Search This Blog

Saturday, 5 November 2022

KARATA YA BARADHULI - 1

 






IMEANDIKWA NA : INNOCENT A. NDAYANSE (ZAGALLO)



*********************************************************************************



Simulizi : Karata Ya Baradhuli

Sehemu Ya Kwanza (1)



HAIKUWA siku ya kawaida kama zilivyokuwa siku nyingine. Hii ilikuwa ni siku tofauti, siku iliyotawaliwa na ukimya wa ajabu ndani ya jumba hili la tajiri Malick Sikonge lililokuwa katika eneo la Masaki jijini Dar es Salaam. Japo kijua chenye mionzi michanga kiliipasua anga taratibu katika asubuhi hii pevu, na kuichomoza miali yake kutokea pwani ya mashariki ya Bahari ya Hindi, bado ilibaki kuwa ni asubuhi ya kipekee, asubuhi ya kukumbukwa.



Kulikuwa na sababu nzito iliyosababisha kuwe na hali hiyo ndani ya eneo hilo lenye wakazi wasiopungua kumi, ambao kwa kawaida walisababisha kuwe na pilikapilika muda wote, wakiongea kwa furaha huku milio ya ndege waliofurika bustanini wakiimba kwa namna yao na hivyo kupafanya mahali hapo pasitofautiane na paradiso.



Ndani ya chumba fulani, chumba maalum, Mzee Malick Sikonge alikuwa hoi bin taaban, akipumua kwa taabu. Kupumua huko kulikuwa kukielekea kuisainisha hati ya mwisho wa uhai wake duniani na kulifungua taratibu pazia la milango ya ahera. Alikuwa amelala kitandani, kando yake akiwepo daktari wake maalum ambaye kila baada ya dakika chache alimwinamia na kumpima hapa na pale ili kujua maendeleo ya afya yake.



Kila kitu chumbani humo kilionekana kwa sura yake. Mapambo yaliyowekwa hapa na pale yalizidi kumetameta na kuvutia zaidi wakati sura ya mgonjwa ilikuwa hoi bin taaban!



Ndiyo, hali ya Mzee Malick ilikuwa mbaya. Uso wake ulizidi kuwa mweupe na kujaa makunyanzi ya mauti. Pua yake ilizidi kuwa ndefu na kusimama kama upanga, macho yakijaa huzuni ya mtu anayeaga dunia!



Pamoja na daktari na Mzee Malick, pia kulikuwa na watu wengine. Hao ni Sharifa ambaye ndiye aliyekuwa mkewe Malick na Abdul aliyekuwa kaka yake Sharifa. Hao wote walikuwa kimya, nyuso zao zikionyesha masikitiko na mara chache, kwa kuibia, walitupiana macho.



Abdul alikuwa nadhifu, akiwa amevaa suti nyeusi iliyompendeza. Sharifa, yeye alivaa gauni zuri, jeupe lililomeremeta lakini akilichukulia kuwa ni nguo ya kawaida tu, ya kushindia nyumbani na wala si ya ‘kutokea.’ Shingoni alivaa mikufu ya dhahabu pamoja na vito vingine vya thamani mikononi.



Wakati daktari akiendelea kumpima Mzee Malick, Sharifa alimsogelea kaka yake na kunong’ona, “Anauweka usiku!”



Abdul alikunja uso na kumtazama Mzee Malick kwa makini. Alihitaji kujua kama anachokifanya daktari huyo ni kutafuta njia ya kutatua tatizo lililomkabili mgonjwa au ni kuthibitisha kama ameshafariki.



Mara daktari alinyanyuka na kuwageukia, majonzi yakionesha kuutawala usowe. Kisha kwa sauti dhaifu akasema, “Mungu mkubwa! Amemsaidia mzee wetu na sasa hali yake inazidi kuimarika.”



Sharifa na Abdul walitazamana, wakashusha pumzi ndefu. Mara Sharifa akamtazama daktari, na macho yao yalipokutana, ni Sharifa aliyekuwa mwepesi kuyaepusha macho yake. Akauinamisha uso wake huku mikono yake laini, iliyonona kihisabati ikichezacheza na mikufu iliyoizingira shingoni yake.



Akamtazama kaka yake mwenye sura ya kimaskini lakini iliyojaa uchu wa utajiri. Walipozikutanisha tena nyuso zao, wakashusha pumzi ndefu na kuketi katika kitanda kingine kilichokuwa kando ya kile alicholala Mzee Malick.



Hatimaye, Sharifa alijikaza na kumuuliza daktari, “Unadhani anaweza kupona lini?”



Lilikuwa ni swali ambalo daktari hakulitarajia, na zaidi lilimshangaza. Lakini alijitahidi kutouweka mshangao wake hadharani. Badala yake akamjibu, “Inategemea kudra za Mwenyezi Mungu. Kwa kweli maradhi yanayomsumbua ni makubwa. Madaktari na madaktari bingwa duniani bado wanahangaika kuisaka tiba halisi ya maradhi haya.



“Kwa kweli…” kufikia hapo akasita na kuinamisha uso. Yalikuwa ni maneno yaliyowarejeshea matumaini Sharifa na Abdul. Kwa mara nyingine tena wakatazamana. Mara Abdul akatikisa kichwa akiashiria kusikitika. Kisha akanyanyuka na kutoka chumbani humo. Akaenda kuketi sebuleni.



Tofauti na alivyokuwa chumbani, pale sebuleni Abdul alionekana kujawa na furaha. Tabasamu lake lilikua, likachanua na kuonekana kuwa tabasamu halisi. Uso wake wa duara ulionekana kunawiri. Macho yakaranda ndani ya kokwa zake huku nywele zikimcheza.



Akanyanyuka na kulifuata jokofu ambako alitoa chupa kubwa ya pombe kali iliyotengenezwa Scotland. Jokofu hilo lilihifadhi vinywaji vya aina mbalimbali lakini zaidi, pombe zilitawala. Ilikuwa ni kawaida kwa Mzee Malick kuhakikisha kuwa pombe hazikauki ndani ya jokofu hilo hususan pombe kali ambazo yeye alipendelea kuzinywa.



Na Abdul alikuwa mnywaji. Yeye aliianza tabia hiyo tangu alipokuwa huko Marekani alikokwenda kujaribu maisha. Unywaji wake, hatimaye aliugeuza kuwa sheria; hakulala usiku bila ya kupitisha walao tone moja la kileo. Ikitokea hivyo, huota ndoto za jinamizi.



Kwa hali hiyo, hata asubuhi hii hakuona taabu kunywa japo alikuwa hajatia kitu kingine tumboni. Alimimina nusu glasi kisha akairejesha chupa jokofuni. Akajitupa tena sofani na kuanza kunywa taratibu.



Mara Sharifa akatokea. Akasimama mbele yake. Wakatazamana. Abdul alimtazama dada yake kuanzia juu mpaka chini. Akakiri kimoyomoyo kuwa ana dada aliyejaaliwa na Mungu katika uumbaji wa sura nzuri na umbo linalovutia.



Sharifa alikuwa na umri wa miaka ishirini na minane ilhali Abdul alikuwa anapiga hodi kwenye miaka thelathini na mitano. Miaka inazidi kwenda, aliwaza. Hajaoa na hana mchumba. Zaidi, hana maisha yenye msimamo na hadhi. Yupoyupo tu! Anaishi hapo kwa heshima ya dada yake. Wabunifu wa semi za Kiswahili husema: ‘Anaishi kwa nguvu ya kiuno cha dada yake.’ Sharifa akitimuliwa lazima na yeye amfuate!



Ni maisha ambayo hakuyapenda na hakutaka yaendelee. Mwanamume mzima anaishi kwa fadhila za shemeji! Akilini mwake aliamini kuwa ipo siku atakayoondokana na mfumo huo wa maisha tegemezi. Lakini alijua fika kuwa hilo lingefanikishwa kama fikra zake na za dada yake zingetokea kuwa kweli.



*****

KATIKA miaka mitano ya kufujwa kimapenzi katika maisha ya ndoa, Mzee Malick hakuweza kulibadili jina lake katika hali ya ubaba na umama. Sharifa aliendelea kuwa Sharifa mkewe Malick, na Malick alibaki kuitwa vivyohivyo, Malick Sikonge! Hakukuwa na matunda ya ndoa ama japo uharibifu wa mimba. Lakini waliishi kama wanandoa. Na ni katika kipindi hicho cha maisha yao ndipo Malick alipoanza kusumbuliwa na maradhi haya na yale. Akatibiwa katika hospitali kubwa za Tanzania na Kenya.



Haikusaidia!



Pesa zikazungumza. Akapaa hadi Ulaya na Marekani alikoamini kuwa ndiko kuna madaktari wasioshindwa na lolote!



Haikusaidia!



Zaidi, ilibainika kuwa ana kansa ya ini, kansa iliyokwishakomaa kiasi ambacho isingewezekana tena kuahulishwa kwa kuunguzwa kwa mionzi mikali na mgonjwa akaendelea kuishi bila ya athari zozote.



Akiwa ni tajiri aliyejulikana kama bilionea, Malick Sikonge alikuwa na kiwanda cha kuunda magari huko Afrika Kusini, hoteli mbili za hadhi kubwa huko London, Uingereza na majumba ya kifahari nchini Marekani.



Pia alikuwa na mashamba ya kahawa, ngano na miwa nchini Tanzania ambako pia alifungua maduka ya kubadili fedha. Kwa ujumla alikuwa ni tajiri, lakini pamoja na pesa zake lukuki, bado ilishindikana kupata tiba ya kumaliza maradhi haya yaliyomlaza kitandani hoi bin taabani. Na, ni nani atakayekuwa msimamizi wa mali hizo kama Mungu ataamua kuitwaa roho yake?



**********



NI nani? Abdul alijiuliza swali hilo mara nyingi kwa siku kadha wa kadha zilizopita. Na hata asubuhi hii akiwa hapo sebuleni, sofani, toti kadhaa za whisky zikiwa zimeshateremka tumboni na kuishtua mishipa ya fahamu, swali hilo lilimjia tena.



Hata alipokuwa akimtazama dada yake aliyemsimamia hapo mbele, akili yake ilizama kwa tajiri Malick na mali zake.



“Vipi?” Sharifa alimuuliza na kumzindua katika fikra zake.



“Poa, tu,” alijibu. Akili yake ilikuwa ikimfikiria mtu aliyestahili kuwa mrithi wa mali hiyo kwa kile alichoamini kuwa Mzee Malick asingeweza kupona na kwamba hii hali tete iliyomkumba isingebadilika na kumletea unafuu tena.



Aliuona utajiri huo ukimnyemelea dada yake, Sharifa kwa kasi ya kimbunga. Taarifa aliyokuwa nayo ni kwamba Malick hakuwa na mtoto wala ndugu, taarifa aliyoamini kuwa ndiyo iliyomfanya dada yake akubali kuishi katika ndoa hiyo kama zuzu; akubali kuwa bwege katika ndoa hiyo kuukuu.



Ukweli ni kwamba, Sharifa hakuwa na mapenzi ya dhati kwa tajiri huyo tangu walipouanzisha uhusiano. Ni Malick aliyempenda Sharifa ilhali Sharifa hakuwa hata na chembe ya mapenzi moyoni mwake.



Pesa ni posa ya roho, pumbazo la moyo, burudani ya akili, faraja ya kiwiliwili, kato la ukata na kikubwa zaidi, pesa ni msingi wa maendeleo na ufunguo wa yote kwa mwanadamu. Huwezi kuwa na taifa lisilo na pesa, lenye dhiki na hali ngumu ya maisha halafu utarajie liwe na maendeleo.



Ni fikra za kiuwendawazimu! Abdul alijiambia kimoyomoyo.



Pesa ni zaidi ya kila kitu. Na pesa za Mzee Malick zilikuwa zikichemka kama chemchemi, zikiwashwa kutumika. Hudaiwa kuwa mpenzi hanenewi kwa midomo mitupu hali hunenenewa kwa tepe za pesa!



Kijana hata uwe mtanashati namna gani, kama huna pesa ni bure. Ni mwanamke gani au binti yupi mbichi atakayekubali kuolewa au kumvulia nguo mtu mwenye rika sawa na babu yake kama mtu huyo hana pesa za kutakata? Ni mwanamke gani atakayekuwa radhi kufanya mapenzi au kuolewa na mvulana mdogo sawa na mwanaye kama siyo nguvu ya pesa?



Ni hicho kilichomfanya Sharifa aangukie kwenye ndoa hiyo ya ‘babu.’ Na baadhi ya waliohudhuria sherehe ya ndoa yao wakashangaa kusikia eti siku hiyo Sharifa alikutwa na bikira!



Bikira!



Abdul akiwa hapo sofani alikaribia kucheka alipoukumbuka uvumi huo jinsi ulivyozagaa mitaani. Alijua kuwa dada yake aliamua kutumia mbinu za kiasili kiasi cha kumhadaa tajiri huyo mshamba wa mapenzi. Sharifa alimnasa Malick kwa ulaini kama kumsukuma mlevi aliyechuchumaa.







*****

HAIKUWA kazi kubwa kwake. Malick alikuwa mcheshi kwa kila mtu. Aliweza kuzoeana na watu wengi, vijana kwa wazee, wanawake kwa wanaume. Hivyo, hata alipokutana na Sharifa katika ukumbi fulani jijini Dar es Salaam siku ya mashindano ya kumsaka mlimbwende wa Miss Utalii ngazi ya Taifa, uliwachukua muda mfupi tu kuzoeana.



Walijikuta wakiwa katika viti vilivyopakana, kila mmoja akiwa na kinywaji chake. Kuzungumzia dosari na ubora wa mrembo mmoja baada ya mwingine ilikuwa ni sababu iliyowafanya wawe karibu. Ndipo katikati ya shindano hilo, Malick akiwa amevutiwa na uzuri wa sura na mavazi ya Sharifa akaamua kurusha ndoana. Mlengwa akanaswa!



Hata hivyo, Sharifa alijitia kuwa na aibu za kike pale Malick alipokuwa akijieleza, na aliitengeneza aibu hiyo kwa kutambua fika kuwa anazungumza na mmoja wa matajiri wakubwa jijini Dar kama siyo Tanzania nzima.



“Sidhani kama itakuwa vibaya kama usiku wa leo tutakuwa pamoja. Unasemaje?”



“Ni ghafla mno,” lilikuwa jibu la Sharifa, jibu alilolitoa huku uso kauinamisha, akifinyafinya vidole vya mikono.



“Usihofu,” Malick alisema kwa kujiamini. “Bado u binti unayepaswa kuifurahia dunia kabla umri haujakutupa. Umesema kwa sasa unaishi peke yako. Huna boy friend wa kukughasi. Kwa nini uniwekee vikwazo visivyokuwa na ulazima?”



Sharifa alibaki kimya. Sasa wote walijikuta wamesahau kulichokuwa kikiendelea jukwaani. Malick alimtazama Sharifa kwa shauku ya mapenzi huku Sharifa akiwa ameuinamisha uso.



‘Dawa ya moto ni moto,’ hatimaye Mzee Malick alisema kimoyomoyo. Akapachika mkono mfukoni na kuchomoa noti kadhaa zilizokuwa katika thamani ya dola za Marekani. Akazibandika mapajani kwa Sharifa huku akimwambia, “Za matumizi madogomadogo.”



Sharifa alipozihesabu akajua kuwa si haba. Kwa hesabu za harakaharaka alijua kuwa mara tu atakapozibadili katika pesa za Tanzania hatakosa milioni moja au zaidi kidogo. Na alipojilinganisha yeye na huyu mzee kwa umri, hakuona kuwa atatokwa jasho pale watakapoingia chumbani na kuchojoa nguo zao.



Itakuwa kazi rahisi, aliwaza.



Na ndivyo ilivyokuwa. Chumba cha hoteli moja maarufu eneo la Oysterbay kilipowalaki, kitanda kikawapokea, kilichofuata ni mateso dhidi ya Malick, mateso matamu yenye kuburudisha, kufariji na kusisimua. Sharifa alimfanyia vituko vingi tajiri huyo kiasi cha kuropoka kuwa hatakuwa radhi kumwacha.



“Na mkeo?”



“Sina mke!”



“Huna mke?!”



“ Ndiyo, sina mke. Ni wewe ndiyo utakayekuwa mke wangu.”

Sharifa hakumwamini siku hiyohiyo. Alikuja kumwamini wiki moja baadaye, na ndipo alipokubali kuolewa naye. Ikawa ni ndoa iliyoambatana na sherehe ya ‘kufa-mtu.’ Watu wakala, watu wakanywa na kusaza. Na kila chombo cha habari kikairipoti sherehe hiyo kwa jinsi ilivyofana.



Baada ya sherehe hiyo, Malick akataka kumwonyesha Sharifa kuwa yeye ni nani. Sasa wakawa ni watu wa kustarehe. Wakasafiri hadi Nairobi, Paris, Athens, Amsterdam na New York kwa ajili ya kufaidi dunia tu!



Katika kipindi hicho cha miaka miwili ya mwanzo ya ndoa yao, Sharifa alizidi kupendeza siku hadi siku. Uzuri wake ukaongezeka maradufu. Kwa wale wasanifu wa uzuri na ukamilifu wa maumbo ya mwanadamu wanaelewa ni jinsi gani uzuri wa namna hiyo ulivyo.



**********

JUA lilizidi kupanda, miali yake ikasanifiwa na bahari na kutoa nuru njema. Anga ikazidi kutakata. Pilikapilika ziliendelea kama kawaida nje ya jumba hili la Mzee Malick. Ndiyo, ni nje siyo ndani ya jumba hilo la kifahari ambamo kulikuwa kimya! Ukimya huo uliashiria taswira tata ya dimbwi la mauti.



Mzee Malick akiwa palepale kitandani huku daktari akiwa kando yake, akafumbua macho yaliyojawa na dalili zote za kukatisha tamaa. Mwili wake ulikuwa umedhoofika sana kiasi kwamba haikuwa vigumu kuzihesabu mbavu zake kuanzia ya kwanza hadi ya mwisho. Na kutokana na madevu yaliyokuwa yameshonana kidevuni mwake, tajiri Malick Sikonge hakutofautiana na mzimu.



Ndiyo, alikuwa katika hali ambayo ingeweza kumkatisha tamaa yeyote amtazamaye. Lakini japo alikuwa hoi bin taaban kimwili, hata hivyo bado akili yake ilikuwa timamu. Alikuwa na uwezo wa kufikiri. Alikuwa na uwezo wa kukumbuka yaliyopita. Kwa ujumla alikuwa timamu katika ubongo wake. Ndipo alipolikumbuka jambo moja muhimu sana alilokuwa kalifanya siku za kisogoni, jambo ambalo sasa lilionekana kuwa na umuhimu mkubwa kuliko yote.



Alikuwa amefanya kosa kubwa ambalo lilimlazimu sasa amwombe Mungu amzidishie umri wa kuishi, japo kidogo ili aweze kuliweka sawa. Akakusanya nguvu na kuita, “Karim!”



Haraka daktari, Suleyman Khalfan akamsogelea na kumgusa begani. Akamwangalia kwa makini na kujenga matumaini kuwa hakuwa katika dalili za kukata roho.



Suleyman Khalfan alikuwa ni daktari bingwa ambaye alikodiwa na tajiri Malick ili afanye kazi katika moja ya hospitali zake zilizokuwepo nchini Tanzania. Alikuwa akisimamia hospitali iliyokuwa jijini Dar es Salaam na Mzee Malick alipozidiwa na maradhi ndipo ikabidi daktari huyo aitwe kwa minajili ya kumhudumia.



Na sasa akiwa amebaki yeye na Mzee Malick tu humo chumbani, alibaki akimkodolea macho mgonjwa wake kwa mshangao. Baada ya kumpima kwa kina, akiwa ni mkongwe katika taaluma hiyo ya udaktari, alijua kuwa tajiri wake anahesabu saa kadhaa tu za kuendelea kupumua. “Hata hivyo ni maajabu ya Mungu yanayofanya adiriki kupanua kinywa,” alinong’ona kwa sauti ambayo hakuwa na hakika kuwa iliyafikia hata masikio yake mwenyewe. Kisha kwa huzuni kubwa akaongeza, “Dah! Maskini tajiri wangu!”



Akamkumbuka Sharifa. Akatoka chumbani humo na kuelekea sebuleni ambako alimkuta Sharifa kasimama akimtazama Abdul aliyekuwa sofani. Akamwashiria kwa mkono amfuate. Sharifa akashtuka na kumfuata haraka, akilini mwake akiwa na fikra za kupokea ujumbe usiopendeza.



“Vipi dokta?” alimuuliza wakati akimfuata daktari ambaye wakati huo alishageuka na kuanza kurudi kule chumbani mwa tajiri Malick.



Daktari Suleyman alisita na kumgeukia Sharifa. “Mzee amezinduka. Mola mkubwa.”



“Amezinduka?!” Sharifa alimtolea macho daktari.



“Yeah. Twende.”



Wakatoka hima wakielekea kule chumbani. Abdul naye akashtuka. Akajitoa sofani na kuwafuata. Walipoingia wakamkuta Mzee Malick akikwapua macho. Kisha kwa mara nyingine akaita, “Karim!”

Sharifa akashtuka zaidi. Akaunda tabasamu la kulazimisha. Akasogea kitandani na kumwinamia mumewe. “Laazizi, umeniita?” alimuuliza taratibu, kwa sauti nyororo ambayo mara nyingi huitumia kwa mumewe tu. Akatwaa kitambaa laini na kumfuta mumewe usoni kisha akambusu mdomoni.



Mzee Malick alifumbua tena macho na kumtazama Sharifa juu mpaka chini. Akazitazama nywele za Sharifa zilizoshiba mafuta. Sharifa, mkewe mwenye sura nzuri na macho matamu yaliyojaa haiba ya mapenzi. Sharifa, mkewe mwenye ngozi laini iburudishayo wakati inapotomaswa.



Kwa mbali akatabasamu, tabasamu lililodhihirisha kuwa halikuwa tabasamu lenye uhalisia. Daktari Suleyman na hata Sharifa wote walilibaini hilo.



“Sharifa,” Mzee Malick aliita kwa sauti iliyodhoofu.



Moyo wa Sharifa ulizidi kugonga kwa nguvu ndi! ndi! ndi! Kwa mara nyingine akamwinamia mumewe. Akambusu mikononi, usoni, mashavuni hata masikioni huku akimwemwesa: “Mume wangu mpenzi. Nipo. Nifanye nini kwa ajili yako mpenzi?”



Tajiri Malick alishusha pumzi ndefu. Akavuta harufu nzuri ya mafuta ambayo Sharifa alizipaka nywele zake zilizomeremeta. Kwa mara nyingine akatabasamu. Hakumwambia chochote mkewe, Sharifa.









Miongoni mwa watu ambao tajiri Malick aliwaamini ni kijana Karim Kisukulu. Na si kwamba alimwamini tu, bali pia alimtegemea. Karim alikuwa ni miongoni mwa wafanyakazi wa Mzee Malick, yeye akiwa ndiye msimamizi mkuu wa miradi ya tajiri huyo. Katika hali hii yenye utata mkubwa kwa tajiri huyo, mtu pekee aliyekuwa akilini mwake ni Karim.



Ni kwa thamani kubwa ya Karim iliyokuwa nafsini mwa tajiri Malick, ndiyo maana mzee huyo alimwita. Hakujua kuwa wakati anamwita, Karim mwenyewe hakuwemo chumbani humo. Badala yake akawaona daktari na Sharifa mbele yake!



Kwa muda fikra zake zikahamia kwa Sharifa. Akajikuta akitabasamu huku akiwa na mengi ambayo aliamini kuwa mtu pekee awezaye kuyafanikisha ni Karim!

Lakini muda mfupi uliopita amemwita Sharifa ambaye tayari yu kando yake, akisubiri kauli yake. Hakuwa na la kumwambia kwa wakati huo. Alimhitaji Karim!



“Karim!” kwa mara ya tatu aliita.



Sharifa akashangaa. Akamtazama mithili ya chochote kile kitishacho. Akayahamisha macho hadi kwa daktari Suleyman. “Ana nini huyu?” alimuuliza huku sasa akiwa ameshasimama, mikono kiunoni, hasira ikiwa bayana usoni pake.



Kwa muda ukimya ulitawala. Mzee Malick aliendelea kutulia palepale, alipolala chali, macho yake makali kayakodoa darini. Akahema kwa nguvu mara mbili. Akakiona kifo kikimnyemelea. Akajiapiza kimoyomoyo ‘Hakuna mtu mwingine wa kumkabidhi mirathi hii isipokuwa Karim. Nitaikabidhi kwake aisimamie kwa niaba ya mwanangu.’



Mara akayarejesha macho kwa Sharifa na daktari. Akawatazama kwa zamu. Kisha kwa sauti yake ileile iliyodhoofu, akasema, “Nataka kuzungumza na…” akasita na kuhema kwa nguvu. Akajishika kifuani kwa mkono wa kulia mithili ya aombaye msamaha.



Papohapo daktari akamsogelea na kumwinamia. “Mzee,” alimwita. “Mzee…mzee unajisikiaje sasa?”



Hakupata jibu. Mzee Malick aliendelea kujishika kifuani, macho kayakodoa darini.

Daktari akaanza kuhangaika tena. Akashika hiki na kile huku akiwa anafikiria ni kipi afanye kutokana na hii hali ya hali ya tajiri wake kuzidi kutisha.



Lakini mara Mzee Malick akaipata sauti yake. “Karim…” alisema kwa taabu. “Nataka kuzungumza na Karim peke yake…peke yake!”



Japo sauti yake ilidhoofu lakini ilikuwa thabiti na yenye msimamo.



Sharifa na Abdul walikonyezana kwa chati. Kisha, kama waliopewa amri waligeuka na kutoka. Hawakwenda mbali, walisimama koridoni, hatua chache tu kutoka chumbani mwa Mzee Malick.



“Ana kipi anachotaka kuzungumza na yule bwege Karim?” Abdul alimuuliza dada yake huku akionekana kukerwa na kauli ya Mzee Malick.



Sharifa alinyanyua mabega juu na kuyashusha huku akibibitua midomo kwa deko. Akagonganisha viganja na kuichanua mikono, akionesha kutojua chochote. Kisha, kwa ujasiri wa kulazimisha, akasema, “Hakuna chochote! Hataki tu nisikie mipango ya biashara yao. Unajua anakiamini sana kile ki-Karim! Amekigeuza kuwa kama kitoto chake cha kuzaa! Anakithamini wakati hata hamjui baba wala mama yake! Anazeeka huku akiwa hana mtoto! Na atakufa na ugumba wake!”



Uso wa Sharifa ulishabadilika. Ulikuwa mwekundu! Macho makali kama ya simba, yakizunguka-zunguka mithili ya mtu aliyepandwa na mashetani. Midomo ikawa ikimchezacheza na kubwibwituka kama amung’unyaye kaa la moto.



Wakati huo daktari alikuwa amekwishakwenda kumwita Karim. Hivyo wakati Sharifa na kaka yake wakiwa pale koridoni, Karim alikuja kasi akiitika wito wa tajiri wake.



Sharifa alipomwona, akatinga mbele yake na kumzuia. Akamtazama usoni sawia. Macho yake yenye mvuto wa kipekee yakaganda machoni mwa Karim. Macho ya wizi ambayo yalielekea kumkaribisha Karim katika jungu la mahaba.

Abdul ambaye alikuwa akiujua ubaradhuli wa dada yake tangu kabla hajaolewa, aliondoka haraka na kuelekea chumbani mwake.



Koridoni wakabaki Sharifa na Karim peke yao. Sharifa akaitua mikono yake mabegani kwa Karim huku akiendelea kumtazama kwa yale macho yake yazungumzayo mapenzi. Hakuishia hivyo alimsogelea zaidi Karim na kuizungusha mikono hiyo nyuma ya shingo.



“Karim,” alimwita kwa sauti nyororo akiendelea kumwangalia kwa namna ileile ya mahaba. Hakusubiri kuitikiwa. Akaendelea, “Unaonekana umechoka sana. Au kwa kuwa uko busy kumhangaikia mzee?”



“Hapana, sijachoka,” Karim alijibu kwa heshima ya woga, akijisikia kusisimkwa mwili kwa hii mikono laini ya Sharifa ilivyomtekenya shingoni. Akajitahidi kujinasua taratibu, kistaarabu. Akarudi nyuma taratibu huku akiyaepuka macho ya Sharifa, macho makubwa kiasi, mazuri, yenye mvuto wa mahaba, macho ambayo tayari yalishaanza kumchanganya.



Sharifa aliangaza macho koridoni na alipogundua wako peke yao, yeye na Karim tu, akamsogelea zaidi Karim na kuharakisha kufanya kile ambacho Karim hakukitarajia. Aliusogeza mdomo wake na kuugusanisha na wa Karim kisha akautoa ulimi na kuutembeza juu ya papi za mdomo wa Karim. Akaonyesha kuwa alidhamiria kuupenyeza ulimi kinywani mwa Karim. Alikuwa akihema kwa nguvu huku mkono mwingine ukiing’ang’ania shingo ya Karim.



Kwa Karim, huo ulikuwwa ni mtihani mkubwa. Akajitahidi kuunasua mdomo na kugeukia kando. Kisha akainyoosha shingo na kumtazama Sharifa usoni. Akayashuhudia macho mazuri ya kike, macho yenye kiu ya mapenzi.



Lakini ujasiri ulimjaa Karim. Akasema, “Tafadhali mama… Kwa heshima na utukufu wako naomba uniruhusu nikaitike wito wa mzee.”



Sharifa hakumwachia. Wakabaki wakitazamana, Sharifa akimtazama Karim kwa shauku ya mapenzi ilhali Karim akimtazama huku akiwa hana hata chembe ya mhemko. Kwa ujumla damu ya Karim ilikuwa baridi na badala yake ni hasira na fikra za kumshangaa Sharifa ndizo zilizomtawala.



*****



WASIWASI ulianza kumwingia Karim kiasi cha mwezi mmoja hivi uliopita, pale alipobaini kuwa Sharifa ambaye ni mke halali wa Mzee Malick ndiye mrithi halali wa mali ya mzee huyo.



Lakini ni kwa nini awe mrithi? alijiuliza. Alijiuliza hivyo mara kumbukumbu ilipomjia kichwani. Alikumbuka kuwa miezi mitatu iliyopita alitumwa mjini Arusha na mzee Malick.



“Nenda ukamtafute mwanangu,” Mzee Malick alimwambia. “Nenda… usione hivi ukadhani kuwa sijawahi kuwa na mtoto. Hapana. Nimezaa. Nimezaa na mwanamke mmoja miaka miwili iliyopita. Lakini sasa sijui huyo mwanangu ana hali gani. Nenda. Ukimpata, usimlete, lakini umwambie kuwa mimi baba yake bado niko hai namkumbuka na ninamhitaji.”



Karim alitekeleza maagizo hayo. Alikwenda Arusha ambako pia Mzee Malick alikuwa na mashamba ya ngano. Wakati Karim alipoondoka, wafanyakazi wote, hata Sharifa walijua kuwa kasafiri kikazi au kwa dharura yoyote ya kawaida.



Alikwenda, lakini safari yake haikuzaa matunda. Hakufanikiwa kumpata mtoto wa Mzee Malick. Ilikuwa ni safari ambayo ni kama vile alikuwa akicheza patapotea. Aliporudi na kumtaarifu Mzee Malick matokeo ya safari yake, bado mzee huyo hakukata tamaa.



“Naamini mwanangu yupo,” alimwambia Karim. “Nilizaa na mwanamke mmoja wa Kimbulu anayeitwa Hanifa. Tulimpa mtoto wetu jina la Ablah. Oooh, Ablah…” Akahema kwa nguvu kisha akaendelea, “Nilimwacha Hanifa ana mimba. Siku moja akanipigia simu, akasema amejifungua.Tukampa jina mtoto. Hakuongea kwa kirefu, na nilipojaribu kupiga tena ile namba yake, haikupatikana!”

Katika siku hiyo ya hatari katika maisha yake, Mzee Malick aliona ni muhimu sana kumwambia Karim juu ya binti yake. Aende tena kumsaka hukohuko Arusha!



Ndipo alipotoa amri kuwa anataka kuonana na Karim peke yake!



*****

PALE koridoni Sharifa hakumwachia Karim. Alimng’ang’ania huku akimtazama kwa namna ya kipekee, tazama iliyojaa haiba ya upendo. Kwa wakati huo alikuwa akimshangaa Karim na kujiuliza kuwa ataendelea kumwogopa Mzee Malick hadi lini? Malick mwenyewe yu hoi bin taaban kitandani, ya nini kuendelea kumhofia? 'Huu ni ulingo wangu,' aliendelea kuwaza huku mikono kaikita shingoni kwa Karim.



“Karim kipenzi changu,” aliita taratibu huku akijisuguasugua kifuani kwa Karim na kuupitisha ulimi shingoni kwake, akilambalamba kwa ari ya mapenzi. Akaongeza, “Karim, utakapomaliza shughuli zako, tafadhali njoo chumbani kwangu. Usikose. Ukifika gonga mara mbili. Nitakusubiri; sawa?”









Yalikuwa ni maneno yaliyozidi kumshangaza Karim. Damu ikamchemka kwa hofu juu ya mwanamke huyo. Hatimaye akashindwa kuidhibiti hasira iliyojikita moyoni mwake. Akamuuliza, “Hivi unathubutu vipi kusema hivyo wakati mumeo yu mahututi ndani? Huoni kama huo ni uchuro?”



Sharifa aliitoa mikono yake shingoni kwa Karim haraka. Akarudi nyuma hatua moja huku akichezeachezea mikufu ya dhahabu shingoni mwake. Akamtazama tena Karim, kwa namna ileile ya mapenzi. Zaidi, safari hii aliachia tabasamu dhaifu, tabasamu lililouweka bayana uzuri wa sura yake.



“Usiwe mpumbavu, Karim,” hatimaye alisema. “Utazidi kushangaa-shangaa mpaka lini? Unaviacha vinono viliwe na mabwege?”



Karim alitabasamu kwa mbali, lakini akiwa na dhamira ya kutolificha tabasamu hilo ambalo haukuhitajika uchunguzi kubaini kuwa lilikuwa ni tabasamu la dhihaka. Na papohapo akasema, “Mama, naomba utambue kuwa sina pupa ya mapenzi. Mapenzi siyo jambo geni kwangu. Ninayajua. Lakini kwa sasa nimeamua kutulia hadi hapo nitakapokuwa na mke.”



“Kwani mimi sistahili kuwa mkeo?”



Ni swali hilo lililomwondoa hapo Karim. Hakulijibu, badala yake aliharakisha kuendelea na safari yake, akimwacha Sharifa kaduwaa!



*****

“KIJANA wangu…” midomo myeupe, iliyokauka ilifunguka na kutamka. Karim alimtazama Mzee Malick kwa makini, akashusha pumzi ndefu, akiliona shimo la mauti likiwa kando ya tajiri wake! Hata hii sauti yake haikuwq ya matumaini. Ilikuwa ikikatisha tamaa zaidi, lakini Karim alimshukuru Mungu kwa kumkuta hai, akiwa na fahamu kiasi cha kuweza kumtambua.



Kwa Karim hii ilikuwa ni miongoni mwa siku tete maishani mwake, leo ikiwa ni zaidi ya siku zote. Na ni katika simanzi hiyo iliyomshika, ndipo alipojikuta akiwaza mengi huku kwa mbali machozi yakilenga machoni.



Alikumbuka mbali. Ndiyo, alikumbuka mara ya kwanza alipokutana na Mzee Malick, wakati huo akiwa na umri wa miaka kumi na saba, na pia akiwa ndiyo anakaribia kufanya mtihani wake wa kidato cha sita.



Shule aliyokuwa akiisoma Karim ilikuwa ikidhaminiwa na Mzee Malick, na alipogundua kuwa Karim hakuwa na baba wala mama, huku maendeleo yake darasani yakiwa mazuri kupindukia, ndipo alipomfuata Mwalimu Mkuu na kuongea naye.



“Nimevutiwa sana na ripoti ya kijana Karim,” alimwambia mwalimu. “Ni kijana mwenye juhudi kubwa na ana akili sana. Kwa kuwa ni yatima, sitamwacha. Nitahakikisha anafika mbali kimaendeleo.”



Alitekeleza ahadi yake kwa kumpeleka katika chuo ambacho zaidi ya elimu ya hisabati, pia alifundishwa kareti. Na alifanya hivyo kwa ajili ya hazina ya hadhari kwa ulinzi wa mali zake.



Kuanzia hapo Karim alimchukulia Mzee Malick kuwa ni mwajiri na mkarimu wake. Alimheshimu na kumpenda. Alimwona kama mtu pekee aliyemtegemea maishani mwake baada ya wazazi wake kufariki katika ajali ya treni huko Igandu-Msagali miaka kumi na mmoja iliyopita.



Katika asubuhi hii ya aina yake, Karim alihisi kuona na kusikia yale asiyoyapenda. Moyo wake ulikosa amani, hivyo alimtazama Mzee Malick kwa makini akitambua kuwa alipaswa kumsikiliza kwa makini na kuyatekeleza kikamilifu maagizo atakayopewa.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Hakutaka kujidanganya kuwa Mzee Malick ana dalili ya kurejea katika afya yake njema ilhali alishapewa taarifa kuwa maradhi aliyokuwanayo hayana tiba. Ni hilo lililomtia simanzi Karim kiasi cha machozi kumlenga machoni. Hata hivyo alijitahidi kuidhibiti hali hiyo, akakaza uso na kuketi kitandani kando ya Mzee Malick.



“Karim…” Mzee Malick alisema kwa sauti iliyodhoofu lakini macho yakiwa makali na kuonyesha msisitizo.



“Naam, baba!” Karim aliitika haraka.



“Nenda Arusha,” Mzee Malick alitamka kwa msisitizo, sauti yake ikiendelea kudhihirisha masaibu yaliyomwandama. Akaongeza, “Nenda Arusha ukamlete mwanangu…kamchukue mwanangu…Karim…! Kamchukue… Mlete katika nyumba hii! Nitakufa nikifurahi kama mwanangu atakuwa akiishi humu, akiishi katika nyumba hii…”



Baada ya kutamka hivyo akashusha pumzi ndefu huku akitweta. Kisha, ghafla kama aliyegusishwa waya wa umeme, akapiga ukelele, “Whisky! Whisky..!”



Haraka daktari Suleyman akakurupuka kukimbilia jokofu ambako alitoa chupa kubwa ya pombe kali na kumsogezea mdomoni. Mzee Malick alikunywa funda moja na kuhema kwa nguvu. Akapepesa macho na kutabasamu kwa mbali, akionekana kupata nafuu kwa kiwango cha wastani.



Macho yake yakazidi kung’ara. Kwa mbali paji la uso wake likatawaliwa na vitone vya jasho. “Karim!” kwa mara nyingine aliita.



“Naam, mzee wangu,” kwa sauti yas unyenyekevu, Karim aliitika.



Mzee Malick alipepesa macho, kwa jitihada akayazungusha huku na kule kama achunguzaye jambo fulani. Kisha tena akahema kwa nguvu. Akasema, “Nenda kule chumbani…” akasita. Kisha tena kama aliyezinduliwa akaongeza, “Kule kwenye chumba chenye mafaili yangu. Unanisikia vizuri?”



“Nakusikia vizuri, mzee,” Karim alijibu haraka, macho yakimtazama Mzee Malick kwa makini zaidi huku akiwa amesogeza stuli jirani zaidi na mzee huyo.



“Kule kuna faili moja lililoandikwa MR. MALICK. Ni faili la bluu. Sina faili jingine lililoandikwa hivyo juu. Lichukue, ulilete.”



Karim aliponyanyuka na kutoka, Mzee Malick alimgeukia daktari wake na kusema, “Samahani, dokta. Nina maongezi muhimu na huyu kijana wangu. Naomba akija, utupe dakika tano tu. Tafadhali.”



“Usijali, mzee,” daktari alijibu huku akinyanyuka kitini.



“Lakini usikae mbali, dokta,” Mzee Malick alimwambia. “Wewe nd’o umeshika roho yangu kwa kipindi hiki…”



“Usihofu mzee wangu,” daktari alimkata kauli. “Nitasubiri hapo koridoni. Usiwe na hofu.”



Dakika chache baadaye Karim alirejea huku akiwa na jalada mkononi. Halikuwa na nyaraka nyingi ndani yake hivyo kuonekana jepesi mkononi mwa Karim. Akavuta kiti na kuketi kisha akamkabidhi Mzee Malick hilo jalada. Mzee Malick alijitahidi kunyanyuka, akashindwa. Lakini hakushindwa kulifungua jalada hilo na kuzisoma nyaraka mbili muhimu na pekee zilizokuwa ndani humo.



Nyaraka hizo zilikuwa na maelezo yaliyohusu mirathi ya mali yake. Miaka miwili iliyopita aliamua kuandika mirathi hiyo, akitambua fika kuwa maradhi yaliyomkumba hayatamnusuru kiasi cha kuishi hata miaka miwili zaidi.



Ndipo aliposhika kalamu na karatasi na kuandika mirathi hiyo, akimtaja mwanaye, Ablah kuwa ndiye atakayerithi mali hiyo. Lakini baada ya kuandika, hakuisaini. Na hakusaini kwa sababu aliona ni mapema mno kufanya hivyo.



“Naweza kupata mtoto mwingine kwa mke wangu, Sharifa. Huyu Ablah huenda nisimwone tena.” Maneno hayo yalijirudia akilini mwake mara kwa mara, akiamini kuwa ipo siku Sharifa atanasa mimba, na miezi tisa baadaye atajifungua mtoto. Ni mtoto huyo aliyetarajiwa kurithi mali hiyo.



Lakini hakuisahau ile siku alipozungumza na Dk. Johnson Kingstone wa Hospitali ya Maryland ilioko jijini London, Uingereza na kupata taarifa isiyopendeza masikioni mwake na kuighilibu akili yake. Ilikuwa ni taarifa iliyomvunja nguvu kimwili na kiakili.



“Hutaweza kupata mtoto tena,” daktari huyo alimwambia, akitoa madai kuwa uchunguzi wa kitabibu ulionyesha kuwa mbegu zake za uzazi hazina uwezo wa kutia mimba.



Taarifa hiyo ilimsononesha maradufu Mzee Malick. Akachanganyikiwa. Ndipo alipozama katika tabia ya unywaji pombe uliokithiri. Ni pombe hizo zilizomwongezea tatizo jingine. Ini likaathirika. Likawa ni tatizo lisilopata ufumbuzi. Akajua kifo hakiko mbali.



Ni kutokana na hali tete iliyomkaabili hapo kitandani, mwili ukiwa dhaifu lakini moyo ukiwa imara, ndipo alipochukua uamuzi usiotenguliwa hata kwa mtutu wa bunduki! Hatamrithisha mtu mwingine yeyote urithi huo isipokuwa mwanae Ablah, na msimamizi mkuu atakuwa Karim!



Hakuwa radhi kumrithisha Sharifa mali hiyo kutokana na unafiki katika mapenzi yake. Alishabaini kuwa Sharifa hampendi bali anapenda mali, anaupenda utajiri ulio mbele yake. Ya nini kumrithisha mtu wa aina hiyo?



*****

“KARIM, n’ambie, unataka shi’ngapi?” Mzee Malick alimuuliza kwa msisitizo. “Nataka umtafute mwanangu Ablah hata kama itakupasa uende katika sayari nyingine! Namtaka Ablah hapa! Nikupe shi’ngapi?”



Lilikuwa ni swali gumu kwa Karim. Hakulitarajia! Kwa sekunde kadhaa aliduwaa akimtazama Mzee Malick bila ya kutamka chochote. Aliyaona macho makali ya Mzee Malick yakitangaza msisitizo katika kauli yake.



Lakini ajibu nini?









Alipomtuma Arusha mara ya kwanza, alimpa fedha za kutosha kwa ajili ya matumizi ya huko safarini. Akazunguka takriban Arusha nzima asiambulie kitu. Leo tena anamtaka kwenda hukohuko Arusha kwa suala lilelile! Na zaidi, safari hii akionesha kuwa hataki kumwona hapo hadi awe amempata Ablah. Ikibidi aizunguke dunia nzima na hata kama itamlazimu kupaa hadi mwezini huyo ni juu yake, muhimu ni kumpata Ablah!



Ablah



“Nakuuliza Karim…!” Mzee Malick alimzindua. “Ujue ninaamini kuwa mwanangu yupo. Mashetani yangu huniambia kuwa mwanangu yuko hai. Sasa namtaka! Na ni wewe ninayekutegemea kwenda kumleta hapa, ale mali ya baba yake! Sina hakika, lakini najisikia kuamini kuwa huyu baradhuli wangu, Sharifa atamtunza, na kama hatamtunza au kumpa ushirikiano, wewe upo.



“Kwanza sio binti mdogo. Ni mkubwa, atakuwa anakaribia miaka ishirini hivi. Kama angekuwa mtoto wa miaka kumi au kumi na miwili labda hapo ningekuwa na wasiwasi. Sasa tamka kianaume, sema, usiogope, unataka shi’ngapi?”



Karim alijitutumua. Akakaza misuli ya kichwa na kupiga moyo konde kulikabili jukumu lililokuwa mbele yake. Akasema, “Mzee wangu, mtihani ulionipa ni mgumu sana. Kumbuka ulishanituma kule mara ya kwanza…”



“Achana na ile safari ya kwanza,” Mzee Malick alimkata kauli. “Tunazungumzia leo, siyo jana! Nitakupa pesa uzunguke Arusha yote! N’naamini hutapata shida ya kupata picha halisi ya wapi aliko. Mama yake anaitwa Hanifa. Alikuwa anaishi na wazazi wake eneo la Majengo, lakini huenda pia akawa ameshaolewa na bwana mwingine. Huyo sina haja naye, nina haja na mwanangu!



“Baba yake Hanifa, yaani huyo mwanamke niliyezaa naye, anaitwa Sukununu. Mzee Sukununu. Ni mtu maarufu katika eneo la Makao Mapya. Ukimuuliza hata mtoto mdogo “kwa Mzee Sukununu ni wapi” umefika. Alipata umaarufu kutokana na kuongea sana, na ni mweupe kama mimi hivi lakini yeye si damu mchinganyiko. Ni mbantu halisi. Mimi kama unavyoniona, nusu Mjerumani kwa baba na nusu Mbondei kwa mama. Lakini na huyo mzee Sukununu naye sijui kama yu hai au nd’o kishatangulia kwa Mola.



“Muhimu ni kufika kwenye nyumba yake. Ukiweza kufika hapo utakuwa umepiga hatua moja kubwa kuelekea kwenye mafanikio. Hivi, pamoja na ujanja wako wote utashindwa kuivinjari Arusha ‘town’ na kuipata hata nyumba ya Mzee Sukununu?”



“Siwezi kushindwa mzee wangu. Kwa hilo usihofu.”



“Nashukuru kijana wangu,” Mzee Karim alisema huku akiachia tabasamu kubwa. “Kesho utaondoka.”



Muda mfupi baadaye Mzee Karim alimwandikia hundi yenye thamani ya shilingi milioni tano na kumkabidhi huku akimwambia, “Nakutegemea, Karim.”



“Tuombe Mungu, mzee. Sidhani kama kwa siku tatu nitashindwa kupata chochote cha maana cha kukueleza. Hakuna kinachoshindikana mbele ya pesa, na pesa ninazo.”



Yalikuwa ni maneno yaliyomtia nguvu Mzee Malick. Akazidi kujawa na matumaini.



Alfajiri ya siku iliyofuata Karim alitia moto moja ya magari yaliyofurika katika yadi ya milki ya Mzee Malick. Nissan Patrol likaingia barabarani, Karim peke yake akiwa nyuma ya usukani. Akasaga lami akielekea Arusha!



Saa tisa alasiri alikuwa akiuingia mji huo tayari kwa kuianza kazi ambayo kwa namna moja au nyingine aliichukulia kuwa haitofautiani na mchezo wa kuigiza. Alikiona giza nene mbele yake, lakini hakutaka kujikatisha tamaa. Akilini mwake aliamini kuwa ufumbuzi pekee ambao ungesaidia ni kutumia magazeti na televisheni kutangaza kuhusu kutafutwa kwa msichana huyo.



Lakini wangetangaza vipi ilhali hawakuwa na picha yake ambayo kwa kiasi kikubwa ndiyo ingekuwa ni msaada mkubwa kwao na kwa yeyote ambaye angelizingatia tangazo hilo? Hawakuwa na njia nyingine ya kufanya hivyo, ilimlazimu Karim kutii matakwa ya tajiri wake na mlezi wake, Mzee Malick.



*****

P & P Guest House eneo la Makao Mapya ndiko alipokanyagia breki yake. Akapanga chumba hapo na kuamua kuianza kazi ya kmsaka Ablah kesho yake. Ilikuwa ni kazi ngumu kwani hadi kufika saa 9 alasiri kesho yake bado alikuwa gizani, hajaambua chochote katika kazi hiyo iliyomleta hapo jijini Arusha.



Akarudi gesti na kuamua kupumzika. Hapo gesti alikaa nje na kuagiza bia ambayo aliinywa taratibu huku akiwaza ni vipi atafanikiwa kuikamilisha kazi yake. Bia hiyo ya kwanza ikaisha. Akaagiza ya pili.



Kabla hata hajaianza bia hiyo, mara kijana mmoja akamsogelea. Alikuwa ni mmoja wa wale vijana wanaozunguka mitaani wakizinadi bidhaa mbalimbali. Papohapo wazo la kumuuliza na ikibidi kumtumia zaidi kijana huyo likamjia kichwani.



Wakati huo kijana huyo alikuwa amesimama mbele yake, mkono wa kulia ukiwa umeshika mashati manne ya mikono mifupi huku wa kushoto ukiwa umeshika leso na mikanda ya suruali.



“Bei gani?” Karim alimuuliza huku akiligusa shati jeupe.



“Bei poa tu, baba’angu,” kijana alijibu huku akimpa Karim alishike. “Cheki lilivyo. Unaweza kulijaribu.”



Karim aliliweka shati hilo kiti cha pili. “Na hili la bluu?”



Kijana akampatia haraka.



“Nipe bei yako.”



“Alfu ishirini tu, baba’angu.”



“Sema bei ya kuuza.”



“Kumi na tano kwa kuwa unaniunga mawili msee wangu.”



Karim hakuwa na nia ya kununua mashati. Alikuwa na lake jambo. Hivyo alipompa kijana huyo malipo yake, akamtaka aketi.



Kijana akashangaa na kusema, “Asante mjomba. Niko kwenye biashara…”



“Us’konde,” Karim alimkata kauli. “Kuna bia yako moja. Dakika tano tu.”



Bado kijana huyo akasita na sasa akamtazama Karim kwa udadisi. Alikuwa na mwezi mzima hajatia kinywani tone la bia, achilia mbali kinywaji kingine cha asili, mbege ambayo aliinywa kwa ubavu wa rafiki zake mara moja-moja. Kinywaji pekee alichomudu kununua kilikuwa ni gongo.

“Kwa hali hii utapata wapi pesa ya bia?” mara kwa mara alidai hivyo ilipotokea rafikize wasiokunywa gongo walipombana.



Leo anakaribishwa bia!



Kiu ya bia alikuwanayo, na alihitaji vilevile kuendelea kukata mitaa akitembeza biashara yake. Aamue lipi?



Karim aliyasoma mawazo yake, akamwahi: “Kaa kidogo. Najua unawaza kuzungusha biashara. Us’konde, kuna buku tatu za kukupa tafu mitaani.”



Kijana huyo akakenua meno kidogo huku akivuta kiti na kuketi. Dakika kumi baadaye maongezi baina yao yalikuwa yamenoga. Kijana huyo akiwa na bia ya pili, tayari alikuwa ameshazungumza mengi. Swali moja, dogo tu, alilitolea maneno mia! Kwa jumla alishachangamka, na pale Karim alipomwagizia viazi mbatata kwa mayai na kumpatia shilingi 3,000 za kutumia, kijana akamwona kama Karim kama nabii kutoka mbinguni.



Ni hapo ndipo maongezi yalipoanza kubadilika. Kijana akauanza udadisi. “Aisee, umesema umekuja huku kibiashara,”



“Nd’o maana’ake.”



“Umefuata biashara gani, au umeleta biashara gani?”



Karim alicheka kidogo. Hakuwa mzoefu wa kusema uongo hivyo hata hakuweza kutunza kumbukumbu ya kile alichokisema akiwa amedanganya. Leo anaweza kukwambia, ‘nimefiwa na baba yangu mdogo’ Kesho ukimuuliza kuhusu msiba huo, ataruka kimanga na kukwambia hajafiwa na mtu wa aina hiyo.



Hivyo, hata muda huu alishindwa kubuni haraka biashara ya kumwambia. Lakini baada ya kufikiri haraka, akajua kuwa huyu kijana hataonana naye mara kwa mara. Huenda leo ndiyo mwanzo na mwisho. Akaitwaa glasi na kugugumia bia yake kwa mkupuo.



Alipoirejesha mezani, alimtazama na kumwambia, “Yupo mtu ambaye ameniambia nije kuchukua mzigo fulani nikaupeleke Dar. Ni hapo ndipo ninapohitaji msaada wako.”







Kijana huyo alikunja uso kidogo na kuwa makini. Lile tabasamu lake lililomtawala kwa muda mrefu sasa likayeyuka.



“Nikusaidie nini msee wangu?”



“Kuna mzee mmoja anaitwa Sukununu. Unamfahamu?”



“Sukununu?”



“Ndiyo.”



“Anaishi huku Makao Mapya?”





“Yeah, nimeelekezwa hukuhuku Makao Mapya.”



Kijana huyo alikunja tena uso akifikiri. Kisha akahoji, “Huyo mzee mwenyewe yukoje?”



“Mweupe, na ni mzungumzaji sana.”



Kijana akachangamka tena. Tabasamu la nguvu likachanua usoni pake. Akatikisa kichwa akiashiria kukubali. Kisha akasema, “Ahaa, namjua.”



“Safi!”



“Ndiyo, namjua. Haishi mbali kutoka hapa. Ni kama mtaa wa tatu au wa nne tu.”



Karim aliona taa ya kijani ikimwakia. Akajiona katoka ndani ya shimo refu lenye kiza kizito. Akahema kwa nguvu na kusema, “Sikuingia choo cha kike. Nilipokuona tangu mwanzo nilijua nimekutana na mtoto wa town.”



Kijana akavimba kichwa kwa sifa alizomiminiwa. Akaachia tabasamu dhaifu huku akiipeleka glasi kinywani na kunywa funda zito la bia yake. Alipoirejesha glasi mezani akasema, “Kwa kweli kwa hii kazi yangu natakiwa kuujua vizuri mji. Huwa natembea asubuhi mpaka usiku; mitaani, kwenye mabaa kama hivi na sehemu nyingine.”



“Poa,” Karim alisema. “Sasa nataka nimwone leo hii. Utanipeleka?”



“Hakuna noma mwanangu.”



Dakika kumi baadaye walikuwa wanamalizia bia zao. Wakatoka, kijana huyo akiwa ametangulia, Karim akimfuata. Mtaa wa kwanza, wa pili hatimaye wakatokea mtaa wa tatu.



“Unaiona nyumba ilee!” kijana huyo alisitisha kutembea na kunyoosha kidole cha shahada kuelekea nyumba iliyokuwa na miti miwili mbele. Miti hiyo iliongeza uzuri wa eneo hilo kutokana na kutengeneza matawi mazito yaliyounda kivuli cha kuburudisha.



Haikuwa nyumba ya kifahari lakini ilistahili kuitwa nyumba bora. Hilo lilijidhihirisha kwa nje. Madirisha mawili makubwa, mlango madhubuti na ukuta uliong’arishwa kwa rangi ya bluu vilikuwa ni vigezo vilivyochangia kuifanya nyumba hiyo ionekanae nadhifu mtaani miongoni mwa nyumba nyingine nadhifu.



Karim aliitika kwa kutikisa kichwa. Kisha akaingiza tena mkono mfukoni na kuchomoa noti ya shilingi 1,000. Akampatia kijana huyo huku akimwambia, “Nakushukuru sana. Na sasa nadhani tuachane. Lakini najua tutaonana tena. Bado nitakuwepo mjini hapa kwa siku nyingi. Kesho ukiwa na chansi taimu kama hizi pitia pale gesti, utanikuta.”



“Poa, mwana.”



Waliachana, kijana akigeuza njia na kuendelea na mihangaiko yake ilhali Karim akifuata maelekezo aliyopewa.



*****



MZEE Sukununu alikuwa ameketi sabuleni kwake katika kiti cha kivivu akisikiliza redio. Ndani ya nyumba hiyo aliishi yeye, mkewe na mjukuu wao, Ablah. Mzee Sukununu aliyekuwa akipiga hodi umri wa miaka sabini, jioni hii alikuwa akimsubiri mkewe aliyekuwa amekwenda kumnunulia mbege.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Akiwa amezama kwenye taarifa ya habari iliyotangazwa na kituo fulani cha nje ya bara la Afrika, mara akasikia mlango ukigongwa. Akashtuka na kupunguza sauti ili asikie vizuri. Hakuyaamini sana masikio yake, na hakutarajia kuwa mkewe angeweza kubisha hodi.



Mlango ukagongwa tena.



“Karibu,” alijibu bila ya kunyanyuka kitini. Akabaki akiukodolea macho mlango. Mara kitasa kikazungushwa. Mlango ukafunguliwa. Akaingia mtu ambaye Mzee Sukununu hakumfahamu. Akamkodolea macho kwa makini zaidi. Hatimaye akasema, “Karibu kijana…karibu sana.”



“Asante, babu,” mgeni alijibu huku akikifuata kiti kilichokuwa jirani na Mzee Sukununu na kuketi. Kisha akampa mkono: “Shikamoo.”



“Marahaba, mjukuu wangu. Karibu sana.”



Dakika chache baadaye ndipo Mzee Sukununu alipojua kuwa huyu mgeni anaitwa Karim na kwamba ametoka jijini Dar es Salaam na kutaja madhumni ya ujio wake.



“Nimekuelewa vizuri, mjukuu wangu,” Mzee Sukununu alisema. “Umefanya vizuri kuja. Lakini bibi yako katoka kidogo, na ametoka na huyo mjukuu wake. Suala lako ni vizuri ukizungumza na yeye akiwepo na zaidi ni kwamba, yeye anastahili zaidi katika hoja hiyo. Tumsubiri aje, tuzungumze vizuri.”



Haukupita muda mrefu mara mkewe Mzee Sukununu aliingia akifuatana na Ablah.



Ablah alikuwa bado binti mbichi aliyekuwa na umri wa miaka ishirini. Alionekana yu binti mcheshi na mweledi tofauti na Karim alivyotarajia. Na alifurahi kupata taarifa kuhusu baba yake lakini pia akawa na huzuni kuambiwa kuwa baba yake huyo anaumwa. Hata bibi yake alionekana kusononeshwa na taarifa hiyo.



“Kwa hiyo ulikuwa unatakaje, mjukuu wangu?” hatimaye bibi huyo alimuuliza Karim.



“Kwanza ilikuwa ni kumfahamau na kumjulia hali huyo Ablah,” Karim alijibu. “La pili ni kuwafahamisheni kuwa Mzee Malick anataka huyu mwanae ndiye akabidhiwe urithi.”



“Kha!” bibi alishangaa. “Hayu mjukuu wangu ataweza? Atawezaje kuimiliki mali ambayo hata haijui? Na huko Dar hata hajawahi kufika! Kwani huyo baba yake hana watoto wengine?”



Karim alitabasamu kidogo kisha akajibu, “Hana mtoto mwengine zaidi ya Ablah! Ana mke, lakini huyo mkewe ana tabia mbaya sana na hajawahi hata kumzalia mtoto! Aliniambia kuwa hayuko radhi kumkabidhi mali yake huyo mkewe isipokuwa huyu mwanae.”



Babu na bibi yake Ablah walibaki vinywa wazi. Leo mjukuu wao kafuatwa kwa ajili ya kwenda Dar kurithi mali ya tajiri Malick! Ni kweli au kiinimacho? Hawakuamini. Kwa muda ukimya ukatawala sebuleni humo. Kisha bibi akatikisa kichwa na kuinamisha uso kwa masikitiko. Mara akayainua macho na kuwatazama kwa zamu Ablah, Karim na Mzee Sukununu.



Kisha akayatua macho kwa Karim. Akamtazama kwa makini na kusema, “Mjukuu wangu, umemkuta Ablah. Mimi sina pingamizi. Na laiti kama mama yake angelikuwepo labda naye angefaidi matunda ya kuzaa. Maskini mwanangu!”



Kufikia hapo aliinamisha tena uso na kuikusanya kanga yake, akajifuta machozi yaliyoanza kujaa machoni.



Alimkumbuka mwanaye, Hanifa!



*****



KATIKA uhusiano wa mapenzi kati ya Mzee Malick na Hanifa ilitokea Hanifa akanasa mimba. Na kwa kuwa ilikuwa ni ukiukwaji wa mila na desturi kwa kabila lao la Kimbulu kwa mwanamke kupata mimba nje ya ndoa, Hanifa alitengwa na jamii. Akajikuta katika hali ngumu kimaisha. Mimba ikamtesa kwa kiasi kikubwa. Akajiona kama ni mtu aliyezaliwa kwa ajili ya kuteseka. Huduma zote muhimu anazopaswa kupata mjamzito, Hanifa hakuzipata kwa kiwango kilichostahili na kwa wakati mwafaka.



Kwa jumla aliiona dunia imemgeuka, Mungu amempa kisogo. Hata hivyo alivumilia, akimhurumia kiumbe aliye tumboni na kumwomba Mungu ajifungue salama.



Ilipofika siku aliyoisubiri, alijifungua mtoto wa kike, mtoto ambaye hata mwendawazimu angegundua kuwa ni chotara. Hakutofautiana na baba yake! Hanifa akampigia simu Mzee Malick na kumtaarifu kwa kifupi juu ya uzazi huo.





Wakakubaliana mtoto aitwe Ablah. Ikawa hivyo. Akaitwa Ablah bint Malick.



Lakini siku saba baadaye, katika hali iliyowashangaza wazazi wake na hata majirani, Hanifa alikunywa sumu na kufariki, akiacha ujumbe kuwa amechukua hatua hiyo ili kuondokana na adha anayokumbana nayo duniani. Ablah akabaki chini ya matunzo ya babu na bibi yake.



Mzee Sukununu na mkewe walihakikisha mjukuu wao anapata elimu. Ndiyo, Ablah alisoma elimu ya msingi na akajaaliwa kuchaguliwa kuingia sekondari na hadi siku hii Karim alipokuwa humo ndani, Ablah alikuwa na miezi miwili miwili tangu alipofanya mtihani wa mwisho wa kidato cha sita.



*****



KARIM alisimuliwa kwa tuo historia ya maisha ya Ablah ya tangu mimba. Sasa akawa na picha kamili. Akashusha pumzi ndefu huku akimtazama Ablah kwa makini. Akamwona jinsi alivyo msichana anayejiamini katika maneno na macho yake.



Kwa siku mbili alizokaa hapo, aliweza kuzungumza na Ablah kwa kirefu na wakakubaliana kuwa Malick arudi Dar es Salaam na kumtaarifu Mzee Malick kuwa Ablah yu hai na ana afya njema, lakini amhakikishie kuwa hatapata msukosuko wowote kutoka kwa huyo ‘mama’ mwingine.



“Nakuhakikishia hatakusumbua, Ablah,” Karim alimwambia kwa msisitizo. “Tutakulinda. Wewe nd’o mwenye haki, nd’o mwenye mali!Yule mkewe hana haki yoyote!”



“Hapana, sikubali,” Ablah alikaza uzi. “We nenda kwanza urekebishe mambo, Karim. Mzee ni tajiri, na kama afya yake ina utata, basi kaa ukijua kuwa watu wengi wanaikodolea macho mali yake! Wataniua! Wataniua, Karim!”



“Hakuui mtu!” Karim naye alisisitiza.



Walizungumza kwa muda mrefu, wakipingana katika hoja hiyo, na hatimaye Karim aliinua mikono. Akakubali kurudi Dar bila ya Ablah.









*****

“MASKINI binti yangu!” Mzee Malick alibgwata siku Karim aliporejea na kumpa taarifa ya kumwona Ablah.



Japo Mzee Malick bado alikuwa hajiwezi, lakini ghafla macho yake yaling’ara, akawa kama mtu aliyepona. Tabasamu likaupamba uso wake. Taarifa aliyopewa na Karim ikamtia faraja kubwa. “Kwa nini hukuja naye?” alimuuliza huku kamkazia macho.



“Ningekuja naye, lakini imeshindikana, mzee.”



“Amekataa?!”



“Hapana, hajakataa…”



“Ila?”



Ni hapo ndipo Karim alipomweleza kinagaubaga sababu iliyomfanya asije na Ablah.



“Maskini mwanangu,” Mzee Malick aliomboleza. “Anaogopa nini? Kwani Karim utashindwa kuwa bega kwa bega na mwanangu kuhakikisha hadhuriki?”



“Sitashindwa, mzee. Lakini nina wazo moja kwako.”



Mzee Malick alishtuka kidogo. Akapepesa macho na kuendelea kumtazama Karim, safari hii kwa mkazo zaidi.



“Wazo gani?” hatimaye alimuuliza.



“Ni vyema umweleze habari hii, mama yetu, Sharifa,” Karim alijibu. “Sidhani kama kuna haja ya kuendelea kumficha. Ni vizuri kuliweka wazi jambo hili kwake ingawa ukweli ni kwamba litamshtua sana. Tusijali kushtuka kwake. Tusijali kama atakasirika au atafurahi. Vyovyote vile atakavyopokea, ieleweke tu kuwa ni muhimu alijue! Ni muhimu aambiwe!”



Mzee Malick alishusha pumzi ndefu na kuyatupa macho darini. Akayatuliza huko kwa muda mfupi kisha akayarejesha kwa Karim. “Ni kweli,” hatimaye alisema kwa utulivu.



Akaendelea, “Kwa kuwa sasa najua kila kitu kimekamilika, basi hakuna haja tena ya kuwa msiri. Najua yupo mwanangu! Yupo Ablah ambaye ndiye mrithi halali wa mali zangu! Na hili lazima mke wangu aambiwe! Ndiyo, lazima aujue ukweli huu!”



Akaachia tabasamau dhaifu na kusema, “Karim, wewe ni tegemeo langu. Umefanya kazi nzuri sana. Lakini bado ninakuhitaji, na nitaendelea kukuhitaji hadi mwisho wa maisha yangu. Naamini hata mzimu wangu utakuwa unakuhitaji, mimi nikiwa nimeshaiacha dunia. Na sasa nataka kufanya jambo jingine muhimu kabla sijaiacha dunia hii. Kalete kitabu cha hundi.”



Karim alitoka na kwenda katika ofisi iliyokuwa ikitumiwa na Mzee Malick. Huko alifungua saraka moja na kutoa kitabu cha hundi. Akarudi kule chumbani na kumkabidhi Mzee Malick.



“Siwezi kuandika,” Mzee Malick alimwambia. “Andika malipo ya shingi milioni hamsini kwa jina la Sharifa Abdulrahman. Ukimaliza nipe niisaini.”





Baada ya zoezi hilo kukamilika, Mzee Malick akamwambia Karim aandike taarifa kuwa mali yote ya Mzee Malick itakuwa ni urithi wa mwanaye, Ablah, chini ya uangalizi wa Karim na kwamba hakuna mtu yeyote mwingine atakayekuwa na mamlaka juu ya mali hiyo.



Kazi hiyo ilifanywa na Karim kwa kuichapa kwenye kompyuta na baada ya kuifyatua, karatasi ilisomeka:



MIMI MALICK SIKONGE, NIKIWA NA AKILI TIMAMU, SIJALEWA WALA KULAZIMISHWA NA MTU, NIMEMKABIDHI MALI YANGU YOTE, MWANANGU ABLAH, AMBAYE NDIYE MRITHI PEKEE. PIA NIMEMKABIDHI HUNDI YA SHILINGI MILIONI HAMSINI (SHS 50,000,000) MKE WANGU SHARIFA ABDULRAHMAN NA KWA MALIPO HAYO NI KWAMBA HATAHUSIKA KWA NAMNA YOYOTE NA MALI NYINGINE NILIYOIACHA. NA HATAKUWA NA HAKI YA KUINGILIA CHOCHOTE KUHUSIANA NA MALI HII BILA IDHINI YA ABLAH.



AIDHA, MFANYAKAZI WANGU, KARIM NDIYE ATAKAYEKUWA BEGA KWA BEGA NA ABLAH NA ATAKUWA MSIMAMIZI MKUU CHINI YA ABLAH.



Mzee Malick aliyasoma maandishi hayo na japo alikuwa dhaifu hata hivyo kwa jitihada aliamka na kusaini huku akiserma, “Mambo haya yalipaswa kufanywa chini ya mwanasheria lakini aaah, Mungu yupo. Naamini hakuna litakaloharibika, na hatuna muda zaidi. Au unasemaje?”



Karim alinyanyua mabega na kuyashusha. Kisha akasema, “Kwa kweli mzee hata mimi naamini kuwa Mungu atakuwa pamoja nasi katika uamuzi huu. Hakuna kitakachoharibika. Na kwani ni nani mwenye mali kama siyo wewe? Na ni wewe vilevile mwenye mamlaka ya kuamua nani arithishwe mali yako.”



“Yeah. Na ni nina jambo jingine moja. Ni muhimu pia.”



Ukimya ukapita, wakitazamana. Karim akawa na tashwishi kufuatia kauli hiyo. Akajiweka vizuri katika stuli hii aliyokalia. Akazidi kumtazama Mzee Malick kwa makini.



“Karim,” Mzee Malick aliita kwa sauti yake ileile iliyodhoofu.



“Ndiyo, mzee,” Karim aliitika haraka.



“Kwa kuwa wewe na Ablah mtabahi mkiwa yatima, kwa nini nisiwaoze? Ni vizuri Ablah awe mkeo badala ya kuchukuliwa na jitu nisilolijua. Kwa kweli nitafarijika sana kama nitakuwa nikijua kuwa nitakufa huku nikimwacha mwanangu akiwa na mchumba wa maana au kaolewa na kijana wangu nimpendaye. Unasemaje Karim?”



Ulikuwa ni mtihani mgumu kwa Karim. Kwa muda ukimya ukatawala, Karim akiyatafahari maneno hayo ya mzee wake. Akajenga imani kuwa kauli yoyote atakayotoa, ambayo itapingana na pendekezo hilo, kwa vyovyote lazima ingemwathiri mzee Malick kwa kiasi kikubwa. Huenda ikawa ni sababu itakayoharakisha kifo chake.



Atoe jibu gani? alijiuliza. Akahema kwa nguvu kiasi cha kumzindua Mzee Malick ambaye alimtazama kwa macho makali zaidi. “Nakusubiri mwanangu,” Mzee Malick alisema.



Karim alishusha pumzi ndefu, akapitisha viganja vya mikono usoni mithili ya apangusaye vumbi, jasho au chochote kile.





Kisha kwa sauti ya unyenyekevu, akasema, “Mzee wangu, nimekua, nikalelewa na wewe hadi kufikia sasa nikiwa ni kijana kamili. Nimepata elimu kwa nguvu yako. Sijui nikushukuru vipi. Kwa kifupi naomba utambue kuwa nafsi yangu inakuchukulia wewe kama baba yangu mzazi. Tangu nilipoweza kuwa na akili ya utambuzi, nilijikuta nalelewa katika kituo cha watoto yatima. Sijawahi kumwona baba yangu mzazi. Naamini Mungu amenipa wewe kuwa ni mlezi na mzazi wangu pekee hapa duniani.”



Alipofikia hapo akahema kwa nguvu na kuyaepuka macho ya Mzee Malick yaliyokuwa yakimtazama kwa makini. Ilikuwa dhahiri Mzee Malick aliyahamishia masikio na akili yake katika maelezo ya Karim.



“Lakini baba,” Karim aliendelea. “Hili suala la kunioza Ablah linaniwia vigumu. Namwona Ablah kama dada yangu wa toka-nitoke. Iweje leo awe mchumba wangu na hatimaye awe mke?”



Kwa mara ya kwanza katika siku hiyo, Mzee Malick alicheka, tendo lililomchanganya Karim. Hakuwa na kumbukumbu sahihi ni lini alimwona Mzee Malick akicheka kicheko halisi katika miezi miwili iliyopita. Tangu maradhi haya yamzidie kiasi cha kumlaza kitandani kutwa, kucha, haikuwahi kutokea akacheka, zaidi alitabasamu tu, tabasamu ambalo wakati fulani lilikuwa la faraja na wakati mwingine lilikuwa la huzuni.



Mara Mzee Malick alikikata kicheko chake. Akasema, “Karim, mwanangu, una akili sana. Nimekubali kuwa wewe ni kijana mwenye akili ya kipekee na uwezo wa kufikiri kwa kiwango cha juu. Ninakupenda na nitaendelea kukupenda. Uyasemayo yana mnana kubwa sana. Lakini napenda utambue kuwa ukweli utabaki palepale! Kwamba mimi ni baba yako mlezi, na nitabaki kuwa mlezi wako tu na siyo baba yako mzazi.



“Hata hivyo, mimi pia nakuchukulia kama mwanangu wa kuzaa. Lakini bado hilo haliwezi kuuacha ukweli kuwa ulizaliwa na mwanamume mwingine asiyekuwa mimi. Kwa hali hiyo, ninachohitaji ni kuukuza ukoo. Wewe ni sehemu ya ukoo na ni sehemu ya familia yangu. Sitaki utoke nje ya familia hii.



“Umechangia kwa kiasi kikubwa kuhakikisha mali yangu haipukutiki. Unapaswa kula matunda ya kazi yako! Na matunda yenyewe ni kwa kumuoa Ablah, muwe bega kwa bega katika kuendesha miradi hii. Itakuwa ni mali yako. Itakuwa ni mali ya Ablah. Itakuwa ni mali yenu! Karim, bado niko palepale! Wewe ni sehemu ya familia. Unaniahidi nini?”



Ulikuwa ni msumari wa mwisho. Moyo wa Karim, moyo iliokuwa mgumu, sasa ulitepeta, ukapondeka. Kwa upole na heshima akasema, “Baba, niko radhi. Nitatii lolote utakalo baba yangu.”



“Unatamka kutoka moyoni?”



“Kutoka rohoni, baba yangu.”



“Vizuri, kijana wangu,” Mzee Malick alisema huku akitikisa kichwa akiashiria kukubali. “Sasa,” aliendelea. “Nenda Arusha. Nenda ukamlete mwanangu. Nategemea Mungu ataniweka hai nimwone.”



“Lakini mzee,” Karim alisema. “Nadhani sasa ni wakati mwafaka wa kumweleza mkeo kuhusu hili kabla sijaenda huko Arusha. Na, ninadhani pia ni vyema hilo lifanyike sasa hivi.”



“Limekubalika.”



Ndipo daktari alipoitwa na kuagizwa kumwita Sharifa









*****

SHARIFA aliingia chumbani humo akiwa amebadilika. Awali, tangu jua lilipochipuka angani alikuwa amevaa gauni jeupe, lakini sasa alikuwa ametinga gauni jeusi lenye tarizi ya kumetameta iliyomfanya apendeze maradufu. Hakutofautiana na malaika aliyeshuka kutoka mbinguni, akiwa amekuja kwa kazi moja tu; kuirejesha afya ya tajiri Malick iliyotetereka na inayotishia maisha yake.



Karim alimtazama kwa chati, akikumbuka bughudha aliyompa ile siku ambayo Mzee Malick alimtuma kwenda Arusha kwa mara ya pili. Akakumbuka jinsi alivyomkumbatia na kulazimisha busu la kinywa. Ni mwanamke mwenye akili timamu? Alijiuliza huku akiendelea kumtazama.



Sharifa alikuwa akinukia kwa manukato ghali aliyojipulizia. Uso wake ulijaa bashasha, na kamwe hakuonekana kuwa mwenye majonzi kufuatia hali hii ya mumewe. Ni chizi? Mumewe yu hoi kitandani, sasa yapata mwezi mzima, lakini Sharifa haonyeshi kuwa hali hiyo inamuumiza kwa namna yoyote ile! Ana akili au ni punguani? Kwa mara nyingine Karim alijiuliza kimoyomoyo.



Akawaza ni kwa namna gani Sharifa ataupokea ujumbe uliokuwa ukimsubiri. Kwamba, mtoto wa Mzee Malick yu hai na anatarajiwa kuwa hapo siku chache zijazo. Akilini mwake alijua kuwa ujumbe huo utazua jambo. Akaamua kutulia ili aone kitakachojiri.



Sharifa alisogea taratibu kitandani kwa Mzee Malick, akitembea kwa madaha mithili ya mlimbwende anayetamba jukwaani akisaka taji. Alipokifikia kitanda, alimwinamia kwa heshima na kumuuliza, “Nimekuja mume wangu mpenzi, nimekuja laazizi. Nipo kwa ajili yako…nikufanyie nini mpenzi?”



Mzee Malick alimtazama kwa macho makali, macho yenye ujasiri lakini yaliyoonyesha tamati ya uhai wake. Kisha, kwa sauti kavu, kama isiyo yake, alimwambia, “Umtunze mwanangu. Nakuomba sana, Sharifa wangu. Nakusihi umlee binti yangu, Ablah.”



Yalikuwa ni maneno ambayo Sharifa hakuyatarajia. Yalimwingia na kumkatakata maini kiasi cha kumfanya ahisi roho ikimtoka. Kijasho kikamtiririka usoni! Uso ulibadilika na kuwa mwekundu zaidi, mishipa ya damu ikamsimama! Hata macho yake mazuri yalibadilika na kuwa kama ya shetani.



Alitisha, akasikitisha!



“Mwanae?! Binti yake!” Sharifa alibwata akimgeukia Karim kama anayesubiri jibu kutoka kwake. Kisha akaongeza, “Mwanae wa wapi? Wa wapi?! Ana maana gani huyu mzee?”



Karim hakutishwa na sauti hiyo kali wala hakubabaishwa na maneno hayo. Badala ya kuhamaki, alitabasamu na kumjibu kwa upole, “Ni habari ndefu inayohitaji utulivu kuielezea. Huna haja ya kupaniki mama. Tulia…”



“Hapana! N’ajua huyu mzee hana mtoto!” Sharifa aliwaka.



Sauti yake iligonga dari na kusambaa chumba chote. Ikawa mfano wa radi hafifu. Huku machozi yakimtoka, aliongeza, “Haiwezekani! Hana…Hana mtoto! Hana mtoto! Hana!”



Zogo hilo lilimfanya daktari aliyekuwa amepisha mazungumzo hayo arudi haraka kujua kulikoni. Macho yake na ya Karim yakagongana. Ikawa ni kama vile Karim alihitaji msaada wa daktari huyo. Lakini Sharifa alionesha kuwa hata angeambiwa vipi, hata angeeleweshwa vipi, asingeambilika wala asingeelewa. Kwa vyovyote vile, alikwishashtuka kuwa ametupwa nje ya urithi wa mali ya Mzee Malick.



“Kuna tatizo gani?” daktari alimuuliza Karim.



“Ni kuhusu mtoto wa mzee,” Karim aliliweka suala hilo bayana. “Mama yetu hataki kusikia kuwa mzee ana mtoto aliye njiani, akija. Kwa ujumla hakubaliani na kauli kuwa Mzee ana mtoto.”



“Hana mtoto!” Sharifa aliendelea kubwata. “Hana! Msinifanye mie chizi! Hapa ni mpaka kieleweke! Msiniletee mashairi yasiyo na vina wala mizani! Nyoo! Hafanywi mtu bwege hapa!”



“Mama tulia!” daktari alifoka. “Mzee anaumwa, halafu wewe unaaanza kupiga kelele ovyo! Unataka tukuelewe vipi?”



“Mnielewe vipi?” Sharifa alimgeukia daktari na kumtazama kama atazamaye kinyesi. “Kwani mnataka mnielewe vipi? Ok, sasa nawaambia hivi nyie vibaraka wa huyu kibabu…mnielewe mnavyoona nyie…vyovyote vile!”



“Ok, Karim,” sasa daktari alikuwa mkali. “Nakijua mnachokizungumza. Sasa umweleze mama yetu habari hiyo kwa tuo, aelewe. Na akishindwa kuelewa basi atalazimishwa kuelewa. Hakuna haja ya kuzua kelele zisizo za lazima.”



Mara akamgeukia Sharifa na kumwamuru: “Mama kakae pale!” akamwonesha kiti kilichokuwa pembezoni mwa mlango.



Sharifa alishindwa kukaidi. Macho ya daktari ambayo hayakutofautiana na ya simba mwenye njaa yalitisha kumfanya asalimu amri.



Karim akatwaa ukanda. Akazungumza kwa kirefu, akiichakatua historia ya Mzee Malick kuhusu mwanamke aliyezaa naye. Akasema kuwa Mzee Malick alikuwa ameihifashi siri hiyo kwa sababu, kwanza; alitarajia kuwa Sharifa angemzalia mtoto lakini bahati mbaya haikutokea hivyo, na Mzee Malick hakupenda kumbughudhi mkewe kuhusu hilo. Alimpenda!



Aidha, Mzee Malick alitambua fika kuwa endapo angeliweka bayana mapema suala hilo la mtoto wake kungekuwa na uwezekano wa Sharifa kumsaka na kumfanyia jambo lolote bata.



“Kha! Kwa nini nifanye hivyo?” Sharifa alizuka tena. “Yaani mmenichukulia kuwa mimi nina roho mbaya kiasi hicho!”



“Ndiyo una roho mbaya mke wengu?” Mzee Malick alijikakamua kusema. “Nimeishi na wewe kwa muda mrefu. Ninakujua na ninakufahamu vizuri. Nakufahamu ndani na nje, Sharifa! Umekuwa ukiishi na mimi kwa kuwa nina mali…Bisha!”



“Mimi!” Sharifa akawaka tena. Akasimama na kujishika kiuno. “Yaani leo mume wangu unanikana ivi-ivi! Unaniletea tungo za kwamba eti una mtoto! Mtoto huyo umemwokota wapi? Umemwiba wapi?”



“Mama!” Daktari aliingilia tena kati. “Jitahidi kuwa na kauli za staha. Tunza ulimi wako! Sote hapa ni watu wazima wenye akili timamu. Tunapaswa kuzungumza kwa staha na kupata ufumbuzi wa suala hili. Siyo kubwata ovyo kama walevi! Tulia! Kinachofuata sasa ni kauli ya mzee.”



“Hapana!” Sharifa alipinga huku kamkazia macho daktari. Sasa hakumwogopa tena daktari kama mwanzo. Alishaamua liwalo na liwe, lazina aipiganie haki yake kwa namna yoyote.



“Nasema, hapana!” aliongeza. “Mimi ni mke wa ndoa wa Mzee Malick! Nina haki ya kuzungumza kile ambacho naona kina utata…”



“Ok, zungumza!” daktari alimkata kauli kwa hasira.



“Sheria ya ndoa hairuhusu wala kuhalalisha mtoto haramu kuwa mrithi,” Sharifa alisema kwa msisitizo. “Na kwanza sikioni kinachosumbua vichwa hapa. Mzee Malick hana mtoto…”



Alisita na kuanza kulia kwa sauti. Akapiga ngumi ukutani mara kadhaa huku akiendelea kulia.



Karim na daktari walifadhaika. Wakauona uzito wa jambo hilo unavyozidi kuongezeka. Daktari, yeye alizidi kukereka. Ni mtu mpole, mstaarabu na mwenye kupenda kuitumia busara katika kupata ufumbuzi wa tatizo lolote. Lakini, asubuhi hii alihisi kushindwa kuvumilia. Akatamani kumzaba Sharifa makofi mawili, matatu ya kumrejeshea akili. Hujiwa na hali ya kuchukua uamuzi huo pale hasira zinapomzidia, na aamuapo kufanya ‘kweli’, huwa mwepesi wa utekelezaji.



Chumbani humu, aligundua kuwa hatua hiyo huenda ikamwongezea athari mzee Malick na labda kusababisha litokee lile wasilolitarajia, wasilolipenda na wasilolihitaji.



Hivyo, alimgeukia Karim na kumwambia, “Jaribu kumwelewesha, aelewe. Na kama nilivyosema mwanzo, akishindwa kuelewa, atalazimishwa kuelewa., apende-asipende. Mimi naona kama ananizingua tu, naweza kujikuta namfanyia kitu mbaya ivi-ivi! Ongea naye!”









Karim alijitutumua na kumfuata Sharifa aliyekuwa bado akilia ingawa alikwishaacha kupiga ngumi ukutani. Sasa alikuwa kaiegemeza mikono ukutani hapo, kichwa kikiwa kimezama katikati ya mikono, akilia kimyakimya na kugugumia.



Karim alimgusa bega polepole na kumuuliza, “Mama yetu, kwani ni sababu gani inayokufanya usiamini kuwa mzee ana mtoto?” hakusubiri jibu. Akaendelea, “Umefahamiana naye wakati tayari alishakuwa mtu mzima. Huna historia yake kamili, kwa nini uwe mbishi kiasi hicho?”



Kama anayetumia nguvu za umeme, Sharifa aligeuka haraka na kumtazama Karim kwa macho makali. Alikuwa ni kama mwanafunzi anayesoma ubaoni yale yaliyoandikwa na mkufunzi wake. “Wewe ni mwongo! Tena mzandiki mkubwa!” yalimtoka kwa ukali. “Nakwambia hakuna kijibwa kama hicho unachodai kuwa ni mbegu ya Mzee Malick! Hakuna! Nasema hivi, mimi ndiye mke wa ndoa wa Mzee Malick, kwa hali hiyo ni mimi pia ndiye mrithi pekee wa mali zake. Siambiwi chochote kingine kuhusu hilo! Full stop!”



“Hakuna cha full stop!” Karim alishindwa kuvumilia. “Nasema wazi, mrithi wa mzee wetu ni mwanaye!”



Sharifa alizidi kughadhibika. Akafura nusu ya kupasuka. Akaachia tabasamu lililotisha, tabasamu lililoibadili sura yake na kuwa kama dude lisilotamanika wala kutazamika. Macho yake baridi yalitua usoni pa Karim na kuwa kama yanayomwambia, ‘NITAKUUA…UTAKUFA KIFO KIBAYA…NA DAMU YAKO ITAKUWA JUU YANGU…’



Karim, kijana ambaye hakuwahi kumjua baba wala mama yake mzazi tangu azaliwe, hakubabaishwa na macho haya makali ya Sharifa. Aliikumbuka safari ya Arusha ambayo ni jana tu amerejea. Akamkumbuka Ablah na yale maneno aliyosema: WE NENDA KWANZA UREKEBISHE MAMBO, KARIM. MZEE NI TAJIRI, NA KAMA AFYA YAKE INA UTATA, BASI KAA UKIJUA KUWA WATU WENGI WANAIMEZEA MATE MALI YAKE. WATANIUA! WATANIUA KARIM!



Akajisemea kimoyomoyo, Ablah alikuwa akijua kuwa huyu mwanamke ana roho mbaya ya kuweza kumuua! Lakini bado akili yake haikukubali kuwa Sharifa anaweza kufanikiwa. Na sasa Sharifa alivyokuwa akimtazama kwa hasira na dharau isiyomithilika, ujasiri na kiburi vikazidi kujenga himaya moyoni mwa Karim.



“Mama, hakuna kitakachobadilika!” Karim aliendelea. “Ablah atakuja kuishi hapa na kumiliki mali ya baba yake!”



Msisitizo wa maneno, sanjari na macho makali huku mikunjo ikiwa imejiunda pajini mwake kulimfanya Karim atishe. Ule upole wake, ule ukimya wake, ule ulaini wa kauli zake uliozoeleka masikioni na machoni mwa wengi sasa ulitoweka!



Ni hali hiyo iliyomfanya Sharifa anywee. Na kwa sauti iliyopwelea, akauliza, “Je, akishaolewa?”



“Kila kitu kitakuwa chini ya uangalizi na udhibiti wa mumewe,” Karim alijibu. “Hayo ndiyo maelekezo ya huyu baba yake mzazi. Kama huamini, ruksa kumuuliza.”



Macho yote yakahamia kwa Mzee Malick aliyekuwa katulia kitandani, chali, macho yake yakipepesa. Ilikuwa bayana kuwa mtafaruku uliozuka humo chumbani ulimuumiza moyo kwa kiasi kikubwa. Macho yakawa yamelengwa machozi. Alihuzunisha! Lakini ni nani aliyemhurumia humo chumbani zaidi ya Karim na daktari Suleyman?



Sharifa!



Sharifa angeweza kupatwa walao na chembe ya huruma ilhali maneno na tazama yake havikuwiana kabisa na upendo au huruma? Sharifa mwenyewe kwa maneno haya aliyoambiwa na Karim, alihisi kukumbwa na hali isiyoelezeka.



Maelekezo ya baba yake mzazi! Sharifa aliwaza kwa simanzi. Akazidi kujisikia vibaya. Akawa kama mtu anayekaribia kukata roho. Nguvu zikamwisha miguuni na kulazimika kuchutama kisha akakaa kabisa zuliani. Uso wake ulibadilika; akaiva kama papai na kuwa mwekundu kisha akawa mweupe. Na kutoka weupe akawa mwekundu tena!



Mara akasimama tena, safari hii mikono yake ikichezeachezea vidani vya dhahabu vilivyoning’inia shingoni. Sasa kilio chake cha kimyakimya kiliandamana na kwikwi, ambayo ilimzindua mumewe, Mzee Malick.



Kama aliyekuwa katoka katika sayari nyingine, Mzee Malick aliibuka na kuugeuza uso wake uliojaa simanzi. Akamtazama Sharifa kwa macho yake meupe!



“Sharifa,” aliita huku akiendelea kumkodolea macho. “Mke wangu, Sharifa, tafadhali naomba unisamehe kwa kutokukujulisha hili mapema…” Kama alikuwa na neno jingine la kuongeza, hakuweza kufanya hivyo.



Kama nyati aliyejeruhiwa, Sharifa alimdaka kwa sauti kali: “Habithi mkubwa! Kaa kimya! Huna la kun’ambia wewe! Dhalimu! Mnyama ul’olaanika! Laghai mkubwa! Ulinilaghai, nikalaghaika, nikakupa uaminifu wangu wote, nikakupa mwili wangu wote…leo umeni…



“Hapana! Siamini, na sitakubali! Kwa kweli unatisha! Hautofautiani na kifo kamili mwanaharamu we! Nakuapia, sitakubali! Sitakubali! Sikubali! Na…”



Akakwama. Akahema kwa nguvu. Kwa mara nyingine akaanza kulia. Mwisho wa maneno hayo aliyoyakata ulikuwa ni kumfahamisha fika Mzee Malick kuwa hata huyo bintiye aliyemtaja kuwa ndiye mrithi halali, yeye Sharifa kama mke wa ndoa hatakuwa radhi kuishi naye na hatampokea, na isitoshe hataki hata kumwona.



Lakini kabla hajafikia haya maneno, macho makali ya Karim na daktari Suleyman yalitosha kuwa onyo zaidi ya onyo la mdomo. Badala yake, akazinduka akibaini kuwa ni kweli hakupaswa kusema kila kitu katika kikao hicho isipokuwa mambo mengine yatajipima na kujiivisha mbele kwa mbele.



Akainama na kumbusu mumewe huku akisema, “Tafadhali kipenzi changu, sikuwa na maana mbaya, nimechanganyikiwa tu kipenzi… laazizi. Mume wangu, kipenzi changu, nitafanya kama ulivyoniagiza.”



Haikusaidia kitu! Yale maneno makali yaliyotamkwa awali yalipenya masikioni mwa Mzee Malick kwa usahihi mkubwa, yakafika ubongoni ambako ni kama vile yalikuwa ni mionzi mikali yenye kuleta madhara ndani ya sekunde mbili tu.



Yalikuwa ni maneno yaliyomtisha na kumfadhaisha kwa kiwango kikubwa. Tangu utoto wake, akiwa na uwezo wa kutambua jema na baya, hakuwahi kufokewa na mwanamke! Hata mama yake mzazi! Leo, akiwa ni mtu mzima, mwenye umri wa kuweza kuwa hata na wajukuu, anakaripiwa kwa maneno makali yenye uzito wa tani mia!



HABITHI MKUBWA! KAA KIMYA! HUNA LA KUN’AMBIA WEWE! DHALIMU! MNYAMA UL’OLAANIKA! LAGHAI MKUBWA…!



Moyo ulishindwa kustahimili. Macho yalimtoka. Akapaza sauti kubwa ambayo hapo kabla hakuwa nayo: “Karim! Karim!”



“Naam, baba!” Karim aliitika haraka huku tayari akiwa ameshamsogelea na kumwinamia.



Mzee Malick akamshika mkono na kusema kwa msisitizo, “Ablah ni mwanangu…ni mwanangu! Kamwe usimwache! Yeye ndiye mrithi wangu! Ndiye atakayebaki na kila kilicho changu! Karim usimwache mwanangu!”



Yalikuwa ni maneno yake ya mwisho. Ziraili mtoa roho akashuka ghafla na kuitimiza kazi yake kwa ukamilifu.



Alikata roho huku akiwa ameushika mkono wa Karim. Macho yalibaki wazi, yakimkodolea Karim ilhali hayaoni. Ni kama vile alikuwa akishangaa!



***** ***** *****









Kwa muda mfupi kila mmoja alibaki kimya. Ndipo daktari akamsogelea marehemu na kuzifunika mboni za macho yake.

Sasa haikuwa siri. Kila mmoja alijua kilichotukia. Lakini Sharifa hakustahimili. Akaanguka chini na kulia kwa sauti kubwa.



Kilikuwa ni kilio cha uchungu kutoka moyoni, kilio cha kufiwa na mumewe sanjari na kutokukamilisha azma yake ya kutwaa urithi mkubwa wa mali ya Mzee Malick Sikonge. Akauangalia mwili wa marehemu kwa uchungu na hasira kisha akajikokota kutoka chumbani humo taratibu.



Huku nyuma, bila ya kujijua, Karim alibubujikwa machozi. Kwa jumla alikuwa na uchungu kutoka ndani kabisa ya mtima wake. Ndiyo, Mzee Malick alikuwa ni zaidi ya mzazi wake. Ni yeye aliyemfikisha hapo alipo; ana afya njema, ana elimu bora.

Nani kama Mzee Malick! Alimgeukia daktari. Wakatazamana kwa huzuni.



“Mzee ametutoka,” hatimaye daktari alisema kwa unyonge. Akaongeza, “Kama ilivyo desturi, maisha ya mwanadamu lazima yawe na kikomo. Ukizaliwa, utambue kuwa lazima ufe. Huo ndio mfumo wa maisha ya mwanadamu. Na kifo ndiyo ukamilifu wa maisha! Tulitoka udongoni na sote udongoni tutarudi. Baba yetu, kipenzi chetu na ndugu yetu Mzee Malick ametangulia, sisi tutafuata siku zetu zitakapofika.”



Alipokwishatamka hayo, naye alibubujikwa machozi. Akajitahidi kuyafuta hafaka kisha akasema, “Karim, kuna kazi kubwa mbele yako. Nadhani mwenyewe umemshuhudia huyu mwanamke alivyoyauma meno kwa hasira, macho yakawa kama ya nyoka, ngozi ikabadilika, akapumua kwa shida huku jasho likimtoka. Ulimwona?”



“Ndiyo, nilimwona.”



“Basi kazi unayo, Karim. Nitakuwa nawe bega kwa bega kama kutakuwa na tatizo lolote. Jambo linalonitia shaka ni yule kaka’ake.”



“Yupi? Abdul?”



“Yeah. Siyo mtu mzuri yule! Ni wa kuchungwa sana!”



Karim alitikisa kichwa akiashiria kukubali. “Umesema kweli. Nitajitahidi kuwa makini. Na kumbe ndiyo maana marehemu kanisisitiza kumwangalia mwanaye! Kweli Sharifa siyo binadamu wa kawaida; nusu mnyama, nusu binadamu. Ee Mungu!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Ukimya ukatawala kwa muda, kisha daktari akahoji kwa sauti ya chini, “ Kwa hiyo ni kipi kinachofuata?”



“Itabidi tufanye mipango ya mazishi haraka ili niende Arusha kumchukua Ablah.”



“Kwani hana simu?”



“Anayo. Kwani vipi?”



“Ungempa taarifa…”



“Haitakuwa poa,” Karim alipinga haraka. “Hatuwezi kujua ataichukuliaje taarifa hii. Kama ana tatizo lolote la kiafya, anaweza kupata athari ambazo zinazoweza kutufanya tukajutia hatua hiyo.”



“Lakini tangu umerudi umekwishawasiliana naye?”



“Yeah. Jana nilipofika nilimtumia meseji kumtaarifu kuwa nimefika salama.”



*****

SHARIFA alizidi kuchanganyikiwa. Alipotoka humo chumbani alitembea kama kivuli, akiangalia mbele huku akili ikiwa imesimama. Alitembea kwa hatua ndefu hadi chumbani kwa kaka yake, Abdul. Ile kuingia tu akabwata, “Abdul! Kafa!”



“Nini?” Abdul aliyekuwa kajilaza kitandani chali, akivuta sigara, aliuliza kwa mshtuko. Na papohapo akajiinua na kuketi. Akamkodolea macho dada yake. “Unasema?”



“Nakwambia mshenzi kavuta!” Sharifa alisema, safari hii kwa msisitizo na huku naye akiketi kitandani. Akajifuta machozi kwa kiganja cha mkono wa kushoto, uso kauinamisha. Kama anayeomboleza akaendelea, “Nakwambia kafa! Kafa, Abdul! Bwege kafa! Mbona unakuwa zoba? Huelewi?”



“Basi, tulia,” Abdul alisema kwa sauti nzito, akionekana kutokuwa na wasiwasi wowote. Akavuta mikupuo miwili ya nguvu ya sigara yake kali kisha akaongeza, “Sasa kunachokuliza ni nini? Ulitaka aendelee kuishi, na aishi milele?”



“S’o ivo Abdul,” Sharifa alijikakamua na kumtazama Abdul sawia. “Tatizo, wale mahabithi wanang’ang’ania kuwa eti alikuwa na mtoto! Eti huyo mtoto wao wa kupandikiza ndiye mrithi halali wa mali yake!”



“Hakuna kitu kama hicho!” Abdul alibwata. Akavuta mkupuo mzito wa sigara kisha akaitupa sakafuni na kuisaga kwa kandambili. Akaendelea, “Ni kosa kubwa sana kuiruhusu takataka, mbwa kama huyo anayedaiwa kuwa ni mwanaye ichukue urithi huu! Na kama angekuwa bado hai, nakuapia ningemchoma kisu sasa hivi! Sasa hivi!”



Akakurupuka kuinua godoro na kuchomoa kisu kirefu. Akamwonyesha Sharifa. “Unaona hii? Bahati yake kishavuta, ningemgeuza bucha kenge brrruuuu! Ningemkata maini na kuyatafuna kudadadek!”



Akakirudisha kisu kwenye chaga za kitanda. Akavuta tena mkupuo wa sigara, safari hii kwa nguvu zaidi. Akatulia kidogo na kuinua uso kisha akaupuliza moshi juu, macho yakitazama dari.



Akilini mwake aliona kuwa sababu kubwa ya mtafaruku huo ni utovu wa nidhamu wa dada yake. Kutokuwa mwaminifu na kutomtii kikamilifu mumewe katika kipindi kirefu cha ndoa yao ndiyo sababu kuu iliyofanya apoteze pointi muhimu ambazo zingemwezesha kuwa mrithi wa mali.



Lakini hakupenda kuliweka bayana hilo kwa Sharifa. Alitambua kuwa kwa muda huo ambao mambo yameshaharibika, mshikamano thabiti ulihitajika. Yeye na dada yake walipaswa kuwa kitu kimoja ili wafike kule wanakotaka kufika.



Hivyo alimwambia, “Sikia, sista. Komaa na ujikaze. Usifanye kelele zitakazowashtua hata hao vijibwa wengine wanaofanya kazi hapa. Na itakuwa noma sana kama huyo msukule wake, Karim atagundua kuwa umechanganyikiwa kwa ajili ya urithi. Jikaze! Jidhibiti ili tuyakamilishe malengo yetu vizuri.



“Kumbuka, ukoo wetu ni maskini! Huo ni ukweli usiopingika! Sasa ukae ukijua kuwa hii ndiyo karata yako ya mwisho. Ukiicheza kimakosa, umeumia, nimeumia. Tutakuwa tumenyea kambi, baba’ake. Tunapaswa kutofanya kosa lolote kwa kipindi hiki!



Risala hiyo ilimwingia Sharifa kwa ukamilifu. Akajitutumua kusimama na kumkazia macho Abdul. Kisha kwa sauti ya chini, akasema, “Ok, ngoja nirudi huko kwa wazushi na maiti yao.”



Abdul alitikisa kichwa akiashiria kukubali. Akachomoa sigara nyingine na kuiwasha.



*****



UTULIVU ulikosekana kichwani mwa Karim. Majukumu yaliyokuwa mbele yake yalikuwa makubwa na hakujua aanze lipi, na lipi lifuate. Zaidi, alimwazia Ablah aliyekuwa Arusha ambaye hadi wakati huo hakujua kuwa baba yake mzazi alikwishafariki dunia.



Alipaswa kuja kuhudhuria mazishi. Safari ya kumleta Dar ilikuwa juu yake Karim. Na alipaswa kulishughulikia suala hilo haraka iwezekanavyo.



Na kuna hili la taratibu za mazishi ya marehemu Malick. Ingawa daktari alikuwapo, lakini Karim aliona kuwa bado mzigo huo ni wake. Afanye nini? Aliwaza huku akielekea chumbani mwake ambako mara tu alipofika alijitupa kitandani na kulala chali, miguu akiwa ameiacha sakafuni. Akaendelea kuwaza kuhusu mzigo huo alioubeba.



*****



SHARIFA alipotokeza koridoni tu, kwa mbali akamwona Karim akifungua mlango wa chumba chake na kuingia. Akili ya Sharifa ikamtuma kumfuata Karim hukohuko chumbani. Alipoufikia mlango, hakubisha hodi. Alikizungusha kitasa, kikatii. Akaingia taratibu na kuurudisha mlango. Kilichofuata kilimshtua na kumshangaza Karim kwa kiasi kikubwa.



Sharifa alichojoa nguo zake, moja baada ya nyingine. Hatimaye akabaki mtupu kama alivyozaliwa! Hakuwa na wasiwasi wala aibu! Alimtazama Karim usoni sawia huku akitabasamu kimahaba!







Akamfuata kitandani na kuketi kando yake. Akaupandisha mguu mmoja juu ya mapaja ya Karim, kisha akajilaza kifuani pake huku akimwemwesa, “Karim… Karim…”



Karim hakuitika. Mara Sharifa akaupandisha mguu huo tumboni huku paja likiwa nje! “Karim vipi?” akauliza huku akiupitisha mkono shingoni mwa Karim. Akamtazama kwa kuyarembua zaidi macho yake. Akaongeza, “Karim, hivi mimi nina kasoro gani?”



Karim alizidi kushangazwa na maneno haya yaliyomtoka Sharifa kinywani sanjari na vituko vyake. Mshangao wake ukachanganyika na hasira ambazo zilimfanya ashindwe kupumua vizuri.



Huyu mwanamke ni kichaa? Swali hilo lilielea ubongoni mwake mara elfu kwa sekunde chache tu. Kama kweli alikuwa ni mke wa ndoa wa Mzee Malick ambaye sasa ni marehemu, maiti ikiwa ndani humo, anaweza kuwa na ujasiri wa kufanya lolote? Hana uchungu wala sononeko moyoni mwake! Hilo lilikuwa bayana. Na zaidi, ina maana yu tayari hata kufanya ngono na mtu mwingine ilhali maiti ya mumewe ikiwa bado na joto lake! Ana akili timamu au yu punguani?



Kwa ujumla alishindwa kumwelewa ndani ya sekunde kama tano hivi, lakini baada ya muda huo alikuwa na akili nyingine. Sasa alimwelewa! Alitambua kuwa Sharifa sio punguani, ni mzima! Ana akili timamu na anajua kila anachokifanya!

Ni kwa kutambua hivyo, Karim akajua kuwa anapaswa kuwa makini. Asiwe na pupa ya kumkaripia au kwa namna yoyote ile kumwonyesha kuwa haafikiani naye kwa haya ayafanyayo.



Kwa upole, huku naye akiwa ameukita mkono wake begani mwa Sharifa, akasema, “Mama…huna kasoro yoyote…”



“Shut up!” Sharifa alibwata kwa sauti ndogo huku akimziba Karim mdomo kwa namna ya mzaha. “Mama…mama…nani mama yako hapa?Mi’ naitwa Sharifa au Sherry, umesikia?”



“Nimesikia, Sharifa.”



“Ok, sema sasa kama sina kasoro yoyote kwa nini unanichunia? Yaani unajitia kuwa na uchungu sana kwa kifo cha Malick kuliko mie mkewe!”

Ukimya mfupi ukapita, Sharifa, macho yake yasiyo hata na chembe ya aibu yakiwa yameganda usoni pa Karim.

“Sasa siki’za,” Sharifa aliendelea.“Mie nataka. Nina siku nyingi sijastarehe. Kama unavyojua, marehemu alikuwa hoi kwa muda mrefu. Ulitegemea nivunje heshima yangu na heshima yake kwa kuivulia nguo mijitu ya ajabu-ajabu halafu baada ya siku mbili iwe ni skendo kwenye magazeti ya udaku?”



Karim hakujibu.



“Nakupenda Karim,” Sharifa aliendelea. “Nakupenda na ninakutaka! Na kama umeweza kuuona mwili wangu wote huu, halafu usinipe ninachokitaka, sasa hivi nitapiga kelele kuwa unataka kunibaka! Wallahi nakuapia! Na nikipiga kelele hakuna atakayesema kuwa nakusingizia! Pinga!”



Karim aliona maji yamemfika shingoni. Kwa upole, huku akimtazama kwa udadisi, akasema, “Acha ukali, Sharifa. Labda tu hunielewi, lakini ukweli ni kwamba, nakupenda kuliko hata wewe unavyonipenda. Naomba tu uwe na subira. Tutafute siku nzuri na sehemu nzuri. Sio freshi kufanya hivi wakati huu ambapo mwili wa marehemu uko ndani. Siyovizuri, mpenzi.”



‘Mpenzi’ lilikuwa ni neno lililomlainisha Sharifa kwa kiwango kikubwa na kuufanya moyo wake uwe baridi. Akakishika kisogo cha Karim na kumvuta karibu. Nyuso zao zikagusana. Midomo ikakutana. Akauchomoza ulimi na kutaka kuupenyeza kinywani mwa Karim.

Safari hii hakukumbana na pingamizi. Karim alimruhusu.Takriban dakika moja ikakatika wakiwa katika busu hilo, Sharifa akisisismkwa mwili kwa kiwango cha juu ilhali Karim akiwa katika wakati mgumu, hana hata chembe ya mhemko!



“Asante mpenzi,” alisema mara tu walipotenganishavinywavyao.

Karim hakuwa na la kusema. Alinyanyuka na kuanza kutoka. Alipofika mlangoni aligeuka na kumtazama tena Sharifa. Akaachia tabasamu la mbali kisha akafunga mlango na kutoka.



*****

“MWANZO mzuri,” Sharifa alinong’ona huku akivaa nguo zake. Aliamini kuwa tendo la kufanikiwa kupata busu la kinywani huku wakati huoKarim akimshika hapa na pale na kumtosa huku na kule, ilikuwa ni hatua kubwa ya kuelekea kwenye mafanikio.



Alichohitaji ni kumpata Karim. Ndiyo, alitaka iwe hivyo, na ulimbo pekee alioutegemea ni mapenzi; apate nafasi ya kufanya naye mapenzi. Aliamini kuwa siku ambayo Karim atadiriki kupenya katikati ya miguu yake, ndipo atakapoudhihirisha umahiri wake mtoto wa kike. Atajitoa kwa kila kitu, akiutumiaujuzi wake wote aliojaaliwa.



Alijiamini, na alikuwa na sababu ya kujiamini. Kabla hajaolewa na Mzee Malick, alikuwa akifanya kazi ya uhudum wa usafi katika hoteli moja ya kitalii jijini Dar es Salaam. Uzuri wa sura na umbo lake viliwavutia wengi hotelini hapo na katika hao ni wazungu ndio walioongoza.



Baadhi ya wazungu hao hawakustahimili kuongea naye maongezi ya kawaida; walimwomba penzi. Naye hakujivunga. Alihitaji pesa, hivyo alikuwa tayari kwa yeyote mwenye dau la kushikika.



Ni katika mfumo huo mara kadhaa alijikuta akidiriki kufanya mapenzi hata na wanaume wawili au watatu na akawamudu.

Kwa ujumla aliweza kufanya mapenzi kwa mtindo wowote kadri mtoa dau alivyotaka. Hakuhofia kuambukizwa maradhi yoyote ya zinaa, alizijali dola walizompa! Hatimaye, kutokana na jinsi pesa nyingi zilivyomiminikia, akaona ajira ya hapo hotelini inambana.



Akaitema!



Sasa akawa ni mtu wa kukutana na watu maarufu jijini Dar es Salaam, Arusha, hataNairobi-Kenya, watu ambao kwao, pesa zilikuwa kama mchanga kwa wingi wake. Hawakusita kuzitoa!

Sharifa alikomaa katika mbinu za kufanya mapenzi, na ndiyo maana ile siku ya kwanza ambayo Mzee Malick alimtongoza na wakajichimbia chumbani usiku kucha, MzeeMalick ‘alitangaza ndoa’.



Kwa hali hiyo, aliamini kuwa siku isiyo na jina, ambayo Karim atachojoa nguo zake kwavyovyote cha moto atakiona. ‘Ataomba poo.’ Na aliamini kuwa baada ya siku hiyo ya kwanza Karim atamganda, akitaka tena na tena. Hatua ya Karim kunogewa, kutatoa taswira mpya, taswira nzuri ya mafaniko kwa Sharifa siku za usoni.



Alipomaliza kuvaa, alitoka huku akicheka kimoyomoyo, akikumbaka jinsi alivyofanikiwa kupiga hatua moja muhimu.



*****

TAARIFA ya kifo cha Mzee Malick ilitolewa kwa wafanyakazi wote waliomhusu. Majonzi yakalitawala eneo hilo. Kazi zote zikasimama. Umakini ukazingatiwa. Ulinzi ukaimarishwa.

Mara nyingi eneo lenye sherehe za ndoa, msiba au shughuli yoyote ile inayokusanya watu wengi, lolote huweza kutokea. Na mara nyingi vilevile, wizi wa vitu mbalimbali hutokea.



Sio kila anayehudhuria kwenye matukio huwa ni mtu mwema. Ni hilo lililomfanya Karim awe makini zaidi, akitambua fika kuwa Mzee Malick kafariki huku akiwa amemkabidhi majukumu ya ulinzi wa mali zake.



Mwili wa marehemu Malick ulipelekwa hospitali na kuhifadhiwa hadi siku ya tatu ambayo walikubaliana kuwa ndiyo iwe siku ya mazishi.







Likatengenezwa sanduku maalumu, madhubuti kwa kioo, na kutaraziwa kwa madini ya dhahabu. Kaburi lake ambalo lilichimbwa ndani ya eneo hilohilo, kando ya jumba lake la kifahari, lilitengenezwa kwa vyuma na vioo ili mwili wake uwe ukionekana daima dumu kama kumbukumbu yao ndani ya ngome hiyo.



Ni wakati hayo yakifanyika, ndipo Karim alipoingiwa na wazo la kutomfuata Ablah kwa ajili ya kuhudhuria mazishi ya baba yake. Hakutaka kuondoka, akiwaacha watu wengine hapo ndani ya ngome ya marehemu Malick Sikonge. Hapana. Hakumwamini mtu mwingine yeyote kwa kipindi hicho.



Ndiyo, hakukuwa na mtu yeyote mwingine ambaye angemwamini, lakini alikuwapo mtu ambaye angeweza kumweleza jambo atakaloona kuwa linastahili kumfikia. Na pia, angeweza kuhitaji ushauri wa jambo ambalo nafsi yake ingeridhia kulisema kwa mtu huyo. Zaidi, alikuwa na uamuzi wa mwisho wa kufanya chochote bila ya kuhitaji ushauri au hata kuukataa ushauri wowote atakaopewa.



Akaamua kumweleza daktari kuhusu kutomfuata Ablah.

“Kwa nini?” Daktari Suleyman alishangaa. “Tulizungumza nini, Karim? Kwa nini uwe kigeugeu?”



“Mazungumzo yetu na makubaliano yetu hayakugeuka kuwa sheria,” Karim alisema kwa utulivu, akionekana kutobabaika. Akamtazama daktari kwa makini akitaka kuthibitisha kama kauli yake imemwingia. Macho yao yakakutana.



“Nimeona ni vyema iwe hivyo,” Karim aliendelea. “Tambua kuwa tunahitaji kufanya mambo kwa uhuru. Kumbuka, Ablah aliachwa na baba yake akiwa bado tumboni kwa mama yake. Hakuwahi hata kuonana naye. Kwa kuwa bado tuna majukumu makubwa, sidhani kama tutakuwa tumefanya kosa la jinai kutomfuata. Siyo kwamba kuna jambo lolote ambalo haliwezi kutekelezwa kama hatakuwepo. Kila kitu kinaweza kufanyika, tena kwa ufanisi.



“Isitoshe, kama unavyoyajua mazingira ya hapa, hatustahili kupaacha hata kwa nusu siku bila ya uangalizi madhubuti. Nikiondoka, unajuaje, huenda ikatokea hujuma kubwa kutoka kwa huyu mwanamke au kaka yake!”



“Yeah,” daktari aliafiki. “Nimekusoma. Ni kweli huu ni wakati wa kuwa makini kuliko wakati mwingine wowote. Kwa hiyo akilini mwako ulipanga kuwa badala ya sasa ulitarajia kumfuata lini?”



“Asubuhi ya siku ya tatu baada ya maziko.”



*****

YALIKUWA ni mazishi yaliyowakusanya watu wengi maarufu. Waziri mmoja alimwakilisha kiongozi mkuu wa nchi. Mawaziri wengine, makatibu wa wizara mbalimbali, wakurugenzi wa taasisi kadhaa na wafanyabiashara maarufu pia walihudhuria.



Kamera za televisheni zilichukua kila tukio na wanahabari wa vyombo vingine nao wakiwa katika pilikapilika, wakitaka kupata chochote cha kuripoti. Karim alipata shida kwa kuulizwa maswali haya na yale na waandishi wa habari hao na swali kubwa ambalo aliulizwa na takriban kila mwanahabari lilikuwa ni “Marehemu alikuwa akisumbuliwa na maradhi gani?”



Alitoa jibu moja tu: “Presha.”



Yeye na daktari walikubaliana hivyo, wakiepuka kutaja kuathirika kwa ini kwani walijua kuwa jibu hilo lingezua maswali zaidi.



Hatimaye mwili wa marehemu ulihifadhiwa ndani ya lile kaburi la aina yake, na ikawa ni rahisi kwa yeyote kuuona.

Siku ya tatu, saa 11 alfajiri Karim aliamka na kujiandaa haraka. Nusu saa baadaye akaingia ndani gari aina ya Range Rover na kulitia moto. Hakukuwa na mtu yeyote mwingine aliyejua chochote kuhusu safari yake hii isipokuwa Daktari Suleyman.



*****



UKIMYA uliendelea kutawala ndani ya jumba hili la marehemu Malick. Wakati Karim akiwa njiani kuelekea Arusha, Sharifa alimwita kaka yake, Abdul faraghani na kumwambia, “Unapaswa kuondoka!”



“Kuondoka?!” Abdul alimshangaa.



“Ndiyo! Unapaswa kuondoka!”



“Kwa nini?”



“Hilo s’o swali! Unapaswa kutambua kuwa ni mimi ninayetambulika hapa! Siyo wewe! Wewe ni shemeji tu ya marehemu. Basi! Lakini mimi najulikana kuwa ni mke wa marehemu!”



Abdul alimwelewa. Papohapo akamdaka: “Lakini sina mkwanja!”



“Nitakupa! Mkwanja s’o tatizo!”



“Na niende wapi? Nirudi tena bush? Maana’ake majuu nd’o hakuna cha kunipeleka!”



“Hakuna cha majuu wala kurudi bush,” Sharifa alisema. “Unaondoka hapa lakini hauondoki Dar. Utajichimbia sehemu fulani na tutakuwa tunawasiliana.”



“Niondoke lini?”



Sharifa alifikiri kidogo, kasha akasema, “Nadhani tusubiri kidogo huyo mbwa anayedaiwa kuwa ni mtoto wa marehemu aje?”



“Atakuja lini?”



Sharifa akayainua mabega juu na kuyashusha. “Siwezi kujua,” hatimaye alisema. Akaongeza, “Lakini sidhani kama atachelewa kuja. Kwa vyovyote taarifa ya kifo cha baba yake, anayo. Na anajua kuwa amekufa akiacha mali nyingi. Unadhani atalemaa tu huko Uchagani bila ya kuwahi kuja kucheki urithi?” Hakusubiri jibu. “Haiwezekani. Najua haitafika wiki atakuwa hapa!”



Ukimya mfupi ukapita. Kisha Sharifa akaongeza, “Najua namna ya kumbana huyu bwege Karim. Nikishamweka kiganjani, basi nitaijua siku ya kuja huyo mbwakoko wao. Isitoshe, hata mipango mingine yote kuhusu mali hii pia nitaijua.”



Abdul alionesha kushangazwa na maneno ya dada yake. Akasema, “Lakini sioni umuhimu wa mimi kumsubiri. Nipe pesa nikakae uswazi kwa uhuru. Kama ulivyosema, ni wewe unayetambulika hapa; siyo mimi.”



“Vuta subira kaka. Tusubiri kidogo. Mambo mazuri…”



“Hayataki haraka.”



*****



ILIKUWA ni kawaida kwa Mzee Sukununu kuketi nje ya nyumba yake jioni kabla jua halijazama. Jioni hii, akiwa hapo kibarazani kwake, kopo la mbege kando yake, alishangaa kuona gari likiegeshwa mbele ya nyumba yake. Gari zuri, la kisasa, ambalo alilifananisha na la tajiri mmoja, Tarimo. Gari hilo lilikuwa la rangi ya ‘damu ya mzee’.



Alibaki amelikodolea macho gari hili, akijiuliza ni nani huyo aliyekuja nalo? Au ndiyo watu wanataka kuanza kumfuatilia mjukuu wake?



Kuhusu wanaume kuanza kumfukuzia mjukuu wake, hilo halikuwa jambo la kumshangaza. Alimwona mjukuu wake alivyovutia, hivyo alijua watu wengi, hususan wenyenazo watajileta wakitaka kuchumbia. Na mbinu ambazo wengine wangetumia ni kuja kwa mkwara mzito wa magari ya kifahari. Akacheka kimoyomoyo akisubiri kumwona huyo aliyekuja kwa mkwara mzito wa Range Rover.



Mvumo wa nguvu wakati gari likisimama, uliyafikia masikio ya Ablah na bibi yake waliokuwa jikoni. Wakatoka na kuja nje kuangalia kinachojiri.



“Haa! Karim!” Ablah alibwata kwa furaha mara tu alipomwona huyo aliyekuja na gari hilo.



Mzee Sukununu na mkewe nao wakarejewa na kumbukumbu kwamba, huyu mgeni ni yule Karim aliyekuja siku chache zilizopita akitokea Dar es Salaam na kujitambulisha kuwa ametumwa na baba yake Ablah.



Karim akalakiwa kwa shangwe huku Ablah akionekana kufurahi maradufu. Akamtazama Karim jinsi alivyopendeza kwa mavazi yake nadhifu. Akamshika mkono na kumwongoza sebuleni. Wazazi nao wakajunuika sebuleni hapo.



“Karibu sana kijana wetu,” Mzee Sukununu alimwambia Karim.



“Karibu mjukuu wangu,” mkewe naye alichangia.



Karim aliitika huku akiachia tabasamu la mbali, akiwaza ni wakati gani mwafaka wa kuwapa taarifa ya kifo cha Mzee Malick.



Hata hivyo, Mzee Sukununu na mkewe walikuwa na upeo mkubwa. Walihisi kuna jambo zaidi ya jambo.



 Karim alipokuja hapo mara ya kwanza siku chache zilizopita alitoa taarifa ya maradhi yanayomsumbua baba yake Ablah. Na aliwaambia kuwa katumwa hapo kwa ajili ya kumchukua Salma aende akarithi mali ya baba yake.



Ilikuwa ni taarifa iliyotoa taswira kuwa Mzee Malick hatapona. Sasa hata siku saba hazijaisha, kisharejea. Tena, karejea huku akionekana yu mnyonge na mwenye wasiwasi.



Hili tabasamu lake halikuwa tabasamu la kumfanya mtu mzima, mwenye akili timamu ya utambuzi alaghaike.



Mzee Sukununu na mkewe nao hawakulaghaika. Ndipo bibi yake Ablah alipochokoza: “Enhe! Vipi mjukuu wangu; kwema huko ulikotoka?”



Karim alikumbwa na kigugumizi, lakini alipowatupia macho wazee hao na kukuta wote wakimtazama kwa makini, akaamua kuutua mzigo.



“Kwa kweli wazee wangu, huko siyo kwema,” alijibu. “Mzee Malick katutoka.”



“Mungu mkubwa!” Mzee Sukununu alisema, akionesha kutoshangazwa na kauli ya Karim.



“Mipango ya Mungu haitenguliwi na binadamu, mjukuu wangu,” mkewe naye alisema kwa unyonge.



Ablah alibaki akimtazama Karim kwa mshangao. Uchungu ukamjaa moyoni. Machozi yakamtoka. Hana baba, hana mama! Zaidi, baba yake amefariki bila hata ya kuonana naye ana kwa ana, afurahie kutamka SHIKAMOO BABA! Afarijike kwa kuzungumza na baba mzazi!



“Nilijua tu,” hatimaye alisema. “Isingekuwa rahisi kuja mapema hivi, na uje na habari njema. Na kwa jinsi ulivyosema kuwa anaumwa…”



“Yameshatokea dada’angu,” Karim alimwambia kwa upole. “Piga moyo konde. Mungu yuko pamoja nawe. Na mimi nitakuwa nawe bega kwa bega! Usihuzunike sana. Ndiyo hali ya dunia, dada’angu.”



Ablah alimwelewa. Ndipo Karim alipowaambia bayana kuwa safari yake hii ni kwa ajili ya kumchukua Ablah.



“Tubaki peke yetu?” bibi yake Ablah alihoji huku katokwa macho pima.



“Ni kwa siku chache tu, bibi,” Karim alimtoa hofu. “Hata nyie mnapaswa kuja kule muishi na mjukuu wenu. Ile mali ni ya mjukuu wenu. Ni mali yenu! Msihofu, mambo yatakwenda vizuri sana.”



Kisha akamgeukia Ablah: “ Pia kama utataka kujiendeleza kimasomo kwa ajili ya kuisimamia miradi ya marehemu mzee kwa ufanisi ni uamuzi wako. Hata hivyo unaweza kufanya yote mawili kwa pamoja na ukafanikiwa.”



Hadi jua lilipozama walikuwa wamekubaliana kuwa siku inayofuata Karim na Ablah waondoke.



Saa 2 asubuhi, siku iliyofuata, Karim aliegesha tena gari nje ya nyumba ya Mzee Sukununu. Muda mfupi baadaye akamwona Ablah akitoka ndani na kibegi kidogo. Ablah alipendeza kiasi chake. Alivaa T-shirt nyeusi, kofia pana kichwani, jaketi na suruali ya jeans. Raba nyeupe zilimkaa vyema miguuni.



Alitoka huku akifuatiwa na babu na bibi yake ambao walionekana kujawa na majonzi ya kuachwa na mjukuu wao. Walipolifikia gari walisalimiana na Karim aliyekuwa kaegemea mlango. Kisha Mzee Sukununu akasema, “Karim, tafadhali umlinde mjukuu wangu.”



“Usihofu babu,” Karim alijibu. “Mjukuu wako hatapata matatizo yoyote. Atakuwa chini ya uangalizi wangu kwa asilimia mia moja. Ninayaheshimu maagizo aliyoniachia marehemu Mzee Malick kuhusu huyu mwanaye.”



Bibi yake Ablah alimsogelea Ablah na kumkumbatia huku akitokwa machozi. Ablah naye akalia, na alikuwa na sababu ya kulia. Alijisikia vibaya kuwaacha babu na bibi yake ambao tangu anakua, amekuwanao bega kwa bega. Wamemtunza na kumsomesha. Alipokumbwa na maradhi walimpeleka hospitali. Sasa anawaacha peke yao!



Ilimuuma!



“Safari njema, mjukuu wangu,” hatimaye bibi alimwambia Ablah.



“Asante, bibi,” Ablah alijibu kwa unyonge, akijifuta machozi kwa leso.



Karim alitwaa mfuko mweisi, laini uliokuwa umetuna, akamkabidhi Mzee Sukununu, akisema, “Babu, zitawasaidia kwa siku chache. Kabla ya mwezi kukatika nitakuja tena kuwajulia hali. Na kabla ya miezi mitatu kupita nyie mtakuwa Dar, mkiishi na mjukuu wenu.”



Mzee Sukununu aliipokea ile bahasha na kuifungua. Akashtuka! Ndani yake kulikuwa na mafungu kumi ya noti za shilingi elfu tano, tano, kila fungu likiwa limefungwa na mpira maalum!



Shilingi 500,000!



*****

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

SAA moja baadaye, Karim na Ablah walikuwa wameshauacha mbali Mji wa Arusha. Karim alikuwa makini katika uendeshaji hivyo alizungumza mara chache na kwa muda mrefu alikuwa macho barabarani mikono kwenye usukani.



Walipofika Korogwe, aliegesha gari ili wapate mlo wa mchana. Ni wakati huo ndipo Ablah ambaye sasa alianza kumzoea Karim, aliamua kuhoji kuhusu huko waendako.



“Karim, kabla hatujafika ni vizuri ukinipa picha halisi ya jinsi baba alivyokuwa akiishi na huyo mkewe.”



Karim alifikiri kidogo kisha akasema, “Ok, tukirudi garini nitakueleza.”



*****







ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog