Search This Blog

Saturday, 5 November 2022

ROHO NYEUSI - 4

 








Simulizi : Roho Nyeusi

Sehemu Ya Nne (4)





“LAKINI kiwango kidogo cha elimu yangu kilinisaidia kupata mwanga wa kuyaendesha maisha katika dunia hii iliyolaaniwa. Nilifanikiwa kuzungumza na Mwingereza mmoja niliyekuwa nikifanya kazi kwake siku chache kabla ya lile zoezi la kuwanyang’anya wananchi mali zao, lile zoezi lililoitwa…”



“Vita vya uhujumu…”



“Hapana!” Kipipa alimkata kauli. “Hilo si la juzijuzi tu! Nazungumzia lile la kwanza. Nadhani umelisahau. Kwani somo la History hukulijali tangu primary school?”



“Nililijali sana baba.”



“Basi kumbuka vizuri,” Kipipa alisema huku akivuta kumbukumbu kichwani.



“Siyo lile la Azimio la Arusha?” Pangapangua alimzindua.



“Yap! Hilohilo!” mzee Kipipa alikubali. “Ni Azimio la Arusha. Hata mwaka siwezi kuusahau; elfu moja mia tisa na sitini na saba. Anyway, tuachane na hayo mambo ya Azimio la Arusha. N’nachotaka utambue ni kuwa, yule mzungu aliyeitwa George Martin ndiye aliyefanya leo tuwe katika hali hii kimaisha. Siwezi kumsahau rafiki yangu yule. Mungu amrehemu.”



Kufikia hapo alitulia tena. Akaitoa miwani usoni na kuipangusa kwa leso. Kisha akayasugua kidogo macho na kuirejesha miwani. Akamtazama tena Pangapangua.



“George alikuwa ni mtu aliyejiweza kimaisha wakati ule,” aliendelea. “Alikuwa na viwanda viwili vya sabuni, na machimbo kadhaa katika mgodi wa dhahabu huko Geita, Mwanza. Lakini George hakuwa mbumbumbu. Alikuwa makini, akifuatilia kwa kina mambo ya serikali. Alikuwa na marafiki ambao ni viongozi wa serikali wa ngazi za juu hapo Songambele. Ni hao waliokuwa wakimpa siri mbalimbali za serikali.



“Ilitokea siku moja akadokezwa juu ya Azimio la Arusha. Hakuzubaa, aliharakisha kuhamishia pesa zake katika akaunti zake za Uingereza na Ugiriki, kisha akauza kiwanda kimoja cha sabuni na kingine akanikabidhi.



“Sikufichi, ni kiwanda hicho alichonipa ndicho kilichonifikisha hapa nilipo. Leo hii tuna mali nyingi, mwenyewe unaona. Lakini ni vizuri pia ukitambua fika kuwa katika uhai wangu huu unaoelekea ukingoni, kuna jambo moja tu ambalo sitalisahau. Uliza ni jambo gani.”



“Ni jambo gani?” Pangapangua aliuliza haraka.



“Dhuluma.”



“Dhuluma?”



“Ndiyo, dhuluma,” Mzee Kipipa Mtakayote alisisitiza. “Usione leo hii tuna biashara zetu kubwa. Usione leo tuna magari mengi. Usione leo hii tuna nyumba nchini Kenya, nchi ambayo sio asili yetu. Yamepita mengi hapo kati mwanangu! Wewe ulikuwa bado mdogo, akili yako ilikuwa haijakomaa. Lakini tayari ulikuwa katika dunia hii iliyofurika tani milioni nyingi za maasi. Kwa kweli mengi yamepita hapo kati.”

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Kufikia hapo alitulia tena, na safari hii machozi yalitanda machoni mwake. Machozi ya mtu mzima!



Kwa Pangapangua, hiki kilikuwa ni kipindi kingine kigumu, kipindi kilichomsisimua na kumtisha kwa kiwango kisichokadirika.



“Basi, basi baba, labda kwa leo tuahirishe maongezi yetu,” alisema kwa tabu huku akimtazama baba yake.



“Hapana, ” mzee Kipipa alitamka kwa namna ya kufoka. Akaongeza, “Hatuwezi kuahirisha. Linalowezekana leo lisingoje kesho. Tafadhali, tafadhali, univumilie kidogo mwanangu.”



Akameza funda la mate kisha akaendelea, “Zamani, wakati wewe ukiwa mdogo, vilizuka vita baina yetu na Uganda. Tanzania yetu ni nchi yenye rekodi nzuri. Ni nchi yenye kupenda amani. Lakini mwishoni mwa mwaka elfu moja mia tisa na sabini na nane tulivamiwa na Uganda…”Akazungumza kwa kirefu juu ya vita vile na athari zake kwa jamii wakati vikiendelea na baada. Hatimaye akafikia kwenye operesheni dhidi ya uhujumu uchumi na ulanguzi mwanzoni mwa mwaka 1983.



“Wafanyabiashara wengi tulikamatwa,” alisema. “Tuliwekwa ndani bila ya sababu yoyote ya maana. Kama sio ujanja, tungeozea jela. Ilitubidi tutumie mbinu kali hadi tukafanikiwa kutoka. Ndiyo, tulitoka, lakini mali zetu zilizodaiwa kuwa tulizipata kwa njia zisizo halali, zilitaifishwa. Kwa kweli tulipata hasara kubwa sana. Siyo rahisi kusahau.



“Hata hivyo, tunamshukuru Mungu kwa kutuokoa na zahama iliyokuwa mbele yetu,” akasita ghafla na kumtazama Pangapangua kwa macho makali.



Kisha akaendelea, “Nilichokuitia leo ni kukufahamisha kuwa, sasa unapaswa kusimamia biashara zangu zote. Hizi ni mali zako, hivyo unapaswa kuzichunga na kuzizalisha zaidi. Kama unavyoniona, hivi sasa afya yangu siyo nzuri. Nimekuwa mtu wa kumwona daktari mara kwa mara. Na haya maradhi ya moyo siyo ya kawaida, huenda nikaiacha dunia saa yoyote na dakika yoyote…”



***********



NAAM, Pangapangua alianza rasmi kusimamia miradi ya baba yake. Pale palipomtatiza hakusita kumshirikisha. Mwaka mmoja baadaye akawa mzoefu. Sasa majukumu yote yakawa chini yake. Miradi ikazidi kupanua wigo. Kwa jumla Pangapangua aliweza kuiendesha miradi yote kwa ufanisi mkubwa.



Hatimaye ikaja siku. Ilikuwa ni Jumamosi, saa 12 jioni, Pangapangua alipokuwa katika duka lao kubwa la bidhaa za jumla, mara akamwona Maselina, binti aliyekuwa akifanya kazi za ndani nyumbani kwao.



Maselina alikuwa akitweta, macho yamemtoka pima, akawa akiangaza huku na kule kabla hajamtia machoni Pangapangua. Ile ingia yake ilimshtua sana Pangapangua, na isitoshe, haikuwa kawaida yake kuja dukani hapo. Mara kwa mara ni Jacob ndiye hutumwa hapo. Jacob ni mfanyakazi wa kiume ambaye alikuwa akitunza kuku na kuwakamua ng’ombe maziwa.



Lakini hilo halikumshangaza sana Pangapangua, kilichomshangaza ni mwonekano wa Maselina. Moyo ukapiga paa! Akaacha kuhesabu mabulungutu ya noti yaliyokuwa mezani. Akamtazama Maselina kwa macho makali. Macho yao yalipokutana, akabaini taharuki iliyosambaa katika mishipa ya fahamu ya Maselina. Papohapo akanyanyuka na kumuuliza: “Maselina, vipi? Kuna nini?”



Maselina hakujibu. Alimtazama zaidi Pangapangua, kisha akayahamishia macho kwa wateja waliokaribia kumi, ambao walionesha kuwa na haraka ya kuhudumiwa. Alipoyarejesha macho kwa Pangapangua, tayari Pangapangua akajua ni nini alichopaswa kufanya.



Huku moyo ukimdunda kwa kasi isiyo ya kawaida, alitoka mezani, akaufuata mlango mdogo na kuufungua. Kisha akamtazama Maselina na kusema, “Njoo. Pita huku.”



Maselina alifuata maagizo hayo. Alipofika mbele ya meza ya Pangapangua, akavuta kiti na kuketi. Pangapangua akamtazama kwa makini zaidi. “Enhe, sema,” alimwambia huku kamkazia macho.



“Kuna tatizo,” Maselina alisema kwa unyonge.



Macho ya Pangapangua yakiendelea kumkodolea Maselina, aliamua kutoyamalizia mambo hayo hapo dukani. Akayakusanya yale mafurushi ya noti na kuyafungia ndani ya saraka ya meza. Kisha akasema, “ Twende ukan’ambie hicho kilichokuleta.” Akatangulia kuelekea sehemu ya nyuma ya duka hilo.



“Kwa hiyo nd’o vipi?” mteja mmoja alihoji kwa hamaki.



“Nakuja,” Pangapangua aligeuka na kumjibu mteja huyo. Kugeuka kwake kulimfanya azigundue hasira za wateja wengine.



“We’ vipi?” mzee mmoja wa kiume alifoka.



“Nyie mnaleta mapenzi kazini!” mama mmoja ‘bongebonge’ alibwata.



“Oyaa! Mambo gani tena hayo mnayotuletea?” kijana mwingine aliuliza.



“Kama mnapendana sana basi fungeni duka mwende kwenu,” msichana mmoja mrembo aliwaropokea.



Ni hao waliodiriki kuvitumia vinywa vyao katika kutoa dukuduku zao. Wengine waliishia kusonya huku wakinung’unika kwa minong’ono, sauti zao zikithibitisha kutoridhishwa na hatua iliyochukuliwa na Pangapangua.



Pangapangua alishusha pumzi ndefu kabla hajawatuliza. “Mnisamehe kidogo, wateja wangu. Kuna tatizo dogo. Nipeni dakika mbili tu, tafadhalini.”



Kelele za kuipinga kauli yake zikatanda dukani humo, kelele ambazo sasa aliamua kutozijali. Akawapungia mkono huku akitabasamu. Akayoyoma na Maselina hadi katika chumba kipana ambacho zaidi ya viti viwili, meza moja na kabati fupi, hakukuwa na samani nyingine. Pangapangua aliketi katika kiti kimojawapo huku akimwashiria kwa mkono Maselina aketi katika kiti kingine.



“Kuna nini, Maselina?” hatimaye alimuuliza huku akiendelea kumkazia macho.



************



KIASI cha miaka 15 iliyopita, mama mmoja wa Kimanyema, akiwa katika dansi la bendi ya Orchestra Super Kibisa, mjini Kigoma, alikutana na bwana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Kisigosigo. “Ninafanya biashara ya kusafirisha dagaa Dar es Salaam,” aliendelea kujitambulisha. “Naishi Katubuka kando ya Barabara ya Mwasenga.”



Mwanamke yule aliyejaaliwa mwili mkubwa na teketeke, alitabasamu kidogo kisha akasema, “Asante kwa kujitambulisha. Mimi niko hapahapa Mwanga, Mtaa wa Legezamwendo.” Hakuendelea zaidi.



Kisigosigo alimtazama kidogo kisha akamuuliza, “Ni vibaya nikilifahamu jina lako?”







HUKU akitabasamu kwa mbali, mwanamke huyo alijibu, “Siyo vibaya. Naitwa Siwazuri Omari.”



“Ndiyo, Bi. Siwazuri. Umeolewa?’



“Bado.”



“Unaishi peke yako?”



“Niko na dada’ngu.”



Hawakuishia hapo dansini tu. Muziki ulipohitimishwa saa 8 usiku, waliondoka pamoja hadi kwa Kisigosigo. Huko wakafungua ukurasa mpya. Sasa Siwazuri akawa wa Kisigosigo na Kisigosigo akawa wa Siwazuri.



Baada ya miezi miwili Siwazuri akayagundua mabadiliko mwilini mwake. Hakupata hedhi kama ilivyo kawaida. Siku zilipozidi kusonga mbele akaamua kumwona daktari, Hospitali ya Maweni.



“Una mimba,” daktari alimwambia.



Ilikuwa ni habari njema kwake kwani alihitaji mtoto. Pia ilikuwa ni habari njema kwa Kisigosigo ambaye alishatengana na mkewe Anita, baada ya kuishi kwa takriban miaka mitano bila ya kujaaliwa mtoto.



Siwazuri akahama kwa dada yake na kwenda kuishi kwa Kisigosigo. Miezi kadhaa baadaye mtoto mzuri wa kike akazaliwa. Furaha ikaongezeka ndani ya nyumba.



“Tumpe jina gani?” Kisigosigo alimuuliza Siwazuri.



“Maselina.”



“Kwa nini?”



“Ni jina la bibi yangu.”



“Sawa,” Kisigosigo aliafiki. “Mungu akitujaalia mtoto wa pili, mimi nd’o n’tachagua jina. Sawa?”



“Sawa.”



Ni kama Mungu angewajaalia mtoto wa pili. Haikuwa hivyo. Wakati Maselina akiwa na umri wa miaka miwili na miezi mitatu, siku moja, Siwazuri akiwa nyumbani, alipokea taarifa za kusikitisha. Kwamba, Kisigosigo kagongwa na daladala jijini Dar es Salaam alikokwenda kwa shughuli zake za biashara ya dagaa. Na kwamba alifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa hospitali.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Lilikuwa ni pigo zito maishani mwa Siwazuri. Na labda angekuwa na ahueni fulani kama angeendelea kuishi katika nyumba ile, lakini mambo yalimgeuka. Ndugu na jamaa wa marehemu Kisigosigo walimfukuza kama mbwa wiki chache tu baada ya mazishi. Lilikuwa ni pigo lingine zito. Pigo la pili! Pigo zito!



Akalazimika kurudi kwa dada yake, Legeza Mwendo. Maisha yake yakawa hayana mbele wala nyuma. Msongamano wa mawazo ukazidi kujikita kichwani mwake. Japo dada yake alijitahidi kumliwaza, hata hivyo hakuliwazika.



Ndipo ikaja siku. Ilikuwa ni asubuhi tulivu yenye kutawaliwa na manyunyu ya mvua. Siwazuri aliamka akatayarisha stafutahi, akashiriki na dada yake pamoja na mwanaye na watoto wawili wa dada yake huku akionekana kuchangamka zaidi, tofauti na siku zilizopita tangu afiwe na mumewe kipenzi.



Baada ya stafutahi hiyo, alitwaa pesa kidogo katika akiba yake kisha akaenda katika duka la dawa ambako alinunua vidonge vinane vya Quinine na sita vya Valium.



Aliporudi nyumbani alivihifadhi mahali fulani pa siri kisha akamtwaa Maselina na kumpakata miguuni. Akamtazama kwa muda mfupi kisha akamuuliza, “ Mwanangu, baba yako yuko wapi?’



“Baba! Yuko kulee..” Maselina alijibu huku akionyesha kwa kidole barabarani.



Siwazuri alitabasamu, tabasamu la huzuni. Akamshusha Maselina na kutwaa kalamu na karatasi. Akaandika maneno machache kisha akaikunja karatasi hiyo na kuitia ndani ya bahasha. Akaifunga bahasha na kuandika juu jina la dada yake: SIKUJUA.



Wakati huo Sikujua alikuwa sokoni kununua vyakula. Hivyo, kwa Siwazuri, huo ulikuwa muda mwafaka wa kutekeleza malengo yake.

Akamtazama tena mwanaye ambaye alikuwa sakafuni akicheza. Akamtwaa na kumbusu kisha akamwambia, “Kwa heri, mwanangu. Nakutakia maisha mema. Kwa heri.”

Maselina alicheka. Kwa jumla hakujua mama yake alimaanisha nini alipomwambia hivyo.



Siwazuri aliingia chumbani mwake na kutandika mashuka yake meupe kitandani, kisha akarudi sebuleni ambako alifungua kabati na kutoa kikombe cha plastiki. Akaufuata mtungi mkubwa na kuchota maji na kurudi tena chumbani. Akaketi na kukiweka kikombe juu ya stuli.



Sasa akavitwaa vidonge vya Quinine na kuvimwaga katika kiganja cha mkono wa kushoto. Akavitazama huku moyo ukimdunda kwa kasi. Akahisi hofu ikimjia kwa mbali. Lakini ghafla akapiga moyo konde na kuamua kuchukua pakiti ya pili iliyokuwa na vile vidonge vya Valium. Nayo akaifungua na kuvimwaga vidonge vyote katika kiganja kilekile. Akawa na jumla ya vidonge kumi na vinne.



Akaguna huku akivikodolea macho jinsi vilivyotua kiganjani hapo. Kwa jumla wingi wake ulimtisha. Alitambua fika kuwa kazi ya Quinine, viwe ni vidonge, iwe ni drip au sindano, ni kupambana na vijidudu vya malaria. Lakini hakuwa na hakika juu ya matumizi ya Valium mwilini mwa binadamu.



Kuna wakati, enzi zile ambazo bado dawa ya Chloroquine ilikuwa ikitumika nchi nzima kama tiba halisi ya malaria, aliwahi kushauriwa na daktari atumie vidonge vya Phenegan, dakika chache kabla hajanywa Chloroquine.



Ushauri huo alipewa baada ya kumtaarifu daktari kuwa hupata usumbufu wa kujikuna mwili mzima kufuatia muwasho unaomsakama, saa 24 baada ya kuzinywa hizo Chloroquine.



Mara wazo la kuvirejesha vidonge hivyo kwenye pakiti likamjia. Lakini, kama lilivyomwingia ghafla, ndivyo pia lilivyoyeyuka akilini kwa kasi ya umeme. Sasa, kama aliyepandwa na mzuka alivitumbukiza vidonge hivyo kinywani, kisha akafuatisha mafunda kadhaa ya maji. Vidonge vikatokomea tumboni!



Dakika tatu za awali hakuhisi mabadiliko yoyote mwilini. Dakika tatu nyingine akaanza kuhisi kichefuchefu ambacho hakikudumu sana. Kilikatika ghafla na koo likawa kavu kupita kiasi. Ukavu huo wa koo ulizidi kuimarika huku pia akihisi uwezo wa macho kuona mbali ukipungua, na nguvu zikimomonyoka taratibu maungoni.

Akakusanya nguvu. Akapanda kitandani na kulala chali, kisha akaitwaa ile bahasha na kuiweka kifuani pake. Taratibu kiza kikaanza kutanda machoni. Usingizi mkali ukamjia. Koo nalo likazidi kumtesa kwa ukame wake. Hatimaye akashusha pumzi ndefu na kutulia tuli!



Sikujua alikuja kubaini kuwa mdogowe kajiua baada ya kuingia chumbani humo na kuukuta mwili wake ukiwa umelala shagalabaghala na povu zito likitoka kinywani. Alipomtikisa na kumwona yu teketeke, kisha akaitwaa ile bahasha na kuifungua, akasoma ujumbe uliomo, hakuhitaji mtu mwingine wa kumthibitishia kuwa Siwazuri kaiaga dunia!



…MPENDWA DADA , NIMESHINDWA KUENDELEA KUISHI KWA MATESO YA MOYO NA MAWAZO YASIYOKWISHA. USIPATE TABU, NIMEKUNYWA QUININE 8 NA VALIUM 6. SITAPONA. BURIANI DADA YANGU. TAFADHALI NITUNZIE MWANANGU.



Yalikuwa ni maandishi aliyoyakuta katika kijikaratasi kilichokuwa ndani ya bahasha ile.



************



KIFO cha Siwazuri kilimfanya Maselina aishi kwa matunzo ya mama yake mkubwa, Sikujua. Miaka kadhaa baadaye alipelekwa shule ambako alisoma hadi darasa la saba na kutochaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari.



Wakati huo, akili ikiwa imeshakomaa kiasi, na akiwa na taarifa za uhakika kuwa wazazi wake walikwishafariki dunia, Maselina hakuwa mbumbumbu wa fikra. Japo alikuwa akila na kulala hapo kwa mama yake mkubwa, lakini hata hivyo alianza kuyagundua mabadiliko fulani katika haki iliyomstahili.



Ni watoto wa Sikujua waliopewa kipaumbele katika huduma muhimu. Kwa mfano; walipelekwa shule za sekondari za binafsi, wakanunuliwa nguo nzuri mara kwa mara, na kadhalika na kadhalika.



Mara mbili, tatu aliwahi kukaripiwa kwa maneno makali na hata kutishiwa kufukuzwa kwa sababu alikutwa akiongea na mvulana mmoja wa nyumba ya pili, japo maongezi yao yalikuwa ya kawaida. Walikuwa katika hali ya kawaida, katika mazingira ya wazi lakini akilini mwa Sikujua zilijengeka hisia kuwa walizungumzia mapenzi, akiamini kuwa hakuna maongezi yoyote kati ya mvulana na msichana zaidi ya yale yahusuyo ngono.



Matukio ya aina hiyo, pamoja na mengine mengi yalimchoma moyo mama mmoja aliyeishi nyumba ya tatu toka kwao Maselina. Mama huyo aliitwa Rukia. Yeye alijaaliwa mtoto mmoja tu, mtoto ambaye hakuwa riziki kwani alifariki wiki moja tu baada ya kuzaliwa.



Maisha ya Rukia yalitegemea biashara ya vitenge kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi, na sabuni za kufua zilizotengenezwa kwa mafuta ya mise hapo mjini Kigoma. Mise ni mbegu zinazotokana na zao la mchikichi ambalo ni zao kuu linalotoa mafuta ya mawese mkoani Kigoma.



Alipeleka bidhaa hizo Songambele ambako alipata faida nzuri na hivyo mjini Kigoma, hususan Mtaa wa Legeza Mwendo, akawa ni miongoni mwa watu walioonekana kuupiga vita na hatimaye kuushinda umaskini.



Kati ya karama alizojaaliwa na Mwenyezi Mungu, huruma ni jambo mojawapo. Na, ni huruma hiyo iliyomfanya siku moja jioni, kitu kama saa 12 hivi, amwite Maselina aliyekuwa kaketi nje ya nyumba ya Sikujua, kajiinamia.



HAKUMWITA kwa sauti bali alimwashiria kwa mkono tu. Maselina alimtazama kisha akanyanyuka. Kabla hajamfuata, aligeuka huku na kule ndipo akavuta hatua.



“Mama yupo?” Rukia alimuuliza.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Hayupo.”



“Baba’ako?”



“Wote hawapo.”



“Wamekwenda wapi?”



“S’jui, lakini wameondoka na dada Siamini.”



“Kwa hiyo uko peke yako nyumbani?”



“Hataa, yupo pia dada Asha.”



“Anafanya nini huyo Asha?”



“Yuko chumbani anasoma.”



Rukia alimtazama kwa makini sana, kisha akarusha swali lingine: “Umeshakula?”



“Ndiyo.”



“Kweli?! ” Rukia alimkazia macho. “Usiwe mwoga! Sema! Umeshakula?”



“Ndio, ni’shakula.”



“Na umeshiba?”



“Ndiyo.”



“Ok, njoo nyumbani mara moja.”



Ni huko ambako Rukia alimpa ‘somo’ kali Maselina na hatimaye kuilainisha akili yake. “Tukiwa Songambele utapata kazi,” alimwambia. “Usijali ni kazi gani, lakini kwa kifupi utakuwa ukijipatia kipato cha kuweza kukidhi baadhi ya mahitaji yako muhimu…”



Siku chache baadaye, Maselina na Rukia walikuwa ndani ya treni wakielekea Songambele, Maselina akiwa ametoroka nyumbani kwao na nguo zake chache tu.



Ni huko Songambele ambako Rukia alimkabidhi Maselina kwa mzee Kipipa Mtakayote, ambaye miezi michache iliyopita, wakati wakiwasiliana kwa biashara ambazo Maselina alimpelekea, alimwagiza amtafutie mfanyakazi wa ndani, mtoto wa kike, ambaye atakuwa na tabia njema tofauti na walivyo mabinti wengi wa Songambele.



Miezi miwili ya awali katika ajira ya Maselina, ilimfanya Mzee Kipipa Mtakayote amsifu Rukia kwa kumletea binti mpole, binti anayejituma katika kazi na ambaye si mnung’unikaji pindi zipitapo siku mbili hajalipwa mshahara wake wa mwezi.



Hatimaye ilitimu miaka mitatu Maselina akifanya kazi hapo kwa Kipipa Mtakayote. Sasa, zaidi ya uzoefu wa kazi, zaidi ya utendaji mzuri wa kazi, alikuwa kipenzi cha mzee Kipipa Mtakayote. Siyo kwamba mzee Kipipa Mtakayote alimchukulia Maselina kama mkwe au kwa namna yoyote ya matamanio. La. Alimpenda kutokana na sifa alizojaaliwa, sifa zilizomfanya mzee huyo amchukulie kama mfanyakazi hodari, zaidi ya wafanyakazi wengine waliopo katika biashara zake.

Ni kutokana na mapenzi makubwa kwake, ndiyo maana hakukosa kumpa majukumu mazito, majukumu ambayo hakuona mwingine wa kumpa, achilia mbali yule mhudumu wa kiume, Jacob, ambaye pia alionesha kuwa ni mpole na mwaminifu.



Akimchukulia kuwa ni binti mzuri, binti mwenye tabia njema, Kipipa Mtakayote alimwita dakika chache baada ya kuhisi mapigo ya moyo wake yakishuka ghafla.



“Kamwite Pangapangua,” alimwagiza huku sauti yake ikidhihirisha udhaifu mkubwa.



“Kwani vipi baba?” Maselina alimuuliza huku akimtazama kwa makini.



“Kamwite!” Kipipa Mtakayote alifoka kwa sauti yake ileile dhaifu. Kisha akaongeza, “Naumwa. Kamwambie, naumwa!”



Hali ya mzee Kipipa Mtakayote ilikuwa mbaya. Hilo lilikuwa dhahiri hata machoni na akilini mwa Maselina. Hivyo, alichokifanya ni kuondoka mbio akielekea dukani, katika lile duka la jumla, ambalo Pangapangua alisema kuwa angekuwa huko kwa siku hiyo yote.



Alilazimika kutumia uchochoro huu na ule ili tu aharakishe kufika hapo dukani. Dakika tano zilitosha. Na kama alivyotarajia, alimkuta Pangapangua akiwajibika, wateja wenye usongo wakimzonga.



Ni lile swali la Kuna nini Maselina? ndilo lililomfanya ampe taarifa kamili Pangapangua, taarifa ya kilichomleta hapo muda huo, akiwa amejivika mavazi hafifu huku usoni katahayari.



************



“BABA anaumwa!” Maselina alisema kwa sauti iliyofurika tani kadhaa za taharuki.



“Anaumwa?!” Pangapangua alibwata. “Ni nini hasa kinachomsumbua?”



“Anasema tu, anaumwa!” Maselina alijibu huku macho yake yakionesha msisitizo mkali wa kauli yake. “Tena anasema uende sasa hivi!” aliongeza.



Haikuwa taarifa ya kumfanya Pangapangua aendelee kuwa hapo hata kwa dakika tano. Papohapo alitoka, akapitia mlango wa nyuma ambako alilifuata gari lake dogo, Mercedes Benz jeusi na kulitia moto haraka.



Alifika nyumbani dakika tano baadaye na akamkuta baba yake mzazi, mzee Kipipa Mtakayote akiwa hoi, pumua yake ikiwa ya shida.



“Baba!” alimwita kwa sauti ya chini huku akimgusa begani na kifuani.



Kilichotokea kiliwashangaza mkewe Kipipa Mtakayote na wazee wengine wa kiume waliokuwa kando ya kitanda alicholala mzee Kipipa Mtakayote.



Alizinduka, akamtazama Pangapangua kwa macho makali kisha akatabasamu kidogo, tabasamu la matumaini. Akanyoosha mikono yake kama anayekusanya nguvu.



“Pangapangua,” alimwita kwa sauti iliyodhoofu.



“Naam, baba,” Pangapangua aliitika haraka.



“Siki’za, mwanangu,” mzee Kipipa Mtakayote alisema kwa sauti ya chini zaidi. “Hali yangu ni mbaya. N’naumwa, mwanangu. Nakuomba,” akasita kidogo, akajikongoja kunyanyuka, akaketi kitandani. Akahema kwa nguvu huku akiwatazama kwa zamu mkewe, Sarafina na mwanaye, Pangapangua.



Kisha akaendelea: “Nakuomba sana uijali familia yetu. Usiwatupe hawa wafanyakazi wetu, Jacob na Maselina. Wao, sasa ni sehemu ya familia.”



Akatulia kidogo. “Jambo lingine ambalo ningependa kukuasa,” aliendelea, “ni kujitahidi kuwa karibu na taasisi muhimu za serikali. Na zaidi, uwe karibu na viongozi wa ngazi za juu wa taasisi hizo.



“Kuna hawa watu wa Mamlaka ya Mapato. Hao ni watu hatari sana, jitahidi kujijenga kwao ili biashara zako zisiyumbe. Pia kuna watu wa Idara ya Biashara ambayo iko chini ya manispaa. Wao ndiyo wanaotoa leseni za biashara. Jitahidi kuwaweka karibu, na matokeo yake utasamehewa mambo mengi. Hata kwa watu wa Usalama Barabarani pia usiwasahau; pata kigogo mmoja katika idara hiyo ili magari yetu yasisumbuliwe.



“Halafu jitahidi pia kuwa karibu na mahakimu, majaji na makamanda wa polisi. Hao, kwa namna moja au nyingine ni kama vile wamekamata mpini. Ukiwa nao karibu, matatizo yoyote yatakayokupata ufumbuzi wa haraka utapatikana. Tumia pesa. Pesa kidogo zitazima kila kitu. Dunia ya leo pesa nd’o kila kitu, mwanangu.



“Jambo lingine, jiingize katika mambo ya siasa. Kichwani mwangu, siasa ni sanaa ambayo watu waliojikita humo huitumia kama kinga ya masilahi yao. Kama fikra zangu ni potofu, basi Mungu anisamehe. Lakini huko nchi inakoelekea ni kugumu. Mwanasiasa, na hasa mwanasiasa ambaye ni mwanachama wa chama tawala ana ahueni zaidi kuliko mwanasiasa wa chama kingine chochote cha upinzani.



Hivi sasa nchi yetu iko katika mfumo wa vyama vingi. Lakini, kwa mtazamo wangu, vyama vya upinzani havijajiimarisha kiasi cha kutokea chama kinachoweza kutwaa madaraka ya nchi. Bado mapema sana. Ingawa naona kadiri siku zinavyokwenda ukomavu katika vyama vya upinzani unazidi kujidhihirisha, hata hivyo sidhani kama vitafanikiwa kutwaa madaraka mapema.



“Vyama hivyo vina sera nzuri na malengo mazuri kwa wananchi, lakini kuviteka vichwa vya mamilioni ya wapiga kura waliokizoea chama fulani inahitaji muda. Hivyo, wewe jiingize kwenye chama tawala. Ikibidi, katika uchaguzi ujao, ugombee ubunge. Ukigombea ubunge kupitia chama tawala kuna uwezekano mkubwa ukashinda. Na ukishinda, mambo yako yatakuwa mazuri zaidi. Ni hayo niliyotaka kukwambia, mwanangu.”



Baada ya kusema hivyo, Kipipa Mtakayote alijilaza tena kitandani. Pangapangua na mama yake wakatazamana.



“Twende, mwanangu. Mwache baba yako apumzike,” mama yake alimwambia.



Waliondoka taratibu chumbani humo, kila mmoja akiwaza lake. Japo mioyo yao ilikuwa mizito, hata hivyo walijipa matumaini kuwa mzee Kipipa Mtakayote atapata nafuu. Vidonge alivyomeza vilikuwa na nguvu ya kumpa usingizi na nafuu ya maumivu.



**********



KUNA imani zinazoaminiwa na jamii nyingi za kibantu kuwa kama jambo fulani limekutokea, basi hiyo, ama ni ishara ya kujiwa na neema ama, ajali, nuksi au balaa lolote linakunyemelea. Hutokea, kama mtu amejikwaa njiani kwa mguu wa kushoto, basi huenda akaahirisha safari au akabadili njia. Itokeapo bundi akatoa mlio huku akiwa juu ya paa la nyumba yoyote, basi wakazi wa nyumba hiyo hugubikwa na hofu, imani kuwa kuna msiba utawatokea ikiwatawala mioyoni mwao. Mtu akikutana na paka mweusi njiani, huamini kuwa huko aendako kuna balaa. Isitoshe, mkono mmoja ukiwasha hususan wa kulia, huzuka imani kuwa utapata pesa au kitu chochote kizuri.



PANGAPANGUA alikuwa mvutaji wa sigara. Mara tu alipotoka chumbani mwa baba yake aliingia garini na kulitia moto akirejea dukani. Akiwa njiani aliwasha sigara na kuanza kuvuta. Wakati huo alikuwa akiwaza jambo fulani kuhusu biashara ya sabuni. Alikuwa mbali kimawazo, kaizamisha akili yake katika suala hilo kiasi cha kutoikumbuka sigara aliyoishika mkono wa kushoto huku ule wa kulia ukishughulika na usukani.



Sigara ile ilijikita katika suruali yake nyeupe, ya kitambaa cha thamani kubwa, na papohapo likaibuka tundu kubwa lililoitia dosari kubwa nguo hiyo.



Alishtuka, akaiangalia sehemu hiyo iliyoathirika, kisha akasonya kwa hasira. Papohapo akaamua kugeuza gari na kurejea nyumbani.

Kilichompokea nyumbani pindi alipofika ni vilio vya kinamama vilivyopenya masikioni mwake sawia kutoka ndani huku wanaume watatu, rika la baba yake wakiwa nje, wameketi kwenye jamvi wakizungumza kwa sauti za chini, nyuso zao zikitangaza bayana majonzi waliyonayo.



Haraka Pangapangua aliingia ndani. Akawapita kinamama takriban kumi sebuleni, mama yake akiwa miongoni mwao, wakilia kwa huzuni.



Akili ikamtuma kuelekea chumbani mwa baba yake. Huko aliwakuta wazee wawili wakimfunika baba yake shuka jeupe.



“Mwenzetu ametutoka,” mzee mmoja alimwambia kwa upole.



“Nini?” Pangapangua hakuyaamini masikio yake. Akakurupuka kumfunua uso baba yake. “Baba! baba!” aliita kwa nguvu huku akimpapasa uso, uso uliokuwa umetulia kama vile kasinzia tu, tena usingizi wa kawaida.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Kwa sekunde kadhaa Pangapangua aliduwaa, macho kayakodoa kwenye uso wa marehemu baba yake. Kisha bila ya yeyote mwingine kutarajia, alianguka chini na kuzirai.



************



1998 –OKTOBA, 2000



ALIZINDUKA nusu saa baadaye. Na zilipokwishapita saa mbili zaidi, akili yake ikaanza kurudi katika hali ya kawaida.



“Hii ndiyo dunia,” mzee mmoja alimwambia. “Sisi ni wapitaji tu. Leo tupo, kesho hatupo.”



“Piga moyo konde; yameshamwagika, hayazoleki,” mwingine alisema.



“Mwanangu, sasa wewe ndiye baba wa nyumba hii. Jikaze. Wewe ni mwanamume. Kuwa jasiri.” Hayo aliambiwa na mzee wa tatu.



Maneno hayo, pamoja na mengine mengi yaliyofanana na hayo ndiyo yaliyompa faraja na kumtia ujasiri kama alivyokuwa kabla baba yake hajakumbwa na mauti.



Baada ya maziko, shughuli ziliendelea kama kawaida, na mwaka mmoja baadaye Pangapangua akawa ameongeza kitu katika biashara zake, kitu kilichotoa taswira kuwa pato lake limekua zaidi.

Alinunua meli ya abiria yenye uwezo wa kubeba abiria mia moja na hamsini ikiwa ni meli pekee yenye mwendo wa kasi zaidi kuliko meli nyingine zote za abiria zilizokuwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.



Meli hiyo ilitia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam na ikawa ikifanya kazi ya kusafirisha abiria kati ya jiji hilo na Zanzibar. Ni meli hiyo iliyolikuza jina la Pangapangua kwa takriban pembe zote za nchi. Hadhi yake ikapanda maradufu.



Hata hivyo, pamoja na jina lake kuwa maarufu nchini, bado hakuona kuwa ni maarufu kwa namna aliyotaka. Alihitaji kuheshimiwa, atukuzwe! Vyombo mbalimbali vya habari viwe vikimtaja mara kwa mara, tena sio kumtaja kwa mabaya bali kwa mazuri tu. Kila jambo baya linalomhusu yeye lisiwe habari, lakini kila zuri hata liwe dogo kiasi gani, liwe ni habari kubwa kwenye magazeti, redio na televisheni zote nchini.



Ataipataje heshima hiyo? Alijiuliza. Akilini mwake alitambua kuwa rais wa nchi, waziri mkuu, Spika wa bunge, mawaziri na wakuu wa mikoa ndio pekee wenye heshima kubwa. Miezi mitano ijayo kulikuwa na Uchaguzi Mkuu. Wazo likamjia; kwamba, agombee nafasi mojawapo kati ya zile nafasi ambazo mtu hupata madaraka kwa kupigiwa kura na wananchi. Rais wa nchi huchaguliwa kwa kura na mamilioni ya wananchi. Kwake, kuwania urais aliona ni kichekesho cha aina yake.



Urais! Ataupataje wadhifa huo wakati hata hajawahi kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Nyumba Kumi? Atawaongoza vipi wananchi mamilioni kwa mamilioni ilhali hajadiriki kuwaongoza watu mia moja! Hilo halikumwingia akilini. Akahamia kwenye ubunge.



Agombee ubunge kwa kila hali, na akiukwaa ndipo heshima itapanda. Jina lake litakuwa likitanguliwa na “Mheshimiwa…”

Kuitwa “Mheshimiwa…! Mheshimiwa mbunge…” kwake ilikuwa ni heshima, zaidi ya heshima aliyonayo. Lakini kwa rika lake; kijana mbichi mwenye umri wa miaka thelathini na miwili, kuipata heshima hiyo ilihitajika kazi kubwa mbele yake. Na aliamini itakuwa ni kazi itakayomgharimu pesa nyingi na mbinu kali, zikiwamo mbinu chafu katika kuhakikisha anafanikiwa.



Hata hivyo, pamoja na gharama zote hizo, pamoja na mbinu atakazotumia, pia aliamini kuwa kitakuwa ni kichekesho kingine pale atakapotangaza kuingia katika kinyang’anyiro hicho huku akiwa hana mke. Kwa vyovyote angechukuliwa kuwa ni mtoto awaniaye ubunge au mhuni mmoja aliyechanganyikiwa.

Dhamira yake hiyo ikiwa thabiti moyoni mwake, siku moja akaamua kumtaka ushauri mama yake mzazi.



“Ubunge?!” mama yake alimtazama kwa mshangao. “Umefikiri nini hadi ukaamua kujikita katika mambo ya siasa?”



“Mama, naukumbuka vizuri ushauri wa marehemu baba,” Pangapangua alimjibu. “Nimeutafakari kwa kina ushauri huo na nikaona hakukosea.”



“Lakini we’ bado mtoto, mwanangu. Mambo ya siasa waachie watu wazima. Kwanza una majukumu mengi uliyoachiwa na marehemu baba yako. Isitoshe, bado hata hujaoa. Utaupataje ubunge wakati bado hujawa na heshima ya kuwa ni mtu mwenye mke?”



“Kuhusu majukumu mengi hilo lisikutishe, mama,” Pangapangua alisema. “Wapo watu wengi, tena wenye umri wa kunizidi kidogo tu, ambao wana miradi mingi na ni wabunge. Majukumu ya ubunge wanayatekeleza vizuri, na miradi yao inaendelea bila ya kutetereka.”



“Na kuhusu mke?”



“Hilo ndilo nakubaliana nawe. Cha muhimu ni kuoa. Na rika langu linaruhusu kufanya hivyo. Tatizo ni kwamba, sijajua n’tamwoa nani, na imebaki miezi michache tu kabla ya uchaguzi, na muda mfupi zaidi wa mtu kutangaza kugombea ubunge.”



“Hilo ndilo linakusumbua?” mama yake alimkazia macho. “Hilo tu! Kwa nini usimchukue Maselina?”



“Maselina! Huyu house girl wetu?”



“Ndiyo!” mama yake alijibu kwa msisitizo. “Ni binti mzuri tu. Hata wewe mwenyewe unamwona jinsi asivyokuwa mapepe. Ni vyema umuoe yeye kuliko kuanza kutafuta mwanamke mwingine. Unaweza kumpata mwanamke mwingine ambaye labda atakuvutia zaidi, lakini utakuwa huijui historia yake au mienendo yake yote. Utajikuta unaoa mwanamke ambaye hatakuwa na mapenzi ya dhati kwako, zaidi ya kuchuma mali yako. Kwa hilo inakubidi uwe makini zaidi.”



Yalimwingia vilivyo Pangapangua. Kwa kauli thabiti toka moyoni akasema, “Nimekubali, mama. Usemayo ni kweli tupu. N’nachokuomba ni kunisaidia kuongea naye kwa kina juu ya hilo.”



“Ondoa shaka, mwanangu,” mama yake alisema huku akitabasamu kwa mbali. “Nitaongea naye, na n’naamini kuwa kila kitu kitakwenda vizuri.”



************



KIFO cha aliyekuwa mwasisi wa taifa la Tanzania, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere tarehe 14 Oktoba, 1999 kiliwashtua na hatimaye kuwasononesha mamilioni ya Watanzania. Nchi iligubikwa na wingu zito la majonzi. Na likawa ni tukio lililowafanya baadhi ya watu wajenge hisia kuwa kifo chake kitaliyumbisha taifa kwa kiwango kisichokadirika.



“Nyerere katuacha! Basi na amani itatoweka!” mzee mmoja alisema kwa masikitiko.



“Na muungano nd’o hautadumu,” mwingine alidai.



“Muungano tu!” wa kwanza alidakia mithili ya aombolezaye. “Hata umoja utakufa! Udini na ukabila vitaibuka. Ee Mungu, bora ungeichukua roho yangu mapema.”



Wazee hao, pamoja na wengine wengi ambao enzi za ukoloni walikuwa vijana, ndiyo waliokuwa na shaka zaidi kutokana na kifo hicho cha Baba wa Taifa. Baadhi yao waliamini kuwa kifo chake kingetoa mwanya kwa vyombo vya dola, mathalani Jeshi la Wananchi na Jeshi la Polisi kuwanyanyasa wananchi. Na kwamba, vyombo hivyo vilimheshimu sana Nyerere tangu akiwa madarakani na hata alipoamua kupumzika.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/





KUNDI lingine lililotikiswa vilivyo na kifo hicho ni lile la kinamama. Wao waliamini kuwa kifo chake siyo tu ni pigo kwa taifa bali zaidi ni pigo kwao. Enzi za uhai wake alihakikisha utu wao unathaminiwa. Walikuwa na sauti. Baadhi yao walikuwa wabunge, baadhi mawaziri. Kwa jumla alihakikisha usawa kati ya wanaume na wanawake unakuwapo. Kifo chake kilichukuliwa na baadhi ya wanawake kuwa taa yao imezimika; hawataona, hawataonwa.



Vijana wasomi nao walihuzunika. Walizikumbuka hekima zake zilizowafanya Watanzania wawe familia moja. Walikumbuka jinsi alivyolitilia mkazo suala la elimu. Alitaka, na akasisitiza kila mtu apate elimu. Na wengi waliipata, japo sio wote waliofikia kiwango cha juu. Na elimu hiyo ilitolewa bure!



“Enzi zake tulikuwa tukigawiwa kalamu na daftari buree! Bure kabisa!” mmoja alisema.



“Hata karo hazikuwapo!” mwingine alidaka na kuongeza: “Na ukiugua we’ nenda hospitali; hakuna cha kuambiwa eti kalipie matibabu. Hakikuwapo kitu hicho!”



Hawakuwa kinababa, kinamama, na vijana wasomi pekee. La. Hata vijana wenye mienendo isiyokubalika katika jamii nao walilalamika na kusononeka hususan wavuta bangi, wabugiaji wa dawa za kulevya, wanawake wanaozurura mitaani usiku wakiinadi miili yao, mashoga hata vibaka na majambazi. Kuna mvutabangi mmoja alikuta kundi la watu wakizungumzia tukio hilo kwa unyonge, yeye akaangua kilio kikubwa huku akipayuka: “Nyerere wetu…! Baba..! Babaaa umetuacha babaaa…!”



Ndiyo, ni wengi walioguswa na mauti hayo kiundani sana. Ni wengi, siyo wote. Walikuwapo wale ambao kwa kiasi fulani walifarijika, wakafurahi na kucheka japo vicheko vyao viliwaka mioyoni mwao ilhali nyusoni wakionekana kusononeka, baadhi hata wakidiriki kuyaacha machozi yatiririke mashavuni. Machozi ya unafiki!

Pangapangua alikuwa miongoni mwa waliochekea mioyoni. Tangu aliposoma gazeti moja kuwa Baba wa Taifa yu mahututi katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas, jijini London, Uingereza, aliamua kuwa makini, akifuatilia kwa kina taarifa zote zilizohusu maradhi yaliyomsibu, sanjari na tiba aliyokuwa akipewa.



Alitokea kupenda na kuziamini zaidi taarifa zilizotangazwa na Idhaa ya Kiswahili ya BBC- London, Sauti ya Amerika na Sauti ya Ujerumani. Alijenga imani hiyo tangu enzi za uhai wa baba yake mzazi, mzee Kipipa Mtakayote, ambaye aliwahi kumwambia kuwa taarifa za vyombo hivyo vya habari ni za kuaminika zaidi.



Hivyo, tangu vyombo vingi vya habari vya Tanzania vilipoanza kuripoti suala la Baba wa Taifa kwenda Uingereza kutibiwa, hatimaye suala hilo likapewa uzito wa juu zaidi pale ilipothibitika kuwa alisumbuliwa na maradhi ya kansa ya damu, Pangapangua hakutaka chochote kimpite, chochote kilichotangazwa redioni, kuonyeshwa kwenye televisheni, na kuandikwa magazetini kuhusu kilichoendelea huko London.



Japo aliziamini zaidi taarifa za vyombo hivyo, hata hivyo hakukosa kufuatilia habari za vyombo vya habari vya Tanzania hususan redio ya Taifa, na, redio, televisheni na magazeti ya binafsi. Pia hakuacha kutupia macho katika magazeti yanayochapwa nchi jirani za Kenya na Uganda kwa lugha ya Kiingereza. Tofauti yoyote iliyojitokeza kati ya taarifa za vyombo vya habari vya Tanzania, Kenya, Uganda hata Afrika Kusini (RSA) na zile taarifa za nje ya Bara la Afrika, ilimfanya aziponde taarifa za Afrika na akaamini kila kilichotangazwa Ulaya na Amerika.



Kuna wakati taarifa nyingi zilidai kuwa Baba wa Taifa ana ahueni. Pangapangua alishangaa, akahuzunika na kisha akapiga moyo konde na kujipa matumaini yaliyotokana na kumbukumbu ya maongezi baina yake na daktari mmoja mkongwe ambaye aliuchambua kwa kina ugonjwa wa kansa ya damu.



“Ni vigumu sana kwa mgonjwa wa kansa ya damu kupona,” daktari huyo alimwambia. “Kwa kweli siyo rahisi kupona, labda kwa huruma tu ya Mwenyezi Mungu.”



Maneno hayo, pamoja na mengine mengi aliyoyasema daktari huyo ndiyo yaliyompa faraja Pangapangua. Ni kumbukumbu ya maneno hayo iliyomfanya Pangapangua, jioni hii, akiwa peke yake chumbani, ajikute akitabasamu kwa furaha, huku moyoni akisema, kwa kawaida mgonjwa asiyepata tiba ya kumponya, kabla ya kifo chake lazima apate nafuu. Hata kama alikuwa hafumbui macho wala kutikisika, sasa atafanya hivyo na si ajabu pia anaweza kutamka maneno mawili, matatu kama vile ni mtu asiyetarajia kufa bali kupona siku chache zijazo.



Mara akajilaza kivivuvivu katika sofa kubwa lililokuwa chumbani humo, tabasamu jepesi likiendelea kuchanua usoni. Akayatazama kwa mbali magazeti kadhaa ya Kiingereza na Kiswahili yaliyokuwa juu ya stuli. Hayo yote alishayasoma na yalikuwa na habari za ‘kumfurahisha.’



Moja lilidai: AFYA YA BABA WA TAIFA YAZIDI KUDORORA. Lingine liliandika: MADAKTARI WAMEANZA KUKATA TAMAA. La tatu: MWALIMU HAFUMBUI MACHO. La nne likaupamba ukurasa wa mbele kwa maandishi makubwa: SASA MWALIMU APUMUA KWA MASHINE MAALUMU…



Kwa Pangapangua habari zote hizo zilikuwa ni ‘habari njema.’ Na kwa kuwa alikuwa peke yake chumbani humo, hakukiona kikwazo cha kumfanya asicheke, tena kucheka kwa sauti. Huenda angeonekana chizi kama angefanya hivyo hadharani, lakini kwa chumbani humo hakuona soni kuifurahisha nafsi yake kwa namna yoyote ile.



Alicheka! Tena alicheka kwa sauti, japo sauti hiyo haikuweza kupenya kuta nene na kugota sebuleni ambako mafundi wawili wa magari yake waliketi katika masofa wakimsubiri. Hakutaka kicheko chake na furaha yake iyafikie masikio yasiyohusika. Nani mwingine asikie? Na kwa nini asikie?



Kwa jumla hakuwa radhi mtu yeyote mwingine, hata mama yake mzazi akijue kinachomfanya afurahie kuugua kwa Baba wa Taifa. Hivyo, ndani ya furaha iliyoutawala moyo wake alinyoosha mkono na kulitwaa gazeti moja ambalo picha ya Baba wa Taifa iliupamba ukurasa wake wa mbele.



Kwa takriban dakika nzima akawa akiitazama picha hiyo huku akinong’ona: “Hata kama una nafuu, humalizi mwaka.”



Akacheka tena, safari hii kwa sauti ya chini zaidi. Alikuwa na sababu ya kufurahia maradhi yaliyomkumba Baba wa Taifa. Sababu moja tu; kumbukumbu ya adha zilizompata baba yake mzazi, marehemu mzee Kipipa Mtakayote wakati wa Operesheni Dhidi ya Wahujumu Uchumi na Walanguzi mwaka 1983.



Katika operesheni ile, ni Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ndiye aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, madaraka ambayo aliyavua kwa hiari yake mnamo mwaka 1985.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Japo kuanzia mwishoni mwa mwaka 1985 ni Ali Hassan Mwinyi ndiye aliyekuwa rais wa pili wa jamhuri, hata hivyo, bado heshima ya Mwalimu Nyerere ilikuwa juu zaidi. Akilini mwa Pangapangua hilo halikuwa na ubishi; simulizi za baba yake hazikuwa zimemtoka katika kumbukumbu zake.



Ndiyo, Nyerere aliheshimika sana hivyo ulipotokea utata wowote, katika suala lolote, uongozi wa juu wa chama tawala na serikali haukusita kumshirikisha. Na japo mwaka 1987 aliivua kofia ya uenyekiti wa chama tawala, bado aliendelea kushiriki katika masuala mbalimbali ya kichama na kiserikali, mapendekezo yake katika jambo moja au lingine yakipewa uzito mkubwa katika utekelezaji.







ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog