Search This Blog

Saturday, 5 November 2022

EPA - 3

 








Simulizi : EPA

Sehemu Ya Tatu (3)







Aligundua kuwa ile ilikuwa stoo ya mkaa ambayo ilikuwa kilomita kama mbili hivi kutoka ilipokuwa hospitali ya taifa ya Muhimbili. Kutoka pale alipo mpaka barabara ya morogoro kulikuwa na umbali wa kama mita mia tatu au mia mbili na ndiko kulikokuwa na barabara ambayo bila shaka yalipita yale magari ambayo yalikuwa uani katika ile stoo.

Kwa makusudi kabisa akaacha kuitumia barabara hiyo, badala yake akaingia katika uchochoro mwembamba akipenya kichaka hiki na kutokea pale kabla hajauvuka mto ule mkubwa uliokuwa ukielekea muhimbili kutakamaki akatokea eneo ambalo ni maarufu kwa jina la kwa macheni.

Hapa akafaulu kukodi taksi iliyomchukua mpaka Kinondoni Mkwajuni, akaiacha na kuchukua nyingine mpaka Msasani. Halafu alichukua pikipiki iliyomfikisha kwake na kwa kutumia mlango wake wa siri aliweza kuingia ndani.

Kelele zilizokuwa zikipigwa katika mlango ule wa siri ambao huwa haufunguliwi mara kwa mara ndio uliomshtua mkewe ambaye usiku kucha hakuweza walau kutungua lepe la usingizi kutokana na wasiwasi uliomjaa kufuatia kutoonekana kwa mumewe ambaye hakuwa na kawaida ya kuchelewa sana kuingia nyumbani.

Tangu ilipojiri saa tano na usiku na mumewe kutoonekana, alianza kumpigia simu mumewe, simu ikaita mara moja tu bila kupokelewa, halafu haikupatikana tena. Alipopiga simu ofisini kwao aliambiwa mumewe alitoka kazini mapema tu. Alipompigia mlinzi wa familia labda anaweza kuwa anajua alipo, mlinzi alimjibu kuwa yeye hajui kwa kuwa aliachana nae mapema baada ya kuruhusiwa na mzee aende nyumbani kwake.

Kutoka hapo aliwapigia ndugu, jamaa na marafiki wengine bila mafanikio. Kuna wakati alifikiria kwenda polisi kutoa taarifa na kisha apitie katika vituo vya afya na hospitali kuulizia kama walipokea majeruhi yeyote mwenye sifa za zinazoshabihiana na mumewe, lakini mwanae Shuwena alikuwa amemkataza kufanya hivyo na kumtuliza akimtaka asubiri mpaka kesho yake.

Hivyo saa kumi na moja hiyo ya alfajiri aliposikia mlango usiotumika wa nyumba yao ukikorokochwa na baadae kufunguliwa, Nadia, Mke wa Mhasibu Jamaldin hakuweza kustahimili kuendelea kukaa kitandani, aliamka mara moja na haraka alikwenda nje ili kuona ni nani aliyeingia.

Akiwa sebule ya chini alikutana na Shuwena ambaye waliongozana pamoja kufungua mlango wa uani na kutoka nje. Walikutana hapa na Mhasibu.

“Hamjambo?!” Mhasibu akajaribu kusalimia. Sauti yake pia ikamsaliti, haikuwa na ule uzito uliozoeleka ambao mara zote huwa faraja kwa familia yake mara waisikiapo. Badala ya kujibiwa, ndio kwanza akachunguzwa vizuri. Ni wakati huu mkewe na mwanae walipoiona sura yake iliyokuwa na majeraha kadha wa kadha hali ikiwa imesawijika na kupoteza nuru.

Mshangao wao haukushia hapo, wakazishuhudia nguo za Jamaldin jinsi zilivyochakaa na kuraruka huku zile damu zilizotapakaa hapa na pale mwilini mwake zikiwatisha zaidi kiasi cha kufanya machozi yatafute njia katika kingo za macho yao.

“Jamaldin!” Mkewe akaita kwa kihoro bila kuitikiwa.

“Daddy!” Shuwena nae akaita kwa sauti iliyotaliwa na kilio.

“What wrong with you Jamaldin eeh!” Alikuwa mkewe tena kwa kiingereza akimaanisha kuna tatizo gani.

Jamaldin akashindwa kuyahimili machozi yake baada ya kuwaona watu hawa aliowapenda upeo wa kuwapenda wakibubujikwa na machozi kwa ajili yake. Hata hivyo akajikaza na kufuta machozi kabla hajawakabili na kuwakumbatia kwa upendo.

“Msihofu wapendwa, ni mambo ya kawaida!” Akawajibu.

“Mambo gani?”

“Ya kawaida tu, yatakwisha!”

“No Daddy! Hatuwezi kuyaacha hivi hivi! Una ngeu na majeraha mengi baba!”

“Nawaelewa sana malaika wangu. Hata hivyo nina njaa sana. Tafadhalini niandalieni chakula wakati ninaingia bafuni na kujimwagia maji. Nikishakula tutazungumza kwa tuo!” Akaomba.

Sasa wakaachiana. “Itabidi tumpigie Dokta Musa Malilo!” Shuwena akashauri. Ulikuwa ushauri muafaka kwa vile kila lilipotokea lolote lililohusu afya katika familia hiyo, ni yeye aliyekuwa akipigiwa simu kwanza, kabla ya kwenda hospitali.

“Hapana msimsumbue, Sijaumia sana! Mpigieni Samson Kidude aje mara moja!” Jamaldin akashauri. Samson alikuwa mlinzi wake binafsi. Yule ambaye alimruhusu aende kwake baada ya kutoka kazini.

“Lakini huwezi kujua kama umeumia mpaka daktari aseme mume wangu!” Mkewe akasema kwa huruma.

“Nimesema nina njaa jamani, au mnataka nifie hapa mlangoni!” Jamaldin akalalama kijanja. Lalamishi hili likawafanya wakurupuke kumshika na kumsaidia kuingia ndani walikomfikishia kumfikisha mesini. Shuwena akaanza kuandaa hiki na kile. Hali mama yake akimsaidia kuandaa tambi, maini na maziwa ambayo ilikuwa staftahi inayopendwa sana na Jamaldin.

Jamaldin akawatoroka na kuelekea bafuni, akajiloweka katika sinki la maji ya moto na kutulia humo kwa muda, alipotoka akalikabili sanduku lake la huduma ya kwanza na kufanya hili na lile katika kuhakikisha anarejea katika hali yake ya kawaida.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Mpaka anarejea katika chumba cha kupatia maakuli alikokuta kuna staftahi ya maana inamsubiri, muda wa kutosha ulikuwa umekatika. Mbali ya mkewe na mwanawe Shuwena, pia alimkuta mtu mmoja zaidi; Samson Kidude ambaye alishauri wamwite badala ya daktari.

“Hujambo Sam!” Akamsalimia akivuta kiti na kuketi.

“Sijambo mkuu, hofu kwako!”

“Kwangu kiasi salama!” Akajibu mwanaye Shuwena akimsogezea bakuli la maji na kumnawisha.

“Karibu chai Samson!” Mhasibu akamkaribisha

“Ahsante mkuu, nimeshakaribia!” Alikuwa Samson kwa upole akifunua kikombe cha chai na kujiwekea maziwa makavu yasiyo na sukari.

“Samahani kukusumbua, Sam!” Akaanza Mhasibu baada ya kujitilia tambi za kutosha, maini rosti na mboga za majani katika sahani yake, kabla hajaanza kula. “Sikudhamiria kukuita asubuhi hii, ila imenilazimu!”

“Usijali mkuu, tangu jana nilipopata habari za kutofika nyumbani na kutopatikana kwako katika simu, niliingiwa na jakamoyo na kufanya kila nililoweza lakini kwa mara ya kwanza jana nilijikuta kila nilichogusa kinashindwa kunifikisha ulipo. Leo nilikuwa na Plan B, baada ya ile A kushindwa kufanya kazi. Nashukuru Mungu kabla sijaianza nikawa nimepigiwa simu kuwa umerejea na unanihitaji!”

“Vizuri!” Alijibu Mhasibu akigugumia funda la maziwa yenye kahawa baada ya kupeleka fungu la kutosha la tambi liliambatana na finyango iliyoshiba ya maini. “Hata hivyo, sidhani kama hiyo plan B itafanya kazi, labda niisikie kwanza!”

“Kwa nini mkuu?”

Mhasibu Jamaldin akatabasamu baada ya kauli hii. “Usitake kunichekesha Samson, wewe ni mtu wa usalama!”

“Sijakuelewa!”

“Utaielewa tu!” Akatua tena na kupeleka msosi wa haja mdomoni “Plan B ilikuwa kwa ajili ya kunitafuta mimi. Na tayari mimi nimeshapatikana. Sasa Plan B ya nini tena?”

Ikawa zamu ya Samson Kidude kutabasamu vitamu. “Ni vizuri kuona umekiri mwenyewe kuwa mimi ni mwanausalama, hivyo kanuni za usalama nazijua. Utashangaa nikikwambia kuwa wakati huu hiyo plan B ndio inahitajika sana kuliko wakati ule ulipokuwa hujapatikana!”

“Kwa nini?”

“Swali zuri!” Alikuwa Samson tena, “Naamini kuna mahala ulikuwa siyo? Aidha kwa shari au kwa bahati mbaya. Tunahitaji kupajua mahala hapo na sababu zake. Ni bahati mbaya sana kuona wameingia katika anga zangu, mtu huwa haingii katika anga zangu na kubaki salama.

Kwa kujibu swali lako, kwanza tunahitaji kupajua, kujua sababu zake na kisha kupakomesha kabisa. Hata kama ilitukia kwa bahati mbaya, hatuhitaji bahati mbaya hiyo iendelee kutuandama!” Samson akatua.

Lilikuwa jibu sawia, jibu lililomgusa Mhasibu Jamaldin hadi chini kabisa ya uvungu wa moyo wake. Ni wakati huu alipoyafikiria mateso ya Ommy Killer na vile vitisho vya Tarish Michael Bagula, akajikuta akisisimkwa na mwili na moyo kumzizima kwa hofu. Kwa kila hali alikuwa mashakani, hofu ya kupoteza maisha yake ikiwa puani kabisa.

Ulikuwa ni wakati huu alipotaka kueleza kile kilichomkuta pale alipoinua uso na kuwaona mke na mtoto wake kwa pamoja. Ambao kwa kila hali walikuwa na kiu ya kujua ni jambo gani lililomtukia mzee wao mpaka ashindwe kurudi usiku, ashindwe kupatikana katika simu na arejee kama mtu aliyetapikwa na Nyoka.

Akajitahidi kupima athari za kisaikolojia zitakazoipata familia yake mara ukweli juu ya kutekwa kwake utakapodhihiri, akajikuta akirudisha moyo nyuma ili atafute namna ya bora zaidi ya kuzungumza na familia yake pasipo kuiumiza au kuiachia athari za kisaikolojia za muda mrefu.

“Nadia mke wangu!” Akamwita kwa upendo. Alikuwa mbioni kuimaliza staftahi ile maridhawa.

“Bee!” Mkewe akaitikia kwa upendo.

“Shuwena mwanangu!”

“Bee!”

“Kwanza poleni kwa mateso yote mliyoyapata wakati mkinitafuta. Hili linaashiria ule upendo wenu wa dhati kwangu ambao haupatikani kwa mtu mwingine yeyote zaidi yenu ninyi...” Angeweza kusema mengi kama simu yake ya dharura isingeita kwa fujo, mwito uliomfanya ahisi kuwa mambo si mazuri. Upesi akaiangalia na kuipeleka sikioni, akasikiliza kwa dakika chache tu, halafu akainuka na kwenda mbali kidogo ambapo alisikiliza kwa tuo zaidi, halafu akauliza swali hili. “Una uhakika Matheo?”

“Nina hakika Mhasibu. Hapa ninavyozungumza na wewe nimetoka katika kibano. Kibano ambacho kimenifanya niseme kila ninalolijua kuhusu mabilioni ya akaunti ya madeni ya nje!”

“My God!” Jamaldin akamudu kutamka akijihisi kama anayevuliwa nguo. “Walitaka kujua kuhusu nini?” Akauliza tena kwa kihoro.

“Kila kitu, fedha ni za nani, kwani umewafanya nini akina Alfred Omary Mbuzi?”

“Alfred Omary Mbuzi ni nani Matheo?! Na anahusiana nini na kibano chako?”





“Alfred ni Afisa usalama mwandamizi wa taifa hili Mhasibu, amelifanyia taifa vingi na mengi. Huyu unaweza kumuweka daraja moja na akina Willy Gamba na Joram Kiango, sema yeye hajaandikwa sana. Ni huyu aliyenitembelea alfajiri hii na kunipa kibano. Kwani umewafanya nini Mhasibu?!” Aliuliza tena katika simu.

“Na wewe umewajibu nini?”

“Nimewaambia ukweli, kwamba fedha ni za wahisani waliotukopesha. Nimewaambia kuwa tulidokoa kidogo kwa ajili ya kugharamia uchaguzi ili chama kirejee madarakani. Niliwaambia kuwa pesa zingali nyingi ila sijajua idadi yake na kwamba wewe ndiye unayefahamu kwa kina!” Akajibu Matheo na kumfanya Mhasibu azidi kugwaya.

“Hawajataka kujua kwa sasa fedha ziko wapi?” Akauliza tena.

“Mie niliwaambia zitakuwa hazina ingawa kulikuwa na mpango wa kuzitawanya katika mabenki mbalimbali ili ziingie katika mzunguko kwa njia ya mikopo zilete faida ya riba ambayo italinufaisha taifa mpaka pale wenyewe watakapokuja kuzichukua!”

“Ni hayo tu uliyowaambia?”

“Eeh! Pia walitaka kujua wewe uko wapi na ukiacha wewe ni nani mwingine anayeshughulika na hazina!”

“Mungu wangu!” Mhasibu akaguta tena. “Usiseme kama ulimtaja Frank Matheo!”

“Nilimtaja Mhasibu. Pengine hujui ila nilikuwa nikizungumza baada ya kubanwa na vizuri huku nikichomwa na kiberiti cha gesi katika nyeti zangu! Nisingeweza kuvumilia Mhasibu, kifo kilikuwa jirani sana kaka!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Efuuu!” Mhasibu akapumua kwa kihoro. “Sasa unanishauri nini ndugu yangu!”

“Kwani umewafanyaje Mhasibu? Ujue kiu yao kubwa ni kujua ulipo. Na ndio maana nimekupigia ili kukutahadharisha. Yaelekea wako njiani wanakuja kwako. Nimekutafuta katika simu yako ya mkononi ukawa hupatikani, ndio maana nimetumia hii ya dharura. Umewafanyaje kaka?!” Matheo akarudia kuuliza swali hili kwa mara ya mia moja na moja.

“Yako mengi kaka! Ila si busara kuyazungumza simuni. Kuna siri kubwa nyuma ya kibano chako na sababu ya kunitafuta. Nitakupigia baadae tuonane uso kwa macho nikueleze kinachoendelea. Ila kwa mtindo huu, itatuchukua karne kadhaa kuwa taifa linaloendelea!”

“Una maana gani?”

“Kufikia mchana wa leo, simu yangu itakuwa hewani tena. Tafadhali nitafute tutazungumza kwa urefu!” Mhasibu akaaga moyo wake ukiingiwa na uoga mwingine.

“Sawa kaka, ila...”

“Ila nini?”

“Jihadhari ndugu yangu!”

“Nitajihadhari!” Akajibu na kukata simu. Akili zikimduru na kufanya tafakuri ya kina. Aliona kuna umuhimu wa kubadili mfumo aliokuwa amejipangia ili kushughulikia matatizo haya. Mfumo ambao alijua unaweza kumfikisha katika mzizi wa tatizo hili haraka na hivyo kumfanya aung’olee mbali na kuanza kuishi maisha ya raha, furaha na bashasha badala ya maisha haya ambayo yanamfanya awe mkimbizi katika nchi yake mwenyewe.

Ilikuwa ni wakati huu alipouinua mkonga wa simu na kubonyesza tarakimu kadhaa alizozinakili vyema. Zilikuwa tarakimu alizopewa siku chache baada ya kukalia kiti kile cha ukurugenzi wa fedha katika benki kuu ya Tanzania. Bado anakumbuka kuwa alipewa namba hizi katika dhifa ya kitaifa iliyofanyikia ikulu baada ya kikao chake na Rais na Waziri wa fedha ambacho kilijadili namna ya kuipandisha thamani shilingi ya Tanzania inayoporomoka kwa kasi.

Alipomaliza kubonyeza tarakimu ya mwisho, simu ile ikawa ikiita.

Alisubiri kwa muda huku moyo ukimdunda kwa nguvu pale kifuani. Hazikupita dakika kadhaa akasikia chombo kikiinuliwa upande wa pili na kufuatiwa na sauti aliyoifahamu vyema.

“Hallow!” Ikaita sauti hiyo simuni.

“Shikamoo mzee!” Akasalimia. Ni wakati sauti inatoka ndipo alipogundua kuwa ilikuwa na kitetemeshi. Akajitahidi kujikaza ili sauti yake isimsaliti zaidi.

“Marahaba, hujambo?” Akajibiwa.

“Sijambo mkuu! Ni Mhasibu Jamaldini hapa. Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania...”

“Naelewa!” Akakatishwa na sauti ile nzito ya upole ambayo huwa haimtambulishi muongeaji kama amechukia au ana furaha. “Kwema lakini?!” Sauti ile ikaongeza.

“Sio kwema Mkuu! Nahitaji kukuona vibaya mno. Nina tatizo kubwa sana, kubwa mno!”

“Ni kweli Jamaldin, hata mimi naona hivyo!” Mtu yule upande wa pili wa simu akasema kwa upole hali sauti yake ikionyesha kile kile kitu ambacho sio Jamaldin pekee ambaye huwa anakiogopa, bali wote wanaofanya nae. Shauku! Naam ilikuwa shauku ya hali ya juu ya kutaka kukijua kitu kimtatizacho Jamaldin.

Ni shauku hii ndiyo huwatisha wasaidizi wake, maana ile sura yake ya kitoto na tabasamu ambalo mara nyingi huutembelea uso wake, vilikuwa vitu ambavyo wasaidizi wake walishindwa kujua kuwa bosi wao amechukia ama amefurahi. Lakini anapoitumia sauti hii, kila mtu hujua kuwa sasa mzee hataki mchezo. Mtu yule akaongeza “Mtu huwa hapigi simu hii, mida kama hii halafu akataka akusalimie. Njoo ofisini kwangu baada ya dakika kumi na tano. Nitakuwa pale nakusubiri!” Akajibiwa na bila kusubiri jibu simu ikakatwa.

Kijasho chembamba kikamtoka. Hata hivyo alikuwa na turufu bado. Bado aliamini kwa kiasi kikubwa hana kosa alilolifanya ambalo linatishia kugharimu maisha yake. Hivyo hatua hii ya kumpigia simu Mkuu wa nchi na kupata miadi ya kukutana nae aliona itakuwa wakati muafaka kwake kulifanya lile ambalo amekuwa akilihofia muda wote.

Taratibu akautua mkono wa simu chini na kurejea mezani ambako aliwataka radhi mkewe na wanawe na kuwaambia atazungumza nao baadae kwa sasa ameitwa Ikulu. Familia yake ililikubali jambo hili kwa shindo upande, ikaondoka sebuleni kinyonge.

Alipobaki na Samson alimpa maelekezo machache kisha wakatoka nje, safari ya kuelekea Ikulu ikaanza. Mhasibu Jamaldin mbele akiendesha Grand Vitara na Samson akimfuatia nyuma akiendesha Toyota Harier huku akiwa ameacha nafasi ya kutosha baina ya gari lake na lile la Mhasibu Jamaldin.



* * *

“Mkuu, mwali ndiyo huyo anatoka, ila ana mkia nyuma yake, nifanyeje?” Mtu mmoja aliyekuwa hatua chache toka ilipo nyumba ya Mhasibu Jamaldin akisingizia kuharibika kwa gari yake akaongea katika simu yake ya mkononi.

Mtu huyu alikuwa amefika hapa tangu walipotaarifiwa kuwa Mhasibu amempiga mwenzao na kitu kizito kichwani na kutoweka. Ambapo walianza kufuatilia wapi anaweza kuwa na huyu ndiyo akawa ameagizwa kuja hapa katika nyumba hii ili kama atamuona Mhasibu anaingia katika nyumba hiyo, atoe taarifa na ikiwezekana amteke upya na kumrudisha katika himaya yao.

Tangu amefika hapa, hakuwa ameona chochote, hii ni kwa vile Mhasibu alirudi nyumbani kwake kwa kutumia njia za panya na kuingia kwa kutumia mlango wa dharura ulipo nyuma ya nyumba yake. Hata hivyo, ni muda mfupi tu uliopita, mtu huyu alikuwa amepokea simu kutoka kwa bosi wake huyu huyu akimtaka awe makini kwani wamepata uhakika kuwa Mhasibu amesharejea nyumbani, na wao wanajipanga kuja kumkata tena.

“Umesema ana mkia?” Akaulizwa simuni.

“Ndiyo! Kuna mtu anamfuatilia na Toyota Harrier!”

“Well. Mchezo unaanza kuwa mtamu. Wafuatilie kama kivuli mpaka nitakapokupa maelekezo mengine. Hakikisha hawagundui chochote! Sawa?!”

“Sawa!”

Simu ikakatwa, jamaa akafungua mlango wa gari, akalifuata boneti la gari yake lililokuwa wazi, akauchomoa ule waya ulioushikilia mfuniko wake, akaulaza mahala pake kwa utulivu, kisha akautua mfuniko wa boneti lile likaifunika injini barabara, halafu akarudi ndani ya gari yake, akaiwasha, akaingiza gia na kuiondoa taratibu. Safari ya kumuandama Mhasibu na mkia wake ikaanza.

“Kwa hiyo Matheo ameamua kuunguza picha siyo?” Castrol alimuuliza Tarish baada ya Tarish kumaliza kuzungumza na yule jamaa aliyemuagiza amfuatilie Mhasibu.

“Inavyoelekea!”

“Dah, ndiyo maana mie nilishauri Matheo auawe tu ila Alfred na uoga wake akasema bado kwanza. Sasa itakuwaje maana Mhasibu ana mkia sasa hivi!” Tarish akalalama.

“Wewe ndiye uliyefanya uzembe Tarish! Unajua kabisa kuwa Mhasibu aliwahi kuwa mwanajeshi, ukamuacha na walinzi goi goi! Unadhani walikosea waliosema Simba hazeeki maini?! Yule alistahili kubaki na Killer tu!”

“Tatizo la Killer ana hasira sana, anaweza kumuua kabla hatujatimiza lengo letu. Hata hivyo Mhasibu yuko under control sasa, wakati wowote, muda wowote anaweza kuwa chini yetu na nitahakikisha sifanyi makosa tena!” Akatua Tarish

“Vipi Alfred ameweza kuambua lolote?”

“Bado Alfred anafanya juhudi za kujua mtu wa mwisho aliyezungumza na Mhasibu ni nani kwa kumtumia mtu wetu wa IT. Muda si mrefu tutakuwa na majibu!”

“Mmejuaje kama Mhasibu amezungumza na mtu mwingine baada ya Matheo?”

“Baada ya Mhasibu kukata simu na sisi kugundua kwamba Matheo amezungumza asiyotakiwa, labda kwa kuwa mie nilikuwa nikikagua vitu vingine wakati yeye akiongea, tulimlazimishe apige simu upya ili amwambie wakutane muda huu huu na sisi tuweze kumakamata Mhasibu.





Matheo alipojaribu kumpigia tena, simu ikawa inatoa majibu kuwa inatumika. Pale ilipopatikana, mkewe akasema ametoka atarudi baadae. Mie nafikiri huruma zetu sasa basi, tunapaswa kuingia kazini mara moja!” Castrol akasema kwa uhakika.

“Una maana gani?” Tarish akauliza tena.

“Unajua sikio la kufa halisikii dawa mpaka liwe jikoni linatokota tayari kwa supu. Yule Matheo tumemtaka ampigie simu Mhasibu kujua kama amerudi kwake au lah. Yeye amemwambia na mambo mengine yasiyomuhusu. Huyu anapaswa kuwa mgeni wa kuzimu mara moja.

“Hilo litafanyika kwa usahihi wake leo hii. Ila Alfred ndio kikwazo!

“Najua ni nini kinasababisha huruma za Alfred. Hilo nitalishughulikia!” Castrol akampa moyo na kuongeza. “Umesema Mhasibu yuko under control sasa?”

“Ndio! Kuna mtu anamfuatilia, wakati wowote ntamuamuru amteke kwa zile mbinu zetu za hali ya juu na kumrejesha mikononi mwetu. Ila ana mkia nyuma!”

“Huo mkia muukatilie mbali! Tunahitaji kuutimiza mpango wetu haraka ili hili genge lisambaratike tuangalie ustaarabu mwingine!”

“Hilo ni jema!” Akamaliza Tarish wakaagana.

Dakika kumi baadae, Tarish akapokea simu kutoka kwa mtu wake, kuwa gari ya Mhasibu imeingia Ikulu. Taarifa hizi zikamchanganya akampigia Castrol simu, simu ikaaita mara nyingi bila kupokelewa. Akaachana nae na kumpigia Alfred.

“Sema Tarish!” Alikuwa Alfred.

“Salama mkuu, nampigia Castrol simu hapokei!”

“Nami hapa nilikuwa namtafuta, hajapokea simu. Kulikoni?”

“Tulikuwa tunamfuatilia Mhasibu baada ya kutoroka, Mhasibu ameingia Ikulu! Sa sijui tunafanyaje?”

“Hilo ndilo nililokuwa nikimtafutia Castrol ili muangalie namna ya kuzitimiliza hizi intelejensia. Maana mtu wa IT ameniambia kwamba Mhasibu ameongea na Rais Jacob Chaguo muda mfupi uliopita. Na kama hicho uniambiacho ni cha ukweli basi watakuwa wamekwenda kuonana!”

“Sasa tunafanyaje?!”

“Ammm! Ngoja nitakupigia baadae!”

“Sawa, wacha nielekee huko. Huyu Mhasibu anajipalia makaa. Ndio maana waswahili walisema mbwa ukimzoea sana atakufuata mpaka msikitini. Nitawapa taarifa baadae!”

Akamaliza kukata simu na kuirejesha mkononi. Akaitupia jicho saa ya ukutani. Muda ulikuwa unakimbia sana. Upesi akalichukua koti lake refu na kulivaa kulivaa upesi upesi, kichwani akaweka kofia ya pama na kuvaa vile viatu vyake vya kazi vinavyofanana sana na viatu vya jeshi. Hivi vikiwa na rangi nyeusi. Alipoweka na miwani myeusi usoni akawa amependeza sana.

Akasogea dirishani na kuangalia nje. Magari zaidi ya manne yalikuwa yametulia katika eneo la kuegeshea magari la nyumba hiyo iliyokuwa Oysterbay Msasani. Kulikuwa na Toyota Harrier, Pick up Hardboard, Toyota Corolla Sedan na Toyota Land Cruiser VX.

Macho yake yakatulia katika ile gari ya mwisho, Toyota Land Cruiser VX. Ilikuwa gari mpya na nzuri zaidi yenye rangi ya jeshi. Zile ngao kubwa za chuma cha pua zilizofungwa mbele na nyuma kwa ustadi wa aina zikilifanya livutie zaidi.

Kutokana na shughuli anayokwenda kuifanya, akaona gari hii hii itamfaa zaidi. Sio tu kwa kuwa lilikuwa na vioo vyeusi pekee, bali ile kasi yake na uwezo wa gari ile ukiachilia mbali uimara vilikuwa sababu nyingine iliyoumfanya aamue kuitumia gari hii.

Akaingia ndani, akachukua funguo akatoka na kujipakia ndani ya gari hiyo, akachoma mafuta na kuelekea viunga vya Ikulu.

Hakusahau kuiweka bastola yake vizuri.



Sura ya Tano

Jacob alipoingia katika ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jacob Kinara Chaguo ile saa kumi na mbili kasorobo asubuhi; alitarajia kukuta ofisi ikiwa tupu na kwamba Chaguo angeenda kuitwa baada ya yeye kuwa amefika. Kinyume chake alimkuta Rais amekaa katika kiti chake maridhawa kilichozidia uzuri wa vile viitwavyo Executive.

Alikuwa akisoma gazeti la Daily News huku kikombe chake kidogo cha rangi ya fedha kilichokuwa juu ya meza ile kikifuka moshi taratibu. Harufu nzuri iliyokuwa ikijaribu kushindana na manukato ya Airfreshner yaliyopuliziwa humo ndani yakimjulisha Mhasibu kuwa ile iliyokuwa ikifuka moshi ilikuwa kahawa chungu.

Mwenyewe Jacob Chaguo alikuwa amependeza ndani ya suti yake nzuri ya pande tatu rangi nyeusi iliyomkaa vyema, hali ile meza ya rangi ya dhahabu iliyokuwa mbele yake ikiwa na faili moja, vitabu vichache, tufe la ramani ya dunia, pamoja na yale maandishi ya Hon. Exellence Jacob K. Chaguo President of United Republic of Tanzania yaliyochongwa kiufundi katika mbao ya Surplus kwa pamoja vikiifanya ofisi ile kuwa nadhifu na inayovutia sana.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Jacob alijikaribisha katika mojawapo ya sofa mbili zilizokaa ubavuni mwa meza ile ya Rais baada ya kumsalimia Chaguo kwa mara nyingine tena. Sofa alizokalia, zikabonyea na kumbana kidogo hali zikiupokea uzito wake vizuri na kumfanya ajisikie starehe isiyo ikifani. Naam, zile zilikuwa sofa nzuri sana za rangi ya kahawia ambazo kuzikalia kwake ilikuwa burudani tosha na daima zilimfanya aliyezikalia asitamani kuondoka.

“Nimefika mkuu!” Jamaldin aliongea kwa unyeyekevu huku akiinua uso kumtazama Rais Chaguo moja kwa moja usoni.

“Nakusikiliza!” Chaguo akajibu huku akilitua gazetile chini, kukisogeza kikombe cha kahawa pembeni na huku akiikutanisha mikono yake mezani na kuyatua macho moja kwa moja katika uso wa Mhasibu. Mhasibu akahisi kama anayetazamwa mpaka katika utumbo. Akayakwepa macho ya Chaguo kwa kujifanya anaangalia vitu vingine humo ofisini, kabla hajasafisha koo na kuanza kueleza.

“Kwanza kumradhi mkuu!”

“Kwa...?”

“Kwa hiki nitakachokueleza, pengine ntakuwa nakukwaza, pengine ntakuwa nakuvunjia adabu na pengine kukuletea tatizo hili kwa wakati huu inaweza kukupunguzia utulivu wa nafsi na kukufanya usifanye mambo yako kwa ukamilifu wake...”

“Go Strictly Jamaldin. Dont go around the bush!” Chaguo akamkatisha akimtaka aache kuzunguka, aeleze kilichompleka.

“Ni kuhusu akina Tarish Mzee! Walinipa kazi, nikaifanya kwa uwezo na moyo wangu wote kutimiza makubaliano yetu, nilipoona wanaanza kukiuka makubaliano tuliyojiwekea; nikaamua kuzuia. Sasa wanataka kuniua!” Akatua akimtazama Rais Chaguo usoni.

Akajikuta akitazamwa vizuri kwa umakini wa hali ya juu mithili ya fundi saa anavyoiangalia saa ya thamani kutafuta tatizo liisumbualo. Hili likaufanya moyo wa Tarish ushtuke. Mtazamo ule ulimjulisha kitu kimoja muhimu, kwamba Rais alikuwa hajamuelewa. Kwa nini asimuelewe? Akajiuliza moyoni hivyo kabla hajalijibu swali hili, akatupiwa swali jingine

“Tarish ni nani?” Alikuwa Chaguo akimtazama Jamaldin moja kwa moja usoni.

“Ni Afisa wa chama pale Makao Makuu. Hufanya kazi chini ya Johstone Mambo!”

Jina la Mambo likamkumbusha lile sakata la ule mchezo mchafu aliotaka kuchezewa wakati ule wa kutafuta mgombea katika chama. Akahisi kuna jambo zito zaidi analotaka kuambiwa. Hili likamfanya azidishe utulivu.

“Kwa nini wanataka kukua?”

“Wanataka niendelee kuwapa hela zaidi, hela zenyewe hakuna! Mi ntabakia kwenye matatizo bure na bado wao hawanielewi na wanataka na kuniua pia!” Sasa alianza kuwa huru, jazba ikianza kumnyemelea.

“Uendelee kuwapa hela?! Hela gani?! Za nini na uwape hela kwa misingi ipi?”

“Hata mimi nashangaa mkuu!”

“Kwani uliwahi kuwapa hela?”

“Ndiyo niliwahi kuwapa, tena nyingi tu!”

“Kiasi gani?”

“Kama bilioni mia tano!”

“My God!” Chaguo akamudu kutamka. “it is a lot of money!”

“Uliwapa za kazi gani?”

“Waliniambia ni za kukiweka chama madarakani!”

“Kitu gani?”

“Eeh! Na nilipigiwa simu na Johnstone kuthibitisha hilo, kabla nami sijatafuta ushauri kwa Mkuu wa jeshi la Polisi na Afisa wa juu pale jeshini. Waliponithibitishia ndio nami nikawapa fedha!”

“Kwa hiyo uliwapa fedha kutoka hazina?!” Moyo wa rais ulikaribia kuchomoka kifuani kwa kupiga kwa nguvu. Alijua ile hazina ya kutosha ya kujivunia ya fedha za kigeni ambayo aliachiwa na Rais Daniel ilikuwa imekwenda na maji!

“Hapana! Niliwapa kutoka katika ile akaunti ya madeni ya nje! Na...”

“Oh My God, oh My God!” Rais akashtuka kuweweseka, akishangaa kwa dhati.

“Jamaldin uliwezaje kufanya maamuzi magumu na mazito ya kutapanya fedha za ngama za taifa kwa urahisi kiasi hiki enhe?! Nani alikwambia Johnstone Mambo na huyo Tarish nani sijui ni watendaji wakuu wa chama?! Usinambie mpaka umri huo hujui taratibu za chama na Serikali kutoa fedha nyingi kiasi hicho!”

Eh! Haya yalikuwa maajabu mapya. Maajabu ya dhati. Kwa mara ya kwanza Mhasibu akatambua kuwa alikuwa ameingizwa mjini.

“Na kwa nini hukuomba ushauri hata kwa Rais Daniel Killango?” Alikuwa Chaguo kwa jazba lile tabasamu lake likiwa limetoweka. Akaendelea kufoka “Kwa nini hukutafuta uthibitisho zaidi au kutaka kujiridhisha kwanza? Kwa nini hukuniuliza hata mimi kabla?”

Mhasibu akababaika asijue aseme nini. Yeye aliamini anakisaidia chama kwa dhati. Na tayari alipiga simu mbili kwa wakubwa zilizomuhakikishia uthabiti wa mipango hii. Sasa ni uthibitisho gani angeutafuta zaidi. Akajitutumua na kujibu.

“Ni... Ni... Nilijua mko pamoja mkuu, dhamira yangu ilikuwa safi lakini!”

“Pamoja kwenye kuchota na kuiba mabilioni ya Taifa? Mabilioni ya watu masikini wa nchi masikini kama yetu!!. No Sir ndugu, mie siko hivyo hata kidogo. Pengine ulikuwa hujui kuwa niliamua kugombea wadhifa huu mkubwa kabisa nchini ili kuwasaidia wananchi kufikia ndoto zao za maendeleo, ili kupambana na ufisadi na uzembe mwingine kama huu ambao unarudisha nyuma juhudi za taifa kujikwamua kutoka katika umasikini uliotamalaki kila pembe ya nchi hali tunazo rasilimali za kutosha!” Rais akapumua.

Mhasibu Jamaldin akagwaya vibaya sana.





“Sikiliza Jamaldin, umefanya uzembe mkubwa. Umefanya uzembe wa hali ya juu. Uzembe ambao sio tu umeligharimu Taifa pekee na wananchi wake, bali pia utakugharimu na wewe pia kama fedha hizo hazitarejeshwa hazina ndani ya siku ishirini na moja kutoka sasa. Huwa sivumilii uzembe. Huyo Tarish akija kwako mwambie namwita na wewe toka!” Akahitimisha.

Mhasibu, akaendelea kukaa akitafuta jambo la kusema ili mwisho wa mazungumzo yake na rais uwe mzuri. Huu haukuwa mwisho alioutaka kabisa.

“Nimesema tokaaah! Ebo!” Rais akafoka akiigonga meza kwa nguvu. Dakika hiyo hiyo wakaingia maafisa usalama wawili mmoja akiwa na bastola mkononi. Jamaldin alipowaona hakusubiri wamshike.

Akasimama mwenyewe na kutoka nje kinyonge hali wale maafisa wakimsindikiza kitemi huku wakiwa tayari kumshughulikia kama angefanya jambo lolote kinyume. Wakati huu mawazo yakiwa zigizaga kichwani mwake, Mhasibu alijiona kama asiye na bahati akiwa ni zaidi ya mtu aliyezama katika dimbwi la mavi.

Tangu amemjua Rais Jacob Chaguo hakuwahi kumuona akiwa amekasirika kiasi kile. Na kule kufukuzwa kwake ofisini ilikuwa ishara tosha kuwa kama kuliwahi kuwa na mahusiano yoyote ya kikazi, ujamaa, urafiki au undugu baina yake na Rais Chaguo; basi uhusiano huo ulikuwa umezikwa rasmi siku hiyo.

Naam! Salama yake ilikuwa moja tu, kuhakikisha fedha hizo zinatoka mikononi mwa akina Tarish na kurejea hazina kama Tarish alivyohitaji. Akijua jukumu hili lilikuwa sawa na kumlazimisha ngamia kupenya kwenye tundu la sindano, Jamaldin alijikuta akilisahau gari lake pale katika viwanja vya Ikulu na kutembea taratibu kutoka nje ya geti.

Ni askari wa getini ndio waliomkumbusha gari lake, akarudi ndani na kuingia ndani ya gari. Akaliwasha na kumpigia Samson simu kumtaka warudi nyumbani wakajadiliane cha kufanya, kichwani akiwaza kuwa ni lazima amwambie Samson ukweli ili amsaidie kuhakikisha fedha hizo zinarejea hazina.

Samson alipomkubalia tu, Mhasibu akaingiza gia na kutoka akakamata njia ya kuelekea feri, akakunja kushoto na kutokea nyuma ya Ikulu, Samson akiwa nyuma yake wakaanza kuitafuta barabara ya Ally Hassan Mwinyi.

Walipofika katika njia panda inayoelekea viwanja vya Gymkhana, huku gari ya Mhasibu ikiwa mbele kabisa; walisimama kwa muda kusubiria magari ambayo yalikuwa yakitokea mtaa wa Ohio yaingie katika barabara yao kisha wao waendelee na safari.

Ilikuwa ni wakati huu Toyota Land Cruiser VX rangi ya jeshi ilipotokeza katika barabara inayotoka viwanja vya Gymghana ikiwa katika mwendo wa kasi kweli kweli, ikaja na kuigonga kwa nguvu gari ya Mhasibu ubavuni. Kishindo kikubwa kikatokea huku gari ya Mhasibu Toyota Grand Vitara ikisukumwa na kupinduka mara mbili kabla haijazuiliwa na ukuta uliojengwa ufukweni mwa bahari ya hindi.

Bila ukuta ule, gari ya Mhasibu ingeangukia baharini.

Samson Kidude ambaye alikuwa ndani ya gari yake nyingine, hatua kadhaa nyuma ya gari ya Mhasibu alijikuta akipiga yowe kubwa “Noooh!”, akafunga breki kali za ghafla huku akifungua mlango na kutoka bastola mkononi kukimbilia kule ilikotokea ajali.

Hata kabla hajafika, alishuhudia ile Land Cruiser VX ikirudi nyuma kwa kasi na kuigonga gari ya nyuma yake, ambayo nayo iligonga gari jingine nalo likagonga jingine. Ikawa ajali ya magari mengine kadhaa kwa nyuma.

Halafu dereva wa Land Cruiser VX akafunga breki kali, kisha akakata kukata kona nyingi kushoto. Kisha akaiondoa kwa kasi kubwa kuelekea kushoto, akipita katika njia yenye nyasi nyingi ambazo zilikuwa zimeota sehemu kubwa ya eneo hilo. Hili lilimfanya akwepe magari haya na yale mpaka alipoipata barabara kwa mbele ambapo alikanyaga mafuta zaidi na kutoweka.

Samson akijua jamaa ndio anatoweka, aliinua bastola yake na kulirushia lile gari risasi tatu kabla risasi katika bastola yake hazijaisha. “Shit!” Akaguta na kurudi mbio katika gari lake. Hii ilikuwa baada ya kukubaliana na mawazo yake kuwa muda ulikuwa haumruhusu kuongeza risasi na kulizuia lile VX.

Akafungua mlango wa Toyota Harrier, akalitia moto na kutoka katika mstari wa foleni ya magari, akapenya hapa na pale mpaka akajikuta akirudi katika barabara ile kwa mbele zaidi, wakati huo huo VX ikitoweka mbele ya macho yake. Akaongeza moto na alipofika usawa wa Hoteli ya Courtyard, akashuhudia ile Land Cruiser ikiingia katika barabara ya Ally Hassan Mwinyi na kukamata uelekeo wa Moroco kama sio Mwenge.

Alipofika katika mataa, gari zinazotoka Salender Bridge zikawa zimeruhusiwa na kumfanya ashindwe kuingia katika barabara ya Ally Hassan Mwinyi. Akajaribu kuangalia kushoto na kulia kama kulikuwa na pikipiki ili aitumie kulifukuzia lile gari, haikuwepo! akafanya fujo na kuilazimisha gari yake kuingia barabara ya Ali Hassan Mwinyi bila kuruhusiwa na taa za barabarani za kuongozea magari.

Milio ya kulalamika kwa tairi ikatokea wakati gari zinazokwenda mjini zikifunga breki kwa nguvu kuepuka kuigonga ile Toyota Harrier. Hali hii ilimkuta pia katika ile barabara ya upande wa pili wa Ali Hassan Mwinyi ambayo ilikuwa ikielekea Morocco. Kutahamaki akawa ameipata na nafasi na kuingia barabarani sawia.

Mbele yake kule aliona ile VX ikikata kulia na kuingia mitaa ya Oysterbay. Akakanyaga mafuta kwa nguvu zaidi. Gari ikaunguruma kwa nguvu zaidi huku ikiongeza kasi kama ndege inayotaka kupaa, na sasa ilikuwa katika kasi kubwa kabisa. Alipoingia ile mitaa ya Oysterbay hakuona chochote. Akajaribu kumuuliza huyu na yule bila mafanikio.

“Shit!” Akaishia kuguta akirejea katika gari lake na kurudi kule ilikotokea ajali ya Mhasibu Jamaldin.

Alikuta watu wameshajaa na kuizunguka gari ya ajali. Vibaka ambao hushinda wamezagaa katika mwambao wa ufukwe huu wa bahari ya hindi walikuwa wameanza kuwasili katika eneo la tukio na sasa walikuwa wakifanya juhudi ya kuiba kila walichoweza. Kwa mbali alisikia ving’ora vya Polisi kuashiria kuwa Polisi walikuwa njiani wakija.

Akaingia ndani ya kundi lile la watu na kuwasogeza nyuma zaidi.

Jamaldin alikuwa ameng’angania katika mlango wa gari ile iliyokuwa ingali imepinduka, huku chini yake kukitengeneza kijidimbwi kidogo cha damu. Aliweza kuyaona pia mataa ya ile Land Cruiser yaliyovunjika yakiwa yametapakaa pale chini.

Kwa kushirikiana na raia wengine walifaulu kumnasua na kumlaza chini, ambapo walimlegeza Tai, kumfungua kamba za viatu na vifungo. Alikuwa ameumia vibaya sana na Samson akajua kuwa Mhasibu hataweza kuishi kwa muda mrefu.

Polisi walifika, wakawatawanya watu na vibaka. Samson kwa kushirikiana nao, walimuweka Mhasibu katika gari lake na safari ya kuelekea Aga Khan hospital ikaanza. Ilikuwa ni wakati huu Samson alipokumbuka kuwapigia simu watu wanaofanya kazi na Mhasibu na kuwajulisha kuhusu ajali ile, kabla hajaijulisha pia familia yake.



* * *

“Pumbavu!” Rais Jacob Chaguo alimsindikiza Mhasibu na tusi hilo mara tu alipoufunga mlango wa ofisi yake na kuondoka. “Eti nilidhani mlikuwa pamoja? Serious kabisa! We unamjua Kinara Chaguo au unamsikia? Kinara awe pamoja na mafisadi! Wezi wa mali za umma! Sasa subiri nikuonyeshe Jacob Kinara Chaguo ni mtu wa aina gani!” Akatua akivuta simu na kupiga mahala.

“Nakuomba uje ofisini mara moja!” Akatoa amri na kukata simu.

Halafu akaigeukia kahawa yake na kuipeleka mdomoni. Ladha yake ilikuwa inaanza kuwa mbaya kutokana na kupoa, akaisogeza pembeni, mkono wake ukazama mahali na kuibuka na kikombe kingine kama kile cha mwanzo. Akajimiminia kahawa nyingine kutoka katika birika dogo la umeme ambalo lilikuwa chini ya meza yake; na kuanza kuinywa taratibu.

Ni wakati huu mlango wa ofisi yake ulipofunguliwa tena, na Katibu wake Thadeo Elias Makoa akaingia. Kama kawaida yake alipendeza ndani ya suti ile ya kaunda rangi ya maziwa, hali tabasamu lake likiifanya sura yake ambayo wengi waliita sura ya kitoto kuchanua wakati wote. Ni sura hii iliyomfanya aendelee kuonekana kijana wa miaka ishirini na ushei wakati umri wake ulikuwa ukikimbilia miaka hamsini sasa.

“Shikamoo Mkuu!” Akasalimia.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Marahaba Makoa hujambo?”

“Sijambo Mkuu, nimeitika wito!”

“Vizuri! Nimekwita hapa kwa mambo mawili makubwa ambayo nahitaji uyafanyie kazi kwa uhakika na ufanisi wa hali ya juu, maana majibu yake nitayahitaji haraka sana. Yaani haraka mno. Umenielewa lakini?! Nina maana haraka iwezekanavyo!”

“Kabisa mkuu!”





“Kuna ufisadi wa kutisha i mean wizi wa fedha za umma umefanyika katika Benki Kuu ya Taifa wakati wa uchaguzi mkuu. Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Benki kuu Mhasibu Jamaldin, wizi huu umefanywa kwa ushirikiano wa watu mbalimbali waliomo ndani ya Chama, Serikalini, vyombo vya Ulinzi pamoja na benki kuu yenyewe ambao hatuwafahamu kwa majina, ingawa wapo watu wa kuwahisi!” Akatua na kupiga funda jingine zito la kahawa chungu.

“Kazi zako zitakuwa mbili tu, kwanza nataka uunde Tume thabiti yenye watu watano ambao watachunguza sakata hili na kutupa majibu sahihi ndani ya wiki moja ikizidi sana mbili. Tume ifanye kazi yake kwa weledi na ufanisi mkubwa. Ongea na Katibu mkuu hazina kuangalia namna Tume hii itakavyowezeshwa kufanya kazi zake bila shida ili kuleta majibu ndani ya muda mfupi.

Andaa barua ya kumsimamisha kazi Mhasibu na nitakapokuwa nikiitangaza Tume hii, pia nitautangazia umma kuwa nimemsimamisha kazi Mhasibu Jamaldin kutokana na uzembe huu. Masaa machache kutoka sasa nataka niwe na orodha ya watu uliowapendekeza na sababu za kuwapendekeza.

Jambo la pili naomba uniitie Kiongozi wa Idara ya Ulinzi na usalama wa Taifa ndugu Chillonga Anderson Chillonga. Nataka naye atumie njia zake za panya kuhakikisha suala hili haliwi mwanzo wa machafuko nchini, ikiwa ni pamoja na kutufikisha kwa wahusika halisi ili pamoja na mambo mengine, tuweze kuwatia nguvuni!”

“Sawa mkuu!”

“Unaweza kwenda!”

Thadeo akainuka na kutoka nje alikoanza kufanya shughuli alizotumwa.

Dakika chache baadae, Rais Jacob Chaguo alikuwa amepokea mgeni mwingine tena. Chillonga Anderson Chillonga. Maelekezo yake kwa Mzee Chilo yalikuwa mafupi baada ya kumueleza kwa ufupi kile kilichojiri katika benki kuu.

Kwamba anahitaji watu hawa wawe wametiwa nguvuni chini ya ushahidi wenye mashiko na ndani ya muda mfupi. Chillonga alilipokea jukumu hilo kama ambavyo huyapokea majukumu mengi anayopewa, halafu akainuka, akapiga saluti na kuondoka.

Mpaka kufikia jioni ya siku hiyo, Tume ya Rais ilikuwa imeundwa, kupewa hadidu za rejea na kuapishwa. Wakati wa kuiapisha, waandishi wa habari walikuwepo na ni hapo Rais alipoieleza jamii kazi na umuhimu wa tume hiyo, na akamalizia kwa kumsimamisha kazi Mhasibu Jamaldin kwa muda mpaka Tume aliyoiunda itakapomaliza uchunguzi wake.

Waandishi walipoulizia sababu za Mhasibu kusimamizishwa walijibiwa kuwa amesimamishwa kwa uzembe alioufanya wa kushindwa kuzisimamia vyema rasilimali za taifa, kiasi cha kuruhusu mafisadi kujichotea fedha za ngama za taifa na zingine kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

Rais aliwahakikishia watanzania kuwa fedha zilizoibiwa na zilizopotea zitarudi Serikalini ndani ya muda mfupi na wahusika watafikishwa mbele ya vyombo vya maamuzi ili sheria ichukue mkondo wake.

Moto uliowaka baada ya taarifa hizo, haukuwa mdogo hata kidogo na hakuna aliyeutarajia.



Sura ya Sita

“Je,” Victoria akauliza kwa kihoro “Amekufa?”

“Taarifa zinasema hajafa, ila hali yake ni mbaya sana, sana wa leo wa kesho!”

“My God!” Vick akazidi kuweweseka. “Anaweza kuzungumza?”

“Mkuu!” Castroh akaita kwa unyenyekevu, “Tumeambiwa hali yake ni mbaya sana. Mbaya mno. Tumeambiwa pia amehamishiwa katika wodi maalum ya wagonjwa mahututi akiwa amevunjika miguu yote miwili, mkono wa kushoto, mbavu sita na bega lake kutenguka. Mtu wa namna hii hatarajiwi kuzungumza mara moja mkuu!”

“I mean ataweza kuzungumza tena?” Maana Alfred ametuambia kuwa muda mfupi kabla ya Matheo wa Benki Kuu kuuawa, alikiri kuwa Mhasibu ameziondoa fedha zote katika hazina ya Benki kuu na kuzificha anakojua mwenyewe. Ndio maana tuliwaambia Mhasibu hatakiwi kufa kwa gharama yoyote mpaka awe ametaja alipozificha fedha hizo ili tuzigawane na kuangalia ustaarabu mwingine. Maana huyu Chaguo hatabiriki kabisa!”

“Hilo la kuzungumza sina hakika nalo. Ila kama atapata tiba nzuri ambazo kwa uhakika zinapatikana nje ya nchi, may be anaweza kuongea tena!”

“Dah!” Vick akahamanika kwa dhati akiwatazama wenzake ambao nao walikuwa wamechanganyikiwa vibaya sana. Akajaribu kufikiria jambo la kufanya hakulipata. Kichwa chake kilikuwa kimevurugika vibaya sana. Alihitaji utulivu lakini nafasi ya kuutafuta utulivu huo haikuwepo.

“Na ni nani aliyetoa amri ya kumgonga Mhasibu na gari?!”

“Hakuna aliyetoa amri kiongozi, ila aliyemgonga ni Tarish Michael Bagula. Yule kijana tuliyekuwa tukimtuma kwa Mhasibu kuchukua fedha zetu mara kwa mara!”

“Yuko wapi?”

“Nani?”

“Ebo! Namzungumzia aliyemgonga Mhasibu!”

“Yuko hapo nje!”

“Hebu mwite!”

Castrol akainuka na kutoka nje. Sekunde chache baadae akarejea akiwa na Tarish. Tarish alikuwa akitetemeka kwa hofu na wasiwasi. Castrol alikuwa amemuonya tangu mara ya kwanza uthabiti wa kundi na jinsi kundi hili lisivyopenda mizaha.

Ukiacha hilo tangu mwanzo alikuwa ameambiwa kuwa Mhasibu hakutakiwa kudhurika mpaka aseme mahala hela zilipokuwa, kitu ambacho alikuwa amejitahidi kukifanya kwa uwezo wake wote ikiwa ni pamoja na kumuweka Ommy Killer mbali na Mhasibu.

Bado anakumbuka vizuri namna alivyoonywa vikali baada ya Mhasibu kutoroka chini ya himaya yake kabla hajatamka chochote kuhusu fedha zilipofichwa huku akiwa amewatia hasara ya kuua mlinzi wao mmoja. Hili ukizingatia na ule ukweli kwamba amekuwa akipewa kila anachohitaji yakiwemo malipo ya kutakata kwa kila kazi ili kuifanya kazi yake kwa ufanisi wote, kwa pamoja vilizidi kumuweka katika jakamoyo kubwa si kidogo.

Hivyo leo hii alipoitwa na Castrol aende katika ofisi yao ya siri kule Mbezi Beach baada ya kumpa taarifa za ajali ya Mhasibu, alikwenda kwa moyo mzito na alipofika kwa Castrol alijikuta kama yuko chini ya ulinzi kufuatia mazingira aliyoyakuta. Hata baada ya kumueleza hakutakiwa kuondoka mpaka atakapopewa taarifa nyingine.

Ilikuwa ni wakati huu alipoanza kuona wale vigogo kadhaa ambao Castrol alikuwa amemsimulia kuwa ndio wenye mpango huu wakiingia mmoja baada ya mwingine mpaka walipotimia wote. Alipojaribu kuuliza kwa mwenzie akaambiwa kulikuwa na kikao cha dharura kujadili mustakabali wa hatima yao.

Na sasa alikuwa ameitwa ndani, mbele ya jopo hili bila shaka kujieleza.

“Ni nani alikupa amri ya kumgonga Mhasibu?” Victoria akamuuliza kwa ile sauti yake nzuri. Ingekuwaia vigumu kujua kama alikuwa amekasirika.

“Kumradhi mama!” Alikuwa Tarish kwa unyenyekevu.

“Hujajibu swali!” Vick akamkumbusha kwa karaha.

“Ujue kazi hii naifanya kwa moyo wote mama. Nami ni sehemu ya familia hii. Kwa maana kwamba kufanikiwa kwenu ndio kufanikiwa kwangu pia. Tangu alipotoroka nimejikuta nikiapa kumtia mikononi haraka iwezekanavyo. Sasa nilipomuona ametoka Ikulu nikajua ametoka kuchoma utambi, ndio nikaghadhibika na kumgonga. Ilikuwa ni hasira na kihoro, lakini sikutumwa na mtu. Hata hivyo nilimtafuta sana Castrol kabla ya kwenda Ikulu ili kupata muongozo, lakini simu yake iliita bila kupokelewa. Hata Alfred anaelewa!” Akajibu kwa urefu. Sentesi hii ya mwisho ikawa kama imemtoa hatiani.

“Eti Alfred ni kweli?” Vick akataka uhakika.

“Ni kweli!” Alfred akakubali na kutikisa kichwa juu na chini kuafiki. “Ni mimi niliyemwambia Tarish kuwa Mhasibu ameongea na Rais katika simu baada ya kumkosa Castrol katika simu. Na yeye akaniambia anakwenda Ikulu!”

“Kwa nini simu zako zilikuwa zinaita bila kupokelewa?” Vick akamgeukia Castrol

“Mkuu mi nafikiri nina haja ya kurudi kutumia simu za kawaida. Hii Smartphone inanizingua kweli, inaelekea niliondoa sauti bila kujua, maana wengi wanalalamikia kuwa sipokei simu zao wakati mimi sisikii zikiita!”

“Na unajua kama kitendo hiki kimetugharimu sana?”

“Najua Mkuu, kumradhi hata hivyo upuuzi huu hautajitokeza tena!”

“Mnasemaje jamani?!” Vick akawauliza wenzake, yakafuatia maoni ya hapa na pale ambayo yalitoa nafasi nyingine kwa Castrol, Tarish na vijana wao ili waweze kurekebisha makosa yao. Walipomaliza Vick akasema “Mnachotakiwa kufanya ni kuhakikisha Mhasibu hafi kabla hajataja fedha zilipo, suala hili lifanyike haraka iwezekanavyo!”

“Tutahahikisha Mkuu!” Akajibu Castrol kwa niaba ya wenzake, Tarish akaambiwa atoke nje, akatoka akiwa na furaha huku akiapa kufanya kila lililo ndani ya uwezo wake kuhakikisha malengo ya mkuu wao na jopo lake yanatimia.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Je,” Vick akauliza baada ya Tarish kuondoka “Kuna la ziada!”

“Lipo Mkuu!” Alfred akajibu na kuongeza “Kuna zile fedha zilizochukuliwa mara ya mwisho!”

“Zipi?”

“Zile zilizopo katika Semitrailler!”

“Enhe?”

“Mie naona kwa mambo yanavyokwenda, nashauri zigawanywe kwa wajumbe, maana Polisi wanaweza kuingilia kati kutaka kujua chanzo cha ile ajali ya Mhasibu, wakimfikia Tarish tutakuwa tumekwisha!”





“Wewe unazungumia bilioni mbele ya Trilioni?! Hukumsikia Matheo wa Benki Kuu? Mhasibu ameficha matrilion kwa matrilion ya shilingi huko anakokujua mwenyewe. Tunazihitaji fedha hizo, tunazihitaji haraka sana. Ni hizo tutakazozigawana nasi kuwa miongoni mwa mabilionea wachache nchini, na sio hivi vibilioni kadhaa! Mmenielewa?”

“Ndiyo Mkuu!”

“Now mnatakiwa kufanya kila jambo ili fedha hizi zipatikane. Liwake jua, inyeshe mvua, lazima pesa hizi zipatikane. Kwetu suala hili kwa sasa ni suala la kufa na kupona!”

“Lakini Polisi... Polisi...!”

“Kwani Tarish alionekana? Mbona naambiwa gari alilotumia lilikuwa na namba za bandia na isitoshe vioo vyake vilikuwa tinted!”

“Ni kweli ila kulikuwa na mtu aliyejaribu kumrushia risasi. Kama gari ile isingekuwa bullet proof pengine Tarishi angekuwa ameshikwa kama sio marehemu!”

“Kwa hiyo unachojaribu kutuambia ni kitu gani?”

“Mtu yule aliyerusha risasi anaweza kuanza kutufuatilia! Tunaweza kuwa hatarini!”

“Huo ni uoga wa kijinga Alfred!” Vick akakemea kwa hasira. “Na hamuwezi kuniambia kuwa mtu mmoja anaweza kukutisheni kiasi cha ninyi kushikwa na kihoro kiasi hiki. Labda tu mniambie kuwa nimezungukwa na walinzi wajinga wasiojua cha kufanya!” Akatua na kupiga funda la maji kisha akaendelea.

“Kwa sasa mna kila kitu, mnazo fedha za kutosha pia. Kama hamuwezi kumnunua mtu muueni! Narudia tena, fedha alizoficha Mhasibu ni nyingi sana. Na sisi hatuwezi kugawana fedha tulizozichukua mara ya mwisho kwa kuwa tunataka zitumike kuhakikisha Mhasibu anapatikana, anapona na kutaja alikoyaficha yale Matrilioni. Thats all! Tukiyapata hayo tutagawana kwa viwango vya kuridhisha na kila mtu ataangalia ustaarabu wake. Sawa?!”

“Sawa Mkuu!” Wakajibu kwa pamoja, wengine wakijibu kwa shingo upande.

“Eeh! Achaneni na vifedha vidogo vidogo!” Akaongezea huku akisimama ikiwa ni ishara ya kikao kufungwa. Wajumbe wengine pia wakasimama na kutoka nje pamoja nae, baadhi wakiumia kimoyomoyo kufuatia uamuzi huu wa Victoria kwa vile walivyoona mambo yanaanza kwenda kombo.

Ilikuwa dhahiri kuwa Victoria hakuwa ameyajali wala kuyapa uzito manung’uniko ya wengine. Dakika ishirini au thelathini baadae Vick alirejea tena, akajifungia ndani na kufanya jambo lingine moja zaidi.



* * *

Ni pale Samson alipofanikiwa kuwatuliza mke na mtoto wa Mhasibu ambao walikuwa wakilia kwa nguvu na kwa muda mrefu wakimuombolezea Mhasibu Jamaldin waliyedhani amepoteza maisha; ndipo Samson alipopata wasaa wa kuingalia simu yake ambapo mara kadhaa alikuwa ameisikia ikiita lakini kutokana na zile hekaheka za kuhakikisha Mhasibu anapata matibabu ya kina chini ya madaktari bingwa wa pale Aga Khan Hospital; alikuwa ameacha kuipokea makusudi na walau kuiangalia tu.

Private Call! Lilikuwa jina la mpigaji katika simu! Akasikia moyo ukimpiga kwa nguvu kifuani. Ni muda sasa alikuwa hajapata simu ya mtu huyu. Ilikuwa ni wakati huu alipoikumbuka ile safari iliyomfanya awe mlinzi binafsi wa Mhasibu Jamldin.

Bado anakumbuka vizuri sana kuwa baada ya kile kikao nyeti baina yake na viongozi waandamizi wa Ulinzi na usalama wa Taifa kilichofanyikia Ikulu chini ya Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania miaka michache iliyopita kufuatia kazi nzuri aliyoifanya katika ule mkasa ambao mtu mmoja ameuandikia kitabu na kukiita NIPE ROHO YAKO; ndipo alipojikuta akipelekwa Benki Kuu ya Tanzania na kutakiwa kuwa mlinzi binafsi wa Mkurugenzi mkuu wa Benki hiyo ndugu, Mhasibu Jamaldin Mhasibu.

Ingawa alipelekwa hapo na usalama wa Taifa baada ya kurejea kutoka katika masomo ya ujasusi na ukomandoo nchini Cuba; lakini alifuata taratibu zote zinazotakiwa kufanywa na mtu anayeomba kazi ya ulinzi wa mtu binafsi. Bordguard!

Aliandika barua, akaitwa katika usaili na kupewa kila aina ya majaribio, ya maneno kwa ya vitendo ni kutokana na kufanya vizuri katika majaribio yote mawili ndipo ‘Serikali’ ikamuajiri kama mlinzi binafsi wa Mhasibu.

Jukumu ambalo lilianza kumchosha siku kadhaa baadae. Kule kukaa nyuma ya mtu kila wakati, ukimuangalia kila anayekutana nae, kujaribu kila anachotakiwa kufanya huku muda mwingi ukiwa nje pale anapokuwa ofisini aliona kama vitu vinavyoweza kumtia wazimu wakati wowote.

Mara kadhaa aliongea na Mzee Anderson Chillonga mtu ambaye alitakiwa kuripoti kwake akimueleza au kuomba kubadilishiwa kazi baada ya kuchoshwa na hali ile, akakataliwa na kutakiwa kuwa mvumilivu. Kwamba hiyo ilikuwa miongoni mwa vipimo vinavyompima kiwango chake cha uvumilivu na utayari wake wa kufanya kazi katika mazingira sio magumu pekee, bali yeyote.

Alimueleza kuwa katika tasnia ya nyanja za usalama, huwa kuna mafunzo mbalimbali. Mafunzo mengine ni upuuzi mtupu na huenda yakakutia hasira. Lakini kadiri unavyofanya mambo yako vizuri kwa uvumilivu, ufanisi na weledi mkubwa, ndivyo unavyojikuta ukipanda kutoka ngazi moja hadi nyingine, na mwisho wa siku utajikuta ukiwa kileleni kabisa ukiwa umetimiza ndoto zako na ndoto za Taifa pia.

Ni hili lililomfanya Samson avumilie. Akavumilia. Taratibu akajikuta akilifanya hili kama sehemu ya maisha yake, huku yale mahusiano yake na familia ya bosi wake yakizidi kumpa faraja na furaha, hata wakati mwingine akajikuta akisahau wajibu wake na kujiona kama ni sehemu ya familia ile. Hakika walikuwa watu wema na wenye upendo sana.

Hata hivyo, siku za hivi karibuni, alijikuta akishikwa na shauku ya aina yake kama sio msisimko, pale aliposhuhudia bosi wake Jamaldn akiingia katika tafakuri za kina za mara kwa mara zilizokuwa zikimtoa alipo na kumpeleka mbali kifikra. Tafakuri ambazo mwisho wake ilikuwa ni Mhasibu kukosa raha na furaha na muda mwingi kuhitaji awe peke yake.

Samson akajikuta kila mara akiambiwa amuache apumzike. Samson alikuwa amejitahidi kuichunguza hali na kujadiliana na Anderson Chillonga aliyeishia kumuomba aendelee kuwa mtulivu, mvumilivu lakini mdadisi.

Msisimko wake kuhusu hali hii mpya ya bosi wake ilizidi pale alipopigiwa simu usiku wa jana na mke wa Jamaldin kuwa Mhasibu alikuwa hajaonekana. Samson angali anavyokumbuka alipoingia katika jukumu zito la kufuatilia nyayo za Mhasibu bila mafanikio mpaka alfajiri ya leo alipopigiwa tena simu kuwa Jamaldin alikuwa amerejea. Hima akawahi huko akijua baada ya maongezi baina yake na Mhasibu atakuwa na jambo la kuripoti kwa mzee Chillonga.

Kilichojiri baadae kilimuacha kinywa wazi, kwani ilionyesha dhahiri kuwa Mhasibu alikuwa na jambo kubwa ambalo hakuwa radhi kulisema mbele ya mkewe wala mtoto, jambo ambalo Samson alijua ataelezwa yeye wakati wowote na hivyo kuwa mwanzo hitimisho la msisimko wake pengine na mwanzo wa safari nyingine ambayo hakuijua.

Ile simu iliyoingia ghafla na kuchukua utulivu wa Mhasibu, safari ya ghafla ya Ikulu huku akitakiwa kumlinda kwa gari tofauti jambo ambalo halikuwa la kawaida kwao, ule mkanganyiko aliouna katika sura ya Mhasibu wakati akitokea Ikulu, yale maagizo pamoja na ile ajali kwa pamoja vilimfanya Samson awe hoi na taabani kifikra, hali hofu na kiuchovu ambavyo humnyemelea mara chache vikianza kuuzingira moyo wake. Naam, ni haki yake kuwa na hofu, hii ni kwa vile alikuwa hajui sababu za kutukia kwa matukio yote haya.

Sasa simu hii kutoka kwa bosi wake wa ukweli aliona kama inataka kumuumbua kwa kuwa atadaiwa maelezo ambayo hakuwa nayo. Hata hivyo ilikuwa ni lazima aipokee kwa kuwa imepiga mara mbili bila kupokelewa na hii ni mara ya tatu sasa. Upesi akaharakisha kutoka hapo katika viti vya wageni na kutoka nje kabisa ya jengo, akasogea mpaka chini na kuipokea.

“Number One!” Aliita Mzee Chillo upande wa pili.

“Yes Chief! On duty Sir!” akajibu Samson.

“Wapi!” Alikuwa Chillonga tena.

“Aga Khan Hospital!”

“Kwema?” Swali hili likamfanya Samson agundue kuwa habari zilikuwa hazijamfikia Mzee Chillo.

“Si kwema, Mhasibu Jamaldin amepata ajali mbaya sana ya gari!”

“Kitu gani!”

“Ajali ya gari mzee, amegongwa makusudi kabisa. Jamaa walidhamiria kumuua, lakini hajafa yuko hapa anapata tiba, lakini ni zaidi ya mahututi! Yaani wa leo wa kesho, sijui kama atapona!”

“Duh!” Chillonga akashangaa kwa dhati, kiasi akijenga hofu huku akihusianisha ile taarifa aliyopewa na Rais kuhusu ule wizi wa mabilioni ya wananchi na ajali hii. Kama watu hawa wako smart kiasi hiki, kiasi cha kumjeruhi Mhasibu muda mfupi baada ya rais kutoa amri, wakati taarifa hizo zikiwa hazijafika kwa umma; basi kulikuwa na shughuli pevu katika kuufikia mzizi wa tatizo na kuung’oa.

“Wakati haya yanatokea wewe ulikuwa wapi?!” Mzee Chillo akauliza tena, safari hii akiwa makini zaidi. Uzito wa sauti yake ukimjulisha Samson kuwa alitakiwa sio tu kujieleza bali na kutoa taarifa ya kitu gani kinaendelea.

Akatumia nafasi hiyo kumueleza kinagaubaga kila kilichojiri kwa ukamilifu wake.

“Duh!” Mzee Chillo akashangaa zaidi. “Mambo yanazidi kuwa magumu. Tusipokuwa makini kuna jambo zito linaweza kuifika nchi hii, na jambo hilo likitokea, mimi na wewe tutakuwa mimavini. Hebu njoo ofisini kwangu mara moja kuna kazi muhimu ya kufanya! Nahisi inahusiana sana na hiyo ajali ya Mhasibu Jamaldin!” Akatua.

“Nakuja Mkuu, niko njiani!” Akajibu Samson na kukata simu.

Haraka akapiga simu mahala pengine na kuagiza kitu fulani, kisha akarudi ndani ya hospitali na kumuaga Mke wa Mhasibu pamoja na mwanae.

“Sam, unaona hali ya mzee ilivyo, unakwenda wapi lakini?”

“Kuna dharura ofisini kwa mzee, natakiwa nikawaelekeze kitu. Sitachukua zaidi ya nusu saa!” Akajibu kuwatoa hofu.

“Sasa na hapa tutabaki na nani? Mie naanza kuogopa kubaki peke yangu!”

“Moses Paschal, ni rafiki yangu na msaidizi wangu mkubwa. Mkiwa na yeye ni kama mko na mimi. Aidha ulinzi wa hospital hii ni imara mara dufu, sidhani kama wanaweza kuwafikia hapa mlipo!”

“Na vipi mume wangu? Atapona kweli?!” Alikuwa Nadia tena akiuliza swali hili kwa mara ya elfu moja na moja, hali machozi yakatafuta njia tena katika kingo za macho yake.

“Madaktari wanafanya kazi kufa na kupona kuhakikisha mumeo anapona na kurejea katika hali yake ya kawaida. Na ujue hii sio hospitali ya mchezo mchezo, inao wataalamu waliobobea ambao wanajua wanachokifanya. Umeelewa mama!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Ndio nimeelewa!” akajibu akifuta machozi.

“Basi usilie, badala yake muombee kwa Mungu ampe nafuu na apone!” Akamalizia akiwapa mikono na kuondoka.

Muda mfupi baadae, Moses Paschal kijana mtanashati mwenye rangi ya maji ya kunde, mrefu kiasi mwenye umri wa miaka ishirini na nane hivi na mwili uliojengeka kimazoezi hasa akafika. Akamsalimia mke wa Mhasibu na mwanae, na kueleza kuwa ameagizwa na Samson aje hapo.

Wakampokea na kumpa kila ushirikiano aliouhitaji.





* * *





ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog