Search This Blog

Saturday, 5 November 2022

EPA - 2

 








Simulizi : EPA

Sehemu Ya Pili (2)





“Kuna mambo yananitatiza Frank. Funguo za hazina umekuja nazo?!”

“Ndiyo, nisingeweza kusahau!”

“Vizuri! Twende hazina mara moja!”

Wakainuka na kuelekea hazina, kule zinakohifadhiwa fedha za aina zote. Za Tanzania kwa za kigeni ikiwa ni pamoja na vito vya thamani na madini ya dhahabu, almasi, tanzanite, rubi na vingine vingi. Wakaendelea kupita wakikagua hapa na pale.

Kutahamaki wakawa wamefika katika vile vyumba vyenye ukubwa wa kutisha vinavyohifadhi fedha za akaunti ya madeni ya nje. Ingawa kulikuwa na fedha za kutosha, lakini pengo la fedha zilizochukuliwa kugharamia uchaguzi pamoja na zile zilizochukuliwa na Tarish muda mfupi uliopita, lilionekana waziwazi.

“Bosi wenyewe wameanza kulipwa nini?” Alikuwa Frank kwa bashasha. Kila mtu alimzoea Frank kwa kuwa alikuwa mtu wa aliyependa mzaha na ucheshi sana.

“Hapana!” Akajibu Mhasibu kwa sauti nzito na kuongeza “Nyingi zimetumika kugharamia kampeni za Chaguo!”

“Amah!” Frank akaachama, sura yake ikakunjuka huku mzaha akiweka kando, akaendelea, “Sasa tukiulizwa tutasemaje? Au una majibu ya kutosha?”

“Majibu yatoke wapi Frank, hawa jamaa wanatutafutia balaa!”

“Sasa tutafanyaje bosi?”

“Nitajua la kufanya. We subiri tu!” Akajibu.

Wakapita hapa na pale na wakikagua hiki na kile mpaka walipotosheka na kutoka hazina. Akamuonya Frank kutosema chochote, kabla hajamuaga na kuondoka. Safari yake iliishia Bar ya New Africa Hotel alikofika anakunywa pombe za haja bila kulewa. Alipokinaishwa na pombe alirudi nyumbani kwake alikopokelewa na mkewe.

Mezani kukiwa na chakula cha haja, Mhasibu alijikuta akishindwa kula chochote jambo ambalo mkewe lilimshangaza sana. Naam, haikuwa kawaida ajikunje kumpikia pilau la kuku limshinde Mhasibu kula. Pilau kilikuwa chakula kilichopendwa sana na Mhasibu.

Maswali machache aliyomuhoji yakampa majibu kuwa hakuwa akijisikia vizuri. Ushauri wa kenda hospitali? Akasema atakwenda kesho. Alipotaka kumwita daktari wa familia, Mhasibu akamkataza pia. Basi ilimradi tu kila aliloshauri, Mhasibu alilikataa au kulitolea hila.

Mwishowe wakakikabili chumba na kupumzika pale usiku ulipoanza kuonyesha dalili za kukomaa.

Chumbani, mkewe alimnyemelea na kuanza utundu kama ilivyo ada yake lakini leo hakupata kile alichokitaka. Vurugu zilipozidi, Mhasibu akalazimika kumkidhia mkewe haja zake na alipohakikisha mkewe ametosheka yeye akageukia upande wa pili na kumuacha mkewe akikoroma.

Masaa yakajongea taratibu akiwa hajatungua japo lepe la usingizi. Kichwa kilimuuma na mawazo ya ajabu kumnyemelea. “Hii Haikubaliki!” Akaropoka.

“Kitu gani hakikubaliki? Au sijakufurahisha mume wangu?!” Alikuwa mkewe Nadia kwa upendo. Machozi yakianza kutafuta njia katika kingo za macho yake. Upesi Mhasibu ambaye alijua mkewe amelala, akatahayari. Akamgeukia na kumkumbatia mkewe huku akimtaka radhi na kumfariji.

“Ooh! Samahani mpenzi wangu! Sijakulenga wewe kabisa. Haki ya Mungu nakuapia!” Akasema baadae.

“Mume wangu?”

“Naam!”

“Una nini lakini?! Huelekei kuwa Jamaldin ninayemjua mimi. Huyu wa leo kama amemeza kaa la moto. Mbona unataka kuniweka roho juu juu mwana wa mwenzio?”

“Kwa nini laaziz?” Ikawa swali juu ya swali.

“Tangu umefika hali yako sio kabisa, nakuona tu kuwa kuna kitu hakiko sawa akilini mwako. Hata nilipokuja ‘kukutembelea’ usiku ni kama nilikulazimisha tu, kuna tatizo gani?”

“Hakuna tatizo!”

“Hutaki kuniambia? Huniamini?!”

“Sio hivyo mke wangu, ni kweli kuna jambo linanitatiza, ila sijajua ni jambo gani. Naomba unipe muda nilitafakari na nikilijua nitakuambia tu!”

“Kweli?”

“Kweli kabisa!”

“Pole!”

“Asante!”

Wakalala tena, Mhasibu akijitahidi kutoacha mawazo yamteke na kumfanya atamke kitu bila ridhaa yake, kitu ambacho kinaweza kuzusha hali ya kutoelewana na mkewe. Akamshukuru Mungu kwa kuwa mkewe alikuwa muelewa na mwenye upendo wa hali ya juu.

Asubuhi pia chakula kilimshinda kula, akadonoa donoa na kuondoka huku mkewe akimsisitiza kuwa asisahau kwenda kumuona daktari wao wa familia, Dokta Musa Malilo. Mhasibu alimuitikia tu kumridhisha. Moyoni akijua tatizo lake lilihitaji jambo jingine zito na sio daktari wa Afya.

Ofisini alifanya kazi kidogo sana. Muda mrefu aliutumia kwa kupiga simu hizi na zile. Mengi ya majibu aliyoyapata katika simu zile, yalikuwa mazuri. Jambo ambalo lilifanya tabasamu lake ambalo siku nzima ya jana halikuweza kuutembelea uso huo, sasa lianze kuwa rafiki. Wakati anajiandaa kuchukua hatua, akawa amepokea tena yule mgeni wa jana.

Ilionekana jamaa wamedhamiria kuchukua fedha kila simu mpaka ziishe.

“Kuna kiwango hiki kinatakiwa tena!”

“Mara hii? Ni jana tu ume...!” Akajibu kwa karaha.

“Jana tulisahau kujumlisha na hizi za leo!” Tarish akamkata kalima.

“Kwa hiyo zinatakiwa lini?”

“Immediately ndugu. Si unajua kazi zetu! Nimekuja na gari kabisa. We fanya taratibu zinazohusika, mie ntakuwa tayari kusubiri hapa hapa hata ikibidi kusubiri mwaka mzima, nitasubiri!”

Mhasibu akajivuta dirishani na kuangalia nje. Scania Double Semitraller lilionekana limepaki. Akauma meno kwa uchungu. Akaziinamia zile karatasi na kusaini tena kwa moyo mzito kabisa. Saini iliyofuatiwa na simu mbili tatu zilizotoka nje ya eneo lile, kabla msaidizi wake hajaagizwa mahala kuchukua barua nyingine ya kuidhinisha kutoka kwa wakubwa zaidi.

Sekunde chache baadae baada ya barua hiyo kupokelewa, mabox kwa mabox ya fedha yalianza kutolewa hazina na kupakiwa katika lile Semitraller. Gari lilipojaa na kuondoka, Mhasibu akaghadhibika na kuipiga kompyuta konde zito. Ikaanguka chini na kuvunjika.

“Aargh! This is too much! Too much!” Akabweka. Hali iliyomfanya Mainuna aingie mbio humo ndani na kuuliza kulikoni. Dk. Mhasibu akamfukuza haraka. Alipoondoka yeye akazunguka nyuma ya meza yake na kujiinamaia. ‘No Mhasibu!’ Mawazo yake yakamwambia. ‘Cool down my friend, Cool down! Mtu thabiti hatakiwi kuwa hivyo, Jidhibiti!’

“Roho inauma lakini!” Akajibu kwa sauti.

‘Najua!’ Mawazo yakamwambia tena na kuongeza, ‘Kila mmoja lazima angeumwa na roho. Take care, Jazba huondoa maarifa akili na ufahamu. Just Cool down Mhasibu!’

“Oke oke okey!” Akajijibu akiinuka na kuokota masalia ya kompyuta yake, akayaweka mezani na kurudi katika kiti chake, akaketi. Koo likamkauka ghafla, akainuka tena na kulikabili friji dogo lililokuwa humo ofisini, akaufungua mlango wake na kutoa chupa moja ya maji baridi, akaifungua na kuipeleka mdomoni. Akayagugumia maji yote yaliyokuwa katika ile chupa ya maji ya nusu lita mpaka ilipokwisha. Akaitua chini na kurudi tena katika kiti chake.

Akamwita Maimuna na kumtaka aondoe ile kompyuta mpakato iliyokumbwa na zahama na kumletea nyingine baada ya kuwa amewasiliana na fundi atakayehamisha data zote kutoka katika komyuta iliyoharibika kuja katika nzima.

Dakika nyingi baadae alipohisi akili yake imetulia alirudi katika simu tena na kupiga mahala. Simu ikapokelewa na yule yule aliyemuhitaji, ambaye tayari alikuwa amezungumza naye kiasi cha kutosha. Mtaalamu wa teknolojia ya habari na mawasiliano (IT) wa pale Benki kuu.

“Naomba unishauri kama tunaweza kubadilisha mipango haraka iwezekanavyo! Huu ni ushenzi wanaotaka kunifanyia. Na mimi siwezi kukubali kufanyiwa ukhabithi!” Akasema simuni mfululizo bila kupumua.

“Kwani wewe ulikuwa unatakaje?” Akaulizwa kwa upole.

Mhasibu akatabasamu kwa swali hili. Ule upole wa aliyemuuliza swali ukamfanya ajione ni kiasi gani alikuwa akitumia nguvu nyingi kuzungumza hili kwa mtu ambaye hakuona kama kuna tatizo la haja. Ni hili lililomfanya arekebishe sauti yake na kurudi kuzungumza katika hali ya kawaida.

Halafu akachukua muda wa kutosha kumueleza lile ambalo alikuwa analitarajia ili kuikomesha hali hii. Alipomaliza aliona kama vile ametua mzigo mzito.

“Mbona hiyo haina shida, nilishakwambia hilo kwangu sio tatizo kabisa!”

“Kwa hiyo inawezekana!”

“Kwa asilimia mia moja! Ni wewe tu kusema unataka suala hili lifanyike lini”

“Nataka lifanyike leo hii hii!”

“Hakuna shida bosi wewe tu!”

“Ila naomba uniahidi jambo moja!”Mhasibu akaomba

“Jambo gani?”

“Kwamba taarifa hizi zitakuwa siri mpaka pale nitakapokamilisha mambo yangu!”

“Nakuahidi!”

“Asante!” Mhasibu akakata simu, uso wake ukirejewa na tabasamu upya. Tabasamu la furaha na matumaini. Tabasamu hili lilidumu kwa muda mpaka pale simu yake ilipotoa mlio wa kuingia kwa ujumbe mfupi wa maandishi. Ujumbe ambao ulimjulisha kitu kimoja muhimu. Kwamba kazi yake ilikuwa imeanza kufanywa na mtaalamu wake wa IT kwa hatua za awali. Akaunakili ujumbe ule mahala halafu akainua simu na kumwita Frank. Akamwambia,

“Fedha zote zilizobakia katika ile akaunti ya madeni ya nje ziwekwe katika mfumo wa electronical kisha zisambazwe katika mabenki mbalimbali kupitia akaunti hii!” Akasema akimkabidhi nambari fulani ya akaunti iliyokuwa katika karatasi na kuendelea “Ukimaliza jukumu hilo unijulishe!”





“Sawa bosi!”

“Halafu nilitaka kusahau, kesho natarajia kwenda Uswis, tafadhali niandalie safari na masurufu yangu haraka!”

“Mara hii bosi?!” Mshangao haukuacha kujitokeza usoni mwa Frank.

“Ni safari ya dharura ya kikazi. Natarajia kuwa huko kwa siku tatu hadi tano!”

“Sawa bosi!”

“Unaweza kwenda!”

Frank alipoondoka na yeye akainuka, funguo za gari mkononi, akamuaga Maimuna na kuondoka. Safari iliishia nyumbani kwake alikomkuta mwanae wa kike Shuwena, mwenye umri wa miaka ishirini na moja aliyekuwa akisoma Shule ya bweni Kijitonyama Sekondari kidato cha sita akiwa amekuja kuwasalimia.

“Oooh! Shuu mwanangu mpenzi, umekuja! Very Good!” Akasema akimkumbatia.

“Naam baba, Nimekuja kuwasalimia mara moja, nimewakumbuka mno. Wakati mwingine masomo yanachusha na kuudhi ati!”

“Usijali, ndio kawaida ya masomo mwanangu, soma kwa bidii, uumie na kulia leo. Lakini kesho utafurahia na kutabasamu. Vipi masomo, unayaonaje mama?”

“Ni mazuri mno Dady na Mungu akipenda wiki mbili zijazo tutanahitimu. Baada ya hapo nitakuwa na uwezo wa kuingia Chuo chochote kwa ajili ya kusomea uchumi ili mwisho wa siku niweze kumiliki shahada hiyo ninayoipenda kuliko kitu chochote kile. Kwa kila hali siwezi kuacha kuwashukuru wazazi wangu. Thanks a lot for those who were you done for me. I love u dad!”Alimalizia kwa lugha ya kiingereza akiwashukuru wazazi wake kwa yote waliyomfanyia.

“Never mind!”

Wakaachiana na kuzungumza hili na lile, mzazi akiuliza ya shule na binti akiuliza ya nyumbani. Baba alipotosheka akamtaka mtoto apumzike na yeye akaingia ndani.

“Mh! Kulikoni mbona leo mapema baba?!” Mke wake akamlaki kwa maswali.

“Sikujua kama siruhisiwi kuwahi nyumbani kwangu!”

“Kumradhi mume wangu, nilidhani kuna tatizo!”

“Hakuna, ofisini vurugu nyingi! Kuna jambo dogo nataka kulifanya hapa nyumbani, nahitaji utulivu!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Karibu!” Mkewe akahitimisha. Mhasibu akaingia ndani na kuanza kuyapangilia mambo yake. Muda mwingi alionekana akiwa ameiinamia kompyuta yake. Mara kadhaa akinakili mambo katika diary yake.

Wakati wakipata chakula cha mchana Mhasibu akamwambia mkewe.

“Kesho natarajia kwenda Uswis mara moja!”

“Umeanza, sikai na wewe tukafurahi. Kila mara safari, kazi, mikutano na mengine mengi. Kwa nini usikae na mwanao kidogo! Ndio kwanza amefika na ana mengi ya kuzungumza na sisi, nasi tuna mengi ya kumwambia. Au siyo?”

“Hilo ni kweli kabisa mama watoto!”

“Kwa hiyo utaahirisha?”

“Safari?!”

“Kumbe kitu gani kingine?”

“Hapana mke wangu. Safari hii ni muhimu kuliko safari zote na shughuli zote zilizotangulia! Kuliko safari zote nilizopata kuzifanya.”

“Kwa nini?”

“Inaamua mustakabali wa maisha yetu ya sasa na ya baadae!”

“Bado sijakuelewa!”

“Utanielewa tu, kuna lile jambo lililokuwa likininyima raha jana. Ndilo linalonifanya nisafiri!”

“Afadhali umenikumbusha!” Mkewe akaanza kwa shauku “Bado hujaniambia kilichokuwa kikikunyima raha!”

“Kulikuwa na matatizo ya kiutendaji ofisini ambayo yalikuwa yakitishia mie kufukuzwa kazi kama yasingepatiwa ufumbuzi!”

“Kwa hiyo ufumbuzi ndio upo huko Uswis?”

“Ndiyo, kuna kikao cha kujadili matatizo hayo ambacho kitafanyika keshokutwa, hivyo ni muhimu sana kuondoka!”

“Kama ni hivyo sawa!”

Ukapita ukimya mfupi, wakila chakula taratibu. Shuu hakuwa hapo, alikuwa amelala, pengine kufidia uchovu wa masomo yake huko shuleni. Ni hili lililowafanya wasimuamshe ili wajumuike pamoja kwa ajili ya mlo huo wa mchana.

“Kwa kuwa nimemkumbuka sana na sitaki nimuache, nimeamua kuwa nitaondoka na Shuwena!” Mhasibu akauvunja ukimya baadae. Mkewe akaacha kula na kumtazama kama ambaye hajamuelewa. Mhasibu akaongeza.

“Na pia kuna kazi kidogo nataka akanisaidie!”

“He! Hata hajapumzika! Baba Jamaldin jamani huna hata huruma?”

“Hatuchelewi sana, siku mbili au tatu tu zinatosha!”

“Kwa hiyo ni lazima sana kwenda naye?”

“Ndiyo, ni lazima sana!”

Ukimya mfupi ukapita Bi Nadia, mkewe Mhasibu na mama wa Shuwena binti wa Mhasibu akitafakari jambo. Kwake yeye hakuona mwanae Shuwena alikuwa na umuhimu kiasi gani katika kazi za kiofisi za mumewe. Hata hivyo kwa kuwa alikuwa akihofia kumkwaza mwenyewe, alijikuta akikubali kinyonge.

“Mie sina neno, mwenyewe akikubali, Sawa!”

“Nashukuru kwa kunielewa mke wangu, ndio maana nakupenda sana. Asante!”

“Mimi pia nakupenda!” Akajibu Nadia.

Wakaendelea kula huku ukimya ukiwa mfalme baina yao. Walipomaliza kula Mhasibu akamuomba radhi mkewe, akahamia katika ofisi yake ndogo ya hapo nyumbani na kuendelea na kazi, pengine zile alizoziacha ofisini. Mkewe akaenda nje kuendelea na kazi zingine za kifamilia, kabla hajaenda kupumzika.

Kufikia saa kumi na moja jioni ya siku hiyo, Frank alimpigia simu Mhasibu na kumjuza kila kitu. “Kazi nimemaliza Mkuu!” Akasema Frank simuni.

“Vizuri sana Frank. Na je” Akauliza Mhasibu, “tiketi umepata!”

“Ndiyo! Utaondoka na ndege ya kesho saa kumi na mbili asubuhi!”

“Asante sana. Naomba uniletee hiyo Flash yenye password na data zote! Halafu angalia uwezekano wa kupata nafasi nyingine moja zaidi katika ndege nitakayoondoka nayo kesho maana nitapenda kuondoka na mwanangu Shuwena!”

“Mwanao amerudi bosi? Nakumbuka uliniambia kama anasoma shule ya bweni vile, na huu sio wakati wa likizo. Kwema lakini?!”

“Ndiyo amerejea mara moja kuja kutusalimia, ameomba ruhusa ya siku chache shuleni. Nimeona sio vibaya nikiandama nae ili akasafishe macho ughaibuni!”

“Vizuri mkuu, nitafanya hivyo, naelewa ni kiasi gani unavyompenda mwanao. Worry not my Boss!”

“Nitashukuru na kufurahi sana!” Alikuwa Mhasibu tena.

“Ngoja nizungumze na Ubalozi wa Uswizi nione kama wanaweza kutupatia visa ya dharura kwa ajili ya Shuwena, maana wewe utatumia zile viza zetu za kidiplomasia!”

“Vizuri sana Frank, fanya hivyo. Waambie chochote kinachotakiwa ili tu, tusikwame. Sawa?”

“Sawa!”

“Nakutegemea Frank!”

“Shaka ondoa kiongozi. Je,” Frank akauliza tena “Kuna jambo la ziada mkuu?”

“Lipo! Masurufu yangu ya safari yaingize katika akaunti yangu ya familia, sawa?”

“Sawa!”

“Kazi njema!”

“Kwako pia!” Wakaagana.

Mhasibu aliendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa umakini mkubwa mpaka pale Frank alipompigia simu masaa mengi baadae na kumwambia kuwa kila kitu kilikuwa sawa, kwamba visa kwa ajili ya Shuwena ilikuwa imepatikana na tiketi pia.

Simu hii ndiyo iliyomfanya aisitishe kazi aliyokuwa akiifanya, akaingia chumbani na kulala. Hii ilikuwa baada ya kumtaka Frank amalizie majukumu muhimu yaliyokuwa yamebakia wakati yeye atakapokuwa safarini. Jambo ambalo Frank alilikubali.



Sura ya Tatu

Asubuhi na mapema ya siku iliyofuata iliwakuta uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kwa kuwa taratibu za wakati huu hazikuruhusu watu kwenda kukaa waving bay kutokana na tishio la ugaidi, Nadia alimkumbatia mumewe kwa mapenzi makuu akiumia kutengana na mwanaume huyu aliyempenda kupita kiasi.

“Baki salama mke wangu, nitakukumbuka sana!” Akasema Mhasibu

“Mimi pia Laaziz. Uende salama urudi salama, uje tufurahie maisha!”

“Amina!”

Nadia akajitoa mikononi mwa mumewe na kumkumbatia binti yake kwa mapenzi mazito, akimuaga na kumtakia safari njema. Alipohisi huzuni inataka kumzidi nguvu, upesi akamuachia, akawaaga na kuondoka.

Halafu wakapita hapa na pale katika vitengo mbalimbali hapo uwanjani wakikaguliwa hiki na kuulizwa kile huku wakiulizwa maswali haya na yale. Kutahamaki walikuwa katika eneo la kusubiria ndege baada ya taratibu zote kukamilika na wao kupatiwa boarding pass.

Dakika chache baadae walikuwa hewani ndani ya ndege ya British Airways wakielea kuelekea Uswis. Wakiwa wamesafiri kwa daraja la kwanza, walipewa huduma za kila namna mpaka wakajikuta wakiifurahia safari hiyo ndefu. Hata hivyo hii haikuwa sababu ya kumfanya Shuwena aliyekuwa na maswali mengi kuliko majibu ashindwe kumuuliza baba yake.

“Lakini dady!” Shuwena akaanza “Mbona safari imekuwa ya ghafla hivi?”

“Imenilazimu mama. Muda ukifika utajua tu!

“Muda wa nini?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Muda wa mimi kukuleza kila kitu, kwa sasa bado ni mapema sana!”

“Huniamini Dady!”

“Nisipokuamini wewe, ntamuamini nani tena Shuwena?! Yote niyafanyao ni kwa ajili yenu wanangu na familia yangu. Nakupenda sana Shuu, nakupenda mno Shuwena! Vumilia kidogo tu utajua kila kitu. Sawa!”

“Sawa!” Shuwena akakubali kwa moyo mkunjufu. Safari ikaendelea.

Baada ya tua tua ya hapa na pale, hatimaye walitua salama salimini katika uwanja wa kimataifa wa Swiss International Airport na kupokelewa na mwenyeji wao, Mr. Henri Comte.





“Karibuni sana!” Akasema Comte kwa lugha ya kiingereza jicho lake likiwa kwa Shuwena.

“Asante sana!” Mhasibu na mwanae wakajibu kwa kiingereza pia.

“Hongera, mwanao mzuri sana!” Comte akashindwa kuvumilia. Shuwena akatazama chini kwa aibu. Mhasibu akaishia kukenua tu, moyoni akianza kumchukia mtu huyu aliyeanza kuonyesha tamaa za kifisifisi kwa mwanae kipenzi.

“Jisikieni mko nyumbani!” Henri Comte akaongeza tena.

“Ahsante sana, Ahsante!”Mhasibu na mwanae wakazidi kushukuru.

Kilichofuata ni kujipakia ndani ya gari ambalo lilianza kukata mitaa hii kwa ile ndani ya jiji lile zuri la Geneva mpaka walipojikuta wakisimama mbele ya jengo lililoandikwa Schweizerische National Bank. Naam hii ilikuwa miongoni mwa benki kubwa na mashuhuri za hapo Uswisi ambapo watu kutoka mataifa mbalimbali ndani na nje ya bara la Ulaya na Amerika, walikuwa wakija kuhifadhi fedha au amana zao.

Jengo lake zuri lililojengwa kwa mchanganyiko adhimu wa mawe na sementi imara liliongeza unadhifu wa jengo hilo lililokuwa katika moja ya mtaa maarufu wa hapo Uswis na kulifanya lionekane kama sehemu ya majumba ya Makumbusho ya nchi hiyo. Mhasibu na mwanawe Shuwena walipowasili katika jengo hili walilakiwa kama waheshimiwa na kuhudumiwa kama wafalme.

Shuwena akaachwa katika korido ya jengo hilo kulikuwa na sofa za kuvutia akisoma kitabu cha Riwaya, Mapenzi Yamelogwa. Baba yake akaingia ndani zaidi alikochukua muda wa kutosha. Dakika chache baadae Henri Comte akaja na kumchukua Shuwena, wakaingia ndani kule kule alikokuwa mzee wake. Walimkuta amekaa katika sofa jingine zuri maradufu akinywa juisi adimu na aghali ya mastafeli, hali mkononi akiwa na gazeti, Daily Mirror la Uingereza.

“Ndiyo huyu bila shaka!” Yule mtu aliyekuwa jirani na baba yake akamuuliza Mhasibu.

“Ndiyo yeye, anaitwa Shuwena Jamaldin. Ni binti wangu wa kwanza. Ana mdogo wake aitwaye Jamaldin ambaye angali anasoma shule ya msingi katika shule moja ya bweni kule Arusha!” Akajibu.

“Vizuri!” Akajibu yule mzee na kumgeukia Shuwena. “Karibu sana binti, pole na safari!”

“Asante, nimekwishapoa!” Akashukuru na kusalimia pia.

“Shuwena!” Mhasibu akamgeukia mwanawe na kumwangalia usoni. Shuwena akakaa tayari tayari. Mhasibu akaendelea “Kutana na Mr Rossy Nicollier, yeye ni Meneja wa Benki hii na ndiye hasa tuliyemfuata!”

“Nashukuru kumfahamu!” Alikuwa Shuwena akishoosha mkono wakasalimiana na Rossy.

Dakika hiyo hiyo akaingia kijana mwingine wa kizungu akiwa na makaratasi kadhaa mkononi na kamera ndogo ya dijitali. Akawekwa vizuri na kupigwa picha kadhaa huku mara kwa mara akionyeshwa jinsi zilivyotoka na kuambiwa achague ile anayoipenda zaidi. Zoezi hili lilipokwisha akapewa yale makaratasi ayasaini.

Shuwena akajikuta akishindwa kuvumilia, akamgeukia baba yake na kumtazama kwa mshangao kama anayemuuliza kulikoni baba. Baba yake akamuelewa haraka na na kumwambia “Do it my Doughter. Ni kwa ajili yetu!”

Bila kusoma zile karatasi, Shuwena akakamata kalamu na kusaini karatasi zile zilizokuwa na wingi wa wastani. Mshangao wake haukuishia hapo, akachukuliwa pia na alama za vidole vya mkononi ‘finger print’ na kufanya mengine yote aliyoelekezwa na wale wazungu kwa shinikizo kama sio ushawishi wa baba yake. Kutahamaki wakawa wamemaliza na kutoka.

Jioni wakiwa hotelini kwao, Zurich in Piramid Golf Resort baada ya kumaliza matembezi mafupi ya kutembea hapa na pale katika jiji hili maarufu la Uswis, Shuwena alimbana baba yake amueleze kulikoni kufanya mambo yaliyomuacha gizani.

“Nakupenda sana mwanangu!” Mhasibu alianza hivi makusudi. Hii ni kwa kuwa kila alipokuwa akimwambia mwanae kuwa anampenda, upinzani au hoja kutoka kwa mwanae Shuwena zilipungua au kukosa nguvu. Akaendelea.

“Hujui hali inayotuzunguka mwanangu. Kwa kuwa wewe ni binti yangu mkubwa na wa pekee, nimeamua uwe mrithi wa mali zangu zote. Natumai hutamtupa mdogo wako Jamaldin!”

“Sitamtupa baba, sitamtupa yeyote katika familia yetu!” Akasema na kuendelea “Hata hivyo bado natatanishwa na matendo haya baba. Kwa nini unanirithisha haraka hivi? Kwani umegundua kuwa unakufa karibuni?!”

“Hapana!”

“Sasa...?”

“Nafanya maandalizi tu ili nikifa msipate taabu. Halafu... halafu... Ooh! Usijali mwanangu!”

“Lakini baba...!” Shuwena hakuelewa hata kidogo.

“Najua mwanangu!” Baba yake akamkata kalima. “Najua kila unachowaza na kufikiria. Mimi pia ningewaza au kufikiria hivyo hivyo. Ila ondoa hofu kwangu, mimi ni baba yako na siwezi kukuingiza sehemu mbaya. Na usidhani ni wewe tu usiyejua, mama yako na Jamaldin pia hawajui na naomba uniahidi kwamba jambo hili utalifanya kuwa la siri baina yetu wawili tu. Sawa!”

“Sawa!” Alikuwa Shuwena kwa moyo mzito.

“Good Shuwena, Very Good mwanangu!” Baba akapongeza akiinuka na kumkumbatia mwanae. Ikawa mwisho wa mjadala. Siku ya pili wakaamkia kule benki tena ambako Mhasibu alizungumza na watu wake kule ndani, akimuacha Shuwena akiendelea kusoma kitabu chake cha Mapenzi Yamelogwa.

Kulingana na maswali na hofu za Shuwena, Mhasibu akawa amewaamuru wale jamaa kufanya jambo moja zaidi. Kitu ambacho walikifanya kwa ukamilifu wake.

Mpaka wanamaliza kazi waliyopewa, Mhasibu alikuwa bado amelisahau tabasamu lake zuri usoni mwake. Wakaagana na watu wale na kuondoka kurejea hotelini kwao. Jioni ya siku ile Mhasibu alimkabidhi Shuwena kadi ndogo ngumu ya rangi ya dhahabu. Kadi ile ilifanana na zile kadi za ATM. Hii ikiwa na sura na jina lake.

“Hizi ni fedha zako tulizozihifadhi huku!” Akamwambia.

“Waaooo!” Shuwena akasema akitabasamu, huku akiigeuza kadi ile mbele na nyuma.

“Ina kiasi gani?”

“Fedha nyingi tu!”

“Jamani Daddy, how much sasa!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Mhasibu akafunua Briefcase lake na kuchomoa karatasi moja bank statement, akamkabidhi Shuwena. Shuwena akaipokea kwa pupa na kuingalia. Kulikuwa na dola elfu hamsini na mbili. Kama milioni mia moja na ushei hivi. Machozi ya furaha na kutoamini yakamlenga lenga Shuwena, kwake zilikuwa fedha nyingi sana.

Akajikuta akiwa hajui afanye nini kati ya kulia kwa au kucheka kwa furaha na kushangilia kwa nguvu. Hatimaye alijikuta akiinuka na kumkumbatia baba yake kwa nguvu zake zote huku akimwambia kwa sauti ya kunong’ona. “Asante baba, asante sana baba yangu, Thank you very much!”

“Usijali mama!” Mhasibu alijibu akimpigapiga mgongoni kwa vikofi hafifu vya upendo. Akaendelea kusema “Kitu kimoja tu nakuasa, usiri! Jambo hili ni siri, niahidi kama hutalisema sio tu hadharani, bali kwa yeyote yule. Niahidi!”

“Nakuahidi baba!”

“Asante, naomba uitunze na kuilinda ahadi yako!”

“Nakuahidi!”

“Very good Shuwena, sasa tunaweza kula!”

Wakala huku furaha na bashasha zikiwa zimezipamba sura zao!

Siku ya pili asubuhi walipita mjini na kufanya shopping ya maana ambapo walinunua vitu mbalimbali kwa ajili yao, familia yao na watu wengine wanaowazunguka. Jioni ya siku hiyo walikuwa hewani wakirejea nyumbani.

Walipokelewa vizuri na mkewe na ndugu wengine, msafara ukaishia nyumbani ambako kulikuwa kama na kitafrija kidogo kutoka na jinsi nyumba ilivyoandaliwa kwa mapambo, chakula na muziki.

Wakati watu wakila, kunywa na kucheza huku zawadi mbalimbali zikigawiwa kwa watu mbalimbali, Mhasibu aliitoroka familia yake kwa muda, akaingia ofisini kwake ambapo alifanya mambo fulani fulani, kisha akaingia chumbani kwa Shuwena na kufanya jambo jingine pia kwa siri.

Aliporudi sebuleni tafrija ilikuwa ikiendelea, ile bendi ya muziki wa dansi Doble M Sound chini ya Mwinjuma Muumini ‘Kocha wa dunia’; iliyoalikwa kupiga muziki laivu, ikiendelea kuwatumbuiza na kuufanya uhai wa pale uzidi kushamiri.

Kila mmoja alifurahi kupita kiasi. Waliendelea kula, kunywa na kufurahia mpaka usiku ulipoingia ambapo waliingia vyumbani mwao na kuimaliza siku. Ile furaha ya kila mmoja, pamoja na zile zawadi bora kabisa kutoka Uswiz, zikawa imemfanya mkewe asahau hata kuulizia matokeo ya safari yao.

Wakalala kila mmoja tabasamu likiwa limeupamba uso wake.

Aliporudi ofisini siku iliyofuata asubuhi, akajikuta akisuuzika na mtima wake. Frank alikuwa amefanya yote aliyomuagiza katika ubora uliomvutia. Akampigia simu na kumpongeza kabla na yeye hajaanza kufanya kazi alizoziacha kiporo ambazo zilikuwa zinamsubiri yeye tu azimalizie.

Maisha yakaendelea kuwa mazuri na ya furaha.



* * *

Siku hii akawa amepokea tena yule mgeni wake wa ajabu. Tarish Michael Bagula. Kama kawaida yake alikuwa katika suti nzuri ya Samawati iliyompendeza vilivyo, akiwa na mkoba mdogo wa kisasa, ile miwani ikiongeza unadhifu usoni mwake.

Akitenda vile ambavyo hutenda kila siku, baada ya salaam Tarish alijikaribisha kitini akafungua mkoba wake na kutoa nyaraka kadhaa akaziweka mezani kwa Mhasibu na kumwambia, “Tunahitaji kiasi hiki kuna kazi mahala!”

“Kazi gani?” Alikuwa Mhasibu kwa upole akiendelea kuchapa kazi kana kwamba hakuna aliyeingia hapo ofisini kwake.





“Umeanza lini kutaka kujua kazi zetu? Kazi zetu ni nyingi na kubwa kwa maslahi ya nchi. Kazi yako ni moja tu. Kuidhinisha fedha. Tafadhali niidhinishie niondoke!” Akatua.

Mhasibu akaendelea kufanya kazi kwa muda na alipotosheka akaisogeza Laptop yake pembeni, akaikutanisha mikono yake juu ya meza na kumtazama Tarish moja kwa moja usoni. Halafu kwa sauti ile ile ya upole na ya taratibu akasema.

“Nasikitika kukwambia kwamba fedha zimekwisha kabisa!”

“Eti?! Unasemaje wewe?” Tarish akajamba. Shuzi lililotoa mlio kama tarumbeta. Utaratibu, upole na kujiamini kwa Mhasibu kukimfanya aingiwe na hofu baridi. Moyo ukamzizima kwa muda asiamini anachokisikia.

“Eti unasemaje wewe?!” Akauliza tena.

“Fedha zimekwisha ndugu yangu!” Mhasibu akarudia tena.

“Ati nini?!!”

“We bwana ni kiziwi au kitu gani. Nimekwambia fedha ZI –ME-KWI-SHA!!”

“Lakini uliniambia fedha zingali nyingi. Uliniambia haziwezi kwisha mara moja. Haziwezi kwisha leo wala kesho, ulisema zitachukua miaka!”

“Na ulipokuja kuchukua na Semmitraller ulidhani zitaendelea kuwepo? Nimekwambia fedha zimekwisha, Finish!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Kwa dakika zingine kadhaa Tarish alibaki amemtumbulia macho Mhasibu hali hamuoni. “Hapana!” Akakataa taratibu kama anayeongea peke yake. “Fedha haziwezi kwisha kirahisi hivi, haziwezi kwisha mara moja. Nadhani unajaribu kutingisha kiberiti. Ila hujui tu sisi ni akina nani. Hujui tuna mamlaka na utashi kiasi gani! Sasa nasema hivi, idhinisha fedha niondoke!”

Wakati anayasema haya, tayari alikuwa ameshafungua mkoba wake na kutoa bastola yake nzuri aina ya Baretta iliyotengenezwa urusi. Akafanya kufungua usalama na kuijaribisha jaribisha. Mhasibu akabaki anamtazama tu.

“Hunielewi au kitu gani?” Akarudia kusema tena “Idhinisha fedha niondoke!”

“Nimekwambia fedha zimeisha ndugu!”

“Unajaribu kutucheza shere?!!”

Kimya.

“Unataka kuishi kwa furaha na amani?”

Kimya!

“Naongea na wewe!” Tarish akabweka na kuigonga meza kwa nguvu.

“Bwana, nimekwambia fedha zimekwisha! Usichoelewa ni kitu gani? Tafadhali ondoka nina kazi zingine!”

Tarish akashangazwa na ujasiri wa Mhasibu. Akamwambia taratibu kwa sauti nzito iliyohifadhi hasira kubwa.

“Hujui uzito wala madhara ya vitendo vyako Mhasibu Jamaldin. Wala hujui ni makaa kiasi gani ya moto unajipalia. Umeamua kuyatafuta matatizo badala ya kuacha matatizo yakutafute wewe. Mie naondoka, lakini utajuta. Tutayafanya maisha yako yawe magumu sana!”

Akamaliza akitoka na kuubamiza mlango kwa hasira nyuma yake. Mhasibu akashusha pumzi kwa matumaini. Akajivuta katika kompyuta yake na kuendelea kufanya kazi taratibu kwa utulivu mkubwa.



* * *



Kufikia saa kumi na nusu jioni ya siku hiyo, akili ya Mhasibu Jamaldin ilikuwa imechoka kiasi cha yeye kujikuta akifanya kazi bila ule ufanisi wake maridhawa ambao huwa unamvutia hata yeye kiasi cha kumfanya aihusudu kazi yake.

Mara kadhaa alifuta paragrafu hii na kuirekebisha ile katika ile taarifa aliyokuwa akiiandaa, hata hivyo baada ya dakika chache aligundua hana anachokifanya hapo na kama angeendelea kulazimisha, basi angejikuta anaiharibu na kuitia doa kazi hii nzuri ambayo alikuwa ameianza siku kadhaa zilizopita.

Akiwa anaijua vyema dawa ya uchovu wake, Mhasibu Jamaldin aliinua simu yake na kuomba aletewe kahawa chungu kavu, halafu akalifunga lile faili la kazi na kufungua faili jingine lililokuwa limehifadhi miziki ya zamani, akacheza kibao cha Mayasa kilichotungwa na gwiji wa muziki dansi Tanzania, Marijani Rajabu.

Dakika chache baadae kahawa yake iliingia, akaanza kuinywa taratibu. Pengine angeinywa kwa muda mrefu zaidi kama asingepokea simu hii kutoka nyumbani kwake ambayo mbali ya kumjulia hali na kumpa pole ya majukumu, ilimtaka asisahau kurejea nyumbani na kopo la maziwa ambayo nyumbani kwake yalikuwa yamekwisha.

Simu hii ndiyo iliyomfanya ajiulize kwa nini asiende kuimalizia kazi hiyo nyumbani kwake ambako pia angepata fursa ya kujumuika na familia yake na kufurahi nayo pamoja? Ni hili lililomfanya amalizie kahawa yake haraka haraka, halafu akaizima kompyuta yake ndogo na kuiweka katika mkoba, akainuka na kuondoka tayari kwa safari ya nyumbani kwake.

Alipolifikia eneo la maegesho ya magari, mlinzi wake Samson Kidude akaja na kumlaki ule mkoba kisha akauingiza ndani ya gari. Kisha akamfungulia mlango, Mhasibu akingia na kuketi huku wote wakifunga mikanda.

“Naona leo mapema sana mzee!” alikuwa Samson.

“Sio mapema Sam, inakimbilia saa kumi na moja sasa. Ila ni kweli leo nimewahi kutoka mapema ukilinganisha na siku nyingine!”

“Dereva wako yuko wapi?! Maana huwa hachezi mbali na gari hili!”

“Oh! My God. Hivi sijakwambia. Aliniambia ana dharura. Mama yake mdogo amefariki huko Urambo Tabora, hivyo nilimruhusu aende akazike na kuhani msiba huo!” Mhasibu akasema baadae na kuongeza. “Nadhani nawe unahitaji kupumzika Samson, nenda tu nyumbani tutaonana kesho asubuhi Mungu akipenda!”

“Oh! Asante sana mkuu. Ila si ningekufikisha kwanza nyumbani?!”

“Usijali, hakuna taabu. Kukiwa na tatizo nitakupigia!”

“Nashukuru bosi!” Samson alishukuru. Mhasibu Jamaldin akampa fedha kiasi kama nauli ili achukue taksi ya kumpeleka nyumbani kwake. Samson alipoondoka tu, naye akaitekenya stata ya gari, gari ikawaka kwa jino moja tu. Akaondoa breki na kuingiza gia kabla hajakanyaga mafuta. Gari ikatii na kuondoka, ikimpeleka kule alipopataka.

Kutoka katika ofisi yake iliyokuwa katikati ya jiji kule Posta Dar es Salaam, safari yake iliishia katika Super Market moja mashuhuri iliyokuwa pembeni ya jengo la Kamata pale Kariakoo. Akaiegesha gari yake aina ya Toyota Harrier katika meneo ya kuegeshea magari iliyo mbele ya Super Market baada ya kukabidhiwa kadi ya kuingia na gari, kisha akashuka na kuingia ndani alikochukua dakika kadhaa ambako alitoka akiwa na bidhaa kedekede zilizokuwa zikisukumwa na mfanyakazi wa mahala hapo, zikiwa katika mkokoteni mdogo wa Super Market hiyo.

Akafungua buti na kuhifadhi bidhaa zake, akampa bakshish yule mhudumu, akawasha gari yake na kuondoka, huku akiburudika na muziki, kibao cha Masudi kutoka kwa Marijani Rajabu. Baada ya kona za hapa, kusubiri foleni pale na kusigana na daladala kule; hatimaye aliipata barabara ya Umoja wa Mataifa tayari kwa kuitafuta nyumba yake aliyokuwa ameijenga maeneo ya Oysterbay.

Alipofika maeneo ya daraja la Salender akakuta kuna foleni nyingine inamsubiri “Shit!” Akaghadhibika akiugonga usukani na kufanya honi ilie. Ilikuwa ni wakati huu aliposikia kitu cha baridi kikimgusa nyuma ya kisogo na kufuatiwa na kauli hii.

“Tulia hivyo hivyo kenge wa bluu wewe! Ukijitikisa kidogo tu nakifumua kichwa chako!”

Kijasho chembamba kikamtoka Mhasibu. Akajilaumu kwa kumruhusu mlinzi wake aende nyumbani mapema hali ni siku chache zilikuwa zimepita tangu alipokosana na akina Tarish Michael Bagula.

“Kama shida yenu ni pesa, semeni niwaachie! Mniache roho yangu!” Akasema Taratibu hali akizungusha jicho kushoto na kulia kwa chati kutazama hali imekaaje huko nje. Shughuli zikiwa zinaendelea kama kawaida. Watu wakitembea kwa miguu, wachuuzi wa biashara ndogondogo wakiendelea kuuza bidhaa zao kwenye magari ambayo yalikuwa katika foleni, huku kwa mbali polisi wa usalama barabarani wakiendelea kuongoza magari yaliyokuwa yakitoka barabara ya Umoja wa Mataifa na kuelekea Mjini.

Ni vile tu gari yake hii mpya na imara ilikuwa na vioo vyenye rangi nzito nyeusi tinted, ambavyo wakati huu vilikuwa vimepandishwa na kipoza hewa kufunguliwa; vinginevyo, watu wa nje wangeweza kuona kitu gani kinaendelea ndani ya gari. Akili zikaanza kumduru Mhasibu kutafuta la kufanya ili kujiepusha na kikombe hiki.

Akiwa mwanajeshi mstaafu licha ya kwamba hakuwahi kufanya mazoezi tangu alipostaafu na kujiunga na benki kuu karibu miaka kumi iliyopita; aliweza kuyaangalia na kuyasoma mazingira ya nje kwa ukamilifu wake. Kwa kila hali, mazingira yalikuwa mazuri kuweza kuanzisha vurugu na kutoweka maeneo hayo bila kupata madhara ya maana. Tatizo hakujua huyu aliyemuwekea kitu cha baridi kichwani yukoje.

Taratibu akazungusha kichwa chake ili kumuangalia huyo aliyemuweka chini ya ulinzi. Akasikia usalama ukiondolewa katika bastola ile na kufanya vinyweleo visimame na moyo kumsisimka. Zoezi la kugeuza shingo likaishia hapo hapo.

“Nimekwambia ukijitikisa kidogo nafumua kichwa chako. Sasa fanya ujinga nifanye upumbavu, Shenzi taip!” Akaonywa tena.

“Mnataka nini kwangu!” Akauliza kijasho kikiendelea kumtoka.

“Roho yako!”

“Eeh!”

“Ng’wee nini, we si unajua kuhoji!” Jamaa akasema na kuongeza “Tulikuahidi utajuta. Utakula ugali kwa moto. Tutayafanya maisha yako yawe mabaya sana!”

“Kosa langu nini jamani?!” Mhasibu akalalama.

“Kukataa kutoa fedha!”

“Fedha si zimekwisha?!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Hazijaisha, kuna sehemu umezificha. Tunataka kujua ni wapi tukazichukue!”

“Mmejuaje?!”

“We unadhani mtandao wetu mdogo? Utaeleza tu!”

Wakati Mhasibu anaeleza haya mkono wake ulikuwa unashuka taratibu kuelekea zilipo lock za mlango ili aziondoe, halafu ampige huyu jamaa na kiwiko ambacho bila shaka kingeikumba bastola yake, kisha afungue mlango na kukimbia akiamini kuwa pengine atapata msaada wa raia na polisi huko nje.

Kama alikuwa ameuhisi wepesi wa yule mtekaji kule nyuma, hakuwa ameuona. Kabla mkono wake haujafikia loki ya mlango, tayari alikuwa amegongwa na kitu kizito kisogoni, akajikuta akitoa mguno hafifu na kuuangukia usukani. Hata hivyo honi haikulia kwani tayari mtekaji alikuwa amemdaka na kumrudisha nyuma.

Huku fahamu zikimtoka taratibu na akiwa hawezi kufanya chochote, Mhasibu alihisi akiondolewa katika kiti cha dereva alikokuwa ameketi na kuwekwa katika kiti cha abiria kushoto kwake. Wakati huo huo, foleni ikaanza kutembea. Akamuona kwa taabu jamaa akirukia kiti cha dereva na kuiondoa gari taratibu kama gari yake vile.

Halafu akapoteza fahamu.



Akamuona kwa taabu jamaa akirukia kiti cha dereva na kuiondoa gari taratibu kama gari yake vile.

Halafu akapoteza fahamu.

Sura ya Nne

Alipozinduka alijikuta ndani ya chumba cha wastani chenye godoro pekee isiyotandikwa shuka ambayo ilikuwa sakafuni. Kichwa kilikuwa kikimuuma kama kidonda huku mwanga wa chumba kile uliotokana na bablu ya kizamani ya wats 60 ikimuumiza macho na kumfanya ayafumbe tena hali akiizungusha akili yake kwa nguvu kukumbuka kilichotukia mpaka akajikuta katika hali ile.

Naam sasa alikumbuka barabara, kwamba alikuwa mbele kidogo ya daraja la Salender wakati alipowekwa chini ya ulinzi na kugongwa na kitu kichwani, kitu kilichomfanya ahisi maumivu makali kabla hajapoteza fahamu.

Kurejea kwa kumbukumbu hizi kukamfanya autume mkono wake kichwani pale alipogongwa na kitu akakutana na nundu ya wastani iliyozungushiwa kitu kama bandeji. Alipofungua macho tena, safari hii macho yake yaliweza kukabiliana na mwanga, akafaulu kuangalia kushoto, kulikuwa na ndoo moja chakavu ya plastiki.

Pembeni ya ndoo hiyo ya plastiki ya lita ishirini kulikuwa na kiti imara cha mbao ambacho miguu yake ilikuwa imechimbiwa ardhini moja kwa moja. Ilikuwa ni wakati huu pua yake ilipopokea harufu kali ya uvundo ambao haulezeki sawasawa ni wa kitu gani. Nyuma ya kile kiti kulikuwa na nyundo, misumari kadhaa na kamba ya nailon. Hakukuwa na kitu kingine.

Akiwa hajui kazi ya vitu hivi, Mhasibu alijitahidi kuzungusha macho kuuangalia ukuta ule hafifu lakini hakuumaliza, kwani alisikia maumivu makali mgongoni mwake ya kitu kama sindano hivi. Akakusanya nguvu zake zilizosalia na kuinuka haraka. Kunguni wawili walioshiba, walionekana wakikimbia kuelekea nyuma ya godoro. Akiwa mtu ambaye hakuwahi kuumwa na kunguni kwa muda mrefu, Mhasibu alijikuta akitabasamu na kuyasahau matatizo yake kwa muda.

Pale alipokaa akahisi kama amekalia sakafu pekee kutokana na wembamba wa godoro lile alilolikalia. Godoro ambalo watoto wa uswahilini hupenda kuita ‘ulimi’ kutokana na wembamba wake. Miguu yake wakati huu ilitua juu ya sakafu ile yenye unyevunyevu ulioshiba na kufanya baridi ianze kuusumbua mwili wake. Akili yake sasa ikiwa imerejea katika hali yake ya utulivu, Mhasibu alijikuta akifikiria ni namna gani anavyoweza kujinasua katika kadhia hii.

Akaingiza mkono mfukoni kulikokuwa na simu na fedha zake, hakukuta hata kimoja.

Dakika chache zikakatika akifikiria cha kufanya. Kutahamaki akasimama na kuukabili mlango. Ulikuwa mlango wa kawaida tu wa mbao za Surplus uliounganishwa na mbao tatu ndogo ambazo zilitengeneza herufi ‘Z’ ndefu. Kwa kila hali ulikuwa mlango dhaifu tu ambao usingeweza kuhimili teke moja zuri la mwanajeshi mstaafu kama yeye.

Hata hivyo kabla hajalitumia teke hilo, aliujaribu kwa kuutikisatikisa, ukaishia kutoa mlio wa kulalamika, mlio uliomjulisha kwamba mlango ule ulikuwa umefungwa kwa nje ima na kufuli au komeo.

“Umeamka eeh!” Akaulizwa kwa sauti nzito kidogo iliyotokea nje. Mhasibu akajua kuwa kumbe nje kulikuwa na ulinzi na kwamba mlio ule wa kulalamika kwa mlango ndio uliomjulisha mlinzi au walinzi kuwa mateka wao alikuwa ameamka. Kwa mara nyingine akajilaumu kwa kutokuwa na bastola yake karibu.

“Nakuuliza wewe nguchiro, umeamka?!” Sauti ikarudia tena, safari hii zikifuatiwa na hatua za kuukaribia mlango. Mhasibu akajiweka tayari kwa mapambano maana kule kwenye gari walimvizia. Ingawa alikuwa dhaifu, akiwa ametoka kuzinduka muda sio mrefu, alijua atapambana nao na atawashinda. Kitu kimoja alikuwa na uhakika nacho, kwamba jamaa hawa hawako makini. Vinginevyo wasingeweza kumuweka katika chumba hafifu chenye mlango dhaifu kama huu.

“Umekuwa bubu ghafla, Well! Utaimba tu. Tena utaimba kama chiriku!” Jamaa akasema na kuongeza “Mathias, mwambie George na Athanas wakae sawa mie namwita Tarish aje kuongea na mtu wake, maana tayari amezinduka!”

Kauli hii ikamfanya mhasibu agwaye kule ndani. Yeye alidhani kuna mlinzi mmoja kumbe kuna kundi la walinzi na inawezekana wana silaha. Kwa hili aliona hata kule kuwa kwake mwanajeshi hakuwezi kumsaidia mbele ya watu wengi wenye silaha. Akabakia kutetemeka na kumuomba Mungu amsaidie.

Ilikuwa ni wakati huu alipomsikia yule jamaa wa mwanzo akizungumza na mkuu wao katika simu juu ya kuzinduka kwake, alipokata simu aliwapanga watu wake kwa umbali wa hatua kadhaa na akawataka kumpiga risasi Mhasibu mara moja endapo angeleta ukorofi wowote. Baada ya hatua hizi ndipo alipoufungua mlango ule na kuingia ndani.

Mhasibu akaweza kumuona jamaa yule ambaye alikuwa pandikizi la baba, jitu la miraba minne hasa lililopanda juu kisukuma na kutanuka vyema kifuani. Kwa lugha ya kimjini mtu huyu huitwa ‘baunsa’.

Baunsa huyu alikuwa amevaa jinsi nzuri ya bluu iliyompendeza sana, viatu vizuri vya raba Reebok pamoja na fulana nyeusi ilikishika kifua chake vizuri. Kichwani alikuwa na kofia ya pama ambayo juu yake ilihifadhi miwani kubwa myeusi. Yale macho makali aliyokuwa nayo, ngeu kadhaa za hapa na pale katika paji la uso na kidevuni pamoja na zile ndevu zilizonyolewa katika mtindo wa ‘O’ kwa pamoja vilimfanya Mhasibu ajue amekutana na Jambazi mtanashati.

Kiunoni alikuwa na bastola iliyohifadhiwa katika kifuko chake.

“Kazi zangu zilikuwa mbili tu!” Mtu yule akaanza baada ya kuingia ndani. Mhasibu akamtumbulia macho hali akirudi kinyumenyume mpaka alipogota ukutani. Sasa aliweza kuikumbuka hata sauti ya mtu huyu. Kwamba huyu ndiye aliyemteka kule daraja la Salender.

“Kazi ya kwanza ni kukuteka na kukuleta hapa, kazi ya pili kuhakikisha unataja fedha ziliko!”

“Nilishamwambia bwana wenu kuwa zimekwisha!”

“Huo ni uongo na wewe unajua ni uongo. Ni afadhali ukasema sasa, kuliko kusubiria useme hali ukimwagika damu!” Sauti yake ilikuwa ya upole kama anayeongea jambo zuri. Ambacho hakukijua ni kwamba Mhasibu alikuwa radhi kufa kuliko kutaja fedha ziliko. Hivyo akaishia kukaa kimya tu, maana hata angesema nini asingeeleweka.

“Well, hebu kaa basi katika hicho kiti ili uweze kufikiria vizuri. Maana nahisi unafikiria kwamba useme au usiseme!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Mhasibu alipochelewa kukaa alijikuta amepigwa kofi zito la kelbu lilitua sawia sikioni na kulifanya sikio lake lipige mbinja ya kukata na shoka, hali yeye mwenyewe akipepesuka na kujigonga ukutani kabla hajarudi chini kama robota la chumvi. Lilikuwa shambulio la kushtukiza sana ambalo hakulitarajia, jambo lililomfanya aumie sana pale alipojigonga ukutani.

Upesi akajipindua na kumchota mtama yule baunsa, baunsa naye akaenda chini na hapo hapo akafyatua teke ili kulitua kifuani kwa Mhasibu, hilo Mhasibu alilitarajia na akavingirika kando akiliacha teke la baunsa likitua chini. Alipoinuka alikuta tayari Baunsa ameshamka na hapo akapokea mapigo mawili ya karate yaliyotua sawia kifuani kwake na kumrejesha chini.

Alipojikakamua kuinuka na kupiga mapigo mawili matatu ambayo Baunsa aliyapoteza, alijikuta akirudi chini tena baada ya kupigwa ngumi mbili za uso zilizopasua mdomo na kufanya damu ianze kuvuja puani na mdomoni huku akiwa hajiwezi kwa maumivu.

“Una bahati Tarish hajatuamuru tukuue kenge wewe!” Akasema baunsa kwa hasira hali akitweta. “Unatuchezea sisi wewe!” Akaongeza hali akimuongeza teke zito la tumboni. Mhasibu akaachia yowe zito la maumivu na kujikunja. Wakati huo huo akaingia jamaa mwingine na kukemea.

“Ommy achana nae bana, utamuua bure mambo yaharibike!”

“Mshenzi sana huyu jamaa, eti alikuwa ameanza kunishambulia. Hajui kama mimi naitwa Killer, Sasa hivi angehamia katika orodha ya watu niliowapeleka kuzimu kwa mkono huu, Pumbavu!” Akajibu Ommy,

“Pamoja na hayo, dhibiti hasira zako Ommy!” Akaongezea yule mtu.

“Poa!” Akakubali Ommy akiinama na kumkusanya kusanya Mhasibu pale chini akamuinua kama unyoya na kumtupa katika kile kiti cha mbao, kisha akaanza kumfunga kamba, alimfunga vizuri katika namna ambayo, Mhasibu alishindwa hata kujitikisa. Ni hapa Mhasibu alipoelewa matumizi ya kiti hiki.

Ommy Killer aliporidhika na kazi yake, akasimama na kumwambia Mhasibu kwa kwa sauti ya upole iliyohifadhi hasira baridi. Pengine hasira hizi zilitokana na yeye kupigwa mtama na Mhasibu kitu ambacho hakikuwahi kumtokea katika miaka yote tangu alipojiunga na akina Tarish.

“Rafiki yangu Mhasibu Jamaldin, maadam umekataa kutaja mahala ziliko fedha kwa hiyari, sasa utataja kwa nguvu. Hakuna mtu aliyewahi kuingia humu akatoka na siri yake kifuani akiwa hai. Hiki kijumba kiko Msasani bonde la mpunga, ni mbali sana na makazi ya watu.

Hiyo misumari na nyundo hapo pembeni ya kiti, kazi yake ni moja tu, kutoboa mikono, miguu, kifua, jicho na hata kichwa cha jasiri yeyote ambaye huwa hawezi kusema kwa hiyari mpaka pale msumari na nyundo vinkapofanya kazi yake. Upo hapo! Ngoja Tarish aje kuturuhusu tukuonyeshe namna ugali unavyoliwa kwa moto! Good day!”

Akageuka na kutoka, akimuacha Mhasibu akiugulia kwa maumivu.

Dakika thelathini baadae chumba hiki kilipata uhai tena. Tarish alikuwa amefika na kuelezwa kilichotukia mwanzo. Kwa hiyo akawataka walinzi wawili wenye silaha kubaki nje hali yeye akiingia ndani na walinzi wawili akiwemo Ommy





“Umefanya vizuri kumfundisha adabu. Ungempiga zaidi, ungempiga sana. Hutakiwi kumuua tu. Huyu anastahili kufa baada ya kutuambia fedha amezificha wapi. Ungemuona alivyokuwa ananipuuza siku ile ofisini kwake eti fedha zimeisha wakati aliniambia mwenyewe kuwa zingali nyingi na haziwezi kuisha leo wala kesho, ndio ungegundua ni mshenzi kiasi gani. Yaani hafai kwa kulumangia wala kutoelea. Hana tofauti na papa la mji!”

Tarish akaachana na Ommy na kumgeukia Mhasibu. Akamuuliza.

“Mhasibu Jamaldin, mtunzaji mkuu wa fedha za benki kuu, nakupa nafasi ya mwisho kueleza kistaarabu. Je, fedha ziko wapi?”

“Niwaambie mara ngapi kwamba zimekwisha!”

“Huo ni uongo!”

“Ukweli ni upi?!”

“Hilo swali ndo unatakiwa utujibu!”

“Sina jibu lingine!”

“Ommy Killer, Uwanja ni wako. Huyu Ustaarabu kwake ni neno la kichina!” Tarish aliamuru na kukaa pembeni. Ommy akavua begi lake dogo lililokuwa mgongoni mwake, akalifungua na kutoa bandeji akazifunga mikononi mwake mithili ya bondia hodari anayejiandaa na pambano la kukata na shoka.

Kana kwamba hiyo haitoshi, akatoa kiberiti cha gesi, waya za kuchomea nyama mishikaki, pamba za kufungia vidonda, dawa za madonda, vibanio vya nguo vya chuma, vibanio vya umeme na vitu vingine kadha wa kadha. Alipohakikisha kila kimoja kipo sawia sasa akamkabili Mhasibu na kumuinamia kwa upendo kama rafikie wa siku nyingi.

“Nakuuliza kwa mara ya mwisho rafiki! Fedha ziko wapi?”

Mhasibu akamtazama kwa hasira na kumtemea mate yaliyotua sawia usoni kwa Ommy. Akayafuta taratibu na kuinuka kwa kasi kabla hajaanza kumshushia Mhasibu mvua ya makonde.

Alimpiga na kumpiga na kumpiga.

Mpaka wenzake walipokumbuka kumshika na kumzuia, Mhasibu alikuwa ameshatepeta na kulegea kama mlenda, hali sura yake ikiwa haitamaniki kwa damu. Ilifanana kama na nyanya lililotumbuka ‘masalo’. Wasaidizi wa Tarish wakagundua kuwa Mhasibu alikuwa amezimia tena.

“Dhibiti hasira Ommy, siku nyingine utaua! Huyu mtu bado ni hazina kwetu!” Tarish akamwambia Ommy. Ommy ambaye wakati alikuwa akipumua kwa nguvu huku hasira zake zikiwa katika kiwango cha juu kabisa alijikuta akijiinamia kwa uchungu huku machozi yakianza kumtoka. “Sorry Bosi!” Akasema kwa sauti nzito na kuongeza.

“Naomba jukumu la kumtesa huyu mtu mpaka ataje fedha zilipo apewe mtu mwingine. Kwa tabia yake hii ya kunitibua kila mara, haki ya Mungu mtakuta nimemuua. Mie sipendi dhihaka wala dharau!”

“Hatwendi hivyo Ommy!” Tarish akakumbusha kwa karaha.

“Akifa hatutakuwa na kujibu ila kumfufua. Ingawa nimewaajiri mimi, mimi siye ninayetoa hizi fedha, wapo wenyewe ambao ndio wanaoitaka siri iliyopo kifuani kwa huyu mtu. Hivyo punguzeni jazba, Sawa?”

“Sawa!” Wakajibu kwa pamoja. Ommy akatoka nje.

“Kwa sasa...” Tarish akaendelea “...mtoeni hapo katika kiti moto, mumlaze katika kitanda chake na kumpatia huduma ya kwanza. Mathias shughulikia suala hili. Wewe na George ndiyo mtakaobaki hapa na Mathias mkitoa huduma ya kwanza na kuimarisha ulinzi. Mie na Athanas na Ommy tunaondoka mara moja kwenda kufanya kazi nyingine mahala fulani. Sawa?” Tarish akatua.

“Sawa mkuu!” Wakajibu kwa pamoja.

“Vizuri, niliyoyasema yatimie na kwa herini!” Akaamuru akitoka na Mathias ambapo walimpitia Ommy huko nje na kuondoka naye. Huku nyuma Mhasibu alitolewa katika zile kamba akaanza kupewa huduma za kwanza ili kumpunguzia athari za maumivu na kumfanya azinduke haraka kama alivyoamuru Tarish.

Jogoo aliyewika kwa mara ya kwanza alfajiri ya siku hiyo, kuashiria kuwasili kwa mapambazuko ya siku mpya, ndiye aliyemzindua Mhasibu kutoka katika ule usingizi wa nusu kifo aliokuwa amelala kufuatia kipigo kitakatifu alichokipata kutoka kwa Ommy Killer.

Akatulia kwa muda akiyasikiliza maumivu makali ambayo yaliiandama na kuizingira sehemu kubwa ya kichwa na uso wake. Alipoutuma mkono wake usoni ukamjulisha ni kiasi gani alikuwa ameumizwa. Mkono ule uliendelea kukagua hapa na pale katika kichwa na uso wake mpaka ulipojiridhisha na hali ilivyo ndipo alipourudisha na kuanza kutafakari upya namna ya kujinasua kutoka katika baa hili.

Matumbo yaliyoanza kunguruma ghafla tumboni mwake, nayo yalimkumbusha kitu kingine muhimu, njaa! Kwamba alikuwa hajapata chakula tangu alivyotekwa jioni ya siku iliyopita. Hili la njaa likamtisha akihofu kwamba atashindwa kuiendesha oparesheni ya kujiokoa aliyokuwa akiipanga kikamilifu. Hata hivyo akajikaza na kuinuka.

Akasogea mlangoni na kuchungulia, hakuweza kuona mtu, nje kulikuwa kungali kiza ila alipotuliza masikio aliweza kusikia kitu kama mkoromo wa mtu aliyetopea usingizini. Wakati akitembeza macho zaidi humo ndani akaona ile nyundo na misumari, vitu ambavyo Ommy alikuwa amemwambia kazi yake. Akatabasamu, kuisogelea na kuikamata.

Ilikuwa nyundo ya wastani yenye uzito wa nusu kilo hivi ambayo alijua itamsaidia vizuri kuitimiza dhamira yake. Akaiweka mahala kijanja kisha akarudi kitandani na kuanza kukohoa kwa nguvu. Alikoa mfululizo na kwa muda kidogo.

“Weweh! Nini?” Mathias akabweka huko nje.

“Njaa... Njaa!...Kiu!” Akasema akikohoa zaidi.

Kauli hii ikamfanya Mathias aachie kicheko cha kebehi kule nje, kabla hajaondoka na kwenda sehemu nyingine. Dakika chache baadae akarejea akiwa na mkate na chupa ya maji. Alipofungua mlango na kuingia ndani alikofungwa Mhasibu tu, harufu ya pombe ikakihanikiza chumba chote.

Mhasibu akatambua kuwa Mathias alikuwa amelewa, hili likamfurahisha zaidi. Alijua upinzani utakuwa mdogo, na hasa aliwahofia walinzi wengine. Maana mpaka hapo alishajua kuwa kuna walinzi wa kutosha huko nje. Mathias alipoinama tu ili kumtengea ule mkate na maji, Mhasibu akakurupuka akiikwapua nyundo pale alipoiweka na kuitua kichwani kwa Mathias kwa nguvu zake zote zilizosalia. Naam, nyundo ilitua barabara juu ya utosi wa adui yake.

Yowe dogo likamtoka Mathias, akapepesuka na kujigonga ukutani kisha akaangukia kile kiti cha mateso na kutulia kimya, damu ikianza kumtiririka kutoka pale utosini alipopigwa na ile nyundo. Kitendo bila kuchelewa, Mhasibu akaikamata nyundo yake na kusimama imara pembeni ya mlango akimsubiri yeyote atakayeingia amzawadie nyundo nyingine ya kichwa.

Alisubiri kwa muda mrefu bila kusikia chochote. Safari hii Mathias ambaye baada ya kupigwa nyundo alikuwa akipumua haraka haraka na kukoroma sasa alikuwa ameacha vitu vyote viwili. Mhasibu akahisi ameua. Akamsogelea na kuanza kumpapasa mifukoni.

Wakati anafanya hivi akaona jamaa alikuwa na bastola kiunoni, akaichukua. Alipoingiza mikono katika mifuko yake akakuta wallet iliyotuna yenye kitambulisho cha mpiga kura, fedha kadhaa na kondomu. Akachambua na kuzitupa kondomu, halafu akaiweka mfukoni, akazima taa na kutoka nje kwa tahadhari.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Mbele yake akaona magunia mengi ya mkaa na magari mawili moja Vitz na jingine Noah ya kizamani. Nyuma ya yale magari kulikuwa na ukuta uliojengwa kwa mabati ambao ulizunguka eneo lote alilokuwemo ikiwemo ile nyumba aliyofungiwa, akasogea taratibu nyuma ya kijumba kile akihofu kupitia mlangoni kutamletea matatizo.

Nyuma ya jengo lile kulikuwa na bati ambalo halikuwa imara sana, akalibinua na kutokea nje. Alipoinuka tu, mataa yaliyotapakaa katika majengo mengi ya ghorofa yaliyokuwa mbele yake yakamlaki. Alikuwa Jangwani eneo ambalo lina sifa ya kupokea mafuriko kila mvua inaponyesha jijini Dar es salaam.







ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog