Search This Blog

Saturday 5 November 2022

MILIONI THELATHINI - 5

 







    Simulizi : Milioni Thelathini

    Sehemu Ya Tano (5)







    “MAMBO yanaweza kuwa yamebumburuka?” Aloyce alimuuliza Chaka huku akimtazama kwa macho makali.



    “Hakuna kitu kama hicho,” Chaka alijibu. “Kama unavyojua, nimemwacha akiwa na mwenye mali hii. Kwa hiyo inabidi atumie mbinu ya kumtoka ili aje.”



    “Atamtoka vipi?” Aloyce alimshangaa. “Kama wako wote tangu mapema na ni watu waliozoeana, unadhani itakuwa rahisi kumtoka?”

    Badala ya Chaka kujibu, alitwaa sigara na kuiwasha kisha akavuta mikupuo miwili, mitatu ya nguvu. Hakuonyesha kujali kwa kutopata mawasiliano na Chris. Baada ya kuvuta sigara hiyo ndipo akasema,



    “Unaonaje, kuna haja ya kumsubiri? We' nipe mzigo niishie. Nitakutana nae hukohuko.”



    “Unasema?” Aloyce alimtazama kwa namna ya dhihaka huku akigongagonga kidole cha kati cha mkono wa kulia, mezani.



    “Hakuna haja ya kumsubiri,” Chaka alisema kwa msisitizo japo sauti yake ilikuwa chini. “Mzigo umeshafika kama mlivyokubaliana. We' nihesabie hapa chapchap nianze. Nitakutana nae hukohuko!”



    Aloyce alicheka. “Hayo s’o mambo, Chaka. Taratibu. Kazi za aina hii hufanyika kwa utaratibu maalum. We vipi?”



    “Una maana gani?” Chaka alimkunjia uso.



    “Yaani, suala hili sio la kulipeleka kwa papara. Tumsubiri kwanza Chris.”



    “Wa nini wakati kazi imekwishakamilika?”



    “Taratibu, bwa'mdogo,” Aloyce alisema kwa sauti ya majivuno. “Uelewe kuwa suala hili linahusu pesa. Tena siyo vichele vya pesa. Ni zaidi ya milioni ishirini. Ni milioni thelathini! Ni suala zito. Unataka tulipeleke kienyeji na kihuni-huni? No, hatuendi hivyo, msh’kaji.”



    Chaka alifikiri mara mbili-mbili na kuona mdudu mbaya ameanza kuingia. Kwanza alishangaa kwa nini Chris awe hajapatikana simuni. Kama kazima simu kwa nini afanye hivyo? Na wakati huohuo hakuwa na hakika ya Chris kusalimika huko aliko. Huenda Salma akamshtukia. Na ikitokea hivyo, basi hatakuwa na pa kutokea!









    Kazi iliyokwishafanyika ni kubwa, kwa nini iharibikie hapa ukingoni? Je, kama Chris kakamatwa huko aliko, akabanwa kisawa-sawa, hatadiriki kuwaleta askari hadi hapo kwa Aloyce na kuwatia mbaroni?



    Ni hili wazo la mwisho lililomtia shaka. Akashusha pumzi ndefu na kusema, “Aloyce, ni mimi ndiye niliyekuja na mzigo. Kama huwezi kunipa pesa sasa hivi, basi nipe swichi niondoke.”



    Yalikuwa ni maneno yaliyopenya masikioni mwa Aloyce kwa usahihi na kuunguruma kama radi. Naye akahisi mchezo unataka kuharibika. Hakuwa tayari kuliacha gari hilo zuri, Toyota Land Cruiser- GX liondoke katika himaya yake. Lakini pia hakuwa radhi kumlipa huyu Chaka pesa ilhali siye waliyezungumza kuhusu mpango huo.



    Chris alihitajika. Ni Chris ndiye aliyekuwa kinara wa mpango huo. Huyu Chaka amefanya kazi ya kulileta gari tu! Chris hakuagiza kuwa Chaka akishaleta gari apewe na malipo ya pesa. Je, akichukua hicho kitita cha pesa na kutokomea kisha nyuma yake Chris akaja, mambo yatakuwaje?



    Akamtazama tena Chaka na kusema, “Hakuna swichi wala pesa!”



    “Nini?!” Chaka alimaka.



    “Nadhani umenisikia na kunielewa,” Aloyce alisisitiza kwa sauti nzito na ya chini, macho yake makali yakimtazama Chaka sawia. “Kiswahili siyo lugha ngumu kwangu na kwako.”



    Chaka hakuyaamini masikio yake. Akamkazia macho Aloyce. Wakatazamana. Mara Aloyce akapeleka mkono katika moja ya saraka za meza yake. Akaifungua na kuangalia ndani kisha akaifunga.



    Akayarejesha macho kwa Chaka na kukutana na macho baridi, macho kama ya nyoka, yakimtazama kwa namna nyingine kabisa!



    “Sikia, Aloyce,” Chaka alisema. “Ni mawili. Nipe pesa au nipe swichi. Vinginevyo...” akaiacha sentensi hiyo ikielea.



    “Unataka pesa, au swichi? Chagua moja.”



    “Nipe pesa. Milioni thelathini!”



    “Na Chris akija nyuma yako nimwambieje?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Kwamba, umeshanipa!”



    “Ok, subiri.”



    Aloyce aliifungua tena ile saraka ya meza yake na kuingiza mkono ambao badala ya kutoka na pesa, ulitoka na bastola kubwa. “Huo ndio mgawo wako!” alisema huku akifyatua risasi moja kwenye paji la uso wa Chaka.



    Lilikuwa ni tukio la ghafla na la haraka sana! Lakini pia lilikuwa ni tukio lililofanyika kwa usahihi mkubwa! Chaka hakunyanyuka wala kuthubutu kufanya lolote. Alitikisika kidogo tu kisha akainamisha kichwa kifuani na kuacha ubongo ukimwagika kisogoni kama uji wa moto.



    “Hizo ndizo milioni thelathini ulizozitaka, mbwakoko we!” Aloyce alisema kwa mnong'ono huku akiirudisha bastola sarakani.





    **********





    AKILI ikifanya kazi kwa haraka na kwa kujiamini, Chris alivuka barabara hadi upande wa pili. Pale akasimama kwa muda mfupi tu na kupata teksi. “Kimara haraka sana!” alisema huku akiingia garini.



    Gari likasaga lami kama liko kwenye mashindano. Wakiwa njiani ndipo Chris akaifungua simu. Kisha akampigia Chaka. Simu ikaita kwa muda mrefu kisha ikakatika. Akapiga tena. Ikaita tena na kukatika tena!



    “Shit!”akasonya kwa hasira na kumpigia Aloyce papohapo.



    Simu ya Aloyce ikaita kwa muda kisha akasikia kama imepokewa, lakini punde ikakatika. “Kuna nini?” alijiuliza kwa mnong'ono ambao haukuweza kuyafikia masikio ya yule dereva. Kwa mbali akahisi mapigo ya moyo yakimdunda kwa wasiwasi.



    Wasiwasi!



    Anahofu nini?





    **********





    KUUA halikuwa jambo ambalo Aloyce alilikusudia. Lakini aliamini kuwa kama asingechukua hatua hiyo, humo ndani pangechimbika. Na sasa amekwishaua. Aliitazama maiti ya Chaka kwa hasira kisha akanyanyuka. Alijua kuwa mlipuko wa risasi aliyofyatua ulisikika mbali na kwa vyovyote ungezua mambo.



    Wakati bado anawaza ni hatua gani iliyostahili kuchukuliwa baada ya tukio hilo, mara akasikia simu ya marehemu Chaka ikiita. Papohapo akaingiza mkono katika mfuko wa shati wa maiti hiyo na kuichomoa simu.



    Alipoitazama kwenye kioo, moyo ukamshtuka. Jina la CHRIS lilitawala! Akairudisha kwenye mfuko huo taratibu na kuiacha ikiita hadi ilipokatika. Mara ikaita tena, na yeye kwa mara nyingine akaipuuza. Hatimaye akasikia simu yake ikiita. Alipoitoa mfukoni akakutana na jina lilelile: CHRIS. Akaikata.



    Akagonga meza kwa nguvu. Jasho likaanza kumtoka. Akauma meno kwa hasira. Alijua kuwa tayari amekwishajiweka katika mazingira magumu kupindukia. Lakini akapiga moyo konde na kuitoa tena ile bastola. Akaipachika mfukoni.



    Sasa akawaza pa kuipeleka hiyo maiti ya Chaka. Ndiyo, alitaka kuiondoa maiti hiyo haraka iwezekanavyo kabla ya mambo mengine hayajaibuka na zaidi, kabla Chris hajafika. Mara simu yake ikaanza kuita tena, na kwa mara nyingine pia alipokitazama kioo chake, akakuta ni Chris aliyepiga. Safari hii akaamua kuipokea.



    “Chris vipi?”



    “Niko njiani. Vipi, shwari?”



    Badala ya kulijibu swali hilo, Aloyce naye aliuliza, “Umefika wapi?”



    “Niko Ubungo. Mbona Chaka hapokei simu? Hayuko hapo?”



    Aloyce hakujibu. Alikata simu kisha akaizima. Akaitazama tena bastola na kusema, “Hakitoki kitu hapa! Hakuna pesa, hakuna gari!”



    **********





    ASKARI walikwenda mbio barabarani, silaha mikononi. Wakajikuta wakiwa wamecheza mchezo wa kitoto. Chris hakuonekana! Hata walipowauliza baadhi ya watu waliokuwa wakipita pale walijikuta wakiambulia patupu.



    Wakarudi kituoni na kumuuliza Salma, “Hivi yule alikuwa mtu wako wa karibu au tapeli?”



    Salma alikosa jibu. Akazidi kulia. Kwa ujumla alikwishachanganyikiwa. Alikwishaona kuwa kila kitu kimeharibika. Kwamba, kumbe Chris hakuwa mtu wa maana kwake bali ni tapeli mkubwa! Hakutaka kujidanganya kuwa Chris hawezi kuhusika na tukio hilo. Kama hahusiki kwa nini kapotea kinyemela?



    Machozi yalizidi kumiminika mashavuni kwa uchungu. Mara ya mwisho kulia kwa uchungu ni wakati mama yake alipofariki wakati akiwa ndiyo kwanza anahitimu kidato cha sita akiwa na umri wa miaka kumi na minane. Baada ya hapo mtoto huyo wa kike alikasirika na kununa kwa uchungu lakini hakuwahi kulia kwa uchungu.



    Leo analia! Analia kwa uchungu na hasira, ameichukia dunia, ameyachukia maisha na hata kujichukia mwenyewe. Hajali uzuri wa sura nzuri na umbo lake. Anaacha kuketi kitini na badala yake anaketi sakafuni.



    Salma kachanganyikiwa. Anaendelea kulia, kilio cha kimyakimya!



    “Haiwezekani….Nasema haiwezekani…” anaropoka kwa sauti kali kisha ananyanyuka.



    Huyu anajaribu kumsihi atulie, hakubali. Yule naye anambembeleza, habembelezeki. “N’acheni…N’acheni…!” anabwata.



    Hakujali kuwa yuko katika kituo cha Polisi akiwa amezungukwa na askari kadhaa wenye nyadhifa zilizotofautiana. Hakujali.



    Alinyanyuka na kumtazama askari mmoja kisha akaropoka, “Hakuna chochote mnachofanya…Mnalipwa mishahara ya bure! Mtu anawatoroka hapa kituoni hivi-hivi…! Nyie ni magandwa tu hakuna kitu vichwani!”



    Mara akanyanyuka, na kuuweka mkoba wake vizuri begani. Kisha akabwata, “Nipisheni n’ende zangu!” akimsukuma askari mmoja na kutoka.



    Askari wakabaki wameduwaa wakimtazama, baadhi yao wakivutiwa na umbo lake la nyma lililosheheni ujazo wa nyama, umbo lililotikisika kinamna yake kama aliyedhamria kuwaadhibu makusudi.



    **********



    “KAKATA simu au imekatika kwa bahati mbaya?” Chris alijiuliza baada ya kuona simu imekatika. Akajaribu kupiga tena. Alichoambulia ni jibu la SIMU UNAYOPIGA KWA SASA HAIPATIKANI. Akasonya kwa hasira na kutulia kitini.



    Dakika kama kumi baadaye alikuwa nje ya geti la Aloyce Tarimo.







    Akalisukuma geti hilo kwa nguvu na kujitoma ndani. Moja kwa moja akaelekea kwenye kijiofisi cha Aloyce Tarimo. Hakuweza kuingia ndani ya ofisi hiyo. Alimkuta Aloyce kasimama mlangoni huku mlango umerudishwa.



    “Vipi, mbona mambo hayaeleweki?” ni swali lililomtoka Chris mara tu alipoingia.



    “Kwa vipi?” Aloyce naye alimrushia swali.



    Chris akashangaa. Akamkazia macho Aloyce na kugundua kuwa hayuko katrika hali ya kawaida. Kengele ya hatari ikagonga kichwani mwa Chris. Akahisi kuna jambo zaidi ya jambo linaloendelea. “Chaka yuko wapi?” hatimaye alimuuliza Aloyce kwa sauti ya kujiamini.



    “Kishaondoka!”



    “Kwa nini aondoke bila ya kuwasiliana na mimi?” Chris alihoji kwa mshangao. “Na kila nikipiga simu yake haipatikani!”





    “Hayo nadhani hayanihusu,”Aloyce alisema kisha akacheka kidogo, hiki kikiwa ni kicheko kilichompa taswira Chris kuwa huyu hakuwa yule Aloyce aliyemfahamu. Kilikuwa ni kicheko tofauti na kile alichozoea kumsikia Aloyce. Akaongeza: “Kwa kifupi tulishamaliza mchezo. Kila kitu tayari!”



    “Unasema?” Chris aliuliza.



    “Najua umesikia. Siongei Kichaga hapa Bwana Chris!”



    Naam, huyu hakuwa yule Aloyce wa kawaida, Aloyce ambaye walikuwa wakizungumza kwa amani na kuelewana. La. Huyu alikuwa Aloyce mwingine, Aloyce mwenye sura ya kishari-shari.



    “Sijakuelewa Aloyce!” Chris alisema kwa msisitizo huku akiendelea kumtazama.



    “Ni kipi ambacho unataka nikueleweshe zaidi?”



    “Mshiko!” Chris alikoroma kijeuri.



    “Ninapokwambia kuwa nimekwishamalizana naye unakuwa bado hunielewi?” Aloyce alikuwa mkali kidogo, akimtazama Chris kwa macho yake ya kuua!



    “Yaani…Yaani umempa pesa Chaka?!” Chris alikuwa ‘macho nyanya!’



    “Nd’o maana’ake!” Aloyce hakutetereka!



    “Kha! ilikuwaje umpe pesa bila kuniuliza? Yeye anahusika vipi na biashara yetu?”



    Aloyce hakujibu. Alichofanya ni kuachia tabasamu dogo lakini la dhihaka, akionekana kutojali chochote. Hakuwa na sura iliyoonyesha kutishwa na maswali ya Chris.



    “Hapo sikuelewi Aloyce! Sikuelewi kabisa!”



    “Unielewe, usinielewe, kaa ukijua huo ndio ukweli wenyewe!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Hasira zilimpanda Chris. Akauliza, “Kwa hiyo nd’o unataka kun’ambiaje?”



    “Hakuna kingine cha kukwambia, Chris!” Aloyce aliwaka. “Ulimtuma jamaa yako alete mzigo. Kishaleta na nimempa mshiko wenu!”



    “Kiasi gani?”



    “Kama tulivyokubaliana!”



    “Lakini Aloyce, hatukukubaliana kuwa na malipo utampa!”



    “Kwa hiyo haumwamini?”



    “Suala siyo kwamba namwamini au simwamini. Suala ni makubaliano kati yangu mimi na wewe! Kukuletea gari siyo pamoja na kumhesabia keshi! We vipi?!”



    “Kwa hiyo unasemaje?”





    Lilikuwa ni swali baya sana masikioni mwa Chris, swali lililojaa dharau kwa uzito wa kilo mia moja! Yeye Chris ni mtu wa kuulizwa eti, ‘Kwa hiyo unasemaje?’ Hapana hakukubaliana na swali hilo ambalo kwake aliliona kuwa ni tusi.



    Akavuta pumzi ndefu na kujifuta jasho lililojiunda ghafla kwenye paji la uso wake. Kisha akasema kwa ukali dhahiri masikioni mwa Aloyce, “Please, nipe switch!”



    Aloyce aliitarajia kauli hii. Na ndipo alipojua kuwa sasa kulikuwa na mteremko zaidi wa mambo. Akamtazama kidogo Chris kisha akalitazama gari zuri, gari jeusi aina ya Toyota Land Cruiser GX lililoegeshwa hatua chache kutoka hapo walipokuwa. Akaukumbuka ‘mzoga’ wa Chaka ambao bado ulikuwa ofisini kwake, kitini, ukiwa umeiinamia meza.



    “Nipe switch niondoke, Aloyce! Huwezi kuniletea hadithi zisizoeleweka hapa!” Chris aliendelea kubwata.



    “Ok, subiri!” Aloyce alisema kwa sauti ya chini huku akisukuma mlango na kurudi ofisini kwake. Muda mfupi baadaye aliita kwa sauti kali: “Chris!”



    Chris hakufikiri chochote kingine baada ya kusikia akiitwa. Papohapo akausukuma mlango wa ofisi ya Aloyce Tarimo na kuingia. Lakini mara akashtuka na kubaki kinywa wazi. Mbele yake kulikuwa na mwili wa Chaka ukivuja damu huku ukiwa umeegemea sofa.



    “Aloyce!” alibwata huku akiukodolea macho mwili wa Chaka kisha akamtazama Aloyce kwa jicho kali. Akakutana na domo la bastola likimwelekea na macho ya Aloyce yakiwa hayatofautiani na ya simba mwenye hasira!



    Hakupata tamko lolote kutoka kwa Aloyce, bali alihisi kitu kikipenya kifuani na kuzua kijiubaridi cha mbali. Punde kijiubaridi hicho kilitoweka na nafasi yake kutwaliwa na joto na kisha tena kijiubaridi kikarudi. Mara maumivu makali yakamvaa. Nguvu ya kupumua ikaanza kumwishia kwa kasi. Macho yakapoteza uwezo wa kuona. Taratibu, mwili ukaanza kurudi nyuma na sekunde chache baadaye akauangukia mwili wa Chaka pale sofani.



    “Hayo ndiyo malipo yako halali, kenge wee!” Aloyce alisema kwa sauti nzito lakini kali.



    Haikuhitajika risasi ya pili katika kuyasimamisha mapigo ya moyo wa Chris!



    **********



    ILIKUWA ni siku mbaya sana kwa Salma. Alihisi kama vile dunia imemgeuka. Alipotoka katika kituo cha Polisi cha Oysterbay, alikodi teksi iliyompeleka nyumbani kwake Kariakoo. Na mara tu alipoingia ndani mwake alikimbilia jokofu na kutwaa chupa ya bia ambayo aliifungua na kunywa kwa pupa.



    Muda mfupi baadaye alikuwa akiianza chupa ya pili. Nayo akainywa kama ya kwanza. Kisha akazitupa chupa hizo tupu zuliani na kujilaza kwenye sofa kubwa. Akaendelea kuwaza kuhusu tukio hilo la kuhuzunisha na kujikuta akishindwa kukizuia kilio kilichomjia kwa nguvu kubwa.



    Hazikumchukua dakika kumi, usingizi ukamvaa. Akasinzia bila kupenda, pombe na mchanganyiko wa mambo kichwani mwake vikiwa ni vigezo vilivyomfanya ajikute akiwa kama mtu aliyepuliziwa dawa ya nusu-kaputi.



    Alizinduka saa nzima baadaye. Na kilichoukatisha usingizi wake huo wa kiajabu-ajabu ni mlio wa simu yake. Akafikicha macho na kuitazama skrini. Akakumbana na namba ambayo hakuijua. Akaguna huku akibonyeza kitufe cha kupokelea.



    “Heloo naongea na Salma?” sauti nzito iliyafikia masikio yake kwa usahihi.



    “Yeah. Nani wewe?”



    “Hapa ni Polisi Oysterbay. Tafadhali njoo hapa kituoni mara moja!”



    “Kuna nini?” Salma aliuliza huku akionyesha kukereka.



    “Tafadhali njoo mara moja!” ilikuwa ni sauti isiyotofautiana na amri. “Nadhani ni kwa faida yako!”



    Sentensi hii ya mwisho ilimshangaza na kumshtua Salma. Akajitoa sofani haraka na kukimbilia bafuni ambako alinawa uso chapchap kisha akaingia chumbani ambako alijitazama kwenye kioo. Akajiona kuwa yuko vizuri japo macho yalikuwa mekundu.



    Akaitwaa pochi, akaifungua na kuangalia ndani. Akasonya na kuitupa kitandani. Haraka akaifungua kabati kubwa ya nguo. Humo kulikuwa na mkoba wake ambao ulitunza baadhi ya vitu hususan nyaraka zake muhimu. Zaidi, pia alikuwa na mazoea ya kuutumia mkoba huo kwa kuhifadhi kiasi cha fedha alizoamua kuwanazo hapo nyumbani.



    Akaufungua na kutoa kiasi cha shilingi laki moja, akazipachika katika pochi yake ndogo. Akatoka huku akitembea kwa hatua za nusu akikimbia na nusu akitembea. Hakufika mbali, alipofika Mtaa wa Msimbazi akaikuta teksi imeegeshwa. “Haraka, Oysterbay,” alimwambia dereva.



    Teksi ikaingia barabarani. Dakika kama ishirini baadaye dereva alikanyaga breki mbele ya jengo la Kituo ca Polisi cha Oysterbay.









    **********



    MADIBA alikuwa ni mmoja wa wafanyakazi wa Aloyce Tarimo. Yeye alikuwa ni fundi mahiri katika karakana na alijihusisha na idara ya upakaji rangi magari mbalimbali. Kila gari lililoingia katika karakana hiyo kwa njia halali au haramu, mtu wa kwanza kulikagua alikuwa ni Madiba.



    Aloyce Tarimo alimpenda sana Madiba kutokana na utendaji wake wa kazi. Lakini Madiba, katika utendaji wake hapo kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi kadhaa, aligundua kuwa alikuwa ni mtu wa kuumia zaidi huku akimnufaisha zaidi Tarimo.



    Hakuwa akipewa malipo mazuri ya mshahara wake, na alipokuwa akizungumza na tajiri wake kuhusu hilo, aliambulia jibu lisiloridhisha na wakati mwingine akijibiwa kwa dharau: “Kama unaona mambo magumu, mlango uko wazi.”



    Alijiona kuwa yuko mahali pasipomstahili. Ananyanyaswa na kudhalilishwa! Lakini alivuta subira. Hakuwa na haraka ya kuacha kazi ilhali hakuwa na sehemu nyingine ambako angejishikisha kwa wakati huo.



    Hatimaye uvumilivu huo ulimshinda. Siku hii ambayo bosi wake alikuwa ameletewa gari zuri, jeusi aina ya Toyota Land Cruiser GX, alikuwa amegusia juu ya kusaidiwa shilingi 50,000 kwa ajili ya kumuuguza mwanaye.



    Alizungumza na bosi wake huyo, Aloyce Tarimo, saa 4 asubuhi, lakini jibu alilolipata halikutofautiana na yale majibu aliyokuwa akiyapata siku zilizopita.



    “Hivi unadhani pesa inapatikana kwa kuiokota njiani?” Aloyce alimbwatukia huku akimtazama kwa dharau. “ Sina hela aisee!Subiri...labda mwisho wa mwezi naweza kupata pesa ya kukupa!”



    Mwisho wa mwezi!



    Mtoto anaumwa, anapaswa kupelekwa hospitali, bosi anasema subiri mwisho wa mwezi! Yalikuwa ni maneno yaliyomuumiza Madiba kwa kiasi kikubwa. Kuanzia saa hiyo akakosa amani na hakufanya kazi yoyote, zaidi ya kukaa ndani ya gari moja bovu lililokuwa ndani ya karakana hiyo kwa zaidi ya miezi mitatu bila ya kutengenezwa!



    Wakati gari jeusi lilipoingizwa ndani ya yadi hiyo aliliona, lakini hakutoka kule alikokuwa ameketi. Kilichomtoa ni pale aliposikia mshindo mkubwa kutoka ndani ya ofisi ya bosi wake. Wazo la kwanza, ambalo aliliamini ni kuwa mlio huo ulikuwa wa risasi!



    Akavuta kumbukumbu ya mambo yaliyotokea hapo kwa muda mrefu wa siku hiyo. Akakumbuka kumwona mtu mmoja akija mapema asubuhi na gari jeusi aina ya Toyota Land Cruiser na kuingia ofisini kwa Aloyce Tarimo. Kisha wakatoka. Aloyce akaonekana akilikagua gari hilo. Hatimaye mtu yule aliondoka na gari hilo. Ni jioni ndipo alipoliona tena gari hilo likiingia katika yadi hiyo lakini safari hii mwendeshaji akiwa ni mtu mwingine.



    Baada ya muda alisikia mabishano huko ndani ya ofisi ya bosi wake, mabishano yaliyotoa taswira kuwa kulikuwa na dalili za uvunjifu wa amani. Ghafla akasikia mshindo mkubwa kisha ukimya ukafuatia.



    Ni hapo Madiba alipojumlisha moja na moja na kupata mbili! Kengele ya hatari ikalia kichwani mwake! Akatulia ndani ya gari hilo huku akiyahofia maisha yake. Akawaza, afanye nini? Hasira na hofu zikamtawala. Lakini ujasiri bado ulikuwa na nafasi moyoni mwake. Akaamua kutulia akitaka kuona mwisho wa sakata hilo. Hakutoka pale alipokuwa. Na hakutaka bosi wake ajue kuwa yuko hapo.



    Muda mfupi baadaye akaona geti likifunguliwa kwa nguvu na mtu mwingine akaingia huku macho yamemtoka pima. Madiba alivuta kumbukumbu zake haraka na kukumbuka kuwa mtu huyu ndiye aliyekuja mchana na hilo gari jeusi kwa mara ya kwanza. Hii ingia yake ilimfanya Madiba awe makini zaidi. Alihisi kuna jambo zaidi ya jambo linalotokea na jambo hilo si la heri.



    Akashuhudia mtu huyo akikutana na Aloyce Tarimo kwenye mlango wa ofisi ya Tarimo. Wakaanza kuzungumza kishari-shari. Lakini safari hii Madiba alinufaika kwa kushuhudia kukutana kwa watu hawa tofauti na kukutana kwa Aloyce pamoja na yule mtu wa kwanza aliyekuja na kuingia ndani na kisha kutokea mshindo mkubwa.



    Alisikia kila walichokizungumza. Akajua kuwa sasa mambo si mambo. Akakuna kichwa akifikiri. Akili yake ikamtuma kufika mbali katika kushughulikia suala hilo. Akajitoa taratibu pale alipokuwa ameketi. Akatumia uchochoro mmoja uliokuwa nyuma ya yadi hiyo. Alipofanikiwa kuwa nje, akaongeza mwendo na kwenda moja kwa moja hadi kwenye kituo kidogo cha Polisi ambako aliwaambia kuhusu gari hilo na mazungumzo aliyoyasikia kwa Chris na Aloyce Tarimo.



    Askari wa kituo hicho kidogo wakashangaa. Mmojawao akamuuliza, “Unasema wewe ni mfanyakazi wa Aloyce?”



    “Ndiyo!”



    “Una muda gani kwake kikazi?”



    “Zaidi ya mwaka mmoja, lakini sijatimiza miaka miwili.”



    “Isije ikawa umeamua kumchongea kwa sababu zako binafsi! Utafungwa!” alitishwa.



    Hakutishika, akasema, “Sina sababu ya kumfitini! Nazungumza kweli tupu!”



    Askari hao wakazidi kushangaa. Katika eneo hilo, Aloyce Tarimo alijulikana kama mmoja wa watu wasiokuwa na doa katika shughuli zao. Hii taarifa iliyotolewa na Madiba iliwashangaza na kuwashtua.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mmojawao akasema, “Lakini si ajabu. Hawa watu wenye miradi yao mikubwa mikubwa si watu wa kuwaamini sana. Wapo ambao ukiangalia chimbuko la mafanikio yao utabaki kinywa wazi. Ni watu wenye mienendo ya kutisha na wasiokubalika katika jamii yoyote iliyostaarabika.”



    “Ni kweli,” mwingine aliafiki. “Kwa hiyo tufanyeje?”



    “Piga simu Oysterbay,” mkuu wa kituo alimwambia mwenzake. “Kumbuka kuna taarifa ilikuja, kuwa kuna gari limeibwa huko Kinondoni. Na kutokana na maelezo ya huyu bwana ni vizuri tuwape habari kuhusu huyu jamaa na wenyewe wataamua la kufanya. Sisi hatuwezi kumvamia pale kumkamata au kumpekua. Ni zoezi linalohitaji uimara na ukamilifu katika kikosi.”



    **********



    TAARIFA kuwa kuna mtafaruku kwenye gereji moja huko Kimara, gereji iliyomilikiwa na Aloyce Tarimo, ilipomfikia Inspekta Samba akahisi kuna hatua moja kubwa mbele. Kwa kiasi fulani alihisi kuuona mwanga wa mafanikio katika tukio la wizi wa gari mchana kule Kingo House.



    Papohapo akaripoti kwa Mkuu wa Kituo ambaye alimpa kibali cha kwenda huko Kimara haraka iwezekanavyo huku akiwa na kikosi kikubwa cha askari.



    “Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya askari wa Kimara, inaonekana huyo jamaa ni mmoja wa wenye mtandao wa wizi wa magari hapa jijini,” mkuu wa kituo alisema. “Kwa hali hiyo, tunapaswa kwenda tukiwa wakamilifu. Watu wa aina ile huwa wanajizatiti sana kiulinzi.”



    Muda mfupi baadaye Land Rover yenye askari sita wasiokuwa na sare lakini wakiwa na silaha, iliondoka katika kituo cha Oysterbay ikielekea Kimara. Walikwenda moja kwa moja hadi katika kituo cha Polisi cha hapo Kimara. Wakamkuta Madiba akiwa na askari wengine wa kituo hicho.



    Hawakukaa sana, wakaenda kwa Aloyce Tarimo kwa mwendo wa kufa-mtu. Muda mfupi baadaye gari likaegeshwa nje ya uzio wa karakana ya Aloyce Tarimo. Askari hao wakaingia kwa hadhari, kila mmojas akiwa na bastola mfukoni tayari kiwa matumizi kama italazimu.



    Macho yao yakatua kwenye mlango wa ofisi ya Aloyce, ambao ulikuwa ukifunguliwa taratibu kisha Aloyce mwenyewe akatokeza. Macho ya Inspekta Samba na Aloyce yakakutana. Inspekta akahisi kuwa kuna jambo zaidi lililokuwa likitokea. Macho ya Aloyce hayakuwa katika utulivu wa kawaida, yalikuwa na nuru isiyoelezeka kwa urahisi.



    “Vipi, kuna tatizo gani?” Aloyce alihoji huku akiwatazama askari hao kwa zamu, mkono wake wa kulia ukiwa umezama ndani ya mfuko wa suruali, umeikamata bastola ambayo muda mfupi tu uliopita ilitoka kutema risasi mbili dhidi ya watu wawili.



    “Askari Polisi kutoka Oysterbay!” Inspekta Samba alisema kwa sauti iliyojaa uaskari kamili. Na papohapo akaongeza: “Tafadhali twende ofisini kwako.”



    “Kuna tatizo gani?” Aloyce alihoji bila ya kuonyesha dalili ya kuwaruhusu askari hao kuingia ofisini mwake.







    “Tafadhali, usitulazimishe tutumie nguvu. Tuingie ofisini na tutazungumzia hukohuko ndani!”



    Aloyce hakuwa tayari kukubaliana na amri hiyo. Huko ofisini kwake kulikuwa na ‘vimeo.’ Kitendo cha askari hao kuingia humo kingetegua kitendawili cha safari yao. Wangezikuta maiti mbili zikiwa zimekaa shaghalabaghala. Na hapo ndipo mambo yangekuwa mabaya kwa upande wake.



    Afanye nini? Aliwaza haraka na kutambua kuwa kikosi hicho cha askari siyo cha kukifanyia masihara. Akaamua kutumia nafasi hiyo kujiokoa. Ndani ya bastola yake kulikuwa bado na risasi saba ambazo aliamini kuwa zingemsaidia.



    Kwa kasi ya umeme akaichomoa bastola hiyo na kumlenga Inspekta Samba usoni. Likawa ni tukio lililochukua sekunde mbili tu! Sekunde ya kwanza bastola ilimtazama Inspekta na sekunde ya pili, risasi ilitua katika paji la uso wake na kukifumua kisogo chake kiasi cha kuacha sura inayoogofya.



    Inspekta hakuomba maji!



    Wakati mwili wa Inspekta Samba ukielekea chini, Aloyce alikuwa amekwishaigeuzia bastola kwa askari wengine, lakini hakufanikiwa kufanya chochote kingine alichodhamiria! Mmoja wa askari waliokuwa katika msafara huo alikuwa mwepesi zaidi. Yeye tayari alikuwa ameitoa bastola yake na kukilenga kichwa cha Aloyce kwa shabaha kali. Hakumkawiza, risasi mbili zikamtoka papohapo!



    Mlipuko mwingine ukatanda hewani huku Aloyce akirushwa juu na kuanguka chini kwa kishindo tii! Haukuhitajika uthibitisho wa daktari kuwa tayari Aloyce kafa!



    **********



    HATIMAYE askari wengine walibaini kuwa Chaka na Chris walishauawa na miili yao ilikuwa ndani ya ofisi ya Aloyce. Maliki, mmoja wa askari hao, akatwaa nafasi ya uongozi wa msafara. Akamgeukia Madiba na kumuuliza, “Huyu bosi wako alikuwa na kawaida ya kuleta magari ya wizi hapa?”



    “Ilikuwa ni kawaida yake!”



    “Na hili gari lililetwa lini?”



    “Leo.”



    “Saa ngapi?”



    “Kwanza lilikuja saa saba hivi likiwa na huyu marehemu,” Madiba akajibu huku akimaanisha Chris. “Kwenye mida ya saa tisa kwenda saa kumi ndipo likaletwa na huyu,” akamwonyesha Chaka.



    Mara mmoja wa wale askari akaguna na kuchomopa kijitabu chake mfukoni, kisha akafunua ukurasa fulani na kusoma. Ghafla akaisogelea ile gari na kutamka kwa sauti ya chini lakini ya kujiamini. “Hii ni ile gari iliyoibwa leo mchana kule Kingo House!”



    Askari wengine wakashtuka na kumfuata. Askari huyo akawaonyesha namba za gari hilo kutoka kwenye kijitabu chake cha kumbukumbu.



    “Yeah, ni lenyewe!” askari mwingine alisema huku akilisogelea gari hilo.

    Muda mfupi baadaye eneo hilo likuwa chini ya ulinzi mkali, na ndipo ilipotolewa taarifa kwa Mkuu wa Kituo cha Oysterbay kuwa inaaminika gari hilo liliibwa mchana eneo la Kinondoni, Kingo House. Pia imethibitika kuwa ni gari la mtu aitwaye Salma aliyeripoti mchana wa siku hiyohiyo juu ya kuibwa kwa gari lake, yeye akiwa ndiye mmiliki halali.



    Kilichofuata ni kumpigia simu Salma kabla ya hatua nyingine kuchukuliwa.



    ******



    KAUNTA ya Kituo cha Polisi cha Oysterbay ilikuwa na askari wawili tu, mwanamume na mwanamke. Salma alipoteremka kwenye teksi alikwenda moja kwa moja na kuwavaa askari hao kwa: “Vipi kuna nini! Nimepigiwa simu kuwa nije hapa haraka!?”



    “Ok, subiri kidogo,” askari wa kike alisema huku akinyanyua simu na kuongea. Muda mfupi baadaye askari mwingine alitokea na kumuuliza, “Salma, una usafiri?”



    “Usafiri?!” Salma alimtazama kwa macho makali, uso kaukunja.



    “Ndiyo. Nina maana yangu kukwambia hivyo. Kwa kiasi fulani tumepiga hatua katika kufuatilia suala lako. Tunachotakiwa kufanya ni kwenda huko kwenye tukio ili kuthibitisha.”



    “Gari langu limepatikana?!” Salma alihoji kwa mshangao, macho kayatoa pima akimtazama huyo askari.



    “Siwezi kusema NDIYO au HAPANA,” askari huyo alijibu kwa upole. “Ninachoweza kukwambia ni kwamba hapa tuna uhaba wa vyombo vya usafiri. Na tunatakiwa kufika Kimara kwa ajili ya kufuatilia suala hili. Lakini naweza kusema kuwa tumepiga hatua kubwa ya mafanikio.”



    Salma alihema kwa nguvu na kuuliza, “Tutapata wapi teksi?”



    “Twende hapo barabarani. Hatutachukua hata dakika tano kupata teksi.”



    Muda mfupi baadaye walikuwa kando ya Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, na hawakuchukua hata dakika tano, teksi ilisimama kando yao.



    Yule askari akaingia mbele na Salma nyuma. “Kimara,” askari alimwambioa dereva teksi. “Tuna haraka! Kama unaweza kupaa angani itakuwa vizuri zaidi, mradi tu ujali usalama wetu.”





    Teksi ikala lami, kila mmoja akiwa kimya. Wakati huo mapigo ya moyo wa Salma yalikuwa katika hali isiyo ya kawaida. Hakujua kama kweli huko wanakokwenda kuna mafanikio. Na hakutaka kudadisi chochote.



    Baada ya dakika isihirini, kwa mawasiliano yaliyokuwepo katika ya askari huyo na askari waliokuwa Kimara, hatimaye walifika nje ya geti la ofisi ya Aloyce Tarimo.



    “Gari languuuu!” Salma alibwata kwa sauti kali huku akijishika kichwani. Wakati huo walikuwa wamepenya getini na kuwakuta Madiba na wale askari wengine wasiokuwa na silaha.



    Hakujali kuwa wakati huo mwili wa Inspekta Samba ulikuwa pale chini ukivuja damu, au ichukuliwe kuwa hakuweza kupeleka macho kwingine zaidi ya kwenye gari, Toyota Land Cruiser jeusi lililokuwa mbele yake. Mara akalikimbilia akitaka kuingia. Hakufanikiwa kutimiza azma yake.



    Askari mmoja alimzuia. “Taratibu mama,” askari huyo alimwambia huku akimvutia pembeni ambako alimwambia kwa sauti ya chini, “Hapa mambo si mazuri. Tukimwacha huyu mkuu wetu, kuna watu wawili wameuawa hapa na maiti zao ziko ndani. Mmoja wa watu hao inaaminika kuwa ni yule mtu wako wa karibu uliyekuwa naye kule Kingo House na ukaja naye kituoni Oysterbay.”



    “Nani?! Chris?” Salma alibwata kwa sauti iliyojaa mshangao na woga.



    “Ndiyo,” askari yule alijibu. “Lakini tulia, mama. Usiwe na papara. Tatizo hili limefikia mwisho. Ni lazima sasa ufumbuzi utapatikana.”



    Mara akaja Martin Peka, yule askari aliyetoka na Salma kule Kituo cha Polisi cha Oyesterbay. Akamgusa bega huyu askari aliyekuwa akiongea na Salma. “Nipe taarifa. Ni kipi kilichoendelea?”



    “Kuna maiti mbili ndani ya ofisi ya huyu marehemu Aloyce.”



    “Za nani na nani?”



    “Moja ni ya yule aliyekuwa na anti kule kituoni.”



    Askari huyu akashangaa na papohapo akasema, “Twendeni ndani tukashuhudie.”



    Wakaanza kuelekea ofisini kwa hatua ndefu. Yule askari maalumu akausukuma mlango na kutangulia kuingia. Martin Peka naye akafuata huku akimshika mkono Salma.



    Macho ya Salma yalipotua kwenye mwili wa Chris, yowe likamtoka, yowe kali lakini fupi. Akatulia huku macho yamemtoka pima, akiutazama mwili wa Chris kama asiyeyaamini macho yake. Kwa sekunde chache aliutazama mwili wa Chaka na akagundua kuwa ni mtu ambaye hakumfahamu hata kidogo.



    “Khaaa! Chrisss!” hatimaye alibwata kwa uchungu lakini kwa sauti ya chini, safari hii mkono wa kulia ukiwa umeganda kwenye kidevu chake na kinywa kikiwa wazi. Kumbukumbu ya jinsi uhusiano baina yake na Chris ulivyoanza na hatimaye kukomaa ikamjia akilini.



    Vitenge! Chris alimwingia kwa hila akimdanganya kuwa yeye ni mfanyabiashara wa vitenge. Na wakati huohuo, saa kadhaa baadaye, moyo wa Salma akawa umetekwa na Chris. Akawa akimhitaji, zaidi ya hitaji la biashara ya vitenge.



    Zile sifa alizompa wakati alipokuja nyumbani kule Mtaa wa Rufiji jioni na zile bia walizokunywa vilikuwa ni vichocheo vingine vilivyomwondolea aibu ya kumfanya alinase windo lake. Na alikuwa na mazoea ya kukandwa mwili kila Abdulrahman Sadick alipokuwa Dar. Hilo lilikuwa ni zoezi ambalo liligeuka kuwa sheria kwa kufanyika kila baada ya siku mbili, tatu.



    Kutokuwepo kwa huyo Mpemba wake kukamwathiri kiasi cha kujikuta damu ikimchemka maradufu na hasa jioni hiyo alipokuwa na mgeni huyo ndani sebuleni siku ya kwanza wakipata vinywaji.



    Ikawa ni siku iliyofungua ukurasa mpya pale nguo zilipochojolewa hapohapo sebuleni na kufanyika kile walichodhamiria kukifanya.



    Penzi likakolea.



    "Kumbe ni jambazi…kumbe nilikuwa nimeingia choo cha… jamani wanaume…! Chris huyuhuyu leo kanigeuka na kuniibia gari!"



    HITIMISHO

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakati jua lilipokuwa likipotelea upande wa magharibi mwa Jiji la Dar es Salaam, Salma alikuwa akiondoka katika eneo la Kituo cha Polisi cha Oysterbay baada ya mamlaka hiyo kumkabidhi rasmi gari lake aina ya Toyota Land Cruiser GX jeusi. Aliondoka huku akimshukuru Mungu kwa kulimaliza tatizo hili.



    Akashusha pumzi huku akibadili gia wakati akiingia Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, akirudi nyumbani Kariakoo. Gari lilipotulia barabarani, alifungulia muziki kisha akawasha kiyoyozi. Lakini bado hakuwa na amani moyoni. Alijisikia kuwa na hasira. Ndiyo, aliwachukia wanaume. Wanaume wote duniani isipokuwa baba yake mzazi na mpenzi wake, Abdulrahman Sadick.





    ****MWISHO***

0 comments:

Post a Comment

Blog