Search This Blog

Saturday 24 December 2022

KILIO CHA MIFEREJI YA DAMU IENDAYO ETHIOPIA - 1

  http://pseudepigraphas.blogspot.com/2020/06/kilio-cha-mifereji-ya-damu-iendayo_10.html

Simulizi :  Kilio Cha Mifereji Ya Damu Iendayo Ethiopia

Sehemu Ya Kwanza (1)



SEHEMU YA KWANZA


“..kama unasoma ujumbe huu, muda huu… uko mpweke! Pengine ushahidi pekee uliobakia ni kijipande hiki cha maandishi. Sijui kama kuna yeyote kati yetu aliyesalimika kufika kizazi chenu mwaka huu mtakaosoma andishi langu. Sijui hata kama tumeshinda au tumeshindwa vita tunayopigana sasa hivi. Sijui, lakini naamini mwaka huu mliopo nyinyi sasa mwaweza kuwa na jibu sahihi. Vyovyote vile lakini jambo lililo dhahiri ni kwamba hakuna yeyote wa kizazi chetu mliye naye sasa hivi kwenye miaka yenu muusomapo ujumbe huu. Kwa hiyo wacha niwaeleze sisi tulikuwa akina nani, na kwa namna gani tulipambana mpaka tone la mwisho la damu mwilini mwetu ili kutetea kizazi chetu kisifutwe juu ya uso wa dunia. Wacha niwaeleze namna ambavyo japo tulikamuliwa damu mpaka kutiririka kufanya mifereji lakini lakini tulisimama kutetea kizazi chenu na ninyi watoto wetu. Wacha niwaeleze kisa kilichotikisa ulimwengu. Wacha niwaeleze kuhusu mifereji ya damu kwenda Ethiopia.!”


– Habib Anga alias The Bold


March 21, 1994 maeneo ya Uganda ambayo yanapakana na Rwanda, katika ziwa viktoria serikali ilituma vikosi vya jeshi kudhibiti eneo hilo kwa hali ya dharura. Agizo hili la serikali kutuma jeshi halikuwa kwa ajili ya kidhibiti eneo hilo kutoka kwa adui bali agizo lilikuwa ni kudhibiti eneo hilo dhidi ya maiti, maiti za binadamu. Sio maiti mbili au tatu, si mamia bali maelfu ya maiti za binadamu ambazo zilikuwa zinaingia ziwani Victoria zikiletwa na maji ya mto Kagera.


Maiti hizi zilikuwa nyingi kwa maelfu kiasi kwamba mapaka zilikuwa zinafanya maji yatoe harufu. Serikali ya Uganda ilituma jeshi eneo hili ili kudhibiti eneo hili maji yake yasitumiwe na wananchi kwa matumizi ya nyumbani au shughuli za uvuvi. Lakini jeshi lilikuwa eneo hili ili kuhakikisha kuwa taharuki iliyozuka baada ya maelfu ya miili hii kuonekana haigeuki na kuvuruga amanai katika eneo hili. Lakini pia jeshi lilikuwa hapa ili kubaini miili hii ilikuwa inatoka wapi.


Kadiri ambavyo jeshi la Uganda lilivyokuwa linafuatilia kwa kurudi nyuma kufuata mto Kagera ndivyo ambavyo walizidi kubaini kwamba maiti hizo zinaletwa na maji kutoka tawi la mto Kagera lililopita kusini mwa Rwanda. Na kadiri ambavyo walizidi kufuata chanzo cha maiti hizo zinakotoka ndivyo ambavyo walikuwa wanaikaribia Rwanda na maji ya mto rangi yake kuwa nyekundu zaidi.


Wanajeshi wa Uganda ambao walishiriki kwenye ukaguzi huu wa mto huu wanakiri kwamba licha ya baadhi yao kupigana mstari wa mbele kwenye vita mbali mbali lakini hakuna yeyote kati yao ambaye aliwahi kushuhudia ukatili mkubwa wa kiasi hiki.


Siku hii jeshi la Uganda linakisia kwamba waliokota si chini ya miili elfu kumi ya binadamu na yote ilionekana kuletwa na maji ya mto Kagera kutoka nchini Rwanda.


Ajabu ni kwamba miili yote hii ilikiwa inamfanano fulani. Maiti zote zilikuwa za watu warefu, wembamba, wenye nyuso ndefu na pua za kuchongoka. Haikuhitaji kufikiria sana kufahamu kuwa maiti hizi zilikuwa za watu wa kabila la Tusi (Tutsi).


Miezi kadhaa baadae ndipo ambapo jeshi la Uganda na ulimwengu wote walikuja kuelewa kwa nini maiti zilikuwa zinatupwa mto Kagera. Ni ujumbe gani ambao ulikuwa unajaribu kutumwa.


Kwamba Watusi nchini Rwanda walikuwa waapenda kujisifu kuwa mababu zao wana asili ya nchi ya Ethiopia. Kitendo hiki cha watesi wao kuwatupa mtoni, walikuwa wanawaua na wakiwa wanatupa maiti zao mto wanawaambia kwamba “wanawasafirisha warudi kwao Ethiopia ambako wamekuwa wakijisifu ndio asili yao.”


Sio kwamba jeshi la Uganda hawakuwa na taarifa juu ya hali tete iliyopo Rwanda kwa muda wa karibia wiki nzima iliyopita bali hawakujua kama hali hiyo tete ilikuwa ni ya kinyama kiasi hicho.


Wanajeshi hawa wa Uganda walikuwa wameshikwa na bumbuwazi na vihoro vilivyo wapasua mioyo kwa kuona miili hii elfu kumi ya binadamu isiyo na uhai. Kitu ambacho walikuwa hawakijua na hakuna ambaye alidhahania ni kwamba ndani ya siku mia moja zijazo ulimwengu ulikuwa unaenda kushuhudia moja ya tukio la kikatili zaidi tangu kuubwa kwa ulimwengu. Karibia maiti za binadamu milioni moja zikiwa zimetapakaa mitaani nchini Rwanda iking’ong’wa na nzi na kuliwa na mbwa.



b27e3a3a6fd670dbc0a4e300cbcc558f.jpg


GENESIS


Rwanda: Kabla ya Ukoloni


Asili rasmi kabisa ya watu wa kwanza kuishi katika eneo ambalo leo tubalitambua kama nchi ya Rwanda ni watu wa kabila la ‘Twa’ (Watwa). Kabila hili la wawindaji si la kibantu bali ni sehemu ya makabila yanayotambulika na wanahistoria kama ‘pygmy’ ambao sifa yao kuu ni ufupi. Mtu mzima anayetoka makabila ya namna hii anakadirwa kuwa na wastani wa urefu chini ya sentimita 150. Watwa waliishi Rwanda enzi za kale sana miaka ya 8000 BC na 3000 BC.


Kuanzia miaka ya 700 BC mpaka 1500 AD makabila ya Kibantu kutoka maeneo ya jirani yalianza kuhamia eneo hili.


Kuna nadharia mbali mbali kuhusu ni namna gani haswa makabila haya ya kibantu yalihamia hapa na baadae kupelekea kutokea Makabila ya sasa ya Wahutu na Watusi.


Nadharia ya kwanza inadai kwamba; Wahutu ndio walikuwa wa kwanza kuhamia eneo hili na kuanzisha shughuli za kilimo. Baadae watu wenye asili ya Ukushi (Watusi wa sasa) nao wakahamia kwenye eneo hili na kulitawala.


Nadharia ya Pili inadai kwamba; kuna uwezekano kwamba Watusi si wakushi bali ni wahamiaji tu kutoka maeneo ya jirani kipindi hicho cha kale ambao walihamia na kujichanganya na jamii waliyoikuta hapo (Wahutu) lakini wao walikuwa wafugaji. Chini ya nadharia hii inadai kwamba kuibuka kwa Wahutu na Watusi hakukutokana na kuwa na utofauti wa kinasaba au asili ya mababu bali ulitokana na utofauti wa kimadaraja/matabaka ya kijamii.


Tabaka la wale walio wa daraja la juu ambao walikuwa wafugaji walijitanabaisha kama Watusi wakati ambapo tabaka la chini ambao walikuwa wakulima walijitanabasha kama Wahutu.


Makabila haya yote matatu, Watwa, Wahutu na Watusi wanazungumza lugha moja na kwa wote kwa pamoja wanajulikana kama ‘Banyarwanda’.


Idadi ya watu ilipoongezeka katika eneo hili walianza kujitambua kupitia makundi madogo madogo yaliyoitwa ‘Ubwoko’ au ‘koo’ kwa kiswahili. Ilipofika katikati ya miaka ya 1700 koo nyingi ziliungana na kuunda ‘Falme’.


Moja ya Falme ambazo zilikuwa imara zaidi ulikuwa ni ‘Kingdom of Rwanda’ ambayo watawala wake wote walitokea katika koo ya Kitusi ya Nyiginya.


Ufalme huu ulifikia kileleni kipindi cha utawala wa Mfalme Kigeli Rwabugiri chini ya falsafa yake ya kujipanua na kuteka falme nyingine na kuzifanya sehemu ya Kingdom of Rwanda.


Chini ya Mfalme Rwabugiri alianzisha mfumi wa kiuchumi wa ‘ubuhake’ na baadae ‘uburetwa’.


Katika mifumo yote hii miwili, iliwanufaisha zaidi Watusi na kuwafanya Wahutu kama vijakazi wao kuwafanyia kazi za uzalishaji na kuwa askari vitani kwa ujira wa kupata fursa ya kumiliki mifugo na kutumia ardhi.


Watusi walipaa juu zaidi na kuwa raia daraja la kwanza ma Wahutu kubakia kuwa tabaka la chini kabisa ndani ya Kingdom of Rwanda.


Rwanda: Wakati wa Ukoloni


Mkutano wa Berlin wa mwaka 1884 ulilitoa eneo hili kuwa koloni la nchi ya Ujerumani. Wajerumani walitawala eneo hili kwa kushirikiana na Mfalme na hivyo kuwapa wepesi wa kutawala koloni bila kuwa na askari wengi wa kijerumani ndani ya ardhi ya Rwanda. Yuhi V Musinga ndiye walikuwa Mfalme wa Rwanda kwa kipindi hiki na anakumbukwa zaidi kwa kuwapokea Wajerumani kwa mikono miwili.


0c654baede81239ccf0ddc5664b343b5.jpg

Ikulu ya Mfalme wa Rwanda maeneo ya Nyanza


Wajerumani ndio walikuwa watu wa kwanza kuanza kuwapandikizia Watusi kasumba ya kuwa wao si Wabantu. Wakoloni wa Ujerumani ndio ambao walieneza propaganda kwa kuwafundisha Watusi kwamba kutokana na tafiti zao za kina wamegundua kwamba wao (Watusi) mababu zao wa kale walihamia eneo hilo kutokea Ethiopia. Hivyo wakawashawishi kuamini kwamba Watusi wana vinasaba vya ‘uzungu’ (Caucasian) na hivyo ni wao pekee ndani ya Rwanda walistahili kupata nafasi za ajira kusaidizana kazi na wazungu chini ya utawala huo wa Wajerumani.


Katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, Ubelgiji iliziteka Rwanda na Burundi kutoka mikononi mwa Ujerumani na mwaka 1919 League Of Nations ilizifanya rasmi nchi hizo kuwa makoloni ya Ubelgiji.


Mwanzoni Wakoloni wa Ubelgiji walianza kuitawala Rwanda kwa mtindo ule ule wa kushirikiana na Ufalme lakini baadae wakajilimbikizia madaraka yote ya kutawala kama ambavyo walifanya kwenye koloni lao la Kongo.


Baadae wakaanza ‘kutaifisha’ mali za Wanyarwanda katika mfumo wa kufanana kabisa na mfumo wa asili wa uburetwa na walioathirika zaidi na kampeni hii ya utaifishaji walikuwa ni Wahutu.

Ardhi yao ilinyang’anywa… Mifugo ilitwaliwa na kuwafanya Wahutu kuwa si tu vijakazi wa Wakoloni bali pia vijakazi wa Watusi.


Mwanzoni mwa miaka ya 1930s Ubelgiji walifanya upanuazi mkubwa wa sekta ya Elimu, afya na ajira za umma. Lakini wanufaika wakuu walikuwa ni Watusi.


Mwaka 1935 Ubelgiji walifanya kitu ch a ajabu sana ambacho kilipanua zaidi mpasuko wa kijamii na kitabaka uliopo ndani ya Rwanda. Walianzisha mfumo wa raia wote kuwa na vitambulisho. Vitambulisho hivi viliwatambua raia wote katika makundi manne kulingana na makabila yao. Watwa, Wahutu, Watusi na Raia wa kuomba (Naturalised).


Kutokana na Watusi kuwa ndio raia wa daraja la kwanza na tabaka la juu huku Wahutu wakiwa ni watu hafifu wa kudharaulika nchini humo, ilifikia hatua Wahutu wenye mali au ushawishi walikuwa wanahonga fedha ili kupatiwa vitambulisho vya Kuonyesha ni Watusi na watawala hawakuwapa Utusi kamili bali waliwapa ‘utusi wa heshima’ (Honorary Tutsi).


Hadhi ya Wahutu wote iliendelea kushuka kwa kasi wakionekana ni kabila na kizazi cha “Washenzi” huku Watusi wakionekana ndicho kizazi cha “wastaarabu” na kabila lenye darja.


Lakini kuna suala ambalo lilifanyika mwanzoni likionekana kuwa na manufaa makubwa lakini kadiri siku zilivyokwenda lilianza kuwa kama mkuki mgongoni. Kanisa Katoliki.


Kanisa Katoliki lilikuwa limeenea sana nchini Rwanda na raia wake wengi wakiwa ni waumini wa kanisa hilo. Tukumbuke kwamba tangu kipindi hicho Wahutu ndio walikuwa idadi kubwa zaidi ya raia wote ndani ya Rwanda. Hii ilimaanisha pia kwamba waumini wengi wa kanisa Katoliki walikuwa ni Wahutu.


Kwa kiasi fulani ndani ya kanisa Katoliki mapadri na watawa wengine walikuwa wanajisikia hatia kuacha waumini wao kuwekwa kwenye kundi la kizazi cha “washenzi” na kudharaulika ndani ya jamii. Kwa hiyo zikaanza juhudi za makusudi za kanisa katoliki kutoa elimu kwa vijana wenye asili ya Kihutu.


Baada ya miaka kadhaa kukaanza kuwepo walau kidogo uwiano wa wasomi wa Kihutu na Kitusi.


Mwaka 1957, mwezi March kikundi cha wasomi na watu wenye ushawishi wenye asili ya Kihutu walifanya jambo la “kimapinduzi” ambalo lilipanda mbegu mpya kwenye nafsi za watu wa kabila na kizazi cha cha Kihutu. Waliandaa waraka ulioitwa _'Manifeste des Bahutu' (Bahutu Manifesto).

Huu ndio ulikuwa waraka wa kwanza rasmi kubainisha kwamba Wahutu na Watusi ni mbari (race) mbili tofauti.


Katika waraka huu, wasomi hawa na watu hawa wenye ushawishi walijenga hoja kuu kwamba… Watusi wanapaswa kutoka kwenye jukumu lao walilojivesha la kuwa watawala wa Rwanda na badala yake nafasi hiyo ya kutawala Rwanda wapewe Wahutu. Hoja yao hii waliijenga kwenye nadharia ambayo wenyewe waliita “Statistical Law”, kwamba kitakwimu Wahutu ni wengi mno kushinda Watusi. Si sawa wakiendelea kutawaliwa na kufanywa vijakazi na Watusi.


Wanasema kwamba kabla kibanda cha nyasi kuungua kwanza utaanza kukiona kinafuka moshi. Kuna vugu vugu lilianza chini kwa chini ndani ya Rwanda.


Waraka huu… Bahutu Manifesto, ulitoka tarehe 4 March mwaka 1957. Japokuwa ilikuwa ni miaka takribani 37 kabla ya mwaka 1994, lakini ndio siku ambayo mbegu ya mauaji ya kimbari ilipandwa.


Usikose sehemu inayofuata….


KILIO CHA MIFEREJI YA DAMU IENDAYO ETHIOPIA




SEHEMU YA PILI






BAHUTU MANIFESTO




“Note sur l’aspect social du probleme racial indigene au Rwanda” (Waraka kuhusu maslahi ya kijamii ya Wazawa halisi wa Rwanda)




Katika sehemu iliyopita nilieleza kwa kifupi sana juu ya Waraka huu. Kwamba mwaka 1957 tarehe 24 March Wasomi wa kihutu na wahutu wenye ushawishi katika jamii ya Rwanda waliandaa waraka huu mahususi kutaka wahutukushika madaraka makuu ya uongozi nchini Rwanda. Hoja kuu ambayo waliijenga ni kwa kutumia nadharia waliyoiita “Statistical Law”. Kwamba wahutu ndio idadi kubwa zaidi ya raia wa Rwanda ambao ni 84% ya raia wote wa Rwanda huku watusi wakiwa ni asilimia 14 na Watwa 15 tu. Kwa hiyo kwa mujibu wao walihisi haikuwa sahihi kuwekwa kama raia wa daraja la pili na pia kuongozwa na kabila ambalo lina watu kiduchu zaidi ndani ya Rwanda.




Waraka huu wa kurasa kumi na wa kichokozi lakini uliojaa hoja nzito uliwasilishwa kwa Gavana wa Rwanda. Katika kurasa hizo kumi wasomi hao waling’aka vikali juu ya unyonyaji unaofanywa na Watusi dhidi ya Watu wakabila la Hutu.




Waraka huu pia ulisambazwa kwenye jamii. Ambako mkazo mkuu uliwekwa kwenye suala ambalo wenyewe waliita “double liberation”. Kwamba Wahutu wanahitaji ukombozi wa vitu viwili kwa mkupuo. Kwanza wanahitaji kujikomboakutoka kwenye makucha ya wakoloni wa kizungu na pili wanahitaji kujikomboa kutoka kwenye makucha ya Watusi.




Waraka huu ndio wenye mchango mkubwa zaidi ambao ulichangia kuweka msingi wa fikra na mtazamo wa Wahutu kuwaona Watusi kama watesi wao, wanyonyaji na wahamiaji kwenye eneo hilo. Pia waraka huu ndio ulifungua macho Wahutu wengi kuona tatizo kubwa la kijamii, kisiasa, na kichumi kutokana na mifumo yote hiyo kumilikiwa na watusi.




Waraka huu pia ndio ambao ulikuja kusababishwa kuzaliwa kwa amri kuu kumi za Wahutu mwaka 1990 (Ten Commandments of The Bahutu) ambazo nitaziongelea hapo baadae.






THE PURGE




Wengi wetu tunafahamu juu ya mauaji ya kimbari ambayo yalitokea mwaka 1994, lakini jambo ambalo wengi tunalisahau ni mfululizo wa matukio ya “kuisafisha Rwanda” ambayo yalitoka kwa muda wa takribani miaka thelathini mpaka kufikia kilele ambacho ndiyo mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.




Nitaeleza kwa ufupi…




Kama ambavyo nimetanabaisha hapo awali kwamba wahutu ni karibia 84% ya raia wote wa Rwanda. Kwa hiyo ulipotoka waraka wa “BAHUTU MANIFESTO” wakoloni wa kibelgiji walitikisika haswa.




Turudi nyuma kidogo…




Moja ya wanaharakati wa kupigania haki za wahutu ambao waliibuka katika miaka ya 1950s aliitwa Gregoire Kayibanda. Kama ilivyo kwa wasomi wengi wa kihutu, Kayibanda alipata elimu yake kutoka kwenye shule za seminari za wakatoliki japokuwa hakutaka kuwa padre. Alipomaliza elimu yake mwaka 1948 alifanya kazi ya ualimu wa shule ya msingi. Mwaka 1952 Kayibanda alipatiwa nafasi ya kuwa muhariri wa jarida la kanisa katoliki nchini Rwanda nafasi ambayo awali ilikuwa inashikiliwa na moja ya wanafalsafa muhimu zaidi nchiniRwanda aliyeitwa Alexis Kagame. Baadae pia alikabidhiwa jukumu la kuwa muhariri wa jarida lingine la kikatoliki lakini lenye mtazamo wa kihutu lilioitwa “Kinyamateka”.


Mwishoni mwa miaka ya 1950s alianzisha vuguvugu lake aliloliita “Mouvement Social Muhutu” (MSM).




Mwanaharakati mwingine wa kihutu aliyekuwa mahiri na maarufu zaidi katika kipindi hicho alikuwa anaitwa Joseph Gitera. Huyu naye alijipatia elimu yake kutoka shule a seminari za kikatoliki. Miaka hiyo hiyo ya 1950sGitera alianzisha chama chake cha siasa kilichoitwa “Association for Social Promotion of the Masses” (APROSOMA). Tofauti na wanaharakati wenzake wa kihutu mfano Bw. Kayibinda, yeye Gitera alikuwa mwanaharakati labda mwenye huruma kidogo lakini pia muda mwingine akiwa na mawazo ya “kihayawani” kabisa au labda tuseme ndoto za mchana. Harakati za Gitera hazikujikita kwenye masuala ya kikabila zaidi mwanzano, yeye alitilia mkazo zaidi kutetea haki za wananchgi masikini ambao walikuwa hawasikilizwi wala kukumbukwa ndaniya Rwanda. Gitera alikuwa ni moja kati ya wanaharakati wa mwanzo kabisa kutaka kuondoshwa kwa utawala wa kifalme nchini Rwanda.




Sasa basi…




Kitendo cha kuibuka kwa wanaharakati wa Kihutu wenye ushawishi ndani ya Rwanda kilianza kumtetemesha mfalme wa Rwanda pamoja na watusi wenye nyadhifa za ngazi za juu. Ili kujiweka katika nafasi salama, Mfalme waRwanda na wenzake walianza kupiga debe la Rwanda kupatiwa uhuru mara moja kutoka kwa Wabelgiji. Walichokuwa wanajiaminisha vichwani ni kwamba, kama Wabelgiji wataipatia uhuru Rwanda basi madaraka yote yataachwa kwa mfalme wa Rwanda na watu wake na hii inewaweka mahala salama kuendelea kuitawala Rwanda na Watusi kuwa Raia wa daraja la kwanza ndani ya Rwanda.




Mwaka 1956 Mfalme Rudahigwa pamoja na baraza lake la ushauri la “Conseil Superieur” walipendekeza kwa wabelgiji kuundwa kwa wizara za Fedha, Wizara ya Elimu, Wizara ya Kazi na Wizara ya Mambo ya Ndani na wakapendekeza watu wa kuongoza wizara hizo ambao wote walikuwa Watusi.



432cfea3e2e31ab56ac55fbe0b59fbbe.jpg

Mwanaharakati wa Kihitu Grogoire Kayibanda


Mwaka 1959 ili kuwafurahisha zaidi wahutu walio wengi, Wabelgiji walitangaza kwamba kuanzia mwaka huo Machifu watakuwa wanachaguliwa kwa kupigiwa kura na si kuteuliwa tena na Mfalme kama ambavyo ilikuwa awali.




Taarifa hii ilipokelewa kwa shangwe na vifijo na Wahutu lakini upande wa Watusi waliipinga vikali. Waltusi wiipinga kwa sababu kuu mbili. Moja, walihisi wanapokonywa tonge mdomoni kwa kuwa nafasi hizi za uchifuzilipokuwa zinateuliwa na Mfalme wote ambao walikuwa wanasimikwa kuwa machifu kwenye maeneo yote nchini Rwanda walikuwa ni Watusi kutokana na yeye mwenyewe Mfalme kuwa mtusi. Sababu ya pili, watusi waliohofia idadi kubwa ya wahutu. Hii ilimaanisha kwamba hakukuwa na tumaini lolote kwao kufua dafu kwenye sanduku la kura kwa sababu wahutu walikuwa ni wengi kupitiliza kuzidi wao.




Hili lilikuwa ni tishio kubwa kwa uhalali na uendelevu wa Ufalme wa Rwanda chini ya Watusi. Woga ambao ulimpata Mfalme Rudahigwa ulimfanya aanze kufanya mambo ya kipuuzi kabisa. Kwa mfano akaanza kutorosha ‘kalinga’(Ngoma kubwa za jadi ambzo ni moja ya ishara kuu za ufalme enzi hizo nchini Rwanda) akaanza kuzitoroshea kwenda nje ya Rwanda. Yote hii ilitokana na Gitera (yule aliyemdhalilisha) kuanzisha kampeni ya kutaka mfalme apokonywe ngoma hizo.


Baadae mfalme Rudahigwa akaanza tabia ya ulevi kupindukia ili kupunguza msongo ambao alikuwa nao kutokana na tishio lililoibuka la wahutu kuelekea kushika hatamu.


Baada ya misukosuko mingi ya msongo wa mawazo Mfalme Rudahigwa alifariki nchini Burundi eneo la Usumbura ambako alienda kutafuta tiba ya ‘celebral haemorrhage’. Japokuwa mpaka leo hii Watusi wengi bado wanaamini kwamba Mfalme wao Rudahigwa aliuwawa kwa kuchomwa sindano ya sumu na kanisa katoliki kwa kushirikiana na Wabelgiji.




Dhahania hii ilifanya vigogo wa Kitusi kuanza kampeni za kulipinga kanisa katoliki pamoja na uwepo wa Wabelgiji nchini humo. Hii iliwafanya pia pasipo kushauriana na Wabelgiji kama ilivyo desturi walimsimika Kigeli V Ndahindurwa ambaye ni ndugu yake yake marehemu Mfalme Rudahigwa kuwa mfalme mpya wa Rwanda.




Watusi wakaanzisha kampeni ya kuwataka Wabelgiji waachie uhuru wa Rwanda haraka kabla ya uchaguzi uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka 1959 kufanyika. Wakaunda na chama cha cha kuongoza vugu vugu hilo, ambacho walikiita “Union Nationale Rwandaise” (UNAR).


Kutokana na hasira UNAR walianza kufanya mambo ya kipuuzi ambayo yalisababisha chama hicho kupingwa kila kona sio tu kwa sababu ya kuwa chama cha kitusi tu. Mfano walianza kushinikiza somo la ‘European History’kuondolewa mashuleni. Walishinikiza pia wamishionari wote waondoke nchini Rwanda. Matokeo yake chama hiki cha kitusi cha UNAR kikajenga taswira kuonekana kama chama chenye kupinga ukristo na mahususi kupinga kanisa katoliki.




Hii ikasababisha kanisa katoliki kuanza kuunga mkono wazi wazi vyama vya kihutu kama vile APROSOMA cha Gitera.









47ab2ee1aab616c7b14268b424a7fa02.jpg

df62a81fd348e05e5b9df1368877778f.jpg

4a13a980b1043379f70b968a47544fa5.jpg

Mfalme Kigeli V wa Rwanda miaka ya 1950s


Wahutu wengine wanaharakati nao wakaona fursa hapa. Kwa mfano Kayibanda alisajili rasmi vuguvugu lake la MSM na kulifanya kuwa chma cha siasa ambacho alikiita “Parti du Mouvement de l’Emancipation Hutu” (PARMEHUTU).


Kayibanda na chama chake cha PARMEHUTU wakaanzisha kampeni za nchi nzima kutaka taifa linalojitegemea la kabila la Wahutu pekee.




Mpaka kufika mwezi octoba mwaka 1959 bunge lilikuwa limepitisha kuwa mwezi unaofuata Novemba ndipo uchaguzi ufanyike.




Wahutu walikuwa wanashangilia kwa vifijo kwa kuwa walikuwa wna uhakika wa ushindi kwenye uchaguzi kutokana na wingi wao. Lakini Watusi walikuwa wapo kwenye hofu kuu. Hali ya nchi ilikuwa tete haswa.




‘Wingu’ zito kabla ya ‘mvua’….




Siku ya tarehe 1 November mwaka 1959, Dominique Mbonyumutwa moja ya viongozi wa Kihutu ambaye pia alikuwa mwanaharakati wa chama cha PARMEHUTU akiwa na mkewe wakitokea kanisani mitaa ya Byimana, eneo la Gitarama alifuatwa na vijana wa chama cha kitusi cha UNAR ili atie sahihi barua inayopinga uwepo wa Wabelgiji nchini Rwanda. Yalitokea mabishano makali huku Mbonyumutwa akikataa kutia sahihi waraka huo. Mabishano haya yalisababisha vijana hawa wa UNAR kuanza kumpigaMbonyumutwa na mkewe. Baada ya kipigo kikali Mbonyumutwa na mkewe walifanikiwa kujiokoa na kutimua mbio mpaka nyumbani kwao. Lakini mitaani ukaanza kuenea uvumi kwamba vijana wa kitusi wa UNAR wamempiga mwanaharakati wa kihutu Mbonyumutwa na mkewe mpaka kumuua.




Taarifa hii iliyokuwa inaenea kwa kasi ilikuwa kama njiti ya kiberiti kwenye jamii ambayo tayari ilikuwa kwenye hali tete ya chuki iliyokuwa inatokota kwa miezi kadhaa. Siku hiyo hiyo vijana wa Kihutu nao wakaanzisha kampeni ya kuchoma moto nyumba za Watusi.


Mwanzoni yalianza kama maandamano ya kupinga kitendo cha Mbonyumutwa ‘kuuwawa’ lakini baadae maandamano hayo yaligeuka kuwa machafuko yenye lengo la kuchoma moto nyumba za watusi na kila mtusi ambaye alikuwa anataka kuwazuia vijana wa kihutu wasichome nyumba yake alikuwa anauwawa. Mwanzoni machafuko yalianzia kwenye eneo dogo la Ndiza lakini kufumba na kufumbua machafuko yalienea nchi nzima. Watusi wengi wakaanza kukimbilia Congo na Uganda ili kunusuru maisha yao.




Wabelgiji walikuwa wamenyamaza kimya kabisa wakiangalia Wanyarwanda wakiwa wanauana na kuchomeana nyumba moto. Walikuwa wanaogopa kuingilia mzozo huu kutokana na uwingi wa Wahutu. Kwa kipindi hiki Ubelgiji walikuwa na wanajeshi 300 tu ndani ya Rwanda. Kwa hiyo “wakaacha wafu wauane”. Machafuko yalipozidi na Watusi wengi kuwawa, Mfalme Kigeli aliomba ruhusa kwa Wabelgiji kuunda jeshi la dharura lakini wabelgiji walikataa kata kata. Walikuwa wanaogopa kuwapa silaha Mfalme(watusi) kwani walihisi ndio wangekuwa kama wana mwaga mafuta ya taa kwenye moto na kuukoleza zadi. Machafuko yangegeuka na kuwa mabaya zaidi.




Licha ya Wabelgiji kumnyima ruhusa Mfalme Kigeli kuunda jeshi la dharura lakini Kigeli alikaidi na kukusanya maelfu ya vijana wa kitusi na kuwapa silaha za jadi na













296c3541295c18cfad3d161b6f3088e1.jpg

f08ad2945977d91d59c2cfd54d7f2fd9.jpg

Machafuko ya mwaka 1959 nchini Rwanda



523e5f5865e92892f74718df9aa72d56.jpg

Watusi wakikimbia Rwanda kwenda Tanzania, Uganda na Congo




bunduki chache. Kigeli aliwapa amri ya kuwatafuta na kuua viongozi wote wa kihutu. Mamia ya viongozi wa kihutu waliuwawa. Moja ya hao walio uwawa alikuwa ni ndugu wa Gitera kiongozi wa APROSOMA. Mamia wenginewalikamatwa na kupelekwa kwenye ikulu ya Mfalme iliyoko Nyanza ambako waliteswa na kisha kuuwawa.




Kayibinda, kiongozi wa PARMEHUTU alikuwa mafichoni kusikojulikana kwa hiyo hakuweza kukamatwa. Gitera alijibu mapigo kwa kuunda jeshi lake pia. Siku ya tarehe 9 na tarehe 10 Novemba 1959 vikosi vya kitusi vya mfalme Kigeli vilivamia maeneo ya milima ya Save ambako ndiko kulikuwa na makazi ya Gitera. Mapambano makali yalitokea kati ya wahutu na vikosi vya mfalme Kigeli mpaka ambapo wabelgiji waliingilia kati kuzuia damu zaidi kumwagika.




Ili kuokoa jahazi, Gavana wa Rwanda na Burundi, Mbelgiji Jean-Paul Harroy alimuita nchini Rwanda kanali Guy Logiest ambaye alikuwa anaongoza majeshi ya Ubelgiji nchini Congo. Alipomuita alimpa jukumu moja tu, kurejesha amani na utulivu nchini Rwanda. Akampatia madaraka yote hata ya ‘ku-veto’ maamuzi ya Mfalme wa Rwanda.




Kanali Guy Logiest alikuja na falsafa rahisi tu. Aliamini wamba kadiri ambavyo Watusi wataendela kuwa wengi kwenye nafasi za utawala na kiserikali nchi hiyo kamwe haiweze kuwa na amni kwa kuwa wahutu ndio wengi zaidi. Ka hiyo akafanya mabadiliko makubwa kwenye mfumo wa serikali. Akateua upya maafisa wote wa kiserikali na nafasi hizo karibia zote aliwapa wahutu tena wanachama wa PARMEHUTU.




Baadae zikaendeshwa kesi kuhusu waliosababisha machafuko nchi nzima mwezi Novemba. Viongozi wengi wa Kitusi walihukumiwa jela huku wenzao wahutu wakiachiwa huru.




Mwaka uliofuata yaani 1960, Kanali Guy Logiest aliitisha uchaguzi nchini humo licha ya Umoja wa Mataifa kupinga uchaguzi usifanyike kwani unaweza kusababisha upya machafuko. Lakini mwezi June na July uchaguzi ulifanyikana jumla ya viti 229 vilikuwa vinawaniwa. Matokeo ya mwisho yalipotangazwa chama cha watusi cha UNAR kiliambulia viti 19 kati ya viti vyote 229 huku chama cha wahutu cha PARMEHUTU wakijizolea viti karibia vyote vilivyobaki.




Mfalme Kigeli akavuliwa madaraka yote na kisha kuwekwa kizuizini nyumbani kwake kusini mwa Rwanda. Mwishoni mwa mwezi July alitoroka na kuanza kuishi kwa kuhama hama akizunguka nchi tofauti tofauti ndani ya AfrikaMashariki. Baadae alikimbilia nchini Marekani ambako aliishi mpaja kupatwa na umauti mwaka jana 2016 Octoba 16 akiwa na miaka 80.




July mwaka 1962 Rwanda ilijipatia Uhuru kamili huku PARMEHUTU kikiwa kama chama tawala na Kayibinda akiwa Rais.




Licha ya wahutu kushika madaraka na kuongoa nchi lakini bado mioyoni walikuwa wanafurukuta kwa visasi na vinyongo kutokana na kuhisi walinyanyaswa kwa miaka mingi sana na watusi. Kwahiyo mateso kwa watusi yaliendelea. Wahutu wengi walihisi kwamba watusi hawastahili kuwemo ndani ya Rwanda. ‘The purge’ ikaendelea.





21a67e6b5455ce0c9d486bc03caf9633.jpg

84108bbf94a45c92e0ce582b0ebe23d5.jpg

Mfalme Kigeli V akiwa nchini Marekani kabla ya kifo chake mwaka jana 2016 October




Hii iliwalazimu Watusi wengi kukimbia Rwanda kwenda Uganda, Congo na hapa kwetu Tanzania na kuwa wakimbizi. Wakiwa huko kwenye kambi za wakimbizi Watusi walianza kuunda vikundi vya wapiganaji ambavyo vilijulikana kama ‘inyezi’ (cockroaches (mende)). Vikundi hivi mara kwa mara vilivamia Rwanda kwa lengo la kutaka kufanya mapinduzi ili kurudisha utawala wa Kitusi, lakni hawakuwahi kufanikiwa wala kufua dafu mbele ya serikali ya PARMEHUTU. Sana sana walikuwa wanazidisha hasira za Wahutu dhidi ya Watusi wenzao ambao bado walibakia ndani ya Rwanda kuteswa, kunyanyaswa na kuuwawa.




Mpaka kufikia mwaka 1964 kulikuwa na karibia wakimbizi wa Kitusi 300,000 kwenye nchi za Congo, Uganda na hapa Tanzania.



ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog