Search This Blog

Saturday, 5 November 2022

JOANA ANAONA KITU USIKU - 3

 








Simulizi : Joana Anaona Kitu Usiku

Sehemu Ya Tatu (3)





Alipata hofu na maswali kwa pamoja. Alijiuliza aliyekuwepo mlangoni ni nani, Moa? Ama mtu mwingine? Kama ni Moa ina maana amerudi tena muda na wakati kama wa jana? Haogopi ukizingatia kile kilichotukia?



Kama si Moa, ni nani mwingine? Je ni salama kwenda kumfungulia majira hayo?



Alinyanyuka akaenda mpaka mlangoni, alijuta kwanini alikuwa wa mwisho kulala kwani asingekutana na adha kama hiyo. Alimtazama Lisa akamuona anakoroma usingizini, akamtamani.



Alipiga moyo konde, akauuliza mlango:



“Nani?”



“Ni mlinzi,” sauti ikasema toka nje.



Kidogo Joana akatua hofu. Sasa akafungua mlango lakini kwa tahadhari. Alichungulia nje akamuona mlinzi: mwanaume mrefu, mwili wa kujaa, nywele fupi nyeusi, amevalia sare, mkononi akibebelea fimbo nyeusi iliyotengenezwa kiustadi.



Kiunoni alikuwa amening’iniza pingu. Sura yake ilikuwa makini, mikono yake ameiweka nyuma ya mgongo.



“Tafadhali hakikisheni milango imefungwa, hakuna mtu yeyote anayetembea nje ya bweni wala kumuingiza mgeni yeyote wakati huu wa usiku” alisema mlinzi. Joana akatikisa kichwa kuupokea ujumbe.



“Samahani kwa usumbufu.” Mlinzi akasema kisha akaenda zake.



Alikuwa anapitia vyumba alivyokuwa anasikia sauti, ama kuona kuna mwanga kumaanisha watu bado wapo macho.



Joana alimtazama mlinzi huyo kwa muda kabla hajaingia ndani na kuufunga mlango.



Hakujua kwanini hana usingizi. Alijitahidi kujilaza lakini hakupata chochote. Baadae baadae kwenye majira ya saa tisa, akiwa kitandani anajigeuzia huku na huko, akasikia hodi tena mlangoni!



Akakurupuka kutazama.



Mlinzi amerejea? Alidhani pengine ni mawenge yake ya kuukosa usingizi basi akangoja kwanza. Punde, hodi ikajirudia. Kumbe alikuwa sahihi, alisikia hodi.



Akataka kupuuzia, ila akajiuliza:



“Hawezi akawa Moa?”



Akanyanyuka na kuusogelea mlango karibu.



“Lakini Moa aje afanye nini muda huu? Ama mlinzi?”



Alihofu.



“Nani?” akauliza kwa sauti ya chini.



“Moa!” sauti ikajibu toka nje. Akastaajabu. Kwa kuhofia Moa asije akaonekana na mlinzi ambaye alikatiza kutoa taarifa muda si mrefu, uoesi akaufungua mlango na kumruhusu aingie ndani.



“Moa, kwanini unakuja wakati huu na unajua kabisa ni hatari?” Joana aliwaka. Moa akatabasamu akiketi kitandani.



“Mbona una hofu hivyo?”



“Mbona nina hofu!” Joana akatahamaki. “We unaona ni sawa hiki unachofanya?”



“Acha hofu, mpenzi. Najua ninachofanya.”



“Kuua walinzi?” Joana akaropoka. Mara akashika mdomo wake na kumshika Moa mkono.



“Nisamehe, haikuwa dhamira yangu. Nimekwazika sana.”



“Usijali,” Moa akasema akimtazama machoni.



“Lakini Moa kwanini unakuja muda huu?”



“Labda ndiyo muda ninaohitaji kukuona zaidi,” Moa akajibu akipapasa uso wa Joana.



“Ukikamatwa na walinzi utasemaje?” Joana akauliza. Asingoje majibu, akauliza tena:



“… Moa, unahusika na kifo cha mlinzi?”



Moa akashusha pumzi ndefu.



“Sihusiki,” akajibu.



“Moa, ni wewe ndiye uliyekuwa umevaa shati la njano jana, na ulitoka huku kwangu usiku mzito, Ni nani kama si wewe?”



“Joana, ilibidi nifanye hivyo la sivyo ingekuwa kesi kubwa,” Moa akajitetea.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Kesi kubwa kuliko ya mauaji?”



Moa akanyamaza.



“Moa, umekuwa muuaji?”



Hawakuketi na shwari, walijibizana hapa na pale kabla Moa hajataka kwenda.



Joana alikumbuka jambo, akamuuliza Moa:



“Unaishi wapi?”



“Kwani hujui ninaishi wapi?”



“Nilikuja na haukuwepo. Moa una nini lakini wewe?”



“Nakushangaa wewe!”



“Ebu, naomba uende!” Joana akasema akinyooshea mkono wake mlangoni. Alikuwa ameghafirika, uso na macho yake vilikuwa vyekundu.



Moa akaondoka.



Joana akashusha pumzi ndefu na kujirejesha kitandani. Mawazo yalikuwa yameongezeka zaidi hivyo akakosa kabisa usingizi akiwaza.



Kwanza aliwaza kama Moa atafanikiwa kutoka salama ndani ya eneo la bweni pasipo kukamatwa. Pili alikuwa anawaza namna Moa alivyobadilika. Alihisi si mzima.



Lakini hakujua wakati anazozana na Moa, Lisa alikuwa anawasikia. Alifungua macho yake kuwatazama kabla hajayafumba na kupoteza ushahidi kama aliamka.



Dakika kama ishirini mbele, Joana bado akiwa hana usingizi, anasikia tena hodi mlangoni. Hodi ilipigwa kwanguvu kiasi cha kumshtua Lisa aliyekuwa usingizini.



Ilipigwa mara tatu alafu ikakoma.



“Joana, nani huyo?” Lisa akauliza kwa sauti yenye kilevi cha usingizi. Joana akajibu kwa kupandisha mabega juu.



Akasimama na kuusogelea mlango.



“Nani?”



“Mlinzi!”



Moyo wa Joana ukapiga fundo! Alafu ukaanza kukimbia haraka.



Moa amekamatwa? Wamegundua nilikuwa na mgeni? Maswali yakapita upesi kichwani mwake. Akajikuta anahofia kufungua mlango.



Hodi ikabishwa tena kwanguvu. Joana akafungua mlango kwa mkono unaotetemeka. Akakutana na mlinzi, yule aliyekuwa anakatiza kuwapasha habari.



“Ulikuwa na mgeni?” lilikuwa swali la kwanza mlinzi kuliuliza.



Joana akatikisa kichwa pasipo kusema kitu, alikuwa ameificha mikono yake kwa kujikumbatia asionekane anavyotetemeka.



“Una uhakika?” mlinzi akauliza akimtazama Joana machoni. Joana akakwepesha macho.



“Ndio, nina uhakika,” alisema huku moyo wake ukivuma. Alihofia pengine mlinzi anaweza akasikia namna moyo wake unavyokita. Basi akaweka kiganja chake kifuani.



“Unaona hii,” Mlinzi akamuonyeshea chini, kulikuwa kuna nyayo za viatu.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Hivi ni viatu vya kiume, madam na inaonyesha zimetokea hapa kama si kuja hapa. Unavitambua?”



“Hapana.” Joana akatikisa kichwa.



“Naweza nikaingia ndani?” Mlinzi aliuliza, Joana akatazama ndani upesi alafu akarudisha uso wake nje.



“Ndio, unaweza.”



Mlinzi akazama ndani na kutazama chini. Bahati kulikuwa kuna zulia gumu rangi ya kijani, halikuonyesha jambo.



Mlinzi akatoka zake nje.



“Nakutakia usiku mwema,” alisema kisha akaondoka. Sura yake ilikuwa inatosha kueleza namna alivyokuwa na mashaka. Joana mwenyewe alilijua hilo, mlinzi alimtilia shaka.



Aliufunga mlango akarudi kitandani.



Hakulala sasa mpaka jua linachomoza. Asubuhi ndiyo akapata usingizi, ambao ulikuja kukatishwa na hodi.



Alikuwa ni inspekta Westgate ndani ya suti yake rangi ya udongo na briefcase nyeusi mkono wake wa kulia.



“Karibu,” Joana alimkarimu inspekta kwa mshangao. Alijawa na hofu sana, moyo wake ulianza kukimbia kwa kasi. Alijikuta anaanza kutetemeka viungo kwa kuhofia mkono wa dola.



“Bila shaka wewe ni Joana …”



Joana akasita kwanza kabla hajapandisha kichwa chake juu taratibu, akajibu kwa sauti ya chini:



“Ndio.”



Inspekta akajitambulisha na kuonyesha kitambulisho chake, kisha akasafisha koo lake na kumtazama Joana machoni.



“Joana, unaongeleaje mauaji yanayotukia hapa chuoni?”



Joana akameza kwanza mate.



“Yanatisha … yanatisha kwakweli,” akajibu, kwa sauti yake ya chini ileile.



Inspekta akafungua briefcase yake na kutoa picha kadhaa. Zilikuwa ni picha za watu wote waliouawa hapo chuoni, kumi na kitu. Akaishika picha ya kwanza ya mwanamke yule marehemu, mnaijeria, akamwonyesha Joana.



“Unamjua huyu?”



Joana akatikisa kichwa kuafiki.



“Anaitwa nani?”



“Anaitwa Judith.”



“Alikuwa anaishi wapi?”



“Alikuwa jirani yangu, chumba kinachofuata.”



“Unadhani aliuawa na nani?”



“Sijui!”



Inspekta alifanya hivyo kwa picha zote akizionyesha na kumuuliza maswali Joana juu ya ufahamu wake kwa marehemu, na kisha nani aliyemuua. Majibu yake yakawa sijui … sijui.



Lakini Inspekta alipofikia kwenye picha ya mwisho, ya marehemu wa mwisho kabisa kuuawa, mlinzi aitwaye bwana Rodney Windows, Joana akasita kutoa jibu kwa wepesi.



Inspekta akamkazia macho na kurudia swali:



“Unadhani nani aliyemuua?”



“Sijui,” akajibu akitikisa kichwa.



“Unadhani muuaji ni jinsia gani?”



“Ya kiume.”



“Umejuaje?”



“Nimebuni tu,” Joana akajibu akipandisha mabega juu.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Joana,” inspekta akaita. “Muuaji alikuwa amevaa shati la njano kwa mujibu wa kamera, na alielekea upande huu wa kipande cha bweni lenu, unadhani alielekea wapi?”

Joana akatikisa kichwa.



“Sijui.”



Mpaka hapo alikuwa anahisi haja zote zinambana. Alihisi baridi vidoleni na kichwa kikimgonga mno. Kila sekunde iliyokuwa inaenda mbele, kwake ilikuwa ngumu zaidi ya nyuma.



“Haukusikia chochote, aidha vishindo vya miguu?”



“Sikusikia, nilikuwa nimelala.”



“Ulizima taa?”



Joana akababaika kidogo. Akawaza, akaona akisema taa ilikuwa inawaka, basi ataulizwa na itabatilisha hoja yake kwamba alikuwa amelala. Na hivyo kama hakuwa amelala basi lazima atakuwa amesikia vishindo vya miguu.



Basi akasema:



“Nilikuwa nimezima, ndio.”



“Kwa mujibu wa kamera za nje, haukuwa umezima taa.”



“Sidhani, pengine mmechanganya vyumba.”



Inspekta akatoa picha fulani hafifu toka kwenye briefcase. Akampatia Joana. Ilikuwa ni picha iliyochukuliwa toka kwenye kamera za cctv zikionyesha muda kwa chini.



Kwa mujibu wa muda huo, ilikuwa ni saa nane na nusu usiku.



“Hicho si chumba chako?”



“Labda mwenzangu aliamka usiku, siwezi jua!”



Inspekta akanyaka picha yake na kurejesha ndani ya briefcase. Hakuuliza kuhusu chumba, akafunga mkoba wake na kumtazama Joana.



“Ulikuwa na mgeni yoyote usiku mzito wa kuamkia leo?”



“Hapana, sikuwa na mgeni.”



“Ila ulikuwa macho na taa ilikuwa inawaka.”



Joana akasita. Akahofia kudanganya.



“Ndio, taa ilikuwa inawaka.”



“Na ulikuwa macho.”



“Yah … n’likuwa macho.”



“Mlinzi aliona alama za viatu katika korido yenu, na mtu aliyekuwa na viatu hivyo alikatiza wakati wa usiku, muda si mrefu sana baada ya mlinzi kukatiza kuwaonya na kuwakataza juu ya ugeni. Mtu huyo hakuja kwako?”



“Hapana, hakuja kwangu.”



“Alielekea wapi?”



“Sijui.”



“Ulimsikia anaenda wapi?”



“Sikumsikia.”



“Na ulikuwa macho!”



“Ndio. Labda kwasababu nilikuwa natazama tamthilia.”



“Nyayo za mtu huyo zilikuwa zinaonekana vema, kumaanisha hakuwa ananyata bali anatembea kawaida. Una uhakika hukusikia kitu?”



Joana alihisi joto kali. Aliona kama vile inspekta amemuweka kwenye uwanja kisha akaketi kumtazama namna anavyohangaika huku na kule. Alitamani ayeyuke. Aliona kama anakabwa.



“Sikusikia kitu.”



Inspekta akashusha pumzi ndefu. Akanyakua mkoba wake na kuukumbatia.



“Mtuhumiwa wa kwanza wa mauaji ya mlinzi, ni mwanaume mwenye viatu vyenye alama hizo kwani alama hizo hizo za viatu ndizo zimebainika kwenye eneo la tukio la mauaji ya mlinzi.”



Inspekta akaweka kituo. Akamkazia macho Joana, Joana akatazama chini.



“Naweza nikaona mguu wako?”



Joana akatahamaki. Mguu wangu wa nini? Akajiuliza kifuani. Ina maana anaufananisha na wa muuaji wa mlinzi? Akaendelea kujiuliza akiunyanyua mguu wake na kumkabidhi inspekta.



Inspekta akafungua mkoba wake, akatoa kipima urefu, akaupima mguu wa Joana, urefu na upana kisha akarudisha kifaa chake ndani.



“Ahsante sana,” Inspekta akasema akinyanyuka. “Naweza nikakutembelea kama nikiona kuna hitaji hilo,” inspekta akaaga kwa hayo maneno, akaenda zake akimwacha Joana hali si muhali.



Joana alishusha pumzi ndefu akajilaza kitandani. Akaamka upesi na kwenda kwanza kupata maji kupooza kifua. Alikunywa glasi mbili kabla hajarejea kitandani na kujilaza tena.



Alishangaa ilikuwaje inspekta akamuacha huru. Alijikuta anapata mawazo mengi sana kichwani ambayo yalizidi kumuumiza kichwa.



Aliona kuna haja ya kuonana na Moa, tena upesi kumpasha habari. Hata hakungoja avae wala kuoga, akaenda zake kama alivyokuwa amelala na kuamka.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Alimtafuta sana Moa, tafuta na tafuta pasipo mafanikio yoyote yale. Alizunguka chuo kizima, kwa gari na miguu, lakini hola! Hakuona wala kumsikia Moa.



Alichoka akarudi ndani.



“Moa, ana matatizo gani? Yupo wapi?”



Siku nzima hakuwa na amani wala raha. Hakula wala kunywa. Alijaribu kumpigia Moa lakini hakupatikana. Alihisi kuchanganyikiwa. Hata Lisa aliporejea hakutaka kuongea naye.



Usiku usingizi haukuja, aliwaza, je atoroke? Ajiue? Au afanye nini?



Usiku ukazidi kusonga na kusonga. Kwenye majira ya saa nane, mlango ukagongwa. Akashtuka na kutazama.



Alimtazama Lisa akamuona amelala hajitambui. Akautazama mlango akijiuliza maswali kifuani. Ni nani huyo? Moa?



Akaamua kunyamaza. Hakutaka kuitikia hodi hiyo.



"Kama ni Moa nilishamwambia asije tena muda huu!"



Hodi ikaendelea kugonga pasipo kukoma, mwishowe Lisa akaamka.



"Joana, nani huyo muda huu?" Akauliza kwa sauti yenye ulevi wa usingizi.



"Sijui!" Joana akajibu, bado alikuwa anatazama mlangoni.



"Umeuliza lakini?"



"Sijataka hata kuuliza."



"Sasa atapiga hodi mpaka lini?"



Joana kimya. Lisa akapaza sauti yake:



"Nanii?"



"Moa!" Sauti ikajibu huko nje.



"Ni Moa!" Lisa akatahamaki akimtazama Joana. Joana alikuwa ametulia kana kwamba hajasikia.



"Kamfungulie, la sivyo atakamatwa hapo nje na wewe utakuwa matatani!" Akasihi Lisa. Basi Joana akanyanyuka na kwenda mlangoni.



Akafungua mlango, Moa akazama ndani upesi.



"Unataka nini muda huu?" Lilikuwa swali la kwanza la Joana.



Hakutaka kabisa kumuelewa Moa pasipo kujali namna gani alivyokuwa anajitetea. Alikuwa ameghafirika na kumchoka Moa kwa matendo yake yasiyoeleweka.



"Unaishi wapi? - kwanini unanijia saa nane za usiku?" Yalikuwa maswali ambayo Moa alishindwa kuyajibu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Pasipo kujali ilikuwa ni majira ya usiku, Joana alijikuta anapaza sauti kufoka na kufoka. Lisa akajaribu kumtuliza pasipo mafanikio.



"Moa, nimechoka. Na tafadhali naomba kila mtu aende na njia yake!"



Kabla Moa hajasema jambo wakasikia hodi mlangoni.



"Mlinzi hapa, kuna shida gani humo ndani?" Ilikuwa sauti ya kike.



Joana na wenzake wakatahamaki. Moa akikutwa humo ndani itakuwa kazi si kidogo, haraka wakashauriana wamfiche ndani ya kabati.



Wakafanya hivyo kisha mlango ukafunguliwa.



"Kuna nini humo ndani?"



"Samahani, tulikwaruzana kidogo," akajibu Joana akijitahidi kutabasamu.

Mlinzi akatazama ndani, akamuona Lisa akiwa ameketi kitandani.



"Kama vile nilisikia sauti ya kiume."



"Hapana! Itakuwa umesikia vibaya tu."



Mlinzi akaingia ndani kuhakikisha. Kwakuwa alikuwa mwanamke basi hakuwa na pingamizi kuwandawanda chumbani humo.



Aliangaza asione lolote la kutilia mashaka.



"Bweni zima lilikuwa limetawaliwa na kelele zenu, hamjui muda huu ni usiku sana?" Mlinzi aliwaka.



"Samahani, tunaahidi haitajirudia tena," akasema Joana.



Mlinzi akawatazama tena kabla hajaondoka zake.



Wakamtoa Moa kabatini.



"Sasa tunafanyaje Joana?" Akauliza Lisa.

"Huoni tukimtoa Moa sasa hivi atakamatwa huko nje?"



Joana hakujibu kitu. Akamtazama Moa na kumwambia:



"Toka chumbani kwangu, usirudi tena hapa!" Kisha akaufungua mlango na kusontea nje.



"Nakupenda, Joana. Na sitaacha ku ..."



"Nenda nje!" Joana hakutaka maelezo. Macho yake yalikuwa mekundu, na pua pia.



Moa akautazama mkufu wa Joana kifuani. Akatabasamu na kwenda zake.



"Ilimradi una huo mkufu kifuani, basi daima utakuwa nami," Moa alisema kifuani akiyoyoma.



Ingali walinzi walikuwa wametapakaa huko nje tangu mauaji yatokee, hakuna hata mmoja aliyemuona Moa.



Alikatiza kwa amani akielekea misituni. Alikwepa taa zote akienenda kwenye njia ya giza.



Kadiri alivyokuwa anazama ndani ya msitu akawa anabadilika umbo, sura na mwendo. Alikuwa anatisha asieleweke kama ni binadamu, kigagula ama kibwengo.



Hakuwa kiumbe chenye taswira ya Moa tena, bali mnyama ama jitu!



Kabla hajapotelea humo msituni, mjumbe mmoja wa ulinzi shirikishi alimuona, akapaza sauti:



"Hey! Unaenda wapi?"



Mlinzi huyo shirikishi alikuwa amebebelea kurunzi na bunduki kubwa.



Kile kiumbe kikamtazama. Mlinzi alipokimulika akastaajabu, hakukielewa! Kilikuwa ni kama kivuli kikubwa kilichoganda.



Ni macho tu ndiyo yalibakia wakati mwili mzima ukiwa mweusi ti na umbo la ujiuji.



La haula! Mlinzi akajikuta anaishiwa nguvu baada ya kuona kiumbe hicho chaja kwa kasi kumfuata.



Haraka alichukua filimbi iliyokuwa inaning'inia kifuani mwake, akapuliza kwanguvu akikimbia.



Hakupata hata wazo la kutumia silaha yake. Pengine aliona atachelewa ama basi haitasaidia lolote.



Alikimbia haraka mno, lakini kile kiumbe kikawa kinamkaribia kwa kasi mno hatua kwa hatua!



Ilikuwa bayana mlinzi asingefika kwenye makazi ya watu kabla hajatiwa nguvuni. Alishakaribiwa kiasi cha kutosha!



Akaanguka chini. Sasa mchezo kwake ukawa umekwisha. Alimtazama kiumbe kilichokuwa kinamkimbiza akahisi hofu kubwa ndani yake.



Haraka akateka bunduki yake na kuanza kufyatua kwa fujo. Hazikusaidia. Ajabu kile kiumbe kikaanza kummeza!



Si kwa mdomo la hasha bali kwa mwili. Kilikuwa kinamsogelea zaidi mlinzi, miguu ya mlinzi ikawa inapotelea ndani ya mwili wa kiumbe isijulikane wapi ilikuwa inaelekea.



Ni kana kwamba alikuwa anazama ndani ya maji!



Katika kuhangaika, mlinzi akateka kurunzi yake na kummulika kiumbe usoni. Kile kiumbe kikapagawa. Kikapiga kelele kali kikijitahidi kujikinga.



Hiyo ikawa salama ya mlinzi.



Alimmulika zaidi na zaidi akijitahidi kukwamua miguu yake toka kwenye tope la mwili wa kiumbe.



Akafanikiwa.



Kiumbe kikashindwa kustahimili zaidi mwanga wa kurunzi, haraka kikapotelea msituni kwa kasi! Punde walinzi wengine, watatu kwa idadi, wakatokea na kumkuta mwenzao akiwa chini.



Wakamuuliza nini kimemkumba, akawaelezea. Wakamnyanyua na kumpeleka mahali salama.



"Ulimuona ametokea wapi?"



"Hapana! Nilimuona tu akielekea msituni."



"Inawezekana akawa ndiye muuaji?"http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



"Sijui! Hakuwa hata na miguu, uso wala umbo la binadamu."



Taarifa zikafikishwa polisi, mapema ya saa kumi na moja polisi wakafika wakiongozwa na inspekta Westgate.



Wakapekua eneo zima la tukio.



"Inaweza ikawa ndiye muuaji," akasema inspekta. "Alama za viatu vilivyopatikana hapa ndivyo vilevile vilivyopatikana eneo la mauaji ya mlinzi."



Basi ikatolewa amri ya kusakwa pori zima. Polisi zaidi wakaongezeka wakiwa na kikosi cha mbwa.



Wakasaka pori lote, lilikuwa na ukubwa wa kilomita za mraba mia mbili hamsini. Walimaliza msako wakitumia muda wa masaa sita, hawakufanikiwa kupata mtu.



Ila wakakuta mifupa ya binaadamu. Waliikusanya mifupa hiyo kwa ajili ya upelelezi zaidi.



Mojawapo ya mifupa ilionyesha mhanga hakuwa ameuawa kwa muda mrefu. Bado mifupa yake ilikuwa na utelezi na mabaki ya damu.



Ila kabla ya polisi hao kuondoka, inspekta akamchukua Lisa, mkazi mwenza wa Joana. Alimwambia ana maswali kadhaa anayotaka kuyapata majibu toka kwake.



Lisa alikuwa peke yake chumbani wakati alipokuja kuchukuliwa. Ila alipotiwa ndani ya gari la polisi, Joana alijitokeza na kushuhudia tukio hilo.



Alipata mashaka sana. Hakuna yeyote anayejua siri yake na Moa zaidi ya Lisa. Je, ataenda kusema?



Alikosa amani kabisa na akajihisi tumbo limemvuruga. Ndani hakukukalika, akaamua kuketi nje alipojichanganya na wengine waliokuwa wamesimama kwenye vikundi vikundi wakiteta na kuongelea swala lile la mlinzi.



Kila mtu alikuwa anaongea lake, na yote Joana alitaka kuyasikia kwa wakati mmoja.



“Ni jini!” mwanafunzi mmoja alisikika akiropoka. Wenzake sita walikuwa wamesimama wakimsikiliza kwa umakini. “Anayemaliza watu ni jini na anaishi msituni. Anapitapita koridoni mwa bweni la wasichana kila nyakati za usiku!”



Maelezo hayo yakamfanya Joana ajisikia vibaya, moja kwa moja alimfikiria Moa. Ina maana Moa ni jini au? Inawezekanaje hili?



“Alibadilika mbele ya mlinzi na kuwa jitu la ajabu!” msimuliaji yule aliyezingirwa na wenzake aliendelea kunena. “Alipomulikwa usoni akakimbilia msituni, la sivyo alikuwa anamuua mlinzi mwingine! Unaambiwa alikuwa jitu kuuubwa jeusi lenye mikono kibao.”



Joana akaona inatosha sasa, akaondoka zake na kwenda mbali alipojitenga na watu. Alijikunja akiwaza kumhusu Moa. Kwa namna moja akili yake ikakiri kuna jambo halipo sawa na Moa.



Hakuwa Moa wa kawaida. Ila ndiyo tuseme amekuwa jini!



Aliutazama mkufu ambayo Moa amempatia, akahisi dunguli kubwa linamkaba koo. Machozi yalikuja upesi machoni, yakatiririka kama mto.



Alijitahidi kuyafuta, lakini hayakukoma. Aliona maisha yake yameharibika na furaha imepotea. Mtu pekee aliyekuwa anamtegemea, nawe amekengeuka. Kwa muda akajihisi mtupu na ulimwengu wote unamcheka.



Kutafuta ahueni, akampigia mama yake na kumweleza. Alihisi akimwambia mtu mambo yanayomsibu basi angalau atapata ahueni kwa kutoa jambo kifuani.



“Rudi nyumbani, mwanangu. Upesi kesho asubuhi uwepo nyumbani,” sauti ya mama iliita simuni. Alishikwa na uchungu kumsikia mwanae analia.



Kabla hata Joana hajaongea neno la ziada, mama akasema:



“Au nakuja huko. Ningoje!”



“Hamna mama, nitakuja!” Joana akawahi.



“Kweli Joana?”



“Ndio, mama. N’takuja,” Joana akasema kwa sauti tumbuizi kabla hajakata simu. Angalau akahisi kifua kinapitisha hewa.



Alirejea chumbani, na baada ya kama lisaa limoja Lisa naye akaingia. Alikuwa na uso mchovu wenye mchanganyiko na mawazo. Aliketi juu ya kitanda akajilaza kana kwamba mtu aliyechoka mno.



“Vipi Lisa?” Joana akamuuliza akimsogelea rafikiye karibu.



“Safi tu,” Lisa akajibu kifupi akichochea hamu ya Joana.



“Wamekuambiaje huko?”



Kabla Lisa hajajibu hilo swali, akavuta kwanza kamasi.



“Joana, hakuna siku nimeongopa kama leo. Nimefanya kwasababu tu wewe ni rafiki yangu, la sivyo nisingeliweza!”



Lisa akaeleza yale yote aliyoulizwa huko kituoni mwa polisi. Na namna alivyoongopa kwamba hamjui Moa na hajawahi kumsikia akija chumbani kwao wala kumtilia mashaka rafiki yake.



“Ahsante sana, Lisa. Sina cha kukulipa.”



“Usijali, Joana. Lakini upo hatarini sana, na inaelekea polisi wanangoja kitu kidogo sana ili wapate kukutia nguvuni.”



“Kitu kidogo?”



“Ndio, kitu kidogo sana. chunnga mienendo yako Joana. Sitaki kukupoteza.”



Joana akakosa cha kusema, alitazama chini akitekwa na mawazo.



“Naamini si wewe uliyeua. Nakuamini Joana. Nitakuwa wa mwisho kuamini kama wewe ni muuaji.”



“Ahsante sana, Lisa.”



“Lakini Moa ni muuaji. Kuwa naye makini sana,” Lisa akatoa nasaha kabla hajageukia kando na kupitiwa na usingizi. Joana alikosa hata cha kusema akabaki akiwa amefumba mdomo kwa kiganja.



Siku ikasonga mpaka majira ya saa nne usiku. Si Joana wala Lisa aliyekuwa ametia kitu tumboni. Japokuwa Joana alifuata chakula kantini, kilibakia tu kwenye vyombo.



“Kesho naondoka kurudi nyumbani,” Joana alivunja ukimya.



“Na vipi kuhusu masomo?” Lisa akauliza.



“Nimechoka, Lisa, sitaweza hata kusoma. Nahisi nahitaji mapumziko, tena marefu. Nataka kutoka mazingira haya kabisa.”



“Unaniacha mpweke?” Lisa akauliza.



“Naomba twende wote,” Joana akashauri. “Naomba twende, Lisa. Twende hata chuo kingine, hilo siyo tatizo.”



“Si rahisi kihivyo, Joana … nitawaelezaje nyumbani?”



Mara wakasikia hodi ikiambatana na sauti ya kike mlangoni, wakatazamana kabla hawajasikia sauti:



“Cecilia!”



Joana akanyanyuka kwenda mlangoni. Cecilia ni kiongozi wao wa bweni. Ni mwanamke mnene machachari anayependa sana kuzungumza. Anafahamika sana kwa mwendo wake wa kibabe na sauti yake nyembamba.



“Hello Joana, tafadhali naweza nikaongea na wewe kidogo?”



Joana akaufunga mlango na kusogea kando kidogo.



“Kumekuwa na sintofahamu ndani ya bweni letu kwa muda sasa. Watu wamekuwa wakiishi kwa taharuki sana, hivyo basi mie kama kiongozi wa bweni nimeona nije kutoa tahadhari,” alisema Cecilia, mpaka hapo Joana hakuonekana kushtushwa.



Alichukulia taarifa hiyo kama zilivyo nyingine. Hakujiuliza kwanini aliitwa pembeni yeye mwenyewe.



“Kuna mwenzetu amekiri kumuona Moa akiwa anakuja kwako nyakati za usiku.” Hapo Joana akashtushwa. Moyo ulikita!



“Joana huwa unampokea Moa wakati wa usiku?”



Joana akakataa katakata, alimbishia kabisa Cecilia. Cecilia akaenda zake akimwachia tahadhari:



“Njia ya mwongo ni fupi.”



Joana akaenda kumweleza Lisa juu ya Cecilia. Alihisi kuchanganyikiwa na akazidi kupata sababu ya kuondoka eneoni hapo haraka iwezekanavyo.



Alilia Lisa akambembeleza sana mpaka kwenye majira ya saa saba usiku. Lisa akalala na kumwacha Joana macho.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Kwenye majira ya saa nane usiku, akiwa mwenyewe macho, akasikia hodi mlangoni. Na mara sauti:



“Moa!”



Joana akajikuta amepandwa na hasira. Alihisi kichwa kimekua cha moto na mwili umenyanyuka pasipo kujitambua.



Alielekea kabatini akatoa rungu moja kubwa, kisha akaenda mlangoni na kufungua. Moa akaingia, lakini akakutana na rungu kubwa kichwani – pam! Akadondoka kama kiroba akivuja damu kichwani.









ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog