Simulizi : Karata Ya Baradhuli
Sehemu Ya Tatu (3)
*****
ABLAH alikuwa akizungumza na Sharifa. Wakati huo, Ablah alikuwa eneo la bustani, mbali kidogo kutoka ndani ya jumba hilo. Na hadi kufikia hatua ya Sharifa kumpigia simu ni kwamba alikuwa ameshakwenda chumbani mwake na hakumkuta na hata aklipozunguka kwenye maeneo mengine ya jengo hilo hakumwona. Ndipo alipoamua kumpigia simu.
“Uko wapi we mtoto?” Sharifa alimuuliza kwa namna ya mzaha huku akijichekesha kinafiki.
“Nipo huku garden,” Ablah alijibu.
“Ok, kwa hiyo si nd’o kama tulivyozungumza jana?”
“Kuhusu?”
“Kwenda Mlimani City.”
Ukimya ukapita kidogo kisha sauti ikapenya sikioni mwa Sharifa, “Itakuwa saa ngapi?”
“Kama saa kumi hivi.”
Ablah aliwaza kidogo kisha akajibu,“Ok, tutakwenda.”
“Poa.”
Sharifa akakata simu huku akitabasamu kwa mbali. Papohapo akampigia simu Jitu. “Jipange,” ilikuwa ni kauli ya kwanza mara tu Jitu alipopokea.
“Uko poa?” Jitu alitaka uhakika.
“Kila kitu kiko poa. Amekubali.”
“Itakuwa saa ngapi?”
“Saa kumi.”
Ukimya ukatawala kwa sekunde chache kisha Jitu akasema, “Ok, tisa na nusu tutakuwa maeneo yale, nitakupigia.”
“Poa.”
Sharifa hakutulia. Papohapo akampigia simu Abdul na kumweleza makubaliano kati yake na Jitu.
“Kwa hiyo mimi sina umuhimu wa kuandamana na nyie, eti sista?” Abdul alimuuliza.
“Wewe hauna ulazima,” Sharifa alijibu. “Cha kufanya ni kwenda naye na nikifika kule kazi itabaki kwa kina Jitu.”
“Na wakishamchukua wanampeleka wapi?”
“Hiyo haituhusu. Muhimu ni kwamba, watatuambia wako wapi, sisi tumfuate na kumlazimisha atupe pesa ya kutosha. Siyo hicho kihundi cha milioni hamsini alichotoa yule maiti aliyekwishaoza.”
“Nimekusoma sista. Kwa hiyo tutawasiliana baadaye, basi. Mi’ niko ghetto.”
“Poa. Ila usianze kulewa ovyo. Uwe makini.”
“Us’konde sista.”
*****
BAADA ya kuendelea na shughuli nyingine kwa muda mfupi, mara tena Karim akaitwaa simu yake na kumpigia Ablah. Hazikupita hata sekunde tano, ikapokewa.
“Karim vipi?”
“Uko wapi Ablah?”
“Garden.”
“Ok, njoo mara moja huku ofisini.”
“Poa.”
Ablah alitoka haraka bustanini na kuitika wito. Alimkuta Karim kaketi ofisini mbele ya kompyuta akiendelea na kazi. Ablah aliketi kwenye kiti kilichokuwa jirani na dirisha. Ni kiti maalum kwa wageni.
Karim alikuwa kazama kwenye kompyuta, akibofyabofya katika kuzifungua nyaraka mbalimbali zilizohifadhiwa kwenye ‘mafolda’ mbalimbali.
Hatimaye akayainua tena macho na kumtazama Ablah. Akasema, “Sogea uangalie hapa.”
Ablah akasogea na kukaa jirani na Karim, macho yakiangalia skrini ya kompyuta.
Zikawachukua takriban dakika thelathini, Karim akimwonesha nyaraka kadhaa za miradi aliyomiliki marehemu mzee Malick.
Kisha akanyanyuka na kulifuata kabati kubwa lililokuwa na majalada kadhaa. Akalitwaa jalada moja na kulifungua, akizivuka nyaraka kadhaa hadi alipoufikia waraka aliouhitaji.
Akayatuliza macho na kumwashiria Ablah asome kilichomo.
Ablah alichukua dakika tano tu kuzijua raslimali mbalimbali zilizomilikiwa na baba yake. Hoteli mbili zenye hadhi ya Nyota Tano katika miji ya Nairobi na Kampala; meli mbili kubwa za mizigo zilizozunguka katika nchi mbalimbali za Afrika na Ulaya na machimbo matatu ya dhahabu nchini Afrika Kusini ni miongoni mwa miradi iliyomilikiwa na Malick Sikonge.
Pia alikuwa na mabasi ya abiria ishirini na matano yenye ubora wa juu nchini Tanzania yakifanya safari zake katika mikoa yote nchini na mengine yakifika Kenya na Uganda.
Katika eneo la Mirerani alikuwa akimiliki migodi kadhaa ya madini ya Tanzanite na kule Musoma pia alikuwa akimiliki migodi mitano ya dhahabu, hivyo kwa jumla miradi ya Tanzania tu ilikuwa kitegauchumi cha kutosha kuyaendesha maisha achilia mbali hiyo miradi mikubwa iliyohusisha mataifa ya nje.
Ni taswira hiyo iliyomfanya Ablah aweze kubaini ni kwa jinsi gani baba yake aliweza kuweka wafanyakazi zaidi ya ishirini hapo kwenye kasri lake na akawa akiwalipa mishahara bila ya matatizo.
“Karim,” hatimaye Ablah alisema kwa sauti ya kutojiamini. “Kwa kweli sikujua kama baba alikuwa na miradi mingi hivi. Nilijua tu kuwa ana miradi lakini haikuniingia akilini kuwa ni mikubwa kwa kiwango hiki.”
“Hiyo ndiyo hali halisi, Ablah,” Karim alimwambia kwa utulivu. “Na ndiyo maana nilikusisitiza uje utwae mali ya mzazi wako, uisimamie miradi na kuiendesha.”
Ablah aliinamisha uso chini, akavuta pumzi kwa nguvu kisha akaunyanyua tena uso na kumtazama Karim sawia. Akasema, “Karim nimekuelewa, lakini naomba na mimi unielewe. Hili nitakalosema, kama hutaliafiki na mimi sitakuelewa na sitaafikiana nawe kwa lolote lingine.”
Karim akashangaa. Akamkodolea macho Ablah kisha akauliza kwa upole, “Kwani vipi tena Ablah?”
“Mimi niwe wako, wewe uwe wangu Karim!” Ablah alisema kwa msisitizo “Tusidanganyane; siwezi kuiendesha miradi ya marehemu baba yangu bila wewe! Kama hauko radhi uniambie. Mimi siyo dada yako, wala wewe siyo kaka yangu! Udada na ukaka baina yetu ni wa kimagumashi tu.
Tuwe wakweli na huo ndio ukweli halisi! Maisha yangu bado siamini kama yako salama mbele ya mali yote hii. Nahitaji mtu wa karibu Karim…nahitaji mtu wa kunipa ushauri…nahitaji mtu wa kunilea…pesa kitu gani Karim?”
Kufikia hapo akainamisha uso. Akapeleka kiganja cha mkono wa kushoto usoni na kujifuta machozi yaliyomjia ghafla.
Alilia!
Karim akashtuka, akashangaa. Papohapo akaupitisha mkono begani kwa Ablah na kumuuliza kwa unyonge, “Kwa nini unalia Ablah? Usilie… Nimekuelewa…nimekuelewa Ablah…tuko pamoja Ablah!”
Ablah alijitahidi kutulia lakini bado kwikwi ilikuwa ikimtoka. Akainama kwa muda na Karim akamwacha ili atulie. Baada ya dakika kama mbili hivi, Karim alimpapasa Ablah mgongoni, akauhamisha mkono na kumshika kidevuni.
Akaunyanyua uso taratibu, Ablah akatii kinyonge. Nyuso zao zikatazamana. Macho mekundu ya Ablah yakakutana na macho yenye huruma ya Karim. Kwa sekunde chache wakabaki wakitazamana huku wakiwa kimya.
Huku kiganja cha mkono wa kulia wa Karim kikiwa bado kidevuni kwa Ablah, Karim alimvuta taratibu, nyuso zao zikasogeleana zaidi kiasi cha kila mmoja kuisikia pumzi ya mwenzake. Midomo yao ikasogeleana, macho yao yakiendelea kutazamana, yakiwa kama yanayozungumza kitu fulani.
Hatimaye midomo ikagusana, Ablah akauhisi ulimi wa Karim ukibisha hodi kinywani mwake. Mtoto wa kike, akaachia kinywa taratibu, ulimi wa Karim ukapenya kwa madaha.
*****
SAA nane na nusu Jitu alikuwa kwenye kigereji bubu cha Makarios, mshirika wao ambaye aliwajua vizuri na walimjua vizuri katika kazi zao zilizowaingizia pesa.
Hapo kwenye kijigereji bubu eneo la Mwananyamala Kwa Mama Zakaria, ndiko gari jeusi aina ya Toyota Corolla lilikohifadhiwa. Gari hilo lilikuwa la Jitu na alilitumia mara chache tena kwa matumizi muhimu tu yenye faida. Na kila alipokwenda kulichukua hapo gereji, Makarios alitonywa kuwa kuna kazi na kazi yenyewe aliambiwa. Hata hivyo, kwa siku hii, Jitu hakutaka kumwambia ukweli halisi wa kazi anayotarajia kwenda kuifanya. Alihisi kuwa si vizuri kuuweka bayana ukweli wa kazi inayomkabili.
“Vipi, kuna kazi?” Makarios alimuuliza.
“Yeah, tunataka kwenda kujaribu ishu f’lani maeneo ya ‘city centre.’ Siyo ishu ya uhakika sana. Hasa ni kama kupeleleza. Kuna bwege fulani tunamfuatilia.”
Jitu akaondoka na gari lake akiwa ameweka lita thelathini za mafuta. Dakika chache baadaye alikuwa Makumbusho ambako alimpitia Kelvin katika kijibaa kilichokuwa jirani na Kituo Kikuu cha Daladala.
Wakakanyaga mafuta wakielekea Mlimani City.
“Watakuja saa ngapi? Naona kama tumewahi sana,” Kelvin alisema wakati wanaikaribia Mwenge.
“Kuwahi siyo dhambi,” Jitu alijibu kwa kujiamini.
“Tunatakiwa tuwe kwenye mazingira mazuri kwa hiyo tunapaswa kuwahi ili tujipange na tumpe maelekezo Sharifa namna ya kututegeshea huyo mtu wao. Chuma unacho?”
“Cha nini?”
“Swali la kijinga hilo, Kelvin,” Jitu alikerewa. “Huwezi jua, pale kuna geti na kuna walinzi. Wanaweza kutufuatilia hata kama tutakuwa tumefanikiwa kumteka huyo mwanamke. Na hapo lazima tujilinde kwa uhakika. Umenisoma?”
“Nimekusoma. Sasa duh..”
“Us’jali. Mimi ninacho kitu hapa na kuna risasi sita. Hakuna kitakachoharibika.”
Na hapo lazima tujilinde kwa uhakika. Umenisoma?”
“Nimekusoma. Sasa duh..”
“Us’jali. Mimi ninacho kitu hapa na kuna risasi sita. Hakuna kitakachoharibika.”
***** SASA ENDELEA*****
“POA,” Kelvin alijibu kwa upole.
Walipaki gari umbali wa kama mita mia tatu hivi kutoka kwenye jengo la NSSF, eneo lililokuwa na baa. Wakaingia ndani ya baa hiyo na Jitu akaagiza mchemsho wa samaki aina ya Sato ilhali mwenzake, Kelvin yeye aliagiza mishkaki kumi na ndizi choma tatu.
Wakati wakisubiri, chupa kubwa za maji zilikuwa mezani na kila mmoja alikuwa akinywa kwa mapozi. Mara Kelvin akairejesha mada kuhusu kazi iliyowapeleka huko.
“Kumbuka Jitu,” alisema kwa upole, baada ya kugeuka mbele na nyuma, kulia na kushoto kwa namna ya kawaida ambayo si rahisi kwa mtu mwenye upeo wa kawaida angeweza kumshtukia.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Asilimia kubwa ya wateja waliokuwa hapo walikuwa mbali na meza waliyokuwapo Kelvin na Jitu, hivyo hakukuwa na taswira ya kuwatia hofu wala maswali kiasi cha kujikuta wakihisi kuwa kuna saitafahamu katika suala linalowakabili.
“Tusijikute tukicheza patapotea,” Kelvin aliendelea. “Milioni tatu ni upuuzi mbele ya wanaume marijali. Mjini hapa mshkaji wangu. Mwanamume wa kweli unatakiwa kupiga pesa ndefu kwa dili zenye moto. Kwa ishu hii, milioni tatu ni shombo tu mshkaji wangu. Zitaishia kwa kunywa bia na kuhonga Malaya.”
Jitu alimtazama Kelvin kwa jicho kali, akihisi kuwa kuna kutoaminiana kwenye kazi iliyokuwa mbele yao. Sekunde tano za awali akawa akimtazama sawia machoni, lakini sekunde ya pili, ukimya ukavunjwa. “Mbona tumeshaongea tukamaliza, Kelvin! Kilicho mbele yetu ni kumaliza kazi, basi!”
“Na hapo nd’o kuna suala ambalo hatujalizungumza,” Kelvin alisema. “Ya Mungu mengi. Huenda dili likatiki, tukaubeba mzigo. Kama tutawini tutakwenda kuweka maskani wapi?”
“Hilo ndilo la kujadili,” Jitu alisema kinyonge. “Kwa mara ya kwanza najisikia kuwa bwege au bwabwa, daaaadek. Anyway, unaonaje kama tutaingia naye maeneo ya Kawe?”
“Kawe?” Kelvin alishangaa. “Kawe maskani kwako au?”
“Hapana, siwezi kuwa fala wewe…tunampeleka chimbo lolote mbali na kwangu, tena mbali sana, tena ni bora iwe hata gesti.”
“Kawe kuna gesti nzuri ambayo hatutashtukiwa? Na tutakaa naye kwa muda gani? Isitoshe huoni kama ishu inaweza kubumburuka msh’kaji wangu? Kwa sababu kule ni maeneo yako, inaweza kutokea wanoko wakakupiga jicho wakati tukiingia chimbo, matokeo yake tukawa tumebugi.”
Kwa hiyo unadhani twende wapi?” Jitu alikosa mbinu mbadala.
“Kule Kunduchi kwangu. Tunampiga kitambaa cha uso na tunasepa naye mpaka getoni kwangu. Tunamtia ndani ya chumba Fulani, halafu tunaendelea na mitkasi inayofuata.”
“Wewe unaona getoni kwako pako shwari?” Jitu alimuuliza.
“Kule pako shwari kwa sana tu. Isitoshe hatutakaa naye hata kwa siku moja. Sisi tunamweka kati kisha tunawatonya kina Abdul, waje tuzungumze nao vizuri. Ni hapo ndipo tunawabadilishia somo.”
“Kama ni hivyo tusiwaruhusu waje mpaka kule. Wanaweza kutugeuka na wakaenda kutuchoma kwa wazee,” Jitu alisema, kauli iliyokubaliwa na Kelvin.
“Yeah, hilo neno. Na tutawaambia waongeze ngapi?”
“Wewe unadhani tuwaambie ngapi?”
“Watoe thelathini,” Kelvin alisema kwa msisitizo. “Milioni thelathini nd’o mpango mzima.”
Jitu alikunja uso, akaguna. “Wakitutolea nje?”
“Tusiwaze nuksi, Jitu,” Kelvin aliwaka. “Tuchukulie kuwa watapunguza kiwango na si kwamba watatutolea nje…”
Jitu akaitazama simu yake kwa dhamira ya kutazama muda. Saa ikamwonyesha kuwa wametumia kama dakika arobaini tu hapo. Bado muda uliruhusu. Akaagiza toti tatu za Glenfiddich, whisky inayotengenzwa Scotland. Alikipenda kinywaji hicho kwa kuwa mara nyingi akinywapo, humtia uchangamfu na viungo huwa katika hali ya ukakamavu sanjari na kujisikia vizuri kisaikolojia.
Mwenzake, Kelvin baada ya kuona hivyo yeye aliagiza kinywaji cha Tanzania, mzinga wa Konyagi na soda. Wakaendelea kuvuta muda huku wakishusha vinywaji.
Muda ulisogea hatimaye saa 9.30 ikawakuta wakiwa hapohapo mezani wakimimina vinywaji vyao tumboni.
“Nadhani sasa tusogee maeneo ya kazi,” Jitu alisema.
“Fanya mawasiliano kwanza na huyo mdada,” Kelvin alisema. “Huwezi jua, labda wameghairi. Bado ngoma nzito. Mpigie uongee naye.”
Jitu alibonyezabonyeza simu yake kisha akaitega sikioni.
Muda mfupi baadaye sauti ya Sharifa ilipenya sikioni mwake.
“Nambie. Umeshatinga kwenye eneo?”
“Tuko jirani. Wewe uko wapi?”
“Bado hatujaondoka. Nitakupigia baada ya dakika kumi hivi.”
“Poa. Lakini usiuweke usiku, maanake hapo Mlimani hatuna kingine kinachotupeleka, hatuendi kushangaa ka’ mabwege wasiopajua Mlimani City. Tunajua kuwa kuna mrundikano wa maduka na msongamano wa watu wanaozagaa na kushangaashangaa bila kununua bidhaa. Fanya mambo fasta tujue kinachoendelea.”
Sharifa aliachia cheko la kimbeya kisha akasema, “Una maneno wewe… Ok, us’konde. Nipe dakika kumi tu.”
*****
ILIWACHUKUA takriban dakika nzima Karim na Ablah wakiwa katika busu zito. Walipotenganisha vinywa vyao, Ablah aliona haya, akauinamisha uso chini. Karim akampapasa nywele na kuuinua uso ule wenye macho yaliyoonekana kuchoka. Wakatazama na kidogo huku wakitabasamu.
Karim akaizungusha mikono mgongoni kwa Ablah, akamsogeza tena karibu. Akanong’ona katika sikio la kulia, “Ablah….nakupenda…”
Ilikuwa ni kauli nzito na yenye kumfanya Ablah ajisikie furaha kubwa. Ni hilo alilolihitaji. “Asante Karim. Nami pia nakupenda Karim. Nakuhitaji katika maisha yangu, Karim. Sina namna ya kukushukuru kwa kuishi vizuri na baba ila tuwe pamoja katika kuyaendesha maisha na miradi yote aliyoiacha. Nakupenda Karim. Unaniahidi vipi Karim wangu?”
“Kufunga ndoa na Ablah mtoto pekee wa Malick Sikonge.”
“Asante… Asante Karim…” Ablah alimwemwesa na kumkumbatia kwa nguvu.
Walibaki kimya kwa muda huku wakiwa wamekumbatiana. Kisha taratibu wakatengana.
Ablah akasimama na kujinyoosha kidogo. “Karim, sasa ngoja nitoke kidogo,” alisema. “Najisikia amani moyoni. Sasa niruhusu niondoke. Nikirudi tutazungumza zaidi.”
“Safari ya wapi tena?” Karim alimuuliza huku akimtazama kwa mshangao kidogo.
“Mlimani City,” Ablah alijibu kwaz upole. “Nampiga tafu maza kwenye shopping.” Akaachia tabasamu dogo, Karim naye akalipokea tabasamu hilo.
“Ok, endelea kulijua vizuri jiji. Nadhani ulikuwa hujafika Mlimani City, eti?”
“ Ni kweli sijafika. Huwa nasikiaga tu eti sijui kunafanyika mashindano ya Miss Tanzania, mara sijui nini, sijui nini, na eti kuna maduka mengi ya nguvu.”
“Ni kweli. Ni eneo kubwa na zuri, na kuna karibu kila kitu.”
Wakacheka.
“Kesho na mimi nitahitaji unisindikize mahali,” Karim alisema.
Ablah aliguna na kucheka kidogo. “Nikusindikize wapi na wewe?”
“Nitakwambia. Kwani ni Sharifa pekee mwenye haki ya kuzunguka na wewe mjini?”
“Masihara hayo, Karim. Ok, usijali wangu. Leo acha nimsindikize mama, kesho namsindikiza wangu wa maisha…”
“Ooooh!” Karim akabwata kwa furaha akijitoa kitini na kumfuata Ablah aliyekuwa kasimama kama hatua mbili kutoka hapo mezani. Akamkumbatia tena na kumbusu shavuni. “Asante beibe.”
Ablah akahema kwa nguvu bila ya kutamka chochote. Na Karim alipomwachia, walitazamana kidogo, macho ya Ablah yakiwa na mvuto zaidi uliomfanya Karim amwone kwa muda huu kawa mzuri zaidi ya uzuri wake halisi.
“Baadaye, basi,” Ablah alisema kwa upole, akaondoka.
Alipokuwa varandani akielekea chumbani mwake kujiandaa, akakutana na Sharifa akiwa tayari kavalia katika namna ya ‘mtoko.’ Alikuwa aking’ara.
“Vipi? Kajiandae basi tutoke zetu,” Sharifa alimwambia huku akimtazama zaidi machoni kwa namna ya kumshangaa.
Ablah aliyaepuka macho ya Sharifa kwa kujihisi kuwa huenda ana mwonekano tofauti baada ya kuwa katika dakika kadhaa za ratiba tofauti na Karim kule ofisini.
“Usijali mama. Nipe dakika kumi tu, najimwagia maji na kubadili nguo.”
“Ok, niko nje garini nakusubiri.”
*****
SHARIFA alipokea simu aliyopigiwa na Jitu wakati akiwa garini akimsubiri Ablah. Wakati alipoanza kuongea naye mara akamwona Ablah akimjia akiwa amevaa gauni jekundu, pana la staha na mkoba begani. Ndipo alipolazimika kuahirisha maongezi na kujiweka vizuri kitini.
Ablah alipofika, Sharifa akalitia moto Mercedes Benz. Likaondoka taratibu huku muziki laini ukiwaburudisha sanjari na kiyoyozi kilichofanya ndani humo patofautiane na dunia ya kawaida waishio binadamu wa kawaida.
Muda mfupi baadaye walikuwa mbali na kasri hilo, wakielekea Mlimani City. Ndipo Sharifa akaitwaa simu yake na kulisaka jina la Jitu. Alipoipata, alipiga.
ILIPOKEWA muda huohuo. Jitu alikuwa hewani. “N’ambie Sharifa.”
“Niko njiani,” Sharifa alisema akiamini kuwa Ablah asingeweza kung’amua chochote.
“Una gari gani?”
Sharifa alisita kulijibu swali hilo kwa kutotaka Ablah kulisikia jibu hilo. Badala yake akajibu, “Nitakuteksti baada ya muda mfupi.”
“Nimekusoma,” sauti ya Jitu ilipenya masikioni mwake kwa utulivu na akajua Jitu ameelewa kwa nini amemwambia hivyo.
Kulikuwa na magari mengi katika barabara hiyo hivyo magari yalikwenda kwa kusuasua na wakati mwingine yalisimama. Hali hiyo ilimrahisishia kazi Sharifa kwani ilipotokea foleni ikasimama, papohapo akaanza kuandika ujumbe kwenye simu yake: BENZ JEUSI. Kisha akaongeza na namba za usajili za gari hilo. Dakika moja baadaye akaamua kupiga kwa kutaka kuthibitishiwa kama ujumbe umefika.
“Vipi, umeiona?”
“Yeah, nimeipata,” alijibiwa. Kisha Jitu akaongeza, “Mtapitia geti gani?”
“La barabara ya kuelekea Chuo Kikuu.”
“Poa,” Jitu alisema. “Mkifika msiingie ndani, punguza mwendo wakati utakapoianza barabara hiyo ya kuelekea chuo. Unanielewa?”
“Ndiyo.”
“Nenda taratibu sana, ukiona gari linatinga mbele yako. Usishangae. Simama. Tuko pamoja? Sitaki tuharibu kitu.”
“Nimekusoma. Usiwe na shaka.”
“Poa. Mmefika wapi?”
“Morocco jirani na jengo lenye ofisi za Airtel.”
“Ok, tuko kamili. Usiuweke usiku.”
Sharifa alikanyaga moto kwa nguvu, wakaikamata Mwenge baada ya dakika kama tano hivi. Sharifa akaanza kuhisi mapigo ya moyo yakipanda. Tukio lililokuwa likimkaabili lilikuwa zito na lililohitaji ujasiri. Kwake, kufanya tukio la aina hii ilikuwa ni mara ya kwanza na hata hivyo pia hakuwahi kufanya chochote kinachofanana na hiki anachotarajia kukifanya dakika chache zijazo.
Kwa mbali pia akahisi jasho likijiunda katika viganja vya mikono yake. Akawa akimtazama Ablah kipembepembe na kumwona akiwa ametopea katika kuchati kwenye mtandao.
“Naona uko busy,” alimchokoza.
Ablah akashtuka na kutabasamu kidogo. “Yeah, nilikuwa nachati na rafiki yangu mmoja wa Eldoret, Kenya. Aliwahi kuja Arusha tukaonana.”
“Wa kiume au wa kike?”
Ablah akacheka kidogo. “Kwa nini unauliza hivyo?”
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mmmh maana’ake, mambo ya mitandao mi’ nayaogopa mwenzio. Niliwahi kuwa na marafiki facebook iliku balaa…karibu wote wakawa wananitongoza. Nikaona ujinga. Nikafunga akaunti.”
Ablah akacheka kwa nguvu. “Mbona kawaida tu hiyo, mama? Hukuwa na haja ya kufunga akaunti. Dawa yao ni kuwa-block tu. Au unakaa kimya tu hakuna kuwajibu.”
“Duh! Labda kuwakalia kimya, lakini kama ni kuwa-block si nitawamaliza marafiki?” Sharifa aliuliza bila ya kuwa hapo kiakili. Ukweli ni kwamba mawazo yake yalikuwa huko walikuwa wakielekea na kwa namna fulani alihisi mapigo ya moyo yakizidi kuongezeka.
“Ni afadhali uwe na marafiki kumi wastaarabu kuliko kuwa na marafiki mia wapuuzi,” Ablah alisema huku akiyarejesha macho kwenye simu yake.
Sharifa aliamua kuacha kuzungumza kwa kuwa walikuwa kwenye mzunguko unaokwenda kuwaunganisha na barabara ya kuelekea Chuo Kikuu. Kwa haraka Sharifa aliyakumbuka maagizo ya Jitu kuhusu kupunguza mwendo wakati atakapokuwa amelisogelea geti la Mlimani City.
Wakati anaumaliza mzunguko wa barabara ya Mandela, akaanza kupunguza mwendo.
*****
MARA Ablah alipoondoka kule ofisini na kumwacha Karim peke yake, Karim hakujisikia kuendelea kufanya chochote, badala yake alifunga ‘mafolda’ ya nyaraka alizokuwa akimwonyesha Ablah kwenye kompyuta kisha akanyanyuka na kurudi chumbani mwake.
Alipofika chumbani alivuta saraka ya kabati lake kubwa la vitabu na vitu vingine, akatoa kijitabu kidogo cha kumbukumbu na kuandika maneno machache; SIKU YA MAPAMBAZIKO NA ABLAH.
Kisha akakirudisha pale alipokitoa na kujitupa kitandani. Hakuwa na usingizi wala uchovu. Kilichomlaza hapo ni kuutafakari huu uhusiano mpya ulioanza kati yake na Ablah, uhusiano ambao kwa kumbukumbu yake, marehemu Mzee Malick Sikonge enzi za uhai wake, akiwa katika dakika za majeruhi za pumzi yake, alimuusia na kumsihi kuwa angependa amuoe mwanaye, Ablah.
Ni jioni hii ndipo wamefikia hatua ya mbali zaidi katika kuiweka taswira iliyohitajika kichwani mwa mzee Malick Sikonge. Nitamuoa Ablah? Alijiuliza kama asiyeamini. Kwa jumla aliona kuwa hatua waliyofikia ni aina fulani ya tamthilia, na utekelezaji utakaofanyika wa kufunga ndoa, ni sinema ya bora ya Kihindi!
Inawezekana? Alijiuliza mara nyingi swali hilo. Eti atakuwa na mke mzuri, mwenye mvuto mkali machoni mwa mwanamume yeyote atakayemwona na hata kuonewa wivu na wanawake wenzake kutokana na uzuri wake, mwanamke aliyerithishwa utajiri mkubwa ilhali katoka kuishi maisha duni.
Atakuwa mume wa mwanamke mzuri, mwanamke tajiri, hivyo naye ataitwa tajiri. Mwanamume tajiri. Nani kama yeye? Utajiri wa ujanani!
Miradi ya ndani na nje ya nchi itakuwa chini yake! Ndiyo, aliamini kuwa itakuwa chini yake kwa kuwa aliamini ‘mwanumume ndiye kichwa’. Na si hivyo tu kwani, kwa karne hii ya ishirini na moja, wanawake wengi wamepevuka kiakili. Wanawake wanajua kubuni miradi na kuitekeleza kwa ufanisi.
Pamoja na ubora wa wanawake wa karne hii katika kubuni, kujituma na hata kutekeleza kwa ufanisi majukumu nyeti ya maendeleo, hata hivyo, aliamini kuwa msaada wa mwanamume huhitajika sana hasa kwa wanandoa waishio vizuri.
Kwa hali hiyo, alijua kuwa yeye na Ablah watakuwa bega kwa bega na watalisukuma gurudumu la maendeleo kwa ushirikiano mkubwa.
Kwamba maisha yao yatakuwa bora pale watakapofunga ndoa, ni mawazo yaliyokitawala kichwa chake kwa muda mrefu, lakini kikafikia kipindi, zikiwa ni kama dakika kumi baada ya kuyatafakari maisha hayo ya baadaye ndipo wazo moja likamwingia. Ni kuhusu taswira iliyokwishajionesha tangu mzee akiwa mahututi ilhali mkewe, Sharifa akionekana kutojali chochote kuhusu maradhi yaliyomsumbua mumewe.
Akajiuliza, huyu mkewe anaishi na Ablah kwa moyo mkunjufu ilhali siku ile mzee Malick akiwa hoi kitandani pamoja na hali yake alimsikia Sharifa huyu akiropoka kuwa hakuna mtoto wa Malick popote pale?
Sharifa hakutamka maneno hayo katika hali ya staha na yakawa ni maneno yaliyozidi kumwathiri mzee yule kiasi cha kukiharakisha kifo chake.
Je, Sharifa huyu hana kingine moyoni mwake? Anaishi na Ablah bila kinyongo chochote?
‘Hapana, siwezi kumwamini kwa asilimia mia moja,’ alijiambia kimoyomoyo. Na akaamua kuwa makini na kuanza kumchunguza bila hata ya Ablah kubaini.
Ni baada ya kuamua hivyo, ndipo akajitoa kitandani hapo na kulifuata Rangu Rover, akalitia moto akielekea Upanga Mtaa wa Magore. Alikwenda katika kituo cha Mjapani aliyekuwa akitoa mazoezi kwa wapenzi wa judo na karate. Mjapani huyo hakuwa akitoza pesa kwa mazoezi hayo, bali alifurahi tu kupata wadau wanaopenda mchezo huo.
Karim alikuwa na mazoea ya kwenda kwa Mjapani huyo mara kwa wiki na hivyo kufikia hatua hata ya Mjapani huyo kumzoea na kujenga urafiki.
Alikuwa na kawaida ya kufanya mazoezi hayo kwa muda wa saa mbili kisha hurudi nyumbani.
*****
JITU na Kelvin waliliegesha gari umbali mfupi kutoka kwenye geti la kuingilia Mlimani City. Macho yao na akili zao zilikuwa kwenye gari walilokuwa wakilisubiri. Jitu alikuwa amesimama nje ya gari, kando ya mlango akiwa tayari kwa hatua itakayofuata.
Kelvin naye alikuwa nje ya gari hilo lakini alikuwa mbali kidogo, akiwa kama hayuko pamoja na Jitu. Alitembea akienda hatua kama kumi hivi mbele kisha aligeuka taratibu na kurejea na kuna wakati alikwenda mpaka kwenye kituo cha daladala cha magari yaendayo chuo kikuu ambako aliungana na watu wachache waliokuwa hapo, akazuga kidogo huku macho yakiwa kwenye mzunguko wa barabara iliyotoka Mwenge.
Kisha alirudi pale alipokuwa Jitu na kumwambia, “Ingia ndani uwe tayari, nikiwaona nakutonya unajaa rodi-kati.”
Jitu akaona ni wazo zuri. Akaingia garini, akalitia moto na kuliacha likitoa mvumo wa chini.
Kelvin aliyekuwa nje alikuwa makini sana akilitupia macho makali gari lolote jeusi kabla ya kuzisoma namba za usajili na aina ya gari.
Hatimaye macho yake makali yakaliona gari walilolisubiri. Ndiyo, lilikuwa ni jeusi aina ya Mercedes Benz na likiwa na namba ambazo Jitu alimtajia kuwa ndizo zilizotajwa na mtu wao. Gari hilo lilikuwa nyuma ya magari mawili mengine madogo. Kwa kuwa Kelvin alikuwa mbali kidogo na gari lao huku Benz hili likija kwa mwendo wa asteaste, alirudi kwa hatua ndefu na kumwahi Jitu, akainamia dirisha na kumwambia, “Wamefika.”
Bila kuchelewa Jitu alitumbukiza gia na kulitupia jicho gari lililosubiriwa, kisha akaanza kuliingiza gari lake barabarani kama anayeomba njia kwa magari yale mawili yaliyolitangulia lile Benz.
Hata hivyo, gari la pili liliposimama kumruhusu aingie barabarani, haraka akilipungia mkono liendelee na likaendelea, ndipo kwa kasi akalitinga lile gari lililokusudiwa, Mercedes Benz jeusi!
Jitu alilijaza gari barabarani kiasi cha kulilazimisha lile Benz lisimamame ghafla na kunesanesa.
Punde Kelvin akaufungua mlango wa kushoto wa gari hilo na kumshika mkono Ablah. Akamvuta nje kwa nguvu!
Ablah akataharuki na kupiga kelele, “Mamaa!”
Nguvu na kasi ya Kelvin haikuwa ya kawaida. Alimvuta na kuufungua mlango wa gari lao kisha akamsukumizia kitini, kiti cha nyuma!
PAPOHAPO naye akaingia haraka na kumziba mdomo Ablah huku akiufunga mlango kwa nguvu. Wakati huohuo, Jitu aliliondoa gari kwa kasi akirudi kwenye makutano ya barabara hiyo na ile ya Sam Nujoma. Injini ikanguruma kwa nguvu kama inayotaka kupasuka.
Kelvin aliyekuwa amemkandamizia kono Ablah kwenye mdomo ili asiendelee kupiga kelele, sasa alimwachia na kwa sauti kali alimwambia, “Tulia. Tulia ili uwe salama. Vinginevyo…” akaiacha sentensi hiyo ikielea.
Kilikuwa ni kipindi kigumu sana kwa Ablah. Hakujua ni kipi kilichosababishwa atekwe. Na kwa nini atekwe yeye peke yake ilhali hana kitu? Kwa muda huo hakuweza hata kutafakari zaidi ni kipi kinachoendelea.
Alibaki akihema kwa nguvu huku kajikunja hapo kitini. Akamwangalia Kelvin kwa macho yenye woga zaidi ya woga wa kawaida.
“Kaa vizuri,” Kelvin alimwamuru.
Kwa namna ileile ya woga uliokitawala kiungo, Ablah alijikongoja kukaa vizuri. Akili yake ikasimama kufanya kazi kwa muda!
Jitu aliingia Barabara ya Sam Nujoma kwa kasi na kushika uelekeo wa kituo kikuu cha zamani cha daladala, Mwenge. Dakika chache baadaye akaingia Barabara ya Bagamoyo; uelekeo wa Tegeta!
Wanaume wakaridhishwa na hali ya barabara; hakukuwa na foleni ikerayo hivyo Jitu alijikuta akikanyaga kibati cha mwendo kwa namna alivyotaka na alivyopenda.
Kelvin aliyekuwa nyuma na Ablah akanyanyuka na kujinyoosha hadi kuifikia dashibodi kule mbele. Akaifungua na kutoa kitambaa kikubwa na kurudi kuketi. Kisha, akamwambia Ablah, “Mrembo wetu samahani kidogo. Siyo lazima upajue unakokwenda. Kwa sasa ni mapema mno kwa hiyo itabidi iwe hivi…”
Kufikia hapo akamfunga kitambaa usoni kwa nguvu huku akikumbana na upinzani dhaifu kutoka kwa Ablah.
“Mama nakufaaa..” Ablah alitoa yowe dogo kabla ya kuzibwa uso wote na kufuatiwa na kofi la nguvu ndogo katika shavu la kulia akionywa kutopiga kelele.
“Usitulazimishe tukufundishe adabu,” Kelvin alimwonya. “Utulivu wako ndio utakuwa salama yako.”
Ablah alilazimika kutii. Akajilaza kitini kama mfu akiwa hajui yuko wapi na anapelekwa wapi. Alikuwa katika ‘sayari’ nyingine!
Gari likaendelea kusaga lami. Kwa takriban dakika tano wote walikuwa kimya, macho mbele, Jitu akionekana kuwa makini zaidi na akizidi kuongeza mwendo kila ilipobidi.
Hatimaye waliachana na barabara hiyo na kuingia barabara ya mchepuko, barabara ambayo ni Kelvin aliyemwelekeza Jitu.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Haifai kufuata barabara moja kwa muda wote. Mchepuko ni muhimu,” alimwambia kabla hawajaingia mchepukoni.
Walipofika umbali kama wa maili moja hivi kabla ya kufika kwa Kelvin, Jitu akakanyaga breki na kumgeukia Kelvin. “Vipi, sasa inafaa tuwasiliane na yule mwanamke si nd’o maanake?”
“Itakuwa poa,” Kelvin alijibu.
Jitu akateremka garini, akaenda umbali mfupi kwa minajili kuwa kile atakachoongea kisiyafikie masikio ya Ablah. Akaitoa simu mfukoni na kubofyabofya kisha akaitega sikioni. Ngurumo ikamfikia kudhihirisha kuwa simu aliyopiga inaita upande wa pili.
Mara sauti ya kike ikapenya sikioni mwake, “N’ambie Jitu?”
Alikuwa ni Sharifa.
“Tuko na mzigo wako hapa,” Jitu alisema kwa msisitizo. “Lakini inabidi tuongee upya.”
“Tuongee upya?” Sharifa akashangaa, mshangao uliokuwa dhahiri hata masikioni mwa Jitu. Na hapo Jitu akajua amemshika pabaya, mpini anao yeye, Sharifa kakamata makali!
“Yeah, tuongee upya, Sharifa,” Jitu aliendelea huku akirandaranda mbele ya gari. “Tusiuweke usiku. Kwa kifupi ni kwamba rekebisha hesabu zako. Milioni na tatu ni shombo tupu. Ni hesabu ya kitoto.”
“Nini?” Sharifa aliwaka. Hakutarajia kuisikia kauli hiyo. Kwa jinsi walivyokwishapanga, na kutolewa kianzio cha utekelezaji wa kazi hii, limekuwa jambo la ajubu kwake kuisikia kauli hii ya Jitu. “Unajua sikuelewi Jitu?” hatimaye alibwata simuni.
“Inabidi unielewe,” Jitu alisema kwa utulivu lakini sauti yake ikiwa ni ya kujiamini. Akaendelea, “Tuko mbali sana na eneo hilo tulikomchukulia. Kinachopaswa kufanyika sasa ni kukwambia tuko wapi na mtu wenu, ili mje mzungumze mnayotaka awafanyie. Lakini kabla ya kukwambia tuko wapi, na kabla ya kukutanisha naye tena, inabidi nikwambie kuwa kumteka mtu mzima mwenye akili timamu kwa ajili ya faida ya watu wengine ni dhambi kuibwa. Nyie mnataka kunufaika kwa utajiri alioachiwa na baba yake. Sawa, hilo halituhusu, lakini inakuingia akilini kuwa kumlipa mtu milioni tatu kwa dhamana ya uhai wa mtu ni halali?”
Ukimya ukapita. Jitu akavuta pumzi akisikilizia jibu kutoka upande wa pili.
Kimya!
*****
SAA 12.30 Karim alikuwa akiingia nyumbani akitokea mazoezini. Alijisikia kuchoka lakini haukuwa uchovu wa kumfanya labda akitafute kitanda mapema. Hapana, ulikuwa ni uchovu wa kawaida kwake.
Alikwenda kuegesha gari bandani kisha akaenda chumbani mwake ambako alivua nguo alizokuwa nazo mazoezini, akavaa boksa na kutwaa taulo. Akaenda bafuni kuoga. Robo saa baadaye alikuwa sebuleni, kajipweteka kwenye sofa kubwa akitazama runinga.
Ni hapo ndipo alipokumbuka jambo na akaangalia saa. Ilikuwa ni saa moja takriban na nusu. Nje, giza lilikuwa limekwishatanda. Akajiuliza, Ablah na Sharifa kwa nini hawajarudi? Kwani kwenda kununua bidhaa huko Mlimani City ndiyo iwe mpaka usiku? Na kuna kipi ambacho kitawafanya wachukue muda wote huo ilhali vitu vingi vilivyoko kule vipo pia kenye maduka mengine? Au Sharifa kaamua kumtembeza zaidi katika maeneo mengine?
Labda wameamua kuendelea kuzurura, alijiambia kimoyomoyo. Akaitwaa rimoti na kutafuta chaneli ambayo huenda wakati huo kukawa na taarifa ya habari. Kituo fulani cha runinga cha Tanzania kilikuwa kikiendelea na taarifa ya habari lakini alikuta zimefika habari za michezo, akaachana nayo. Alihitaji kuona taarifa za habari za kimataifa.
Akaganda kwenye kituo fulani cha Amerika, akiangalia matukio ya Somalia, Nigeria, Syria na Afrika Kusini.
Hatimaye taarifa hiyo ikahitimishwa na ndipo alipobaini kuwa saa mbili ilitimu.
Wazo kuhusu Ablah likamrudia. Tangu wawe pamoja jioni ile kule ofisini, ambako waliiweka bayana mioyo yao kiuhusiano, Karim alijisikia kumhitaji sana Ablah. Alipenda muda wote wawe pamoja. Aliyakumbuka yale macho mekundu ya Ablah, ambayo yalimtazama muda mfupi baada ya kutoka kulia.
Akayakumbuka jinsi yalivyokuwa yakisihi na kubembeleza.
Akakumbuka jinsi ndimi zao zilivyosabahiana kwa namna ivutiayo, uvuguvugu wa mate ya Ablah ukimtia msisimko wa kipekee. Akaikumbuka rehe ya jasho la Ablah, rehe ambayo ilishabihiana na ya ganda la limao na akajikuta akitamani kumlamba usoni na ikibidi mwili mzima!
‘Mbona anachelewa?’ alijiuliza huku akiitazama tena saa. Ule upendo wa kawaida kwa Ablah, upendo wa ‘kaka na dada’ sasa ulitoweka akilini mwake. Sasa alijisikia kumwona Ablah kama mke mtarajiwa. Ndiyo, zile nasaha zilizotolewa na marehemu mzee Malick kabla uhai haujamtoka, sanjari na pendekezo la dhati kutoka kwa Ablah zilikuwa ni changamoto kwake hivyo hakuwa tayari kubatilisha ahadi aliyoutoa kwa mzee Malick na kwa Ablah.
‘Uko wapi Ablah?’ alijikuta akiuliza kimoyomoyo kama vile amemuuliza Ablah bayana. Mara akajiwa na wazo la kumpigia simu Ablah. Hakuona kuwa atakuwa anafanya kosa kumpigia na kumuuliza kuwa mbona amechelewa kurudi ilhali hata Ablah mwenyewe anatambua fika kuwa hatua waliyofikia jioni ya siku hiyo ni kubwa na ni hatua mpya katika maisha yao.
Akaitwaa simu na kubofyabofya kisha akaitega sikioni. Ukimya wa sekunde chache ukapita kisha wimbo wa msanii maarufu wa kizazi kipya wa Tanzania ukapenya sikioni mwake, ikidhihirisha kuwa simu ya Ablah iko hewani. Wimbo huo ukaimba na kuimba, hatimaye ukakata. Akapiga tena, ikaita tena na kisha ikakata tena.
Akashangaa. Iweje ampigie simu Ablah na asipokee? Ni makusudi au ana tatizo? Au yuko na mwanamume mwingine?
Wazo kuhusu Ablah kuwa na mwanamume hakupenda kulipa uzito akilini mwake. Alijisikia kutenda dhambi kama atamwazia hivyo mapema hivyo japo kiubindamu siyo ajabu kwa Ablah kumhadaa kuwa anataka waishi pamoja kumbe ana bwana mwingine. Inawezekana; lakini Karim hakutaka kuamini hivyo.
“Ablah kwa muda huu mfupi anaweza kunikaushia kupokea simu yangu?” alijikuta akijiuliza kwea sauti ya mnong’ono na kwa kiasi fulani wivu ukiwa umejengeka kichwani mwake.
Akaitua simu kando na kuamua kutulia kwanza. Aliamini kuwa kama labda Ablah atakuwa kwenye mazingira magumu yatakayomfanya ashindwe kupokea simu, basi baadaye atampigia au atamtumia ujumbe wa maandishi.
Dakika kumi zikapita hajapigiwa wala hajapata ujumbe. Lakini kwa nini iwe hivi? Na mbona muda unazidi kwenda? Alijliuliza tena.
Akajiwa na akili mpya. Kumpigia simu Sharifa!
TUKIO la Ablah kutekwa pale Mlimani City llikuwa kama sinema machoni mwa watu waliokuwa katika eneo lile. Wengi walibaki wameduwaa na hata walipokuja kupata akili ya kuchukua hatua, walikuwa wameshachelewa.
Sharifa ambaye aliuratibu mpango huo kwa asilimia mia moja, yeye alikuwa makini sana. Mara tu Kelvin alipomchukua Ablah na kuondoka kigaidigaidi, yeye aliigiza kutaharuki na akawa akipiga honi mfululizo huku akihangaika kuligeuza gari palepale. Na alipofanikiwa aliondoka kwa kasi kama anayewafukuza kina Kelvin.
Hata hivyo, alipofika kwenye mzunguko unaoelekea Mwenge na Ubungo, alishika njia ya Ubungo! Hakuna aliyejua kuwa amebadili uelekeo na hakuna aliyemfuatilia. Watu ambao labda wangeweza kuwa na la kusema kwa uhakika ni wale walinzi wa geti la pale Mlimani City; wao waliona kila kitu lakini mazingira ya kazi yao yaliwanyima uhuru wa kuliingilia tukio hilo. Hivyo walibaki wakitazama tu.
Sharifa alikanyaga moto kwa nguvu na alipohakikisha kuwa yuko mbali na eneo la pale Mlimani akakata kushoto, akaingia kwenye mitaa ya uswahilini. Akakanyaga moto hadi alipohakikisha kuwa yuko sehemu ambayo huenda hakuna mtu atakayembaini haraka.
Akaegesha gari mbele ya duka moja dogo la rejareja. Mbele ya duka hilo kulikuwa na meza mbili na viti huku kwenye meza moja kukiwa na chupa tupu ya bia, taswira iliyoonyesha kuwa hapo kuna huduma ya vinywaji.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akateremka garini na kwenda dukani huku akihema kwa nguvu. Akili yake ilikuwa haijatulia na hata macho yake pia hayakutulia. Bado hakuamini kuwa atashinda katika mchezo huu anaoucheza.
Alivuta kiti na kuketi, akaikita mikono mezani viganja vikiwa vimefunikwa. Akabaki kaduwaa akitazama mbele kama vile kavutiwa na tukio lolote, lakini ukweli ni kwamba hakuwa akivutiwa na chochote na wala mawazo hayakuwa hapo.
Aliwaza kuwa, je, wakati huo Jitu na Kelvin watakuwa wamefika wapi? Hakujua kuwa watakuwa wamekwenda kujichimbia wapi lakini lengo lilikuwa ni kumchukua kwanza huyu Ablah na kumpeleka mafichoni. Baada ya hapo waende kukutana naye na kumshinikiza atoe shilingi milioni mia tatu au nne katika akaunti ya marehemu baba yake na kuwapatia.
Namna atakavyofanya atajua mwenyewe lakini pia wakati huohuo, Sharifa aliamini kuwa Karim atakuwa anajua mengi na anaweza kutekeleza hilo wakati Ablah akiwa mateka. Atishwe kuwa Ablah atakatwa kichwa kama pesa hizo hazitatoka!
Huenda kukaa na ugumu wa kuzitwaa pesa katika akaunti kwa kuwa kanuni za benki zina makali yake kwa yeyote anayetaka kughushi kwa njia moja au nyingine. Lakini kwani ni lazima pesa hizo zitoke benki? Akilini mwake Sharifa alijua kuwa miradi iliyosheheni mikononi mwa Ablah chini ya uangalizi wa Karim inatosha kusababisha milioni mia tatu zikapatikana bila ya kwenda benki.
Kuna miradi ya ndani na nje ya nchi. Haiwezi kuwa vigumu kwa kuamua kuuza mgodi mmoja na malori mawili au matatu na kujipatia mamia ya mamilioni ya pesa.
“Watazipata! Watake wasitake!” alijikuta akinong’ona huku akipiga ngumi dhaifu mezani.
Mara binti mmoja akamjia akitoka ndani ya duka. “Karibu dada,” alimkaribisha.
Sharifa akazinduka na kumtazama msichana huyo mdogo mwenye umri kiasi cha miaka kumi na saba au minane. Akaona haya kidogo, akihisi kuwa huenda huyo msichana kamsikia alivyoropoka. “Asante. Kuna Malta?”
“Ipo?”
“Nipe.”
“Baridi, moto?”
“Baridi.”
Ya chupa au ya kopo?”
“Ya kopo.”
Ni wakati akiisubiri hiyo Malta ndipo simu yake ilipoita. Akashtuka alipokuta jina la JITU likielea kwenye skrini. Papohapo akaitega sikioni na ndipo alipoupokea ule ujumbe ambao hakutarajia kuusikia kutoka kwa Jitu. Alijikuta akikaa kimya kwa muda bila ya kumjibu kitu Jitu.
Ukimya huo ukazinduliwa na Jitu. “Sharifa unanisikia?”
Hasira zikiwa zimekwishajikita akilini mwa Sharifa, akajikuta akiropoka, “Kusikia nini?”
“Una maana gani kuniuliza hivyo?” sauti ya Jitu ilikuwa ya kisharishari.
“Sijakuelewa ujue Jitu!” Sharifa aliwaka. “Tulikutana, tukazungumza kila kitu na tukakubaliana. Leo unakuja na mada nyingine. Unadhani ni mwanadamu gani mwenye akili timamu anayeweza kukubaliana na akili kama yako?”
“Akili ya mwendawazimu eti, eeh?”
“Hayo unayasema wewe.”
“Ninayasema mimi ndio! Lakini unadhani unataka nikuelewe vipi? Si ina maana unaniona chizi?”
Ukimya ukatawala tena lakini safari hii kwa muda mfupi zaidi. Kisha Sharifa akasema, “Sikia Jitu. Itakuwa vigumu kukuelewa kwa sasa. Fanya kitu kimoja. Tukutane ana kwa ana tuzungumze upya.”
“Lini?” Jitu aliuliza haraka lakini sauti yake ikionesha kukereka.
“Kesho.”
“Kwa nini isiwe leo? Hujui kuwa mambo ya aina hii hayapaswi kuchukua muda mrefu kama bunge la katiba au tume na bodi zinazoundwa serikalini kila kukicha eti kwa ajili ya kuchunguza upuuzi fulani? Unajua hivyo?
“Sikia we’ mwanamke, tunataka pesa inayoeleweka tumalize biashara hii, umenisoma? Zungumza na kaka yako ambaye alinifuata mwanzo kwa ajili ya kazi hii. Yeye kanipasulia kila kitu kuhusu huyu mdada. Nashangaa wewe unataka kuuweka usiku kwa jambo dogo tu. Kwani unadhani tunataka milioni mia moja? We vipi? Ok, n’ambie moja?”, tutaonana leo au nd’o unaleta za kuleta?”
Ukimya ukajaa tena kwenye simu zao. Kisha pumzi ndefu kutoka kwa Sharifa ikatua masikioni mwa Jitu. Na muda mfupi baadaye sauti ikapenya, “Nitakupigia baada ya dakika ishirini. Ujue kuwa mpaka sasa tangu mlipoondolka pale siyo kwamba niko sehemu nzuri, hapana. Niko Sinza tu hapa nimepumzika. Kwa hiyo vuta subira nitakupigia.”
“Nakupa nusu saa kabisa,” Jitu alisema na kukata simu.
Kwa mara nyingine Sharifa alishusha pumzi ndefu na kuisahau Malta yake pale mezani. Akabaki amekodoa macho barabarani, akiwatazama watu waliopita ilhali hawaoni. Jitu katoa tamko la kuwa anamsubiri kwa nusu saa na papohapo kakata simu. Anaonyesha jeuri kwa kuwa sasa ana Ablah.
Akilini mwa Sharifa aliamini kuwa ilimpasa kujali kuwa yeye kashika makali na Jitu kashika mpini. Ablah yuko chini ya ulinzi wa Jitu na mwenzake, Kelvin, hivyo ni dhahiri kuwa wanaweza kumfanya chochote watakavyo iwe kumdhuru au hata wakitaka wanaweza kumwachia huru.
Pia alihofia kuwa kama hawatafikia makubaliano, huenda kina Jitu wakalipeleka suala hilo mbali zaidi mathalani Polisi au wakampasulia ukweli wote Ablah, kwamba wamemteka kwa ajili gani.
Ni hili la pili ndilo lililomtisha Sharifa. Aliamini kuwa kama wataharibu kwa kumwaga kila kitu kwa Ablah, basi yeye na Abdul watakuwa katika wakati mgumu zaidi. Kwa hali hiyo akaamua kuwa mpole. Akaamua kutumia akili zaidi katika kufanikisha lile alilopanga kulifanikisha.
Akalitwaa kopo la Malta na kunywa kinywaji hicho kwa mfululizo kisha akalitupa kopo hilo kando.
Kisha akabonyeza hapa na pale katika simu yake. Chini ya dakika moja, alikuwa akisikia mlio wa simu iliyoita upande wa pili.
Kisha ghafla sauti ikapenya sikioni mwake, “Sister vipi?”
Alikuwa ni Abdul. Kwa kiasi fulani alionesha kuwa kalewa sana muda huo. Hata hivyo, hilo halikumsumbua Sharifa. Alichohitaji yeye ni kuzungumza naye.
“Uko wapi?” Sharifa alimuuliza.
“Niko gheto. Vipi, n’ambie, kimeeleweka?”
“Kitaelewaeka tu. Wala kwa hilo usikonde.. sasa nisikilize vizuri…tuko pamoja?”
“Yeah, tuko pamoja sister.”
Ukimya ukapita kwa sekunde chache kisha tena Sharifa akaibuka, “Ni hivi…wale watu wako ulioniletea wameanza kuleta ushoga.”
“Nini?”
“Tulia, usipaniki…lakini naona umeniletea maboya tu tena mabwabwa wa kutupwa! Wezi wa kishamba!”
Ukimya ukatawala kwa sekunde chache kisha Abdul akauliza, “Mbona sikuelewi sister?”
“Watu wako wametaka nyongeza. Eti ule mshiko tuliowapa hauwatoshi!”
“Mmmh!” Abdul alitoa mguno wa nguvu. “Hauwatoshi!?”
“Ndivyo wanavyodai.”
“Wanakaje? Na wanadai kuwa huwatoshi kwa vigezo gani wanavyotumia?”
“Basi tu wamecharuka sasa hivi wananipigia simu wakati wameshamchukua yule mwanamke.”
“Wasitufanye mabwege,” Abdul alisema kwa hasira. “Hebu subiri nimpigie Jitu simu! Dah! Hakuna kitu kama hicho! Na wanataka waongezwe shilingi ngapi?”
“Hajataja kiwango ila tu amesema kuwa milioni tatu ni shombo tena ni pesa za kitoto!”
“Hiiii! Nampigia sasa hivi asilete ujinga hapa! Patakuwahapatoshi hapa Dar daaaadek! Hanijui? Ni mawili; ama afanye kazi au arudishe pesa!”
“Acha! Sharifa aliwaka. “Usipaniki Abdul! Usimpigie!” “Usiwe na pupa uwe makini!”
“SISTER vipi? Mbona sikusomi? Inabidi tuwe makini na suala hili! Wale ni watu wa mishen-tauni tu. Huwezi kujua, huenda walishapanga kuingia mitini na mshiko waliopokea!”
“Hiyo hainiingii akilini, Abdul,” Sharifa alisema kwa kujiamini. “Wale ni watu wa njaa-njaa. Bado wanataka pesa. Tatizo hatujui wanataka kiasi gani. Nadhani cha muhimu ni kukutana na kuzungumza nao. Tatizo wewe uliweka nje kila kitu, eti ukawaambia kuwa tunafukuzia mkwanja kwa wale mabwege. Hapo naona ndipo ulipobugi. Sasa wanatugeuza sisi mradi.”
Ukimya ukapita kidogo. Sharifa alikuwa akipumua baada ya kuongea kwa jazba, Abdul alikuwa akiyatafakari maneno aliyoambiwa.
Hata hivyo, pombe ikiwa bado na utawala kichwani mwake, Abdul hakukubali kushindwa. “Sijabugi kitu, sister. Ila nakubaliana na pendekezo lako kuwa tukutane nao. Naona kuwa kweli hapo hakuna namna. Kwa kuwa wako na yule malaya, wanaweza kufanya chochote. Si unajua hivyo?”
“Najua sana,” Sharifa alijibu. “Nilishaona mbali. Sasa sikia, nitampigia simu Jitu, lakini nimwambie tukutane wapi?”
“Getoni kwangu hapa!” Abdul alisema kwa hasira na msisitizo. “Ni hapa tulipokutania na kuingia mkataba kwa hiyo hata mazungumzo mengine ni hapahapa!”
Ukimya ukatawala tena. Kisha Sharifa akawa hewani. “Chukulia kama atakataa kuja hapo. Kwa sasa wanajua kabisa kuwa wameshatutibua kwa kuingiza hoja mpya ya ongezeko la pesa. Na wanajua kabisa kuwa hatutakubali na huku wao tayari wana advansi waliyokwishaila. Kwa hali hiyo, wanaweza kuhisi kuwa tunataka kuwafanyia kitu mbaya. Sidhani kama watakuwa mabwege kiasi hicho.”
“Poa, hapo umechukulia kuwa watakataa,” Abdul alisema kwa sauti yake iliyokoroma kilevi. “Lakini pia sasa tuchukulie kuwa wamekubali kuja; hapo ni kwamba ni mawili; ama tukubali kuwaongeza mshiko au waturudishie pesa yetu…”
“Waturudishie vipi wakati naamini wameshakula hata kama hawajamaliza!”
“Ok, wewe unasemaje?”
“Tukubali hasara,” Sharifa alisema kwa unyonge. “Hakuna namna Abdul.”
“Tukubali hasara? Yaani tuwaongeze pesa, sio?”
“Ndiyo.”
“Kama kiasi gani?”
Ukimya ukapita kama kwa sekunde kumi kisha: “Zisizidi milioni kumi.”
Abdul akashusha pumzi ndefu kiasi hata cha dada yake kuipata sikioni mwake. “Dah! Lakini poa. Cha muhimu tukutane ndio tutajua kama patatosha.”
“Kwa hiyo nawapigia.”
“Wapigie.”
**********
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment