Search This Blog

Saturday 24 December 2022

KILIO CHA MIFEREJI YA DAMU IENDAYO ETHIOPIA - 2

   http://pseudepigraphas.blogspot.com/2020/06/kilio-cha-mifereji-ya-damu-iendayo_10.html

Simulizi :  Kilio Cha Mifereji Ya Damu Iendayo Ethiopia

Sehemu Ya Pili (2)



Kutokana ma nchi ya Rwanda kutotulia kwa muda wote huu, mwaka 1973 yalitokea mapinduzi nchini Rwanda ambayo yalimuondoa madarakani Rais Gregoire Kayibanda na PARMEHUTU yake na kumingiza madarakati Rais mpya Juvenal Habyarimana.




Kitu cha haraka sana ambacho ni cha kukumbukwa ambacho alikifanya Rais mpya Juvenal Habyarimana ni kuituliza Rwanda. Chini yake miaka hiyo ya 1970s nchi ilitulia kabisa. Machafuko ya mara kwa mara yaliyokuwa yanatokea kwenye utawala uliopita yalikoma. Hata Watusi ambao walikuwa kwenye kambi za ukimbizi Uganda, Congo na Tanzania walianza kurejea. Juvenal Hibyarimana alionekana kama malaika wa ukombozi aliyetumwa kutoka mbinguni. Nchi ilitulia tuliii.!!




Lakini hawakujua… hawakujua kwamba ndani ya miaka michache ijayo Hibyarimana anaweza kuwa ndoto yao mmbaya zaidi kuwahi kuiota. Hawakujua kwamba shetani wa damu alikuwa ametua ndani ya Rwanda.!




Nchi ilitulia kabisa, na kila mtu alikuwa na tumaini jipya. Hata jamii ya kimatifa ilianza kumpongeza Hibyarimana kwa kuituliza Rwanda.


Lakini ulikuwa ni kama moto wa pumba za mpunga. Juu unaweza kuiona inapendeza kufaa hata kucheza ‘cha ndimu’ juu yake lakini kumbe chini kuna moto unatokota. Ilikuwa ni kama vile bwawa lenye maji yaliyotulia tuli kabisa kiasi kwamba hata ukidondosha punje ya mchanga unaweza kusikia inavyodondoka, lakini maji yenye utulivu mkubwa kiasi hiki ndiyo ambayo siku zote yana ‘chunusi’ ndani yake!




Kama kungelikuwa na mtu mwenye pua zenye ufanisi zaidi… labda angeliweza kusikia harufu ya damu kwa mbali ikiinyemelea Rwanda…!




SEHEMU YA TATU




Rais mpya wa Rwanda Bw. Juvenal Habyarimana aliingia rasmi madarakani siku ya Tare 5 July mwaka 1973. Kabla ya hapo alikuwa ni Jenerali katika jeshi la Rwanda akishikilia cheo cha Mnadhimu Mkuu wa jeshi. Mapinduzi yaliyofanywa na Habyarimana kumuondoa madarakani Rais Gregoire Kayibanda hayakuwa mapinduzi ya kumwaga damu.




Mapinduzi haya yalipokelewa kwa shangwe na vifijo hasa maeneo ya mijini nchini Rwanda. Rais aliyepinduliwa, Bw. Kayibanda ilifika kipindi alianza kuchukiwa mno na wananchi kutokana na kushindwa kabisa kuituliza Rwanda na kuiletea maendeleo badala yake aliendeleza visasi dhihi ya Watusi. Hii ilisababisha Rwanda kutengwa na majiranio zake, hasa jirani yao muhimu zaidi, nchi ya Uganda ambayo ilikuwa na Watusi wengi wanaoishi nchini humo. Hii iliathiri hata maendeleo ya Kiuchumi ya Rwanda.




Hivyo basi kitendo cha Jererali Jevenal Habyarimana kumuondoa madarakani Rais Kayibanda kilipokelekwa kwa furaha na wananchi wengi na Habyarimana alionekana kama shujaa.




Japokuwa nimeeleza kuwa mapinduzi yaliyomuingiza madarakani Habyarimana hayakuwa ya umwagaji damu, lakini kati ya mwaka 1974 mpaka mwaka 1977 takribani watu hamsini na sita, hasa wale ambao walikuwa na nyadhifa za juu kwenye serikali iliyopita ya Kayibanda waliuwawa kwa maelekezo ya Habyarimana mwenyewe huku Rais aliyeondolewa madarakani Gregoire Kayibanda akifariki mwaka 1976 akiwa gerezani kwa sababu inayoelezwa ilitokana na kunyimwa chakula kwa muda mrefu.




Baada tu ya kuingia madarakani Habyarimana alivifuta vyama vyote vya siasa nchini humo akieleza kuwa hataki Rwanda iendekeze majibishano ya kisiasa kila siku badala ya “kuchapa kazi” na mara nyingine akituhumu vyama vya siasa kutumika na maadui wa Rwanda ili kuvuruga taifa. Mwanzoni wananchi karibia wote waliunga mkonmo msimamo wake huu. Lakini ajabu ni kwamba mwaka uliofuata baada ya kuingia madarakani, yaani mwaka 1975 Rais Juvenal Habyarimana aliunda chama chake cha siasa ambacho alikiita Mouvement Revolutionnaire National pour le Developpement (MRND) na kutangaza kwamba hicho ndicho kitakuwa chama pekee cha siasa nchin Rwanda.




Mwanzoni Habyarimana alipendwa na watu wa makundi karibia yote, yaani Wahutu na Watusi. Wahutu walimpenda kwa kuwa alikuwa ni Muhutu mwenzao na Watusi walimpenda kwa kuwa mwanzoni mwa uongozi wake baada ya kumpindua Kayibanda, alipiga marufuku sera ambazo mtangulizi wake alizitengeneza kwa ajili ya kuwapendelea Wahutu pekee. Watusi walifurahishwa sana na hatua hii. Kwa upande wa Wahutu wenzake japokuwa suala hili liliwaudhi lakini hapa mwanzoni walimvumilia na kuendelea kumuunga mkono kwa kuwa alikuwa ni mwenzao (Muhutu).




Kwa muda wote huu serikali ilikuwa chini ya jeshi, yaani hakukuwa na serikali ya kiraia. Jeshi ndilo lilikuwa serikali nay eye Habyarimana akiwa kiongozi mkuu wa nchi. Lakini kufika mwaka 1978 kulifanyika mabadiliko mengine ya kikatiba ambayo yalitaka kurejea kwa serikali ya kiraia. Kwa hiyo mwaka huo ukaitishwa “Uchaguzi Mkuu”. Haukuwa uchaguzi mkuu haswa kwa maana ya uchaguzi mkuu kama ambavyo unapaswa kuwa, kwa maana ulikuwa ni kiroja cha kuchekesha ambazo kilitoa taswira kwamba kuna harufu ya shari iliyo mbele.



Ni kwamba kwa kuwa vyama vyote vya siasa vilipigwa marufuku nchini humo, hivyo basi MRND, chama cha Juvenal Habyarimana ndicho chama pekee ambacho kilishiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huo 1978 kwa kusimamisha wagombea na katika nafasi ya Urais kulikuwa na mgombea mmoja tu, Juvenal Habyarimana.


Siku ya Desemba 24 mwaka huo 1978 matokeo ya uchaguzi yalitangazwa ambapo Habyarimana alishinda ‘kwa kishindo’ akipata 98.99% ya kura zote na kuapishwa kuwa Rais wa Rwanda kwa muhula wa miaka mitano. Uchaguzi uliofuata miaka mitano baadae, yaani mwaka 1983 kwa mara nyingine tena, MRND kikiwa chama pekee cha siasa killichoshiriki uchaguzi huo na katika nafasi ya Urais Juvenal Habyarimana akiwa mgombea pekee, alipata tena ‘ushindi wa kishindo’ ambapo siku ya Desemba 19 matokeo ya uchaguzi yalipotangazwa Habyarimana alipata ushindi wa 99.97% ya kura zote zilizopigwa. Kama hiyo haitoshi, miaka mingine mitanao tena baadae, yaani mwaka 1988 siku ya Desemba 19 matokeo yalitangazwa na kumpa tena Habyarimana ushindi wa 99.98% ya kura zote zilizopigwa huku MRND kikiwa chama pekee kilichoshiriki uchaguzi na Habyarimana akiwa mgombea peke wa nafasi ya Urais.


Watu wenye hekima na wanao ona mbali walianza kuhisi joto ambalo lilikuwa na dalili ya kurudi tena ndani ya Rwanda .


Habyarimana hakuishia hapo tu, bali pia wafuasi wake wallianzisha utaratibu wa kufundisha raia mitaani kwa lazima nyimbo na tungo zilizotungwa kwa ajili ya kumsifu Rais Habyarimana pamoja na staili za kucheza nyimbo hizo. Katika mikutano yake ya siasa raia wa Rwanda walitakiwa kuimba nyimbo hizi za kumsifu na kucheza kwa staili ya kufanana kama ambavyo walikuwa wamefundishwa.


Kwa kifupi Rais Juvenal Habyarimana aligeuka kutoka kuwa ‘malaika wa ukombozi’ ambaye Warwanda walihisi ameshushwa labda kutoka juu na bila kupindisha maneno Habyariamana sasa alikuwa ni Dikteta.


Udikteta wake ulikuwa ni udikteta haswa… sio udikteta uchwara! Ilikuwa ni ngumu kuchora mstari kati ya chama chake cha MRND na pia nghumu zaidi kuchora mstari wa ukubwa wa madaraka yake ndani ya chama tawala cha MRND. MRND ndio ilikuwa serikali na Habyarimana ndiye alikuwa MRND. Kwa hiyo yeye ndiye alilkuwa serikali na yeye ndiye alikuwa chama tawala.


Ofisi zote za serikali pia zilifanya kazi kama ofisi za MRND. Katika serikali za mitaa, ‘Maafisa Watendaji’ wa kata au vijiji au mitaa pia ndio walifanya kazi kama makatibu wa chama.


Kadiri ambavyo Habyarimana alikuwa anajivika utukufu na kukoleza makali yake ya udikteta ndivyo ambavyo hata watu wa kabila lake, Wahutu walianza kumchukia.


Kama dikteta mwingine yeyote yule duniani, naye akaanza kufanya makosa ya kipuuzi kabisa ya kimkakati. Ati ili kuwafurahisha watu wa kabila lake, Habyarimana taratibu akaanza kurejesha sera za mtangulizi wake ambazo zilikuwa zinawabagua Watusi. Kwa mfano kwenye udahili wa vyuo vikuu au ajira za serikali, walirejesha vipengele ambavyo moja kwa moja vilikuwa vinamnyima fursa Mtusi.


Hili lilikuwa ni kosa kubwa kwake kwani watu wa kabila lake tayari walikuwa ‘watembukiwa nyongo’, wengi walikuwa hawamtaki na hata Watusi ambao walikuwa wanamuunga mkono nao wakamchukia kutokana na kurejesha sera za kibaguzi. Kwa kifupi alikuwa anaenda kinyume na misingi na sababu ambazo alizitumia kuhalalisha mapinduzi yake mwaka 1973 na vitu ambavyo vilifanya Wahutu na Watusi kwa pamoja kumpenda.


Tofauti na ambavyo nchii ilitulia mara baada ya Habyarimana kumpindua Kayibanda, lakini kutokana na udikteta wake na kutokubalika tena kwa wananchi, ‘order’ ilianza kupotea mitaani na taratibu chuki za kikabila ambazo zilikuwa zinawafurukuta watu zikaanza kumea tena upya.


Lakini hapa ndipo ambapo msemo wa “kila mwanaume mwenye mafanikio nyuma yake kuna mwanamke imara” ulidhihirika.


Hapa nieleze kidogo japo kwa uchache lakini kwa mawanda…


Katika kipindi chote cha uongozi wa Rais Habyarimana kulikuwa na minong’ono kwamba maamuzi mengi sana yalikuwa yanafanyika kwa ushawishi wa mke wake aitwaye Agathe Kanziga Habyarimana. Minongono hii ilidhihirika ukweli wake katika kipindi hiki ambacho kiwango cha kukubalika cha Rais Habyarimana kilifikia chini kabisa nchini Rwanda.


Kwa kifupi ni kwamba; Agathe anatoka kwenye familia ambayo ukoo wao walikuwa ni watawala wa eneo la magharibi mwa Rwanda kwa miaka mingi sana sana. Mizizi na mataji wa kisiasa wa familia yake ndio ambao inasemekana kumsaidia kwa kiwango kikubwa Habyarimana kuingia madarakani na kukubalika japo alikuwa kiongozi wa kijeshi asiye na umahiri mkubwa wa medani za siasa.


Hivyo basi, pia katika kipindi hiki cha mumewe kutokukubalika na wananchi ndani ya Rwanda na hata viongozi wenzake wa kiserikali kuanza kumfitini, Agathe alichukua hatua ya kuhakikisha madaraka ya mumewe hayatetereki. Agathe akaunda makakti na kufanya uratibu wa weledi wa hali ya juu sana mpaka kuanzishwa kwa jumuiya ya siri (ilikuwa ya siri mwanzoni) ambayo ilijumuisha Wahutu wenye ushawishi mkubwa ndani ya Rwanda na wenye msimamo mkali dhidi ya Watusi. Jumuiya hii iliitwa ‘Akazu’.


Kwa hiyo Akazu iliundwa na ndugu wa Habyarimana ambao aliwajaza kwenye nyadhifa za juu serikalini, ndugu wa Agathe na marafiki zao wenye ushawishi mkubwa.



7ae01e8f546bce8847eb5319fa123fd6.jpg

Agathe Kanziga Hibyarimana


Lengo la jumuiya hii ilikuwa ni nini?


Akazu kama nilivyoeleza kuwa iliundwa na watu wenye ushawishi kwenye jamii ya Rwanda (hasa kwa Wahutu)lakini wote walikuwa ni Wahutu wenye msimamo mkali. Kama ambavyo wenyewe walijipambanua kwenye nyaraka zao za siri kwamba lengo la lilikuwa ni kuona “Rwanda with zero Tutsi” (Rwanda yenye Watusi sufuri). Hii ndio sababu ya muda mwingine mafungamano ya jumuiya hii kuitwa ‘zero networks’. Kiu yao kuu ilikuwa ni kuona ‘watesi’ wao wa kale, Watusi hawapo ndani ya ardhi ya Rwanda.


Sasa kwa nini Habyarimana afungamane na watu wa dizaini hii? Nimeeleza hapo awali kwamba ushawishi wa Habyariamana kwa wananchi ulidodorora kupitiliza. Pia kule mwanzoni kabisa nilieleza kwamba, Wahutu ni 84% ya Wanyarwanda wote. Kwa hiyo ili uweze kuitawala Rwanda ni vyema kuhakikisha kwamba unaishika mioyo ya Wahutu. Lakini Wahutu hawa tayari walikuwa wametumbukiwa nyongo dhidi ya Habyarimana… kwa hiyo mkewe alianzisha mafungamano haya na Wahutu hawa wenye ushaiwshi mkubwa japo wana misimamo mikali kwa lengo la kuiteka tena upya mioyo ya Wahutu. Pia watu hawa wa Akazu ilikuwa kwa faida kwao kufungamana na Rais Habyarimana ili kushawishi kutungwa kwa sera za kuwabagua Watusi.


Uwepo wa jumuiya hii ya Akazu san asana iliwasaidia Wahutu wenye msisimamo mikali kufanikisha sera zao na chuki yao dhidi ya Watusi lakini hakuwa na manufaa sana kwa Habyarimana kwani ushawishi wake uliendelea kudorora na kuambulia kuungwa mkono mtaani na Wahutu wenye misimamo mikali pekee huku sehemu kubwa ya jamii ya Rwanda ikiwa kinyume chake.


Nilieleza pia hapo mwanzo kuhusu vikundi vidogo vidogo vya waasi wa Kitusi walioko kwenye ukimbizi nchi za jirani na Rwanda vilivyokuwa vimebatizwa jina la ‘Inyezi’ (cockroaches (mende)) kufanya mashambulio ya mara kwa mara bila mafanikio yoyote. Lakini mwanzoni mwaka 1973 Habyarimana alipochukua nchi hali itulia kidogo na hata Inyezi walikuwa kimya. Lakini baada ya Habyarimana kukengeuka, tena kukengeuka kwa hali ya juu na mateso kwa watusi kurudi… Inyezi walianza tena mashambulizi yao.!!


Safari hii vikundiu hivi vilikuwa na dira madhubuti na thabiti zaidi. Walitaka kukomesha milele mateso dhidi ya Watusi nchini Rwanda.


Mfano mzuri wa Watusi hao ambao walikuwa wamejiapiza kukomesha mateso hayo ya ndugu zao nchini Rwanda walikuwa ni wale waliokuwa wanaishi uhamishoni nchini Uganda. Hawa walikuwa na dira madhubuti, weledi na morali ya kuwaokoa ndugu zao Watusi ndani ya Rwanda.


Pale Uganda kulikuwa na maelfu kadhaa ya Watusi ambao walikuwa na morari hiyo ya kukomesha mateso ya ndugu zao waliosalia Rwanda na kuondoa uongozi gandamizi na wa kidikteta. Lakini kati ya hawa maelfu wote, kulikuwa na Watusi wawili ambao walikuwa muhimu zaidi, walikuwa na morarli zaidi na weledi zaidi. Watusi hawa wawili naamini historia yao itabakia hata miaka mia tatu kutoka leo hii. Nawaongelea Paul Kagame na Fred Rwigyema.


Nafahamu wengi wamesimulia mengi kuhusu Mauaji ya Kimbari y Rwanda ya mwaka 1994, na hata makala hii ndilo lengo lake kuu kujadili tukio lile la kihistoria. Lakini tangu mwanzo nimeanzia mbali tangu kuanzishwa kwa Taifa la Rwanda karne kadhaa zilizopita nikiwa na lengo hasa la kuonyesha kiini cha mgogoro wa Wahutu na Watusi ni upi na walifikaje kwenye Kimbari ya mwaka 1994. Katika kujadili kwangu huku kiini cha mgogoro kabla sijajitosa miguu yote kuongelea mauaji yenyewe ya mwaka 1994, sitakuwa nimekata kiu kama sitawaongelea watu hawa wawili na chimbuko lao na kuibuka kuwa wakimbizi wenye ushawishi zaidi. Paul Kagame na Fred Rwigyema. Pia sitakuwa nimekata kiu kama sitochambua ni kwa namna gani Paul Kagame na Fred Rwigyema wakiwa bado ni “wakimbizi” nchni Uganda lakini waliweza kuiweka kiganjani mwao serikali ya Rais Yoweri Musseveni. Sitakuwa nimekata kiu kama sitaeleza ‘ufundi’ waliotumia mpaka kupata nyadhifa ndani ya baraza la mawaziri la Uganda wangali bado ni “wakimbizi”! lakini pia sitakuwa nimekata kiu kama sitoeleza namna ambavo waliunganisha Watusiu mia tano tu, na kuazisha harakati za kijeshi ambazo zilikuja kuling’oa madarakani jeshi la Kihutu lenye maelfu ya maafisa wa kijeshi na silaha za kisasa.


064687168479d4dc5b5eb996944d308e.jpg

Paul Kagame enzi hizo


2a5e2f7ac0f34ea8fd934ad90e7a3771.jpg

Fred Rwigyema


Kwa wanaokumbuka, nilipokuwa nachambua “Operation Entebbe” iliyofanywa na jeshi la Israel kuokoa raia wao walioshikiliwa mateka nchini Uganda kwenye uwanja wa ndege wa Entebbe, mwishoni mwa ile makala niliuliza swali, Kwamba oparesheni ile ilifanywa na jeshi la Israel mwaka 1976 ndani ya ardhi ya Uganda, baada ya hapo mahusianio ya Uganda na Israel yalidorora mno. Miaka miwili baadae ndipo sisi Tanzania majeshi yetu yalivamia Uganda na kumtoa Idd Ami madarakani nakukimbilia uhamishoni mpaka mwisho wa maisha yake. Nikauliza, je tunafahamu kuna uhusiano gani kati ya Operation Enntebbe ya Waisrael na Vita ya Kagera? Katika makala hii nitagusia kiduchu jawabu la swali hili. Lakini sitaishia hapo tu bali pia tutajadili ushiriki wa Paul Kagame na Fred Rwigyema kwenye vita ya Kagera.!! Yes, Vita ya KAgera…na si vita ya Kagera tu bali pia uhusika wao katika harakati za FRELIMO nchini msumbuji.! Natamani tuweze kufahamu kinagaubaga kabisa kuhusu mnyororo uliopelekea kukatikia kwenye mauaji yale ya 1994.



Lakini pia, tutajadili namna ambavyo Paul Kagame alifunzwa na kufundwa na Idara yetu ya Usalama wa Taifa (kabla ya kuanza kuitwa TISS) na hatimaye kuwa ‘Jasusi’ mbobezi wa daraja la kwanza vile ambavyo yuko sasa.!


Nimeeleza hapo juu kwamba, lengo kuu la makala hii ni kujadili mauaji ya Kimbari ya mwaka 1994 lakini nimeanzia mbali tangu historia ya Taifa la Rwanda kwa makusudi kabisa ili kuonyesha kiini cha tatizo. Kwa sababu mauaji ya 1994 ni “Matokeo” ya tatizo kubwa la muda mrefu lenye mzizi ya karne kadhaa nyuma ambayo mizizi hiyo ilikuja kumea mwaka 1994. Kwa hiyo kabla siajajadili tukio lenyewe la 1994 nataka tufahamu mnyororo wa matukio muhimu niliyoyaeleza hapo juu kwamba kiu haitakata kama sitayajadili. Lakini pia kuna msululu wa wahusika na matukio ambayo vitabu vya historia kwa makusudi au kwa kutokuwa na uelewa nayo hayasemwi (naamini hayasemwi kwa makusudi kabisa).


Katika sehemu ya nne, nitajadili, nitachambua na kuelezea wahusika, mfululizo wa matukio na yale ambayo yalitokea ‘nyuma ya pazia’ mpaka kufikia mauaji ya Kimbari ya mwaka 1994 yaliyogharimu maisha ya watu karibia milioni moja ambayo damu yake mpaka leo hii bado inalia kwenye ardh ya Rwanda na nyingine ikiendelea kutiririka kwenye mifereji ambayo wauaji wao walisema “mifereji iendayo Ethiopia.!”



Itaendelea…



SEHMU YA NNE





Kabla ya mvua ni mawingu.! Je, kabla ya mawingu ni nini?


JUA KALI…


Katika mapambano yoyote yale mara nyingi ili kufikia lengo unapaswa kufanya mambo ya mzunguko mno kana kwamba unatoka nje ya lengo hilo lakini hatimaye uje kutimiza lengo hilo hilo.


Nitaomba kunena kwa mifano ya uhalisia…


Nimekuwa nikieleza mara kadhaa kwamba nimesoma masomo ya bibilia darasani kwa muda wa miaka sita. Nakumbuka nikiwa kijana wa sekondari mwalimu wangu wa somo la ‘Divinity’ tuliwahi kujadili nae sana kuhusu kisa cha wana wa Israel kutoka Misri kwenda Kanani. Mimi na wanafunzi wenzangu kwenye mjadala huo tulikuwa tunauliza ni kwa nini wana wa Israel watumie miaka arobaini kusafiri kutoka Misri kwenda Kanani wakati kiuhalisia kwa mwendo wa kutembea kwa miguu hata sasa kama utatembea utatumia kama siku tatu tu hivi kama utapita njia sahihi ambayo imekuwa inatumiwa na watu tangu mwanzoni mwa kizazi agano jipya (miaka ya 300 B.C na kuendelea mpaka sasa).


Tulilikoleza swali letu zaidi kwa kuongeza hoja ya kwamba wana wa Israel kama ambavyo tunasoma kwenye vitabu vitakatifu ni kwamba, katika safari yao hii mbele yao, juu angani kulikuwa na kama wingu au muda mwingine nguzo ya moto ambayo iliwa inawaongoza njia ya kupita. Tulijenga hoja kwamba nguzo hii ya moto na hilo wingu wingu lilikuwa lina wamiss lead kufuata muelekeo na njia ambayo siyo sahihi n hiki ndicho kiliwafanya wazunguke jangwani kwa miaka takribani arobaini ambapo kiuhalisia walipaswa kutumia siku tatu tu.


Tulijenga hoja kwamba, kama ambavyo tunasioma kwenye bibilia, yafaa kusema kwamba nguzo hiyo ya moto na wingu hilo vilikuwa ni vitu vya kimiujiza kutoka kwa Mwenyezi Mungu mwenyewe, sasa kwa nini Mwenyezi Mungu awaongoze watu wake kwenye njia ambayo si sahihi? Kutokana na ukaribui wa Misri na Israel hii ina maana kwamba kwa muda wa miaka arobaini ambayo wana wa Israel walikuwa wanarandaranda jangwani, ‘they were moving in circles’… walikuwa wanazunguruka milima tu kufuata wingu na nguzo ya moto. Yaani wanaweza wakapiata sehemu ‘A’ alafu mwakani wakapita tena pale pale bila kujua. Walikuwa hawaendi mbele, walikuwa wanazunguruka tu milima na majangwa. Tukauliza, kwa nini Mwenyezi Mungu awafanye namna hii ‘wateule’ hawa?


Mwalimu wetu huyu, nguli wa theolojia na masula ya ‘Uungu’ alitupatia majawabu kadhaa ambayo mengine yalikuwa yanatokana na tafasiri za kimantiki na mengine kutokana na tafasiri za kitheolojia. Mfano, alitueleza kwamba Mwenyezi Mungu hakutaka kizazi kilichotoka Misri kiingie kanani na badala yake alitaka watoto wao tu ndio waingie kanani. Kwa hiyo kwa miaka arobaini ile kizazi kile kilichotoka kanani chote kilipotea na kuibuka kizazi kipya cha watoto ambao walilzaliwa ndani ya miaka hiyo arobaini. Lakini pia alitueleza kwamba Mwenyezi Mungu alikuwa anataka kuwaonyesha wana wa Israel ukuu wake na miujiza yake… ndipo hapa alitupa mifano ya Mana kudondoka kutoka mbinguni, makundi ya ndege aina ya kware kudondoka ili Waisrael wachinje na kula baada ya kulalama kuwa wameikosa sana nyama… na mifano mingine mingi.


Mfalme Mutara III ambaye ana undugu wa kihistoria na baba yake Kagame, Mr. Geogratias


Lakini binafsi yangui jawabu ambalo lilinikosha zaidi lilikuwa ni nadharia aliyotupa mwanatheolojia huyu pamoja na mstari kwen ye biblia uliosema kuwa “..,nataka kuifundisha mikono yako kupigana vita..”


Kwamba Mwenyezi Mungu alikuwa anataka kuwafundisha Waisrael namna ya kupambana vita kabla hawajaingia kanani. Kwa hiyo kwa miaka hiyo arobaini waliyokuwa wanarandaranda jangwani walikutana na misuko suko mingi ya mapambano ya kivita ambayo iliwafanya wawe bora katika medani hizo za kivita. Hii ilikuja kuwasaidia pia pindi walipoingia Kanani ambako walikuta kuna taifa la watu ambao wanaishi hapo na walikuwa hodari kweli kweli katika vita. Mojawapo ya wapelelezi waliotumwa na Musa kwenda kuipeleleza kanani na wakazi wake, alieleza kuwa watu hao ni wenye miraba minne na hodari kweli kweli mpaka alifikia hatua ya kusema “…sisi ni kama panzi tu mbele yao..”


Lakini uzoefu wa miaka arobaini ya mapambano ya vita uliwawezesga Israel kuivamia kanani na kuua wakazi wake wote na kuifanya nchi yao, nchi yao ya ahadi, nchi yao ya maziwa na asali. Jawabu hili la mwanatheolojia yule ndilo ambalo lilinikosha zaidi.


Kwa nini nimeeleza haya yote…


Katika sehemu iliyopita nilieleza kuhusu vikundi vidogo vidogo vya wapiganaji wa kitusi waliopo kwenye kambi za wakimbizi ambavyo viliitwa ‘Inyezi’. Vikundi hivi mara kwa mara vilikuwa vinavamia Rwanda kwa majaribio ya kuipindua serikali lakini bila mafanikio yoyote kwa muda wa zaidi ya miaka thelathini.


Licha ya nia ‘njema’ ya vikundi hivi kutaka kuipindua serikali lakini katika picha kubwa zaidi vilikuwa vinaongeza tu mateso kwa Watusi wenzao ambao bado walikuwa wamebakia nchini Rwanda. Kwa sababu kila jaribio la mapinduzi lilipokuwa likifanywa na vikundi hivi vya Inyezi, serikali ya Rwanda yenye mlengo wa Kihutu iliwatia jela watusi waliopmo ndani ya nchi na kuua mamia wengine kwa lengo la kutuma ujumbe kwa Watusi wengine kwamba wanatakiwa ‘kuwa wapole’. Wasilete fyokofyoko zozote.


Lakini mateso ya Watusi yalipoongezeka chini ya Rais Juvenal Habyarimana, kulikuwa na ulazima wa jambo fulani kufanyika. Lakini wapo Watusi wenye kuona kwa jicho la tatu ambao walijua kabisa kwaba jambo hilo haliwezi kufanikishwa na vikundi vya Inyezi kutoka kwenye kambi za ukimbizi. Walifahamu fika kwamba jambo hilo linapaswa kuwa la kimkakati na utekelezaji wa weledi wa hali ya juu kabisa. Wanahitaji ‘kutoka nje ya lengo ili kutimiza lengo’. Wanahitaji ‘kurandaranda jangwani kwa miaka arobaini kabla ya kuingia kanani’. Wanahitaji kupotea jangwani ili wafike nyumbani.


Watusi hawa ambao walipata ‘maono’ haya niliwaeleza katika sehemu iliyopita, walikuwa ni Fred Rwigyema na Paul Kagame.


Nitaeleza nadharia hii ya krandaranda jangwani kwa miaka arobaini inashabihiana vipi na kilichofanywa na Kagame na mwenzake Rwigyema… lakini kabla hatujaenda huko nhebu tuwafahamu japo kwa uchache… paul Kgame na Fred Rwigyema ni akina nani?




Fred Gisa Rwigyema


Alipozaliwa jina ambalo alipewa na wazazi wake aliitwa Emmanuel Gisa, alizaliwa tarahe 10 April mwaka 1957 kijijini Mukiranza katika eneo maarufu la Gitamara kusini mwa Rwanda. Katika machafuko ya mwaka 1959 na 1960 ambayo pia yalimuondoa Mflame Kigeri na kukomesha utwala wa Kifalme wa Watusi, visa ambavyo nilivieleza katika sehemu iliyopita, Fred pamoja na familia yake walikimbia nchi ya Rwanda na kwenda Uganda kwenye kambi za wakimbizi.



Akiwa nchini Uganda na hasa alipokuwa sekondari alikutana na kuwa marafiki na Salim Saleh (jina halisia alipozaliwa aliitwa Caleb Akandwanaho) mdogo wake Rais Yoweri Museni. Wote wawili mwaka 1976 walipomaliza shule ya upili walisafiri mpaka hapa Tanzabnia kuungana na kaka yake Salim Saleh, yaani Bw. Yoweri Museveni ambaye alikuwa ameanzisha vugi vugu la FRONASA (Front For National Salvation). Vuguvugu hili ambalo mwanzoni lilianza kama kikundi tu cha wanaharakati ambao walikuwa wanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es Salaam ambako Museveni alikuwa anasomea shahada yake ya uchumi na sayansi ya siasa. Lakini baadae harakati hizi zilipamba moto na kuzaliwa kikundi cha waasi wa FRONASA chini ya uongozi wa Yoweri Museveni ambacho mwanzoni kilikuwa na lengo kuu moja la kumuondoa madarakani Rais Dikteta wa Uganda kipindi hicho, Nduli Idd Amin Dadaa. Ndicho kikundi hiki ambacho Fred Rwigyema na Salim Saleh walikuja kujiunga nacho walipoingia Tanzania.


Baadae Fred na wenzake welipelekwa na Museveni nchini msumbiji katika harakati za wenzao wa FRELIMO, hii nitaeleza zaidi hapo baadae.




Paul Kagame


Paul Kagame amezaliwa kwenye kijiji kinachoitwa Tambwe pia maeneo ya kusini mwa Rwanda mwaka 1957, tarehe 23 October. Baba yake anayeitwa Deogratias familia yao ilikuwa na ukaribu sana na familia ya kifalme kipindi hicho Rwanda bado ikitambulika kama ‘Kingdom of Rwanda’. Pia Mr. Deogratia familia yao pia ilikuwa na undugu wa karibu na Mfalme Mutara III lakini baba yake Paul Kagame hakupendelea kutumikia mfumo wa kiserikali mfano labda kuwa afisa fulani wa serikali au mpambe wa mfalme, badala yake aligeukia masuala ya biashara ambayo alifanikiwa kwa kiasi kikubwa.


Pia mama yake Paul Kagame, Asteria Rutagambwa, anatokea kwenye familia ya Malkia wa mwisho wa Rwanda, Rosalia Gicanda.


Baada ya machafuko ya mwaka 1959 na mwaka 1960 ambayo niliyaeleza kwenye sehemu zilizopita, ambayo yalisababisha maelfu ya Watusi kukimbia Rwanda, familia ya akina Paul Kagame nayo ilikuwa ni moja ya familia ambazo zilikimbilia kwenye kambi ya wakimbizi nchini Uganda. Ikumbukwe kwamba kipindi ambacho familia yao inakimblia Rwanda, Paul Kagame alikuwa ni mtoto wa miaka miwili tu. Kwa hiyo ni vizuri kukumbuka huko mbele tunavyoendelea na makala hii kwamba Paul Kagame amekulia nje ya Rwanda. Kwamba alirejea Rwanda walau kwenda kuugusa mchanga wa ardhi ya nchi yake tayari akiwa ni mtu mzima kabisa.


Walipofika Uganda yeye na familia yake waliishi katika kambi ya wakimbizi ya Nshungerezi iliyopo kaskazini mwa Uganda mkoa mdogo wa Toro. Ni mahala hapa kwenye kambi ya wakimbizi na kwenye hali hii ya utoto ndipo ambapo Paul Kagame na Fred Rwigyema walikutana na kuwa marafiki wa ‘kufa na kuzikana’.


Kagame alianza shule ya msingi kwenye shule maalumu ambayo ilijengwa karibia na kambi, maalumu kwa ajili ya watoto wa wakimbizi ‘kutoa tongotongo’ walau. Mwenyewe Paul Kgame anasema kwamba kitu kikubwa ambacho alijifunza kwenye shule hii ya wakimbizi ambacho anakithamini zaidi mpaka leo hii ilikuwa nikijua lugha ya Kingereza na pia kuweza kuelewa na kujichanganya (integrate) na tamaduni za Uganda.


Kutokana na kufanya vizuri sana darasani kushinda watoto wenzake wengine wa kikimbizi alipofikisha umri wa miaka tisa alihamishiwa kwenye mojawapo ya shule zenye heshima kubwa sana kipindi hicho ambayo ilikuwa inaitwa Rwengoro Primary School ambayo ilikuwa umbali wa kilomita zipatazo 16 kutoka kwenye kambi ya wakimbizi ambayo alikuwa anaishi na familia yake. lakini Licha ya umbali huu mkubwa kutoka kati ya shule anayosoma na kwenye kambi ya wakimbizi ambayo walikuwa wanaishi na familia yake, Paul Kagame alimaliza shule hii ya msingi kwa kupata alama za juu zaidi kuliko mwanafunzi yeyote yule kwenye Wilaya nzima.


Kutokana na kupata alama za juu kiasi hicho, Paul Kagame alipelekwa kwenye shule ya upili ambayo tunaweza kusema ndiyo ilikuwa bora zaidi nchini Uganda kwa kipindi hicho ambayo inaitwa Ntare School. Hii ndiyo shule ambayo pia hata Yoweri Museveni alisoma.


Mwanzoni masomo yake hapa shule ya Ntare yalienda vizuri sana, lakini muda si muda mambo yakaanza kubadilika.


Mwaka 1975 baba yake mzazi Kagame, Mr. Deogratias alifariki dunia tukio ambalo lilimuumiza moyo sana Kagame na kumpa msongo mkubwa wa mawazo. Lakini pia kabla ya kidonda cha kuondokewa na baba yake hakijapoana mwaka uliofuata rafiki yake kipenzi Fred Rwigyema aliondoka kwenda mahala kusikojulikana bila kumuaga yeyote yule. (nilieleza hapo juu kuwa mwaka huu ndio ambao Fred alijiunga na vuguvugu la FRONASA chini ya Yoweri Museveni… lakini hakuna ambaye alikuwa analijua hili kwa kipindi hicho).


Matukio haya makubwa mawili, baba yake kufariki na baadae rafiki yake kupotea kwenye mazingira ya kutatanisha, kulimfanya Kagame awe kama vile ‘nusu amechanganyikiwa’. Ilikuwa karibia kila siku walimu shuleni kwake Ntare wanaletewa kesi ya Paul Kagame kupigana na wanafunzi wenzake. Alikuwa akimsikia mtu anatamka neno hata liwe dogo kiaisi gani lakini kama lina uelekeo la kuikosoa au kukashifu Rwanda basi atakuvaa na kuanza kurusha ngumi.


Mabadiliko yake haya hasi ya kitabia yalifanya maendeleo yake kitaalumu kushuka na pia walimu kuchoka utovu wake wa nidhamu na hatimaye kutimuliwa hapa Ntare School. Wazazi wake walipambana na akapata nafasi shule ya Old Kampala Secondary ambako alimalizia huko shule yake ya upili lakini akiwa na alama za chini kabisa kuliko ilivyo kawaida yake.


Baada ya kumaliza shule ya upili Paul Kagame alikuwa kwenye msongo mkubwa wa mawazo. Alikuwa anajihisi kama vile amepotea na kupoteza dira ya maisha. He needed to find himself. Alikuwa anahitaji sababu ya kuendelea kuishi. Na si kuishi tu bali pia kuishi kwa kutimiza kusudi la yeye kuwepo duniani.


Paul Kagame alihitaji kuamsha tena hari na morari ndani yake. Na ndipo hapa ambapo alikata shauri ya kuitembelea nchi yake ya Rwanda kwa mara ya kwanza kabisa tangu alipoondoka akiwa na miaka miwili tu.


Hii ilikuwa ni mwaka 1977 ambapo Kagame alikata shauri ya kwenda Rwanda kwa mara ya kwanza maishani mwake. Safari yake hii ya Rwanda ndiyo ambayo iliamsha hari na morali ya kumjenga Kgame huyu ambaye tunaye siku hii ya leo. Nitarudi kueleza.




SEHEMU YA TANO



Ni jambo la kusikitisha sana kwamba Historia yetu ambayo watoto wetu wanafundishwa mashuleni na kuandikwa kwenye vitabu imechujwa mno kiasi kwamba inakuwa kama ni hadithi tu za kusadikika.

Kwa mfano kama umebahatika kuijui historia ya ukweli kuhusu Vita ya Kagera kisha ukasoma 'version' ambazo zimeandikwa kwenye vitabu na kuaminishwa kwa umma, machozi yanaweza kukutoka.


Ubaya ni kwamba hata wale ambao wamebahatika kujua ukweli halisi wa matukio na vilivyo nyuma ya pazia hawawezi kuthubutu kutia mkono na kuandika kile ambacho wanakijua.


Ndio maana naamini ni busara hata kwangu pia niandike kwa sehemu kile ambacho historia zetu hakivisemi lakini pia ni muhimu kuandika kwa "ustaarabu" kwa faida ya pande zote.




Kutengenezwa kwa Jasusi Paul Kagame


Katika sehemu iliyopita nilieleza kwamba, Paul Kagame mwaka 1977 alitembelea nchi ya Rwanda ambapo hakuwahi kuikanyaga tangu alipokuwa mtoto wa miaka miwili tu. Paul Kagame alifanya safari hii kutokana na kukosa amani ndani ya moyo wake. Alikuwa anatafuta 'kusudi' lake la maisha. Katika kipindi hiki alikuwa amempoteza baba yake mzazi na pia rafiki yake kipenzi Fred Rwigyema alikuwa amepotelea kusikojulikana.


Kwa hiyo Paul Kagame alienda Rwanda kwa ajili ya 'soul searching'. Alikuwa anataka kupata hamasa kwenye roho yake ili aweze kujua kusudi la maisha yake.


Kutokana na historia ya familia yake kuwa na ushawishi kwa kiasi fulani (nilieleza kwamba baba yake ana undugu wa kiukoo na Mfalme Kigeli na mama yake ana undugu wa damu na Malkia wa mwisho wa Rwanda) kwa hiyo hizi safari zake za Rwanda alizifanya kwa siri kubwa pia ukizingatia kwamba serikali ilikuwa makini sana na watusi ambao wako nje ya Rwanda kama wakimbizi kutokana na harakati zao na kiu yao ya kutaka kuipindua serikali mara kwa mara.

Safari hii ilikuwa ya maana sana kwa Kagame na alijenga 'connection' ambazo zilikuja kumsaidia sana miaka ya baadae kwenye harakati zake.


Mwaka 1978 alifanya safari nyingine kwenda Rwanda na safari hii hakupitia mpaka wa Uganda bali aliingia kupitia Zaire (Congo). Kwa wiki kadhaa ambazo alikaa Kigali kwa siri kubwa, alitumia muda huo kuimarisha 'connection' ambazo alikuwa nazo na pia kusoma hali ya kisiasa na uimara wa serikali.


Safari hizi mbili ziliamsha hari kubwa mno katika nafsi ya Paul Kagame. Aliona kwa uhalisia kabisa mateso na manyanyaso ambayo watusi walikuwa wanapitia nchini Rwanda. Akajihisi kabisa kwamba alikuwa ana jukumu la kufanya kitu kuyamaliza mateso hayo.


Aliporejea nchini Uganda Kagame akageuka kama mwanaharakati hivi katika kambi za wakimbizi akihamasisha vijana wenzake kujizatiti na kuweka mipango ya kuikombia Rwanda.


Wakati huo huo, rafiki yake Fred Rwigyema ambaye alipotea bila yeyote kujua ni wapi alikuwa ameelekea… alikuwa nchini Tanzania katika kambi ya FRONASA chini ya uongozi wa Yoweri Musseveni ambao walikuwa wanaweka mikakati ya kumuondoka madarakani Dikteta Idd Amin.


Habari kuhusu kijana mahiri, mwanaharakati Paul Kagame zilimfikia Yoweri Musseveni na alitamani awe sehemu ya 'timu' yake.

Ndipo hapa ambapo Fred Rwigyema ambapo ndio kwanza alikuwa amerejea Tanzania kutoka msumbuji ambako alipelekwa na Musseveni kwenye mafunzo ya pamoja na wapiganaji FRELIMO juu ya vita za msituni…alitumwa kwenda nchini Uganda kwa ajili ya masuala kadhaa lakini mojawapo ilikuwa kumshawishi Paul Kagame kujiunga na wapiganaji wa Yoweri Musseveni walioko nchini Tanzania.



Sasa basi…


Kuna mahala mkoani Morogoro, sitapaja kwa jina au exactly sehemu gani… lakini ni nje ya mji kidogo kuna 'Espionage Farm' ya siri ambayo mwaka 1978 Paul Kagame na maafisa kadhaa wa kikundi cha FRONASA walikuwa recruited na kupata mafunzo ya Ujasusi na masuala ya Intelijensia.


Niseme kwamba Paul Kagame ni moja ya maafisa bora na hodari kabisa kuwahi kuzalishwa na Idara yetu Usalama wa Taifa.



Kagame amewahi kutumia kwenye 'high profile missions' kadhaa lakini kubwa zaidi ni ile ambayo aliongoza kikosi cha Intelijensia ya wapiganaji wa UNLA (Ugandan National Liberation Front) katika vita ya Kagera.


Tofauti na historia ilivyoandikwa kuhusu vita ya Kagera, lakini ukweli na uhalisia ni kwamba wapiganaji wa UNLA ambao walikuwa ni zaidi ya 20,000 walikuwa ni kiungo muhimu sana katika ushindi wa vita ya Kagera. Suala hili tutalizungumzia siku moja kama tukipata wasaa wa kuichambua vita ya Kagera.


Kuna kikao cha siri sana kilifanyika pale Moshi ambacho kinajulikana kana "Moshi Conference" ambacho kiliudhuliwa na watu adhimu kabisa wapatao 28 na mmoja wao alikiwa Paul Kagame.

Katika kipindi hiki, Rais ambaye alikuwa amepinduliwa na Amin na kukimbilia Tanzania, Bw. Milton Obote alikuwa na kikundi chake cha wapiganajia ambacho alikiita kwa jina la Kiswahili "KIKOSI MAALUM" ambacho makamanda wake walikuwa ni Tito Okello na David Oyite Ojok. Hawa nao pamoja na Obote mwenyewe walikuwepo kwenye kikao cha mjini Moshi.

Pia Yoweri Musseveni alikuwepo kuiwakilisha FRONASA. Pia walikuwepi wanaharakati wengine mashuhuri kama vile Akena p'Ojok, William Omaria, Ateka Ejalu, Godfrey Binaisa, Andrew Kayiira, Olara Otunnu pamoja na baadhi ya 'wakubwa' kutoka kwenye vyombo vya ulinzi vya nchi yetu ambao kwa sababu ya 'staha' sitaandika majina. Jumla walikuwa watu ishirini na wanane.


Kikao hiki kilizaa mpango mkakati wa kijeshi ambao ndio ulitumika kwenye vita ya Kagera na kumshinda Amin. Paul Kagame ndiye ambaye alibebeshwa mzigo wa mikakati ya Intelijensia ya kijeshi.


Octoba 1978 tukaingia vitani dhidi ya majeshi ya Amin. Licha ya swahiba wake Kanali Muammar Gaddafi kutuma wapiganaji 2,500 pamoja na silaha nzito za mivita na za kisasa kwa kipindi hichi kama vifaru aina ya T-54, T-55, magari ya kivita ya kisovieti aina ya BTR APC na Grad MRL pamoja na ndege za kivita aina ya MiG 21 na ndege hatari za kivita (supersonic bombers) aina ya Tu-22 kumsaidia Amin… ajabu ni kwamba licha ya majeshi ya amini kuwa imara kiasi hiki kwa maana ya vifaa vya kivita lakini mwanzoni mwa mwezi April 1979 tulimpiga Amin mpaka "Ikulu" na kumlazimu kukimbilia Libya kwa swahiba wake Gaddafi na baadae kukimbilia Saudi Arabia.


Siku moja kabla ya kutangaza kuisha kwa vita ya Kagera, yaani April 10 Tanzania tukamsimika Yusufu Lule kuwa Rais mpya wa Uganda. Yusufu Lule ameishi sana hapa Tanzania hasa baada ya Idd Amin kuingia madarakani.

Pamoja na hilo lakini akina Musseveni nao waliunda chombo chao cha kijeshi ambacho kiliitwa National Consultative Commission (NCC). Hiki kwa kiasi fulani ndio walikifanya kama chombo chenye maamuzi ya mwisho kuhusu nchi.


SILAHA NZITO ZA KIJESHI AMBAZO UGANDA ILIPOKEA KUTOKA KWA KANALI GADDAFI


c602b90a718adb6d70906ae3d79c1bbf.jpg

Vifaru aina ya T-54 na T-55


2743bb95c3a98150af0cb66d13f9067a.jpg

Supersonic Bomber Tu-22



c8c265894db490554db478de4e2fa40f.jpg

Ndege za kivita aina ya MiG-21


68fe96eca1cfee365ee5361c87c3b2f6.jpg

Gari za kivita aina ya Grad MRL




1fa390e0b95ce0e569636ce5414c5cb0.jpg

Gari za kivita aina ya BTR APC



Miezi miwili tu baada ya majeshi ya Tanzania kumsimika Yusufu Lule kuwa Rais, kukaanza kutokea mvutano mkali kati ya NCC ya kina Musseveni na Rais Yusuf Lule. Mvutano huu ulikuwa ni juu ya mamlaka ya Rais ambayo NCC walimuona Lule kama anavuka mipaka yake. Lule naye kwa upande wake alikuwa anaonekana hataki nchi kuingozwa na jeshi (NCC).

Hatimaye tarehe 10 June mwaka huo 1979 NCC kwa ushawishi mkubwa wa Musseveni wakamuondoa madarakani Godfrey Binaisa kuwa Rais mpya wa Uganda.


Kimsingi Binaisa alikuwa kama 'kikaragosi' tu lakini kiuhalisia NCC ndio walikuwa wanaongoza nchi.


Lakini taratibu naye utamu wa madaraka ukaanza kumkolea.


Ikumbukwe kwamba katika kipindi hiki chote Milton Obote bado alikuwa nchini Tanzania hajarejea Uganda.

Kulianza kuzuka taarifa kwamba mnadhimu mkuu wa jeshi Brigedia Jenerali David Oyite Ojok ambaye kipindi cha vita ya Kagera alikuwa kamanda wa jeshhi ka pamoja la Tanzania na UNLA, alikuwa anafanya maandalizi ya kuhakikisha Obote anarejea Uganda.



Jeneralari Ojok anatokea eneo la kaskazini mwa Uganda kama ilivyo kwa Obote. Licha ya Ojok kuanza mikakati ya kumrudisha Uganda Obote lakini pia kwenye jeshi nyadhifa za juu zote alikuwa anahakikisha zinashikiliwa na watu wanaotoka ukanda wa kaskazini mwa nchi.


Harakati zote hizi Binaisi aliziona kama juhudi za kumuondoa madarakani ili kusafisha njia kwa Obote kurejea madarakani.


Mwezi May 1980 Rais Godfrey Binaisa alimuondoa Ojok kwenye cheo cha Mnadhimu mkuu wa jeshi.

Suala hili lilipingwa vikali na NCC na wakafikia hatua ya kumuondoa madarakani Rais Binaisa na kuunda tume maalumu ambayo waliita Presidential Commision ambayo ndiyo ilifanya kazi ya kuongoza nchi badala ya Rais.

Tume hii wanakamati wake walikuwa ni Museveni, Oyite Ojok, Okello na Muwanga.

Muwanga alipewa cheo cha uenyekiti wa tume japokuwa kiuhalisia wenye nguvu za ushawishi kwenye tume walikuwa ni Museveni na Ojok.


Baada ya hapa ndipo ambapo hasa umahiri wa Paul Kagame unaonekana. Ikumbukwe kwamba wakati yote haya yaliendelea Paul Kagame alikuwa na ushawishi mkubwa sana kwenye jeshi la Uganda kutokana na umahiri wake wa masuala ya Intelijensia. Kwa hiyo yeye ndiye ambaye alikuwa anawashauri ni nani anafaa kuwa Rais na nani hafai.


Baada tu ya nchi kuanza kuongozwa na Tume maalumu niliyoitaja hapo juu, Ojok akaanza tena mipango ya kumrejesha Milton Obote ndani ya Uganda. Ilikuwa wazi kwamba Ojok alikuwa anataka Obote ashike madaraka. Lakini watu wengi wa kabila la Baganda/Waganda walikuwa wanampinga Obete kwa kuwa yeye ndiye ambaye alimpindua Mfalme wao wa Baganda miaka kadhaa nyuma na kushika Urais kabla ya yeye pia kupinduliwa na Ids Amin. Kwa hiyo kulikiwa na mvutano kati ya watu wa maeneo ya kaskazini na kusini mwa Uganda.



ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog