Simulizi : Plata O Plomo Ulimwengu Wa Siri Kiganjani Kwa Binadamu Mmoja [ Pablo Escobar]
Sehemu Ya Pili (2)
Mwaka 1985 baada ya mabishano ya muda mrefu bungeni kuhusu vifungu vya kikatiba vinavyokataza raia wa nchi ya Colombia kukabidhiwa kwa nchi ya kigeni akiwa kama muhalifu hatimae serikali ikafungua kesi ya kikatiba mahakama kuu ya Colombia ikitaka ruhusu ya kukabidhi baadhi ya wahalifu kwa serikali ya Marekani ikitokea wakikamatwa.
Suala hili lilikuwa linamlenga moja kwa moja Pablo Escobar kwani serikali ya Colombia ilikuwa inapewa shinikizo kubwa na Marekani kuwa wafanye marekebisho ya katiba ili iruhusu raia wa nchi hiyo ambaye ni muhalifu kukabidhiwa kwa nchi ya kigeni. Haya yalikuwa ni maandalizi endapo ikitokea Pablo Escobar akikamatwa.
Pablo akajitahidi kwa juhudi zake zote kuhonga serikalini na hata kutoa onyo kuwa mabadiliko hayo ya kikatiba yasifanyike lakini serikali iliendelea na mchakato kutokana na shinikizo walikuwa wanapata kutoka kwa marekani.
Inajulikana kwamba Pablo mara kwa mara alikuwa akiapa mbele za watu wake wa karibu kuwa kamwe hatokubali kufungwa katika nchi ya marekani na alikuwa na msemo anaoupenda kuusema kwamba "ni heri kuwa kaburini Colombia kuliko kuwa hai kwenye gereza la Marekani".
Baada ya juhudi zake zote za kuionya serikali kutobadili katiba kushindikana hatimaye Pablo akakodi kikundi cha wapiganaji wa msituni kilichoitwa M-19 ili wasaidie kumaliza tatizo lake.
Siku ya Novemba 6, 1985 majaji 25 wa mahakama kuu walikuwa katika vikao vya mwisho kujadili na hatimae waweze kuridhia mabadiliko hayo ya katiba lakini kabla ya kumaliza vikao vyao na kuridhia mabadiliko hayo walivamiwa na wapiganaji wa kikundi cha M-19.
Wapiganaji hawa walivamia na kuteka mahakama kuu kwa muda wa siku mbili na zaidi ya nusu ya majaji waliuwawa na waliosalia walichukuliwa mateka.
Majaji hawa waliochukuliwa mateka walikuja kutumiaka kama sharti muhimu la kuibana serikali waache kurekebisha katiba ili waweze kuachiwa. Baada ya serikali kukubali kuacha kubadili katiba hasa kipengele cha kukabidhi wahalifu kwa nchi ya kigeni, majaji wote waliotekwa wakaachiwa.
Pili; Mauaji Mgombea Urais Luis Carlos Galán
Tukio la pili linalokumbukwa sana la utekelezaji wa sera ya 'Plata o Plomo' lilikuwa ni mauaji ya mgombea Urais wa Colombia aliyeitwa Luis Carlos Galán. Galán alikuwa anaongoza kwenye kura za maoni nchi nzima na alikuwa anatarajiwa kushinda kwenye uchaguzi mkuu wa urais wa Colombia wa mwaka 1990.
Moja ya sera kubwa aliyokuwa anaihubiri kila kona ya nchi ilikuwa ni kupambaa na Magenge ya Mihadarati hasa hasa akililenga Genge la Medellíne Cartel na kiongozi wake Pablo Escobar.
Pablo alimtumia barua kadhaa ambazo ziliwekwa nje ya nyumba yake kwenye kisanduku cha barua akimuonya na kumtaka aachane na sera hiyo ya kumsakama yeye pamoja na washirika wake wa Medellíne Cartel lakini Bwana Galán alionekana dhahiri amezamilia kutekeleza sera hiyo endapo angechaguliwa kuwa rais wa Colombia.
Akiwa katika kampeni Bwana Galán alifanikiwa kufika kwenye mji wa Madellín ambapo Pablo alikuwa na ushawishi mkubwa na wapo wananchi waliojaribu kumuua Galán kwa kumrushia guruneti la kutupa kwa roketi (Rocket Propelled grenade) lakini kwa bahati nzuri Bwana Galán akisalimika.
Baada ya hapo Pablo akakodi wadunguaji maalumu kufatilia nyendo za Galán na akawapa amri ya kumpiga risasi mara tu wakipata upenyo wa kufanya hivyo.
Wiki kadhaa baadae akiwa kwenye kampeni katika mji wa Saocho Kiranga alipokwenda kuhutubia wafuasi wake wapatao 10,000 waliokusanyika wakisubiri kumsikia na mara baada ya kuwasili na kupanda jukwaani kuhutubia kabla hajatoa hata salamu kwa wafuasi wake alidunguliwa na risasi na kupoteza maisha papo hapo.
Tukio hili lilizua taharuki nchi nzima na imekuwa skendali yenye utata mpaka leo hii nchini Colombia kwani kuna tetesi kuwa viongozi wa serikali, polisi, pamoja na mashushushu walishirikiana na Pablo Escobar kutekeleza mauaji haya.
Licha ya Pablo kuonekana kama adui namba moja nchini marekani na baadhi wa watendaji wa serikali ya Colombia hali ili kuwa tofauti kwa raia masikini wa Colombia ambao wengi wao walimuona kama shujaa wao na katika mji aliozaliwa na kushi wa Medellín anaonekana zaidi ya shujaa kwani mpaka leo hii wanamuona kama ni aina fulani hivi ya masihi walipewa.
Hii inatokana na umahiri wa Pablo Escobar katika mahusiano na jamii iliyokuwa inamzunguka.
Pablo alikuwa ni mtu mwenye kusaidia masikini nchini Colombia pengine kuliko hata serikali yenyewe.
Pablo alijitolea kweli kweli katika kuboresha huduma za jamii kama vile kujenga mahospitali, shule, nyumba za wazee, nyumba za kuishi kwa ajili ya masikini na akawekeza fedha nyungi kujenga miundo mbinu ya Kanisa Katoliki na nyumba za kuabudia. Pia Pablo alijenga vya kuendeleza watoto katika mpira wa miguu, alifadhili klabu mbali mbali za wakubwa za mpira wa miguu na alijenga viwanja vya kisasa kabisa vya mpira na michezo mingine.
Ilifikia hatua mpaka Pablo alikuwa anawapa fedha taslimu wananchi wa Madellíne ili waweze kujikimu kimaisha.
Mambo haya yote yalifanya wananchi wampende na kufumbia macho uhalifu wote aliokuwa anaufanya.
Kwa mfano katika mji wa Madellín ilifikia hatua kana kwamba wananchi wote walikuwa ni walinzi wake binafsi kwani walikuwa wakimtonya kila walipoona polisi wageni wakiingia hata kwa siri kwenye mji huo. Au wakati mwingine walikuwa wakitoa taarifa za uongo au kukataa kusema chochote pindi wakiulizwa na vyombo vya ulinzi kuhusu nyendo za Pablo.
Hii ilimfanya Pablo azidi kujizatiti na kuongeza mahaba kwa wakazi wa Medellín na raia wa Colombia kwa ujumla.
VITA KUU YA KWANZA YA MAGENGE YA MIHADARATI.
Kuna msemo wanasema 'adui wa adui yako ni rafiki yako'! Swali: je, inakuwaje pale adui wa adui yako akitishia maslahi yako??
Adui wa Adui yako (Kikao cha Kwanza)
Hapo baadae nitaeleza kwa kifupi kuhusu kuibuka kwa genge lingine ambalo nalo lilishamiri katika biashara ya Cocaine lililoitwa Cali Cartel hivyo kufanya kuwe na uwepo wa magenge mawili yanayoshindana kibiashara yaani Medellín Cartel chini ya Pablo Escobar na Cali Cartel.
Licha ya ushindani wao wa kibiashara mwaka 1983 iliwabidi washirikiane kwa sababu za msingi kabisa. kuliibuka kikundi cha wahuni waliokuwa wanateka watu na kudai fedha kutoka kwa ndugu ili wawaachie. Baada ya kuteka ndugu kadhaa wa viongozi wa serikali wahuni hawa wakaanza kuteka ndugu wa mabosi wa Cartels na kudai pesa.
Moja ya watu muhimu waliowateka alikuwa ni Marta Nieves Ochoa dada wa moja ya mabosi wa Cali Cartel na watekaji walikuwa wanataka wapewe dila milioni 10 ili wamuachie. Hii ndio ilikuwa sababu kubwa ya mabosi wa Cali Cartel na Medellín Cartel kukutana ili kuweka mkakati maalumu ambao utapeleka ujumbe kwa wahuni na watekaji wote kuwa familia za mabosi wa Magenge ya mihadarati ni mwiko kuzigusa.
Katika kikao hiki cha kwanza Medellín Cartel na Cali Cartel waliunda kikosi kazi maalumu walichokiita Muerte a Secuestradores (Death to kidnappers (Kifo kwa Watekaji)) au kama kilivyojulikana kwa kifupi MAS.
Kila Genge lilichangia fedha, vifaa (silaha), na askari kwa ajili ya kikosi kazi cha MAS.
Kesho yake baada ya kikundi hiki kuundwa ndege ilipita juu ya uwanja wa mpira wa miguu kuliko kuwa na mechi kubwa ikifanyika na kumwaga vipeperushi kuhusu kutangaza zawadi nono kwa yeyeto atakayetoa taarifa kuhusu kufahamu lolote juu ya wahuni wanaoteka watu na kushinikiza wapewe hela. Jioni ya siku hiyo taarifa muhimu kutoka kwa wananchi zikaanza kuletwa na kikosi kazi cha MAS mara moja kikaanza kukamata wahuni wa vikundi vya utekaji na kuwatesa huku wakiwarekodi na kuwatumia wenzao wanaoshikilia dada wa bosi wa Cali Cartel.
Ndani ya siku tatu Marta Naives dada wa bosi wa Cali Cartel aliachiwa akiwa salama salimini na huo ndio ukawa mwisho wa magenge ya wahuni kuteka wanafamilia wa mabosi wa magenge ya mihadarati.
Kama ni rafiki yako, anaweza kuwa mshirika wako: Kikao cha Pili
Licha ya ushindani wa kibiashara kuendelea kuwepo kati ya Medellin Cartel ya Pablo Escobar na Cali Cartel lakini kufanikiwa kwa mkakati wa MAS kuliwapa moyo kuwa yako maeneo mengine mengi wanayoweza kufanya kwa kushirikiana na yakawa na faida kwa pande zote mbili.
Sehemu ya kwanza ambayo waliona inaweza kuwa na faida kwa pande zote mbili ilikuwa ni Cali Cartel kukubali Pablo Escobar aweze kupitisha fedha zake haramu katika benki ya First InterAmericans Bank ambayo ilikuwa inamilikiwa na maswahiba wa mabosi wa Cali Cartel. Hii ilikuwa na faida kwa kubwa kwa Pablo kwani ilikuwa ni njia rahisi na salama kwake kuweza kusafisha fedha zake haramu lakini pia ilikuwa na faida upande wa wamiliki wa benki maswahiba wa mabosi wa Cali Cartel kwani nao wangepata faida kwa kutoa huduma hiyo kwa Pablo kutokana mabilioni ya dola ya dola ambayo atakuwa anayapitisha kwenye benki yao.
Sehemu ya pili waliyokubaliana kushirikiana ilikuwa ni namna ya kuratibu bei ya Cocaine mtaani, kuratibu viwango vya ubora wa uzalishaji na njia salama za kusafirisha mizigo.
Sehemu ya tatu walikubaliana kuhusu kugawana soko. Cali Cartel wakakubaliwa kuendesha biashara kwenye jiji la New York na Medellín Cartel ya Pablo Escobar wakapewa Florida na Miami. Jiji la Los Angels likaachwa kama sehemu huru ambayo yeyote anaweza kufanya biashara.
Kwa pamoja wakasonga na biashara ikashamiri.
Rafiki yako anapotishia maslahi yako: Vita Kuu ya Kwanza (Pablo Escobar VS Cali Cartel).
Biashara ya madawa ya kulevya katika America ya Kusini na duniani kote kwa miaka yote imetawaliwa na vita kati ya magenge yanayopambana ili kumiliki na kujipatia ushawishi zaidi katika soko. Lakini katika historia hakuna vita ya magenge ya mihadarati iliyotisha na kuitikisa Marekani na Amerika ya Kusini kama vita kati Medellín Cartel ya Pablo Escobar dhidi ya Cali Cartel.
Vita hii ilitishia hata usalama wa uwepo wa Taifa la Colombia na kuleta aibu kubwa kwa serikali za Colombia na Marekani.
Lakini kabla sijaeleza chochote kuhusu vita hii, nieleze kwa ufupi tu kuhusu Cali Cartel.
The Cali Cartel
Cali Catel ilianzishwa mwishoni mwa miaka ya 1970 kikiwa kama kikundi maalumu cha wapiganaji kilichokuwa kinatumiwa na Pablo Escobar na kilijulikana kama Las Chemas.
Moja wapo ya kazi walizozifanya kwa mafanikio ilikuwa ni utekaji wa raia wawili wa nchi wa uswisi na wakalipwa kiasi cha dola laki saba.
Baada ya malipo haya washirika wa kikundi cha Las Chemas wakajitenga na Pablo Escobar na kukimbilia kusini mwa nchi ya Colombia katika mji wa Cali na wakatumia fedha hiyo kuanzisha biashara yao ya mihadarati na wakafahamika kama The Cali Cartel.
Baada ya biashara yao kuanza kukua wakafanikiwa kuwashawishi wanajeshi kadhaa waasi na kujiunga nao katika biashara na wakafanikiwa kuwapata wengi.
Uwepo wa wanajeshi katika Cali Cartel unadhihirishwa na mfumo wao wa kibiashara pamoja na uwezo wao wa kufanya upelelezi na ushushushu (counterintelligence).
Kwa mfano mfumo wao wa kibiashara ulikuwa tofauti na Medellín Cartel ya Pablo Escobar ambayo yenyewe ilikuwa ni genge linalomilikiwa na mtu mmoja (Pablo) ambapo Cali Cartel wenyewe walikuwa ni muunganiko wa wafanyabiashara wanaojitegemea wanaounda genge/mtandao mmoja wa mihadarati (Cali Cartel).
Kwa upande wa ushushushu na upelelezi walikuwa mahili kiasi kwamba katika baadhi ya ripoti za CIA walikuwa wanawaita kwa jina la utani "Cali the KGB", wakiwafananisha na shirika la upelelezi la Urusi ya kipindi hicho.
Turejee kwenye...'Vita Kuu'
0 comments:
Post a Comment