Search This Blog

Saturday, 5 November 2022

JUDITH...JUDITH - 2

 








Simulizi : Judith....Judith

Sehemu Ya Pili (2)





Akakumbuka kuwa muda mfupi baada ya yule mfanyakazi wa hoteli kuwafungulia mlango, alimkabidhi ufunguo Makella. Kwa vyovyote ndio utakuwa huu, alijiaminisha.



Hata hivyo, aliwaza, hata kama ufunguo ndio huo, bado ilihitajika akili ya ziada katika kumzidi ujanja Makella. Akili yake ikaendelea kumjengea imani kuwa ndani ya jokofu lililo mbele yake kuna vinywaji na miongoni mwa vinywaji hivyo ni Primus, bia inayoaminika, kukubalika na kuheshimika kwa Wanyarwanda na Warundi wengi.



Judith aliomba Mungu kimoyomoyo, Makella awe mnywaji, anywe Primus na huo ndio utakuwa mwanzo wa yeye, Judith kunusurika. Kwamba atajinusuru vipi, hilo hakutaka kulifikiria wakati huo, lakini aliamini hivyo. Na aliamini kuwa Mungu yupo na atakuwa upande wake!



Bado mkono wa Makella ulikuwa katika ziara mwilini mwa Judith. Sasa ulikuwa umehama pajani na kutua kifuani ambako ulianza kuyatomasa matiti machanga, yenye joto la uhai, joto liwezalo kumsisimua mwanamume yeyote mkamilifu.



Judith akiwa ni mwanadamu kamili, mwenye viungo vilivyokamilika, kwa mbali alijikuta akisisimkwa. Ndiyo, aliuhisi msisimko mwilini mwake lakini ukawa ni msisimko ambao haukudumu zaidi ya sekunde kumi. Angepata raha gani, angeupataje msisimko wakati familia yake yote imeteketezwa muda mfupi uliopita?



Kwa ustaarabu aliushika mkono wa Makella na kuutoa kifuani pake taratibu huku akiuminyamimya kiganjani katika namna iliyomchanganya zaidi Makella.



“Judi…Judi…” Makella alinong’ona kwa taabu huku akimvuta Judith na kumbusu shavuni. Kisha akataka kumbusu kinywani, tendo lililokumbana na kipingamizi kutoka kwa Judith lakini kikiwa ni kipingamizi kilichowekwa kwa namna nyingine ya kistaarabu.



Alichofanya Judith ni kuukwepesha mdomo wake kwa namna ya kuona aibu huku akiachia tabasamu laini na kuuinamisha uso.



“Judi…” kwa mara nyingine Makella alinong’ona, safari hii akiwa kama anayeomboleza.



“Bwana nimechoka!” sauti ya Judith ilikuwa ya deko.



“Umechoka?” likamtoka Makella bila ya kutarajia.



Judith akaitika kwa kutikisa kichwa, kisha akaongeza kwa sauti, “Halafu nasikia kiu!”



“Kiu!” Makella aliropoka. Papohapo alinyanyuka na kulifuata jokofu. Akalifungua na kuliacha wazi. Macho yakatua ndani na kushuhudia shehena ya vinywaji mbalimbali; soda, maji, mvinyo, bia na pombe kali.



“Kinywaji gani mrembo?” Makella alimuuliza Judith huku bado akiwa ameuach wazi mlango wa jokofu labda ili na Judith pia avishuhudie vinywaji hivyo.



“Maji.”



“Maji?” Makella alishangaa. “Kwa nini usinywe bia au wine?”



“Sijazoea.”



Makella akacheka kidogo. “Ni vinywaji vizuri na bora kwa afya,” alisema huku akitoa chupa mbili za bia. Akaongeza, “Jaribu. Ukizoea utaitaka kila siku. Kwa leo ukinywa moja tu itatosha. Na utachangamka kimwili na kiakili. Sipendi uwe katika lindi la mawazo mtoto mzuri kama wewe.” Akaziweka chupa hizo juu ya kimeza na kuzifungua. “Nikupatie glasi?”



“Hapana, nitakunywa hivihivi,” Judith alijibu. Wakati huo alikuwa akiwaza jinsi atakavyojisikia pale atakapolipenyeza funda la pombe kinywani mwake kwa mara ya kwanza maishani mwake.



“Hapo umeonyesha kuwa wewe ni binti wa kisasa,” Makella alisema huku akiachia tabasamu kubwa. Akaongeza, “Ningeshangaa, binti mzuri wa Kitutsi asinywe bia! Lingekuwa ni jambo la ajabu! Hapo kwa kweli nisingekuelewa. Wasichana wa Kitanzania ndio wenye ushamba wa aina hiyo.



“Kule Tanzania nilishakaa kwa mwezi mmoja na kitu. Nilikuwa Dar es Salaam. Tuache uongo, Dar es Salaam ni mji mkubwa sana…mkubwa sana kuliko Kigali hata Bujumbura! Ni jiji kubwa, jiji lenye wakazi wengi sana, kama milioni tano au kumi!



“Ni jiji lenye majumba mengi, mazuri na makubwa sana! Kwa sasa kila kukicha jiji lile linabadilika. Kama ulikuwa kule miaka mitano iliyopita leo ukiingia utapotea! Wallahi nakuapia! Kila siku linazidi kupendeza, na hayo majumba yenyewe yanayojengwa acha tu…ni mazuri!



“Dar es Salaam pia ni jiji lenye mambo mengi kama ambavyo lina wakazi wengi. Ni jiji lenye maraha na karaha. Kuna baa nyingi na kumbi nyingi za starehe na pia kuna bendi nyingi za dansi, taarabu na bongo fleva. Ukilinganisha na huku kwetu, ni majirani zetu tu wa Burundi ambao miaka ya themanini walikuwa na vikundi vya taarabu ambavyo kwa kweli vilitikisa sana katika Ukanda wa Maziwa Makuu. Kulikuwa na vikundi vya Jasmine Musical Taarab na Shani Musical Taarab ambavyo vilitisha!



“Lakini siyo leo…! Leo Tanzania ina vikundi vya taarabu vinavyopiga huu mtindo mpya wa sebene…mmmh acha tu! Watu wanakata viuno kama wanamuziki wa Kikongo! Hahahahahaha…” kicheko chake kikatisha badala ya kupendeza masikioni mwa Judith.



Akaendelea, “Na siyo taarabu tu, pia kuna wapenzi wa bongo fleva ambao ni vijana wa kishkaji-shkaji na wengine nd’o wanapenda dansi. Kuna bendi za Kikongo zilizolowea hapo Dar na nyingine ni za hapohapo Tanzania kama kongwe za Msondo Ngoma, Mlimani, African Stars na nyingine ndogondogo.”



Ukimya mfupi ukatawala. Makella akanyanyua chupa na kuipeleka kinywani. Akagugumia funda kadhaa na kuirejesha juu ya kimeza. Akayagandisha macho usoni pa Judith kama vile anayemuuliza, “mbona na wewe hunywi?”



Judith hakuwa mbumbumbu wa fikra. Dhamira yake ya kuhakikisha kuwa anailinda heshima na uhai wake ilikuwa palepale! Na hakukuwa na binadamu wa kuweza kuitengua. Alimtazama mara moja tu Makella na kubaini ni kipi alichohitaji. Kwamba anywe bia yake hiyo iliyokwishafunguliwa.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Hakutaka kumfanya Makella ahisi tofauti yoyote. Bado ilikuwa ni mapema hivyo Judith alijali kuwa makini ili mambo yasiharibike. Alitaka afanye kila jambo kwa uangalifu na umakini wa hali ya juu ili kisiharibike kitu. Akaitwaa chupa hiyo na kuipeleka kinywani. Akameza funda moja kwa jitihada kubwa. Mwili ukamsisimka lakini akajitahidi kutoukunja uso. Akataka aonekane kuwa ni mtu aliyekwishakizoea kinywaji hicho.



Hakuwa na kumbukumbu sahihi za maisha yake wakati akiwa mtoto mdogo. Lakini alikumbuka vizuri kuwa tangu aanze kuwa na akili ya kutambua jema na baya, hadi usiku huu, hakuwahi kupitisha tone la pombe kinywani mwake. Katika umri huu mkubwa aliokwishafikia, aliwahi kusikia kuwa baadhi ya wazazi huwa na tabia ya kuwanywesha watoto wao wachanga kijiko kimoja cha pombe kali kwa kile walichodai kuwa ni ‘kuua michango.’



Hakuwa na hakika kuwa na yeye alifanyiwa hivyo na wazazi wake. Hakujua na kwa usiku huu asingeweza kujua na hakuwa na haja ya kujua. Alichojua hapo ni kwamba, kwa mara ya kwanza anaipitisha pombe kinywani mwake na kuiruhusu iteremke tumboni mwake!



Mara ya kwanza kunywa pombe!



Funda la kwanza lilipopenya kooni alihisi kanywa shubiri. Akajikaza kisabuni, akainama kidogo na kwa sekunde chache akaukunja uso katika namna ambayo Makella hakumwona na punde akaunyanyua na kumtazama sawia.



Hata hivyo haikumwingia akilini Makella kuwa kinywaji hicho kilimsumbua Judith hata kidogo. Aliamini hivyo na ndivyo akili yake ilivyomtuma kuamini kuwa kila Mhutu, kila Mtutsi na yeyote wa kabila lolote nchini humo, pombe ni sehemu ya maisha yake.



Hivyo, yeye pia aliitwaa chupa yake ya bia na kunywa funda kadhaa kwa pupa kabla hajaitua kwenye kijimeza. Kisha akaendelea, “Turudi kwenye hoja yetu. Cha kushangaza, wanawake wengi wa Tanzania, wana tabia za ajabu. Utakuta mwanamke kaingia baa tangu saa sita mchana na kuganda akinywa ile mimaji yao ya chupa! Shaa! Sijui wako-aje? Au labda…” akasita na kukunja uso.



Akamtazama Judith kwa macho makali. Kisha akasema, “Ndiyo, nina shaka huenda wengi wao wako kwenye dozi kubwa.”



Akacheka kicheko cha dhihaka.



Kicheko hicho kilimshangaza Judith kiasi cha kumuuliza, “Dozi kubwa?! Una maana gani?”



Kwa mara nyingine Makella alicheka. Kisha kwa sauti ya bezo akasema, “Wengi wameshaukwaa…!” akacheka tena, safari hii kwa sauti ya chini zaidi. Akaongeza, “Hili gonjwa la Ukimwi limeharibu mambo. Utakuta mwanamke mzuri…lakini kumbe yuko kwenye dozi ya zile dawa ya kuongeza siku za kuishi. Mtu unakunywa kila siku mpaka siku yako ya mwisho ya kuishi. Na zamani nasikia ilikuwa ukishaanza kunywa midawa ile, wewe na bia basi! Yaani wewe na raha za dunia nd’o basi tena! Unakuwa mtu wa kula sana na kuhakikisha kila siku unakunywa dawa hizo! Lakini siku hizi nasikia mtu anaweza kuwa anapiga hizo dawa…wenyewe wanaziita ‘karanga’ na bia akanywa na hata sigara anavuta!”



“Hee!” Judith alishangaa, mkono kaziba mdomo, macho yamemtoka, akimtazama Makella.



“Basi tuachane na mambo hayo,” Makella alisema huku akitwaa chupa yake na kugugumia tena kinywaji chake.



Judith hakutaka makuu. Naye alitwaa chupa na kuipeleka kinywani, akashusha kooni funda dogo la kinywaji hicho kisha akamtazama Makella. Akamwona jinsi anavyojisikia kuwa huru zaidi.



“Nadhani nikaoge,” Makella alisema huku akiimaliza bia yake chupani.

Akasimama na kuchojoa nguo zake. Papohapo harufu kali ya jasho ikajitokeza na kumfanya Judith akunje uso kidogo na kwa siri.



“Sasa hivi?” Judith aliilazimisha sauti yake. Kwa ujumla swali hilo lilimtoka tu wala hakuwa amepanga kuhoji chochote, na ukweli ni kwamba hakuwa mtu wa kuzungumza chochote na Makella.



“Ndiyo, ni vizuri nikaoge sasa hivi. Pilikapilka za mchana kutwa zimenifanya nijisikie ovyo na kunitia kichefuchefu. Nadhani nikioga nitajisikia fresh kiasi. Nitakunywa bia kwa starehe na tutaongea kwa amani na utulivu, eti mpenzi?”



Judith hakujibu. Alitwaa tena chupa yake na kuipeleka kinywani. Sasa alikunywa bia hiyo kama anywaye maji ya kawaida. Hakikuwa kinywaji kigeni. Ulimi ulishazoea. Funda tatu zikapita kooni kwa mkupuo. Na Makella aliamini kuwa, kama Judith ataimaliza bia hiyo basi lazima atakuwa hoi, na hatakuwa na kipingamizi chochote cha kutendwa vyovyote. Zaidi, atatoa ushirikiano mkubwa bila ya woga wala aibu.



“Wewe endelea,” Makella alimwambia Judith. “Ikiisha, s’o vibaya ukiongeza moja. Nakuhakikishia, kinywaji hicho kitakufanya ujisikie vizuri sana kisaikolojia.”



Alipomaliza kuchojoa nguo, alitwaa taulo iliyokuwa imetundikwa kwenye eneo maalum, taulo ya hoteli, akajifunga kiunoni na kuelekea bafuni.



**********



DAKIKA ya kwanza baada ya Makella kuingia bafuni Judith alikuwa ameduwaa. Dakika ya pili ndipo akili yake ilipochangamka. Akazitazama zile chupa za bia zilizokuwa mbele yake. Akatema mate chini huku kakunja uso. Akasimama haraka na kutupa macho kitandani ambako bunduki ilikuwa imetulia. Akayahamishia macho kwenye nguo za Makella. Papohapo akazifuata na kuanza kuzipekua.



Sasa alikwishabadilika. Hakuwa yule Judith mwenye macho yaliyolegea kiasi cha kumfanya Makella ajiamini na kuwa na matumaini ya kustarehe kwa usiku huo. Hapana. Huyu alikuwa Judith mwingine, Judith ambaye alitaka aitimize azma yake iwe, isiwe! Kiwango cha bia aliyokunywa pia kikawa kinamwongezea ujasiri na kumwondolea woga.



Mfuko wa kwanza wa suruali hakuambulia kitu. Akauvaa mfuko wa pili. Humo akatoa kitambulisho cha uraia, na kitambulisho cha jeshi, akavitupa zuliani na kuukimbilia mfuko mwingine uliokuwa umetuna kidogo. Akashtuka baada ya kutoa bulungutu la pesa! Moyo ukapiga paa! Akashusha pumzi kwa nguvu.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Noti alizozitoa zilikuwa ni dola za Marekani 2,000. Hakuyaamini macho yake! Hakuwa mgeni wa noti hizi. Miezi kadhaa iliyopita marehemu baba yake mzazi aliwahi kumwonyesha sarafu na noti za Rwanda, Kenya, Tanzania, Uingereza, Ufaransa na Marekani.



Katika zoezi hilo alimwambia, “Mwanangu Judi, pesa za Wazungu zina thamani sana, na hasa pauni na dola. Pauni ni za Uingereza na Dola za Marekani. Hizo zina nguvu zaidi dunia nzima! Lakini haya mafaranga yetu ya Kinyarwanda, Kirundi na vikorokoro vya Tanzania, Uganda na Kongo mmh! Havina kitu! Afadhalli kidogo pesa ya Kenya, ile ina nguvu kuliko zingine za ukanda huu.”



Maneno hayo hakuyasahau, na sura za noti hizo hazikutoka katika kumbukumbu zake kichwani tangu siku hiyo. Na usiku huo, akiwa humo chumbani, peke yake, dola 2,000 za Marekani zikiwa mkononi mwake, alijiona kishaiweka Rwanda katika himaya yake.



Dola 2,000! Mungu ampe nini? Ndiyo, Mungu ampe nini yeye mtoto wa kike ambaye hajawahi kumiliki dola 100?



Akashusha pumzi ndefu huku akizipachika kwenye mfuko wa bukta yake aliyoivaa ndani ya sketi. Akairudia tena suruali hiyo. Akaukagua mfuko wa mwisho lakini hakupata kitu. Akahamia kwenye mfuko wa shati. Huko akaambulia sigara tatu na kibiriti. Akasonya na kuvirudisha.



Sasa akayatupa macho kwenye mlango wa bafu. Ni muda mfupi tu uliopita tangu Makella alipoingia bafuni humo, na kwa mbali alisikia michirizi ya maji, hali iliyompa taswira kuwa tayari Makella kishaanza kuoga.



Papohapo Judith akaifuata ile bunduki, AK-47 na kuikamata mkononi. Akaguna. Uzito wa silaha hiyo ukamvunja moyo. Hakutaka kujidanganya kuwa anaweza kuitumia silaha hiyo dhidi ya adui yake yeyote kama akiamua kutoroka nayo.



Kwanza, ni nzito. Pili, hajawahi hata kujifunza jinsi ya kuitumia. Akahema kwa nguvu huku akiirudisha taratibu kitandani. Akahisi woga ukimjia, lakini akajitahidi kujipa ujasiri, akijua kuwa hakuna mtu wa kumwokoa bali anapaswa kutumia akili yake yote ili ajinusuru dhidi ya jahili huyo.



Huo ulikuwa ni muda pekee ambao aliamini kuwa ndiyo angeweza kuutumia katika kujiokoa. Akapiga ngumi kiganjani na kuamua kuondoka. Papohapo akautwaa ufunguo na kutoka taratibu, kisha taratibu vilevile akaurudisha mlango na kuuchomeka ufunguo kwenye kitasa. Akafunga taratibu na kwa umakini huku akiangaza macho kushoto na kulia katika korido hiyo. Korido yote ilikuwa tulivu na hakukuwa na mtu yeyote.



Akafurahishwa na hali hiyo na papohapo akauchomoa ufunguo katika kitasa, akautumbukiza katika mfuko wa bukta yake. Akatoka taratibu, akipita katika korido hiyo ya ghorofa ya kwanza ya hoteli hiyo yenye ghorofa nne, mwendo wake ukiwa ni wa mtu wa kawaida na asiye na wasiwasi. Watu wawili aliokutana nao, mmojawao akiwa ni mwanamke wa Kizungu hawakumtilia shaka wala kumshangaa.



Alipofika chini alikwenda moja kwa moja mapokezi na kumtazama yule mhudumu kwa uso wa kirafiki, huku akiachia tabasamu la mbali. Kisha, akamwambia, “Dada, natoka kidogo. Nafika mtaa wa pili mara moja. Sitachelewa.”



“Ok,” mhudumu yule alimjibu huku akimtazama kwa macho ya wivu, akivutiwa na umbo zuri alilojaaliwa Judith hususan yale ‘makalio ya kumimina’ ambayo yalijitupa huku na kule wakati Judith alipokuwa akiondoka.



Ilikuwa ni saa 5 usiku!



**********



MIONGONI mwa kanuni ambazo Makella hakuwa tayari kuzitengua ni kuoga maji baridi. Awe na malaria, awe amekumbwa na uchovu mkali kiasi gani au hata awe anaihisi baridi kali maungoni, kamwe hakuwa tayari kuoga maji moto.



Usiku huo, pale tu alipoingia bafuni hakuwa na haraka. Alifungua bomba na kuyaacha maji yaingie kwa wingi ndani ya sinki ndipo akaingia na kuoga kwa raha zake.



Alioga kwa utulivu, moyoni akijihisi amani, akikumbuka kuwa huko chumbani kamwacha msichana mzuri ambaye kwa muda mrefu amekuwa akihangaika ili ampate. Leo, usiku huu, yuko naye! Ni raha iliyoje?



Akajifariji kwa imani kuwa, pindi watakapokiangukia kitanda, ataburudika kwa kuyanyonya yale matiti yaliyoshiba, yenye joto la uhai na ambayo ujazo wake pale kifuani uliongeza urembo wa Judith badala ya kutoa sura ya kuchusha. Hataishia hapo, ataendelea kujiliwaza kwa kuyatomasa na kuyapapasa maeneo mengine nyeti ya mwili huo unaovutia kabla ya kuhitimisha starehe kwa hatua nyingine muhimu zaidi.



Mungu ampe nini?



Dakika kumi baadaye alikuwa akijifuta maji mwilini kisha akajifunga taulo kiunoni kama awali na kutoka taratibu bafuni humo.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



**********



NJE ya Kiyovu Hotel, Judith alitembea kwa mwendo uleule wa kawaida huku kwa macho ya wizi akiwatazama askari watatu wenye silaha waliokuwa wakiilinda hoteli hiyo. Askari hao hawakumjali wala kumshuku, zaidi walimtazama kwa namna nyingine kabisa, umbo lake lililotengeneza robota kubwa chini ya nyonga yake likiwa ni kivutio kikubwa machoni mwa askari hao kiasi cha kujikuta wakitikisa vichwa kwa matamanio na kutabasamu kisirisiri.



Judith aliwaona jinsi walivyomtazama. Akaijua sababu ya kufanya hivyo. Hakushangazwa na macho hayo, wanaume wengi walishamkodolea macho hususan kwenye makalio yake makubwa pale inapotokea akavaa nguo yoyote iliyomshika vilivyo maungoni. Hawa askari walikuwa kama hao wanaume wengine wengi waliokwishapita, hivyo hakuwajali. Akaendelea kutembea taratibu vilevile, kama mtu anayejiamini ilhali ni Mungu tu aliyejua hali aliyokuwa nayo moyoni mwake.



Muda mfupi baadaye alikuwa kando ya Barabara ya 17/18. Barabara hiyo ilikuwa maarufu, yenye kutumiwa na magari mengi, makubwa kwa madogo, kuingia na kutoka nchini Rwanda. Kwa dakika chache tu, kama mbili alizosimama kando ya barabara hiyo tayari magari mawili makubwa ya mizigo, yenye nambari za usajili za Tanzania yalipita.



Akilini mwake, Judith aliamini kuwa, kwa kutumia magari hayo ya mizigo atafanikiwa kufika mbali na mkono wa Makella. Hivyo, aliamua kuhakikisha anafikia makubaliano na mmoja wa madereva wa magari hayo.



Lakini kuna wepesi gani katika kulifanikisha suala hilo? alijiuliza. Hakuwa zaidi ya hatua mia mbili kutoka Kiyovu Hotel ambako ametoroka huku kaiba fedha kutoka katika mifuko ya suruali ya ‘mpenzi’ wake aliyemleta humo.



Hakupenda kujipa matumaini kuwa Makella atatulia tu pindi atakapogundua kuwa dola zake 2,000 za Marekani zimeibwa. Hatatulia! Judith alilitambua fika hilo jambo. Atakachofanya Makella ni kulivalia njuga suala hilo. Atawakimbilia wahudumu wa hoteli ambao nao wataharakisha kuwasiliana na walinzi. Walinzi nao katika kutaka kuhakikisha kuwa siyo wafanyakazi ‘wachovu’, watahaha huku na kule, nje na ndani ya hoteli wakimsaka mithili ya msako wa gaidi au haini!



Usingepita muda mrefu kabla hawajamkuta pale kando ya barabara na kumsulubu kwa jinsi watakavyo kabla ya hatua yoyote nyingine kuchukuliwa na labda hatua hiyo ikiwa ni kumchinja kama kuku!



Hakuwa tayari kutiwa mbaroni na watu hao na kwa kuwa alijua kuwa ana pesa, hakutaka kusababisha uzembe utakaowafaidisha hao watakaomsaka. Alijua kuwa mbele ya pesa lolote linawezekana hata kama ni gumu kiasi gani.



Mbele kidogo, kiasi cha hatua hamsini hivi, kulikuwa na duka kubwa lililosheheni bidhaa mbalimbali. Lilikuwa wazi, wateja wakiingia na kutoka. Kando ya duka hilo kulikuwa na teksi kadhaa zilizokuwa zikiwasubiri wateja. Judith aliichangamsha akili yake katika kufanya kila jambo kwa haraka na kwa umakini, hivyo aliifuata teksi moja na kuingia haraka.



**********



AWALI ilimwia vigumu Makella kuamini kuwa Judith hayumo chumbani. Kwa sekunde kadhaa aliduwaa katika mlango wa bafu akikodoa macho chumbani. Kaenda wapi? Swali hilo lilirandaranda akilini mwake kwa mshangao.



Taratibu akatoka bafuni humo na kuufunga mlango taratibu vilevile. Akahisi kengele ya hadhari ikilia kichwani mwake. Nywele zikamsimama, na mara hima akaufuata mlango mkubwa wa kutokea chumbani humo. Akajaribu kuufungua.



Haukufunguka!



“Umefungwa!” akaropoka kwa sauti iliyojaa fadhaa na kugeuka huku na kule kama atazamiaye kuupata ufumbuzi wa tatizo lililojitokeza. Akashusha pumzi ndefu, macho kayatoa pima!



Akageuka na kurudi haraka kwenye nguo zake. Akainyanyua suruali iliyokuwa sofani ili aivae. Lakini jambo jingine likamshtua; kitambulisho cha uraia kilikuwa sofani huku mifuko ya nyuma ikiwa ikining’inia nje.



Hakuhitaji kukisumbua kichwa kufikiria ni kipi kilichomsibu.

Ameibiwa! Ndiyo, ameibiwa! Hilo halikuwa jambo la siri tena. Mmoja wa mifuko ya suruali ulikuwa umehifadhi pesa nyingi, dola 2,000 za Marekani, pesa alizozipata mchana katika harakati zake za uwajibikaji dhidi ya Watutsi.



Sasa hazimo!



“Mungu wangu!” aliropoka tena. Mara akakurupuka kuitwaa bunduki na kuishika mikononi mithili ya mtu aliye tayari kuitumia dakika hiyohiyo! Kwa takriban dakika nzima akabaki kaduwaa, akili imedumaa!



Mara kama aliyezinduliwa, akaitupa bunduki hiyo pale kitandani. Akili mpya ikamjia. Akaifuata simu na kubonyeza tarakimu kadhaa, akilenga mapokezi.



“Tukusaidie?” sauti ya kike ilipenya masikioni mwake baada ya muda mfupi.



“Njooni mnifungulie!” Makella alibwata simuni. “Njooni haraka nimefungiwa mlango kwa nje!”



Ulikuwa ni ujumbe uliomshtua na kumshangaza mhudumu wa mapokezi. “Chumba namba ngapi?” aliuliza.



“Kumi na moja!”



Papohapo mhudumu akautwaa ufunguo wa akiba wa chumba namba 11 na kutoka hima. Akaiona lifti ya kupandia huko ghorofani ni kama vile itamchelewesha. Akazikwea ngazi mbili, mbili hadi huko katika ghorofa ya kwanza. Punde akawa ameshaufungua mlango wa chumba namba 11. Akakutana uso kwa uso na Makella.



“Umemwona yule malaya?” lilikuwa ni swali lililomtoka Makella kwa jazba, akimtazama mhudumu huyo kama aliyehusika na kufungiwa kwake.



“Malaya! Malaya gani?”



“Yule niliyekuja naye!”



Mhudumu akatokwa macho pima. Kisha akauliza, “Kwani imekuwaje?”



Makella akazidi kughadhibika. Akamkwida mhudumu huyo. “Umeshirikiana naye, siyo?” alimuuliza huku akiendelea kumkwida.



“Kwani vipi…?”



Kofi kali lililotua katika shavu lake la kulia lilimkata kauli.



“Sema! yule malaya yuko wapi?”



“Ametoka!” binti yule alijibu.



Kofi la pili!



“Jamani utaniua bure!” mhudumu huyo alilalamika kwa sauti iliyoashiria kilio.



“Nitakuua kweli!” Makella aliwaka. “Sema yuko wapi…sema…sema au nakuua!”



“Subiri nikwambie!” mhudumu alisihi.



Makella alimwachia. Akamtazama kwa macho makali huku akihema kwa nguvu. “Yuko wapi?” akarusha swali kwa ukali uleule huku akiendelea kuhema kama mtu anayekaribia kufa.



“Katoka!” mhudumu alijibu kwa woga.



“Katoka?!” Makella akamkodolea macho zaidi, pumzi zikapanda na kushuka kwa kasi. Pua zikamcheza kama nguruwe-pori!



“Ndiyo!”

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Kaenda wapi?”



“Kasema eti anafika hapo mtaa wa pili!”



“Kaniibia!” Makella aliropoka kwa nguvu.



“Nini?” mhudumu alibaki kinywa wazi.







ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog