Search This Blog

Saturday 24 December 2022

KILIO CHA MIFEREJI YA DAMU IENDAYO ETHIOPIA - 5

   http://pseudepigraphas.blogspot.com/2020/06/kilio-cha-mifereji-ya-damu-iendayo_10.html

Simulizi :  Kilio Cha Mifereji Ya Damu Iendayo Ethiopia

Sehemu Ya Tano (5)



Makubaliano haya yalikuwa ya maana sana kwa Kagame, kwani hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa rais Habyarimana kukubali rasmi kushindwa. Japokuwa bado kuna makamanda ndani ya RPF walikuwa wanahisi kama Kagame amemwachia Habyarimana upenyo mkubwa zaidi wa kupumua, lakini Kagame mwenyewe alisimamia msimamo wake thabiti kabisa kwamba anataka kulinda taswira chanya ya RPF kwenye jumuiya ya kimataifa na kuwaonyesha kuwa RPF wako tayari pia kushughulikia migogoro kidiplomasia.


Lakini kipindi mazungumzo haya yanaendelea na makubaliani yanafikiwa, nyuma ya pazia Rais Juvenile Hibyarimana akishirikiana na serikali ya Ufaransa walikuwa wanaunganisha nguvu ya waunga mkono wao chini kwa chini ili kuipinga RPF. Katika mpango wao huu walienda mbali hata kiwajumuisha viongozi wa CDR.


Kadiri muda ulivyokuwa unaenda kukaanza kuibuka mkanganyiko. Kuna kundi la watu ndani ya MRND na CDR walitoa tamko kwamba hawakubaliani na jinsi ambavyo Ufaransa inajiingiza kwenye uratibu wa mkakati huo wa chini kwa chini. Waliona kama vile wanatwanga maji kwenye kinu. Yaani wanapambana kumuondoka "mkoloni mweusi" (watusi) na wakati huo huo viongozi wao wanaacha mwanya wa mkoloni mweupe kurudi (Ufaransa). Ndipo hapa kwa hasira wakaanza kushinikiza kwamba mkataba ulio sainiwa Arusha uheshimiwe.


Lakini pia bado walibakia lile kundi lenye msimamo ambalo walikuwa tayari lolote lifanyike (hata kama ikibidi kushirikiana na Ufaransa) kuhakikisha kwamba watusi wanaondoshwa ndani ya Rwanda.


Ndipo hapa kwenye kipindi hiki kulipamba moto vuguvugu la 'Hutu Power'.


Vyama vyote vya siasa ndani yake viligawanyika katika makundi mawili. Kulikuwa na kundi ambalo walikuwa na msimamo wa kati (moderate) ambao waliunga mkono mazungumzo ya Arusha. Alafu kulikuwa na kundi la wale wenye msimamo mkali, ndio hawa waliitwa 'Power Wing' (Hutu Power). Hawa wao walikuwa tayari kufanya lolote na kwa gharama yoyote ile kuhakikisha kwamba watusi hawawi sehemu ya uongozi wa nchi na hawaishi Rwanda kama raia mwingine.


Hiki ndicho ambacho kilitokea kwenye vyama vyote vya siasa nchini Rwanda katika kipindi hiki. Kila chama kilikuwa na hizi 'two wings'. Lakini wing ambayo ilikuwa na nguvu na ushawishi kwenye kila chama ilikuwa ni 'Hutu Power'.




61cdcbc6276b6bb0e155365264282c61.jpg

Rais Juvenile Habyarimana na ujumbe wake kwenye mkutano Arusha



Hapa nchini kwetu Tanzania katika vyama vya siasa kwa miaka mingi tumekuwa na kasumba katika vyama vyetu vya siasa kwa kila chama kuwa na kikundi cha "ulinzi" cha chama. Pengine kuna walianzisha utaratibu huj walikuwa na sababu za msingi mpaka leo hii kuwa na 'Green Guard' ndani ya Chama Cha Mapinduzi na 'Red Brigade' ndani ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo. Lakini kama tungekuwa tunaijua historia na kutumia mafunzo yake kujisahihisha si dhani kama tungelikumbatia kasumba hii ya vikundi vya ulinzi.





Kuibuka kwa Intarehamwe na Impuzamugambi


Intarahamwe na Impuzamugambi vilianza kama vikundi vya ulinzi katika vyama vya MRND na CDR kama ambavyo hapa kwetu Taznania tuna Green Guard na Red Brigade ndani ya CCM na Chadema.



Interahamwe

Maana halisi ya neno hilo ni "wanaopambana pamoja". Ni muunganiko wa maneno mawili ya kihutu, 'intera' ambayo ina maanisha 'kazi' na 'hamwe' ikimaanisha pamoja. Kwa nini sijasema "wanaofanyakazi pamoja" na badala yake nimesema "wanaopambana pamoja".

Hili neno 'kazi' (work) lilikuwa linatumika kama kauli mbiu katika radio za kibaguzi za kihutu wakimaanisha 'shughuli ya mauaji' kwa kutumia panga. Kwa hiyo lengo lao la kuchaganya neno hili halikiwa kwa ajili ya kumaanisha kazi ya uzalishaji bali ni kazi ya mauaji.


Kikundi hiki cha kihutu kilikuwa chini ya chama cha siasa cha MRND.

Ajabu ni kwamba kiongozi wa Kitaifa alikuwa ni muhutu aliyeitwa Robert Kajuga. Kajuga familia yake ilikuwa ni ya Kitusi lakini baba yake alifanikiwa kupata nyaraka za kiserikali ambazo ziliipa utambulisho familia yake yote kama wahutu. Kajuga mwenyewe alikuwa anafanya kazi kubwa sana kuficha ukweli wa mizizi ya familia yake ya Kitusi. Moja ya visa ambavyo vinasisimua sana ni namna ambavyo Kajuga alijitahidi kuificha familia yake Hôtel des Mille Collines ndani ya Kigaki kipindi mauaji yalipoanza. Tutakirejea kisa hiki hapo baadae.




Impuzamugambi

Kikundi hiki nacho pia cha kihutu kilikuwa chini ya chama cha CDR. Japokuwa hakikuwa kikubwa au maarufu kama Interahamwe lakini vyote viliwi vilikuwa na lengo moja linalofanana.


Makamanda wa kikundi hiki walikuwa ni viongozi wakuu wa chama cha CDR, yaani Hassan Ngeze na Jean Bosco Barayagwiza.


Kipindi mauaji ya kimbari yalipoanza kikundi hiki kilifanya kazi bega kwa bega na Iterahamwe kama ambavyo tutaona hapo mbele kidogo.




Vikundi vyote hivi viwili vilijizolea umaarufu mkubwa ndani ya Rwanda na vijana wengi wa Kihutu waliojitafsiri kama 'wazalendo' wa nchi yao walijiunga navyo.


Wahutu wenye msimamo mkali ndani ya vyombo vya usalama ambao walikuwa na nyadhifa za juu kama vile mkui wa jeshi la polisi na mnadhimu mkuu wa jeshi la Rwanda walianza kuweka utaratibu ambapo wanachama wa vikundi hivi walikuwa wanapatiwa mafunzo ya awali ya kijeshi.

Kwa hiyo ndani ya muda mfupi sana vikundi hivi nguvu yake na ushawishi wake ukawa mkubwa kuzidi hata namna ambavyo watu walitegemea.


Japokuwa alikaa kimya na kufumbia macho lakini hii haikuwa dalili nzuri kwa uongozi wa Rais Habyarimana. Kwa sababu aliona fukuto ambalo lilikuwepo chini kwa chini. Kwamba kadiri ambavyo alikuwa anaviacha vikundi hivyo vikue na kuwa na nguvu zaidi, siku vikilipuka kwa ghasia kubwa nchi hiyo haitakuwa salama tena. Na si kama alijali zaidi usalama wa nchi bali aliogopa zaidi kupoteza madaraka kutokana na presha ambayo atapewa na jumuiya ya Kimataifa.



75d6e0719bd6a12cc9295f839286864c.jpg

7b98de27f56aee8b8751b4960c25afa5.jpg

7b4a1b9e2e0f3b952342c62aaa43a5a9.jpg

Wanachama wa Interahamwe na Impuzamugambi




Lakini pia nilieleza huko nyuma kwamba vuguvugu hili la Hutu Power lilikuwa linaratibiwa na 'inner cirlce' ya Akazu ambayo ilikuwa inafahamika kama 'le clan de madame'.

Hawa walikuwa ni maswahiba na ndugu wa karibu kabisa wa Agathe Hibyarimana, mkewe Rais.


Kwa upande mwingine pia kitendo cha Rais Hibyarimana kuendelea na mzungumzo ya Arusha kulikuwa kunazidi kuwachukiza wahutu wenye msimamo mkali na Habyarimana alihisi kabisa hasira hizi zinaweza kufikia kilele cha wahutu hao wakamuondoa madarakani kwa nguvu.


Hivyo basi Habyarimana tegemeo lake pekee katika kipindi hiki cha sintofahamu kubwa lilikuwa ni jumuiya ya kimataifa na RPF.


Habyarimana alikata shauri sasa kuingia kwa miguu yote miwili kwenye mazungumzo ta Arusha. Lengo lake lilikuwa ni kwanza kupata huruma na kuaminika na jamii ya kimataifa na pili aliamini kuwa kama RPF wangekuwa sehemu ya uongozi wa nchi basi ilikuwa ni njia nzuri ya kuwadhibiti wahutu wenye msimamo mkalai.


Safari hii kwenye mazungumzo alikubaliana karibia na kila sharti la RPF. Kwa mfano alikubali 40% ya jeshi jipya la nchi ambalo litaundwa liwe na wanajeshi wa RPF. Alikubali pia uongozi wa juu wa jeshi 50% wawe ni RPF na masuala mengine mengi zaidi ambayo yalikuwa ni ushindi mkubwa kwa Kagame na RPF.

Mkataba wa makubaliano haya ulisainiwa tarehe 4 August 1993.


Pia waliweka makubaliano kwamba katika kipindi hiki cha mpito lazima amani ya nchi isimamiwe na jeshi la kimataifa ili kuepuka upande wowote, wa serikali au RPF kutumia mwanya huo vibaya kujiongezea madaraka au ushaiwishi.

Ndipo hapa mwezi octoba jeshi maalumu la Umoja wa Mataifa vikosi vilivyopewa jina la UNAMIR (United Nations Assistance Mission for Rwanda) likiongozwa na Jenerali Roméo Dallaire raia wa Canada liliingia nchini Rwanda kwa ajili ya kulinda amani.


Kipengele kingine ambacho Kagame alikitaka kilikuwa ni kutaka uwakilishi wa RPF ndani ya Bunge la Rwanda katika kipindi hiki cha mpito.


Bunge la Rwanda muundo wake uko hivi; kuna 'Uper Chamber' (au Sena kwa kinyarwanda (senate kwa umombo ) na kuna 'Lower Chamber' (au Umutwe w'Abadepite (chamber of deputies kwa umombo).

Muundo na mfumo wa ufanyaji kazi wa Chamber hizi mbili ni kama vile Congress ya Marekani (House of Representatives na Senate).


Rais Hibyarimana alikubali kutoa nafasi za uwakilishi kwa RPF katika Chamber of Deputies.


Uhalisia ni kwamba Kagame hakuwa na haja sana na nafasi hizo za uwakilishi bali alikuwa ametumia akili ya mbali sana ambayo kwa kipindi hiki hawakumshitukia.

Kagame aliwaeleza kwamba, wanadiplomasia wake hao ambao wataiwakilisha RPF kwenye Bunge ni lazima wapewe ulinzi na wanajeshi wake wa RPF na si jeshi la serikali au UNAMIR ya umoja wa mataifa. Na alipendekeza kwamba itawapasa RPF kuingiza wanajeshi 1000 kwenye mji mkuu wa Kigali kwa ajili ya ulinzi wa wanadiplomasia wao.


Mwezi December 1993, kupitia mpango wa vikosi vya umoja wa Mataifa vya UNAMIR uliokuwa unaitwa 'operation Clean Corridor', wanajeshi 1000 wa weledi (special forces) kutoka RPF ya Kagame waliruhusiwa kuingia kwenye mji mkuu wa Kigali na kuweka makazi yao kwenye majengo ya Bunge.


Hii ndio moja ya akili adhimu ambayo Kagame amejaaliwa (psychological warfare)… alikuwa amefanikiwa kuingiza special forces wake elfu moja ndani ya Kigali tena kwa ruhusa ya serikali bila kumwaga hata tone la damu au kufyatua hata risasi moja.

Wanajeshi hawa 1000 aliowaingiza ndani ya Kigali walikuja kuwa nguzo ya ushindi wake dhidi ya wahutu na kuingia madarakani kama ambavyo tutaona hapo mbeleni.



Wahutu wenye msimamo mkali hili lilikuwa ni tishio kubwa sana kwao. Waliona kila dalili ya 'adui' yao kurejea kwenye kiti cha enzi.


Mbaya zaidi, nchini Burundi ambako nako kwa miongo mingi serikali ilikuwa inaendeshwa na Watusi mwezi october kwa mara ya kwanza wananchi walimchagua Melchior Ndadaye kuwa rais wa kwanza wa Burundi mwenye asili ya Kihutu.

Ndadaye alikuwa ni msomi na mwanazuoni, mtu wa fikra pevu. Huyu hakuwa mtu wa itikadi ya 'Hutu Power' bali alikuwa amelenga kumaliza utengano wa kikabila ndani ya Burundi.



Alitaka nchi hiyo iongozwe kwa pamoja. Akaanza kufanya mabadiliko kwenye jeshi ambalo lilitawaliwa na watusi pekee na kuanza kuwajumuisha wahutu.


Wanasema kwamba uking'atwa na nyoka hata ukikanyaga jani unashituka, ndicho ambacho watusi wa Burundi kilichiwashitua. Japokuwa Ndadaye alikuwa najaribu kuiunganisha nchi lakini watusi wa Burindi walimuona kama tishio na anataka kuwaletea maswahibu kama yale ambayo yanatokea Rwanda.


Kwa hiyo wanajeshi wa Kitusi wenye msimamo mkali walimtandika risasi Rais Melchoir Ndadaye mwishoni mwa mwezi octoba na kuzua vita kubwa ya kikabila nchini Burundi.



Wahutu wa nchini Rwanda walitumia kitendo cha muhutu mwenzao kupigwa risasi nchini Burundi kuhalalisha propaganda yao ya siku nyingi kwamba Watusi kamwe hawawezi kukubali kutawaliwa na Wahutu na watafanya chochote wawezacho ili kuitawala Rwanda na kuwafanya wahutu raia wa daraja la pili.


Propaganda hii safari hii ilikuwa na msisimko kwa wapokeaji huko mtaani hasa baada ya kushuhudia Kagame ameingiza wanadiplomasia wake ndani ya Bunge la Rwanda na wanajeshi elfu moja wa RPF ndani ya Kigali.


Kwenye jumuiya ya kimataifa Kagame na Habyarimana walikuwa wanapongezwa kwa hatua hiyo ya makubaliano. Lakini mtaani ilikuwa kana kwamba petroli imemwagwa ardhini na njiti ya kiberiti imeshikwa kiganjani tayari kufanya mlipuko.


Habyarimana alijua. Na Kagame alijua. Kwamba wakati ulikuwa uko karibu. Wakati ambao hakuna mtu aliombea ifikie. Wakati ambao utautikisa ulimwengu kwa mauaji ambayo hayajawahi kushuhudiwa kwenye historia ya karibu. Wakati wa jino kwa jino, msumari kwa msumari… wakati wa panga na shingo za watu.


e882b6735139b877adae8bf71fd98953.jpg

Rais wa zamani wa Burundi marehemu Melchoir Ndadaye


Nikirejea tutajadili kuuwawa kwa Rais Habyarimana na Kuanza kwa mauaji yenyewe ya Kimbari.



Stay here.



SEHEMU YA 12


0e55bff26bd918cdd108f425f45b9876.jpg


KUUWAWA KWA RAIS JUVENILE HIBYARIMANA NA KUANZA KWA MAUAJI YA KIMBARI


Moja kati ya visa vyenye utata zaidi kwenye historia ya Africa basi ni tukio la mauaji ya Rais Juvenile Habyarimana.

Na utata huu unakuwa mkubwa zaidi kutokana na hata jumuiya ya Umoja wa Mataifa kuficha ficha mno na kukwepa kulijadili suala hili kwa uwazi.


Lakini utata huu unakuwa mkubwa zaidi kutokana na kuwa na zaidi ya makundi matatu ambayo yote yalikuwa na dhamira ya kuona Rais Habyarimana anaondoka madarakani kwa maslahi yao.


Kundi la kwanza lilikuwa ni 'Hutu Power', wahutu wenye itikadi kali dhidi ya Watusi. Hawa katika kipindi hiki walikuwa wamechukizwa mno na kitendo cha Rais Habyarimana kujiingiza kwa nguvu zote kwenye mazungumzo ya amani na RPF jijini Arusha. Katika kipindi hiki walikuwa wanamuona kama ni kikwazo kwao kutimiza azma yao ya kuwa na Rwanda yenye idadi sifuri ya Watusi. Walikuwa wanamuona Rais Habyarimana kama daraja la ambalo linaleta tishio la 'adui' zao hao kurejea tena kwenye utawala wa nch na kurejesha tena 'Ufalme wa Watusi' na kuwafanya wahutu watumwa. Kwa hiyo moja kwa moja wahutu wenye msimamo mkali walikuwa na 'motive' ya kutaka kuona Rais Habyarimana hayupo.


Kundi la Pili ni RPF na Kagame mwenyewe. Hawa nia yao kuu ilikuwa ni kushika madaraka na pia kukomesha manyanyaso ya Watusi ndani ya Rwanda. Rais Habyarimana licha ya kukubali kurudi kwenye meza ya majadiliano lakini ilikuwa dhahiri kabisa kwamba ndani ya moyo wake hakuwa tayari kuachia madaraka. Lakini pia Kagame alimuona Habyarimana si kama mtu mwenye uwezo wa kuwadhibiti Wahutu wenzake wenye msimamo mkali waache kuendeleza mauaji ya watusi na pia hakumuona kama anatosha kwenye kuijenga upya Rwanda na kuwafanya Wahutu na Watusi wakubali kuishi pamoja. Kwa hiyo RPF na Kagame walikuwa na 'motive' pia ya kuona Rais Habyarimana hayupo.


Kundi la tatu hili huwa halizungumzwi kabisa na hata kwenye maandiko yote yanayoeleza utata wa kisa hiki huwa hawaligusii hili jambo. Lakini ni kundi muhimu sana ambalo nalo walikuwa na kila sababu ya kuona Rais Habyarimana hayupo. Kundi hili ni nchi za nje zenye maslahi ya moja kwa moja na Rwanda, ambazo Marekani, Ubelgiji na Ufaransa.

Hawa walikuwa na mslahi ya kijeshi, kidiplomasia na kihistoria. Na ni wazi licha ya kumsaidia sana Rais Habyarimana lakini ilifika kipindi waliuona ukweli kwamba Rais Habyarimana hakuwa na uwezo wa kuituliza Rwanda na kuiunganisha.


Makundi haya matatu kila moja lilikuwa na motive ya kutaka kuona Habyarimana hayupo. Na hii ndio sababu ya kwa nini kisa hili kimejawa na utata mkubwa sana. Unaweza kutengeneza nadharia ya kulituhumu kundi lolote lile kati ya haya.


Na ndio maana katika sehemu hii nimedhamiria kuandika maoni yangu binafsi kwa 100% namna ambavyo naliona suala hili. Si lazima sana kukubaliana na hiki nitakachoandika kwenye sehemu hii, lakini binafsi hiki ndicho ninachoamini kilitokea na tunaweza kutumia maoni haya kama kichocheo cha kuanzisha mjadala wa hoja kwa wale ambao wanaamini labda wahusika walikuwa ni kundi lingine.


(Unaweza kunitumia maoni yako inbox na nitayaweka hapa kwenye group).



Maoni yangu ni haya hapa;



Tuanzie mwanzo kabisa….


Hebu kwanza tuangalie tukio hili katika ujumla wake namna ambavyo lilitokea kabla hatujachambua dalili za wale waliohusika kwenye hili tukio.


c33ea941a59a21c52a370d901f5aaec0.jpg


Rais Habyarimana alikuwa kwenye ziara yake ya nchi za maziwa makuu ambayo aliianza tarehe 4 April mwaka 1994 (siku mbili kabla ya ndege yake kudunguliwa).

Ziara hii aliinza kwa kumtembelea swahiba wake mkubwa Rais za Zaire Jenerali Mobutu Sese Seko. Alikaa Zaire kwa muda wa siku mbili na kisha siku ya tarehe 6 April aliruka kuja Dar es Salaam, hapa Tanzania kwenye mkutano wa wakuu wa nchi ambao ulikuwa umeitishwa na mwenyeji wao Rais Ali Hassan Mwinyi.


Jioni ya siku hiyo baada ya mkutano huo wa wakuu wa nchi kuisha Rais Juvenile Hibyarimana aliamua kurejea nchini kwake Rwanda.

Rais mpya wa Burundi Mhe. Cyprien Ntaryamira ambaye alikuwa na miezi miwili tu tangu achaguliwe kuwa rais wa Burundi ambaye naye alikuwepo kwenye kikao cha Dar es Salaam aliomba 'lifti' kwenye ndege ya Rais Habyarimana. Rais Cyprien alipendelea apande ndege ya swahiba wake, muhutu mwenzake Habyarimana kutokana na ndege hiyo ya Habyarimana kuwa na kasi kubwa na ya kisasa zaidi.


Rais Habyarimana alikuwa anatumia ndege aina ya Dassault Falcon 50. Kwa kipindi kile cha mwanzoni mwa miaka ya tisini, ndege hizi zilikuwa ni moja ya ndege bora zaidi za daraja la kibiashara na hata matumizi ya kijeshi na ilikuwa inagharimu zaidi ya shilingi bilioni 45 za kitanzania kuinunua.

Ndege za Dassault Falcon 50 zilitengenezwa na kampuni ya Dassault Aviation kwa ajili ya wateja wao ambao walikuwa ni jeshi la anga la Ufaransa, Afrika ya Kusini, Ureno na Italia na zingali zinatumika mpaka leo hii.

Kwa hiyo waweza kupata picha ni kwa jinsi gani ndege hii ya Rais Habyarimana ilikuwa adhimu. Ndege hii Rais Habyarimana alipewa na serikali ya Ufaransa kama 'zawadi' na hata marubani ambao walikuwa wanamuendesha walikuwa ni raia wa Ufaransa.


Kwa hiyo jioni hii ya tarehe 6 April 1994 ndege iliruka kutoka uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (Kipindi kile ukiitwa Dar es Salaam International Airport) ndani yake ikiwa na watu kumi na mbili.


- Rais Juvenile Habyarimana

- Rais Cyprien Ntaryamira

- Bernard Ciza (Waziri wa Kazi wa Burundi)

- Cyraque Simbizi (Waziri wa Mawasiliano wa Burundi)

- Meja Jenerali Déogratias Nsambimana (Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Rwanda)

- Meja Thaddée Bagaragaza (Mpambe wa Rais Habyarimana)

- Kanali Elie Sagatwa (Kiongozi wa Baraza la kijeshi la Rais wa Rwanda)

- Juvénal Renaho (Mshauri wa Rais wa Rwanda kuhusu masuala ya Kimataifa)

- Dr. Emmanuel Akingeneye (Daktari wa Rais Habyarimana)

- Jacky Héraud (Rubani)

- Jean-Pierre Minaberry (Rubani)

- Jean-Micheo Perrine (Injinia wa ndege)


Hawa ndio watu wote ambao walikuwa ndani ya ndege ya Rais Habyarimana alipokuwa anarejea Kigali Rwanda.



Majira ya kama saa mbili na dakika ishirini hivi usiku ndege ya Rais Habyarimana ilikuwa iko juu ya anga la uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kigali ikizunguka kabla ya kufanya 'final approach'.


Lakini katika muda huu huu pia angani kulikuwa na ndege ya kijeshi aina ya C-130 Hercules ambayo ilikuwa inamilikiwa na jeshi la ubelgiji ikiwa imebeba wanajeshi sehemu ya vikosi vya UNAMIR ambao waliokuwa wanarejea kutoka likizo nchini kwao.

Ndege hii iliamuliwa kubakia angani kwanza wapishe ndege ya rais kutua.


56c47ff6044e5a3012557dbdeed25f15.jpg

8cd6ebf5c48c152e15cbbde7e98af814.jpg

Dassault Falcon 50


Ndege ya rais ilipata ruhusa kutua na ikaanza kufanya final approach. Lakini ikiwa kwenye 'approach slope' (inateremka kutoka angani ili kutua) ghafla ilishuhudiwa kitu kama moto kutoka ardhini ukipanda kwa kasi kubwa kuelekea juu usawa ule ule wa ndege inavyoshuka kutua. Lilikuwa ni bomu, "surface-to-air missile".


Bomu hili la kwanza lilipiga bawa la moja la ndege. Kufumba na kufumbua bomu lingine lilirushwa na kuipata ndege mkiani.

Ndege ilianza kuwaka moto ikiwa bado huku huko juu angani na kupoteza muelekeo.


Makazi ya Rais, Ikulu ya Kanombe yalikuwa karibu kabisa na uwanja wa ndege wa Kigali. Ni kama 'pua na mdomo'… umbali wa kilomita mbili tu kutoka uwanja wa ndege na kufika kwenye Kasri la Rais Juvenaile Habyarimana. Ndege ilipopoteza uelekeo baada ya kuwaka moto angani ilienda kudondokea kwenye bustani ya Ikulu na kulipuka kwa moto.


Watu kadhaa walishuhudia tukio hili likitokea lakini wengi hawakujua hasa ni nini kilikuwa kimetokea na hata wale waliojua kuwa ilikuwa ni ndege imedondoka hakuna ambaye alikuwa na hakika ilikuwa ni ndege ya nani au imembeba nani.


Sintofahamu hii ilizua taharuki kubwa sana. Walinzi wa Rais ambao walikuwa uwanja wa ndege kumpokea Rais waliwaweka watu wote waliopo uwanja wa ndege chini ya ulinzi.

Pia kulikuwa na wanajeshi wa Ubelgiji kama sehemu ya vikosi vya UNAMIR ambao walikuwa wanalinda maeneo ya nje kuzunguka uwanja wa ndege walizungukwa nao pia na Kikosi hiki maalumu cha ulinzi wa Rais na kupokonywa silaha.

Ile ndege ya kijeshi ya Ubelgiji kule angani ilikatazwa kutua na kuamuriwa kwenda kutua jijini Nairobi nchini Kenya.


Kwenye kambi ya jeshi ya pale Kanombe, ilipigwa mbiu ya kijeshi kuashiria kwamba kambi imevamiwa na RPF. Wanajeshi wote walijikusanya na kuchukua silaha za kivita tayari kwa mapambano.

Kwenye viwanja vya parade kikosi maalumu cha makomando nacho tayari kilokuwa kimejikusanya majira ya saa tatu kamili usiku.


Maafisa wa juu wa jeshi wa hapo Kigali walipiga simu mpaka Wizara ya Ulinzi kwa waziri ili kuweza kupata maelezo yoyote yale kama yapo.

Bahati mbaya Waziri wa Ulinzi Augustin Bizimana alikuwa nje ya nchi. Afisa ambaye alipokea simu hiyo ya wanajeshi hakufanikiwa pia kumpata Kanali Théoneste Bagorosa ambaye alikuwa mkurugenzi wa Ofisi ya Waziri wa Ulinzi. Kanali Bagorosa alikuwa kwenye sherehe ya kuwapokea wanajeshi kutpka Bangladesh kama sehemu ya vikosi vya UNAMIR.


Kutokana na sintofahamu ya nini hasa kilikuwa kimetokea, katika mfumo wa mawasiliano ya jeshi kuliripotiwa kwamba ghala la silaha la UNAMIR la kigali lilikuwa limelipuka.

Taarifa hii ilimfikia kamanda wa vikosi vya UNAMIR, Jenerali Dallaire na akamuamuru kamanda wa wanajeshi wa UNAMIR waliopo mji wa kigali aliyeitwa Luc Marchal aende mpaka sehemu iliyotokea mlipuko na ili kuchunguza ni nini hasa kilikuwa kimetokea.


Sasa utata wote kuhusu tukio hili ambao tunao mpaka leo hii… 'mchezo mchafu' ulianza kufanyika hapa.


Wanajeshi wa UNAMIR waliotumwa na Jenerali Dallaire kwenda kuchunguza mlipuko unahusu nini (walikiwa wanajeshi wa ubelgiji) walikutana na kizuizi cha wanajeshi wa Rwanda umbali wa mita kadhaa kukaribia Ikulu ya Rais. Kinyume kabisa na sheria na protokali na maadili ya kijeshi, wanajeshi wa Rwanda waliwaweka chini ya Ulinzi wanajeshi hawa wa UNAMIR na kwenda kuwaweka kwenye uwanja wa ndege pamoja na wenzao wengine wale wa awali.


Ajabu ni kwamba dakika chache baadae wanajeshi wawili wa Ufaransa (wanajeshi wa Ufaransa hawakuwa sehemu ya UNAMIR) walifika eneo hili la Ikulu ndege ilipodondoka na kuchukua "flight data recorder" ambayo ilikiwa imeshapatikana na wanajeshi wa Rwanda wanaolinda hapo Ikulu. (Kifaa hii mpaka leo hii hakijulikani kilipelekwa wapi au kiko wapi).

Kisha jeshi la Ufaransa wakapiga simu kwa Jenerali Dallaire kamanda wa vikosi vyote vya UNAMIR nchini Rwanda kumuomba awaachie wao suala zima la kuchunguza mlipuko huo. Bila kusita sita au kujiuliza mara mbili, Jenerali Dallaire alikataa vikali na mzozo mkali ukatokea.


Dallaire kwa muda ambao alikuwa amekaa ndani ya Rwanda alokuwa ameng'amua dhamira ya majeshi ya Ufaransa nchini humo ilikuwa ni ovu kabisa na hivyo hakuwa na imani nao kabisa kabisa.


Wakiwa kwenye mabishano hayo ghafla Dallaire alipigiwa simu kutoka kwa Agathe Uwilingiyimana ambaye alikuwa ni Waziri Mkuu wa Rwanda kumweleza kwamba Mawaziri wake wote ambao wana msimamo mkali (Hutu Hardliners) hawapati kwenye mawasiliano ya simu na hajui waliko.


Tukumbuke kwamba mpaka muda huu hakuna ambaye alikuwa na hakika kwamba ile iliyodunguliwa ilikuwa ni ndege ya Rais Habyarimana.


Dallaire alimlalamikia pia Agathe Uwilingiyimana kwamba wanajeshi wanaolinda Ikulu wanawazuia kufanya kazi yao na wanahisi kuna kitu cha siri wanakifanya wao kwa kushirikiana na jeshi la Ufaransa.


Kwa kutambua kwamba kwa mujibu utaratibu wa mtiririko wa kimadaraka kama kweli aliyedunguliwa alikuwa ni Rais Habyarimana basi Agathe Uwilingiyimana ndiye anachukua madaraka. Hivyo alikiwa anahitaji ushauri wake wa nini hasa cha kufanya. Agathe alikata simu kwa madai kwamba anahitaji kwanza kupata uhakika wa nini kimetokea ndipo atajua nini kifanyike na atamjulisha kwa simu.


Dallaire alimshirikisha taarifa hii mkuu wa kitengo cha siasa cha UNAMIR aliyeitwa Jacquies-Roger Booh-Booh. Na Jacquise alimshauri wasubiri kwanza taarifa rasmi kutoka kwa waziri mkuh Agathe Uwilingiyimana.


845115bb67cfe39fe628e725c91349fa.jpg

Kanombe Presidential Palace


Alipomaliza tu kuongea na simu na Jacquice Dallaire alipokea simu kutoka kwa Ephrem Rwabalinda ambaye alikuwa ni mwakilishi wa serikali ya Rwanda kwenye vikosi vya UNAMIR na alimueleza kuwa anahitajika kwenye kikao. Alipomuuliza kikao cha nini? Alijibiwa kwamba ni kikao cha Kamati ya dharura ya jeshi.

Dallaire alishangaa maana mwenye mamlaka ya kuitisha kikao hiki kwa nchi ya Rwanda alikuwa ni mnadhimu mkuu wa jeshi ambaye alisafiri na Rais kwenda Tanzania.

Ephrem Rwabalinda alijibu kuwa kikao kimeitishwa na Kanali Théoneste Bagorosa. Ambaye anajulikana kwa msimamo wake mkali dhidi ya watusi.


Dallaire aling'amua haraka kwamba kuna kitu ambacho si cha kawaida kilikuwa kinaendelea na kwa namna suala hilo linavyokwenda, kulikuwa na mkono wa mataifa ya nje na hata RPF nyuma ya pazia.



Nitarudi kueleza...


SEHEMU YA 13




Mnamo majira ya kama saa nne kasoro usiku Waziri Mkuu Agathe Uwilingiyimana alimpigia simu Jenerali Dallaire kumjulisha kwamba kwa taarifa za uhakika kabisa alizo nazo ni kwamna ndege iliyodunguliwa ilikuwa ni ya Rais Juvenile Habyarimana na Rais alikuwa ndani ya hiyo ndege.


Dallaire alipiga simu mpaka makao makuu ya UN nchini Marekani kuwajulisha kuhusu taarifa hii na kisha akaelekea kwenye kikao cha kamati ya dharura ya kijeshi iliyoitoshwa na Kanali Bagorosa.




Twende mbele kidogo….




Nadharia: 'nani alimfunga paka kengele'


Kumekuwa na ripoti nyingi mno mno kila moja ikijaribu kuchambua ni nani hasa walihusika kudungua ndege ya Rais Habyarimana.

Na kwa mfano tukisema tuchukue ripoti 100 juu ya kisa hiki… ripoti 50 kati ya hizo zitatuhumu Wahutu wenye msimamo mkali na ripoti 50 zitatuhumu Kagame na RPF.


Lakini kwa wale ambao wanaamini kwamba Wahutu wenye msimamo mkali walitekeleza tukio la kumuua Rais Juvenile Habyarimana hoja yao kuu ambayo wanaitumia ni juu ya ushahidi wa baadhi ya watu wanaodai walishuhudia tukio lile kwa macho.


Kwamba; kuna askari wa kibelgiji ambaye alikuwa juu kwenye moja ya mnara wa kuongozea ndege ambao ulikuwa hautumiki, na wanajeshi waliutumia kama sehemu ya kuweka askari wa ulinzi. Mwanajeshi huyu anadai kwamba wakati ndege ya Rais inafanya 'final approach' ili iweze kutua aliona kitu kama moto (surface-to-air missile) ikitoka ardhini na kwenda kudungua ndege. Sekunde kadhaa baadae aliona moto mwingine ukipamda juu na kwenda kuidungua tena ndege na kuidondosha ardhini kwenye eneo la Ikulu.


Mwanajeshi huyu alipoulizwa aeleze eneo ambalo bomu lilirushwa kutoka ardhini alieleza eneo ambalo liko karibu kabisa na Kanombe Barracks ambayo ni kambi ya kijeshi ya Jeshi la Rwanda.


Pia kuna mwanajeshi mwingine na raia nao wanatoa maelezo kama haya.


Sasa basi kama bomu lilirushwa kutoka eneo la Kanombe Barracks ambalo ni himaya ya jeshi la Rwanda (Maana yake ngome ya Wahutu) hii inawaondoa kabisa RPF kwenye lawama ya kuidungua ndege.


Hii ndio nadharia ambayo inatumika sana kwenye kuhusisha Wahutu wenye msimamo mkali na udunguji wa ndege ya Rais Habyarimana.


Hoja nyingine inayotumika sana ni kama ile ambayo nilieleza awali, kwamba katika kipindi hiki wahutu wenye msimamo mkali walikuwa wanamchukia mno Rais Habyarimana kwa kitendo chake cha kujiingiza kwa migui yote kwenye mazungumzo ya amani jijini Arusha.


Lakini nadharia hii ni ya ujumla mno na inaacha masuala muhimi sana. Uchunguzi wa kisa hiki haupaswi kutegemea ushahidi wa watu na kufikia hitimisho. Watu wanaweza kukaririshwa tu cha kusema na kupotosha.

Kisa hiki kinapaswa kuchunguzwa kitaalamu kwa ushahidi wa Ballistics, acoustics na masuala ya forensic. Ubaya ni kwamba Umoja wa Mataifa ni kama vile hawataki kabisa kulizungumza suala hili. Na serikali ya Rwanda ya sasa chini ya Paul Kagame msimamo wao ni kwamba wahusika wa tukio lile walikuwa ni wahutu wenye msimamo mkali, na serikali haitaki mjadala wowote wala uchunguzi wowoye zaidi.


Pengine nia yao ni njema… hawataki kufukua makaburi ambayo yanaweza kutonesha vidonda na kuiweka nchi yao katika hali tete au kuwarudisha tena kwenye misuguano na chuki za kikabila.


Lakini japokuwa labda suala hili halitakiwi kuguswa kwa sababu za msingi kabisa… lakini wanadamu tumeumbwa na 'curiosity'.! Kiu ya kutaka kujua… na kiu hii ni kama vile upele, mpaka pale utakapojikuna ndipo utaacha kuwasha. Binafsi nadhani suala hili lingeruhisiwa (au kutolewa majibu sahihi) tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000s pengine watu wangekuwa wamesha 'move on' na masuala mengine na kuacha kukuna vichwa juu ya nani hasa alihusika.


Sasa basi, binafsi naliona sula hili kama ifuatavyo;


fe3d143539e3534a19118a08dcb5634e.jpg

Jenerali Romeo Dallaire kamanda wa vikosi vya UNAMIR nchini Rwanda



Kwanza kabisa nionyeshe wasiwasi wangu juu ya hii nadharia kwamba Wahutu wenye msimamo mkali ndio walidungua ndege ya Raia Juvenal Habyarimana.


Kwanza kabisa mpaka sasa kwa chunguzi zote ambazo zimefanyika na ushahidi wa ballistics zinaonyesha kwamba bomu la 'surface-to-air' ambalo lilitumika kudungua ndege ya Rais Habyarimana na kuweza kuidondosha ilikuwa ni aina ya 'SA-16'. Bomu hili lenye uzito wa kilo 11 yalitengenezwa nchini Urusi.


Sasa mwanzoni mwa miaka ya tisini baada ya kuisha vita baridi Urusi waliuza silaha nyingi sana kwa nchi za Ulimwengu wa tatu. Moja wapo ya biashara hizi walifanya na jeshi la Uganda ambalo pamoja na silaha nyingine pia waliwauzi kiasi kikubwa cha mizinga ya SA-16.

Kwa upande wa jeshii la Rwanda halikuwa kununua au kuwa na mizinga aina ya SA-16. Watu pekee ambao walikuwa na uwezo wa kuwa na mizinga ya aina hii walikuwa ni RPF kutokana na uswahiba wao na jeshi la Uganda na Yoweri Museveni ambao waliuziwa mizinga hii na Urusi.


Hii ni suala la kwanza ambalo linafanya kidole kilichonyooshwa kugeukia RPF.



Lakini pia kuna masuala kadhaa ya kuyaangalia na kuyakumbuka tukiwa tunajadili na kujaribu kutegua kitendawili hiki… tuangalie masuala kadhaa haraka haraka.



Wakati wa kuundwa kwa kikosi cha UNAMIR kulitokea mabishano makali sana kwenye baraza la kudumu la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN Security Council) ambapo Marekani alikuwa anapingana na wajumbe wengine wote wa baraza kuhusu uwepo wa vikosi vya UNAMIR nchini Rwanda na akitaka viondolewe haraka. Hoja ambayo walikuwa wanaijenga ni ati kwamba hawataki kitokee kama kile ambacho kilitokea mwaka mmoja nyuma nchini Somalia katika "Battle of Mogadishu" ambayo ilizua mzozo mkubwa wa Kidoplomasia baada ya majeshi ya Marekani kuingila mzozo wa ndani wa nchi ya Somalia.

Hoja hii haikuwa na mashiko sana kutokana na utofauti mkubwa wa asili za oparesheni hizo. Ilikiwa dhahiri kwamba Marekani walikuwa na dhamira nyingine kabisa ambayo hawakuwa wakiisema.


Mwishoni wakafikia 'compromise' kwamba UNAMIR iongezewe muda wa miezi mitatu wakati baraza la Usalama likitafakari kama kuviondoa vikosi hivyo moja kwa moja au viendelee kubaki.

Hivi ndio namna ambavyo uwepo wa UNAMIR uliendelea na mpaka muda wa mauaji ya kimbari yalipoanza. Safari hii ilikuwa ni oparesheni ya muda mfupi na Marekani alipinga kwa nguvu zote na kukataa kuchangia askari.


Hili ni suala la kwanza ambalo nahitaji ulijue na ulikumbuke tunavyojadili suala hili.


Suala la pili ni kwamba katika moja ya nyaraka za siri ambazo zimekuwa 'declassified' na serikali ya Marekani na kuwekwa kwenye programu ya 'National Security Archives' kwenye chuo kikuu cha George Washington inaonyesha balozi wa Marekani nchini Rwanda kipindi hicho aliandika 'memo' kwenda kwa Waziri wa Ulinzi kuonyesha wasiwasi wake kwamba kuna uwezekano wa tukio la hatari kutokea na akasisitiza kama tukio hilo likitokea basi kuna uwezekano wa zaidi ya watu laki tano kuuwawa ndani ya Rwanda. (Sehemu ambazo tukio hilo balozi analitaja zimefutwa kwenye nyaraka).


Hii inathibitishwa pia na nyaraka nyingine za CIA zenye tarehe za mwanzoni kabisa mwa mwaka 1994 (January na February) zikionyesha kutabiri kutokea kwa vifo vya watu nusu milioni nchini Rwanda kutokana na uchambuzi wa mfululizo wa matukio ambao walifanya pamoja na intelijensia ambayo walikuwa nayo.


Kwa hiyo unaweza kuona kwamba Marekani alikuwa ana hakika kabisa kwamba kulikuwa kunaenda kutokea tukio kubwa ambalo litagharimu maisha ya zaidi ya nusu milioni wa raia wa Rwanda lakini ajabu halikuwa kwenye vikao vya baraza la Usalama wa Umoja wa Mataifa anapinga UNAMIR kuendelea kuwepo nchini Rwanda.


Hili ni jambo la pili ambalo nataka ulikimbuke tunapoangalia kutokea kwa tukio hili la ndege ya Rais Habyarimana kudunguliwa na hatimaye mauaji ya kimbari kuanza.


492b01a62e8a738136eacf4f60617080.jpg


Lakini pia trehe 22 January 1994, ndege ya mizigo aina ya DC-8 (wengine huziita McDonnell Douglas DC-8) ilitua kwenye uwanja wa ndege wa Kigali ikiwa imebeba shehena ya silaha kwa ajili ya jeshi la Rwanda.

Hii ilikiwa kinyume kabisa na mazungumzo ambayo yalikuwa yanaendelea Arusha ambapo kila upande (yaani RPF na Serikali) walitakiwa kuacha kununua silaha au kuongeza ukubwa wa jeshi.


Kuna mtu alimpenyezea taarifa hii Jenerali Dallaire kuhusu ndege hiyo iliyoleta shehena ya mizigo. Dallaire alichukua wanajeshi wake na kwenda mpaka uwanja wa ndege wa Kigali na kuiweka chini ya Ulinzi ile ndege kwa hoja kwamba kilichokuwa kinafanyika ilikuwa ni kinyume kabisa na Makubaliano ya Arusha (Arusha Accords).

Dallaire alituma telegram mpaka UN kuwataarifu kuhusu hiki kinachoendelea. Ajabu ni kwamba UN walimuamuru asijihusishe na chochote kile zaidi ya "kulinda amani". Yalitokea mabishano makubwa sana kati ya Dallaire na wakubwa wake.


UN walikuwa na hoja pengine ya msingi kwamba vikosi vya UNAMIR vilikuwa Rwanda kwa ajili ya kulinda amani na si kujihusisha moja kwa moja migogoro ya nchi ambayo ilikuwa inaendelea.

Lakini Dallaire alijenga hoja kwamba mitaani wanajeshi wa Rwanda walikuwa wameanzisha utaratibu wa kukagua vitambulisho vya raia ili kujua kama ni Muhutu au Mtusi. Aliwaeleza kwamba kuna jambo la hatari linapangwa na wanaweza kulizuia kabla halijatokea. Lakini UN (wakiongozwa na Marekani) waliweka msimamo kwamba hawampi ruhusa ya kukamata shehena hiyo.


Hili ni tukio lingine la nne ambalo tunahitaji tulifahamu na tulikumbuke.


Tuangalie suala lingine muhimu pia…


Kama ambavyo nimeeleza tangu mwanzo wa makala hii kwamba RPF iliundwa nchini Uganda kwa msaada mkubwa wa Jeshi la Uganda na Museveni kutokana na uswahiba wake na kushibana na Paul Kagame na Fred Gusa Rwigyema.


Suala hili la uundwaji wa RPF na msaada wa jeshi la Uganda lilikuwa linajulikana linajulikana vyema na CIA kupitia ofisi yao ya balozi jijini Kampala Uganda kama ambavyo inathibitidhwa na nyaraka ambazo CIA wameziachia kwenye National Security Archive chuo kikuu cha George Washington. Suala hili la uundwaji wa RPF na msaada wa jeshi la Uganda kwenye uundwaji wake ilikuwa kinyume kabisa na UN Charter pamoja na kanuni za Umoja wa Africa.


Lakini CIA hawakuwahi kusema lolote kuufungua macho ulimwengu kuhusu hiki ambacho kilikuwa kinaendelea kwa siri kubwa.


Badala yake kwenye mwanzoni mwa miaka ya tisini Marekani iliongeza kiwango cha misaada ya kiutu na misaada ya kijeshi maradufu kwa Uganda.


Jenerali Dallaire wa vikosi vya UNAMIR alianza kupata wasiwasi kwamba kuna uwezekano mkubwa wa jeshi Uganda walikuwa wanasaidia wapiganaji wa RPF kinyume na makubaliano ya Arusha, kanuni za Umoja wa Mataifa na UN Charter.


Mwanzoni Museveni alitoa tamko kwamba wanajeshi wote wa Uganda waliokwenda kupigana nchini Rwanda (RPF) hatowaruhusu kuvuka mpaka kurejea Uganda.

Hij ilikuwa ni geresha tu kwani Kagame na wapiganaji wake walikuwa wakivuka kwenda na kurudi mpaka wa Rwanda na Uganda kama watakavyo.


Kwa hiyo hata UN ilipomuamuru Museveni kutosaidia RPF licha ya Museveni kuahidi kwamba hawezi kufanya hivyo, Jenerali Dallaire alikuwa na kila sababu ya kuamini kwamba Uganda bado walikuwa wanasaidia RPF kwa siri.


Ndipo hapa akaomba ruhusa awe anakagua mpaka wa Uganda na Rwanda ili kuhakikisha kwamba hakuna silaha ambazo zilikuwa zinakatiza mpakani hapo kuingia Rwanda. UN walimruhusu. Lakini Uganda walitoa sharti kwamba kabla ya Dallaire na wanajeshi wake hawajaenda mpakani wanapaswa kutoa taarifa masaa 12 kabla ili wawapatie 'escort'.


9e6a5d51b0eab07a426486e8ca12043e.jpg


Dallaire alipinga vikali kwanza akisema kuwa hawahitaji 'escort' lakini pia ukaguzi huo unatakiwa kufanywa kwa 'suprise' kwani kama taarifa ikitolewa masaa kumi na mbili kabla kama kuna shughuli zozote za upitishaji silaha utafanyika haraka au kusitishwa kabla hawajaenda.

Mabishano yalikuwa makali na hatimaye Dallaire hakuwa na namna nyingine zaidi ya kukubaliana na sharti hilo la kutoa taarifa masaa kumi na mbili kabla hawajaenda kwenye uchunguzi.


Katika ushahidi wake ambao Dallaire aliutoa kwa Bunge la Congress nchini Marekani mwaka 2004 alisema kwamba, alipata taarifa pia juu ya uwepo wa ghala kubwa la silaha ambalo lilikuwa linatumiwa na Uganda kwa ajili ya wapiganaji wa RPF. Ghala hili lilikuwa kwenye mji wa Mbarara ambao huko kilomita 80 tu kutoka mpakani.

Dallaire alipotaka kufanya uchunguzi kwenye ghala hili jeshi la Uganda lilikataa katakata.


Masuala yote haya juu ya visanga hivi vya jeshi la Uganda na serikali yake pamoja na msaada wao wa siri wanautoa kwa RPF ulikuwa unajulikana na ofisi za ubalozi wa Marekani jijini Kampala na CIA pia walikuwa wanajua.


Lakini ajabu ni kwamba hawakuwahi kusema lolote na badala yake walizidisha ukaribu na nchi ya Uganda.


Mwanzoni mwa mwaka 1994 kilifanyika kitu cha ajabu na kushitua sana ambapo sasa tukitazama nyuma historia tunaweza kusema kwa hakika kabisa kulikuwa na maslahi yaliyowafanya Marekani kujihusisha kwa siri kubwa kwenye mgogoro wa Rwanda na hata kusaidia kwenye mchoro wa Kudunguliwa kwa ndege ya Rais Habyarimana.

Mwanzoni mwa mwaka 1994 nchi ya Uganda ilifanya manunuzi ya kihistoria ya silaha kutoka Marekani. Manunuzi haya yalikuwa yanazidi kwa mara kumi manunuzi yote ya silaha Uganda iliyofanya kwa Marekani kwa muda wa miaka arobaini iliyopita. Yaani kwamba ukijumlisha manunuzi ya silaha ya Uganda kutoka Marekani kwa muda wa miaka arobaini iliyopita, hayafikii yale yaliyofanyika mwanzoni mwa mwaka 1994 pekee na yanazidi mara kumi manunuzi ya nyuma ya miaka arobaini.

Kwa mwaka huo bajeti ya serikali ilikuwa 48% ya fedha yote ya bajeti ilienda kwenye jeshi huku 13% tu ikitengwa kwa ajili ya elimu na 5% kwa ajili ya Afya.


Kwa wachambuzi wa masuala ya jeshi hii ilikuwa ni dalili tosha kuashiria kwamba kuna maandalizi ya kitu fulani cha kijeshi yanafanyika.


Marekani na CIA walikuwa wanajua kila ambacho kilikuwa kinaendelea na japokuwa suala hili lilikuwa linavunja kanuni za kimataifa Marekani walikaa kimya.

Ni katika kipindi hiki pia ndipo ambapo Marekani waliongoza nchi nyingine kumpigia upatu rais Yoweri Museveni kuwa ni kiongozi bora na mfano wa kuigwa barani Afrika.


Tofauti na sasa ambapo Museveni anapigwa vita na mataifa ya magharibi, hii ilikuwa ni tofauti kabisa na mwanzoni mwa miaka ya tisini ambapo Museveni alipigwa upatu kama shujaa, mwanafalsafa na kiongozi wa kuigwa na wote Afika licha ya masuala yote ya siri yaliyikuwa yanaendelea nyuma ya pazia huki Marekani na CIA wakiyafahamu.


Mwishoni mwa mwezi March 1993… (wiki chache tu kabla ya ndege ya Rais Habyarimana kudunguliwa na Mauaji ya Kimabari kuanza), Rais Yoweri Museveni alisafiri kwenda Minneapolis, Marekani ambako alitunukiwa tuzo ya utumishi uliotukuka ya Hubert H. Humphrey na kisha kutunukiwa shahada ya heshima ya uzamivu (Honorary Doctarate) kutoka chuo kikuu cha Minnesota.


Dean chuoni hapo (ambaye ni afisa mstaafu wa World Bank) alimsifu Yoweri Museveni kama kiongozi mahiri ambaye ni tumaini kwa kurejea kwa demokrasia Afrika. Vyombo vya habari navyo vilimwagia sifa kede kede, kuna gazeti liliandika "Uganda is one of the few flickers of hope for the future of black Africa."

Gazeti maarufu la New York Times walimfananisha Museveni na Nelson Mandela. Huku jarida maarufu la TIME wakimuita Museveni kuwa ni "herdsman and philosopher….. and central Africa's intellectual compass."


Ilikuwa ni ajabu mno kuona utukufu huu ambao Musevi alikuwa anapewa na mataifa ya magharibi wakiongozwa na Marekani ukilinganisha na kile ambacho kilikuwa kikiendelea kwa siri huku Marekani na CIA wakijua.


Baada ya kutoka chuo Kikuu cha Minnesota, Yoweri Museveni alielekea White House ambako alifanya kikao cha faragha na Rais Bill Clinton pamoja na National Security Adviser aliyeitwa Anthony Lake. Rekodi za kuhusu walichoongea hazipo mpaka leo hij ikimaanisha kwamba bado ziko sealed, lakini kwa mfululizo huu wa matukio nilioeleza unaweza kukisia ni nini kiliongelewa.


MWISHO


0 comments:

Post a Comment

Blog