Search This Blog

Saturday 5 November 2022

ROHO NYEUSI - 5

 







    Simulizi : Roho Nyeusi

    Sehemu Ya Tano (5)





    Alikumbuka jinsi Baba wa Taifa alivyozunguka katika mikoa kadhaa nchini akimpigia debe mgombea pekee wa chama tawala katika kiti cha urais mwaka 1995 wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi.



    Ni hilo lililomtisha Pangapangua. Akilini mwake alimchukulia Baba wa Taifa kama kikwazo cha maendeleo yake. Alimwona kuwa ni mtu anayeendelea kuiongoza nchi kwa remote control toka Butiama. Hivyo, kama atasema fulani ataifishwe mali zake, kiongozi aliyekaa ikulu atatekeleza mara moja.



    Kwa jumla, Pangapangua hakupenda nafuu ya Baba wa Taifa iendelee kushamiri na hatimaye maradhi hayo kutoweka. Na ile siku ambayo serikali ilitoa tamko rasmi kuwa Baba wa Taifa kafariki dunia, Pangapangua, tofauti na mamilioni ya Watanzania walioshtushwa na kusononeshwa na taarifa hiyo, yeye alijifungia chumbani ambako alifungua chupa ya whisky na kujaza glasi kisha akanywa kwa takriban nusu saa, usoni akitabasamu, moyoni akifarijika!



    ************



    “KAMWITE Maselina,” mama yake Pangapangua alimwambia Jacob.



    Ilikuwa ni saa 9 alasiri, muda mfupi baada ya mama huyo kumaliza kula. Akiwa ameketi sebuleni, chupa ya soda mbele yake, aliamua kuongea na Maselina kile alichoagizwa na mwanaye, Pangapangua.

    Jacob alikwenda hadi jikoni na kuufikisha ujumbe huo kwa Maselina.



    “Kuna nini?” Maselina alimkazia macho Jacob.



    “S’jui. Yeye kan’ambia nikuite.”



    “Yuko wapi?”





    *******************



    TULIPOKOMEA KATIKA TOLEO LILILOPITA...



    Alisoma kitu fulani katika macho yao. Udadisi. Macho ya kila mmoja yalitazama kwa namna ya kuhoji maswali mengi yaliyohitaji majibu ya haraka. Ndiyo, hilo lilikuwa bayana machoni mwa Ayatollah Matto. Tabasamu jepesi likamtoka, likifuatiwa na kikohozi kingine kikavu.



    Kisha: “Nisiwacheleweshe. Kwa kifupi, tunahitaji kuwa na mbunge. Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza rasmi kuwa Mkwajuni ni jimbo jipya. Sisi pia ni miongoni mwa wakaazi wa jimbo hili jipya. Na ni ukweli usiopingika kuwa sisi ndio watu wenye majina makubwa hapa Mkwajuni, majina makubwa yanayotokana na nguvu zetu za kiuchumi.” Kufikia hapo tabasamu lake likachanua zaidi.



    *****SASA ENDELEA*****



    “NILICHOWAITIA ni kuwatajia mtu ambaye mimi binafsi, baada ya kutafakari kwa muda nimeona kuwa atatufaa katika uwakilishi bungeni.”



    Mzee Kambi, mmoja wa waalikwa aligonga meza na kunyoosha mkono juu.



    “Ndiyo, mzee Kambi, unasemaje?” Ayatollah Matto alimuuliza.



    Huku akiwa na glasi ya kinywaji mkononi, mzee Kambi alisimama na kusema, “Samahani mwenyekiti. Naomba usizungukezunguke. Muda umeshakwenda sana. Samahani sana.”

    Akaketi.



    Baadhi ya waalikwa wakamuunga mkono kwa makofi machache, baadhi waliachia vicheko vya chinichini.



    “Sawa, mzee,” Ayatollah alisema huku akijiweka sawa kitini. “Kijana wetu aliyefunga ndoa leo ndiye anayetarajia kuingia kwenye kinyang’anyiro cha ubunge.”



    “Huyu bwana harusi wetu?” mzee mwingine alihoji.



    “Ndiyo, ni huyuhuyu!” Ayatollah Matto alisisitiza. “Ni huyuhuyu Pangapangua!”



    Miguno michache ikazuka na kuyeyuka ghafla.



    “Ni kijana ambaye naamini kuwa anaweza kutuwakilisha vizuri bungeni,” Ayatollah aliongeza.



    Mkono mwingine ulinyooka juu.



    “Ndiyo, mzee Simba,” Ayatollah aliruhusu.



    Mzee Simba alisimama kwa madaha, naye akiwa na glasi ya bia mkononi. Akarekebisha tai shingoni kisha akakohoa kidogo. Akaangaza macho kwa wajumbe wote, mmoja baaada ya mwingine kisha akasema, “Sina hakika kuwa ni mtu wa rika gani anayestahili kuwa mbunge,” mzee Simba alisema. “Lakini takwimu zinaonyesha kuwa kwa miaka mingi wabunge wetu huwa ni wale waliokwishakuwa watu wazima, watu wenye umri wa kuanzia miaka arobaini na kuendelea. Huyu kijana, kwa mtazamo wangu, ni mwenye umri wa kati ya miaka ishirini na mitano na thelathini na mitano. Bado kijana sana, na n’na wasiwasi juu ya ukomavu wake katika mambo ya siasa. Tafadhali tupe mwanga kuhusu hilo.”



    Ukimya ukatawala kwa sekunde kadhaa. Kisha minong’ono ya hapa na pale ikazuka, minong’ono ambayo hatimaye ilififia taratibu na kutokomea.



    Mara mzee Ayatollah akasema, “Ni kweli, wabunge wetu wengi wana umri mkubwa kama ulivyosema. Lakini pia kwa sasa wapo wengi ambao bado vijana sana. Bungeni wamo kama saba au wanane hivi vijana sana. Na hata hivyo umri siyo sheria. Tunapaswa kutambua hivyo. Mtu yeyote anayekubalika jimboni kwake anaweza kuwa mbunge.



    “Hivyo, bwana Pangapangua hana kipingamizi chochote cha kugombea ubunge. Kipingamizi kikubwa kilikuwa ni ndoa. Kingekuwa ni kichekesho cha aina yake kama angeamua kutangaza azma hiyo huku akiwa kapera. Jamii isingemwelewa, na asingekubalika. Nadhani mpaka hapo nimeeleweka. Au kuna yeyote mwenye dukuduku zaidi kuhusu hilo?”



    Ukimya mfupi ukatawala. Kisha mzee Simba, bila ya kunyanyua mkono, alisimama na kusema, “Kwa upande wangu sina kipingamizi. Lakini ni vyema tutambue kuwa mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ndiyo mwisho wa mchezo. Pamoja na hayo tutambue pia kuwa vikao vya awali vya chama huwa ama ni vikwazo vya kumfikisha mteule wetu kule tunakotaka ama ni njia nyeupe ya kufanikisha malengo yetu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Kwa hilo, tusidanganyane. Zinahitajika gharama.” Akanyamaza kidogo na kuwatupia macho wajumbe huku mkono mmoja ukikipapasa kitambi. Kisha akaendelea: “Kijana wetu ana elimu ya kutosha, na ana mvuto machoni mwa watu. Akilini mwangu bado sijampata mtu wa kuweza kumwangusha katika kura za maoni. Bado. Lakini ni vyema pia tukikumbuka kuwa dunia ya leo ni dunia ya pesa. Pesa kwanza, haki baadaye. Hivyo, tusilichukulie suala hili kwa uzito wa kawaida, tukiamini tu kwamba kwa kutumia vinywa vyetu katika kukampeni, mgombea wetu atapita. Hapana. Kama ni’vyosema awali, gharama zitahitajika. Na hilo, bwa’mdogo anapaswa kulijua, ikibidi, ahusike kwa asilimia tisini.”



    Yalikuwa ni maneno mazito vichwani mwa wajumbe wenzake. Na wote waliafikiana naye. Zaidi, mzee Kisauti, ambaye aliwahi kujizolea umaarufu mkubwa miaka kadhaa iliyopita, wakati akiwa ni mbunge wa jimbo fulani, aliahidi kuonana na baadhi ya vigogo wa chama tawala ili kuhakikisha Pangapangua anavuka katika kikao cha kura za maoni, kikao kitakachoamua nani aingie kwenye kinyang’anyiro cha kuwania ubunge, nani awekwe kando.

    Wajumbe wengine wa kikao hicho waliahidi kuzunguka huku na kule jimboni wakimpigia debe Pangapangua kwa wananchi.



    ************



    ZILIPITA wiki tatu baada ya kikao hicho cha siri. Tayari Pangapangua alishadokezwa kuwa mambo yalikuwa yakienda vizuri. Dalili za mafanikio zilishajitokeza.



    “Umeonyesha kukubalika kwa watu wengi,” Deker Manji, mzee mwenye asili ya Kiasia, ambaye alikuwa miongoni mwa waliopewa jukumu la kumnadi Pangapangua kisirisiri kwa wananchi, siku moja alimdokeza.



    “Kuna watu wawili ambao nao wanataka kujiingiza kwenye kinyang’anyiro cha ubunge,” mzee Ayatollah Matto alimwambia. “Ni mzee Sanga na Bibi Zamda. Lakini ni wepesi sana, hawatishi. Kwanza wana elimu finyu sana, na hata sio maarufu. Katika rekodi zao, hakuna chochote walichofanya kinachoonyesha kuwa wameliendeleza jimbo hili kiasi cha kukubalika kwa wananchi. Ni wepesi sana katika mizani.”



    Hizo ni baadhi tu ya taarifa zilizomfikia Pangapangua, taarifa zilizomfanya ajenge matumaini ya mafanikio ya asilimia 100. Na ni matumaini hayo yaliyomfanya usiku wa siku moja aamue kuliweka bayana suala hilo kwa mkewe, Maselina.



    Aliingia chumbani na kumkuta Maselina akiutazama mkanda wa video ulioonyesha matukio ya harusi yao. Hakumwacha aendelee kuutazama mkanda huo, alimvuta na kumlazimisha asimame, kisha akamkumbatia na kumbusu shavuni kabla ya kutamka kwa mnong’ono: “Baada ya miezi michache hutaitwa ‘mke wa Pangapangua’ bali, MKE WA MHESHIMIWA MBUNGE…”



    Maselina alijing’atua mikononi mwa Pangapangua taratibu, kisha akamtazama usoni huku akitabasamu kwa mbali. Kauli za aina hii, kutoka kinywani mwa Pangapangua hazikuwa ngeni masikioni mwake, na hata kauli hii aliichukulia kama moja ya mizaha aliyozowea kutamka.



    “Utakuwa ukitembelea shangingi la mbunge,” Pangapangua aliongeza. “Na ikiwezekana, wewe nd’o utakuwa sekretari wa mbunge,” akambusu kwa mara nyingine, safari hii ikiwa ni kwenye shavu la pili.



    “Na mbunge mwenyewe ni Pangapangua?” Maselina alirusha swali kwa mzaha.



    “Yap! Mbunge mwenyewe ni Pangapangua mtoto wa marehemu Kipipa Mtakayote! Ndiyo, kwa mara ya kwanza Songambele itakuwa na jimbo lenye mbunge kijana zaidi kuliko majimbo mengine. Na litakuwa ni jimbo lita’lopiga hatua kimaendeleo kwa kasi isiyo ya kawaida! Kasi ya kimbunga!”



    Maselina aliachia kicheko kikali kisha akasonya na kurudi kitandani ambako alijilaza na kuitwaa remote control ya televisheni, akabonyeza mahala fulani na picha ile ikawa inajirudia. Kwa jumla hakuonesha dalili yoyote ya kuyajali maneno ya Pangapangua. Aliirejesha akili kwenye mkanda.



    “Sikia, mamaa,” Pangapangua alimfuata pale kitandani. “Najua umezoea kunisikia nikitamka mizaha mingi. Suala hili silichukulii kama mzaha mwingine. Naomba ufahamu hivyo.”



    “Suala gani?” Maselina alimtazama kwa macho makali.



    “Hili nililokwambia sasa hivi.”



    “Hili la ubunge?”



    “Ndiyo,” Pangapangua alijibu kwa sauti nzito na ya chini, macho yake yakidhihirisha umakini wa kauli. Akaendelea: “Sina utani kuhusu hilo. Niko serious. Naomba uamini hivyo.”



    Maselina alikunja uso, akamtazama mumewe kwa makini. Sasa akauona uso ambao tangu amfahamu na tangu wafunge ndoa, hakubahatika kuuona. Ulikuwa ni uso mwingine, uso wenye sura isiyo hata na chembechembe za furaha au tabasamu, macho yakizidi kuwa makali kadri Maselina alivyozidi kuyatazama, yakibadilika rangi toka hii hadi ile. Kwa jumla, Pangapangua huyu alitisha machoni na akilini mwa Maselina.



    Naam, utani au mzaha wa aina yoyote ni mambo yaliyokuwa umbali wa kilometa 1,000 kutoka moyoni mwa Pangapangua. Hilo lilikuwa bayana hata akilini mwa Maselina. Na katika kupata ufafanuzi sahihi kuhusu kauli hiyo ya Pangapangua, Maselina aliamua kukaa vizuri kitandani hapo, akaizima deki ya video na papohapo, kwa sauti ya chini, yenye msisitizo mkali, akamuuliza, “Unaweza kunieleza kwa kina hayo unayosema?”



    “Sina mengi ya kukwambia,” Pangapangua alijibu huku akiyatupa macho sakafuni. “Unachopaswa kutambua ni kwamba, sikutanii. Nimedhamiria kugombea ubunge. Na n’na uhakika wa kuupata.”



    Baada ya kusema hivyo, alinyanyuka na kuvua shati, akalitundika kwenye msumari. Kisha akaanza kuvua suruali. Wakati akiendelea na zoezi hilo, mara Maselina akamtupia swali: “Kwa nini umejiingiza kwenye masuala ya siasa mapema hivyo?”



    “SIYO mapema. Ni muda mwafaka kwangu. Na kwa nini unadai ni mapema?”



    “Umri. Umri wako.”



    “Umri wangu ukoje?”



    “Bado kijana sana.”



    “Ujana siyo kigezo cha kumkosesha mtu ubunge,” Pangapangua alijibu kwa msisitizo. “Na hakuna sheria inayombana mtu anayetaka kugombea ubunge eti lazima awe na umri fulani au awe mzee. Hakuna! Tunao wabunge wengi wazee ambao kila wanapoingia kwenye vikao, kazi yao ni kuuchapa usingizi tu. Sasa tunahitaji mabadiliko, tuondoe ule usemi wa VIJANA NI TAIFA LA KESHO. Badala yake ichukuliwe kuwa VIJANA NDIYO NGUZO YA TAIFA LA LEO.”



    “Lakini…”



    “Lakini nini tena?”



    “Utaweza kutumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja?” Maselina alizidi kumkazia macho.



    “Una maana gani?”



    “N’na maana, siasa na biashara zako.”



    Kwa mara ya kwanza Pangapangua aliachia kicheko kikali. Kisha akampapasa Maselina mgongoni. “Siasa hainipi tabu, baby,” hatimaye alisema. “Siasa ni aina fulani ya usanii. Na usanii ni jadi yangu. Siwezi kushindwa kusimama jukwaani na kuwaahidi wananchi kuwa nikiwa mbunge nitawajengea barabara za lami kila mtaa. Nitawaahidi, na wataamini kwa kuwa wataona anayetoa kauli ni mtu mwenye uwezo wa kutimiza ahadi zake.



    “Isitoshe, nitawafurahisha wazazi, ambao hasa nd’o wapigakura, kwa kuwaahidi kuwaletea mabasi kwa usafiri wa wanafunzi, badala ya hali ya sasa ambapo wanafunzi wanataabika na kunyanyaswa na makondakta wa daladala. Najua wao pia wataniamini. Kwa jumla, kila nitakachoahidi watakiamini kwa kuwa wanajua pesa n’nayo!”



    Japo Pangapangua alitoa maelezo mengi, hata hivyo bado Maselina aliona kama vile anasimuliwa hadithi ya kubuni. Na hata walipozima taa na kulala, bado Pangapangua aliendelea kuzungumza. Maneno mengine Maselina hakuyasikia, alipitiwa na usingizi wakati mumewe akiendelea kuzungumza.



    ************

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    BALAA lifananalo na kansa lilianza kuonekana peupe wakati wa zoezi la kura za maoni kwa wagombea ubunge na udiwani kwa tikiti ya chama tawala. Haikuwa siri, watu wenye vipato vikubwa waliamua kutumia pesa kununua nafasi hizo kutoka kwa wale wajumbe wa vikao vya awali, wajumbe wenye kupiga kura ya kumchagua mgombea atakayekiwakilisha chama kwenye kinyang’anyiro hicho, dhidi ya wagombea wengine wa vyama vya upinzani.



    Kilikuwa ni kipindi cha patashika kubwa. Baadhi ya wagombea wa majimbo tofauti wakazua malumbano kupitia vyombo vya habari, huyu akizungumzia udhaifu wa yule, na yule akiutangaza unyonge wa huyu. Na wakati huo kila mgombea alihakikisha analisafisha jina lake kwa kutumia kila aina ya nyenzo kujiweka sawa mbele ya jamii, pesa zikiwa miongoni mwa nyenzo kuu zilizotumika.



    Kuna ambao walijitolea kukarabati barabara kadhaa ambazo awali zilikuwa zikitisha kwa mashimo yaliyozitawala. Wengine walianzisha mashirika binafsi yenye kutoa mikopo ya masharti nafuu zaidi. Wale waliokuwa na mabasi ya usafiri mjini, walishusha viwango vya nauli kwa asilimia hamsini huku wakidiriki kutowatoza wanafunzi nauli waendapo na watokapo shuleni.



    Hayo ni baadhi tu ya yaliyofanywa na wale waliodhamiria kujikita katika kinyang’anyiro cha kuwania ubunge wa jimbo jipya la Mkwajuni. Na kwa hakika takrima ilitwaa nafasi kubwa katika jimbo hilo, jimbo ambalo robo tatu ya wakazi wake walikuwa ni wale ambao huwezi kuwaweka katika kundi la waliokwishajikwamua toka kwenye minyororo ya umaskini.



    Akitambua fika kuwa alikuwa na wapinzani katika kuiwania nafasi hiyo moja ya uwakilishi wa wananchi wa jimbo hilo bungeni, Pangapangua aliamua kulivalia njuga suala hilo, akiwa tayari kutumia ‘silaha’ zote alizokuwanazo katika kufanikisha lengo lake.



    Hivyo, alitenga fungu la shilingi milioni 50 kwa ajili ya kampeni za awali. Aliamini kuwa kazi kubwa ilikuwa ni kwenye kura za maoni, zoezi litakalochuja mchele na pumba. Akivuka hapo, basi mchezo utakaokuwa mbele yake utakuwa mdogo sana. Dhiki ya maisha ya wakaazi wengi wa jimbo hilo ingekuwa sababu tosha ya kumfikisha bungeni. Angewateka wapiga kura kwa kiasi kidogo cha pesa.



    Harakati zake hazikuwa za bure. Jopo la wale washirika wake lilipita hapa na pale, likimwaga pesa kwa huyu na yule, kikundi hiki na kile, pesa zilizoyateka mawazo ya wajumbe wengi wa vikao vya chini na hivyo wakajikuta wakitoa uamuzi wasioutarajia katika kulipa fadhila ya zile takrima walizopokea.



    Yote kwa yote, hatimaye jina la Pangapangua likapitishwa. Akawa ni miongoni mwa wagombea wengine kutoka majimbo mengine yote nchini, ambao wangekutana katika kikao maalumu kilichopangwa kufanyika mjini Dodoma chini ya Mwenyekiti wa Taifa na viongozi wengine wa chama tawala ngazi ya taifa.



    Kwa Pangapangua, huo ulikuwa mwanzo mzuri. Siku ambayo jina lake lilipitishwa alifanya sherehe kubwa, akawaalika watu wengi. Ngoma zikachezwa, watu wakala, wakanywa hadi usiku wa manane. Kwa hakika furaha ililitawala eneo hilo la sherehe. Kila aliyehudhuria alionekana kujawa na furaha.



    Ndiyo, kila mmoja alifurahi, lakini, zaidi furaha ya Pangapangua ilivuka kiwango. Sasa si tu kwamba aliamini kuwa atakumbana na upinzani mdogo wa wagombea kutoka vyama vya upinzani, bali pia aliamini kuwa hakuna kitakachomzuia kuukwaa ubunge.



    Wakati wengi wa wakaazi wa Jimbo la Mkwajuni walishangilia ushindi wa awali wa Pangapangua kwa matarajio kuwa atatoa mchango mkubwa wa hali na mali katika kuliendeleza jimbo hilo, yeye alikuwa na sababu ya kufurahi.



    Alishaijua faida ya mtu kuwa mbunge. Kwamba, posho zake ni kubwa, na siyo lazima ufanye chochote cha kuliendeleza jimbo iwe kwa gharama zako binafsi au kwa gharama za serikali baada ya kupiga kelele sana vikaoni. Hata kama mbunge utakuwa mtu wa kuuchapa usingizi tu vikaoni, bado utaendelea kuwa mbunge hadi kipindi chako kitakapokwisha. Zaidi, aliamini kuwa kama hataishambulia serikali kwa udhaifu wowote utakaojitokeza, basi huenda akajikuta akiukwaa uwaziri hivihivi! Kijana kama yeye kuupata ubunge halafu kabla uzee haujapiga hodi anaupata uwaziri! Ni raha iliyoje?



    Aliwaza hayo kwa furaha usiku huo wa sherehe wakati akiwa chumbani, kitandani, mkewe akiwa kando yake, akimtazama huku tabasamu jepesi likichanua usoni pake.



    “Hayawihayawi, yamekuwa mume wangu,” Maselina alimwambia huku akimsogelea na kumkumbatia kisha akambusu kinywani, busu lililodumu kwa takriban dakika nzima.



    Hatimaye wakatazamana tena, macho ya Maselina yakionesha kutoa pongezi, zaidi ya pongezi za matamshi ya kinywani. Ampongeze kivitendo, akitumia kiwiliwili chake kwa namna ambayo aliamini kuwa Pangapangua angefurahi, angeburudika na angeridhika.



    Naam, yalikuwa ni macho yaliyomvutia Pangapangua sanjari na kupata msisimko wa ajabu kutokana na mikono ya Maselina kukosa adabu kwa kuteleza hadi kwenye ‘migodi ya dhahabu.’ Kwa usiku huo akamwona Maselina kama mwanamke wa kipekee; mrembo hadharani, hodari sana jikoni na mtundu zaidi faraghani.

    Na kwa mara ya kwanza akamwona Maselina kama mwanamke jasiri, mwenye kustahili kuwa mke wa MHESHIMIWA MBUNGE.



    “Nimekubali,” Maselina aliongeza. “Huo ni mwanzo mzuri. Naamini ubunge utaupata. Sikioni cha kukuzuia hata katika kikao cha Dodoma. Mungu atakuwa pamoja nawe siku ya kikao na jua litakapotokomea, jina lako litakuwa limepitishwa.”



    Wakatazamana tena. Pangapangua akajawa na nguvu. Maneno haya ya mkewe yalimpa nguvu ya kusimama jukwaani na kujieleza mbele ya halaiki na pia kuwa na matumaini ya kushinda kwenye uchaguzi.



    Tabasamu zito likiutawala uso wake, Pangapangua alimvuta Maselina na kumbusu kinywani, kisha akiwa hajajiandaa kutamka lolote, kwa sauti nzito, sauti ya chini, alipata maneno mawili tu kinywani mwake: “Asante, mpenzi.” Kisha akanyoosha mkono katika swichi iliyokuwa jirani na kitanda, akazima taa.



    Ukawa ni usiku mwingine mzuri kwao.



    ************



    NI usiku huohuo ambao kwa Maselina na mumewe, Pangapangua ulikuwa ni mzuri kupindukia, katika chumba fulani katikati ya Jiji la Dar es Salaam kulikuwa na watu ambao hawakuwa na dalili yoyote ya kuipumzisha miili yao wala akili zao.



    Ndani ya chumba hicho kilichokuwa katika jengo fulani lililomilikiwa na Shirika la Nyumba la Taifa, kulikuwa na watu watano, wanaume, ambao kwa zaidi ya saa mbili walikuwa wakijadiliana kuhusu jambo muhimu lililojitokeza katika kipindi hicho kilichokuwa kikielekea katika Uchaguzi Mkuu uliotarajiwa kufanyika miezi michache baadaye.









    JENGO hilo la ghorofa tatu, lilikuwa ni miongoni mwa yale majengo aliyochakaa, ambayo zaidi ya kuwa ni kati ya majengo yaliyolishushia hadhi jiji hilo, pia yalikuwa ni uchafu, zaidi ya uchafu uliozolewa kila siku na kampuni zilizopewa zabuni ya kulisafisha jiji. Na kilichodhihirisha zaidi kuwa ni uchafu ni kwa kuwa lilipakana na majengo mengine mawili; moja la ghorofa kumi na lingine la ghorofa kumi na mbili yakiwa katika ubora wake, yakipendeza kwa kiwango cha kufanya yatazamwe na kila jicho.



    Katika eneo la chini la jengo hili chakavu, kulikuwa na maduka matatu ya Watanzania wenye asili ya Kiasia huku ghorofa ya kwanza na ya pili zikitumiwa na wafanyabiashara hao kwa makazi. Ghorofa ya tatu ambayo kama ghorofa mbili za awali ilikuwa na vyumba vinne, ndipo kulikokuwa na chumba hiki maalumu, ambacho walikitumia kwa vikao maalumu. Vyumba vitatu vilivyosalia havikuwa na wapangaji na inasemekana Shirika la Nyumba la Taifa lilishinikizwa kutompangisha mtu yeyote katika vyumba hivyo. Ilikuwa ni amri, amri toka ‘juu.’



    Mtu mmoja, mfupi na mwenye mwili mkubwa, kichwa chake kikiwa na upara uliomeremeta, ndiye aliyeketi nyuma ya meza kubwa, meza iliyotandikwa kitambaa chenye rangi za bluu, nyeusi, njano na kijani huku globu ya umeme ikishusha mwanga mkali mezani hapo. Mbele yake, meza mbili ndefu zilikuwa zimetazamana huku watu wawili wakiwa katika meza moja na wengine wawili, meza nyingine.



    Ilikwishatimu saa saba usiku na walikuwa hawajakimaliza kikao chao muhimu. Kwa takriban dakika ishirini zilizopita, yule mtu mfupi alikuwa akizungumzia athari zilizojitokeza ndani ya chama tawala katika harakati za kinyang’anyiro cha ubunge zilizoendelea kote nchini.



    “Inashangaza sana,” aliendelea kusema, usowe ukiwa na mikunjo ya ghadhabu. “Sijawahi kushuhudia mchezo mchafu wa aina hii. Uchaguzi wa mwaka huu umekuwa na mambo ya ajabu sana. Yaani watu wameamua kutumia pesa ili wapitishwe kwenye mchujo na Halmashauri Kuu! Tanzania inakwenda wapi? Nchi wahisani zitatuelewa vipi kama tutalifumbia macho suala hili?”



    Akatulia kidogo na kuchukua karatasi moja kati ya nyingi zilizokuwa mezani hapo. Akampa mmoja wa wale wanne huku akisema, “Hii nd’o taarifa ya Tume ya Uchunguzi. Tazameni idadi ya watu ambao tayari wameshatumia mamilioni ya shilingi ili waweze kuingia bungeni. Huu ni mtikisiko mkubwa katika nyanja ya kisiasa. Taifa linakuwa na siasa za aina hii?! Tazameni!”



    Karatasi hiyo iliyokuwa na majina kumi na matano ya watu waliokuwa wakiwania nafasi za ubunge, ilimfikia kila mmojawao. Na kila mmoja alitoa mguno wa mshangao baada ya kuisoma. Kumi kati ya waliokuwa katika orodha hiyo ni wabunge waliokuwa wakiwania nafasi hiyo kwa mara nyingine. Watano walikuwa wapya na wawili kati ya hao watano walikuwa ni vijana wenye utajiri uliodhihirika machoni mwa watu.



    Mtu huyo mfupi ambaye kwa namna yoyote alionekana ndiye mwenyekiti wa kikao hicho, alisubiri karatasi hiyo izunguke kwa kila mmoja wa wajumbe wake, kisha akaendelea: “Nadhani mmejionea wenyewe. Hii siyo hali ya kawaida! Na haivumiliki! Hatuwezi kuacha uozo huu uendelee kufukuta ndani ya chama. Haiwezekani! Haiwezekani! Nasema haiwezekani! Hatuwezi kukiangalia hivi tu chama kikipakwa matope na wajinga wachache wenye uroho wa fisi. Hatuwezi! Hali hii inaweza kuzua mtikisiko mkubwa ndani ya chama.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Na, nadhani mtikisiko wenyewe umeshaanza. Mtikisiko huo utazua nyufa kadhaa na hivyo kuhatarisha uimara wa taifa letu lenye sifa ya amani na utulivu. Nikiwa ni mwenyekiti wa taifa, sitakubali mambo yaendelee kuwa hivi...”



    Akasita kidogo na kuwatupia macho wajumbe, mmoja baada ya mwingine. Kisha, kwa sauti isiyokuwa na msisitizo mkali, alisema, “Lakini, basi. Sina la kusema zaidi. Tuachie hapa kwa leo. Mambo yote yataishia Dodoma. Asanteni sana.”



    Mara baada ya kutamka hivyo, alinyanyuka na kutoka hima, akapita katika mlango wa siri uliokuwa nyuma ya meza yake, akatokomea.



    Wajumbe wakabaki wakinong’ona:



    “Mzee kachukia!” mmoja alisema.



    “Ni lazima achukie,” mwingine akadakia.



    “Mwaka huu moto utawaka Dodoma,” wa tatu alisema.



    “Vyovyote itakavyokuwa, ni lazima haki itendeke kwa masilahi ya taifa,” wa nne alisema kwa msisitizo.



    Waliendelea kuchangia hoja hiyo kwa uhuru zaidi, mara chache wakibishana na kutaniana.



    Baada ya nusu saa chumba hicho kilikuwa tupu huku ngurumo za magari yanayoondoka zikisikika chini ya jengo hilo, kila mjumbe akitokomea.



    ************



    UPANDE mwingine, harakati za Pangapangua ziliendelea kama kawaida. Zilipobaki siku chache kabla ya kikao cha Dodoma, mzee Kisauti ambaye ndiye aliyekuwa kinara wa kampeni za Pangapangua aliitisha kikao kilichowahusu wao wawili tu.



    “Utapita! Nakuapia utapita tu!” mzee huyo alimwambia. “Huna rekodi chafu zinazoweza kukukosesha nafasi hiyo. Isitoshe, kuna watu wawili, watatu wanaojua kushinikiza nani apite, nani atupwe. Hao watakuwamo kikaoni. Tayari ni’shawaona. Ni watu wanaoheshimika, wanaotukuzwa na kuogopwa. Kila mmojawao ana uwezo wa kulikingia kifua jina lako. Lakini kama unavyojua, uzito unahitajika ili kuwapa nguvu jamaa hao. Nadhani umenielewa.”



    Isingekuwa vigumu kwa Pangapangua kuelewa. Rushwa ilishasambaa katika mishipa ya damu yake. Alishajenga imani kuwa jambo lolote lenye manufaa hupatikana au hufanikishwa kwa gharama za ziada, gharama zinazohusisha mikataba ya siri sana na aghalabu mikataba hiyo huwa siyo ya maandishi.



    “Hilo s’o tatizo, mzee wangu,” Pangapangua alijibu. “Katika hatua tuliyokwishafika, sipendi kiharibike kitu. Zungumza tu; ni kiasi gani kinahitajika?”



    “Fanya hamsini kama kuna uwezekano.”



    “Hamsini. Yaani milioni hamsini, sio?”



    “Yeah. Kitakuwa kiwango cha kutosha kwa wale makada wawili wenye nguvu na misimamo thabiti.”



    Pangapangua alikunja uso kidogo, akimtazama mzee Kisauti kwa makini. Kisha akauliza, “Hakutakuwa na wajumbe wengine wa NEC ambao watazua vijiswali vingi visivyo na maana lakini vinavyoweza kutuharibia malengo yetu?”



    Mzee Kisauti aliachia tabasamu hafifu. “Kwa kawaida watu wa aina hiyo hawakosekani,” alisema kwa kujiamini. “Watakuwamo. Lakini hilo lisikutishe, kijana. Watazimwa na makada hao niliokwambia. Hofu yangu ni kwa hao makada wenye mdomo sana. Maana’ake hata bungeni hawashikiki, wakiamua kulivalia njuga jambo fulani, waziri anakiona cha moto. Tukiwaweka mfukoni wale, ujue ndio watakaolishikia bango suala la kuhakikisha unapenya! Wanazijua fitina hao! Siku hiyo ya kikao kutapambazuka lakini jua litakapotokomea mambo yako yatakuwa supa.”



    Pangapangua aliujua uzito wa kikao kile cha Dodoma, hivyo, baada ya kujumlisha moja na moja na kupata mbili, hakusita kumpatia mzee Kisauti kiasi hicho cha pesa.



    Wakati akipokea pesa hizo, tabasamu jepesi likichanua usoni, akasema, “Ubunge ni wako. Japo una umri mdogo tofauti na wengine wanaowania nafasi hiyo, lakini wewe ni mtu unayekubalika jimboni hapa. Una elimu kubwa, na ni Mtanzania halisi. Isitoshe, umaarufu wa marehemu baba yako umekujengea jina hata wewe. Serikali imeshautambua mchango wako katika masuala mbalimbali ya kijamii. Kwa ufupi, huna haja ya kuwa na shaka yoyote; ubunge wa Jimbo la Mkwajuni ni wako.”



    Akashusha pumzi ndefu na kumeza funda la mate. Kisha akaongeza, “Kesho n’taondoka. Nitakwenda Dodoma kuwahi kutengeneza mambo. Kwa muda wa siku mbili naamini mambo yote yatakuwa safi; nitakuwa nimesharekebisha kila kitu na wahusika muhimu.”



    “Safi,” Pangapangua aliitika. “Nakutegemea kwa kila kitu, mzee. Kama kutahitajika chochote zaidi, usisite kun’taarifu. Sitaki kiharibike kitu.”



    “Hakuna kitakachoharibika, kijana,” Mzee Kisauti alisema kwa kujiamini. “Fitina za kisiasa nazijua kijana wangu. Uwe na matumaini kijana.”



    Baada ya kutamka hayo, mzee Kisauti aliutwaa mkoba wake ambao ulikuwa ni nadra kutembea nao, akaufungua na kuzitumbukiza zile pesa kisha akanyanyuka na kuanza kutoka. Akavuta hatua mbili na kugeuka. “Tuombe Mungu,” alisema kisha akaugeukia tena mlango na kuondoka.









    BASI kubwa lililosheheni abiria 65 lilikuwa katika mwendo wa kasi katika Barabara ya Dodoma iliyotandazwa lami maridadi. Baadhi ya abiria walizungumza kwa furaha, baadhi wakiwa kimya na baadhi wakiwa wametopea usingizini.



    Mzee Kisauti alikuwa mmoja wa abiria hao. Yeye, kama baadhi ya abiria wengine, alikuwa kimya akiangaza macho nje kupitia dirishani. Kwa ujumla, japo kiwiliwili chake kilikuwa humo garini, lakini mawazo yake yalikuwa mbali, kiasi cha kilometa 120 mbele. Alifikiria kilichompeleka huko Dodoma. Akacheka kimoyomoyo, kicheko cha huzuni, pindi alipoyatafakari majukumu aliyonayo pale atakapokutana na wajumbe fulani wa Halmashauri Kuu ya chama tawala.



    Kazi iliyompeleka huko haikuwa ndogo kama ambavyo mtu yeyote angefikiria. Ilikuwa ni kazi ngumu, tena ngumu sana kwa kuzingatia kuwa ingewahusisha watu wachache sana lakini wenye akili timamu, watu waliokomaa kisiasa na ambao hawakuwa wepesi kurubunika kwa kutumia pesa. Ilikuwa ni kazi ya kuwashawishi wajumbe kulipitisha jina la Pangapangua, mgombea wa kiti cha ubunge, Jimbo la Mkwajuni.



    Kama ndoto alihisi mtu kamsimamia kando huku akimsuta: “Wewe! Hata wewe mzee Kisauti unadiriki kuiuza nchi yako? Hata wewe uliyekuwa kiongozi bora leo unafikia hatua ya kushiriki katika mpango huu mchafu?”



    Akasonya kwa uchungu. Sasa akajisikia kujiwa na nguvu fulani ya ujasiri; aitetee haki bila ya woga. Ayalinde masilahi ya chama bila ya kusita. Papohapo kumbukumbu ya maneno aliyoyatamka Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, ikamjia kichwani.



    “…Ikulu! Ikulu kuna biashara gani…Ikulu…”

    Ni katika hotuba hiyo, Mwalimu aligusia juu ya watu waliokuwa radhi kutumia pesa ili tu waingie Ikulu. Akizungumza kwa uchungu mkubwa, Mwalimu Nyerere alisema kuwa yeye alikaa Ikulu kwa zaidi ya miaka 25, na akagundua kuwa ni sehemu yenye matatizo makubwa. Sasa akashangaa kuona watu wanahangaika kupakimbilia Ikulu.



    Mzee Kisauti aliyatafakari maneno hayo, akayalinganisha na utaratibu huu wa wagombea wengi wa ubunge, wagombea ambao baadhi walishatumia mamilioni ya shilingi katika kuhakikisha wanapita katika kura za maoni za vikao vya awali na bado wanadhamiria kutumia kiasi chochote cha pesa kulingana na uwezo ili tu waukwae ubunge.



    “Haiwezekani!” alijikuta akifoka kwa mnong’ono ulioyafikia masikio ya abiria mwenzake waliyeketi pamoja.



    “Unasemaje?” abiria huyo, mwanamke mwenye umri uliokaribia miaka 40, alimuuliza huku akimtazama kwa mshangao.



    Mzee Kisauti aliguna huku kauinamisha uso. Alihisi kuingiwa na soni. Lakini hakutaka mshangao uendelee kumtawala mwanamke huyo, hivyo alijitutumua na kutabasamu kidogo kisha akasema, “Us’jali, nadhani nimepitiwa kidogo.”



    Yule mwanamke ambaye bado alikuwa akimtazama, sasa naye alitabasamu kidogo. “Au unaota?” hatimaye alimuuliza.



    “Inawezekana,” Mzee Kisauti aliongopa. “Unajua tena, kausingizi kalinipitia ghafla.”



    “Lakini,” mwanamke yule aliendelea, “pamoja na hayo inaonekana una mawazo mengi!”



    “Mimi ni binadamu kama binadamu yeyote mwingine mwenye akili timamu,” Mzee Kisauti alijibu huku akiyaepuka macho ya mwanamke huyo. Akaongeza, “Na binadamu yeyote mwenye akili timamu lazima awe na mawazo. Mimi pia niko hivyo.”



    “Lakini unaonekana kama umekerwa na jambo f’lani,” mwanmke huyo aliendeleza udadisi wake. “Hali uliyonayo sio ya kawaida kwa binadamu wa kawaida.”



    Mzee Kisauti alihitaji utulivu. Haya maswali ya huyu abiria mwenzake kwa kiasi fulani yalikuwa ni kero nyingine kwake.



    Alitamani kumuuliza, ‘kero yoyote inayonisumbua unaweza kuitatua?’



    Hakufanya hivyo, badala yake aliunyanyua usowe na kumtazama mwanamke huyo kisha akasema, “Uko sahihi. Siwezi kukubali nchi yangu ichukuliwe na majambazi. Siko tayari! Hapana! Sitakubali nchi nyangu iuzwe!”

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Una maana gani?” mama yule alimganda, sasa akimkodolea zaidi macho.



    Mzee Kisauti alishusha pumzi ndefu, akaegemea kiti na kufumba macho kwa sekunde chache. Alipoyafumbua, alimtazama mwanamke yule kwa macho ya upole. Kisha kwa upole vilevile akasema, “Huwezi kunielewa. Itanilazimu kutumia robo au nusu saa kukufanya ukielewe nikisemacho. Kwa bahati mbaya sina nafasi hiyo. Tuyaache kama yalivyo.”



    Mwanamke yule aliendelea kumtazama mzee Kisauti kwa takriban dakika nzima bila ya kutamka chochote. Kisha akajiegemeza kitini na kuyapeleka macho nje. Kwake, maneno hayo ya mzee Kisauti yalikuwa mazito na yaliyomshinikiza asitishe maswali yake. Hakutaka shari, hivyo aliitii kauli aliyoambiwa. Kuanzia wakati huo, hadi mwisho wa safari hawakuzungumza chochote.



    ***************



    MJINI Dodoma mzee Kisauti alikuwa na akili nyingine tofauti na alivyomuaga Pangapangua. Akiwa ni mtu aliyefahamiana na wajumbe wengi waliofika mjini humo kwa ajili ya kikao maalumu, aliamua kuitumia nafasi hiyo kuwapiga vita vya waziwazi wagombea ubunge wote walioshukiwa kutumia pesa ili kupitishwa na wajumbe kwenye kikao cha kura za maoni.



    Kitu kimoja kilimsumbua kichwani; kwa nini mtu ahangaike kutumia pesa nyingi kwa kuwahonga wapigakura ili apate ubunge? Kwa nini? Ni kweli ana uchungu mkubwa na jimbo lake kiasi cha kuwa radhi kumwaga pesa ili achaguliwe?



    Kama ni mfanyabiashara maarufu kwa mfano, anatupa mamilioni ya shilingi kwa wajumbe wa kamati husika na kwa wananchi ili apate ubunge, je, ina maana yuko radhi hata kuiteteresha biashara yake anayoitegemea, iliyompatia umaarufu huo mradi tu awe mbunge?



    Je, atakapoukwaa ubunge huo ataitunza vipi familia yake ilhali wakati huo huenda akawa hohehahe wa kutupa?



    Akavuta kumbukumbu kichwani na kujaribu kujiuliza ni kwa nini watu fulani wanne, wafanyabiashara maarufu wa baadhi ya mikoa

    wameamua kujitosa kwenye kinyang’anyiro hicho ilhali siku zilizopita walikuwa wakiuponda waziwazi uongozi wa serikali iliyokuwa madarakani hususan chama tawala.



    Mbona sasa wanaonekana kukipenda sana chama? Wanakipenda kweli au ni unafiki mtupu? Yule mmoja aliwahi kudiriki kuropoka kwenye vyombo mbalimbali vya habari kuwa hata atishwe kwa bastola asingeweza kujiunga na chama tawala. Mwingine alikuwa tayari kukisaidia chama fulani cha upinzani kwa hali na mali ili kitwae viti vingi bungeni na ikibidi, kiweze kutoa mgombea urais atakayekubalika zaidi kwa wananchi.



    Leo, watu haohao wanazitangaza sera za chama tawala kwa nguvu zote, wakikipigia debe kama hawana akili nzuri!



    Ni wanafiki, wana lao jambo, alijisemea kimoyomoyo.



    Hakusita kuziweka hisia zake hizo bayana kwa wajumbe wachache aliowafahamu kiundani na aliowaamini. Na hao pia hawakuwa tofauti na yeye kifikra. Walishangazwa na kukerwa na hali ya rushwa ilivyoshamiri miongoni mwa wabunge sanjari na utitiri wa matajiri kujikita katika kuwania ubunge.



    “Watanzania tusipokuwa makini, tunaweza kujikuta tumeiuza nchi kwa matajiri bila hata ya sisi wenyewe kujua,” Mzee Kisauti aliwaambia wajumbe hao. Akaongeza: “Nyie mnaoingia mkutanoni muwe makini kuhusu uteuzi wa wagombea.”



    Hadi Mzee Kisauti anahitimisha maongezi na wajumbe hao ilikwishatimu saa 5 usiku. Akaenda kulala huku moyoni mwake akiwa na matumaini ya matokeo mazuri katika kikao cha Halmashauri Kuu ya chama tawala, kikao kilichotarajiwa kufanyika kesho yake.



    ***************



    ILIKUWA ni siku ya Jumamosi, Agosti 12, mwaka 2000 ulipofanyika mkutano maalum wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama tawala mjini Dodoma. Mwenyekiti wa chama hicho, ambaye pia ndiye aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin William Mkapa alikifungua kikao hicho kwa hotuba iliyopenya hadi mifupani mwa kila mjumbe aliyehudhuria.



    *Mwanzoni tu mwa hotuba hiyo, mwenyekiti huyo hakuacha kuvitaja vigezo muhimu vya kiongozi bora, vigezo alivyotamka bayana kuwa ni miongoni mwa urithi alioachiwa na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Hilo likawa ni kombora zito kwa baadhi ya wajumbe, wale ambao kwa namna moja au nyingine hawakuafikiana na sera za Mwalimu Nyerere enzi za uongozi wake.



    Mwenyekiti aliendelea kutoa hotuba, akizungumza kwa makini katika kuhakikisha kuwa hakuna mjumbe atakayetoka kapa. Hakusita kutamka kuwa wagombea ubunge watakaoteuliwa siku hiyo, kazi yao, kupitia Bunge na Baraza la Wawakilishi itakuwa ni kuhamasisha, kuongoza na kudhibiti utekelezaji wa ilani ya chama.



    Akaongeza: “KWA KILA MTU TUNAYEMPITISHA, TUJIRIDHISHE KUWA, KWANZA ANACHAGULIKA NA PILI TUWE NA UHAKIKA NA UWEZO WAKE WA KUTETEA HISTORIA YETU, MAADILI YETU NA MISINGI YETU YA UHURU, HESHIMA HAKI NA USAWA.”



    Haikuwa siri, baadhi ya wajumbe walitiririkwa jasho jembamba, wakaona taa nyekundu ikiwaka mbele yao.



    “KWA MAANA NYINGINE,” Mwenyekiti aliendelea, “LAZIMA TUWE NA UHAKIKA KUWA TUNAYEMTEUA NI MWENZETU, SI KWA MAANA POTOFU YA KULINDANA PASIPOSTAHILI, BALI KWA VILE REKODI YAKE NDANI YA CHAMA NA NDANI YA JAMII, INATHIBITISHA KUWA NI MWENZETU KIITIKADI, KIMAADILI NA KWA MALENGO YETU.”



    Kufikia hapo mjumbe mmoja alimtazama mwingine. Wakagonganisha macho, wakatabasamu. Wote waliyafurahia matamshi hayo ya mwenyekiti wao. Kisha walinong’ona kidogo, minong’ono ya kumpongeza mwenyekiti wao.



    Mkapa aliwasisimua zaidi wajumbe wengi na labda kuwakwaza wachache pale alipodiriki kusema, “TUWE NA UHAKIKA PIA KUWA MALENGO YAKE KATIKA KUOMBA UONGOZI YANASHABIHIANA NA MALENGO YA CHAMA, KWA MASILAHI YA WANANCHI WOTE, NA SI KWA MASILAHI YAKE BINAFSI, AU MASILAHI YA JAMII YAKE, AU MASILAHI YA KIKUNDI FULANI CHA WATU.



    “NI WAZI KURA ZA MAONI SAFARI HII ZIMEZUA MANENO MENGI, SHUTUMA NYINGI NA TUHUMA NYINGI. KUBWA KATIKA TUHUMA HIZO NI MATUMIZI YA RUSHWA KWA LENGO LA KUNUNUA KURA, NA WIMBI LA MATAJIRI WANAOIBUKA TU NA KUTAKA UBUNGE AU UWAKILISHI, NA KWA KUTUMIA FEDHA ZAO KWA LENGO LA KUKIMILIKI CHAMA.”



    Mjumbe mmoja alimtazama mwingine, uso ukiwa umekunjamana. Kuna wajumbe waliotazamana huku wakitabasamu, tabasamu la ushindi. Labda kila mmoja alihitaji kumwambia mwenzake jinsi alivyofurahishwa na matamshi ya mwenyekiti. Wengine walitazamana huku nyuso zao zikiwa zimekunjamana. Hao, huenda walikerwa na maneno hayo, lakini kwa kukiheshimu kikao, wakaishia kununa na wengine wakikenua meno kwa furaha bila ya kutamka lolote. Wakayarejesha macho na masikio kwa mwenyekiti.



    “…HATUWEZI KUKUBALI CHAMA KINUNULIWE NA MTU AU KUNDI LA WATU KWA KIBURI CHA FEDHA ZAO…” ni maneno yaliyomtoka mwenyekiti huyo muda mfupi baada ya kutamka yale yaliyowafurahisha na kuwakera baadhi ya wajumbe wa mkutano huo. Hii pia ilikuwa ni kauli iliyopenya moja kwa moja kwa wajumbe, mioyoni mwao, hadi mifupani, ikawakuna vilivyo!



    Bila woga wala aibu, mwenyekiti, kwa ujasiri, aligusia kuwa chama hakiko tayari kumilikiwa na wachache na kwenda kinyume kabisa na roho na uhai wa kile wanachokijua Watanzania. “HAKUNA TAJIRI AU MNYONGE ANAYEWEZA KUDAI ANA HATIMILIKI YA CHAMA. MWAMUZI SI MTU, MWAMUZI NI REKODI YAKE,” aliongeza.



    “REKODI HIYO,” aliendelea, “NI KUHUSU JINSI ALIVYOUPATA UTAJIRI WAKE. JE, NI UTAJIRI UNAOZOELEKA, ULIOPATIKANA KWA NJIA HALALI, AU LA. MAANA KATIKA NCHI YETU UTAJIRI HAUMNYIMI MTU SIFA YA KUWA KIONGOZI BORA. LAKINI LAZIMA UWE NI UTAJIRI ULIOPATIKANA KWA NJIA ZA HALALI, SI UTAJIRI UNAOTOKANA NA WIZI, UBADHIRIFU WA MALI YA UMMA, DHULUMA, KUKWEPA KODI, BIASHARA HARAMU NA KADHALIKA.”



    Mwenyekiti aliendelea kuzungumza, akiifafanua kwa kina kila kauli aliyoitoa. Na hadi alipohitimisha hotuba yake, asilimia kubwa walilielewa jukumu lililokuwa mbele yao katika mkutano huo maalumu.



    ***************



    UTEUZI uliofanywa na Halmashauri Kuu ya chama tawala mjini Dodoma uliwashtua wengi. Baadhi ya wagombea ubunge walioshinda katika kura za maoni za majimboni walienguliwa katika mkutano huo maalumu. Ulikuwa ni uteuzi ambao haukujali umaarufu wa mtu wala wadhifa wake serikalini. Pia haukujali jinsia wala rangi ya mtu.



    Baadhi ya walioenguliwa walifadhaika kwa kiasi kikubwa. Hawakutarajia kuipoteza nafasi hiyo muhimu. Walishajenga imani kuwa kutokana na umaarufu wao na fedha walizomwaga kiaina, kwa vyovyote lazima wangepitishwa katika uteuzi.



    Miongoni mwa hao waliokuwa na ‘roho nyeusi’ ni Pangapangua, mmoja wa wagombea waliotarajia kupitishwa katika kikao hicho kwa asilimia mia moja.Taarifa ya kuenguliwa kwake katika uteuzi wa wagombea ilimfikia kupitia vyombo vya habari usiku huohuo.

    Hakuamini!



    Na hakukubali hadi alipompigia simu mzee Kisauti na kumuuliza, “Ninayosikia ni kweli au uzushi mtupu?”



    “Ni kweli kijana wangu,” mzee Kisauti alijibu kwa unyonge. “Hata mimi nashindwa kuamini.”



    “Haiwezekani!” Pangapangua aliropoka huku akimkodolea macho mtangazaji wa televisheni aliyekuwa akiendelea kuitiririsha taarifa ya habari. Kwa jumla haikumwingia akilini kuwa kufuatia kazi iliyofanywa na jopo la wazee na kuhitimishwa na Mzee Kisauti aliyebeba fungu la pesa nyingi, shilingi milioni hamsini, eti imeishia kwa yeye kutemwa! Hakuamini!



    Huku simu ikiwa bado sikioni akafoka, “Una maana gani kuniambia kuwa unashindwa kuamini mzee? Umetoa mgawo kwa namna inavyotakiwa?”



    Kimya!



    “Mzee Kisauti unanisikia au hunisikii?”



    Mzee Kisauti alikuwa kama kachanganyikiwa. Alijisikia kuona aibu kuulizwa swali kwa namna ya kukaripiwa na huyu kijana mdogo kwa kuwa tu kampa mamilioni ya pesa. Lakini afanye nini? Alipaswa kujibu.



    “Nakusikia kijana wangu,” hatimaye alijibu. Na sasa akahisi ujasiri fulani ukimjia, ujasiri kwa kutamka bayana kuwa hayuko radhi kuisaliti nchi yake na kukisaliti chama chake. “Nimeshindwa. Na kwa kweli sikufichi, pesa zako ninazo. Siwezi kucheza mchezo huo mchafu. Ninaipenda nchi yangu. Ninawapenda Watanzania. Ninawapenda wakazi wote wa Jimbo la Mkwajuni. Nadhani shetani alikuwa amenitawala; shetani wa uchu wa pesa, na sasa nimemwepuka. Pesa zako chafu ninazo! Nitakurudishia!



    “Unasikia kijana,” aliendelea. “Kesho nitapanda basi na kurudi nyumbani. Nitakapofika, nitakuja moja kwa moja kwako kukurejeshea milioni zako hamsini. Umenielewa?”



    Yalikuwa maneno mazito sana masikioni mwa Pangapangua. Akiwa ameketi sebuleni peke yake, mkewe akiwa chumbani, kama aliyechanganyikiwa, alibwata, “Sikia we’ mzee! Sikuzitoa pesa hizo kwa minajili ya kwenda kuzurura! Nimezitoa zikafanye kazi, na wewe uliniaminisha kuwa kila kitu kitakwenda sawa. Leo unaniletea habari zisizoeleweka! Sikuelewi ujue! Sasa nakwambia hivi, sitaki pesa nautaka ubunge wangu, full stop!”

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Papohapo akakata simu kisha akaizima! Haraka akanyanyuka na kuelekea chumbani kama aliyechanganyikiwa. Akamkuta mkewe akipanga nguo kabatini. Haraka akalifuata begi maalum lenye vifaa vyake maalum. Akalifungua na kuitoa bastola, akaishika madhubuti katika mkono wa kulia, akaielekeza kwenye paji lake kisha akafyatua risasi moja tu!



    Wakati Maselina aliposhtuka, Pangapangua alikuwa akianguka sakafuni huku ubongo ukichuruzika kama uji wa moto!



    MWISHO
    Pseudepigraphasnoreply@blogger.comtag:blogger.com,1999:blog-7805201032262348818.post-82326853683181358512020-02-29T19:33:00.002+03:002020-03-06T14:50:29.612+03:00

0 comments:

Post a Comment

Blog