Simulizi : Joana Anaona Kitu Usiku
Sehemu Ya Tano (5)
Alifoka akiendelea kumpiga Rabiot, akagundua Rabiot hakuwa hai. Hakuwa anahema wala kutikisika.
Nani kamuua? Akajikuta anajiuliza upesi.
Alipomtazama Rabiot shingoni akagundua alikuwa ana michubuko, na mivilio ya damu. Ndani hakukuwa na mtu mwingine yoyote bali wao, sasa nani kamuua?
Ni yeye!
Aligundua ana alama za meno kwenye mkono wake wa kuume. Maana yake nini? Ina maana aling'atwa wakati anamkaba Rabiot?
Mbali na hayo ilibidi kwanza atoke eneo hilo upesi kabla mambo hayajaharibika, ila huko napo anapoenda ataeleza nini? Mpaka muda ule itakuwa tayari imeshajulikana kambini kuwa hayupo!
Alivaa akaangaza usalama nje. Alichukua kila kilicho chake. Akafanikiwa kuchoropoka ila maeneo ya getini ndipo akakutana na mwanamke fulani ambaye hata hakumsalimia, akaenda na zake.
Alijikagua kama ana pesa, akapanda taksi mpaka hotelini ilipo kambi yao, akanyookea moja kwa moja chumbani kwake ambapo hakumkuta mtu. Watu wote walikuwa wameondoka asijue wameenda wapi.
Alikaa mwenyewe akapitiwa na usingizi. Alikuja kuamshwa na Rosie majira ya mchana wa saa nane. Rosie akamwambia walikuwa walienda kufanya mazoezi na matembezi kidogo.
Pia mkufunzi alikuwa anamuulizia kupita kiasi.
“Amekasirika sana,” Rosie alisema. “Amenigombeza kwa kutokujua umeenda wapi akiamini nimekufichia siri.”
Joana akamtuliza Rosie na kumpa pole, ataenda kuonana naye mwenyewe na kumweleza yaliyomsibu.
“Kwani ulienda wapi, Joana?” Rosie akauliza.
Joana akamzungusha zungusha asimpatie jibu. Punde kidogo akatoka kwenda kuonana na mkufunzi.
Mkufunzi alikuwa amefura kwa hasira, hakuona mantiki kwenye maneno ya Joana akawaka na kumtaka aondoke kwani awamuhitaji tena kwenye timu.
“Hatuwezi kuongea na wewe ilhali umegoma kuelewa. Tunakuomba uondoke!”
Haikujalisha namna gani Joana aliongea, mkufunzi hakutaka kumwelewa. Kutoroka kambini na kwenda klabu nyakati za usiku, ni kosa kubwa kwa mazingira ya kambi ya michezo.
Mkufunzi akampatia nauli Joana na kumtaka arudi kwao Ubelgiji. Joana akaumia sana kwani hakutaka kurudi. Ile ndiyo ilikuwa fursa pekee kwake kubadilisha maisha yake.
Akalia sana, mkufunzi asimjali akaondoka zake na kumwacha peke yake. Akajinyanyua na kwenda chumbani ambapo akampasha habari Rosie.
“Sasa inakuaje, Joana?” Rosie akauliza.
“Siwezi nikaondoka, Rosie. Siwezi!”
Joana akaendelea kulia. Baadae akanyamaza na kumwambia Rosie kwamba hataondoka kwenda popote pale.
Basi zikapita siku mbili Joana akiwa bado yupo pale kambini ila hashiriki kwenye mazoezi ya pamoja na wenzake. Wenzake wakienda mazoezini basi naye anaenda kufanya mazoezi yake binafsi kwenye gym.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Rosie akamwambia mkufunzi kuhusu hayo mambo, ikiwa imebakia masaa tu kabla mashindano hayajaanza rasmi, mkufunzi akaonana na Joana. Akamsikiliza na kumsamehe.
“Natumai hili jambo halitajirudia tena, Joana,” mkufunzi alimalizia kwa kusema hivyo.
Joana akafurahi sana. Akamshukuru sana Rosie kwa kumsaidia, amefurahi na hana cha kumlipa kumtosheleza.
“Wewe ni rafiki wa kweli, Rosie!”
Joana akapangwa kwenye kikosi cha kwanza kwa ajili ya mechi ya kwanza kabisa ya ufunguzi. Kwa jitihada zote, akacheza na wakafanikiwa kuibuka na ushindi. Wenzake wakampongenza sana kwa kazi yake.
Wakiwa wanatoka uwanjani kurejea kwenye basi kurudi kambini, miongoni mwa watu waliokuwa wamesongamana kupiga picha na kuomba sahihi za wachezaji, Joana akamwona mtu yule mfanana na Moa.
Mtu huyu alikuwa amesimama mbali, ng’ambo ya barabara, akiwa amefunikwa na koti la mvua lenye kofia iliyoziba uso wake. Ni mdomo tu na kidevu ndivyo ambavyo vilionekana.
Mikono yake alikuwa ameitumbukiza ndani ya mifuko ya koti. Akiwa ametanua miguu kusimama kama vile mnara wa Eiffel.
Joana alimtazama na kuzubaa kabla hajashtuliwa asije angushwa na ngazi za gari. Alipopanda garini na kuangaza, mtu yule hakuwepo. Alitazama kila pande, lakini hakumwona yeyote.
Basi likaondoka, bado Joana akimtafakari yule mtu kiasi kwamba hakujua hata wapi basi lilipo na linapoelekea mbali na kujua tu ya kwamba wanaelekea kambini.
Furaha yake ya mchezo ilipotea kwa muda akizamia mawazoni. Alikuja kushtuliwa na makelele makali ya wenzake ndnai ya basi. Kutazama akaona basi likienda mrama, likiparamia watu na magari mengine.
Kufumba na kufumbua, basi likabiduka na kugaragara mara tatu!
Baada ya hapo Joana hakujua kilichoendelea kwani alikuwa gizani. Alipokuja kupata fahamu, alikuwa juu ya kitanda cha hospitali. Kwa nje, kupitia dirisha la kioo, wazazi wake walikuwa wanaongea na daktari.
Punde tu taarifa ya habari iliporushwa kuhusu ajali mbaya iliyowakumba, wazazi wake wakapanda ndege kwenda kumtazama. Baba alitokea Korea, mama akitokea Ubelgiji wakakutania Paris, Ufaransa.
Joana alikuwa anasikia maumivu makali ya kichwa na mbavu. Mkono wake wa kushoto ulikuwa umefungwa na bandeji ngumu. Usoni alikuwa amewekewa mashine ya kumsaidia kuhema.
Haikupita muda mrefu akaonana na mamaye ambaye alifurahi sana kumwona binti yake akiwa hai. Kitu cha kwanza Joana kuuliza, ikawa ni wenzake. Wanaendeleaje na wapo wapi.
“Wamebakia watatu tu basi zima, wamewekwa vyumba vya watu mahututi,” mama akamweleza.
Joana akaumia sana. Alianza kulia hali ambayo ikampelekea apate maumivu maradufu ya mbavu. Daktari alikuja kumtoa mama ndani ya chumba cha mgonjwa na kumtaka amwache mgonjwa apumzike.
“Anahitaji muda zaidi wa kupumzika. Naomba umpatie nafasi hiyo.”
Joana akakaa hospitalini kwa juma moja kabla hajaruhusiwa kurudi nyumbani. Ndoto zake za furaha akawa ameziacha huko Paris. Alirudi mwenyewe ingali walienda wengi.
Hata mkufu aliokuwa nao, ule aliompatia Moa, nao alikuwa ameuacha huko. Hakuuona tangu alipopata fahamu.
Basi maisha yakaendelea. Na kama ulidhani Joana alikuwa ameacha mabalaa yote baada ya kuuondoa mkufu wa Moa kifuani, basi umekosea tena sana.
Majaribu yalikuwa na njia yake yapekee kumfikia Joana.
Zikapita wiki tatu akiwa nyumbani. Wiki hizo hakuona kitu wala chochote cha kumuogofya. Ilipowadia wiki ya nne, Joana akaanza kusumbuliwa na ndoto za ajabu. Ndoto za watu waliokufa.
Ndoto za wale wote aliowaua!
Joana akawa anaona kitu usiku. Watu wakimjia toka makaburini. Wakiwa wamevalia sanda zilizochakaa na kuoza. Wakiwa na nyuso zilizoliwa na wadudu. Wakiwa na viungo vilivyokatika katika.
Usiku kwake ukawa mtihani mkubwa. Alikuwa anakurupuka mara kwa mara na kuangaza. Akawa anaona vitu vinacheza. Sauti za watu zinateta zikiyoyoma. Mlango na madirisha yakiwa wazi.
Siku nyingine alikuwa anasikia sauti za vishindo vya miguu na watu hawaoni. Ama anakuta ujumbe mezani!
Akakosa kabisa furaha. Kwani watu hao aliokuwa anawaona kila usiku, hawakuishia tu kumsumbua yeye bali na wengineo aliokuwa nao karibu.
Mara kadhaa mama yake alikuwa anakurupuka na kusema anaona kitu. Anaona watu wakizunguka ama kutembea huku na huko.
Hata baba yake aliporejea nyumbani, alisadiki kusumbuliwa na watu fulani fulani usiku.
Siku moja usiku, baba yake Joana alikurupuka baada ya kusikia sauti ya kugonga mlangoni. Ilikuwa ni majira ya saa tisa hivi usiku.
Baba akanyanyuka na kwenda kutazama akiwa kabebelea bunduki yake ndogo kwa ajili ya ulinzi. Hakukuta mtu. Akageuza uso wake huku na huko, hakuona kitu.
Basi akageuka atizame ndani anapoenda. Lah! Si ndiyo akakutana na mtu mrefu mweusi mwenye uso mweupe!
Kabla hajafanya jambo, akala kofi zito mpaka chini.
Kutazama, hamna mtu!
Akapaza sauti kumwita mlinzi ambaye alikuja upesi na kumtazama bosi wake akiwa chini. Akamuuliza mlinzi kama ameona mtu, mlinzi akatahamaki kwani alikuwa peke yake nje.
Siku nyingine, wakiwa wamelala wakasikia tena mtu akipita dirishani. Ulikuwa ni usiku mzito. Mama akamwamsha baba na kumwambia kuna mtu anapita dirishani.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Punde tu wakasikia sauti ya Joana ikilia kwanguvu! Haraka baba akanyakua bunduki yake na kukimbilia huko chumbani, nyuma akiwa na mama.
Walifika wakamkuta Joana amefumba macho, ameziba masikio anapiga makelele kuomba asiuawe.
Walipomkurupusha akasema alikuwa usingizini na kuna mtu alikuwa anamkimbiza akitaka kumuua.
"Alikuwa ameshikilia shoka kubwa. Nguo yake ilikuwa imetepeta damu na kuchafuka."
Sasa ikalazimu familia ikae kujadili hili swala maana limekuwa zito sasa na halibebeki. Ilibidi sasa watafute namna ya kujikomboa na swahibu hili ili kurejea kwenye maisha yao ya awali.
Mama akashauri wamuite mtu mwenye wadhfa kanisani aje kuwaombea na kuwatakia kheri.
Baba yake Joana ni mtu asiyeamini katika Mungu, yaani Atheists, hakuafiki hilo jambo. Hata mwanzoni alikuwa mgumu sana kuamini yale Joana alikuwa anasema mpaka pale alipoyashuhudia mwenyewe kwa macho.
Badala ya kumleta mtu toka kanisani, yeye akaonelea awalete wataalamu wa haya mambo. Yani wa haya mambo ya kiimani zaidi.
Kesho yake mapema baba yake Joana akapiga simu kuwaita wataalamu, basi kwakuwa walikuwa na miadi na watu wengine, wataalamu wakasema watafika hapo kesho kutwa.
Kwahiyo wakina Joana wakawa na siku mbili, yani usiku mmoja na wa pili, zaidi wa kuhangaika nao kabla ya kuonana na wataalamu.
Usiku wa siku hiyo vibweka vikaendelea kama kawaida. Usiku huo ni sauti za wanyama ndizo zilizokuwa zinasumbua nyumba, kila mnyama akisikika huku na huko.
Picha za watu waliokufa zilirandaranda na kudai uhai.
Siku hiyo ndiyo baba yake Joana akauawa kwa kuchomwa kisu.
Alikuwa anasikia sauti ya kitu kikivutwa kwa kuburuzwa maeneo ya koridoni. Alipotoka kwenda kutazama akakutana na taswira ya mtu aliyekuwa anatisha kwa macho ya bundi, mikono mirefu na kucha ndefu kama dubu.
Mtu huyo akamrarua rarua. Na kama haitoshi akamsindika kisu chote kifuani.
Akiwa anakata roho mtu yule akamwambia neno moja tu:
"Usithubutu."
Mama alipokuja kutazama, akamwona mtu huyo akipotea kama upepo. Akaachwa akilia kwa uchungu akimwita mumewe aliyeanza kuwa baridi kwa ufu.
Basi kutokana na shuruti za msiba, hata wale wataalamu waliotakiwa kuja wakapangiwa tena kalenda kupisha msiba ambao ulikuwa mkubwa kwa kuhudhuriwa na watu wakubwa na wazito.
Mpaka walipokuja kutengemaa ilikuwa ni karibia juma zima. Wakawatafuta tena wale wataalamu mara hii mama akiwa ndiye aliyewapigia simu.
Watalamu hawa walikuwa wanatokea Ureno. Hivyo kuja kwao haikuwa rahisi sana. Ukiachia mbali na taratibu zingine za usafiri kama unazozijua toka nchi moja kwenda nyingine.
Wakatoa miadi ya kuja kesho yake tu, wakiwa wamejitahidi sana kutafuta upenyo.
Hivyo mama na Joana wakatakiwa kusubiri masaa kadhaa tu kabla ya kuonana na wataalamu hao.
Usiku ulipowadia, Joana akiwa yupo chumbani kwake hajalala, yupo macho amejikunyata, akasikia sauti ya pupa iliyomshtua moyo!
Ilikuwa ni yowe kali ya sauti ya mama yake. Kabla hajanyanyuka, mlango wake ukafunguliwa na jirani akaingia ndani.
Jirani huyu alikuwa analala na mama yake Joana akimpa kampani kutokana na hofu ya kulala peke yake.
Alimtazama Joana kwa macho yaliyojaa hofu nzito na taharuki, akaropoka:
"Mama amekufa!"
Haraka Joana akakimbilia huko .... kweli mama alikuwa amekufa. Alikuwa amelala chini, sakafuni, akichuruza damu puani na mdomoni.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hata jirani hakuwa anajua nini kimemuua zaidi ya kusikia kishindo na kuhamaki akamwona mama amelala chini, hajitambui na hana uhai!
Hapo sasa mzunguko wa Joana ukawa umekamilika kamili. Hakubakiziwa sasa hata nguzo moja ya kuegamia.
Watu wake wote wa karibu, aliowapenda na kuwategemea wakawa wameenda ... wamekufa ... wamepotea!
Na haya ndiyo maisha Joana anayoishi mpaka sasa. Hana ndugu, rafiki wala jamaa. Amekuwa mtu wa kujitenga, mtu aliyekondeana, mtu aliyejikatia tamaa ya maisha.
Hakutaka kuishi wala kuwa karibu na yeyote yule kwa kuhofia kupoteza maisha yake na hatimaye wakaanza kumfuata nyakati za usiku. Kwani hata mama na baba yake nao wameungana, wote humtokea usiku na kumkosesha amani.
Nyuso zao zimekengeuka. Miili yao imemomonyoka. Wana macho ya kuogofya na mwendo wa wafu.
Joana amejaribu mara kadhaa kujiua lakini inashindikana. Kila anapojaribu zoezi hufeli, hushindikana.
Alijaribu kunywa sumu, kujinyonga na kujichoma kisu akaishia kupata jeraha tu akiwahishwa hospitali.
Hajui afanye nini. Amekuwa akiishi mwenyewe ndani ya jengo ambalo limeanza nalo kuwa ghofu kwa kutokupata matunzo.
Siku moja akiwa sebuleni, alishangaa akitembelewa na inspekta Westgate. Alikuwa amevalia suti yake ya kahawia na kofia ambatano.
Inspekta alimwonea huruma Joana kwa namna alivyokuwa. Ila akafurahi kumkuta hai.
"Pole sana, Joana. Najua umepitia mengi sana. Nipo tayari kukusaidia."
Joana hakujua ni namna gani inspekta anaweza kumsaidia. Alivyomwona tu, akili yake ilianza kuwaza kesi.
Ila ikawa ndivyo sivyo.
Joana akaelezea. Phillip akamwambia watu hao aliowaona huko ndipo yalipo makazi yao. Huku duniani ni vivuli tu.
Sasa watafanyaje?
Safari ya kwenda Brazil ikabidi ianze kuandaliwa. Kule ambapo agano lilipoanzia, ndipo pa kulikatia
ENDELEA
Baada ya maandalizi ya siku mbili, Joana pamoja na Phillips, Teddy na Inspekta Westgate wakawa tayari kwa ajili ya safari.
Wakachukua ndege mpaka Brazili, wakaweka makazi yao kwenye hoteli fulani ndogo malipo yakisimamiwa na Inspekta.
Wakapanga kwenda nyumbani kwa wakina Moa kwa ajili ya kutazama mambo fulani fulani ambayo Phillips na Teddy waliona ni muhimu kwenye harakati zao.
Basi ilipofika majira ya saa mbili usiku, kwa maelekezo ya Joana, wakaelekea kwa wakina Moa. Phillips na Teddy wakakagua eneo hilo kwa macho na kushuhudia watu ambao Joana aliwaona akiwa ulimwengu mwingine.
Katika mazingira hayo hayo, Joana akamwona Moa pia. Hawakuchukua muda sana, wakaondoka zao.
Lakini haya yanayoendelea, Mama Moa alikuwa ameshayafahamu. Akiwa kule ulimwengu mwingine, alimwona Joana. Na basi kwa namna moja ama nyingine akajiandaa kwa ajili ya vita.
Alijua fika Joana hakuwa peke yake. Kuna watu wapo nyuma yake.
Hata pale walipokuja nyumbani kwake kumpekua, basi alikuwa amewaona vile vile. Na kuzidi kuthibitisha kuwa kuna mipango juu yake.
Akaazimia kujipanga vema kwa ajili ya vita.
Ilipofika majira ya saa saba kuelekea usiku, Joana akiwa na kijikundi chake huko hotelini wakazima taa ndani ya chumba chao, mazingira yakaanza kuandaliwa kwa ajili ya kumsafirisha Joana kwenda ulimwengu wa pili.
Mishumaa miwili ikawashwa, na kisha Phillips na Teddy wakapulizia marashi fulani ndani ya chumba. Alafu wakawasha redio yao ndogo iliyokuwa inaimba wimbo fulani usioeleweka.
Wimbo huu ulikuwa ni wa kutetema. Mwimbaji akiwa mwanamke mwenye sauti nyembamba. Na baadae akisaidiwa kuimba na mwanaume mwenye sauti nzito.
Vyombo vilivyokuwa vinatumika ndani ya wimbo vilimezwa na sauti ya gitaa kali iliyokuwa inapuliza na kuacha.
Wimbo ulikuwa unatisha. Unasisimua ukijumlisha na mazingira yaliyokuwa yametengenezwa.
Joana akawekwa kwenye kiti, kabla hajafunga macho yake Phillips akamwambia:
"Inabidi ushinde. Inabidi urudi na roho yako duniani. Haijalishi utakachokutana nacho. Hili ni jambo la kifo na uhai. Pambana. Okoa nafsi yako na za wengine."
Kisha Joana akafunga macho. Sauti ya wimbo ikaongezwa akiachwa kwenye kiti mwenyewe.
Phillips, Teddy na Westgate wakakaa kando wakimtazama Joana kwa umakini.
Zikapita dakika nane, wimbo ule uliowekwa redioni ukabeba fikra na roho ya Joana na kuipeleka ulimwengu mwingine.
Joana akajikuta yupo nje ya mwili wake. Sauti ya wimbo redioni ikiwa imefifia, na kusikika kwa mbali.
Akawaona Teddy, Phillips na Westgate wakiwa wamekaa kitini kumtazama. Kabla hajaondoka eneo hilo, Teddy akapaza sauti yake kusema:
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Nenda nyumbani kwa kina Moa, Joana."
Joana akasikia kauli hiyo kwa mbali ikitetema masikioni mwake, basi akafuata mlango na kuufungua, akatoka zake nje.
Nje huko ambapo palikuwa giza. Taa zilizokuwa zinawaka katika ulimwengu huo, hazikuwa zinang'aa kabisa. Huu ulikuwa ni ulimwengu wa giza!
Upepo ulikuwa unavuma na kusababisha baridi. Joana akajikumbatia kujilinda.
Katika hali isiyo ya kawaida, akatembea kuelekea kwa wakina Moa, upesi akafika huko tofauti na majira yale walipoenda na usafiri.
Nyumba ya wakina Moa ilikuwa kimya na giza. Hakukuwa na taa hata moja iliyokuwa inawaka. Joana aliitazama vema na pembeni yake akaliona lile banda aliloliona kipindi kile, lile banda kubwa ambalo mama Moa alikuwa anataka kulifungua kabla hajaghairi.
Taratibu akalifuata lile banda kwa hatua zake ndogo ndogo. Kabla hajalifikia, akasikia sauti za vishindo vya miguu nyuma yake.
Kutazama, akamwona baba yake Moa. Alikuwa amevalia suti nyeusi akiwa amebebelea mnyororo mkubwa mkono wake wa kuume.
Akasikia tena sauti ya vishindo mbele yake. Na mara akamwona kaka zake Moa, wawili! Punde Moa naye akatokea kabla mama hajamalizia kwa kuibukia upande wa kushoto.
Alikuwa amevalia gauni jeusi lililokaba koo. Kofia nyeusi kichwani. Na mikono iliyofunikwa glovu za nyavu.
Kofia hii ilikuwa imefunika jicho lake moja, moja likiwa wazi. Macho yake yalikuwa yanang'aa kama kito cha dhahabu.
Mdomo wake ulikuwa mwekundu.
"Karibu, Joana," mama akasema akishika kiuno chake. "Leo itakuwa mwisho wako. Leo yote yatakoma."
Joana akaogopa sana. Kwa namna gani ataweza kupambana na watu watano? Tena wanaotisha vile?
Watu hawa hawakuwa wa kawaida. Macho yao yalikuwa ya simba. Rangi zao zilikuwa za tai, ziking'aa. Walikuwa wanamtazama kwa uchu wa kummaliza, na hata kumla nyama.
"Tukikuua katika ulimwengu huu, hutarudi tena katika ulimwengu wa walio hai. Nitaiteka roho yako na utakuwa mtumwa wangu milele!" Akasema mama Moa.
Basi kuokoa uhai wake Joana akachoropoka mbio! Mama Moa na watu wake wakasimama kumtazama katika macho ya furaha. Walimtazama kana kwamba katoto ka swala kanachojifunza mbio mbele ya umati wa simba.
Joana akakimbia sana. Usipite muda mrefu, akamwona mama yake Moa mbele yake! Mama huyo akamkandika kofi zito Joana. Akadondoka chini.
Haikujulikana wapi alitoa kisu, akamdondokea Joana, na kutaka kumchoma kisu.
Joana akaudaka mkono huo na kupambana kwa muda akizuia kisu kisimchome. Lakini mama Moa alikuwa na nguvu kumshinda, taratibu ncha ya kisu ikawa inasonga kifuani mwake.
Akaona muda si punde, atauawa. Basi akamtemea mate mama Moa machoni. Mama akapoteza mazingatio, Joana akamsukumia kando. Ila mara hii hakukimbia, akapambana kukamata kisu.
Akiwa anafanya hivyo, mara Moa, baba na kaka zake wakatokea. Wakamkamata Joana na kumpeleka nyumbani kwao. Wakamfungia mnyororo kitini.
Kisha sahani ikasogezwa mezani, sahani nyeupe iiliyokuwa imebebelea kila aina ya nyenzo. Kama haitoshi, ikaletwa na bakuli nyeusi, pamoja na kitabu kimoja kikuukuu.
Kitabu hichi kilikuwa kina jarada gumu lililoandikwa kwa maneno ya lugha ya kirumi: *MWANZO na MWISHO.*
Wakati wanaume wakiwa wamesimama, mama Moa akaketi kitabu kikiwa karibu. Bakuli akalisogezea kwa Joana aliyefungwa na minyororo.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Joana," mama akaita. "Sasa ni wakati wa kumaliza kila kitu. Kuziba mashimo yote na kutia viraka. Ni wakati wa kuufanya mwanzo uwe mwisho."
Mara mama aliponyamaza, wanaume wakadakia kwa kuimba wakinguruma.
Japokuwa Joana hakujua kilichomo ndani ya kitabu, ila alifahamu si jambo jema. Si jambo lenye kheri kwake. Na endapo likifanyika, basi atakumbwa!
Lakini atafanyaje wakati yupo ndani ya minyororo?
Kitabu kikafunguliwa. Mama Moa akatia kidole ndani ya bakuli na kisha akapakaa damu kitabuni kwenye sehemu ile aliyokuwa anataka kusoma.
Kisha akaanza kusoma. Wakati huo sauti za mngurumo za wanaume zikiendelea kuita.
Basi kadiri mama anavyosoma, Joana akaanza kupapatika. Hata ule mwili wake aliouacha kule hotelini ulikuwa unahangaika. Teddy na Phillips wakijaribu kuutuliza.
Kama dakika tatu zikapita, ikawa imebakia aya moja tu ambayo mama Moa alikuwa anamalizia kusoma.
Kila alipokuwa anamaliza aya moja, ifuatayo akawa anaipakaza damu kwa kuchovya kidole bakulini.
Basi ni Mungu, ghafla wakasikia sauti ya mtu akiita Joana huko nje. Mama Moa akaacha kusoma.
Akawatazama wanaume wale waliokuwepo hapo wakimzingira. Akawatikisia kichwa kuwapa agizo, wanaume hao wakaenda huko nje. Ila sasa ibada ikiwa imeharibika. Kwani ili itimie ilibidi hao wanaume wawepo.
Hao wanaume wakaenda huko nje na kuangaza kutafuta. Hawakuona kitu. Wakakasirika sana. Wakatazamana na kujigawa kwenda kila upande.
Huko wakazamia gizani kusaka.
Lakini sasa wakatafuta kweli pasipo kuona jambo. Ikabidi warudi kule nyumbani kurejesha taarifa kwamba hawajaona mtu. Lakini wakafika na hawakumkuta mtu. Mama hakuwepo, ila Joana bado alikuwa ndani ya minyororo!
Lakini ajabu zaidi, watu hao hawakuwa wanaweza kuongea. Isipokuwa kuonyesheana tu ishara. Basi wakapeana ishara wakatazame ndani. Huko napo wakaenda, lakini mmoja wao, ambaye ni Moa, kuna kitu akawa amegundua.
Walipofika kule chumbani akaona kuna haja ya kurejea sebuleni. Haraka akafanya hivyo na kukiendea kile kitabu. Akakipekuapekua. Muda huo Joana akiwa anamuita na kumkubusha kwamba yeye ni mpenzi wake wa enzi.
Lakini Moa hakuonekana kujali wala kusikia. Akaendelea na kazi yake ya kupekua kitabu. Na kweli, akaona kuna karatasi fulani ilikuwa imechanwa!
Akamtazama Joana na kumuuliza kwa ishara akionyeshea karatasi ile iliyochanwa. Nani kachana na yupo wapi?
Ila akiwa anahangaika na Joana ampatie majibu, akasikia sauti kubwa huko nje. Mara akatoka na kwenda huko. Akawakuta wenzake wakiwa wamemzingira Mama akiwa amelala chini. Hakuonekana kama mtu mwenye fahamu.
Walimtikisa tikisa lakini haikusaidia. Kumbe karatasi ile iliyokuwa imechanwa kwenye kile kitabu cha kilozi ndicho kilichokuwa kinampatia mamlaka na uwezo mama huyo kupata kuwepo duniani na kule walipo wafu kwa wakati mmoja.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Sasa walikuwa wamemwondoa na kumrejesha duniani kwa kuchana mkataba wake kitabuni.
Wakina Moa wakiwa hapo wamemzingira huyo mama, Phillip na Teddy wakazama ndani ya nyumba isijulikane walitokea wapi. Teddy akafuata kitabu, wakati Phillip akimfuata Joana kumfungua dhidi ya minyororo.
Teddy akafungua akipepesa huku na kule mpaka alipofikia karatasi fulani mbili ambazo zilikuwa karibia na katikati. Karatasi hizo zilikuwa zina picha ya binadamu mmoja akigawika mara mbili.
Teddy akasoma maelezo upesi, akajiridhisha. Basi akachana karatasi hizo kwa wakati mmoja na kuzigawa kwenye vipande vipande. Wakati huo wakina Moa walikuwa wameshafika mlangoni wakitaka kuingia ndani.
Ila karatasi hizo zilipochanwa, wakaanguka chini na kuwa kimya. Teddy, Phillips pamoja na Moa wakatoka ndani. Ndani ya jalada gumu la kitabu, Teddy akatoa funguo kubwa na kumkabidhi Joana.
“Twende tukafungue lile banda.”
Wakaenda huko upesi na kulifungua banda. Lakini ndani hakukuwa na mtu! Banda lilikuwa tupu likitikwa na giza.
“Joana, wale watu wote uliokuwa unawaua, walikuwa wanafungiwa humu,” Teddy akasema.
“Sasa mbona hawamo?” Joana akauliza.
“Hii ina maana kwamba agano lako lilivunjika. Siku ulipopata ajali, mkufu wako utakuwa ulikatika hivyo basi nafsi zote zilizokuwa zimeshikiliwa na roho yako iliyokuwepo huku, zikatoka kifungoni,” akasema Phillips. Na mara Teddy akaongezea.
“Ila sasa nafsi hizo zilizotoka kifungoni, zimekuwa zikikurudia kukufuata na kukudai. Na yote hayo yamewezekana kwasababu nafsi hizo zimeshikishwa kwako na damu. Damu ile uliyoimwaga kwenye ajali.”
“Sasa tunafanyaje ziache kunisumbua?” Joana akauliza kwa hofu.
“Ni lazima watu hao waitwe, na wafungiwe humu ndani maana wapo huko nje wanazurura kisha mlango ufungwe.”
Basi wakarejea ndani na kutafuta chanzo kizuri cha mwanga, kisha wakarejea karibu na banda ambalo lilikuwa limeachwa wazi. Teddy akafungua kitabu kutafuta karatasi anazotakiwa kuzisoma.
Akamwambia Joana.
“Kazi hii itakuwa ngumu. Inahitaji uvumilivu mkubwa na mazingatio. Nafsi hizo zinaweza kuja hapa na kusumbua, ila haitakiwi kusumbuka nazo. Fuata kile nitakachokuambia ufanye.”
Baada ya muda kidogo, Teddy akawa amepata mahali pa kusoma. Ila bado hakuwa na uhakika asilimia mia moja kama mahali hapo ndipo sahihi. Hivyo akamtahadharisha Joana.
“Kuna sehemu tatu na mojawapo kati ya hizo ni sahihi, kwahiyo itabidi tujaribu zote. Tuwe tayari kukabiliana na lolote litakalotokea. Tulia na usifumbue macho yako.”
Baada ya hapo Teddy akaanza kusoma sehemu ya kwanza. Wakati anaendelea kusoma, mlango wa banda ukaanza kuchezacheza kwenda mbele na nyuma. Kadiri ambavyo Teddy alikuwa anasoma, na mlango ule ukawa unacheza zaidi na zaidi!
Ikafikia mahala ukawa unajibamiza kujifunga na kujifungua. Mpaka Teddy anamaliza kusoma hakuna kitu kilichotokea.
Ikabidi wahamie sehemu ya pili. Teddy akaanza kusoma. Akamaliza sehemu yote hiyo pasipo lolote kutokea! Sasa ikawa imebakia sehemu moja tu. Sehemu ambayo Teddy akaamini ndiyo ambayo walikuwa wanaitaka.
Akaanza kusoma. Na kweli muda si mwingi, wakaanza kusikia sauti za watu toka mbali. Sauti hizo zikajongea karibu na karibu. Na mara wakajikuta wamezingira na nafsi za watu zikiwazunguka kama upepo.
Sura za watu hao ungepata kuziona kwa mbali zikikatika kama pepo. Zimeachama midomo.
Zikawajeruhi wakina Joana. Kwa kuwang’ata na kuwachana chana. Ila Teddy hakukoma kuendelea kusoma. Na pia Joana hakufumbua macho.
Lakini mpaka Teddy anamaliza kusoma. Hakuna kilichotokea. Zile nafsi zikapotea! Wakaachwa na majeraha mwilini na mafadhaiko.
“Inabidi Joana ndiyo asome,” Phillips akashauri.
“Lakini hajui hii lugha,” Teddy naye akasema.
“Hakuna namna, inabidi ajue kusoma. La sivyo hatutafanikisha hili,” Phillips akakazia uzi.
Basi ikabidi Teddy amwelekeze Joana herufi za lugha ile. Moja baada ya moja. Kwa muda wa kama dakika kumi na tano, Joana akaanza kujikongoja kusoma.
“Jitahidi. Huu mtihani inabidi uumalize wewe!” Phillips alimsisitizia.
Taratibu akaanza kusoma. Kadiri alivyokuwa anasonga mbele, akagundua lugha ile ilikuwa ni Kilatini kilichogeuzwa kushoto kwenda kulia. Sasa basi akatumia ufahamu wake kwenye lugha hiyo kusoma vema.
Ndani ya muda mfupi, zile nafsi zikaja. Zikawazunguka na kuwasumbua zaidi ya mara ya kwanza! Ziliwachanja na kuwang’ata. Zilipiga kila aina ya makelele. Ila Joana akapiga moyo konde. Akaendelea kusoma.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mpaka anamaliza, nafsi zote zikawa zimeingia ndani ya banda. Na mlango ukajifunga wenyewe. Joana akaenda kumalizia kwa kuufunga na funguo. Kisha wakachimba shimo na kuzika kitabu kile na funguo yake kabla hawajarejea duniani.
Huo ukawa ndiyo mwisho wa Joana kuteseka daima!
MWISHO
0 comments:
Post a Comment