Simulizi : EPA
Sehemu Ya Tano (5)
“Kwa asilimia mia moja, tayari Mhasibu yuko Uingereza, anapata matibabu ya hali ya juu kutoka kwa madaktari waliobobea. Na kwa makusudi kabisa, tumeamua kuichukua na familia yake sio tu kujijengea mazingira ya kuaminika zaidi, bali tunajua inaweza kuwa rahisi kwa Mhasibu kuongea chochote na mkewe, na chochote hicho kikatufikisha mahala.
Tumemtaka Tarishi akae nae mbali kwa muda mpaka pale atakapoona muda umefika. Hii ni kwa vile Mhasibu anamtambua Tarishi vizuri sana. Kwa hila hali naamini mambo yatakuwa mazuri.
Tayari pia timu ya watu wetu tunaowaamini akiwemo Dr Gilbert wamepenyezwa miongoni mwa madaktari wa pale St Thomas Hospital. Kwa muktadha huu, naamini kila kitu turufu iko upande wetu. Na ndio maana baada ya kupata zile habari za Ikulu kuifahamu issue hii nikaona niwaite tujadiliane tena!”
“Na je” Alfred akauliza tena. “Tumefanya busara kumpeleka hospitali ile ambayo viongozi wa Tanzania huwa wanapenda kuitumia mara kwa mara? Hatuoni kama tumejipeleka mwenyewe katika domo la mamba lililo wazi tayari kututafua?”
“Mwanzo tulidhani ni uamuzi wa hatari, lakini kulingana na umuhimu wa taarifa tunazozihitaji kutoka kwa Mhasibu, na ubora wa tiba na vifaa wa hospitali ile, kulikuwa hakuna jinsi. Jambo la muhimu ni kwamba tayari tumewanunua karibuni madaktari na viongozi wote wa pale hospital kwa dola milioni tano, na ndio maana tumeigeuza hospitali kama ngome yetu kwa muda huku tukipata kila taarifa tunayoihitaji ndani na nje ya hospitali!” Akajibu kwa kirefu Vick.
“Na hali ya Mhasibu ikoje mpaka sasa?”
“Tayari anaendelea kupata matibabu na tumehakikishiwa anaweza kuzungumza tena! Hili likitokea atataja fedha, tukishazichukua Mhasibu atauawa na sisi tutatoweka na kwenda mbali na Tanzania na tukirejea tutakuwa watu wengine kabisa na hakuna anayeweza kutuhisi kama ndio sisi, wachilia mbali kututambua!”
“Tunajipangaje na hili suala la Rais kuunda Tume?” Alfred akauliza tena
“Hili ndilo nililowaitia tulijadili!”
“Je,” akauliza Vick “Mnaowaonaje wajumbe wa Tume, hawawezi kuwa na bei wale?”
“Unataka kusema nini?” Mambo akauliza kwa hofu.
“Tuangalie uwezekano wa kuwanunua! Najua watalipwa posho wakati wakifanya uchunguzi wao. Na posho yao hata iwe kubwa vipi kwa muda waliopewa haiwezi kufika milioni mia tano. Tukiwapa bilioni mbili au tatu kila mmoja ili wapindishe matokeo hawatakubali kweli?!”
“Hizo fedha zitakuwa nyingi sana Mkuu!” Johnstone Mambo akapinga.
“Sio nyingi Mambo, wajumbe wako watano, tukiwapa fedha hizo tutatumia bilioni kumi haidhuru kumi na tano. Sie tuna zaidi ya Bilioni mia tatu na hamsini!”
“Mie sikubaliani na ushauri huo mkuu!”
“Kwa nini?”
“Unaweza kuwafikiwa na kuwapa rushwa. Wakikubali ni heri, wakigoma je? Huoni kama tutakuwa tumemualika adui atufuatilie vizuri. Na kuna mjumbe mmoja mle ni kichwa maji na hamnazo kweli kweli, sijui anataka kugombea Urais baada ya chaguo maana huo utakatifu wake unashinda hata wa Yesu Masiha!”
Wakacheka
“Kwa hiyo?” Alikuwa Vick baada ya kumaliza kucheka.
“Mie nashauri jambo moja. Kwa kuwa Mambo ndio muhusika Mkuu, anatakiwa asionekane tena hadharani, ahame kwake na simu zake zote zizimwe. Tumuagize Tarish ahakikishe Mhasibu anaeleza pesa alipozificha, na baada ya hapo Gilbert amchome Mhasibu Sindano ya sumu imuue baada ya muda mfupi, maana baada ya kuongea na sisi hatakiwi kuongea na mtu mwingine yeyote!”
“Halafu?” Alikuwa Mambo tena.
“Twende tukazichukue hizo fedha na kugawana kisha kutoweka! Labda ushauri wangu mmoja tu kwa mkuu, mambo haya yasichukue muda mrefu tena, zikizidi sana ziwe siku mbili au tatu. Na tusikutane tena kabla fedha hazijawa mikononi mwetu. Tukikutana mara ya mwisho iwe ni kwa ajili ya kugawana tu, ama fedha zilizofichwa na Mhasibu au zile zilizopo katika Semitraller!”
“Hapo umenena Alfred!” Alisema Vick kwa tabasamu “Sasa ninyi mnaweza kwenda, ila Johnstone, wewe naomba ubaki hapa mara moja tujadili namna unavyotakiwa kutoweka ili kuikimbia tume ya Rais na familia yako unavyoiacha!”
“Hakuna shida mkuu!”
Alfred Omary Mbuzi akainuka na kuondoka, kabla Vick hajasema chochote, Simu ya Mambo ikaanza kuita. Ilikuwa namba ngeni. Akaitazama kwa muda mpaka ikakata. Ikaita tena akaitazama mpaka ikata.
“Mbona hupokei simu Mambo?”
“Ni namba ngeni! Na kwa kwa muundo huu wa mambo unavyojipeleka, naogopa hata kupokea simu mkuu!” Akajibu na ile simu ikaanza kuita tena
“Come on Johnstone, pokea simu bwana tujadili. Muda si rafiki yetu kabisa!”
“Hallow!” Akaita kwa sauti isiyo yake.
“Habari yako bwana Mambo!” Ilikuwa sauti ya kiume ambayo ilikuwa ngeni masikioni mwake kabisa.
“Salama, ndugu! Sijui ni nani mwenzangu?”
“Naitwa Partick Leonard. Nafanya kazi tume ya maadili ya viongozi. Ila kwa sasa ninaongea kama Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya kufuatilia matumizi ya fedha za akaunti ya madeni ya nje!”
“Ndiyo, nakusikiliza!”
“Tuko ofisini kwako na tunahitaji kupata maoni yako mawili matatu juu ya sakata hili!” Partick akatua. Mambo akasikia mwili unakufa ganzi na kijasho chembamba kikaanza kumtoka. Kwa kuwa alikuwa akiongea kwa kutumia Loud Speaker, Vick alikuwa akisikia kila kitu.
“Upo Johnstone!” Partick akauliza kule simuni. Vick akamhimiza kwa ishara azungumze, asikae kimya.
“Nipo ndugu yangu. Ila...”
“Ila nini?!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kuhusu utaratibu, ilitakiwa mniandikie barua nijiandae. Kwa sasa niko na majukumu mengine mbali sana na ofisi. Na kwa foleni ya Dar es salaam itanichukua muda kufika huko. Ndio maana nimekaa kimya. Hii ni kwa vile naelewa umuhimu wa jukumu mlilonalo!”
Akatua na kusikia pumzi za kitu kama kukata tamaa zikishushwa na Partick upande wa pili. Hili likamfanya Vick atabasamu huku akimpa ishara Mambo ashushe presha. “Cool down John!” Akamwambia kwa mnong’ono.
“Ni kweli ilitakiwa tukuandikie barua Johnstone!” Partick akaanza tena. Ila muda tuliopewa ni mchache sana. Isitoshe tumemuuliza Mwenyekiti wa chama akasema hamna majukumu mazito kwa sasa, ndio maana tukaamua kuja kinyemela. Kwani uko wapi?”
Mate yakampalia Mambo. Akakohoa kwa muda hali Vick akiendelea kumsihi atulie.
“Niko Kipawa, Uwanja wa Ndege kuna jamaa yangu nimekuja kumsindikiza, anakwenda Uganda!” Akajibu na Vick akamfanyia alama ya dole gumba kumpongeza.
“Okay! Tunakusubiri. Chukua pikipiki uje utuwahi. Tunakupa nusu saa tu, tunaamini itakutosha kutoka hapo Kipawa Airport hadi hapa Kinondoni Makao makuu ya Chama!” Partick akasema na kukata simu. Johnstone Mambo akabaki ameduwaa, ilikuwa amri.
Ile kauli ya kusema Mwenyekiti amewaambia hakuna shughuli yoyote muhimu ikawa imemuogopesha zaidi. Ndiyo, ina maana walianza kuzungumza na Mwenyekiti kabla hawajaja kuzungumza na yeye. Alimjua Mwenyekiti wao vizuri sana vile asivyopenda uzembe na anavyochukia wizi na ubadhirifu wa mali za umma, Mambo hakuwa na shaka kwamba Mwenyekiti huyo Daniel Killango, atakuwa ameimba kama chiriku na kuwaambia kila kitu.
Kwamba chama hakikuhusika kutoa fedha zile Benki kuu ili kugharamia uchaguzi mkuu kwa kuwa kilikuwa na akiba ya kutosha kutoka katika fedha zake za ruzuku ambazo zilianza kuhifadhiwa miaka miwili na nusu kabla ya uchaguzi.
Na vile yeye ndiye aliyehusika kichwa na miguu akijifanya kukiwakilisha chama, aliona amezama katika lindi la kinyesi sio kidogo. Kwa dakika kadhaa alijikuta akiogopa kuikabili hali halisi. Hata Vick alipomuuliza anafikiriaje, Mambo akamueleza kila kitu kuhusu hofu yake.
“Mambo, hutakiwi kwenda huko!” Vick alimwambia baadae.
“Sasa nitafanyaje mkuu?”
“Ile mipango yetu ya kutoweka inabidi ianze sasa hivi, muda huu huu! Hutakiwi kuonekana tena barababarani. Hebu nipe simu yako!”
“Na kuhusu familia yangu?!” Mambo akauliza akikaribia kulia wakati akimpa simu Vick.
“Hilo niachie mimi, umekuwa mshirika mzuri katika mpango huu tangu mwanzo hadi sasa!” Alikuwa Vick akiizima simu ya Johnstone, kutoa laini yake na kuivunja! Kisha akamwita mlinzi wake binafsi, William. Akamkabidhi akimtaka aihifadhi.
“Ondoa hofu, utajificha katika nyumba yangu ya Kibamba, wakati tukifanya mipango ya kukutoroshea Kenya, baadae Marekani! Mambo yameenda haraka kuliko tulivyofikiria, hata hivyo chini ya Victoria Brayson Kamugisha hakuna kitakachoharibika. Sijawahi kuasisi kitu kikawa na matokeo mabaya tangu niko jeshini, bungeni, usalama wa Taifa, Serikalini na sasa mstaafu!”
“Kuhusu mgao wangu je?!”
“Mgao utapata, tunaelewa ni mgao huo utakaoyafanya maisha yako yawe mazuri popote utapokuwa ulimwenguni. Worry not my dear Mambo, kokote utakaokuweko mgao wako utapata! Hofu ondoa!”
“Nitashukuru mama!” Akajibu kwa unyonge. Kiasi Vick alimuonea imani ila ndio hivyo tena.
Dakika chache baadae walikuwa barabarani wakielekea Kibamba ili kumficha Johnstone Mambo.
* * *
Matibabu yalikuwa mazuri na ya hali ya juu sana. Mara kwa mara aliitwa ndani alikokuwa akishughulikiwa mumewe na kuelezwa hiki na kile kabla hajaruhusiwa tena kutoka. Mara ya mwisho ilikuwa ile aliyoitwa na kuambiwa kuwa kwa kuwa Mhasibu alikuwa amevunjika miguu yote miwili, mkono wa kushoto, mbavu mbili na bega lake kuteguka ilikuwa ni lazima wamfanyie operation ili kuingiza vyuma, plastiki na viungo vingie vya bandia vyenye dawa ili aweze kupona kwa haraka.
“Je,” Akawauliza madaktari kwa hofu “Atapona?!”
“Kupona atapona tu mama! Serikali yenu imetutaka kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha mtu huyu anapona. Ila...”
“Ila nini?!” Mke wa Mhasibu akawahi kwa kihoro.
“itamchukua muda kidogo kurejea katika hali yake ya kawaida. Atatembelea kiti cha magurudumu kwa muda, baadae atatembelea magongo, kisha atachechemea na halafu atarudi kutembea kidogo kidogo kabla hajapona kabisa! Yote haya yanahitaji muda, subira na mazoezi ya mara kwa mara!”
“Potelea mbali, muhimu ni uzima wake tu! Na itachukua muda gani?”
“Muda wa nini?”
“Wa yeye kupona kabisa kabisa!”
“Si chini ya miezi kumi na minane!”
“Sawa!” Akajibu mke wa Mhasibu kinyonge.
“Basi saini hapa ili tuweze kuimalizia hii kazi kubwa ya mwisho!” Akaambiwa akikabidhiwa zile karatasi. Akazisoma kwa muda, kabla hajazielewa na kusaini pale alipotakiwa kufanya hivyo.
Alipomaliza hapo alitoka nje ili kuwapisha madaktari wafanye kazi yao kwa tuo.
Akiwa hapa nje, akawaona tena Bazzi, Joseph, wale madakatari wawili wa kule Aga Khan hospital na mwafrika mwingine mmoja ambaye alikuwa miongoni mwa wale waliokuja kuwapokea kule uwanjani wakimkaribia. Akainuka na kuwakaribisha.
“Mama Mhasibu?” Bazzi akaita.
“Bee!”
“Tunashukuru sana kwa ushirikiano wako na wenu kama familia!”
“Mimi ndiye ninayepaswa kuwashukuru baba!”
“Usijali Mama! Hata hivyo nilitaka kukwambia kitu kidogo tu, kuwa sisi sasa tumemaliza jukumu letu, jukumu lililobaki ni la madaktari ambao wamepewa kazi ya kuhakikisha mtu huyu anapona kwa gharama yoyote!
Kufanikiwa kwa jukumu hili, kunatufanya sisi turudi nyumbani kuendelea na majukumu yetu mengine. Hapa atabakia huyu mwenzetu Michael na mwenzie mmoja ambaye hajafika. Ni hawa wanaobakia kuiwakilisha Serikali hapa, bila shaka na ninyi mtabaki ili kuendelea kuangalia hali ya mzee au siyo?”
“Ndiyo!” Akakubali huku akitikisa kichwa taratibu juu na chini.
“Kukiwa na shida yoyote muone Michael au msaidizi wake Amani ambaye atafika muda wowote kutoka sasa!” Akamaliziahttp://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hakuna taabu!” Mke wa Mhasibu akasema, wakapena mikono ya kuagana wale wengine, na ilipofika kwa Michael, ikawa kama wanakaribishana.
“Nafurahi kukufahamu!” Kila mmoja alisema kabla hawajamuacha mke wa Mhasibu na kutokomea katika vyumba vingine. Mama Mhasibu akahisi ndio wanaondoka. Akaendelea kuketi pale akiangalia Televisheni na kuperuzi mitandao mbalimbali ya kijamii kwa kupitia simu yake.
Masaa sita baadae madaktari walimaliza ile operation yao kwa Mhasibu Jamaldin. Operation ambayo iliondokea kuwa miongoni mwa zile kazi ngumu walizopata kuzifanya. Baada ya Operation walimtoa katika chumba cha upasuaji na kumuingiza katika chumba kingine cha kupumzikia, na katika chumba hiki, ni mke wa Mhasibu pekee, aliyeruhusiwa kukaa naye jirani. Mlinzi Moses alitakiwa kubaki nje muda wote.
Michael alifika baadae na kuitazama hali ya Mhasibu kwa matumaini na tabasamu kuu, hali akimshuru Mungu kwa kusikia maombi yao. akamgusa Mhasibu hapa na pale na kuondoka baada ya kumhakikishia mke wa Mhasibu asiwe na hofu tena, kwani kwa mujibu wa madaktari, hali ya Mhasibu inakwenda kuimarika.
Kuondoka kwa Michael, kulimfanya Mke wa Mhasibu aendelee kuperuzi na kuangalia mitandao mbalimbali ya kijamii inasema nini, alipoifungua ile ya Tanzania, habari za mumewe kusimamishwa kazi kwa tuhuma za kukwapua mabilioni zikajirudia. Akaizima Smart phone yake na kulala.
Labda angeweza kulala kwa masaa mengi zaidi kama asingemsikia Mhasibu akikihoa kwa taabu, akainuka na kumuangalia kwa umakini hali akimsuka suka kifuani katika namna ya kumpa ridhiko na starehe ya hali ya juu.
“Pole Mahabuba, Pole laaziz! Pole sana barafu wa moyo wangu!” Akamwambia akiendelea kumsukasuka kifuani taratibu. Mhasibu akafumbua macho taratibu, mwanga wa taa ukamfanya ayafumbe tena. Dakika chache baadae akayafumbua tena taratibu mpaka akafaulu kuyafumbua kabisa. Kitu cha kwanza kukiona lilikuwa tabasamu zuri la mkewe Nadia. Lile ambalo humfanya awe na furaha usoni na raha moyoni.
Ule mwanya maridhawa pale katikati ya meno ya mbele juu, na vile vishimo vilivyotokeza hapa na pale katika mashavu na kidevu chake wachilia mbali lile shingo zuri la miraba miraba wakati huu likiwa limebeba cheni nzuri, nyembamba ya dhahabu kwa pamoja vilimfanya Mhasibu ahisi kama anayemuangalia hurulain; yule malaika mzuri wa peponi ambaye atatolewa kama zawadi na Mungu, aolewe na wanaume wafanyao mema hapa duniani.
“Nadia!” Mhasibu akaita taratibu hali akijitahidi kutengeneza kitu kama tabasamu.
“Mimi hapa bwana wangu!” Sauti yake ilikuwa liwazo lingine kwa Mhasibu.
“Hujambo?!” Akamuuliza. Swali hili likamfanya Nadia atabasamu zaidi na kuvutia mara dufu. Ni yeye aliyetakiwa kumuuliza swali hili mgonjwa, sio mgonjwa amuulize yeye.
“Mie sijambo!” Akajibu kwa sauti ile ile tamu na kuongeza “Unajisikiaje sasa?”
“Mi mzima!” Akasema. “Niko wapi hapa?”
“Uko hospitali, ulipata ajali ya gari!” Kauli hii ikamfanya Mhasibu akumbuke kila kitu.
“Sio ajali Nadia, niligongwa na akina Tarish mke wangu! Tena kwa makusudi. Walidhamiria kuniua wale!” Zikawa habari zilizomshtua Nadia. Hata hivyo akajitahidi kutounyesha mshtuko huo kwa lengo la kumuondoa hofu mumewe hasa akizingatia kuwa ulikuwa umepita muda mfupi tu tangu arejewe na fahamu!”
“Usijali Laaziz. Bahati nzuri hukufa, na hutakufa!”
“Lazima nijali Nadia, wakigundua kuwa niko hapa na niko hai, watakuja kuniua tena!”
“Kwa nini unasema hivyo!”
“Arg! Ni hadithi ndefu sana mke wangu!”
“Huwezi kunisimulia hadithi hiyo?”
“Ninaweza, lakini sio sasa. Samson yuko wapi?”
“Samson amebaki Tanzania!”
“Tanzania?! Hapa ni wapi?!”
“Uingereza! Uko Hospitali ya Saint Thomas!”
“Oh my Lord... Oh My God!” Mhasibu akaweweseka na kuuliza kwa kihoro “Nani amenileta huku?!”
“Serikali!”
“Kitu gani?” Akashtuka akikaribia kuinuka.
“Basi taratibu mume wangu, ungali na majeraha mabichi bado. Bado hujapona kabisa. Tuliza kichwa chako dawa ifanye kazi kwanza!”
“Samahani!” Mhasibu akasema akijitahidi kujituliza. Akaendelea “Pengine hujui kauli yako ilivyonishtua. Hebu nithibitishie tena, na naomba usinidanganye kabisa mke wangu. Niambie ukweli mtupu. Ni nani aliyenileta huku?”
“Ni Serikali mume wangu. Ikulu na Benki kuu!”
“Wao walipataje habari zangu?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mi sijui kwa kweli, ila nilipigiwa simu na Samson muda mfupi baada ya wewe kupata ajali, tukakimbilia Aga Khan ambako tuliambiwa kuwa unapata matibabu na haturuhusiwi kukuona!”
“Enhe!”
“Mara akaja daktari akatuita ofisini kwake tukakutane na wale maafisa, ndio ikawa sababu ya wewe kuletwa huku!”
“Maafisa gani?”
“Wa Ikulu na Benki kuu!”
Mhasibu akaendelea kumuangalia mkewe kwa namna ya kutoelewa kabisa. Hapo tena ilimlazimu Nadia kumueleza mumewe kila kitu kwa tuo, tangu mkasa ule ulipoanza mpaka pale ulipofikia. Zikawa taarifa zilizomuacha Mhasibu hoi. Kwa sekunde kadhaa alibaki kimya akitafakari ukweli na uhalisia wa yale mambo.
Naam! Inawezekanaje uende ukamwambie Rais juu ya wizi fulani, Rais akufukuze kama mbwa, upate ajali halafu rais huyo huyo aingie gharama za kukusafirisha nje ili upone?! Au ni kwa sababu wanataka kujua zile fedha zilizosalia ziko wapi? Aliendelea kujiuliza maswali juu ya maswali bila kupata majibu yaliyouridhisha moyo wake.
“Mhasibu?!” Mkewe akamshtua toka katika lindi la mawazo.
“Naam!”
“Eti ni kweli?”
“Ni kweli nini?!”
“Kwamba umeshirikiana na wenzako kuiba fedha zote zilizokuwa zimetengwa kulipia madeni ya Tanzania nje ya nchi?!”
“My God!” Mhasibu akamudu kutamka. Tayari habari hizi zilikuwa zimevuja na kumfikia mkewe kabla yeye hajamueleza. Kabla yeye hajachukua hatua yoyote kukamilisha ule mpango wake wa kuhakikisha fedha hizi zinarejea hazina. Kabla yeye haja...”
“Na kwa nini ukafanya hivi Jamaldin enhe?” Mkewe akaendelea kumbana hali machozi yakitafuta njia katika kingo za macho yake, “Mtu mzima kama wewe, uliyepewa dhamana kubwa kama ile kwa maslahi ya taifa masikini, lenye wananchi masikini unawezaje kuwa na moyo wa chuma, ukaifanya roho yako iwe ya paka na kujivika ujasiri wa kifisadi namna hii?! Hapana mume wangu, Jamaldin ninayemjua mimi hakuwezi kuiba hata shilingi moja ya masikini!” Akatua na kulia kimya kimya.
Mhasibu hakujibu chochote. Ukimya wa kutisha ukapita.
“Nakuomba kitu kimoja mpenzi wangu” Nadia akasema baadae na kuuvunja ukimya uliokuwa umetamalaki. Kule kutojibiwa kitu na mumewe kukimfanya ahisi kuwa ni kweli mumewe alikuwa anahusika katika wizi ule mkubwa kabisa. Akaendelea “Ukifanya hiki utanijulisha ni kiasi gani unanipenda kunijali na kunithamini. Utanifanya niendelee kukupenda milele mume wangu. kama uliteleza ukashawishika kuiba, nakuomba sana sana, tena zaidi ya sana, uzirudishe pesa zote na uombe msamaha kwa watanzania. Hali ilipofikia ni mbaya mno. Nakuomba mume wangu!” Akatua na kubaki akilia kwa muda.
“Umenielewa Jamaldin?” Akauliza tena alipoona hapati jibu.
“Mie sijaiba hela Nadia!”
“Kweli?!”
“Wewe unanifahamu vizuri sana Nadia, mimi ni mtanzania kwa kuzaliwa. Mtanzania! Wa damu iliyosafishwa na maji safi ya maziwa na mito na ya vijito vya Taifa langu zuri.
Mtanzania mwenye maono kutoka juu ya mlima Kilimanjaro na uaminifu angavu kama mbuga ya Serengeti. Mtanzania mwenye moyo safi kama fukwe bikira za Zanzibar. Matumaini kwa kuwa zao la azimio. Ng'aavu kama vito vya Tanzanite kwenye ardhi ya wamasai. Mimi ni mtanzania. Mtoto wa watu wa Afrika, wa Tanzania. Uchungu wa mapambano ya ukombozi wa Afrika.
Maumivu ya Mapinduzi. Vyovyote vikwazo vya sasa, hakuna chochote kitakachoweza kunizuia mimi kuwa Mtanzania, mwana wa Afrika. Nchi ya Kambarage. Dola tuliyoumba wenyewe. Nimekaa pale benki kuu huu mwaka wa kumi na tatu, nimeboresha uchumi wa nchi na kuinua thamani ya shilingi ya Tanzania kwa ushauri na utendaji wangu ulioutukuka. Naijua nchi yangu, nazijua changamoto zake Nadia, Nakuapia mimi sijaiba, na sitakaa nije niibe walau shilingi moja ya nchi hii!” Jamaldin aliongea kwa hisia mpaka machozi yakamlenga lenga machoni.
“Sasa kama hujaiba ni kwa nini Rais amekufukuza kazi?!”
“Kitu gani!” Mshtuko uliompata Mhasibu ni Mungu tu aliyejua kwa nini hakuzirai tena.
“Taratibu mume wangu, ungali unaumwa usisahau hilo!”
“Najua, najua!” Mhasibu akakubali akijitahidi kujituliza. Hakufaulu. Kiu ya kuyajua mambo haya, ambayo kwake yalikuwa yakitokea haraka sana ikamfanya ashindwe kabisa kuidhibiti akili yake na kuwa mtulivu.
“Nadia mpenzi!” Jamaldin akaita kwa sauti isiyo yake. “Niambie mpenzi, mama wa watoto wangu, naomba uniambie ukweli mtupu! Je, ni kweli Rais amenifukuza kazi?!!”
“Ni kweli mume wangu, na sio kukufukuza kazi tu, ameunda tume kuchunguza namna wizi huu ulivyofanyika, Tume imepewa chache nne tu za kuikamilisha kazi hiyo!”
“We habari hizi umezipata wapi na hali unaniambia hapa tuko Uingereza?”
“Nimezipata hapa hapa kupitia taarifa ya habari ya BBC!”
“Ooh My Lord! Ooh my God!” Mhasibu akaweweseka zaidi. Sasa alitambua kuwa haiba yote aliyokuwa ameijenga mbele ya nchi yake na mataifa rafiki ilikuwa imechafuka vibaya sana. Na kwamba itatakiwa juhudi kubwa na muda wa kutosha kuweza kujisafisha na kubakia akiwa hana waa hata moja litokanalo na kashfa hii. Kiasi hili lilimfanya apandwe na ghadhabu hata kujikuta akitokwa na machozi taratibu.
Akakumbuka jinsi alivyoingia katika madaraka haya yaliyomgharimu kwa kuombwa na Serikali ya nchi yake kwa vile alivyofanikisha nchi za Afrika ya kati kupiga hatua kubwa kimaendeleo ikiwa ni pamoja na kuimarisha sarafu ya nchi hizo. Akafikiria namna alivyopambana kwa nguvu zake zote kuhakikisha uchumi wa Tanzania unakuwa na sarafu yake inaimarika, jambo ambalo alikuwa amefanikiwa kwa kuudhibiti mfumuko wa bei kwa kipindi chote cha utawala wake pale benki kuu, kuzuia shilingi isishuke thamani na kuupandisha uchumi kutoka asilimia tatu alizozikuta hadi asilimia tisa pointi kumi na moja!.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Leo hii anakuja kufukuzwa ki’mbwa ki’nguruwe huku dunia ikitangaziwa kuwa alikuwa fisadi nambari moja nchini, Hapana! Akakataa kwa dhati. Hata kama alikuwa na makosa, haya hayakuwa malipo yaliyomstahili. Kwa ujumla aliona kama Serikali ilikuwa ikishirikiana na akina Tarish kumdidimiza katika lindi la kashfa, umasikini na dhalala iliyovuka mipaka.
Na pale alipopambazukiwa na ukweli kuwa haya yametokea akijitahidi kukisaidia chama na nchi yake roho ilimuuma kama kidonda. Aliumia pia pale rais Chaguo aliposhindwa kuingia ndani ya moyo wake na kuona namna Mhasibu anavyoumia kwa wizi huo kutokea chini yake. “Mshenzi!” Akabweka akijitahidi kuinuka.
Haraka Mkewe akamzuia na kumtuliza akimtaka kuwa na subira na uvumilivu. Akiwa hapa chini, Jamaldin alitoa matusi ya kila aina kumtukana Rais Chaguo, wasaidizi wake na akina Tarish ilikuwa ni dhahiri kwamba alikuwa amechanganyikiwa haswaa.
Mkewe aliendelea kumfariji mpaka alipotulia kabisa ndipo alipomuuliza tena kulikoni hali hii. Mhasibu akiwa ameshaamua liwalo na liwe, na akiwa ameamua kutoweka na fedha alizozificha Uswiz kwa jina la mwanae; hakuona kama ilimstahili kuendelea kukaa kimya na kuificha familia yake, huku akiistahi Serikali ambayo kwake haikujua maana ya staha.
Alieleza kila kitu, tangu kilivyoanza, fedha zalizotoka, jamaa walivyoendelea kuchukua fedha hata baada ya uchaguzi, namna alivyowagomea, walivyomtishia kumuua, alivyozihamisha fedha zilizosalia na kuzificha mahala pengine, alivyotekwa mpaka simu aliyopigiwa na mfanyakazi mwenzake, alivyokwenda Ikulu na kuhitimishwa na ajali iliyomtokea.
Alichokificha ni kitu kimoja tu, kwamba zile fedha alizificha kule Uswiz kwa jina la Shuwena Jamaldin Mhasibu. Na alilificha hilo kwa sababu moja kubwa, alimjua mkewe vizuri sana. Kwamba ni mtu mwenye huruma, upendo na mapenzi ya kweli kwa familia na nchi yake. Kumueleza jambo hilo kabla yeye hajawa na uhakika atapona lini, aliona ni sawa na kuwaalika kuku wenye njaa kwenye mchele mwingi.
Kwa Nadia kwenda Ikulu kueleza ukweli wote na kumshawishi Shuwena waende Uswiz wakayatoe yale matrilioni ya shilingi na kuyarejesha mikononi mwa Serikali lisingekuwa jambo gumu hata kidogo. Ni hili lililomfanya amfiche.
“Masikini mume wangu... Poor Jamaldin!” Mkewe akahuzunika kwa dhati na kuongeza. “Pole sana!”
“Asante!” Akajibu Mhasibu.
“Unisamehe bure, sikujua kama umebeba mzigo mzito namna hii!”
“Usijali!”
“Na kwa nini ulificha mambo yote haya? Mie ningeweza kukushauri vizuri kabla!”
“Huo ndio ujinga wangu mke wangu, sikujua kama mambo yatakuwa mabaya hivi. Niliamini ni masuala ya kikazi na yana baraka za wakubwa!”
“Dah! Sasa utafanyaje?”
“Nitajua la kufanya tu, wacha nitulize kichwa na kufikiria. Hawawezi kunifanya mie ni mpumbavu kiasi hiki. Lazima wajute kwa yote waliyoyafanya!”
“Lakini kulipiza kisasi ni dhambi mume wangu!”
“Najua, mie silipizi kisasi, najitetea kwa udhalimu walionifanyia! Ila naomba unisaidie kitu kimoja!”
“Naomba uende ukamueleze mambo haya kaka Hafidh, mueleze mambo yote niliyoongea na wewe, mwambie na hali yangu, yeye atajua la kufanya!”
“Nitafanya hivyo!”
“Sio utafanya hivyo, ufanye sasa hivi!”
“Una maana nirudi Dar es Salaam? Na wewe nani atakuangalia?!”
“Hilo usihofu, Samson atafanya kazi yake!”
“Nilishakwambia Samson hayupo, ame...!’’
Mara mlango ukafunguliwa na Samson Kidude akaingia “Nimefika tayari!” Akajibu akiingia na kuongozana na kijana mwingine mmoja wa kizungu, nyuma yake akiwepo Moses.
“Waoooh! Samson mwanangu!” Nadia akashindwa kuvumilia akainuka na kumkumbatia Samson, kabla hajamkaribisha ambapo kwa pamoja walimjulia hali Mhasibu Jamaldin na kuongea naye mawili matatu. Baadae Samson alimgeukia yule kijana wa kizungu na kumwambia kwa lugha ya kiingereza, “Nashukuru sana kwa msaada wenu kaka! Mungu awabariki sana.
“Usijali! Kazi zetu wote hizi. Usisahau pia kuwa Tanzania imekuwa mshirika mzuri kwetu na imetusaidia mengi, tusingeweza kushindwa kutekeleza jukumu dogo kama hili!”
“Asante!”
“Asante, Kwa heri!” Mzungu akaaga na kuondoka.
“Kwa heri, tutaonana Mungu akipenda!” Samson akamjibu.
“Yule ni nani?” Mke wa Mhasibu akashindwa kuvumilia.
“Ni rafiki yangu, anafanya kazi shirika la Interpool”
“Interpol?!”
“Ndiyo!”
“Umemjuaje sasa?”
“Ni rafiki yangu, si umesikia kuwa kuna kazi nilikuwa nimemuomba anisaidie?”
“Kazi gani?”
“Ya kuwalinda ninyi!”
“Sijakuelewa Samson!”
“Utanielewa tu, kwanza mgonjwa anaendeleaje?”
“Anaendelea vizuri, ni muda mfupi tu nilikuwa nikiongea nae na akawa amesema nikuite! Nawe ukatokea kama malaika. Ulijuaje kuwa tuko hapa?”
“Ni hadithi ndefu!”
“Na Shuu umemuacha wapi? au umekuja nae?”
“Hapana!”
“Bado hujaniambia umejuaje?”
Kabla hajajibu swali hili, mara daktari mmoja akatokea na kuwaomba wampe nafasi mgonjwa anahitaji kupumzika hahitaji zogo, wakampa nafasi, akamkagua mgonjwa na kumpa dawa kisha akaondoka baada ya kuwatahadharisha kuwa dawa hiyo ilikuwa na nguvu na kama kutatokea lolote wasisite kumwita.
Daktari alipoondoka ndipo, Mke wa mhasibu alipomueleza Samson kwa kifupi kile kilichojiri na yale maagizo ya kufikisha taarifa zile kwa kaka yake. Samson alipotaka uhakika kwa mzee, tayari Jamaldin alikuwa amelala huku jasho jingi likimtoka, hali akionekana kukoroma kwa mbali.
Samson akakubaliana na mawazo ya Mhasibu, kwamba mke wa Mhasibu na Moses warudi Tanzania, na yeye atabakia kusubiri mzee aamke, azungumze naye masuala kadha wa kadha ikibidi wahame hospitali kwa kuwa pale hapakuwa salama sana.
Mke wa Mhasibu alipohoji sababu ndipo alipoelezwa kuwa, ndege iliyowasafirisha haikuwa chini ya Serikali kama walivyoongopewa, na ni jambo hilo lililomfanya aitaarifu Interpol juu ya ndege hii, na kwamba ilianza kufuatiliwa tangu ingali angani na ikawekwa chini ya ulinzi tangu mara tu ilipotua, na watu wake kufuatiliwa kwa karibu kwa kila hatua wanayochukua.
Kilichofanya watu wale wasikamatwe wala kuuawa ni kwa kuwa walimleta Mhasibu katika Hospitali ya kweli na wakampa matibabu ya kweli, chini ya madakatari halisi na bingwa wa hospitali hii. Hilo tu. Na alimhakikishia kuwa bado Polisi hao wa Interpool wanaendelea kuilinda hospital hii na hakuna jambo lolote baya linaloweza kumfika Mhasibu.
Nadia akachoka kabisa.
Kutoka hapo, Samson alimuuliza maswali haya na yale mpaka alipotosheka ambapo alimpigia jamaa yake mwingine Interpool ambaye alikuja na kuwachukua mke wa Mhasibu na Moses na kuwapeleka Uwanja wa ndege, ambapo waliondoka saa nyingi baadae kurudi Tanzania. Nadia akiapa kurudi Uingereza mara baada ya kulikamilisha jukumu alilopewa.
Ilikuwa ni baada ya akina Moses kuondoka, ndipo alipoingia jamaa mwingine wa kiafrika aliyekuwa amevaa mavazi ya kidaktari. Jamaa huyu alipomuona Samson tu akashtuka, Ingawa Samson alikuwa anasoma gazeti aliouona mshtuko wa mtu yule, akahisi labda pengine mshtuko ule unatokana na kubadilika kwa mlinzi kutoka Moses mpaka yeye.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Pamoja na hayo hakupuuza chochote akawa makini kuona kitu gani kitatokea, kama ni hatari aiepushe. Mtu yule akamsalimia Samson, akauliza hali ya mgonjwa na kuingia katika kile chumba cha madaktari, hakukaa sana akatoka.
Kutoka kwa mtu yule kulifuatiwa na Mhasibu kuanza kutetemeka na kukamaa kama mtu anayeelekea kushikwa na degedege, Samson akalitupa gazetile kando na kukimbilia chumbani kwa daktari, dakika chache baadae akatoka akiwa na daktari, wakamkokota Mhasibu na kumrudisha tena katika chumba cha wagonjwa mahututi. Ambapo huduma zilianza upya kwa kasi ya aina yake.
“Itakuwa zile dawa zimemzidi nguvu, itabidi tumpe dawa za kupunguza makali na tumsaidie kupumua kwa kutumia mashine yenye hewa ya oksijeni!” Daktari akamwambia Samson, Samson akakubali.
“Basi tunaomba utusubiri nje mara moja, ili tutimize majukumu yetu!”
“Endeleeni tu, mimi nipo hapa hapa. Mie ni mlinzi wake binafsi. Msihofu!”
“Mlinzi wake ni yule mwingine, sio wewe. Na yeye hakuwa mbishi kama wewe! Tunaomba utupishe tuokoe maisha ya mgonjwa tafadhali!”
“Lakini...”
“Au tumuache umtibu wewe?”
“No! No Sir. Sina maana hiyo!”
“Haya tupishe tafadhali!”
Samson akajikuta amekwama, kitu fulani kikimshawishi kutoamini kuwa kama hali ilikuwa shwari kama anavyoiona. Kule kupewa dawa kwa Mhasibu, kule kuzidiwa na hii huduma anayotaka kupewa ya kupewa dawa na kuwekwa katika mashine ya hewa, hakuona kama ni huduma ambazo yeye hakustahili kuzishuhudia.
Akahisi kuna hila inayotaka kufanyika. Jambo ambalo hakuwa tayari kuliruhusu.
“Sawa!” Akakubali kinyonge huku akiinua miguu yake tayari kutoka nje.
Ghafla kama umeme, bastola ndogo ya kisasa ikawa mkononi mwake ikiwa imefunguliwa usalama kabisa. “Haya!” Akabweka, sauti yake haikuwa ya kinyonge tena. Akamsogelea kitemi huku akimwambia,
“Utamtibu mgonjwa huyu kwa tiba anazostahili na mimi nikiwa humu humu ndani Shenzi taip!”
“Sa... Sa..... Saawa bwana Mkubwa!” Daktari akakubali akitetemeka kwa hofu.
“Na ole wako ufanye hila yoyote ndio utagundua Samson Kidude ni nani ndoroobo wewe!”
“Usiwe na hofu bwana mkubwa!” Alikuwa Daktari akimsogelea mgonjwa na kuanza kumtibu taratibu. Alikuwa hajafanya chochote pale Samson aliposikia mlango ukifunguliwa kwa fujo na wakaingia watu wawili waliovalia makoti ya kidaktari pia, kila mmoja akiwa na bastola mkononi.
Haraka Samson akawageukia na kuwanyooshea bastola watu hawa. Ikawa anatazamana na mitutu miwili ya bastola kwa wake mmoja. Bastola zile zilikuwa zimeondolewa usalama tayari.
Akiwa anapiga mahesabu ya kuwazidi kete watu hawa, akasikia chuma kingine cha baridi kikimgusa kisogoni. “Haya dondosha chini hilo kopo lako kabla sijalifunua hili bichwa lako bovu na bishi, kisha nimalizie kwa kumuua huyu nguchiro mwenzio!” Ilikuwa sauti ya yule daktari.
Samson hakuwa na jinsi, alihitaji nafasi zaidi ili kujiokoa, kumuokoa Mhasibu na kutoweka nae, maana alishajua mahali hapa si salama tena, ingawa Interpol walikuwa wamemuhakikishia kuwa kila kitu kilikuwa sawa. Akajikuta akiiachia bastola yake ikadondoka chini. Yule daktari wa nyuma yake akaipiga teke ikaenda na kugota miguuni mwa yule daktari wa mwanzo ambaye aliingia humo ndani kidogo na kutoka baada ya kumuona Samson na kushtuka.
Alipomuangalia yule wa pili, hakukumbuka kama alipata kumuona mahala. Kilichomshangaza ni kuona yule wa pili naye akimtumbulia macho kama anayemfananisha na mtu fulani. Hata hivyo hali hii haikuendelea sana, pale alipojikuta akipigwa na kitu kizito kisogoni, akaanguka chini na kupoteza fahamu!
“Shenzi taip!” Michael Bagula maarufu kama Tarish akasema na kuongeza “Ndiyo yeye huyu!”
“Nani?” Mwingine akauliza.
“Yule aliyetufukuza na gari baada ya kumgonga huyu mzee kule Dar es salaam!”
“Asee!” Yule daktari aliyempiga Samson naye akashangaa.
“Mie nilianza kupata mashaka nilipoyaangalia yale macho yake. Ujue ana macho makali sana. Macho yoyote ya jasusi aliyefundwa vyema huwa kama haya. Sasa tumfanyaje, tumuue?!”
“Kufa atakufa, watu mabwege kama huyu zawadi ya yao nzuri huwa ni jeneza. Ila kabla ya kumuua, nadhani tungependa kujua yeye ni nani, kwa nini alikuwa anatufukuza siku ile, imekuwaje amejua tuko Uingereza wakati tuliaga tunakwenda Ujerumani na imekuwaje ameibuka ghafla katika chumba hiki kama mzimu.
Baada ya hapo ndipo tutakapomuua. Najua bosi atapenda kuyasikia hayo. Lakini kwanza tukamue habari kutoka katika kifua cha huyu Mhasibu maluuni!”
“Tunamuhifadhi wapi?” Mwingine akasaili.
“Kipo chumba kimoja tu humu ndani ambacho hutumika kama Stoo ya kuhifadhia dawa, tunaweza kumuhifadhi humo wakati tukikamua habari zote zilizomo kichwani mwa huyu mpuuzi. Tukimaliza hapo tutaanza kushughulika na huyu jamaa!” Akasema akimsota Samsonn.
Kule kitandani Mhasibu alikuwa kukamaa pale kitandani huku akitoa miguno ya ajabu ajabu mithili ya mgonjwa aliyeshikwa na degedege. Udenda ulikuwa ukiendelea kumtoka hali mdomo ukianza kuelekea upande. Ile miguno ikafanya wote wamtazame.
“Imekuwaje tena?” Mwingine akauliza.
“Baada ya kupata fahamu, Mhasibu alikuwa ameanza kutoa siri, ndio nikampa zile dawa ili kumnyamanzisha!”
“Sasa?” Alikuwa Tarish tena “Anaweza kuzungumza tena?”
“Yap! Ataweza!”
“Sasa hivi?”
“Ndiyo, itachukua kama dakika tano sita hivi, ila haitazidi dakika kumi. Ntamdunga sindano kuondoa sumu ya ile dawa mwilini, kisha nitamdunga nyingine arejee katika hali yake na hapo tutaweza kuzungumza naye!”
“Basi fanya hivyo, Chap! Muda si rafiki yetu sana!”
Samson akachukuliwa na kukotewa kule stoo, halafu jitihada za kumpa Mhasibu uwezo wa kuongea zikaanza tena. Juhudi ambazo zilizaa matunda dakika kumi na tano baadae. Mhasibu alipopata fahamu tu akajikuta akitazamana ana kwa ana na Tarish Michael Bagula.
“Pole sana Jamaldin!” Tarish akadhihaki.
Mhasibu akabakia kimya bila kujibu chochote moyo ukimpiga na kumdunda vibaya sana kwa hofu pale kifuani kwake. Kukutana na mtu huyu tena katika mazingira kama haya baada ya yote yaliyotokea ilikuwa sawa na kukutana na iziraili mtoa roho za watu ili hali huna uwezo wa kumkimbia au kufanya lolote.
Hakujua hali imefikiaje hapo na hakujua Samson yuko wapi, hata hivyo moyoni alijiapia kupambana mpaka dakika ya mwisho, alijiandaa kufa kiume. Kitu kimoja tu alikuwa na uhakika nacho, kwamba watu hawa hawawezi kumuua mpaka amewaeleza alipozifichja pesa.
Hilo tu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hutaki kujibu sio?” Tarish akauliza tena.
Kimya
“Ulidhani utaendelea kutukimbia mpaka lini?” Tarish akaendelea kumkoromea Mhasibu. “Kitu kimoja tu umesahau Jamaldin, sie ni kama mbingu na ardhi. Huwezi kutukwepa, unaweza kujificha kwa muda, lakini huwezi kujificha muda wote na wakati wote! Umesikia?”
Kimya
“Hutaki kujibu. Ngoja nikuonyeshe ni kiasi gani sisi tuko mbele yako!” Alikuwa Tarish tena kwa mbwembwe akiinama chini ya kitanda cha Mhasibu na kutoka na kitu fulani cheusi chenye ukubwa sawa na kipande cha sabuni ya mche ya kufulia. Akakibonyeza hapa na kukifungua pale, kabla kifaa kile hakijaanza kutoa mbinja chache, zikifuatiwa na kauli chache za misuguano ya matairi, kabla kelele hizo hazijatulia na kufuatiwa na sauti hii.
...Pole Mahabuba, Pole laaziz! Pole sana barafu wa moyo wangu..! Hapo tena ulifuatia mlolongo wa mazungumzo yake na mkewe, mazungumzo yao na Samson na ile mipango ya kumsafirisha mkewe akatoe taarifa kwa kaka yake.
“Kaka yako unataka afuatilie nini?”
Kimya
“Naongea na wewe pumbavu!” Tarish akamchapa kofi zuri shavuni.
Mhasibu akagugmia kwa maumivu.
“Bado yuko katika dawa Tarish, angalia usiharibu tena!” Daktari akamuonya
“Argh! Anatia hasira sana huyu!”
“Eh! Lazima ujifunze kuzidhibiti hasira zako ndugu yangu. La sivyo yatatokea yale ya Dar es salaam. Na ujue yakitokea hapa hakuna atakayekuelewa!” Mwenzie mwingine akaonya pia. Likaondokea kuwa onyo bichi likamkumbusha kadhia nzima ya kule Dar es salaam na jinsi alivyofaulu kuuepuka msala ule kwa tundu la sindano. Akaona maswali ya kaka yake hayana maana, akamuuliza yale yanayomuhusu.
“Haya tuambie! Fedha umezificha wapi wewe?!”
“Zimeisha!”
“Unaona! Tarish akabweka, zimeisha wakati umetoka kumwambia mkeo kuwa umelazimika kuzihamisha?”
“Hizo zote zilikuwa ghilba, lakini ukweli ni kwamba fedha zimeisha!”
“Hata tukikuambia kuwa rafiki yako Matheo tumemuua kwa jeuri hii na sasa tunamshikilia Frank na wote wanakiri kuwa wewe ndiye unajua pesa zilipo, bado utaendelea kukataa?”
“Ukweli ni kwamba fedha zimeisha!”
Tarish alimminya mbavuni kwa muda kumtonesha hapa na pale huku akimtikisa kwa nguvu kumtaka ataje, pesa amezificha wapi. Ikawa kazi bure. Ingawa Mhasibu aliumia na kulia sana, akisikitika na kuomboleza, bado jibu lake lilikuwa moja tu. Kwamba fedha zimeisha. Na aliamua kuling’ang;ania jibu hili kwa kuwa alijua ni kama limeshika roho yake.
Naam! Kwa kanuni nyingi za majasusi, wakimaliza kuikamua siri iliyomo moyoni mwako, hatua inayofuata ni kukua. Hivyo ili aendelee kuwa hai, alikuwa hana budi kuitunza siri hiyo kwa gharama yoyote, ikibidi hata kwa gharama ya uhai wake.
“Sikiza Mbogo!” Tarish alimwambia yule kijana aliyekuwa akiendelea kumtonesha Mhasibu katika majeraha yake. “Muache!” Akaamrisha. Mbogo yule mlinzi aliyemuona Samson na kushtuka kabla, akaacha kumtesa Mhasibu na kusikiliza amri ya Tarish.
“Gillbert!” Tarish akaita “Ile sumu yako inayoua taratibu iko wapi?!”
“Hii hapa!” Gillbert, yule daktari mwingine akajibu.
“Iandae, muda wake wa kutumika umefika!”
Haraka Gilbert akaiandaa kwa kuichanganya na maji maalum kidogo na kuiweka katika sindano ilipokuwa tayari, Tarish akamuinamia Mhasibu kwa upendo na kumwambia taratibu
“Tumejaribu kuwa muungwana kwako kwa kipindi kirefu ila huonekani kufurahishwa na uungwana huu! Iliyopo mkononi ni sumu hatari inayoua taratibu ndani ya masaa ishirini na nne, arobaini na nane mpaka sabini na mbili. Sie tumeirekebisha na kuifanya iweze kuua ndani ya masaa arobaini na nane tu, yaani siku mbili. Dawa yake ni hii na ninayo mimi peke yangu, ukijisikia kuzungumza we zungumza, mi nitajua kama umezungumza na nitakuja kukuletea dawa mara moja. Je” akatua na kumuuliza tena “Bado tu hutaki kusema fedha ziko wapi?”
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ungekuwa wewe ndiyo Mhasibu ungejibu vipi?! Je, Mhasibu atatoa jibu gani? Je, Jibu hilo litakuwa na Faida au hasara kwake, Vipi Samson atafanikiwa kumuokoa Mhasibu, Vipi kuhusu akina Vick, Tarish na kundi lao lote?!
MWISHO
0 comments:
Post a Comment