Search This Blog

Saturday, 5 November 2022

KARATA YA BARADHULI - 5

 







    Simulizi : Karata Ya Baradhuli

    Sehemu Ya Tano (5)





    Karim alimwelewa, lakini akampungia mkono akimwashiria kuachana na suala hilo. Papohapo akasimama, akaitwaa ile bastola ya marehemu Malick Sikonge mfukoni na kuirusha juu akidaka kwa mkono wa kushoto na kulia kwa madaha ya aina yake, akionesha kujiamini kwa kiasi kikubwa. Kisha: “Dokta, niko vizuri. Baki na Ablah hapa halafu nitakwambia kinachoendelea. Najua yule mwanamke anaweza kuwa na nia ovu kwangu ili tu lengo lake litimie. Ni hapo patakapochimbika pale nyumbani.”



    “Kwa hiyo nitaelewaje kinachoendelea?” daktari aliuliza akiwa na shaka. “Au nije huko kama nitaona dakika kumi zimekwisha?”



    “Nitakushtua kama mambo yataleta sura tofauti,” Karim alijibu huku akionesha kuanza kuondoka. Akavuta hatua mbili, tatu na kusita. Akageuka na kumtazama Ablah. Macho yao yalipokutana yaliongea mengi, lakini zaidi ilikuwa ni kama kila mmoja hakutaka kumwacha mwenzake kwa kipindi hicho.



    “Ablah,” Kamba aliita kwa sauti ya unyonge. “Niruhusu niondoke Ablah. Niombee kwa Mungu mambo yaende vizuri.”



    Macho yao yalikuwa kama vile yametengeneza kitu kingine tofauti, yakisihi na kubembeleza huku pia yakiwa kama yanayoshutumu na kulaumu.



    “Karim…” Ablah aliita kwa majonzi. “Karim unaniacha Karim…”



    “Binti,” daktari aliingilia kati akimtazama Ablah kwa jicho kali. “Tulia. Usihofu. Tuko pamoja. Ukiniona mimi ujue umemwona Karim. Huyu ni kijana wangu. Tuko pamoja siku nyingi kabla hata baba yako hajafariki. Tulia binti.”



    Ablah alimatazama Daktari Suleyman kwa muda mfupi kisha akayerejesha macho kwa Karim. Macho yao yakakutana tena. Karim akabaini kuwa Ablah hajaridhika na kuondoka kwake. Akamfuata na kumnyanyua, akamkumbatia. Kisha akamnong’oneza sikioni, “Tulia mpenzi. Niombee kwa Mungu. Nataka nimwonyeshe yule mbwa kuwa mimi ni nani na wewe ni nani.”



    Baada ya kusema hivyo alimbusu shavuni kisha akajing’atua na kutoka.



    Alipofika nje, Suleyman alimfuata na kumwambia, “Fanya chochote lakini tuwasiliane baada ya kama robo saa. Vinginevyo napiga simu polisi na ninakuja na ‘pistol’ yangu. Jihadhari sana. Umenielewa Karim?”



    Karim alimtazama Dr. Suleyman kwa namna ya kutoamini akisemacho. Kisha, akaitika kwa kutikisa kichwa. Papohapo akaingia garini na kuling’oa kwa makeke, akili yake ikiwa huko nyumbani.



    ABLAH alimatazama Daktari Suleyman kwa muda mfupi kisha akayerejesha kwa Karim. Macho yao yakakutana. Karim akabaini kuwa Ablah hajaridhika na kuondoka kwake. Akamfuata na kumnyanyua na kumkumbatia. Kisha akamnong’oneza sikioni, “Tulia mpenzi. Niombee kwa Mungu. Nataka nimwonyeshe yule mbwa kuwa mimi ni nani na wewe ni nani.”



    Baada ya kusema hivyo alimbusu shavuni kisha akajing’atua na kutoka.



    Alipofika nje, Suleyman alimfuata na kumwambia, “Fanya chochote lakini tuwasiliane baada ya kama robo saa. Vinginevyo napiga simu polisi na ninakuja na ‘pistol’ yangu. Umenielewa?”



    Karim alimtazama Dr. Suleyman kwa namna ya kutoamini akisemacho. Kisha, akaitika kwa kutikisa kichwa. Papohapo akaingia garini na kuling’oa kwa makeke, akili yake ikiwa huko alikoelekea.



    *****SASA ENDELEA*****



    MARA tu Abdul alipoongea na dada yake, Sharifa, akahisi kiwango cha ulevi kichwani kikikatika kila baada ya sekunde chache. Na papohapo akaiangalia chupa ya pombe kali iliyokuwa kwenye kistuli. Kulikuwa na kinywaji kisichofika hata nusu. Kwa hasira akaitwa na kukinywa kama anayefukuzwa.



    Chupa ilipofilisika, aliitupa chini na kulifunua godoro haraka. Kile kisu chake ambacho mwenyewe alizoea kukiita ‘Kisu cha Kigogo’ kwa kuwa alikinunua kwa mkazi mmoja wa Kondoa siku alipotembelea huko, kilikuwa kikihifadhiwa humo.



    Akakitoa ndani ya ala yake na kukiangalia huku akiwa ameuinua mkono kama anayetaka kuhakikisha kuwa ni kizima. Akawa ameweka kwenye uelekeo wa taa na kukizungusha huku na huku katika uchunguzi wake.



    Kisha akausogelea ukuta na kukiparaza kwa pande zote mbili kwa awamu. Mlio mkali ukasikika na kumwongezea kiburi.

    Hata hivyo, bado hakuwa na imani na makali yake hivyo, haraka akalisogelea godoro huku akijisemea, ‘kwani ni langu, si ni la gesti.’



    Akafanya majaribio ya kukata; kikatimiza wajibu wake kwa kupenya kwa usahihi ndani ya godoro. Akashusha pumzi za matumaini na ndipo alipojiwa na sura ya Karim fikrani mwake; akamtukania mama yake mzazi kwa sauti kama vile atukanwaye yuko humo chumbani. Akakirudisha kisu alani mwake na kuvaa viatu ambavyo alivivua akijua kuwa sasa yu huru na kilichobaki ni kunywa kisha kulala.



    Akajiangalia kidogo kwenye kioo na kujiona kuwa yuko kawaida. Akakipachika kisu hicho kwenye mfuko mwembamba lakini mrefu uliokuwa pembeni mwa suruali yake hii ya khaki nzito.



    Kisha akajitazama kwenye pochi kuna shilingi ngapi. Shilingi 70,000 zilikuwamo.



    “Zinatosha!” alisema kwa sauti ya mkoromo wa kilevi kisha akatoka, macho yake mekundu yakiashiria shari kamili.



    Kutoka kwenye gesti hiyo hadi eneo la Biafra siyo mbali. Hivyo alitembea haraka na alipotokea Biafra akachukua teksi. “Haraka sana Masaki,” alimwamuru dereva.



    Dakika iliyofuata teksi hiyo ilikuwa katika mwendo mkali ikielekea Masaki kwenye jumba la Malick Sikonge.



    ****



    DAKTARI Suleyman hakuwa na akili iliyolala. Mara tu Karim alipoondoka yeye alirudi ndani huku akiitafakari hii hali iliyoibuka katika wakati usiotarajiwa. Akawaza je, huyu Karim ana mpango wa kufanya nini katika kuwaumbua hawa Sharifa na kaka yake? Ni kwa nini hakutaka kumshirikisha kwa asilimia mia moja katika kulishughulikia suala hilo?



    Alitambua fika kuwa Karim alikuwa ni mtu wa mazoezi na kwamba mara kwa mara alikuwa akienda kufanya mazoezi na Mjapani wake huko Upanga. Lakini je, hayo mazoezi ya kareti na judo yanaweza kuwa nyenzo thabiti ya kukabiliana na kashkash nzito zinazoweza kuibuka muda wowote?



    Akilini mwake aliamini kuwa, ujana unaweza kuwa pia unamtia kiburi Karim na ndiyo maana hakutaka kumshirikisha sana katika kipindi hiki kinachoweza kutoa taswira tofauti kwa familia ya jengo hilo.



    Ndipo alijiwa na wazo aliloamua kulifanyia utekelezaji papohapo. Ndiyo, aliamua kulishirikisha Jeshi la Polisi kwa kuwa aliamini hii hatua iliyofikiwa siyo nzuri na wala haipaswi kuchukuliwa kama hatua inayoweza kupatiwa ufumbuzi kwa maana nyepesi.



    Huko nyumbani kwa Karim na Ablah, akilini mwa daktari alijenga hisia kuwa kunaweza kuwa kwenye msukosuko na hata labda yakatokea mauaji kama siyo madhara yatakayotoa matokeo ya baadhi ya watu kujeruhiwa. Ni hilo ambalo hakuwa tayari kulishuhudia likitokea.



    Ndipo alipoamua kumpigia Inspekta Massawe ambaye ni rafiki yake pia kwa namna nyingine. Akaingia chumbani ili hata akiongea na Massawe, kule sebuleni Ablah asisikie.



    Haraka akaitwaa simu na kubofyabofya kisha akaitega sikioni. Muda mfupi baadaye ikapokewa na Inspekta Massawe.



    “Yeah, dokta,” sauti ya Massawe ilitoka katika mazingira ya utulivu sana.



    “Massawe,”daktari alisema kwa utulivu. “Kuna tatizo kubwa. Nimeona kuwa ni vizuri nikupigie wewe ili nikupe mkasa kamili. Uko fresh nikusimulie? Na utakuwa tayari kunisaidia licha ya kuwa ni katika majukumu ya kazi yako?”



    Ukimya mfupi ukatawala, kisha Massawe akajibu, “Ungeniambia hilo tatizo lenyewe.”



    “Nyumbani kwa marehemu Malick kuna tatizo la kifamilia,” Suleyman aliipunguza zaidi sauti. “Binti yake ambaye ndiye aliyeachiwa urithi alitekwa leo na inasadikika kuwa mhusika mkuu ni mke wa marehemu. Hivi ninavyoongea na wewe ni kwamba kijana anayeishi hapo akiwa amelelewa na marehemu Malick na ambaye pia marehemu alimtaka awe bega kwa bega na bintiye na wawe kama familia moja, amekwenda huko nyumbani kukabiliana na mkewe marehemu.



    “Binti aliyetekwa, kijana huyo kamkomboa huko Kunduchi. Niko aye hapa kwangu lakini nahisi kunaweza kutokea machafuko huko kwenye jumba la marehemu.”



    “Sikia kwanza, dokta,” Inspekta Massawe alimkata kauli. “Una hakika kuwa huko nyumbani kunaweza kutokea vurugu? Kuna viashiria gani vya kukufanya uamini hivyo?”



    “Inspekta,” Suleyman alisema kwa utulivu. “Sina uhakika lakini kwa namna ninavyoona, huenda kukatokea shida. Tatizo afande ni kwamba yule mke wa marehemu alionekana kujali sana mali ya marehemu kuliko mapenzi. Amelipwa milioni hamsini ili aachane na familia hii lakini haondoki. Matokeo yake ndiyo haya, binti katekwa halafu huyu mwanamke kwa upumbavu wake eti anaulizwa wako wapi anajitia kudanganya kuwa bado wako Mlimani City. Yaani ni vigumu kunielewa vizuri, afande. Kama tungekutana ana kwa ana nadhani ungenielewa.”



    Ukimya tena. Kisha Inspekta Massawe akasema, “Ok, nakuja hapo kwako muda huu. Dakika kumi tu.”



    “Nakusubiri, afande.”



    Inspekta Massawe hakuwa anaishi mbali kutoka hapo kwa Daktari Suleyman hivyo alitumia dakika kumi tu kwa gari lake kufika kwa Suleyman. Moja kwa moja akapiga honi na geti lilipofunguliwa akaliingiza gari ndani.



    Dakika mbili baadaye alikuwa sebuleni kwa daktari Suleyman ambako alimwona Ablah akiwa ameketi sofani kwa unyonge. Katika sofa lingine Suleyman alikuwa kaketi, Massawe akakaribishwa katika sofa lingine.



    “Karibu sana, afande,” Suleyman alisema wakati Inspekta Massawe akijitupa sofani. “Umekuja katika muda mwafaka. Huyu ndiye binti yetu na ndiye mlengwa katika sakata hili. Nadhani ni vizuri akakuhadithia hata kwa kifupi yeye mwenyewe ili ujue ni kipi kinachopaswa kufanywa.”



    Ablah akamsimulia Massawe kwa kina na ndipo askari huyo alipoamini kuwa kuna jambo zaidi ya jambo. Papohapo akamrudia Suleyman. “Huyo kijana kaenda huko muda gani?”



    “Kwanza napenda ujue kuwa kijana huyo anaitwa Karim,” Suleyman alianza kuzungumza. Kisha akaendelea, “Kaenda kama robo saa iliyopita,” Suleyman alijibu.



    “Na hakuna mawasiliano yoyote tangu wakati huo. Yaani hujawasiliana naye?”



    “Bado. Ila nilimwambia kuwa zikipita dakika kumi naona kimya nitachukua hatua nyingine. Tatizo kijana yule anajiamini sana. Na sipendi aje kudhurika. Tufanye nini Inspekta?”



    “Mpigie! Ukiona kimya twende fasta! Binti aachwe hapa! Sawa?”



    Daktari hakujibu. Papohapao akaitwaa simu na kubonyeza vitufe akilisaka jina la Karim na muda mfupi baadaye akaiweka sikioni. Ngurumo kutoka upande wa pili ikayafikia masikio yake.



    *****



    KARIM alikanyaga breki nje ya geti la nyumbani dakika kama tano tu baada ya kutoka kwa Suleyman. Akapiga honi kali na mara mlinzi alipogundua kuwa ni Karim haraka akalifungua geti hilo. Karim akapenya kwa makeke yaleyale. Akaenda kuliegesha gari mbele ya mlango wa kuingilia ndani ya jumba badala ya kuegesha kule kwenye eneo lake la kawaida.



    Haraka akaufungua mlango na kutoka. Akakutana na mlinzi ambaye alionekana wazi kutokuwa katika utulivu. “Vipi,”



    “Poa tu kaka,” mlinzi alijibu kwa namna ya kutojiamini.



    Karim akamtazama kwa jicho kali kasha: “Kuna nani na nani ndani?”



    Kwa swali hili mlinzi alimwelewa. “Yupo mama.”



    “Peke yake?”



    “Kaka Abdul naye kaingia muda huu-huu. Hata dakika kumi nadhani hazijaisha.”



    “Mmmhh!” Karim aliguna huku akiupeleka mkono kwenye mfuko wa suruali wa kulia.







    TEKSI ilimwacha Abdul nje ya kasri la marehemu Malick. Akabonyeza kengele ya mlangoni na muda mfupi baadaye kijidirisha kidogo cha getini kikafunguliwa. Mlinzi akachungulia na alipomwona Abdul, akatabasamu kidogo huku akilifungua geti.

    “Karibu…karibu kaka Abdul,” alimkaribisha huku akiendelea kuachia tabasamu la mbali na kuonesha unyenyekevu mkubwa.



    “Poa,” Abdul alijibu kwa sauti ya chini bila ya kumtazama sana. Macho yake yalikuwa yakitalii ndani ya uwanja mpana wa eneo hilo na mara chache akimtazama mlinzi huyo. Kisha: “Kuna nani ndani?”



    “Yupo mama,” mlinzi alijibu huku naye akionekana kumshangaa kidogo Abdul kwa kuwa hakuwa katika ule mwonekano wake wa kawaida kama alivyokuwa siku zote katika kipindi alichokuwa akiishi hapo.



    “Peke yake?”



    “Ndiyo.”



    Kutambua kuwa Karim hajaingia ndani ya kasri hilo, ilikuwa ni faraja kubwa kwa Abdul. Haraka akazikwaa ngazi akielekea sebuleni ambako dada yake alimwambia kuwa ndiko aliko. Akamkuta kaketi sofani kihasarahasara; sasa akiwa amebadili vazi, katinga dera.



    Akajitupa katika sofa lililokuwa likitazamana na lile alilokaa dada yake. Akakaa kwa kujiamini huku akijua kuwa bado kuna kizungumkuti.



    Akatoa kibiriti na sigara, akataka kuwasha lakini akasita baada ya kukumbuka kuwa suala lilichomleta hapo ni nyeti na umakini unahitajika na hata ikibidi, uvumilivu pia unahitajika. Akabaki kaishika sigara na kibiriti bila ya kufanya chochote. Akamtazama dada yake kwa umakini na kubaini kuwa hayuko vizuri kisaikolojia.



    Sharifa alikuwa kakaa huku akitazama ukutani na uso wake ulionyesha dhahiri kuwa hayuko sawa.



    “Vipi sista, inakuwaje?” Abdul alimuuliza.



    Sharifa alimtazama kidogo kisha akayarejesha macho kule alikokuwa akiangalia. Mara tena akamrudia Abdul. “Bado hakijaeleweka. Tangu nimefika sijajua ni kipi kinachoendelea.”



    “Una maana bwege hajafika?”



    “Nd’o maana’ake,” Sharifa alijibu huku sasa akimtazama Abdul kwa umakini. “Na sijui atakuwa wapi.”



    “Us’konde,” Abdul alisema kwa majidai. “Sasa la kufanya ngoja niingie kule kwenye ‘rumu’ yako, akija nitamsikia. Na akishatinga hapa sebuleni mzubaishe kiaina mpaka mimi nizuke nifunge kazi. Umenisoma?”



    Sharifa aliguna. “Lakini bado kuna ugunu hapo,” alisema kwa namna ya shaka. “Nimekwambia sijiu yuko wapi. Itakuwa ni wendawazimu kukaa hapa na kujipanga kwa lolote huku hatujui kama bwehge mwenyewe atakuja. Tuko pamoja?”



    “Hapo sawa,” Abdul alikiri. “Kwa hiyo tufanyeje? Au umpandie tena hewani ili ujue yuko wapi.”



    “Point! Ni afadhali nifanye hivyo.”



    Muda mfupi baadaye Sharifa alikuwa akilisaka jina la Karim kwenye simu yake na zilimchukua sekunde chache tu, akalipata. Papohapo akapiga. Simu hiyo ilionesha kuwa inatumika. Akasubiri kidogo kisha akapiga tena, sasa ikaita hadi ikakata bila ya kupokewa.



    Sharifa akasonya. Kwa hasira akamrudia kaka yake. “Mshenzi hapokei. Naamini ishu hii kaishtukia. Tatizo sijui atakuwa kabana wapi. Sasa tufanye hivi,” kufikia hapo Sharifa aliishusha zaidi sauti yake.



    “Tufanye nini?” Abdul alimdaka.



    “Wewe nenda kajichimbie chumbani mwangu. Mimi nitaendelea kubana hapa. Kama atazuka muda wowote, nitakubipu. Na ukiona nimekubipu, ujue yuko hapa na kakaa, hivyo itakuwa ni rahisi kwako. Lakini ukiona sijakubipu ujue mazingira hayaruhusu.”



    “Na nikija, nakuja kumaliza kazi,” Abdul alisema.



    “Kwani ulitaka kuja kumbwelambwela hapa? We’ mwenyewe unaona mambo yanavyozidi kuchelewa. Yaani kikwazo hapa ni huyu mshenzi. Tukimzimisha yeye basi mchezo utakuwa kama vile kumsukuma mlevi aliyechuchumaa! Daaadek!”



    “Poa,” Abdul alikubali japo sauti yake ilionekana kutoridhika. Akavuta hatua kama tano hivi kisha akasita na kumgeukia tena dada yake. “Vipi, huna kitu cha kueleweka hapa?”



    Sharifa alimkazia macho ya kutoelewa alimaanisha nini. “Unasema?”



    “Huna kitu?” Abdul aliendelea kuzua utata kwa maswali yake.



    “Kitu gani? Au unataka kuendelea kulewa?”



    “Ni kupata stimu tu sista,” Abdul alijibu kwa kunyenyekea, sauti yake pia ikiwa ya chini kama ya Sharifa. Akaendelea, “Unajua sista, kazi iliyo mbele yangu inahitaji ukichaa f’lani hivi. Kumzimisha mtu na kuhakikisha kuwa kweli kazima, unahitaji ujasiri f’lani hivi. Nd’o maana nataka nipate kitu cha kuichangamsha akili kidogo na kuniondolea mi-u-wogawoga ya kitoto.”



    Sharifa alishusha pumzi ndefu kisha akasema, “Kacheki kwenye friza, nadhani bado hata ile mipombe mikali aliyokuwa akinywa yule babu kabla hajakata kamba itakuwemo. We’ kacheki tu.”



    “Poa,” Abdul alisema kwa matumaini na sasa alilifuata hilo jokofu, akalifungua na kukuta kuna chupa moja ya pombe kali ambayo haijafunguliwa. Akaitoa haraka na kuridhishwa na udogo wa chupa hiyo kwani hakutaka kunywa pombe nyingi, alitaka ajipange kwa kuikabli kazi iliyokuwa mbele yake.



    Akaelekea katika chumba alichoelekezwa. Bado alikuwa makini hivyo hata alipoifungua chupa hiyo ndogo, hakunywa kwa pupa kwa kuwa alijua kuwa hii ilikuwa ni siku muhimu kwake.



    Akawa tayari kwa utekelezaji wa azma yake!



    *****



    KABLA hajaanza kuufuata mlango mkubwa wa kuingia sebuleni, Karim alisikia mlio wa simu yake mfukoni kwa mbali. Haraka akaitoa na kuangalia. Akaliona jina la Dr. Suleyman likielea kwenye kioo. Akaipokea.



    “Yes, dokta,” alisema kwa utulivu na sauti yake ilikuwa ya chini sana.



    “Uko shwari? Umeshaingia ndani?”



    “Ndiyo kwanza nimeingia lakini sijafika ndani kabisa.”



    “Lakini huhitaji msaada wowote?”



    “Subiri dokta,” Karim alijibu. “Ngoja niingie ndani kwanza. Kama kutakuwa na lolote, nitakutumia meseji fasta.”



    “Ok, nakupa dakika kumi tu.”



    Karim alipokata simu mara akasikia ikiita tena. Sasa akagundua kuwa apigaye ni Sharifa. Akaitazama kidogo kisha akayapeleka macho mlangoni ambako kulikuwa ni kama hatua ishirini tu kutoka hapo alipo. Akasonya na kutoipokea simu hiyo.



    Ilipokatika, aliirejesha mfukoni na kuvuta hatua ndefu akilifuata lango la kuingilia sebuleni. Alipofika alikizungusha kitasa kikatii, akaingia taratibu na kurudisha mlango nyuma yake. Mbele yake alimwona Sharifa ndani ya dera lake akiwa amejipweteka sofani kihasarahasara, akicheza na vitufe vya simu.



    Mara tu Karim alipourudisha mlango, Sharifa aliinua uso na kumtazama kama asiyejali vile, kisha akaendelea kucheza na simu.



    “Vipi?” Karim alimwingia huku naye akiketi kwenye sofa lingine, akimtazama kwa makini.



    Sharifa aliunyanyua uso na kumtazama tena, safari hii akionekana kutokuwa na masihara. “Poa tu, nakupigia simu hupokei. Vipi?”



    “Hakukuwa na umuhimu. We’ unapiga kumbe niko hapo nje.”



    Ukimya mfupi ukapita, labda kila mmoja akiwaza lake. Karim naye akaitoa simu na kujitia kufinyafinya ilhali hakuwa akifanya chochote, zaidi alikuwa akiwaza aanze vipi kuzungmzia kuhusu Ablah. Kisha akaamua. Akajikohoza kidogo na kumuuliza, “Ablah yuko wapi?”



    Sharifa hakujibu haraka, akaendelea kuchati na simu kama kweli alikuwa anachati. Ilikuwa ni kama vile hajamsikia Karim, ingawa masikio yake yalilinasa kwa usahihi swali hilo.



    Karim alipandwa na jazba, uvumilivu ukamshinda. Akauliza tena, safari hii kwa ukali, “Nakuuliza, Ablah yuko wapi?”



    Sasa Sharifa aliuinua uso na kumtazama Karim kwa macho makali, macho ya kujiamini, akionesha bayana kutobabaika. “Kwani mimi niko naye mkobani mwangu?” lilikuwa ni jibu la Sharifa, na alitamka hivyo bila ya wasiwasi, kwa sauti ya juu, akiendelea kumtazama Karim sawia. Akaendelea, “Kwani unamwona yule mtoto mdogo? We’ vipi? Mwanamke mzima mi’ nikae namchunga! Kha! Yuko huko aliko anakojua mwenyewe!”



    “Kwa hiyo, kwa kifupi hukuja naye?” Karim aliendelea kumbana, safari hii akitumia sauti ya upole kidogo.



    “Bwana we, kamwangalie chumbani mwake! Kama hayupo basi usiniulize tena!”



    “Nini?” Karim alibwata kwa ukali zaidi.



    “Una maana hujanisikia au?” Sharifa alipaza sauti, labda akiwa na sababu maalumu ya kufanya hivyo.



    *****



    WAKATI Karim alipoingia humo sebuleni kule chumbani Abdul hakusikia, lakini alipolisikia lile swali la dada yake eti, “Kwani mimi niko naye mkobani mwangu?” akajua kumekucha. Akatega sikio vizuri. Ndipo akabaini kuwa Karim kishaingia. Akaitwaa ile chupa ya pombe kali na kupiga mafunda mawili mazito kisha akaiweka chini na kuifunga. Sasa hakuwa na mpango nayo tena. Alikuwa na mpango uliomleta.



    Akasimama na kujinyoosha kidogo kisha akafungua mlango na kutoka. Moja kwa moja akatokeza sebuleni huku kayatoa macho pima usoni pa Karim.



    “We’ msukule unabwabwaja nini hapa?” alimbwatukia huku akimsogelea taratibu, akitanua kifua kimkwara. “Una lolote linalokuhusu hapa? Wewe ni nani ndani ya nyumba hii? Huyo mwanamke anakuhusu nini? Nakuuliza wewe, huyo malaya anakuhusu nini wewe?”



    Karim alimtazama Abdul kwa mshangao. Hakutarajia kuwa hali inaweza kufikia hapo ilipofikia. Huyu Abdul wa leo sio yule wa siku zote kabla hajaondoka hapo. Alikuwa anaendekeza ulevi, ndiyo, lakini hakuwa na tabia ya ushari kama hivi leo. Aliendelea kushangaa kumwona Abdul akizidi kumsogelea. Na kabla hajajua ni kipi kitafuata, Abdul alirusha teke lililompata kidevuni, lakini halikuwa teke lenye uhai wa kuzua madhara makubwa.



    Karim akajua kuwa sasa kumekucha! Teke la pili aliliona, akalikinga kwa mkono wa kulia na papohapo akanyanyuka na kumrushia mateke mawili mazito kwa usahihi kwa mguu wa kushoto kasha, kulia. Yalikuwa ni mateke yenye uzito uliostahili, yakamrudisha nyuma Abdul na kutokana na nguvu ya pombe bado kuwa na kiwango fulani mwilini, alijikuta akiiangukia meza ndogo iliyokuwa nyuma yake.



    Kikawa ni kitendo kilichomfadhaisha yeye na hata dada yake kwa kiasi kikubwa.



    “Abdul vipi wewe! Maliza kazi! Unamchelewesha wa nini huyu fala?” Sharifa alifoka huku kasimama na kufumba na kufumbua alikuwa amenyanyua stuli, akamrushia Karim mgongoni kwa nguvu. Stuli hiyo haikupotea njia, ikampata Karim kwa usahihi. Maumivu makali yakampata, akajikunja kidogo na kumgeukia Sharifa.



    Sasa akajua kuwa kumbe kinachoendelea hapo kilishapangwa na wote hao. Akiwa amemgeukia Sharifa, ndipo Abdul alijua kuwa huyu siyo mwanadamu wa kawaida na hakutaka kumfanyia mchezo. Haraka akakichomoa kisu chake cha ‘kigogo,’ akajinyanyua haraka na kumvaa tena Karim.



    Karim naye alikuwa mwepesi, alikwishageuka na kukutana na Abdul na kisu chake. Akili ya kuichomoa bastola ikamjia papohapo, lakini alikuwa amechelewa sana. Wakati mkono ukiishika bastola mfukoni tayari kwa kuichomoa, Abdul alimvaa na kukielekeza kisu tumboni lakini Karim alimkwepa, ukwepaji ambao haukuwa msaada sana kwani bado kisu hicho kilipenya mbavuni na wakati akielekea kuanguka sakafuni, Abdul naye alipepesuka kutokana kutopata shabaha aliyoitarajia; akaelekea upande wa pili katika upepesukaji huo.



    Umbali mdogo uliokuwapo katika yao ulimpa mwanya Karim kuichomoa bastola huku akigugumia kwa maumivu na kumlenga Abdul. Risasi ikamtoka! Risasi hiyo ambayo haikuwa katika shabaha kamili ilikwenda kumpata Abdul katika bega la kulia!



    “Abdul!” Sharifa alipiga kelele. “Mungu wangu! Mungu wangu!”



    Abdul alilishika bega huku kakunja uso na kukiachia kisu sakafuni, akajitupa sofani huku akilalamika kwa maumivu.



    Pale sakafuni Karim alizidiwa na maumivu, damu ikamtoka kwa wingi, nguvu zikamwishia. Bastola iliyokuwa mkononi mwake ikaanguka sakafuni!





    ***** ***** *****

    TULIPOKOMEA TOLEO LILILOPITA...



    WAKATIi huo yule mlinzi naye alimnyanyua Abdul na kumsaidia kumpeleka nje. Baadhi ya wafanyakazi wengine wa kasri hilo walikuwa wamesogea katika eneo hilo na kushangaa walipomwona Abdul akitembea kwa shida huku shati lake likiwa limeloa damu na Sharifa akiongozwa kama aliye chini ya ulinzi japo hakuwa amevikwa pingu.



    Kwa hali yoyote ile kwa yeyote ambaye angewaona hapo, angejua kuna saitafahamu kati yao. Suleyman alitangulia garini na wengine wakamfuata. Kijana mmoja, kati ya watu waliokuwa hapo alikwenda kufungua geti gari likaondoka.



    ****SASA ENDELEA*****



    KILIKUWA ni kipindi kigumu sana kwa Ablah dakika kama kumi na tano hivi baada ya Dr. Suleyman na Inspekta Massawe kuondoka. Waliondoka bila ya kumwambia lolote. Na kwa hali ilivyokuwa hakuwa na uamuzi wa kufanya chochote. Alihitaji kuwa na uamuzi sahihi, unaoweza kutolewa kwa wakati sahihi kwa namna isiyoweza kuleta athari yoyote kwake.



    Alikumbuka maneno ya mwisho ambayo Dk.. Suleyman alimwambia Inspekta Massawe kabla hawajaondoka… ‘Nimepata simu ya mtu sijui ni nani lakini kasema kuwa kuna tatizo hapo kwa mzee Malick.’



    Haikuwa kauli ya kukisumbua kichwa cha Ablah ambaye saa kadhaa zilizopita alikuwa katika hali isiyoeleweka na hata mpaka muda huu bado hajajua kuwa yuko salama au la.



    Alijikuta akijilaumu kwa kukubaliana na Karim siku zile, kule Arusha kuwa aje kuonyeshwa na kisha kukabidhiwa nyaraka sahihi zinazothibitisha uhalali wake wa kumiliki mali iliyoachwa na baba yake mzazi, Malick Sikonge. Urithi gani huu wa roho mkononi?



    Hakuwa na amani tena na mali hii ya marehemu baba yake. Katekwa na kapata msukosuko mkubwa kisaikolojia japo kimwili hajadhurika kwa namna yoyote ile. Ni kwa nini hili litokee? Je, kama atakabidhiwa urithi huo iwe kwa amani au kwa shinikizo la kisheria kupitia vyombo vya dola, ataweza kuishi kwa amani kwa namna inavyostahili?



    Aliona kizungumkuti bado kimetawala. Akajiweka sawa sofani hapo na kujipapasa akiisaka simu yake. Ni hapo akili ilipomjia kuwa simu hiyo ilibaki katika himaya ya Kelvin. Akilini mwake alihitaji kuongea na mtu wake wa karibu, Karim. Lakini sasa haiwezekani kwa kuwa simu hana. Na labda huendea huko Karim aliko anampigia lakini hampati.



    Kilichomuuma zaidi ni kuwa huenda huyo Kelvin akapokea simu na kuongea naye kwa namna yoyote ile ya kifedhuli kwa makusudi tu ya kumkera Karim.



    Siyo ajabu kwa mtu kupokea simu na kumwambia Karim kuwa mtu anayemtafuta kwa kipindi hicho anatoa huduma ya ngono kwa kiwango cha juu na kwamba yuko tayari kutoa ushirikiano hata kwa watu watatu kwa mkupuo! Yatakuwa ni matamshi ya makusudi yaliyodhamiriwa kumuudhi mtumiwaji.



    Kitakachofuata ni hatua itakayochukuliwa bila ya kuzingatia hadhari au umakini. Yeye hakuwa tayari kufanya hivyo. Akaamua kuwa mpole. Akabaki amejilaza kihasarahasara hapo sofani akiwa hajui afanye nini.



    Dakika kumi zikapita, kumi na tano hadi nusu saa. Sasa akawa na wasiwasi zaidi, hasa kuhusu Karim. Kama kweli Karim kafanya jitihada zote zile hadi kumwokoa, itawezekana kuacha kushughulikia usalama wake kwa kina kutokana na hisia alizokuwa nazo kuhusu Sharifa?

    Akilini mwa Ablah aliona kuwa kuna hatari zaidi kwa Karim hasa kutokana na kauli hii aliyoisikia kutoka kwa Suleyman kwenda kwa Massawe.



    Akaangaza huku na kule sebuleni humo. Kulikuwa kimya kuliko kimya halisi. Akashangaa. Mara akakurupuka na kufungua mlango mkubwa, mlango ukamtii. Akausukuma na kutoka kwa hatua za kawaida japo aliona kila dakika inapotea kwa namna isiyopendeza. Kiza kinene kilitanda mbele yake. Akagwaya na kurudi ndani. Akaketi huku pia akishangaa kuona nyumba hiyo hakuna mtu mwingine. Kwa nini Dr. Suleyman yuko peke yake ilhali yu mtu mzima anayepaswa kuwa na familia? Ina maana huyu daktari ni kapera?



    Hata hivyo, mawazo hayo yakamtoka kwa kuona maisha ya mtu hayamhusu. Akili yake ilikuwa ni kujua hatima yake! Akaketi tena sofani na kubaki akiiokodolea macho runinga huku akiwa haoni kitu.



    Dakika arobaini na tano zilikuwa zimekwishakatika hadi muda huo. Akajikuta akilia kimyakimya, machozi yakawa yakimtoka na kuchuruzika mashavuni kwa uchungu. Wazo kuwa huenda Karim kadhuriwa likamjia na likamtisha. Zaidi, hakupenda kufikiria kuwa kauawa.



    Karim alikuwa ni kama mzazi wake wa pili, kaka yake na sasa alikuwa akimchukulia kama mwenza, mtu pekee atakayeubeba moyo wake. Ni Karim aliyekuwa kamwingia moyoni; alitarajia yeye ndiye amuoe. Hakuwa tayari kuolewa na mtu mwingine zaidi ya Karim!



    Sasa vipi inakuja taarifa kuwa kuna tatizo huko nyumbani? Karim kaua au kauawa? Kajeruhi au kajeruhiwa?



    Kutokuwa na taswira halisi ya huko nyumbani ndiko kulikomweka katika saitafahamu hiyo kiasi cha kumtoa machozi ya uchungu.



    *****



    ILILAZIMIKA Abdul kupewa PF 3 Polisi kisha akapelekwa hospitali na Inspekta Massawe akihakikisha Sharifa analala mahabusu huku akimwambia, “Mama yetu usijali. Ni katika hatua za utekelezaji ili kupata ufumbuzi wa mgogoro uliopo. Usihofu wala usijali. Asubuhi tutazungumza vizuri.”



    Abdul alipelekwa Hospitali ya Mwananyamala ambako alilazwa wodini huku akiwa chini ya ulinzi. Ndipo Massawe na Dr. Suleyman waliporudi nyumbani kwa Dr. Suleyman wakiwa wamechoka miili na akili lakini bado wakitambua kuwa majukumu yaliyo mbele yao ni makubwa.



    Walipofika walimkuta Ablah akiwa amenyong’onyea na sasa, akiwa kama aliyechanganyikiwa, akambana Dr. Suleyman, “N’ambie dokta, ni kipi kimetokea nyumbani?”



    Dr. Suleyman alimtazama kwa makini na kubaini kuwa ni kweli hayuko sawa. Akawa mpole na kumjibu: “Hakuna tatizo kubwa Ablah…”



    “Kuna nini?” Ablah alikuwa king’ang’anizi. “Mbona mliondoka mbiombio? Na kwani unadhani sikukusikia ukimpa ujumbe huyu mwenzio? Nilisikia kila kitu.”



    Inspekta Massawe na Dr. Suleyman walitazamana kidogo. Ni kama vile Massawe alikuwa akimwambia Suleyman ‘hajui kama mimi ni askari’ na pia ni kama vile Suleyman alikuwa akimwambia, ‘hajui kama wewe ni afande.’



    Dr. Suleyman alijikohoza kidogo na kujiweka sawa sofani kisha akasema, “Ablah, ni kweli kulikuwa na tatizo nd’o maana tukaondoka,” aliamua kupasua. “Kulitokea vurugu nyumbani na Karim amejeruhiwa…”



    “Nini dokta?!” Ablah alibwata kwa nguvu, macho kayatoa. “Karim kawaje?”



    “Tulia binti, usihofu,” Inspekta Massawe naye akaingilia. “Tunaendelea na jitihada ya kutatuta tatizo hili…”



    “Siwaelewi ujue!” Ablah alimkata kauli Massawe. “N’ambieni, Karim kaumia vipi? Kapigwa risasi? Na hali yake inaendeaje? Yuko wapi? Nyumbani au wapi?”

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Binti, taratibu,” Dr. Suleyman alisema kwa utulivu. “Ukweli ni kwamba Karim yuko hospitali, anapewa matibabu baada ya kujeruhiwa. Wewe usiwe na hofu. Kwa leo itabidi upumzike hapa.”



    “Na vipi kuhusu mama Sharifa?” Ablah alizidi kumbana.



    “Tumempuzisha kituo cha polisi,” Inspekta Massawe alijibu. “Kwa kuwa mambo hayajatulia, inabidi apumzike kule. Wewe usiwe na wasiwasi wowote…”



    Walijitahidi kumweleza kinagaubaga, akawaelewa. Huu ukawa ni usiku wa aina yake kwake, usiku mgumu kuliko siku zilizopita, japo hakupata tatizo lolote. Ndiyo ulikuwa ni usiku mgumu kwa kuwa alihitaji kujua hali ya Karim na chochote kinachoendelea kuhusu sakata hilo.



    Usingizi ulimpitia saa tisa na akajikuta kazinduka saa kumi kasorobo. Hakusinzia tena hadi kunakucha!



    ******



    SAA moja kasorobo asubuhi, wakati Dr. Suleyman akirudi chumbani mwake baada ya kutoka kuoga, alisikia mlio wa simu yake iliyokuwa kitandani ikiita. Haraka akaifuata na kuiangalia. Jina la Dr. Aboubakary lilielea kwenye skrini.

    Haraka Dr. Suleyman akaipokea na kutega sikioni. “Yes, dokta.”



    “Unaweza kuja mara moja?” Aboubakary alimuuliza.



    “Uko kazini?”



    “Yeah, niko wodini na mgonjwa wetu. Kiasi ana nafuu. Nadhani inafaa uje tuzungumze. Au huna chance?”



    “Dokta, hata kama ningekuwa busy kiasi gani, kwa suala la hawa vijana kila kitu nitasimamisha. Nipe dakika tano au kumi tu.”



    Simu ilipokatwa, Dr. Suleyman alikwenda kwenye chumba alicholala Ablah. Akagonga mara mbili kistaarabu. Ablah ambaye alikuwa macho, alikurupuka kufungua mlango na akakutana na Dr. Suleyman.



    “Binti, nafika hospitali kidogo,” alimwambia “Baada ya nusu saa nitakuwa hapa.”



    “Twende wote dokta!” Ablah alikurupuka na kuketi kitandani. “Twende wote nikamwone Karim dokta! Sikubali kubaki!”



    “Tulia binti,” Dr. Suleyman alimsihi. “Nitarudi na nitakwambia anaendeleaje.”



    “No!” Ablah aliwaka, macho kayatoa. “Sikuelewi dokta ujue! Kwa nini hutaki nikamwone Karim? Ni yeye ndiye alinifuata Arusha. Babu na bibi wanamfahamu yeye. Na aliwaahidi kuwa atakwenda kuwachukua na kuwaleta waishi na mimi huku. Hujui namchukulia Karim kama nani. Baada ya baba kufariki, namtegemea yeye kwa kila kitu kwa sasa. Kuniambia kuwa amejeruhiwa na kupelekwa hospitalini ambako amelazwa na bado hutaki nikamwone, unataka nikueleweje? Au unanidanganya? Au Karim si mzima?! Sema…sema dokta, Karim ni mzima au si mzima?”



    “Binti, Karim ni mzima,” Dr. Suleyman alijibu kwa upole huku akimtazama Ablah kwa makini zaidi. Sasa aliona kuwa itakuwa vigumu sana kumkatalia kwenda naye hospitali.



    Hata hivyo, bado aliuona ugumu wa kwenda naye kwa kuwa huu wito wa Dr. Aboubakary haukuwa wa kawaida. Huenda kuna taarifa tete na isiyopendeza huko hospitali. Kwa mbali akajisikia kuingiwa na woga fulani. Ndiyo, hakupenda kufika hospitali na kupata taarifa isiyopendeza.



    Kama atakwenda na Ablah huko hospitali huenda akajilaumu kwa kufanya hivyo na hasa kama atakuwa amechukua hatua hiyo bila ya kumshirikisha Aboubakary.



    Kwa ujasiri akasema, “Binti, tulia. Naomba unielewe. Naujua ukaribu ulionao na Karim. Lakini kwa sasa bado kuna mambo mengi yanayonihusu mimi na daktari mwenzangu huko hospitali. Na kwa kifupi, hata tukienda wote hautaweza kumwona kwa kuwa yuko kwenye chumba maalum…”



    Ablah alishtuka zaidi. “Una maana yuko mahututi dokta?” aliuliza huku machozi yakimlengalenga machoni.



    “Siyo mahututi lakini anahitaji mapumziko zaidi kama kwa saa ishirini na nne hivi.”



    Ablah alishusha pumzi ndefu na kuonekana kukata tamaa. Kisha kwa unyonge akasema, “Dokta nenda, lakini nakusubiri unipe taarifa anaendeleaje.”



    “Usihofu, binti. Baada ya nusu saa nitakuwa hapa,” Dr. Suleyman alisema huku akiondoka.







    MAUMIVU makali yaliendelea kumsumbua Kelvin usiku kucha. Yakaanza kupungua wakati wa mapambazuko. Hatimaye nafuu ikamjia kwa mbali japo mbavu za kulia bado zilimnyima raha.



    “Yule bwege amechanjia?” alijiuliza kwa mnong’ono. Alikuwa akikumbuka jinsi alivyokumbwa na vipigo kutoka kwa Karim.



    Muda huu akiwa amejilaza kitandani, alitwaa simu yake na kuiangalia saa. Ilikuwa imetimu saa moja asubuhi. Akajitutumua na kuamka. Akaketi kitandani hapo na kuhema kwa nguvu huku akijipapasa mbavuni. Kisha akanyanyuka na kuelekea msalani. Aliporudi hakufunga mlango, aliurudishia tu na kurudi kitandani kujilaza.



    Akajisikia kupumua kwa shida. Sasa mabadiliko yakazidi; hema yake ikawa ya shida. Akajawa na wasiwasi. Alikuwa na kumbukumbu ya mtu mmoja ambaye alipata madhara kwa kupigwa, hali yake ikawa ikibadilika taratibu lakini akajenga imani kuwa ni tatizo dogo. Akanywa tembe za Diclopar, maumivu yakapungua.



    Hata hivyo, saa sita baadaye maumivu yakazidi. Ndugu zake walipoamua, kumpeleka hospitali wakawa wamechelewa. Alifariki dunia akiwa mikononi mwa daktari na ikabainika kuwa alipata madhara kwenye bandama.



    Ni kumbukumbu hiyo iliyomfanaya hata yeye, asubuhi hii ajishtukie na kuamua kuchukua hatua. Haraka akatwaa simu yake na kulisaka jina la Jitu. Alipolipata akapiga. Wakati akisubiri kupokewa, akahisi mamuvu mbavuni yakizidi kuongezeka. Mara kifua nacho kikawa kikimbana na akawa akipumua kwa shida.



    Woga ukamjaa. Upande wa pili simu ilikuwa ikiita bila kupokewa. Akashangaa, mbona kumekucha? Kwani Jitu atakuwa bado amelala? Au anaoga? Simu ikakatika. Hakukuta tamaa, akapiga tena. Safari hii ikachukua muda mfupi tu, ikapokewa.



    “Haloo,” sauti ya kichovu ilipenya masikioni mwake. Akahisi kuwa Jitu bado kalala.



    “Jitu, bado umelala?”



    “Nilikuwa naoga. Vipi, unaendeleaje?”



    Kelvin alivuta pumzi na kuzishusha kwa nguvu. Maumivu yakazidi kumtesa. Akajitahidi kujibu, “Siko poa msh’kaji….hali mbaya…” akashindwa kuendelea.



    Upande wa pili Jitu alishtuka. Kwa namna alivyomjua Kelvin, hii haikuwa sauti ya kawaida kwake. Isitoshe, jana waliporudi, Kelvin alikuwa akiugulia maumivu. Na kutokana na taarifa zilizotolewa na watu walioshuhudia vurugu za kule Kunduchi, Kelvin alipata vipigo vikubwa sana hivyo inawezekana akawa amepata madhara makubwa kwa ndani.



    Kwa namna sauti hii ilivyomfikia sikioni, hakutaka kujidanganya kuwa Kelvin anaigiza kuwa ana hali mbaya. Hapana, huwa siyo kawaida yake kufanya masihara yanayohusu tatizo la afya.



    “Maumivu yamezidi?” aliuliza haraka.



    “Mbavu zinauma sana na ninashi…ni…ninashindwa kupumua vizuri…” Kelvin alijibu kwa shida.



    “Nakuja! Nakuja sasa hivi!” Jitu akasema na kukata simu. Akavaa harakaharaka na kutoka. Dakika tano baadaye alikuwa kishaiacha Kawe, akiwa makini nyuma ya usukani akielekea Kunduchi.



    Dakika ishirini baadaye alikuwa akipaki gari nje ya nyumba aliyoishi Kelvin. Haraka akatoka na kwenda mlangoni. Alipoufikia akakishika kitasa na kujaribu kufungua. Kitasa kikamtii, akausukuma mlango taratibu na kuingia sebuleni. Akaurudishia taratibu na kukifuata chumba cha malazi cha Kelvin.



    Jitu aliwaza haraka nini kifanyike. Kwa jinsi alivyomwona Kelvin, ilikuwa dhahiri kuwa yalihitajika matibabu ya haraka. Akataka kumuuliza ni wapi ilipo hospitali lakini akaona kuwa kitendo cha kuendelea kumsemesha kitakuwa kikimzidishia maumivu.



    Akatoka haraka akielekea nje ambako alimkuta muuza kahawa akipita kwa mwendo wa asteaste. Akamsimamisha na kumuuliza, “Hapa jirani kuna hospitali?”



    Muuzakahawa alitua birika chini na kumwangalia kwa makini Jitu. Kisha akajibu kwa kutojiamini, “Kuna hospitali mbali kidogo. Kule mbele ninakoelekea.”



    Jitu alimtazama kutoka juu hadi chini na kuyaona macho yake yakiwa ni kutokuwa na hakika ya kile alichokisema. Akatupa macho kushoto na kulia. Akawaona wanawake wawili waliojitanda kanga wakija. Walikuwa ni wanawake wa umri wa kati ya miaka thelathini na arobaini.



    Akajenga imani kuwa hao wanaweza kumpa jibu lenye ufumbuzi wa tatizo lililo mbele yake. Walipomkaribia akawasimamisha na kuwasalimia. Kisha: “Samahani kina dada, hivi kuna hospitali hapa jirani?”



    “Hospitali kubwa au ndogo, kaka?” mmojawao alimuuliza.



    “Kubwa, yenye huduma zote muhimu.”



    “Ipo huko mbele,” mwingine alimjibu.



    “Ni mbali sana?”



    “Kama robo saa kwa kutembea,” mwanamke wa kwanza alimjibu.



    Jitu akakuna kichwa. Kama kwa kutembea itamlazimu kutumia robo saa, ni mbali. Na alipoizingatia hali aliyokuwa nayo Kelvin huko ndani, akajua kuwa haiwezekani kutumia miguu.



    Akawatazama kinamama hao na kuwasihi, “Naombeni msaada wenu…nina ndugu yangu huko ndani anaumwa sana. Hawezi kutembea, na mimi hapa ni mgeni lakini nina usafiri huo hapo,” akawaonesha gari lake lililokuwa upande wa pili wa barabara.



    Akatulia akiwatazama akitaka kuthibitisha kama wanamwelewa. Kisha akaendelea, “Ninawaomba mnisaidie, twende pamoja hadi eneo hilo nikamwache tu mgonjwa wangu halafu nitawapeleka mnakokwenda. Tafadhalini sana kina dada.”



    “Mgonjwa mwenyewe yuko wapi?”



    Jitu akapata tumaini jipya. “Yuko ndani,” alijibu. “Ngoja nikamfuate fasta.”



    Akakimbilia ndani na kumkuta Kelvin akiendelea kupumua kwa shida na zaidi, sasa mate mazito yalikuwa yakimtoka mdomoni. Hali hiyo ikazidi kumtia hofu Jitu. Akamnyanyua na kukita mikono makwapani mwake. “Kelvin jikaze nikupeleke hospitali…jitahidi msh’kaji wamgu,” alimwambia akiwa ametaharuki. Akajitutumua kumsimamisha, Kelvin naye akajitahidi kujikokota huku macho yamemtoka, akiwa na taswira ya mtu akionaye kifo kikimchungulia.



    Akatembea kwa kujiburuta akiwa ameshikwa na Jitu. Walipofika nje, Jitu alimwingiza kwenye kiti cha mbele na kuwaambia wale wanawake wakae nyuma. Kelvin alikaa huku kajikunja, akiendelea kupumua kwa shida. Kwa mara ya kwanza Jitu akajiona yu katika kipindi kigumu zaidi maishani mwake.



    Hii hali aliyonayo Kelvin ilimfanya Jitu ahofie matokeo yoyote mengine yasiyotarajiwa. Huku mapigo ya moyo yakimwenda mbio alitia moto gari na kuliondoa taratibu. Mara sauti kutoka kwa mmoja wa wale wanawake ikamfikia. “Kaka pita barabara hiyo hapo kushoto na ukifika mbele utaona jumba kubwa la ghorofa moja. Kata kulia, mbele kidogo utaona majengo makubwa matatu na geti jeusi. Hapo ndipo kwenye hospitali yenyewe.”



    Jitu alifuata maelekezo hayo. Dakika kama tano hivi baadaye akaegesha gari nje ya hospitali hiyo.



    “Piga honi,” mmoja wa wale wanawake alimwambia. Akaongeza, “Walinzi wa hapa hawafungui mpaka wasikie honi.”



    Jitu akafuata maelekezo hayo. Mara geti likafunguliwa. Mzee aliyevalia sare za kampuni moja ya ulinzi akatokea. Akaja garini upande wa dereva na kumuuliza, “Una mgonjwa anayepaswa kuingizwa na gari?”



    Lilikuwa ni swali lililomkera Jitu lakini kwa kuwa wakati huo alikwshayavulia maji nguo, hakuwa na budi kuwa mpole. Akashusha pumzi ndefu na kujibu, “Nina mgonjwa ambaye hali yake ni mbaya.”



    “Yuko wapi?”



    Jitu akashusha zaidi kioo na kumwambia, “Mwangalie. Ni huyu,” alimgeukia Kelvin kidogo kisha akamrudia yule mlinzi.



    Kama Jitu alivyotarajia, yule mlinzi aliinama na kuchungulia ndani ya gari na baada ya kumwona Kelvin, haraka akasema, “Subiri.”



    Papohapo akarudi getini na kufungua geti kubwa kama kichaa. Jitu hakuhitaji kutoa shukrani wala kutamka chochote kingine. Akakanyaga moto na kutinga ndani ya eneo la hospitali hiyo. Alielekezwa eneo la kuegesha gari na alipokwishaegesha, akamwomba mlinzi huyo msaada wa kumteremsha Kelvin.



    “Siruhusiwi kufanya hivyo,” mlinzi alimjibu. “Subiri nikawaite wahudumu.”



    Akatoka hima akiingia ndani. Dakika chache baadaye wahudumu wawili wa kiume wakaja na machela. Wakambeba Kelvin na kumlaza kwenye machela hiyo kisha wakaisukumua wakiingia ndani.



    Jitu aliwageukia wanawake wale na kuwaambia, “Nawashukuru sana dada zangu. Mungu awabariki sana.” Baada ya kusema hivyo, akachomoa noti moja ya shilingi 5,000 na kumpa mmojawao. Hakuipokea.



    “Hapana kaka,” alisema huyo aliyekataa kuipokea noti hiyo. “Tumekusaidia tu kukuonyesha hapa. Siyo kwamba tunahitaji malipo. Uko kwenye kipindi kigumu kwa sasa, kaka. Mshughulikie mgonjwa wako. Pesa ya nini tena kwetu?”



    Tabasamu changa likamtoka Jitu huku akiirudisha mfukoni noti ile. Kisha akasema, “Ok, dada zangu, basi ngoja nimshughulikie mtu wangu kwa madokta huko ndani. Asanteni sana.”



    Akaondoka kwa hatua ndefu akiwafuata wale wahudumu waliokuwa mbali kidogo kwenye k.orido wakielekea chumba cha daktari. Akawawahi na kuingia nao kwa daktari.



    Kelvin hakuionyesha dalili yoyote ya kutambua kinachoendelea. Alikuwa akikoroma kwa mbali.



    Daktari alifungua jalada na kumkaribisha Jitu kiti kilichokuwa kando ya meza.



    “Mgonjwa anaitwa nani?” alimuuliza.



    Jitu hakuwa tayari kutaja jina halisi. Katika mazingira ya kazi zao na kutokana na hii hali aliyonayo Kelvin, aliamini kuwa tahadhari ilipaswa kuzingatiwa. Hivyo aliamua kubuni jina la kumwambia huyu daktari.



    “Masumbuko Malingumu.”



    “Makazi yake?...Umri…” na maswali mengine kwa jinsi taaluma yake ilivyomruhusu. Jitu akayajibu yote kwa namna ambayo na yeye aliona kuwa ndivyo inavyofaa. Hata daktari alipomuuliza jinale, pia uongo ukaendelea kutawala. Danford Kalikumtima ndilo jina alilotamkiwa daktari huyo.



    Kisha daktari alianza kumfanyia vipimo Kelvin. Jitu ambaye hakuwa timamu kisaikolojia, alibaki kasimama huku akizichezesha funguo za gari taratibu, macho kayakodoa akimwangalia daktari kama vile anajua kinachoendelea au anataka kumsaidia.



    Daktari alimgeukia, akamwonesha kiti kilichokuwa jirani na mlango na kumwambia, “ Keti pale upumzike. Itanichukua muda kidogo.”



    Kwa shingo upande, Jitu alilazimika kutii agizo hilo. Akaketi na kushusha pumzi ndefu. Akainama hna kujishika kichwa huku akijisemea kimoyomoyo, ‘Huyu Karim…huyu Karim nikimpata…’ Alikuwa na hasira kwa kuiona hali ya Kelvin ambayo ilitokana na kipigo alichopata kutoka kwa Karim.



    Dakika kama kumi hivi baadaye, Jitu akiwa katika hali hiyo ya saitafahamu, mara akazinduliwa na wito wa daktari. Alipounyanyua uso akakuta kumbe daktari alikwisharudi kitini, akiandikaandika katika lile jalada la mgonjwa.



    “Naam dokta,” Jitu alikurupuika kujibu.



    Daktari akaacha kuandika, akaipeleka kalamu mdomoni na kuiuma kidogo huku akimwangalia Jitu kwa macho yaliyozungumza, zaidi ya kile alichodhamiria kukizungumza.



    “Mista Danford,” aliita tena, safari hii kwa sauti ya chini zaidi na kusita.



    *****



    DR. Suleyman aliingia ndani ya gari lake na kulitia moto huku akiwaza ni kwa nini Dr. Aboubakary amemtaka aende huko hospitali mapema hivyo? Je, kuna utata katika hali ya Karim? Kuna…kuna…alijikuta akijiuliza maswali yaliyakosa majibu na kwa kiasi fulani alijikuta akikosa amani moyoni.



    Muda mfupi baadaye aliegesha gari kwenye hospitali hiyo na kutoka hima. Alipofika mapokezi akamwambia binti aliyemkuta hapo, “Ninahitaji kuonana na Dr. Aboubakary.”







    Binti yule alimtazama kwa muda mfupi kisha akamuuliza, “Una apointimenti naye?”



    “Amenipigia simu asubuhi hii,” lilikuwa jibu la Dk. Suleyman.



    “Nadhani yuko ICU. Mpigie umwambie kuwa umefika na uko mapokezi.”



    Dk. Suleyman alikerwa na utaratibu huu ambao yeye aliona kama ni wa kuzidi kumchelewawesha kukutana na Dk. Aboubakary. Hata hivyo kwa kuwa alijua kuwa huyu binti hamfahamu, akaamua kuwa mtulivu na kutii matakwa yake. Papohapo akaitwaa simu yake na kumpigia Dk, Aboubakary.



    “Niko reception.”



    “Mpe simu huyo binti.”



    Dk. Suleyman akampa simu huyo binti wa mapokezi. “Sikia Cathy, mwelekeze huyo dokta huku ICU,” agizo lilimfikia binti huyo sawia, naye akamrudishia simu Dk. Suleyman huku akijitoa kitini na kutangulia huku akimwashiria amfuate.



    Walipofika kwenye mlango wa chumba kilichokuwa kimefungwa, binti huyo aliufungua na kutangulia kuingia na alipomwona Dk. Aboubakary, akampisha Dk. Suleyman aingie kisha yeye akaondoka.



    Macho ya Dk. Suleyman yalikwenda moja kwa moja kwenye kitanda alicholazwa Karim. Alikuwa akipumua taratibu, macho kayafumba huku chupa ya damu ikiwa imetundikwa kando ya kitanda chake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Alipoteza damu nyingi,” Dk. Aboubakary alisema. “Lakini hali inaendelea vizuri. Ila atalazimika kupumzika kwa siku mbili tatu kwa kuwa ameshonwa nyuzi nane.”



    Dk. Suleyman alitikisa kichwa akiashiria kuafikiana na maneno ya daktari huyu mwenzake. Kisha akasema, “Hakikisha unasimamia matibabu yake dokta. Na nina imani na hapa kwako kiulinzi, ndiyo maana sikutaka kumpeleka katika hospitali nyingine yoyote. Ameweza kuzungumza chochote?”



    “Bado. Na sipendi kuibughudhi akili yake. Nimemchoma sindano apumzike kwa kama saa sita hivi.”



    “Good,” Dk. Suleyman alisema huku akitikisa kichwa kuafiki. “Sasa ngoja nirudi nyumbani. Au kuna ziada?”



    “Hapana. Nilitaka uje tu kumwona na kukupa taarifa hii.”



    Ukimya ukapita kisha Dk. Suleyman akasema, “Bado mambo si shwari dokta. Kwa hiyo hakikisha taarifa kuwa kalazwa hapa kwako zisivuje.”



    “Nimekuelewa. Hakuna kitakachovuja.”



    Dk. Suleyman alirejea nyumbani huku akiwaza atamwambia nini Ablah ambaye anaonekana dhahiri kutaka ama kumwona Karim kwa jicho lake au kupata taarifa sahihi na za kina kuhusu hali yake.



    Alikumbuka alivyomwona asubuhi hii na kugundua kuwa hata siha yake imeshatetereka. Si ajabu kutokea hali hiyo. Misukosuko iliyompata Ablah tangu jana alasiri kule Mlimani City ilitosha kumvuruga mwili na akili. Huruma ikamwingia daktari huyu huku hasira dhidi ya Sharifa na Abdul ikizidi kujikita katika mtima wake.



    Alipofika nyumbani alikuwa ameamua kuketi na Ablah na kumweleza kuhusu hali ya Karim na pia kumweleza mipango mingine aliyoifikiria kulingana na hali ilivyokuwa katika familia hiyo.



    Alimkuta Ablah akaketi sebuleni, kinyonge, macho mekundu hali iliyoashiria kuwa huenda alikuwa akilia muda uliopita.



    “Binti pole kwa upweke,” alimwambia huku akiketi katika sofa lingine. “Hali ya Karim inaendelea vizuri ila ana dozi ya usingizi, hivyo nilimwacha apumzike hadi baadaye. Usihofu. Huenda baadaye atatoka na kurudi nyumani.”



    Dk. Suleyman alisema hayo akitambua fika kuwa ni uongo lakini ili amwondolee hofu maradufu Ablah ndiyo maana aliyatamka. Akamwangalia usoni kwa makini. Macho yao yakakutana, akaugundua udadisi zaidi katika macho ya Ablah na akiwa kama anayemuuliza, ‘unadhani naweza kuukubali huo uongo wako?’



    Dk. Suleyman akaendelea, “Jambo lingine nililolifikiria ni kwamba, kwa uhakika wa usalama wako, kwa sasa endelea kukaa hapa mpaka tujue mwisho wa wale mabaradhuli. Sharifa yuko polisi na Abdul yuko hospitali lakini akiwa chini ya ulinzi.



    “Wao ndio wabaya wako, na hatuwezi kujua wana mtandao mkubwa kiasi gani. Wafanyakazi wengine wa pale kwenu, huwezi kujua, labda kuna ambao wameshajumuishwa katika mpango wao. Kwa hali hiyo nimefikiria uendelee kuwa hapa kwa muda. Jisikie huru, usihofu ingawa nyumba haina watu. Niko peke yangu. Mke wangu yuko Lusaka kikazi katika ofisi ya ubalozi wa Tanzania. Nina watoto watatu, wawili ni wa rika lako. Nao wako huko na mama yao; mtoto kwa mama…!”



    Akameza funda zito la mate na kutulia akiendelea kumtazama Ablah katika kujiridhisha kama anayosema yamemwingia na anakubaliana nayo?



    Ablah alishusha pumzi ndefu na kulirazama dari kisha akmrudia Dk. Suleyman lakini safari hii akiepuka kumtazama usoni sawia. Hatimaye kwa sauti dhaifu akasema, “Nimekuelewa dokta. Lakini naomba uifuatilie hali ya Karim. Sina raha bila kumwona na kujiridhisha. Ikiwezekana jioni nipeleke nikamwone kama atakuwa hajawa na hali nzuri ya kumwezesha kutoka.”



    Maneno hayo yakamtia faraja daktari. Akaamini kuwa sasa Ablah amemwelewa. Haraka akajibu, “Usijali. Nitawasiliana na daktari wake kila baada ya muda mfupi anipe maendeleo. Kwa sasa ninatoka. Nakwenda kituo cha polisi kushughulikia suala la Sharifa. Halafu nitakwenda hospitali aliyolazwa Abdul.



    “Ukiingia kule jikoni kuna kila kitu, jitayarishie upate break fast. Usijiumize kwa njaa na mawazo. Kila kitu kitakuwa sawa baada ya muda mfupi. Kama utaona kuna upungufu wa chochote, hapo nje kuna duka kubwa la Mchaga, mwambie akupe chochote au akiwa na shaka anipigie.



    “Unielewe binti, usishinde njaa. Nitarudi baada ya saa moja hivi au saa mbili. Na ni vizuri tukiwa na mawasiliano.” Papohapo daktari akaingia chumbani ambako alitoka na simu nyingine, akamkabidhi Ablah huku akisema, “Hiyo ni laini yangu. Chukua namba yangu kwa simu hii.” Akapiga namba fulani, simu aliyoishika Ablah ikaita na herufi za DK zikatawala kwenye skrini.



    “Ok, unaweza kunipigia kama kutakuwa na tatizo. Kuna vocha ya wiki nzima.”



    Baada ya kusema hivyo, Dk. Suleyman aliondoka.



    *****



    KILA kitu kilikuwa kama ndoto kwa Sharifa. Hakuwahi kujiwa na wazo kuwa mpango wake na kaka yake unaweza kutibuka. Sasa yuko mahabusu kituo cha polisi. Tangu jana usiku yuko humu. Haya ni maisha ambayo haikuwahi kumwingia akilini kuwa yanaweza kumkuta.



    Hata hivyo, bado hakutaka kuamini kuwa ndio mwisho wa kila kitu. Lazima maisha yaendelee na lazima aitumie akili yake bila ya kukata tamaa. Hakujua kaka yake, Abdul ana hali gani muda huo lakini alitaka kuhakikisha anapata ufumbuzi wa kujiokoa yeye ndipo mengine yatafuata.



    Alikuwa ndani ya chumba ambacho hakikuwa kama vyumba vingine vya mahabusu ambavyo havikosi kuwa na kasoro nyingi mathalani uchafu na kunguni.



    Hiki, japo kilikuwa chumba kidogo lakini kilikuwa na sakafu safi. Alipoingizwa jana hapa kituoni, alipokewa na askari wa kiume na kutokana na maelezo yaliyomfanya askari huyo atambue kuwa huyu ni mke wa marehemu Malick, ikawa ni sababu iliyomfanya askari asimpeleke kwenye kile chumba cha mahabusu. Badala yake, akaingizwa katika chumba hiki.



    Akakumbuka jinsi askari aliyempokea usiku alivyokuwa akimwangalia kwa macho yenye zaidi ya utazamaji wa kawaida. Na hata alipomleta huku chumbani, alishindwa kuonyesha uvumilivu, akampapasa matiti huku akimwambia, “Kifaa kizuri kama wewe haustahili kukaa kule kwenye kunguni…pumzika huku mrembo…”



    Ni asubuhi hii ndipo wazo lilipomjia Sharifa kuhusu yule askari. Akaomba aje tena kama atakuwa hajaondoka. Na ni kama ombi lake lilikubaliwa na Mungu. Dakika chache tu baadaye mlango ukafunguliwa. Alikuwa ni Sajini Michael ambaye ndiye aliyemleta humo chumbani.



    “Vipi mama? Hujalala?” alimuuliza baada ya kumwona ameketi huku mikono kaikunyata katikati ya miguu, macho makavu!



    “Niupate wapi usingizi kaka?” Sharifa aliserma kwa unyonge huku akimtazama usoni sawia.



    Askari huyo aliitazama saa yake na kubaini kuwa ilikuwa ni saa moja kasoro dakika ishirini. Akayarejesha macho kwa Sharifa na kumwambia, “Nyanyuka uje huku kaunta.”



    Sharifa alinyanyuka na alipomwona askari huyo akigeuka kuelekea mlangoni akamwahi, “Samahani afande. Subiri kidogo tafadhali.”



    Askari aligeuka na kumtazama Sharifa huku kakunja uso. “Vipi tena mrembo?”



    Sharifa alimsogelea na kumgusa bega. “Nahitaji msaada wako, afande. Uko tayari kunisikiliza?”



    Askari huyo alishusha pumzi ndefu, akaurudisha mlango taratibu. “Unasemaje ma’mdogo?”



    Sharifa akamsogelea zaidi. Akapachika mkono wa pili katika bega la pili.



    “Afande, wewe ni mwanaume,” alianza kusema. “Uwe mjanja. Niachie niondoke. Uko tayari?”



    “Sikuelewi ujue!” askari huyo alisema kwa mshangao.



    “Hunielewi vipi wewe? Unanifahamu mimi ni nani. Kwangu unapafahamu. We’ nipe namba ya simu, nikifika nyumbani nakurushia kitu.”



    Askari huyo aliguna. Akawa amezama mawazoni, akijua kuwa ushawishi huu anaopewa na huyu mke wa marehemu Malick ni mgumu kiutekelezaji na hasa kwa kuwa hajui hicho atakachorushiwa kitakuwa na uzito kiasi gani.



    Maisha yake katika ajira yalikuwa duni. Alihitaji pesa, na huyu anayeongea naye ni mke wa aliyekuwa tajiri sana nchini hivyo ni wazi pesa anazo tena si haba! Akimwachia hapa yeye atapata nini?



    “Changamka afande!” Sharifa alisema huku sasa akikosa adabu kwa kumpapasa shingoni na kumsogeza karibu, miili yao ikagusana!









    SAJINI Michael akapatwa na msisimko taratibu. Hali hiyo ikawa ikimzidia kila sekunde zilivyozidi kusonga mbele. Naye akajikuta amejisahau, akamvuta zaidi Sharifa na kumkumbatia, mikono yake ikitalii mgongoni mwa Sharifa kwa namna iashiriayo hitaji zaidi la starehe.



    Naye Sharifa akiyagundua mabadiliko fulani katika maungo ya askari huyo, hakutaka kuicheza vibaya karata yake hiyo ya kipekee. Akausogeza uso wake na kuugandisha mdomo kwenye papi za mdomo wa Sajini Michael. Ulimi wake wa moto ukajitokeza na kupiga hodi kinywani mwa Michael.



    Hakukuwa na kipingamizi; Sajini Michael alikuwa katika sayari nyingine, uaskari wake ukawekwa pembeni, akazidi kuchanganyikiwa pale alipouhisi mkono wa Sharifa ukitalii eneo la chini ya kitovu chake, utalii wa kitaalamu na usisimuao.



    Ndiyo, hiki kiganja cha Sharifa kilitomasa na kutofya kwa mfumo uliompagawisha kwa kiasi kikubwa. Akahema kwa nguvu na kukiachia kinywa, ulimi wa moto wa Sharifa ukapenya kwa madaha na mbwembwe za aina yake. Na kwa kudhamiria Sharifa akausukuma mlango kwa mguu nyuma yake.



    Mlango ukajifunga taratibu. Wakabaki peke yao. Uhuru ukawatawala. Umbo kubwa la Sharifa likawa kichocheo halisi cha kumwongezea mhemko Sajini Michael. Msisimko zaidi ukampata askari huyo pale mikono yake ilipoteleza taratibu kutoka mgongoni kwa Sharifa na kutua pale kwenye milima miwili iliyonona na laini. Mikono hiyo ikakosa staha zaidi kwa kuminyaminya eneo hilo taratibu. Kwa namna walivyokuwa, kila mmoja alizisikia pumzi za mwenzake akihema kwa namna ya kuzidiwa na hanjamu, hawaa na mashamshamu katika mishipa ya damu.



    Lakini, ni kweli wote walikuwa wakisisimkwa kutokana na hayo waliyokuwa wakiyatenda? Hapana. Wakati Sajini Michael akijihisi yu katika sayari nyingine, sayari yenye kila starehe ambayo mwanadamu huihitaji, Sharifa alikuwa mbali kifikra. Hakuwa bwege; akili yake ilikuwa na uwezo zaidi ya akili ya mtu wa kawaida, anayefikiri kwa kiwango cha kawaida.



    Alitambua fika kuwa kumepambazuka na wakati wowote suala lake linaweza kuchukua uzito mkubwa na labda akapelekwa kwa askari wa ngazi za juu, jambo ambalo hakutaka limkute. Alitaka kumwepuka Inspekta Massawe, ambaye ndiye aliyekuja nyumbani jana na kumchukua hadi hapa. Alimwona inspekta huyo kama nuksi zaidi ya nuksi alizozijua.



    Hivyo alihitaji kujali muda huu alionao, autumie vizuri ili asije kuujutia. Wakati Sajini Michael akionekana kunogewa na hii hali waliyokuwa nayo, Sharifa akajing’atua taratibu na kumtazama usoni sajini.



    Kisha kwa namna ileile ya uchokozi usisimuao, akaupeleka mkono pale alipopakusudia, akapapasa, akaminya kidogo kisha kwa mnong’ono akasema, “Mmmh…uko vizuri afande. Lakini tunahitaji muda tuonyeshane umwamba. Na nitakupa zawadi utakayoipenda. Sasa niambie…niondoke? Kunazidi kupambazuka afande! Niachie nisepe!”



    Sajini Michael alishusha pumzi kwa nguvu, akiyatafakari haya maneno ya Sharifa. Mhemko ulikuwa ukimsumbua. Uzuri wa sura, umbo na vimbwanga vya Sharifa vilimchanganya sana askari huyu. Lakini akubaliane na ombi hili? Akimwachia aondoke, atajieleza vipi kwa Inspekta Massawe?



    “Mwanaume changamka!” Sharifa alisema huku akimkazia macho. “Muda…muda afande…Kuna milioni tano zako za haraka…”



    Milioni tano! Sajini Michael aliwaza haraka. Papohapo akajumlisha moja na moja na kupata mbili, kwamba tangu aajiriwe hapo Jeshi la Polisi, hajawahi kushika milioni moja nje ya mshahara wake ambao hakupenda hata kuufikiria kwa kuwa aliona kuwa ni kama shombo tupu.



    Sasa anatamkiwa shilingi milioni tano! Kwa kazi ndogo sana ya kumruhusu tu huyu mwanamke aondoke! Milioni tano zikawa zinamjia machoni kama njozi vile. Akajiona kama yuko ndani ya hoteli kubwa akipata vinywaji huku akipapaswa na warembo wawili wa nguvu, tabia aliyokuwa akiipenda ila tu pesa za matumizi hayo zilimpiga chenga.

    Liwalo na liwe, alijisemea kimoyomoyo.



    “Ziko wapi?” alimuuliza Sharifa huku akimtazama kwa macho ya uchu, vitone vya jasho vikiwa vimejiunda kwenye paji lake.



    “Akili yako ndiyo itakufanya uzipate. Nipe namba zako, nikifika home nakurushia.”



    Hapo Sajini Michael hakukubaliana naye. Kuaminiana kwa kipindi hicho lilikuwa ni suala gumu. Eti ampe namba na kumwachia kwa matarajio ya kutumiwa pesa muda mfupi ujao. Milioni tano kimchezomchezo tu!



    Machale yalimcheza askari huyo. Akaamua kupasua, “Itakuwa ngumu Sharifa. “Ukiondoka, mimi nikabaki, na muda mfupi ujao akaja afande Massawe, nitamwambia nini? Ni yeye aliyekuleta, na ndiye atakuwa na jukumu kuhusu wewe. Umenisoma?”



    “Afande,” Sharifa aliita kwa sauti ya mshangao, akimtazama Sajini Michael kwa macho makali. “Unapokea mshahara unaokutosheleza mahitaji yako yote? Mbona unaonekana kuwa unapenda kufia kwenye hii ajira isiyo na kichwa wala miguu maishani? Yaani unadhani unaweza kupata rushwa ya zaidi ya shilingi elfu hamsini kutoka kwa mtuhumiwa? Labda wakubwa zako. Mimi nimekwambia nakupa milioni tano bado unambwelambwela. Chukua hatua kianaume afande!



    “Sawa,” hapo akaipoza sauti na kuachia tabasamu la mbali na la mwonekano wa dhihaka. Akaendelea, “Tuliache dili hili. Namsubiri afande aliyenikamata aje. Nikizungumza naye, tukaelewana, unadhani wewe utaambulia nini? Fikiri vizuri afande. Utaendelea kuringia ajira yako ya uaskari na hivyo vilivyositiriwa ndani ya suruali yako. Kazi unayo!”



    Ilikuwa ni risala iliyopenya moyoni mwa Sajini Michael kama radi. Ikamuuma. Ndipo alipojitathmini kuhusu maisha yake ya sasa na yajayo.



    Ni kapera bado. Ni yeye na chumba chake kila arudipo nyumbani. Zaidi ya kitanda kikubwa, televisheni bapa, kabati mbili ndogo za kisasa na masofa mawili, hakukuwa na kitu kingine katika chumba hicho alichopanga Msasani.



    Hakuwa utaratibu wa kupika. Njaa ilipomsakama, alikwenda mgahawani au kwenye vibanda vya chipsi. Pia, mara mbili au tatu kwa wiki, Catherine alikuja usiku wakastarehe na kuagana asubuhi. Huyo ndiye aliyekuwa mpenzi wake wa kike, ambaye hawakuwahi kukubaliana kuwa ipo siku watafunga ndoa.



    Kwa hali hiyo, haya maneno ya Sharifa yalimfanya awaze kuchukua hatua, kuchukua uamuzi mgumu! Aondoke na Sharifa! Aliamini kuwa kama ataishia kumpa namba Sharifa hapa, hatatofautiana na mtu aliyetupa shilingi chooni. Hakutakuwa na mawasiliano yoyote, milioni tano zitabaki kuwa simulizi tu akilini mwake. Zaidi, kitakachofuata ni kukumbana na kipindi kigumu zaidi pale Inspekta Massawe atakapokuja; atamwambia kuwa Sharifa yuko wapi?



    Ndipo alipomkazia macho Sharifa na kumwambia, “Tunaondoka wote. Na usije kuniletea akili za wehu huko mbele ya safari! Twende unipe changu, tuachane. Sema! Tena tuondoke muda huu maana’ake kama afande Massawe atafika muda huu utapelekwa Oysterbay.”



    Kuondoka wote, lilikuwa ni suala ambalo Sharifa hakulitarajia kutamkwa na Michael. Na hata hivyo, nyumbani hakuwa hizo fedha taslimu shilingi milioni tano. Kwenye simu yake kulikuwa na shilingi laki mbili tu. Pamoja na hayo, kutokuwa na fedha kwenye mtandao wa simu halikuwa tatizo kwani kama angetaka angeongeza salio kwa kuhamisha kiasi cha fedha anachotaka kutoka katika akiba yake iliyoko benki.



    Akitambua fika kuwa yuko katika kipindi kigumu tangu akamatwe jana, Sharifa alitambua kuwa anapaswa kulazimisha hata lile lisilowezekana ili tu ajiokoe. Aliamini kuwa karata yake iko vibaya hivyo ni kudra tu za Mwenyezi Mungu ndizo zitakazomwokoa.



    Ili asiendelee kupoteza muda ndani ya kituo hicho kidogo cha Polisi, Sharifa alimwambia Michael, “Ok, twende…”

    Baada ya kusema hivyo alianza kufungua mlango na kutangulia kutoka.



    “Subiri,” Michael alimzuia, akamrudisha ndani na yeye ndiye akatoka. Akamfungia Sharifa kwa nje. Hakuna kuaminiana; mtuhumiwa ni mtuhumiwa tu hadi kitakapoeleweka!



    Dakika kama moja hivi baadaye akarudi na kumwambia Sharifa, “Toka…tangulia, niko nyuma yako.”



    Sharifa akatoka taratibu, akielekea nyumbani. Sekunde kadhaa baadaye, Sajini Michael ambaye alikuwa akihakikisha Sharifa hampotei machoni, naye akatoka akikiacha kituo hicho kidogo cha polisi kikiwa tupu.



    Wakati akiondoka, hakujiwa na fikra za kugeukia kwenye barabara ya vumbi iliyokuwa kushoto ambako Inspekta Massawe alikuwa akitokea akija hapo kituoni.



    *****



    DK. Suleyman aliingia ndani ya gari lake na kuling’oa akielekea kituo kidogo cha Polisi huku akijihisi uchovu kutokana na pilikapilika za tangu jana. Njiani akapiga simu akimtafuta Inspekta Massawe. Simu ikaita kwa muda mfupi tu na kupokewa.



    “N’ambie dokta,” Massawe alikuwa hewani.



    “Niko njiani nakuja kituoni,” Dk. Suleyman alisema.



    “Ok, hata mimi niko njiani,” Inspekta Massawe alisema. “Tutakutana hapo baada ya dakika kumi hivi. Nadhani huyo mwanamke atakuwa amepata akili. Tukizungumza naye tutapata picha kamili. Na baada ya hapo ndipo tutaamua kama tumpeleke Oysterbay au vipi. Kisha nitakwenda Mwananyamala kumcheki Abdul. Sawa?”



    “Sawa kabisa, Massawe. Tutaongea vizuri tukifika.”





    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ************************************************************************

    ***************************************************

    *******************************

    *******************

    ****************

    *********

    ******



    TULIPOKOMEA TOLEO LILILOPITA



    “Wametoroka!” Massawe alidakia. “Au mtuhumiwa kaachiwa na askari huyu aliyekuwa zamu. Unadhani ni tafsiri gani nyingine tunayoweza kupata hapa? Sasa wewe kaa hapa kituoni. Usitoke! Na huyo Michael akija usimwambie chochote. Jifanye kama hujui kuwa jana tulimleta mtu hapa. Umenielewa?”



    “Ndiyo, afande.”



    Papohapo Massawe akarudi kwa Dk. Suleyman na kumwambia, “Twende dokta. Tutumie gari langu kwa kuwa najua halijulikani sana kwenu.”



    Wakati huo tayari alishafungua mlango wa gari na kuingia. Dk. Suleyman naye akaingia haraka. Inspekta Massawe akatia moto na kuliondoa gari kwa kasi ya aina yake wakielekea kwenye kasri la Malick Sikonge!



    *****SASA ENDELEA*****



    ZILIWACHUKUA dakika chache sana kufika mbele ya geti la kasri la marehemu Malick. Papohapo Inspekta Massawe akapiga honi kwa nguvu kisha akateremka. Dk. Suleyman naye aliteremka harakaharaka na kukimbilia getini na alipolifikia akaligonga kwa nguvu mara mbili.



    Mara kidirisha kidogo kikafunguliwa. Mlinzi akachungulia. Alipomwona Dk. Suleyman hakusita kufungua geti haraka huku akishanngaa ni kipi kilichosababisha hii saitafahamu iliyozuka. Massawe na Suleyman waliliacha gari nje wakaingia ndani kwa kishindo na papohapo Dk. Suleyman akamuuliza mlinzi, “Mama yupo?”



    Mlinzi akatokwa macho pima. Sasa hakutaka kujidanganya kuwa kuna tatizo au hakuna. Hii tazama ya Dk, Suleyman, sanjari na macho ya kutisha ya Inspekta Massawe vilitosha kutoa taswira kuwa kuna jambo zaidi ya jambo.



    “Hayupo…” alijibu kwa wasiwasi.



    “Hajarudi?”

    “Aliku…alikuja lakini hakukaa…”



    Muda gani umepita?”



    “Ni kama dakika kumi hivi zimepita….kwa kweli siyo muda mrefu dokta.”



    Dk. Suleyman alisonya na kumgeukia Inspekta Massawe kama atazamiaye msaada kutoka kwake. Massawe aligundua kuwa mwenzake kachanganyikiwa; haraka akadakia, “Ulimwona yuko katika hali ya kawaida?”



    “Hapana,” mlinzi alijibu haraka. “Alikuwa kama kapaniki-paniki hivi, na ile kuingia tu akaniuliza eti kuna nani ndani. Nikamwambia kuwa kuna kina Zai wanafanya usafi. Akaniacha, akakimbia kuingia ndani. Akachukua muda kidogo kisha akatoka huku kabadili nguo. Akanipa maagizo kuhusu Ablah, eti akija amsubiri…kuna sehemu anataka amsindikize. Halafu eti Karim akija nimwambie kuwa kaenda Namanga mara moja.”



    Inspekta Massawe na Dk. Suleyman wakaguna kwa hasira huku wakitazamana. Kisha, papohapo Dk. Suleyman akauliza, “Kaondoka kivipi? Alikuwa na mizigo? Katumia gari?’



    “Mbona katumia ile gari ya siku zote!” mlinzi alijibu kwa kujiamini.



    “Ipi…Benz nyeusi?” Dk. Suleyman alitokwa macho pima.



    “Ndiyo!”



    Alikuwa na mizigo?”



    “Alitoka ndani akiwa na begi kubwa jeusi, na ni kama lilikuwa likimzidia uzito.”



    “Kasepa!” Inspekta Massawe alisema kwa sauti ya chini akimtazama Dk. Suleyman kwa namna ya kukata tamaa.



    “Itakuwa hivyo,” Dk. Suleyman alikiri. Akajishika kiuno, naye akionekana kukata tamaa. Lakini mara akazinduka na kumgeukia yule mlinzi. “Hakikisha hautoki hapa getini,” alimwambia.



    Akaendelea, “Na akija mtu yeyote usiyemjua na akawa anamhitaji mama, tumia akili kumkalisha kisha utupigie simu fasta. Umenielewa?”



    “Nimekuelewa dokta,” mlinzi alijibu.



    “Hata kama Abdul atakuja, tumia kila mbinu uhakikishe haondoki mpaka tufike. Utaweza kumzuia kwa mbinu ambayo hataishtukia?”



    Mlinzi alionekana kuwa na hali ya kutojiamini, hali ambayo hata Massawe na Suleyman waliiona machoni pake. Hata hivyo hawakusubiri jibu, Dk. Suleyman akamwahi, “Tunatoka. Fuata maelekezo yangu. Ukitibua na sisi tutakutibua!”



    “Nitajitahidi dokta. Msiwe na wasiwasi. Naomba mniamini.”



    Dk. Suleyman na Inspekta Massawe hawakuyasikia maneno hayo ya mlinzi, tayari walishakuwa nje, kando ya gari, wakiwa wameliegemea boneti.



    “Tumegeuzwa mafala, dokta,” Inspekta Massawe alisema huku akimtazama Dk. Suleyman kwa uso uliokata tamaa.



    “Dah, yaani sijui vipi!” Dk. Suleyman naye alitokwa na sauti. “Kinachonitisha ni kuwa kaondoka na gari. Na kaondoka na begi. Unadhani atakuwa anakwenda hapa karibu. Ameshajua kuwa kaharibu, unadhani ataichezea nafasi hii aliyopata? Na kingine kinachonivuruga kichwa Massawe, ni kwamba, hata lile benzi sijawahi kulishika namba…”



    “Acha hizo dokta!” Inspekta Massawe alimdaka. “Huyu mtu wa getini hawezi kushindwa kujua namba za magari yenu. Ngoja nimuulize.”



    Papohapo Inspekta Massawe akamrudia mlinzi, naye Dk. Suleyman akimfuata hima.



    “Bwa’ mdogo nipe namba za hilo gari aliloondoka nalo mama,” Inspekta alimwamuru mlinzi.



    Mlinzi alinyanyuka haraka na kuchukua leja iliyokuwa ndani ya saraka ya meza. Akaifunua na kuangalia ukurasa wa magari yanayotoka na kuingia humo ndani ya kasri. Mara akauacha ukurasa huo na kufungua ukurasa mwingine; huo ulikuwa na majina ya magari yaliyomilikiwa na marehemu Malick Sikonge.



    Orodha ilikuwa ndefu kidogo lakini mlinzi alikuwa akilitafuta lile Mercedes Benz C-350 aliloondoka nalo Sharifa Abdulrahman. Alipolipata akamtajia huyo askari nambari hizo. Haraka askari akachukua kalamu na karatasi toka mfukoni mwa shati lake, akazinakili nambari hizo kisha akamnyooshea dole gumba mlinzi huyo, akionesha kuridhika kwa alichokipata.



    Wakatoka na sasa Inspekta Massawe akamwambia Suleyman, “Unajua dokta, labda huyu mwanamke awe mchawi. Lakini naamini sasa tunaye.”



    “Tunaye kivipi Massawe?”



    “Narusha taarifa kwanza Oysterbay, natengeneza uongo kuwa ni mtuhumiwa mwenye silaha na ameiba pesa nyingi nyumbani kwa tajiri Malick. Sitataja kuwa ni mkewe Malick kwa kuwa wanaweza kumtia mbaroni lakini wakamgeuza mradi; wakamtoa pesa na kumwachia atokomee.



    “Kwa hiyo mimi namtengenezea zengwe ili usawa wa Tegeta, Bunju, usawa wa Kimara kwenda Kibaha hata njia za Kisarawe nao wawe tayari. Ninachotaka ni kumtia mbaroni tu. Na ninajua baada ya hapo, watakachofanya ni kunisubiri mimi. Hapo ndipo tutakapokuwa tumebeti utamu.”



    Dk. Suleyman ambaye bado alionekana kuishiwa matumaini, aliitika kwa kutikisa kichwa tu bila ya kutamka chochote. Dakika iliyofuata, Inspekta Massawe alikuwa akizungumza na Mkuu wa Kituo cha Oysterbay kwa kina. Ushirikiano aliopewa katika mazungumzo hayo ukazidi kumjaza matumaini askari huyo.



    Alipokata simu alimrudia Dk. Suleyman. “Dokta, sasa tuendeleea na ratiba zetu. OCS wa Oysterbay kaniahidi kunipa taarifa baada ya nusu saa. Kwa sasa anauweka mtandao vizuri na trafiki wa kona zote kwa kushirikiana na RTO. Kwa hiyo, kwa sasa sirudi kituo kidogo. Najua labda yule askari alipewa mkwanja na huyo mwanamke. Hata hivyo, sina hakika na hilo kwa kuwa sidhani kama yule mwanamke alikuwa na pesa wakati tumempleka kituoni na hata kama alikuwa na pesa alikuwa kazificha wapi? Kwenye sidiria? Au kwenye nguo ya ndani?



    “Kwa mwanamke wa aina yake, aliyekuwa ananukia utajiri, akiishi maisha ya raha, atakuwa na muda wa kuficha pesa kwenye maeneo hayo? Kwani alijua kuwa tutampeleka kituoni? Hapo ndipo nakuwa na shaka, ilikuwaje askari yule akamwachia. Naamini kuwa hata kama mama huyo alikuwa na pesa basi siyo za kumbadili mwanamume mwenye akili na anayejali ajira kiasi cha kuhatarisha hiyo ajira yake. Labda alikuwa na shilingi zisizozidi laki mbili mfukoni. Hata kama angekuwa na milioni moja, askari mzima unaweza kumwachia mtuhumiwa kwa pesa ndogo kama shilingi milioni moja au mbili hivi?”



    “Usishangae Massawe,” Dk. Suleyman alisema. “Kuna wengi wanaoweza kuchukua pesa ndogo tu kulingana na njaa yao. Kwani hata trafiki wa hapa mjini wanachukua shilingi ngapi kwa daladadala moja? Sema tu unaweza kukuta kwa siku trafiki anasanya kwenye magari mengi pesa kidogodogo na matokeo yake anajikuta ana mkwanja wa nguvu.”



    ‘Hilo nalijua,” Inspekta Massawe alisema. “Tatizo la trafiki nalijua sana. Lakini huyo askari aliyekuwa zamu nd’o kanishangaza. Au inawezekana huyu mwanamke alipokuja, walikuja wote lakini akamwacha sehemu ili siri isifichuke na alipoondoka wakakutana mahali, akamkeshi mkwanja wake na yeye akasepa.”



    Dk. Suleyman aliitika kwa kutikisa kichwa.



    Kisha Inspekta Massawe akasema, “Sasa twende Mwananyamala kumwona huyo bedui, Abdul. Tukitoka pale, tupitie kwa Karim halafu wewe urudi nyumbani kumcheki yule binti na mimi niende kituoni Oysterbay kuendelea kufuatilia hatua kwa hatua kuhusu huyu mwanamke. Tusikubali atuzidi ujanja. Itakuwa aibu sana.”



    Wakaingia garini na safari ya kuelekea Hospitali ya Mwananyamala ikaanza.



    **********



    ASKARI aliyetumwa na Abdul soda na keki, alipoondoka tu, Abdul akawaza haraka ni kipi afanye. Kwake, hii aliiona kuwa ni karata muhimu aliyopaswa kuicheza kwa makini japo ana jeraha la risasi linalomtia maumivu makali. Aliamini kuwa kama huyu askari atarejea na kumkuta hapo basi hakutakuwa na uwezekano mwingine wa kufanikisha azma yake.



    Akaliangalia jeraha lake na kuiangalia dripu. Zaidi ya maumivu ya jeraha, hakujiona kuwa ana tatizo lingine. Hivyo, akainyofoa dripu mkononi taratibu huku akiangaza macho kwa wagonjwa wengine. Huyu wa kulia alikuwa katopea usingizini. Wa kushoto alikuwa akigugumia kwa chinichini, akionekana kuzidiwa na maumivu.



    Abdul akashusha pumzi kwa nguvu na kuangaza kwenye mlango mkubwa ambako watu waliingia, watu walitoka. Taratibu, akajitoa kitandani huku akikunja uso kutokana na maumivu ya jeraha. Akaikita miguu sakafuni. Akavuta viatu na kuupachika mguu wa kushoto, mkono usiojeruhiwa ukawa ukimsaidia kuvika. Alipohitimisha, mguu wa kulia ukafuata.



    Hatimaye akawa amevaa viatu vyote. Akasimama taratibu na kuanza kutoka. Maumivu ya jeraha yakazidi kumtesa lakini akajikaza, wanaita ‘kujikaza kiume.’ Akatembea huku kaukunja uso. Akapishana na watu wengine, wagonjwa kwa wazima waliokuwa wakiingia wodini humo kwani ulikuwa ni muda wa kuwaangalia wagonjwa.



    Huku moyo ukimdunda, Abdul alikuwa akiomba kimoyomoyo askari yule asiwahi kurejea. Akatembea kwa umakini, macho yakiwa mbele, yakimtazama kila aliyekuwa akija, hisia kuwa huenda pia askari wengine wakaja hapo zikawa zikimjia kichwani. Hatimaye akajikuta kwenye eneo aliloweza kuliona geti la kuingilia hospitalini hapo.



    Machale yakamcheza. Mbele yake, kwa mbali alimwona yule askari aliyemtuma soda akija. Akawaza, askari huyo atamwelewaje pale atakapomkuta yuko huku nje ilhali kamwacha kitandani akiwa na dripu ya maji? Akiwa ni mtuhumiwa aliye chini ya ulinzi, askari anaweza kuelewa chochote ambacho ataambiwa?



    Akili ya Abdul ikafanya kazi haraka. Akajitahidi kujisogeza eneo lililokuwa na watu takriban kumi wakiwa wameketi wakiongea. Idadi hiyo ya watu ilimridhisha sana Abdul kwa kuamini kuwa kama atajichanganya na watu hao, yule askari hatabaini chochote na kitakachofuata ni kumwacha aende wodini ambako atakutana na taswira tofauti.



    Akiwa katika kundi la watu hao ambao ni dhahiri walikuwa wakiwasubiri wenzao waliokuwa wodini, alimwona askari yule akiwapita kwa kasi huku akiwa amebeba mfuko mweusi wa plastiki ambao akilini mwa Abdul aliamini kuwa kulikuwa na soda na keki.





    MARA tu askari yule alipokuwa umbali wa takriban hatua ishirini kutoka hapo, na akionekana kuwa na haraka ya aendako, Abdul aliwahi kulitoka kundi hilo. Kwa mwendo wa kulazimisha, kiupandeupande, akiteswa na maumivu ya lile jeraha, alitembea akielekea getini.



    Moyoni alikuwa wasiwasi kwa kuwa eneo hilo lilikuwa wazi na alikuwa na hofu kuwa, kama yule askari atashtuka na kurudi hima huku nje, asingepata shida kumnasa. Akawa akiomba Mungu balaa lisimkute!



    Akaendelea kujikokota kwa hatua ndefu za kulazimisha. Hatimaye akafika getini. Mlinzi mmoja akamtazama kwa huruma kisha: “Pole sana kaka. Vipi, umeruhusiwa?”



    “Bado. Lakini sina ndugu wa kunisaidia. Nafika hapo dukani kuchukua soda.”



    “I see, pole sana,” mlinzi huyo wa kike alisema kwa upole, macho yake yakizidi kumtazama kwa huruma zaidi.



    “Asante sana,” Abdul alijibu huku akizidi kuvuta hatua kiupandeupande akielekea barabarani. Akilini mwake alipanga kuchukua teksi ambayo atakwenda kuachana nayo eneo la Sinza. Huko, atakodi bajaji na kuingia nayo mitaa ya ndani zaidi hukohuko Sinza ambako atajichimbia huku akitibiwa kwenye hospitali yoyote ndogo.



    Alijiaminisha kuwa jeraha lake siyo baya sana liwezalo kuhatarisha maisha yake. Kama mfupa haukudhurika, ya nini kulitilia shaka? Mbele yake akaiona teksi upande wa pili, ikimshusha mteja. Papohapo, huku akihema kwa nguvu na mapigo ya moyo kuongeza kasi, akapuliza mluzi mkali. Dereva yule akamsikia na kumtazama. Matumaini yakazidi kumjaa Abdul. Akampungia dereva huyo mkono amsubiri. Dereva akaitika kwa kutikisa kichwa.



    “Yes!” Abdul alijikuta akiropoka kwa furaha huku akivuta hatua zaidi kuifuata teksi hiyo.



    Kulikuwa na magari mengi yaliyopita muda huo. Na kati ya hayo, daladala zilikuwa nyingi zaidi. Wakati Abdul alipoanza kuvuka barabara, furaha ya kufanikiwa kupata usafiri wa kumtoa katika eneo hilo ikimtawala kichwani, hakukumbuka kuangalia kulia na kushoto mwa barabara hiyo kabla ya kuvuka. Akili yake ilikuwa ni kuiwahi teksi!



    Basi kubwa lililotoka Makumbusho likienda Mbagala lilikuwa katika mwendo wa wastani. Dereva alipomwona Abdul akivuka barabara, akapiga honi kubwa! Honi kama ya treni! Abdul akazinduka na kuliona basi hilo ambalo lilikuwa hatua kama ishirini hivi. Akajizindua na kujirusha kwa nguvu bila kujali ataangukia wapi!



    Alikuwa amechelewa! Basi lilimkumba mzimamzima, likamrusha juu na aliporudi chini tairi la mbele kushoto lilimpanda kifuani! Hadi basi hilo liliposimama, tairi la nyuma nalo lilikuwa limepanda palepale kifuani!



    Haukuhitajika uthibitisho wa daktari kuwa kilichobaki pale ni mwili wa marehemu Abdul uliopondekapondeka.



    *****



    KWA namna daktari alivyoita, sauti yake ikiwa tofauti na awali, Jitu alishtuka na kuwa makini. Hakuitika, badala yake aliuinua uso na kumkazia macho daktari.



    “Mr. Danford,” kwa mara nyingine daktari aliita lakini akiwa kama asiyetarajiwa kuitikiwa. Macho yake yakaganda usoni pa Jitu na yakizungumza zaidi ya kutazama!



    Ulikuwa ni utazamaji usio wa kawaida, na ukamweka Jitu katika saitafahamu isiyopendeza. “Ndiyo, dokta,” hatimaye aliipata sauti yake.



    Daktari alishusha pumzi na kusema, “Mgonjwa wetu hali yake siyo njema. Itanichukua muda sana kukupa maelezo ya athari kubwa alizopata. Lakini kwa kifupi tu inaonekana amedhurika kwa ndani eneo la kichwani, kifuani na mbavuni. Hali yake inahitaji vipimo zaidi, ikibidi, CT-Scan. Hapa kwangu hatuna vipimo vikubwa. Nakushauri tu kama utaweza wahi Regency au Muhimbili…”



    “Dokta,” Jitu alimkatisha. “Mbona unanitisha? Yaani huna uwezo wa kumtibu hapa? Na unajua tuko mbali sana huku! Kutoka hapa mpaka huko unakosema unadhani itachukua muda gani? Please dokta, jitahidi!”



    Jitu alikuwa na sababu ya kuwa king’ang’anizi kwa daktari huyo. Kumbeba tena Kelvin na kumpeleka katika hospitali yoyote kati ya hizo zilizopendekezwa na daktari, ilikuwa ni kama kucheza patapotea. Hii hali aliyonayo Kelvin ni ya kuhangaika kwa umbli wote huo? Na, je, huko Regency ataimudu gharama kama hiyo ya CT-Scan kama kweli watataka kutoa huduma hiyo?



    Pamoja na hayo, hapa kwenye hospitali hii huyu daktari kakubali kufanya vipimo vya awali. Lakini akilini mwa Jitu hakutaka kujidanganya kuwa hiki alichokifanya daktari huyu ni utaratibu wa kawaida. Hapana. Taswira halisi imeonesha kuwa Kelvin kapata majeraha makubwa sana kwa ndani na inaonesha dhahiri kuwa ni kutokana na shambulizi la mwili.



    Kwa vyovyote vile, kitu cha kwanza ambacho Jitu angedaiwa ni fomu ya matibabu ya Jeshi la Polisi (PF 3) kabla ya matibabu. Akilini mwa Jitu alimwona daktari huyo kama msamaria mwema kwa kuwa amempa taswura halisi ya hali ya mgonjwa. Hivyo aliamua kuondoka na mengine atayajua mbele ya safari.



    Akamwomba daktari huyo awaambie wale wahudumu waliomsaidia kumleta Kelvin waje kutoa msaada tena. Muda mfupi ujao, vijana watatu wakaingia na kumweka Kelvin kwenye machela kisha wakaikokota taratibu hadi kando ya gari la Jitu.



    Huku akiwa amechanganyikiwa kwa kiasi kikubwa, Jitu alipohakikisha kuwa Kelvin kakaa vizuri kitini, aliondoa gari taratibu akilini mwake akiwa amekwishaamua kumpeleka Hospitali ya Mwananyamala. Aliamua hivyo kwa kuwa aliona haitakuwa vyema kumrudisha nyumbani kwake akiwa katika hali hiyo. Mtu mwenyewe ni kapera, kwa hali hiyo usalama wake ungezidi kuwa shakani kama atamfikisha kwake na kumwacha peke yake!



    Akaendesha gari kwa umakini, kwa mwendo huohuo wa asteaste na baada ya nusu saa alikuwa nje ya geti la lango la Hospitali ya Mwanayamala. Huyu hakuwa yule Jitu mwenye ujasiri, hapana. Hii hali ya kiafya aliyokuwa nayo Kelvin ilimfadhaisha kwa kiwango kikubwa. Aliingiliwa na mambo mengi kichwani kwa mkupuo, lakini, kubwa zaidi ni jinsi ya kuwasiliana tena na Sharifa. Alizihitaji sana pesa alizoahidiwa lakini atazipataje ilhali kazi waliyotumwa imewashinda?



    Je, Sharifa na ASbdul watachukua hatua gani pale watakapotambua kuwa pesa zao zimeteketea bila ya kazi kufanyika? Hata hivyo, alijipa matumaini kuwa, ilimradi ana hizo pesa kidogo za awali, atajua namna ya kuwakwepa. Muhimu ni kujua Abdul yuko wapi na ana mpango gani. Ni Abdul ambaye anamfahamu hata anakoishi hivyo huenda pale watakapoingiwa na wasiwasi, akaamua kumfuata kimyakimya na labda akitumia mbinu tofauti sanjari na nyenzo tofauti. Huenda akamjia akiwa na dhamira nyingine, akiwa tayari kumfanyia lolote!



    Papohapo akaamua kufikiria vizuri hatua ya kufanya baada ya kumkabidhi Kelvin kwa wauguzi hapo hospitali.



    Baada ya dakika kama ishirini hivi, alikuwa amehakikisha Kelvin amepelekwa wodini baada ya kupata vipimo kwa daktari. Alimwambia daktari, kuwa Kelvin alianguka kwenye mfereji mkubwa kando ya barabara, ukawa ni uongo uliokuwa ni ukweli akilini mwa daktari huyo.



    Kilichomtia uchungu ni kuwa hata alipojaribu kumuaga, Kelvin hakuwa akimtambua wala hakuweza kutamka chochote. Hata wauguzi wawili waliokuwa pale kando ya kitanda walimtazama Kelvin kwa namna ya kukata tamaa na hata waliposoma maelezo ya daktari kwenye cheti, walionesha nyuso za mfadhaiko wa mbali japo walijitahidi kuificha hali hiyo mbele ya Jitu.



    Sasa Jitu alikata tamaa. Lakini hakuwa na njia nyingine zaidi, isipokuwa ni kumwacha hapo wodini na baada ya hapo aanze mikakati mingine. Wakati akiondoka huku akisindikizwa na manesi wawili wa wodi hiyo, mmoja alimuuliza, “Kaka kwa nini usimpeleke Regency? Hali yake kwa kweli siyo nzuri. Anahitaji vipimo vikubwa zaidi.”



    Hii kauli ilizidi kumthibitishia Jitu kuwa sasa Kelvin ‘ndiyo basi tena!’ Akajikuta akitokwa jasho jembamba huku akihema kwa nguvu. Hakutaka kujidanganya kuwa Kelvin atapona. Kama hawa manesi pia wanadiriki kumshauri hivi kama yule daktari wa kule Kunduchi, kuna usalama kweli hapo? Kama wenye taaluma yao wameonyesha kukata tamaa si ni dhahiri kuwa wameshaona hakuna litakalowezekana kwa mgonjwa huyo?



    Akamtazama kidogo huyo nesi ksha akamjibu, “Ngoja niende kujiandaa nesi. Nitarudi baadaye kumchukua.”



    Aliondoka haraka huku akizidi kuchanganyikiwa!







    MERCEDES Benz jeusi lilitokomea, Sharifa akiwa makini nyuma ya usukani, akilini akihisi kuzidiwa na mambo na akiwa hajui hatima ya hatua hii aliyoichukua. Muhimu kwake aliona ni kuliepuka eneo hili na mengine atayajulia huko mbele ya safari.



    Dakika kadhaa baada ya kulikimbia kasri la Malick Sikonge, alikuwa eneo la Ada Estate, ambako alipita mitaa miwili mitatu na kuibukia Barabara ya Kinondoni. Askari wawili watatu wa Usalama Barabarani waliokuwa kando ya barabara hiyo, walimshtua na kujikuta akijiwa na wazo lingine.



    Ndiyo, alitambua kuwa huenda kitendo cha kuondoka kule kituoni kikazua hatua nyingine kubwa dhidi yake. Itachukuliwa katoroka au katoroshwa! Na kama huyu askari aliyemwachia pesa kiduchu tofauti na makubaliano yao, atachukizwa na hilo, basi huenda kwa hasira akaamua kurudi kituoni ambako atakuwa tayari kuutengeneza uongo ufananao na ukweli kuwa hahusiki na utorokaji bali ni hila tu zake, Sharifa.



    Hakuwa akimfahamu Inspekta Massawe lakini kwa namna alivyokuwa akizungumza kwa kujiamini na jinsi alivyokuwa akitoa maagizo kule kituo kidogo usiku, ilitosha kuwa taswira halisi kuwa ni askari mwenye cheo, hata kama siyo cha juu sana.



    Kama kweli Inspekta Massawe atakuwa ni askari mwenye kuweza kuheshimika vile pale kituoni, basi huenda pia akawa na kauli ya kukubalika na kuheshimika kwenye kituo chochote kikubwa. Kituo cha Polisi cha Oysterbay ndicho kikubwa kwa ukanda huo, kituo ambacho pia huenda kikahusika kwa tukio hili, hivyo aliamini kama askari huyo atabaini kuwa kazidiwa ujanja katika mkasa huo, kwa vyovyote hatakubali heshima yake ishuke.



    Kuaminiwa na mtu kama Dk. Suleyman, daktari ambaye kitaaluma aliheshimika sana kiasi cha kuwa daktari bingwa na maalumu kwa tajiri Malick Sikonge enzi za uhai wake, kwa Inspekta Massawe aliona kuwa ile haikutofautiana na tuzo maalumu, hivyo hatasita kulifikisha suala hilo katika kituo cha Oysterbay na huko kutachukuliwa hatua zaidi za kiutendaji. Hilo ndilo alilolihofia Sharifa, hivyo akaamua kuwa makini zaidi.



    ‘Kukurupuka kama chizi tu na kuukimbia mji unaweza kuwa upumbavu zaidi ya upumbavu halisi,’ alijisemea kimoyomoyo. Wakati huo alikuwa ameiacha Barabara ya Tunisia na ameshika Barabara ya Kinondoni eneo la makaburi huku moyo ukimdunda kwa nguvu.



    Muda mfupi baada ya kuwapita wale askari aliwatupia macho kwa kutumia kioo, na akaona wakilisimamisha daladala lililotokea Stesheni. Sharifa akashusha pumzi ndefu na kuongeza mwendo. Alipofika Kinondoni ‘A’ akashtuka tena alipowaona askari wengine wawili kwenye makutano ya barabara hiyo na Barabara ya Rashid Kawawa. Alishangaa kuwa alishtuka kila anapowaona hao watu wenye sare nyeupe na hali hiyo ilimfanya ahisi kuwa kuna jambo.



    Akaifuata barabara ya Rashid Kawawa akielekea magomeni. Sasas aliamua kwenda sehemu yoyote na kuliegesha gari hilo kwa kuwa alianza kuhisi linaweza kuwa kiini cha kukamatwa kama askari watakuwa wameamua kumvalia njuga.



    Hata hivyo, alihitaji kupata uhakika kama kweli anasakwa kwa nguvu kubwa. Hakuona kama itakuwa sahihi kujawa na woga ilhali huenda hakuna lolote linalomnyemelea.



    Alikuwa ni mtoto wa mjini, hivyo hakuwa mtu wa kufikiria ajichimbie katika mtaa upi wa mafichoni kwa muda kisha akasaka mawasiliano na mtu aliyeamini kuwa anaweza kumpa mwanga halisi wa kinachoendelea.



    Alikanyaga mafuta kwa nguvu hadi Magomeni-Morocco ambako alikata kulia na kuingia Mtaa wa Chemchemi. Mita kama mia tatu hivi kutoka barabara kuu, aliegesha gari kando kisha akatwaa simu. Alishukuru Mungu kwa kuwa na namba za watu muhimu kwake waliokuwa wakiishi ndani ya kasri la marehemu Malick. Miongoni mwao ni yule mlinzi, Robert wa geti kubwa.



    Akaitoa simu mkobani na kuiwasha. Baada ya nusu saa ilikuwa tayari kwa matumizi. Akalisaka jina la Robert na alipolipata akapiga. Ala ya wimbo wa dini ikayafikia masikio yake. Akatulia akisubiri. Simu ikaita mpaka ikakatika. Akashangaa, iweje isipokewe?



    Akajiuliza apige tena au aache? Huenda Robert hakupokea ili askari kama wako hapo awaambie? Akatulia kwa takriban dakika nzima kisha akaamua, liwalo na liwe! Akapiga tena, safari hii akiamua kuwa kama haitapokewa basi asipige tena.



    Ikapokewa!



    *****



    INSPEKTA Massawe alikuwa bora sana pale aketipo nyuma ya usukani. Kabla ya kujiunga na Jeshi la Polisi miaka kadhaa nyuma, alikuwa fundi makanika katika gereji bubu kadhaa, ufundi uliomwimarisha zaidi katika uendeshaji wa gari.



    Akiwa na hasira ya kuzidiwa mbinu na Sharifa, na akiamini kuwa bado ngoma nzito, aliling’oa gari kwa kasi ya aina yake mbele ya kasri la Malick Sikonge, gia zikibadilishwa kutoka moja hadi nyingine, macho makali barabarani na umakini ukiwa umezingatiwa. Mwendo ulikuwa mkali, akiyapita magari kadhaa kila alipoona ana nafasi ya kufanya hivyo.



    Walipofika kando ya geti la Hospitali ya Mwananyamala, wakakuta mkusanyiko mkubwa wa watu. Hali hiyo ilisababaisha hata wakose nafasi ya kuingia hivyo Inspekta Massawe akatafuta eneo hapo nje ya hospitali na kuegesha gari kisha wakateremka haraka.



    Macho yao yakawashuhudia wahudumu watatu wa hospitali wakiwa wamebeba mwili wa mtu na kuweka kwenye machela. Massawe na Dk. Suleyman hawakushangaa sana kwa kuwa walijua kuwa matukio ya kuwaona watu mahututi ndani au nje ya hospitali kubwa kama hiyo siyo ya kustaajabisha. Akili zao zikawatuma kuwa huenda ni mgonjwa kaletwa hapo akiwa hajiwezi.

    Wao wakaharakisha kwenda ndani lakini wakashtuka pale walipomwona askari aliyekuwa akimlinda Abdul, akija mbio huku getini. Ni Inspekta Massawe aliyemgundua haraka licha ya kuwa na watu wengi waliokuwa wakielekea wodini na wengine wakitoka.



    Askari yule naye akamwona Inspekta Massawe. Macho yao yakagongana! Askari yule akajiwa na wasiwasi. Kwa jumla kilichomtoa huko ndani mbio ni baada ya kugundua kuwa mtuhumiwa hayupo, na alipozungukia kila sehemu humo wodini hakumwona, ndipo alipojenga hisia kuwa katoroka!



    Wakati alipotoka wodini humo akasikia taarifa ya mtu aliyekanyagwa na basi wakati akikimbilia teksi kutoka hospitali ilihali akionekana kuwa hayuko katika afya njema kutokana na jinsi alivyotembea.



    Ni taarifa hiyo ndiyo iliyomtisha askari huyo, akaamini kuwa Abdul atakuwa ametoroka.



    “Vipi? Unakwenda wapi na kumwacha mtuhumiwa peke yake?” Inspekta Massawe alimuuliza kwa ukali, akimtazama usoni sawia.



    “Afa…afande…mtuhumiwa katoroka…” askari huyo alisema kwa sauti yenye kitetemeshi.



    “Nini?” Dk. Suleyman na Massawe wote wakauliza, macho yamewatoka pima.



    “Katoroka afande…”



    Hawakuzungumza zaidi mara wale wahudumu waliokuwa na machela walipowapita hima wakielekea ndani. Askari yule akiyakumbuka maneno aliyoyasikia kule wodini, haraka akawafuata wahudumu wale na kuwasihi wasimame. Sare zake za kiaskari zilimlinda, vinginevyo angekumbana na kauli za kukera. Mhudumu mmoja akamuuliza, “Vipi, afande? Huyu marehemu tunamwahisha mochwari maana’ke kaharibiwa sana…kakanyagwa mara mbili!”



    “Tafadhali…mara moja tu, tumwone sura,” askari huyo aliwaambia.



    Haikuwa kazi ngumu kwa wahudumu hao, mmojawao aliufunua uso wa mtu waliyembeba. Wakati huo Inspekta Massawe na Dk. Suleyman walikuwa wameshasogea.



    “Haaa! Abdul!” Dk. Suleyman alibwata.



    Inspekta Massawe akashangaa huku kamkazia macho yule askari. “Ilikuwaje akaja mpaka huku barabarani?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Afande ni taarifa ndefu kidogo.”



    Massawe akamgeukia Suleyman na kumuuliza, “Kuna umuhimu wa kuendelea kuwa hapa? Kumbuka yule mwanamke ndiyo msingi wa kazi yetu!”



    “Ni kweli inspekta,” Dk. Suleyman alijibu huku akiwaangalia wale wahudumu waliokuwa wamekwishaanza kuondoka. “Huyu kishatangulia, tushughulikie kuhusu dada yake.”



    Inspekta Massawe akamgeukia yule askari. “Wewe ni askari wa pili leo kuliaibisha Jeshi la Polisi. Naondoka na wewe hadi kwa OCS. Atajua la kukufanya.”



    **MWISHO???????????



0 comments:

Post a Comment

Blog