Simulizi : Milioni Thelathini
Sehemu Ya Tatu (3)
Baada ya siku tatu hawakuwa marafiki tena bali kama ndugu wa tumbo moja. Wakawa wakishirikiana kwa shida na raha. Na ilipotokea mmoja wao, au hata wote wakakumbwa na dhoruba za askari mgambo wa Jiji, hawakutupana. Walishirikiana katika kujikwamua.
Ndipo ikaja siku ambayo Aloyce Tarimo alitengeneza pesa kwa kiasi kikubwa katika biashara yake hiyo. Kufanya biashara na hatimaye jioni mtu unajikuta ukiwa na faida ya shilingi 30, 000 ni jambo ambalo halikuwahi kumtokea Aloyce Tarimo tangu alipoianza biashara hiyo.
Kwa siku hii, kufanya biashara na kupata faida hiyo kwake yalikuwa ni maajabu yasiyoelezeka. Hivyo walipofunga biashara zao huku jua likiwa limeshatokomea, Aloyce alimwambia Sabba waende kunywa pombe yao ya asili, Mbege katika baa moja hapohapo Kariakoo.
Ni huko kwenye baa hiyo ndipo Aloyce alipoamua kupasua jipu. Akaamua kumtamkia bayana Antony kuwa ana mpango wa kuachana na biashara hiyo.
“Uache?” Antony alimuuliza huku akimtazama kwa mshangao.
“Ndiyo.”
“Uache halafu uishije katika jiji hili?”
“Hilo sio tatizo,” Aloyce Tarimo alijibu kwa sauti ya chini na ya kujiamini. “Sikufichi, Antony, binadamu tunapaswa kufanya mambo yetu kwa malengo. Kwa upande wangu naona kuwa hii biashara ya kufukuzana na askari wa jiji kila kukicha haitanifikisha popote! Huo nd’o ukweli aisee!”
“Kwa hiyo unataka kujishughulisha na nini?”
“Kazi zipo nyingi tu, Antony. Na ukae ukijua kuwa ule msemo wa 'kazi ni kazi, mradi mkono uende kinywani' ni msemo wa kizamani. Kwa kizazi hiki tunapaswa kutafuta kazi za kutupaisha kimaisha bila kujali ni kazi za aina gani. Tufanye kazi za kututoa aisee!”
Antony aliguna. Kisha akasema, “Nakuelewa. Lakini ukifuatilia kwa makini utagundua kuwa wengi wa walionufaika sana kimaisha hawakupitia njia nzuri, Aloyce.”
“Utaishia hivyohivyo,” Aloyce alisema kwa dharau. “Utategemea kubadilika kimaisha kwa njia nzuri tu? Shauri yako! We' endelea kufukuzana-fukuzana na mgambo wa jiji. Kuna siku nitasikia uko Keko!”
Siku ya tatu Aloyce Tarimo hakuonekana katika eneo lake la biashara. Wiki ikakatika. Miezi mitatu ikapita, hatimaye mwaka ukaisha. Sasa Antony Sabba akawa hana matumaini tena ya kumwona rafikiye, Aloyce Tarimo. Lakini upo usemi wa 'milima haikutani bali binadamu hukutana.'
Siku moja, asubuhi, Antony Sabba akiwa katika kituo cha daladala cha Manzese Darajani aliliona gari dogo la rangi ya kijivu likiegeshwa kando yake. Kisha akasikia jina lake likiitwa. Hakuitika. Alitega sikio vizuri, akisubiri kama ataitwa tena.
“Sabba!” kwa mara nyingine sauti ilipenya masikioni mwake.
Sasa akayatupa macho kwenye gari hilo na kulisogelea. Alipolifikia alichungulia ndani ambako aliamini kuwa ndiko ilikotokea sauti iliyomwita. “Haaa! Aloyce!” alitamka kwa mshangao, macho kayatoa pima.
“Ingia twende.”
Alikuwa ni Aloyce Tarimo nyuma ya usukani. Antony aliingia. Gari likaondoka taratibu.
“Yes, Antony,” Aloyce alisema. “Habari za miaka ndugu yangu?”
Antony hakukumbuka kuitika. Alimtazama Aloyce kwa macho yasiyoamini. Akilini mwake huyu hakuwa yule Aloyce wa miaka miwili iliyopita, Aloyce mwenye mwili uliodhoofu na akiishi katika makazi duni huku pia akitegemea kupigania daladala ili aweze kufika katikati ya jiji.
La. Huyu alikuwa Aloyce mwingine, tofauti na yule aliyemfahamu.
Aloyce huyu kanenepa, Aloyce huyu kanawiri! Aloyce wa leo ana gari! Akilini mwa Antony, alichukulia kuwa siyo rahisi mtu kumiliki gari halafu akawa hana nyumba. Kwa vyovyote Aloyce ana nyumba, alijisemea moyoni. Alijenga imani hiyo japo pia alihitaji kupata uthibitisho kutoka kwa Aloyce mwenyewe kwani pia alitambua kuwa wapo watu wengi wenye magari ambayo huyalaza kwenye yadi za watu wengine na kulipia huku wao wakiishi kwenye nyumba za kupanga.
“Ni siku nyingi hatujaonana, Antony,” Aloyce alimzindua.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ndipo Antony alipozinduka na kuipata sauti yake. “Ni kweli. Zaidi ya mwaka sasa, na mwenzangu naona mambo yamekunyookea kishenzi.”
Aloyce akacheka kidogo. “Aaah, wapi ndugu yangu,” alisema. “Ni mahangaiko tu duniani hapa. Bila ya kuhangaika mtu unaweza kujikuta uko palepale hadi unazeeka, hadi kufa.”
Ukimya wa muda mfupi ukatawala, Antony akionekana kuyatafakari maneno ya Aloyce aliyosema muda mfupi uliopita. Kwa upande mmoja akaona kuwa ni kijembe kwake. Walikuwa pamoja kwenye biashara ya Kimachinga. Aloyce akamwacha huku akiwa ameshampa nasaha za kubadilika kimaisha. Leo hii ana gari, yeye Antony bado ni hohehahe! Bado yuko kwenye biashara yake ileile ya kufukuzana na mgambo wa jiji.
“Vipi, unafanya shughuli gani siku hizi?” Aloyce aliuvunja ukimya ule.
“Bado niko palepale ndugu yangu,” Antony alijibu kwa unyonge.
“Palepale Msimbazi?!” sauti ya Aloyce ilijaa mshangao.
Antony hakujibu.
“Na unaendelea na biashara ileile?”
“N'tafanyaje ndugu yangu?”
“S'o mbaya,” Aloyce alisema. “Mambo ni taratibu. Harakaharaka haina baraka. Ipo siku hata hiyo biashara itakutoa tu gwashee.”
Antony hakumwelewa, lakini hakusema kitu.
“Mimi siku hizi nina kibiashara kingine,” Aloyce alisema.
“Biashara gani ndugu yangu?” Antony alimwuliza kwa shauku.
“Ya kawaida tu, ndugu yangu. Nina kijigrosari nauza-uza bia mbili, tatu kwa siku.”
Antony aliguna kisha akauendeleza udadisi wake, “Ulipataje mtaji?”
Aloyce alicheka. “Akili kichwani ndugu yangu. Tanzania ya leo inamtaka mtu awe mjanja kama kweli anataka kupiga hatua, na hasa kwa watu kama sisi ambao hatuna elimu ya kutosha.”
Kwa mara nyingine Antony aliguna. Akabakia kumtazama Aloyce kama atazamaye kitu chochote kistaajabishacho. Aloyce hakupenda kuweka bayana kuwa usiku wa siku fulani alishirikiana na wenzake wenye visu, mapanga na bunduki isiyokuwa na risasi, wakawateka wateja katika baa ya Sunflower eneo la Sinza na kuwapora fedha na simu sanjari na kupora kiasi kikubwa cha fedha kwa muuzaji wa baa hiyo.
Lilikuwa ni tukio lililowaingizia faida kubwa kwani baada ya kugawana alijikuta na fedha zilizotosha kuanzisha biashara ya grosari katika kitongoji cha Mwananyamala. Matukio mengine mawili makubwa baada ya hilo la uporaji kwenye baa nayo yalimwingizia pesa lukuki kiasi cha kuweza kufungua baa tatu na kuwa na karakana mbili za magari. Hayo yote yalitokea katika kipindi cha mwaka mmoja ambao alipoteana na rafiki yake, Antony.
Lakini hakutaka kuiweka bayana habari hiyo. Na katika kuyaepuka maswali mengine ya Antony, alisema, “Ipo siku tutaongea kwa kirefu.” Akazamisha mkono katika mfuko wa shati na kuchomoa noti mbili zenye thamani ya shilingi 20,000 na kumpatia Antony huku akimwambia, “Utapata angalau soda ndugu yangu.” Kisha tena akatoa kadi ndogo na kuongeza, “Namba zangu za simu ziko hapo.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Antony alishukia jirani na Mahakama ya Mwanzo ya Kariakoo baada ya Aloyce kumwambia kuwa anaelekea jirani na jengo la Ushirika. Walikubaliana kuonana tena baada ya siku mbili, tatu lakini hawakuonana wala kuwasiliana tena. Kila mtu akaendelea na mihangaiko yake, kivyake-vyake.
**********
HUYO ndiye Aloyce Tarimo. Ndiye Aloyce ambaye pamoja na kuwa na biashara hizo zilizomshushia pesa lukuki, bado alihitaji zaidi na zaidi. Sasa akaongeza 'idara' nyingine katika sekta ya uzalishaji. Akawa akinunua magari yaliyoibwa kisha naye huyauza baada ya kuyafanyia mabadiliko katika sehemu nyeti. Chris alikuwa miongoni mwa waliomletea magari bora kwa bei nafuu. Hivyo, wakati walipoagana alasiri hiyo, tayari alishakuwa na matumaini ya kufanya biashara yenye faida nzuri.
**********
BREKI ya kwanza baada ya Chris kuondoka kwa Aloyce Tarimo ilikuwa ni kwenye gereji moja iliyokuwa mafichoni eneo la Tandale. Pale alimfuata Champanda, fundi magari na mchonga funguo mahiri. Mara tu alipofika pale, alikanyaga breki na kushusha kioo cha dirisha.
Hakutoka garini, alipiga honi mara mbili na mara akamwona kijana mmoja akimjia. “Karibu, mzee,” kijana yule alimwambia.
“Yupo?” ilikuwa ni kauli ya kwanza ya Chris.
“Nani, mzee Champanda?”
Chris aliitika kwa kutikisa kichwa.
“Yupo.”
“Kamwite.”
Kijana yule alimtazama Chris kwa macho yaliyofurika maswali mengi. Kwa ujumla alishangazwa na agizo hilo la kumfuata bosi wake ndani na kumwambia kuwa kuna mtu anamwita, tena mtu mwenyewe hamjui na yuko ndani ya gari akiwa haonyeshi dalili ya kuteremka.
“Kamwite!” Chris alirudia, safari hii akionyesha msisitizo. Akaongeza, “Mwambie ni Chris!”
Kijana yule aliondoka na baada ya muda mfupi Champanda alitoka ndani ya ofisi yake na kumfuata Chris.
“Mambo vipi?” Chris alimwahi.
“Shwari.”
“Una kazi nyingi?”
“Kazi haziishi, na zikiisha zinatafutwa haraka. Nipe kazi.”
“Nataka swichi kama hii haraka,” Chris alimwambia kwa sauti ya chini huku akimwonyesha ufunguo wa gari hilo.
Champanda aliupokea na kuutazama, akiugeuza huku na huku.
“Inawezekana?” Chris alimuuliza huku akimtazama kwa jicho kali.
“Inawezekana, mbona ni kazi ndogo tu! Unakuwa kama hunijui, mwanangu?” sauti na macho ya Champanda yalitoa taswira ni jinsi gani anajiamini kwa kila jambo analolitenda. Akaongeza: “Unaitaka lini?”
“Siyo suala la lini, ni leo hiihii! Uliza naitaka baada ya dakika ngapi.”
Chris alisema huku kamkazia macho, huenda akiona ndiyo njia pekee ya kumwonyesha umuhimu wa suala hilo.
“Leo,” Champanda alinong'ona huku akitupa macho angani. Akawa kama mtu anayetafuta kitu fulani kwenye anga hiyo. Hatimaye aliyashusha na kumtazama Chris sawia. “Nipe kama saa moja hivi,” alisema kwa uthabiti.
Chris aliitazama saa yake na kumuuliza, “Una hakika?”
“Yeah. Saa moja inatosha.”
“Poa.”
Champanda akaingia ofisini kwake na baada ya dakika takriban tano akarudi na kumkabidhi Chris ufunguo huo. “Nakuhakikishia, baada ya saa moja mambo yatakuwa supa,” alimwambia.
“Kwa hiyo itakuwa shi'ngapi?” alimuuliza.
“Kama kawaida yetu.”
“Kama kawaida yetu nd'o kiswahili gani msh’kaji wangu?”
Champanda akacheka. Kisha akasema, “Fanya fifty.”
“No, rekebisha.”
“Poa tusipoteze muda; arobaini tufanye kazi.”
“Ok, Natoa advance.”
“Poa.”
Dakika ishirini baadaye Chris alikuwa akiingiza hiyo Land Cruiser pale Kingo House. Akamkuta Salma katika meza ileile, lakini safari hii akiwa na chupa ya bia mbele yake. “Nimechelewa sana, baby?”
“Siyo sana,” Salma alimtazama kidogo na kuachia tabasamu hafifu. “Vipi umefanikiwa?”
“Nimefanikiwa. Tatizo lilikuwa ni ajali niliyoikuta huko.
“Ajali?”
“Yeah, kuna magari yamegongana pale kwenye taa za makutano ya Bibi Titi Road, Ohio na Ali Hassan Mwinyi. Ni hiyo iliyonichelewesha.”
Muda mfupi baadaye Chris pia alikuwa na bia mbele yake. Na wakati huohuo akamtazama Chaka na kumwona akiwa palepale alipomwacha kaketi, bia mbele yake, sigara mkononi. Akamkonyezea jicho. Chaka akatikisa kichwa akionyesha ishara ya kukubali.
Mara Chris akanyanyuka na kuelekea msalani. Alipofika jirani na meza aliyokuwapo Chaka akamwashiria kwa mkono amfuate. Dakika ya pili Chaka akakiacha kiti na kumfuata huko msalani.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Siki'za,” Chris alisema kwa sauti nzito, sauti ya chini na yenye msisitizo mkali. “Ukishamaliza hiyo bia yako nenda haraka kwa Champanda...”
“Champanda yule wa Tandale?” Chaka alimkata kauli.
“Yeah. Nimeshampa advance kwa kuchonga swichi mpya. Nimempa alfu ishirini. Una alfu ishirini hapo?”
“N'nayo.”
“Ok, umpe hiyo ili tuondokane na deni. Nitampigia simu...aah, no, ukishafika we’ mwambie kuwa nimekutuma. Kama utaona anasitasita, mwambie anipigie. Ana namba zangu.”
Mara mtu mmoja aliyeonyesha kukolewa na kinywaji akaingia msalani humo huku akipepesuka. Chris na Chaka ambao wakati huo walikwishajisahau katika mazungumzo yao wakazinduka na kujifanya kama vile wanajiandaa kujisaidia haja ndogo.
Yule mtu alijisaidia haja ndogo na kuondoka bila ya kuwajali au labda hata hakuwa na kumbukumbu kuwa kuna watu wengine humo msalani. Kwa ujumla alikuwa hoi. Chris na Chaka nao hawakumjali. Wakarudi kwenye mada yao.
“Umeiloki milango ya gari?” hatimaye Chaka alimuuliza Chris.
“Siwezi kuwa fala kiasi hicho,” Chris alijibu. “Ukiiangalia vizuri utagundua kuwa hata namna nilivyoipaki ni kwa namna ambayo hutapata shida pindi utakapokuja.”
“Hapo umecheza, babaa'ake. Twen'zetu.”
*********
CHAMPANDA alishangaa kumwona Chaka akiingia katika kijiofisi chake kidogo kilichokuwa ndani ya gereji yake. Chaka aliingia humo baada ya kuelekezwa na kijana mmoja aliyekuwa akisafisha bolt za gari moja lililokuwa matengenezoni.
Champanda aliyekuwa akiimalizia kazi aliyopewa na Chris, alimtazama Chaka kwa makini na kumuuliza, “Vipi, una shida na mimi?”
“Ndiyo. Wewe si nd'o Champanda?”
“Kwani vipi?” Champanda alimkazia macho zaidi. Kwa ujumla Champanda hakuwa akimjua Chaka, na wala hakuwa amepewa taarifa yoyote na Chris kuhusu ujio wake. Na katika kipindi hiki alipokuwa akiifanya kazi ya Chris, hakupenda kupata ugeni wa aina yoyote.
Chaka aligundua kuwa Champanda hakumjua, hivyo akaharakisha kuumaliza utata huo. “Nimetumwa na Chris kuchukua mzigo wake,” alisema.
“Chris?” Champanda alimuuliza kwa sauti ya chini huku akiendelea kumkazia macho.
“Ndiyo, Chris.”
“Kakutuma mzigo gani kutoka kwangu?”
“Swichi ya gari.”
Mkono wa kulia wa Champanda ukazama katika mfuko wa shati na kuibua simu. Akabonyeza tarakimu hii na ile kisha akaiweka sikioni. “Vipi kuna mtu uliyemtuma kuja kuchukua mzigo wako?” alihoji. “Anaitwa nani...amevaaje...ana malipo ya kumalizia...?” kisha akakata simu na kuirejesha mfukoni.
“Wewe ni nani?” hatimaye alimgeukia Chaka.
“Chaka.”
“Ok, malizia ishirini iliyobaki.”
Chaka alitoa shilingi 20,000 na akapewa funguo ya gari. Mchezo ukawa umekamilika. Sasa hakukuwa na jingine la kumweka hapo Chaka. Akatoka. Hatua chache baada ya kuiacha gereji hiyo teksi ilipita mbele yake. Akaipungia mkono. Dereva alipopaki, Chaka alimfuata na kumuuliza, “Una kazi?”
“Sina, mjomba. Nilikuwa narudi kituoni tu kusubiri kazi.”
“Ok, twende Kinondoni mara moja,” Chaka alisema huku akizunguka upande wa pili na kufungua mlango kisha akajitoma garini, kushoto mwa dereva.
Wakiwa njiani, Chaka akampigia Chris simu akihitaji maelekezo mengine.
***********
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“HALLOW dear, leo usiku unaonaje kama tutakwenda dansi?” Salma alimuuliza Chris wakati akiianza bia ya tatu.
Chris hakuwa hapo kimawazo. Alikuwa akifikiria kulitimiza lengo lake la kuja hapo Kingo House. Hadi wakati huo zilikwishapita dakika thelathini tangu Chaka alipoondoka akienda kwa Champanda. Na baada ya kuongea na Champanda kuhusu kumkabidhi Chaka ule ufunguo dakika kumi nyingine zilishakatika.
Je, Champanda hakuwa radhi kumpa Chaka ufunguo ule? Na kwa nini asimpe ilhali ameshamwambia katika mazungumzo yao ya simu? Na kama Chaka amenyimwa kwa nini hampi taarifa? Na hata kama amempa ni jambo la busara kumtaarifu. Akilini mwa Chris, kwa hatua waliyofikia ilikuwa ni muhimu sana kuwasiliana kila wakati.
Ni upuuzi ulioje kama watashindwa kulitimiza lengo lao katika dakika ya mwisho huku wamehangaika vizuri na kufanikiwa huko kote walikopitia? Ni fikra kuhusu hilo ndizo zilizomfanya hata asilisikie swali hili la Salma.
“Chris,” Salma alimwita huku akimtazama kwa macho makali.
Chris alizinduka, akashusha pumzi ndefu kisha: “Oooh, nilikuwa mbali kidogo, samahani.”
“Unawaza nini?”
Chris aliwaza haraka na kupata jibu aliloamini kuwa litamridhisha Salma. “Ni kuhusu yule fala niliyekwenda kumchukulia pesa yake.”
“Achana nae. Kwa nini akusumbue kichwa? Kama hakuja ni juu yake.”
Chris hakusema kitu. Akaitwaa glasi na kuipeleka mdomoni. Akanywa mafunda mawili, matatu na kuirejesha mezani. Mara simu yake ikaita. Akaitoa mfukoni haraka na kuitazama. Jina la Chaka likawa linaelea kwenye kioo.
Papohapo akatoka kitini na kumwambia Salma, “Samahani kidogo, ngoja niongee naye.”
“Ndiye kakupigia?”
Chris aliitika kwa kutikisa kichwa huku akielekea msalani.
“Vipi, shwari?” Chris aliuliza simuni mara tu alipohakikisha kuwa yuko mbali na Salma.
“Barida. Niko njiani nakuja. Kinachoendelea?”
“Uje moja kwa moja na kuchukua mzigo,” Chris alitoa maelekezo. “Na ukishafika kwa jamaa unisubiri mpaka nitakapofika. Sawa?”
“Nimekusoma, mtu wangu.”
Chris aliporudi mezani akamkuta Salma katika hali ya kutochangamka, akimtazama kwa macho makali kisha akambwatukia, “Huyo jamaa yako nd’o akufanye uende kuongea chooni au ulikuwa unaongea na
demu wako?”
Chris alicheka kidogo kisha akajibu, “Demu ninayeongea naye na niliyenaye ni mmoja tu hapa duniani.”
“N'nani?” Salma alimdaka.
“Yule niliyenaye muda huu mezani hapa Kingo House, yeye akiwa na Tusker baridi na mimi nikiwa Kilimanjaro moto.”
Salma alibibitua midomo, akasonya, na kwa sauti ya maringo akasema, “Mshenzi! Utamdanganya nani? Kamdanganye mtoto mdogo au mwendawazimu, siyo mimi.”
“Kwa bahati mbaya mie ni mcha Mungu; uongo sijauzoea.”
Salma hakuongeza neno kuhusu hoja hiyo, badala yake alinyanyuka na kuelekea msalani. Huku nyuma Chris aliitazama saa yake ya mkononi.
Ilikuwa ni saa 9.20 alasiri. Akatupa macho jirani na geti ambako aliliegesha lile Land Cruiser la Salma. Akashusha pumzi ndefu baada ya kuliona liko katika eneo zuri, halijazibiwa njia na gari jingine. Matumaini ya mafanikio yakazidi kujengeka moyoni mwake.
**********
CHAKA alimwamuru dereva teksi amwache kwenye soko la Juhudi, maarufu kama 'Soko la Ma-TX' Barabara ya Kinondoni. Kutoka hapo alivuta hatua za asteaste akielekea Kingo House. Alipofika katika eneo hilo hakuzubaa, alilifuata Land Cruiser jeusi lililoegeshwa karibu na geti, akafungua mlango na kuingia. Akionekana kujiamini kwa kiwango kikubwa, alishusha kioo kisha akawasha sigara na kuanza kuvuta.
Walinzi wawili waliokuwa bandani walimtazama bila ya kuwa na wasiwasi nae, wakiamini kuwa huyo ndiye mwenye gari hilo. Baada ya kuvuta mikupuo kadhaa ya sigara, Chaka alitia moto gari. Injini ikaunguruma. Akaweka gia namba moja na kuliondoa taratibu.
Akapita getini na kuwapungia mkono wale walinzi, nao wakamjibu kwa kumpungia mikono. Akaingia Barabara ya Kinondoni na kukata kulia.
Gari lilipokwishatulia barabarani akaongeza mwendo. Alipofika Kinondoni 'A' akakata kushoto akipita Mtaa wa Sekenke hadi alipokuja kukutana na Mtaa wa Togo kisha tena akazukia Barabara ya Kawawa.
Yote hiyo ilikuwa ni katika kumwepuka yeyote ambaye labda angemfuatilia. Alipovuka eneo la Mkwajuni, ‘akapaa,’ gari likawa kama vile liko kwenye mashindano! Ndipo akaitwaa simu na kupiga namba ya Chris. Ilipoita kidogo, akakata. Sekunde chache baadaye simu yake ikaita. Akaiweka sikioni na kusema, “Ni'shavuka Mkwajuni.”
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Uko poa?”
“Barida.”
Ukimya kutoka upande wa pili ukamwashiria kuwa Chris kakata simu. Naye akatulia nyuma ya usukani.
Safari ya Kimara!
**********
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment