Simulizi : Roho Nyeusi
Sehemu Ya Pili (2)
KISU alipopewa taarifa na Premji, mdogowe Sadrudin, alijua kuwa pesa zilikuwa zikinukia mbele yake. Hivyo, siku iliyofuata aliamka mapema, akaoga na kuvaa suti yake ya ‘bei’ kisha akaingia ndani ya gari lake na kuchoma mafuta hadi Hotel Paradise ambako alipata stafutahi.
Akiwa hapo aliwaza juu ya wito ulioletwa kwake, wito wa kumtaka akaonane na watuhumiwa wa uhujumu uchumi walioswekwa katika mahabusu maalumu ya Gereza la Chamoto. Tayari alishajenga hisia kuwa wito huo ni wa kutaka azungumze nao jinsi ya kuwasaidia katika kuepukana na adhabu yoyote ambayo ingewakabili.
Aliamini kuwa mbinu aliyotumia katika kuimaliza kesi ya uuzaji kahawa nchini Kenya bila ya idhini ya serikali, kesi iliyomkaabili Sadrudin miaka kadhaa iliyopita ndiyo iliyompa changamoto Mwasia huyo hadi akamtuma mdogowe, Premji jana.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Na kama kweli hiyo ndiyo sababu ya kumwita, basi hakuwa na shaka yoyote. Japo operesheni hiyo dhidi ya walanguzi na wahujumu uchumi ilikuwa ikifuatiliwa kwa karibu sana na uongozi wa juu serikalini, hata hivyo bado hakukiona kikwazo cha kufanya kazi yake. Kwa jumla alijiamini. Hivyo alipata stafutahi yake kwa utulivu, moyoni akijenga hisia kuwa donge nono la pesa linamsubiri.
Saa 3:30 alikuwa tena garini, sasa safari ikiwa ni ya Chamoto-gerezani moja kwa moja. Na alipofika aliomba kuonana na mkuu wa gereza. Alipopewa nafasi hiyo aliingia ofisini kwa mkuu huyo, na baada ya maongezi mafupi ya kawaida, hatimaye alimtamkia bayana kuwa anahitaji kuonana na Sadrudin Lalji.
Mkuu wa gereza hakuwa mbumbumbu. Alimjua vizuri Kisu jinsi alivyo mtu wa mipango mikubwa ya pesa. Huku akiachia tabasamu pana alimuuliza, “Vipi, Kisu? Hatuambiani? Unataka kula peke yako?”
Kicheko dhaifu kilimtoka Kisu, kisha akasema, “Usijali mkuu. Bado mapema mno kukupa jibu sahihi. Labda nikishajua ninachoitiwa ndipo nitakuwa na la kukwambia.”
“Unataka kun’ambia kuwa hujui?” mkuu wa gereza alimtazama kwa macho yaliyojaa udadisi. Akaongeza, “Kisu ninayemjua mimi hawezi kuchoma mafuta hadi huku bila kukijua anachoitiwa. Kwa vyovyote vile huyo atakuwa ni Kisu mwingine, siye huyu niliyenaye humu ofisini.”
“Unaweza kuwa sahihi, mkuu. Lakini pia ni vyema ukitambua kuwa Kisu wa jana sio wa leo.”
“Una maana gani?” mkuu wa gereza alimuuliza. “Usinichekeshe Kisu. Yaani unataka kun’ambia Kisu ninayemjua mimi…”
“Tuache mizunguko, mkuu,” Kisu alimkata kauli. “Najua hatujaonana siku nyingi, lakini sidhani kama kwa leo huu ni muda mwafaka wa kupanga lolote. Niruhusu kwanza nikamwone huyo mzee wa Kihindi.”
“Hilo si tatizo,” mkuu wa gereza alijibu huku lile tabasamu lake likiwa limeshayeyuka. “Ruksa hata sasa hivi. Wale sio wahaini au magaidi wa kimataifa. Ni watuhumiwa wa makosa ya kawaida tu.”
“Shukrani, mkuu. Na ninakuahidi kuwa kama maongezi yetu yatakuwa mazuri, basi sitakusahau. Baada ya siku mbili, tatu hivi nitakuja kukuona kikamilifu. Na, n’nadhani utaridhishwa na ujio wangu.”
“Us’jali,” kwa mara nyingine mkuu wa gereza alitabasamu huku akinyanyuka kitini, maneno ‘nitakuja kukuona kikamilifu’ yakielea kichwani kwa namna ya kumtia faraja.
“Nipitie wapi?” Kisu naye akiwa amenyanyuka alimuuliza mkuu huyo.
“Subiri. Twende nikupeleke.”
Walipita hapa kisha pale huku baadhi ya askari wakimshangaa mkuu wao kwa kitendo cha kumpeleka mgeni kwenye mahabusu maalum badala ya kuwatumia wao.
Muda mfupi baadaye, mkuu wa gereza alisimama kwenye mlango uliolindwa na askari mwenye silaha. “Huyu,” akamgusa Kisu begani, “anahitaji kuonana na Sadrudin. Mfungulieni.”
“Sawa, afande.”
“Ok, Mr. Kisu,” alimgeukia Kisu. “Kaonane na mtu wako. Tutaongea zaidi siku nyingine.”
“Ok, mkuu.”
WATUHUMIWA sita wa kesi ya uhujumu uchumi; Kipipa Mtakayote, Kichewele, Sadrudin Lalji, Kipangachuma, Lomolomo na Ayatollah Matto waliukodolea macho mlango wa chumba walimohifadhiwa, pale waliposikia kitasa kikichokonolewa.
Punde mlango ukafunguliwa. Askari mwenye bunduki akaingia na kumtolea macho makali Sadrudin Lalji. “We’Mhindi kuna mgeni wako, njoo huku!” alimwambia kwa sauti kali lakini ya chini.
Sadrudin alimjua askari huyo asivyo mstaarabu. Mara mbili, kwa siku mbili tofauti, alidiriki kumwagiza awaambie Wahindi wenzake wachange pesa kiasi cha kutimia shilingi 10,000, wampatie ili awe anawapa nafasi ya kuonana. Na alipaswa kukusanya kiasi hicho kila wiki!
Kwa hilo, Sadrudin hakuwa radhi kulitekeleza. Ingawa alikuwa tayari kutumia hata shilingi milioni moja ili anusurike kutiwa hatiani kwa tuhuma zilizomkaabili, hata hivyo kuhonga 10,000/= kila wiki eti kwa ajili ya kukutana tu na jamaa zake, kwake lilikuwa ni jambo lisilowezekana wala kukubalika.
Kitendo cha kutotekeleza maagizo hayo kilijenga chuki moyoni mwa askari huyo kiasi kwamba akawa hamchangamkii tena, na mara kadhaa ilipotokea akawa zamu, na mtu yeyote akaja kumjulia hali Sadrudin, basi jibu ambalo mgeni angepewa lingemkatisha tamaa.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hayupo!” au “haruhusiwi kuonana na mtu yeyote leo” au “daktari ameshauri apumzike..” na kadhalika na kadhalika.
Kwa kuwa tayari uhusiano wao ulishazingirwa na ‘dudubaya,’ Sadrudin hakutaka kutamka chochote japo alikerwa na amri ya askari huyo. Akasimama na kuelekea mlangoni. Alipotokeza nje tabasamu kubwa likamtoka.
“Kisu!” hatimaye alibwata huku akimfuata Kisu aliyekuwa hatua tano hivi kutoka mlangoni. “Afadhali umekuja…afadhali umekuja mheshimiwa. Tulikuwa tukikusubiri wewe…”
“Basi, poa anko Sadru,” Kisu alisema huku akimpa mkono. Akaongeza, “Nadhani nimefika katika muda mwafaka kwa mazungumzo yetu. Ni wapi panapostahili kuketi na kuzungumza kwa utulivu?”
Sadrudin Lalji alikunja uso kidogo, akamtazama yule askari kisha akayarejesha macho kwa Kisu. Kwa unyonge akasema, “Kwa kweli, sijui. Sijui wapi patafaa rafiki yangu. Sote tulioko huko ndani tunakuhitaji sana. Lakini nadhani sheria za hapa haziruhusu sisi watuhumiwa kutoka na kuja kuketi hapa nje kwa zaidi ya robo saa…”
“Subiri,” Kisu alimkata kauli. Akaingiza mkono ndani ya mfuko wa shati na kutoa kibiriti cha gesi. Kisha tena akauzamisha mkono huohuo mfukoni na safari hii akatoa pakiti ya sigara. Akaifungua pakiti hiyo na kuchomoa sigara moja ambayo aliipachika mdomoni kwa madaha.
Akionekana kutokuwa na wasiwasi wala haraka, aliiwasha sigara hiyo na kukirudisha kibiriti mfukoni. Akavuta mikupuo miwili ya nguvu na kupuliza moshi angani, moshi ambao kwa nyakati tofauti ulitokea mdomoni na puani.
Macho yake makali, macho ya kujiamini, yaliwatazama kwa zamu Sadrudin na yule askari jela. Tabasamu pevu likamtoka. Sigara ikiwa imeshikwa na mkono wa kushoto, mkono wa kulia ulizipapasa sharubu chache zilizomwongezea mvuto usoni pake. Kisha, mkono huo ukaziacha sharubu na kuzama katika mfuko wa kulia wa suruali. Akaendelea kutabasamu, tabasamu la kifahari, tabasamu lililoonesha ni jinsi gani alivyojiamini.
Mara akaupeleka mkono shingoni na kuishikashika tai yenye mchanganyiko wa mistari ya rangi nyekundu na nyeupe, tai iliyowiana vyema na shati jeupe lililolitangulia koti jeusi maridadi. Wakati huohuo, japo alikuwa akiwatazama Sadrudin na askari huyo kwa zamu, lakini zaidi alikuwa akijaribu kuusoma uso wa askari kwa makini na akabaini kuwa hakuwa na aina yoyote ya furaha au amani moyoni mwake.
Akiwa na uzoefu wa kukutana na watu wa marika, nyadhifa, tabia na jinsia tofauti, Kisu hakutishwa wala kubabaishwa na sura ya askari huyo ambaye wakati huo alikuwa akimtazama kwa macho makali, mikunjo michache ikiwa imejiunda katika paji lake.
Atishike, yeye ambaye alikuwa na uwezo wa kuingia ofisini kwa Waziri wa Mambo ya Ndani na kumweleza shida yake bila ya kumtangulizia ‘shikamoo mzee’, ‘asalaam aleykum’ au ‘habari za kazi?’
Ababaike, yeye ambaye mara kadhaa aliombwa na kamanda wa polisi wa Songambele kukutana kwenye hoteli fulani yenye hadhi ya juu kwa ajili ya chakula cha mchana au usiku?
Aogope, yeye ambaye si mara moja au mbili majaji na mahakimu kadhaa walishadiriki kumpa asilimia thelathini au arobaini ya mapato aliyowatengenezea? Mapato ambayo ukweli ni kwamba yalipatikana yakiwa ni katika utaratibu wa kuigeuza haramu kuwa halali!
Naam, hakuwa mtu wa kutishika wala kubabaika. Na akizingatia kuwa mkuu wa gereza alidiriki kukiacha kiti na ofisi yake, akamleta hadi hapo kwa watuhumiwa, na kumwamuru askari huyo amruhusu kuonana na Sadrudin, kiburi cha aina yake kikamvaa, kiburi kilichomfanya amtazame askari huyo kwa macho yasiyopepesa, macho ya kujiamini.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nadhani itanipasa nizungumze na mwenyeji wangu, faragha,” alimwambia kwa sauti iliyo thabiti.
“Hakuna kitu kama hicho!” askari alimaka.
Tabasamu bandia likajiunda usoni pa Kisu. Papohapo akaipeleka sigara mdomoni na kuvuta mikupuo mingine miwili, kisha akamtazama tena yule askari, safari hii lile tabasamu likiwa limeshayeyuka.
Mara akayahamishia macho angani na kupuliza moshi wa sigara. Alipomrudia yule askari, alisema, “Jitahidi kuwa hata na ustaarabu wa bandia. Naweza kuitii kauli yako. Lakini kama nitamrudia bosi wako aliyenileta, na nikamtaarifu juu ya uamuzi uliochukua, sidhani kama hatua itakayofuata itakuwa nzuri kwa upande wako. Sidhani. Mimi ninamjua vizuri bosi wako, na yeye ananijua vizuri.
“Kwa kifupi ni kwamba tunafahamiana. Na kufahamiana kwetu sio kijuujuu. Tunafahamiana na kuelewana zaidi ya unavyoweza kukadiria. Elewa hivyo, tafadhali. Kauli yoyote nitakayoitoa kwake, kauli itakayotoa picha kuwa sikuridhishwa na utendaji wako wa kazi, kwa vyovyote vile itakuponza. Nakusihi kwa mara ya mwisho, uwe makini na uamuzi wako.”
Akatulia kidogo kisha akaendelea: “Usiweke sheria au kanuni na taratibu za kazi yako mbele, ukitarajia kupata walao tepe moja begani. No! Vyeo havipatikani kwa mfumo huo, bwa’mdogo. Zipo mbinu za kupata cheo hata kama wewe utakuwa ni mvunja sheria namba moja.”
Akatulia akimtazama yule askari kwa makini katika kumchunguza kama ameyapokea vizuri maneno yake.
“Kwa bahati mbaya au nzuri mimi siyo mwanasiasa wala mhubiri wa dini,” aliendelea. “Hivyo sikujaaliwa kipaji cha kuzungumza sana. Naamini maelezo machache niliyokupa umeyaelewa. N’nachohitaji ni kupata wasaa wa kuzungumza kwa utulivu na huyu ndugu pamoja na hao wenzake.”
“Wewe ni wakili wao?” askari huyo aliuliza kwa sauti ya mashaka.
“Haikuhusu. Wewe nipe msimamo wako; utaniruhusu niingie huko ndani, au je, utawatoa huko, waje hapa tuzungumze, au hautakuwa tayari kwa lolote kati ya hayo mawili?”
Sura ya askari yule ilishabadilika. Haikuhitaji kumtafuta mtu mwenye upeo mkubwa katika kutambua kuwa kakumbwa na jakamoyo. Uso wake ulisomeka bayana. Na kwa sauti yenye kitetemeshi cha mbali, alisema, “Ingieni… ingieni ndani mkazungumze.”
Ilitosha.
Dakika iliyofuata Kisu alikuwa kati ya watuhumiwa sita wa kesi ya uhujumu uchumi. Sadrudin akiwa kinara wa kikao, alizungumza kile alichoagizwa na wenzake.
“Hilo ni tatizo la kawaida,” Kisu alisema baada ya Sadrudin kuhitimisha maelezo yake. Akaongeza, “Ni kazi itakayonichukua siku mbili au tatu tu. Lakini nina imani mtafurahishwa na matokeo yake. Cha muhimu ni pesa. Kila mmoja wenu anaujua uzito wa tuhuma inayomkaabili, hivyo itakuwa vizuri kama tutaanza utekelezaji wa kazi hii kivitendo na kinadharia kwa pamoja ili kisiharibike kitu.”
Sadrudin aliwatazama wenzake kisha akamrudia Kisu. “Hilo tu’shalizungumzia. Lakini kauli ya mwisho, hasa kuhusu kiwango cha pesa, inatoka kwako.”
“Sawa.”
Baada ya dakika kumi hivi walifikia mwafaka. Kisu alihitaji shilingi milioni sita. Na kwa kuwa Sadrudin na wenzake hawakuwa na pesa humo gerezani, walikubaliana kumtuma Kisu kwa jamaa zao, uraiani, akachukue robo tatu ya kila kiwango ambacho kila mmoja wao alipaswa kutoa.
Walimkabidhi Kisu taarifa za maandishi kwenda kwa jamaa zao huku wakitia saini na majina yao katika kila karatasi ya mtumiwaji.
“Tuna imani na wewe,” Sadrudin alimwambia Kisu wakati akimkabidhi vijikaratasi hivyo.
“Tulieni,” Kisu aliwaambia wakati akizifutika mfukoni zile taarifa walizompatia. “Nawaombeni mnipe siku tatu za kushughulikia suala hili.”
Wakati akitoka mara alisita na kuwageukia watuhumiwa hao. Kwa sauti ya chini akasema, “Yaliyozungumzwa humu, yabaki humuhumu.Tafadhalini, yasifike kwenye masikio yasiyohusika.”
“Kwa hilo, usihofu,” Sadrudin alisema kwa sauti thabiti. “Sisi s’o watoto wadogo, na tuna akili timamu. Hakutakuwa na upuuzi wowote utakaofanyika.”
Kisu alipoondoka, Kipipa Mtakayote na wenzake walibaki wakitazamana kwa nyuso zilizojaa matumaini.
“Naamini Mungu yuko upande wetu,” Kichewele alisema.
“N’na hakika tutashinda tu,” Kipangachuma alidakia.
“Mungu utusaidie,” Lomolomo alikuwa kama anayesali.
“Sijui itakuwaje,” Ayatollah Matto alinong’ona.
“Kila kitu kiko shwari,” Kipipa Mtakayote alitamka kijasiri.
“Mie sina hata chembe ya shaka,” Sadrudin naye aliweka bayana.
BAA ya Kumekucha ilikuwa imefurika watu jioni hii. Baadhi walikuwa wakinywa bia, baadhi soda na waliobaki walikuwa wakinywa maji. Vipazasauti vinne vilivyobandikwa sehemu tofauti vilitoa muziki kwa sauti ya wastani, sauti isiyokera masikioni mwa wateja.
Kisu akiwa amevaa shati jekundu, lenye mikono mirefu, suruali nyeusi na viatu vya rangi ya kahawia, aliingia ndani ya baa hiyo kwa mwendo wa asteaste huku akiwatupia macho mara chache wateja waliokuwa jirani naye. Mkono wa kushoto ukiwa umezama ndani ya mfuko wa suruali huku mkono wa kulia ukiwa na sigara iliyofuka moshi, hakuonekana kuwa na haraka ya kuketi, hata pale wahudumu wawili wa kike walipomfuata na kumkaribisha kwa sauti nyororo na tabasamu usoni.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Asanteni,” aliwajibu huku akiwa amesitisha zoezi la kutembea na akawa akiangaza macho pande zote za ukumbi huo.
“Au unamtafuta mtu?” mhudumu mmoja alimtupia swali huku akimtazama kwa macho malegevu.
Kisu alimtazama kidogo mhudumu huyo huku akizichezesha funguo za gari mkononi. Kisha akatikisa kichwa kwa madaha ya kipesapesa na kuubana kidogo mdomo. Akashusha pumzi ndefu na kujibu, “Ndiyo, kuna mtu nimemfuata hapa.”
“N’nani huyo?” mwingine alidakia.
Kisu aliwatazama wahudumu hao kwa zamu kisha akayahamisha tena macho na kulirudia zoezi la kuangaza ukumbini. Aliyaamini zaidi macho yake. Kwa kipindi hicho kifupi tayari alishaamini kuwa aliyekuwa akimhitaji hakuwapo.
Ni Jaji Pesambele.
Asubuhi ya jana, mara tu alipotoka kuongea na wale watuhumiwa kule Gereza la Chamoto, alimpigia simu Pesambele na kumwambia kuwa alihitaji kuonanaye kwa maongezi nyeti.
Kama mahakimu na majaji wengine walivyomjua Kisu, tayari Jaji Pesambele naye akahisi kuwa mwisho wa maongezi hayo ni faida mifukoni mwake. Hivyo, hakukataa, alimpa jibu moja: “Fanya kesho jioni, saa kumi na mbili. Tukutane Kumekucha Club. Kama utawahi basi unisubiri.”
Hii ilikuwa ni saa 12:15 jioni. Kisu alikuwa na dakika tano tu tangu aikanyage sakafu ya ukumbi huo. Hakuamini kuwa amechelewa kiasi cha Pesambele kufika na kuondoka baada ya kutomwona. La. Alikuwa na rekodi ya uhakika kuwa hii ndiyo klabu ambayo Pesambele aliipenda, hivyo asingeingia na kukaa kidogo tu kisha akaondoka.
Mara akajiwa na wazo la kuwauliza wahudumu hao katika kupata uhakika. Lakini kama wazo hilo lilivyomwingia kwa kasi, ndivyo pia lilivyoyeyuka akilini mwake. Badala yake aliwaambia, “Nitafutieni nafasi nzuri.”
“Hilo s’o tatizo, kaka,” mhudumu mmoja alimwambia. “Unapenda kuketi humu ndani au kule uani?”
“Uani?” Kisu aliwauliza kwa mshangao. Kwa jumla alikuwa mgeni ndani ya klabu hiyo. Japo alikuwa mpenzi wa bia, lakini hakupenda kunywa kinywaji hicho ndani ya klabu hiyo katika miaka yake saba aliyoishi hapo Songambele. Na alikuwa na sababu.
Ufuska! Vibaka!
Idadi kubwa ya wateja wa kiume waliokuja hapo walikuwa wakware. Waliingia hapo kwa ‘gia’ ya kunywa bia, mvinyo, wiski au soda, lakini mioyoni wakiwa na yao. Baadhi ya wateja wa kike, wengi wao wakiwa ni warembo wa haja, waliingia hapo kwa lengo moja tu; kuwasaka wanaume waroho, wale wanaume wasiostahimili kumwangalia mwanamke mara moja na kuachananaye. Pia, kulikuwa na wale ambao kazi yao ilikuwa ni kuangalia nani kazidiwa na kilevi, wampekue.
Ni hayo yaliyomfanya Kisu aiepuke klabu hiyo. Na jioni hii, kama si miadi kati yake na Jaji Pesambele katu asingekanyaga hapo.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hivi kuna sehemu nyingine zaidi ya hii?” aliongeza swali, macho yake makali yakiwatazama wahudumu hao kwa zamu.
“Ipo,” mhudumu mmoja alimjibu. “Ni sehemu inayowastahili watu wa aina yako; wanaume watanashati na wenye mvuto mbele ya wanawake wapendao wanaume wazuri. Pia huwafaa wapenzi wanaohitaji faragha kwa raha zao.”
Kisu hakuyajali maneno ya mhudumu huyo. Yalikuwa ni maneno aliyokwishayazoea, maneno yatokayo kwenye vinywa vya wanawake wanaowawinda wanaume.
“Nipelekeni,” hatimaye aliwaambia.
************
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment