IMEANDIKWA NA : HUSSEIN WAMAYWA
*********************************************************************************
Simulizi : EPA
Sehemu Ya Kwanza (1)
Ukumbi wa mikutano wa Arusha, Arusha International Conference Centre (AICC) ulikuwa umetulia tuli. Muziki mwepesi wa taratibu uliokuwa ukitoka katika spika kubwa zilizowekwa katika pembe hii na ile, ndio pekee uliochangia kuupa uhai ukumbi huu mkubwa.
Wajumbe wa mkutano mkuu wa chama tawala; Chama cha Umoja wa Umma na Demokrasia waliokuwa wamevalia nadhifu mavazi yanayorandana na rangi za bendera ya chama, pinki na bluu bahari, walikuwa wakiingia taratibu kwa madaha.
Leo ndio leo! Baadhi waliwaza wakiketi na kuchukua nafasi zao, huku wachache wakiongeza. Asemaye kesho muongo!
Halafu wagombea urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wakaanza kuingia mmoja baada ya mwingine, kila mmoja akishangiliwa vizuri sana na washabiki wake. Jacob Chaguo alikuwa mtu wa mwisho kuingia, yeye alishangiliwa zaidi ingawa hakuwa na furaha kama wengi walivyokuwa. Naye alikuwa na Mlinzi (Bodigadi) kama walivyokuwa wenzake. Akaenda katika nafasi yake na kuketi, mlinzi wake akisimama nyuma yake.
Muda si mrefu Johnstone Peter Mambo Katibu mkuu wa chama, akaingia haraka kama aliyechelewa. Mkononi alikuwa na faili kubwa. Alipochukua nafasi yake, akalifungua faili na kutoa nyaraka kadhaa, akampa bosi wake Daniel Killango. Killango akaanza kuzipitia taratibu. Mara kadhaa alikuwa akikunja sura.
Wakati huu moyo wa Mgombea Jacob Chaguo ulikaribia kung’oka kwa kupiga kifuani. Dua, sala na matumaini yake ya mwisho yalibakia kwa Rais Killango anayemaliza muda wake ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti wa kikao hiki cha juu kabisa cha uteuzi wa mgombea urais atakayekiwakilisha chama katika uchaguzi mkuu.
Ni vyema Chaguo awe na hofu, kwa sababu toka alipotangaza nia yake ya kugombea wadhifa huo mkubwa kabisa nchini, vitimbwi na vituko vimekuwa vikimuandama kila uchao.
Kwanza ilikuwa ni nyumba yake kuvamiwa na majambazi, akapekuliwa na kuchukuliwa nyaraka zake za siri, nyaraka zenye mipango, mbinu na nia yake ya kuelekea Ikulu. Wazazi wake waliokuwa kanda ya ziwa nao wakafanyiwa hivyo. Wakati mshangao ukiwa hata haujamtoka, akajikuta akiibiwa simu yake ya kisasa Smartphone HTC 201D iliyokuwa na zaidi ya kila kitu chake muhimu.
Akiwa amehifadhi hata mbinu zake za kimkakati za kampeni zake ndani ya simu ile; Jacob alijikuta akihamanika vibaya, akaitafuta simu kwa siku kadhaa kila alipoweza. Bado hakufanikiwa kuipata. Akiwa ameanza kukata tamaa, akaikuta simu hiyo juu ya meza ofisini kwake ikiwa sehemu ya wazi kabisa!
Kwa kila hali ilikuwa imerejeshwa.
Akaichukua na kuiangalia kwa pupa, kila kitu chake kilikuwepo. Akachoka kabisa. Akajua vita imeanza. Akabadili mfumo mzima wa kampeni zake naye akazalisha mamluki na kuwapenyeza katika kambi za wenzake, huku akifanya kampeni zake kisayansi zaidi.
Licha ya wananchi walio wengi kumuunga mkono, bado vitimbwi hivi na vile havikuacha kumuandama sio tu nje, bali hata ndani ya chama.
Kwanza alikuwa ametakiwa kutoandaa wasifu wake, wakidai hiyo ni kazi ya chama! Na hata chama kilipoandaa wasifu huo, bado Chaguo hakuweza kuupata ili ahakiki taarifa zake. Hata alipoudai kwa mara kadhaa, bado hakupewa.
Walinzi aliopewa, hawakuwa walinzi wa maana tofauti na walinzi waliopewa wagombea wenzake. Akiwa mwanajeshi mstaafu, tena aliyeshiriki vyema kumngoa nduli kule Uganda, Chaguo hakujali. Alijua walinzi wakishindwa yeye atayakabili. Na alipokuja kufanya mazoezi na walinzi wale ambao kwa wakati huu waliondokea kuwa rafiki zake, mwenyewe akajikuta akitabasamu. Vijana wake walikuwa bora kabisa! Walichokosa ni uzoefu tu, kitu ambacho Chaguo hakukiona kama cha maana sana.
Akaridhika nao.
Akaendelea na harakati zake huku timu yake aliyoiita ‘Wana Umoja!’ ikimuhakikishia kwamba mambo yalikuwa mazuri. Kwamba Ikulu ilikuwa yake wakati huu. Kwamba nyota yake inang’ara vizuri kuliko wagombea wengine. Aliendelea kuwa na matumaini mpaka pale mmoja kati ya mamluki wake aliowapandikiza katika kambi za wenzake, alipomletea habari zilizommaliza nguvu.
Kwamba kulikuwa na mbinu chafu zimesukwa juu yake.
Akiwa nje ya ‘system’ ya chama kwa wakati huu, kichwa kilimuuma akitafuta namna anavyoweza kuzipangua mbinu hizo chafu ambazo zilikuwa na lengo la kumfanya asishinde katika uchaguzi huo wa chama ili akiwakilishe chama katika uchaguzi mkuu wa vyama vingi vya siasa ambao ulitarajiwa kufanyika miezi michache ijayo.
Aliposhindwa kabisa, akafunga safari mpaka kwa Mwenyekiti wa chama, mheshimiwa Daniel Killango. Akamueleza kila kitu, akamtaka akumbuke jinsi ambavyo walisaidiana katika uchaguzi uliopita na mambo mbalimbali ambayo yeye Chaguo alikuwa ameyafanya kwa niaba ya Killango katika kumsaidia.
Zaidi akamtaka akumbuke dhana za wanafalsafa mbalimbali.
Zilikuwa habari mpya na nzito kwa Daniel! Kwanza hakuamini kama fitina hizi zimeasisiwa na Johnstone Peter Mambo Katibu wake mtiifu kabisa. Akamuahidi atafuatilia kujua ukweli na kumtaka Jacob Chaguo asiwe na hofu.
“Ukishindwa kunisaidia, ujue sitashindwa kuitumia turufu yangu, na nikiitumia nchi haitatawalika hii!” Jacob akaonya. Daniel akacheka na kumtoa hofu.
“Haina haja Jacob, baada ya jinamizi la uchaguzi uliopita, sitapenda tena machafuko yatokee. Najua kuna kitu siyo kizuri ndiyo maana hata katibu wangu Johnstone amenificha. Wewe niamini mimi, nimekusikia! Nimetafakari na nitafuatilia kwa siri bila kumshtua yoyote na mwisho wa siku nitachukua hatua. Sawa ndugu yangu?!”
“Sawa!”
“Vizuri. Mi’ nakuahidi, sitataka kuchafua historia ya utendaji wangu mzuri uliotukuka baada ya kumaliza awamu yangu na kustaafu!” Rais Killango akaahidi. Ilikuwa ahadi nzuri kwa kila hali. Jacob akaondoka akiwa na matumaini chanya. Matarajio yakimrejea tena kwa kasi.
Huku nyuma Daniel alianza kufuatilia. Katika pekua pekua yake akagundua kuwa mambo mengi yalikuwa yamejadiliwa katika kikao kilichopita cha Kamati kuu, na kuandaliwa muhtasari wake. Kikao cha kuchuja wagombea urais na kuandaa kanuni mpya na maadili ya chama ya uchaguzi.
Kikao ambacho yeye hakushiriki kwa kuwa alikuwa Marekani katika mwaliko maalum aliotumiwa na Rais wa nchi hiyo, George W. Bush. Kikao hicho kilikuwa kimeongozwa na Makamu wake Mashaka Mkesso ambaye wakati huu alikuwa Venezuela, na kuratibiwa vilivyo na Katibu mkuu Johnstone Peter Mambo.
Lakini kwa maajabu, sio muhtasari wala kanuni hizo zilizoonekana ofisini. Alijitahidi kutafuta kadiri alivyoweza kwa kusaidiana na Katibu muhtasi wake na wasaidizi wengine wa ofisi bila mafanikio.
Aliposhindwa kabisa akampigia simu Johnstone na kumtaka amletee vitu hivyo mara moja, Johnstone akamjibu kwamba hakuwa jirani, atamletea usiku nyumbani kwake. Roho ya Daniel ikatua akijua usiku utakapoingia ataletewa nyaraka hizo na ataweza kujua mbivu na mbichi.
Usiku hakuletewa!
Siku iliyofuata Johnstone hakuonekana ofisini na simu yake ikawa haipatikani. Daniel akaanza kupata shaka. Kwa siku mbili nzima, Daniel aliendelea kumtafuta Johnstone bila kumuona. Hatimaye siku ya mkutano ikafika.
Daniel alipoingia katika chumba cha mkutano pale AICC Arusha na kwenda kukaa katika kiti chake, ndipo Johnstone alipotokea na kumkabidhi zile nyaraka, huku akivujwa na jasho mithili ya mkimbiaji aliyemaliza mbio ndefu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati Daniel anaanza kusoma nyaraka zile ambazo kwa hakika zilikuwa nyingi kiasi, muongozaji wa shughuli ya mkutano maarufu kama Master of Ceremony nae alikuwa ameshaanza kuelezea utaratibu utakavyokuwa kwa kusoma ratiba. Alipomaliza kusoma, Daniel akatabasamu na kumtazama Jacob. Kwa siri sana akamuonyesha ishara ya dole gumba.
Jacob akatabasamu na kumshukuru Mungu.
Hotuba za utangulizi zikatolewa. Wagombea wakajieleza na kuulizwa maswali. Ulipofika wasaa wa chama kutoa wasifu wa wagombea, na Johnstone Peter Mambo akiwa tayari kabisa kufanya hivyo, Daniel akamzuia na kuwasha kipaza sauti chake. Akasema.
“Chama hoyee!”
“Hoyeee!” Watu wote wakajibu..
“Bado sijasiki, bado sijasikia. Nataka mpaka wapinzani wapate habari huko nje kuwa leo chama tawala kiko hapa. Uchaguzi hoyeeh!” Daniel akasema tena kwa hamasa na sauti kubwa zaidi!
“Hoyeeeeeeeeh!!” Umati ukazizima kwa sauti kubwa zaidi.
“Hapo sasa sawa!” akasema huku akitabasamu, akaendelea “Ndugu wajumbe mliohudhuria, itifaki imezingatiwa. Naomba tuulizane kitu kimoja jamani, hivi sote si tumewasikia wagombea wetu wakijieleza?”
“Ndiyoooh!”
“Mbali ya kueleza sababu za wao kutaka kugombea, si wameeleza wasifu wao, tangu walipotoka, walipo na wanapoelekea?”
“Ndiyoooh!”
“Na kila mmoja wetu hapa si anamjua mwenzake kinagaubaga? Je kuna asiyemjua mwenzake ndani ya chama chetu?! Je, kuna haja ya wasifu mwingine kutolewa na chama?!”
“Hakunaaaaaaaaah!”
“Je kuna asiyemjua mwenzake hapa?”
“Hakunaaaaaaaaah!” Jibu hili likafuatiwa na kibwagizo cha chama. Daniel akamgeukia Johnstone na kuamuru, “Katibu endelea na hatua inayofuata!”
“Lakini Mwenyekiti...” John akaanza “Haya ni maagizo ya kamati Kuu! Muhtasari unasema hivyo na umepewa...!”
“Mwenyekiti wa kikao hiki ni nani?” Daniel akamkata Kalima.
“Wewe!”
“Na walio na maamuzi katika kikao hiki ni akina nani?”
“Wanachama!”
“Wanachama wamesemaje?”
“Lakini Mwenyekiti...!”
“Jibu swali John!”
“Wamesema hakuna haja. Lakini...”
“Nimekwambia endelea na hatua inayofuata!” Daniel akaamrisha kwa sauti yake nzito na nene. Kiasi Johnstone akaogopa. Wakati huu kibwagizo cha wimbo wa chama kilikuwa kimeisha. Johnstone akawa akihamanika kama kuku anayetafuta mahala pa kutagia. Mikono ilikuwa ikimtetemeka, na kijasho chembamba kumtoka.
Johnstone akawasha kipaza sauti na kuendelea. “Ufuatao ni utaratibu wa uchaguzi!”
Daniel akamzuia na kuwasha kipaza sauti chake tena. Akasema tena “Uchaguzi hoyeee!”
“Hoyeee!”
“Jamani nataka tushauriane jambo jingine ili kuokoa muda. Tunao wagombea kumi na tano. Je kutoka kwao tunataka wagombea wangapi ili wakiwakilishe chama chetu katika uchaguzi Mkuu?”
Umati wote ukajibu kwa msisimko “Mmojaaaaaaaaah!”
“Sio wagombea watatu?”
“Siyoooooh, tuanataka mmojaaaa!”
“Kwa hiyo mnataka kuniambia kuwa tunatakiwa kuchagua mgombea mmoja si ndivyo?”
“Ndiyooooooh!”
“Ahsanteni!” Daniel akashukuru na kumgeukia Johnstone. Wakati huo huo kibwagizo cha chama kikaanza upya. Akamwambia “Unasikia John, hakuna haja ya kuchagua wagombea watatu kwanza, halafu baadae mmoja. Tunahitaji mgombea mmoja tu na tutampata kwa wingi wa kura na sio vinginevyo. Sawa?!” ilikuwa mfano wa amri.
“Lakini ... Lakini...!”
“Hakuna cha lakini... endelea na uchaguzi kama wajumbe walivyotaka!”
“Tunakiuka maelekezo ya kamati kuu lakini!” John akajikakamua.
“Hatukiuki Johnstone. Na usidhani sizijui mbinu zako chafu na wenzako, za kutaka mumchafue Chaguo kwa kutumia kigezo cha wasifu wake, ili muweze kumpitisha mtu wenu Paul George Mwakilembe! Na amini amini nawaambia, hilo sitalikubali asilani. Sitalikubali kamwe!”
Lilikuwa sawa na shambulio asilolitegemea. Johnstone akatepeta. Maneno yale yakammaliza nguvu. Akaendelea na utaratibu kwa moyo mzito. Kwa kila hali walikuwa wamezidiwa kete!
Wakati haya yakiendelea, kikundi cha watu wachache kilikuwa hakitulii katika sehemu moja mle ndani. Aliyetia fora katika hili alikuwa Castor Mathias Kinyamagoha, ambaye ilikuwa mara asimame, mara akae. Roho ilimuuma kuona mpango uliowagharimu jinsi unavyoharibika mithili ya nyumba ya tofali za udongo ambayo haijaezekwa inayopigiwa na mvua kubwa ya mawe.
Akajuta kwa nini alipinga wazo la wenzake la kumshirikisha Daniel Kilango katika mpango huu ambao ulielekea kuharibiwa na huyo huyo Daniel Kilango.
Alikuwa na sababu za maana za kukataa Kilango asishirikishwe. Kwanza alikuwa anamaliza muda wake. Muda si muda atakabidhi urais na uenyekiti wa chama kwa mtu waliyemteua Paul George Mwakilembe. Kumuingiza huyu katika orodha ni kutaka aendelee kuwanyonya hata wakati akiwa hana cha kuchangia tena.
Pili alimjua vyema Daniel na namna akili yake isivyofanya kazi sawasawa. Angeweza kabisa kutouafiki mpango huo na ikawa imetibua kila kitu. Hili lilikuwa jambo lililomtisha sana.
Na tatu na mwisho ni vile Daniel alivyoshinikiza yeye anyimwe tenda ya kuchapa vitambulisho vya Taifa, eti kwa vile hakuwa na mtaji wa kutosha. Wangapi wanapata tenda hawana mitaji, wanafanya hila na kupata mitaji toka kwa waliowapa tenda? Hili pamoja na hayo mawili hapo juu, wachilia mbali hili la sasa hivi la kuutia mchanga kitumbua chao, kwa pamoja vikamfanya amchukie Daniel isivyo kawaida.
Akainuka taratibu na kuelekea chooni, ambako alipiga simu mahala fulani.
* * *
Dakika chache baadae Johstone akaingia Chooni na kumkuta Castor ameliinamia sinki la maji la kunawia mikono. Kwa msaada wa kioo akaweza kumuona jinsi alivyokuwa ameghadhibika na kuchukia.
“John?” Akaita taratibu kwa hasira baridi akingali amekitumbulia macho kioo na kufanya watazamane moja kwa moja machoni kupitia katika kioo kile. Johnstone akaitika kwa uoga.
“Naam!”
“Kimetokea kitu gani?”
“Hata mimi sijui mkuu! Nilijitahidi kufanya kila nililoagizwa kwa umakini wa hali ya juu. Lakini sijui imekuwaje!”
“Je” Castor akauliza tena “Ni mara ya ngapi Daniel anakwenda kinyume na vile ulivyoandaa?”
“Ni mara ya kwanza!”
“Oooh!” Castor akasema akigeuka. “Sasa ninapata picha, kuna mtu anayetusaliti!”
“Eti?”
“Yes Of Course! Unakumbuka ofisini kwenu watu walivyohangaika kuzitafuta kanuni na muhtasari wa kamati kuu?”
“Nakumbuka!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Na unakumbuka Daniel alivyokuwa akikupigia simu na kukutafuta umpelekee zile nyaraka, hata tukakushauri uzime simu na usiende ofisini?!”
“Nakumbuka vizuri sana. Ni mpumbavu pekee anayeweza kusahau!”
“Kuna mtu atakuwa alimwambia kabla. Thus why Daniel akawa akihangaika. Mtu huyu lazima apatikane alipie hasara tuliyoingia kuuandaa mpango huu! Any way hayo tuyaache nitajua la kufanya!” Akaingiza mkono mfukoni, ukatoka ukiwa na paketi ya Sigara Portsman. Akaichana na kwa kutumia vidole viwili cha shahada na kinachofuatia, akaigonga ile paketi na sigara mbili tatu zikapanda juu ambapo alichomoa moja na kuipachika mdomoni.
“Vipi? Mambo yanakwendaje huko ndani? Kuna matumaini?” Akawasha sigara.
Johstone akatikisa kichwa kushoto na kulia kwa masikitiko “Hakuna! Hakuna kabisa. Kura zimeshapigwa na jamaa anaongoza kwa kura nyingi sana. Zaidi ya robo tatu ya wajumbe wamempigia yeye!”
Castor akavuta pafu mbili ndeefu na kuuachia moshi utoke taratibu sana hapa na pale katika mdomo na matundu ya pua lake.
“Vipi Paul?” Akauliza moshi ukiendelea kufuka taratibu.
“Yupo, naye amelowa kuliko kawaida!”
Castor akatabasamu kama aliyefurahishwa na jibu la Johstone. Kisha akasema tena. “Worry not my gentleman! Bado tuna turufu. Lazima tufanye kitu. Tena haraka sana. Tayari nimewaita vijana wangu wanne ninaowaamini sana, na tayari wamekwishafika. Nipatie system ya ulinzi ilivyopangwa, halafu wewe kaendelee na shughuli zako.
Johstone Mambo akampatia na kuondoka.
* * *
Aliporejea ukumbini, matokeo yakatangazwa.
Jacob Chaguo alikuwa ameshinda kwa zaidi ya asilimia themenini na tano. Ukumbi mzima ukalipukwa kwa shangwe, hoi hoi, vifijo, nderemo na vigelegele. Mwenyekiti wa chama akainuka na kumpa mkono wa hongera, kabla hajamkumbatia.
Wakafuatia viongozi wengine, Makamu mwenyekiti, Rais wa Zanzibar na wajumbe wengine. Bendi ya chama ilikuwa ikitumbuiza vitamu na kuwainua wajumbe kusakata dansi. Ilikuwa ni baada ya salaam za shukrani na pongezi kutolewa huku kila mmoja akiomba makundi yavunjwe ili kujiandaa kupambana na wapinzani huko nje; ndipo wageni walipoanza kuondoka.
Chaguo akasindikizwa na wajumbe wachache wa timu yake ya kampeni.
Walipofika eneo la magari, Jacob chaguo akashangaa kuona sura mpya tupu kasoro Castor tu. Akamgeukia Castor aliyeambiwa anashughulikia masuala ya ulinzi na usalama, akamuuliza “We Castor mbona umeniwekea walinzi wapya watupu?! Vijana wangu wa awali wako wapi?”
“Mzee wewe umeshakuwa tegemeo la chama, umeshakuwa mgombea mteule. Ni wajibu wetu kuhakikisha usalama wako. Tumekuandalia watu madhubuti zaidi!” Castor akajibu.
“Sawa! Watu wangu wako wapi?”
“Tumewagawanya mzee. Baadhi wamerudi CCP Moshi, wengine wameenda Monduli na wengine Mgulani. Usihofu kiongozi, hawa ni wazuri zaidi! Isitoshe na mimi nitakuwepo!”
“Hivi we Castor, unadhani watu hawana akili siyo?”
“Kwa nini mzee?”
“Tangu lini Mrakibu Mwandamizi wa Polisi akamlinda mgombea Urais?! Msiniletee upuuzi! Nataka watu wangu wale wale, tena haraka!” Akafoka na kuongeza “Sitaondoka mahala hapa hadi nimewaona watu wangu! Na jambo hili lazima Daniel alijue!”
Akageuka na kurudi ndani.
Kijasho chembamba kikamtoka Castor tena. Kwa mara nyingine, ndege wake alikuwa ametoka katika shabaha tena! Hakuwa na jinsi, akawasiliana na Johnstone na wakaanza kuwatafuta walinzi wa awali wa Chaguo.
Wakati wakihangaika kuwapata, Jacob Chaguo na wafuasi wake watiifu walikuwa wakicheza na bendi ya chama. Wimbo maalumu aliowaomba wamtungie. Saa moja baadae Johnstone akarudi tena ukumbini na kumwambia Chaguo.
“Mzee vijana wako, wako tayari!”
“Waambie waingie ndani!”
Walinzi wakaingia ndani.
“Vipi?” Chaguo akawasalimia.
“Safi!” Wakajibu kwa pamoja. Jacob akaendelea
“Naona mlitaka kuondoka bila kuniaga. Najua waliwafukuza. Upuuzi huu sitaupa nafasi hata kidogo!” Akatua. Walinzi wakaishia kutabasamu tu. Akabadilishana nao mawazo kwa muda na muda mfupi baadae gari jingine likafika. Jacob na watu wake wakaondoka na gari hili wakiliacha gari aliloandaliwa kulipanda.
Castor akauma meno kwa uchungu.
* * *
Ukimya uliendelea kutawala kana kwamba hakuna mtu.
Fikra ziliendelea kuwaduru zikivivuruga vichwa vyao kiroho mbaya. Kutokukamilika kwa mpango wao uliowagharimu muda, nguvu na fedha za kutosha, kuliendelea kuwatisha. Kuwatisha kwa maana ya kutokujua hatima yao baada ya uchaguzi mkuu kwa sura hii hii wanayoiona.
Kila mmoja alikuwa akisugua fikra zake ili aweze kupata mwelekeo utakaoifanya hatima yao kuwa na sura inayopendeza. Sura ambayo itawafanya waishi kama walivyokuwa wakiishi kabla.
“Je,” Mmoja aliyekuwa Mwenyekiti wa kikao hicho akauliza “Kuna mafanikio yoyote?”
Wajumbe wote wanne wakainua macho na kumtazama kama wanayemuuliza Una maana gani?
“Kuhusu Uchaguzi!” Akajibu kama aliyesoma kitu katika nyuso za wenzake na kuongeza, “Kweli tumeshindwa kufanya lolote? Aibu iliyoje!”
“Kuhusu uchaguzi!” Alikuwa Johnstone “Hatuwezi kumuepuka Jacob Kinara Chaguo. Kama mnavyojua, uchaguzi uliopita tulimshinda kwa mbinde baada ya kutushinda mara kadhaa, na isingelikuwa ushawishi wa wanadiplomasia akiwemo mzazi wake aliyemshawishi akubali kushindwa, tusingelimshinda.
Ni bahati mbaya sana baba yake hayupo tena. Tulishamzika baada ya kuugua Malaria kali ya muda mfupi. Zaidi na zaidi Mikutano ya Kamati kuu, Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu tayari imeshampitisha kwa kishindo. Kwa kweli safari hii Ikulu ni ya yule jamaa kwa kila hali!”
“Kwa hiyo?!” Mwenyekiti akaingilia kwa hasira.
“Inabidi tutafute njia nyingine Mkuu. Njia ya kuendelea kuneemeka!”
“Stupid!” Mkuu akabweka akigonga meza. Sauti yake nzuri ikishindwa kuwatisha wajumbe kwa kiwango alichotarajia, lakini ikafaulu kuwafanya wamakinike zaidi.
“Nilipowaambia tufanye Brain stroming nilikuwa na maana tutafute njia hiyo. Hakuna haja ya kurudia rudia. Jacob katushinda katika sanduku la kura, hajatushinda kiakili.
Bado tunaweza tukatafuta namna itakayomfanya awe chini yetu. Asiwe na kauli yoyote kwetu. Tukiipata namna hiyo tutaendelea kuongoza nchi kwa mgongo wa Jacob Chaguo, na tutaendelea kuneemeka na kuneemeka na kuneemeka. Naitaka namna hiyo. Tuna dakika tano tu!” Akatua akihema.
Vichwa vikachemka tena. Dakika sita baadae, mmoja akakohoa. Mwenyekiti akamtazama na kumwambia, “Go on!”
“Tunaweza kumuweka under Control Mama. Tunazo rekodi za kutosha za uchafu wake!”
“Good! Uchafu gani? Mauaji, Rushwa, Wizi wa mali za umma au...?”
“Jacob ni mbovu sana kwa wanawake na...!”
“Castrooooh!” Alikuwa Mwenyekiti kwa karaha. Rekodi za ufuska pekee hazitoshi kuwabadili wananchi. Kunahitajika jambo kubwa zaidi. Jambo ambalo linaweza kumtisha Jacob na kumfanya atutetemekee na sio tu kutusikiliza, bali na kufanya lile tulitakalo.
Kumbuka wananchi wa sasa ni waerevu, na kumbuka wamepewa ahadi nyingi ambazo hazijatekelezwa vile inavyopaswa. Maisha yao yameendelea kuwa magumu siku hata siku na sasa wana imani kubwa na Chaguo. Hapana, lazima lipatikane jambo kubwa zaidi!”
“Kwani!” Alfred aliibuka kama mtu aliyetoka usingizini. “Shida yetu ni nini hasa, kuiongoza nchi au kuendelea kuvuna rasilimali, neema na hazina za nchi hii?!”
“Vyote viwili Alfred!” Alikuwa Mwenyekiti “Chemchem ya hazina iko Ikulu. Pale ndio penye control ya kila kitu. Tuitawale nchi halafu tuvune!”
“Basi kama ni hivyo ipo njia rahisi ya kumkamata Jacob!”
“Njia gani?” Wote wakagutuka na kumtazama kwa shauku.
“Kumsimika madarakani! Hilo tu. Tukishamuweka pale Ikulu hatakuwa na ujanja tena. Kila wakati atahitaji kulipa fadhila. Wakati huu ndipo tutakapoanza kumuamrisha. Fanya hiki... fanya kile... Sisi tunaendelea kula nchi taratibu!”
“Tutamsimikaje Alfred?”
“Tugharamie kampeni zake!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kitu gani?” Mkubwa akaguta, hewa ikimtoka makalioni bila kujitambua “Unaelewa uzito wa kitu unachokizungumza wewe?!”
“Naelewa vizuri sana!” Alikuwa Alfred akitabasamu vitamu kuona alivyowachanganya wenzake.
“Hii sio kampeni ya jimbo moja lenye kata kadhaa Alfred!” Johstone akakumbusha kwa karaha. “Ni kampeni ya mikoa isiyopungua thelathini. Ni kampeni ya Wilaya tele na Kata chungu nzima. Hicho chama chenyewe kinakuna kichwa jinsi kitakavyozifanikisha kampeni za Kinara! Hili si jambo dogo hata kidogo. Ni zito mno, ni zito kweli kweli!”
“Naelewa!” Alikuwa Alfred tena kwa lugha ya upole zaidi. “Katika hili kundi letu tuna kila kitu. Wapo wanajeshi, Polisi, Watu wa Usalama na watu kutoka katika chama. Kila idara imekamilika.
Kila mmoja ni mtaalamu na muhimu katika nafasi yake, kila mmoja! Sidhani kama tutaamua kwa dhati kutafuta fedha za kumsimika Jacob pale Ikulu tutazikosa! Kwa upande wangu naona itakuwa rahisi kutafuta mtu mmoja mpenda pesa pale benki kuu, tukamuuzia wazo hili kwa minajili ya kupata mkopo japo wa bilioni hamsini au mia moja ambao unaweza kufutwa baada ya Chaguo kuwa Rais.
Au hata akatuwezesha kupata hela za bandia, tukazitumia kuwarubuni wananchi na kuwamwagia malaki kwa malaki ya shilingi na baada ya uchaguzi fedha hizo zikakusanywa na kuondolewa katika mzunguko, kisha kuharibiwa!” Akamaliza Alfred.
Ikawa kama amewasha taa katika bongo zao ambazo awali zilikuwa giza totoro kwa kutotambua cha kufanya. Mjadala uliendelea kwa muda kabla ya Castor Mathias kupewa jukumu la kuhakikisha anamlisha neno mtu wa Benki Kuu mpaka anafanya kile wanachokitaka.
Jukumu ambalo Castor kwa kumtumia kijana wake aliyemuamini, Tarish Michael Bagula, alilikamilisha vizuri sana.
* * *
“Kutengeneza pesa bandia ni hatari!” Akaanza Mhasibu Jamaldin, Mkurugenzi wa Benki kuu ya Tanzania. Hii ilikuwa mara ya pili kukutana na mtu huyu. Mara ya kwanza alikuwa amempuuza na kumtimua baada ya kukisikiliza kile ambacho yeye alikiona upuuzi.
Lakini simu aliyopokea baadae toka Makao Makuu ya Chama kutoka kwa Afisa wa juu yakamfanya anywee. Alipojaribu kuomba ushauri kwa rafikie aliye Polisi Makao Makuu mwenye cheo cha juu pia, akahakikishiwa kwamba huu ulikuwa mpango maalum kuhakikisha chama kinarejea madarakani tena.
Rafiki zake wengine wa Usalama wa Taifa na walio Serikalini nao walikuwa wamempa zaidi ya uhakika.
Ni kufuatia hali hii ndipo alipokubali kumpokea tena jamaa huyu ambaye kwake alijitambulisha kama Tarish Michael Bagula. Akausikiliza mpango wake tena kwa umakini na utulivu wa hali ya juu kama alivyoshauriwa na wakubwa. Halafu akamuomba muda afikirie.
Na sasa alikuwa amemwita kumpa jibu. Akaendelea.
“Ni hatari kwa kuwa pesa hizo bandia, zitagharimu fedha nyingi za kigeni kuzitengeneza. Tena zitasambaa sana, kuzikusanya itakuwa kazi kubwa na ngumu. Lakini pia itakuwa aibu kwa Taifa baadae pesa hizo zitakapovuka mipaka na kuingia katika nchi za nje, hasa kwa wadau wetu wa maendeleo. Ukweli tunahitaji kufikiria upya!”
“Sasa tufanyeje ndugu? Maana mpaka jana wazee kikaoni walikuwa wameona kwamba hiyo ndiyo njia pekee iliyobakia!”
“Najua!”
“Na kingine, mafanikio ya uchaguzi yanakutegemea sana. Wewe ndiye ambaye umeshika funguo za kukifunga au kukifungulia chama katika madaraka!”
“Labda,” Mkurugenzi akasema baada ya tafakuri ya muda. “Mnaonaje tukitumia fedha za akaunti ya madeni ya nje?”
“Ndiyo fedha gani hizo?”
“Kila mwaka Serikali yetu huwa inakopa fedha kutoka kwa wahisani mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa kazi anuai za maendeleo ikiwa ni pamoja na kugharamia bajeti yetu!”
“Hilo nalifahamu!”
“Na kila mwaka pia Serikali hii hii hutoa kiasi fulani cha mapato yake ili kulipa madeni hayo. Na kwa kuwa fedha hizo huwa zinatolewa kidogo kidogo, Serikali kupitia benki kuu huwa wanazifungulia akaunti na kuzilimbikiza mpaka zinapokuwa nyingi ndipo tunakwenda kuwalipa waliotukopesha. Kwa hiyo tuna fedha za kutosha katika akaunti hiyo ambazo zinaweza kusaidia kufanya kampeni katika kiwango mnachotaka ninyi!”
“Na wanaotudai je? Kama tukizitumia hazitaleta madhara?”
Mhasibu Jamaldin akaangua kicheko kwa kauli hii. “Usinichekeshe kaka, Madhara hayawezi kukosa, huwezi kukopa hela ya mtu ukaitumia bila kumlipa halafu madhara yakose!” Akatua kwa muda na kumeza funda la mate, alipoendelea tena alikuwa makini zaidi. Akasema,
“Madhara yapo! Ila wakati huo si Rais atakuwa Chaguo? Atajua namna ya kuyazuia. Wanaotudai wanaweza kuendelea kusubiri kama wanavyosubiri hivi sasa!”
“Good!” Tarish akafurahia. “Good Idea Mhasibu! Umeturahisishia kazi. Nina hakika wakubwa watakuzama kwa jicho linalofaa. Watahakikisha unaishi vizuri na kupata kila unachohitaji!”
Mhasibu akatabasamu. “Usijali!” Akajibu taratibu. “Ni wajibu wangu kusaidia harakati za chama!”
“Sasa tunafanyaje ili kuzichukua?”
“Zipo njia nyingi. Lakini iliyo nyepesi ni ile ya kurithishwa madeni!”
“Kwa namna gani?”
“Mnaanzisha kampuni za kutosha, mnarithishwa madeni na kampuni zilizotukopesha, halafu ninyi mnaandika barua za madai, kudai mlipwe!”
“How?!” bado Tarish alikuwa hajaelewa sawasawa.
“Usitake kuniambia ninyi nyote mtashindwa kugushi mikataba ya kurithishana madeni ili muwe na uhalali wa kuchukua fedha hizo!”
“Alaa, kumbe!!”
“Eeeh! Simple like that!”
“Je” Alikuwa Tarish baada ya kuelewa vizuri. “Kuna la kufanya zaidi? Maana muda si rafiki yetu kabisa!”
“Of Course Tarish, Njoo huku nikupe orodha ya makampuni na nchi zinazotudai!”
Akamwambia akiinuka. Tarish nae akainuka. Wakaingia katika chumba kingine kilichokuwa na mafaili na nyaraka za kutosha. Dakika kadhaa zikapita wakipekua hapa na pale kabla hawajapata mafaili waliyoyahitaji.
Dakika nyingine nyingi zikapita wakiwa katika mashine ya kudurufu karatasi. Walitoa nakala ya kila karatasi waliyoihitaji. Dakika nyingine zilikatika wakati Mhasibu akimpa maelekezo haya na yale ili kurahisisha mambo.
Mpaka anaondoka kwa Mkurugenzi wa Benki Kuu, moyo wake ulikuwa unakaribia kupasuka kwa raha na furaha.
* * *
Kikao cha kwanza na cha pili vilikuwa kwa ajili ya kujadili namna watakavyochota pesa hizo na kujineemesha huku wakigawana majukumu nani afanye nini na kwa nini! Kikao cha tatu kikawa namna watakavyojiingiza katika kampeni za chama, na namna gani sehemu ya fedha watakazoiba zitakavyotumika kuwarubuni wengine na kuzifanya kampeni za chama kutia fora.
Kikao cha nne na cha mwisho kilikuwa baina yao na mgombea mteule wa Chama cha Umoja wa Umma na Demokrasia Mheshimiwa Jacob Kinara Chaguo.
Hiki kilifanyika katika Hotel ya New Africa. Awali Chaguo alikuwa amekataa kwenda akihofia kuhujumiwa. Lakini taarifa za uchunguzi alizopewa baadae na vijana wake watiifu kwamba hakuwa na sababu ya kutokwenda, zikamfanya aende bila hofu.
Aliingia katika chumba cha mikutano dakika ishirini mbele zaidi ya muda aliopangiwa. Alikuta waalikwa wote wameshafika. Ni wakati alipoingia ndipo akawa amejua ni kiasi gani kikao hicho kilivyo kikubwa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mwenyekiti na pengine kiongozi wa kikao alikuwa Victoria Brayson Kamugisha, Brigedia Jenerali Mstaafu wa Jeshi la wananchi wa Tanzania. Alikuwa mwanamama hodari, shupavu na mpambanaji kweli kweli ambaye licha ya kumpokea Chaguo pale Jeshini, lakini ndiye aliyekuwa mwalimu wake. Na alimsimamia vyema tangu Chaguo akiwa kuruta mzungu wa reli hadi alipoanza kupata mbavu moja baada ya nyingine kabla hajaanza kupata nyota.
Ukiacha huyo alikuwepo Alfed Omary Mbuzi; Afisa usalama mwandamizi ambaye naye pia alikuwa mwalimu wa Chaguo katika masuala mazima ya usalama, akimuelekeza hili na lile hadi wakati ule Chaguo alipoamua kujiingiza katika chama kichwa na miguu.
Johnstone Peter Mambo alikuwa kiongozi na Katibu mkuu wa chama. Akiwa mzee wa chama aliyeshiriki vingi na mengi, naye alikuwa ametoa mchango mkubwa kisiasa ambao ulikuwa umemsaidia Chaguo Jacob Kinara kufika hapo alipo leo.
Ambaye hakuwa na mchango mkubwa kwake alikuwa Castor Mathias Kinyamagoha. Huyu ambaye kiumri hawakupishana nae sana alikuwa akitokea Wizara ya mambo ya ndani katika Jeshi la Polisi alikokuwa na cheo cha Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi kabla hajashushwa cheo na kuwa Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, baada ya kushindwa kuyasimamia kwa weledi majukumu aliyopewa. Cheo ambacho anacho mpaka hivi sasa; akiwa na ofisi yake pale makao makuu.
Jacob aliwasalimia kwa heshima zote, akachukua nafasi yake na kuketi. Aliwatazama wenyeji wake usoni ili aone kama anaweza kuambua lolote, hakufanikiwa. Sura zote zilikuwa safi za kiungwana zilizobeba tabasamu jepesi la kirafiki kabisa.
“Nimeitika wito wazee wangu!” Akavunja ukimya na kuwaambia.
“Umefanya vizuri Chaguo!” Akaanza Vick “Umefanya vizuri sana. Well done Jacob!” Akatua na kupiga funda la maji. Halafu kwa pozi zote za kike akaendelea.
“Tumekuita hapa kama wazee wa chama, kama wazee wa Serikali. Lakini pia kama wazee wa nchi tukiwa zaidi ya wazee wako. Na sisi utuonao hapa ni Task Force maalum ya S.K.A; Saidia Kinara Ashinde. Task Force iliyoundwa kwa siri na Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais kwa lengo la kuondoa kila kikwazo kitakachofanya lengo lako lisitimie!
Ndani ya umoja huu wapo polisi, mawaziri, maafisa usalama, wanajeshi, mahakimu na wengine wengi ambao sisi ni sehemu yao!” Vick akatua tena na kupiga funda la maji wenzake wakatikisa kichwa juu na chini kuafiki. Akaendelea.
“Tumekuita kwanza kwa jili ya kukupongeza kwa ushindi ulioupata katika chama. Lakini pia kwa ajili ya kukutoa hofu! Kwamba usiwe na shaka tena. Nchi ni yako kwa kila hali. Sisi ndio wazee wa nchi na tuko pamoja na wewe!”
Jacob akaduwaa.
Hakuona ni vipi nchi isiwe yake, wakati chama kilishamteua, Tume ya uchaguzi ikamridhia na kumpitisha. Waliokuwa wakisubiriwa ni wananchi tu ambao wengi walikuwa upande wake wakivutiwa na falsafa ya sera zake, hasa ile ya Umasikini sasa basi! Akawa makini zaidi ili pengine hawa jamaa wasije kumuingiza choo cha kike.
“Nashukuru wazee!” Akajibu.
“Uwe huru, huru kabisa! Jua una baraka za kutosha za wazee wako. Ukiwa na tatizo lolote usisite kutuambia!”
“Sawa!”
Ukimya mfupi ukapita. “Je,” Vick akauvunja kwa kuuliza “Hauna tatizo lolote?”
“Ammm!” Jacob akafikiria “Matatizo hayakosekani, lakini nadhani nitakabiliana nayo. Yakinizidia nitaomba msaada wenu! Nashukuru kwa kuniunga mkono na kuwa pamoja na mimi!”
“Kweli hauna tatizo Jacob?” Vick akakazania “mbona Johnstone ametuambia pesa mlizonazo katika chama haziwezi kufanya kampeni katika namna mnayoitaka?!”
“Ni kweli chama hakina fedha za kutosha kwa sasa. Ila...”
“Basi basi!” Vick akamkata kalima na kuongeza “Johstone ametuletea bajeti tayari. Na tayari tumepata fedha za kutosha kutoka kwa marafiki zetu. Tunakuhakikishia tutaifanya kampeni katika kiwango kitakachowafanya wapinzani watuhusudu na kutupigia magoti!”
Jacob akakaa kimya. Hakujua aseme nini. Yeye pia kupitia timu yake ya kampeni alikuwa na akiba ya kutosha tu. Hata hivyo hakuona kama ni busara kubishana na wazee hawa aliowaheshimu na kuwaamini sana ambao kwake walikuwa zaidi ya wazazi. Baadhi walimlea, baadhi ni walimu wake na baadhi wamepata kuwa marafiki zake na wakingali marafiki zake hadi sasa. Ni hili pia lililomfanya asihoji matarajio ya wazee hawa baada ya kumpa fedha hizo. Akaendelea kukaa kimya.
“Usihofu kabisa kuhusu gharama!” Vick alikuwa akiendelea kuongea “Panga kila unachotaka kifanyike au kupatikana, tena katika ubora ambao ni the best kabisa, halafu tuambie na sisi tutatatua! Ukitaka fedha tasilimu pia ni kiasi cha kusema tu, sawa Jacob?”
Ukimya mfupi ukapita Jacob akitafakari. Vick alipouliza tena Jacob akajibu.
“Sawa!”
* * *
Halafu kampeni zikaanza. Viroja vya aina yake vikafuatia. Wako walioomba kura kwa shikamoo kama watoto, waliopita nyumba kwa nyumba na viroba vya mchele, unga, sukari, chumvi na nafaka zingine.
Wengine waliahidi hata wasivyoweza kutimiza, kama kuleta mvua kwenye ukame na kadhalika na kadhalika. Yuko mgombea mmoja kule kanda ya ziwa alikwenda mbali zaidi kwa kuahidi kuwajengea daraja wapiga kura wake. Walipomuuliza mbona hawana mto, akawaambia na mto pia atawaletea.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Jacob kampeni zake zilikuwa za aina yake.
Zilichapishwa fulana, khanga, kofia, kalamu za wino, penseli, shajara, miamvuli, madaftari, viberiti na vingine vingi. Jacob alifika kila mkoa, kila wilaya. Sera zake zikiwavutia na kuwaweka karibu maelfu kwa malaki ya watu, huku wale wasioweza kufikiwa moja kwa moja wakifikiwa kwa njia ya mabango, picha kubwa za rangi (Posters), vipeperushi, magazeti, redio na televisheni kupitia vipindi maalum.
Nchi zima ikaimba Chaguo Chaguo.
Tarish akaendelea kuhudhuria kwa Mhasibu Jamaldin na kuchukua fedha. Bado hiki, bado kile! Akadai akiendelea kuchukua fedha tu, mambo yakaenda kama yalivyopangwa huku nyingi kati ya fedha hizo wakigawana wale waheshimiwa wazito kabisa.
Na ili kuweka mambo sawa, kundi lile lilitenga fedha kidogo sana ambazo alipewa Johnstone ili ampe Chaguo. Johnstone hakufikisha kwa Chaguo hata senti moja. Na vile Jacob hakuwahi kuwaomba chochote, ikawa raha juu ya raha kwa Johstone Peter Mambo.
Hatimaye uchaguzi ukafanyika, kura zikahesabiwa na matokeo kutangazwa. Chaguo Jacob Kinara alikuwa ameshinda kwa asilimia kubwa sana.
Watu walijimwaga barabarani wakaandamana kusherehekea ushindi! Fataki zikarushwa, matairi yakachomwa hali matawi ya miti yakikatwa kwa wingi kusherehekea ushindi ule wa kishindo.
Tambo kwa wapinzani zikatolewa, kwamba walikuwa watoto, kwamba hawawezi kitu. Nderemo, hoi hoi na vifijo vikapigwa na kutawala. Hakika kwa chama tawala ilikuwa raha juu ya raha.
Furaha na hoi hoi hizi zilihamia uwanja wa taifa wa Dar es salaam siku chache baadae baada ya matokeo kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi pale Diamond Jubilee na Rais mteule kupewa hati ya ushindi. Watu wengi walijitokeza kushuhudia Rais Jacob Chaguo Kinara akiapishwa.
Mizinga ishirini na moja ikapigwa na kwa mara ya kwanza akakagua gwaride la heshima.
Wakati huu wale vigogo wanne, Victoria Brayson, Alfred Omary Mbuzi, Johnstone Mambo na Castor Mathias walikuwa wamestarehe katika sebule kubwa ya chumba Suit kilichopo katika hoteli moja kubwa ya kitalii, huku wakifuatilia kila kilichokuwa kikiendelea uwanja wa Taifa kupitia luninga kubwa iliyokuwa ukutani.
Hawakutaka kwenda uwanjani, kwa vile mbali ya kutaka kufuatilia kila kitu kwa ufanisi wake, lakini pia walitaka kufanya sherehe ndogo ya kujipongeza kwa jinsi walivyofaulu kwa hatua ya kwanza.
Hatua ya ‘kumsaidia’ Rais Mteule Jacob Kinara kuingia Ikulu.
Hatua ya pili ambayo waliamini ingekuwa nyepesi ni kumpenyezea orodha ya watu wao watiifu, watu ambao Rais angepaswa kuwateua kama mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa Halmsahauri.
Baada ya hatua hii ndipo ingefuata ile hatua muhimu ya kuukamua uchumi wa nchi uliotapakaa huko na huko katika Nishati, Gesi, Madini, Bahari na wanyama. Hatua ambayo waliona kwa msaada wa watu wao ambao wakati huu wangekuwa viongozi waandamizi katika Serikali ya Chaguo katika kila nyanja; wataikamilisha bila shida.
Kwa hatua hii hawakuona ni kwa nini wasijipongeze!
Ni pale Jacob Chaguo alipomaliza kuapa na mlinzi wa Rais Bodigadi katoka kwa Rais Mstaafu Daniel Killango na kuhamia kwa Rais Jacob Kinara Chaguo, na baadae Chaguo kuanza kukagua gwaride la heshima; ndipo walipoanza kushangilia. Walishangilia mno, walishangilia kweli kweli. Walishangilia na kucheka mpaka machozi yakawatoka.
Naam, kwa kila hali nchi ilikuwa ikielekea kuwa mikononi mwao.
Kushangilia huku kulihitimishwa na safari yao ya Ikulu siku chache baadae katika kile walichokiita kwenda kumpongeza Chaguo na dhamira ya maombi ya ushirikiano ili kuifanya nchi iweze kuinuka na kupiga hatua kubwa kimaendeleo ili iingie katika nchi zinazoendelea kwa kishindo.
Wakati wanaondoka walimuachia Chaguo bahasha kubwa ya khaki A4, ambayo mbali ya kuwa na kadi ya Pongezi, lakini pia ilikuwa na majina ya watu waliokuwa wakipendekezwa kuingia katika Baraza jipya la Mawaziri la Serikali yake.
Chaguo alipokuwa akiipitia baada ya watu hao kuondoka, akashindwa kulizuia tabasamu lake. Tabasamu hilo lilidumu usoni mwake kwa muda mrefu hadi alipomaliza kusoma waraka ule na kuuhifadhi.
“Nadhani hawanijui vizuri hawa watu!” Akahitimisha akiuchukua mkoba wake wenye nyaraka za kazi kadhaa ambazo aliona bado zinahitaji kupitiwa upya, akatoka na kuelekea nyumbani kwake.
Jioni ya siku ile alikuwa na mtu wake wa Intelejensia ambae pamoja na mambo mengine alimpa ile orodha ya wale jamaa na kumtaka awafanyie udukuzi kwa siri sana na kufuatilia unyayo wa kila mmoja wao.
Ingawa haikuwa kazi rahisi na nyepesi, baada ya subira ya muda wa kutosha, siku chache baadae akajikuta akimiliki taarifa ya siri ya watu ambayo ilikuwa na mengi yaliyohitaji ushahidi wa kutosha ili wapandishwe kizimbani kwa makosa ya ufisadi na kuhujumu taifa.
“Sasa nitawaonyesha mimi ni mtu wa namna gani!” Jacob akaamua baada ya kumwambia mtu wake amtafutie ushahidi wa tuhuma zile.
* * *
Kama kina Alfred Omary Mbuzi walitegemea maoni yao yangefanyiwa kazi, walikosea vibaya sana. Siku chache baadae Baraza la Mawaziri likatangazwa na kuapishwa. Katika orodha waliyompelekea Jacob Chaguo hakukuwa na jina hata moja lililoingia katika Baraza jipya la Mawaziri. Pamoja na kutaharuki kupita kiasi, bado walijionya kuwa watulivu kwa kuwa Serikali ni kubwa na yenye vitengo vingi.
Uteuzi wa wakuu wa mikoa wapya, kuwahamisha vituo vya kazi wengine ukafuatia. Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmshauri, mabalozi wa Tanzania nje ya nchi, Makatibu Wakuu wa Wizara, Wakuu wa Idara za Serikali na wengine wengi. Jacob alikwenda mbali zaidi kwa kuwaondoa kazini baadhi yao. Jambo lililowafanya wakose hata mahali pa kushika.
Hatua hii iliwafanya wakutane siku chache baadae na kuujadili mustakabali wao.
Mjadala ulikuwa mrefu na maswali yalikuwa mengi lakini hatima haikuonekana. Ilikuwa ni baadae sana pale Victoria alipokuja na wazo ambalo lilikuwa kama ahueni kwao. Wazo lililowaambia kuwa ingawa wamekosa mwana, basi wasikose na maji ya moto. Wote wakaamua kulifanyia kazi.
Naam! Waliamua kuutekeleza ule usemi wa unapotaka kumuua nyani, usimuangalie usoni. Sasa hawakuwa na huruma wala simile. Walidhamiria kumuonyesha Chaguo kuwa kama yeye aliujua huu wenzake waliujua ule. Ndiyo, wakapanga na kupanga na mambo yakapangika. Ukabaki ukisubiriwa utekelezaji tu.
Upande wa pili nchi ilianza kuongozwa, wananchi wakijituma kwa bidii katika kazi zao za uzalishaji mali wa kila siku. Kila mtu akiwa na matumaini na imani kubwa na Serikali nzuri ya Jacob Kinara Chaguo. Serikali waliyoichagua wenyewe kwa ushindi sio tu wa kishindo pekee bali na mnono pia! Uteuzi wa watu watakaomsaidia Jacob ukiwa umeungwa mkono na mamia kwa mamia ya watu, hali hotuba yake ya kwanza aliyoitoa Bungeni ikiwaliza watu kwa furaha.
Ndiyo! Wangekosaje kuwa na matumaini na mtu wao? Mtu wa Watu. Jacob Kinara Chaguo?!!
Sura ya Pili
Nchi ilikuwa inaanza kupata uhai baada ya ukungu ulioikabili kutoka saa kumi na moja za alfajiri. Jua lilikuwa likichomoza vizuri katika kingo za mashariki ya jiji la Dar es Salaam na kuifanya miale yake ya dhahabu kuifikia ardhi bila shida na kubadili rangi ya kila kimoja.
Uhai huu ulitiwa nakshi na pilika pilika za siku mpya, harakati za watu magari na kufunguliwa kwa ofisi kulilifanya jiji la Dar es salaam kuianza siku mpya kwa mikikimikiki ya aina yake kila mmoja akiwahi kule ambako mkate wake wa siku ulikuwa ukipatikana.
Katika ofisi moja iliyopo ndani ya jengo moja kati ya majengo mawili pacha ya Benki kuu ya Tanzania, harakati zilikuwa zikiendelea vile vile. Dk. Mhasibu Jamaldin alikuwa ameiinamia meza yake akifanya kazi kwa bidii. Tangu alipoingia ofisini hapo alfajiri ya siku hiyo na kuwasha kompyuta yake, hakuwa amekumbuka walau kuvuta hata sigara.
Katibu muhtasi wake Maimuna alipoingia baadae muda wa kazi ulipotimu na kumtaka radhi ili afanye usafi, alikuwa amemkatalia kistaarabu na kumwambia kuwa ofisi sio chafu sana hivyo aendelee na shughuli zake zingine, huku akimwambia kuwa asingependa kusumbuliwa na wafanyakazi au wageni wasio na miadi. Jambo ambalo Maimuna aliliafiki.
Pengine angeendelea kuchapa kazi kwa muda mrefu zaidi, pengine asingekumbuka kunywa hata chai kama isingelikuwa simu iliyoingia katika moja ya simu nyingi zilizokuwa pale mezani, hii ikimjulisha kuwa inatoka kwa Maimuna, Katibu muhtasi wake. Akaicha ikaita kwa muda huku akiendelea kuchapa kazi mpaka ikakatika. Ikaita tena na kukatika. Ilipoita mara ya tatu ili kuondoa kero akaipokea.
“Nimekwambia sitaki usumbufu wa...!”
“Samahani bosi, kuna mgeni analazimisha kukuona, nimemwambia una shughuli lakini ame...!”
“Usinambie hujui cha kufanya Maimuna!” Akafoka.
“Nimemwambia amuone Matheo Leonard badala yako amegoma. Nimemwambia una kazi nyingi!”
“Kwa hiyo?”
“Amelazimisha kukuona, kasema kama simruhusu ataingia kwa nguvu!”
“Kitu gani?”
“Eeh! Ndiyo hivyo, nadhani kosa nililolifanya ni kumwambia upo!”
“Umewapigia walinzi waje wamtoe, maana hiyo ni fujo!”
“Nahofia, nikianza kuwapigia wakati yupo hapa hapa, anaweza kuchukua maamuzi ya kuingia kwa nguvu, na hivyo mpaka walinzi wafike tayari watakuwa wamechelewa!”
Mhasibu akapumua, hasira zikishuka. “Ana shida gani?”
“Amekataa kuniambia, amesema anataka akwambie wewe tu, na ni lazima akwambie leo hii na muda huu na si vinginevyo!”
“Anaitwa nani?”
“Jina lake gumu, kitu kama Bagwe au Bigu!”
“Anatokea wapi?”
“Makao makuu ya chama!”
“Okay! Muache aingie. Mwingine akija mwambie sipo. Hii ripoti ninayoiandaa inatakiwa isomwe Bungeni keshokutwa, na ndio kwanza sijafika popote na kuna msululu wa watu wa kuipitia na kuisahihisha!”
“Nimeelewa bosi!” Maimuna akakata simu.
Mhasibu akaacha kufanya kila alichokuwa akikifanya na kuyaelekeza macho mlangoni kumsubiria huyo mgeni mkorofi anayevuruga taratibu za ofisi za watu. Aliazimia kumfukuza na kumuonya asijaribu tena kuleta kwato zake katika ofisi yake.
Mlango ulipofunguliwa, likaingia pande la mtu lililovalia suti nzuri ya pande tatu ya rangi nyeusi. Mhasibu asingeweza kumsahau mtu huyo ambaye kwa upande mmoja alikuwa rafiki yake, kwa upande yeye akiwa mshauri ambaye walishiriki pamoja katika zile harakati zilizomuwezesha Jacob Kinara Chaguo kupata ushindi wa kishindo na kuingia Ikulu kiulaini.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kule kutomtarajia kwake katika muda na siku kama hiyo, ndiko kulikomfanya aendelee kushangaa wakati mtu huyo akiisogelea meza yake kwa uso wa tabasamu, kabla hajavuta kiti na kuketi. Ingawa usoni alikuwa akitabasamu, Mhasibu hakuona kama sura hiyo ilibeba tabasamu, badala yake akasoma kitu tofauti ambacho kilimjulisha kuwa tabasamu lile lilikuwa la kebehi au la kinafiki. Tabasamu ambalo lilikuwa kama linalonong’ona, haya sasa nimeshaingia, Amua! Mhasibu akatulia, hatari za kuitibua ratiba yake akaziona waziwazi.
“Je,” Mtu yule akasema baada ya kujikaribisha kitini. “Hujambo?”
“Sijambo bwana Tarish!” Akajibu Mhasibu na kuongeza “Habari za Asubuhi?”
“Njema! Sijui za kwenu nyie mnaokataa kuona wageni asubuhi!”
“Hapa pia kwema!” Akatua. Ukimya wa sekunde mbili tatu ukapita. Mhasibu akasema.
“Nadhani sikutarajia kukuona asubuhi hii, naweza kukusaidia ndugu yangu!”
“Kabisa kaka! Hata mimi sikutarajia kuja kukutembelea asubuhi hii ila imenilazimu!”
“Nakusikiliza!”
Tarish akaliinua Briefcase lake na kuliweka mapajani. Akakibetua kifungo chake na briefcase ikafunguka. Mhasibu aliweza kuiona bastola iliyolala kitulivu pembeni mwa briefcase hiyo, hela za kutosha za Tanzania na Marekani. Tarishi akapeleka mkono nyuma ya Briefcase ile kulikokuwa na kitu kama mfuko hivi, akatoa bahasha moja yenye ukubwa wa wastani na kumkabidhi Mhasibu.
Mhasibu akaipokea na kuifungua, barua iliyotanguliwa na nembo ya chama tawala ikatokeza. Mhasibu akaisoma kimya haraka haraka na alipomaliza akaitua mezani kwake na kuikandamiza kwa mikono yake miwili juu ya meza hiyo. Akasema.
“Nadhani sijakuelewa Tarish!”
“Hujaelewa kitu gani? Barua haijaandikwa kiingereza hiyo, imeandikwa Kiswahili. Lugha adhimu kabisa ya taifa letu! Usinambie hujui Kiswahili kaka!”
“Kiswahili nakijua vizuri sana!”
“Kumbe usichoelewa ni kitu gani?”
“Sijaelewa kila kitu! Siajelewa maudhui ya barua nzima!”
“Lete nikusomee hiyo barua kwa sauti! Pengine utaelewa!”
“Sitaki unisomee, nataka maelezo!”
“Maelezo gani?”
“Ya pesa hizi!”
“Ark!” Tarish akakereheka. “Maelezo gani sasa. Barua inasema kuna fedha zinatakiwa mahala haraka sana. Maelezo gani unayoyataka zaidi? Au hujui kama mie natumwa tu wako wenyewe?!”
“Tulikubaliana kwamba fedha hizi ni kwa ajili ya kugharamia uchaguzi. Na Uchaguzi umekwishaisha. Hapa ninaandaa taarifa ya fedha hizo hizo inayotakiwa ikasomwe bungeni. Nasikia wapinzani wameshapata fununu juu ya fedha hizi na wameanza kuhoji. Ndio maana nataka unipe maelezo yanayojitosheleza kuhusu pesa hizi unazozitaka hivi sasa!”
“Sikiza Mhasibu!” Akaanza Tarish kwa msisitizo. “Uchaguzi ni jambo moja, makovu ya uchaguzi ni jambo jingine. Pengine wakubwa wanataka kutibu makovu ya uchaguzi. Tafadhali idhinisha pesa hizo zitoke!”
“Makovu ya Uchaguzi ndio nini?” Mhasibu akapuuza amri ya Tarish.
“Utaidhinisha pesa au huidhinishi?” Tarish nae akauliza. Mkono wake ukisafiri na kuifikia bastola ambayo ilikuwa ingali imelala pale pale katika Briefcase lililokuwa mapajani mwake. Mhasibu akaogopa.
“Lakini Tarish, matumizi tuliyokwisha kuyafanya ni makubwa sana. Na bado pesa hizi unazozihitaji ni nyingi pia. Huku tunakoelekea mwisho wa siku nitashindwa kujibu!”
“We ukiulizwa waambie waje watuulize sisi. Kwanza nani wa kukuliza?”
“Nimekwambia wapinzani wanaanza kupiga kelele! Nao huwa hawaji kuuliza hapa kama unavyokuja wewe. Wao huulizia habari maelezo au bungeni!”
“Ark! Wale mafala! Sikujua kama huwa unaogopa mafala!”
“Unanielewa vizuri sana!”
“Una maana gani?”
“Juzi mmoja amepeleka swali kuuliza kuwa amepata fununu kuwa fedha hizi zimetumika katika uchaguzi, kwa hiyo anataka kujua mpaka sasa ziko shilingi ngapi, wanaotudai ni akina nani na tuna mpango gani wa kuwalipa!”
“Sasa kinakutisha kitu gani? Wewe ndio umeshika funguo za hazina. Ndiye unayejua kuna kiasi gani. Au unadhani kuna mtu atakayekuja kukagua na kuhesabu shilingi moja baada ya nyingine baada ya jibu lako? Waambie ziko vile vile kama alivyoziacha rais Mstaafu Daniel Killango!”
“Na Bunge likiamua kubadilisha matumizi ya fedha hizo, badala ya kuwalipa wenyewe ziende katika matumizi mengine? Mie hizo fedha nitazinya wapi?!”
“Kitu kama hicho hakitatokea Mhasibu! Bungeni kusikutishe, tuna wabunge wengi mara tatu ya wabunge wao. We waache wapige kelele tutawashinda katika kupitisha au kutopitisha hoja! Umeelewa?”
“Lakini.... Lakini!”
“Au fedha zimekwisha?”
“No... No.... Sir! Haziwezi kwisha leo wala kesho. Bado zingali nyingi sana. Maana zilizochukuliwa ni moja ya nane ya pesa zote. Lakini sio za kwetu, zina wenyewe!”
“Wenyewe akina nani?”
“Usiniambe hujui pesa hizi ni za akina nani!”
“Kwa hiyo?”
“Hao wapinzani mkiwaburuza huko bungeni watakwenda mitaani na kuanzisha maandamano yasiyokoma. Maafa yanaweza kutokea katika kuzima maandamano hayo. Hili likatokea, vyombo vya habari vikakamata ajenda hiyo uwezekano wa kuwafikia wenyewe ni mkubwa kaka. Naomba...!”
“Nimekusikiliza kiasi cha kutosha!” Tarish akamkata kalima na kuongeza. “Katika uliyozungumza hakuna zima hata moja. Naona tu unazidi kunipotezea muda wangu wa thamani bure. Sasa nitakuuliza kitu kimoja, na nitakuuliza kwa mara ya mwisho kabla sijachukua hatua moja ya kipuuzi ambayo inawafaa watu kama ninyi. Je, utaidhinisha fedha au huidhinishi?”
Mhasibu Jamaldin hakuwa na jinsi. Akavuta droo na kutoa karatasi kadhaa akaziinamia na kusaini. Roho ilimuuma kuona kiasi kile kikubwa cha fedha, lakini ile bastola mikononi mwa Tarish ilimuonya kutofanya chochote. Alipomaliza akamkabidhi mgeni wake zile karatasi na kumpa maelezo machache ya mwisho. Alipomaliza Tarish akasimama tayari kwa kuondoka.
“Ukiendelea hivi, duniani patakuwa mahala bora kabisa pa kuishi kwako!”
Mhasibu akamtazama tu. Mawazo yakiwa mbali, alishindwa kujibu chochote. Akamkodolea macho Tarish hadi alipotoweka mbele ya macho yake. Kwa dakika kadhaa alibaki amejiinamia mbele ya Laptop yake kichwa kikimduru kama fotokopi. “Hali hii mpaka lini?!” Akajikuta akiropoka kujiuliza bila kupata jibu.
Alipoinuka akapata wazo. Akainua simu na kubonyeza nambari kadhaa. Simu ikaita kwa muda hadi ikakatika. Akaipiga tena na tena, hali ikawa ile ile. Akasonya na kutukana. Akabadili namba na kupiga namba nyingine. Safari hii iliita kidogo kabla haijapokelwa.
“Shikamoo Bosi!” Akasalimiwa simuni.
“Vipi Frank, funguo za hazina unazo?”
“Zitakuwa ofisini Bosi, Mie nimetoka mara moja kunywa chai!”
“Kwa nini unasema zitakuwa?”
“Mara hii umesahau kuwa ulinipigia asubuhi ukaniambia nimpe Matheo kuna dharura? Nilimpa na nikawa nimetoka. Ndio maana nakwambia zitakuwa ofisini!”
“Ooh! Sawa, kumradhi Frank!” Mhasibu akatahayari.
“Usijali!”
“Kwa hiyo uko wapi?”
“Steers! Nimekuja kupata chai!” Akajibu tena.
“Basi naomba ukirudi uje unione!”
“Haina shida mzee wangu, dakika kumi tu!”
“Sawa!” Akakubali na kukata simu.
Alijitahidi kufanya kazi kwa uwezo wake wote na kwa bidii ile ile ya aliyoanza nayo asubuhi bila mfanikio. Kila mara alikuwa akikosea au kuandika mambo yasiyo na mahusiano na kile anachokifanya. Mara kadhaa alifuta na kufuta na kufuta. Alipoona hana anchokifanya, aliifunga programu ya kufanya kazi, akafungua nyingine ya muziki. Akaanza kuburudika.
Dakika thelathini baadae Frank alimkuta katika hali hiyo.
“Nimefika bosi!”
“Vizuri!” Akajibu akiinuka na kulitungua koti lake nyuma ya kiti alichokalia.
“Yaelekea huna furaha bosi!” Alikuwa Frank kwa unyenyuekevu “Kumezidi kitu gani tena?!”
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment