Search This Blog

Saturday 5 November 2022

ROHO NYEUSI - 3

 








Simulizi : Roho Nyeusi

Sehemu Ya Tatu (3)







LILIKUWA ni eneo ambalo mandhari yake yalionyesha kuwa ni maalumu kwa watu maalumu, watu wenye tabia au hulka tofauti na wale wanaoketi kule kwenye ukumbi wa wazi. Nuru hafifu kutoka katika globu za rangi tofauti, ililifanya eneo hilo lipendeze na kuwa kivutio hususan kwa watu wanaohitaji faragha.



Isitoshe. meza chache zilizokuwa mbali, mbali ziliwahifadhi wateja wawili tu kila meza, wateja waliokuwa wa jinsia tofauti. Haikuhitaji kusumbua kichwa katika kutambua kuwa hao ni wapenzi au la. Hawa walikuwa wamekumbatiana na kubusiana. Wale walikuwa wakitomasana. Na, wale kule walikuwa wakinong’onezana huku mikono yao ikitalii miilini mwao.



Labda picha hiyo isingemshangaza sana Kisu, kama asingemgundua mmoja wa wateja hao, huyu aliyeketi katika meza iliyo jirani na mlango. Alikuwa ni Jaji Pesambele!

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Ilimshangaza Kisu kumwona mheshimiwa huyo, mtu ambaye ana mke na watoto wakubwa, akiwa amezungukwa na wanawake watatu ambao kwa rika ni sawa na wanawe. Wanawake hao walikuwa wakimshikashika, wakimbusu na kumtomasa, wakionekana kuzisahau bia zilizofurika mezani.



Kisu aliuruhusu mshangao huo ukitawale kichwa chake kwa muda mfupi tu, kitu kama sekunde ishirini hivi kasha zikatoweka. Alizijua tabia za baadhi ya wale ambao baadhi ya vyombo vya habari vimewabatiza jina la ‘vigogo’ ikimaanisha kuwa ni viongozi wa ngazi za juu serikalini.



Tuhuma mbalimbali za ufuska zilishawakumba vigogo hao, Pesambele akiwa miongoni mwao.



Pesa ni kitu ambacho hakikuwa adimu mifukoni mwa Jaji Pesambeleke. Ni ukwasi huo uliomfanya ayafurahie maisha ya ukubwani kwa kustarehe na wanawake warembo kila apendapo. Wengi wa vigogo wenye hulka ya ufuska, ambao wana njia nyingi za kujipatia pesa, tofauti na mishahara yao, hawatofautiani na huyu Jaji Pesambele. Kisu aliamini hivyo. Na ni imani hiyo iliyomfanya auondoe haraka mshangao akilini mwake. Akaisogelea meza ile taratibu, mkono wa kushoto mfukoni, sigara mkono wa kulia.



************



“KAMA mko tayari, tutaondoka wote,” Pesambele aliwaambia wanawake hao kwa sauti ya chini.



“Kwa hilo us’konde babu,” mwanamke mmoja alisema.



“Sie hatuna noma, wewe tu,” mwingine alidakia.



“Wewe tu na mfuko wako,” wa tatu alichangia.



“Lakini…” Pesambele alisema na kusita papohapo.



“Lakini nini, babu?” mwanamke wa kwanza alihoji. Kwa mtazamo wa harakaharaka, mwanamke huyo ndiye aliyekuwa kipenzi kikuu cha Jaji Pesambele. Ni yeye aliyeruhusiwa kupenyeza mkono katika mifuko ya Pesambele na kutoa pesa. Ni yeye aliyekuwa na uwezo wa kuagiza nyamachoma. Na, ni yeye aliyeruhusiwa na Pesambele kusema, ‘sasa pombe,basi. Tuondoke’.



Huyo aliitwa Zinduna. Mwingine aliitwa Shani, na wa tatu ni Jane. Wote hao walikuwa ni wanawake ambao kula yao, vaa yao na kunywa yao ilitegemea wanaume, tena wanaume wenye pesa, wanaume wasiokuwa na zile kauli za ‘nataka tufunge ndoa.’ Nyuso zao na maumbile yao vilikuwa vivutio machoni mwa wanaume wakware.



Isitoshe, mavazi yao pia yalichangia katika kumfanya mwanamume mpenda warembo awatazame kwa macho yasiyo ya kawaida. Tazama huyo Zinduna alivyovaa kijiblauzi kilichoiacha wazi sehemu kubwa ya kifua chake na chini akiwa ametinga suruali ya kitambaa chepesi iliyomshika vilivyo mwilini. Hebu waone Shani na Jane na vijisketi vyao vifupi vilivyoyaanika hadharani mapaja yao makubwa bila ya wenyewe kujali.



“Hakuna tatizo, babu,” Zinduna aliongeza. “Ndani ya chumba kimoja, sote tutahakikisha tunairidhisha nafsi yako na kuuburudisha mwili wako. Tuna hakika utafurahi, na utauona usiku mfupi kuliko ulivyo.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Yalikuwa ni maneno yaliyomsisimua vilivyo Pesambele. Akaachia tabasamu kubwa, tabasamu la dhati huku mkono mmoja ukizipapasa nywele za Zinduna na mwingine ukiteleza katika mapaja ya Shani. Mara akafumbua mdomo akitaka kutamka neno, lakini akasita; hatua chache kutoka mezani hapo alimwona mtu aliyemfahamu na aliyetarajia kumwona jioni hiyo.





“YEAH, master Kisu!” hatimaye alitamka. “Karibu sana. Umefika katika muda mwafaka. Ulijuaje kuwa nimejichimbia huku?”



“Nimebahatisha tu, mheshimiwa,” Kisu alijibu huku akiisogelea meza hiyo.



“Ok, chukua kiti tujumuike pamoja.”



Kisu hakuwa amepanga kuchukua zaidi ya robo saa mahali hapo. Hata hivyo, aliamua kutekeleza matakwa ya Pesambele katika kumlindia heshima mbele ya warembo hao waliomzunguka.

Kiti kililetwa na mmoja wa wale wahudumu waliomleta hapo. Kisha akaulizwa, “Kinywaji gani, kaka?”



“Double Cola baridi.”



“Double Cola?!” Jaji Pesambele alimtazama kwa mshangao.



“Imekuwaje? Au siku hizi umeokoka?”



“Hapana, mheshimiwa.”



“Kumbe ni vipi tena?”



“Niko kwenye dozi ya malaria,” Kisu aliongopa.



“Oh! pole sana.”



Mara soda ilitua mezani. Dakika iliyofuata Kisu alikuwa ameshusha mafunda kadhaa kinywani. Wakati huo ukimya ukaitawala meza hiyo, ukimya uliompa Kisu nafasi ya kupiga hatua moja mbele.



“Samahani, mkuu,” alisema kwa heshima huku akimtazama sawia Jaji Pesambele. “Nina muda mfupi wa kukaa hapa. Tafadhali…”



“Us’jali,” Pesambele alimkata kauli. “N’na bia tatu tu kichwani. Sijalewa. Naikumbuka miadi yetu. Nipe dakika moja tu.”



“Sawa, mheshimiwa.”



Mara Pesambele alimimina kinywaji ndani ya glasi kisha akanywa kwa mkupuo na kuirejesha glasi mezani ikiwa tupu. Akamgeukia Zinduna na kumbusu kinywani. Hatimaye akawaambia wanawake hao, “Niko pembeni kidogo, nazungumza na huyu bwa’mdogo. Bia zikiisha, ongezeni.”



************



ZILIMCHUKUA Kisu takriban dakika kumi kumweleza Jaji Pesambele madhumuni ya ujio wake. Kwa Pesambele yalikuwa ni maelezo ya kusisimua na kufurahisha. Japo tangu aukwae u-jaji kiasi cha miaka saba iliyopita hakuwahi kushughulikia suala zito kama hilo kwa manufaa yake binafsi, hata hivyo hilo halikuwa jambo la kumfanya afikirie kupingana na Kisu.



Alitambua bayana kuwa uongozi wa ngazi za juu serikalini, kuanzia mkuu wa nchi, ulifuatilia kwa makini operesheni dhidi ya wahujumu uchumi. Yeye, akiwa ni miongoni mwa majaji walioteuliwa kuendesha kesi hizo, alijua kuwa serikali na wananchi kwa jumla walitarajia haki kutendeka.



Haki! aliwaza huku akicheka kimoyomoyo. Alikumbuka kuwa aliendesha kesi kwa kanuni zote za sheria na kutoa uamuzi wa haki tupu katika mwaka wake wa kwanza kwenye taaluma hiyo akiwa ni hakimu wa wilaya fulani. Mwaka wa pili, akiwa ameshakomaa kitaaluma, hakufanya mchezo tena. Ilipobidi, aliipinda sheria mradi tu mifuko yake iwe imepokea chochote.



Tangu wakati huo hadi siku hii alipokuwa faragha na Kisu, tayari alikwishabobea katika mipango iliyomwingizia pesa kupitia kesi mbalimbali. Hivyo hakuhofia chochote katika kuutekeleza mpango ulioletwa na Kisu.



Hivyo, kabla ya kufikia makubaliano yoyote aliamua kuwa wazi. Akamtazama Kisu kwa makini kisha akasema, “Kuwanusurisha na sakata hili ni jambo linalowezekana. Lakini hata wewe unajua jinsi sakata lenyewe lilivyo zito. Mpaka Mzee kalivalia njuga! Ni hapo ndipo naona suala hili linakuwa zito kuliko lilivyo. Sasa hebu n’ambie, hao jamaa wamejiandaa vipi?”



“Kwa kiasi chao, mzee.”



“Hilo sio jibu. Wanazo ngapi? Tusizungukezunguke bure!”



“Hilo ni juu yako, mheshimiwa,” Kisu alijibu. “Uzito au wepesi wa jukumu la kuwaokoa unaujua wewe. Hivyo ni bora wewe nd’o ungetaja kiwango kinachostahili.”



Jaji Pesambele alifikiri kidogo kisha akauliza, “Umesema wako sita?”



“Yeah, wako sita.”



“Sita,” Pesambele alinong’ona kama anayezungumza peke yake. Akatupa macho juu akionekana kuzama katika fikra. Hatimaye akayarejesha macho kwa Kisu na kusema, “Kila kichwa kimoja kinagharimiwa milioni mbili.”



Kisu alishtushwa na kauli hiyo. Makubaliano baina yake na kina Sadrudin yalikuwa ni wao kujifunga mkanda na kukusanya shilingi milioni 6 kwa jumla. Milioni 6 ni sawa na milioni 1 kwa kila mmoja. Na kwa siku mbili zilizopita alikuwa akizunguka kwa ndugu na jamaa wa watuhumiwa akikusanya pesa hizo.



Katika kanuni zake za mipango ya pesa, kiasi chochote kinachopitia mikononi mwake lazima ‘kipigwe panga.’ Kwa hilo hakuwa mzembe. Wakati huu akiongea na Pesambele, tayari milioni 6 zilikuwa ndani ya moja ya saraka za kabati yake, nyumbani. Kilichohitajika hapa ni makubaliano tu ili kiasi fulani cha pesa hizo kihamie katika himaya ya Pesambele.



Ndiyo, alitaka kuhakikisha kuwa ni kiasi fulani tu cha pesa hizo kitakachomfikia jaji huyo. Japo alitambua fika kuwa kulikuwa na ‘asante’ yake kutoka kwa kina Sadrudin, baada ya mafanikio yake, hata hivyo tamaa ilimtawala.



“Mheshimiwa, tafadhali punguza kidogo,” alimwambia.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



“Nipunguze?!” Pesambele alimkazia macho. “Kwani unadhani kazi n’takayoifanya ni ndogo? Ujue kuwa itanilazimu kuchukua si chini ya wiki moja au moja na nusu katika kuulazimisha uongo uwe ukweli na ukweli uwe uongo. Upo hapo?”



“Najua hivyo.”



“Sa’ kama unajua, nd’o unataka kun’ambia nini?” uso wa Pesambele ulishatengana na masikhara kwa maelfu ya kilomita. Akaongeza, “Hujui kuwa kupinda sheria na kuhakikisha serikali na jamii kwa jumla inakubaliana na uamuzi wangu ni kazi ngumu sana? Kazi itakayonilazimu nipunguze hata muda wa kulala usiku!”



“Najua.”



“Basi kawaambie hao jamaa zako waandae mzigo huo.” sasa ni kama vile Jaji Pesambele alikuwa akifoka.



Ukimya wa muda mfupi ulitawala kisha Jaji Pesambele alisimama na kuonyesha dalili ya kurudi kule kwenye meza yake.



“Tafadhali mheshimiwa, subiri kidogo,” Kisu alimshika mkono.

Pesambele aligeuka na kuhoji, “Kwani kuna la ziada?”



“Ndiyo.”



“Jipya?”



“Hapana. Ni kuhusu ishu hiyohiyo.”



“Enhe, sema.”



“Kwa kweli wao walijiandaa kwa milioni moja kila kichwa,” Kisu alisema. “Wasaidie mzee…”



“Moja tu?”



“Ndiyo, mzee.”



Kwa mara nyingine Pesambele alifikiri, kisha tena kwa mnong’ono akasema, “One million.” Kisha akaongeza sauti kidogo: “Na umesema wako sita tu?”



“Ndiyo, mzee.”



Jaji Pesambele alikitafakari kiwango hicho. Akacheka kimoyomoyo kwa kujua kuwa kazi atakayoifanya haitakuwa kubwa sana tofauti na alivyomwambia Kisu. Alijua kuwa ataifanya kazi hiyo ndani ya siku tatu na kumaliza.



Akamatazama Kisu huku kakunja uso kisha akamwambia, “Kazilete. Chukua laki tano. Nyingine kazilete. Na zisiwe za mafungu. Ziwe zimetimia ili nifanye kazi; sawa?”



“Sawa, mzee,” Kisu alijibu haraka. “Kwa hiyo tufanye lini na wapi?”



“Sema wewe.”



“Kesho. Au unaonaje?”



“Kesho?” Jaji Pesambele alionekana kufikiri. “Kesho ni Jumamosi, sio?”



“Ndiyo. Ni siku ya mtu kulala tu mchana na jioni unastarehe.”



Tabasamu la mbali lilichanua usoni pa Jaji Pesambele. “Ok, njoo nyumbani kabla ya saa tatu asubuhi. Na usije na hadithi nyingine. Uje na mzigo uliotimia; milioni tano na nusu. Kinyume chake ni afadhali usitie mguu kabisa!”



************



KWAMBA, mbele ya pesa hakuna linaloshindikana ni usemi na imani iliyojikita vichwani na vinywani mwa watu wengi hasa pale inapobidi kutumia pesa katika kugeuza hili kuwa lile; kubadili halali kuwa haramu au haramu kuwa halali.



Kitita kizito, kitita cha fedha taslimu, shilingi 5,500,000 kilipotua mikononi mwa Jaji Pesambele, akili ya jaji huyo ikaanza kufanya kazi kwa kasi. Zikamchukua takriban siku tano ‘akicheza’ na ‘misahafu’ ya sheria katika kuhakikisha anafanikiwa kutimiza matakwa ya waliozitoa hizo pesa.

Ndiyo, aliamua kulivalia njuga suala hilo ili siku atakapotoa hukumu, wanasheria wenzake, serikali pamoja na jamii nzima kwa jumla wasibaki na dukuduku lolote hususan hisia kuwa kesi hiyo ilizungukwa na mazingira ya rushwa.



Hatimaye ikaja siku. Ndiyo, ilikuwa ni siku ambayo Kipipa Mtakayote na wenzake walipanda kizimbani kwa ajili ya kusikilizwa kesi yao. Maelezo ya upande wa mashtaka na upande wa utetezi yakapokewa. Mwishoni, Jaji Pesambele akatoa tamko la ghafla, tamko ambalo halikutarajiwa na wengi hususan wale walioamini kuwa itapangwa tarehe nyingine itakayowahusisha mashahidi kutoka pande zote.



Alichofanya Pesambele ni kuisoma hukumu kwa takriban saa tano huku hitimisho lake likiwaacha wengi wakishangilia na wachache wakishangaa.



************



1984 – 1997



“BABAA! Babaa!” Pangapangua, mtoto pekee wa Kipipa Mtakayote alipiga kelele za furaha pindi alipomwona baba yake akitoka nje ya jengo la mahakama. Ilikuwa ni hekaheka tupu nje ya jengo hilo. Ndugu wa watuhumiwa wa kesi ya uhujumu uchumi walikuwa wakishangilia pale Jaji Pesambele alipotamka kuwa watuhumiwa hao hawana hatia.







Katika taarifa hiyo ya kimahakama aliyoitoa tangu saa 4 asubuhi hadi saa 9.40 alasiri, jaji huyo alisisitiza mara kwa mara kuwa hakukuwa na sababu yoyote ya kuwafungulia mashtaka watuhumiwa hao kwani upande wa mashtaka haukuthibitisha kuwa mali walizokutwa nazo hazikuwa za halali.



Furaha iliutawala uwanja wa mahakama hiyo, uwanja uliofurika umati wa watu ambao asilimia kubwa ilikuwa ya ndugu, jamaa na marafiki wa watuhumiwa.



Ilikuwa ni kama ndoto kwa watuhumiwa watano kati ya sita walionusurika kutiwa hatiani. Hao ni Lomolomo, Sadrudin, Kipangachuma, Kichewele na Ayatollah Matto. Wao, pamoja na kupokewa kwa shangwe pindi walipokuwa nje ya mahakama, hata hivyo hawakuwa tayari kuendelea kuwepo katika eneo hilo. Hivyo, bila ya kuchelewa walijitoma ndani ya magari yao na kuondoka.



Ni Kipipa Mtakayote ambaye alionekana kutokuwa na wasiwasi wowote. Yeye alimkumbatia mwanaye, Pangapangua na kumbusu mashavuni kisha kwa mnong’ono alimuuliza, “Mwanangu… mwanangu upo?”



Pangapangua ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 12, hakujibu kitu, zaidi alionekana mwenye furaha kupita kiasi.



“Mwanangu,” kwa mara nyingine Kipipa alimwita. “Mwanangu, mama yako yuko wapi?”



“Yule kulee…!” hatimaye Pangapangua alionyesha kwa kidole.



Kipipa Mtakayote aliangaza macho upande kilikoelekea kidole cha mwanaye. Akamwona mkewe akimtazama kwa macho ya huruma, macho yaliyolengwa machozi yaliyotokana na furaha iliyojikita moyoni mwake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Akamshika mkono mwanaye na kumfuata mkewe aliyekuwa kaegemea gari dogo, jeusi aina ya Mercedes Benz. Kadri alivyozidi kumsogelea ndivyo alivyozidi kuuona usowe ukizidi kung’ara kwa furaha. Na alipomfikia alimkumbatia kwa nguvu na kutulia kimya kwa sekunde kadhaa kabla hawajatengana na kutazamana tena.



“Mke wangu…”



“Mume wangu…”



************



JERAHA lililompata Kipipa Mtakayote wakati wa vita dhidi ya uhujumu uchumi halikuwa dogo. Lilikuwa ni jeraha kubwa, labda kuliko majeraha mengine aliyowahi kupata siku za kisogoni, majeraha ya kimwili na kiakili. Hata hivyo, pamoja na ukubwa wa jeraha hilo, taratibu lilianza kupona mara tu alipoachiwa huru. Ndiyo, lilipungua kadri siku, wiki na miezi ilivyosonga mbele. Miaka miwili baadaye halikuwa jeraha tena bali, kovu.



Ingawa lilibaki kovu, bado halikuwa ni kovu la kawaida. La hasha. Hili lilikuwa ni kovu lililomkumbusha mengi, mengi yaliyomzulia sononeko moyoni. Japo kilifikia kipindi ambacho utawala wa nchi uliwaruhusu wafanyabiashara wakubwa kwa wadogo kuagiza bidhaa kutoka nchi za ng’ambo na kujipangia bei kutokana na gharama walizoingia katika uagizaji, hata hivyo hiyo haikuwa nafuu ya kuweza kumfanya mtu kama Kipipa Mtakayote ayasahau yaliyomkuta.



Umri ukizidi kumkimbia, huku akiwa na mtoto mmoja tu, Pangapangua, mtoto aliyempenda na kumjali kama nafsi yake na kumchunga kama mboni ya jicho lake, sasa Mzee Kipipa Mtakayote aliiona Tanzania kama nchi ya ukimbizi. Kumbukumbu ya yaliyotokea mwaka 1967 katika Azimio la Arusha na yale masaibu yaliyomkuta mwaka 1983 katika vita dhidi ya uhujumu uchumi zilimfanya ashindwe kuiamini serikali yake. Hakuwa na hakika kesho serikali itatamka nini kuhusu wafanyabiashara.



Kutokana na wasiwasi kuhusu mali zake, aliamua kununua nyumba katika mji maarufu wa Eldoret nchini Kenya na kumsomesha mwanaye, Pangapangua katika shule moja ya kimataifa jijini Nairobi miaka miwili baada ya kuwa huru.



Huko Nairobi, Pangapangua alipata elimu ya msingi, sekondari, hatimaye akasoma elimu ya biashara na kuhitimu baada ya miaka miwili.



Hadi Pangapangua alipohitimu elimu hiyo, Kipipa Mtakayote alikuwa na umri wa miaka sitini na tatu. Alikuwa ni mzee tosha. Sasa hakuwa na uwezo wa kusoma baadhi ya maandishi bila ya kuvaa miwani maalumu. Hakuwa na uwezo wa kutembea kwa muda mrefu kutokana na maumivu ya miguu. Ilimradi uzee ulimzulia dosari nyingi mwilini, dosari zilizomfanya ashindwe kutekeleza baadhi ya majukumu yaliyomkaabili.



Hata hivyo, pamoja na dosari zote hizo, kitu kimoja kilimtia faraja moyoni; Pangapangua. Ndiyo, ni mwanaye, Pangapangua aliyemfanya ajione bado amekamilika kimwili na kiakili. Elimu aliyopata Pangapangua nchini Kenya ilimtia kiburi mzee huyo. Sasa aliamini kuwa mali yake haitapotea bure, itakuwa chini ya mwangalizi makini, mwangalizi msomi, mwangalizi ambaye kwa kiwango chake cha elimu haitakuwa rahisi kumtapeli au kumhujumu kwa namna yoyote ile.



Ni imani hiyo iliyomfanya azue kikao cha dharura siku chache baada ya Pangapangua kurejea nchini akitokea Kenya.



Ilikuwa ni usiku, saa 3:30, dakika chache baada ya maakuli, ndipo mzee Kipipa Mtakayote alipomtaka mwanaye, Pangapangua, wakutane katika chumba ambacho mzee huyo hukitumia pindi apatapo wageni wa kikazi. Kilikuwa ni chumba kisichotofautiana na ofisi za kawaida. Zaidi ya meza kubwa, kiti cha mwenyeji nyuma yake, kabati iliyofurika majalada, na jokofu dogo lililosheheni vinywaji laini, hakukuwa na kitu kingine.



Halikuwa jambo la ajabu akilini mwa Pangapangua kuitwa na baba yake katika chumba hicho. Hii haikuwa mara ya kwanza. Kuna siku aliwahi kumwita kwa ajili ya kumkabidhi pesa za kununulia bidhaa fulani. Siku nyingine alimwita humo chumbani akimwonya juu ya tabia ya kuchelewa kurejea nyumbani toka matembezini; huo ulikuwa ni wakati yuko katika likizo ya masomo. Kwa jumla, ni mara nyingi aliongea naye chumbani humo kwa ajili ya jambo moja au lingine kuhusu maisha.



Ndiyo, sio mara moja au mbili ilishatokea hivyo. Lakini, tofauti ni kwamba, katika kipindi hicho, walikuwa wakikutana mchana kweupee! Lakini leo, ni usiku, tena ni usiku ambao kwa kawaida huwa wakijiandaa kulala.



Kuna nini? Pangapangua alijiuliza kimoyomoyo.

Hakupata jibu. Hivyo, kwa hatua za kinyonge alimfuata mzazi wake ambaye mara tu alipoingia katika chumba hicho, alipitiliza hadi katika kile kiti chake cha kuzunguka na kujipweteka kivivuvivu.



Pangapangua aliketi katika kiti kimojawapo, kati ya vile viti maalumu kwa wageni. Ukimya wa muda mfupi ukatawala chumbani humo. Wakati huo mzee Kipipa Mtakayote alitwaa jalada moja zito na kuliweka mezani. Kisha akaitwaa miwani mfukoni na kuipachika usoni. Akalifunua jalada lile na kupitia nyaraka kadhaa kisha akalifunika. Wakati huo lile la swali la kuna nini? Liliendelea kurandaranda kichwani mwa Pangapangua na bado hakuweza kupata jibu lake.



“Mwanangu,” hatimaye Kipipa Mtakayote aliuvunja ukimya ule. “Nakuomba uwe mvumilivu kidogo. Najua utashangaa kwa nini nimekuita huku ofisini wakati huu ambao huwa ni kawaida yetu kuwa tumelala au tunajiandaa kulala. Ruksa kushangaa.”



Akatulia kidogo akimkodolea macho Pangapangua. Kisha akaendelea, “Ninalo jambo moja muhimu. Nimekuita kwa jambo muhimu ambalo naamini ni la manufaa katika familia yetu, na zaidi, kwako binafsi.”

Kwa mara nyingine alivuta muda pasi ya kutamka chochote, kitendo kilichomwongezea shaka Pangapangua na kuhisi kiti kina moto huku maswali zaidi yakizidi kujikita akilini mwake.



Kuna mali iliyoibwa?



Amekorofishana na mama?



Ana maradhi yanayomkatisha tamaa ya kuishi?



Kuna…



Kuna…



Hayo ni baadhi tu ya maswali yaliyomjia kichwani kwa kipindi hicho kifupi. Lakini pia, kama alivyokosa jibu la lile swali la awali lililomjia zaidi ya mara kumi akilini, majibu ya maswali haya pia hayakupatikana. Akaamua kutulia akimsubiri mzee Kipipa atamke alichomwitia, mzee ambaye wakati huo alikuwa akimtazama kwa macho makali kupitia katika miwani yake maalum ya kusomea.



“Mwanangu,” kinywa cha mzee Kipipa kilifumbuka tena.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Mwanangu, sasa umekua. Sasa unastahili kuitwa mwanamume. Umesoma. Elimu yako ndiyo kinga na fahari kwetu sisi wazazi wako. Hujisikii fahari kwa kiwango cha elimu uliyonayo?”



“Baba kwa kweli najisikia fahari,” Pangapangua alijibu kwa unyenyekevu, sauti yake ikidhihirisha mchanganyiko wa mshangao na udadisi moyoni mwake.



“Ndiyo, unayo haki ya kujisikia fahari. Mimi baba yako niko tofauti na wewe, tena huenda tofauti yetu ni kubwa sana. Kwa kweli sikusoma sana, niliishia darasa la nne miaka ile ya sitini, miaka michache tu baada ya uhuru wetu.











ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog