisha akasema, “ Asante, mpenzi. Lakini kwa sasa sijisikii kula. Nimechoka sana, labda baadaye .”
“Ok, kaoge, upumzike,” Baraki alisema huku akimbusu katika shavu la kulia. Akaongeza, “Muda huu ngoja nirudi ofisini, usihofu kitu. Hutapata matatizo yoyote.”
Akatwaa kalamu na karatasi kisha akaandika tarakimu kadhaa na kumpatia Judith karatasi hiyo, akisema, “Hii ni namba yangu ya simu. Ukiwa na shida yoyote unipigie. Kama leo hatutaonana, basi kesho asubuhi nitakuja. Na, nadhani inabidi uwe na simu. Suala hilo nitalishughulikia kesho hiyohiyo.”
“Nitashukuru sana, baby,” Judith alisema huku naye akimbusu shavuni.
Kisha Baraki alimfuata mhudumu wa gesti na kumwambia, “Yohana, mgeni wangu asipate shida yoyote. Nimekuachia kazi hiyo wewe. Kukiwa na tatizo lolote, unitaarifu. Sawa?”
“Poa tu, wala usikonde, msh’kaji wangu.”
**********
JUDITH aliachwa peke yake. Akawa peke yake chumbani, na akawa peke yake Magomeni. Aliketi kitandani na kushusha pumzi ndefu, akivuta kumbukumbu ya matukio ya kutisha na kusikitisha yaliyomkuta ile siku asiyoisahau, siku ambayo baba, mama na wadogo zake watatu waliuawa kikatili mbele yake, nyumbani, mjini Kigali, Rwanda saa 2 usiku.
Machozi yakamtoka! “Nimebaki peke yangu!” alinong’ona huku akiendelea kulia. Ndiyo, alikuwa katika kipindi kigumu maishani. Hakujua nini kitafuata. Japo alifanikiwa kumtoroka Makella, hata hivyo hakuwa na dira yoyote mbele yake.
Dakika takriban kumi zilikatika akiwa hapo kitandani akiwaza hili na lile, mawazo ambayo hayakumpa mwanga wowote wa mafanikio mbele yake.
Hatimaye akapiga moyo konde na kujipa ujasiri, akinong’ona, “Kama ni kufa bora nifie huku. Wazazi wangu na wadogo zangu wameuawa na hata makaburi yao sitayaona, bora hata na mimi nife. Kifo changu hakitakuwa cha ajabu!”
Akasimama na kuchojoa nguo zake, na ndipo alipobaini kuwa bado alikuwa na mtihani mbele yake. Hakuwa na nguo nyingine zaidi ya hizo. Lakini alikumbuka kuwa alikuwa na dola 2000, isitoshe, Baraki alipoondoka alimwachia shilingi 30,000 za Tanzania .
Akatwaa zile shilingi 30,000 na kuvaa tena nguo zake. Akaenda mapokezi ambako baada ya kuzungumza na mhusika, akapata msaada aliouhitaji.
“Subiri nikuitie mtu wa kukusaidia,” aliambiwa.
Muda mfupi baadaye aliondoka na binti mmoja mcheshi ambaye alimwongoza hadi soko kuu la Magomeni, eneo ambalo Judith alitarajia kupata nguo.
Wakiwa njiani, msichana yule aliyeitwa Swaumu alimdadisi, “Kwani umetokea wapi?”
Akili ya Judith ilifanya kazi haraka. Hakutaka kusema kweli kwani aliamini kuwa kwa kufanya hivyo atakuwa amejiweka katika mazingira magumu zaidi. Akaukumbuka mji wa Kahama ambako walilala siku mbili wakiwa njiani kuja Dar.
“Kahama,” alimjibu.
“Kahama?”
“Ndiyo.”
“Sasa huku umekuja kibiashara au?”
“Ndiyo, kwa mambo ya biashara.”
“Lakini ulishakuja Dar hapo kabla?”
“Hapana. Hii ndiyo mara yangu ya kwanza.”
“Umeleta biashara gani?”
“Sikuleta biashara, nimekuja kuangalia vitu vitakavyofaa kupeleka Kahama.”
“Ok,” Swaumu alionyesha kuridhika.
Kutoka hapo Magomeni Kondoa hadi sokoni ziliwachukua takriban dakika ishirini. Swaumu akampeleka hadi kwenye eneo lililotawaliwa na wauza nguo. Hapo Judith akanunua blauzi tatu, sketi mbili na nguo chache za ndani. 20,000/- zikawa zimekatika!
“Kwa nini hukuja na nguo?” Swaumu alirudia kudadisi.
Akiwa amekereka kwa maswali ya Swaumu, Judith aliachia tabasamu bandia kisha akajibu, “Ilikuwa ni safari ya ghafla.”
Na katika kuhakikisha kuwa Swaumu haendelei kumsumbua kwa maswali naye alimuuliza, “Hivi huku kuna sehemu ya kubadili pesa?”
“Pesa?” Swaumu alimtazama kwa mshangao. “Pesa gani? Una dola?”
“Ndiyo,” Judith alijibu huku kwa kiasi fulani akijilaumu kwa kuuliza hivyo. Kwa kuwa aliona kuwa ‘maji yamekwishamwagika,’ aliongeza uongo, “ Nina dola tano. Nitazibadilishaje?”
“Ni kazi ndogo sana hiyo,” Saumu alijibu. “Kariakoo au katikati ya jiji kuna maduka mengi tu ya kubadilisha pesa. Uwe na Dola, Yen, Pauni, Yuro na nyingine zote utapata tu. Wala us’konde. Vipi, twende town?”
“Hapana,” Judith alipinga haraka. Akaongeza, “Tufanye kesho, au unaonaje?”
“Poa tu.”
Judith hakutaka Swaumu awe rafiki wa karibu. Ni ugeni wake tu uliomfanya aambatane naye. Kwa mtazamo wa haraka haraka alimwona Swaumu kuwa ni mwanamke ambaye hajatulia. Yuko macho juu-juu. Maswali mengi, udadisi usiokoma. Kichwani mwake hakumwona kuwa ni mtu anayefaa kwa ushirikiano wowote baina yao. Akaamua kujihadhari naye, lakini kwa namna ambayo Swaumu mwenyewe hatamshtukia.
Jioni ilifika, usiku ukaingia. Baraki hakuonekana. Lakini ilipotimu saa 4 usiku Judith akamwona Yohana, mhudumu wa gesti akimjia na simu mkononi. “Simu yako,” alimwambia huku akimpatia simu hiyo.
Alikuwa ni Baraki aliyepiga. Judith alipoipokea na kusikiliza, akapokea taarifa kutoka kwa Baraki kuwa kwa siku hiyo hatafika kwa kuwa amekuta matatizo katika familia yake.
“Kesho mchana tutawasiliana, sawa?” Baraki alimalizia.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sawa,” Judith alijibu kwa unyonge.
Usiku huo Judith akaamua kupiga pasi nguo zile alizonunua mchana kisha akaziweka juu ya kiti kilichokuwa chumbani humo. Angeziweka wapi wakati hakuwa hata na kijibegi kidogo? Baada ya hapo akalala. Usingizi haukumjia mapema.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment