Search This Blog

Saturday, 5 November 2022

KARATA YA BARADHULI - 4

 








Simulizi : Karata Ya Baradhuli

Sehemu Ya Nne (4)





JITU aliporudi garini alimwambia Kelvin atoke ili Ablah asisikie watakachoongea. Kelvin akampekua kwanza Ablah na kumkuta na simu. Akaichukua huku akimwambia, “Samahani mrembo, hata mawasiliano kwa sasa inabidi uyasitishe kwa muda. Akafikiria kuizima lakini akasita kufanya hivyo. Alitaka kujua ni nani atampigia simu Ablah, zaidi alitaka hata kujua jina tu hata kama haitasaidia sana japo pia hakuwa na nia ya kuipokea simu yoyote itakayopigwa.



Akamfuata Jitu na wakasimama hatua kama mbili kutoka garini.



“Tumewashika pabaya,” hatimaye Jitu alimwambia. “Amesema atapiga baada ya dakika ishirini. Mi nimempa nusu saa kamili. Daadek wasitufanye vidampa, watajirike kupitia kwetu. Sasa najua ataongea kwanza na Abdul na baada ya hapo nadhani Abdul atapiga na atapingana na matakwa yetu. Sisi tuweke msimamo kuwa pesa iongezwe; hapo ush’kaji na Abdul unawekwa pembeni. Milioni kumi ziongezwe, unaonaje?”



“Suala ni kuwa watakubali?”



“Wasipokubali tunamwachia huru huyu demu na tunamweleza kila kitu!”



“Na huyu demu akienda kutuchoma kwa wazee?”



Watatuona wapi?” Jitu alicheka. “Tunakwenda kumdampo Mwenge au hata kabla ya kufika Mwenge usiku na tunaachananae. Demu mwenyewe Abdul aliniambia kuwa kaletwa majuzi tu toka Arusha, hata Dar haijui vizuri.”



Kelvin aliafikiana na Jitu. Akachomoa sigara na kuiwasha kisha akavuta taratibu huku kaegemea mlango wa gari. Hawakuwa na wasiwasi kuhusu Ablah ambaye muda huo alikuwa ndani ya gari huku kazibwa uso kwa kitambaa kichafu. Kwamba, Ablah anaweza kuamua kujifungua kitambaa hicho kwa kuwa hakufungwa mikono, ni jambo ambalo halikuwasumbua vichwa wanaume hao.



**********

ABLAH hakuwa timamu kisaikolojia. Alibaki garini huku akipumua kwa shida, akivuta hewa yenye harufu ya petroli kupitia kitambaa hiki kichafu kilichomziba uso.



Aliponyang’anywa simu sasa akaamini kuwa amebaki peke yake, lakini aliwasikiawanaume hao wakiongea hapo nje ya gari japo hakuyasikia mazungumzo yao. Akawaza je, kama Karim atampigia simu itakuwaje? Na kwa nini tangu pale alipotekwa kule Mlimani City, Sharifa hakumpigia simu? Ni muda mrefu sana, ina maana Sharifa hakujali tukio la utekaji huo? Au anahusika?



Kwa mbali akaanza kujiwa na hisia za Sharifa kuhusika. Wametoka wote nyumbani. Tukio limetokea wakiwa wote garini, na hadi muda huu simu inachukuliwa na Kelvin hakuwahi kusikia mtu yeyote akimpigia! Ina maana hata Sharifa hakujali kumpigia! Labda atakuwa ameogopa kupiga kwa hisia kuwa baada ya kutekwa atakuwa amenyang’anywa simu. Lakini si angejaribu hata kupiga! Hilo lingemfanya aone kuwa amemjali, sasa hadi muda huu kimya!



Anahusika! Aliwaza kwa kujiaminisha. Papohapo machozi yakamtoka na kumzulia mwasho kutokana na kulowanisha kitambaa hiki kichafu kilichombana macho.



Akafikiria kujifungua kwa kuwa hakuwa na kipingamizi chochote mikononi. Lakini akasita, akihofia usalama wake. Onyo alilopewa mwanzoni lilitosha kumthibitishia kuwa hawa ni watu wa aina gani. Aliipenda rho yake, hivyo alijisikia kuuhitaji muda tu kwa imani kuwa lolote la manufaa kwake linaweza kutokea kwa mapenzi ya Mungu. Na akawa akisali kimoyomoyo anusurike na madhila haya.



Ni wakati ametulia humo garini akiwa haijui hatima yake, mara akasikia mlango ukifunguliwa kisha mikono iliyokakamaa ikamshika kichwa na kufunguliwa kile kitambaa.



“Pole mrembo wetu,” alikuwa ni Kelvin. “Pata mapumziko kidogo. Ukiendelea kuwa mstaarabu hivi tunaweza kuelewana na tukaishia pazuri.”



Baada ya kukifungua kitambaa kile alikirudisha kule kwenye dashibodi na kumtazama kidogo Ablah. Macho yao yakakutana, Kelvin akamkonyezea jicho la kimahaba, jicho lililokuwa kero tupu kwa Ablah japo alijitahidi kuvumilia.



Kelvin alirudi kwa Jitu na hazikupita hata dakika mbili mara simu ya Jitu ikaita. Jitu akaitazama skrini na kukuta jina la SHARIFA likielea. Haraka akabonyeza kitufe cha kupokelea na kuitega sikioni. “Sema,” ndivyo alivyoipokea.



“Tukutane,” Sharifa alijibu simuni.



“Wapi na muda gani?”



“Palepale tulipowekeana mkataba huu wa kwanza.”



“Yaani una maana hotelini kwa Abdul?”



“Nd’o maana’ake.”



“Dah!” Jitu alionekana kutoafiki. “Mbona mbali? Tukutane Mwenge basi…”



“Mbali ki-vipi wakati una usafiri?”



“Yaani tuanze kuzungukazunguka na huu mzigo wenu? We’ vipi? Tuko mbali nimeshakwambia!”



“Nyie si mko wawili!?” Sharifa aliwaka. “Njoo wewe tuzungumze. Huyo mwenzako abaki na huyo mtu.”



Ukimya ukatawala kwa muda kisha Jitu akasema, “Sikia we’ sister. Amua moja, uje Mwenge au biashara ife. Na ikifa itabidi tumwachie ‘free’ huyu mtu na kumweleza ukweli. Hapo tutakuwa tumewaachia mpira na mtajua namna mtakavyoucheza.”



“Ok, tunakuja Mwenge,” Sharifa alisema kwa uchungu, akijisikia vibaya kutiwa roba la kiaina na Jitu. Kwa upole wa kinafiki akauliza, “Tukutane wapi?”



“Mkifika kwenye kituo cha daladala cha ITV nipigie nikuelekeze namna ya kukutana.”



“Ok,” Sharifa alijibu na kukata simu huku akisonya.



Jitu akacheka huku akimtazama Kelvin. “Bado tumemshika vibaya,” alisema. “Sasa fanya hivi, baki na huyu demu mimi niende. Mpaka kieleweke. Hatu yoyote tutakayofikia nitakupigia. Hasa kuhusu kiwango cha pesa, maana’ake sisi tunaweza kusema hivi na wao wakasema hivi. Wewe nenda na demu huyu sehemu yoyote hata kama siyo kwako. Kaa naye ukisubiri tuzungumze.”



Akaingiza mkono mfukoni na kumpatia Kelvin shilingi 50,000 huku akimwambia, “Zikulinde.”



Kelvin akateremka garini na Ablah, Jitu akatia moto akirudi Mwenge.



Ilikuwa ni saa 12.30 jioni.







WAKATI Abdul alipokuwa akiiwasha sigara nyingine huku akiwa na glasi ya pombe kali na chupa mezani, simu yake ikaita. Akaitwaa na kuangalia kwenye skrini. Jina la SHARIFA likaonekana. Haraka akabonyeza kitufe cha kupokelea na kuitega sikioni.



“Sister vipi? Inakuwaje?”



“Usitoke, Abdul,” Sharifa alisema kwa hasira. “Nakuja sasa hivi. Mambo mengine siyo ya kuongelea kwenye simu.”



Abdul aliitambua hasira ya dada yake kutokana na kigugumizi cha mbali wakati akizungumza. Akamjibu kwa kifupi, “Poa, nakusubiri.”



Papohapo Sharifa akachoma mafuta kwa nguvu akielekea kwa Abdul, Kinondoni. Dakika kumi zilitosha kumfikisha kwa Abdul na kitu cha kwanza alichomwambia mara tu alipoingia chumbani mwake ni kumtaka ushauri kama kweli waende Mwenge na pesa au waende bila pesa.



“Kwani kinachotupeleka Mwenge ni kuwapa pesa?” Abdul alimshangaa dada yake. “Ni mjadala na kutafuta mwafaka. Ni kweli wanataka nyongeza na umekubali kuwapa, lakini kwani kuna shinikizo la kuwapa sasa hivi?”



Nina shaka kuwa kama hawatapata pesa leo wanaweza kutugeuzia kibao,” Sharifa alisema huku akionekana kutokuwa na utulivu akilini.



“Tusiwaogope sana, sister,” Abdul alipinga huku akitwaa glasi na kunywa funda zito la pombe yake. Kisha akaukunja uso na kumtazama Sharifa kwa macho makali. Akaendelea, “Wametaka tukakutane Mwenge. Sisi twende. Kukutana ni jambo moja, kupeana pesa ni jambo lingine.”



Ukimya ukapita huku Sharifa akiwa ameyagandisha macho mezani kama vile katekwa na chupa na glasi ya pombe vilivyokuwa mezani ilhali akili yake haikuwa hapo kabisa.



Kisha akasema, “Ok, jiandae twende. Mengine tutayajulia hukohuko.”



Abdul hakuwa mtu wa kujiandaa. Hakuwa na muda huo, lakini alikuwa na muda wa kunywa bia, pombe kali au kuvuta sigara. Akioga asubuhi siyo lazima aoge jioni; akioga leo siyo lazima aoge kesho. Hivyo hata jioni hii hakuwa na muda wa kujiandaa. Alitwaa shati alilokuwa amelivua muda mrefu uliopita, akalivaa haraka na kisha akatinga viatu vya raba.



Akanyanyuka na kumwambia dada yake, “Niko fresh, tusepe. Ni Mwenge sehemu gani?”



“Amesema tukifika kituo cha daladala cha ITV nimpigie atuelekeze pa kukutania.”



Muda mfupi baadaye walikuwa ndani ya gari wakielekea Mwenge. Na ni wakati huo ndipo Sharifa alipomkumbuka Karim. Tangu alipoondoka na Ablah saa 10 jioni hadi muda huu saa moja kasoro, giza likiwa limekwishaingia, kwa vyovyote Karim anaweza kushangaa na kujiuliza ni kipi kilichotokea. Na kama ataingiwa na wasiwasi, atapiga simu?



Je, kina Jitu watakuwa hawakumnyang’anya simu Ablah? Na kama hawakumnyang’anya, je, kama Karim atampigia watamruhusu kuzungumza naye? Kama watamruhusu kuzungumza naye, atakuwa na uhuru wa kumweleza ukweli kuwa ametekwa?



Kitu kilichomtia wasiwasi Sharifa ni kuwa, huenda Karim kama hatapata mawasiliano na Ablah, ataamua kumpigia yeye. Na je, kama akimpigia atamwambia kuwa wako wapi? Alihisi mchanganyiko wa mambo kichwani kiasi cha kuamua kumwondoa akilini Karim.



Haikusaidia, kwani muda huohuo, wakati wakiwa wanapita eneo la Victoria, mara simu yake ikaita, alipokitazama kioo akakuta jina la KARIM likielea. Akawaza, aipokee au asiipokee? Lakini kama asipoipokea italeta taswira gani akilini mwa mpigaji?



Akapiga moyo konde na kuamua kuipokea.



*****



DAKIKA tano ambazo Karim alizungumza na Sharifa zilimwacha njiapanda na zaidi zikamtia wasiwasi. Sharifa alimwambia kuwa bado wako Mwenge kwa rafiki yake baada ya kutoka Mlimani City, alipomuuliza mbona Ablah hapokei simu, akasita kidogo kisha akasema katoka kidogo na simu kaiacha.



‘Sharifa atakuwa kamkuwadia Ablah kwa mwanamume? Na inawezekana kweli Ablah akawa na tabia hiyo mapema kiasi hiki?’ Karim alijiuliza kwa uchungu. Na kilichomshangaza zaidi ni pale alipomuuliza, “Mko Mwenge eneo gani?”



Sharifa hakujibu, badala yake akakata simu kisha akaizima. Karim alipopiga tena na tena ikamjibu kuwa namba anayopiga haipatikani. Kengele ya hatari ikalia kichwani mwa Karim. Lakini afanye nini?



*****



ABLAH aliamriwa na Kelvin kutoka garini kisha akamwambia kirafiki, “Usiogope mrembo. Twende hapo jirani tupate soda kidogo. Jitahidi kuwa katika mwonekano wa kawaida. Tuwe kama mtu na mpenzi wake. Hiyo itakusaidia sana mbel e ya safari yetu.”



Wakatembea taratibu, wakiwa wameshikana mikono na kuleta taswira kuwa ni wapenzi. Kuna wakati Kelvin alizungumza neno la kawaida na kujichekesha, Ablah naye akajitahidi kuachia tabasamu japo la kinafiki.



Hatimaye walifika kwenye baa iliyokuwa na mkusanyiko wa watu. Kelvin akamwongoza Ablah kwenye meza iliyokuwa pembezoni ambako kulikuwa na mtu mmoja aliyekuwa akipata mlo.



Walipoketi, Kelvin akaagiza bia na mhudumu alipomgeukia Ablah, kwa tabu akaagiza maji baridi.



Huduma zilipoletwa, kabla hata hawajaanza kunywa, simu ya Ablah iliyokuwa kwa Kelvin, ikaanza kuita. Kelvin akaitoa na kuiangalia. “Karim,” alisema taratibu huku akimwonesha skrini Ablah. Ukweli ni kwamba Kelvin hakumjua Karim, si kwa kumwona tu bali hata kumsikia. Wakati mpango huu uliposukwa, ni Jitu, Abdul na Sharifa walioongea. Na simulizi ya kwanza kabisa ilisimuliwa na Abdul, akimsimulia Jitu.



Hivyo, hata hapa hakuwaza kuwa huyu Karim anaweza kuwa ni mtu wa karibu sana kwa Ablah na muhimu zaidi kwa wakati huu mgumu. Akamuuliza, “Unamfahamu?”



Ablah akawaza haraka, ajibu kama anamfahamu au hamfahamu? Kama atajibu hamfahamu, kwa vyovyote Kelvin atajua kuwa kadanganywa. “Namfahamu,” aliamua kupasua ukweli wake.



“Ni nani yako?”



“Kaka yangu.”



“Yuko wapi? Anaishi hapahapa Dar?”



Machale yakamcheza tena Ablah. “Hapana, yuko Mwanza,” aliongopa.



Simu ilikatika, ikapigwa tena na tena. Kelvin akaona kero, akamsogezea simu Ablah huku akimwamibia kama amri, “Mwambie akupigie baadaye, uko kwenye kikao. Fikiria mwenyewe utamwambia ni kikao gani. Lakini ukiharibu na mimi nakuharibu hapahapa. Sitakuwa na simile.”



Wakati huo walikuwa wamebaki peke yao baada ya yule mteja waliyemkuta kuondoka.



Ablah alipoipokea simu, papohapo ikakatika. Akamwangalia Kelvin kwa macho ya huruma huku kajishika kiunoni.



“Vipi, imekatika?”



Ablah akajibu kwa kutikisa kichwa.



“Ok, lete. Akipiga nitakupa uongee naye.”



Ablah akajiona bado yuko shimoni ndani ya shimo lenye kina kirefu huku kukiwa hakuna dalili ya kuokoka.



Kelvin akainywa bia haraka na kuagiza ya pili, safari hii akiwasha na sigara na kuanza kuvuta kwa majidai. Ule mzinga wa Konyagi aliokunywa kule jirani na Mlimani City na kuchanganya na hizi bia mbili, majibu yakawa maradufu kichwani. Ndiyo, alikuwa amechangamka, zaidi kidogo ya uchangamkaji wa kawaida. Mzunguko wa damu ukawa mkubwa. Kibofu kikamtumia salamu.



Akaangaza macho na kumwona mhudumu wa kike akipita katika meza iliyokuwa jirani nao. Akamwita kwa nguvu na kiamriamri.



Mhudumu huyo alipomjia, akamuuliza, “Toilet wapi?”



“Pita hapo…nenda kule nyuma,” mhudumu alimwelekeza.



Papohapo, Kelvin akanyanyuka kisha akamwambia huyo mhudumu, “Unisubiri hapa mpaka nirudi. Kaa na mgeni wangu. Kuna bia yako.” Kisha akavuta hatua ndefu akielekea msalani.



Ablah akashusha pumzi ndefu na kumshika mkono yule mhudumu. “Samahani dada, naomba msaada wako.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



“Yule mhudumu akashtuka na kumwangalia Ablah kwa makini. “Vipi kwani?”



“Tafadhali sana, kama una simu naomba niwasiliane na jamaa yangu fasta. Nina tatizo kubwa dada yangu. Tafadhali sana. Papohapo akaifungua pochi haraka na kumpa shilingi 10,000.



“Shika dada yangu. Dakika moja tu, tafadhali.”



Pesa ni kitu kingine. Yule mhudumu, alimpa simu haraka huku akimuuliza, “Namba yake unayo kichwani?”



“Ndiyo.”



“Haya fasta basi, Jamaa yako asinikute akaona nimemuuza.

Dah! Mwanamume, wanaume wang’oe kwa Kiivu!”

Huku mikono ikimtetemeka, Ablah aliishika simu na kubonyeza tarakimu za namba ya Karim haraka kisha akapiga, wakati huo macho yakiwa eneo la vyoo, akihofu. Alishaonywa; akiharibu, ataharibiwa.

Simu iliita kidogo na kupokewa.



“Nani?”



\

Ilikuwa ni sauti ya Karim. Kwa hilo Ablah hakuwa na shaka. Haraka na kwa mnong’ono ambao haukuyafikia hata masikio ya huyu mhudumu, akasema, “Karim….Karim nimetekwa…nimetekwa Karim.

“Ablah!



“Nimetekwa Karim….please njoo uniokoe my dear.”



“Uko wapi?”



Papohapo Ablah akamwangalia yule mhudumu na kumuuliza, “Hii baa inaitwaje?”



Mhudumu akamjibu, “KK Beach.”



“Na hapa ni wapi?”



“Kunduchi.”



Haraka Ablah akairudia simu. “Niko KK Beach Kunduchi. Wataniua Karim. Njoo uniokoe. Simu yangu imeshikwa nao. Usinipigie.”



Simu ikakatwa. Mhudumu akarudishiwa haraka huku akishukuriwa ilhali naye akishangaa kumwona Ablah akitokwa machozi baada ya kuzungumza kwa chini sana na huyo mtu wake kisha analia. Hata hivyo, hakutaka kukisumbua kichwa. Ya Ngoswe…



Wakati mhudumu huyo akiirejesha simu himayani mwake, kwa mbali Kelvin alionekana akirejea kutoka msalani.









ABLAH akajifuta machozi haraka na kujitahidi kujiweka sawa ili Kelvin asimshtukie.



“Mambo vipi baby?” Kelvin alimuuliza huku akimpapasa kichwani kwa namna ya kuonesha mapenzi.



‘Baby!’ Ablah aliwaza kwa hasira, akilini akijisikia kumwonea kinyaa Kelvin. Hata hvyo, alitambua fika kuwa bado alihitaji muda wa kuinusuru roho yake. Hakuwa akijua kama kweli Karim atakuja na kama atakuja, je, ataweza kumwokoa? Na kwani Karim ana silaha yoyote au mbinu zozote za kukabiliana naye kama kutazuka mapigano? Kama hawa watu wana silaha ya hatari kama bastola itakuwaje? Na akaendelea kujiuliza, kwani mwenzake huyu jamaa amekwenda wapi?



Alijiona kuwa yuko kwenye dunia isiyotambulika bayana. Hakuwa akiijua hatima yake. Hata hivyo, akawa anamwomba Mungu kimoyomoyo, lolote litokee, lolote litakaloweza kuibadili hii ndoto isiyopendeza inayoendelea kumsumbua.



Huu mkono wa Kelvin uliokuwa ukimpapasa nywele na kuleta taswira ya kwamba ni wapenzi machoni mwa wateja wengine waliowaona, kwake ilikuwa ni kero nyingine aliyolazimka kuivumilia, apende, asipende.



Kelvin aliinama na kumbusu shavuni kisha akakifuata kiti chake na kuketi. Akamimina tena kinywaji kwenye glasi na kuendelea kunywa.



*********



KENGELE ya hatari ilikwishalia kichwani mwa Karim. Sharifa kaepuka kujibu swali lake kwamba ‘yuko wapi’ na badala yake kakata simu na kuzima kabisa. Kwa nini? Kumbukumbu ya kauli za hatari alizozitoa Sharifa wakati baba yake Ablah, mzee Malick Sikonge akiwa mahututi zikamjia akilini.



Ni siku ile ndipo alipobaini kuwa Sharifa ana roho ya kikatili zaidi ya ukatili wa binadamu wa kawaida aliyezaliwa chini ya jua. Aliamini kuwa kwa vyovyote vile, Sharifa hawezi kuridhika na ile hundi ya shilingi milioni hamsini aliyokabdhiwa ilhali anatambua fika kuwa marehemu alikuwa na miradi ya mabilioni. Asingeweza kuridhika na zaidi atatumia akili ya ziada kutaka kujinufaisha zaidi.



Leo kaondoka na Ablah na mpaka sasa hawajarudi na badala yake anamkatia simu! Kuna nini hapo? Akaitupa simu sofani na kupiga ngumi kiganjani. “Haiwezekani!” akajikuta akiropoka baada ya kusonya kwa nguvu.



Akawa akirandaranda humo sebuleni akiwa amechanganyikiwa. Mara akakurupuka na kuitwaa tena ile simu kisha akaenda kule ofisini ambako aliifungua ile saraka na kuitoa bastola. Kwa mara nyingine akaifungua na kuziangalia zile risasi tatu zilizokuwamo. Akashusha pumzi ndefu na kuifunga. Sasa hakuirejesha tena sarakani, badala yake akaifutika mfukoni na kutoka.



Hakujua afanye nini, lakini alihisi kuna jambo zito mbele yake. Hivyo, alichofanya ni kutoka na kwenda bustanini ambako nako hakukuwa na burudani yoyote kwake; alizungukazunguka kama anayekagua kitu ilhali hakuwa na lolote. Alijiona kuwa yu gizani tena ndani ya giza nene!



Ni wakati akrandaranda huko bustanini ndipo simu yake ilipoita. Akashtuka na kuitoa mfukoni haraka. Akaitupia jicho kwenye skrini na kukuta ni namba asiyoijua. Akawaza aipokee au asiipokee. Hata hivyo, haraka akatambua kuwa katika wakati huu mgumu anaokumbana na saitafahamu hii, anaweza kupokea simu asiyojua kuwa inatoka kwa nani, ikawa ni uamuzi mbaya lakini pia huenda kitendo cha kutoipokea kikamfanya aujutie uamuzi huo baadaye. Akafumba macho na kuipokea, na ni hapo alipojikuta akipata ujumbe wa hatari kutoka kwa Ablah!



Katekwa!



Yale maneno ya mwisho yakamtisha na kumuumiza zaidi. “Wataniua Karim. Njoo uniokoe. Simu yangu imeshikwa nao. Usinipigie.”



Kwa uchungu na hasira zisizomithilika na kitu chochote, akatoka mkuku akikimbilia ndani ambako alichukua swichi ya Range Rover kisha akatoka nusu akitembea nusu akikimbia. Wafanyakazi wawili, watatu aliokutana nao nje wakabaki wakimshangaa kwa kuwa hawajawahi kumwona katika hali hiyo.



“Martin fungua geti…fungua geti fasta…!” alifoka wakati akiingia ndani ya gari na kutumbukiza swichi na kuiwasha injini. Range Rover ikamtii. Akatupia jicho kwenye geji ya mafuta na kukuta kuna kiwango kizuri cha petroli. Angeweza kufika hata Arusha.



Kama kichaa, kama mlevi, akaliondoa gari kwa makeke ya aina yake, akalikuta geti limekwishafunguliwa, akapita kwa namna iliyomtisha hata mlinzi wa geti. Akaingia barabarani na kukanyaga moto zaidi, akidhihirisha kuwa sasa yeye ni mwendawazimu mwenye akili!



Dakika kama kumi hivi baadaye akawa akiiacha Barabara ya Haile Sellasie na kuingia Barabara ya Ali Hassan Mwinyi. Mungu akawa upande wake kwa siku hiyo kwani hakukuwa na foleni kama ilivyozoeleka. Magari yalikuwa yakipita kwa kasi. Akatumia ujanja aliojaaliwa akitaka kulazimisha kuingia barabarani.



Mara gari moja likamhurumia, likapunguza mwendo na yeye akafanikiwa kupenya, akaingia kwa makeke yaleyale kama alivyotoka ndani ya lile kasri la marehemu Malick. Akavuta mafuta kiwendawazimu zaidi, macho mbele bila kupepesa ilhali akiziuma papi za midomo yake kwa nguvu. Punde akajikuta akiisogelea Victoria. Magari yaliyokuwa mbele yake yakazidi kumwacha, jambo lililomtia ari ya kuongeza mwendo akiiamini Range Rover hiyo kuwa ni gari, lakini pia ni zaidi ya gari.



Akaifikia Kijitonyama na kuivuka kama vile haijui. Sayansi hiyoooo, nayo akaipita kama hajaiona. Ilikuwa nusura apae! Muda mfupi baadaye akajikuta akipiga ngumi kwa mkono wa kulia katika kiganja cha mkono wa kushoto, hiyo ni baada ya kubaini kuwa taa ya kijani katika makutano ya barabara hiyo na ile ya Shekilango ilikuwa ikiwaka.



“Mungu mkubwa…” alijikuta akiropoka kwa furaha. Akaivuka Bamaga kwa namna ileile ya uendeshaji wa kiwendawazimu, injini ikinguruma kama inayokaribia kupasuka!



Mwenge ikavukwa!



Alipoanza kuliingia eneo la Makongo, akaishika bastola iliyokuwa mfukoni na kushusha pumzi. Sasa aliamini kuwa Kunduchi ni baada ya dakika chache sana. “KK Beach!” akanong’ona akitaja baa aliyoambiwa na Ablah kwenye simu. Akazidi kuvuta mafuta, nayo Range Rover ikazidi kumtii.



Ni kama ilikuwa ikipaa!



*********



“HUYU mpuuzi naye anataka kunivuruga tu hapa!” Sharifa alisema kwa hasira mara tu alipoikata simu aliyokuwa akiongea na Karim.



“Anataka nini shoga huyo?” Abdul alimuuliza.



“Si umbulula wake tu…eti anauliza tuko wapi mbona hatujarudi. Nimeona ananizingua tu, kwani mimi ni mkewe?”



“Hakuna muda wa kupoteza na mabwabwa muda huu. Si twende tukawasikie hao watu maana’ake naona nao ni mizinguo tu.”



Muda mfupi baadaye walikuwa eneo la kituo cha daladala cha ITV. Sharifa akamgeukia Abdul. “Mpigie wewe. Simu yangu siiwashi kwanza maana’ake yule bwege naye anaweza kunipigia tena.”



Abdul aliibofyabofya simu yake na kulipata jina la Jitu. Akapiga. Hazikupita hata sekunde tano ikapokewa.



“Abdul, n’ambie,” Jitu alikoroma.



“Tuko Kituo cha ITV,” Abdul alisema naye kibabebabe. “Ni kipi kinachoendelea?”



“Ok, nimegundua kuwa mazingira ya hapo siyo mazuri. Rudini hadi Bamaga. Shikeni Shekilango Road, mje Corner Bar. Niko kwenye eneo la nje…”



“Mbona unatuzingua tena?” Abdul aliwaka. “Ulisema tuje ITV sasa unaanza kusema tena turudi huko kwenye maskani ya machangu...”



“Sikiliza Abdul,” Jitu naye alimkatiza kibabe. “Unataka tufanye kazi au hutaki? Huu sio muda wa kulalamika, we’ vipi? Au kama vipi rudini nyumbani na mie niendelee na mambo yangu, ishu ife! Na kama mko tayari, njooni tuzungumze…muda unakwenda…”



Abdul alisonya na kukata simu. Kwa jumla aliona kuwa hadi muda huo bado mpini kaushika Jitu ilhali yeye na dada yake wameshika makali; hawana ujanja zaidi ya kutii matakwa ya Jitu. Akamtaarifu Sharifa na mara wakageuza gari na kwenda Corner Bar.



Walimkuta Jitu akinywa bia huku akivuta sigara katika eneo la nje ya baa hiyo. Katika meza ya pili kulikuwa na kinadada watatu na chupa zao za maji wakinywa taratibu lakini zaidi wakionekana kuwa hayo maji ni kigezo tu cha kuwakalisha hapo kwani macho yao yalikuwa kikazi zaidi.



Abdul alitangulia kuketi kisha Sharifa akafuatia. “Haya imekuwaje tena msh’kaji wangu?” alianza Abdul akionekana kutotaka kupoteza muda. Kiwango cha pombe kichwani nacho kilichangia kumfanya awe na haraka ya kujua sababu ya mpango wao kuingiwa na saitafahamu.

“Ni kama sista alivyokwambia,” Jitu alijibu kwa utulivu na kwa sauti ya chini. “Kazi imekwishafanyika, lakini kwa akili yako unaona kuwa zile senti mlizotupa na hata zilizobaki ni pesa za kumfanyisha kazi mwanamume wa kazi? Ile kazi unaichukulia kuwa ni poa sana?”



Sharifa alitikisa kichwa kwa uchungu, akataka kusema lakini Abdul akamzuia. Akamgeulia Jitu. “Unakumbuka tulivyoongea? Na kwa nini ulikubali? Kwa tafsiri sahihi ni kwamba baada ya kuielewa kazi yenyewe na kuupima uzito wa kazi hiyo, ndipo ukakubali kuingia mkataba na ukakubali kiwango cha malipo huku pia ukiwa mwepesi wa kuchukua advansi. Tuko pamoja?”



“Nakusoma msh’kaji wangu,” Jitu alijibu kwa utulivu akionekana kutobabaika wala kutishwa na mtiririko huu wa maneno ya Abdul. Akapiga funda zito la bia. Kisha kwa hali hiyohiyo ya kutobabaika akasema, “Nilikubali kwa kuwa sikuwa na pesa. Nilihitaji pesa Abdul, lakini ukweli ni kwamba wewe na dada yako mnataka kujinufaisha mara bilioni kwa kazi hii uliyonipa.



“Milioni tatu ni shombo tupu msh’kaji wangu. Ongeza pesa, nimeshamwambia sista jioni. Ongeza pesa au tukubaliane, niwarudishie mkwanja wenu, yule mtoto mzuri tumwachie huku tukimwomba radhi na kumweleza ukweli kuhusu hili.”



Kitu kama kisu kikali kikapenya moyoni mwa Abdul huku masikio ya Sharifa yakivuma vuu…vuuu…vuuu na maneno ya Jitu yakizua mwangwi mzito na kujirudia mara mia kama dude la ajabu lifokalo kutoka milimani.









“UKIMYA ukatanda mezani hapo. Sharifa akamkodolea macho Jitu, hali kadhalika Abdul naye akawa akimtumbulia macho kama atazamaye mzimu.



“Unasema?”



“Mbona nimeongea Kiswahili chepesi sana watu wangu,” Jitu alisema kwa majidai. “Kuna ambacho sikueleweka hapo? Tulieni mfikirie vizuri. Ni suala dogo tu la kuchukulia uamuzi. Muhimu tujali muda tu. Hatuko bungeni hapa.”



Abdul alishussha pumzi kwa nguvu, akahisi akili yake kama imesimama kufanya kazi. Kwa sauti ya kukera, sauti ya kipombepombe, macho yake yaliyotangaza kuwa yamebobea katika vinywaji vikali yakimtazama Jitu sawia, akasema, “Tusipoteze muda. Sema, unataka nyongeza ya kiasi gani?”



“Fanyeni milioni ishirini.”



“Ishirini? Kwa kazi ndogo tu hii?” Abdul aliwaka.



“Ni kazi ndogo, ndiyo. Basi msingenipa tenda hiyo, mngeifanya wenyewe. Kwa nini hata muwe wepesi wa kutoa pesa kama ni kazi ndogo?”



Yalikuwa ni maneno mengine yaliyowakata maini Abdul na dada yake.



“Lakini Jitu,” Sharifa alisema kwa upole. “Hayo hayakuwa makubaliano yetu…”



“Sista,” Jitu alimkata kauli papohapo. “Hakuna haja ya kuuendeleza mjadala huu. Sisi siyo wanasiasa. Tuongee kiutu uzima na tujali muda. Semeni mko tayari au ishu ife?”



“Ishu haifi, Jitu!” Abdul alijibu haraka. “La kufanya hapo ni kurekebisha hesabu zako.”



“Nirekebishe hesabu zangu ki-vipi?”



“Tutakupa kumi.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



“Hailipi. Tufunge mjadala kwa kukubaliana, mtoe kumi na tano.”



Abdul na Sharifa wakatazamana, Sharifa akamkonyezea jicho Abdul ikiwa ni ishara ya kukubali. Ingawa alikubaliana na Abdul kule gesti kuwa wasizidishe shilingi milioni kumi katika pesa hizo, hata hivyo kwa muda huu aliona kuwa wanaweza kuzidi kupoteza muda. Milioni tano hakuona kama kiwango kikubwa katika nyongeza hiyo.



“Poa,” hatimaye Abdul alisema huku akiwa amemgeukia tena Jitu. “Mtazihitaji lini?”



“Hata leo kama inawezekana. Kwani mnapenda suala hili liendelee kuchelewa? Tufanye kitu fasta, kiishe, tuendelee na mambo mengine.”



“Kwa muda huu itakuwa ngumu,” Sharifa alisema. “Siwezi kuwa na keshi zote hizo ni mpaka benki.”



“Benki mnayo hapahapa. Tumia simu yako kuhamisha pesa, sista.”



Sharifa akazinduka. Ni kweli angeweza kuhamisha pesa benki na kuingiza kwenye simu yake kwa kutumia mtandao. Lakini akawaza, atoe pesa zote hizo mara hii ilhali hata hawajui kama wataikamilisha kazi yao kwa ufanisi? Hapana. Kwa hilo hakuwa tayari na papohapo akamwambia Jitu, “Inawezekana, lakini hakuna ulazima wa kufanya hivyo. Kwanza tueleze, mtu wetu yuko wapi? Au tuseme mmemuhifadhi wapi?”



“Yupo salama salimini. Hajaguswa hata ukucha. Labda saa hizi atakuwa anakunywa bia na kula nyamachoma.”



“Suala ni kwamba yuko wapi,” Abdul aliingilia kati. “Elewa Jitu tunazungumzia uhai na usalama wa mtu na pia tunazungumzia pesa. Sasa hatutaki kuzinguana. Wewe unataka pesa lakini unaanza kutuletea mashairi hapa. Sema mtu wetu yuko wapi.”



“Kunduchi.”



Abdul na Sharifa wakazitazama saa zao na kuguna. Ilikuwa ni saa mbili kasoro. Wakatazamana kama wanaoulizana kuwa wanaweza kwenda huko Kunduchi? Na huyu Jitu anaweza kuwapeleka huko Kunduchi kama hawatampa kiasi hicho cha pesa anachotaka au hata kiasi fulani anachoweza kuridhika nacho?



“Tunaweza kuonana naye leo?” hatimaye Abdul aliamua kuchokonoa.



“Hivihivi tu?” Jitu aliuliza huku akiachia tabasamu la dhihaka. “Tumalizane kwanza kwa mambo ya mkwanja, ndipo tucheki uwezekano huo wa kwenda huko bush.”



Abdul alimtazama dada yake na kumuuliza, “Sista unaniambiaje? Una akiba kidogo hapo?”



Sharifa alikumbuka kuwa kwenye mtandao wake fulani, kati ya mitandao miwili anayotumia kwenye simu yake kulikuwa na shilingi milioni mbili. Na angeweza kuhamisha kiasi hicho cha pesa kwa mfumo huohuo wa simu na pesa zikamfikia huyu Jitu.



Hata hivyo, itakapomlazimu kuchukua pesa zaidi na hasa kwa kiwango chote wanachotaka, hapo itabidi aingie benki na kujaza fomu kisha kusubiri dirishani. Hiyo haitakuwa usiku huu tena. Ni lazima iwe kesho au keshokutwa.



Sharifa alipotaka kujibu mara wakawaona wahudumu wawili wa kike kando yao. Papohapo Abdul akachomoa noti moja ya shilingi elfu kumi na kumpatia mmojawao. “Mimi niletee Konyagi ndogo.”



“Na wewe dada?” mhudumu alimgeukia Sharifa.



“Bavaria.”



Papo hapo Jitu akamwambia mhudumu huyo, “Mimi siongezi.”



Wahudumu wale walipoondoka, Sharifa akamgeukia Jitu. “Nitakurushia milioni moja tu, ambayo iko hapa kwenye simu.”



“Milioni moja tu, sista!”



“Nd’o maana’ake,” Sharifa alijibu kwa kujiamini. “Mtandao ninaotumia mimi hauna mfumo wa kuhamisha pesa benki. Kwa hiyo, zaidi ya milioni moja hakuna uwezekano, inabidi kwenda dirishani.”



Jitu alionekana kutoridhishwa na kauli hiyo. Akchukua glasi yake na kunywa pombe kwa mkupuo hadi ikaisha. Akaegemea kiti kivivuvivu. Sharifa na Abdul walikawa wakimtazama kwa makini.



“Milioni moja tu!” alisema kwa sauti ya chini lakini iliyoyafikia masikio ya Abdul na dada yake.



“Yeah, milioni moja. Kama unakubali nikurushie sasa hivi.”



Jitu akamnyooshea Sharifa mkono kwa ishara ya kumtaka asitishe kufanya hivyo. Na mara akaitwaa simu yake na kubonyeza tarakimu kadhaa kisha akaitega sikioni. Wakati ilipoanza kuita upande wa pili, akasimama na kusogea pembeni, lakini akiwa anawatazama Abdul na dada yake waliokuwa kama hatua tatu hivi mezani kutoka aliposimama yeye.



*********



AKILI ya Karim ilikuwa haiko sawa kwa namna moja lakini ilikuwa sawa kwa namna nyingine. Alikwenda kasi hadi alipofika eneo la Kunduchi ndipo aliposhtuka kuwa alikuwa haijui hiyo Hoteli ya KK Beach ilipo. Akaegesha gari kwenye baa ya Makondeambayo ilikuwa kubwa na maarufu kwa namna alivyoona yeye. Kulikuwa na watu wengi na kulikuwa na shoo kubwa jukwaani, wasichana na wavulana waliovaa sare wakicheza muziki wa Kikongo huku mshereheshaji akipiga promosheni ya bia fulani ambayo labda ilianza kutetereka kimauzo licha ya kuwa uzalishaji wake ni wa tangu miaka mingi iliyopita.



Akaamua kuanzia hapo kuitafuta hiyo KK Beach Hotel.

Hakuwa mnywaji wa pombe lakini hicho hakikuwa kigezo cha kumfanya asiingie kwenye sehemu kama hizo. Hivyo, mara tu alipovuta kiti na kuketi, japo kila dakika aliiona inapotea akizingatia kuwa hajui hali ya Ablah huko aliko, bado aliamini kuwa Mungu atakuwa kiongozi wake na atafanikiwa katika malengo yake.



“Kaka habari yako?” mhudumu wa kike alimsalimia akiwa mbele yake.



Karim alimtazama kidogo kisha akajibu, “Nzuri.”



“Umeshasikilizwa?”



“Bado.”



“Nikuhudumie nini?”



“Soda. Fanta Tropical.”



“Naomba hela kabisa.”



Karim alizamisha mkono mfukoni na kutoa noti ya shilingi elfu mbili. “Leta baridi.”



Mhudumu alipoondoka, Karim akawaza kuwa ni vyema kumtumia huyohuyo mhudumu katika kuijua hiyo KK Beach ilipo. Na kwa wakati huo hakutaka hata kujisumbua kumtafuta tena Sharifa. Alishamwona mwanamke huyo kuwa yuko katika daraja tofauti na binadamu wa kawaida kama alivyokuwa akimwazia na kumjua.



Akawa akiwaangalia wale wacheza shoo jukwaani ilhali hata hayazingatii yale waliyokuwa wakiyafanya. Macho yalikuwa yameganda jukwaani, akili ikiwa kwa Ablah ambaye hakujua yuko wapi na ana hali gani.



Dakika kama tatu, nne hivi baadaye mhudumu yule alirejea na soda aliyoagizwa. Akaifungua na kutaka kuondoka baada ya kumsogezea glasi kubwa ya kinywaji hicho.



Karim akamwahi kwa kumshika mkono kistaarabu. “Samahani dada, nina shida kidogo.”



Yule mhudumu alimgeukia Karim na kumtazama kwa macho ya kikazi zaidi. “Kuna tatizo gani kaka’angu?”



“Uko busy sana?” Karim alijisahau na kuonesha kukerwa na namna mhudumu huyo alivyomuuliza.



“Hapana,” mhudumu alijibu akiyaepuka macho ya Karim baada ya kugundua kuwa labda kamkwaza.



“Ok, kaa kidogo tuzungumze. Dakika mbili tu dada’angu.”



Mhudumu yule aliinua shingo na kuangaza macho huku na kule labda akitafuta namna ya kuuepuka umbeya wa watu wasiokuwa na simile pale waonapo chochote kisichowahusu.

Alipogundua kuwa kote kuko shwari, akamrudia Karim. Akasogeza kiti na kuketi. “Enhe, n’ambie,” alimwambia akimkodolea macho.”



Karim alipiga hesabu ya moja na moja na kupata mbili. Akajua kuwa huyu mhudumu katii ombi lake akizingatia kupata ziada ya pato analopata hapo kazini. Akamheshimu kwa hilo. Akaamua kuugusa mfuko wake kisayansi.



“Umeniambia kuwa hauko busy, haupati hata kinywaji?”



“Bia, Tusker,”mhudumu alijibu.



“Chukua.”



Wakati mhudumu huyo aliposimama kukifuata kinywaji chake, Karim aliwaza, huyu mhudumu atamshtukia kama atamuuliza kuhusu KK Beach? Wazo hilo likayeyuka ghafla alipoamini kuwa kupajua KK Beach siyo ajabu. Labda zaidi atawaza kuwa anataka kwenda pia huko kustarehesha macho.



Muda mfupi baadaye mhudumu huyo alirejea na bia yake. Akatulia kitini na kuketi kwa mapozi.



Dakika tano baada ya mazungumzo ya hapa na pale hatimaye Karim akachokoza, “KK Beach iko wapi?”







MHUDUMU yule alimwangalia Karim kwa namna ya kumshangaa. Kisha akajibu, “Haiko mbali. Kwani vipi? Unataka kwenda kunywa bia huko?”



“Ninataka kufika huko,” Karim alijibu. “Kuna jamaa yangu ameniambia nikutane naye saa mbili.” Baada ya kusema hivyo akaibonyeza simu yake na kuyagandisha macho kwenye skrini. Akagundua kuwa ni saa moja na nusu. Kwa hali hiyo akaona kuwa huyu mhudumu hata kama atataka kumganda kwa mfumo anaotaka yeye, bado hatakosa mbinu ya kumwacha hapo na bia yake.



Mhudumu huyo naye aliichukua simu yake kwenye pochi lake, akaibonyeza sehemu fulani na mwanga mkali ukatokea kwenye skrini. Akatulia kwa muda mfupi akisoma saa, kisha akamwangalia Karim usoni sawia. “Bado. Kutoka hapa mpaka hapo KK ni kama dakika kumi na tano ukitembea. Kwa usafiri wako, ni dakika mbili tu.”



Karim hakusema kitu. Alikunywa soda yake haraka kisha akaitua chupa na kutoa mbwewe kubwa.



“Vipi, soda imekujaza tumbo?” mhudumu huyo alimuuliza.



“Ni kama umeijua hali niliyonayo,” Karim alijibu kwa unyonge. Alichokuwa akikifanya muda wote huo ni kuhitaji kuijua KK Beach ilipo na baada ya hapo amwache huyu mhudumu.



“Basi kunywa Konyagi.”



“Siku nyingine,” Karim alijibu huku akiachia tabasamu ambalo halikuwa halisi bali bandia. “Huwa napenda kunywa kama nimefika sehemu ambayo labda nitakaa kwa muda wa saa tatu, nne hadi tano. Lakini kwa kuwa hapa nimepita tu, nitashindwa kuendelea kupasha.”



“Umesema kweli kaka yangu,” mhudumu huyo alisema. “Inafaa upate kinywaji ukiwa katika kituo chako cha mwisho. Ingawa pia siyo vibaya kushtua akili hata ukiwa njiani. Kwani huwezi kupata toti mbili tatu za kukuchangamsha?”



Karim alimtazama kwa macho makali mhudumu huyo, macho ambayo alihitajika mtaalamu wa kiwango cha juu wa kutambua kuwa alimtazama tofauti na utazamaji wa kawaida. Ukweli ni kwamba, mhudumu hakujua kuwa Karim hakuwa hapo kwa ajili ya starehe. Hakuwa mtu wa kuendelea kukaa hapo, bali alihitaji kuwahi kufika Hoteli ya KK Beach ili ajue kama kinachompeleka huko kitapata ufumbuzi au la.



“Ingewezekana,” Karim alijibu kwa upole. “Tatizo ni muda dada. Hata hivyo, kitakachonikutanisha pale ni kitu cha dakika zisizozidi tano. Nitarudi tu hapa. Nimepapenda.”



Mhudumu huyo alimwangalia Karim kwa namna ya kutangaza hitaji lake la mapenzi. Akaachia tabasamu zuri la kinafiki. Akamkonyezea jicho Karim, ukonyezaji ambao akilini mwa Karim, ulikuwa miongoni mwa kero alizoweza kuzistahimili. Akamsamehe kinyemela.



“Utachukua muda mrefu?” mhudumu huyo aliuliza tena.



Sasa Karim alikuwa kakereka na maswali haya ya ‘kipolisi-polisi.’ Lakini bado alijitambua kuwa alipaswa kuwa makini na kuchukua uamuzi kwa umakini zaidi. “Dakika kumi tu,” alijibu.



Kisha, akiwa amechoshwa kubanwa na huyu mhudumu afanyaye kazi kibiashara zaidi, alisimama na kujinyoosha kisha akaisogeza chupa ya soda mbali zaidi katika hiyo meza, jambo lililotoa taswira kuwa anataka kuondoka.



“Kwa hiyo nd’o unaondoka?” mhudumu huyo alimuuliza.



“Ndiyo. Lakini sichelewi.”



“Huniachii hata bia moja wangu?”



Zilimchukua Karim sekunde zisizozidi tano kuchukua uamuzi. Alitambua fika kuwa hana uhakika wa kurejea kwenye baa hiyo. Kwani kilichomleta huku Kunduchi ni kustarehe na wanawake? Hapana. Kuna lililomleta, na ni hilo alilopaswa kulitekeleza na hatimaye ieleweke kama ameweza au ameshindwa.



Hata hivyo, alipaswa kuondoka hapo kwa namna ambayo haitawakwaza hawa wenyeji. Katika mazingira aliyonayo, hakujua kama labda anaweza kuhitaji msaada wao wakati wowote kwa sababu bado ana jukumu zito mbele yake hapo jirani tu. Kwa hali hiyo aliingiza mkono mfukoni na kuchomoa noti ya shilingi 5,000, akampatia mhudumu huyo na kumwambia, “Kaniletee elfu mbili.”



Mhudumu alipokea kwa bashasha zito. Dakika mbili, tatu hivi baadaye, alirejea akiwa na noti ya shilingi 2,000. “Asante, kaka,” alisema kwa unyenyekevu.



“Usijali, mtoto mzuri,” Karim alijibu huku akiipokea noti ile. Akampiga kijikofi cha mahaba shavuni huku akiongeza, “Nikirudi nataka uwe na nafasi zaidi tupige stori kwa uhuru na ukiniruhusu hata kwa mengineyo itakuwa poa zaidi. Umenielewa?”



“Nimekuelewa mwanaume handsome,” mhudumu huyo alijibu huku akichanua tabasamu kubwa zaidi. Kisha akaibeba chupa na kuigugumia bia iliyokuwemo. Akasimama na kuonyesha kutaka kuondoka. Lakini hakuondoka. Alimsogelea Karim zaidi na kumwegemea kwa namna ya kutaka matiti yake makubwa yakite kifuani kwa Karim.



Karim akampokea kistaarabu, akimkumbatia na kumpapasa kidogo mgongoni. Kisha, kwa sauti ya upendo na ustaarabu akamnong’oneza, “Tuko pamoja wangu. Nipe dakika chache tu.”



Mhudumu huyo alimwelewa kwa kiwango fulani. Hakuweza kumwelewa kwa kiwango chote na kuyaamini yote aliyoyasema. Hii ilikuwa ni wiki ya tatu hajakutana na mwanamume wa kumnunulia japo bia mpja. Huyu mwanamume ndiye kamnunulia. Isitoshe, kwa muda mrefu zaidi hajawahi kukutana kimwili na mwanamume yeyote. Damu ilimchemka lakini pia hakuwa radhi kumchojolea mwanamume yeyote labda kwa sababu hii au ile. Huenda huyu atatumia pesa nyingi akitaka kumhonga. Yule atatumia misamiati mingi ya lugha. Je, amvulie nguo kila atakayemtongoza?



Hapana. Kwa hilo hakuwa radhi kulitekeleza. Alihitaji mwanamume asiye mroho, mwanamume ambaye ataonesha dhahiri si kwamba anamhitaji kwa minajili ya kujistarehesha bali kwa mapenzi ya kweli.



Akilini mwake, huyu mwanamume aliyekuja kiajabuajabu na akiwa hajamwona hapo kabla, ndiye aliyestahili kumtuliza akili. Alimpenda!



Kwa sekunde chache ambazo walizitumia kukumbatiana hapo, mhudumu huyo alifarijika kwa kiwango fulani. Na alipojing’atua kifuani kwa Katrim alihema kwa nguvu kasha kwa tabu kidogo akasema, “Nakusubiri.”



“Poa,” Karim alijibu kwa dharau iliyofichika akilini mwake. Papohapo akageuka na kuangaza macho huku na kule, kisha akamrudia mhudumu, “Nitarudi baada ya nusu saa.”



“Poa wangu.”



Karim aliondoka, na hakugeuka. Na kwa kuwa ameambiwa kuwa KK Beach siyo mbali kutoka hapo, hakutaka kutumia gari hili alilokuja nalo. Alifanya makusudi kwa kuona kuwa huenda akawa anajitangaza zaidi kama atakwenda na gari hilo hapo KK Beach.



Wakati yuko hapo aliweza kuziona pikipiki tano, sita hivi zikiwa zimeegeshwa eneo la kuegeshwa magari. Na juu ya pikipiki hizi kulikuwa na watu. Karim hakuhitaji kujiuliza mara mbili kuwa hao ndio wale ‘bodaboda.’ Mazingira yaliliweka wazi jibu hilo.



Akamfuata mmojawao na kumgusa begani. Dereva huyo akashtuka na kumwangalia Karim. “Twende mjomba,” alisema kwa shauku kuwa ‘kapata kichwa.’



Kilichomfanya Karim aahirishe kupata huduma kwa huyo dereva ni ile harufu ya pombe kali iliyosikika kinywani mwake. Haraka akamfuata mwingine na kumnong’oneza, “KK Beach shilingi ngapi?”



Dereva huyo akageuka na kumtazama huyu mteja kwa haraka. “Siyo mbali mjomba. Buku mbili tu nakufikisha hadi mlangoni.



“Twende!” Karim alibwata huku akipanda pikipiki hiyo.



Dakika tano baadaye dereva wa bodaboda alikuwa akikanyaga breki nje ya hoteli maarufu ya KK Beach. Hawakuagana. Kila mmoja alishika njia yake.



Karim alisimama na kuhakikisha kuwa ile pikipiki imeshatokomea, ndipo alipoigeukia hoteli hiyo. Akayakumbuka maneno aliyoambiwa na Ablah. Akajawa na hasira sanjari na uchungu na akawa tayari kwa lolote litakalomkabili humo.



Hii ilikuwa ni hoteli kubwa kwake. Lakini haikuwa ya kumfanya awe mshamba. Hapana. Alijiamini kwa hilo, hivyo, hili lango la kioo lililokuwa mbele yake halikumstaajabisha pale alipolisogelea na likafunguka lenyewe kama vile ni kwa nguvu ya jini. Ndiyo, lilifunguka na alipopita likajifunga tena nyuma yake. Mambo ya Wazungu!



Karim akawa eneo lenye ukumbi mkubwa ambako watu walipata vinywaji na wengine wakipata maakuli. Hakukuwa na watu wengi, lakini hao wachache waliokuwepao walidhihirisha kuwa wana haki kuwa ndani ya hoteli hiyo. Sura zao zilizong’ara na mavazi yao ya gharama kubwa ilikuwa ni taswira kuwa hili ni daraja lingine.



Karim hakuwa mtu wa daraja la wengi waliokuwa humo lakini pia alibaini hakuwa peke yake. Kuna huyu mtu mmoja jirani naye, yeye alivaa kikawaida sana na akaonekana wa kawaida sana miongoni mwa wateja. Yeye alikuwa daraja lingine. Karim hakujali kuwa yuko daraja lipi, alijali kilichomleta humo.



Macho yake makali yakipita hapa na pale ukumbini humo, hakufanikiwa kumwona aliyemtafuta. Akabaini kuwa ukumbi huo ni mkubwa sana. Akaingizxa mkono mfukoni na kuikamata bastola kwa umakini huku akivuta hatua.



Muda mfupi baadaye akamwona mtu ambaye alimtilia wasiwasi. Akahisi moyo ukimwenda mbio. Akamkodolea macho zaidi japo mtu huyo alikuwa amempa mgongo, kakiegemea kiti hiki cha plastiki huku kajishika shavu.



Katika meza hiyo alikuwapo mwanamume. Akili ya Karim ikaamua kufa au kupona. Hizi nywele na hizi pete za kish’kaji zilizotapakaa vidoleni ilikuwa ni taswira halisi kuwa huyu ni Ablah. Kila siku tangu aje Dar na kuzunguka na Sharifa huku na kule hatimaye alinunua pete na kuzijaza vidoleni.



“Ni mwenyewe,” Karim alinong’ona kwa hasira. Na papohapo akaisogelea ile meza. Alipoipita kwa mbele akiwa kama aelekeaye msalani, akageuka na kumtazama huyu mwanamke mwenye urembo vidoleni.



Ablah!



Safari ya msalani ikafa. Papohapo akaifuata meza hiyo huku akimtazama huyu mwanamume aliyeketi na Ablah. Akasogea kwa hatua fupi lakini za umakini, macho yakiwa kwa watu hawa sawia. Sasa alikuwa tayari kwa lolote, akaukita mkono ndani ya mfuko wa suruali ambako aliishika ile bastola ya marehemu mzee Malick Sikonge!



Ablah!” alijikuta akiropoka kwa nguvu bila ya kujali faida au athari yake.



“Karim!” Ablah naye alishtuka na kubwata.



Kelvin aliyekuwa na glasi mkononi alishtuka na kumtazama Karim sawia, macho yake mekundu yakimkodolea bila ya kupepesa! Macho ya Karim yakahamia kwa Kelvin.



Wakatazamana!









SIMU iliita upande wa pili na Jitu alitulia akisubiri ipokewe. Sekunde kadhaa baadaye ikapokewa. Alikuwa ni Kelvin.



“N’ambie.”



“Jamaa wanataka kutoa em moja msh’kaji wangu,” alisema kwa sauti ya chini akiwa na hakika haiyafikii masikio ya Sharifa wala Abdul.



“Pesa ndogo hiyo ya nini, Jitu?” Kelvin aliwaka simuni. “Kwani mmekubaliana kiasi gani?”



Jitu akampa maelezo yote bila kuficha. Kelvin akamwelewa.



“Kwa hiyo inakuwaje kuhusu huo mzigo mwingine? Maana’ake hiyo ni kama shombo tu!” bado Kelvin alimbana.



“Hata wao wanaelewa hivyo,” Jitu alijibu. “Lakini ni bora tupate pesa ya kula halafu huyo malaya wao tumweke gesti fulani mafichoni hukohuko. Kwani uko wapi mida hii?”



“Niko KK Beach,” Kelvin alijibu. “Nimeshachoka msh’kaji wangu. Niko naye hapa, mimi napata kitu yeye anakunywa soda…”



“Hata akinywa mikojo siyo mbaya,” Jitu alisema kijeuri. “Endelea kukaa naye halafu baada ya dakika kama kumi hivi, nitakutumia kitu cha kueleweka, mkakodi chumba gesti. Huko gesti itabidi ubonyee naye hadi tufike.”



“Na mkishafika?”



“Hatutafikia hapo!” Jitu aligundua kuwa Kelvin alikuwa na haraka. “Tutafikia sehemu fulani halafu wakikamilisha mpango mzima, tunawaletea mtu wao. Yaani ni lazima wanithibitishie kuwa watatoa pesa yetu kamili kabla ya kuwapa mtu wao, basi hilo ni jambo lingine. Wala usiwe na mchecheto. Nimelisimamia suala hili kwa umakini kama vile nafikiria kumpendekeza rais atakayefaa kuiongoza Tanzania.”



Ukimya ukapita kati yao. Haya maneno ya mwisho ya Jitu, akilini mwa Kelvin yalikuwa ni sawa na kumpa mtu chai na kitafunwa kikawa ni mbegu za kukamulia mafuta bora ya Mawese au mtu unywe bia kwa vipande kadhaa vya viazi vitamu. Hakuna uwiano hapo!



Urais wa Tanzania na pato lao la mfukoni wapi na wapi? Akilini mwa Kelvin, siasa ulikuwa ni usanii asioupenda asilani. Hakuelewa ni kwa nini watu wanapoteza muda mwingi kwenye siasa, wakiumbuana, wakalumbana na kushutumiana. Hakuwaelewa! Yeye alijali amani na utulivu. Hakujali kelele za kisiasa.



Hivyo, moyoni akajikuta akimhusisha Jitu na fikra za wanaume wanaoingiliwa kinyume na maumbile. Akaendelea kuwa kimya huku kakunja uso.



Mara tena Jitu akaibuka, “Nipe muda. Usinipigie mpaka nikupigie. Narudi mezani kumalizana nao.”



“Poa,” kwa mbali sauti ya Kelvin ilipenya sikioni mwa Jitu.



Jitu aliirejesha simu kwenye mfuko wa shati na kuanza kurudi pale kitini.



Akawakuta Sharifa na Abdul wakiwa katika hali ya kawaida. Akaketi na kumtazama Sharifa kisha akamgeukia Abdul. Mara tena akamrudia Sharifa na kusema, “Sista rusha kwanza huo mzigo. Mwenzangu kakubali lakini kwa masharti.”



Sharifa akamkazia macho ndani ya kijigiza hicho cha wastani. “Masharti gani tena?”



“Kwamba, kabla ya kukutana na mtu wenu lazima tumalizane. Hapa tumeshakubaliana lakini umesema kwa hapa huna kiwango hicho. Kwa hiyo mtu wenu tutaendelea kumtunza hadi sisi na nyie tumalizane kimkwanja. Tuko pamoja?”



Hapo Abdul akaingilia. “Tuko pamoja, Jitu. Lakini tambua kuwa tumekuja hapa siyo kuahirisha mambo ila kuyamaliza. Kuchelewa kunaweza kuharibu kila kitu.”



“Hakuna kitakachoharibika kama nyie mtafanya mambo ndani ya saa ishirini na nne,” Jitu alisema kwa kujiamini.



“Unatuhakikishiaje kuwa hutatugeuka?” Sharifa aliibuka.



“Huwa sina tabia za kitoto, sista,” Jitu alijibu kwa majidai. Akakunja uso kisha akaongeza, “Ninachoona hapa ni kuzidi kupoteza muda. Hebu amueni moja basi.”



Kauli hii ya mwisho iliwashtua Abdul na dada yake. Papohapo Sharifa akasema, “Nakurushia milioni moja hii. Halafu kesho tukubaliane sehemu ya kukutana nikiwa kamili na tukutane na mtu wetu. N’ambie.”



Jitu akatikisa kichwa akionesha kuafiki. “Hapo sawa. Paisha basi huo mkwanja.”



Sharifa alishika simu na kuanza kubofyabofya. Wote walikuwa kimya huku Abdul akijishughulisha na kinywaji chake hali kadhalika Jitu. Baada ya kama dakika moja hivi, Sharifa akayainua macho na kumtazama Jitu. “Itanipa jina gani?”



Jitu akalitaja jina alilojua kuwa ndilo lililosajiliwa katika namba hiyo ya simu. Sharifa akarejea kubofyabofya kisha akayainua macho tena na kumtazama Jitu sawia. “Tayari,” alisema.



Sekunde chache baadaye mlio wa ujumbe mfupi ukasikika katika simu ya Jitu. Papohapo akaibonyeza sehemu fulani na kuzama akisoma. Tabasamu dogo likamtoka. “Ok, hapa nimekusoma sista. Lakini kesho uje kamili zaidi.”



“Usijali,” Sharifa alijibu.



Bila kuchelewa Jitu akanyanyuka tena na kusogea pembeni. Akampigia simu Kelvin. Simu ikaita mpaka ikakatika. Akapiga tena, ikaita tena na kukatika tena. Akakereka na kuamua kurudi mezani. Sasa akapiga kinywaji chake kwa mkupuo.



“Nadhani sasa tunaweza kuachana, tukutane kesho kumaliza mchezo,” alisema kwa utulivu huku akizichezesha funguo za gari mkononi kwa madaha.



“Saa ngapi?” Sharifa aliuliza.



“Nyie mkishakuwa tayari pigeni tupange namna ya kukutana. Mie tangu alfajiri huwa jicho kavu.”



Dakika tano baadaye Jitu alikuwa akibadili gia ndani ya gari akielekea Kunduchi. Kabla hajaiacha Barabara ya Shekilango na kuingia Barabara ya Bagamoyo, akiwa kwenye foleni, akaona ni muda mwafaka wa kumtafuta tena Kelvin. Akapiga. Simu ikaita na kukatika bila ya kupokewa.



Akashangaa na kujiwa na hisia zenye utata. Hakufikiri kama kuna baya lolote linaloweza kumpata Kelvin kutokana na kumshikilia Ablah na hasa ni kutokana na mazingira ya Kunduchi na huku Sinza kuwa tofauti sana.



Nani anajua kuwa Ablah kafichwa huko Kunduchi? Lakini alihisi kuwa huenda ubora wa Ablah katika sura na umbo lake vikawa ni vishawishi vya kumfanya Kelvin aamue kufanya ngono na Ablah. Na kwa fikra hizo akahisi kuwa labda muda huo wako katika kipindi ambacho Kelvin alikuwa akipata burudani halisi kiasi cha kutojali chochote kuhusu simu.



Akasonya na kuitupa simu kiti cha pili. Akatulia akisubiri taa ziruhusu. Hatimaye akaungana na msafara wa kuelekea Mwenge, Tegeta na kwingineko. Akavuta mafuta kwa nguvu huku umakini ukizingatiwa japo alikuwa anashangaa ni kwa nini Kelvin kamfanyia hivyo. Yaani anaweza kujali kustarehe na mwanamke ilhali wako katika mkakati mzito wa kujipatia pesa za kutakata? Hakumwelewa!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Hakutaka kupiga tena simu. Alipokaribia Makongo, alipaki gari pembeni, akawasha sigara na kuvuta mikupuo miwili, mitatu ya nguvu kabla hajaitupa nje na kujiweka vyema kitini. Akarudi barabarani kwa namna isiyo ya kawaida. Sasa gari lilikuwa kama linapaa!



*****



HAIKUHITAJI akili ya ziada kwa Karim kuyagundua macho ya Kelvin kuwa ni ya mtu wa kuchukuliwa hadhari kubwa. Yalikuwa ni macho makali, yaliyoashiria kuua au kufanya jambo lolote lile linaloweza kuhatarisha maisha ya mtu. Sekunde ya kwanza alimtazama, sekunde ya pili akawa amemrudia Ablah.



Kufumba na kufumbua Ablah akamrukia Karim na kumkumbatia. Lilikuwa ni tukio la ghafla lakini Karim alikubaliana nalo huku akizingatia kuwa umakini ulipaswa kupewa kipaumbele. Kisha Ablah akamnyooshea kidole Kelvin. Karim akaelewa, lakini Kelvin bado alikuwa kizani. Haraka Karim akageuza kichwa na kumtazama Kelvin kwa macho makali.



Akilini mwa Kelvin aliona kuwa dudubaya limeingia. Huyu Karim ni nani? Hakuwa na kumbukumbu sahihi kuhusu huyu mtu. Hakukumbuka kuwa kuna muda fulani simu iliita na kuliona jina hilo. Atakumbuka vipi ilhali hakuwa na wasiwasi wote wa kuvamiwa?



Hata hivyo, aliamini kuwa huenda Ablah anamtegemea sana huyu mtu kumwokoa, kwani asingediriki kumrukia na kumkumbatia kama asingekuwa anahitaji msaada wake. Hapo alipo alijua fika kuwa ametekwa, kwa hali hiyo, alitambua kuwa kama asipopata mkombozi basi atakuwa hatarini. Na akitambua fika kuwa kuna zaidi ya milioni kumi zinasubiriwa kwa kumtumia huyu Ablah kama kitegauchumi, papohapo akili yake ikazinduka.

Kwa kasi ya ajabu akajitoa kitini na kuwafuata Karim na Ablah. Umbo lake lilikuwa tishio kwa yeyote ambaye angemwona wakati huo. Kulikuwa na tofauti kubwa sana kimaumbile kati yake na Karim. Kwa urefu walilingana lakini kwa ukubwa wa miili, Kelvin alitisha! Baunsa! Hata tazama yao ilitofautiana. Kelvin alikuwa na aina ya utazamaji wa kuua au kujeruhi ilhali Karim tazama yake ilikuwa ya amani zaidi, tabasamu likichanua mara kwa mara usoni pake.



Kelvin alipowafikia, hakuuliza, aliinua kono la kulia na kulikita kati ya mabega yao kwa nguvu kubwa. Akavunja muunganiko wao kwa namna iliyowatia maumivu. Lilikuwa ni tukio la ghafla na la uhakika sana. Karim alishtuka, Ablah akataharuki.



“Unamjua huyu?” Kelvin alimuulza Karim kwa sauti ya kumtisha. Akamsogelea zaidi akimtanulia kifua kuonesha kuwa yuko vizuri zaidi kimapambano. Ikatokea taswira ya mmoja kumwonea mwingine.



“Wewe unamjua?” Karim naye akamuuliza, akirudi nyuma katika kuonesha kuwa anajiweka sawa.



“Unamjua?” Kelvin alizidi kumsogelea kisharishari.



Sasa Karim akaamua liwalo na liwe. “Simjui! We unasemaje?”



Ilikuwa ni kauli ikerayo masikioni mwa Kelvin. Mchanganyiko wa pombe na hisia za mpango wao kutibuliwa zilimfanya aamue kuchukua uamuzi papohapo. Akarusha ngumi kwa kasi, Karim akaiona, akainama kidogo na kuiacha ikipita peupe!



Hata hivyo, hiyo haikuwa dawa. Kelvin alikuwa amekunywa pombe nyingi lakini hakuwa mwehu, alikuwa na kiwango fulani cha kuweza kujipangia mipango kwa wakati kama huu. Kitendo cha Karim kuinama Kelvin alikitarajia, japo pia hakutarajia kuwa ataweza kuikwepa ngumi hiyo. Hivyo kwa umakini aliokuwa nao, hakumchelewesha, papohapo akamtwisha teke kwa guu la kulia, teke lililotua palepale palipokusudiwa!



Karima alihisi maumivu makali kwenye taya, akainuka na kujikuta akirudi nyuma hatua mbili bila stamina! Akaifikia meza ambayo haikuwa na watu, meza hiyo ikajivuta nyuma na kmwacha akianguka sakafuni peke yake mzimamzima!



“Mamaaaaa Karim!” Ablah alipiga yowe huku kajishika kichwa kwa kukata tamaa.



Kelvin akajikusanya upya, akiikunja na kuikunjua mikono kibaunsa huku akimsogelea Karim pale chini. Karim akaonekana kutoweza kumkaabili.







AKAUONA ugumu wa kazi iliyo mbele yake. Akajiuliza hapo anapambana na mtu au jini? Teke alilozawadiwa lilimtia maumivu makali, lakini akatambua kuwa kila sekunde iliyo mbele yake ingebidi aitumie kwa faida yake na ya Ablah.



Akili ikafumbuka zaidi na kuikumbuka ile bastola yenye risasi tatu. Haraka akaupeleka mkono mfukoni kuichomoa, lakini kama alijiona kuwa ana akili zaidi ya Kelvin, basi alikosea. Kelvin alikwishaijua dhamira yake; kwenye tukio kama hili la kutekwa mtu na halafu akatokea mkombozi, kwa vyovyote vile mkombozi huyo atakuwa amejipanga kwa silaha.



Hivyo, kwa mazingira haya, aliamini kuwa huenda Karim anataka kutoa silaha baada ya kuona amezidiwa kwa kipigo, na pia labda silaha hiyo ni bastola au kisu.



Kwa wepesi wa aina yake Kelvin aliukita mguu kwenye mkono wa Karim, hapo Karim akakumbana na maumivu makali huku pia akiwa ameshindwa kutimiza azma yake ya kuichomoa bastola.



Kelvin akawa amedhamiria kumshushia vipigo vya mfululizo ili kumwondolea kabisa nguvu za kujitutumua na baada ya hapo aondoke haraka na Ablah kwa kuwa alipaona hapo panaanza kuingiwa na nuksi.



Wakati huo watu wachache waliokuwa humo ukumbini walishasimama na kusogelea hapo labda kwa minajili ya kushuhudia kinachoendelea au kusuluhisha kwa kuingilia kati. Kelvin alihitaji kuwawahi hao waliotaka kumharibia programu ya kummaliza mtu.



Hata hivyo, kabla hajanyanyua guu la kushoto kwa ajili ya kukandamiza teke la nguvu kifuani pa Karim, kilitokea kile ambacho hakukitarajia. Karim alijikunja na kwa kasi akasukuma teke zito kwa guu lake la kulia, teke lililotua katikati ya maungio ya miguu ya Kelvin na kumzushia maumvu makali kwenye korodani, maumivu yasiyostahimilika hivyo akajikuta akishindwa kuendelea na programu yake. Akajikunja na kuikita mikono kwenye eneo lililojeruhiwa.



Ukawa ni mwanya wa Karim kuweza kunyanyuka na kujitutumua. Wakati mmoja wa watu wawili waliokwishafika hapo alipotaka kuingilia kati, Karim alimsukuma kando kisha, kwa wepesi wake uleule ambao ulimshangaza Ablah na hata watu wengine, alimrushia Kelvin mateke mawili kwa mguu wa kushoto kisha wa kulia na yote yakiwa katika shabaha kali na yenye uzito wa kilo nyingi, moja likampata mbavuni na lingine usoni.



Yalikuwa ni mashambulizi ya kushtukiza, yaliyomfanya Kelvin ajikute akiwaangukia wateja waliokuwa kwenye meza iliyokuwa nyuma yake, lakini nao kwa hasira wakamsukuma na kujikuta akirejea kwa Karim ambaye alimzawadia konde zito kidevuni, konde lililomsukuma hadi ukutani. Akajibamiza kwa nguvu na kubonyea taratibu chini akiwa hajiwezi, damu ikimvuja mdomoni na puani kwa wingi.



Hasira zikiwa bado katika mzunguko mkali akilini mwa Karim, alijipanga kumrukia pale chini kwa minajili ya kumaliza mchezo na kama siyo ujasiri wa wanaume wawili walioshiba, waliomtinga mbele na kumkinga Kelvin asidhurike, huenda kipigo ambacho kingefuatia kingezua simulizi nyingine kuhusu Kelvin.

“Kuna nini? Kwani vipi?” mmoja wa walinzi wa hoteli hiyo alimuuliza Karim huku walinzi wengine wenye virungu wakiwa wamemzunguka.



“Muulizeni mwenyewe,” Karim alijibu kwa hasira, sasa ule uso wa upole ukiwa hauonekani tena.



“Wewe ndiye ungetueleza brother,” mlinzi mmoja alimsihi Karim. “Unajua wewe ulipofika tu ndiyo haya yamezuka. Tatizo ni nini? Ni huyu dada?” akamgeukia Ablah.



Ni hapo ndipo Karim alipozinduka na kuamua kuliacha eneo hilo haraka. Alihisi kuwa huenda Kelvin akawa na wenzake au mwenzake, hivyo hatari kwa Ablah huenda ikawa bado ipo. Aliamini kuwa kama watu hawa watagundua kuwa mpango wao umetibuliwa, wanaweza kuchukua hatua yoyote hata kama itawalazimu kuyasimamisha mapigo ya moyo wa Ablah.



Akamfuata A blah na kumshika mkono. “Twen’ zetu.”



Mlinzi mmoja akamfuata Karim na kumzuia. “Mjomba, subiri kwanza. Hapa mmeleta vurugu na kutuvurugia biashara.”



“Tafadhali, nipe nafasi niondoke!” Karim alimwambia huku akimtazama kwa jicho kali zaidi, jicho lililomtisha yule mlinzi, na kwa kuzingatia jinsi alivyoshuhudia vipigo alivyoshushiwa Kelvin, akajenga imani kuwa Karim yuko katika daraja la juu kwa mapigano; siyo mtu wa kujaribiwa, atakuua! Akamgwaya!



Karim akamvuta Ablah na kutoka kasi huku Ablah akiwa kama anayeburutwa. Walipofika nje, akaziona pikipiki mbili, akaifuata moja haraka na kumwamuru dereva awapeleke Makonde Bar.



Wakapanda ‘kimshkaki.’ Kijana akiwa hajui kilichotokea huko ndani, akawasha pikipiki na kuiondoa haraka. Dakika chache baadaye walikuwa Makonde Bar. Karim akampa kijana huyo noti ya shilingi elfu tano. Kijana alipomwambia amsubiri kidogo akaombe chenji kwa madereva wenzake wa bodaboda waliokuwa hapo, Karim akamwambia, “Chenji yako hiyo. Hatuna muda mchafu wa kusubiri.”



Kijana akatabasamu na kugeuza pikipiki akirejea KK Beach.



******



JITU alipofika KK Beach alitafutra sehemu nzuri na kuegesha gari. Alipoipata akampigia Kelvin akiwa humohumo garini. Simu ikaita hadi kukatika. Akasonya kwa mara nyingine. Kwa kiasi fulani akailaani tabia ya Kelvin ya kuondoa mlio katika simu na hata mtetemo wa kuweza kumsaidia kujua kama anapigiwa simu hasa kama kama iko mfukoni.



“Huyu Kelvin ana tabia ya kibwege,” alijikuta akiropoka kwa hasira huku akifungua mlango na kutoka akilifuata geti kuu la kuingilia hotelini hapo.



Huku akizichezesha funguo za gari mkononi kwa namna ya madaha, aliwapita walinzi wawili waliokuwa wakizungumza kwa chini huku nyuso zao zikiwa zimetahayari. Aliwatazama mara moja tu na wao wakamtazama kama mteja wa kawaida, akawapita na kuingia ndani zaidi akielekea eneo la ukumbi wa vinywaji.



Kwa mbali akauona mkusanyiko wa watu, baadhi wakiwa wameinamia kitu ambacho hakukiona. Akawa amefika katikati ya ukumbi, akaangaza macho huku na kule, akitarajia kuwaona Ablah na Kelvin katika meza mojawapo. Hakuwaona. Akaamua kuusogelea mkusanyiko ule wa watu huku moyoni akihisi jambo lisilo la kawaida. Akaukita mkono mfukoni na kuishika bastola na hakuutoa mkono huo hata alipowafikia watu hao.



Akiwa hajafanikiwa kukiona hicho wanachokitazama wengine kwa kuwa walikuwa wamemziba, akasikia baadhi wakisema, “Daa jamaa anazijua yule…maana’ake yale mateke mawili ya mwisho yalikuwa ya kuua mtu…



“Labda ni askari yule…” wa pili alidakia.



“Na kaondoka na yule demu…” mwingine akasema.



“Hakuna cha askari…hawa wanagombea yule malaya aliyeondoka na jamaa…” wa nne akasema huku akigeuka na kujitoa hapo.



Ni hapo Jitu alipopata mwanya wa kusogea na ndipo aliposhushudia kile ambacho hakukitarajia.



“Kelvin!” aliropoka kwa uchungu. “Kelvin…imekuwaje wewe…”



Watu wote waliokuwa hapo wakamgeukia Jitu. Mlinzi aliyekuwa kamwinamia Kelvin akanyanyuka na kumtazama Jitu. “Unamfahamu? Ni nani yako?”



Jitu hakujibu. Akawasukuma watu wawili na kuchuchumaa mbele ya Kelvin.



Ilimwia vigumu Jitu kuamini kuwa amwonaye hapa ni yule Kelvin anayemfahamu. Uso ulikuwa umevimba, damu zikimtoka mdomoni, meno mawili ya mbele yakiwa yametoka. Alikuwa akihema kwa shida huku akijishika mbavuni.



Jitu akiwa ametaharuki, alimshika kichwa na kumwinua. Wakatazamana ilhali Kelvin akionekana bayana kuwa yuko hoi.



“Vipi mtu wangu, imekuwaje?”



“Alinivamia...”



“Nani? Nani kakuvamia?” Jitu aliuliza haraka huku akimsukasuka begani kama anayemzindua.



“Bwana’ake,” bado Kelvin alisema kwa tabu.



“Bwana’ake? Ni nani huyo?” Jitu alikuwa akihema kwa nguvu, hasira ikiwa imeutawala moyo wake.



Kelvin hakuwa na kumbukumbu ya kila kitu kilichotokea baada ya kuanza kupokea vipigo. Akabaki akihema kwa shida, mara akijishika mbavu mara akijipapasa mdomoni. Akatikisa kichwa kwa uchungu. Pombe zote ni kama zilikwishayeyuka kichwani.



Mara mmoja wa wateja waliokuwa kwenye meza zilizokuwa jirani na pale walipokuwa wameketi Kelvin na Ablah akamgusa begani Jitu na kumwambia, “Anko, sikia kwanza. Najua hujui kilichomkuta huyu jamaa yako. Kwa kifupi kama una usafiri mchukue maana’ake kaumia sana.”



Jitu alisimama na kumtazama jamaa huyo huku akitikisa kichwa kwa masikitiko. Kisha akamuuliza, “Mjomba unajua chochote kuhusu mkasa wa huyu msh’kaji wangu?”



Jamaa yule akatabasamu kwa mbali na kusema, “Inaonekana tatizo hapa ni mapenzi. Jamaa yako alikuwa kaketi na sijui ni demu wake yule au vipi, mara tukaona demu anakurupuka na kuita Karim! Papohapo akajitoa mezani na kumrukia huyo jamaa aliyemwita kwa jina la Karim. Akamkumbatia. Haukupita muda ndipo timbwili kati ya wanaume hao likazuka. Huyu jamaa yako kamshushia kipigo yule mgeni lakini mara kibao kikamgeukia na kaumizwa sana kwa kweli msh’kaji.”



“Demu aliita Karim?!” Jitu aliuliza kama anayehitaji uthibitisho.



“Yeah, kamtaja yule jamaa kwa jina la Karim. Ni bwa’mdogo tu hivi wa kawaida lakini anaonekana ana mazoezi fulani ya kimwili manaake…” sentensi ikaachwa ikielea.



“Shit!” Jitu akabwata. Kutajiwa jina la Karim kukawa kumemfumbulia kitendawili. Wakati Abdul alipomfuata kwa mara ya kwanza akimpa tenda ya kumteka Ablah, alimtaja Karim kama kibaraka aliyejipendekeza kuitunza mali iliyoachwa na marehemu Malick Sikonge. Na akamwambia ni huyo Karim ndiye kamleta Ablah kutoka Arusha na anampa mwongozo wa jinsi ya kuiendesha miradi ya marehemu.



Kilichomshangaza hapa ni jinsi Karim alivyoweza kujua kuwa Ablah katekwa na yuko huku KK Beach. Alijuaje ilhali simu ya Ablah ilikuwa kwenye himaya ya Kelvin? Au Kelvin alijisahau na kuiacha mezani, akaenda msalani? Hapana, hilo halikumwingia akilini Jitu. Alijua jinsi Kelvn anavyokuwa makini hata anapokuwa amekunywa pombe nyingi.



Sasa akajua kuwa Karim huyu aliyetajwa na huyu jamaa ndiye yule Karim kibaraka wa marehemu Malick. Akajishika kiuno kwa sekunde tano tu kisha akachukua uamuzi.

Akainama na kuipitisha mikono makwapani mwa Kelvin. “Jikaze Kelvin…jikaze, twende kwenye gari nikupeleke hospitali,” alisema huku akitambua fika kuwa hawezi kumpeleka hospitali bali nyumbani.



Walinzi wawili wakamsaidia kumwinua Kelvin ambaye alilalamika maumivu mbavuni.



“Mshike vizuri, isije kuwa amevunjika mbavu,” mlinzi mmoja alimwambia mwenzake.



Walipofika nje, wakamwingiza kwenye kiti cha nyuma, akalala huku akiendelea kugugumia kwa maumivu.



******



“HARAKA Ablah,” Karim alimwambia Ablah walipoachana na ile pikipiki. Akamshika mkono na kutembea haraka wakilifuata Range Rover.



Dakika tatu baadaye Karim alikuwa akibadili gia kwa mkupuo wakiliacha eneo la Makonde Bar, Ablah akiwa ameketi kiti cha pili.



Baada ya dakika chache za ukimya, huku kila mmoja akihema kwa kukosa utulivu akilini, Karim akauvunja ukimya.



“Ablah, maisha yako na yangu yako hatarini. Nadhani sasa umemjua vizuri Sharifa. Naamini kwa asilimia zote kuwa anahusika. Na hajui kama nimekuokoa, ila akijua anaweza kupanga chochote kibaya zaidi.”



“Jamani Karim, nimemkosea nini Mungu… jamani…tutafanyaje Karim?” Ablah alikuwa akiomboleza.



“Nilifikiria kuripoti polisi lakini naona kama hatuna ushahidi wa kuwatia hatiani. Tutacheza nao. Tuombe Mungu Ablah, naamini yuko upande wetu. Na sasa inabidi tuanze kuwa makini kabla hata hatujafika nyumbani. Hatujui Sharifa yuko wapi, na alinikatia simu muda nilipompigia.”



“Na unasema ulitekwa na watu wawili, sio?”



“Ndiyo. Walikuwa wawili, halafu baadaye wakaongea nje kwenye gari, kisha mmoja akaondoka na gari na huyu mwingine ndiye akabaki ananidhibiti. Sijui yule wa kwanza alikwenda wapi.”



Ni nani huyo? Karim alijiuliza na kukosa jibu. Pia hakujua huyo mwenza wa huyu aliyemtia vipigo KK Beach atakapokuta mateka wao kaokolewa atachukua hatua gani. Bado kulikuwa na kizungumkuti.











MARA tu Jitu alipoondoka Corner Bar, Sinza, Sharifa na Abdul nao wakaondoka. Njiani Sharifa akamkumbuka tena Karim. Huku akiendesha gari kwa mwendo wa wastani, akasema, “Abdul, yule bwege naona kama anataka kutuharibia siku.”



“Bwege gani, Karim?”



“Nd’o mwenyewe!” Sharifa alisema kwa msisitizo. “Si unaona kama vile machale yamemcheza…”



“Ni kweli, lakini usihofu. Tukiona kama anataka kutuletea usiku tunammliza tu. Au?”



“Ndicho nilichotaka kukwambia. Yule daktari najua hawezi kufanya chochote, na kwanza hata haonyeshi kama anayafuatilia mambo haya. Yeye yuko bize na mambo ya taaluma yake.”



Ukimya ukapita kisha Sharifa akaendelea, “Najua atamaindi sana kwa kumkatia simu, na ndiyo maana hajapiga tena.”



“Anakusubiri nyumbani akuulize umemwacha wapi huyo malaya wake…” Karim alimkata kauli.



“Najua ndicho kitakuwa cha kwanza kuhoji,” Sharifa alisema huku akisonya.



Sharifa akamwacha kaka yake pale kwenye maskani yake na yeye akaendelea na safari ya nyumbani. Njiani hakuwa na utulivu akilini. Kile alichokitarajia sicho kilichotokea.



Alitarajia kuwa baada ya Jitu na mwenzake kumteka Ablah, dakika kadhaa baadaye wangemtaarifu kuwa kazi imemalizika hivyo wakutane kwa ajili ya kumaliza biashara, yaani malipo yaliyosalia; shilingi milioni moja na nusu. Lakini sivyo ilivyotokea, badala yake ni kuanza kuongea biashara upya!



Ilimkera kwa kuwa hakujua kuwa Karim atakuwa amewaza nini na ana mpango wa kufanya nini. Kwa muda huu walioachana na Jitu akienda huko aliko Ablah, hakujua watakachoamua yeye na mwenzake watakapokutana.



Mwanadamu wa leo ni wa kuaminika? Akilini mwa Sharifa, wakati akibadili gia akiingia Barabara ya Haile Sellasie, hakutaka kujidanganya kuwa Jitu ni mwaminifu kwa asilimia mia moja. Hapana, Jitu ni mwanadamu wa kawaida, aishiye maisha ya kawaida, katika mazingira ya kawaida. Ni kipi kitamfanya leo awe mwaminifu kama ameshabaini kuwa mpango unaofanyika unahusu mamilioni ya pesa? Kwa vyovyote vile, atahisi kuwa pesa inayofukuziwa, ambayo inasababisha binti huyo atekwe ni zaidi ya pesa za kawaida.



Kesho itakuwa kama leo? alijiuliza swali hilo akizingatia kuwa huenda mwenzake Jitu asikubaliane na malipo haya yaliyotolewa usiku huu na wala asiwe tayari kupewa ahadi nyingine. Kitakachofuata, kwa namna moja au nyingine huenda kikawa ni kile kisichopendeza akilini mwake.



Mpango unaweza kutibuka kwa asilimia mia moja na hapo ndipo atakapojikuta katika wakati mgumu zaidi. Hata hivyo hakutaka kukiumiza kichwa chake kuhusu hilo. Aliamua kutuliza akili barabarani hadi atakapofika nyumbani na huko ndipo atakapojua kinachoendelea. Akatulia nyuma ya usukani na kuwa makini hadi akajikuta nje ya geti la jumba la kifahari la marehemu Malick Sikonge. Akapiga honi mara mbili.



Mlinzi aliyekuwa bandani akatoka hima na kuja getini. Akachungulia kwenye kijitundu kidogo cha getini, alipoliona gari lililoegeshwa, akajua ni nani aliyekuja. Haraka akalifungua geti.



Sharifa akaingia kwa makeke, kwa namna iliyomshangaza hata mlinzi, lakini akabaki kaduwaa. Mara tu Sharifa alipokwishaegesha gari aliteremka haraka na kumfuata mlinzi.



“Juma,” alimwita wakati akimsogelea. Hakusuburi kuitikiwa. Likamtoka swali: “Karim yuko ndani?”



Mlinzi huyo alimtumbulia macho Sharifa tofauti na siku nyingine. Alihisi kuwa bosi wake huyo hayuko katika hali nzuri. Kwa namna alivyomwona, hakutaka kuchelewa kumjibu. “Hayupo mama,” alijibu.



“Yuko wapi?” Sharifa alimuuliza papohapo huku akimtazama kwa macho makali.



“Sijui kaenda wapi lakini katoka muda mrefu kidogo, mama,” mlinzi alijibu kwa sauti ya nidhanu zote.



“Katumia gari kubwa?”



“Ndiyo, mama. Katumia ile Range. Na ni kama alikuwa na hasira hivi maana’ake alivyotoka mmhhhh…”



Sharifa akahema kwa nguvu akiwaza, Karim atakuwa kaenda wapi? Baada ya kumkatia simu alikasirika na kuamua kuchukua hatua nyingine kutokana na hasira za kukatiwa simu? Na je, hatua hiyo itakuwa ipi? Kaenda wapi?



Zilimchukua sekunde chache tu kufikiri na kuamua kuchukua uamuzi. Akamwacha mlinzi huyo na kuelekea ndani. Akitemnbea kwa hatua ndefu huku akihema kwa tabu, ilikuwa ni bahati tu kuwa hakukuwa na mtu yeyote mwingine ambaye alimwona au kukutana naye njiani. Dakika kama mbili hivi baadaye alikuwa chumbani mwake.



Humo chumbani hakukaa wala kulala. Mara tu alipokwishafunga mlango alijitupa kwenye sofa kubwa na kubofya tarakimu kadhaa za namba ya simu ya Abdul. Simu ikaita kwa muda hadi ikakatika, lakini papohapo akapiga tena na punde ikapokewa.



“Nambie sista,” Abdul alipokea kwa namna ya mshtuko. “Inakuwaje?”



Kimya cha sekunde chache kilipita kisha Sharifa akaibuka. “Abdul, huyu mtwana hayupo,” Sharifa alisema kwa hasira. “Hayupo, na nimeambiwa getini kuwa kaondoka katika namna isiyo ya kawaida. Nina wasiwasi kuwa huenda ishu imebuma.”



Abdul alisonya kwa sauti iliyoyafikia masikio ya Sharifa sawia. Kisha: “Yule ni bwabwa tu sista. Kwani baada ya kumkatia simu alikupigia tena?”



“Hajapiga, na hicho ndicho kinanifanya niwaze mengi hapa,” Sharifa alijibu.



Abdul akaguna. “Unajua yule ni bwege mwenye akili nyingi kwenye bichwa lake lile…tena anaweza kuwa amewaza mengine kwa kuwa siku ile yule bwege wako kibabu alipokuwa akikaribia kukata kamba alidiriki kuropoka kuwa hukubaliani na ishu kuwa kuna mtoto wa yule kibabu. Unalikumbuka hilo?”



“Nakumbuka,” Sharifa alijibu haraka na kuongeza, “Kwa hiyo inakuwaje?”



“Mshenzi atakuwa labda amekwenda polisi baada ya wewe kumkatia simu na huku yule malaya wake hajarudi.”



Kwa mara nyingine Sharifa akahisi kuwa yuko kwenye kipindi kigumu. Karim kwenda polisi? Aliona ni kiinimacho kisichopendeza, lakini pia alihisi kuna ukweli fulani katika maneno hayo. Alitambua fika kuwa siku ile siku ambayo mzee Malick alikuwa hoi bin taaban ni Karim huyuhuyu aliyesikia kila klichosemwa na yule mzee.



Ni kwamba, Karim hakuwa na imani naye kuanzia siku ile na pia ndiyo sababu iliyomfanya jioni hii ampigie simu akiuliza kuhusu kuchelewa kwao.



Hii kauli ya kaka yake ilikuwa sahihi kwa asilimia nyingi. Sharifa akajiona kuwa yu katika wakati mgumu zaidi. Akabaki katulia huku simu ikiwa imeganda sikioni.



“Unasikia sista,” hatimaye Abdul aliibuka. “Us’konde. Hawatuwezi mbwakoko hao. Si uko homu?”



“Nd’o naingia. Nd’o nimepaki gari.”



“Ok, usijali dada yangu,” Abdul alisema kwa upole. “Jarkumpigia uone kama na yeye atauchuna.”



Sharifa akiwa amesimama nje ya mlango wa chumba chake, alimpigia simu Karim.



*****



HIKI kilikuwa ni kipindi kigumu sana kwa JItu. Alijiona kuwa yuko katika wakati mgumu zaidi. Hata hivyo hakuwa tayari kuinua mikono. Hapana. Japo Kelvin, mtu aliyemtegemea kwa kila hatua iliyokuwa mbele yao katika mpango huu ndiyo kishajeruhiwa kwa kiasi kubwa hivi, bado hakukata tamaa.



Akaendesha gari hadi nyumbani kwa Kelvin. Alipokwishafika nje ya nyumba hiyo akateremka haraka na kulifuata geti ambalo alilifungua kisha akarudi garini na kuliendesha taratibu. Alipokwishahakikisha kuwa yuko ndani, akapaki na kuzima gari.



Akamgeukia Kelvin aliyeonekana kuwa yu hoi. “Oyaa Kelvin jikaze mwanaume…we vipi?”



Kelvin ambaye alitekwa na usingizi ghafla, aliibuka na kubwata, “Vipi?”



“Tu’shatia tim hapa kwako hapa ujue!” Jitu alisema kwa sauti yenye mchanganyiko wa hasira na fadhaa. “Teremka msh’kaji wangu. Ulishaliharibu we’ teremka uingie maskani kwako. Kitakachobaki acha nicheze nitakavyoweza. Umeendekeza sana mipombe Kelvin…”



Kauli hii ya mwisho ilimzindua Kelvin na kumpandishia munkari. “Acha upumbavu wewe…” alibwata. “Ukiona mtu kanywa bia aua hata pome kali usidhani kuwa kawa mwehu! We vipi mwanangu? Unakuwa na tabia za kishoga m’shkaji wangu…”



Ilimwingia Jitu kama kisu chenye makali ya kutisha. Kufananishwa na shoga! Hata hivyo alijitahidi kustahimili, akiamini kuwa kinywa cha Kelvin kilitumia nguvu ya kilevi. Akamsamehe.



“Ok,” hatimaye Jitu alisema. “Us’jali, sasa we’ ingia ndani, kwa sasa niachie mimi mchezo uliobaki.”



Kilichofuata ni kumsaidia Kelvin kuingia ndani mwake na baada ya hapo, alirudi garini ili arudi nyumbani. Dakika kumi baadaye alikuwa akiliegesha gari eneo fulani pale Kawe, mbali sana na kwake, akalipia gharama za kulilaza gari kisha akatembea taratibu akienda nyumbani kwake.



Kichwani mwake hakuwa timamu, na wala hakutarajia kuwa hili lililotokea ndilo ambalo lingetokea. Kwa mbali alihisi kuwa karata inayochezwa huenda imeangukia pabaya, hisia ambazo hakuwa tayari kukubaliana nazo.



Kilichomsumbua akilini ni jinsi ya kuwakabili Sharifa na kaka yake na kuwaambia bayana kuwa Ablah katoroshwa? Atawaambia vipi? Tayari wameshachukua pesa, halafu eti wadai kuwa mlengwa katoroshwa! Ni hii taarifa ambayo hakujua kuwa itachukuliwa vipi kwa watakaopewa taariufa.



Hata hivyo aliamua kuumaliza usiku huo kwa namna hiyo, bila ya kukisumbua kichwa. Alipokivaa kitanda, aliizima simu, akalala huku mara kwa mara akisonya kwa hasira.



Saa tano usiku hakuiona!



*****



NDIYO, kilikuwa ni kizungumkuti. Karim alijiona kama yuko kwenye sayari nyingine. Alijitambua fika kuwa alikuwa na jukumu la kumlinda Ablah na kuyalinda masilahi ya marehemu mzee Malick. Lakini yuko peke yake! Ataweza?



Walijikuta wakiwa kimya hadi walipokaribia kufika nyumbani. Na hapo ndipo aliposikia mtetemo wa simu yake. Haraka akaitoa mfukoni. Alipotazama kwenye skrini akashtuka, jina la SHARIFA lilikuwa likielea. Akawaza, aipokee au aachane nayo? Simu ikaita mpaka ikakata.



Mara ikaanza kuita tena. Karim akiwa na hasira kichwani, akasonya na kuamua kuipokea.









KWANZA akapunguza mwendo na kuegesha gari kando ya barabara. Kisha akabonyeza kitufe cha kupokelea na kwa sauti ya chini sana akasema, “Haloo.”



Upande wa pili Sharifa alihisi tofauti na kwa kiasi kikubwa akaamini kuwa tayari Karim kishaushtukia mchezo.



Huku kiroho kikimdunda, akajitia kuiweka sauti yake katika hali ya kawaida na kuhoji, “Haloo Karim vipi? chaji ilikata ghafla. Ulikuwa unasema?”



“Basi tena ilishapita hiyo,” Karim alijitahidi kuidhibiti hasira yake. “Kwani mko wapi? Bado mko Mlimani City?”



Lilikuwa ni swali lililokita kwenye mtima wa Sharifa kama kisu. Akawaza amjibu kuwa bado wako Mlimani City wakati siyo kweli? Na kama atazuka hapo nyumbani na kutomkuta Ablah, kitakachofuata ni nini? Patatosha kweli humo ndani? Huyu Karim alistahili kufa mapema zaidi kabla hata ya leo! Aliwaza kwa hasira.



Ukimya wake ulimfanya Karim upande wa pili aachie tabasamu dhaifu, tabasamu lililofurika hasira kila alipomtazama Ablah kando yake. Tayari alijua kuwa kamshika pabaya Sharifa na katika kuzidi kumchanganya akamuuliza, “Mbona kimya?”



Sharifa akajikohoza kidogo kisha akasema, “Aaaa hatuko Mlimani…tumesharejea muda tu. Kwani we’ uko wapi?”



“Nimetoka kidogo,”Karim aliamua kujibu hivyo.



“Uko mbali?” swali hili lilipenya masikioni mwa Karim papohapo na kuwa kama lililohitaji jibu la papo kwa papo.



“Yeah, niko mbali,” Karim alitega. “Kwani vipi, kuna tatizo?”



“Aaa…” Sharifa alisema na kusita. Kisha akaipata sauti yake, “Hakuna tatizo…basi tu si unajua tena tumezoea kukuona mida hii kwenye kucheki taarifa ya habari au muvi.”



“Kawaida tu,” Karim alisema kwa namna ileile ya kujitahidi kuidhibiti hasira. Kisha katika kuzidi kupata taswira halisi, akamuuliza, “Ablah yuko hapo jirani? Nataka kuongea naye.”



Ulikuwa ni msumari mwingine akilini mwa Sharifa. Alipoulizwa awali kama wamesharejea alijibu ndiyo, huku akijua fika karudi peke yake. Hata hivyo, alitumia akili kuwahi kujibu kulingana na aina ya swali aliloulizwa.



“Yuko bafuni anaoga.”



Kitu kama mwali mkali ulipita mbele ya macho ya Karim. Akahisi mapigo ya moyo yakibadilika. Nyama za mdomo zikamcheza. Akauma meno kutokana na hasira zilizozidi kujikita katika mtima wake. Akakunja ngumi huku kakaza macho mbele. Kauli hii ya Sharifa ilimkera sana. Eti Ablah yuko bafuni huku kakaa hapa kiti cha pili!



Kwa sekunde mbili alizokuwa kimya hazikumfanya Sharifa ashuku lolote kwani tayari alipachika neno, “Kachoka sana na hajaizoea hii hali ya joto lililoanza sasa.”



Mpumbavu! Karim alijikuta akitukana kimoyomoyo. Kisha kwa sauti ileile ya kawaida, akasema, “Ok, tutaonana baadaye. Bado kuna suala nalifuatilia huku Kariakoo.”



“Ok, poa,” Sharifa alijibu huku akifarijika kwa kiasi fulani.



Mara tu walipokata maongezi, papohapo Sharifa akaharakisha kumpigia kaka yake, Abdul. Simu iliita kwa muda mfupi tu na kupokewa.



“N’ambie sista.”



“Sikia Abdul, “ Sharifa alisema kwa namna ya kujawa na taharuki. “Nina wazo moja. Huyu bwege nahisi ni kama ameshtukia mchezo. Kwa namna nilivyoongea naye anaonekana kuhisi kitu.”



“Woga wako tu sista,” Abdul alimpinga. “Kwani anasemaje? Amegundua kuwa malaya wake yuko wapi?”



“Hajagundua lakini anaonyesha tu kuwa hayuko vizuri. Kaniuliza yuko wapi nikamwambia anaoga.”



“Na yeye anasema yuko wapi?”



“Nani, huyu bwege?”



“Ndiyo!”



“Kasema yuko Kariakoo.”



“Kwa hiyo ulikuwa unataka tufanyeje sista?”



Wazo langu ni hili…” kufikia hapo Sharifa alisita kidogo kisha akaishusha zaidi sauti na kusema, “Tumzimishe!”



Lilipenyea kwa usahihi sikioni mwa Abdul. Papohapo akamwahi, “Unasema?”



“Hujanisikia?” sauti ya Sharifa ilipaa kidogo na kuwa kama aliyekasirika.



Abdul akanywea kidogo. Haraka akasema, “Nimekusoma, sista. Lakini mbona hapo pagumu kidogo. Unadhani tutaweza? Na ulidhani iwe lini?”



Msonyo mkali ukatoka kwa Sharifa. “Hivi we’ Abdul mbona unakuwa kama si mwanaume. Upoupo tu kilevilevi. Huna hata wazo la namna ya kufanya ili tuue hii soo inayotunyemelea! Nimekwambia bwege kishashtukia mchezo. Na hata kama hajashtukia, tuseme kweli tu ni kwamba, akitoka huko Kariakoo na kutomkuta hapa malaya wake unadhani atawaza vipi? Nd’o maana nakwambia ni afadhali tummalize yeye kwanza haraka kwa sababu siwezi kumwambia chochote akanielewa, Abdul.”



“Tatizo lako sista hujiamini na unauruhusu woga ukutawale,” Abdul alisema. “We’ msubiri aje na akiendelea kumuulizia mwambie huyo mwanamke siyo mtoto, kwa hiyo umemwacha na jamaa fulani huko Mlimani City wanaongea. Kama anaona vipi, basi mwambie ampigie simu. Akimpigia hatampata. Na chezo nd’o litaishia hapo! Atabaki anambwelambwela tu.”



Kwa muda mfupi ukimya ulitawala, kisha Sharifa akaona kuwa hilo ni wazo zuri. Akashusha pumzi na kusema, “Poa. Nitafanya hivyo, lakini bado nahisi mambo hayajawa shwari kiviile.”



“Usihofu. Fanya hivyo kwanza. Hata hivyo na mimi nakuja huko kinamna. Nitajifanya nakuja kuwasalimia tu. Lakini nakuja huku nimejipanga.”



“Hapo sawa. Kodi teksi uje fasta. Ikiwezekana yeye akukute u’shafika.”



*****



KARIM alimgeukia Ablah na kusonya. Akashusha pumzi ndefu huku akiugongagonga usukani taratibu. Kisha, “Ablah, kuna kazi nzito hapa. Wazo langu ni kwamba wewe usiende kwanza nyumbani.”



“Kwa nini Karim?” Ablah aliuliza, hofu ikijidhihirisha katika sauti yake.



“Nataka niwaelewe hao washenzi,” Karim alijibu. “Kwa hiyo kwa kuwa tuko mbali kidogo itabidi twende kwa Dokta Suleyman ubaki pale kwa muda halafu mimi nitatangulia nyumbani. Usihofu, hakuna baya litakalonipata ila nitajua kiini cha wewe kutekwa na kipi kinachoendelea. Sawa?”



“Sawa.”



Kutoka hapo walipoegesha gari hakukuwa mbali na nyumbani kwa Daktari Suleyman, daktari mahususi wa marehemu tajiri Malick Sikonge. Karim alitwaa kwanza simu yake na kumpigia simu daktari huyo. Daktari alikuwapo nyumbani na aliipokea simu hiyo akiwa sebuleni akinywa kahawa.



Muda mfupi baadaye Karim alikuwa akiegesha gari nje ya geti la daktari huyo. Punde mlinzi akalifungua geti na kuwakaribisha. Karim na Ablah walitembea harakaharaka hadi ndani.



“Imekuwaje Karim?” daktari alimuuliza huku akibaini kuwa kuna saitafahamu iliyojitokeza kutokana na mwonekano wa Karim kuwa tofauti na siku zote.



“Dokta, baki na Ablah hapa kwa muda,” Karim alisema kwa sauti thabiti. “Si unaujua ubaradhuli wa yule mwanamke baradhuli?”



Kauli hii ilikuwa ya ajabu akilini mwa Daktari Suleyman. Papohapo akayakumbuka yale yaliyojiri siku ile mzee Malick alipofariki dunia. Akajua kuwa yale waliyoyahisi ndiyo yaliyoanza kujitokeza.



“Amefanya nini?” aliuliza huku akizima televisheni iliyokuwa ikitangaza habari za kituo fulani cha Amerika. Sasa akajiweka sawa kitini na kumkodolea macho Karim.



Zikamchukua dakika kadhaa Karim akimweleza lakini zaidi ni Ablah aliyezungumza kwa kirefu yaliyojiri kuanzia kule Mlimani City hadi Kunduchi kabla Karim hajafika kumwokoa.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Mwisho wa maelezo Daktari hakuonekana kusita. Papohapo akasema, “Binti, baki hapa. Yule ndiye Sharifa mke wa marehemu baba yako mzazi. Umeona alivyo na dhamira mbaya kwako? Unadhani ulitekwa bila yeye kujua? Ni nani anayekujua wewe hapa Dar? Wewe si umezaliwa Arusha na kukulia Arusha? Nani anakujua hapa Dar kiasi cha kufikia hatua ya kukuteka kama siyo mbinu chafu iliyofanyika?



“Baki hapa Ablah!” daktari alisema kwa jazba. Kisha, akionekana kuwa na hasira maradufu, akamrudia Karim. “Kwani Karim uko vipi? Unategemea mikono yako peke yake mbele ya suala zito kama hili? Unajiamini vipi? Nikupe kifaa?”



Hapo Daktari Suleyman alikuwa anamaanisha bastola. Ndani mwake alikuwa na bastola yenye risasi tano aliyoimiliki kihalali. Kwa hali ilivyo, aliona kuwa Karim hatakuwa salama sana; akataka aitumie silaha hiyo.







ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog