Search This Blog

Saturday, 5 November 2022

SAYARI YA KIFO - 1

 






IMEANDIKWA NA : RAMAAH MZAHAM



*********************************************************************************



Simulizi : Sayari Ya Kifo

Sehemu Ya Kwanza (1)



Utangulizi



Mara nyingi sana katika maisha yetu wanadamu,

huwa tunapokuwa kwenye kilele cha mafanikio, basi hupatwa na mitihani

zaidi ya ile ya awali, wakati ambao tunakuwa hatuna mafanikio,

hivyo kama hatupo makini,

basi hujikuta tunapoteza kila kitu na hata watu wetu wa karibu.

Kwanini kunakuwa na ujumbe huu hapo juu?

Hilo ni fumbo ambalo linahitajika kufumbuliwa.

Kutana na Inspekta Kalindimya akifanya yake baada ya kufanikiwa

kutoka salama kwenye zengwe aliloundiwa, lililoitwa

‘Afande anahusika’ sasa anarudi akiwa ni mtu mwenye mke,

anapambana tena kwenye

'SAYARI YA KIFO'



Ilikua siku ya Alhamis jua likiwa linawaka kwa kutoa miale mikali sana iliofanya Jiji zima la Dar es Salaam kutawaliwa na joto, Inspekta kalindimya alikuwa anawasili kazini kwake muda ukiwa ni saa 5 na nusu za asubuhi.

Merina, binti wa kipogoro mwenyeji wa mkoa wa Morogoro alikuwa akishushwa kwenye gari ya Polisi huku akimwaga chozi, kitenge chake kikiwa hakikazi kiunoni, suruali aliyovaa ndio ilifanya hata kazi ya kitenge kile ionekane si muhimu.



Kwenye mlango wa kuingia ndani ya jingo la Polisi kanda maalum, ndio macho ya Inspekta Kalindimya yalipomuona binti huyo ambae alionekana ni mrembo lakini aliesawijika mno kutokana na kilio ambasiho kilijionesha kuwa ni cha muda mrefu.



Moja kwa moja alielekea kwenye dawati la maulizo na kupokea saluti za kijeshi na kusimama pembeni kukagua daftari la maelezo ya matatizo yaliyotokea usiku uliopita.

Akiwa anakagua daftari hilo, ndio akakutana na maelezo kuhusu binti huyo alieingia hapo ndani akiwa chini ya ulinzi na kilio kizito. Akasoma maelezo hayo na aliporidhika akafunika daftari hilo na kutokomea ofisini kwake kuendelea na majukumu yake mengine.

*****



Chidi, jambazi sugu ambae kihistoria amelisumbua sana jeshi la Polisi Tanzania kwa kufanya matukio makubwa makubwa kwenye sehemu tofauti za nchi adhimu ya Tanzania huku akiacha masikitiko na majonzi kwa familia nyingi kwa kufanya mauaji na kutokomea pasipojulikana.



Kutokana na muendelezo wa matukio yake anayofanya mara kwa mara na kuacha alama ya ‘V’ kwenye eneo alilofanya tukio ama mauaji aliyoyafanya, inawafanya jeshi la Polisi kujua tu muhusika ni nani pindi linapotokea tatizo.



Lakini inawawia vigumu mno kujua ni wapi alipo huyo muuaji, kwani kwa wakati mmoja alama hiyo ilionekana sehemu mbili tofauti zenye umbali mkubwa mno, mauaji yalitokea Amboni huko Tanga na Vikindu Jijini Dar kwa tofauti ya saa moja. Lakini alama iliyotumika ni hiyo hiyo moja tu.

Hapo sasa ndio jeshi la Polisi likaanza kubaini kuwa muuaji sio Chidi peke yake, bali kutakuwa na kundi kubwa ambalo huenda Chidi analiongoza, na ili kuukata mzizi wa fitna, ni heri huyo Chidi ndio apatikane.



Inspekta alikuwa yupo mbele ya makabrasha yake akitafuta moja ya majalada kwa ajili ya kuendelea na kesi zake, simu yake ya mezani ikaita, kwa kuwa alikuwa ofisini, wala hakushtuliwa na simu hiyo, bali aliipokea na kusalimia.



Ajabu aliepiga simu akaanza kucheka na kumwambia kuwa amembamba. Inspekta alimtambua fika mtu aliepiga simu hiyo, alikuwa ni mkewe kipenzi Bi Zuwena ambae ni takriban wapo nae kwenye ndoa kwa miezi isiopungua tisa sasa.



Upendo wao ulikuwa kwenye kilele, kama ni joto basi walipata maji baridi, hakuna ambae alikuwa yu tayari kuwa mbali na mwenzie kwa siku hata moja, achana tu na ule muda wa kazi ambao uliwatenganisha katika kutafuta mkate.



Zuwena alikuwa ni mwajiriwa kwenye kampuni moja inayojihusisha na uuzaji wa Vioo na bidhaa za Aluminium akiwa kama Sales Manager ambae alikutana na Kalindimya wakiwa kwenye kazi zao.

Wizi mkubwa uliosababisha upotevu wa mamilioni ya pesa kwenye kampuni miaka miwili iliopita, ndio uliopelekea kuzaliwa kwa penzi baina ya wawili hao mara tu upelelzi ulipokamilika mwaka mmoja na nusu uliopita na Inspekta akafanikiwa kuwatia nguvuni wahalifu.

Kupatikana kwa wahalifu hao ndio kuliko sababisha Zuwena kuwa huru tena na kurejeshwa kazini baada ya kugundulika kuwa hakuhusika kwa lolote bali ni njama iliokuwa imepangwa na mmoja wa wafanyakazi wenzie ambae alikuwa akivutiwa sana na nafasi ile ya kazi aliyokuwa nayo yeye.

Mahusiano hayo yalioanza kikazi, yakabadilika na kuwa ya kimapenzi yaliyodumu kwa takriban mwaka mmoja na nusu kisha yakabarikiwa kwa ndoa iliyofungwa nyumbani kwa kina Zuwena huko Kondoa kwenye kijiji cha Pahi miezi tisa iliopita.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Ofisi zote mbili, yaani ofisi ya Zuwena anapofanya kazi na hata wafanyakazi wa jeshi la Polisi Kanda maalum, walikuwa wakitambua fika ni kiasi gani watu wale wanapendana.



Siku hiyo baada ya Inspekta Kalindimya kutoka nyumbani, mkewe alikuwa amebaki tu akiendelea na shughuli zake hadi pale alipojisikia kutaka kuongea na mumewe ambae alikuwa amewasili kazini tayari.

Kwa kuwa kila siku alikuwa amezoea kumpigia simu kwa kutumia simu ya mkononi, lakini siku hiyo sasa akaamua kutumia hiyo simu ya mezani na kumfanyia Surprise.

Walitaniana na kucheka kwa furaha hadi walipoagana baada ya mlango wa ofisi ya Inspekta kugongwa na kisha kuingia askari wawili, mmoja wa kike na mwingine wa kiume wakiwa wamefuatana na binti Yule ambae alikuwa ameingia sambamba na Inspekta pale kituoni.





Binti huyo sasa alikuwa halii tena, bali alionesha kuwa na macho mekundu sana kuonesha kuwa ameisha lia kiasi cha kutosha, Inspekta akaweka mkonga wa simu mahala pake, akawatazama walioingia na kuwasikiliza kilicho waleta.

Inspekta Marsha ndio alikua mtu wa kwanza kuongea, akamjulisha bosi wake kuwa kuna tatizo wanahitaji msaada wake, Inspekta Kalindimya akaendelea kumtazama tu ishara ya kumsikiliza.



“Inspekta, huyu binti ana tatizo kubwa, mimi ndio ninahusika na kesi hii, lakini kuna tatizo lingine limejitokeza sasa hivi, nalazimika kuondoka, ila tu jambo moja ni kuwa, shida ya huyu inapaswa kusikilizwa sasa, kwani anasubiriwa, nahitaji msaada wako mkuu!”



“Unahitaji msaada gani Marsha?” alisema huku akivuta jalada lililokuwepo pale mezani na kuanza kulifunua, Marsha akamjibu;



“Naomba umfanyie mahojiano kutokana na jalada hilo ambalo unalo mikononi mwako Mkuu, anasubiriwa kwa ajili ya mazishi, habari zaidi zipo ndani ya jalada hilohilo mkuu,”



“We unaelekea wapi muda huu?”



“Inspekta nakwenda kwenye ile kazi uliyonipa jana, huenda leo nikaimaliza, kwani muda huu ndio muafaka wa jambo hilo,”



“Aaah ok! Kazi ile ya Waziri sio?” Inspekta alikumbuka na kutikisa kichwa huku akimtazama Marsha ambae alikubali kisha akatoka sambamba na yule askari mwingine.



Inspekta Kalindimya akafunua jalada sasa kwa marefu na mapana, awali akiwa amemkaribisha binti huyo kwenye kiti kilichokuwa mbele ya meza yake na kisha akaanza kulisoma jalada hilo ambalo alitakiwa apate maswali humo.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Baada ya kuliperuzi kwa dakika chache, akamtazama binti yule na kumuita kwa majina yake matatu



“Merina Angotwa Likweti…”



“Naam!” nae akaitika kifupi tu, kisha Inspekta akamwambia;



“Nimepitia kidogo kesi yako na nimegundua kuwa kuna mengi sana ya kukuhoji, hivyo basi kabla hata sijaanza maswali yangu lukuki, naomba unieleze mwenyewe mwanzo wa kisa hiki ambasiho kimesababisha wewe uwepo hapa,” alimueleza huku akimtazama usoni angali mikono yake yote ameifumbata pamoja kuanzia kwenye vitanga hadi kwenye fundo mbili za mikono.



“Labda sijaelewa vizuri afande, ina maana unataka nitoe maelezo upya kama niliyoyatoa hapo jana?”



“Nafikiri hapo utakuwa umenielewa, unaweza kuanza sasa, na ningependa uanzie siku ya Jumanne, sawa Merina?” alimuuliza huku akilifunga kabisa lile jalada.



Kwa akili zake za kiupelelezi, aliweza kugundua kuwa aliefanya nae mahojiano ya awali, kuna maswali muhimu mno aliyaruka, ambayo kama leo yatapata majibu, yataifanya kesi ile iwe ni nyepesi kwa Jeshi la Polisi.



Merina akajiweka vizuri na kuanza kueleza;



“Siku hiyo ya Jumanne ni siku ambayo sitoisahau katika maisha yangu, kwani kabla ya siku hiyo, yaani siku ya jumatatu, Allen alikua na maneno ya ajabu na ya vituko, kwa kweli nilishangaa sana, maana haikuwa kawaida yake. Kama vile mtu ambae ashajijua mwisho wake. Siku hiyo, Allen alikua na kawaida ya kuoga kwanza, mara tu anaporudi kutoka katika mishemishe zake, kabla ya kula chochote, lakini siku hiyo nilishangaa pale alipofika akiwa mbio mbio na kuniambia,



"Mke wangu niwekee chakula kwanza, nina njaa sana leo," Mimi nikamwambia



"Vipi huendi kuoga kwanza?" akanijbu



"Hata nikioga haita nisaidia chochote" nikishangaa mno, kuona kunahusiana nini na mambo ya msaada? Nilipomtazama vizuri nikagundua kuwa siku hiyo alionekana na furaha ya kupitiliza, maana alikua anacheka hadi sehemu ambayo si ya kuchekesha. Jambo hili lilinipa wasiwasi sana, nikamuuliza



"Hivi darling umelewa leo?" akanambia, hapana sijawahi kulewa wala sitakunywa pombe ya aina yoyote hadi siku yangu ya mwisho hapa Duniani.” Nikahisi huyu leo hayupo sawa, ili kumuweka sawa, nikampikia kahawa ili kichwa chake kitulie. Lakini aliendelea na vituko vyake.



Usiku ule wa Jumanne, hatukulala maana alikua kila mara anaongea mambo ya ajabu, mara aniulize maswali ambayo yalikosa majawabu, hakika alinishangaza mno hasa pale aliponiulizia kuhusu mtoto wetu ambae anatarajia kuanza darasa la kwanza mwanzoni mwa mwaka ujao, akaniuliza



"Hivi Mariana yuko darasa la ngapi kwani?" nikamwambia mtoto wake mwenyewe na wewe ndie unamlipia ada, ndio umesahau? Akaniambia



"Ah! Nimekumbuka mke wangu, kumbe yuko Nursery! Anatakiwa asome hadi mwenyewe aseme basi," nilipigwa na butwaa tu, maana nilikuwa simuelewi.

Basi ilipofika asubuhi hiyo siku ya jumatano, kama saa mbili hivi, mume wangu Allen akapigiwa simu na jamaa yake aitwae Kelvin, huyu ni jamaa ambae alikuwa nae mtaani hapo awali, sasa amfanya kuwa ni meneja kwenye maduka yake akamwambia anaomba tuonane, maana kuna tatizo limetokea, katika duka analouza Geofrey, Allen akamuuliza ni tatizo gani?



Kelvin akamwambia kwamba yeye hamuelewi Geofrey na jana tulitaka kupigana,

Allen akamwambia basi yeye ndio aje huku nyumbani, kwani siku hiyo alikuwa na safari ambayo alisema itakuwa ni safari ya kutoka kimaisha.” Alitulia kidogo Merina na kisha akaendelea kuongea





“Na kweli siku hiyo asubuhi ile ilikuwa ameisha jitayarisha kwa ajili ya safari, safari ambayo nami nilikuwa nina imani kuwa akirudi huko aina yetu ya maisha itabadilika, kwani aliahidi kumfungulia mtoto akaunti maalum na kumuwekea pesa ya kusoma hadi chuo kikuu hata kama ni nje ya nchi, pia abadili na kuongeza gari kuacha zile ambazo tulikuwa tukitumia.



Alipanga aondoke na Lexus, kwani pa tulikuwa na Pick Up ambayo alikua anatumia Kelvin, nami gari yangu ni GX 110, ndio gari ambazo tunazo hizo tatu.



Basi Kelvin akamwambia haitawezekana kwa yeye kuja huko, isipokua wakapanga kuwa kwa kuwa Allen anaenda Tanga, basi apitie njia ya Bagamoyo na hapo watakutana ili waongee kisha akakata simu na kumuacha mume wangu akitikisa kichwa.



Kisha akanikiss na kuondoka, Wallah sikujua kama hilo ni kiss la mwisho toka kwa mume wangu kipenzi Allen…” kilio kikafuatia na kutulizwa na Inspekta ambae alimpa pole.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Kwanini unasema hilo lilikuwa ni Kiss la mwisho kwako?”



“Afande, Allen hakurudi tena ile siku aliyotoka hadi jana alipopatikana akiwa amefariki,” kilio kikaongezeka zaidi na kufanya Inspekta sasa asimame na kuja jirani na alipoketi Merina na kumpoza huku akimwambia asiwe na shaka, jambo hilo limeisha tokea na watamfuta machozi kwa kumtia nguvuni muuaji.



“Bado tunahitaji sana msaada wako Merina, hakika bila wewe sidhani kama tunaweza kumtia hatiani muuaji, hivyo naomba usituchoke, najua kabisa kuwa unachoshwa na maswali yetu, lakini majibu yako ndio mwanga kwetu wa kututoa nje, sawa Merina?” alimuuliza kiupole tu.



“Sawa afande, mi nipo tayari wakati wowote, mumkamate nasie tumuue tu huyo mshenzi,” masikini bila kujua kuwa mtuhumiwa hahukumiwi na raia bali hupelekwa mbele ya sheria.



Inspekta huku akitembea kutoka pale na kurejea kwenye kiti alichoketi, akamuuliza Merina kama anajua ni wapi anaishi Kelvin. Merina alimwambia anajua ni wapi anapoishi na akamuelekeza.



Inspekta akamuuliza utaratibu ulivyo kuhusu mazishi? Merina akamwambia kuwa maiti wanasubiri watakapopewa na Polisi kwani wao hawajaiona. Inspekta akanyanyua simu na kuongea na mtu Fulani kisha akaweka simu chini na kutoka akiwa ameongozana na Merina kuelekea nje.



Kufika Kaunta, akamwambia askari mmoja amuite afande Jitu ambae ni afisa wa chini yake kwenye kitengo cha upelelezi, alipofika pale akampa jukumu la kufuatilia maiti ya Allen na kama utaratibu umekamilika basi wapewe maiti yao kwa ajili ya hatua zingine.



Yeye akarudi ndani na kuketi, miguu ikiwa mezani, anapiga mluzi tu anaona kama hana cha kufanya vile, mikono kaiweka kwa nyuma ya kichwa, amejiweka kizembe kabisa.



Mawazo yake yakarudi kwa mkewe ambae alikuwa akiongea nae kabla ya kufanya mahojiano na Merina, akachukua simu ya mkononi akiwa na tabasamu usoni pasina kujua hilo tabasamu limetoka wapi, akampigia mkewe na kuongea nae kwa furaha, furaha ambayo aliamini inatoka ndani ya moyo kabisa.

*****



Askari maalum kutoka kanda maalum ya Kipolisi Jijini Dar es Salaam, walifika maeneo ya Ubungo Kibo, eneo ambalo anaishi Kelvin na familia yake kwa ajili ya kumtia nguvuni mtuhumiwa wa kwanza wa mauaji ya mfanyabiashara mchanga, Allen.



Waliwasili na kuiweka nyumba nzima chini ya ulinzi wakiamini kuwa watamkuta Kelvin, kwani waliiona gari anayoitumia, gari ambayo tayari walikuwa wamejulishwa kwamba ni mali ya Marehemu Allen ikiwa imepaki nje ya nyumba hiyo, ishara kuwa alikuwa yupo ndani.



Baada ya kufuata sheria za Jamhuri yetu kama inavyo stahili kwa mshukiwa yeyote, hatua zikaanza kuchukuliwa ikiwepo kumuulizia Kelvin ambapo familia yake ilijibu kuwa Kelvin hayupo, kwani hajarudi tangu alivyotoka siku iliopita hajarejea hadi muda ule.



Mkewe akazidi kuwachanganya kabisa pale aliposema kuwa hiyo sio kawaida yake Kelvin kuchelewa kurejea kiasi hicho tena bila taarifa. Afande Jitu akamuuliza kwani wakati akitoka alimueleza anaelekea wapi.



Mkewe akamjibu kuwa alikuwa akiongea na bosi wake aitwae Allen na wakapanga wakutane sehemu,



“Hakukujulisha ni sehemu gani ambayo anaelekea?”



“Kwa kweli hakunieleza na wala mimi pia sikumuuliza,”



“Ok! Ikawaje baada ya hapo?”



“Sasa kwa kuwa muda ulikuwa ni mchache kwani bosi wake alikuwa na safari, ikamlazimu achukue pikipiki yake ambayo huwa hapendi kuitumia na kuondoka nayo.” Alijibu kwa kujiamini mkewe.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Hapo sasa Inspekta Jitu akawa ametambua kwanini gari ipo nyumbani muda ule, wakatazamana na wenzie kisha Jitu akauliza tena



“Unaweza kujua namba za pikipiki ya mumeo?” swali ambalo hata askari waliokuwa nae wakaliona lina mashiko, mke wa Kelvin akasema ndio na kuzitaja palepale alipo na Jitu akaziandika, kisha akamwambia kuwa wakati wowote ambao Kelvin atarejea, basi amwambie afike kituo kikuu cha Polisi kwa ufafanuzi wa kutafutwa kwake, wakaingia magarini na kuondoka.

*****





Zuwena alikuwa jikoni akipika chakula ambacho aliamini mumewe hukipenda, alikuwa amevaa kanga tupu kwa kujifunga lubega, ndani ya nyumba ambayo anaishi yeye na mumewe tu ambae kwa muda huo alikuwa hayupo, hivyo ndani ya nyumba nzima alikuwa yupo peke yake.



Alikuwa huru sana kujiachia, na ndio alichokifanya. Huku akiimba kila aina ya nyimbo za taratibu kwa furaha, mumewe aliwasili na kuingia moja kwa moja hadi jikoni huku akitembea kwa kunyata.



Alifanikiwa kuingia hadi jikoni na kumkuta mkewe akiwa amesimama anakanda unga, headphone masikioni, sauti laini ikiimba RnB, akaegamia mlango na kuachia tabasamu, mikono akiwa ameiweka kifuani na kulisanifu vizuri umbo la mkewe ambae hakujua katu kama kuna mtu anamtazama.



Alisimama kwa sekunde kadhaa na kugeuka, alipanga aende chumbani kwao kubadili mavazi. Lakini akiwa anakaribia kugusa mlango, simu yake ikaita.



Namba ya mpigaji ilionesha kuwa ni Jitu, akapokea na kumwambia juu ya kile kilichojiri huko walipokuwa, Inspekta akamwambia mwanzo huo si mbaya, lakini kwa sasa wanatakiwa kujua ni wapi alipo Kelvin.



“Iwapo tutampata Kelvin, ina maana ndio tunaweza kuupata mwanga na kujua ni wapi pa kuanzia, sasa mmejiapangaje?” aliuliza Inspekta Kalindimya.



“Nafikiria tu kurudi tena nyumbani kwa marehemu kwa ajili ya kutaka kujua ratiba zao za mazishi na utaratibu mwingine, nahisi huko naweza kupata hata moja ambalo litatusaidia, ama unasemaje mkuu?”



“Ni sawa, lakini mimi naona ngoja nikusaidie kitu kimoja, mimi acha nitoke sasa hivi niende nyumbani kwa marehemu, sawa? Nawe nakushauri nenda ile sehemu iliotokea mauaji kwa ajili ya kufuatilia tu iwapo kama kuna pikipiki ilionekana maeneo hayo na ama kuna chochote ambacho kilikuwa na utofauti, sidhani kama tupo pamoja?”



“Vizuri sana mkuu, nimekuelewa sana, sasa nami naona huo ushauri wako ni bora zaidi, basi mkuu tutawasiliana baadae,” wakamaliza maongezi yao.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Inspekta hakubadili tena mavazi yake, bali alitoka na kwenda kumchungulia mkewe ambae muda huo sasa alikuwa akijitikisa kabisa kutokana na kupandwa na mzuka wa muziki.



Inspekta akafikiri ni nini anafanye bila kumshitua Mpenzi wake, akatoa notebook toka kwenye koti la suti alilovaa na kalamu, akarudi nyuma taratibu na kuchomoa kalamu, kisha akaandika ujumbe mmoja na kurejea pale usawa wa mlango na kuiweka karatasi ile kwa kuikandamiza na kalamu.



Aliiweka chini kabisa kwenye Tiles na kurudi nyuma taratibu bila kelele na kutoka nje kwa kupitia mlango wa mbele ambao aliingilia hapo awali na kuufunga kama alivyoukuta mwanzo, akaelekea garini na kutokomea huko alipopanga mwenyewe.

*****





ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog