IMEANDIKWA NA : INNOCENT A. NDAYANSE (ZAGALLO)
*********************************************************************************
Simulizi : Milioni Thelathini
Sehemu Ya Kwanza (1)
HAKUWA na sababu ya kutojiamini. Aliishi maisha ya juu. Alijaaliwa afya njema. Akaunti yake benki ilinona. Lakini leo kuna jambo zaidi ya jambo linalomfanya chozi limdondoke. Analia!
Japo hii haikuwa mara ya kwanza kwake kulia tangu afikishe umri huu wa miaka ishirini na tano, lakini haikuwa kulia kwa uchungu kama hivi. Alilia, lakini vilio hivyo vya ukubwani vilikuwa ni vilio vya faraja na furaha.
Mara ya mwisho kulia kwa uchungu ni wakati mama yake alipofariki wakati akiwa ndiyo kwanza anahitimu kidato cha sita akiwa na umri wa miaka kumi na minane. Baada ya hapo mtoto huyo wa kike alikasirika na kununa kwa uchungu lakini hakuwahi kulia kwa uchungu.
Leo analia! Analia kwa uchungu na hasira, ameichukia dunia, ameyachukia maisha na hata kujichukia mwenyewe. Hajali uzuri wa sura yake na umbo lake. Anajiachia hapo chini machozi yakimtiririka, kilio cha kimyakimya!
“Haiwezekani….Nasema haiwezekani…” anaropoka kwa sauti kali kisha ananyanyuka.
Huyu anajaribu kumsihi atulie, hakubali. Yule naye anambembeleza, habembelezeki.
“N’acheni…N’acheni…!” anabwata.
Hakujali kuwa yuko katika kituo cha Polisi akiwa amezungukwa na askari kadhaa wenye nyadhifa zilizotofautiana. Hakujali. Alinyanyuka na kumtazama askari mmoja kisha akaropoka, “Hakuna chochote mnachofanya…Mnalipwa mishahara ya bure!”
“Nipisheni n’ende zangu,” akasema huku akimsukuma askari mmoja na kutoka.
Askari wakabaki wameduwaa wakimtazama, baadhi yao wakivutiwa na umbo lake lililotikisika kinamna yake kama aliyedhamiria kuwaadhibu makusudi.
*****
UKUMBI wa Seya Garden ulikuwa na idadi ndogo ya watu jioni hii. Hali hiyo haikuwa ya ajabu, ilikuwa ni kawaida watu kufurika ukumbini hapo siku za mwishoni mwa wiki wakati bendi moja maarufu inapotumbuiza. Kwa jioni hii, baadhi ya meza zilikuwa na watu na nyingine zikiwa tupu. Muziki laini kutoka kwenye vipaza sauti ulikuwa kivutio kingine kilichowafanya wateja wajikute wakiendelea kuwa ndani humo, wakinywa na kula.
Seya Garden ni ukumbi uliotokea kujizolea umaarufu mkubwa katika kitongoji cha Kinondoni, jijini Dar es Salaam. Ulikuwa Barabara ya Mwinjuma, jirani na kumbi nyingine kongwe za Mango, Vijana na MK. Haukuwa ukumbi mkubwa lakini ulitengenezwa kwa namna iliyowavutia wale waliodiriki kuingia kwa mara ya kwanza na hivyo kujikuta wakipenda kurejea kesho na keshokutwa. Ni ukumbi uliosheheni takriban kila kilichomstahili mpenzi wa starehe, amani na utulivu.
Kulikuwa na vinywaji kochokocho na vyakula vya kila aina. Wahudumu wa hapo ambao walikuwa ni wanawake pekee, nao pia walichangia kwa kiasi kikubwa katika kuwagandisha wateja mahali hapo. Robo tatu yao walikuwa warefu, wenye nyuso zilizojaa tabasamu nyakati zote, maumbile ya ujazo mkubwa, ujazo wa kati na unadhifu wa hali ya juu.
Robo iliyobaki ni ya wanawake tusioweza kuwaweka kwenye kundi la warefu au wafupi, na wanawake ambao sura zao ziliyavuta vilivyo macho ya wanaume wakware huku makalio yao makubwa yakiwa ni miongoni mwa vigezo vilivyowaweka katika daraja la wanawake warembo, machoni mwa marijali.
Ni ubora wa mandhari pamoja na uzuri wa wahudumu uliomfanya kijana mwenye umbile la wastani, mweusi ambaye alijulikana kwa jina la Chris apachukulie hapo Seya Garden kama sehemu pekee ya kuiliwaza akili yake. Jioni hii alikuwa miongoni mwa wateja wachache ambao, kama yeye, mavazi yao yaliwaonesha kuwa hawakuwa miongoni mwa Watanzania au raia wa nchi yoyote waishio maisha ya kubahatisha.
Mbele yake, katika meza hiyo aliyokuwapo, ambayo kulikuwa na viti vingine viwili kulikuwa na chupa ya soda ya Fanta. Kwa takriban robo saa tangu alipoletewa soda hiyo hakuwa amekunywa kiwango hata cha nusu chupa. Lakini hakuwa na haraka. Alikuja kustarehe na kuvuta muda.
Isitoshe, alipenda kuitumia baa hiyo kwa kupanga mipango yake ambayo aliamini kuwa ingemwingizia pesa za kutosha. Kwa muda mrefu amekuwa akitumia bila ya kuingiza, na hilo kwake lilikuwa ni pigo. Hakuwa tayari kuendelea kupata hasara siku hadi siku. Hapana. Alipaswa kuingiza maradufu kabla ya kutumia.
Kwa jioni hii, hadi giza lilipoingia bado alikuwa hajapata mbinu yoyote mpya na ya maana, ambayo ingemwingizia pesa nzuri na bila ya kumletea matatizo yoyote. Kwa hali hiyo hakuona kama ingemstahili kuendelea kukaa hapo. Akanunua pakiti tatu za pombe kali na kuondoka nazo.
**********
CHRIS ni jina lililokwishazoeleka na kukomaa mitaani. Kila mtu alimwita “Chris.” Jina lake kamili lilikuwa ni Christopher. Lakini umaarufu wa wasanii wakubwa nchini na katika mataifa makubwa ya Bara la Amerika, ambao walitumia majina ya Chris badala ya Christopher, uliwafanya hata majirani walioishi na wazazi wa Chris wamwite mtoto huyo, Chris. Kitongoji cha Kinondoni Shamba jijini Dar alikoishi na wazazi wake, jina la Chris ndilo likakua na kukomaa.
Alisoma elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Hannanasif, kisha wazazi wake wakamtafutia nafasi katika Shule ya Sekondari ya Muslim hapohapo Kinondoni, shule ambayo aliitema pindi alipofika kidato cha tatu. Kitendo hicho kiliwashangaza na kuwashtua wazazi wake. Ndiyo, wazazi wake walishangaa siku alipowatamkia bayana kuwa kishachoka kusoma.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nini?” baba yake alimuuliza kwa ukali.
“Shule haina maana,” alijibu kijasiri. “Wangapi wamesoma na sasa hivi wanasota na vyeti vyao vibindoni? Tanzania ya leo mtu unapaswa kutumia akili ya kuzaliwa tu. Mtu unatakiwa kuwa mjanja, utaishi na utawini. Siyo kupoteza muda bure kwa kubukua halafu matokeo yake unaishia kupiga mizinga hata kwa nauli ya daladala.”
“Unasemaje?” mama yake aliingilia. “Hujui kuwa dunia ya leo siyo ile ya enzi zetu sisi wazazi wako? Hebu ona, enzi zetu ilikuwa rahisi kwa mtu mwenye kiwango cha elimu ya msingi kuweza kupata ajira kwenye mashirika au katika idara za serikali. Hata kwenye kampuni za kigeni ilikuwa ni rahisi kupata ajira.
“Lakini siyo leo. Siyo leo, mwanangu. Leo hii, mtu aliyemaliza form four au form six anaweza kupata uhudumu wa ofisi kwa mbinde tena kwa kupitia mlango wa nyuma! Sanasana, siku hizi mtu aliyebeba vidato sita kichwani pamoja na kaujuzi fulani ka maana kutoka katika vyuo vinavyokubalika na serikali, huyo anaweza kupewa kipaumbele katika kuajiriwa. Isitoshe, siku hizi nd’o s’jui mnaita dunia ya Sayansi na Teknolojia, eti?”
“Ndiyo!”
“Basi itakubidi ukubaliane nasi kuwa elimu ndiyo nguzo ya maisha yako ya usoni,” mama yake alisema. “ Nakuomba mwanangu, nakuomba sana uangalie mbele kabla ya kuchukua huo uamuzi wako wa kuacha shule.”
Hazikuwa nasaha zilizomwingia akilini Chris. Alikuwa na kumbukumbu za watu kadhaa walioneemeka kimaisha japo ‘darasa’ hawakuliona. Mmojawao ni Ntiruyamba.
Huyo naye alipofika darasa la tatu, enzi zile za mkoloni, akaiona shule chungu. Mambo ya kuwahi namba asubuhi, kuchapwa viboko kwa makosa ambayo kwake aliona kuwa ni ‘vijikosa’ sanjari na kulazimika kuandaa sare kila siku za mwishoni na katikati ya wiki, kwake ilikuwa ni kero isiyovumilika. Akiwa na tabia ya ukatili tangu utotoni, Ntiruyamba aliamua kujiingiza kwenye fani ya udokozi.Udokozi huo, hatimaye ulizaa ujambazi kamili pindi alipotimiza umri wa miaka 20. Akawa ni mtu wa kulazimisha kupata kila akitakacho kutoka kwa yeyote bila ya woga wala kusita.
Miaka kumi na mitano baadaye, Ntiruyamba alikuwa Mbezi Beach, ndani ya jumba lake la kifahari, malori matatu ya mizigo, mabasi mawili ya kusafirisha abiria katika mikoa mbalimbali na duka kubwa la bidhaa za jumla vikiwa ni vitegauchumi vyake vikuu.
Sasa Ntiruyamba alikuwa muumini mzuri wa kanisa moja maarufu hukohuko Mbezi Beach. Alichangia kila kilichohitajika usharikani hapo. Na mara kwa mara alikuwa akipata nafasi ya kuhubiri ibadani, mwonekano wake na kauli zake vikionyesha kuwa ‘amempokea Yesu.’
Chris alizipata habari zilizomhusu Ntiruyamba siku moja alipokuwa katika kijiwe cha kahawa. Mzee mmoja aliyedai kuwa alisoma na Ntiruyamba shule moja enzi za ujana wao, ndiye alikuwa akizungumzia siri ya mafanikio ya Ntiruyamba. Habari hiyo ikawa ni imemchochea Chris na kuanzia siku hiyo akawa na dhamira maalumu kichwani mwake. Alitaka kubadilika.
Aliwaza pesa!
Aliwaza kutajirika!
Ni mawazo hayo yaliyomfanya awabwatukie wazazi wake juu ya uamuzi wa kuachana na elimu. “Kuangalia mbele ni kutafuta maendeleo ya kimaisha,” alimwambia mama yake kwa msisitizo. “Siyo kushinda darasani watu hamsini mkipumuliana kama nguruwe. Hapana, kwa hilo hatukubaliani!”
Iliwalazimu wazazi wake kunawa mikono. Hawakuwa na mbinu nyingine ya kuyabadili mawazo au kuutengua uamuzi wa Chris. Miezi mitatu baada ya Chris kuitema elimu, tayari akawa ameshafanya matukio matatu yaliyomwingizia pato la kuiridhisha nafsi yake. Tukio la kwanza alilifanya akiwa na wenzake wawili.
Siku hiyo walimpora mkoba mwanamke wa Kitaliano Barabara ya Ocean majira ya jioni. Walichokikuta ndani ya mkoba ni fedha taslimu za Tanzania shilingi 800,000, pauni 500 za Uingereza na dola 10,000 za Marekani. Pia kulikuwa na simu ndogo ambayo hawakupata taabu kuiuza kwa bei ya kutupa kwa wanunuzi wa simu za wizi katika mtaa fulani katikati ya kitongoji cha Kariakoo.
Mgawo alioupata katika tukio hilo ulimwongezea ari ya kusaka kazi nyingine, ikibidi iwe ni kazi yenye kipato kikubwa zaidi. Ndipo ikatokea siku nyingine yenye neema. Akiwa na wenzake walewale wawili, walimpora gari dereva teksi baada ya kumkodi na kwenda naye hadi Bunju ‘A.’
Huko walimshurutisha kuendesha gari hadi eneo ambalo halikuwa hata na nyumba moja, kisha wakamshindilia vitambaa kinywani na kumfunga kamba mwili wote kabla ya kumpora shilingi 80,000 na kumtupa kando ya barabara. Usiku huohuo, gari hilo liliegeshwa Kimara Baruti kwa Aloyce Tarimo, Mchaga mwenye pesa lukuki.
Muda mfupi baadaye waliondoka hapo kwa Aloyce wakiwa na kitita cha shilingi milioni kumi.
Tukio la tatu walilifanya mwezi mmoja baada ya tukio la pili. Na katika kuhakikisha kuwa mipango yao katika kufanikisha utekelezaji wa tukio hilo haivurugiki, iliwalazimu kutumia pesa zisizo haba; kumhonga mtu mmoja ambaye aliwapa siri kamili na jinsi ya kuufanikisha mpango wao. Tukio hilo lilipangwa kufanyika katika duka la kubadilisha fedha lililoko Oysterbay.
Siku ya tukio, mmiliki wa duka hilo alitoka na fuko kubwa lililofurika fedha kwa safari ya benki. Lakini kabla hajalifikia gari lake lililokuwa hatua kama kumi tu kutoka katika mlango wa duka, mara risasi tatu zilivuma mbele yake. Alishtuka, akashangaa na kusimama akiangaza macho huku na kule!
Sekunde mbili baadaye alishtukia akiporwa fuko lile na mtu aliyekuwa na bastola mkononi. Baada ya muda mfupi akashuhudia gari dogo jeupe likiondoka hapo kwa kasi ya kutisha!
Sasa Chris alikuwa na pesa lukuki. Wazazi wake walibaki wakijiuliza ni vipi mtoto wao ana pesa nyingi kiasi hicho, maswali ambayo hawakuthubutu kumuuliza bayana. Na hata Chris mwenyewe hakutaka kuwadokeza chochote kuhusu mafanikio yake.
Ili kuwafanya wazidi kumpenda na hata kumwombea kwa Mungu azidi kufanikiwa, aliwanunulia nguo za thamani kubwa na kuwapa pesa nyingi za matumizi.
Isitoshe, katika kipindi hicho alichofanya matukio matatu makubwa, aliikarabati nyumba yao kwa kununua mabati mapya na kubadili milango na madirisha. Pia alinunua redio kubwa na kuijaza sebule masofa ya kisasa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hakuishia hapo, aliifanya nyumba hiyo ing’are kwa kuweka globu ndefu za umeme kila pembe kwa nje na globu nyingine zikiongeza umaridadi ndani ya vyumba. Sasa nyumba hiyo ikawa miongoni mwa nyumba chache zenye mvuto katika kitongoji cha Kinondoni Shamba.
Hata hivyo, baada ya matukio hayo matatu sasa akajiwa na wazo jipya, wazo la kupata pesa kwa mbinu ambayo aliamini kuwa hakutakuwa na raia wa kawaida, mwenye macho ya kawaida na akili ya kawaida, atakayemshuku. Si hao tu, bali pia aliamini kuwa hakutakuwa na askari atakayemtuhumu.
Alihitaji kudhihirisha kivitendo ile imani yake kuwa ‘kuishi mjini ni ujanja, na maendeleo hayatokani na elimu pekee.’ Lakini pia alitambua fika kuwa utekelezaji wa hilo ungemgharimu pesa, tena siyo pesa kidogo, ni pesa nyingi.
Hata hivyo, hilo halikumtisha. Aliamini kuwa matumizi ya pesa kwa umakini huzaa faida ya pesa nyingine, nyingi. Hakujali kutumia kiasi cha shilingi laki tatu au nne kama kwa kufanya hivyo atazalisha shilingi laki sita au saba. “Tumia pesa, upate pesa…” kauli hiyo ilimjia kichwani mara kwa mara, na ikampa ujasiri mkubwa wa kutorudi nyuma.
**********
SAA 8 mchana, Salma, mwanamke aliyekuwa akifanya kazi Makao Makuu ya Wizara ya Fedha alitoka ofisini na kulifuata gari lake lililokuwa hatua chache nje ya jengo hilo. Akalitia moto akiwa na dhamira ya kwenda kwenye ofisi za TRA, Barabara ya Samora.
Alishika Barabara ya Shaaban Robert kisha akaiacha na kuifuata Barabara ya Sokoine. Dakika kadhaa baadaye aliliegesha gari kando ya jengo lenye ofisi aliyoifuata, na dakika thelathini baadaye alitoka ndani ya jengo hilo, akaingia ndani ya gari lake na kuondoka.
**********
TANGU asubuhi Chris alikuwa Kurasini akiwa na maongezi muhimu na mmoja kati ya rafiki zake ambao walishirikiana katika kazi yao iliyowaingizia pesa lukuki.
Alipotoka Kurasini aliamua kupitia eneo la katikati ya jiji kwa jamaa yake mwingine, hivyo alipanda daladala na kuteremkia Stesheni. Kutoka hapo alitembea taratibu hadi akazukia Barabara ya Samora. Magari mengi yalipita katika barabara hiyo, na mengi kati ya hayo yakiwa ni ya kuvutia. Chris aliyaangalia tu magari hayo na kuendelea kutembea taratibu, akivutiwa na ubora wa majengo mapya yaliyozuka katika mtaa huo maarufu.
Hatimaye akafika jirani na jengo lenye ofisi za TRA. Hapo pia akayakuta magari kadhaa yakiwa yameegeshwa. Mara akaliona gari jingine likiondoka taratibu huku hata ngurumo yake ikiwa haisikiki. Lilikuwa ni gari zuri, aina ya Toyota Land Cruiser. Akavutiwa na gari hilo jeusi. Akasimama kidogo na kulitazama kwa makini.
Akavuta hatua na kulifuata na akalifikia wakati bado limesimama. Akatupa macho ndani na kumwona mwanadada mweupe kiasi, mnene anayeonekana dhahiri kuwa na afya njema. Akili ya Chris ikahama; sasa akavutria na mwanadada huyo ambaye hata tazama yake ilikuwa yenye mvuto wa aina yake. Kwa mwanamume dhaifu kwa viumbe wazuri wa kike, haya macho ya mwanadada huyu yangeweza kumfanya aamini kuwa anapendwa. Macho yaliyozungumza mapenzi, macho yaliyobembeleza, macho yaliyosihi, macho yenye njaa.
Macho ya Chris yalishindwa kubanduka mwilini mwa mwanadada huyo hadi gari lilipoondoka tena. Hata hivyo Chris hakuishia hapo. Akaitoa simu mfukoni na kuitazama. Hakuwa na tabia ya kuvaa saa mkononi kwa kuwa alijua kuwa akitaka kufahamu ni saa ngapi ataitumia simu yake.
Akaguna huku akiendelea kuitazama simu hiyo. Ilikwishatimu saa 8.45 mchana. Akashusha pumzi ndefu huku akijiuliza ni kwa nini amekurupukia kumfuatilia mrembo huyo ilhali hakuwa kwenye programu yake. Uzuri wake tu ndiyo umchanganye kiasi hicho?
Au naanza kuzeeka? Alijiuliza huku sasa akishuhudia lile gari likiendelea na safari taratibu. Hata hivyo, akaliponda swali hilo kwa kukumbuka kuwa muda wowote na kwa wakati wowote anapaswa kufanya jambo lolote katika mpango wowote utakaozuka. Yuko huru akiwa ni mwamamume aliyekamilika. Anaweza kumtamani au kumpenda mwanamke yeyote atakayemvutia. Ni kosa kumtamani au kumpenda huyu mwanadada mzuri aliyependeza ndani ya gari hilo zuri?
Akaachia tabasamu dogo huku akiifuata teksi na kumwambia dereva alifuate gari hilo.
Land Cruiser hilo liliendelea na safari yake likiifuata barabara hiyohiyo ya Samora hadi tena lilipoukuta Mtaa wa Shaaban Robert na kukata kulia hadi Makao Makuu ya Wizara ya Fedha. Chris akiwa nyuma ya gari hilo alipoliona limeingia kwenye ofisi za Wizara ya Fedha alimwamuru dereva aegeshe teksi. Akamlipa ujira wake na kuteremka.
Akamfuata fundi viatu aliyekuwa kando ya barabara hiyo.
“Fundi vipi, shwari?” ndivyo alivyomwingia huku akiketi katika benchi.
“Shwari tu, mjomba,” fundi alijibu huku akimtazama Chris miguuni. Akaongeza: “Kubrashi au kukarabati?”
“Kubrashi tu, mwanangu,” Chris alijibu huku akivua viatu. “Chaji yako ni kiasi gani?”
Fundi alimtazama Chris kwa chati na kumpigia hesabu za kibiashara zaidi. Hili shati alilovaa lilikuwa zuri na fundi alikwishawaona wengi wenye hali njema mifukoni wakiwa wamelivaa. Isitoshe alikwishaliona kwenye maduka mawili yanayouza nguo za bei ya kutisha, shati hili likiwa mojawapo. Bei yake ni shilingi 120,000. Hata suruali na viatu vyake havikuwa vile vya mafungu, vya kuvizia furushi lifunguliwe kwa ‘chinga’ kisha wateja mjichagulie. Hapana, hivi navyo vilikuwa vya daraja la wenye-nazo.
Kwa hali hiyo, hakutaka kumchekea mteja huyu aliyekuja na teksi ya nguvu. “Buku tu, mjomba,” alimwambia huku akiendelea kubrashi viatu vingine ambavyo wateja hawakuwapo.
Siyo kwamba Chris alikuwa mshamba sana kiasi cha kutojua kuwa fundi kampigia hesabu. Alijua lakini hakujali. Alitambua fika kuwa mfanyabiashara yeyote wa Dar atokapo Vingunguti, Buguruni, Mwananyamala, Ukonga au popote pale na kuja na biashara yake maeneo haya ya ‘Uhindini’ huwa lazima bei ibadilike, na haishuki, hupanda tena labda maradufu!
Hivyo hakutaka kupoteza muda kubishana na fundi huyo, akili yake ilikuwa mbali na isitoshe mfukoni alikuwa na shilingi 120,000 ambazo hazikuwa na lengo la ununuzi wowote wa kifaa cha bei kubwa; zilikuwa ni za kuulinda utanashati wake na uwanaume wake.
Akatabasmu kidogo huku akivua viatu. Fundi akaling’amua tabasamu hilo na kuhisi hila yake imebainika. Akajihami ‘kimjinimjini’ akiropoka, “Mjomba, hapa ni ulaya. Tenga hizo buti hapa uone. Nakwambia, mwenyewe utakubali kuwa kweli umefika kwa mtaalamu.”
Chris alichomoa noti moja ya shilingi 5,000 na kumpatia fundi huyo. Kisha akasema, “Kata buku yako ya kazi na chukua buku kwa nauli. Buku nyingine kaniagizie gazeti.”
Fundi alikenua meno mpaka gego la mwisho. “Asante sana mjomba,” alisema. “Hapo umeniwezesha kwa kiasi ambacho sikutegemea, mwana.” Papohapo akasimama na kuuliza, “Gazeti gani baba’angu?”
“KIMBEMBE.”
Dakika chache baadaye Chris alikuwa na gazeti la KIMBEMBE lililokuwa na habari mchanganyiko; za siasa, matukio ya kila siku kutoka mikoa mbalimbali, makala za michezo, uchumi, afya, riwaya na katuni.
Wakati fundi huyo akiendelea na kazi ya kubrashi, Chris alikuwa akipitia habari hii na ile katika gazeti hilo. Kukawa na ukimya wa dakika kadhaa wakati huyu akisoma na huyu akibrashi.
Hatimaye Chris aliacha kusoma na kukuna kidevu, macho kayakodoa barabarani. Kisha, kama aliyezinduliwa usingizini, alimtupia swali fundi: “Huyu demu aliyeingia na shangingi jeusi, unamfahamu?”
“Namfahamu kwa sana tu, mjomba,” fundi alijibu haraka. “Ni mtu wa siku nyingi hapa wizarani. Na pia ni mteja wangu. Huwa anakuja-kuja hapa nambrashia viatu au kuvishona, si unajua tena hivi viatu vya dada zetu ni magumashi tu msh’kaji wangu.”
Mlolongo mrefu wa maneno aliyosema huyo fundi ulipitiliza tu masikioni mwa Chris, yeye alihitaji kujua yanayomhusu huyo aliyemuulizia. Kushona au kubrashi viatu hapo hayakumhusu. Hata hivyo alikuwa ‘mpole.’ Huku akiachia tabasamu hafifu na kumtazama usoni fundi, akamuuliza kibwege, “Kumbe yuko humo wizarani?”
“Ndiyo.”
“Anaitwa nani?”
“Salma. Sie tumezoea kumwita Salma- Mnyamwezi,” fundi alijibu na kisha akamtazama Chris usoni huku naye tabasamu likichanua kwa mbali. Kisha akamuuliza, “Vipi, unataka kumtokea?”
“Nd’o maana’ake. Ni kifaa kilichotimia kila idara. We' mwenyewe si unakiona?”
“Ni kweli,” fundi alijibu. “Wash’kaji wengi wanaomwona hapa humzimia kishenzi, mwanangu.Wengine ni ka' vile wewe. Huniuliza-uliza kuhusu yeye.”
“Kaolewa?”
“Nasikia ana jamaa yake mmoja, Mpemba anayemiliki mali.”
“Na hilo gari?”
“Ni lake!” fundi alijibu haraka. “Inasemekana huyo Mpemba wake nd’o kamshushia kutoka majuu.”
“Kwani…” Chris alisema na kusita ghafla. Kisha tena akaendelea, “Kwani anafanya kazi hapa wizarani?”
“Ndiyo! Mbona ni’shakwambia mjomba!” Sasa fundi akamtazama Chris kama vile anamtazama mtu mwenye upungufu wa akili au kachero aliye kazini muda huo.
“Aaah, nimesahau,” kwa mara nyingine Chris akajibu kibwege-bwege.
“Basi nd’o ivo. Yuko hapo wizarani. Mi’ n’na mwaka na kitu hapa kijiweni, na nilimkuta.”
“I see.”
Kwa mara nyingine kimya kikatwaa nafasi. Chris akamwita kijana mmoja aliyekuwa akipita kando ya barabara huku akinadi maji ya chupa. Akanunua chupa moja na kuanza kunywa taratibu.
“Anaishi wapi?” Chris aliuvunja ukimya ule.
“Kariakoo.”
“Una hakika?” Chris alimkazia macho.
“Aaah…kwa kweli sijawahi kufika kwake. Aliniambia mwenyewe.”
“Alikwambia anakaa mtaa gani?”
“Rufiji.”
“Kwake, au kapanga?”
“Kwake, mwanangu,” fundi alijibu huku akimtazama Chris kwa tabasamu la mbali. “Mdada mwenyewe ana chombo cha nguvu kiasi kile halafu awe anapanga?”
“Hili sio la ajabu,” Chris alisema. “Wapo watu wengi tu wanaotanua na magari mitaani huku hawana hata kibanda cha mbavu za mbwa.”
“Usemayo ni kweli tupu. Lakini sio huyo demu, mjomba. Kanihakikishia mwenyewe kuwa anaishi kwake, siyo kwamba kapanga!”
Chris alitikisa kichwa akionyesha ishara ya kuafiki. Akaipeleka chupa mdomoni na kugugumia mafunda kadhaa ya maji. Kisha: “Ni nyumba aliyonunuliwa na huyo Mpemba wake?”
“Inawezekana. Maana’ake nasikia jamaa mwenyewe hasikii kitu kwa huyo demu.”
“Na huyo Mpemba mwenyewe anaishi naye?”
“Haishi naye. Yeye ni mkazi wa Magomeni. Ana mke na watoto. Lakini mara nyingi huwa safarini, na safari zake nyingi ni za Uarabuni. Sijui anajishughulisha na nini. Labda nd’o hawa wash’kaji zetu wa zile biashara nyingine.”
“Unga?”
“Nd’o maana’ake.”
Chris akacheka kidogo, fundi naye akakipokea kicheko hicho. Kisha Chris akasema, “Yote maisha. Hata mmimi nikipta mchongo huo najitosa tu, nchi yenyewe hii haina mpango tena baba’ake.”
Kwa maranyingine wote wakacheka.
Chris aligugumia maji yote na kuitupa chupa kando. Akakohoa kidogo na kurusha swali jingine: “Kuna mtu anayepafahamu vizuri kwake?”
“Kwake?” fundi alisitisha kazi ya kubrashi viatu vya Chris. Akamtazama usoni kwa makini na kuuliza, “Kwake…nani? Salma au huyo Mpemba wake?”
“Mpemba wa nini? Hapa tunamzungumzia huyo demu!”
Fundi aliendelea kubrashi. Kisha, bila ya kuyainua macho tena, akajibu, “Kwa kweli sijui nani anapafahamu kwake. Hata mimi aliniambia tu kwamba anaishi Kariakoo, Mtaa wa Rufiji.”
Chris alitabasamu kidogo kisha akatamka kwa sauti ya chini, “Nitampata tu. Sina gari, sina nyumba, lakini hawezi kunishinda. Baada ya siku mbili nitakuja kukwambia.”
Fundi alicheka kidogo na kudondosha, “Poa, mwanangu. Aminia. Fukuzia, juhudi yako tu! Na kama damu yake na yako zikipatana, umewini.”
Chris aliondoka hapo akiwa amedhamiria kuendelea kumfuatilia mrembo mwenye mvuto mkali, Salma.
**********
SIKU iliyofuata, Chris alitulia nyumbani akifanya shughuli ndogondogo tangu asubuhi hadi mchana. Ilipofika saa 8 alikuwa ndani ya teksi akielekea katikati ya jiji.
Teksi hiyo ilimwacha kwenye makutano ya Barabara za Sokoine na Shaaban Robert. Kutoka hapo alitembea taratibu hadi umbali wa takriban meta mia mbili kabla ya kumfikia yule fundi viatu. Hakutaka fundi huyo ajue kuwa leo tena kaja. Hivyo, safari hii alisimama kando ya kijimeza cha pipi, biskuti na vikorokoro vingine ambavyo vilikuwa vya biashara rasmi ya kijana mmoja, kwenye makutano ya Barabara ya Shaaban Robert na Sokoine.
Alifika hapo zikiwa ni dakika kumi kabla ya kutimu saa 9.30. Wakati huo wote macho yake hayakucheza mbali na geti la Makao Makuu ya Wizara ya Fedha. Hata hivyo hakutaka kuwa ni mtu anayeonekana kutokuwa na chochote cha maana kilichomweka hapo.
Akaifuata meza ya muuza magazeti na kununua gazeti la udaku kisha akaegemea ukuta wa Shule ya Msingi ya Bunge akiwa katika mawindo yake japo aliyagandisha macho kwenye kurasa za gazeti hilo.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hatimaye alichokisubiri kilitokea. Gari jeusi, Land Cruiser GX lilitoka ndani ya uzio wa jengo la Wizara ya Fedha. Macho ya Chris yakalikodolea gari hilo zuri. Akalikumbuka! Akachunguza kuona idadi ya watu waliokuwemo ndani yake. Akagundua kuwa kulikuwa na mtu mmoja tu, mwanamke aliyekuwa akiliendesha.
Chris akiwa ndani ya suti maridadi, alijisikia kujiamini kwa kiwango cha juu, hivyo hakusita kusogea barabarani na kulipungia mkono.
**********
AKIENDESHA gari kwa mwendo wa kistaarabu, Salma alimwona kijana mmoja wa kiume, mtanashati akipunga mkono mbele yake. “Ni nani tena huyu, na anataka nini?” Salma alijiuliza kwa mnong'ono huku akimwangalia kwa makini mtu huyo.
Alijaribu kuvuta kumbukumbu ni wapi aliwahi kumwona, lakini hakukuwa na kumbukumbu yoyote iliyomjia. Hata hivyo, aliamua kuutii mkono ule, akapunguza mwendo wa gari na hatimaye akapaki kando ya mtu huyo ambaye hakuwa mwingine, bali ni Chris.
“Unasemaje, anko?” Salma alimuuliza.
Tabasamu hafifu likamtoka Chris. “Msaada wako, shangazi,” alijibu. Wakati huo alikuwa kwenye mlango wa mbele, kushoto.
“Msaada gani?” Salma alimtazama kwa macho makali kwa namna ya kumshangaa.
“Naomba unisogeze hadi hapo Posta tu, shangazi,” Chris alijibu kisha akatupa macho angani na kuongeza, “Si unaona wingu hili?”
Ni kweli, anga yote ilikuwa imebeba mawingu mazito, mawingu yaliyoashiria mvua kubwa muda mfupi ujao. Salma akamtazama kwa makini zaidi Chris. Hisia nyingine zikamjia akilini. Mara kwa mara alizisikia habari zilizohusu waporaji magari ambao, wengi wao huwa na nyuso zisizokosa ucheshi kila wakati huku pia utanashati ukiwa umepewa kipaumbele.
Hudaiwa kuwa waporaji hao hutumia hila za juu kiasi cha kutobainika mapema hadi wanapotimiza malengo yao. Salma hakuwa akimjua Chris lakini pia hakupenda kuamini kuwa kila mcheshi na mtanashati ni jambazi. Hivyo, kwa moyo mweupe alimruhusu kuingia.
Land Cruiser likashika Barabara ya Shaaban Robert kisha likaingia Sokoine Drive. Hapo wakakumbana na msururu mkubwa wa magari. Safari yao ikawa ya kusuasua kama kinyonga. Ni katika kipindi hicho ndipo Chris alipoanza kumdodosa Salma.
“Shangazi, mi' naitwa Chris,” alijitambulisha. Haikuwa kawaida yake kujitambulisha kwa jina lake halisi. Mara kwa mara alikuwa akibuni jina bandia hususan kwa mtu ambaye ndiyo kwanza wanaonana. Na tabia hiyo aliianza tangu alipojiingiza katika mfumo mpya wa maisha, mfumo wa kusaka pesa kwa njia yoyote, ikibidi hata kumuua mtu.
Lakini kwa huyu Salma, hakuiona haja ya kulificha jinale. Na alifanya hivyo katika kuepusha kujisahau hapo baadaye na akajikuta akilikana jina jipya atakalokuwa amejitambulisha kama ikitokea wakafahamiana zaidi na kuzoeana kwa kiasi kikubwa.
“Chris?” Salma alimuuliza huku akimtazama.
“Yeah, Chris.”
“Unaishi wapi?”
“Kinondoni. Kinondoni Shamba. Na ninajishughulisha na biashara ya bidhaa mbalimbali.”
Ukimya ukapita kwa sekunde kadhaa. Salma hakuonyesha dalili ya kujali utambulisho uliotolewa na Chris na hata yeye hakujitambulisha. Safariikaendelea huku Salma akionekana kuwa makini na uendeshaji.
Chris akaamua kuchokoza. “Kama utaridhia, nami ningependa kukufahamu.”
Salma aliguna, mguno ambao haukuyafikia masikio ya Chris. Kisha akaachia tabasamu dhaifu. “Nashukuru kukufahamu,” hatimaye alisema. “Mimi naitwa Salma Amour, mzaliwa wa Tabora, Wilaya ya Urambo. Kwa hapa Dar naishi Kariakoo, Rufiji Street.” Kufikia hapo Salma hakuonyesha kuendelea kuzungumza.
“Kikazi?” Chris aliuliza.
“Niko hapo Wizara ya Fedha.”
“I see.”
“Kwani wewe unajishughulisha na biashara gani?” Salma alimtupia swali.
Lilikuwa ni swali ambalo Chris hakulitarajia. Ukweli ni kwamba hakuwa akifanya biashara yoyote. Hata hivyo alijitutumua na kupata jibu la haraka, jibu alilotarajia kuwa lingemridhisha Salma. “Huwa nanunua vitenge vya Wax kwa bei ya jumla kutoka huko Kigoma,” alisema. “Zile Wax-original. Nikivileta hapa huwauzia wenye maduka ya rejareja. Ni biashara ninayoitegemea mpaka sasa, na ndiyo iliyonipatia nyumba ya pili huko Tegeta.”
Uongo mtupu! Lakini ukiwa ni uongo ambao masikioni na akilini mwa Salma ulikuwa ni ukweli usiokuwa na dosari. Msururu wa magari ulikuwa ukizidi kusogea mbele. Sasa walikuwa jirani na Hoteli ya New Africa. Salma alimtazama tena Chris, lakini safari hii kwa chati, akiyakagua mavazi yake.
Hii suti aliyovaa Chris haikuwa ngeni machoni mwa Salma. Ni kati ya zile suti maridadi zinazouzwa katika maduka ya wenye-nazo, maduka ambayo ni Watanzania wachache sana wanaodiriki kuingia.
Katika kumbukumbu za Salma, hii suti aliyovaa Chris haikutofautiana na suti ya Mpemba wake mwenye utitiri wa pesa. Bei ya dukani ni shilingi 500,000. Akilini kwa Salma sasa alimchukulia Chris kuwa ni mtu mwenye heshima, na asiyeishi maisha ya kubahatisha. Sura yake, urefu wake, tabasamu lake na tazama yake sanjari na utanashati wake, vilimfanya Salma ajikute akivutiwa naye na kujiambia kimoyomoyo, ‘kwani kila mtu anayekujia kwa bashasha ni mwizi au tapeli?’ Akakana papohapo.
Hapo kando ya New Africa Hotel kwenye makutano ya barabara za Sokoine na Azikiwe, Salma alilazimika kusubiri tena kwani daladala na magari mengine yalipita kwa wingi na kwa kasi, baadhi yakielekea Kivukoni na mengine, Posta ya Zamani.
“Utateremkia wapi? Mie naelekea Kariakoo,” Salma alimtazama Chris usoni, akiendelea kuonyesha aina ya utazamaji wa majidai, utazamaji wa mtu aliyeridhika na maisha aliyonayo. Ni hapo ndipo Chris alipokumbuka kuwa aliomba lifti ya kukomea Posta.
“Hata hapa panatosha, shangazi,” alisema huku akijiandaa kufungua mlango. Kisha ghafla akaongeza, “Lakini nadhani na wewe unaweza kuwa mteja wangu mzuri. Vipi, hauhitaji hata doti moja?”
Tabasamu jingine likachanua usoni pa Salma. “Nahitaji sana,” alisema. “Kwa kweli nahitaji, labda tutashindana tu kwenye bei.”
“Hapana, hatuwezi kushindana, shangazi. Nina doti tatu zilizosalia nyumbani. Hizo nilipanga nimtunzie mama yangu. Kwa kweli ni nzuri sana. Nitakuonaje ili nikuonyeshe, ujichagulie?”
“Ulipanga kumtunzia mama yako,” Salam alisema huku akimtazama kwa namna ya kumsuta. Papohapo akarusha swali, “Sasa kwa nini uziuze?”
“Hilo sio tatizo,” Chris aliitetea hoja yake. “Baada ya wiki mbili nitakuwa na mzigo mwingine wa nguvu, zaidi ya doti thelathini za Wax. Nitampatia katika doti hizo. Kwa hiyo?” akamtazama Salma kwa makini akionyesha bayana kuwa anasubiri jibu.
Macho yao yakagongana. “Uzilete ofisini,” Salma alisema.
“Ofisini?”
“Ndiyo, kwani huwezi kuja ofisini?”
Chris alifikiri kidogo kisha akasema, “Naweza, lakini nadhani siyo vizuri kuja ofisini wakati huenda utakuwa kwenye majukumu yako ya kikazi. Kwani hatuwezi kukutana sehemu nyingine zaidi ya ofisini kwako?”
“Inawezekana, lakini kama siyo ofisini, basi labda uje nyumbani kwangu.”
“Hakuna matatizo yoyote huko nyumbani kwako?”
“Matatizo! Matatizo gani?” Salma alimtazama kwa mshangao.
“Mzee hawezi kunifikiria vibaya?”
Salma alisonya kisha akaachia tabasamu kubwa. “Mzee ana mambo ya kizungu. Hana mawazo ya kijinga-jinga. Hana tabia za Waswahili.We njoo tu wala usihofu.”
“Basi kumbe shwari,” Chris alisema. “Umesema uko Rufiji Street?”
“Yeah, Rufiji Street.”
“Nyumba namba ngapi?”
“Namba T 16 PPK.”
Chris alitwaa simu yake na kuziandiaka namba hizo kisha ‘akazisevu.’ “Nikija jioni, kitu kama saa kumi na moja, nitakukuta?”
“Utanikuta.”
Mara tu Chris alipoachana na Salma, alikwenda kando ya bustani mbele ya Benki ya Taifa ya Biashara na kuivaa teksi moja kati ya nyingi zilizoegeshwa hapo.
“Kariakoo,” dereva aliambiwa.
Teksi ilikula lami hadi Makutano ya Barabara za Uhuru na Sikukuu. Hapo, Chris aliachana nayo, akachepuka kwa miguu hadi Mtaa wa Aggrey. Baada ya kuingia katika maduka mawili, hatimaye alitua katika duka la tatu lililosheheni vitenge vya Wax. Akachagua doti tatu na kuzilipia. Kisha akatoka. Akaendelea kusaga miguu hadi Mtaa wa Msimbazi ambako alikodi teksi nyingine iliyomrudisha nyumbani.
**********
SURA ya Chris ilimjia kichwani Salma mara kwa mara baada ya kuachana pale kando ya New Africa Hotel. Alijisikia kumhitaji, zaidi ya kukutana kwa ajili ya biashara ya vitenge.
“Ana mvuto kiasi chake,” alijikuta akinong'ona, mnong'ono ambao haukuweza kuyafikia hata masikio yake mwenyewe.
Huu ulikuwa ni mwezi wa pili tangu hawara yake wa Kipemba, Abdulrahman Sadick alipokwenda Muscat. Miezi miwili haikuwa haba kwa Salma. Tangu uhusiano wa mapenzi kati yake na Abdulrahman Sadick ulipozaliwa, Abdulrahman alikuwa akimridhisha Salma kwa mambo mengi. Alikuwa akimpa pesa zisizo haba, alimnunulia hiyo nyumba ya Mtaa wa Rufiji, na isitoshe, pindi walipojitupa kitandani, Abdulrahman alikuwa akimfanyia ziada ya yale aliyowahi kufanyiwa na wapenzi wake wa siku za kisogoni.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ni utundu wa Abdulrahman chumbani ndio uliomlemaza Salma kiasi cha kujikuta akitaabika pale ilipotokea akaikosa huduma hiyo japo kwa wiki moja tu. Mara kadhaa alijikuta akivutiwa na baadhi ya wanaume aliowatia machoni lakini alisita kuwatamkia chochote kwa kile alichoamini kuwa angeonekana ni malaya.
Huyu Chris ni kati ya wanaume hao waliomvutia. Alimpenda na alijisikia kumhitaji. Akaomba Mungu jioni hiyo Chris amtamkie kile anachohitaji kutamkiwa; aombwe uhusiano wa mapenzi na ikiwezekana, aombwe penzi! “Itakuwa bahati ilioje kama atataka leo hii?” alijiuliza wakati akiwa bafuni akijitazama kwenye kioo kirefu kilicholibeba umbo lake lote.
Wakati huo alikuwa ndiyo kwanza amemaliza kuoga, akawa akijitazama kwa kupitia kioo hicho kirefu. Akajipa asilimia mia moja kuwa ana umbo zuri na sura nzuri. Ni mwanamke anayeweza kumfanya mwanamume yeyote amsaliti mkewe.
“Sijui anakunywa bia?” aliendelea kunong'ona. “Kuna kijana wa kileo asiyekunywa bia, wine au whisky? Labda awe Mlokole au Mujahidina.”
Akacheka kwa sauti huku akijipapasa-papasa mapaja na kuyapigapiga kiasi cha kuyafanya yatetemeke. Akilini mwake aliamini kuwa hata kama Chris hanywi bia, kinywaji ambacho hudaiwa na watu wengi kuwa huwa na nguvu ya kuilegeza misimamo ya wasiopenda ngono, basi macho yake na umbo lake vitakuwa ni vigezo tosha katika kumchanganya mwanamume huyo.
Kuhusu uzuri wa umbo lake, Salma hakuwa na shaka. Mara kadhaa aliwafumania wanaume wakimtazama kwa matamanio ilipotokea siku hiyo akawa amevaa suruali ya kitambaa chepesi, iliyomshika vilivyo maungoni au gauni lisilompwaya.
Mbinuko wa makalio yake makubwa na unene wa mapaja ulitosha kuwafanya baadhi ya wasiovumilia kwa macho wamtupie maneno mawili, matatu na ahadi kochokocho. Yeye hakuwa mtu wa kudanganywa kwa ahadi ya pesa au zawadi nyingine yoyote, na wala hakuwa mtu wa kurubunika kwa sifa za uzuri wa sura na umbo lake.
Hayo hayakuwa mambo yenye faida yoyote kwake. Alihitaji mwanamume, lakini pia alihitaji mwanamume mwenye mvuto na sio wingi wa pesa au mali zake. Chris alikuwa miongoni mwa wanaume aliowahitaji, hivyo hakuwa tayari kumpoteza. ‘Nikimkosa leo, basi labda mie sio mwanamke, mie sio Salma.’
**********
SAA 10:30 jioni ilimkuta Chris akitoka bafuni kuoga. Akaingia chumbani mwake ambako alichagua suti nyingine, suti ambayo thamani yake haikutofautiana sana na ile aliyovaa asubuhi. Tofauti ilikuwa ni rangi tu; ile ya asubuhi ilikuwa ni ya bluu, hii ilikuwa ya kijivu. Akaitwaa pochi na kuangalia kiasi cha fedha zilizomo.
“Hazitoshi,” alinong'ona baada ya kubaini kuwa kulikuwa na shilingi 30,000 tu. Akaifungua saraka moja ya kabati ambamo kulikuwa na pesa kiasi cha shilingi 600,000. Akachukua 300,000/= tu na kuzipachika ndani ya hiyo pochi yake. Sasa akajiona amekamilika!
“Iweje mtu uvae suti ya zaidi ya laki mbili halafu mfukoni huna hata alfu hamsini?” alijiuliza huku akianza kutoka.
Baada ya kupita mitaa michache akaibukia kituo cha daladala cha Mwembejini. Pale teksi hazikosekani, na kwa jinsi alivyokuwa mtanashati, madereva teksi walianza 'kujigongagonga.'
“Teksi, mzee,” dereva mmoja alimwambia.
“Twende, mjomba...” mwingine alimpigia kelele.
“Anko, teksi hizo mbovu, njoo hapa mjomba! Hii imetoka kwa mama juzi tu,” mwingine 'alijifagilia.'
Wote hao hakuwajali. Aliifuata teksi nyingine iliyoendeshwa na kijana mmoja waliyeishi mtaa mmoja. “Moze, twende Kariakoo,” alimwambia. Dakika iliyofuata teksi hiyo ilikuwa ikisaga lami.
“Ni mtaa gani?” Moze alimuuliza Chris wakati walipofika kwenye makutano ya Barabara za Umoja wa Mataifa, Morogoro na Swahili. Walikuwa wakisubiri ruhusa ya taa za Usalama Barabarani.
“Mtaa wa Rufiji,” Chris alijibu. Kisha akamkazia macho na kumuuliza,
“Unaufahamu mtaa wenyewe?”
“Hakuna mtaa unaonipa shida hapa Kariakoo, Chris,” Moze alijibu kwa kujiamini. “Labda ingekuwa ni mitaa ya Buguruni au Mbagala.”
Taa zilipowaruhusu, Moze akauvaa Mtaa wa Swahili kisha huko mbele akaupata Mtaa wa Rufiji.
“Kulia au kushoto?” alimtupia tena swali Chris huku akipunguza mwendo.
“Hapahapa panatosha,” Chris alijibu baada ya kukiona kibati kando ya barabara kilichoandikwa maandishi ya herufi kubwa: RUFIJI STREET.
Muda mfupi baadaye alikuwa akipita katika Mtaa wa Rufiji huku akiangaza macho kwenye milango ya nyumba moja baada ya nyingine, za kulia na kushoto.
Hakupenda kupiga simu japo namba alikuwa nayo. Alitaka kwanza kuhakikisha kuwa anaipata nyumba hiyo kwanza.
Hatimaye aliifikia nyumba iliyokuwa na namba T 16 PPK, mlangoni. Ilikuwa ni nyumba iliyojengwa kisasa na ilivutia mtaani hapo. Ukuta ulipakwa rangi nyekundu na geti lilikuwa jeusi. Paa lake lilikuwa la vigae. Chris alisimama akijiuliza kama abishe hodi au aache na arudi zake alikotoka.
Wakati huo alikuwa akijilaumu kwa kutokujua kama Salma anaweza kuwa na mwanamume huko ndani au la. Hakutaka kuiamini taarifa ya yule fundi viatu wa kule nje ya jengo la Wizara ya Fedha, kuwa hawara yake huwa safarini mara kwa mara. Hapana, hilo hakulipa nafasi kichwani mwake hata kidogo.
Kama karudi jana? Na kama yupo, hatajenga hisia za 'kuibiwa' mke? Kauli ya Salama eti bwana wake “ana mambo ya kizungu.... hana mawazo ya kijingajinga” haikuwa ni kauli ya kumfanya Chris abweteke.
Alizijua hasira na uchungu anaokuwa nao mtu anayemgundua 'mwizi' wa mke wake, tena mtu mwenyewe awe kama huyo Mpemba wa Salma, Mpemba mwenye pesa kama mchanga! Abdulrahman Sadick!
Mwenye pesa za kutakata ana kiburi na hujiamini kwa kiwango cha juu. Hilo, hata Chris alilitambua fika. Mwenye pesa anaweza kushindilia risasi kwenye kifua cha mtu, na kwa kutumia pesa, kesi dhidi yake ikayeyuka siku kadhaa baada ya kufunguliwa kwa jalada la kesi ya mauaji. Kuuawa na hawara yake Salma ni jambo ambalo Chris alilihisi, na hakupenda limkute.
Lakini, je, abatilishe dhamira yake wakati tayari yuko nje ya geti? Hapana, kwa hilo moyo wake haukumkubalia. Akapiga moyo konde na kulisogelea geti. Akabonyeza kengele. Muda mfupi baadaye akasikia vishindo vyepesi vya mtu akisogea getini.
Kisha geti likafunguliwa. Mbele yake alisimama Salma, akiwa ndani ya vazi moja tu, kanga aliyojifunga kifuani.
“Karibu,” Salma alisema huku akimtazama na tabasamu changa likichanua usoni pake. Kisha akasogea pembeni na kumwashiria kwa mkono apite ndani.
“Asante,” Chris alijibu kwa sauti isiyokuwa ya kujiamini. Akaingia kwa hatua za asteaste kisha akamsubiri mwenyeji wake. Salma akafunga geti na kutangulia kwenda ndani, akitembea kwa madaha, akijua fika kuwa Chris atayagandisha macho kwenye umbo lake ambalo kwa wakati huo, zaidi ya hiyo kanga iliyousitiri mwili wake, hakukuwa na nguo nyingine huko ndani.
Hatimaye walitinga sebuleni. Chris akaketi katika sofa lililokuwa jirani na mlango. Akaanza kuikagua sebule hiyo kubwa kwa macho.
Kwa jumla ilikuwa ni sebule iliyovutia. Kulikuwa na seti mbili za masofa zilizopangwa vizuri na pia kulikuwa na meza mbili, moja ikiwa ni maalumu kwa maakuli na hiyo ikiwa imezungukwa na viti sita na nyingine ndogo ilikuwa katikati ya sebule.
Pia kulikuwa na kabati mbili kubwa, moja ilisheheni vyombo vya kauri na nyingine ilikuwa imefurika majarida na vitabu vya aina mbalimbali. Televisheni kubwa na deki ya video vilikuwa juu ya kimeza chake maalumu pembezoni mwa sebule na kuongeza unadhifu wa chumba hicho.
Sakafu ilifunikwa na zulia jekundu lenye mvuto mkubwa kiasi cha kumfanya yeyote aingiaye humo ajenge imani kuwa kaingia ndani ya nyumba ya mtu aishiye maisha yasiyo ya kubahatisha. Ubaridi wa wastani uliosababishwa na kiyoyozi kilichojengwa ukutani ilikuwa ni burudani nyingine ndani humo.
Kwa msimu huo ambao Jiji la Dar es Salaam liligubikwa na joto kali, ukiingia ndani ya nyumba hiyo hutataka kutoka. Kwa jumla ilikuwa ni sebule iliyotimia kwa maisha bora ya binadamu apendaye maisha bora.
“Hapa nd'o nyumbani, Mr. Chris,” Salma alisema huku akijipweteka katika sofa aliloketi Chris, sofa lililotosha kuwaketisha watu watatu wenye miili mikubwa.
“Nashukuru kupafahamu. Vipi, uko peke yako?”
“Kwa nini?” Salma alimtazama usoni huku bado lile tabasamu lake jepesi likichanua.
“Naona kuna ukimya sana,” Chris alisema huku akiangaza macho pande zote za sebule hiyo. “Au mzee kapumzika?”
Kicheko cha wastani kikamtoka Salma. Kisha akasema, “Kwa kweli niko peke yangu...”
“Haiwezekani! Si uliniambia kuwa una mista, ila mista mwenyewe hana noma, mambo yake ni ya kizungu?”
“Ukaniamini?”
“Kwa nini nisikuamini?”
“Basi ukweli ni kwamba niko single,” Salma alisema kwa msisitizo, akimtazama Chris kwa namna iliyoonyesha kuwa mzaha uko kando.
“Hapana, Salma. Haiwezekani.”
“Kha! Kwa nini isiwezekane?”
“Kwa jinsi unavyoonyesha.”
“Kwa jinsi ninavyoonyesha? Kwani nikoje?”
“U mzuri zaidi ya wazuri.”
Salma alibibitua midomo, akasonya kisha akampiga Chris kijikofi chepesi cha begani. “U'shawaona wangapi wazuri?”
“Wengi! Nadhani ni zaidi ya mia moja.”
“Kati ya hao zaidi ya mia moja, wangapi walikuwa ni ma-girl friend wako?”
“Hata mmoja!” Chris aliruka kimanga. “Mi' huwa ni mtu wa kuifurahisha nafsi kwa kutazama tu.”
Salma aliguna. Kisha akauliza, “Ya kweli hayo?”
“Kwa nini nikudanganye, Salma?”
“Unataka kun'ambia kuwa tangu uzaliwe hujawahi kuwa na demu?” Salma alimbana, safari hii akimtazama kwa macho makali zaidi, akionyesha kutomwamini.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“S’o hivyo,” Chris alijibu. “Lakini huwa sina hulka na mambo hayo.”
“Umeoa?”
Lilikuwa ni swali ambalo Chris hakulitarajia, hivyo hakuweza kulipata jibu lake mapema. Alifikiri kama ingempasa kuongopa au kutoa jibu la kweli. Hata hivyo, baada ya kufikiri kidogo akaona hakuna haja ya kuongopa. “Kwa kweli sijaoa,” alisema.
“Hujaoa? Unasubiri nini?”
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment