Search This Blog

Tuesday 20 December 2022

PLATA O PLOMO ULIMWENGU WA SIRI KIGANJANI KWA BINADAMU MMOJA [ PABLO ESCOBAR] - 1

 


http://pseudepigraphas.blogspot.com/2020/06/plata-o-plomo-ulimwengu-wa-siri_10.html

IMEANDIKWA NA THE BOLD

************************************************************************

Simulizi : Plata O Plomo  Ulimwengu Wa Siri Kiganjani Kwa Binadamu Mmoja [ Pablo Escobar] 

Sehemu Ya Kwanza (1)



Katika milima inayotazamana na mji wa Medellín nchini Colombia, yapo majengo ya kifahari kabisa ndani ya milima hiyo ambayo kwa sasa majengo haya yanatumika kama nyumba ya watawa wa Kanisa Katoliki lakini kabla ya watawa hawa kupewa majengo haya mwaka 2007, majengo haya yalikuwa ni gereza ambalo lilijengwa mwaka 1991 kumuhifadhi mfungwa maalumu raia wa Colombia.


Gereza hili lilikuwa ni tofauti kabisa na magereza yote ambayo umewahi kuyasikia kwani gereza hili licha ya kuwa mali ya serikali lakini michoro yake ilichorwa na kubuniwa na mfungwa mwenyewe.


Si hivyo tu, bali hata maaskari magereza ambao walikuwa wanalinda gereza hili walichaguliwa na mfungwa mwenyewe na hata polisi wa nchi ya Colombia walikuwa hawaruhusiwi kusogolea gereza hilo hata umbali wa maili 12. Kama hiyo haitoshi gereza hili lilikuwa na uwanja wa mpira wa miguu, lilikuwa na bafu lenye Jaccuzi, lilikuwa na bar, lilikuwa na maporomoko ya maji (water falls) yaliyobuniwa kiustadi, na pia chumba (selo) alicholala mfungwa huyu kilikuwa na kitanda kikubwa cha duara chenye kuzunguka pamoja na televisheni kubwa.


Kama hii haitoshi kwenye gereza hilo pia kulikuwa na chumba maalumu cha michezo ya watoto maalumu kwa ajili ya watoto wa mfungwa huyo pindi akitembelewa na familia yake. Na pia ndani ya gereza kuliwekwa darubini kali (Telescope) ya kumuwezesha mfungwa huyo kuangalia katika mji wa Medellín ambako familia ya mfungwa huyu iliishi na kila siku jioni walitoka nje kibarazani kuongea naye kwenye simu huku akiwatazama kwa darubini.


Gereza hili lilijulikana kama La Catedral (the cathedral) na lilimuhifadhi mfungwa muhimu zaidi duniani na binadamu aliyeifinyanga na kuifanya biashara ya mihadarati iwe jinsi ilivyo hivi leo. Marafiki zake wa karibu walipenda kumuita El Patrón (The Boss) au El Zar de la Cocaína (The Tsar of Cocaine) lakini alipozaliwa wazazi wake walimuita Pablo Emilio Escober Gaviria au kwa kifupi Pablo Escobar kama ulimwengu wote ulivyomtambua.


The Boss


Akiwa mtoto wa tatu kwenye familia ya watoto saba ambapo baba yake alikuwa ni mkulima na mama yeke mwalimu wa shule ya chekechea, Pablo Escobar alikuwa ni mwenye kutamani mambo mazito na mwenye maono makubwa tangu angali mtoto.


Akiwa bado kwenye umri wa makumi (teenage) Pablo mara kwa mara aliwaambia ndugu zake na marafiki zake kuwa anataka awe na utajiri wa kiasi cha Peso Milioni 1 za Colombia (COL$ 1 Million) atakapofikisha umri wa miaka 22.


Ndoto hizi zilimfanya ashindwe kumaliza Chuo kikuu alipokuwa anasoma (Universidad Autónoma LatinoAmericana of Madellín) na kujiingiza katika biashara za halali na haramu na hatimaye aliacha masomo chuoni. Moja ya biashara zake haramu za kwanza kabisa akiwa kijana chini ya miaka 21 ilikuwa ni kutengeneza vyeti bandia vya stashahada vya chuo alichokuwa anasoma na kuwauzia watu waliohitaji kwa ajili ya kwenda kupata ajira.


Pamoja na biashara hiyo pia Pablo alijihusisha na kusambaza mizigo ya sigara zilizokuwa haziruhusiwi nchini Colombia (Marlboro), pia alifanya kazi kama mlinzi binafsi (bodyguard) pamoja na wizi wa magari.


Moja ya matukio muhimu ya ujana wa Pablo yaliyochangia kuamsha ari ndani yake na kumfanya atamani kuwa moja wa manguli wa biashara haramu lilikuwa ni tukio ambalo alipofikisha miaka 26 alifanikiwa kuweka benki (Cash Deposit) kiasi cha Peso Millioni 100 za Colombia (COL$ 100 Million).

Mafanikio haya yaliwasha taa ndani yake na kuamsha ari ya kutaka kuwa 'Papa' katika 'Dunia' ya siri ya ulimwengu wa biashara haramu.


Katika miaka ya 1970 mamlaka ya kupambana na matumizi mabaya ya madawa nchini marekani (US Drug Enforcement Agency) waliwahi kutangaza kuwa wamewekeza zaidi rasilimali zao kupambana na matumizi na uingizaji wa dawa aina ya Heroin nchini marekani na kwa maoni yao walisema kuwa wanadhani madawa aina ya Cocaine hayakuwa na uwezo wa kuleta uteja (addiction) au kufanya mtumiaji kuwa muhalifu tofauti na dawa aina ya Heroin. Hivyo basi walielekeza nguvu zao zote na rasilimali kupambana na biashara ya usafirishaji wa Heroin kama kipaumbele cha kazi zao.


Hili lilikuwa ni kosa kubwa sana kwa upande wao. Kwani kijana Pablo aliona mwanya huu na udhaifu huu upande wa DEA au pengine tusema kwamba Pablo alifahamu zaidi kuhusu ulimwengu wa mihadarati kuliko DEA.


Kitu kikubwa ambacho Pablo alikiona na watu wakiwemo DEA hawakukiona ilikuwa ni uwezekano (potential) ya kuifanya Cocaine kuwa moja ya madawa yenye soko zaidi Amerika ya Kaskazini. Katika kipindi hiki kulikuwa na watumiaji wachache sana wa Cocaine nchini marekani lakini Pablo aliona fursa ya kuifanya mihadarati hiyo kuwa moja ya madawa yenye kuhitajika sana nchini marekani na ulimwenguni kiujumla.


Kutokana na uzoefu wake wa ulimwengu wa kihalifu, Pablo aligundua kuwa zao la Coca linalimwa nchini Bolivia ambalo linatumika kutengeneza Cocaine ni bora zaidi kuliko Coca inayolimwa nchini kwake Colombia. Hivyo basi Pablo akadhamiria kuwa kama anaingia kwenye biashara hii ya kusafirisha Cocaine ni lazima mihadarati yake iwe tofauti na bora zaidi kuliko Cocaine nyingine watu waliyozoea kutumia. Akadhamiria kufanya Cocaine yake iwe daraja la kwanza ili kuvutia watumiaji na kufanya soko likue kwa haraka.


Kama sehemu ya mkakati wake wa kuingia rasmi kwenye biashara ya kusafirisha mihadarati aina ya Cocaine, mwaka 1975 kijana Pablo alisafiri mpaka nchini Bolivia kukutana na Roberto Suaréz Goméz ambaye marafiki zake walipenda kumuita El Padrino (The Godfather) kiongozi wa Genge lililoitwa La Corparacíon (The Corporation). Suaréz alikuwa ndiye mtu pekee anayeendesha na kuratibu uzalishaji wa zao la Coca katika nchi ya Bolivia na Peru. Kipindi hiki Suaréz tayari alikuwa na mtandao mkubwa katika America ya kusini na alikuwa na jina kubwa, ushawishi na nguvu ya kijeshi hivyo haikuwa kazi rahisi kwa kijana Pablo kumshawishi Suaréz akubali kufanya naye biashara.


Huyu bwana Suaréz alikuwa na nguvu kiasi kwamba alikuwa na jeshi lake binafsi la anga (Air force) na wanajeshi wa miguu 1,500 ambao walipatiwa mafunzo nchini libya.

Pablo alitumia uwezo wake wa kujieleza na uzoefu wake wa ulimwengu wa kihalifu kumshawishi Suaréz na kumueleza kuhusu mkakati wake wa kuiteka biashara ya mihadarati ya Cocaine nchini marekani na akamdadavulia jinsi ambavyo yeye Suaréz atapata utajiri wa kupindukia kama atakubali kufanya nae biashara.


Pia Pablo alimpa wazo Suaréz kuwa atumie ushawishi wake alionao serikalini (Suaréz alikuwa amefanikiwa kumpenyeza Mdogo wake serikalini na kuwa Waziri wa mambo ya ndani) ahakikishe wanakutana na kiongozi wa Cuba Fidel Castro ili wamuombe kuwa mshirika wao katika mambo kadhaa.


Suala hili lilifanikiwa kwani Pablo na Suaréz walipata fursa adhimu na wakakutana na Fidel Castro na ombi lao kubwa kwake lilikuwa ni kuwaruhusu kupitisha mizigo yao nchini kwake Cuba na nchi za jirani pasipo bugudha. Pia walimuomba aruhusu ndege zao za mizigo zitue kwenye viwanja vya ndege vya Cuba na kujaza mafuta pale inapobidi kufanya hivyo.


Castro akawakubalia kwa masharti mawili, moja ni kwamba atakuwa anawachaji mamilioni ya dola za marekani kwa huduma hizo na pili mihadarati hiyo isiuzwe ndani ya Amerika ya Kusini bali isafirishwe na kuuzwa Marekani ambapo Fidel Castro alisisitiza kuwa atafurahi akiona vijana wa Mabepari wakiharibika na mihadarati.


Masharti yote mawili haya yakakubaliwa na Pablo na Suaréz kisha wakarejea Bolivia. Baada ya kufanya mazungumzo juu ya namna watakavyo fanya biashara hatimae Pablo na Suaréz walifikia muafaka na kwa mzigo wake wa kwanza alioununua nchini Bolivia kutoka kwa Suaréz ulikuwa ni kilo 14 za unga gafi za Cocaine.


Baada ya unga gafi kufikishwa nchini Colombia kwenye mji wa Medellín, Pablo alikuwa ameandaa jengo maalum la ghorofa mbili ambalo alilitengeneza kuwa maabara maalumu ambapo Cocaine gafi kutoka Bolivia ilichanganywa na maligafi nyingine na kuboreshwa zaidi kikemia na hatimaye kupata Cocaine daraja la kwanza aliyoihitaji tayari kusafirishwa nchini Marekani kwa 'walaji'.


Baada ya Cocaine kutoka kwa Pablo kuingia kwenye soko la Marekani uhitaji na biashara ya mihadarati ya Cocaine ilipaa kwa kasi ya ajabu na Pablo Escobar akaanzisha rasmi genge lake la biashara ya mihadarati na akaliita Medellíne Cartel.


Pablo akatengeneza mtandao madhubuti wa wasambazaji wa mihadarati yake katika miji ya Florida na California pamoja na majimbo mengine ya Marekani.

Pia akabuni njia mpya ya kupitisha mihadarati kupitia Bahamasi katika kisiwa cha Norman's Cay takribani kilomita 350 kusini mashariki mwa pwani ya Florida.


Ili kufanikisha zaidi azma yake Pablo Escobar alinunua nusu ya ardhi ya kisiwa cha Norman's Cay na nusu nyingine ikanunuliwa na swahiba wake wa kimarekani aliyeitwa Robert Vesco ambaye pia alikuwa ndiye anashughulikia masuala yake ya kibenki na uhasibu.


Katika Kisiwa hiki Pablo alitengeneza uwanja wa ndege, bandari, hoteli, nyumba za kuishi pamoja na ghala kubwa la jokofu maalumu kwa ajili ya kuhifadhi mizigo ya Cocaine kabla ya kuisafirisha kwenda marekani. Kwa kifupi hapa ndipo kilikuwa kitovu cha kibiashara cha Genge lake la Medellíne Cartel.


Pablo Escobar alikuwa amepania haswa kuliteka soko la Cocaine Amerika ya Kaskazini na hii ilijidhihirisha kutokana na juhudi zake alizozifanya kibiashara ili mda wote awe hatua kadhaa mbele tofauti na washindani wenzake kibiashara.


Ili kufanikisha usafirishaji wa mizigo yake kwa ufasaha na uhakika Pablo alinunua ndege za mizigo 15 za ukubwa wa kati na helikopta 6. Pia alinunua Nyambizi ndogo mbili (submarines) kwa ajili ya kusafirisha mizigo mikubwa ya mihadarati.


Hadi kufikia mwaka 1985 Pablo alikuwa anasafirisha takribani tani 70 mpaka 80 za Cocaine kwa mwezi na alikuwa ameshikilia asilimia 80 (80%) ya soko la mihadarati la Marekani.

Na katika kipindi hiki Genge lake la Medellíne Cartel lilikuwa linaingiza kipato cha cha Dola Milioni 70 kwa siku (Shilingi Bilioni 140 za Kitanzania) na mapato yao kwa mwaka mzima yalifikia Dola Bilioni 21.9. (Shilingi Trilioni 46 za Kitanzania).


Katika miaka ya 1990 utajiri wake binafsi ulifikia kiasi cha Dola za kimarekani Bilioni 30 ambazo ni sawa na Dola Bilioni 54 kwa hesabu za sasa (Shilingi Trilioni 110 za kitanzania)

Ni katika kipindi hiki ambacho Jarida maarufu la Forbes lilimuorodhesha Pablo Escobar kama mtu namba 5 tajiri zaidi ulimwenguni na muhalifu tajiri zaidi katika historia ya Ulimwengu.


Kutokana na nguvu na ushawishi alionao, Pablo aliteuliwa na serikali kama mjumbe wa baraza la wawakilishi la Colombia (Chamber of Representatives of Colombia) kupitia chama cha Kiliberali Cha Colombia (Colombia Liberal Party).


Moja ya majukumu muhimu aliyoyafanya akiwa kama Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kilikuwa ni kwenda kuiwakilisha Serikali ya Colombia katika sherehe za kuapishwa kwa Waziri Mkuu mpya wa Uhispania Bw. Felipe González mwaka 1982 ambapo Pablo alitumia nafasi hii ya Safari ya kiserikali nchini Uhispania kuanzisha tawi jipya la Genge lake la Medellíne Cartel katika nchi ya Uhispania.


Hacienda Nápoles: Pepo Juu ya Uso wa Dunia


Kutokana na utajiri uliopitiliza wa Pablo Escobar alithubutu kutengeneza makazi ya kuishi ambayo namna pekee ya kuyaelezea ni kana kwamba alijitengenezea 'pepo' akiwa duniani.


Katika mji mdogo wa Puerto Triunfo, takribani kilomita 150 kutoka katika mji wa Medellín, Pablo alinunua eneo lenye ukubwa wa Kilomita za mraba 20 na kujenga makazi yake na familia yake na akayaita makazi haya Hacienda Nápoles (Naples Estate).


Licha ya majengo ya kifahari ya kuishi yeye na familia yake pia makazi haya yaliwekwa anasa lukuki zisizomothirika. Ndani ya makazi haya kulikuwa na Uwanja wa ndege binafsi (private airport), bustani maalumu ya sanamu za kuchonga na kufinyanga (Sculpture Park), kulikuwa na sehemu maalumu ya kuhifadhi magari ya kifahari na pikipiki za kifahari kwa ajili ya kutazama tu (collection), kulikuwa na uwanja wa mbio za magari magogo (kart racing track), kulikuwa na uwanja wa mapigano ya ng'ombe (Bullring), na pia ndani ya makazi haya kulikuwa na mbuga ya wanyama ya kutengeneza (Zoo) ambapo Pablo alikusanya aina mbali mbali za wanyama kutoka kila kona ya dunia na kuwaweka humo.


Katika geti la kuingia kwenye 'pepo' ya Pablo sehemu ya juu ya geti ilininginizwa ndege (ndege halisi) kama urembo. Ndege hii aina ya Piper PA-18 Super Cub yenye namba ya mkia HK-617-P hii ndio ilikuwa ndege ya kwanza aliyoitumia Pablo kuingiza mzigo wake wa kwanza wa Cocaine nchini Marekani.


Hapa katika 'pepo' hii ndipo ambapo Pablo Escobar aliishi yeye na familia yake.


Plata o Plomo


Moja ya vitu muhimu vya kihalifu alivyovifanya Pablo na kufanikiwa kuibuka kama kinara wa uhalifu Amerika ya kusini ilikuwa ni kutekeleza sera yake aliyoianzisha yeye mwenyewe ili kuidhibiti serikali na vyombo vya ulinzi ambapo sera hii aliita "Plata o Plomo" (silver of lead (fedha au risasi)). Akiwa na maana kwamba kama wewe ni mtu wa serikali na ikitokea mmesigana basi atakupa fedha (rushwa) kama ukikataa kupokea fedha basi anakupiga risasi.


Sera hii ilimfanya Pablo aogopwe na watendaji wa serikali pamoja na vyombo vya usalama na ikapelekea wengi kukubali 'Plata' (silver (fedha)) wakihofia kupoteza maisha endapo wangekataa fedha kutoka kwa Pablo. Hii ilimsaidia Pablo Escobar kuwa na vibaraka wengi katika serikali na vyombo vya ulinzi na usalama.


Lakini sera hii iligharimu maisha ya watu wengi sana wale ambao walikataa kupokea fedha kutoka kwa Pablo na mojawapo ya matukio mawili yanayokumbukwa sana ya utekelezaji wa sera ya 'Plata o Plomo' ni haya:-


Mosi; Uvamizi wa Mahakama Kuu ya Colombia 1985.



    0 comments:

    Post a Comment

    Blog