Simulizi : Judith....Judith
Sehemu Ya Tatu (3)
Hata hivyo Makella hakuwa na muda wa kumsimulia mhudumu huyo hadithi nzima. Hakuuona umuhimu wa kufanya hivyo. Hasira zikiwa zinazidi kuongezeka kichwani mwake, alifoka, “Toka! Potea machoni kwangu kabla sijakisambaratisha kichwa chako mbwa wee!”
Haikuwa amri ambayo ilihitaji swali au mjadala wowote kwa wakati huo. Kwa kuuhofia usalama wake, mhudumu huyo alitoka mkuku, ufunguo wa akiba wa chumba hicho akiwa ameuacha kwenye kitasa cha mlango.
Makella alizidi kuchanganyikiwa. Akaivua taulo na kuitupa kitandani. Kisha akavaa nguo zake kwa kasi isiyokuwa ya kawaida. Dakika ya pili alikuwa akitoka chumbani humo mithili ya chizi, akiteremka ngazi za ghorofa hiyo kwa kukimbia. Aliikamata bunduki imara mkononi akionekana kuwa yuko tayari kuitumia muda mfupi ujao dhidi ya yeyote atakayestahili!
Alipofika nje ya geti akamfuata mlinzi aliyekuwa akirandaranda katika eneo hilo. “Kuna mwanamke yeyote mrefu, kavaa fulana ya bluu na sketi nyeusi aliyepita hapa?”
Yule mlinzi, kama ilivyokuwa awali kwa yule mhudumu naye alimtazama Makella kwa mshangao.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nakuuliza wewe!” Makella aliwaka.
Sasa yule mlinzi aliituliza akili yake na kumuuliza Makella, “Umbo lake likoje?”
“Mrefu! Mweusi!”
Yule mlinzi aliitika kwa kutikisa kichwa kisha akasema, “Kapita hapa kama dakika kumi zilizopita!”
“Ni malaya! Kaniibia!”
“Kakuibia?”
Makella hakujibu. Badala yake akarusha swali: “Kaelekea wapi?”
“Kaelekea huko!” mlinzi akajibu huku akionyesha kwa kidole upande wa mashariki.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Makella hakusubiri, kama kichaa alitoka mkuku, akaivaa Barabara ya 17/18. Akavuta hatua ndefu, akilini mwake akiwa hana hakika ya kufanikiwa katika harakati alizozianzisha. Lakini alijipa imani kuwa atafanikiwa.
Akazidi kukaza mwendo. Mara akasonya kwa nguvu na kuinyanyua juu bunduki yake AK-47 yenye risasi ishirini. Kisha akajikuta akibwata kwa mnong’ono uliofurika tani kadhaa za hasira, “Nitampata! Na ole wake nimpate, atajuta kuzaliwa Mtutsi! Kwanza nachukua pesa zangu, halafu…” akaiacha sentensi hiyo ikielea.
**********
KITENDO cha dereva teksi kumwona mtu akiingia garini haraka vile, naye akajitoa kwenye kundi la wenzake alikokuwa akiongea, akajitoma garini. Judith alikuwa ameketi kiti cha mbele. Wakatazamana. Judith akashusha pumzi ndefu na kumuuliza, “Una mafuta ya kutosha?”
“Yapo, dada. Kwani una safari ndefu?”
“Nakwenda mpakani.”
“Yanatosha. Kuna lita thelathini. Kwa mpakani yanatosha. Vipi, mbona safari ya huko saa hizi? Kuna tatizo?”
Lilikuwa ni swali ambalo Judith hakulipenda na hakulitarajia. Kwa hali hiyo hakuwa tayari pia kulijibu. Zaidi, alisema, “Twende.”
Dereva alimtazama kidogo na kugeukia mbele. Alishagundua kuwa abiria wake hayuko katika hali ya kawaida. Akaling’oa gari taratibu na kuingia barabara kubwa. Dakika tano baadaye, Judith alimwambia, “Kama unaweza, tafadhali ongeza mwendo. Nina haraka.”
Kwa mara nyingine dereva alimtazama Judith na safari hii akauona uso wake ukiwa umebadilika. Alionekana kuchangamka kidogo. Ndiyo, Judith aliamua kuirejesha hali hiyo ili kumfanya dereva asiwe na wasiwasi naye na amchukulie kama abiria wengine wa kawaida.
“Sawa, dada,” dereva alisema huku akibadili gia na kuongeza mwendo. Kwa kiasi fulani Judith akajisikia afueni.
Kwa jumla alikuwa na hofu kuhusu Makella. Akili yake ilimwambia kuwa kwa vyovyote vile, Makella atakapookolewa na wafanyakazi wa Hoteli ya Kiyovu, kitakachofuata ni kumsaka. Na huenda akapata fununu zitakazomsaidia kumfikisha huko mpakani. Na kama atafanikiwa kufika mpakani na akamwona, kitakachofuata ni kumshindilia risasi zote zitakazokuwa kwenye bunduki yake.
Akawa akiomba Mungu kimoyomoyo, lisitokee hilo analolifikiria.
Nusu saa baadaye walikuwa wamefika mwisho wa safari yao. Lilikuwa ni eneo lililochangamka sana. Magari mengi makubwa yalikuwa yameegeshwa huku wahusika wake wakiwa wameketi kwenye baa zilizofurika katika eneo hilo.
Judith alipita katika makundi hayo na kwenda kwenye kijibanda kilichokuwa sehemu yenye kijigiza ambako aliketi na kuagiza bia baridi. Aliamua kukaa huko ili ajipange jinsi ya kuondoka eneo hilo na kwenda mbali zaidi ambako aliamini kuwa huenda ndiko kwenye usalama. Na aliamua kuendelea kunywa bia kwa kuwa aliona kuwa ndiyo nguzo pekee iliyomwondolea woga na kumwongezea ujasiri.
Kama alitarajia kuwa angepata utulivu kwa kuketi peke yake basi haikuwa hivyo. Muda mfupi baadaye wanaume wawili walikuja katika kibanda hicho huku wakiwa na chupa za bia. Aliyetangulia alikuwa ni Baraki, dereva wa gari kubwa lililokuwa na safari ya kuelekea Tanzania. Mwenzake alikuwa ni Livingstone ambaye alikuwa ni utingo.
Wakamsalimia Judith na kuketi katika meza ya pili iliyokuwa na viti vitatu. Lakini Baraki hakukaa muda mrefu mara akamgeukia Judith na kumuuliza, “Dada yetu mbona umekaa peke yako? Karibu hapa tujumuike pamoja.”
“Asante,” Judith alijibu bila ya kuwafuata.
Baraki hakukubali, akanyanyuka na kumfuata. Na ni hapo sentensi hii na ile ilipowaunganisha. Katika zungumza hiyo ndipo Baraki alipojua kuwa Judith alikuwa ni mtoto yatima. Hakuwa na baba wala mama, na ndugu zake wote walikwishauawa.
Lakini Judith hakusema kuwa mauaji hayo yalifanyika kwa usiku huo. Kwa kuwa ujasiri ulikwishamwingia, alijitahidi kuwa makini kwa kila jambo sanjari na kutoonesha bayana usoni kuwa kuna madhila yaliyomkuta.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Maongezi yao yaliponoga ndipo Judith alipogundua kuwa watu hao walikuwa ni Watanzania na walikuwa safarini usiku huo.
“Kumbe nyie ni Watanzania?” alimuuliza Baraki ambaye wakati huo mkono wake mmoja ulikuwa umetua kwenye bega la Judith.
“Ndiyo, sisi ni Watanzania,” Baraki alijibu. “Tunakukaribisha kwetu Tanzania, upaone. Hakuna fujo, ni amani tupu. Kwani wewe ni kabila gani? Mhutu au Mtutsi?”
Judith alisita kidogo kisha kwa sauti ya chini akajibu, “Mtutsi.”
“Ok, nd’o maana ni mzuri,” Baraki alisema huku akitabasamu na kumtazama kwa namna ya kipekee, wakati huohuo, mkono uliogota begani sasa ukimpigapiga.
Judith aliguna na kutwaa chupa ya bia, akanywa funda moja kubwa kisha akairejesha mezani. Akahisi kitu kikimnong’oneza kichwani: ‘Hii ndiyo nafasi yako. Itumie kikamilifu.’ Papohapo akamtupia macho Baraki na kuachia tabasamu la kirafiki, zaidi ya lile tabasamu la urafiki wa kawaida. Yale macho yake yanayobembeleza na kushawishi yakamsisimua Baraki kiasi cha kumpa nguvu ya kuendeleza hoja yake.
“Judith, twende Tanzania,” yalimtoka Baraki kwa sauti yenye kigugumizi cha mbali.
“Siyo kwamba nakataa. Hata mimi huwa napenda sana kwenda Tanzania kutembea. Nasikia huko kwenu hakuna mambo ya ukabila wala udini japo makabila ni mengi sana na dini ni nyingi sana…”
“Yeah,” Baraki alimkata kauli. “Kwa kweli Tanzania ni kisiwa cha amani na utulivu. Kuna makabila zaidi ya mia moja, lakini hayaleti mtafaruku wowote! Nashangaa hapa kwenu kuna makabila mawili tu lakini duu!”
Judith aliinamisha kichwa kwa huzuni. Kumbukumbu ya mauaji ya wazazi wake ikamrudia kichwani kwa nguvu kubwa kiasi cha kujikuta akibubujikwa machozi bila ya kujitambua.
Baraki aliiona hali hiyo na haraka akamuuliza, “Kwa nini unalia Judith? Samahani sana kama kwa kukwambia hivyo nimekuudhi.”
Judith alishtuka na kujifuta machozi haraka. Hakutaka Baraki ajue chochote cha ziada; kwamba siku hiyo wazazi wake waliuawa na kwamba alikuwa na Makella na akafanikiwa kumtoroka huku akiwa amemwibia dola 2,000! Ndiyo, alipanga kuwa hiyo iwe ni siri yake!
“Judith…” Baraki alimwita huku akimwinamia.
“Baraki usijali, ” Judith alimwahi. “Nimekumbuka mbali.”
“Umekumbuka nini, Judith?”
“Mwaka jana kuna mtu aliniambia kuwa niende kujiendeleza kimasomo huko Tanzania, nikakataa. Leo yeye mwenzangu mambo yake mazuri. Nasikia amemaliza Chuo cha Biashara na tayari anafanya kazi.”
“Ooh pole sana,” Baraki alisema. “Sasa unasemaje mtoto mzuri. Hauko tayari kwenda na sisi?”
Judith aliachia tabasamu la kirafiki na kumtazama Baraki kwa yale macho yake yanayoshawishi. Kwa ujumla alikuwa akitaka kuipata nafasi hiyo muhimu ya kwenda nje ya nchi. Amtoroke haraka Makella!
Hali hiyo ilimpa nguvu zaidi Baraki, na sasa aliutupa mkono wake juu ya paja laini la Judith. Akautelezesha kwa namna isisimuayo. Judith akaguna na kuushika mkono huo, akiuzuia kuendelea na ziara yake.
Lilikuwa ni zuio ambalo hata Baraki aliona kuwa ni la bandia. Hivyo, zaidi alimsogelea na kumbusu sikioni. Judith akaguna na kuruka kidogo. “Jamaani…”
“Sema Judith, uko tayari twende wote?”
“Sawa.”
**********
KUTOROKWA, tena kutorokwa na mwanamke, kwa Makella ilikuwa ni zaidi ya tusi la nguoni. Isitoshe, mwanamke mwenyewe katoroka huku pia akiwa amemwibia pesa, dola 2,000 za Marekani! Lilikuwa ni tukio zito, tukio ambalo Makella alilichukulia kwa uzito mkubwa. Hivyo, mara tu alipokuwa nje ya Kiyovu Hotel alitembea kwa hatua ndefu akiifuata Barabara ya 17/18 ambako aliambiwa kuwa ndiko Judith alikoelekea.
Dakika tano baadaye alikuwa mbele ya duka lililomilikiwa na ofisa wa Jeshi la Rwanda . Hapo, licha ya kuwa na huduma za bidhaa mbalimbali pia vinywaji kama bia za aina tofauti zilipatikana.
Kulikuwa na wateja wengi waliojiburudisha kwa vinywaji. Kwa sekunde chache alisimama akiduwaa, lakini hakuduwaa kama taahira. Alikuwa na sababu. Alizungusha macho kwa kila mtu aliyekuwa hapo huku akilini mwake sura ya Judith ikimjia.
Alitarajia kumwona Judith mahali hapo, lakini hakuambulia kitu. Akazidi kuchanganyikiwa. Akasonya kwa hasira huku akijiapiza kimoyomoyo kuwa akimwona, kwanza atamtia risasi ya kichwa kisha atainajisi maiti yake!
“Vipi, umekosa nafasi?” sauti kutoka nyuma yake ilipenya masikioni mwake.
Akageuka haraka kumtazama muulizaji. Akashusha pumzi baada ya kumwona Luteni Kasa, mmiliki wa duka hilo.
“Hapana, afande,” Makella alijibu huku akifuatisha saluti ambayo Luteni Kasa hakuonyesha kuijibu. “Kuna mtu…” aliongeza na kusita.
“Subiri,” Luteni Kasa alimwahi. Papohapo akamwita kijana mmoja na kumwamuru alete viti viwili na meza moja.
“Lete na bia mbili,” Luteni aliongeza huku akimgeukia Makella na kumuuliza, “Bia gani?”
“ Asante . Labda maji tu.”
Sauti na mwonekano wa Makella vilitosha kumfanya Luteni Kasa ahisi kuwa Makella ana tatizo; kuna jambo lililomkera.
Muda mfupi baadaye walikuwa pamoja, Luteni Kasa akinywa bia na Makella akinywa maji.
“Uko kazini?” hatimaye Luteni Kasa alimwanza.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndiyo,” Makella alijibu, kisha akafuatisha hadithi nzima ya operesheni dhidi ya Watutsi mchana kutwa lakini akiepuka kuuweka bayana ukweli wa kilichomsibu dakika chache zilizopita.
“Ok, lakini siyo vizuri kujiamini kiasi cha kutembea peke yako eti kwa kuwa una silaha,” Luteni Kasa alimwonya. “Ni vyema kama mngekuwa wawili, watatu hivi. Ukiwa peke yako kama hivi, adui akikuona na silaha atakuwahi.”
“Ni kweli, lakini kuna sababu iliyonifanya niwe peke yangu.”
“Sababu gani?”
“Namfuatilia shushushu mmoja wa Kitutsi.”
“Shushushu?!”
“Ndiyo. Tena ni mwanamke!”
“Mwanamke?!” Luteni alimkazia macho Makella. Akairejesha mezani glasi ya bia iliyokuwa mikononi. Kisha akaongeza, “Una hakika kapita hapa au unabahatisha?”
“Taarifa nilizonazo zinanifanya niamini kuwa amepita hapa!” Makella alisisitiza.
Kimya kifupi kilitawala. Luteni Kasa akamtumbulia zaidi macho, Makella. Kisha: “Nina zaidi ya saa nzima niko hapa nje. Huyo mtu kapita muda gani?”
“Siyo zaidi ya robo saa.”
“Kavaaje?”
“Fulana ndefu ya bluu na sketi nyeusi.”
“Kichwani?”
“Ana nywele ndefu zilizomwagika hadi mabegani.”
Tabasamu la mbali likamtoka Luteni Kasa. Akasema, “Nadhani nimemwona.”
“Afande, umemwona?” Makella akamtolea macho.
“Ndiyo, na nadhani ni mwenyewe.”
“Yuko wapi?”
“Hapa hakukaa,” Luteni Kasa alijibu kwa utulivu. Akaongeza, “Kawaulize hao madereva teksi. Nadhani watakuwa na jibu la kukuridhisha.”
Makella aligugumia maji na kuitua chupa mezani ikiwa tupu. Kisha akanyanyuka na kutoa saluti nyingine, saluti ambayo kama ile ya awali, hii pia Luteni Kasa alionyesha kutoijali, zaidi alitamka neno moja tu: “Asante.”
Makella akatoka. Moja kwa moja hadi kwenye teksi ambayo dereva wake alikuwa nje, kaegemea bodi. Akazungumza naye kwa kifupi tu na kuambiwa kuwa mwanamke huyo alikodi teksi na kuelekea mashariki mwa nchi.
“Labda anakimbia hizi vurugu,” dereva huyo alimalizia.
“Teksi hiyo imeelekea kule mpakani?”
“Inawezekana.”
Makella alifikiri kidogo kisha akauliza, “Una mafuta ya kutosha?”
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Full tank.”
“Ok, twende. Chaji yako utaileta hapa kwa afande, Luteni Kasa. Sawa?”
Haikuwa rahisi kwa dereva huyo kupinga amri ya Makella. Kwa siku hiyo, kila askari wa jeshi alikuwa na sauti. Kama dereva huyo angekataa, isingemwia vigumu Makella kumshindilia risasi na kumchukua dereva mwingine. Angeweza, na asingetokea mtu yeyote wa kumuuliza chochote!
**********
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment