Search This Blog

Saturday, 5 November 2022

MILIONI THELATHINI - 4

 








Simulizi : Milioni Thelathini

Sehemu Ya Nne (4)









MOYO wake ukiwa na faraja kwa kupiga hatua moja muhimu katika utekelezaji wa malengo yake, Chris alimtazama Salma kwa chati na kuachia tabasamu dhaifu kisha akamuuliza, “Utaongeza?”



“Hapana. Sijazoea kunywa zaidi ya bia mbili, mchana. Leo nimekunywa tatu, ni nyingi sana.”



“Sawa,” Chris alisema na kuongeza: “Lakini leo siyo kama siku nyingine. Leo hakuna jua. Manyunyu haya na kijiubaridi hiki kinamruhusu mtu kunywa hata bia tano.”



“Ni kweli, lakini hii hali ya hewa inawafaa wapendanao, na wawe chumbani, kitandani. Twen'zetu. Kama ni kunywa tutakunywa hukohuko nyumbani.”



“Huko nyumbani bia zitanyweka kweli kwa kijiubaridi hiki? Au ndio itakuwa hiyo ndiyo hali inayowastahili wapendanao?” Chris alitia mzaha.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Vyovyote vile. Kwani kuna kipangamizi?”



“Kwa vyovyote kutakuwa na mengineyo.”



“Hayo mengineyo ni jambo la kawaida na ni muhimu kwa wapendanao.”



“Tunywe basi moja-moja za mwisho,” Chris alikuwa king'ang'anizi.



“Hapana, bwana,” Salma alikaza uzi. “Twen'zetu. Bia zilikuwepo, zipo na zitaendelea kuwepo. Tutakufa na kuziacha. Ya nini kuwa waroho?”



Papohapo Salma akanyanyuka na kuutia mkoba wake begani. Akageuka na kuangaza macho kule alikoegesha gari awali. Akakunja uso na kutazama kwa makini zaidi. Wakati huo Chris naye alikwishanyanyuka na akawa akitiririsha kooni mwake bia iliyokuwa ndani ya glasi huku kwa chati akimtazama Salma.



“Hivi...” Salma alisema na kusita. Akaendelea kukodoa macho kule alikotarajia kuliona gari lake. Kisha akaendelea, “ Uliporudi ulipaki gari palepale?”



“Palepale,” Chris alijibu baada ya kuitua glasi mezani. Kisha naye akatupa macho kule getini. Japo kulikuwa na magari zaidi ya matano katika eneo hilo, hata hivyo haikuwa vigumu kuliona lile Land Cruiser jeusi. Magari mengine yaliyokuwa hapo yalikuwa ni madogo aina ya Corolla, Chaser na kadhalika.



Hakukuwa na Land Cruiser lolote; liwe jeupe, jekundu, jeusi hata la rangi isiyojulikana. Kwa vyovyote vile gari lile jeusi la Salma lingeonekana kwa uwazi. Lakini macho manne ya Salma na Chris hayakuliona!



“Mbona silioni?” sauti ya Salma ilitoka kwa kitetemeshi cha mbali. Akavuta hatua akielekea getini, Chris nyuma yake. Macho yalimtoka Salma. Sasa akaanza kukimbia.



“Halipo!” alibwata baada ya kufika pale lilipokuwa Land Cruiser lake. Akamgeukia Chris na kumtazama kwa macho makali.



“Mbona nililipaki hapa? Si uliniona?” Chris aliuliza huku akilitazama eneo ambalo alidai kuwa ndipo alipoliegesha gari wakati aliporejea.



“Ndiyo, nilikuona! Lakini mbona halipo?! Liko wapi?”



Chris akionyesha mikunjo usoni, aliwafuata wale walinzi na kuwauliza kwa ukali, “Nyie si nd’o walinzi wa hapa?”



“Ndiyo!” mlinzi mmoja alijibu.



Mwingine akauliza, “Kwani vipi?”



Chris akawakazia macho zaidi, akiwatazama kwa zamu, mmoja baada ya mwingine. “Gari letu liko wapi?!” akawarushia swali kwa ukali.



“Gari gani?”



“Land Cruiser jeusi!” Chris akajibu haraka. “Land Cruiser GX jeusi. Liko wapi?”



Mmoja wa walinzi hao akanyanyuka na kusema kwa kujiamini, “Gari lenu! Gari lenu lipi hilo?! Gari lililokuwa hapo aina ya Land Cruiser jeusi lilishaondoka!”



“Lilishaondoka?!” Salma aliwauliza kwa hamaki. “Nani aliyeondoka nalo wakati ni mimi ndiye mwenye nalo?”



“Wewe!” walinzi wale walitamka kwa pamoja, mshangao ukizitawala nyuso zao.



“Mimi, ndiyo!” Salma alisisitiza.. “Ni mimi! Kwani hamkuniona nilipoingia hapa kitu kama saa saba kasoro? Hamkuniona?”

Wale walinzi waliguna. Wakatazamana

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/







Kwa ujumla hawakuwa na kumbukumbu ya yaliyojiri zaidi ya saa mbili zilizopita. Salma akamgusa begani Chris huku akiwatazama hao walinzi, macho yakiwa yamemwiva. Akaongeza, “Na huyu anko alipoondoka na kurudi nalo pia hamkumwona?”



“Lakini shangazi...” mlinzi mmoja alisema kwa mashaka.



“Lakini nini?” Salma alimkata kauli huku akiufungua mkoba wake na kutoa funguo kadhaa zilizokuwa pamoja. Akautoa ufunguo mmoja na kuunyosha juu. “Hii ndiyo swichi yake. Mnataka kun'ambia nini?Mnataka...”



“Mtatueleza...mtatueleza vizuri...” Chris alishawafikia na kuwakwida mashati kwa pamoja. Akawasukasuka huku akiwauliza, “Bosi wenu yuko wapi? Semeni nyie mbwa! Bosi wenu yuko wapi?” Kabla hajajibiwa akawapiga ngwala, wakaanguka kama magunia ya mashudu puu! Papohapo akamgeukia Salma huku akihema kama nguruwe pori.



Akabwata:“No! Haiwezekanai! Hapa kuna jambo! Kuna hujuma imefanyika! Haiwezekani!”



Salma hakuwa na kauli. Machozi yalimtoka kwa wingi, kwikwi zikambana. Pumua yake ikawa ya shida. Nguvu zikamwisha maungoni. Akaketi chini bila ya kujali maji-maji ya manyunyu ya mvua iliyoendelea kunyesha.



Kwa jumla alihisi yu ndotoni, tena hii ikiwa ni miongoni mwa ndoto mbaya sana alizowahi kuota tangu azaliwe. Ndiyo, alijihisi yu ndotoni lakini ukweli ni kuwa hii haikuwa ndoto bali ni tukio halisi ambalo pia lilimchanganya akili kwa kiwango kisichokadirika.



Mara alikurupuka kunyanyuka, akajipigapiga kifuani kwa uchungu huku machozi yakiendelea kumtoka kwa wingi. Akamtazama Chris kisha akayahamishia macho kwa wale walinzi wawili. Akafumbua mdomo ili atamke neno.



Akashindwa kufanya hivyo. Akashusha pumzi na kurudi kuketi palepale chini. Wakati yuko hapo chini, kwa mbali akili ikaanza kutulia. Na ni hapo kumbukumbu ilipomjia kichwani, kumbukumbu ya kila alichokifanya na kila kilichojiri siku hiyo.



Ni asubuhi ya siku hiyo Chris alipomtaka waimalizie wiki kwa kutembelea katika maeneo mapya. Na alipendekeza mchana wa Jumamosi hiyo wakapate chakula cha mchana hapoKingo House BarabarayaKinondoni. Kwa hilo waliafikiana. Saa 6.30 alikuwa akiingia hapo Kingo House na hilo gari lake.



Akamkuta Chris kishafika na wakaagiza chakula; yeye, Ndizi-Bukoba kwa kuku na Chris, ugali kwa mugebuka, samaki maarufu wa Ziwa Tanganyika. Hakusahau kuwa muda mfupi baada ya kuanza kula, Chris alisema kuwa amesahau kumchukulia jamaa yake fedha benki, na kwamba jamaa huyo walikubaliana kukutana hapo, hivyo akamwomba ufunguo wa gari ili aende benki ya CRDB, Tawi la Azikiwe kushughulikia suala hilo.



Alikwenda, akarudi. Kwa hilo, Salma alikuwa na hakika nalo. Kwa macho yake alimwona Chris akipita getini na alipoliegesha gari alimletea funguo zake. Sasa eti gari halipo! Limetokaje ilhali funguo anazo yeye? Labda lingekuwa limevutwa na gari maalum la kuvuta magari, hapoangeelewa. Lakini hata hivyo lazima angeona, na watu wengine walioko hapo wangeona.



Kitendo cha gari moja kuvuta gari jingine hakiwezi kufanyika kwa siri hususan sehemu kama hiyo ambayo imejaza magari na watu. Kwamba gari lake limeondoka kwa kuvutwa na gari jingine ni wazo lililoota mbawa wakati huohuo. Wazo likamwangukia Chris; kwamba labda angedai kuwa katorokanalo.



Lakini na Chris naye tangu arejee hajatoka tena! Na hadi sasa wako wote hapa getini! Ni kipi kilichotokea?Ni kiinimacho?Anaota? Hapana, hiki siyo kiinimacho wala siyo kwamba yuko ndotoni. Alikuwa timamu.



Sasa alikusanya nguvu, akanyanyuka tena. Akajifuta machozi kwa kutumia viganja vya mikono yake. Kisha akamsogelea Chris na kumgusa begani. Chris alipogeuka alikumbana na swali:“Ni kipi kinachoendelea?”



Chris alimtazama kasha kwa mara nyingine, akabwata, “Haiwezekani! Nasema haiwezekani!”



Mara simu yake ikaita. Akaitoa mfukoni na kuiegesha sikioni. Maneno machache tu, maneno ambayo huenda alikuwa akiyatarajia, yakamfikia.“TAYARI, NIKO KWA TAJIRI NA MZIGO, SALAMA SALIMINI.”



Chris hakujibu kitu. Aliikata simu na kuirudisha mfukoni. Akawageukia tena wale walinzi. Akawatazama kwa macho yake makali, mikono ikiwa imekunja ngumi huku midomo imeumana kwa hasira. Kisha akamgeukia Salma, akilikumbuka swali aliloulizwa punde.



Salma alijaaliwa macho malegevu, macho ambayo kwa vyovyote vile humvutia mwanamume mpenda wanawake wazuri. Hayakuwa macho makubwa wala madogo, fikiria mwenyewe yalikuwaje kasha ujumlishe na aina yake ya utazamaji kabla hujazidisha na urembuaji wake wa asili.



Salma alikuwa na sauti nyororo, sauti iliyopendeza masikioni mwa mwanamume yeyote na katika unyororo huo haikuwa kali sana, haikuwa nzito japo hata ukiisikia bila ya kumwona lazima utabaini kuwa ni ya mwanamke. Hayo ndiyo yaliyokuwa macho yake, na hiyo ndiyo iliyokuwa sauti yake.



Lakini alasiri hii, hapo getini, Kingo House hakuitumia sauti hiyo wala hakumtazama Chris kwa ile tazama yake ya kawaida. Hilo lilikuwa dhahiri hata kwa Chris ambaye alishamzoea kwa aina moja ya kutazama na aina moja ya sauti. Labda tunaweza kusema huyu alikuwa ni Salma mwingine, Salma mwenye macho makali, macho ambayo hayakuwa hata na chembechembe za kitu kiitwacho “UREMBUAJI.”



Haya yalikuwa ni macho yaliyotisha, macho yenye kutamka neon moja tu: “UNAHUSIKA!” Labda tunaweza kusema kuwa huyu ni Salma mwingine, Salma mwenye sauti kavu, sauti yenye kijimkwaruzo cha mbali na kinachokera, sauti ambayo licha ya Chris kutoisikia tangu uhusiano wao uzaliwe, ni sauti inayoashiria shari.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Nakuuliza wewe? Ni kipi kinachoendelea?” kwa mara nyingine Salma alimuuliza.



“Nadhani tuwasiliane na uongozi wa hoteli,” Chris alijibu huku akimtazama Salma kwa ujasiri wa kulazimisha.



Ni vile tu yeye alikuwa ni mwanamume lakini moyoni mwake alikiri kuwa Salma huyu ni kama alikuwa akimwona mpaka moyoni mwake.



“Tuwasiliane na uongozi?!” Salma alikuwa mkali.“Tuuone uongozi... uongozi utatusaidia nini?”



“Tulia,” Chris alimtuliza huku akimgusa begani.“Jambo hili ni zito.Twende taratibu tusije haribu mambo.”



“Lakini Chris,” Salma alimshika mkono, “unadhani ufumbuzi ni kuwasiliana na utawala wa hapa au kuiripoti Kingo House polisi?”



“Yote ni mazuri,” Chris alijibu kwa utulivu. “Lakini nadhani hatuaya kwanza ni kutoa taarifa kwa utawala wa jingo hili. Polisi ni hatua ya pili.”



“Unadhani itasaidia?”



“Naamini itasaidia.”



“No! Haitasaidia!” ni kama vile Salma alikuwa akifoka. “Kingo House hawawezi kunirudishia gari langu...” akasita ghafla. Kisha akamkazia zaidi Chris macho yake yanayotisha. “Sikia Chris. Thamani ya gari langu siyo ndogo kama unavyoweza kuikadiria! Nataka ulitambue hilo! Na sitaki kukuficha; naamini wizi umefanyika! Gari langu limeibwa! Namna lilivyoibwa, nani aliyeiba na nani anahusika na wizi huo, Mungu ndiye anajua. Na sikubali, ama gari langu lirudi, au mtu aingie jela! Hivyo ndivyo itakavyokuwa!”



“Siyo wewe tu unayeamini kuwa gari limeibwa!” Chris alisema kwa kujiamini. “Hata mimi naamini hivyo. Na ndiyo maana unaniona nimewaweka sawa hawa washenzi!” Hapo aliwageukia tena wale walinzi na kuwatupia macho makali.



“Siki'za Chris,” Salma aliishusha sauti. “Sidhani kama kuna haja ya kuzua mjadala kama tuko Dodoma, bungeni. Nawasiliana na Polisi Oysterbay sasa hivi. Kitakachofuata n'takwambia.”







Papohapo akaitwaa simu yake ya mkononi na kuzungumza kwa takriban dakika mbili kisha akaizima. Akamgeukia Chris. “Tuwasubiri, wanakuja,” alisema.



“Tuwasubiri?!”



“Nd'o maana'ake! ”



Chris alikunja uso kisha akamuuliza, “Hivi unayajua vizuri mambo ya Polisi?” hakusubiri jibu. Akaendelea kumimina maswali kama anasoma shairi. “Unaamini kuwa watakuja? Polisi wa Tanzania unawajua au unawasikia tu? Na hata kama watakuja, watakuja baada ya muda gani? Wakifika hapa baada ya nusu saa unadhani mwizi wa gari hilo atakuwa amefika wapi? Na huo ujio wao utasaidia nini? Gari litarejeshwa?”



“Watakuja!” Salma alisema bila ya kujali mlolongo wa maswali aliyoulizwa. Akaongeza, “Watakuja! Ni lazima tuwasubiri hata kama watakuja baada ya leo. Na ninaamini kuwa ujio wao utasaidia hata kama gari langu halitapatikana. Kumbuka nimesema kuwa ama gari langu lirudi au mtu aingie jela. Umenielewa?!”



**********



GARI jeusi, gari maridadi, Toyota Land Cruiser liliegeshwa ndani ya eneo lililomilikiwa na Aloyce Tarimo dakika kumi tu baada ya Chaka kuling'oa pale Kingo House. Muda mfupi baadaye Chaka alikuwa ndani ya ofisi ya Aloyce Tarimo. Chaka alimwingia Aloyce Tarimo kwa maneno machache tu: “Mchezo umekwisha. Kazi kwako.”



“Nimeona,” Aloyce alisema bila hata ya kumtazama Chaka. Akawa akiendelea kupekuapekua nyaraka zilizokuwa mezani pake. Takriban dakika nzima ikakatika akiwa na hili zoezi lake. Kisha akaunyanyua uso na kumtazama Chaka kwa namna isiyoashiria mzaha wa aina yoyote.

“Haukupata tatizo lolote?” hatimaye alimuuliza.



“Tatizo litoke wapi?” Chaka alijibu kwa mfumo wa swali. “Kama unavyotujua, hatufanyi mambo yetu kwa kubahatisha.”



Ni kama vile Aloyce alikuwa hamsikilizi. Alikuwa akiendelea kuchakurachakura katika moja ya saraka za meza yake, macho akiwa ameyazamisha ndani ya saraka hiyo.



Hatimaye akaunyanyua tena uso na kumtazama Chaka sawia. “Kwa hiyo?”



“Nakusikiliza wewe.”



“Ok, nadhani tumsubiri Chris,” Aloyce alisema. “Mradi umeufikisha mzigo ukiwa salama, basi tuvute subira. Mambo haya yanapaswa kwenda kwa utaratibu unaoeleweka. Kwani umemwacha wapi?”



“Kulekule.”



“Kulekule wapi? Una maana huko ulikouchukulia mzigo?”



“Nd'o maana'ake.”



Aloyce alikunja uso, akaitwaa chupa kubwa ya maji iliyokuwa hapo mezani. Akagugumia mafunda kadhaa kinywani kisha akaitua. Akamkodolea tena macho Chaka. “Amebaki anafanya nini?” aliuliza.



“Kuna mambo madogomadogo anashughulikia,” Chaka alijibu. “Lakini kuja, atakuja tu. Na, nadhani hazitazidi dakika kumi au kumi na tano. Atakachokuwa akikifanya saa'izi ni kuweka mambo sawa.”



Dakika kumi zilikatika Chris hajafika.



Dakika ishirini!



Mara Aloyce akaitwaa simu na kumpigia Chris. Wakati akisubiri alisikia simu ikiunguruma kwa muda mrefu, hali iliyotoa taswira kuwa huko upande wa pili simu ilikuwa ikiita lakini haipokewi. Ikaita, ikaita hadi ikakatika.



“Kha!” Aloyce alibwata huku kakunja uso. Akamtazama tena Chaka, safari hii sura yake ikionyesha bayana kakereka. “Huyu mtu vipi?”



“Kwani vipi?” Chaka naye alimuuliza.



Sasa nyuso zao zikaonyesha mshangao. “Hapokei simu!” Aloyce alitamka kwa ukali.



“Hapokei?!” Chaka naye akatoa macho pima. Akaitwaa simu yake na kumpigia Chris. Tofauti na Aloyce, yeye aliambulia jibu: NAMBA ULIYOPIGA KWA SASA HAIPATIKANI TAFADHALI JARIBU TENA BAADAYE.



“Kaizima!” Chaka alibwata.



“Kaizima?!” Aloyce alihoji kwa mshangao. “Hajaizima! Sasa hivi tu nimepiga nikasikia inaita!”



“Hebu piga tena.”



Aloyce alipiga tena. Sekunde chache baadaye akaachia kinywa wazi kwa mshangao mwingine; jibu alilopewa Chaka ndilo pia lililomfikia yeye.



“Kuna nini?” walijiuliza.



*****



MTETEMO wa simu ya Chris mfukoni mwake ulimshtua, na kabla hajaitoa akawa ameshahisi mpigaji ni nani. Kama siyo Chaka basi ni Aloyce. Alihisi hivyo kwa kuwa tangu Chaka aondoke tayari zilishapita dakika zaidi ya kumi pasi ya mawasiliano. Aliitoa simu hiyo na kuitazama. Jina la ALOYCE likatawala katika kioo cha simu.

Alitaka kuipokea lakini akasita. Na alikuwa na sababu ya kusita; angeongea naye nini wakati huo ambao Salma alikuwa kando yake akionyesha dhahiri kutokuwa timamu kifikra? Kwa vyovyote vile Salma angehisi kitu.



Hivyo alichokifanya ni kuiacha iite hadi ikakatika. Na hapo ndipo alipoamua kuizima kabisa kwani alihisi kuwa Aloyce angepiga tena, na kama siyo yeye, basi Chaka angepiga.



Baada ya kuizima aliirudisha mfukoni na kumgeukia Salma ambaye haikuhitaji kutumia hata sekunde tano kuutambua mfadhaiko uliomkumba. Hakuonyesha kumjali Chris bali macho yake yaliangaza katika Barabara ya Kinondoni akilitazama kila gari lililopita. Hatimaye, dakika kadhaa baadaye aliliona gari jeupe, Land Rover- defender likisimama nje ya geti la Kingo House.



Ndani ya gari hilo, kwa mbele, zaidi ya dereva pia kulikuwa na watu wawili, mmojawao akiwa amevaa sare za Jeshi la Polisi. Nyuma kulikuwa na watu watatu, wanaume ambao hawakuwa katika mavazi ya kiaskari. Kabla geti halijafunguliwa, wote hao waliteremka na kulisukuma geti. Wakaingia kwa hatua za kiaskari, wakiwafuata Chris na Salma.



“Ndiyo,” alianza yule askari mwenye sare, wakati huo akimtazama Salma kwa makini. Akaongeza, “Ni wewe uliyepiga simu?”

“Ndiyo,” Salma alijibu.



“Hebu nieleze vizuri mkasa ulivyokuwa.”

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Salma alimwambia kila kitu bila kuficha.



Askari wote na hata wale walinzi walimsikiliza kwa makini huku wakiwa wamemkodolea macho.



“Gari lako ni namba ngapi?” mkuu wa msafara wa wale askari alimuuliza Salma.



Salma akazitaja namba za gari lake. Wakati huo, askari mwingine alikuwa akitumia simu kuwasiliana na askari wengine waliotapakaa katika barabara za ndani na zinazotoka nje ya Jiji la Dar es Salaam.



“Na huyu ni nani?” askari huyo aliendelea kuhoji, safari hii akimtazama Chris.



“Ni rafiki yangu.”



“Mlikuwa pamoja kabla na baada ya tukio?”



“Tulikuwa pamoja.”



Mara askari huyo akawageukia wale walinzi. “Na nyie?” aliwauliza kwa mshangao.



“Sisi ni walinzi wa hapa, afande,” mlinzi mmoja alijibu haraka.



“Walinzi!” askari yule aliwatazama kwa mshangao mkubwa zaidi. “Walinzi gani na gari limeondoka mkiwa hapahapa?!”



“Afande...unajua...” mlinzi mmoja alijitahidi kujitetea lakini hakuipata fursa hiyo.



“Najua nini?” askari aliwaka. “Sijui! N'ambieni ni kwa nini tusiwachukulie kuwa nyie nd'o wezi wenyewe?”



“Siyo sisi, afande,” mlinzi mwingine alisema. “Kwa kweli kilichotokea ni kama vile mazingaombwe, afande.”



“Mazingaombwe! Mazingaombwe nd'o mdudu gani?” askari huyo alifoka, macho yake makali yakimtazama mlinzi huyo. “Hebu simameni haraka!”



Walinzi wale walinyanyuka huku wakijifuta michanga iliyoganda kwenye nguo.









“Ingieni garini,” amri nyingine. Kisha, akiyarejesha macho kwa Salma, alisema, “Suala lako ni gumu. Uongozi wa juu wa hapa una taarifa?”



“Hapana,” Salma alijibu.



“Yaani umewasiliana na sisi kabla haujafikisha taarifa kwao?”



“Ndiyo. Na sikuona umuhimu wa kuharakisha kuwaambia hao.Wangenisaidia nini?” Sauti ya Salma ilikuwa kavu, macho yake yaliyovimba kwa uchungu yakimkodolea Inspekta Samba bila ya kupepesa.



Inspekta aliguna. Akawageukia askari wenzake ambao hawakuwa na sare. “Tia pingu hao walinzi. Tutakwenda nao Oysterbay.” Kisha tena akawageukia Salma na Chris na kuwaambia, “Twendeni tukamwone Meneja.”



“Lakini wa nini, afande?” Salma alihoji.



“Nyie twendeni! Mengine tutayajulia hukohuko!”



Tayari Inspekta Samba alishaanza kutembea. Chris na Salma wakamfuata. Hawakufika mbali, mara wakakutana na mhudumu mmoja wa kike akiwa na chupa za soda.



“Binti,” Inspekta Samba alimsimamisha. “Namhitaji Meneja wa jengo hili haraka.”



Mhudumu huyo akionyesha dhahiri kukumbwa na fadhaa, alisema, “Yuko ofisini.”



“Ofisi yake iko wapi?”



“Twendeni niwapeleke.”



Wakamfuata kimyakimya.



**********





“YAANI huna taarifa yoyote?” Inspekta Samba alimhoji Sanga Makela, Meneja wa Kingo House, baada ya kumweleza taarifa alizopewa na Salma.



“Kwa kweli ni wewe ndiye uliyenipa taarifa hiyo,” Sanga alijibu kwa kujiamini. “Nina zaidi ya saa mbili humu ofisini. Sijatoka hata kwenda toilet.”



“Basi hali ndiyo hiyo, meneja,” Inspekta Samba alisema. “Kwa mujibu wa hawa wateja wako, gari lao limeibwa. Limeibwa likiwa ndani ya yadi!”



“Inawezekana,” Sanga alisema kwa sauti ya unyonge. “Lakini nadhani taarifa za uhakika zitapatikana kwa watu wa getini.”



“Ok, tafuta watu wa kushika nafasi za walinzi wako wa getini. Hao unaosema kuwa watakuwa na taarifa za uhakika, naondoka nao.”



“Sawa,” Sanga aliitika huku akinyanyuka.



Wakati huo Inspekta alishaanza kutoka, nyuma yake akifuata Salma, Chris kisha meneja. Walishuka kutoka ghorofani kila mtu akiwa kimya.



Lakini wakati huohuo, Chris alikuwa mbali kimawazo. Na kwa ujumla kila alipojumlisha moja na moja, badala ya kupata mbili akapata nne. Wazo moja lilimjia kichwani; kwamba, na yeye atapaswa kwenda Kituo cha Polisi cha Oysterbay! Huko ataandikisha maelezo!



Hakuwa mgeni wa kuingia katika vituo vya polisi, hivyo aliamini kuwa pindi watakapofika huko huenda wakachukua muda mrefu jambo ambalo hakutaka litokee. Na alikuwa na wasiwasi kuhusu maelezo ambayo hao walinzi watayatoa huko kituoni sanjari na maelezo atakayoandikisha Salma.



Kwa vyovyote vile, aliwaza, Salma atasema kuwa kuna wakati yeye aliondoka na gari hilo na kurudi nalo baadaye. Labda ni Salma atakayesema hivyo, lakini, wale walinzi, kwa kudhamiria kudanganya au kwa kutokuwa na hakika, huenda wakadai kuwa alipotoka na gari hakurudi nalo.



Kauli hiyo ya walinzi huenda ikawa ni msaada mkubwa kwao. Huenda ikaonekana kuwa hawana hatia na madai yao kuwa gari lililoondoka hapo lilikuwa na wamiliki wake yakaonekana kuwa ni ya kweli. Na kama itadaiwa kuwa aliondoka na gari wakati fulani basi hiyo itatosha kuwafanya polisi wamchukulie kuwa yeye ndiye awe msaidizi mkuu wa tukio hilo.



Vyovyote vile itakavyokuwa, lakini kitendo cha yeye kuhusishwa na uendeshaji wa gari hilo kwa kipindi cha saa moja iliyopita kitamtia dosari. Askari wangezidi kumbana kwa maswali haya na yale, maswali ambayo huenda hatima yake ingekuwa ni kuswekwa mahabusu kwa kile kinachodaiwa kuwa ni 'kuwasaidia polisi.' Je, Salma atakuwa radhi mpenziwe aingizwe mahabusu akihusishwa na kutoweka kwa gari? Ni swali ambalo Chris alijiuliza.



Hakuwa na uwezo wa ki-Mungu, uwezo wa kutambua kuwa Salma anawaza nini au anamchukulia vipi katika tukio hilo. Hivyo, hakuweza kujipa matumaini ya moja kwa moja kuwa mambo yatakwenda vizuri awe amekwenda huko Oysterbay au hakwenda. Lakini kwa wakati huo hakuwa na nguvu ya kutoafikiana haraka na uamuzi utakaotolewa na Salma au Inspekta Samba.



Walipokwishafika nje, Inspekta Samba alimgeukia Salma. “Itabidi wote tufuatane kituoni kwa hatua zaidi. Sawa?”



“Nakusikiliza wewe!” Salma alisema kwa msisitizo mkali.



Muda mfupi baadaye ile Land Rover iliondoka hapo Kingo House. Salma na Inspekta Samba waliketi mbele huku Chris, wale walinzi wa getini na askari wengine walikuwa nyuma. Wakati wale askari walikuwa wamesimama huku wameshika mabomba, Chris na wale walinzi waliketi chini na kutoa taswira halisi ya kutuhumiwa kwa kosa fulani.



Chris alikerwa na hali hiyo. Kwa kiasi kikubwa alijiona kadhalilishwa. Na alijenga imani kuwa huenda watakapofika kituoni, akajumuishwa na hawa walinzi wa getini, jambo ambalo hakuwa radhi kulitekeleza.

Ameshakula ng'ombe mzima, iweje mkia umshinde? Tangu alipoanza kuliwinda lile gari la Salma hadi mpango ukakamilika, si chini ya shilingi milioni moja zilizotumika. Na tayari gari hilo limeshafika kwa mlengwa. Huko kuna mamilioni ya pesa. Si chini ya shilingi milioni 30 zinazomsubiri.



Lakini afanye nini? aliwaza kuwa aruke na kutokomea, lakini wazo hilo liliyeyuka ghafla. Alitambua fika kuwa kitendo cha kujaribu kuwakimbia askari hao kingezua mtafaruku mkubwa na lisingekuwa jambo la ajabu kujikuta akishindiliwa risasi za mgongoni ambazo zingeyakatisha maisha yake papohapo.



Siyo kwamba aliogopa kufa, la hasha. Alikuwa tayari kufa siku yoyote na kwa namna yoyote ile, lakini si kabla ya kutimiza malengo yake hususan malengo mazito kama hili la kupata zaidi ya shilingi milioni 20.



Hata hivyo hakutaka kufanya papara. Akatulia akisubiri kupata nafasi atakayoona kuwa inafaa kwa kuwaacha askari hao na Salma wao. Gari likashika kasi katika Barabara ya Ruhinde na baada ya muda mfupi wakafika katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay.



Wale walinzi wakatupwa selo huku Salma na Chris wakibaki kaunta kwa ajili ya kuandikisha maelezo. Ni katika kipindi hicho ndipo Chris alipoamua kufanya kile alichotaka kukifanya. Salma alipoanza kuandikisha maelezo, Chris alimwambia askari mmoja aliyekuwa hapo kuwa anataka kwenda msalani.



“Pita hapo...” askari yule alimwelekeza.



Chris akanyanyuka na kutoka taratibu. Hakuna aliyemjali wala kumchunga. Nani ajali kumchunga ilhali yeye sio mtuhumiwa? Alitoka kwa mwendo wa taratibu, akipishana na watu wengine wawili walioingia humo huku wakivuja damu puani na midomoni. Na ni watu hao ambao waliziteka akili za askari wengine kwa muda huo kiasi cha kumsahau Chris.



Akitembea kama mtu aliyeamua kwenda ufukoni mwa bahari kubarizi, Chris aliendelea kutembea, mkono wa kushoto ukiwa umezama katika mfuko wa suruali huku wa kulia ukiichezeachezea simu. Alipokaribia Barabara ya Ali Hassan Mwinyi ndipo alipogeuka nyuma akiangalia kama kuna yeyote ambaye labda atamfuata au atakuwa akimchunguza.







**********http://deusdeditmahunda.blogspot.com/





“ENHE, hebu tueleze bibie, ilikuwa-kuwaje hadi gari lako likapotea kimiujiza?” askari mmoja alianza kumhoji Salma.



Salma alianza kuzungumza. Akataja muda alioingia Kingo House na kwamba kuna wakati mpenzi wake, Chris aliondoka na gari hilo na kurejea baada ya muda kama wa nusu saa.



Inspekta Samba akatwaa nafasi ya yule askari mwingine. “Mlikwenda hapo Kingo House kufanya nini?” alimuuliza.



“Tuliamua kwenda hapo kwa ajili ya chakula cha mchana.”



“Huwa mna mazoea ya kwenda hapo?”



“Mimi binafsi sina mazoea ya kwenda pale.”



“Lakini ulishawahi kwenda zaidi ya leo?”



“Leo ndiyo ilikuwa siku yangu ya kwanza.”



“Na hata huyu mzee wako?”



“Yeye ndiye aliyependekeza twende hapo.”



“Kwa hiyo tunaweza kusema yeye si mgeni wa Kingo House, eti?”



“Sio mgeni.”



Inspekta Samba alifikiri kidogo kisha akaendelea, “Wakati mko hapo Kingo House hamkuwa na mawasiliano na mtu mwingine yeyote?”



“Mawasiliano ya aina gani?” Salma alihitaji ufafanuzi.



“Yaani hakukuwa na mtu mwingine mliyekuwa mkijumuika naye?”



“Hakuna. Kulikuwa na watu wengine kama ishirini au thelathini

kwenye meza nyingine, lakini mimi na jamaa yangu tulikuwa peke yetu.”



“Na kuna wakati yeyote kati yenu alikuwa akiongea na mtu mwingine kwa simu?”



“Ni yeye, sio mimi.”



Kwa mara nyingine Inspekta Samba akaonekana kufikiri, kisha akaendelea, “Umesema kuna wakati mista wako alitoka na gari?”



“Ndiyo. Alitoka nalo na akarudi nalo.”



“Aliporudi ulimwona?”



“Nilimwona.”



“Halafu?”



“Tuliendelea kunywa bia zetu hadi muda wa kuondoka ulipofika ndipo tukagundua kuwa gari halipo.”



“Nani alikuwa wa kwanza kugundua?”



“Mimi,” Salma alijibu.



“Mlipofika hapo Kingo House mliripoti kwa walinzi?”



“Kuna cha kuripoti pale? Kila mtu akifika basi anapaki gari lake na kuendelea na mambo yaliyompeleka!”



“Na huyu mista wako alipoondoka alikwambia kuwa anakwenda wapi?”



“Benki, kuchukua pesa.”



“Benki gani?”



“CRDB, Azikiwe Branch.”



“Na aliporudi ulihakikisha kuwa karudi na gari?”



“Kha!” Salma alibwata. “Kwani mna maana gani?! Mna maana gani kuniuliza ivo?! Mbona maswali yenu yanajirudia-rudia?”



“Tulia mama,” Inspekta alimpoza. “ Tatizo lako ni kubwa, tunatafuta namna ya kulipatia ufumbuzi haraka iwezekanavyo.”



Ukimya ukatawala. Salma alionekana kuzama mawazoni.



“Bibie, hujanijibu swali langu,” Inspekta alisema huku kamkazia macho Salma.



“Nilimwona aliporudi.”



“Alirudi akiliendesha gari hilo?”



“Nd'o maana'ake!”



Askari wote waliokuwa hapo walitazamana. Kisha mmojawao akasema, “Nadhani hata huyo jamaa yake pia anapaswa kutupa maelezo.”



“Ndiyo,” Inspekta Samba aliafikiana na kauli ya askari wa kwanza. “Na yuko wapi?”



“Kaenda msalani,” askari mwingine alijibu.



“Ok, tumsubiri,” Inspekta alisema.



Dakika tano zilikatika, Chris hajarudi.



Dakika kumi!



Kumi na tano!



Wasiwasi ukawaingia askari hao. “Huyu mtu bado tu yuko msalani?” askari mmoja alihoji.



“Hata mimi nashangaa,” mwingine alisema.



“Au ana tumbo la kuhara?” wa tatu alihoji kwa mnong'ono ambao haukuyafikia masikio ya mtu mwingine humo ndani.



“Tuna shughuli nyingine za kufanya,” Inspekta Samba alisema kwa ukali kidogo. Akamwamuru askari mwingine amfuate Chris hukohuko msalani! “Kama kazidiwa tutamhoji hukohuko msalani!”



Dakika chache baadaye zikaja taarifa nyingine za kushangaza. Chris hakuwemo msalani!



“Nini?” Inspekta alimkazia macho askari huyo.



“Hayumo, afande!” askari aliyetoka msalani alijibu huku macho yamemtoka pima.



“Yuko wapi?!”



“Sijui, afande. Lakini aliaga kuwa anafika msalani mara moja.”



Inspekta Samba alimtazama Salma kwa macho makali kama anayemshutumu kwa namna fulani. Akakutana na macho ya Salma nayo yakiwaka bila ya kupepesa.



Mara askari mmoja wa kike ambaye aliingia humo dakika chache zilizopita akauliza, “Kwani huyo mtu mnayemuulizia yukoje?”



Salma alimtazama askari huyo kisha akawahi kujibu, “Ni mkaka mrefu na kavaa kapelo nyeusi.”



“Na kavaa shati jeusi?”



“Ndiyo,” Salma alijibu haraka. “Jeusi la mikono mirefu.”



“Suruali ya jeans?”



“Ndiyo.”



“Viatu?”



“Raba nyeupe,” Salma alijibu haraka.



Askari yule wa kike aliguna, kisha akasema, “Kama ni huyo nimekutana nae muda huu-huu akielekea barabara kuu.”



“Kweli?!” Salma aliuliza kwa sauti iliyojaa mshangao na hasira.



“Sitanii. Naamini ni huyo mnayemzungumzia.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Salma alikiacha kiti na kusimama. Ni wazi miguu ilikuwa ikimtetemeka. Akawatupia macho askari wote mmoja baada ya mwingine. Hakujua ni kipi alipaswa kufanya. Kwa ujumla akili yake ilisimama kufanya kazi.



“Mfuateni!” Inspekta Samba alifoka akiwaangalia askari wawili wa kiume waliokuwa kando yake.



Zoezi lililokuwa likiendelea lilisitishwa mara moja. Askari wale walitoka hima wakimfuata Chris. Wakamwacha Salma akiwa vilevile kasimama, kaduwaa, machozi yakimtiririka kwa mara nyingine.



**********









ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog