Search This Blog

Saturday, 5 November 2022

EPA - 4

 








Simulizi : EPA

Sehemu Ya Nne (4)





Dakika kumi na tano baada ya Samson Kidude kuondoka pale hospitalini, mlango wa kile chumba walichokuwa wameketi kwa mapumziko wakati wakisubiri kusikia maendeleo ya Jamaldin ukafunguliwa. Mtu mmoja mrefu ambaye alikuwa miongoni mwa wale madaktari akaingia na kuwasalimia.

“Hamjambo?!”

“Hatujambo!” wakajibu.

“Naitwa Dr. Martin Limbe, ni daktari na afisa utawala wa hapa Aga Khan. Aidha ni mmoja wa watu wanaoshughulikia tiba ya mgonjwa wenu!” Akatua na kuwatazama usoni kwa muda kila mmoja.

“Je,” Mke wa Mhasibu akakurupuka na kuuliza “ Mhasibu anaendeleaje?”

“Hali ya Mhasibu siyo mbaya wala sio nzuri!”

“Una maana gani Mhasibu au ame.... ame... amekufa! Niambie tu!”

“Hajafa mama, na hatakufa labda iwe ameandikiwa. Madaktari wanafanya juhudi za kila aina kuhakikisha anapona!”

“Asanteni na Mungu awabariki!” Akajibu.

“Kuna wageni ofisini kwangu ambao wangependa kuongea na ninyi!”

“Kuongea na sisi?!” Nadia mke wa Mhasibu akahamanika, huku akimtazama Moses haraka na kurudia kumtazma Dr. Martn. Ule mtazamo ukamfanya Moses awe tayari kwa lolote. Nadia akauliza

“Kimezidi kitu gani tena?”

“Hakuna kilichozidi. Ni jambo la kawaida tu ambalo mie nimeona linahitaji ridhaa yenu kwanza!” Dr Martin akazidi kuwachanganya.

“Jambo gani?”

“Twendeni ofisini kwangu basi!” Akajibu Dr Martin huku miguu yake ikinyanyuka na kuanza kutengeneza hatua ndefu za taratibu kuelekea ofisini kwake. Mkewe Mhasibu, Shuwena pamoja na Moses wakainuka na kumfuata.

Ofisi ya Dr Martin ilikuwa nzuri na kubwa ikiwa na zana za utawala na zile za udaktari kwa pamoja. Mbele ya meza yake ya kukalia kulikuwa na viti viwili vilivyokaliwa na watu wawili wenye miili mikubwa ya wastani.

Walivalia suti nzuri za rangi nyeusi, shati nyeupe na tai nyeusi. Mmoja alikuwa na miwani usoni, hali yule mwingine akiwa na briefcase zuri ambalo alililaza mapajani mwake. Kwa kila hali walionekana kama watu walioridhika na wasio na haraka ya chochote.

“Karibuni sana!” Martn alisema tena akikaa huku akiwaonyesha sofa nzuri zilizojipanga kuizunguka ofisi ile huku yeye mwenyewe akikaa katika sofa mojawapo. Mke wa Mhasibu na wenzake walipokaa, Martin akawageukia wale wageni na kusema.

“Hawa ndio wanafamilia, mnaweza kuzungumza nao!”

“Vizuri!” Wale watu wakajibu nao wakiamka kutoka katika vile viti wakaja pale na kuwasalimia Mke wa Mhasibu na wenzake, halafu nao wakakaa katika sofa zile zile wakitazamana na watu hawa.

“Mie Naitwa Bazzi Bazile. Natokea Ofisi ya Rais Ikulu inayoshughulika na uchumi!” Akajitambulisha yule wa kwanza mwenye miwani.

“Na mimi naitwa Joseph Singano natokea Benki Kuu ya Tanzania. Ni afisa mipango na mahusiano!” Akajitambulisha na yule wa pili. Halafu yule wa kwanza aliyeonekana kama msemaji mkuu akaendelea.

“Tumezipokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za ajali ya ndugu yetu Mhasibu, na baada ya taarifa hizo kulifanyika kikao cha dharura kati ya benki kuu na Serikali na kutokana na umuhimu wa mtu huyu katika uchumi wa taifa, tumeamua kwamba inabidi mtu huyu akatibiwe Ujerumani kwenye, huduma na vifaa bora haraka iwezekananvyo!

Kwa hiyo tulikuja hapa, kufanya juhudi za kumsafirisha kumpeleka Ujerumani, ndipo tukaambiwa kuwa nanyi mpo hapa, tukaona sio vyema kuendelea na harakati hizi bila ninyi kujua!” Akatua.

Kitu fulani kikamkaba mke wa Mhasibu, Nadia kifuani. Yale maringo na majiganmbo ya watu hawa, ule utayari wao na zile kauli zao ambazo zilisomeka kama amri fulani hivi zikimfanya awatilie shaka watu hawa. Akawauliza.

“Kwa kuwa mmemuajiri Mhasibu, basi mnadhani mna dhamana ya kufanya kila jambo mnalotaka juu yake. Hamjui kama nje ya kazi mtu huyu ana familia na ukoo wake?! Kwa nini msishauriane na familia kwanza?!”

“Ndio maana tuko hapa Mrs Jamaldin Mhasibu! Tungeweza kuondoka naye bila kuwajulisha, na msingeweza kuzuia chochote!”

“Kwa hiyo kama tungekuwa hatupo hospitalini, tungeishia tu kupewa taarifa kuwa mgonjwa wenu amesafirishwa kwenda Ujerumani baas?! Hii ndiyo sawa Bazzi?!. Ndivyo maadili ya kazi yenu yanavyosema?!”

“Sio sawa, na kamwe tusingeweza kufanya hivyo mama. Baada ya kikao, kuna watu walitumwa nyumbani kwenu waje kuongea na ninyi, na sio kuongea pekee ila kuwajuza kuhusu hatua hii.

Watu hawa wasingeongea na nyie pekee bali wangewachukua na watu ambao ninyi mngependa waondoke na Mhasibu na kwenda naye Ujerumani katika matibabu ya Mhasibu kwa gharama za Serikali!

Watu hao walipofika nyumbani, wakaambiwa kuwa wote mmekwenda hospital. Ndio jukumu hilo likahamishiwa kwetu! Kumradhi Mama Mhasibu” Bazzi akatua.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Ingawa maongezi yalikuwa yamenyooka, bado kitu fulani kilikuwa kikimtia shaka mke wa Mhasibu. Akajikuta akiwaangalia usoni kabla ya kuuliza lile swali lililokuwa likimkereketa sana moyoni.

“Je, naweza kuona vitambulisho vyenu tafadhali?” Watu wale wakaangaliana wao kwanza kisha wakatabasamu kabla mmoja hajaangua kicheko laini kilichobeba kitu kama dhihaka hivi “Mama Mhasibu bana, hutuamini? Unadhani tunatarajia kukuingiza mjini?!” Akasema na kucheka zaidi.

“Hujajibu swali langu!” Mama Mhasibu akauliza tena kwa dhati safari hii akiwaangalia usoni moja kwa moja. Mtazamo ambao kwa kiasi fulani nusura uwababaishe wale watu. Hata hivyo waliingiza mikono yao katika mifuko ya makoti yao kila mmoja kwa wakati wake na kila mmoja akatoa kitambulisho, mmoja akakichukua cha mwenzake, akachanganya na chake na kumkabidhi mama Mhasibu vitambulisho vyote viwili kwa pamoja.

Mke wa Jamaldin akavipokea na kuviangalia kwa muda huku akivigeuza kila upande. Vilielekea kuwa vitambulisho vya ukweli. Hiki cha jamaa wa benki kuu kikifanana na kile ambacho mumewe alikuwa nacho. Vyote vilikuwa vitambulisho muruwa, vyenye nembo nzuri ya Taifa huku vikibeba sura, nyadhifa zao na muda wa kumalizika wa vitambulisho vile.

Kiasi mashaka ya Nadia, mke wa Mhasibu yakapungua. Akashusha pumzi ndefu na kuuliza.

“Ujerumani anaenda kutibiwa hospitali gani?”

“Hospitali ya Rufaa ya Berlin!” Akajibiwa.

“Na tunaondoka lini?!”

“Leo hii, sasa hivi!”

“You must be joking Bazzi. Right Now! Kuna maswala ya tiketi, viza, kubadili nguo, kujiandaa kwa safari na mengine mengi! Tunawezaje kusafiri katika hali hii. Haiwezekani, tuondoke japo kesho!”

Kauli hii ya Mke wa Mhasibu ikamfanya Bazzi acheke tena. Alicheka kwa muda na kwa sauti kabla hajanyamanza na kusema “Tatizo lako Mama Mhasibu unadhani unashughulika na mtu binafsi. No Sir, unashughulika na Serikali. Afya ya Mhasibu ni muhimu kuliko unavyoweza kufikiria, ni muhimu kuliko vyote unavyovisema.

Ndio maana tumeamua kumpeleka muda huu kwa ndege ya kukodi ambayo haitatua popote zaidi ya Berlin, Ujerumani. Unachotakiwa kufanya wewe ni kutuambia ni nani nani tutaambatana nao kwa ajili ya itifaki tu. Hayo mengine tuachie sisi!”

“Sie tutaondoka wote watatu!” Akajibu haraka Mama Mhasibu.

“Hata mkitaka kuondoka kumi, ruksa. Ndege tuliyopewa ina uwezo wa kuchukua watu thelathini na sita!”

“Mimi nina ushauri!” Moses Paschal, yule kijana aliyeachwa na Samson akasema taratibu kwa mara ya kwanza. Hali iliyofanya watu wote wageuke na kumtazama. Akaendelea!”

“Kuondoka wote sioni kama ni uamuzi wa busara. Lazima apatikane wa kubaki nyumbani. Nami kwa ushauri wangu naona Shuwena ndiye haswaa anayetakiwa kubaki.

“Kitu gani?!” Shuwena akaja juu.

“Unatakiwa ubaki ili uiangalie nyumba, hatuwezi kuondoka nyumba nzima na..!”

“Eti nibaki! As if nyumba ikibaki peke yake inaweza kuibiwa. Unaonaje wewe na anko Sam ndio mbaki, mimi nikamuuguze baba yangu?! Wewe unaujua uchungu wa mzazi kweli?!” Alikuwa Shuwena kwa hasira huku akimtazama kijana yule kwa jicho baya.

“Najua unavyojisikia kwa hili lililompata mzazi wako Shuwena. Kila mmoja hapa anajisikia vibaya. Nimesema ubaki kwa kuwa Samson aliniambia kwamba ruhusa yako shuleni ilikuwa ya siku wiki moja tu, na zimesalia siku moja au mbili, imalizike. Unatakiwa kurudi ukajiandae na mitihani yako wiki ijayo. Na kwa kuwa baba ana matatizo sisi twende naye ili wewe ubaki kumalizia mitihani yako mama, unaonaje?!”

Kila mmoja akatikisa kichwa kukubaliana naye

“Afadhali umenikumbusha mwanangu!” Mama Mhasibu akaanza akimtazama Moses na baadae Shuwena. Akaendelea, “Nimechanganyikiwa kiasi cha kusahau kila kitu. Nakubali baba ni muhimu sana, lakini mitihani hasa ya hii ya mwisho ni muhimu pia. Naona bora ubaki tu!”

“Lakini... Lakini...!” Shuwena alitaka kusema kitu akashindwa.

“Najua unachotaka kusema mwanangu, ni juu ya wewe kuja ukimaliza mitihani. Hilo sio tu halina mjada bali limepita kwa asilimia zote. Sawa?!”

“Sawa!” Akalazimika kukubali baada ya kukaa kimya kwa sekunde kadhaa. Mama yake akalazimika kusimama na kumkumbatia mwanae kwa upendo huku akimpiga piga vikofi vya upendo mgongoni. Donge la uchungu likamshika Shuwena lakini akajitahidi kulizuia huku akifuta machozi. Alijua yeye akilia, mama yake atalia mara kumi zaidi.

“Ukiacha hilo!” Mama Mhasibu alikuwa akiendelea, “Unatakiwa kuzungumza na Mkuu wa shule yetu ili kupata nafasi ya kujisomea. Pamoja na kwamba kuna matatizo, nakuomba sana tusifanye kila kitu chetu kikasimama na kusubiria mzee apone. Mambo mengine yanapaswa kuendelea wakati Mzee akipata tiba. Sawa?”

“Sawa mama!” Shuwena akakubali na kuongeza “Kwa maana hii utaondoka wewe, pengine na anko Sam, ili mimi nibaki shule, huku Meneja wetu akiendelea kufuatilia mambo mengine ya mzee. Kama hali itabadilika tutawasiliana nami ntakuja haraka sana!” .

“Tena unaona, umenikumbusha Samson, acha nimpigie simu ili aje tujumuike pamoja! Ushauri wako ni mzuri mama, ndiyo maana baba yako anakupenda kama mboni ya jicho lake. Nitaenda mimi na Samson, wewe utakuja siku nyingine!” Akatua.

“Je,” Bazz ambaye alikuwa akiufuatilia mjadala ule akauliza “Kuna la ziada?!”

“Hakuna baba!” Akajibu Mke wa Mhasibu kwa moyo mkunjufu na kuongeza “Naomba mniwie radhi kwa imani haba niliyokuwa nayo kwenu. Dunia imebadilika sana ndugu zangu, Tangu mume wangu apate ajali kwa kugongwa makusudi hali hana ubaya na mtu yeyote, nimekuwa sina imani na mtu yeyote!” Kauli hii iliwajulisha kitu kimoja muhimu, kuwa mama huyu alikuwa hana tatizo tena na akina Bazzi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



“Usijali mama, kila mmoja anaweza kuwa kama wewe au hata zaidi!” Joseph akamjibu.

Kutoka hapo Mke wa Mhasibu aliitoa simu yake na kumpigia Samson. Simu ilizunguka kwa muda mrefu bila kutoka. Akajaribu tena na tena hali ile ile ikajirudia. Alipowataka na wenzake wajaribu kumpigia Samson hali hiyo ikajitokeza tena.

“Itakuwa tatizo la mtandao!” Moses akajibu naye akiirudisha simu mfukoni baada ya kujaribu kumpigia simu Samson na jamaa zake wengine bila mafanikio. Hakusahau kumtumia ujumbe Samson ili mtandao ukikaa sawa aweze kumtafuta.

Ilikuwa ni wakati huu Dr Martin alipopewa amri ya kumuandaa mgonjwa haraka haraka tayari kwa safari huku na yeye akitakiwa kutoa madaktari wawili watakaoambatana na Mhasibu huko Ujerumani.

Dakika chache baadae Mhasibu, Mke wake Nadia, Bazzi, Moses Paschal, madaktari wawili akiwemo Martin na wale maafisa wengine walikuwa njiani wakielekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere tayari kwa safari hiyo ndefu kabisa.

Bado Mhasibu alikuwa hajitambui, sasa alikuwa amefungwa bandeji vizuri kwa kila sehemu iliyokuwa na jeraha, na alilala kitulivu pale juu ya kile kitanda chake chenye matairi hali chupa ya maji iliyokuwa ikining’nia katika kona ya kitanda chake ikitiririsha maji taratibu kuingia katika mishipa ya mwili wake.

Pale uwanja wa ndege gari lilipitiliza moja kwa moja na kwenda kutokea katika uwanja mwingine mdogo uliokuwa na ndege kadha wa kadha za kukodi. Uwanja huu ulikuwa mbali kidogo na ule uwanja mkuu, ndege ya wastani ambayo wangeitumia kwa safari ilikuwa tayari kwa safari.

Kwa mara ya kenda sasa, Moses na mke wa Mhasibu walijaribu tena kumpigia Samson, na hali ile ile ikajirudia. Hatimaye walikubaliana kuwa Moses aondoke nao badala ya Samson wakati juhudi za kumtafuta Samson zikifanyika.

Kitu kimoja tu hawakukijua, kuwa Bazz alikuwa na kifaa fulani mfukoni mwake ambacho kilifanya kila mwenye simu aliyekuwa jirani nae, simu yake ishindwe kufanya kazi.

Mpaka ndege inaondoka na kukamata usawa unaotakiwa huko angani, sio mke wa Mhasibu, Moses wala Dr Limbe waliojua kuwa kwamba sasa walikuwa chini ya himaya ya akina Castrol Mathias, wakiongozwa na yule mwanamama hatari Victoria Brayson.



* * *

“Likizo yako iliyokuwa ikikuchusha na kukuudhi imekwisha Samson!” Ndivyo alivyoanza Mzee Chilo mara tu Samson alipoingia ofisini kwake, kumuamkia na kumpa maendeleo ya afya ya Mhasibu.

“Usiniambie Mkuu!” Samson akajibu kwa shauku, furaha ya dhati ikiuvaa moyo wake na kuututumua kiasi cha kuufanya mwili ujisikie vizuri, hali tabasamu la kukata na shoka likiuvamia uso wake. Tabasamu ambalo liliendelea kukomaa na baadae kuwa kicheko kidogo kilichoifanya sura yake ing’ae mithili ya maua katika jua la asubuhi.

Kwao, ile kazi ya kuwa mlinzi binafsi wa Mhasibu ambayo Samson ilikuwa ikimchosha siku zote ilikuwa sawa na likizo, na kila alipokuwa akihitaji kuhamishwa alikuwa akimuuliza bosi wake huyu kuwa ‘likizo yangu itaisha lini’.

Hivyo leo hii, alipoitwa na kuambiwa kuwa likizo yake imekwisha hakuweza kujizuia kufurahi. Ni hili lililomfanya afurahi, atabasamu na baadae aangue kicheko. Hata hivyo kicheko chake kilikuwa cha muda mfupi, pale alipojikumbusha kuwa likizo yake ilikuwa imeanza kunoga kufuatia yale matukio ya mfululizo yaliyokuwa yakimuandama bosi wake Mhasibu.

Matukio ya kutoweka na kurejea akiwa na dalili zote za kutoka msambweni. Matukio ya kutotaka kuzungumza alikokuwa na ile simu ya ajabu iliyomnyanyua na kumpeleka hadi Ikulu ikifuatiwa na ajali yake matata ambayo sio tu aliishuhudia pekee, bali alijitahidi kumfukuza mpaka mtu aliyesababisha ajali na kama isingelikuwa ile foleni huenda sasa angekuwa anajua kiini cha mambo haya.

Mlolongo wa mambo haya ulijikuta ukiifanya ile ari yake iliyokuwa imelala kwa muda iamke. Na kwa kweli alijikuta akipania kufanya kila analoliweza ili kuhakikisha ukweli wa mambo unajulikana. Lakini mambo yanavyotokea ni kinyume chake, wakati akiwa amejipangia hayo, ndipo anaitwa na kuambiwa kuwa ile likizo yake imeisha. Kwa maneno mengine ni kwamba hatakiwi kujihusisha na mambo yote yanayomuhusu Mhasibu kwa sasa ila asubirie jukumu lingine ambalo hakulijua.

Ni hiki kilichofanya tabasamu lake lizimike na sura yake kurejewa na ule utulivu wa awali. Utulivu ambao ulitafsiriwa na Chillonga kuwa Samson alikuwa tayari kupokea maagizo mapya. Mzee Chilo akaendelea.

“Sasa unaingia kazini rasmi. Inaweza ikawa kazi nzito na ya hatari pengine kuliko zote ulizowahi kuzifanya!” Akatua na kumtazama Samson usoni.

“Nakusikiliza!” Samson akajibu kwa mkato.

“Vizuri. Nimepokea maagizo kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwamba fedha za kutosha zilizokuwa zimetunzwa kwa ajili ya kulipia deni la Taifa zilikuwa zimechotwa hazina na mafisadi wachache wenye uchu na kiu ya utajiri wa haraka kwa kutumia hila.

Kwamba ni Mhasibu aliyerahisisha uchotaji huo bila kujua yeye akidhani anakisaidia chama kurejea madarakani. Hivyo Rais ameagiza fedha zote zilizochukuliwa, zinatakiwa kurudi hazina na wote walioasisi wizi huu wakamatwe na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

“Kitu gani?” Samson kahoji kwa mshtuko.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Eeh! Ni Mhasibu huyu huyu unayemlinda!” Akajibu Mzee Chillonga na hapo tena akamueleza kwa kirefu yote aliyoongea baina yake na Rais baada ya Mhasibu kutoka Ikulu. Naam! Zilikuwa habari mpya kwa Samson, habari ambazo zilimpa mwanga kwa kumfanya ajumlishe moja na moja na kupata mbili.

Kwamba wale waliomgonga Mhasibu ndio hao hao walioiba fedha hizo, na kumgonga kwao kulitokana na hofu yao ya kuhofia asiwataje na kuwaingiza matatani. Jambo ambalo aliliona ni kama wendawazimu kwa kuwa walitakiwa kuchukua hatua hizo kabla ya Mhasibu kwenda Ikulu.

Hata hivyo alipokumbuka kuwa Mhasibu alitoweka kuanzia jioni ya jana na kutokea alfajiri ya siku ya leo akaweza kuongeza mbili na mbili na kupata nne. Kwamba inawezakana wale mafisadi walimkamata, akawatoroka na walipomtisha kwa simu akawa amekimbilia Ikulu jambo ambalo hawakulitarajia, ndio wakawa wameghadhibika na kumgonga.

Kitu hiki kikamfanya auhofie zaidi usalama wa Mhasibu kwa wakati huo. Akaitoa simu yake na kumpigia Moses aliyemuacha kule hospitali amsaidie kumlinda Mhasibu wakati yeye akija huku kwa chifu wake. Simu yake ikawa haipatikani. Akajaribu mara mbili zaidi haikupatikana pia. Akaachana nayo na kumgeukia Mzee Chilo. Akamuuliza.

“Mhasibu amemtajia Rais majina ya watu walioiba fedha hizo?”

“Amemtajia wawili tu, Johnstone Mambo na Tarish Michael Bagula, wote wako Makao Makuu ya Chama, ingawa anahisi wako wengi!”

“Ni lazima wawe wengi, watu wawili peke yao wasingeweza kufanikisha jambo kubwa na zito kama hili!”

“Hilo moja, lipo kubwa zaidi Samson!”

“Lipi tena!”

“Kwa mujibu wa simu aliyonipigia Rais muda mfupi kabla wewe haujafika, inaonyesha fedha walizochukua kina Tarish ni moja ya nane ya fedha zote zilizokuwa katika akunti ya madeni ya nje. Kuna fedha nyingi zaidi ambazo hazijulikani zilipo. Pengine hii ndiyo sababu ya ajali ya Mhasibu asubuhi ya leo!”

“My God!” Samson akamudu kutamka tena “ Isije ikawa na hizi zimeangukia mikononi mwa akina Tarish!”

“Inawezekana. Mhasibu anaweza kuwa na majibu ya maswali haya vizuri zaidi!”

“Sasa tunachotakiwa kufanya ni kitu gani Chifu?”

“Swali zuri Samson! Siku zote kazi zetu zimekuwa hazina tofauti na kutupa jiwe gizani, ukisikia aiii unajua limempata na hapo unaanza kufanya yako!”

“Sijakuelewa Mkuu!”

“Taratibu utanielewa, wewe ulipelekwa pale benki kuu kwa kisingizio cha mlinzi binafsi wa Mhasibu ili kuangalia mienendo ya watumishi wa pale na kuhakikisha hawazitumii rasilimali zile vibaya kwa maslahi yao binafsi. Jukumu ambalo ulilifanya vizuri sana!”

“Ni kweli Mkuu!”

“Sasa unayo majukumu mawili tu, kwanza ni kuhakikisha Mhasibu hapotezi maisha na anasema ziliko zile fedha nyingi zaidi ambazo hazijulikani zilipo. Jambo la pili, ni kuhakikisha fedha walizochukua akina Tarish zinarudi na akina Tarish wanakuwa chini ya mikono ya vyombo vya Sheria! Sawa?”

“Sawa Mkuu!”

“Sasa unazo dakika chache za kuandaa mpango wako wa namna utakavyoyafaikisha majukumu haya. Msaada wowote unaoutaka utapatiwa. Kukiwa na tatizo au suala lolote, usisite kuniambia. Rais ametoa wiki moja au mbili. Sisi tunatakiwa kufanya kazi hii kwa muda usiozidi masaa sabini na mawili!” Akamaliza Chilonga

“Itakuwa hivyo Mkuu!” Samson akajibu na kuinuka. Akaingia katika ofisi yake ya dharura iliyopo katika jengo hilo hilo na kujifungia kwa muda akichorachora makaratasi yake. Mara kwa mara aliendelea kumpigia simu Moses bila simu hiyo kupatikana.

Nusu saa baadae alikuwa amekabidhi mpango wake wa kuifanya kazi hiyo kwa Chifu Chillonga Anderson Chillonga. Chifu aliupitia mpango ule na kuboresha hapa na pale kabla hajamwambia Samson kuwa mpango huo kwa kuanzia ulikuwa umekaa vizuri na ulikuwa na baraka zote kutoka kwake.

Kubarikiwa kwa mpango huu kulifuatiwa na Samson kupewa vitu kadha wa kadha ambavyo vilidhihirisha kitu kimoja tu, kwamba Samson Hussein Kidude alikuwa anaingia kazini rasmi.

“Samson!” Chilonga alimwita wakati akifungua mlango wa ofisi yake ili aondoke.

“Neno langu ni lile lile, jihadhari mwanangu!”

“Ondoa hofu mzee wangu!” Akajibu akiurudisha mlango na kuondoka.

Akiwa ndani ya gari alijaribu tena kupiga simu ya Moses bila mafanikio. Safari yake iliishia Aga Khan hospital ambako alikuta hakuna mtu. Alipouliza kwa wahudumu akaambiwa aliona mgonjwa akihamishwa tu ingawa hawakujua amepelekwa wapi.

Daktari aliyekuwa akimshughulikia Mhasibu, nae hakuonekana hapo ofisini wala simu yake haikupatikana. Ilikuwa ni wakati huu Samson alipojaribu kupiga namba ya mke wa Mhasibu baada ya ile ya Moses kushindwa kupatikana kwa mara nyingine tena.

Kwa maajabu na hii ikawa haipatikani. Kengele ya tahadhari ikalia kichwani mwake. Akajaribu tena, ilipogoma ndipo alipojaribu ya Shuwena. Mungu bariki simu hii ikaanza kuita. Akashusha pumzi za matumaini na kuendelea kusubiria.



http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

* * *

Mara tu mama yake alipoondoka na wale watu wengine, Shuwena mtoto wa Mhasibu Jamaldin naye alijipakia katika gari yake tayari kwa kuelekea nyumbani kuweka mambo yake sawa.

Akiwa hajatia chochote tangu usiku wa jana, baada ya baba yao kutorejea nyumbani, sasa alianza kusikia njaa ikimuuma kwa ukamilifu wake. Akaachana na ile njia inayokwenda nyumbani kwao, akakata kushoto na kusonga mbele zaidi kulikokuwa na mgahawa mzuri wa kisasa uliokuwa hatua chache toka kilipo kituo cha utamaduni wa watu wa Urusi, Russian Culture Centre.

Hapa aliagiza maini rosti, kwa chapati nne za maji na supu ya kuku wa kienyeji. Alikula chakula kile vizuri sana hasa ukizingatia njaa aliyokuwa akiisikia. Wakati akiwa ukingoni kukimaliza chakula kile, akasikia simu yake ikiita. Akachukua tishu na kujifuta haraka, kisha akaichukua na kuingalia. Jina la Uncle Sam likatokea mbele ya kioo chake. Akafanya haraka kuipokea.

“Sema anko!”

“Fresh uko wapi Shuwena?! Maana simu za wengine wote hazipatikani!”

Shuwena akamtajia mahala aliko na kumuuliza. “Wewe je, uko wapi?”

“Nakuja sasa hivi!” Samson akasema na kukata simu. Shuwena akaendelea kumalizia chakula chake, muda mfupi baadae Shuwena akamuona Samason akijikaribisha mwenyewe kitini. “Yaelekea ulikuwa na njaa sana, sahani imebaki nyeupe kabisa, Na vile ilivyokuwa imejaa, sipati picha huko tumboni kukoje!” Samson akatania.

“Wacha anko, kama ulikuwepo vile, kama sijavimbiwa leo, sijui!” Shuwena akajibu akitabasamu, huku akitoa mbwewe ya kushiba.

Ule mwanya wake ukamfanya apendeze zaidi hali vile vishimo viwili vitatu vilivyotokea hapa na pale katika mashavu na kidevu chake vikimfanya awe mzuri mara dufu. Akaongeza “Toka jana mchana nilikuwa sijaweka chochote cha maana tumboni!”

“Usijali! Mambo yatakuwa mazuri tu!”

“ Naomba Mungu iwe hivyo!”

“Mzee yuko wapi? Nimefika hospitali nikaambiwa amehamishwa, daktari aliyempokea ambaye naambiwa ndiye pia aliyeshughulikia uhamisho wake hayupo na sio simu ya daktari, Mama wala ya Moses iliyopatikana. Bahati nzuri simu yako tu ndiyo imepatikana!”

“Ni kweli, leo tangu asubuhi simu zinasumbua sana. Nahisi ni mitandao ya simu. Maana hata sie tulijaribu kukupigia kwa muda bila mafanikio. Mzee amesafirishwa kwenda Ujerumani kwa matibabu zaidi. Tulikutafuta sana ili uondoke pamoja nae, lakini hukupatikana!”

“Kwa nini mlifikia uamuzi huu?” Samson akashtuka kwa dhati kengele ya tahadhari ikilia kwa nguvu kichwani mwake. Hata hivyo alijitahidi, Shuwena asiouone mshtuko huu.

“Sisi sio tuliofikia maamuzi haya anko! Ni Serikali!” Shuwena akang’aka kujitoa lawamani. “Na wamelazimika kufanya hivi ili kuokoa maisha ya Mzee. Tumefanya kikao na kukubaliana, tena na mimi ilikuwa niondoke kama isingekuwa kukabiliwa na mitihani inayoanza kesho Shuleni!” Akatua na kupiga funda la supu kabla hajaanza kumueleza Samson kwa kina, kinagaubaga kila kilichojiri nyuma yake tangu yeye alivyoondoka na kuwaacha pale hospitalini mpaka sasa.

“My God!” Samson alimudu kusema baada ya Shuwena kumaliza kumpa yale maelezo. Kwa mara ya pili jamaa wametuzidi kete! Samson akawaza kwa hasira, Hata hivyo bado tunayo turufu!” Akajiambia akiinuka, halafu akaongeza kwa sauti, “Wewe nenda nyumbani, mie wacha niende mahala. Ntakujulisha baadae kinachojiri!”

“Hatwendi hivyo anko!” Shuwena akachachamaa nae akisimama. “Hujaniambia kwa nini simu zako zilikuwa hazipatikani. Hatujajadili kwa nini simu za mama na daktari hazipatikani wakati sisi za kwetu ziko hewani na hakuna tatizo la mtandao!” Shuwena akatua.

Samson akajikuta akitabasamu, akili ya Shuwena ilikuwa inafanya kazi vizuri sana.

“Hayo ndiyo ninayokwenda kuyafuatilia Anko! Ndio maana nimekwambia nitakujulisha baadae kitakachojiri!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Sikia Anko, mwanzo nilikubali kubaki Tanzania kwa ajili ya mitihani baada ya kuhisi mzee yuko katika mikono salama. Kwa hali ilivyo sasa, naanza kuhisi mzee hayuko ndani ya mikono salama. Naomba tu nikutaarifu kuwa siendi kokote, mguu wangu, mguu wako mpaka tunaijua hatima ya Baba yangu, mama yangu na yote yanayowazunguka!”

“Ukifanya hivyo unakosea Shuwena. Suala hili ni kubwa kuliko unavyoweza kufikiria. Naomba unipe muda nishughulikie masuala haya haraka ili baadae tujue jambo la kufanya, tafadhali Shuwena, nina sababu zangu za kufanya hivyo!”

“Sababu gani?”

“Kama Mzee atakuwa hayupo katika mikono salama, na kama sisi tutaonekana kufuatilia. Yanaweza kutokea mapambano pengine ya kutupiana hata risasi za moto, mapambano ambayo yanaweza kupelekea vifo. Haitapendeza tukifa kabla ya kumuweka mzee katika mikono salama, kama ni kweli hayuko katika mikono salama!”

“Sijali anko. Kwa ajili ya baba yangu, niko tayari kufa!”

“Ni sawa uwe hujali!” Alikuwa Samson kwa sauti ya upole, hali moyoni akiwa na hasira kali sana dhidi ya yeyote aliye nyuma ya mikasa hii. “Lakini umejiuliza kama mie na wewe tutauawa kwa pamoja kitu gani kitatokea?”

“Una maana gani?”

“Tutawaacha wote wanaomfanyia mzee hila wakitimiza mipango yao kiulaini na kuifanya familia yenu kuishi kwa taabu baadae, Je ndilo jambo unalotaka litokee?”

“Of Course hapana!”

“Basi naomba uniache mimi niwe mbele, wewe uwe nyuma yangu, ili kama itatokea nitauawa mimi, wewe unaweza kufuatilia suala hili na hatimaye ukafanikisha kuwatia nguvuni wafanya hila wote na hapo utakuwa umeifanya familia yenu kuishi vyema!”

“Kwa hiyo unataka kuniambia nini?”

“Wewe kaendelee na shughuli zako, baadae tutawasiliana, kukutana na kujadiliana ili kujua jambo la kufanya, Sawa!”

“Sawa anko!” Alikuwa Shuwena baada ya kukubaliana na Samson.

Samson akamuacha na kuondoka kichwa chake kikiwa kimevurugika vibaya sana. Safari yake iliishia ofisini kwa Chifu wake mzee Anderson Chillonga. Alikofika anamueleza yote yaliyojiri baada ya yeye kuondoka hospitalini.

“Duh!” Mzee Chillo akashangaa kwa dhati na kuuliza “Kwa hiyo?”

“Naomba unitafutie uthibitisho kama kweli safari hii imeratibiwa na Ikulu na Benki Kuu. Na uniulizie kwa nini imekuwa haraka hivi!”

“Subiri kidogo!” Mzee Chilo akasema akizungusha nambari za Katibu muhtasi wake na akamuomba amuunganishe na watu kadhaa. Alibakia akisubiria hivyo hivyo katika simu kwa muda mpaka alipoanza kuongea.

Aliongea kwa muda kabla hajakata simu na kuunganishwa sehemu nyingine tena. Baada ya kufanya hivyo mara tatu, akatua chini mkonga wa simu na kumtazama Samson. Kwa mbali akitengeneza kitu kama tabasamu la husuda, hata hivyo hakufaulu. Akamwambia Samson, “Nadhani sakata hili ni kubwa kuliko yote yaliyotangulia Samson!”

“Kwa nini Chifu?”

“Safari hii hukabiliani na watoto, unakabiliana na watu wazoefu wanaojua wanachokifanya barabara!”

“Bado sijakuelewa Chifu!:

“Sio Benki kuu wala Ikulu walioshughulikia uhamisho wa Mhasibu. Simu ya mwisho nimezungumza na jamaa wetu anayeshughulika na masuala ya anga, amenambia hakuna ndege yeyote iliyoondoka au inayoondoka kwenda Ujerumani muda huu. Ni ndege mbili tu za abiria zilizokwenda Uingereza leo, British Airways na Gulf Air na zote zimeondoka asubuhi sana!”

“Hii itakuwa na maana gani Chifu?”

“Itakuwa na maana moja tu Samson, kwamba ama akina Mhasibu wameondoka na ndege ya kukodi ama bado wako hapa hapa Tanzania, wameamua kumpeleka katika eneo ambalo wanaweza kuwa na uhuru naye, swali la kujiuliza bado ni lile lile. Wamempeleka wapi na wanadhamiria kumfanya nini?!”

Samson akachoka kwa kila hali mambo yalielekea kuwa magumu. Akazungumza na Chifu wake na kumuomba amsaidie mambo fulani, Chifu akamuahidi zaidi ya ushirikiano. Akaaga na kuondoka.

Lile la kutopatikana kwa simu zake wala za mke wa Mhasibu na Moses halikumuumiza kichwa. Alijua wale waliomgonga Mhasibu asubuhi ya leo, ambao alihisi ndio waliomteka tena kwa kujisingizia ni watu kutoka Ikulu na Benki Kuu; walitumia kifaa cha kisasa cha kupeperusha mbali mawasiliano ya simu kiitwacho No Network!

Hiki kilikuwa kifaa kidogo chenye ukubwa wa kiberiti cha gesi ambacho kwa kawaida huwa kina umbo la kifaru, ile mashine ya kivita itumikayo kurusha makombora kwa masafa ya kati na marefu.

Kifaa kile kinapowashwa hupeperusha mbali mawasiliano ya simu kwa umbali wa mita hamsini mpaka mia moja kutoka mahala kilipo kifaa hicho. Hii ilikuwa teknolojia iliyotumiwa sana na majasusi wa C.I.A wakati wanapotaka kuvamia au kuteka mahala, ili kuzuia mawasiliano yasiingie wala kutoka katika eneo ambalo wanataka kufanya kazi zao.



http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Kifaa hiki kilikuwa na uwezo wa kuzuia hata simu za mezani na kwa Tanzania kiliwahi kutumiwa na maafisa usalama wa Marekani pale Rais George W. Bush alipotembelea Tanzania na kufanya mkutano na waandishi wa habari Ikulu, ambapo waandishi waliruhusiwa kuingia na Ikulu na simu zao bila kuzima, lakini hakuna iliyokuwa ikitoa wala kupokea mawasiliano yoyote.

Dawa ya kifaa hiki aliijua. Ilikuwa ni lazima upate nambari za kifaa hiki na kwa kuwatumia wataalamu wa IT unaweza kukizima na simu za watu wa jirani zikafanya kazi. Lakini hili linahitaji muda sana na utaalamu wa hali ya juu wa kuiingilia masailiano ya internet, maarufu kama hacking. Utaalamu haukuwa tatizo, tatizo ni muda wa kutosha kulishughulikia hili.

Hilo la kwanza, la pili kufanikiwa kwa jambo hili kutamfanya yeyote mwenye kifaa hicho huko aliko atambue kuwa mbinu yake imebainika na kuna mtu au watu wanajaribu kumfikia. Hakuhitaji digrii kujua kitakachotokea. Jamaa wanaweza kumpoteza Mhasibu na mkewe ili wao waendelee kuwa salama. Ni hili lililomfanya aachane na mawazo hayo na kutafuta njia mbadala.

Ni hili pia lililomfanya asijisumbue hata kuendelea na mpango wake aliokuwa amejipangia wa namna ya kuitekeleza kazi hii. Hata hivyo kwa kuwa alikuwa amempa jukumu fulani, mtu fulani, mahala fulani; alijua akifika huko aendako atakuwa na uhakika wa kupata anachokifikiria na kutoka hapo atajua la kufanya.

Safari yake iliishia kwa yule jamaa yao, mtaalamu wa mambo ya anga ambaye awali alikuwa ameongea na Mzee Chillo, mtaalamu ambaye idara ya ujasusi ya taifa ilikuwa ikimtumia kukabiliana na hila zozote za upande wa anga.

Ni huyu aliyempa taarifa za uhakika kuwa kulikuwa na ndege moja tu ya kukodi iliyoondoka kwenda Uingereza na sio Ujerumani muda mfupi uliopita kwa ajili ya kupeleka mgonjwa.

Zikiwa taarifa ambazo hakuzitarajia, Samson aliulizia ndege hiyo inamilikiwa na kampuni gani. Majibu aliyoyapata yalimfanya awe katika ofisi za kampuni ile muda mfupi baadae ambapo kwa kutumia mbinu zake za hali ya juu aliweza kujua ndege hiyo ni ya aina gani, iliondoka muda gani, imebeba watu wangapi, itatua wapi na muda gani.

Akapata majibu yaliyomridhisha, halafu akarudi tena kwa yule mtaalamu wa masuala ya anga, akamshukuru na kuondoka baada ya kumuomba amsaidie jambo jingine moja zaidi.

Kutoka hapo alikuwa kwa mtaalamu wake mwingine wa mawasiliano ya simu. Huyu alimuomba ampatie taarifa za simu iliyopigwa asubuhi nyumbani kwa Mhasibu. Dakika chache baadae alikuwa na mazungumzo yote ya Mhasibu na Matheo. Mazungumzo ambayo yalimfanya atabasamu baadae na kumgeukia yule mtaalamu wake.

“Unaweza kuniambia anapoishi Matheo?”

“Kwa nini nisikwambie? Subiri dakika chache tu!” Akajibiwa. Dakika chache baadae akaambiwa. “Matheo anaishi mtaa wa Kajenge road Kijitonyama, nyumba namba 24!”

“Asante kaka!” Samson akashukuru akisimama. “Wacha niende huko Kajenge Road. Nikiwa na tatizo jingine nitakuja kukuona. Akashukuru na kuondoka.

Hakupata taabu kuiona nyumba ya Matheo iliyokuwa katika kona ya mwisho ya Mtaa wa Kajenge, jirani na madalali maarufu wa nyumba na magari Bahari Baazar. Pengine kilichomtisha ni kule kukuta nyumba ikiwa imezungukwa na maturubai matatu, pamoja viti vya kutosha vya plastiki hali kukiwa na watu kadhaa walioketi katika viti hivyo; huku muziki wa taratibu kutoka katika spika mbili kubwa ukiwaburudisha taratibu kwa nyimbo za maombolezo.

Kwa kila hali kulikuwa na msiba.

Samson akaegesha gari lake sehemu kulikokuwa na nafasi, na kujikaribisha katika viti vile hali akiwasalimia aliowakuta na kujiunga nao katika mazungumzo. Dakika chache baadae alikuwa amepata taarifa alizohitaji. Kwamba Matheo alikuwa akiishi na mdogo wake wa kiume katika nyumba hii na kwamba likuwa na mipango ya kuoa mwezi ujao baada ya kutalikiana na mkewe miaka michache iliyopita kutokana na matatizo ya uaminifu.

Kwamba baada ya kutengana, mkewe alikuwa ameondoka na wanae wawili mmoja mwenye miaka nane na mwingine miwili na kumfanya aishi mpweke mpaka alipokuja mdogo wake huyu ambaye alikuwa akimtafutia nafasi ya kujiunga na Chuo cha Ustawi wa Jamii pale Kijitonyama. Ni huyu mdogo wake aliyeigundua maiti ya kaka yake wakati akijiandaa kwenda Chuoni asubuhi ya leo.

Kwa kutumia hila, Samson aliweza kumfikia kijana yule aliyekuwa na umri wa miaka ishirini au ishirini na moja hivi. Huyu alidai kuwa kaka yake alipokea mgeni jana usiku ambaye alidai ana mazungumzo naye ya faragha, ambapo aliwaacha na kwenda kumuona Shangazi yake Mikocheni ambako alilazimika kulala baada shangazi kumlazimisha alale.

Na aliporudi nyumbani leo asubuhi ndipo aliposhangaa kukuta mlango ukiwa wazi jambo ambalo halikuwa la kawaida, kwani muda huo Matheo huwa ameenda kazini na huwa anafunga milango na kuiweka funguo mahala ambapo ni yeye tu anayepajua.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Hili likamfanya ahisi wameibiwa, na alipoingia ndani ndipo akakuta mwili wa kaka yake ukiwa umepigwa risasi shingoni. Taarifa kutoka kwa majirani kuwa hawakusikia mlio wowote wa risasi ilimfanya kijana yule ahisi kuwa yeyote aliyemuua kaka yake alitumia bastola iliyofungwa kiwambo cha kuzuia sauti.

Pamoja na taharuki aliyoipata, aliweza kutoa taarifa polisi ikiwa ni pamoja na kuwajulisha ndugu jamaa na marafiki ambao walifika baadae kwa ajili ya kupanga taratibu za mazishi.

Ilitosha

Samson akamshukuru, kumuaga na kuondoka. Naam! Samson akawaza. Shughuli inaanza kuwa tamu. Ndani ya siku moja, tayari mtu mmoja ameuawa na mwingine kugongwa na gari. Huyu aliyegongwa hali yake ni mahututi ametoroshwa kwenda kusikojulikana. Lazima tu kuna jambo kubwa linalolikabili au litakalolikabili taifa.

Safari yake iliishia kwa yule mtaalamu wa mawasiliano wa awali, ambaye alimtaka ampatie mawasiliano ya simu zilizoingia katika namba ya Matheo kabla na baada ya kifo chake. Jambo ambalo halikuwa rahisi tena, kwani ilionekana kuna mtu aliingia katika system na kufuta kila kilichotokea baina ya simu ya Matheo na nyingine yoyote.

Hali ambayo ilimfanya ajione kama ambaye hajafika popote.

Ikambidi arejee nyumbani kwake akifikiria upya namna ya kuliendesha na kulikamilisha zoezi lake katika muda mfupi wa saa sabini na mbili alizopewa, huku saa tano zikiwa zimekatika tayari. Foleni ya kukimbia hapa na pale ikiwa ni pamoja na kwenda Kijitonyama na kurudi ikiwa imetumia zaidi ya muda huo na kumkera sana. Ilikuwa ni wakati huu simu yake ya mkononi ilipoita.

“Ndiyo Chifu!” Akasema akiipeleka simu yake sikioni.

“Interpol watakuwa online dakika kumi na tano zijazo!”

“Ooh thanks a lot Chifu wangu! Nakuja mzee!” Akasema haraka akiliparamia gari lake na kuelekea ofisini kwa Chifu. Alizungumza na Interpol kwa dakika kumi na tano hivi na alipomaliza, alijikuta akiwa na ahueni fulani kwa kuwa alijua baadhi ya mambo yanayomtatiza yatakuwa yamepatiwa majibu saa chache zijazo.

Halafu akampigia simu wakala wake wa safari na kumtaka amuandalie safari ya kwenda Uingereza kwa ndege nzuri haraka iwezekanavyo. Naam, kwa hali ilipofikia hapo ilikuwa ni lazima aondoke akaichezee ngoma hiyo London Uingereza.

Dakika chache baadae alikuwa akipokea maagizo kutoka kwa wakala wake wa usafiri.

“Utaondoka leo saa moja jioni!”

“Na ndege gani?”

“British Airways itakayotoka South Africa!”

“Asante!”

“Usijali kaka, tiketi yako ninaiscan hapa na nitakutumia soon kupitia email address yako!”





“Nitashukuru!” Samson akashukuru na kuaga.

Kutoka hapo alikwenda nyumbani kwa Mhasibu kwa ajili ya kuongea na Shuwena. Maongezi yake na Shuwena yalikuwa mafupi tu, kwamba Shuwena aendelee na masomo kama kawaida, ampe muda Samson afuatilie suala hili kwa ukaribu zaidi kwa kuwa amefikia mahala pazuri sana.

Alimwambia kuwa Mzee amefika salama Ujerumani na tayari ameanza matibabu. Alimwambia kuwa kutopatikana kwa zile simu ilikuwa tatizo la mtandao ambalo Mkurugenzi wa mamlaka ya mawasiliano alikuwa amemwambia yalitokea kwa dharura tu. Yote haya aliyafanya ili kuutuliza wahka wa binti huyu ili aweze kufanya mitihani yake ya mwisho vizuri hiyo kesho.

Jambo la muhimu ambalo Samson alimuomba Shuwena kulidumisha ni mawasiliano baina yao sio tu kwa kujua hali ya mzee pekee, bali pia na endapo ataona au kuhisi au sikia kitu chochote kisicho cha kawaida. Jambo ambalo Shuwena alilikubali na kuahidi kulifanyia kazi.

Maswali mengine machache ya Shuwena kwake aliyajibu kwa umahiri huku akitumia hila zaidi na kuongopa na hapa na pale ili tu kumfanya binti huyu atulie na aendelee na shughuli zake na asing’ang’anie kufuatana naye katika kila hatua. Jambo ambalo alifanikiwa pia kwa kiwango kikubwa.

Mpaka anaachana na Shuwena na kuelekea mahala pengine, Shuwena alibaki akiwa na matumaini makubwa na shughuli zinazofanywa na Samson Kidude. Kitu ambacho Shuwena hakukijua ni kuwa Samson alikuwa amemuwekea mtu mwingine ambaye alikuwa akiangalia nyendo zake ili kuhakikisha binti huyu hakabiliwi na hatari yoyote, wakati yeye atakapokuwa nje ya nchi.

Kufikia saa moja na nusu usiku wa siku hiyo, Samson alikuwa hewani, ndani ya ndege kubwa ya British Air ways akielekea London Uingereza.



* * *http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Baada ya tua tua ya hapa na pale, kuongeza mafuta na sababu nyingine za kiitifaki; hatimaye Mke wa Mhasibu, na wale maafisa wa ‘ikulu’ walijikuta wakitua salama usalimini katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Heathrow jijini London nchini Uingereza.

“Na mbona tumeshuka Uingereza badala ya Ujerumani?” Nadia alimuuliza yule jamaa waliyeambatana naye baada ya kusoma neno Heathrow International Air port.

“Ni kweli mama, wale madakatari tuliotarajia kuwakuta Berlin wako katika mkutano mzito unaoendelea sasa katika hospital ya St. Thomas. Ile aliyolazwa baba wa Taifa mwalimu Nyerere. Tumeona ni afadhali tuwawahi ili mgonjwa wetu apate tiba. Au tumekosea mama?”

“Hapana baba, mko sahihi kabisa. Jambo la muhimu ni afya ya mume wangu tu!” Akajibu.

Sasa walianza kutoka nje. Watu kadhaa wazungu kwa waswahili ambao Mke wa Mhasibu hakuwajua walikuja na kuwapokea, kisha wote kwa pamoja wakaanza ile safari kuelekea katika ile hospitali maarufu ya Saint Thomas ambako walipokelewa vizuri na Mhasibu kuanza kupata matibabu ya hali ya juu. Madaktari wakitakiwa kufanya kila wanaloweza ili maisha ya mtu yule yaokolewe.

Ni baada ya Mhasibu kuingizwa katika chumba cha matibabu maalum na kuanza kupata huduma, ndipo mkewe Nadia alipoweza kutulia kwa maana ya kupata nafasi ya kula, kuoga na kubadili nguo.

Na sasa alikuwa amejipumzisha juu ya kitanda kile ambacho kilikuwa chumba kimoja na kile ambacho Mhasibu angerudi kupumzishwa baada ya kutolewa katika kile chumba maalum cha matibabu.

Hapa kulikuwa na TV moja nzuri ya kisasa ambayo wakati huu Chanel ya BBC ilikuwa ikirusha matangazo mbalimbali sambamba na muziki. Aliingalia kidogo na kuipuuza kabla hajaendelea na mambo yake. Lakini mlio usio wa kawaida uliotokea katika Luninga ile ulimfanya aachane na chochote alichokuwa akikifanya na badala yake ainue macho na kuitulizia TV kana kwamba amegundua inataka kumtoroka.

Habari!

Haya yalikuwa maandishi ya awali aliyoyaona yaliyoandikwa katika lugha ya kiingereza, yakiwa na vikorombwezo vya dunia inayozunguka na picha za vitu anuai ambazo kwa hakika ziliyavuta macho yake. Hayakuwa maandishi yaliyomshangaza kwa kuwa alishaona mara nyingi sana katika maeneo mengi aliyokwenda na kuangalia Televisheni.

Kilichomshangaza ni zile picha za nyumbani kwao Dar es salaam, picha ya mumewe Mhasibu Jamaldin na picha ya Katibu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa na waandishi wa habari.

‘Afrika yaendelea kutimiza wajibu wake kwa wananchi wake, huko Tanzania fedha za kutosha zilizokuwa zikiwekwa kwa ajili ya kulipia madeni kwa mataifa hisani zaibiwa katika benki kuu ya Tanzania, Rais amtimua Kazi Jamaldin Mhasibu Mkurugenzi wa Benki hiyo na...!’

Hii ilikuwa sauti ya mtangazaji iliyozisindikiza picha zile. Sauti iliyomfanya Mke wa Mhasibu ainuke na kukaa vizuri huku akitumbua macho yake kwa nguvu zake zote kuitazama TV ile kana kwamba ana mashaka na anaowaona, kwamba huenda watatokeza nje ya Televisheni ile.

Naam! Alipokea habari kwa ukamilifu wake, kwamba mumewe alikuwa ametimuliwa kazi kwa wizi wa kutisha wa fedha za umma kule nyumbani kwao Tanzania katika benki anayoitumikia na kuiongoza. Hapa habari hizi zikiwa zimeongezwa chumvi na kuzifanya zionekane mbaya zaidi kama kawaida ya vyombo vya Magharibi vinapotangaza habari za Afrika.

Kwa mfano habari hizi zilisema Mhasibu ametimuliwa kazi, wakati ukweli ni kuwa alisimamishwa kupisha uchunguzi wa tume. Zilisema fedha zote zimeibiwa, wakati zilizochukuliwa ni sehemu tu ya fedha hizo, zilisema baada ya wizi huo Mhasibu alikuwa ametoweka na hajulikani aliko, wakati Mhasibu alikuwa hoi hajitambui kitandani. Na mengine kadha wa kadha.

Ni haya yaliyompandisha hasira mke wa Jamaldin hata akajikuta akiwaka kwa hasira huku akiumia moyoni. Hakujua mumewe alikuwa anapungukiwa na nini hata atende wizi huo wa kutisha kwa kuchukua fedha za ngama ambazo nchi yake ilikuwa ikizitegemea kama dawa ili kuikwepa ile aibu ambayo kwa miaka na miaka Taifa lake limeshindwa kuiepuka. Aibu ya kudaiwa. Aibu ya kuwa na madeni kwa nchi mbalimbali za Ulaya na Amerika.

Naam, Serikali ilikuwa inajitahidi kwa kila hali kwa kufunga mkanda ili kulimbikiza vijihela vyake ili ije kulipa na kuepuka aibu, ikishindwa kufanya maendeleo kwa watu wake kwa kiwango inachotaka, hali ya umasikini ikizidi kushamiri na shilingi kuporomoka thamani.

Halafu katika kilele hicho, anakuja mtu kutoka kusikojulikana na kuipora fedha hiyo kikatili kabisa! “Hapana! Huu ni zaidi ya unyama, Ni zaidi ya ufisadi. Naam, hili halikubaliki!” Aliamua mke wa Mhasibu kwa dhati. Ilikuwa ni wakati huu pia alipoanza kuzihusisha harakati za mumewe ambazo hakuwa akizielewa na na wizi huu mkubwa kabisa kutokea nchini mwake.

“Lazima azirudishe!” Akaamua kwa dhati na kubakia akimsubiri aamke.



Sura ya Saba

Kikao kingine cha akina Victoria, kilikuwa kikifanyika mahala pengine tena pa siri zaidi. Safari hii kikiwa na wajumbe watatu tu, Victoria Brayson ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao kama ilivyo ada, Alfred Omary Mbuzi na Johnstone Mambo.

“Mkuu mie nafikiri wakati umefika wa kuachana na hii issue na kutoweka. Mbona tumeshapiga hela za kutosha tu, iliyobaki tugawane zile zilizobakia tutoweke. Ningejua huja mwisho wa safari mkuu!” Akaanza Johnstone Mambo.

“Wenzenu sijawaalika katika kikao hiki kwa kuwa nilihisi wana uoga wa kike! Nyie ni wanaume bana!” Alikuwa Victoria kwa karaha na kuongeza. “Mwanaume wa shoka hufa kiume! Hufa kiofisa na tai shingoni. Kitu gani kinakuogopesha hadi unataka tugawane. Nilishasema sitagana vibilioni, mie nitagawana matrilioni tu! Umeelewa?!”

“Taarifa za wizi wetu zimeshafika Ikulu kwa mkuu wa nchi, Rais ameshamsimamisha kazi Mhasibu na kana kwamba hiyo haitoshi ameunda Tume ya kufuatilia suala hili haraka ndani ya muda mfupi!”

“Sasa kinachokutisha ni kitu gani?”

“Mie ni kiongozi mkuu wa chama, barua nyingi za kwenda kule hazina kuchota fedha zilikuwa na saini yangu. Kwa maneno mengine mimi nitakuwa muhusika nambari moja katika kadhia hii. Mtu wa kwanza kuhojiwa na tume. Huoni kama njia ya kushikwa ni nyeupe na iko wazi?!”

“Kwa namna gani?!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Nitaulizwa fedha zile zilikuwa zinakwenda wapi na niliandika barua ile kwa mamlaka yapi na kwa idhini ya kikao gani? Nitashindwa kujibu na nitakuwa mtuhumiwa nambari moja. Njia nzuri hapa ni kugawana kilichopo na kutoweka tu!”

“Na wewe Alfred unasemaje?”

“Ile misheni ya kumtorosha Mhasibu si imefanikiwa vizuri?”







ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog