Simulizi : Mapigo Ya Moyo
Sehemu Ya Nne (4)
Dar es salaam;
Kwa mala nyingine tena nikiwa ndani ya gari dogo aina ya Alteza, gari ambalo aliweza kulimiliki dada yangu Rose. Lilipaki nje ya nyumba ya mzee Jastin, kwakuwa hakukuwa na mtu yeyote yule wa kutufungulia geti, ilibidi Rose ashuke ndani ya gari na kisha kwenda kufungua geti lile na baadaye aliweza kurudi na kuliingiza gari ndani.
“Haya mpenzi tumefika! shuka ukaoge, ule chakula na kisha uniambie chanzo cha wewe kupoteza fahamu “,kwa kauli ya upole sana Rose alizungumza maneno yaliyouchoma moyo wangu, na kunifanya nipandwe na hasira kichwani mwangu. Sentesi ambayo Rose aliweza kuizungumza muda mfupi tu baada ya kufika nyumbani, tukitokea katika hospitali ya manispaa ya Temeke. Hospitali ambayo nilikuwa nikipatiwa matibabu baada ya kupoteza fahamu, asubuhi siku ya jumamosi.
“Mimi sio mpenzi wako kuanzia sasa! wewe ni dada yangu, wewe ni Jacline dada yangu kipenzi,na wala sio Rose kama unavyojifahamu wewe, hicho ndicho chanzo cha mimi kuzimia “,nilifoka kwa hasira, nilifoka kama vile Jacline ndiye aliyekuwa na makosa, wakati sio kweli! chanzo cha matatizo yote ambayo yalikuwa yametokea ilikuwa ni mzee Jastini.
“Mpenzi unaongea nini?, mbona sikuelewi! mimi nimezaliwa Dar es salaam na nimesomea hapa mpaka kumaliza, chuo tu ndio nimesomea Morogoro. “,Rose alinijibu kauli yangu, alionekana kushangazwa na maneno yangu na kuniona kama vile niliingiliwa na wendawazimu. Ndani hakukuendeka tena, wala chakula hakikulika tena. Ilibidi niahirishe kwenda kuoga, wala kula japo nilikuwa sijala tangu asubuhi na kuamua kumuelezea Rose kwa urefu na mapana aweze kunielewa.
“Ile picha inaonesha ukiwa una ombaomba katika eneo la minzani, Mikese, Morogoro, kijiji ambacho mimi nimezaliwa na kukulia. Chini ya picha yako imeandikwa Jacline, jina hili la Jacline lilikuwa jina lako, jina ambalo alilitumia dada yangu kipenzi aliyepotea wakati anaomba omba abiria wa mabasi katika eneo la minzani, na huyo mdogo wangu sio mwingine bali ni wewe Rose. Tulikutafuta bila mafanikio, tulilia na kunyamanza, tukaweka msiba na kutandua. Hatimaye mwezi ulikatika mpaka miaka ukiwa haujarudi na kuamini kuwa uliweza kufariki dunia “,niliongea kwa huzuni sana, maneno ambayo yalimuingia vilivyo Rose na kujikuta machozi yakianza kumchuruzika katika uso wake.
“Kama huamini, mzee Jastini ameshawahi kukuonyesha mama yako? ,vipi kuhusu ndugu zake, ameshakuonyesha? hapa kuna siri anaifahamu na ndio maana kakuita mwanaharamu na kusema alikuokota “,niliendelea kumwelezea Rose na hatimaye alinielewa, alikimbia kwa huzuni na kisha kupiga magoti na kunikumbatia. Maneno yangu aliweza kuyaamini na yalikuwa sahihi kabisa.
“Nimeamini Robert, wewe ni kaka yangu, ndio maana muda mwingine nilikuwa nataka kukumbuka lakini nashindwa, itakua alifuta kumbukumbu za kichwa changu! lakini nina mimba yako Robert, nilipokuwa hospitalini nimepima mkojo kwani ni muda mrefu sasa sijapata siku zangu “,Rose akiwa analia, alitonesha kidonda changu kwa mala nyingine tena, nilikumbuka jinsi ambavyo tuliweza kufanya mapenzi mala kadhaa bila kutumia kinga. Sikuamini kama kweli dada yangu wa tumbo moja, alikuwa na ujauzito wangu. Nililia kwa uchungu na kujutia jambo lile ambalo lilikuwa limetokea, na kumuomba Mungu anisamehe kwani sikujua kama niliyempenda kwa dhati na kumkabizi moyo wangu, alikuwa ni dada yangu.
Niliamini Mungu alinisamehe kwa dhambi hiyo kwani sikuwa tayali kuona Rose akitoa mimba ya kiumbe kisichokuwa na hatia. Lakini kazi pekee ambayo ilikuwa imebakia, ni kutambua chanzo kilichomfanya mzee Jastin kumuiba Rose na kumdanganya kuwa alikuwa ni mwanae halali wa kumzaa, kumbe sivyo!
………………………………
Hatimaye Kendrick anaamua kusafiri haraka sana kwa kutumia ndege ya serikali, ni baada ya kupokea taarifa kutoka kwa baadhi ya raia wema wa Kenya, ambao walidai kumuona mtu aliyefanana na Rodgers akikatiza mtaani.
Japo alipuuzia tetesi hizo, lakini alikuja kuamini maneno ya watu hao kwani baada ya kupeleleza ndege ambayo Rodgers aliipanda na kufanikiwa kutoroka nchini Tanzania. Wahudumu walidai kumpandisha mtu ambaye alijifanya mgonjwa, na alifanana sana na Rodgers. Walikili hayo yote baada ya Kendrick kutumia mbinu zake za upelelezi, na kuwapatia vitisho vya hali ya juu sana wahudumu wale na kujikuta wakizungumza kila kitu.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mombasa is beautiful (Mombasa ni nzuri)”,ilikuwa ni sauti ya upole sana kutoka kwa kijana Kendrick, akizungumza na kufurahia muonekano mzuri wa mji mkongwe wa Mombasa. Maneno hayo aliweza kuyazungumza wakati ndege ya raisi, ndege ambayo ilimleta Kenya Kendrick kwa amli na agizo kutoka kwa raisi wa nchi hii inayokua kwa kasi kiuchumi, nchi inayosifika kwa amani duniani. Si nyingine, bali nchi ya Tanzania. Ndege hii ilikuwa ikitua katika uwanja wa kimataifa wa Mombasa unaojulikana kama (MOI).
…………………………………
Hatimaye Rodgers anafanikiwa kuufikisha mzigo wa madawa ya kulevya aina ya cocaine jijini Nairobi.Hakuwa na budi kumshukuru msichana yule mrembo aliyempatia lifti, kwani gari lao halikuweza kukaguliwa na polisi njiani, kama ujuavyo wanaume rijali wanavyokuwa dhaifu kwa mabinti wazuri wa kike. Ndivo ilivyotokea! Kila askari aliyetaka kukagua gari la msichana yule wa Kijaruo, alijikuta akisitisha zoezi lake pale tu msichana yule alipotabasamu huku akiyashika matiti yake kwa makusudi kuyaweka sawa. Kamchezo haka kalimsaidia msichana yule aliyeonekana kuwa mnjanja wa mjini, kumfikisha Rodgers Nairobi kwa muda mfupi, na bila kukamatwa na askari yoyote yule.
“Haloo! mzee sogeza gari lako eneo la parking ya magari nje ya uwanja wa ndege, nataka nishuke na kufika naingia moja kwa moja ndani ya gari lenu “,Rodgers alipiga simu, mala baada ya kukaribia eneo la uwanja wa ndege wa kimataifa jijini Nairobi. Msichana yule aliyempakiza kwenye gari lake, hakuweza kutambua ni kwanini Rodgers aliwakwepa sana polisi. Kwasababu alikuwa ni binti aliyekulia mjini, ilibidi apotezee na kuendelea kuisogeza gari katika eneo la uwanja wa ndege, ili Rodgers aweze kuonana na mtu aliyedai anampelekea mzigo, mzigo ambao msichana yule aliamini ulikuwa ni wa pesa nyingi bila kutambua kuwa ilikuwa ni madawa ya kulevya.
Kenya;
Hali ya wasiwasi inaikumba kasri ya John Owino, tajiri na mfanyabiashara maarufu nchini Kenya.John Owino Hakuishia kuwa mfanyabiashara tu, bali alikuwa kiongozi mkuu wa chama cha upinzani nchini Kenya, chama ambacho kilijipatia umaarufu wake kutokana na kuikosoa serikali mara kwa mara ilipokwenda kinyume, na kuifanya serikali ya chama tawala kuongoza nchi kwa haki na usawa kwa hofu ya kupinduliwa na chama hiki cha upinzani. Chama hiki kilipendwa sana na Wakenya wengi hasa vijana wapenda maendereo, kiasi kwamba John Owino kila alipopita na gari lake la kifahari, wananchi walilisukuma na pengine kutandika hata nguo zao chini kama ishara ya upendo wao kwa kiongozi huyu mkuu wa chama cha KOP, bwana John Owino.
Nyuma ya pazia John Owino alikua mtu mubaya sana, tena muuaji na katili, huku biashara haramu ya madawa ya kulevya ikiwa moja ya shughuri zake kuu za kumuingizia kipato. John Owino aliamua kujiingiza katika siasa miaka kadhaa iliyopita nyuma, kama njia pekee ya kurahisisha biashara zake huku akitumia siasa kama pango la kufichia maovu yake. Hatimaye malengo yake yalitimia, kwani chama cha KOP (Kenya Opposition party) alichokianzisha kilileta changamoto kwa serikali ya Kenya, hali iliyopelekea raisi wa Kenya bwana Emmanuel Odinga kumteua John Owino kuwa makamu wake wa raisi. Raisi hakuwa na namna nyingine ya kufanya,aliamua kumteua bwana John Owino kama makamu wake wa raisi ili kukwepa kupinduliwa na kiongozi huyu aliyeonekana kujitwalia wafuasi wengi kila kukicha. Kinyume kabisa na fikra zake! John Owino hakuwahi kufikilia kumpindua raisi huyu na yeye kuwa raisi wa Kenya, bali alikuwa na lengo la kuwa waziri wa biashara na uchukuzi, ili tu biashara zake ziende vizuri na kutozwa kodi ndogo.
Hivyo basi, alifurahi sana alipoteuliwa kuwa makamu wa raisi. Kwani alikuwa amepata mafanikio zaidi ya matarajio yake. Hatimaye umaarufu wake ukaongezeka kila kona ya Afrika Mashariki na kati.
John Owino akaamua kuanzisha kundi lake binafsi, tofauti na awali alivyokuwa akifanya biashara haramu ya madawa ya kulevya akiwa chini ya watu fulani,kwa sasa yeye ndiye alikuwa kama bosi mkuu na kuajiri watu hasa vijana wenye uwezo mkubwa katika mapambano na matumizi ya siraha. Hakuishi tena jijini Nairobi, jiji kubwa na zuri nchini Kenya bali aliamua kuhamia mji mkongwe wa Mombasa. Lengo la kuhamia Mombasa na kuanzisha ngome yake kubwa sana, alitaka kuwa karibu na bahari kwa ajiri ya kusafirisha na kupokea madawa ya kulevya kutoka sehemu mbalimbali duniani.
John Owino ili kuimarisha kundi lake, akaamua kumteua rafiki yake kutoka Tanzania. Mfanyabiashara waliyekuwa wakishirikiana pamoja katika biashara hizi haramu kuwa kiongozi msaidizi wa kundi lake, na mtu huyu si mwingine bali mzee Jastin.
John Owino hakuishia hapo, alitaka kuimarisha kundi lake la EADD (East African Drugs Dealers) zaidi na zaidi. Akamteua askari mmoja mwenye nyazifa za juu sana nchini Uganda,kuwa kama msafirishaji mkuu wa madawa katika kundi lake. Kutokana na tamaa ya pesa, bwana George Kibira alikubali ombi la makamu wa raisi wa Kenya John Owino na kujiunga na kundi lake hili linalohusika na biashara haramu.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hatimaye kundi likawa kubwa na lenye mafanikio makubwa sana katika biashara hii, kutokana na viongozi wa serikali kuwa miongoni mwa viongozi wakubwa wa kundi hili, umoja wa Afrika Mashariki ulishindwa kulidhibiti na kuwakamata viongozi wakuu, kwani kila upelelezi wa siri pamoja na oparesheni za kijeshi kupangwa kwa ajili ya kuliteketeza kundi hili, bwana John Owino bila kugundilika kuwa ndiye muhusika mkuu aliweza kupata habari mapema sana na kuwataarifu vijana wake kuhusu taarifa yoyote aliyoipata. Hali hii ilipelekea kundi hili kuendelea kukua kwa kasi, na kuwa kundi kubwa duniani huku likijihusisha na biashara haramu kimataifa. Miongoni mwa biashara hizi ni kuwakamata watoto wa kike hasa ombaomba na yatima, na kisha kuwauza barani Ulaya na Asia.
………………………………
Ujio wa Kendrick mjini Mombasa ndio uliomshitua makamu wa raisi wa Kenya, na kiongozi mkuu wa kundi hili la EADD. Alizidi kuchanganyikiwa na kuingiliwa na hofu zaidi, pale alipopokea taarifa kutoka Tanzania. Taarifa iliyosema kuwa Kendrick alikuja Mombasa kumtafuta Rodgers kwa makosa mawili, kosa la kwanza aweze kujibu shitaka lake kuhusu kuhusika na mauaji ya mtoto wa raisi wa Tanzania, na pia kosa la pili aweze kujibu tuhuma ya kujihusisha na biashara haramu ya usambazaji wa madawa ya kulevya, na aweze kuwataja viongozi wake wa kundi la EADD.
“Mnachotakiwa kufanya ni kuwa makini, nawaamini sana vijana wangu, mtu huyu aliyekuja Kenya kutupeleleza ni mtu hatari sana, mpaka sasa anajua kuwa Rodgers ni mmoja kati yetu na mbaya zaidi tayali amefika Mombasa leo hii kwa ajili ya kumtafuta kijana wangu Rodgers, “,Japo John Owino alikuwa Mkenya, lakini alizungumza kiswahili kizuri sana kilichoeleweka na kila mmoja.Alitoa kauli yake mbele ya jeshi lake la vijana miatano,vijana walioiva katika karate na utumiaji wa siraha mbalimbali za kivita.Bwana John Owino akiwa amesimama sambamba na mzee Jastin,katika kasri lao kubwa lililojengwa ndani ya handaki,waliendelea kuwaandaa vijana wao kisaikolojia kwa ajili ya kupambana na Kendrick.
Nyumba kubwa ya kifahari ,nyumba ambayo ilijengwa katika mitaa ya Kisauni mjini Mombasa iliendelea kuimarishwa kwa ulinzi wa hali ya juu sana kama zilivyo nyumba nyingi za viongozi wakubwa wa nchi mbalimbali duniani
Jengo hili la kifahari ambalo ndiyo yalikuwa makazi makuu ya makamu wa raisi wa Kenya bwana John Owino,liliwashangaza wengi sana kwani kutokana na uzuri wake na wazifa alionao bwana John Owino hakupaswa kuishi eneo ambalo waliishi watu wa kipato cha chini,watu wa uswazi,katika mtaa huu wa kisauni uliofananishwa kama Tandale,Dar es salaam nchini Tanzania.
Hawakufahamu kuwa jengo lile la kifahari la John Owino,lilikuwa limeficha siri nzito.Kwani chini ya jengo hili,kulikuwa na handaki kubwa sana,handaki ambalo lilikuwa na uwezo wa kuhifadhi watu zaidi ya elfu kumi.Barabara za lami zilizotengenezwa kwa ubunifu wa hali ya juu,zilipendezesha handaki hili na kuwa kama taifa jingine ambalo lilipatikana ndani ya ardhi.
Majengo mbalimbali mazuri na ya kifahari,yaliyopatikana ndani ya handaki hili na kumfanya kila aliyekanyaga ndani yake kushangaa mji huu,hakusita kumshukuru Mungu kwa kuwapatia wanadamu maarifa na akili ya kubuni vitu vizuri,japo muda mwingine walimkosea Mungu na kutumia maarifa ambayo Mungu aliwapatia kwa kujinufaisha wao wenyewe.
Kwani watoto wengi wa kike walikuwa wamefungiwa katika moja ya majengo yaliyopo ndani ya handaki hili wakisubili kuuzwa, na majengo mengine yalitumikia kuhifadhia siraha pamoja na madawa ya kulevya.
Tanzania
Hatimaye machozi yananitoka kwa mala nyingine tena,kwani baada ya kumwelezea Rose kuwa alikuwa dada yangu,tulielekea ndani na kupekua tena kompyuta ya mzee Jastin kwa ajili ya kujua chanzo cha Rose kuwepo katika jengo la mzee Jastini kama mwanae.
“Usilie kaka ,yote ni mipango ya Mungu,tunatakiwa tumripoti mtu huyu haraka sana polisi” Rose aliongea ,hakulia tena kwani alikuwa na hasira na mzee Jastini baada ya kutazama historia nyingine ndefu iliyokuwa imefichwa katika kompyuta ya mzee Jastini.
**********
****************
Kendrick akiwa ndani ya chumba cha hoteli, katika hoteli ya kitarii inayopatikana katika ufukwe wa bahari ya hindi mjini Mombasa.Kwa utaalamu wake wa kutumia kompyuta aliokuwa nao, ulimuwezesha kugundua mambo mengi sana kumuhusu Rodgers. Lakini alishindwa kupata taarifa kuhusu, viongozi wa kundi hili la EADD. Hakutambua kuwa bwana John Owino, alikuwa msomi na mjanja sana. Alitambua kuwa muda wowote taarifa kuhusu kundi lake zingeweza kutafutwa katika mtandao, hivyo basi! aliamua kuajiri wataalamu wa Kompyuta kutoka Marekani, na kisha kuziwekea namba ya siri taarifa zozote ambazo zilihusu kundi hili la EADD.
Kendrick ujanja ulimuishia, japo alipata taarifa kuwa Rodgers aliweza kukimbilia Mombasa, lakini hakufahamu ni eneo gani la Mombasa ambalo Rodgers aliweza kujificha.Lakini aliamini kuwa mtu aliyemtafuta alikua hatari sana,kwani sura ya Rodgers haikua ngeni machoni pake,aliamini pengine alikuwa miongoni mwa askari aliosoma nao nchini Marekani,kumbe sivyo! aliweza kukutana na Rodgers nchini Tanzania,wakiwa kikosi kimoja katika mafunzo ya JKT,kabla Kendrick hajachaguliwa na kwenda Marekani,huku Rodgers akitoroka kambini na kisha kujiunga na kundi hili la John Owino pamoja na Mzee Jastini.
“Inabidi nimtafute kijana huyu alietupatia taarifa kuhusu Rodgers kwa mala ya kwanza,naamini anaweza nisaidia chochote”,mpelelezi wa Kimataifa,raia wa Tanzania,aliongea baada ya kimya kirefu huku akipekua simu yake na kisha kuitafuta namba ya kijana mmoja raia wa Kenya aliyeripoti taarifa polisi baada ya kukiri kumuona Rodgers Mombasa,na kujipatia pesa taslimu shilingi milioni tano huku ulinzi wa polisi ukikabidhiwa jukumu la kumlinda,pale maisha yake yatakapokuwa hatarini
“Halooo!naongea na Yusto?”,
“Ndio,nani mwenzangu?”,
“Kuwa na amani kaka!,unaongea na afande Kendrick” ,
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ohooo,niambie mheshimiwa,nikusaidie nini?”
“Kabla ya kuongea lolote,nakuomba baada ya mazungumzo yetu,sajili namba mpya,kuhusu pesa usijali nitakutumia,”
“Sawa mkuu”
“Sasa kijana,unaweza niambia ni wapi uliweza kuonana na Rodgers?”,
“Kijana Rodgers iko kisauni,nimeiona siku moja karibu na kwa nyumba ya heshimiwa John Owino”
“Asante sana kwa ushirikiano,utapokea pesa baada ya muda mfupi,kisha toa pesa hiyo,na ukimaliza vunja vunja laini yako na wewe utasajili laini nyingine,bila hivyo watu wabaya wanaweza kunasa maongezi yetu”,
“Sawa mkuu,mimi shujaa kama wewe,naweza tandika mbwa yoyote kama ikijaribu kuja mbele yangu”,
Yalikuwa ni mazungumzo kati ya Kendrick,na kijana mmoja wa Kikenya aliyejulikana kwa jina la Yusto.Kijana huyu alipenda sana kujiunga na jeshi la Kenya,lakini kutokana na umaskini aliokuwa nao alikosa pesa za kuhonga na kisha kupata nafasi hiyo ya kujiunga na jeshi.Aliamua kuendeleza harakati zake za kuripoti waharifu akiwa uraiani,kwani alikuwa tayali amekata tamaa ya kujiunga na jeshi tangu nafasi yake ilipotolewa kwa watu wengine,pale alipokosa laki tano,pesa ya Kenya na kuitetea nafasi yake isiweze kuuzwa.Serikali ya Kenyailimtambua sana kwani alikuwa miongoni mwa vijana hodari ambao hawakuogopa kuwaripoti serikalini waharifu,akiwemo Rodgers pamoja na wengine wengi.
………………………………
Haraka sana Kendrick alijiandaa,saa yake yenye kufanya kazi kama kompyuta ilikua mkononi mwake.Saa yake ilikuwa na uwezo mkubwa wa kutambua siraha za kivita kama mabomu pamoja na bunduki.Hakusahau miwani,miwani yake aliyopatiwa kama zawadi alipokuwa mshindi wa kwanza katika mafunzo ya kijeshi yaliyoendeshwa na nchi wanachama wa umoja wa mataifa nchini Marekani.Miwani yake ilikuwa na mionzi mikali,mionzi ambayo ilikuwa na uwezo wa kuzima kompyuta zote katika eneo lolote ambalo Kendrick angekuwepo,na kubonyeza kibatani kilichoko sehemu ya juu ya miwani yake kuzima kompyuta husika.Uwezo wa miwani ya Kendrick haukuishia hapo,miwani yake ilikuwa na uwezo wa kuona mpaka vitu vya ndani katika mwili wa binadamu.Hivyo usingeweza kumdanganya Kendrick kirahisi,mpaka anachaguliwa na FBI kufanya nao kazi,alikuwa mtu hatari na mwenye uwezo mkubwa duniani.
“Mungu wangu nimemsahau mke wangu pamoja na mwanangu!”,Kendrick akiwa ameshatoka nje ya jengo la hoteli ya kitarii iliyojulikana kwa jina la Mombasa picnic Hotel,aliamua kurudi chumbani kwake baada ya kusahau vitu muhimu juu ya kitanda chake.
Vitu hivyo ambavyo alivipatia majina ambayo yalikuwa na maana tofauti kabisa na maana halisi.Siku zote alipenda bastora yake isiyokuwa na sauti,kama vile alivyokuwa akiapa kumpenda mke wake siku atakapo funga ndoa,na pia kila mahali alitembea na kisu chake kama jinsi alivyokuwa akifikiri,jinsi atakavyompenda mtoto wake siku moja Mungu atalapomjalia.Haraka sana alipakia bastora na kisu chake katika gwanda lake la kijeshi na kisha kuanza safari ya kuelekea kisauni.
Tanzania
Tabasamu linaipamba sura ya mheshiwa raisi kwa mala nyingine. Hakuamini kama aliweza kutembelewa na vijana wadogo na wazuri waliopigania penzi lao kufa na kupona. Furaha yake iliongezeka pale alipomuona Rose akiwa mjamzito, aliamini kuwa mimi ndiye muhusika wa mimba ile, na kumfanya azidi kujawa na tabasamu pamoja na furaha kuu.Tangu anifahamu siku ambayo mtoto wake aliweza kuuawa kwa kupigwa risasi, upendo wote aliweza kuhamishia kwangu. Kwani aliamini nilikuwa rafiki mzuri kwa mwanae na ndio maana kijana wake alikubali kupigwa risasi badala yangu, aliamini nilikuwa sina hatia kufa ndio maana Jacob akafa badala yangu.
Lakini japo mheshimiwa raisi alikuwa na furaha sana kutuona ikulu, lakini alishangaa kwa upande wetu tukiwa wanyonge na tusio na furaha hata kidogo. Mambo mazito kuzidi umri wetu yalikuwa katika vichwa vyetu, na kuondoa amani katika maisha yetu.
“Karibuni vijana wangu, nafurahi sana kuwaona mkiwa bado pamoja japo mmekutana na vikwazo vingi katika mapenzi yenu, lakini naomba muwe na furaha!!! Rose unaponuna, hata kiumbe chako kilichoko tumboni kitadhoofika, na mtashindwa kuwa kama wazazi bora “, raisi wa Tanzania aliongea na sisi kama vile watoto wake, tofauti na zamani niliweza kumuogopa na kumsikiliza kwenye redio, lakini kwa sasa alikuwa kama ndugu yangu kutokana na mazoea yaliyoanza siku ambayo mtoto wake alipigwa risasi na Rodgers na kisha kupoteza maisha.
Machozi yaliongezeka katika nyuso zetu, ikulu ikageuka kama sehemu ya msiba kwani tulilia kwa sauti kubwa mimi pamoja na dada yangu Rose. Maneno ambayo raisi aliweza kuyaongea kuhusu mahusiano yangu mimi na Rose, pamoja na mtoto wetu aliyeko tumboni ndio chanzo cha kilio chetu.
“Msilie wanangu, niambieni nani kawakwaza na kuwaumiza ni mshunghulikie, hata kama ni baba yako Rose, mzee Jastini, niko tayali kumfunga japo ni mmoja kati ya wafanyabiashara wakubwa ambao wanaliongezea pato taifa letu kutokana na kodi anayolipa katika biashara zake “,raisi alizidi kuongea na kutuliza kilio chetu, siku zote aliamini kuwa mzee Jastini alihusika na utengenezaji wa sabuni za kuogea,pamoja na mafuta ya kujipaka. Kumbe sivyo! kiwanda ambacho mzee Jastini alikimiliki kilikua sehemu ya kuficha maovu ya mzee huyu hatari na katili
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kenya;
Siku zote Kendrick alijiamini, hakuogopa kufahamika kuwa alikuwa askari, siku zote alifanya upelelezi wake bila kujificha.Hatimaye kwa msaada wa bodaboda, aliweza kufikishwa katika mitaa ya Kisauni, na kusimama mbali kidogo na jengo la kifahari, jengo ambalo mheshimiwa makamu wa raisi bwana John Owino alikuwa akiishi.
“Hapa sio bure, kuna kitu! Kwanini Yusto aniambie alimuona Rodgers akitokea katika jengo hili la makamu wa raisi, na alienda kufanya nini? “,kijana Kendrick aliendelea kujiuliza maswali, akiwa amesimama umbali wa mita kadhaa kutoka sehemu ambapo jengo kubwa na la kifahari la muheshimiwa raisi lilikuwepo. Aliamua kusogea karibu kabisa na jengo hili, kwa lengo la kufanya uchunguzi zaidi. Kipindi hayo yote yakitokea, wananchi wengi walionekana kumshangaa Kendrick, vazi la kijeshi ambalo lilivaliwa na wanajeshi wa umoja wa mataifa, ndio ambalo liliwafanya watu kumshangaa mpelelezi huyu.
“Danger …!Danger area …!take care! (Hatari …!eneo la hatari …! Kuwa makini!) hatimaye saa ya Kendrick iliweza kutoa sauti, sauti ambayo iliashiria uwepo wa hatari katika eneo ambalo Kendrick alikuwepo. Saa ya Kendrick ilitoa mlio huu wa hatari, baada ya kulisogelea geti kuu la ngome ya John Owino.
“Hapa kuna kitu, lazima niingie ndani, lazima kuna jambo “,fikra za Kendrick zilimsukuma kuingia ndani ya Jengo hili, lakini roho yake ilisita. Hakuwa na jinsi, ilibidi aingie ndani kufanya uchunguzi zaidi, japo saa yake pengine ilitoa mlio huo kutokana na kuhisi siraha ambazo walinzi wa getini ambao wengi walikuwa ni askari wa jeshi la polisi, waliweza kuzishika katika mikono yao na kutimiza majukumu yao ya kumlinda kiongozi wao wa nyazifa za juu serikalini, bwana John Owino.
“Naitwa Kendrick, mpelelezi wa kimataifa, nahitaji kuonana na John Owino ……”,ilikuwa ni sauti ya amli, sauti ambayo siku zote haikuzungusha maelezo. Sauti ambayo ilitoka kwa Kendrick, huku akionyesha kitambulisho chake.
“Bosi hayupo!,njoo wakati mwingine “,askari wale hawakutambua mtu waliyemjibu kauli hii alikuwa ni hatari sana kiasi gani, hawakutambua kuwa alifahamu kuwa bwana John Owino alikuwemo ndani kwa wakati ule kwani ilikuwa mida ya asubuhi sana. Muda mrefu Kendrick alisimama mbali kidogo na jengo hili, na wala hakuweza kuona msafara wowote wa kiongozi huyu ukitoka ndani ya jengo.
Kendrick aliona akiendelea kubishana na askari hawa, malengo yake yasingeweza kutimia. Alikumbuka miwani yake ambayo aliivua, pale alipopanda bodaboda iliyomleta mpaka Kisauni. Miwani yake ndio msaada pekee ambao ungemsaidia kutambua siri ambazo zilikuwemo ndani ya jengo lile.
“Naomba niingie ndani nifanye upelelezi na baada ya dakika kumi nitatoka “,kauli ya busara na upole ilitoka kwa Kendrick, huku akivaa miwani yake machoni na kisha kubonyeza kibatani kilichoruhusu mionzi mikali ya miwani yake.
“Sawa ingia, na kisha utoke haraka baada ya kukamilisha uchunguzi wako “,askari aliyekuwa akiongea na simu, alimruhusu Kendrick kuingia ndani ya jengo la John Owino kwa hasira, mala baada ya simu yake kukata mawasiliano. Hakutambua kuwa miwani aliyoivaa Kendrick, ndiyo chanzo cha simu yake kukata mawasiliano.
………………………………
Mzee Jastini pamoja na John Owino, wanaamua kusitisha shughuli zote ambazo zilikuwa zikiendelea chini ya handaki kubwa. Handaki ambalo lilipatikana chini ya jengo la John Owino. Magari ambayo yalisafirisha madawa kutoka stoo moja mpaka nyingine, yalisitisha misafara yake kwani waliamini Kendrick angeweza kugundua mtikiso huu wa ardhi uliosababishwa na misafara ya magari kisha kuhisi jambo.
Kamera ambazo zilipatikana kila kona ya jengo la John Owino, ziliweza kumuonesha Kendrick akiitembelea ngome yao kwa lengo la kuifanyia upelelezi. Lakini kompyuta zilizima ghafla, walishindwa kutambua chanzo cha kompyuta zao kukata mawasiliano. Hali iliyowafanya kusitisha shughuri zote ambazo zilikuwa zikiendelea ndani ya handaki.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“We can’t see him, there is no network “,(Hatuwezi kumuona, hakuna mtandao), ilikuwa ni sauti kutoka kwa mzungu mmoja raia wa Marekani, mzungu ambaye aliajiriwa na John Owino kwa lengo la kukiongoza kitengo cha mawasiliano katika ngome yake.
“Nazani kila mmoja amesikia, naomba askari wangu wote kamateni siraha, adui akibahatika kuingia humu, kauli ni moja tu ya kumuua “,John Owino, kiongozi wa kundi la EADD alitoa amli, na kisha askari wake kutekeleza amli iliyotolewa na kujiandaa kwa mapambano.
…………………………………
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment