Search This Blog

Friday 18 November 2022

MPANGO WA SIRI - 5

 





    Simulizi : Mpango Wa Siri
    Sehemu Ya Tano (5)




    Muuza mahindi alikuwa jasusi wa kuaminika. Alikuwa ana uwezo mkubwa wa kumsoma na kumuelewa adui. Alimuona vizuri mtu akiwasili na pikipiki mitaa ile. Kumuangalia tu akahisi kitu. Alimtilia wasiwasi muendesha pikipiki, ambaye ndiye alikuwa Inspekta Nyange. Akaanza kumfatilia kwa macho. Alimuona alivyopaki pikipiki nje ya Baa ya Satelite na kuingia ndani ya Baa ile. Adrian aliacha mahindi jikoni kwa mwendo na mavazi yake dhaifu akawa anamfata mtu yule aliyemtilia shaka.



    Kipindi Inspekta Nyange akipewa maelezo na Daniel, Adrian mchoma mahindi alikuwa anawasiliana na Masaga. Kilimchomshitua zaidi ni kumuona mtu wakiyemtafuta jana akiiongea na muendesha pikipiki aliyemtilia shaka kuwa ni Polisi.



    Akamtumia ujumbe mfupi John Masaga.



    “Bosi jamaa karudi tena leo”



    “Yupo wapi?”



    “Satelite Baa”



    “Yuko peke yake?”



    “Yuko na mwenzio anaongea nae,inaonesha huyo mtu ni Polisi”



    “Tunakuja na Lee”



    “Sawa bosi”



    Pale walipokaa Daniel na inspekta Nyange waliona mlango mkubwa wa nyumba wakiyoilenga ikifunguliwa. Walitoka watu wawili. Daniel na Inspekta Nyange walipigwa na mshangao mzito. Watu waliotoka mle ndani Daniel na Inspekta Nyange walimfahamu mmoja, Lee, adui namba moja wa Inspekta Nyange.



    “Mbona kama wanawafahamu Bosi” Ujumbe ulitoka kwa Adrian kwenda kwa Masaga.



    “Kwanini ? ”



    “Nimeona mshangao katika sura zao baada ya kuwaona mmetoka”



    “Subiri, tutafanya kitu”



    Lee na Masaga walipanda gari yao pale nje. Walivyoona wanaondoka Daniel na Inspekta Nyange wakapanda pikipiki wakiwafatilia. Wakati wanaoondoka Daniel aliangalia ile sehemu aliyokuwa anachomea mahindi Adrian, hakumwona,



    ”Kumekucha” alijisemea mwenyewe. Walivyotoka Adrian nae akachukua pikipiki.

    Nae akawafata!



    “Wanawafata kwa pikipiki” Adrian akamtumia ujumbe Masaga.



    “Wote wawili?”



    “Ndio”

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “We upo wapi ?"



    “Nyuma yao na pikipiki”



    “Hakikisha hawakuoni”



    “Haina shida Bosi”



    Sasa walikuwa wanakaribia Bamaga. Wakakata kulia barabara ya Shekilango. Nyuma wakifuatwa na Daniel na Inspekta Nyange, huku kina Daniel wakifuatwa na Adrian mchoma mahindi.

    Mwendo wao haukuwa wa haraka. Ulikuwa wa taratibu sana. kila mmoja akiwa hana haraka na mwenzie.



    “Bado wanatufuata?”



    “Ndio bosi”



    “Sasa tutakata hii njia ya vumbi inayoelekea shule ya Sinza Maalum hapo Sinza mapambano halafu tunaenda kuwaweka mtu kati mbele”



    “Sawa bosi”



    “Kuwa makini”



    “Niko makini Bosi”



    Walipofika Sinza Mapambano wakakata kushoto. Sasa walikuwa njia ya vumbi wakiwa na nia ya kwenda kuweka mtego mbele. Inspekta Nyange aliyekuwa aliyekuwa anaendesha pikipiki machale yalimcheza alihisi kitu



    ”Kuna pikipiki ipo nyuma yetu tangu Tegeta” Inspekta alimwambia Daniel.



    Daniel aligeuka, alimtambua Mchoma mahindi” Usijari ngoja tumuoneshe”



    Wakati kina Masaga na Lee wamekata kulia. Kina inspekta Nyange walikata kushoto. Sasa walimuacha njiapanda Adrian. Alisimama kwenye kituo cha daladala na kumpigia Masaga.



    “Wao wamekata kulia”



    “Wafate sisi tunarudi,hakikisha hawapotei katika macho yako”



    “Sawa Bosi”



    Sasa msafara ulibadilika.Mbele Daniel na Inspekta Nyange, katikakati Adrian Mchoma mahindi, nyuma Masaga na Lee. Wafatiliaji wakawa wanafuatwa wao!



    “Ongeza kasi” Daniel alimuamrisha Inspekta Nyange. Bila ajizi Inspekta akaongeza kasi. Adrian Mchoma mahindi nae akaongeza kasi. Sasa ukawa mkimbizano kweli. Kabla hawajatokea barabara ya Sam Nujoma Inspekta Nyange akakata kushoto, na Adrian naye akakata. Adrian bastola mkononi sasa alidhamiria kuuwa. Wakina Masaga walinyoosha, wakatokea njia panda, kushoto kuelekea Ubungo, kulia kuelekea Mwenge. Hawakuona kitu.

    Hawakujua waelekee wapi?.

    Akamtumia ujumbe Adrian.



    “Mmepita njia gani” Hakujibiwa muda ule.



    Adrian hakusikia mlio wa ujumbe toka kwa Masaga. Yeye damu imeamchemka sasa. Shetani amepanda anataka damu. Akapiga risasi iliwakosa kidogo kina Daniel. Ilipita pembeni kidogo ya pikipiki yao.



    ”Tunashambuliwaaa”Inspekta alipiga kelele.



    ”Tulia”Daniel alijibu kwa sauti ya upole. Akatoa bastola yake mfukoni akageuka nyuma. Wakati anageuka Adrian alirusha risasi nyingine iliyowapita juu ya vichwa vyao. Daniel nae aliamua kujibu mapigo. Alirusha risasi moja iliyopotelea kwenye kifua cha Adrian, Adrian mchoma mahindi.



    Wakarudi eneo la tukio. Walimkuta Adrian ananyang’anyana roho na Izrael, na mtoa roho ndiye aliibuka mshindi.

    Huo ndio ukawa mwisho wa Adrian. Wakampekua mfukoni walimkuta na simu tu ya mkononi na ujumbe mmoja haujafunguliwa.

    Daniel akaufungua.



    “Mmepita njia gani”Ujumbe ulitoka kwa bosi.



    “Wameingia Mlimani city ila wamenipotea” Danny akadanganya.



    “Tunakuja”



    “Sawa Bosi”



    Daniel na Inspekta Nyange wakapanda pikipiki safari Mlimani city.

    Walifika Mlimani city na kubana kwenye gari moja pale ‘parking’



    “Mko wapi Bosi?”Daniel alituma ujumbe.



    “Tunakaribia Mlimani City”

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mulienda Mwenge?”



    “Ndio, mlitupotea”



    “Sawa Bosi, nawasubiri ili tuwamalize vizuri”



    “sawa Adrian kuwa makini”



    “Sawa Mkuu”



    Daniel na inspekta Nyange walikuwa tayari. Tayari kwa kuua.

    Waliliona gari la wakina Masaga ikiingia ndani ya uwanja wa Mlimani city. Ilikuwa ni ileile Range rover. Masaga alikuwa anashuka huku anapiga simu. Daniel hakupokea simu. Ilivyokatika akatuma ujumbe wa maneno.



    “Nipo karibu ya benki ya CRDB hapa mlangoni”



    “Mbona hujapokea simu?”



    “Mazingira niliyopo siyo mazuri Bosi”



    “Poa tunakuja tushafika”



    Masaga na Lee wakawa wanaenda kuingia Mlimani city. Mikono mfukoni bila shaka walikuwa wameshikila bastola. Daniel na Inspekta Nyange wakawa wanawafata kwa nyuma wakiwa wananyatia. Daniel alikuwa mkabala na Masaga na Inspekta Nyange alikuwa mkabala na adui yake namba moja duniani, Lee.







    Waliwavamia kwa kasi kwa nyuma wakawakaba shingoni kwa mkono mmoja huku mkono mwengine ukishika mkono wa adui ule ulioshika silaha. Ilikuwa patashika ndani ya viwanja vya Mlimani city. Hizo roba zilikuwa roba zilizoshiba. Lee alianza kuishiwa nguvu wakati Masaga alikuwa ngangari kidogo.



    Mara walinzi kutoka kampuni binafsi walifika eneo la tukio. Wakawa wanawaonesha silaha zao bila kujua adui nani?Wanaume walikuwa hawaongei, hawa wanakandamiza roba, hawa wanajitahidi kuzitoa.



    “Halo”



    “Halo”



    “Tunaomba msaada wa Polisi”



    “Wapi?”



    “Mlimani city”



    “Kuna nini ?”



    “Majambazi tunahisi”



    “tunakuja”



    Mkuu wa ulinzi pale Mlimani city aliomba msaada kituo cha Polisi .Ndani ya dakika kumi Polisi walifika. Waliwakuta wanaume wako vilevile. Polisi walimtambua Daniel Mwaseba. Sasa wakawa wanatafuta namna ya kumuokoa. Ilikuwa hatari, kosa dogo tu lingesababisha kifo.



    Lee akaona hawezi kukamatwa kikondoo vile. Alijivuta mbele halafu alijirudisha nyuma kwa nguvu. Alimpiga Inspekta Nyange kichwa cha kinyumenyume, Inspekta aliachia ile kabali.



    Sasa walikuwa wanatazamana uso kwa uso.



    Inspekta Nyange alilikumbuka pambano lake la awali na Lee kule Kilwa Kisiwani.

    Wasakana wapatana!



    Polisi sasa walifanywa kuwa mashuhuda wa mpambano wa Inspekta Nyange na Lee. Wakiwa wamewaelekeza bunduki watu wale. Kichwa kile cha ghafla alichopigwa Inspekta Nyange. Daniel naye aliangalia kilichomkumba mwenzie. Alipoteza umakini kidogo. Lilikuwa kosa, Masaga alirudisha mkono kwa nguvu kiwiko !

    Daniel alipigwa kipepsi takatifu cha shavu.



    Kule upande wa Lee patashika ilikuwa imeanza, Lee aliruka juu kama paka na akawa anataka kutua katika kichwa cha Inspekta Nyange. Alimkuta Inspekta Nyange yuko imara safari hii, alimkwepa na Lee kufika kwenye ‘tiles’ za Mlimani city. Alipofika chini Lee hakuchelewa. Alimbutua teke moja kama anabutua mpira. Teke lilimpata Lee vizuri usoni. Alivyotua chini alijikuta yupo chini ya ulinzi. Askari wawili walimuwahi pale chini. Wakamfunga pingu kwa nyuma.



    Masaga nae akawa anataka kupimana nguvu na Daniel. Hakujua kama Daniel ni kiboko yao. Alirusha teke, likadakwa na mkono wa kuume wa Daniel. Daniel akaupinda ule mguu kwa nguvu ukastuka!

    Masaga alikuwa dhaifu sasa kutokana na maumivu ya mguu. Daniel alimpiga teke lilitua kwenye goti. Masaga alilia. Naye alifungwa pingu na wale askari.



    Masaga na Lee sasa waliwekwa katika gari la Polisi. Safari kituo kikuu cha kati cha Polisi.



    ”Tangulieni nao sisi tunakuja” Daniel aliwaambia wale askari Polisi. Daniel na Inspekta Nyange wakapanda pikipiki yao wakawa wanasindikiza msafara ule. Dereva wa pikipiki sasa alikuwa Daniel Mwaseba.

    Walipelekwa Kituo cha Polisi cha Kati.



    Baada ya kuandikishwa kila kitu walipelekwa selo. Kila mmoja akiwekwa selo yake.



    Taarifa za kukamatwa kwa Masaga na Lee zilifikia Mkurugenzi wa Mpango huu Ndugu Andrew Chikoka kupitia taarifa ya habari. Tangu kupata habari ile Chikoka alichanganyikiwa sana. Akapata wazo la kumpigia mtu anayeweza kumsaidia.Sasa aliona mipango yao yote inaenda kombo sababu akiwa ni Daniel Mwaseba. Ingawa taarifa ya habari ile haikueleza Masaga na Lee wamekamatwa na nani. Ila alijua ni Daniel lazima atakuwa anahusika kwa namna yoyote ile.



    “Halo”



    “Nambie Bwana Chikoka”



    “Hali siyo salama,umeangalia taarifa ya habari”



    “Hapana, nipo kijijini kwetu huku hata runinga hakuna,kuna nini?”



    “Mambo yameharibika Mheshimiwa”



    “Kuna nini tena? ”



    “Masaga na Lee wamekamatwa na askari wako”



    “Nini?”



    “Wamekamatwa kamanda Mahiwa,na tunavyoongea wapo central”



    “Imekuwaje mpaka wamekamatwa?”



    “Ni Daniel Mwaseba mkuu”



    “Kwahiyo unataka msaada gani?”



    “Uwaamrishe askari wako wasiwafanye chochote mpaka urudi wewe”



    “Sawa haina shida”Simu ikakatwa. Sasa Andrew Chikoka alijisikia afueni kidogo. Maana alijua kina John Masaga wakiteswa na Polisi lazima watamtaja.

    Muda uleule Kamanda wa kanda Maalum ya Dar es salaam akapiga simu kituo cha kati cha polisi.



    “Halo”



    “Unaongea na kamanda Mahiwa”



    “Shikamoo mkuu”



    “Kuna taarifa gani mpya ? ”



    “Zipo nyingi afande”



    “Zinazomhusu John Masaga kafanya nin ?”



    “Tumeambiwa tusizungumzie kesi hii”



    “Mimi sindo kamanda mkuu wa mkoa ? ”



    “Ni agizo toka kwa mkuu wa Polisi Nchini”



    “Nani anaichunguza kesi hiyo ?”



    “Ni Daniel Mwaseba”



    “Kashaongea na Watuhumiwa ? ”



    “Tumeambiwa tusitoe taarifa yoyote na IGP”



    “Acha ujinga, unajua mimi ni mkuu wako ?.Nipe taarifa kuna zawadi yako nikirudi”



    “Zawadi gani mkuu ?”



    “Nitakupeleka kusoma na milioni tano zitakuwa kwenye akaunti yako ya benki”



    “Sawa mkuu Daniel ashawahoji watuhumiwa wote”



    “Wametoa maelezo gani ? ”



    “Hawajasema kitu,wamekuwa wagumu kusema”



    “Sawa afande nipe namba yako ya mkononi uwe uananipa maendeleo ya kesi hiyo”



    “071226444….”



    “Ni afande nani?”



    “Naitwa DANIEL MWASEBA!”



    Kamanda Mahiwa alitupa simu yake chini. Alianguka chini kwa Shinikizo la damu palepale. Hakuamini kama kajikamatisha kirahisi namna ile. Aliipa kazi familia yake kwenda kuchota maji kisimani kuja kummwagia.





    Ule upande wa pili kituo cha Polisi hawana mbavu.Simu ile iliwekwa katika mtindo wa ‘loud speker’ na simu ile kurekodiwa pia. Alichoongea Kamanda Mahiwa kilisikika na Jopo la watu watatu, na kilirikodiwa kwa ajili ya kumbukumbu. Kulikuwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini(IGP) John Rondo, Mkuu wa Jeshi la Wananhi Nchini, Festo Ndunga na kijana machachari aliyekuwa anaongea na simu ile Daniel Mwaseba.



    Daniel ndie aliyetoa wazo la kurekodi simu ile. Baada ya Masaga kukamatwa alijua lazima Kamanda Mahiwa atafanya kitu. Alikuwa anaujua vizuri urafiki wa Masaga na Kamanda Mahiwa. Kuhusika kwa Masaga na kadhia lile alijua moja kwa moja na Kamanda Mahiwa atakuwa anahusika kwa namna moja ama nyingine. Na simu ile iliwajulisha kitu.



    Inspekta Jenerali wa Polisi alimsifu sana Daniel Mwaseba.



    ”Wewe siyo mpelelezi namba moja Tanzania, wewe ni mpelelezi namba moja Afrika nzima, Tanzania tuna kila sababu ya kujivunia kuzaliwa wewe katika nchi hii” IGP John Rondo kuanzia siku ile alimheshimu sana Daniel.



    Muda wa kwenda kuwahoji waarifu ulifika, ni Daniel ndiye alikuwa na jukumu lile. Chumba cha mahojiano kilizungushwa kamera. Watu waliokuwepo katika ofisi ya IGP Rondo walikuwa wanaona na kusikia kila kitu kilichoongelewa ndani mle.



    Askari wawili walimbeba Lee na kumpeleka katika chumba cha mahojiano. Walimuweka katika kiti cha kawaida cha mbao. Lee alikaa pale akiwa haoni chochote. Alikuwa amefungwa kitambaa cheusi usoni.



    ”Mfungueni” Daniel aliamuru. Akafunguliwa. Mfungueni na pingu, wale askari wakawa wanamwangalia Daniel kwa mshangao. Hawakutegemea kama wataambiwa kauli namna ile, wao wenyewe na pingu zake walikuwa wanamuogopa Lee. Askari walimfungua pingu Lee.

    Wakatoka nje ya chumba kile maalum cha mahojiano wakiwaacha watu wawili tu ndani.

    Danel Mwaseba na Lee Technics!



    “Naitwa Daniel Mwaseba”

    Lee hakujibu,aliendeleza tabia yake ya ububu.



    “Naitwa Daniel Mwaseba wewe waitwa nani?”



    Lee kimyaaa !



    “Jina lako nani ? ”



    Lee anamwangalia tuu.

    Daniel akanyanyuka kwenye kiti chake akamsogelea Lee. Wakawa wanaangaliana.



    “Unaitwa nani?”Alimuuliza kwa ukali sasa

    Lee akavuta kohozi refu. Akamtemea Daniel usoni. Daniel akachukua kitambaa akajifuta.

    Daniel akasimama wima, na Lee akasimama wakawa wamekaribiana sana kiasi vifua vyao vimegusana. Kule ndani IGP Rondo akasema leo kazi ipo!



    Lee alijirudisha nyuma kidogo akapiga kichwa cha nguvu. Alikuta Daniel kakomaza kichwa,aliumia mwenyewe.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Sitaki kuwasumbua wahudumu kuja kudeki damu yako humu ndani”Daniel alionya.

    Kule kwa IGP Mbavu hawana. Lakini Lee alikuwa kimya!



    Lee alikuwa kishari zaidi. Daniel hakutaka shari hakutaka kupigana alikuwa anataka maelezo. Lakini Lee alikuwa anamlazimisha Daniel apigane.



    “Rafiki unapenda kuendelea kuvuta hewa nzuri ya duniani ?”



    Lee anamwangalia tu!



    “Naomb…..”Hakumalizia kuzungumza Lee alirusha ngumi kali iliyotua barabara katika bega la Daniel. Daniel akaona ngoja amuoneshe kilichomtoa kanga manyoya.

    Daniel alipiga mapigo mfululizo hakuna aliyejua kapiga kwa kiungo gani cha mwili wake. Alipiga mapigo matatu mfululizo yaliyomuacha Lee akiwa chini anavuja damu.Pigo alilopiga Daniel linaitwa ‘kificho’.Unapigwa kwa kasi ya haraka kama umeme na kumuacha na mshangao mpigwaji na muangaliaji.Pigo la ‘kificho’ wanatumia sana wapiganaji wa Thailand.



    Kule kwa kina IGP Rondo hawakuelewa nini kimetokea. Walimuona Mtuhumiwa akianguka chini akiwa anatokwa damu.Daniel alienda kwenye kabati pekee lililokuwepo ndani ya chumba kile. Akachukua bisibisi na spana.



    “Naomba ujibu maswali yangu kabla sijakufungua kiungo kimoja kimoja”



    Lee alijifanya jeuri. Alikuwa anamsikia tu Daniel. Kwa nguvu na haraka alipitisha ile bisibisi jichoni kwa Lee. Jicho lilikuwa linatoa majimaji. Akapeleka ile spana jichoni halafu akaiacha inaning’ing’inia.

    Lee alikuwa analia kama mtoto mdogo, lile pigo la kificho alilopigwa lilimmaliza nguvu kabisa ukichanganya na mateso haya?.



    ‘Bora uniue tu kuliko mateso haya” Lee ububu ulimuisha.



    “Nimekuja kutesa siyo kuua “

    Daniel alikomaza mkono akitaka kupeleka bisibisi kwenye jicho la pili.



    “Noo nitasema kila kitu”



    “Sawa”



    Daniel alibonyaza swichi moja mule ndani,wakaja madaktari wawili.Wakaanza kumtibia Lee. Daniel alitoka nje.

    Baada ya saa moja mahojiano kati ya Daniel na Lee yalianza. Lee aliongea mambo yaliyowashangaza sana Daniel pamoja na jopo lililokuwepo kule ndani!



    “Naitwa Daniel Mwaseba”



    “Naitwa Zedi Nungwi “



    “Una miaka mingapi ?”



    “35”



    “Kabila ?”



    “Mmatumbi”



    “Unaelewa nini juu ya Mchezo mchafu ?”



    “Ni mchezo wa kuwauwa watu wote wanaokwenda kunyume na sisi”



    “Nyinyi ni akina nani ?”



    “Ocafona army”



    “Nani muasisi wa Mchezo mchafu ?”



    “Mimi”



    “Mlikuwa munauwa vipi watu kwa kutumia mchezo mchafu ?”



    “Tunakatakata vipande na kutoa utumbo”



    “Mpango wa siri ni nini ?”



    “Ni mpango wa kuwakomboa watu wa mkoa wa Lindi”



    “Kuwakomboa dhidi ya nini ?"



    “Uonevu toka Serikalini”



    “Kama uonevu gani ?”



    “Mkoa wa Lindi kuwa nyuma katika huduma za afya”



    “Nani muasisi wa mpango huu ?”



    “Mimi sijui, ila nimeajiriwa kazi na John Masaga”



    “Masaga ndio nani ?”



    “Yule tuliyekamatwa naye”



    “Kuna uhusiano gani kati ya mpango wa siri na Mchezo mchafu ?”



    “Mchezo mchafu niliubuni mimi, lengo ni kuwauwa watu wote wanaufatilia Mpango wa siri”



    “Kama ulivyoelezwa mpango huu ulikuwa na lengo zuri kuwasaidia watu wa Mkoa wa Lindi, ingawa njia mlizotumia siyo sahihi, sasa kwanini uitwe mpango wa siri?”



    “Mimi sijui hilo jina mimi nimepewa hivyohivyo”



    “Mkuu wa mpango huu ni nani ?”



    “Mimi nilikuwa naripoti kwa John Masaga,naye alikuwa anaripoti kwa Mkurugenzi’



    “Mkurugenzi anaitwa nani ?”



    “sijui”



    “Sawa nashukuru kwa ushirikiano wako. Lee au Zedi Nungwi kama alivyojitambulisha alirudishwa selo.



    Sasa aliletwa Masaga. Uzuri wa Masaga hakuwa bubu, alimwaga mchele wote bila kuguswa hata na wembe.



    “Habari bwana Msaga ? ”



    “Nzuri”



    “Sina haja ya kukutoa jicho kama mwenzio, ukweli wako ndio usalama wako”



    “Sawa”



    “Naambie nani Mkurugenzi wa Mpango wa siri ?” Daniel aliamua aanzie hapo maana mengine yote ashayapata kwa Lee.





    “Naambie nani Mkurugenzi wa Mpango wa siri ?”Daniel aliamua aanzie hapo maana mengine yote ashayapata kwa Lee.



    “Bosi mimi simjui”



    “Wewe bosi wako nani? "

    Masaga akasita.



    “Hatuna siku mzima hapa !”



    “Bwana Chikoka”



    “Chikoka yupi ?”



    “Mkuu wa wilaya wa zamani wa Bagamoyo”



    “Mpango wa siri upo chini ya nani ?”



    “OCAFONA”



    “OCAFONA ndio nini ?”



    “mimi sijui”



    “Nani kiongozi wa Ocafona ?”



    “Simjui”



    Daniel akaona huyu naye hakuwa anayajua mengi, aliingia katika mpango asioujua vizuri. Sasa Daniel shabaha yake ilikuwa kumpata Bwana Chikoka na Kamanda Mahiwa. Akajua akiwanasa hao itakuwa kaumaliza mchezo.

    Alitoka nje akakutana na Inspekta Nyange.



    “Inabidi twende kwa IGP Rondo Inspekta”



    “Sawa ila naombi moja Daniel”



    “Nakusikiliza Inspekta”



    “Nipe hata dakika kumi nikamuoneshe Lee”



    “Sio utaratibu kaka, mtuhumiwa kaeleza kila kitu sasa wewe utaenda kumtesa kwa lipi?Tuache sheria ichukue mkondo wake”



    “Daah sawa afande”



    “Lakini umemuona Lee lakini sahivi ?”



    “Hapana”



    “Ana jicho moja”



    “Nani kamtoa lengine?”



    “Mimi”



    “Daah afadhali kidogo nasikia faraja”



    Daniel na Inspekta Nyange waliingia kwa mkuu wa polisi nchi. IGP Rondo aliwasifia sana kwa kazi nzuri.



    “Sasa ndio muda wa kuimaliza hii kazi.Lazima tuhakikishe Chikoka na Mahiwa tunawakamata. Suala la nani atakwenda wapi nakuachia wewe Daniel. Sisi kama Polisi tutawapeni msaada wowote ule munaoutaka. Semeni mnataka nini kukamilisha operesheni hii”



    “Hakuna tunachohitaji zaidi ya dua zenu” Daniel alijibu kwa kujiamini. Baada ya maagano wakatoka nje. Walipofika nje waligawana majukumu. Daniel kwenda kumkamata Bwana Chikoka. Na Inspekta Nyange kwenda kumkamata Kamanda Mahiwa. Walitakiana kila la heri. Walipeana mkono. Huo ndio ulikuwa mkono wao wa mwisho kushikana!



    ****



    Daniel alielekea Bagamoyo kwa mkuu wa wilaya wa zamani wa Bagamoyo, wakati Inspekta Nyange akienda kijijini Mchinga kwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Dar es salaam Bwana Mahiwa. Wote walikuwa wanawafata watu waliokuwa wanawajua washiriki wanaojua siri za mpango huu. Sasa wakina Daniel walikuwa wamesogelea jibu kwa asilimia nyingi, lakini pia walikuwa hawajui wanakisogelea kifo pia!

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kikao cha siri na dharura kilikuwa kinafanyika katika nyumba cha Waziri Mkuu. Kilikuwa kikao cha siri kweli ambacho haikutakiwa mtu asiyehusika kusikia maneno kuhusu kikao kile. Hakukuwa na mke, watoto wala ndugu yeyote katika nyumba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu Abdallah Kilumbaki kupisha kikao hiki. Wote walitolewa makusudi kupisha kikao hiki.



    Kilikuwa kikao muhimu kwa mustakhabari wa Mpango wa siri.Waliona mipango yao inaenda halijojo. Ililazimu kuitishwa kikao hiki ili kuunusuru mpango wao. Na kunusururu maisha yao pia. Usalama kuhusu maisha yao ulikuwa hatarini na ukamilifu wa Mpango wa siri ulikuwa mashakani.Kilikuwa lazima kikao cha siri na haraka kiitishwe ili wapange nini cha kufanya ?.



    Kukakamatwa kwa Lee na Masaga kuliwapa wasiwasi mkubwa sana. Waliona sasa mtandao wao wote upo njiani kujulikana. Hawakuwa wanamuhofia sana Lee, walijua Lee ni mtoto mtukutu anayeweza kuvumilia mateso makali ya Polisi. Pia Lee hakuwa anajua taarifa nyingi kama ajuavyo Masaga. Hivyo kukamatwa kwa Masaga kuliwaumiza zaidi. Kamanda Mahiwa ndio alichanganyikiwa zaidi. Yeye ndiye aliyekuwa anajulikana na Masaga. Na alijua kwa vyovyote Masaga atamtaja.

    Simu aliyopigiwa Kamanda Mahiwa siku jana yake na mtu aliyejitambulisha kama Daniel Mwaseba ilimkondesha sana. Baada ya kupokea simu ile hakujua kilitokea nini, lakini habari alizosimuliwa na mtoto wake wa mwisho kuwa baada ya simu ile alianguka. Alikimbizwa hospitali na kufanikiwa kuamka ndani ya masaa mawili. Hakuna aliyejua sababu ya kuanguka kwa Kamanda Mahiwa kule kijijini Mchinga zaidi ya yeye mwenyewe.



    Saa moja mbele alipokea simu toka kwa Waziri mkuu ikimtaka kuwahi kikao cha dharula kesho asubuhi. Ilibidi aombe ruhsa hospitali na kwenda uwanja wa ndege wa Lindi, bahati ilikuwa yake alipata nafasi katika ndege ya saa mbili usiku na kuwahi kikao kitakachofanyika kesho yake.



    Kamanda Albert Mahiwa hakuondoka hivihivi. Nyuma aliacha wafuasi ambao aliwapa amri ya kumuua mtu yeyote atakayeonesha nia ya kumfatilia. Vijana wale aliwaweka nyumbani kwake. Inspekta Nyange alinasa katika mtego huo. Alipofika kijijini Mchinga moja kwa moja aliulizia nyumba ya Kamanda Albert Mahiwa. Kutokana na umaarufu wa Kamanda hakupata shida kupajua. Alimuuliza dereva mmoja tu wa bodaboda na kumpeleka moja kwa moja nyumbani kwa Albert Mahiwa.

    Huko ndipo kifo cha kupigwa risasi tatu za mgongoni kilipomkuta. Alienda vizuri pale nyumbani kwa Albert Mahiwa. Kwa bahati mbaya aliwakuta wale vijana waliowekwa na Kamnda Mahiwa, waliwekwa kwa makusudi, kuhakikisha wanamuua mtu yeyote watakayemtilia shaka atakayekuja kumuulizia Kamanda Mahiwa. Vijana wale wahalifu wazoefu katika mkoa wa Lindi, walimtilia shaka Inspekta Nyange. Wakati anaondoka baada ya kumwambia Kamanda Mahiwa katoka kidogo, walimshindilia risasi tatu za mgongo.Na kuyakatisha maisha ya askari yule muaminifu kwa jeshi la Polisi na Serikali kwa ujumla.







    Hiki kilikuwa kikao kikubwa zaidi tangu mpango huu uanze. Kikao kilichosababisha washiriki wengine wasiojuana leo wajuane. Kikao kilipangwa kiwakutanishe watu kumi muhimu wa mpango huu. Wazungu wanne wenye asili ya nchi ya Ujerumani. Wazungu wanaotoka katika familia moja. Dickson Lambart, Allen Lambart, John Lambart, Alex Lambart. Hawa ndio walikuwa waasisi wa mpango huu, na waasisi wa kundi hatari la mauaji likilojulikana kama Ocafona Army.



    Kikao kile alikuwepo mtu wa tano, mtu mwenye dhamana na heshima kubwa katika serikali ya Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Abdallah Kilumbaki. Kikao pia kiliwakutanisha mawaziri wanne, ambao nao bila kujitambua waliingia kwenye mpango huu wa siri.



    Kulikuwa na Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Mheshimiwa Haridi Buto, Waziri wa Ulinzi na jeshi la kujenga Taifa, Mheshimiwa Zaidi Njame, Waziri wa Ujenzi Dr Wahabu Nyamzungu na Mwanamama pekee aliyekuwa anashiriki katika mpango huu kwa ngazi za juu, Mheshimiwa Dr Kazija Juma.

    Watu hao walikamilisha idadi ya watu kumi.



    Katika viti vilivyoizunguka meza yao kubwa. Wao walihisi walikuwa watu kumi. Lakini hawakuwa kumi. Kulikuwa na mtu wa kumi na moja. Mtu aliyeingia mkutanoni kabla ya watu wote kufika. Mtu ambaye alikuwa fundi mitambo katika chumba cha mkutano ule, ili kuhakikisha habari na maelezo ya mkutano ule vinafika moja kwa moja Ikulu tukufu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mtu huyu alijulikana kama Daniel Mwaseba. Mtoto wa kinyakyusa mwenye mbinu za hali ya juu za kijasusi. Yeye hakutaka kiti katika mkutano ule. Alijilaza vizuri juu ya dari kuhakikisha anaona na kusikia kila kitu labda ambacho hakitasikiwa na kinasa sauti alichokitega mle Mkutanoni au kuonwa na kamera mbili alizozitega mule ndani.



    Ilikuwa hivi..



    Wakati Inspekta Nyange alienda kuuwawa kule Mchinga. Daniel Mwaseba alienda kupata mambo ya siri huko Bagamoyo nyumbani kwa Bwana Chikoka. Kiasili Chikoka alikuwa mwenyeji wa mkoa wa Lindi lakini alikuwa amepazoea sana Bagamoyo. Alifanya kazi ya Ukuu wa Wilaya katika Wilaya ya Bagamoyo kwa miaka tisa. Alikuwa kama mzawa wa wilaya ile.



    ****



    Safari ya Daniel Mwaseba ilimfikisha hadi Bagamoyo. Miongoni mwa miji ya Kihistoria ndani ya nchi ya Tanzania. Hakumuuliza mtu mahali anapokaa Bwana Chikoka. Alikuwa anapafahamu. Alifika mapema sana, lakini alisubiri giza liingie ili akavamie nyumbani kwa Chikoka. Alipoteza muda kwa kwenda Pwani kubarizi. Chikoka alikuwa anakaa nyumba bora na ya kisasa mtaa wa Magomeni, nyumba ikiyolindwa na walinzi watano kutoka kampuni binafsi ya ulinzi saa ishirini na nne. Daniel hakupita mlangoni. Alizunguka nyuma ya nyumba ya Bwana Chikoka. Alipanda ukuta mrefu wa Bwana Chikoka bila kuonekana. Akaruka upande wa pili na kuingia ndani. Ndani kulikuwa na taa zikizowaka vizuri, taa maalumu kwa ajili ya ulinzi.



    Kishindo alichotua nacho Daniel wakati anatua chini kilimshtua mlinzi mmoja. Akawa anaenda upande ule aliokuwepo Daniel. Daniel aliingia kwenye pipa tupu lililokuwepo karibu na pale aliposhukia. Yule mlinzi alifika hadi pale kwa mwendo wa kujiamini huku akivuta sigara. Akaangaliaangalia hakuona kitu. Akawa anaondoka huku akipiga mluzi. Alipogeuka ilikuwa faida kwa Daniel. Alimpiga karate ‘lala’ na yule mlinzi alianguka chini. Akambeba na kwenda kumuhifadhi kwenye lile pipa tupu lililokuwa ficho lake hapo mwanzo. Karate ‘lala’huwa inamlaza usingizi mpigwaji masaa yasiyopungua tisa.

    Daniel alijikohoza kidogo.



    ”Na wewe Ben sigara zitakuuwa hizo” Mlinzi mmoja alikuwa anaongea huku anakuja upande aliokuwepo Daniel. Daniel akajua kumbe yule mlinzi aliyegeuka maji ndani ya pipa alikuwa anaitwa Ben, kiuwezo hakufanana hata robo na Ben Kiroboto lakini.



    Yule mlinzi alikuwa anakwenda bila uwoga akiamini upande ule atakutana na Ben. Alipofika alishikwa na bumbuwazi. Hakumuona Ben bali kiumbe kingine kabisa. Daniel alirusha kisu kiustadi kilichotua kifuani kwa yule mlinzi. Alikufa akiwa na butwaa yake na mguno kidogo. Mguno uliowastua walinzi wawili. Mmoja alitokea upande wa kushoto na mwengine upande wa kulia. Daniel alitoa Bastola zake mbili zenye kiwambo cha kuzuia sauti. Risasi moja ilitua katika kifua cha mlinzi aliyekuwa anatokea upande wa kulia, na risasi ya pili ilitua katika utosi wa mlinzi aliyekuwa anatokea upande wa kushoto. Risasi zilipigwa muda mmoja.Bila Daniel kuwaangalia walinzi wale. Yeye alikuwa anaangalia mbele !Walienda kuzimu walinzi wale wakiwa na bunduki zao mabegani mwao.



    Sasa Daniel akawa anaelekea upande wa mbele wa nyumba ile. Alimuona mlinzi mmoja akiwa mlangoni amekaa kwenye kiti. Ameivuta kofia yake hadi usoni. Bila shaka alikuwa amesinzia. Kwa mwendo wa kunyatia alimsogelea yule mlinzi. Alimpiga karate moja ya shingo. Mlinzi yule hakuwa Devotha aliyeweza kuistahamili karate kama ile. Mlinzi yule alienda kuzimu akiwa usingizini.



    Daniel alingiia ndani. Alifungua mlango wa ukumbini taratibu. Akajikuta amefika kwenye sebule kimya. Kwa mbali alisikia mtu akiongea na simu. Daniel kwa mwendo wa kunyata akaenda kwenye kile chumba ambacho alisikia mtu anaongea na simu. Akabana mlangoni kusikiliza maongezi yale.



    “Mtafanya kesho saa ngapi ?”



    “Kitafanyika wapi?”



    “eeeh”



    “Bora kaka hali ishakuwa mbaya”



    “Tunaweza,tukimdhibiti tu”



    “Mtawaita na mawaziri?”



    “Bora tujuane”



    “Basi nitakutafuta kesho baaada ya kikao”



    “sawa,haina shida”



    Bwana Chikoka akaweka simu yake mezani. Akaa kwenye sofa dogo mule chumbani akichezea ngamizi mpakato yake. Daniel alijaribu kuufungua mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani na funguo. Akaamua kupiga hodi.



    “Ngo ngo ngo”



    “nani ?”



    “Ben”



    Akasikia hatua za mtu zikija mlangoni. Akaona kitasa kinazunguka ishara ya mlango kufunguliwa. Alivyofungua tu mlango walizama wote ndani. Bwana Chikoka akakutana na Daniel Mwaseba!!

    Akasikia hatua za mtu zikija mlangoni. Akaona kitasa kinazunguka ishara ya mlango kufunguliwa. Alivyofungua tu mlango walizama wote ndani. Bwana Chikoka akakutana na Daniel Mwaseba !



    “Naitwa Daniel Mwaseba”



    “Adabu gani ya kuingia nyumba ya mtu namna hiyo”



    “Nimefata majibu ya maswali mawili tu”



    “We mtoto wewe!”



    “Kikao kitafanyika wapi?,na saa ngapi ?”



    “Kikao gani mbona unaniuliza mambo nisiyoyaelewa?”



    “Kikao kitafanyika wapi? Na saa ngapi?”



    “Wewe mtoto utakuwa mwehu!”

    Akajibiwa na ngumi yenye uzito wa wastani ya tumbo.



    “Saa nne asubuhi nyumbani kwa waziri mkuu”



    “Geuka nyuma”



    Akageuka.



    “Nyosha mikono kwa nyuma”

    Akanyoosha.



    Daniel Mwaseba akamfunga pingu bwa Chikoka na kurudi naye Dar es salaam usiku uleule.



    Saa tano ya usiku ilimkuta Daniel kituo cha kati cha Polisi akimkabidhi Bwana Chikoka pale Polisi.

    Akatoka nje, akabofya namba fulani akawa anasikiliza, simu upande wa pili ikapokelewa.



    “Halo mkuu”

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sema Daniel”



    “Mambo safi mkuu”



    “Umemkamata Chikoka ?”



    “Yuko selo sasahivi”



    “Mambo ya Mchinga umeyasikia ?”



    “Hapana mkuu”



    “Inspekta Nyange ameuwawa kwa risasi”



    “Aisee Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Alikuwa askari mtiifu na mzalendo kwa nchi yake. Hakika pengo lake haliwezi kuzibika”



    “Kweli kabisa Daniel”



    “Sasa bosi kesho tunaumaliza mchezo. Nataka tuumalize kabla Inspekta Nyange hajazikwa ili iwe heshima kwake na kwa wote waliotangulia katika harakati za mchezo huu”



    “Mpango ukoje ?”



    “Kesho saa nne kuna mkutano wao”



    “Wapi?”



    “Kwa waziri mkuu”



    “Waziri mkuu!”



    “Ndiyo nae ni mshirika wao”



    “Mimi sahivi naenda Ikulu kurekebisha mambo. Nataka muone kikao chao mkiwa na Mheshimiwa raisi ‘Live’Baada ya hapo nitaenda nyumbani kwa waziri mkuu kufanya mambo yangu. Kesho kabla ya saa nne uwe ikulu”



    “Ama kwa hakika sijawahi kuona kijana kama….”



    Alikuwa anataka kumsifia simu ikakatwa, Daniel aliona huu siyo muda wa kusifiana. Huu ni muda wa kazi! IGP Rondo alibaki anacheka mwenyewe.

    Daniel alienda Ikulu na kuunga vitu vyake. Saa saba kamili usiku alikuwa anatoka Ikulu anaelekea nyumbani kwa waziri mkuu. Hakukuwa mbali sana. Hakupata shida kuingia. Waziri mkuu alikuwa ameisafirisha familia yake yote kijijini kwao kupisha Mkutano wa kesho. Hata walinzi wake aliwapa ruhusa akidai hatolala pale siku ile. Alibaki Mbwa tu mmoja ambaye alikuwa anaifahamu vizuri harufu ya Daniel. Ni Daniel ndiye aliyemfundisha mbwa Yule kutambua harufu za wahalifu. Mbwa yule hakupiga kelele kabisa.

    Kwa kutumia funguo Malaya, Daniel alifungua mlango wa mbele wa nyumba ile. Alienda kwenye chumba cha Waziri mkuu na kupulizia dawa ya usingizi. Waziri mkuu alilala usingizi mnono huku Daniel akifanya yake. Aliweka kamera mbili kwa siri na kinasa sauti katika chumba cha mikutano. Akaweka vitu katika viti vyote kumi.Baada ya kumaliza akapanda juu ya dari kuisubiri kesho saa nne asubuhi, alilala juu ya dari siku ile.



    ***

    Wakati watu kumi wakianza kikao nyumbani kwa Waziri mkuu. Jopo la watu sita walikuwa Ikulu wakiangalia runinga. Wote walikuwa na hofu juu ya watakachokuja kukiona mbele yao.



    Alikuwako Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa David Lugongo. Makamu wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Baraka Izack, Raisi wa Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar Mheshimiwa Ally Jabir, Mkuu wa jeshi la Wananchi Tanzania, Festo Ndunga, Mkuu wa jeshi la Polisi Tanzania, John Rondo. Pamoja na spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dina Joshua.



    Nyumbani kwa Waziri mkuu kikao kilianza Waziri mkuu mwenyewe ndiye alikuwa mwenyekiti wa kikao.



    “Hiki ni kikao cheti kikubwa zaidi tangu tuanze harakati za kufanikisha Mpango huu wa Siri. Wengine ndio kwanza tunaonana leo, kwahiyo nachukua fursa hii kukaribisha kila mmoja kusimama kujitambulisha ili ajulikane na mwenzie”

    Alianza kusimama mzungu mmoja.



    “Naitwa Dickson Lambart,ni raia wa Ujerumani, na ni Raisi wa jeshi la siri lijulikanalo kama Ocafona. Na ni muasisi wa Mpango huu wa siri”.Mzungu Yule aliongea kwa Kiswahili sanifu na fasaha. Ingawa alikuwa na lafudhi ya kizungu.



    “Naitwa Allen Lambart, ni raia wa asili wa nchi ya Ujerumani, pia ni makamu wa Raisi wa jeshi la siri duniani liitwalo Ocafona.



    “Naitwa Alex Lambart ni raia wa Ujerumani, pia ni mkuu wa wanajeshi wote wa jeshi la Ocafona”



    “Naitwa John Lambart ni Mwenyekiti wa mipango na uchumi wa Jeshi la Ocafona”

    Baadae walijitambulisha wale mawaziri watano, na kumpa nafasi mwenyekiti aendelee na kikao.



    “Nashukuru sana ndugu wajumbe kwa utambulisho wenu, kikao chetu ni kifupi sana,na utekelezaji wa tutakachoamua utaanza muda mfupi baada ya kuinuka katika viti vyetu. Waheshimiwa Mawaziri hawa munaowaona ndio waasisi wa mpango huu wa siri. Kikao chetu kitakuwa na ajenda kuu tano. Ajenda zitakuwa kama ifuatavyo.



    1. Kufungua kikao.

    2.Kuutambulisha Mpango wa siri kwa wasioufahamu vizuri.

    3.Kumuua Daniel Mwaseba.

    4.Kutekeleza mpango kazi.

    5.Kufunga kikao.



    Waheshimiwa Mawaziri, Mpango kazi ni mpango ulioasisiwa na ndugu Dickson Lambart kwa ajiri ya kunyonya maliasili iliyogunduliwa huko mkoani Lindi. Kama mjuavyo Mkoa wa Lindi, wilaya ya Kilwa katika Visiwa vya Songosongo na Nyuni kumegundulika kuwepo kwa gesi nyingi sana ya asili. Hivyo mpango huu una dhumuni la kwenda kuwashawishi wakazi wa mkoa wa Lindi kujitenga kutoka katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

    Wakishajitenga nyinyi mliopo hapa ndio mtakuwa viongozi wa nchi hiyo mpya na kuhakikisha tunaihodhi vitalu vyote vya gesi na mafuta . Sisi ndio tutakuwa na maamuzi juu ya gesi hiyo tuitumie vipi na tumuuzie nani? Kwa bei gani ? Tutaingiza pesa nyingi sana kutokana na Gesi hiyo.

    Lakini ili kuwashawishi Wananchi wa mkoa wa Lindi watuunge mkono juu ya Mpango huu wa siri. Tutaenda kwa njia ya kueneza chuki juu ya Serikali yao kwa kuwaambia kuwa imewatenga. Hawapewi huduma za kijamii kama vile maji, elimu ,umeme na miundombinu kama ilivyo kwa mikoa mingine. Habari hiyo itawafanya Wananchi wawe na hasira na Serikali yao na itakuwa rahisi sisi kuwashawishi wajitenge.

    Tukishindwa Mpango wa kueneza chuki tutatumia njia nyingine ya nguvu.Tutatumia silaha kuuchukua Mkoa wa Lindi na kuimiliki Gesi yote iliyopo katika visiwa vya Songosongo na Nyuni.Hilo ndio dhumuni kuu la Mpango huu wa siri.

    Waziri mkuu aliweka nukta na kuchukua chupa ya maji safi na kuanza kunywa akiacha maneno yale yale yawaingia vizuri wale Mawaziri.



    Mawaziri wote walipigwa na mshangao. Hawakuwa wanajua kabisa Mpango huu hasa ulivyo. Mwanzoni walidanganywa kuwa ulikuwa mpango wa kuwatetea watu wa Mkoa wa Lindi ili nao wapate huduma bora za Jamii. Nao kwakuwa walikuwa wazawa wa mkoa wa Lindi waliingia kwenye Mpango huu. Sasa Waziri mkuu alikuwa anaongea vitu tofauti kabisa na wakivyovifahamu. Ila walikaa kimya watafanyaje ? Na hela wanazitaka! Maji washayavulia nguo…..!



    Baada ya kunywa maji Waziri mkuu aliendelea.



    “Ajenda ya tatu inahusu kumuua Daniel Mwase…….”Waziri mkuu hakumalizia kauli yake. Kauli ile ilimaliziwa na mtu mwengine kabisa. Hakualikwa kwenye kikao lakini alihudhuria.



    “….baa”Daniel alimalizia huku akishuka toka darini. Watu wote kwenye kikao kile walipigwa na mshangao. Kuangalia juu waliona uwazi mkubwa. Hawakuelewa Daniel kaingia muda gani mule ndani. Kila mmoja alitaharuki kwa aina yake. Wajumbe wote kumi waliingiwa na hofu kuu!



    .





    “Ajenda ya tatu ni kumuua Daniel Mwaseba, ndiye mimi. Nimekuja ili muniue na kuiruka hiyo ajenda ya tatu. Muiongelee ajenda ya nne ya utekelezaji wa Mpango kazi” Daniel Mwaseba aliongea kwa mbwembwe huku akirandaranda mule ndani.

    Kule Ikulu viongozi wote walibaki midomo wazi. Hawakutegemea kitendo alichokifanya Daniel.



    Ikulu nako waliingiwa na Hofu.Wakijua muda wowote Daniel anauwawa. Walijua watu wote mule ndani walikuwa na bastola, ina maana wanaweza kumuua Daniel sekunde yoyote wakitaka.



    “Kila mmoja wenu hapo alipo amekalia kiti. Kiti kilichotegwa bomu. Na rimoti ya mabomu hayo ni hii hapa. Hayo yanaitwa mabomu msituo. Nikibonyeza rimoti unatoka mlipuko mdogo tu, wenye madhara kwa mtu aliyekaa kwenye kiti tu. Mimi sitodhurika kamwe, na hata hii nyumba yako Mtukufu waziri mkuu haitodhurika. Utapata hasara ya viti tu.” Daniel aliongea huku akiwaonesha ile rimoti ndogo aliyoishika mkononi.



    “Nikiona Paka wa mtu anajitingisha tu nabonyeza rimoti hii. Mnaweza mkajiona muko wengi mukadhani siwaoni. Kwa macho haya mawili naona kila kitendo cha kila mtu. Daniel Mwaseba hana macho mawili, Daniel Mwaseba ana macho mia mbili !”



    Wale wazungu waliiva wakawa wekundu! Waliustaajabu sana uwezo wa akili wa mtu mweusi yule. Walikuwa hawaamini kama Mtu Mweusi anaweza kuwa na akili kiasi kile. Mawaziri wote machozi yalikuwa yanawatoka. Dr Kazija Juma alikuwa anapiga mayowe kabisa!



    Kule Ikulu walikuwa wanashangilia kama watoto wadogo. Wote hawakuamini uwezo wa akili wa Daniel. Sasa walikuwa wanakumbatiana kwa furaha. Hofu ziliwaisha. Kwa mara nyingine tena Daniel Mwaseba, mpelelezi namba moja Tanzania. Alikuwa ameiokoa nchi yake katika hofu kuu ikiyotaka isababishwe na viongozi hawa wenye nyadhifa kubwa Serikalini lakini hawaridhiki kabisa.



    Ghafla ! Mlango wa ukumbi wa mikutano ulifunguliwa na kuingia wanajeshi wengi wa jeshi la Wananchi Tanzania, na kuwatia mbaroni viongozi wale.



    Saa saba mchana Daniel Mwaseba alihudhuria maziko ya rafiki yake kipenzi, Inspekta Nyange. Chozi lilimdondoka wakati Inspekta Nyange akihifadhiwa katika nyumba yake ya Milele.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wiki moja baadae, Daniel akiwa nyumbani kwake akiangalia taarifa ya habari. Alisikia habari iliyomfurahisha sana.



    “…Waziri mkuu wa Tanzania, Mheshimiwa Abdallah Kilumbaki na mawaziri wanne pamoja na wazungu wanne raia wa Ujerumani wamehukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa…….” Daniel hakuendelea kusikiliza taarifa ya habari ile. Alimpigia simu Raisi na kumuomba mapumziko ya kwenda kupumzika Ujerumani.



    Aliruhusiwa.



    Mwisho.

0 comments:

Post a Comment

Blog