Search This Blog

Saturday, 5 November 2022

ROHO NYEUSI - 1

 






IMEANDIKWA NA : INNOCENT A. NDAYANSE (ZAGALLO)



*********************************************************************************



Simulizi : Roho Nyeusi

Sehemu Ya Kwanza (1)



***** ***** ***** *****



KILA MWANADAMU AISHIYE CHINI YA JUA HUPENDA KUISHI MAISHA BORA. SUALA LINAKUJA KUWA NI VIPI UTAFANIKIWA. KILA MMOJA ANA MBINU YAKE YA KUTIMIZA NDOTO YAKE KWA NAMNA ANAYOONA INAFAA. RIWAYA HII INAGUSA JAMII TULIYONAYO NA IKIFICHUA YALE YALIYOTENDEKA MIAKA YA NYUMA NA YANAYOENDELEA KUTENDEKA. SONGA NAYO…



JANUARI, 1983



ILITOKEA kama aina fulani ya tamthiliya akilini na machoni mwa mzee Kipipa Mtakayote. Ikiwa ni siku ya Jumatano, saa 3:45 asubuhi, kama kawaida yake mzee huyo alikuwa dukani mwake, kaketi kitini akipokea oda na malipo kutoka kwa wateja mbalimbali waliofurika mbele ya kaunta.



Pamoja naye, pia walikuwapo wafanyakazi wake wawili, vijana wa kiume, waliokuwa wasaidizi wake wakuu dukani hapo.

Ni wakati akiendelea kutoa huduma hiyo, ndipo kile ambacho hakukitarajia, kile kilichomshangaza na kumfanya ahisi kuwa anashuhudia tamthiliya inayosisimua au anaota ndoto isiyopendeza, kilipomtokea mbele yake.



Watu wawili, wanaume wenye miili iliyojengeka vyema, warefu wa kadri ya futi tano kila mmoja, walifungua mlango mdogo uliotenganisha eneo la wateja na eneo la duka, wakapenya wakimfuata mzee Kipipa Mtakayote mezani.



Japo nyuso za watu hao zilinawiri, miili yao ikiwa imefunikwa na suti nyeusi, suti maridadi, hata hivyo macho na midomo yao havikuwa na uhusiano wowote na tabasamu. Mara tu walipokuwa mbele yake, mmojawao alitumbukiza mkono ndani ya mfuko wa shati lake na kuchomoa kitambulisho ambacho alimwonesha Kipipa Mtakayote na kwa sauti nzito, sauti ya chini, iliyojaa ukakamavu, akasema, “Tuko kazini, mzee. Tafadhali, simamisha shughuli zote za biashara yako.”



Yalikuwa ni maneno machache lakini yenye uzito wa kilo mia moja akilini mwa Kipipa Mtakayote. Hakuhitaji kutumia hata sekunde tano katika kuwatambua wageni hawa waliomjia bila ya taarifa. Kile kitambulisho alichooneshwa muda mfupi uliopita kilitosha kuitambulisha kazi yao.



Askari!



“Kuna nini? Kuna tatizo gani?” maswali yalimtoka Kipipa Mtakayote, macho yake madogo lakini makali yakiwatazama kwa zamu watu hao.



“Ni mapema mno kuzungumza chochote, mzee,” askari mwingine alisema. “Kwa sasa hatuna muda wa maongezi. Tunakushauri ufuate maelekezo yetu.”



“Lakini…!”



“Tafadhali, mzee,” askari wa awali alimkunjia uso na kumnyooshea kidole.



Mzee Kipipa Mtakayote alitii. Vitone vya jasho vikajiunda katika paji la uso wake. Upara wa asili uliotawala robo tatu ya kichwa chake ukazidi kumeremeta huku pia, kama ilivyotokea pajini, nao ukawa umeshavamiwa na vitone vya jasho.



Wakati hayo yakitokea, umati wa wateja haukujua. Wao waliendelea kuhimiza kupewa huduma, baadhi ya wenye nguvu wakiwasukuma wanyonge na kuwaacha wakinung’unika.

Mmoja wa wafanyakazi wa Kipipa alipokea pesa na kumpelekea mezani huku akisema, “Katoni mbili za betri, mzee.”



Mara kono la askari mmoja lilimzuia kijana huyo na kufuatiwa na amri kali: “Kaa chini!”



Sekunde chache baadaye mfanyakazi wa pili alipewa amri hiyohiyo. Kisha askari mmoja akawageukia wateja na kuwaambia kwa sauti kubwa, “Tafadhalini wateja, mnaombwa kuondoka kwa utulivu. Huduma imesimama kwa muda hadi hapo mtakapotaarifiwa tena.”

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Umati ule ulishangaa. Minong’ono ikazuka.



“Kwani kuna nini?” mmoja alimuuliza jirani yake.



“Hata mie sijui.”



“Kwani vipi tena?” mzee mmoja aliyevaa kanzu nyeupe na baraghashia kichwani, alihoji kwa sauti kubwa.



“Ni amri!” askari mmoja alijibu huku akimtazama mzee huyo kwa macho makali. Kisha, kwa msisitizo mkali, macho yake yakitambaa takriban kwa kila mteja, aliongeza, “Tafadhalini ondokeni. Hii ni amri ya serikali. Full stop!”



Taratibu, kama walionyeshewa mvua, wateja hao waling’atuka mmoja baada ya mwingine ndani ya duka hilo. Na wakati wakitoka huku wakishangaa na kujiuliza maswali mengi, mara wakaona Land-Rover yenye askari wasiopungua kumi wakiwa na silaha mikononi ikiegeshwa nje ya duka hilo.



“Kwani mzee Kipipa kakosa nini?” mama mmoja alimdadisi mwanamke mwingine ambaye naye alikuwa akiondoka katika eneo hilo.



Hakujibiwa.



******



MWISHONI mwa mwaka 1978, Taifa la Tanzania lilikumbwa na dhoruba kali, dhoruba ambayo ni vigumu kufutika katika historia ya nchi kwa karne zijazo. Majeshi ya Uganda, nchi ambayo kwa wakati huo ilikuwa ikitawaliwa na Dikteta Idi Amin Dada, yaliivamia Tanzania kupitia kaskazini mwa Mto Kagera katika mkoa ambao wakati huo uliitwa Ziwa Magharibi. Ulikuwa ni uvamizi mkubwa, uvamizi ulioambatana na vitendo vya kikatili vikiwamo vya mauaji ya kinyama dhidi ya wanaume na watoto, wanawake wakabakwa na hatimaye kuuawa vilevile.



Askari hao waliokuwa na mioyo isiyotofautiana na ya malaika wa shetani, pia walidiriki kuchoma moto baadhi ya mashamba na nyumba za Watanzania huku wakikusanya vitu ambavyo waliona vingewafaa hususan magari na samani za ndani.



Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi chache duniani zenye kuheshimu uhuru wa nchi nyingine na kupenda amani na utulivu, kwa tukio hilo ilishindwa kuvumilia. Ivumilie vipi wakati tayari mamia ya raia wake wameuawa kikatili? Ivumilie vipi wakati viwanda kadhaa vilivyotengeneza bidhaa zilizolinufaisha taifa kiuchumi vimeteketezwa na wavamizi hao? Ivumilie vipi wakati nyumba za makazi ya raia na nyumba za ibada zimebomolewa na vifaru pamoja na makombora ya mizinga ya majeshi hayo?



Naam, taifa halikuvumilia. Likaingia vitani. Vikawa ni vita vikali, vita vilivyoyagharimu maisha ya Watanzania wengi. Pia, vilikuwa ni vita vilivyouteteresha uchumi wa nchi kwa kiasi kikubwa. Ingawa ushindi ulipatikana katika vita hivyo vilivyopiganwa ndani na nje ya ardhi ya Tanzania, lakini ulikuwa ni ushindi uliowaachia Watanzania makovu yasiyofutika.



Mamilioni ya Watanzania walijikuta wakitumbukia katika mkondo mwingine wa maisha. Gharama za maisha zilipanda maradufu. Wananchi, hususan wale walioshi maisha ya daraja la kati na la chini wakawa katika kipindi kigumu, labda zaidi ya vipindi vingine vigumu vilivyopita.



Ndiyo, ni wengi walioathiriwa na vita hivyo. Ni wengi, siyo wote. Walikuwapo baadhi, ambao kwa kutumia njia hii na ile na hila hizi na zile, walifanikiwa kula raha watakavyo, wakiyaendesha maisha kwa mifumo waliyoichagua. Hao, walizinufaisha nafsi zao na familia zao pekee.



Mmoja kati ya hao walioelea peponi ni Kipipa Mtakayote, mfanyabiashara maarufu, aliyekuwa nguzo kuu na tegemeo kwa wakazi wa Mkoa wa Songambele, mkoa uliokuwa miongoni mwa mikoa michache nchini Tanzania iliyofanikiwa kupiga hatua kimaendeleo katika nyanja mbalimbali.



Kipipa Mtakayote alikuwa na maduka kumi makubwa mkoani humo. Vituo saba vya mafuta ya nishati vilikuwa chini ya himaya yake. Alimiliki mabasi kumi na matano ya abiria yaliyofanya safari zake katika mikoa mbalimbali nchini Tanzania na hata nchi jirani za Kenya, Uganda, Malawi na Zambia. Isitoshe, alikuwa na viwanda viwili vya mafuta ya kula na vitatu vya sabuni za kuogea.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Alikuwa ni tajiri, na alistahili kuitwa tajiri mkubwa. Na utajiri wake si kwamba ulijulikana katika Mkoa wa Songambele pekee, la hasha. Ulijulikana nchi nzima. Utajiri huo uliompatia umaarufu mkubwa ulizidi kulitangaza jina lake baada ya kujihusisha na mambo mbalimbali ya kijamii. Kuna wakati alitoa mchango wa mamilioni ya pesa kwa vikundi vya walemavu.



Isitoshe, aliwahi kuhudhuria sherehe moja ya kitaifa, na akatoa ahadi mbele ya mkuu wa nchi kuwa angejenga hospitali kubwa kwa ajili ya wakazi wa Mkoa wa Songambele, ahadi iliyowafanya wakuu wa serikali wampongeze. Ndani ya miaka miwili hospitali hiyo ikawa imekamilika.



Kujitolea kuwa mfadhili wa timu moja maarufu ya soka, timu yenye mamilioni ya mashabiki nchini, ilikuwa ni hatua nyingine iliyomjengea hadhi kwa watu wa marika na jinsia zote.



Akiwa ni miongoni mwa matajiri wachache sana waliojulikana nchini, hakuwa na hiyana pale serikali ilipomtaka atoe magari yake kwa ajili ya kuwasafirisha askari wa Jeshi la Wapiganaji kwenda msitari wa mbele kupambana na Nduli Idi Amin Dada. Wala hakusita kutoa katoni kadhaa za mafuta ya kula kwa ajili ya wakombozi hao. Pia, serikali ilipoomba misaada ya vyakula kwa yeyote mwenye uwezo, yeye alikuwa ni mtu wa kwanza kutekeleza ombi hilo. Alitoa tani kumi za mchele zilizokuwa zimehifadhiwa katika maghala yake.



Kwa jumla, Kipipa Mtakayote alichukuliwa kama mmoja wa wananchi wenye mioyo safi, mioyo ya kujitolea, aliyelipenda, akalithamini na kulijali taifa lake. Ni taswira hiyo iliyowafanya wakuu wa vyombo vya dola na taasisi nyingine za serikali wamwone kama raia mwema, Mtanzania asiye na doa lolote katika biashara zake.



Ndiyo, alionekana hivyo, na zaidi alichukuliwa kuwa ni miongoni mwa wanadamu wachache sana barani Afrika, kama siyo dunia nzima, ambao kichwa cha mmojawao huwa na uwezo wa kufikiri, kupanga na hata kutatua tatizo ambalo lingewalazimu watu wazima wasiopungua kumi kufanya kikao maalumu katika kutafuta ufumbuzi.





AKIWAKA na historia ya mataifa kadhaa yaliyopigana vita japo vya miezi miwili tu, Kipipa Mtakayote aliyajua matokeo ya vita vilivyoikabili nchi yake ya Tanzania. Alitambua kuwa vita si lelemama. Vita baina ya mtu na mtu, au, vita baina ya nchi na nchi, ni jambo ambalo hugharimu pesa au maisha kutoka upande mmoja kama siyo pande zote.



Kufa vitani ni jambo la kawaida kwa nchi yoyote ambayo raia wake, hata viongozi wake wa ngazi za juu hutambua kuwa pindi litokeapo, haliwezi kuchukuliwa kama la ajabu na hasa kama vita hivyo vitahusisha silaha nzito, zilizotengenezwa kitaalamu zaidi.



Pia, vita hugharimu pesa. Kichwani mwa Kipipa Mtakayote hilo halikuwa na ubishi. Vita, hususan vita baina ya taifa moja na lingine hugharimu kiasi kikubwa cha pesa. Aghalabu huilazimu nchi iliyo vitani kuchota hata ile akiba ya hazina yake katika kupambana na vita hivyo. Na huenda pia nchi hiyo ikalazimika kukopa pesa au silaha kwa nchi zilizo rafiki ili tu mambo yaende kama ilivyopangwa.



Baada ya vita, nchi iwe imeshinda, iwe imeshindwa, mara nyingi huwa imetetereka kiuchumi kwa kiasi kikubwa. Kichwani mwake aliamini kuwa ni hilo litakaloikumba nchi yake.



Hivyo, akiwa na hakika ya kuaminika kuwa yu mtu safi, wakati nchi yake ikiwa vitani, yeye aliingia katika hatua nyingine. Akaanza kulimbikiza bidhaa mbalimbali katika maghala yake makubwa yaliyojengwa katika maeneo mbalimbali nchini. Bidhaa za kutoka ng’ambo, mathalani dawa za meno, sabuni za kufua na kuoga ziliagizwa kwa wingi na kuhifadhiwa kwa siri katika hayo maghala yake akidhamiria kuziuza baadaye kwa bei atakayotaka yeye.



Hakuishia kwenye bidhaa hizo tu. La. Uchu wa pesa ulizidi kumpanda, hivyo alianza kupunguza viwango vya mafuta ya nishati aliyouza katika vituo alivyovimiliki. Aliuza lita chache tu, robo ya viwango vya kawaida kisha hudai kuwa “mafuta yamekwisha” huku baadaye akiyauza kwa wale waliokuwa tayari kununua kwa bei aliyowapangia.



Isitoshe, alitambua kuwa mazao kama mchele na ngano ni bidhaa muhimu kwa mahitaji ya binadamu. Kwa hilo pia hakuzembea, pesa zilizungumza. Alinunua mamia ya tani za bidhaa hizo kutoka kwa wakulima na kufanya kama alivyofanya kwa bidhaa nyingine. Alifanya hivyo akiamini kuwa miezi kadhaa baadaye, pale vita vitakapomalizika, ataanza kufaidi matunda ya zoezi lake.

Alitarajia hivyo na akaamini kuwa hakuna litakaloharibika.



************



“…TUTAKUWA NA HALI NGUMU SANA KATIKA KIPINDI CHA MIEZI KUMI NA MINANE HIVI IJAYO…” Hiyo ilikuwa ni sehemu ya hotuba ya aliyekuwa kiongozi mkuu wa nchi, Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ndugu Julius Kambarage Nyerere, hotuba aliyoitoa miezi michache baada ya kumalizika kwa vita baina ya Tanzania na Uganda mwaka 1979.



Katika hotuba hiyo aliyoitoa siku ya kuwapongeza Mashujaa wa Jeshi la Wapiganaji, mkuu huyo alizungumzia hali mbaya ya kiuchumi iliyokuwapo kabla ya vita na kuongezeka maradufu baada ya vita hivyo. Hivyo, akawataka Watanzania kujifunga mikanda, na kuivumilia hali hiyo wakati serikali ikijitahidi kupata ufumbuzi wa tatizo hilo kubwa.



Ndiyo, hali ilikuwa mbaya. Na ilizidi kuwa mbaya hata pale miaka miwili ilipokatika. Makali hayo ya maisha yalizidi kushika kasi siku hadi siku, yakitoa taswira ya kutopatikana ahueni yoyote katika siku za usoni.



Baadhi ya Watanzania walikiona cha moto. Bidhaa muhimu zikaadimika madukani kiasi cha kusababisha uzao wa neno ‘BIDHAA ADIMU’ kwa baadhi ya bidhaa. Mambo yakawa si mambo.



Kanga, adimu!



Vitenge, adimu!



Vibiriti, adimu!



Dawa za meno, adimu!



Mchele, adimu!



Ngano, adimu!



Sukari, adimu!

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Betri, adimu!



Naam, kila bidhaa muhimu zikageuka kuwa bidhaa adimu. Zikawa zikipatikana kwa taabu, kwa foleni katika maduka ya kaya!



Ilikuwa ni adha kubwa kwa wananchi, lakini haikuwa adha kwa wananchi wote, la. Walikuwapo wachache, ambao walizidi kula kuku kwa mrija. Kati yao ni Kipipa Mtakayote ambaye mara tu vita vilipomalizika akaanza kufaidi matunda ya kazi yake. Pesa lukuki zikawa zikimmiminikia. Faida zikaingia maradufu.



Kwa jumla mambo yalimwendea kama alivyotarajia. Akanufaika kwa jinsi alivyotaka. Vitegauchumi vyake vikazidi kupanua wigo. Na kwa kuwa alifanya mambo yake kwa umakini wa hali ya juu, hakukuwa na Mtanzania mwenye macho ya kawaida na akili ya kawaida, aliyeweza kuijua siri ya mafanikio yake. Wengi walitambua kuwa ni tajiri asiye na doa lolote, tajiri mwenye roho nyeupe, roho ya kupenda kusaidia wanyonge, na kwamba, Mungu amezidi kumshushia neema kiasi cha kupata mafanikio zaidi katika shughuli zake.



Hizo zilikuwa ni fikra na imani za baadhi ya raia wa kawaida na watendaji wa kawaida serikalini. Hazikuwa fikra wala imani za watendaji wakuu wa serikali, wale waliojaaliwa akili zisizo za kawaida, macho na masikio yasiyo ya kawaida, wale waliokuwa na uchungu mkubwa kwa taifa lao lililozidi kutetereka kiuchumi.



Martin Peka alikuwa ni mmoja wa watendaji hao walioumia kwa hali mbaya ya taifa lao. Akiwa ni Mkuu wa Idara Maalumu iliyokuwa chini ya Ofisi ya Mkuu wa Nchi, alishabaini kuwa jahazi lilikaribia kuzama. Japo alitambua fika kuwa ni jambo la kawaida kwa nchi yoyote duniani kutetereka kiuchumi pindi ikumbwapo na vita, hata hivyo hakuamini kuwa nchi kama Tanzania ingefikia kiwango ilichofikia.



Ni kweli kuwa Tanzania ilikuwa miongoni mwa zile nchi zilizokuwa kwenye daraja la NCHI ZINAZOENDELEA, nchi za dunia ya tatu. Lakini, mazao ya biashara mathalani, pareto, pamba, tumbaku, mkonge, kahawa; madini ya almasi na dhahabu na; bandari za Tanga, Dar es Salaam na Kigoma, vilikuwa ni vitegauchumi vilivyotosha kuulinda uchumi japo kwa asilimia fulani.



Hivyo, hali iliyokuwa ikiendelea kwa kipindi hicho ilimfanya ajenge imani kuwa kulikuwa na jambo zaidi ya jambo linalotukia. Ni hapo alipoamua kufanya uchunguzi wa kina, uchunguzi uliotoa matokeo ya kuridhisha wiki mbili baadaye. Na yalikuwa ni matokeo yenye picha ya kuogofya kwa kiwango kisichokadirika. Sasa hakutulia tena mezani, akaharakisha kuonana na mkuu wa nchi.



Akamtobolea kila kitu, akidiriki hata kumtajia majina ya baadhi ya viongozi wa ngazi za juu serikalini na wale matajiri waliojivika ngozi za kondoo ilhali mioyo yao haikutofautiana na ya chui wenye njaa.



Ilikuwa ni taarifa ya kwanza mbaya kwa mkuu huyo wa nchi, baada ya ile taarifa ya uvamizi wa majeshi ya nduli Idi Amin Dada.

“Wakamatwe!” alifoka mkuu huyo. “Wakamatwe mara moja! Na operesheni hii ianze mara moja nchi nzima! Na iwe ni operesheni isiyotazama sura ya mtu, rangi, utaifa wala hadhi yake..!”



Ilikuwa ni kauli nzito, kauli isiyohitaji mjadala wowote. Suala hilo halikupelekwa bungeni kujadiliwa wala haikuundwa tume ya kuchunguza au kulifuatilia. Kwake, mkuu huyo wa nchi aliona kuwa tume na bunge vingechelewesha hatua iliyopaswa kuchukuliwa kulingana na yeye alivyoona inafaa.



Isitoshe, kutokana na taifa kutetereka kiuchumi baada ya vita, aliepuka matumizi makubwa ya pesa zitakazotumika kuwalipa wajumbe watakaokuwa katika hiyo tume ambayo angeiunda na pia kama suala hilo lingepelekwa bungeni, huenda kungezuka ubishani utakaozidi kuchelewesha utekelezaji au wabunge kuweka pingamizi la kutekeleza azimio hilo. Hayo ndiyo mambo ya siasa, na siasa yeye aliijua vizuri na aliyajua madhara ya kuingiza siasa katika baadhi ya masuala nyeti ya kiserikali.



Na alikuwa akiamini kuwa demokrasia siyo njia pekee ya kuonyesha kuwa taifa linaongozwa kwa misingi ya usawa na haki. Kwamba, kila kitu lazima kijadiliwe na wengi, kila jambo lazima lipelekwe kwenye vikao vya kamati fulani, bodi, au bungeni. Hapana, yeye hakuwa muumini wa sera hizo. Aliamini kuwa kiongozi wa nchi, wakati mwingine anapaswa kuchukua uamuzi hata kama utakuwa ni uamuzi mgumu, lakini uwe ni kwa manufaa ya taifa na wananchi kwa jumla

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Agizo hili alilolitoa kuhusu wahujumu uchumi lilikuwa ni miongoni mwa uamuzi mgumu alioamua kuuchukua.



Naam, kazi ikafanyika. Walanguzi na wahujumu uchumi wakakiona cha moto. Baadhi ya wafanyabiashara maarufu na viongozi wasio waaminifu serikalini wakawa matumbo moto, wengine wakikumbwa na mishtuko ya mioyo pindi walipousikia mfumo uliopangwa kutumika katika kuwanasa wahusika wenye tuhuma za ulanguzi na biashara za magendo.



Ndipo ikatokea siku hii ambayo Kipipa Mtakayote alijikuta akipokea ugeni asioutarajia, ugeni uliomfanya ajione akiingia katika sayari nyingine.





SIRI ya uovu wa tajiri Kipipa Mtakayote ilianza kufichukia mle dukani mwake. Nyuma ya jumba alilolimiliki kulikuwa na chumba kikubwa kilichofurika bidhaa lukuki. Chini ya uongozi wa Martin Peka, kikosi cha askari kumi wenye sare kilikivaa chumba hicho kwa upekuzi wa kina. Kitu cha kwanza kilichomshtua kisha kikamshangaza Martin Peka ni wingi wa mifuko ya sukari yenye ujazo wa kilogramu 50 kila mmoja.



Hicho kilikuwa ni kipindi ambacho bidhaa hiyo iliadimika sana madukani. Haikuwa siri, wala halikuwa jambo la ajabu kununua sukari katika duka lolote la mtu binafsi kwa bei maradufu ya ile bei halali. Lakini ndani ya chumba hiki kulisheheni sukari!



“N’nini hiki, mzee?” Martin Peka alimgeukia Kipipa Mtakayote aliyekuwa kushoto kwake.



“Aa…ni… ni sukari tu,” Kipipa Mtakayote alijibu huku akililazimisha tabasamu usoni.



“Sukari!” Martin Peka alimtolea macho. “Ni mifuko mingapi?”



“Iko kama…” Kipipa alisita.



“Siki’za, mzee,” Martin Peka alifoka. “Ni vizuri kama utakuwa mkweli. Nadhani unaliona kundi nililonalo. Ni askari wenye nguvu zao. Kila mmoja anaweza kubeba mifuko miwili begani na kutulia nayo kwa zaidi ya robo saa. Hivyo usidhani kuwa tunashindwa kuhesabu mfuko mmoja, mmoja katika kuthibitisha idadi yake. Tunachojali hapa ni muda tu. Ok, zungumza bila kusita na uzungumze kitu kinachoeleweka. Ni mifuko mingapi?”



“Mia moja tu, afande.”



“Umeinunua kiwanda gani?”



“Kwa kweli…” kwa mara nyingine Kipipa Mtakayote alisita.



“Naona we’ mzee utatupotezea muda wetu bure!” Martin Peka alifoka tena. Kisha akamwamuru, “Keti! Kaa chini!”



Huku jasho likimtoka kwa wingi, Kipipa Mtakayote alichuchumaa.



“Unaelewa Kiswahili? Nimesema kaa chini!”



“Lakini kwani mie n’na kosa gani jamani?”



“Hatuna muda wa kuzungumza zaidi,” Martin aliendelea kubwata.

“Amua moja, kuketi mwenyewe au kuketishwa na jopo lililonizunguka.”



Sasa Kipipa Mtakayote akajihisi yu jehanamu. Akaitazama sakafu ya chumba hicho iliyotapakaa vumbi zito. Akawaza, yeye tajiri mkubwa, tajiri aliyewahi kuketi meza moja na waziri mkuu, yeye anayetambulika kama mmoja wa waliotokea kulisaidia taifa kwa hali na mali wakati wa vita, leo anashurutishwa na huyu ‘kinyangarika’ kukaa chini!



Yeye!



Hakuyaamini masikio yake, wala hakuwa tayari kuitii amri hiyo. Alichokifanya ni kumtazama usoni Martin Peka kwa macho makali, akidhamiria kumkaripia kwa utaratibu alioutumia katika uwajibikaji wa majukumu yaliyomleta. Lakini hakupata nafasi ya kutamka chochote; kofi kali la kisogoni kutoka kwa askari mwingine lilimlazimisha kuketi sakafuni papohapo. Dakika iliyofuata pingu zikawa zimeizingira mikono yake.



Upekuzi rasmi ukafanyika ndani ya chumba hicho. Ile mifuko ya sukari haikuwa mia moja kama ilivyodaiwa na Kipipa Mtakayote. La. Ilikuwa ni mia mbili na hamsini, na chapa katika mifuko yake ilionyesha kuwa ilitoka ng’ambo katika kiwanda kimoja kilichokuwa Kitwe, Zambia.



Ilibainika baadaye kuwa sukari hiyo iliingizwa nchini kwa njia za magendo, pia haikuuzwa bayana kwa Watanzania bali iliuzwa kwa siri kubwa, na ‘wenye pesa’ ndio waliofanikiwa kuinunua.



Waliyoyakuta chumbani humo yaliwapandisha mori askari hao. Martin Peka akatoa taarifa kwa makamanda wa Polisi wa mikoa yote nchini, hususan ile mikoa yenye vitegauchumi vya Kipipa Mtakayote, akiwataka waweke ulinzi madhubuti sambamba na kufanya upekuzi wa kina katika maghala yake yote ikiwa ni kutekeleza amri ya mkuu wa nchi; OPERESHENI DHIDI YA UHUJUMU UCHUMI.



Siku hiyo Kipipa Mtakayote alilazimika kulala mahabusu pamoja na watu wengine sita aliowafahamu, na hao wakiwa na tuhuma zisizotofautiana na zake. Humo walikuwa katika muungano wa kujikwamua na dhoruba iliyowakumba. Mazungumzo yao usiku wa siku hiyo yakawa ni ya kuwapa matumaini ya kuokoka.



Siku iliyofuata walipelekwa katika Gereza la Chamoto ambako walifungiwa ndani ya chumba maalumu wakisubiri kupelekwa Mahakama Maalumu kusomewa mashtaka yaliyowakabili.



Siku mbili baadaye baadaye ndipo mtuhumiwa mmoja mwenye asili ya Kiasia alipotoa pendekezo kwa wenzake, pendekezo la kujiokoa na tuhuma zilizowakaabili. Mwasia huyo, Sadrudin Lalji, alionekana kuathiriwa sana na kizuizi hicho kwani tayari afya yake ilikuwa imedhoofu kwa kiasi kikubwa.



Macho yakiwa yamemtoka kama mgonjwa anayehofia mauti, aliwatazama wenzake kwa zamu usiku huo, saa 4 kabla hajatamka lolote. Kisha akafumbua mdomo kutaka kusema lakini kikohozi kikavu kikamjia ghafla. Akakohoa bila ya kukoma kwa takriban dakika moja. Kikohozi hicho kilipokoma alihema kwa nguvu, akashusha pumzi ndefu huku akitoa leso mfukoni na kuyafuta machozi yaliyojiunda ghafla machoni pake.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Tusipokuwa makini tunaweza kufia humu,” hatimaye aliwaambia wenzake huku akiendelea kufuta machozi. Muda mfupi baadaye alisitisha zoezi hilo, akawatazama wenzake na kuongeza, “Tunapaswa kutumia kila mbinu ili tutoke. Na nyenzo pekee ya kutuokoa ni pesa.”



“Ni kweli,” Kipipa Mtakayote aliafiki.



“Pesa!” mzee Kichewele alishangaa. “Tutatumia kiasi gani ili tujiokoe? Tambueni kuwa tuhuma zetu ni nzito, na huenda zimekuwa habari kubwa katika vyombo vya habari vya nje ya nchi. Kwa sasa sisi hatutofautiani na wahaini, hatutofautiani na magaidi. Unadhani ni jaji gani asiyeipenda kazi yake, ambaye atakuwa mwepesi wa kuipinda sheria ili tuokoke?”



“Hapana, usikate tamaa mapema hivyo,” Kipipa Mtakayote alipinga. “Hakuna mtu asiyeipenda pesa hapa duniani. Hakuna! Kama waziri wa nchi ya Uingereza au Marekani, ambaye sio mtu wa njaa-njaa huweza kutoa au kupokea pesa au rushwa ya aina yoyote na akalazimisha haramu kuwa halali, itakuwa ngumu kwa mtu mweusi kutoka nchi ya dunia ya tatu?”



“Mimi sioni kama kuna kikwazo chochote,” Sadrudin alichangia kwa sauti yenye msisitizo mkali. “Wote hapa tuna pesa. Cha muhimu ni kukubaliana kufanya mikakati ya kutoka!”



Yalikuwa ni maongezi yaliyodumu kwa takriban nusu saa. Hatimaye wakafikia makubaliano ya kumtumia Jaji Pesambele kwa minajili ya kutatua tatizo lao. Hata hivyo, kumtumia jaji huyo lilikuwa ni jambo moja. Kuonana na kuzungumza naye kuhusu suala hilo lilikuwa ni jambo lingine.



Kati yao, hakukuwa na yeyote aliyekuwa na uwezo wa kuonana ana kwa ana na Jaji Pesambele. Tuhuma zilizowakaabili zilikuwa kipingamizi kikubwa cha kukutana na mheshimiwa huyo. Hivyo, waliazimia kumtafuta mwakilishi, na mwakilishi huyo awe ni mtu mwenye kujiamini, ambaye ana sifa na uwezo wa kukutana na kuongea na viongozi mbalimbali wa ngazi za juu serikalini bila ya kukumbana na vikwazo vyovyote.



“Yupo mtu mmoja ambaye nadhani atatufaa,” Sadrudin aliwaambia wenzake.



“N’nani huyo?” mzee Kichewele alimdaka.



“Kisu.”



“Kisu?!” Kipipa Mtakayote alimkazia macho.



“Ndiyo, Kisu!” Sadrudin alisisitiza.



“Wa wapi huyo?” Kipangachuma alihoji.



“Yuko hapahapa Songambele.”



“Una hakika atatufaa?” Kipipa Mtakayote alizidi kumbana Sadrudin.



“N’na hakika!”



“Hapana,” mzee Kichewele alionesha kusita. “Huyo mtu we’ nd’o unamjua, na we’ nd’o unamwamini. Sisi wengine hatumjui, hivyo hatuwezi kuwa na imani naye. Ni vyema ungetupa picha yake halisi ili tuone kama kweli atatufaa.”



Ukimya ukatanda ghafla. Macho ya wengine yakahamia kwa Sadrudin huku baadhi wakitikisa vichwa kuafikiana na pendekezo la mzee Kichewele.



Sadrudin alikohoa kwa mara nyingine, lakini safari hii kikiwa ni kikohozi kifupi na kama vile cha kulazimisha. Akawatazama wenzake hao kwa zamu, hatimaye akayatua macho kwa mzee Kipipa na kwa sauti ya chini lakini iliyoyafikia masikio ya wote, akasema, “Kwa kweli Kisu sio mtu wa kawaida katika nchi hii. Alishawahi kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje. Baadaye alihamishwa Wizara ya Afya. Miaka minne iliyopita alikuwa Wizara ya Biashara kwa wadhifa huohuo wa Unaibu Katibu Mkuu. Lakini ghafla, aliacha kazi bila ya kufukuzwa!”



Akatulia kidogo na kulirudia lile zoezi lake la kuwatazama wenzake, mmoja baada ya mwingine. Wote walikuwa makini, wakimtazama, jambo lililomtia moyo wa kuendelea kuzungumza.



“Lakini,” aliendelea. “Siwafichi. Bado huyo mtu ni maarufu sana. Mawaziri wengi ni maswahiba wake. Makatibu wengi wa wizara mbalimbali wako karibu naye! Hata vigogo wa vyombo vya dola wanamjua, na humpa ushirikiano mkubwa pindi awafuatapo kwa shida au suala lolote.



“Baadhi ya watu wanaokumbwa na kesi kubwa humwona yeye. Kesi hizo zitageuka kuwa ndogo na hatimaye zitakwisha kwa watuhumiwa kucheka hadi magego ya mwisho. Kwa kweli yule ni mtu wa ajabu kwani hata Mwanasheria Mkuu ni mtu wake wa karibu. Na jambo lingine linalonifanya nimchukulie Kisu kama binadamu asiye wa kawaida ni uwezo wake wa kupita katika geti la ikulu kama mtu anayeingia nyumbani kwake. Nadhani mpaka hapo mnaweza kuwa mmepata taswira halisi ya mtu huyo.”



Akatulia na kuwatazama kwa makini zaidi wenzake. Sasa akayabaini mabadiliko katika nyuso zao. Hapo awali, wakati akitoa maelezo nyuso hizo zilikuwa zikimtazama kwa umakini wa kupokea kila alichosema. Lakini sasa, zilimtazama kwa namna ya udadisi mkubwa, zikionyesha bayana kutoridhika na maelezo ya awali.



Kichewele ambaye alimtazama Sadrudin kwa macho yasiyopepesa, alihoji, “Unamwamini vipi mtu huyo kwa ishu yetu? Hawezi kuwa miongoni mwa mashushushu?”



Kicheko hafifu kikamtoka Sadrudin. “Hata mimi nilishashuku hivyo siku nyingi zilizopita. Nikafanya uchunguzi wa kina. Baada ya muda nilianza kuwa na imani naye kwa mbali sana. Imani ambayo sikupenda kuipa uzito mkubwa kichwani mwangu.



“Lakini kuna wakati nilikumbwa na kesi ya kuuza tani tano za kahawa, Kenya, bila ya kibali cha serikali. Ilikuwa ni kesi iliyonikalia kooni vibaya! Nisingepona! Akanijia mtu mmoja ambaye alinishauri nikazungumze na Kisu; nikaafikiana naye nikiwa sitofautiani na mfa maji. Siku ya siku tukafuatana hadi kwa Kisu, na jamaa yangu huyo akawa kinara wa maongezi.



“Kisu alituelewa. Akanichota milioni mbili keshi. Na akanipa matumaini ya kuishinda kesi ile. Bado sikumwamini! Sana-sana nilihisi kuwa huenda Kisu na huyo jamaa yangu wamefanya njama za kuniibia. Hata hivyo, siku tatu baadaye yule jamaa yangu alinijia nyumbani na kunitaarifu kuwa mambo yanakwenda vizuri; eti tayari Kisu kishazungumza na Mwanasheria Mkuu na hakimu aliyeisimamia kesi ile.



“Bado sikuamini! Lakini, maajabu yaliyotokea siku moja kati ya siku ambazo kesi hiyo iliendeshwa, ndiyo yaliyonifanya nimchukulie Kisu kama ‘Mungu-mtu.’ Kwa kweli ilikuwa ni vigumu kuyaamini masikio yangu!”



Akatulia tena na kuachia tabasamu dogo, tabasamu la kujiamini. Kisha akaendelea, “Mahakama ilitoa tamko kuwa kesi yangu imefutwa na Mkurugenzi wa Mashtaka kwa kipengele fulani, sijui namba ngapi na cha lini. Yaani kwangu ni kama ulikuwa muujiza.”



“Basi, tosha,” Kipipa Mtakayote alimkata kauli. “Binafsi nadhani tumtumie mtu huyo. Au kuna mwenye wazo tofauti?”



“Hata mimi naona huyo mtu anaweza kutufaa, lakini atahitaji pesa,” Kichewele alichangia.



Baadhi waliachia vicheko dhaifu, baadhi wakaishia kutabasamu. Vichwani mwao, kauli hiyo ya Kichewele ilikuwa na upeo finyu wa fikra.



“Hilo ni lazima!” Kipipa Mtakayote alitamka kwa msisitizo mkali, akimkodolea macho mzee Kichewele.



“Suala la pesa halina mjadala,” Lomolomo, mtu ambaye kwa muda mwingi hakuwa akizungumza, hatimaye naye aliipata sauti yake.



“Unadhani atataka shi’ngapi kwa ishu hii?” Kipipa Mtakayote alimuuliza Sadrudin.



“Kwa kweli siwezi kujua,” Sadrudin alijibu. “Lakini huwa anachaji kulingana na uzito wa suala lenyewe. Cha muhimu hapo ni kuonana naye ana kwa ana.”



“Tutaonana naye vipi?” Kichewele alihoji.



“Kama nivyowaambia awali, yule siyo mtu wa kawaida. Kama anaweza kutinga Ikulu kimchezo-mchezo, atashindwa kutufikia sisi?”



Mzee Kichewele alifyata.



“Ok, tunakuachia wewe kazi hiyo,” Kipipa Mtakayote alisema. “Fanya kila liwezekanalo, uhakikishe tunakutana naye ndani ya siku mbili zijazo.”



************



HAIKUWA kazi kubwa kwa Sadrudin Lalji. Afya yake dhaifu ilikuwa nyenzo mojawapo ya kumkutanisha na watu mbalimbali walio huru, hususan ndugu zake. Asubuhi ya siku iliyofuata, askari mmoja alimjia na kumtaarifu kuwa ana mgeni.



“Ni nani?” Sadrudin alimhoji askari huyo.



“Yule mdogo wako.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Sadrudin alicheka kimoyomoyo kisha akawambia, “Asante afande. Huyo bwa’mdogo atakuona tukimaliza kuongea. Nakuja sasa hivi.”



Askari huyo alimwelewa na akaondoka huku tabasamu la mbali likichanua usoni pake.



Sadrudin aliwageukia wenzake na kwa mnong’ono akasema, “Ni huyo bwa’mdogo n’takayemtumia. Nadhani…ah… no! Tuseme n’na hakika kesho tutakuwa na Kisu humu ndani.”



Akatoka.



************





ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog