Simulizi : Joana Anaona Kitu Usiku
Sehemu Ya Nne (4)
Joana akatahamaki kwa mshangao. Ni kama vile si yeye aliyefanya hilo tukio.
"Mungu wangu, nimeua!" alisema akishika kichwa. Lisa alikuwa ameachana mdomo macho yakimtoka.
"Lisa tunafanyaje sasa?" Joana akauliza akikung'uta viganja vyake. Jasho lilikuwa tayari limeshamvuja.
Lisa akanyanyuka upesi toka kitandani na kwenda kuweka mgongo wa kiganja chake mbele ya pua ya Moa. Akasikilizia kwa sekunde kadhaa.
Loh! Moa hakuwa anahema!
"Ina maana amekufa?" Joana akawahi kuuliza. Uso wake ulifinyangwa na hofu kubwa. Hajawahi kuua akiwa na akili zake timamu.
"Inawezekana akawa amekufa," Lisa akajibu kwa sauti ya chini.
"Sasa tunafanyaje jamani! Lisa tunafanyaje?"
"Sijui, Joana! Hii ni kesi kubwa, tutaenda kufia jela."
Joana akazidi kuchanganyikiwa. Lisa alijaribu kumtuliza na kumwambia:
"Usijali, Joana. Hakuna mtu anayejua kama Moa amekuja humu."
"Una maanisha nini, Lisa? Hata kama hakuna mtu anayejua, tutaupeleka wapi mwili wa Moa?"
"Joana, inabidi ufikirie mara tatu zaidi. Upo radhi tukamatwe na kufia jela?"
Joana akajibu kwa chozi.
"Basi ndiyo tutafute namna ya kufanya. Tatizo tayari limeshatokea, na kulia kwetu hakutasaidia."
Wakakaa kama dakika tano, bado mwili wa Moa ulikuwepo chini ila umeacha kumwaga damu.
"Tukautupie mwili wake huko mbali," akashauri Joana aliyekuwa anatetemeka.
"Tutapitia wapi?" Lisa akauliza.
"Tutapitia hii njia ya huku uani. Hamna kamera, na ni fupi zaidi."
Wakatazama saa, ilikuwa saa tisa usiku na dakika za mapema. Wakakubaliana kupiga moyo konde na kufanya hivyo ili kujiepusha na kadhia ya mkono wa dola.
Ila wakati wanahangaika na kumnyanyua Moa, wakasikia vishindo vya miguu nje ya mlango. Miili yao ikapoa ghafla kwa baridi la hofu. Walijikuta wanatetemeka kama wametoka kuogea maji ya barafu.
Wakaona ni hatari tena kwenda nje, hivyo wakakubaliana kuutia mwili wa Moa ndani ya kabati na watafanya tukio la kwenda kuutupa kesho usiku wakiona shwari.
"Huyo atakuwa ni mlinzi anazunguka huko nje!" Alisema Joana.
Mara mlango unagongwa. Tambalizi la uwoga linakamata chumba. wanatazamana kama mizimu.
Damu ilikuwa chini kwenye zulia, na mwili wa Moa ulikuwa bado haujanyanyuliwa kupelekwa kabatini.
Bahati kwao, mgonga mlango hakungoja afunguliwe, akapaza sauti:
"Ni muda wa kulala, tafadhali zimeni taa."
Kisha vishindo vya miguu vikasikika vikienda mbali. Wakashusha pumzi ndefu. Haraka wakaubeba mwili wa Moa na kuutia kabatini.
Wakafunga.
Wakaligeuza na zulia chini juu, juu chini, kisha wakaketi kitandani. Usingizi ulikuwa hauji kila mtu akibanwa na maswali kichwani. Kulala na maiti ndani ya kabati si kitu kirahisi.
Kila mmoja alikuwa anahofia na kujiuliza kuhusu kesho yake. Joana akajutia alichokifanya akishangaa na kujiuliza ilikuwaje akajitia matatizoni kiasi hicho. Basi wakajikuta hawana raha wala amani.
Muda ukasonga zaidi mpaka saa kumi na moja. Lisa alikuwa amebanwa na usingizi vibaya mno akaegesha kichwa chake kitandani akilala kana kwamba yupo vitani.
Joana yeye alikuwa ameketi vilevile ila akiwa anapiga 'magoli ya vichwa', macho yalikuwa yanafumba kwa lazima, kichwa kikidondoka na kusimama.
Katika muda huo huo, Joana akashtuliwa kwa kusikia sauti kabatini! Mlango wa kabati ulikuwa unagongwa na sauti ya mtu akinguruma.
Haraka akamshtua Lisa na kumwonyeshea kidole kabatini.
"Moa mzima!"
Kabla Lisa hajasema jambo, Joana akakimbilia kabatini na kufungua. Moa akatoka akiwa hoi. Alikuwa ameshikilia kichwa akikunja sura kwa kulalama maumivu.
"Moa, mzima!" Joana alimpapasa papasa Moa akiwa haamini. Moa hakusema jambo, akaketi kitandani bado akishikilia kichwa chake na kulalama.
Alikuwa anasikia maumivu makali.
"Nisamehe Moa, haikuwa dhamira yangu," Joana akajitetea.
"Haikuwa dhamira yako nini?" Moa akauliza. Hakuonekana kama anajua kilichotokea. Lisa akambinya mkono Joana kumwashiria anyamaze.
"Ni saa ngapi sasa?" Moa akauliza.
"Saa kumi na moja na robo," Lisa akajibu. Moa akakurupuka kusimama.
"Inabidi niende!"
"Uende wapi?" Joana akawahi kuuliza.
"Inabidi niende!" Moa akarudia kauli yake pasipo kujibu. hakumngoja tena mtu aongee, akaufuata mlango upesi, akaufungua na kutimka!
Joana akafunga mlango kwa ufunguo haraka, kisha akatulia kwanza hapo mlangoni kutega kama atasikia lolote huko. baada ya kama dakika mbili, akarejea kitandani kumkuta Lisa aliyekuwa ameketi kitako.
"Joana, Moa siyo binadamu," akasema Lisa kwa macho ya kujiamini.
"Kwanini wasema hivyo?"http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Moa hakuwa anapumua!" Lisa akalipuka.
"Kwa akili zangu nilipima pumzi zake, sikuhisi kitu!"
"Pengine alikuwa anapumua kwa mbali."
"Hapana! Hapana. Alikuwa hapumui kabisa. nimemtazama pia hata hapa alipokuwepo kitandani, sikuona kifua chake kikisinyaa na kutanuka. Naapa kwa Mungu wangu!"
Sasa ile hoja kwamba Moa ni jini ikaanza kuleta mashiko kichwani mwa Joana.
"Unajua Moa anakaa wapi?" Lisa akauliza.
"Sijui!" Moa akatikisa kichwa.
"Kuna kitu, Joana. Ni wazi kuna kitu hapa. We unahisi atakuwa anaishi wapi?"
"Msituni!" haraka likaja jibu kichwani mwa Joana.
Kama alihaha kutafuta makazi ya Moa akayakosa, basi Moa ndiye yule anayeishi msituni. Ndiye yeye muuaji. Ndiye yeye anayegeuka kuwa kiumbe cha ajabu! Aliyakumbuka maneno ya yule mwanafunzi aliyekuwa anawasimulia wenzake.
"Moa anakuja hapa saa nane za usiku tu. Anaonekana nyakati za usiku peke yake, tena akiwa mwenye nguvu. Si bure aliondoka haraka punde alipojua ni saa kumi na moja, maana jua linakaribia kuchomoza!"
Maneno hayo ya Lisa yalipenya vizuri masikioni mwa Joana na kujenga nyumba kuu ya hoja. yalikuwa na mantiki ndaniye. Yalimfumbua Joana macho ambayo alikuwa ameyafumba kwa kutokujua ama kwa kujua kwasababu tu ya upofu wa mapenzi.
"Naondoka, Lisa," akasema Joana. "Siwezi nikakaa tena hapa. Tafadhali naomba uniwie radhi nakuacha peke yako. Ila ni kwa mema."
"Naelewa, Joana. Nenda," akasema Lisa. Hakuona tena sababu ya kuzozana na Joana. Alimwonea huruma rafiki yake, akamshika bega na kumvuta kumkumbatia.
"Yote yatapita Joana, hata na hili."
Joana akaangua kilio. Alipanga vitu vyake ndani ya begi dogo tu la mgongoni maana hakutaka yeyote ajue kama anaondoka, akavalia nguoze na kumwaga Lisa.
"Tutaonana pale majira yatakapofika."
Uzuri alishakata tiketi jana yake kwa kupitia mtandao, hivyo hakupata shida. Alifika uwanja wa ndege akajipaki chomboni na kuondoka Ujerumani kwenda kwao Ubelgiji moja kwa moja.
Alijisema kifuani anataka kusahau yote ya huko alipotoka akaanze maisha mapya.
Lakini utaanzaje mapya ukiwa umeyabebelea ya zamani? Shingoni mwake bado alikuwa amebebelea mkufu aliomkabidhi Moa.
Mkufu huo alikuwa anarudi nao nyumbani. Alikuwa anaupeleka nyumbani, je utamwacha salama ilhali Moa alisema ilimradi ana mkufu huo na basi atakuwa naye?
Mama yake alimpokea kwa bashasha na kumpeleka mpaka nyumbani ambapo pasipo kuficha akamweleza mamaye yale aliyokumbana nayo huko chuoni.
Mama akampa moyo na kumsihi apige moyo konde, atafanya mpango apate chuo hapa hapa nyumbani awe anamuona na kumpatia nasaha.
Zikapita siku mbili akiwa nyumbani. Siku ya tatu Joana akapata habari kwa kupitia runinga. Lisa alikuwa ameuawa na mtu asiyejulikana!
Habari hizo zilimshtua na kumpa jakamoyo. Lisa kwake hakuwa rafiki tu bali mtu mwenye umuhimu mkubwa. Japokuwa alimjulia chuoni walitokea kutengeneza urafiki mpana wenye tija.
Alijikuta anaumia sana rohoni kila alipokumbuka sura ya Lisa na tabasamu lake. Namna alivyopambana kumfichia siri yake na kusimama upande wake siku zote hizo tangu anamjua.
Alishindwa kuzuia machozi kumbubujika. Ndoto yake ya kuonana na Lisa siku za usoni zilikata. Ina maana hatomuona tena.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Lakini zaidi ya yote, alijihisi atakuwa anahusika na kifo cha Lisa kwa namna moja ama nyingine, nafsi yake ilimwambia vivyo. Ilimshtumu, ilimshtaki.
Alijiona mkosefu na mkono wake ndiyo ambao umempeleka Lisa machinjioni.
Ila ngoja kwanza kabla ya kujihukumu, akaona basi ni vema akapata taarifa ya kutosha juu ya kifo hicho. Aliapa endapo akiwa anahusika kwa namna yoyote na mauaji hayo, hatasamehe nafsi yake kwa kuangamiza nafsi moja zuri aliyowahi kukutana nayo ulimwenguni.
Usiku kwake ulikuwa mgumu sana kwani hakulala kwa amani kabisa. Kila alipolala alimuona Lisa kando yake. Aidha akiongea, kucheka ama kutabasamu.
Alikurupuka kila mara, na kulia pia.
Asubuhi ilipowadia, akanyanyuka na kwenda kupata gazeti. Hakuwa na ‘smart phone’ hivyo hiyo ilikuwa ndiyo njia pekee kwake kupata taarifa kwa kina.
Akanunua gazeti moja la Kijerumani ambalo lilikuwa limeweka taarifa ya Lisa ukurasa wake wa kwanza kabisa, ila ikiwa pembeni kidogo ya habari kuu iliyobeba gazeti kwa ujumla.
Picha ndogo ya Lisa iliyo kwenye ‘black and white’ akiwa anatabasamu ilivuta machozi ya Joana kwa haraka sana. Akilipokea gazeti hilo alikuwa tayari anamwaga machozi na kubanwa kwikwi za kilio.
Akalifungua gazeti na kulisoma papo hapo.
Lisa aliuawa kwa kunyongwa majira ya usiku na mtu asiyefahamika ila akihisiwa ni muuaji fulani ambaye amekuwa akifanya mauaji maeneo hayo maeneo ya chuoni.
Kwa mujibu wa maelezo ya gazetini, Joana akajua ni Moa ndiye ambaye amehusika na kifo hicho. Ushahidi uliotolewa na wanafunzi wengine ulimwendea yeye kama mtu aliyewahi kuonekana hapo majira ya usiku mzito.
Lakini zaidi ya yote, Joana akatajwa kama mojawapo wa watu wanaotafutwa na polisi akituhumiwa kuhusika.
Kwanini aliondoka pasipo kuaga wakati alikuwa kwenye uchunguzi? Mbona kuondoka kwake na kufa kwa Lisa kwafuatana? Pia Moa, ambaye ndiyo mtuhumiwa wa kwanza wa mauaji, anahusishwa na yeye.
Joana akatetemeka akisoma gazeti hilo. Alihisi kichwa chake kimekuwa cha moto wakati kiwiliwili kikiwa kwenye baridi kali.
Haraka alirejea nyumbani kwao, akajifungia chumbani. Aliwaza na kuwazua. Alijiona akienda jela karibuni. Alikata shauri kumwambia mama yake juu ya taarifa hizo huenda anaweza kumsaidia kimawazo.
Baadae jioni mama yake aliporejea akamwambia. Mama yake akashtushwa sana na hizo taarifa, ila akampa moyo mwanae asipate shaka kwani atamsaidia kwa kumpatia wakili mzuri atakayemsaidia kumsafisha.
“Hatuwezi kukimbia hili, kadiri tutakavyolikimbia ndivyo tutakavyoonekana wahusika,” Mama alisema na kumalizia: “Itabidi twende huko tukakabiliane nalo.”
Mama akawasiliana na mwanasheria wake. Akampanga tayari kwa ajili ya kesi ya mwanae. Wakakubaliana wakutane siku ya kesho majira ya mchana.
Kesho wakakutana na Joana akaeleza kila kitu kwa mwanasheria huyo ambaye alijitambulisha kwa jina la Stewart McCoy. Alikuwa ni mwanaume mrefu aliyependezea ndani ya suti yake ya bluu.
Nywele zake zilikuwa nyekundu akizichana utamu. Alikuwa na macho ya kujiamini na sauti ya mamlaka.
Alitabasamu na kumshika bega Joana, akamwambia:
“Hiyo kesi yako ni ndogo sana. Wala usikose usingizi kwa kuiwaza.”
Baada ya hapo wakaongea maneno machache na mama yake Joana kabla hawajaagana.
“Kesho tutaenda Ujerumani,” mama alimwambia Joana. “Mwanasheria atafanya mawasiliano na polisi wa huko watarajie ujio wetu.”
Kweli kesho yake wakajipaki kwenye ndege kwenda Ujerumani. Waliripoti polisi ambapo huko Joana hakusema lolote lile kwa kigezo cha kumwachia kazi mwanasheria, Stewart McCoy.
Polisi wakaongea na mwanasheria. Baada ya siku moja tu siku ya kusikilizwa kesi ikapangwa.
Siku hiyo inspekta Westgate pamoja na walinzi wawili wa chuo, na msimamizi wa bweni – Cecillia walikuwa ndani ya mahakama wakiwa upande pinzani na Joana.
Joana alikuwa anatetemeka mno. Alihisi mwili wake umekuwa mzito na miguu yake haiwezi tena kumbeba, lakini Stewart akamtia moyo. Alimtazama kwa tabasamu pana akimwambia:
“Tunashinda hii kesi. Amini.”
Stewart alifanya mahakama kama chumba chake cha uani. Aliitawala na kuipelekesha atakavyo. Alikosoa ushahidi wote ulioletwa hapo kwa kusema ni wa kufikirika tu. Na ukitazama kesi hii ilikuwa na mlengwa wa kiroho zaidi, kiimani, mambo ambayo hayawezi kuthibitishwa na logiki ya kawaida. Mambo haya hayaaminiki mahakamani.
Nyundo ya hakimu ikagongwa, Joana akashinda.
Mahakama ikiwa inatawanyika, Inspekta Westgate akamfuata Joana na kumpatia mkono kumpongeza kwa kushinda kesi. Ila akamwambia:
“Najua unahusika, Joana. Ni swala la muda tu.” akaongezea: “Kama sitakushika mimi, atakushika mwingine.”
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akaenda zake akimwachia Joana parazo la mawazo alilokuja kutolewa na mama yake aliyemkumbatia kwa furaha.
“Umeshinda!” mama alisema kwa tabasamu akimtikisa mwanae. Walipanga kuondoka kurejea Ubelgiji kesho yake mapema.
“Utasoma huko huko, sawa?”
“Ndio, mama.”
Furaha hii ya Joana ilikuwa ni ya halaiki tu. Akiwa mwenyewe alikuwa anaumia na kuteswa na mawazo. Picha ya Moa na Lisa zilimjia na kumnyima raha.
“Nimemuua Lisa …” kuna sauti ilikuwa inajirudia masikioni mwake kila alipotulia. Hata akifumba masikio alikuwa bado anasikia. “Nimemuua Lisa …”
Alitazama mkufu aliopewa na Moa, machozi yakamdondoka.
“Moa yupo wapi?” alijiuliza. “Yule Moa yupo wapi?”
Maisha yake hayakuwa sawa … hayakuwa sawa … hayakuwa sawa.
Usiku mzima hakulala mpaka pale alipokuja kuamshwa kwa ajili ya safari. Walikwea ndege na ikawachukua muda mfupi tu kuwa ndani ya Ubelgiji.
Siku hiyo Joana akashinda kutazama ‘movies’ ili kupumzisha ubongo wake dhidi ya mawazo. Alitazama movies bandika bandua mpaka usiku wa saa sita.
Akapitiwa usingizi akiwa ameshikilia rimoti ya televisheni.
Kwenye mishale ya saa nane usiku, akashtushwa na hodi mlangoni. Alitazama televisheni, bado ilikuwa inaongea na kuonyesha. Akatazama saa, akaona ni saa nane.
Akatazama mlangoni.
“Nani?”
Akajiuliza. Haraka mwili wake ukaanza kutetemeka kwa hofu. Aliuliza nani yupo mlangoni ila sauti haikusikika. Ilikuwa kavu iliyokithiri woga.
Haraka akili yake ilikimbia akajiuliza: vipi kama ni Moa? Hayo ndiyo majira yake, saa nane za usiku, ina maana amemfuata mpaka Ubelgiji?
Akijiuliza maswali hayo ambayo yalizidi kumpatiia hofu, hodi ikagongwa zaidi mlangoni. Joana alijikuta hajui cha kufanya zaidi ya kutazama tu.
Alikuwa kama zezeta. Alikuwa kama vile hayupo eneo hilo, haoni ilhali anatazama. Ni kama vile alipooza mwili na macho pekee ndiyo yamebakia yakifanya kazi.
Alishtuliwa na mkono wa mama yake uliomdaka bega na kumtikisa tikisa kama dawa ya mbu.
“We Joana! Joana!”
Akakurupuka kumtazama mamaye kwa macho ya kutumbua.
“Una nini?” mama akauliza. “Mbona nabisha hodi unifungulii? Taa zinawaka mpaka muda huu?”
Joana akamwomba radhi mamaye. Akamwambia hakusikia kwani alikuwa amezama kwenye dimbwi la mawazo. Mama akaketi kitako na kuongea naye mawili matatu.
“Una shida gani Joana? Niambie mama yako nakusikiliza,” mama akasema kwa sauti ya upole akimtazama mwanaye.
Alikuwa amevalia gauni jeupe la kulalia, macho yake yakifunikwa na miwani.
Kabla ya Joana hajasema jambo akaanza kudondosha machozi na makamasi. Akalala begani mwa mama yake na kulia kwa sekunde kadhaa kabla hajasema:
“Mama nayakumbuka maisha yangu ya zamani. Natamani yarudi.”
Mama akambembeleza. Akamsihi kila jambo na wakati wake, maisha yanasonga hayasimami. Inabidi sasa atazame na kuzingatia mbele, si nyuma.
“Najua ni ngumu, lakini inabidi sasa ufungue ukurasa mpya wa maisha yako. Wewe bado msichana mdogo sana. Mambo mengi mazuri yanakungoja mbele. Tazama ndoto zako.”
Maneno hayo yakampatia faraja Joana. Mama alimwomba akalale pamoja naye kwa usiku huo. Na kwakuwa baba hakuwepo, hilo halikuwa na shida, akaenda kulala na mama.
Yakapita majuma mawili. Joana akaanza sasa kurudia maisha yake ya kawaida kwa kuwa mtu mwenye furaha akitabasamu na kucheka toka moyoni. Hata mwili wake ulipata uangavu.
Alikula na kunywa vizuri. Lakini pia akajishughulisha na michezo kwa ajili ya kumnyima muda wa kujifungia ndani na hata kuboresha afya yake.
Akajiunga na klabu moja jijini ambayo alikuwa akiambatana nayo kwenye mchezo wa mpira wa pete. Alikuwa anaupenda mchezo huo toka udogoni, na hata alipourejea ilimchukua muda kidogo tu kuwa sawa.
Kwasababu tatizo lilikuwa pumzi, akawa anafanya sana mazoezi ya kukimbia. Aliunda urafiki na wachezaji wenzake. Akajihisi amekuwa mpya.
Alipokuwa akitoka mazoezini alioga na kujipumzisha. Na kwasababu za uchovu wa mazoezi basi akawa haangaiki kutafuta usingizi. Alilala fofofo.
Baada ya mwezi mmoja klabu yake ikapanga safari ya kwenda Paris – Ufaransa ambapo huko kulikuwa kuna mashindao ya mpira wa pete wa kikanda. Joana alikuwa ni mmoja wa wachezaji ambao walijumuishwa kikosini hivyo ilibidi naye aende.
Akaaga wazazi wake. Mama akampatia kiasi kikubwa cha pesa kikamfae huko aendako.
“Fuata wapi furaha yako ilipo,” mama alimwambia kabla hajambusu na kumkumbatia.
Kesho yake mapema, Joana akaungana na wenzake na kukwea basi kuelekea Paris. Ni safari ya masaa matatu au manne, ila kwakuwa hawakuwa na haraka yoyote ile, wakachukua masaa sita kufika.
Walikuwa wanasimama mara kwa mara njiani, kula kunywa na hata kupumzika.
Walipozama ndani ya jiji la Paris wenye kamera zao wakatoa na kuanza kumulikamulika huku na kule, mmojawao alikuwa Joana. Alikuwa anahakikisha kila tukio analipata akalitunze kumbukumbuni.
Ila wakiwa wamebakiza umbali mdogo wapate kufika kwenye hoteli wanayotakiwa kuweka kambi, ghafla tairi la basi likapasuka. Gari likaenda mrama kama jahazi ndani ya bahari iliyochafukwa.
Bahati njema dereva alimudu chombo na kukiweka kando kikiwa kimesababisha uharibifu mdogo. Liligonga gari moja dogo na nguzo moja ya barabarani.
“Nashangaa nini shida. Lilifanyiwa huduma zote kabla halijaanza safari,” dereva alisikika akilaumu.
Alikuwa mwanaume mfupi mnene aliyevalia traki nyekundu na kapelo rangi ya manjano.
Sasa basi kwakuwa umbali ulikuwa mdogo, wakaamua kumalizia kwa kutembea na miguu wakiacha basi linafanyiwa matengenezo.
Wakiwa wanatembea Joana akaendelea na zoezi lake la kupiga picha. Akafotoa huku na huko akiwa anatabasamu. Akawapiga wenzake picha, pia na majengo.
Mara akiwa anafanya zoezi lake hilo, kwa mbali akamwona mtu ambaye hakuwa mgeni. Alihisi amempiga picha mtu huyu kwakuwa kamera yake ilikuwa imeelekea upande wake.
Ila alipotazama kwenye kamera, hakumwona! Akabakia ameduwaa. Akatazama upande ule, hakumwona mtu. Akabakia akiangaza mpaka pale aliposhtuliwa na wenzake nusura agongwe na gari.
Akashindwa kuelewa, ni mach0 yake ama nini? La hasha! Siyo macho yake bali ni uhalisia, yaani macho yaonyeshe kitu kimoja mara zote hizo?http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Basi akakodoa sana macho yake kama atamuona tena mtu huyo, lakini wapi. Hakukuwa na kitu, hakuona jambo mpaka wanafika huko kiwanjani walipoenda kusabahi.
Wakazunguka sana huko na Joana akaendelea kupiga picha. Akafurahia sana na kwa kiasi fulani akasahau shida aliyokuwa nayo.
Marafiki zake pia wakafurahia uwepo wake, wakaweka mapozi mbalimbali Joana awafotoe picha. Wakapiga pia picha ya wote, klabu nzima, kama ukumbusho.
Walichukua muda wa kama masaa mawili ndani ya eneo hilo kabla hawajaondoka. Wakaelekea kwenye hoteli fulani mpya iitwayo La Princessita. Huko Joana akapewa chumba kimoja na mwenzake aitwaye Rosie – mwanamke mnene mweupe.
Kama kawaida chumba hicho kilikuwa kimepakana na dirisha. Na basi kilikuwa katika sakafu ya kumi na mbili ya ghorofa la hoteli ambapo Joana alikuwa na uwezo wa kutazama jiji vizuri kabisa.
Alikifurahia chumba maana kilikuwa kikubwa na chenye samani nzuri za kuvutia. Akapiga picha.
Mwenzake akampatia wazo.
“Kwanini tusiende Eiffel Tower? – kule kuna mandhari mazuri kwa ajili ya kumbukumbu.”
Na kweli. Nani aende Paris: Ufaransa pasipo kutembelea mnara wa Eiffel. Mnara maarufu dunia nzima. Ishara ya Paris na Ufaransa kwa ujumla.
Joana akapendezwa na hilo wazo. Basi wakavaa na kwenda safari. Wakachukua muda mchache sana kufika mnarani kwani hoteli ilikuwa karibu na mnara huo.
Wakapiga picha kadhaa kisha wakaenda mgahawani kula.
“Umeona hii! Imetoka bomba,” alisema Rosie akionyeshea picha mojawapo ndani ya kamera.
“Mie naona zote nzuri,” Joana naye akatia neno wakizikagua picha zingine.
“Joana, nataka nizisafishe picha hizi niwe nazo kwenye nakala ngumu,” akasema Rosie.
“Nataka nikazibandike ukutani mwa chumba changu.”
“Unataka kusafisha ngapi?”
“Zote. Si umesema zote nzuri?”
“Sawa. Twende tukatafute studio.”
Basi wakaenda kuhaha ndani ya jiji. Punde wakapata studio na kusafisha picha. Rosie akalipia na kuchukua picha zake. Joana naye akasafisha kadhaa alizozipenda. Wakazitia bahashani na kurudi hotelini.
Baadae wakaenda mazoezini kwa ajili ya kupasha viungo vya mwili na kuviweka tenge. Wakarejea hotelini kwenye majira ya saa kumi na mbili jioni.
Kwenye majira ya saa mbili usiku baada ya kupata chakula cha usiku, Joana akaketi kitandani na kuanza kupekuwa picha zake. Wakati huo Rosie alikuwa yupo bafuni anaoga.
Zilikuwa nzuri kweli. Zikamfanya mpaka atabasamu.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alizitazama kwa mara ya kwanza, akarudia kwa mara ya pili. Alipozirudia kwa mara ya tatu, akaona kitu pichani.
Picha ya kwanza … ya pili … ya tatu na ya nne!
Kulikuwa kuna picha ya kivuli cha mtu pembeni yake. Kivuli hichi kilikuwa kimefifia na kuonekana kwa mbali. Kama mtu hautazami kwa karibu huwezi kuona kitu.
Kilikuwa ni kivuli cha mwanaume. Kilikaa upande wa kushoto wa Joana katika kila picha.
Joana akashtuka sana. akatafuta kamera yake na kuanza kupekua picha zote. Haki hakuona kitu. Kivuli hakikuwepo abadani.
Hata pale alipotazama picha zile ambazo alizisafisha, ndani ya kamera hazikuonyesha kivuli. Sasa hichi kivuli kimetoka wapi? Akajiuliza.
Rosie alivyotoka bafuni akamwomba picha zake walizozisafisha azitazame, Rosie akamkubalia na kumpatia. Joana akazikagua zote, hakuona picha ya kivuli hata moja.
Ina maana kivuli alikuwa kwenye picha zake tu. Picha alizomo yeye tu. La haula!
“Kuna nini Jo?” akauliza Rosie akijifuta maji. Alimwona Joana akizikagua picha zake kana kwamba polisi.
“Hamna kitu!” akasema Joana kisha akamkabidhi Rosie picha zake. Rosie akazitazama hizo picha kama zina mushkeli. Hakuona kitu, akazirejesha begini.
Akavaa na kulala akitazama runinga.
Ila Joana hakuwa hapo, alikuwa mbali kimawazo. Aliwaza kile kivuli, kwa namna moja akahisi kinaweza kikawa na mahusiano na taswira aliyokuwa anaiona huku na kule ndani ya jiji.
Akajitahidi kupuuza mawazo hayo na kuhamishia mawazo yake kwenye runinga. Akajumuika na Rosie kutazama tamthilia mpaka mishale ya saa nne usiku. Rosie akalala.
Muda si mwingi naye Joana akapitiwa na usingizi.
Kwenye majira ya usiku wa manane, kukiwa kimya kabisa, Rosie akaanza kutapatapa kama samaki aliyetupiwa jangwani. Alikuwa anahangaika kutafuta hewa kwanguvu zote akibana shingo yake.
Akifanya hayo, alikuwa bado usingizi kwani macho alikuwa ameyafumba.
Alikuwa anataka kupiga kelele lakini sauti haitoki. Alikuwa anataka kufumbua macho lakini kope zilikuwa nzito mno. Akaishia kupapatika!
Jasho lilikuwa linamtoka, na kadiri muda ulivyokuwa unaenda, akawa anapoteza nguvu za kupambana.
Bahati akampiga teke Joana, Joana akakurupuka usingizini na kuangaza. Mara Rosie naye akaamka akishikilia shingo yake, akikohoa na akihema kwanguvu. Joana akatahamaki.
“Vipi Rosie?”
Rosie hakusema jambo. Alikuwa bize anakusanya hewa kwanza. Alipokuja kutengemaa akamwambia Joana alikuwa amekabwa na mwanamke ambaye hakumwona uso wake.
“Alikuaje?” Joana akauliza.
“Alikuwa ana nywele ndefu zikimziba uso!” Rosie akasema kwa sura ya woga. Akatikisa kichwa na kusema: “Nilikuwa nakufa, Joana.”
Tangu hapo Rosie akakosa kukosa usingizi. Yeye na Joana wakabaki macho wakiteta mambo kadha wa kadha. Kila Rosie alipotaka kulala akashtuka na kujilazimisha akae macho.
Alikuwa ana usingizi mzito ila alikuwa na hofu huenda akakabwa tena.
Kwa upande wa Joana yeye alikuwa amekabwa na maswali. Akili yake ilikuwa inawaza huyo mkabaji ni nani? Na je anahusiana na yule mhanga wa ukabwaji kwenye hoteli ya kwanza?
Vipi kama Rosie asingempiga teke? Alikuwa anakufa?
Mawazo ambayo alikuwa ameanza kuyasahau, sasa yanaanza kumrejea.
Alikosa raha kabisa. Mpaka usiku unaisha hakulala kabisa. Walienda kunywa chai asubuhi na mapema lakini bado akiendelea kuwaza.
Walikula na kurejea mapumziko, baadae majira ya jioni wakatoka kwenda mazoezini kupasha viungo.
Ilikuwa imebakia siku mbili tu ili mashindano yaanze rasmi. Mkufunzi wao aliwapa maelekezo ya kuzingatia na kuwataka waanze kujenga picha ya shindano vichwani mwao.
"Hatujaja hapa kushiriki bali kupambana. Kumbukeni lengo letu ni kufika robo fainali."
Pengine lengo hilo waweza liona ni la chini, ila kwa hiyo klabu lilikuwa ni lengo mujarab tu ukilinganisha na uchanga wao.
Pale kwenye mashindao watakutana na klabu kubwa, zoefu na zenye ujuzi mkudufu. Hivyo kuchomoza na kufika hatua ya robo fainali, kwao itakuwa hatua kubwa mno.
Wakapeana motisha wakiamini kila kitu kinawezekana pakiwa na nia.
"Tule vizuri. Tupumzike na tuzingatie," mkufunzi alisisitiza.
Ila kabla watu hawajatawanyika kwenda kujiandaa ili warudi kambini, huko hotelini, mkufunzi akamwomba Joana waonane.
"Nina maongezi nawe."
Wakawa wanatembea wakiteta. Mkufunzi alikuwa anata kuulizia hali ya Joana kwani hakuonekana kama yupo sawa mazoezini.
"Ulikuwa unamis sana mipira. Hata energy na passion ilikuwa chini. Kuna tatizo?"
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Joana akamwomgopea Mkufunzi kwamba alikuwa sawa, pengine ni siku tu haikuwa njema kwake.
Alihofia kama angesema ukweli kuwa hakulala basi mkufunzi angeng'aka kumgombeza.
Kwa shingo upande, mkufunzi akakubali ila akamtaka azingatie kazi kubwa iliyopo mbeleni.
"Tunakutegemea kwa kiasi kikubwa. Usije ukatuangusha."
Basi wakarudi hotelini. Baadae majira ya usiku, Joana akiwa amejitenga mwenyewe akachukua picha zake na kurudia kuzitazama.
Alizitazama kwa umakini sana. Alitazama kile kivuli alichokuwa anakiona na hakutaka hata kujiuliza maswali.
Alipapasa papasa na vidole vyake kabla hajafunga hizo picha na kubakia akiwanda wanda.
Hakutaka kulala. Aliogopa kulala japokuwa kwa muda ni kama vile hakuwa anajua kwanini anaogopa kufanya hivyo.
Alimtazama Rosie akamwona tayari ameshalala. Amejifunika shuka akikoroma kabisa. Akatamani angelikuwa yeye.
Basi kwasababu hakuwa na usingizi na usiku ni mrefu, akaamua kutafuta jambo litakalomsogezea muda. Asingeliweza kukaa macho muda wote vile.
Akili yake ikampatia wazo. Ila wazo hatarishi. La kwenda mojawapo ya klabu ndani ya jiji la Paris akaukatie usiku huko.
Swala la pesa halikuwa na shida kwani alikuwa ana kiasi cha maana tu alichopewa na mamaye.
Ila akasita ... akawaza ... akaamua kukata shauri kwenda. Abaki pale hotelini kufanya nini na wakati amekuwa bundi?
Akavaa na kutoka, akachukua taksi iliyompeleka moja kwa moja mpaka kwenye klabu moja ya usiku inayoitwa ROGUE. Humo akazama ndani na kushawishika kunywa vileo.
Akaagiza whisky moja kali ya kumsahaulisha mawazo. Taratibu akawa anapiga tarumbeta akitazama watu wakicheza muziki kwenye mwanga hafifu unaong'arishwa na vijitaa vya rangi rangi.
Alipokuwa amekaa palikuwa ni kochi kubwa gizani. Mwanga ulikuwa unamulika mara moja moja na Joana alitokea kupenda hayo mazingira.
Akatulia hapo akinywa na kunywa. Muda si mwingi akapata kampani ya mwanaume fulani mnene aliyejitambulisha kwa jina la Rabiot.
Mwanaume huyo alikuwa amebebelea glasi ya mvinyo na alikuwa anapata shida kuongea kiingereza kuelewana na Joana.
Ni mtu mwenye asili ya Ufaransa. Kiingereza chake kilikuwa kimemezwa na lafudhi ya kifaransa akiongea maneno utadhani anayameza.
Joana alifurahia kampani hiyo kwani ilimwondolea upweke. Lakini pia ilikuwa imamsogezea muda.
"Unahitaji nyingine?" Akauliza Rabiot baada ya kuona Joana anatikisa chupa ya whisky. Kabla Joana hajajibu, Rabiot akamuita mhudumu na kumpatia chupa ya Joana.
"Leta kama hiyo!" Akasema kwa kifaransa. Mhudumu akaleta nyingine, Joana akaendelea kujimiminia.
Kwenye majira ya saa tisa usiku, Rabiot akatoka na Joana. Joana alikuwa amelewa na maamuzi anayoyafanya yakisukumwa na kileo kichwani.
Aliridhia kwenda kulala na Rabiot nyumbani kwake. Jambo ambalo kama angelikuwa mzima asingelifanya.
Rabiot yeye hakuwa amelewa. Alikuwa mzima na anayejitambua. Na alikuwa anajua kile anachokifanya.
Alimpakia Joana kwenye gari lake, Volkswagen ndogo rangi ya kijivu, wakaelekea mpaka nyumbani kwake.
Ilikuwa ni apartment moja nzuri inayopatikana pembezoni mwa jiji. Ndani yake kulikuwa kumepangiliwa vizuri, na rangi za kupendeza.
Rabiot akampeleka Joana chumbani kumlaza, kisha akaenda kuoga. Aliporudi akamvua nguo Joana na kuanza kumkagua kwa macho ya uchu.
Alitimiza haja yake pasipo shaka kisha akajilaza pembeni hoi. Alijiona mwenye bahati siku hiyo tangu aanze mtindo wake wa kwenda klabu za usiku.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alipitiwa na usingizi mzito akalala kama mfu. Yalikuwa ni majira ya saa kumi na dakika kadhaa.
Usichukue muda mrefu, Rabiot akajikuta anakabwa na mikono migumu yenye nguvu. Alifurukuta kwa namna zote ila hakufanikiwa kabisa. Alidakwa shingo mpaka akakata moto.
Aliachama mdomo ulimi ukienda kando. Kisha kama hakuna kilichofanyika muda ukasonga kukiwa kimya.
Yalipofika majira ya saa tatu asubuhi, Joana akashtuka. Alijikuta uchi amelala kando mwanaume. Akaangaza huku na huko kabla hajampiga kofi Rabiot na kufoka kwanini kamfanyia tendo lile pasipo ridhaa yake.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment