Search This Blog

Saturday 5 November 2022

SURA MBILI - 1

 






IMEANDIKWA NA : PATRICK J. MASSAWE



*********************************************************************************



Simulizi : Sura Mbili

Sehemu Ya Kwanza (1)



*******



Hali ya utulivu ilitawala eneo zima la Upanga Mashariki. Ni eneo wanaloishi watu wenye kipato cha juu na wenye hali bora kimaisha tofauti na maeneo mengine ya uswahilini. Ni mvumo wa mawimbi ya bahari uliosikika ukigonga katika kingo za miamba iliyokuwa ufukweni katikati ya ukimya ule.

Vilevile, wingu zito lilikuwa limetanda angani hasa ukizingatia mvua za masika zilikuwa zinayesha mfululizo ndani ya Jiji la Dar es Salaam zaidi ya wiki mbili hivi.

Baadhi ya wakazi wengi, walikuwa wamejifungia ndani, kuhofia mvua ile ambayo ingenyesha wakati wowote na waliokuwa njiani, walikuwa wakiharakisha kurudi majumbani mwao.

Usiku huo wa saa mbili hivi, ndani ya jumba moja la kifahari lililoko umbali wa mita hamsini kutoka ufukweni mwa Bahari ya Hindi, eneo la Sea View, mtu mmoja, kipande cha baba, aliyeshiba ipasavyo, alikuwa amekaa kwenye sofa la gharama ndani ya sebule nadhifu, akinywa kinywaji chake, pombe kali aina ya Jack Daniels taratibu. Mawazo yake yalikuwa mbali sana huku akiangalia runinga kubwa ya bapa, iliyokuwa juu ya meza maalum, umbali mfupi mbele yake.

Mtu huyo aliyekuwa amezama katika mawazo mengi, pia, akiangalia taarifa ya habari iliyokuwa inaendelea kurushwa kwenye runinga hiyo. Kwa muda huo wote alikosa utulivu wa kukaa pale kitini, kutokana na kile alichokuwa anaangalia, kiasi cha kumfanya akose utulivu.

Ni taarifa aliyokuwa anaifuatilia kwa makini sana, kwani kilichokuwa kinatangazwa mle, kilikuwa kinamwathiri moja kwa moja kuhusu biashara zake mbalimbali alizokuwa anazifanya hapa nchini Tanzania, ambazo nyingi ya hizo ni za haramu.

Habari hiyo iliyokuwa ikitangazwa muda huo, ilikuwa inazungumzia kuhusu Jeshi la Polisi nchini Tanzania, lililokuwa likiendesha Operesheni Maalumu dhidi ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya, ambao kwa kiasi kikubwa walikuwa wamefanikiwa kuwakamata wafanyabiashara kadhaa waliokuwa katika mtandao mkubwa hapa nchini nje ya nchi.

Ni mafanikio makubwa yaliyowafanya makamanda wengi kutabasamu kwa mafanikio hayo, kwani walikuwa hawapati usingizi baada ya biashara hiyo kushamiri kwa kuendeshwa kiholela pasipo wahusika kudhibitiwa ipasavyo! Ni rushwa ilitembea!

Mtu huyo aliyekaa pale sebuleni akiangalia taarifa ya habari katika runinga, alijulikana kwa jina la Salum Zakwa Mnube, ambaye alikuwa ni mtu mzito serikalini, ‘kigogo,’ akiwa na cheo cha Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti wa Udongo. Kabla ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pia alikuwa Ofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, aliyefikia cheo cha Kanali wakati akilitumika jeshi hilo. Hata hivyo hapo awali, pia aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa mmoja ulioko mpakani mwa nchi yetu, kabla ya kuteuliwa kuwa mkurugenzi.

Salum Zakwa Mnube, alikuwa na umri wa miaka 55 hivi, akiwa mwenye afya njema iliyomfanya aonekane mdogo kuliko umri wake. Kwa namna moja ama nyingine, yeye alikuwa akijishughulisha na biashara hiyo haramu, kwa kivuli cha mtu mwadilifu, asiyekuwa na kashfa yoyote tangu alipoamua kujitoa jeshini na kuendelea na mambo ya siasa.

Aliacha jeshi akiwa ni ofisa aliyekuwa akifanya kazi makao makuu ya jeshi, akiwa katika Kitengo cha Uhusiano, alichokitumikia kwa miaka kadhaa tangia akiwa na cheo cha Luteni Usu.

Kwanza kabisa, Salum Zakwa alikuwa amehitimu elimu ya sekondari, kidato cha sita, halafu akajiunga na Chuo cha Diplomasia, Kurasini na alipata shahada yake ya kwanza ya uhusiano wa kimataifa. Baada ya hapo, akiwa na kiu ya kujiendeleza kielimu, alisomea tena shahada yake ya pili, hivyo akawa ni mmoja kati ya maofisa wa kijeshi waliokuwa wakisafiri katika nchi mbalimbali duniani, kuhudhuria mikutano inayohusiana na mambo ya kijeshi, kitu ambacho kilimfanya ajulikane sana na pia, kuwa na marafiki wa aina mbalimbali, wazuri na wabaya.

Basi, kati ya hao marafiki wabaya, ndiyo waliomshawishi akaacha jeshi na kujiunga na biashara ile haramu ya dawa za kulevya, ambayo ilimpatia fedha nyingi sana na kuonekana mtu kati ya watu wenye fedha hapa nchini.

Mbali ya kujihusisha na biashara ile haramu, lakini hakuna mtu aliyekuwa anajua, kwa jinsi alivyokuwa amejificha kwa kivuli cha Mkurugenzi wa Shirika la Utafiti wa Udongo, aliyeteuliwa na Mtukufu Rais, ambapo alikula kiapo cha utii! Hakika, alijua alichokuwa anafanya!

Akiwa bado amekaa pale kwenye sofa, Salum Zakwa aliendelea kuangalia ile taarifa ya habari, huku pia akikumbuka jinsi wafanyabiashara wenzake mashuhuri waliokuwa na nguvu kubwa za kiuchumi, wakiwa wamekamatwa hivi karibuni, katika operesheni hiyo kali iliyokuwa bado inaendelea nchini. Akasonya kwa nguvu, halafu akanyanyua glasi yake na kupiga funda moja la mkupuo, kisha akabaki akisikiliza iliyokuwa inashuka tumboni.

Ukweli ni kwamba hofu kubwa ilikuwa imemjaa, hasa ukizingatia biashara ile yake ndiyo ilikuwa imeshamiri na kumpatia kipato kikubwa. Ni kipato kilichomfanya aweze kumiliki vitege uchumi vingi ndani ya Jiji la Dar es Salaam. Hata hivyo, akiwa ni mtu mzitiifu serikalini, aliona kuwa hakuna mtu wa kumbabaisha katika nchi hii kamwe, kwani angetumia wadhifa wake aliopewa katika kuendelea na biashara hiyo haramu kadri anavyotaka!

Mawazo yaliendelea kumtawala Salum Zakwa na baada ya kuwaza sana, ndipo alipojipanga jinsi ya kukutana na watu wake wa kazi, ili kupanga mikakati ya kuweza kuepuka na msako ule na pia akiendelea na biashara kwa uficho wa hali ya juu.

Yeye alikuwa anajiita mtu mwenye ‘SURA MBILI.’ Yaani sura ya kwanza: ‘Ni ile ya upole, ucheshi, iliyounda tabasamu pana muda wote. Mtu mkarimu mwenye kupenda watu wa aina zote, kiasi cha kupendwa na wafanyakazi wa chi yake aliokuwa nawaongoza!’. Sura ya pili: ‘Ni ile ya ukatili wa hali ya juu, isiyokuwa na chembe ya mzaha hasa anapokuwa katika biashara ile haramu ya dawa za kulevya.

Ni mtu ambaye alikuwa hasiti kutoa roho ya mtu anapomdhulumu mali zake, hivyo katika maisha yake!’ Alijitahidi sana kuishi katika mazingira hayo!

Hivyo alichukua simu yake ya mkononi, iliyokuwa juu ya meza, halafu akawapigia simu vijana wake maalumu waliojulikana kwa majina ya David Osmond, Bosco Zambi na John Peka. Baada ya kuwapigia na kuwapata, aliwaambia kuwa kesho yake jioni wakutane katika sehemu husika haraka sana, ili kupanga cha kufanya.

Wale walikuwa ni vijana maalumu aliokuwa amewaajiri kwa siri kubwa, katika kukamilisha biashara ile haramu na kila mmoja alikuwa akikaa katika sehemu mbalimbali za jiji la Dar es Salaam.

Baada ya kuwajulisha, Salum Zakwa akaendelea na starehe yake ya kunywa pombe taratibu huku akikaza macho yake kwenye runinga ikiwa wakati huo taarifa ile ilikuwa imeshamalizika na vipindi vingine vilivyokuwa vinaendelea. Hata hivyo hakuendelea kuiangalia tena zaidi ya kuwaza kilichokuwa kinamsumbua!

Wakati wote huo, familia yake, mke wake na watoto, walikuwa wamekaa katika sebule nyingine iliyokuwa upande wa pili, wakiendelea na mambo yao, kwani mara nyingi alikuwa hapendi kujichanganya nao kama kuna kitu kilichokuwa kinamkera juu ya shughuli zake za kikazi.

Huo ulikuwa ni utaratibu aliokuwa amejiwekea Salum Zakwa, na wote pale nyumbani walikuwa wameshamzoea. Ni hadi alipotosheka na kinywaji chake, ndipo alipoendelea na ratiba nyingine ya kuimalizia siku ile!





*******

Wingu zito lilikuwa bado limetanda angani, lakini halikuwazuia watu kufanya shughuli zao kwa kuihofia mvua hiyo iliyokuwa inategemea kunyesha muda wowote. Majira ya saa kumi na mbili za jioni hiyo, siku ya pili, Salum Zakwa, alikutana na vijana wake wa kazi, David Osmond, Bosco Zambi na John Peka. Walikutana katika Hoteli nadhifu ya Mawingu Resort, iliyoko Kijitonyama, umbali mfupi kutoka katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi. Kila mmoja alifika hapo kwa wakati wake, ambapo walikutana ndani ya chumba maalumu kilichotengwa kwa maongezi yao muhimu sana, ambayo hawakutaka mtu mwingine yeyote wa nje aweze kuyasikia.

Kama kawaida mhudumu mwanadada mrembo, aliyejulikana kwa jina la Clara, alifika ndani ya chumba hicho baada ya kuitwa na Salum Zakwa, akiwa ni mtu aliyekuwa akimhudumia mara kwa mara kila anapofika katika hoteli hiyo.

Kamwe hakupenda kuhudumiwa na mwingine kwa kile alichokiita kutozoeana nao sana. Mara alipoingia , alisalimia kwa heshima, ambapo aliagizwa awahudumia walichohitaji kwa bili yake yeye. Wote walihudumiwa vinywaji, pombe na nyama ya kuchoma, ambapo waliendelea kunywa na kula taratibu.

Wakati huo kila mmoja alikuwa na mawazo yake kichwani hasa kwa vijana wale wakiwaza juu ya walichoitiwa na bosi wao, Salum Zakwa. Yeye alikuwa amekaa kwenye kiti cha katikati huku vijana hao wakiwa wamekaa kando yake, tayari kumsikiliza.

“Vijana wangu...” Salum Zakwa akasema huku akiwaangalia kwa makini kana kwamba alikuwa anawakagua.

“Bosi!” Wote watatu wakajibu kwa mara moja huku wakimwangalia.

“Nimewaiteni hapa katika kikao cha faragha...” Salum Zakwa akaendelea kusema huku akinyanyua glasi yake na kupiga mafunda kadhaa ya pombe.

“Ni sawa bosi...”

“Natumaini nyote mmesikiliza katika vyombo vya habari kwa makini!”

“Ndiyo bosi, tumesikia,” David Osmond akasema.

“Tumesikiza...” akasema Bosco.

“Wote tumesikiliza…” John Peka akamalizia kusema.

“Hali ni mbaya sana. Jeshi la Polisi limechachamaa. Ni msako kila kukicha, biashara yetu imeingiliwa, nafikiri hata nyie mnaona. Kuna baadhi ya wenzetu wameshakamatwa na wamefikishwa katika vyombo ya usalama. Sasa mnafikiri na sisi tuogope na kusitisha biashara yetu hii?”

“Hapana bosi, haiwezekani, hatuwezi kusitisha!” David Osmond akasema.

“Sasa unafikiri tufanyeje?” Salum Zakwa akauliza.

“Inadidi tuifanye kwa akili bosi. Tunaweza kuwakwepa na kufanikisha.”

“Nafurahi sana kwa kunipa moyo. Yaani nilikaribia kusimama kidogo, kitu ambacho kingetuathiri sana, hasa ukizingatia bado kuna mzigo wangu mkubwa uko nchini Pakistan na unasubiri kwenda kuchukuliwa wakati wowote.”

“Hilo usijali bosi. Mzigo ufuatiliwe, tutakulinda kwa njia yoyote. Kama ni wazee, tutakula nao sambamba kama tunavyofanya siku zote!”

“Nashukuru sana. Ndiyo maana nikawakutanisha ili tuchangie mawazo.”

“Tuko wote bosi.”

“Mbali ya mzigo wa kutoka Pakistani, ambao utaletwa na wale vijana maalumu kwa kutumia njia ile ya kuumeza, pia, kuna mwingine unaokuja kwa njia ya meli ya mizigo. Ni ule mzigo ambao huwa tunaupokea katika ufukwe wa Kunduchi, kwa kutumia boti yao maalumu kutoka ndani ya meli yao waliyoipaki mbali baharini. Natumaini mnanielewa…” Salum Zakwa akaendelea kuwaambia vijana hao ambao bado walikuwa wakimwangalia kwa makini sana!

“Tumekuelewa bosi,” wote wakasema kwa pamoja.

“Haya, kama mnanielewa vizuri, tuendelee na vinywaji, kisha tuagane, muende mkapumzika.”

“Sawa, bosi!”

Salum Zakwa na vijana wake, David Osmond, Bosco Zambi na John Peka, waliendelea huku wakiongea mengi yanayohusu biashara yao kwa ujumla. Baada ya kumaliza kupanga mipango yao, ilikuwa imetimu saa tatu za usiku. Wakawa wametosheka na kuondoka kurudi majumbani kwao, ambapo Salum Zakwa aliondoka kurudi nyumbani kwake, Sea View, Upanga, na David alielekea nyumbani kwale, mtaa wa Kisangilo, Magomeni Mapipa, Bosco akaelekea nyumbani kwake, eneo la Maghorofa ya Faya, na John akaelekea nyumbani kwake, Kinondoni, mtaa wa Sekenke. Kwa ujumla, wote waliamua kumlinda bosi wao kwa kadhia ile ya msako wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya!



********

Salum Zakwa hakuishia pale, kwani baada ya kukutana na watu wake, David Osmond, Bosco Zambi na John Peka, siku inayofuata alikutana na watu wengine muhimu huwa anaowashirikisha katika ‘Mtandao’ wa biashara ile haramu ya dawa za kulevya. Ni watu ambao yeye akiwa ni mtu makini, alikuwa amewapanga katika makundi matatu, yasiyofahamiana, ili kukamilisha lengo lake bila kuharibikiwa. Watu hao ni vijana, Vasco Nunda, na Liston Kihongwe, ambao walikuwa wamepewa kazi maalum ya kumlinda yeye kila anapokwenda.

Ni watu ambao walikuwa hawajuani na wale watu wengine watatu, David, Bosco na John, ikiwa ni mbinu yake ili asiweze kutambulika na adui zake, na mbali ya kumlinda, pia, walikuwa wakipewa kazi ya kumwangamiza mtu yeyote aliyeingilia biashara za bosi wao, Salum, au hata kumdhulumu mzigo wa dawa za kulevya unaopelewa au kuingia sokoni.

Baada ya kuwapigia simu, Salum Zakwa akawaambia wakutane katika Hoteli ya Msasani Pensula, iliyoko ufukweni mwa Bahari ya Hindi, katika eneo tulivu la Msasani. Ni kama alivyokuwa anapanga mipango yake kimpangilio, kwani alikuwa akikutana na vijana hao katika sehemu mbalimbali bila wao kujuana, katika kuepuka kujulikana kwa siri zake. Alipomaliza kuwapigia simu, naye alipanda gari lake la kifahari, aina ya Ranger Rover Fogue, akitokea nyumbani kwake, Sea View, Upanga, na kuelekea Msasani ilipo hoteli ile yenye hadhi ya kitalii. Wakati huo ilikuwa ni majira ya saa kumi na mbili za jioni.

Salum Zakwa alipofika Msasani Pensula Hotel, alilipaki gari lake katika sehemu ya kubwa ya maegesho, iliyoko upande wa mbele ya hoteli ile iliyokuwa na uwezo wa kupaki magari yapatayo thelathini hivi kwa wakati mmoja. Kabla ya kushuka garini, kwanza aliyazungusha macho yake pande zote na hata upande wa nyuma. Alipohakikisha kuwa hali ni ya usalama, ndipo aliposhuka na kuelekea moja kwa moja katika sehemu ile ya ufukweni mwa bahari, alipokuwa anapendelea kukaa siku zote, anapokuwa na dharura kama ile.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Kama kawaida, Salum Zakwa alikaa ndani ya kibanda kimoja kilichojengwa mjengo wa mduara na kuezekwa kwa makuti ya mnazi. Halafu akaagiza pombe kali aina ya Jack Daniels, aliyopendelea sana kunywa, kasha akabaki akiwasubiri vijana wake, huku akivuta sigara kwa mkupuo na kupuliza moshi angani. Macho yake alikuwa ameyaelekekeza baharini na kuziona baadhi ya meli kubwa zilizokuwa zimetia nanga kusubiri kuruhusiwa kuelekea bandarini. Kwa vile giza lilikuwa limeanza kuingia, zilionekana kama ni mtaa uliokuwa unaelea baharini kwa umbali ule.

Baada ya nusu saa hivi, tokea Salum Zakwa akae pale ndani ya kibanda, vijana wale, Vasco Nunda na Liston Kihongwe, walifika wakiwa na gari moja aina ya Toyota Mark 11 Grande, inayomilikiwa na Liston, ambayo waliipaki katika maegesho, siyo mbali sana na gari la bosi wao. Halafu wakashuka na kumfuata kwa hatua fupifupi kule ufukweni mwa bahari alipokuwa amekaa. Wote wawili walikuwa wamevalia mavazi ya ya kileo wanayovalia vijana wengi, ikiwa ni fulana na suruali za Jeans. Machoni mwao walikuwa wamevalia miwani mieusi, ingawa hali ya hewa haikuruhusu. Baada ya kufika pale kwenye kibanda, walimkuta bosi wao amekaa ndani ya kibanda hicho akijinywea pombe kali, nao wakamfuata na kusimama mbele yake baada ya kumsalimia.

Salum Zakwa aliwapa ishara ya kukaa vitini kwa mkono. Vasco na Liston wakakaa kwenye viti vilivyokuwa pale sambamba na meza. Halafu akawaambia waagize vinywaji wanavyopendelea kunywa ili walainishe makoo yao. Vijana hao wakaagiza bia na kuendelea kunywa taratibu wakisubiri kumsikiliza bosi wao awaeleze kile alichowaitia. Muda wote huo, Salum Zakwa alikuwa bado ameyakaza macho yake kuangalia kule baharini bila kusema chochote, na baada ya muda, ndipo walipoanza mazungumzo yao yaliyowakutanisha pale.





*******

Mazungumzo yaliyoendelea pale baina ya watu wale watatu, yalikuwa ni yaleyale ya kukumbushana na kuwapa tahadhari juu ya ile Operesheni Maalum iliyokuwa inaendeshwa na Jeshi la Polisi nchini, juu ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya.

“Vijana wangu...” Salum Zakwa akawaambia huku akiwaangalia kwa makini. Huo ulikuwa ndiyo utaratibu wake, alitaka kumsoma kila mtu kwa kile alichokuwa anawaza mawazoni mwake.

“Naam bosi...” wote wakaitikia kwa pamoja.

“Nimewaita hapa kwa mazungumzo muhimu sana...”

“Tumeitikia wito bosi...” Vasco Nunda akasema.

“Tumekuja bosi,” Liston Kihongwe naye akasema.

“Natumaini hali halisi mnaiona inavyoendelea hapa nchi, au sivyo?”

“Ndiyo, tunaiona. Ni msako mkali unaendelea!”

“Sawa kabisa. Ndicho nilichowaitia,” Salum Zakwa alisema na kuongeza. “Ninawasihi muwe macho sana na hali inayoendelea, kwa vile kuna mizigo yetu mingine inayotegemea kuingia, ambayo bado iko njiani inakuja. Inabidi mizigo hiyo ifike salama bila kushtukiwa na Jeshi la Polisi, hivyo basi, mtabidi mkae imara na kulinda mali hiyo, sijui mnanielewa?”

“Tunakuelewa bosi,” Vasco Nunda akasema.

“Tupo na wewe bosi,” Liston Kihongwe akaongeza.

“Kuna mizigo muhimu iko njiani,” Salum Zakwa akasema na kuendelea. “Kuna ule unaotoka nchini Pakistani, ambao utakuja kwa ndege. Utaletwa na wale vijana wetu, Joel Besha, Roki Sekulu na Bomeza Jadu. Pia, kuna mzigo mwingine utakuja kwa njia ya meli kama kawaida, ambayo huwa inatia nanga baharini kabla ya kufika bandarini. Mzigo huo utakwenda kuchukuliwa na boti maalum, na kuufikisha ufukweni. Kazi ya kuuchukua inajulikana, sina haja ya kuwakumbusha!”

“Ni sawa bosi,” Vasco Nunda akasema kwa niaba ya Liston.

“Halafu,” Salum Zakwa akaendelea kusema. “Kuna kazi nyingine nataka kuwapa!”

“Kazi gani bosi?”

“Natumaini nyote mnamfahamu mtu anayeitwa Abdul Zengekala?”

“Ndiyo, tunamfahamu bosi...” Liston akasema huku akivuta kumbukumbu zake, ni kweli alimfahamu mtu huyo.

“Mtu huyo anafahamika sana bosi, tupe maelekezo…” Vasco naye akasema, akiwa pia ni mtu anayemfahamu sana katika biashara ile haramu.

“Basi, mtu huyo natakiwa kushughulikiwa mara moja! Amenidhulumu mali yenye thamani kubwa! Salum Zakwa akasema na kuongeza. “Halafu baada ya kunidhulumu, ameishia katika ulevi wa kupindukia, kucheza kamari kwenye ma- Casino, na pia kuendekeza wanawake wa bei mbaya ilhali ni fukara! Ni mshenzi sana!”

Vasco Nunda na Liston Kihongwe walikuwa bado wanamsikiliza kwa makini. Kwa vyovyote walijua kwamba bosi wao alikuwa ana kitu kikubwa kilichokuwa kinamsumbua, ambacho siyo kidogo!

“Hivyo basi, mimi nimewaitia jambo hilo, na mkae mkijua. Sikupenda kuwaeleza jambo hili katika simu hasa ukizingatia kwa wakati huu siyo vizuri sana kutumia simu zetu za mkononi kwa kuepuka kunaswa kwa mazungumzo yetu. Nafikiri kila hatua ninayopiga, ni lazima kuna makachero watakaokuwa wananifuatilia hasa kwa wale wanaonifahamu. Wengi wao ni wale walioko katika orodha ya malipo ninayotoa. Kwa kawaida huwa hawatosheki na fedha ninazowapa, na wengine wako tayari kuniletea hata habari za uongo, ili mradi uwapatie fedha! Wana njaa sana!” Salum Zakwa aliendelea kusema huku amekunja sura yake!

Vasco Nunda na Liston Kihongwe wakaendelea kumsikiliza.

“Baada ya kuwaambia hayo yote, sina cha zaidi. Tuendelee na vinywaji, halafu mkae mkijua nitawapa kazi jinsi ya kumshughulikia!” Salum Zakwa akamaliza kusema huku akiendelea kuwaangalia.

“Sawa bosi, tumekuelewa. Tunasubiri tu maelekezo yako!” Vasco akasema akasema kwa niaba ya Liston.

Salum Zakwa aliwapa maelekezo mengi sana, Vasco na Liston hadi walipoafikiana. Nao wakaapa kumlinda kwa gharama yoyote hasa ukizingatia yeye ndiye aliyekuwa kinara mkuu na anayewalipa vizuri. Walipomaliza mazungumzo yao, vijana wale wakamuaga na kuondoka pale kibandani na kumwacha bosi wao akiendelea kukaa akinywa kinywaji chake, na kwa kiasi fulani alikuwa ameridhika.

Walipofika sehemu ile walikopaki gari lao, walipanda gari na kuondoka, Liston akiwa dereva. Waliondoka na kumwacha Salum Zakwa akiendelea kunywa kama alivyokuwa anakunywa tokea muda mrefu. Chupa kubwa ya pombe kali na gasi ndefu vilikuwa pale juu ya meza, huku pia pakiti la sigara Sportsman ikiwa kando ya yeke. Alikuwa kila akimaliza pegi moja, alikuwa akiunganisha nyingine kadri alivyojisikia.

Akiwa bado anavuta sigara yake kwa fujo, Salum Zakwa alianza kuwaza jinsi alivyokutana na vijana wale hatari, Vasco Nunda na Liston Kihongwe. Walikuwa ni vijana hatari sana aliokuwa anawaamini katika kazi za kumlinda yeye, na pia kuwaadabisha wale wote wanaomdhulumu mali zake. Ni watu aliokutana nao katika mazingira ya aina yake!



*******

Tukianza na Vasco Nunda. Maisha yake ya utotoni yalikuwa magumu sana na ya huzuni kuliko maisha ya mtoto yatima. Siyo tu mama yake aliyemzaa kuwa Malaya wa kutupwa, mlevi mbwa, na mkali kama pilipili manga, pia alikuwa hamjali kabisa. Muda mwingi hakuwa anashinda nyumbani. Alikuwa akizunguka katika viwanja kusaka wanaume wa kuweza kumpatia chochote cha kumuwezesha kusukuma maisha yake ya kila siku.

Muda mwingi Vasco alikuwa anabaki peke yake nyumbani, akiwa mtoto wa umri wa miaka mitatu, njaa ikimuuma. Kulala na njaa lilikuwa jambo la kawaida kabisa kwake. Alianza kula vyakula vya kwenye mapipa na majalalani, mara tu alipogundua kuwa viporo vilitupwa katika mapipa na majalala. Hali ikawa nafuu kuliko kulala na njaa, na hatua iliyofuata, ilikuwa ni udokozi. Kudokoa chochote kile kilichomkalia vizuri, pesa, chakula na vinginevyo vilikuwa halali yake!

Wizi wa dhati haukukawia kufuatia. Vasco Nunda alijiunga na makundi ya watoto wa mitaani waliokuwa na shida kama yeye, wa pale mtaani kwao, Manzese, na hata mitaa mingine ya jirani. Watoto wale waliomzidi umri, walimfundisha kuiba vitu vidogovidogo wakati wa mchana, kama vile vitu vya nyumbani, mashuka, nguo, sufuria, ndoo za maji, saa, redio na vinginevyo. Vitendo vyote vile, mama yake hakuwa anajua kabisa, kutokana na kutokuwa karibu naye. Yeye ilikuwa kukicha ni kiguu na njia kuingia katika vilabu vya pombe kuchapa maji!

Hata hivyo mambo yaliendelea hivyohivyo kati ya mama na mwana, wakipishana kama paka na panya. Siku moja, mama yake huyo alimfuma Vasco akiwa na kitenge kipya cha waksi, alichoiba kwenye duka moja la Mpemba. Lakini badala ya kuadhibiwa, mama yake akakisifu kitendo hicho cha mwanae na kukichukua kitenge hicho tayari kwa matumizi. Vasco akawa amefunguliwa lango la Jehanam!

Mambo yakasonga mbele kwa kasi ya ajabu. Vasco akaanza kuvuta bangi na kuzurura usiku na kikosi chake cha kazi za uporaji, akiwa na umri wa miaka kumi na mbili tu. Mtu wake wa kwanza kumuua, alikuwa ni mlevi mmoja aliyekuwa akikatiza mtaani, akitokea katika kilabu kimoja cha pombez za kienyeji, ambapo walitaka kumpora fedha alizokuwa nazo mfukoni mwake, saa ya mkononi na viatu vizuri vya ngozi. Katika purukushani za kumpora mlevi huyo kijana wa kileo, mbeba mizigo wa soko la Tandale, aliyezidiwa na kilevi tu, alichachamaa na kuwazidi nguvu akionekana ni mtu aliyekuwa imara kimapigano kuwazidi wao, na hakutaka mzaha hata kidogo.

Lakini Vasco Nunda aliyekuwa na kisu kubwa mkononi mwake, alimshindilia cha tumboni mtu yule aliyekuwa amelewa. Mlevi huyo kijana alipiga kelele huku akilikumbatia tumbo lake lililokuwa linavuja damu kwa wingi sana, na pia akiyumba kabla ya kuanguka chini na kubaki akitapatapa kwa maumivu makali. Hakuna hata mmoja aliyemsaidia, kwani Vasco na wenzake walikimbia kila mmoja kivyake, ambao yeye alirudi nyumbani kwao akitweta na kutetemeka, akijua fika kuwa alikuwa ametenda kile kitendo kiovu kuliko vitendo vyote duniani!

Alikuwa ameua!

Baada ya kufika nyumbani, Vasco alikitupa kile kisu chooni, halafu akalifua shati lake lililokuwa limelowa damu. Kisha akaoga na kuingia chumbani kwake ambapo alijifungia na kulala kama vile hakuwa amefanya kosa lolote, na wakati huo yeye na mama yake, walikuwa wakiishi katika nyumba tofauti, na hakuna aliyekuwa anafuatilia maisha ya mwenzake. Hata hivyo usiku ule Vasco hakuweza kulala, kila aliposinzia, aliweza kulisikia lile yowe la yule mtu, mlevi aliyemchoma kisu. Akawa anaweweseka ovyo!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Siku ya pili yake Vasco alijitokeza tena mtaani, ambapo aligundua kuwa vijana wenzake wa mtaani walikuwa wanamheshimu na kumuogopa kwa kile kitendo chake cha mauaji, hata wale waliokuwa wakubwa na wenye nguvu kuliko yeye, walianza kumwita Vasco ‘Nunda!’ Na kwa akili ya kitoto, Vasco alivimba kichwa karibu kipasuke, ambapo alitafuta kisu kingine kilichokuwa bora zaidi, ambacho alikitoa mara kwa mara kwa wenzake ili waweze kutishika. Mara akate kucha, mara akinoe kwenye ukingo wa vibaraza vya nyumba, ili mradi akionyeshe! Hakumgusa mtu!

Vasco Nunda alipotimiza umri wa miaka ishirini, alishakuwa jambazi sugu, anayesakwa na Jeshi la Polisi kwa matukio kadhaa ya kihalifu yaliyokuwa yanatokea katika maeneo mbalimbali ndani ya jiji la Dar es Salaam na kwingineko. Na ni wakati huo alipokutana na kijana mwenzake, Liston Kihongwe, mtu shupavu na mwenye roho ya kikatili kama ya kwake. Ndipo walipokuja kuwa marafiki wakubwa kwa vile pia walikuwa wamekaribiana kiumri, Vasco akiwa mdogo kwa Liston, aliyekuwa amempita mwaka mmoja. Ni Liston aliyekuja kumfundisha Vasco namna ya kutumia, silaha kali za moto, kama bastola na bunduki! Na ni yeye pia aliyempeleka kwa bosi wao, ‘Zungu la Unga,’ Salum Zakwa Mnube!







*******

Siku hiyo Vasco Nunda na Liston Kihongwe walikuwa wamekaa kijiweni, kwenye kibaraza cha nyumba moja kkuukuu iliyokuwa katika mtaa wa jirani, wakitafakari maisha kwa ujumla. Ulikuwa ni utaratibu wao kukutana kila mara na kujadiliana mambo muhimu ya kimaisha, ili kujiepusha na vitendo vya kijambazi walivyokuwa wanafanya, ambavyo ni vya roho mkononi. Ukweli ni kwamba walikuwa wamechoka kukimbizana na wanausalama muda wote na hata nyakati nyingine kunusurika kuuawa na wananchi wenye hasira kali!

Liston aliyekuwa anavuta sigara sigara yake taratibu, aliupuliza moshi juu angani halafu akauangalia ulivyokuwa ukizunguka kimafungu. Kisha akamwangalia mwenzake, Vasco, aliyekuwa akiwaza mambo ambayo hata hakuweza kuyajua, lakini ni kwamba alimwona akiwa kimya tu. Akamwita kwa sauti ya chini:

“Vasco, jamaa yangu...”

“Naam...” Vasco aliitikia huku akimwangalia.

“Natumaini wewe ni mwenyeji mzuri wa jiji hili la Dar es Salaam…” Liston akamwambia.

“Ah, swali gani hilo mshikaji?” Vasco akamuuliza huku akimwangalia kwa dharau! Alimuuliza swali la kijinga!”

“Nina maana ya kukuuliza hivyo!”

“Ndiyo, mimi ni mwenyejio na mzaliwa wa hapahapa jijini…natumaini umeridhika!”

“Ndiyo, nimeridhika,” Liston akasema na kuongeza. “Hivi umeshawahi kumsikia mtu mmoja, tajiri, anayeitwa Salum Zakwa Mnube?”

“Mtu huyo huwa namsikiaga akizungumzwa na watu kama unavyoniambia wewe,” Vasco akasema na kuendelea. “Lakini sijawahi kumuona hata kumfahamu kwa sura!”

“Aisee, basi mtu huyo huwezi kuonana naye hivi hivi, mpaka apende mwenyewe! Na huwezi kuamini, mimi ndiye mpambe wake mkuu kwa sasa.”

“Unasema kweli?” Vasco akauliza huku akiwa amesisimka!

“Ni kweli kabisa. Je, unaijua kazi yake?”

“Ndiyo, nasikia ni Mkurugenzi wa Shirika la Utafiti wa Udongo hapa nchini. Na pia, aliwahi kuwa mwanajeshi hapo siku za nyuma, hayo ndiyo ninayoyajua ndugu yangu.”

“Ndiyo, watu wengi wanajua hivyo...”

“Kwa wewe unamjua vipi?”

“Mbali ya kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Utafiti wa Udongo, pis anajihusisha na biashara ya unga!”

“Biashara ya dawa za kulevya?” Vasco akamuuliza!

“Ndiyo, anajishughulisha na biashara hiyo.”

“Unasema kweli?”

“Ni kweli kabisa. Lakini hakuna mtu anayejua, zaidi ya watu wa mtandao wake, kama mimi hapa!”

“Aisee? Nafikiri atakuwa anafanya biashara ya uhakika.”

“Ndiyo, hafanyi biashara ya kipuuzi. Yeye anaagiza shehena hasa, kuanzia kilo hamsini, hadi tani mbili. Halafu maajenti wake wanasambaza Afrika Mashariki yote na hata nchi nyinginezo za jirani!”

“Lazima atakuwa tajiri sana!” Vasco Nunda akasema huku akijiwashia sigara.

“Hiyo ni wazi, mawakala wake, na sisi wapambe huwa anatulipa vizuri sana. Ama sivyo, nisingeweza kujenga nyumba na kununua gari la maana! Nimeshakwambia ni mtu mzito mweye uwezo mkubwa, na anayeheshimiwa!”

“Aisee!” Vasco Nunda akaishia kusema hivyo.

“Je, unahitaji kuonana naye?” Liston akamuuliza.

“Wa nini sasa?” Vasco naye akamuuliza.

“Hutaki kazi?”

“Kazi nataka...” Vasco akasema. “Lakini ni kazi gani?”

“Kazi ya upambe wa kumlinda kama ninavyofanya mimi, ambaye ni mpambe wake wa siri, ingawa pia ana wapambe wengine ambao hawanifahamu mimi!”

“Ninahitaji kuonana naye. Kama ni kazi hiyo, niko tayari ndugu yangu...”

“Kwa hivyo uko tayari nikupeleke?”

“Niko tayari kama chuma cha pua!” Vasco akajibu kwa shauku kubwa!

“Poa, ngoja niwasiliane naye,” Liston akasema huku akitoa simu yake ya mkononi. Akaanza kubofya namba fulani, na alipojibiwa akasema neno moja tu, “Liston...” Baada ya kusema hivyo akakata mara moja!

“Mbona umeikata?” Vasco akamuuliza baada ya kumuona amekata simu.

“Ndiyo, huo ni utaratibu wa kuongea na bosi wangu, Salum Zakwa. Yeye ametupangia hiyo, hivyo mara baada ya kumtajia jina langu, huikata simu yake na sauti yangu inaingia ndani ya mashine maalum ya kompyuta inayochunguza sauti. Mashine hiyo inathibitisha kuwa ni mimi niliyezungumza na yeye, na baadaye ndipo atanipigia mimi!” Liston akamwambia Vasco.

“Mzunguko wote wa nini?” Vasco akamuuliza.

“Kwa ajili ya tahadhari,” Liston akasema na kuendelea. “Hata kama mtu asiyehusika akifanikiwa kuipata namba yake, ambayo wanayo watu wachache tu, na akaamua kumpigia akitumia jina langu, hataweza kuzungumza naye. Mashine haitatambua sauti yake, hivyo bosi hatamjibu, upo?”

“Duh, inaelekea huyu bwana ni kiboko!”

“Ni kiboko, kwani anafanya biashara hiyo kwa uficho sana, ili asiweze kushtukiwa hasa ukizingatia ni mtu mzito serikalini, na hiyo nakwambia wewe tu kwa vile ni jamaa yangu tumetokea mbali sana. Vilevile ninataka nikuunganishe na wewe uweze kula matunda ya mtu huyo anayenuka fedha!”

“Nitashukuru sana kama nitafanikiwa.”

“Usijali sana, nitakupigia debe…”

“Hakuna shaka, lakini ndiyo kusema anaendesha biashara bila wasiwasi, na askari polisi hawawezi kumshika? Maana mimi hainiingii akilini hata kidogo!”

“Hawataweza kumkamata kamwe,” Liston akajigamba na kuongeza. “Bosi ni mjanja kweli, kwani anajua kula na vipofu!”

Wakati wakiendelea na maongezi yao, baada ya dakika tano kupita, simu ya Liston iliita. Laston akaichukua na kuangalia namba za mpigaji, ambapo aliona ni simu iliyokuwa inatoka kwa Salum Zakwa! Akaiweka sikioni na kusema:

“Liston hapa bosi...”

“Ndiyo, Liston...nipe taarifa…” Salum Zakwa akamwambia upande wa pili.

“Nina taarifa bosi…”

“Taarifa gani hiyo?”

“Kama tulivyokuwa tumeongea hapo mwanzo. Nimempata mtu wa kusaidiana kazi...” Liston akamwambia huku ameukuna uso wake utadhani walikuwa wakiongea naye ana kwa ana!

“Vizuri. Saa moja na nusu, tukutane Mikambo Beach, Kigamboni...”

“Sawa bosi...”

Simu ikakatwa.

Liston akairudisha simu yake mfukoni na kusema, “Tutakutana naye saa moja na nusu, eneo la Mikambo Beach, Kigamboni...”

“Ufukweni Kigamboni?” Vasco Nunda akauliza kana kwamba alikuwa hajamwelewa.

“Ndiyo, ni mahala petu pa kukutana. Hivyo hata kama polisi watakuwa wameyanasa mazungumzo yetu katika vyombo vyao, hawawezi kuelewa tutakutana wapi!”

“Mh, huyo bwana ni moto wa kuotea mbali.”

“Ni kweli kabisa...jiandae, baadaye tunakwenda kukutana naye,” Liston akamwambia Vasco.

“Hakuna shaka, najiandaa…”

*******

Liston Kihongwe na Vasco Nunda waliwasili kwenye ufukwe wa Mikambo Beach kunako majira ya saa kumi na mbili na nusu za jioni, na giza lilikuwa limeshaingia kitu ambacho kiliwafurahisha.Walitumia usafiri wa gari lao kwa kupitia kwenye kivuko cha Kigamboni, hadi walipofika huko. Lakini sehemu ile ya ufukweni, palikuwa bado na watu waliokuwa wanapunga upepo uliotokea baharini na hawakuonyesha na haraka ya kuondoka kurudi majumbani kwao.

Baada ya kushuka ndani ya gari lao katika sehemu ya maegesho, Liston na Vasco walielekea upande wa baharini kwa hatua fupifupi, huku mawazo ya Vasco yakiwa mbali sana kuhusiana na yule mtu wanayekwenda kukutana naye. Hakuweza kumfananisha na nani kati ya watu aliowahi kukutana nao, ambao ni tishio na wenye uwezo mkubwa wakifedha hapa nchini Tanzania.

Wakati Liston na Vasco wakielekea ufukweni, kwa bali kidogo walimwona mtu mmoja aliyekuwa amekaa peke yake kwenye kiti kimoja kilichojengwa kwa zege, umbali wa mita ishirini kutoka baharini. Alikuwa mwenye sharafa nyingi, na amevalia miwani mieusi, kofia ya pama kichwani na pia alivalia suti nyeusi iliyomkaa vizuri. Mdomoni mwake alikuwa anavuta sigara na moshi mzito ulionekana ukielea hewani. Katika mwangaza hafifu wa jioni, mtu huyo alionekana kama kivuli, na watu walikuwa wakimpita hata bila kumwangalia.

Baadhi ya watu waliokuwa wakimpita pale alipokuwa amekaa, kamwe hawakujua kama alikuwa ni Salum Zakwa, Mkurugenzi wa Shirika la Utafiti wa Udongo, ambaye ni mtu hatari kuliko maelezo, anapokuwa katika himaya yake ya kazi za haramu, na ni mpole sana anapokuwa katika kazi zake za halali, ndani ya ofisi nadhifu. Hivyo Vasco na Liston walimwendea kwa zile hatua fupi hadi walipofika karibu yake. Halafu wakasimama huku wakimwangalia kusubiri maelekezo, ambapo yeye bado alikuwa amekazia macho yake upande wa baharini!

“Habari za jioni, bosi...” Liston akamsabahi kwa nidhamu ya hali ya juu.

“Nzuri Liston...” Salum Zakwa akajibu kwa sauti ya chini angali sigara yake ikiwa katika ncha ya pembe ya mdomo wake.

“Bosi, huyu ndiye yule kijana, nimekuja naye...” Liston akamwambia wakiwa bado wamesimama wima.

“Ndiye huyu sivyo?” Salum Zakwa akauliza.

“Ndiyo bosi...”

“Haya, hebu kaeni!” Salum Zakwa akawaambia huku akiwaelekeza wakae kwenye kiti kingine cha zege kilichokuwa mbele yake. Ni viti vilivyokuwa vinatazamana, vikiwa katika umbali mfupi.

“Sawa, bosi,” Liston alisema huku wakikaa. Naye Vasco alikaa sambamba na Liston wakimtazama mtu huyo hatari aliyekuwa amekaa mbele yao!

“Lakini anatufaa huyu? Au unaniletea mtu ni mtu?” Salum Zakwa akauliza huku akimwangalia Vasco kwa dharau kana kwamba aliona kinyesi!

“Anatufaa bosi…nimemchunguza. Ni kati ya watu tunaowahitaji katika kazi yetu!”

“Unaitwa nani kijana?” Salum Zakwa akamuuliza huku akiendelea kumwangalia.

“Ninaitwa Vasco Nunda…” Vasco akamwambia kwa kujiamini sana.

“Unaitwa Vasco Nunda?”

“Ndiyo, bosi ninaitwa hivyo…”

“Wewe ni Nunda kweli? Unayaweza?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Ndiyo, mimi ni Nunda kweli, na ninayaweza. Ndiyo maana wakanikatia jina la Nunda!”

“Yeah, vizuri sana. Kama anafaa, nitamchukua na kuanza kazi mara moja. Na ili kumuamini, nitaanza naye kwa kazi maalum mnayotakiwa kuifanya hivi karibuni. Hiyo kazi ndiyo itakayonifanya mimi nimwamini kama kweli ni Nunda, na sivinginevyo!”

“Sawa bosi...” Liston aliendelea kusema.







*******

“Basi Liston, nashukuru sana kwa kumleta kwangu huyu mtu ili kumwona na kufahamiana. Sasa mnaweza kuondoka na tutakutana tupange vizuri...” Salum Zakwa akamwambia Liston.

Baada ya kumaliza kuongea na Salum Zakwa, Liston na Vasco waliaga na kuondoka katika eneo lile la Mikambo Beach. Kama kawaida walimwacha bosi wao amekaa palepale kama kivuli kilichotulia, huku akivuta sigara yake kwa mkupuo na macho yake kayaelekeza baharini.

Ukweli ni kwamba, Vasco alikuwa bado anajiuliza juu ya mtu yule aliyekutanishwa naye, ambaye anaambiwa kuwa ni hatari, na pia ni mtu anayetegemea kufanya naye kazi. Je, watawezana kwa jinsi alivyoonekana na dharau iliyopitiliza? Hata hivyo aliamua kujaribu bahati yake. Na wakiwa ndani ya gari wakati wakivuka kivuko kurudi katikati ya jiji, Vasco akasema:

“Ndugu yangu, Liston…”

“Naam…” Liston akaitikia na kumwangalia.

“Mimi nashukuru sana kwa kunikutanisha na bosi wako, Salum Zakwa. Lakini hujaniaeleza jinsi ulivyokutana naye mpaka ukawa mpambe wake. Ni vizuri na mimi nikijua…” Vasco akamwambia Liston.

“Ni kweli, sijakwambia. Lakini ni vyema nikufahamishe kwa vile na wewe unaingia kwenye mtandao wetu...”

“Sawa...” Liston akasema na kukaa tayari kumwelezea alivyokutana na Salum Zakwa!



********

Mtaa wa Kipata ni mmoja wa mitaa maarufu ndani ya jiji la Dar es Salaam. Ni mtaa mrefu unaoanzia kutokea katika mtaa wa Lumumba, eneo la Mnazi Mmoja na kuishia katika mtaa wa Msimbazi, kwa kukatiza katika mitaa mingineyo inayounganisha eneo zima la Kariakoo. Kwa ujumla ni mtaa wenye pilikapilika nyingi muda wote huku pia ukiwa na maduka mengi yaliyojengwa vibarazani mwa nyumba zilizopo mtaani hapo.

Katikati ya mitaa ya Nyamwezi na Sikukuu, pana nyumba moja kubwa, ilioyojengwa mjengo wa kisasa, ambayo kwa mbele imezungukwa na hayo maduka kadhaa yanaouza bidhaa za aina mbalimbali. Upande wa kushoto mbele ya nyumba hiyo, pana mti mmoja mkubwa wa Mzambarau, ambao umedumu pale kwa miaka mingi, kiasi kwamba eneo hilo likaitwa kwa jina la Mzambarauni.

Upande wa kulia mwa nyumba ile pana na geti dogo la chuma, ambalo linatokeza upande wa nyuma. Huko kulikuwa na makazi ya watu waliokuwa wanaishi kifamilia, ambapo pia palikuwa panaendeshwa huduma za biashara ya vinywaji vya aina mbalimbali vya kilevi. Mbali ya hayo, pia palikuwa na huduna za danguro walipokuwa wanapatikana wanawake warembo wa kila aina kuanzia umri wa chini, umri wa kati na hata watu wazima wa makamo wanaojipenda na kuonekana warembo wa nguvu.

Palijulikana kwa jina la ‘Mzambarauni kwa Mama Hidaya,’ ikiwa ni sehemu mashuhuri sana, na si kwa sababu ilikuwa katikati ya jiji, bali kutokana na huduma bora zilikuwa zinatolewa pale kwa wateja. Wengi wao waliokuwa wanafika pale, wakiwa watu wakubwa wenye fedha zao, ambao walikuwa wakifika kwa magari ya kifahari wakiyathaminisha gharama yake!

Mama Hidaya Songoro, alikuwa ni mwanamke mrembo wa kimanyema, ambaye, si tu yeye alikuwa shangingi, bali pia alifuga wanawake, wasichana wazuri wa kila rangi, weusi, weupe, maji ya kunde na nyinginezo. Walikuwepo, Waarabu, Wahindi, Wasomali na wengineo, ambao walimwita kwa jina la ‘Anti.’ Yeye mama Hidaya alikuwa hajazaa mtoto hata mmoja, na huyo Hidaya mwenyewe, ambaye alikuwa anafanya biashara ya kuuzia bia kule uani, alikuwa mtoto wa binamu yake. Lakini hilo walilijua watu wachache sana, kwani alimlea tangu akiwa mtoto mdogo.

Usiku mmoja, Liston Kihongwe alikuwa ni mmoja wa wateja waliokuwa wamefika pale kujipatia kinywaji ikiwa ni sehemu aliyokuwa ameizoea sana. Alikuwa amekaa katika sebule nadhifu akinywa bia yake taratibu na pengine akiangalia runinga iliyokuwa ikiendelea na vipindi vyake. Kwa upande mwingine alikuwa akitaniana na Mama Hidaya, ambaye alikuwa na umri wa miaka arobaini na arobaini sita hivi, lakini akiwa bado anang’aa kama kigori kutoka na matunzo aliyokuwa akijitunza.

“Mama Hidaya...” Liston alimwita.

“Bee,” Mama Hidaya akaitikia huku akimwangalia kwa macho yake malegevu, yaliyokuwa yamelishwa kungu. Pia nyusi zake zilikuwa zimekolezwa kwa wanja.

“Kwa nini uko tofauti na wanawake wengine?” Liston akamuuliza.

“Tofauti yangu nini?”

“Ninaijua mwenyewe...”

“Una maana gani? Nina matiti matatu?”

“Hapana, una mawili kama kawaida. Tena vifuu vya nazi, yanamshinda hata mwanamwali aliyewekwa mkoleni...”

“Kumbe nina tofauti gani?”

“Nina maana katika ‘seksi.’ Sijawahi kukutana na mwanamke mtundu kama wewe. Unaweza kumfanya mwanaume asiye rijali awe rijali. Ni halali kukumba shilingi milioni moja kwa usiku mmoja.”

“Ehehehe!” Mama Hidaya akacheka. Alipenda sana kusifiwa kwa maneno kama yale, pengine kila mwanamke alipenda kuambiwa hivyo hata wale wabaya kama ukuta wa choo!

Baada ya kumaliza kucheka, Mama Hidaya akaendelea kusema, “Basi, iko siku utakuja kutoa milioni kumi kwa moyo mweupe kabisaa!”

“Sipingi kwa hilo...” Liston akasema na kuongeza. “Lakini umeupata wapi ujuzi huo mwanamke wewe? Mkoani Kigoma au Manyema ya Congo DRC?”

“Umanyema mwakwetu,” Mama Hidaya akasema na kuendelea. “Baba yangu alitutelekeza mimi na mama yangu, nikiwa na umri wa miaka mitano. Ndipo niliposafiri na mama yangu, kuja hapa Dar es Salaam, baada ya kumaliza elimu ya msingi tu. Nilipofika hapa ndipo nilipoendelea ma masomo ya sekondari hadi nilipomaliza kidato cha nne...”

“Sasa nani aliyekufundisha seksi? Au ulirudi Kigoma tena?”

“Hapana, nimejifunza hapa hapa Bongo, kwani makungwi wako wengi, ambao walikuwa mashoga za mama yangu, Aisha Binti Songoro. Nilihamia Kigamboni kwa kungwi mkuu kwa miezi miwili kwa ajili ya mafunzo, ambayo yalikuwa si mafunzo bali mateso matupu. Wiki ya kwanza ilikuwa ni kuchapwa na kulia tu. Mizungu ndivyo ilivyo, ni unyago huo!”

“Ukoje mizungu hiyo?”

“Iko siku nitakuonyesha,” Mama Hidaya akasema. “Siku hiyo ndiyo utakayotema shilingi milioni kumi kwa hiari yako mweyewe!

“Aise, mabinti zako je, nao pia ni mabingwa kama wewe?”

“Kwa nini usijaribu mwenyewe?”

“Yaani wewe hutajali, wakati nimeshakupitia?”

“Kwa nini nijali? Wewe hukuja kuoa hapa! Umekuja kupata huduma na kuondoka zako. Ndiyo kazi inayotuweka na kutuvisha mimi na binti zangu. Je, nikuitie mmoja? Au wawili? Ni pochi lako tu!”

“Hapana, siyo leo,” Liston akamwambia Mama Hidaya huku akicheka kicheko cha chini.

Ukweli ni kwamba, Mama Hidaya alikuwa hachoki, hasa akizungumzia suala linalohusu Ngono! Alikuwa mtaalam wa mada hiyo, ambapo alitaka kuendelea, lakini simu ya mezani iliyokuwa pale sebuleni iliita. Hivyo akaichukua na kuiweka sikioni.

“Haloo...Mama Hidaya hapa...” Mama Hidaya akasema huku amekamata kiwiko cha simu.

“Ah, mpenzi...habari za hapo...” sauti nzito ya mtu, mwanamume ilisikika upande wa pili wa simu.

“Habari ni nzuri...ni nani mwenzangu?” Mama Hidaya akauliza.

“Mimi naitwa Zakwa!”

“Nani?” Mama Hidaya akauliza.

“Nimesema Zakwa!” Sauti ikajibu na kuendelea. “Vipi mama mwenye sauti nzuri, wewe hujawahi kusikia jina hilo hilo hapa jijini?”

“Sijui kama nimewahi kulisikia…” Mama Hidaya akasema na kuongeza. “Hivi kuna mtu anayeitwa Zakwa hapa jijini?”

“Ndiyo, mtu huyo yupo. Ina maana huamini?”

“Naweza kuamini au nisiamini...”

“Basi, ndiye huyu unayezungumza naye muda huu. Hapa Dar es Salaam usishangae mambo mpenzi...”

“Ningependa kukuona basi...mbona waongelea kwenye simu angali sura yako siifahamu?”

“Kuniona umeshaniona. Tatizo liko kwenye kunitambua. Awe mwanamke au mwanaume hawezi kuishi zaidi saa ishirini na nne. Hivyo si rahisi mtu anitambue mimi ni nani. Nakushauri usiombe kunitambua!”

“Umesema nimewahi kukuona?”

“Ndiyo.”

“Wapi?”

“Hapo hapo nyumbani kwako, Mzambarauni...nimeshawahi kufika mara kadhaa...”

“Siamini..”

“Tatizo ni kwamba, ninapokuwa hapo kwako, hata baba yangu mzazi hawezi kunitambua kwa jinsi nilivyojibadilisha. Na ninapokuwa mtu wakawaida, nakuwa mtu maarufu sana hapa nchini. Mtu mwenye hadhi kubwa, na ninayependwa na kila mtu, hata askari polisi. Huwezi kunituhumu kama mimi ni mtu wa aina yake! Zungu la Unga!”

“Si umeshanipa fununu kuwa wewe ni nani. Basi, ukija tena hapa Mzambarauni, nitakutambua...”

“Thubutu. Kwani una mteja mmoja tu mwenye hadhi kubwa?”

“Hapana, wako wengi. Wengine ni Mameneja wa makampuni makubwa, wengine wabunge...na wawili au watatu ni mawaziri wenye wadhifa serikalini.”

“Unaona?” Upande wa pili ukasema.“Hivyo huwezi kujua mimi ni nani kati yao!”

“Aisee, sasa ulitaka nikusaidie nini kwa leo? Mtoto wa kike, au mimi mwenyewe?”

“Huwezi kunipata kipumbavu hivyo. Na nimeshakwambia usijaribu kugundua mimi ni nani, ni mbaya sana. Au umechoka kuishi?”

“Sasa kumbe unataka nini?” Mama Hidaya akasema kwa karaha! Yeye na watu wa vitisho walikuwa mbali sana. Halafu akaendelea kusema:

“Au umenipigia simu unisalimu, na kunitisha?”

“Hapana, sikutishi. Nimekueleza ukweli, ni juu yako kuzingatia au kutozingatia!”

“Ok, unataka nini?”

“Nataka kuzungumza na mtu mmoja ambaye muda huu yupo hapo nyumbai kwako. Anaitwa Liston Kihongwe! Umenipata?”

“Ndiyo, yupo. Subiri kidogo...” Mama Hidaya akamwambia,



*******

Mama Hidaya akampatia mkonga wa simu Liston akimwambia, “Simu ya Zakwa...anataka kuongea na wewe…”

Liston akaupokea ule mkonga wa simu kana kwamba alikuwa hataki. Halafu akauweka sikioni na kuanza kusikiliza kwa makini:

“Haloo...” Liston akasema kwa sauti ndogo.

“Ni Liston?” upande wa pili Salum Zakwa akauliza.

“Ndiyo, ni mimi Liston, unasemaje ndugu yangu?”

“Mimi ni Salum Zakwa Mnube. Je, ni jina geni kwako?”

“Hapana, si geni sana. Je, unasemaje bwana mkubwa?”

“Ndiyo, Liston. Hakika jina lako pia sigeni kwangu. Nimefanya uchunguzi na kugundua kuwa wewe ndiye mtemi hapa jijini Dar es Salaam....na pia mtu mwaminifu sana!”

“Kwa hivyo unasemaje?” Liston akauliza. Lakini alishakuwa na fununu kuwa, Salum Zakwa Mnube alikuwa akimhitaji kwa kazi maalum!

“Nataka kukuajiri!”

“Kuniajiri?”

“Ndiyo!”

“Kuniajiri kazi gani?”

“Tutakapokutana nitakwambia…”

“Mimi siuzi unga kama wafanyavyo mafala wengine!” Liston akamwambia kwa hasira!

“Ahahahaaaa!” Salum Zakwa akacheka sana. Halafu akaendelea kumwambia. “Inaelekea unajiamini sana kijana! Ina maana huniogopi?”

“Hapana! Hakuna mtu ninayemuogopa hapa duniani. Namuogopa Mungu tu kama kweli yupo!”

“Inaelekea hata Mungu humuogopi. Kutokana na utemi wako, na kauli yako. Pia, yaelekea huna hakika kama Mungu yupo au hayupo. Wanaomuogopa Mungu, wanaamini asilimia mia moja yupo!” Salum Zakwa akamwambia kwa msisitizo!

“Ni wanafiki watupu. Vinginevyo Misikitini na Makanisani yangefurika kila siku, siyo Ijumaa na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani au Krismasi. Na kama kweli yupo, kwa nini aache vitendo vya kishenzi vitendekea hapa duniani?” Liston akamwambia kwa hasira!

“Wenyewe wanasema Mungu hataki kuviingilia vitendo vya binadamu hapa duniani. Anatuacha tutende tutakavyo, wewe na mimi. Hukumu ni huko ahera!” Salum Zakwa akaendelea kumwambia.

“Ndiyo kusema tukiwa hai Mungu anatuogopa? Anatusubiri mpaka tukifa ndiyo atuadhibu?”

“Sikiliza Liston...mimi si mtaalam wa dini...” Salum Zakwa akamwambia kwa sauti ya upole.

“Hata mimi vilevile, sasa kama tumemaliza mazungumzo yetu, acha tuagane. Kama nilivyokujulisha, mimi situmii wala sishughuliki na unga, au dawa za kulevya!” Liston akasema.

“Hilo nalifahamu. Kama nilivyokwambia, nimekuchunguza sana, na kugundua kuwa wewe ndiye kiboko yao hapa jijini, na pia ni mwaminifu sana. Hupendi kumzunguka mtu baada ya mapatano. Adui yako ni yule anayekuzunguka, na ndiye unayempiga, na unapompiga unampiga kiuhakika! Huyo ndie mtu ninayemtaka!”

“Lakini mimi sishughuliki na unga!” Liston akasema kwa ghadhabu!

Ukweli ni kwamba alikuwa ameshachoshwa na huyo mtum aliyejiita Salum Zakwa Mnube! Lakini cha ajabu ni kwamba alishindwa kukata mawasiliano. Alipendelea aendelee kuzungumza naye!

“Hilo nalifahamu, nimegundua kuwa hutumii wala hujihusishi na biashara ya unga na dawa za kulevya. Nimeambiwa vitu hivyo unavichukia!”

“Umeambiwa na nani?”

“Nina watu wengi sana ninaowatumia. Wengine ni askari polisi wa kawaida, na wengine ni maafisa. Sina shida ya kupata taarifa, si unajua jinsi fedha inavyoweza kufanya kazi hapa duniani. Na kwangu fedha ni kitu poa kabisa!”

“Kwa hivyo?”

“Hivyo nitakupa kazi hiyo. Sina shida ya wauzaji, ninao wa kutosha. Nina shida ya Mpambe!”

“Nilidhani mtu kama wewe huwezi kukosa Mpambe!”

“Ninao kadhaa, lakini ni vijana wadogo, na karibu wote wanatumia unga. Ujasiri wao ni wa bandia, hata mbwa koko akibweka, wanakimbia. Pia, wana tamaa ya ajabu, hawaridhiki na ujira ninaowapa, ingawa nawalipa vizuri sana. Nashindwa kuwaamini!”

“Kwa hivyo?”

“Ninahitaji mtu mzima kama wewe, jabali usiyeogopa chochote, na asiyetumia dawa za kulevya. Nataka uwe mpambe wangu mkuu ili yeyote yule akileta upumbavu umkomeshe. Je, unasemaje?”

“Inategemea ujira wangu.”

“Hilo lisikusumbue. Nimeshakwambia fedha siyo tatizo kwangu na sina choyo. Nitakupa kiasi chochote utakacho. Mradi tu kiwe kiasi cha kuridhisha na kazi iwe ya kuridhisha...”

“Mimi sifanyi kazi isiyoridhisha. Na ikitokea kwa bahati mbaya au sababu moja au nyingine, nikaboronga, huwa sidai malipo!”

“Safi! Huyo ndiye mtu ninayemtaka!”

“Kuanziam lini?”

“Sasa hivi. Baada ya nusu saa, mtu wangu atakufuata hapo kwa Mama Hidaya!”

“Sawa, namsubiri...”

Baada ya maongezi yao yaliyochukua muda mrefu, simu ikakatwa na Liston akaurudisha ule mkonga wa simu.

“Mmemalizana?” Mama Hidaya akamuuliza.

“Na nani?”

“Na huyo uliyekuwa unaongea naye...”

“Ndiyo...”



********

Baada ya nusu saa, gari moja la kifahari aina ya Mercedes Benz la rangi ya fedha lilisimamishwa nje ya nyumba ya Mzambarauni, mtaa wa Kipata. Halafu akashuka kijana mmoja mtanashati aliyevalia nguo nadhifu, aliyetumwa na bosi wake, Salum Zakwa, kwenda kumchukua Liston. Baada ya kuingia mle ndani, alitafuta sehemu nzuri iliyokuwa na nafasi, halafu akakaa huku akiangaza macho yake pande zote.

Liston aliyekuwa amekaa upande wa pili, umbali mfupi tu, aliweza kumwona kijana huyo tangu alipokuwa anaingia mle ndani. Akiwa ni mtu mwepesi kutambua na kunusa harufu za watu, hata wakiwa ni makachero, alinyanyuka na kutoka nje, na wakati akimpita yule kijana, alimpa ishara kuwa amfuate kule nje. Kijana huyo naye alinyanyuka na kumfuata nyuma hadi walipolifikia lile gari pale lilipokuwa limepaki.

“Natumaini bosi amekutuma,” Liston akamwambia bila hata kumsalimia.

“Ndiyo, bosi amenituma,” kijana huyo akasema huku akichezea funguo za gari alizokuwa ameshika mkononi.

“Tunakutana naye wapi?”

“Tutamkuta sehemu anatusubiri…”

“Sehemu gani sasa?” Liston akaendelea kumuuliza.

“Atanijulisha kwa simu mara tutakapoondoka hapa. Huo ndiyo utaratibu wake alioupanga bosi…” kijana yule akasema kwa sauti ndogo.

“Sawa, twende…” Liston akamwambia kijana huyo, halafu

akazunguka upande wa kushoto mwa gari lile.

Liston akaufungua mlango na kuingia. Halikadhalika kijana yule naye aliufungua mlango wa kulia na kuingia ndani upande wa dereva. Akalitia moto na kuliacha linanguruma kwa mda, halafu kabla ya kuliondoa, akatoa simu yake na kuwasiliana na Salum Zakwa.

“Bosi, timamu kama ulivyoniagiza…” kijana akamwambia mtu aliyekuwa upande wa pili wa simu.

“Umeshaonana naye?” sauti ya upande wa pili ikamuuliza.

“Ndiyo, niko naye ndani ya gari…”

“Ok, njoo naye hadi hapa Baraka Pub, mtaa wa Jamhuri…”

“Sawa, bosi.”

Kijana yule alilioondoa gari katika mtaa wa Kipata, kuelekea katikati ya jiji ilipo Baraka Pub. Muda wote huo, Liston alikuwa akiyafuatilia maongezi yao hadi pale walipomaliza kuongea. Ukweli ni kwamba alishangaa sana juu ya huyo mtu aliyejiita Zakwa, jinsi alivyokuwa akijificha sana, hata hivyo kwa watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya wala hakushangaa sana.

“Amesema tumkute wapi?” Liston akamuuliza baada ya kuona kijana huyo amenyamaza kimya.

“Tutamkuta Baraka Pub, mtaa wa Jamhuri,” kijana akamjibu.

“Poa,” Liston akasema bila kuongeza neon lolote.

Lakini hata hivyo Liston akawa bado anajiuliza ni kwanini wakutane katika mazingira yale, hasa ukizingatia Salum Zakwe alikuwa ni mtu mkubwa ambaye hakulingana na mazingira ya kukaa katika sehemu hiyo. Yeye alikuwa ni mtu wa kukutana naye katika hoteli zenye hadhi kama, New Africa Hotel, Holiday Inn na nyinginezo. Hata hivyo akatulia huku akimwangalia kijana alivyokuwa akikatiza katika mitaa kadhaa ya jiji hadi alipofik akatika mtaa wa Jamhuri.

Baada ya kufika katika mtaa huo, kijana yule aliufuata mtaa mdogo unaoelekea eneo la Kisutu, nyuma ya Zanzibar Hotel. Ni eneo ambalo wanaishi raia wengi wenye asili ya kiasia, hivyo basi akaliendesha gari hadi nje ya Baraka Pub iliyoko katika makazi ya watu, ambayo kwa wakati huo wa usiku wa saa tatu hivi, palikuwa kimya na ni magai machache tu yaliyoonekana yakikatiza. Kimandhari, eneo hilo lilikuwa limezungukwa na ukuta, huku kukiwa na geti dogo la kuingia mle ndani.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Wote wawili walishuka kutoka garini, halafu wakaingia mle ndani. Kwa ujumla eneo hilo lilikuwa lina taa zenye mwanga hafifu wa rangi kiasi cha kutoweza kumwona mtu vizuri. Wateja walikuwa ni wachache tu, wakiwemo waasia na waswahili wachache waliokuwa wakila na kunywa. Muda wote huo Liston alikuwa amenyamaza kimya tu, akimfuata kijana yule alipokuwa anaelekea, hadi walipofika mwisho kabisa palipokuwa na meza iliyokuwa na viti vitatu. Kiti kimoja wapo kilikuwa kimekaliwa na mtu mmoja aliyekuwa amevalia kofia kubwa na miwani mieusi, alikuwa amekaa pake yake akivuta sigara. Alikuwa ni salum Zakwa Mnube!

“Karibu!” Sauti nzito ilisema. Ni sauti iliyotoka kwa Salum Zakwa aliyekuwa amekaa peke yake.

“Ahsante,” Liston akasema huku akijikalia kwenye kiti.

“Wewe Peni unaweza kwenda kumsubiri kwenye gari, nikimaliza mazungumzo nitakuita,” Salum Zakwa akamwambia yule kijana ambapo kwa muda ule ndipo Liston alipojua kuwa alikuwa anaitwa Peni.

“Sawa, bosi,” kijana Peni akasema huku akiondoka kuelekea nje.

“Ndiyo Liston, karibu sana,” Salum Zakwa akamwambia.

“Nimekaribia,” Liston akasema huku akiendelea kumwangalia Salum Zakwa.

“Nimekuita tukutane hapa,” Salum zakwa akaendelea kusema na kuongeza. “Natambua kuwa hii si sehemu ya hadhi yangu nikiwa mtu mzito serikalini, lakini imenibidi nifanye hivyo kutokana na shughuli zangu ninazofanya, ambao ni za haramu.”

“Hakuna shaka, hata hapa panafaa, ili mradi ulichoniitia kieleweke,” Liston akamwambia Salum Zakwa.

“Vizuri sana. Sasa bila kuzunguka sana, natumaini unanifahamu sivyo?”

“Nakufahamu,…”

“Kama tulivyoongea kwenye simu, mimi ninahijai mapambe wa kunilinda. Nimetuma watu wangu wakakuchunguza na kuona kuwa wewe unanifaa sana….” Salum Zakwa alimweleza kirefu na shughuli zile za biashara haramu ya dawa za kulevya. Mwishoni akamalizia. “Sasa tuongee kikazi, mimi nataka kukuajiri, na nitakulipa vizuri sana, mshahara mkubwa na marupurupu kibao!”

“Unataka kuniajiri sivyo?” Liston alirudia kuuliza.

“Ndiyo manaake, na ndicho nilichokuitia!”

“Ok, mimi niko tayari, tupange taratibu za kazi…”

Baada ya kukubaliana, Salum Zakwa na Liston walipanga hili na lile kuhusu maslahi kwa ujumla, ndipo walivyokubaliana kufanya kazi wote.

Basi, hivyo ndivyo Liston Kihongwe, rafiki yake na Vasco Nunda, alivyokutana na Salum Zakwa, ambaye alikuja kumwajiri na kuwa “Mpambe” wake, wakiongozana katika kila sehemu anapokwenda katika mishughuliko ya kibiashara na nyinginezo!





*******

Hali ya hewa ilikuwa nzuri na bahari ilikiwa imetulia kiasi, huku upepo mwananana ukivuna na kutoa burudani ya pekee. Giza lilikuwa limeenea kote na mwanga wa taa uliweza kuonekana kwa mbali kidogo kutoka kwenye majengo ya hoteli ya Mikambo Beach, iliyokuwa umbali wa mita

hamsini kutoka katika sehemu maalum ya kupumzikia watu wanaofika kupunga upepo.

Muda huo wa saa moja za usiku. Watu watatu walionekana wamekaa juu ya kiti cha zege, ufukweni mwa Bahari ya Hindi, eneo hilo la Mikambo Beach, Kigamboni.Walikuwa wakipanga mikakati yao ya kazi iliyokuwa inawakabili mbele yao, kama walivyokuwa wamepanga bada ya kukutana wiki moja iliyopita.

Kama kawaida, watu hao watatu walikuwa ni, Salum Zakwa, Vasco Nunda na Liston Kihongwe. Walikuwa wamefika pale zaidi ya nusu saa iliyopita, kila mmoja akifika kivyake hasa kwa Salum Zakwa, ambaye hakutaka kamwe hajulikane nyendo zake na watu waliokuwa wanamfuatilia.

“Tumekutana hapa tena...” Salum Zakwa akawaambia huku akipuliza moshi mzito wa sigara hewani.

“Sawa bosi...” wote wakajibu huku mwakimwangalia.

“Basi, leo ndiyo ile siku ya kumfungia kazi na kumuondoa duniani mtu wetu, Abdul Zengekala. Na kazi hiyo ni kipimo kwa wewe Vasco Nunda, ambaye unajiunga na mtandao wangu, sijui unanipata?”

“Ndiyo, nakupata…” Vasco Nunda akamjibu huku akimwangalia kwa makini Salum Zakwa, ambaye alikuwa akiongea huku naye akimwangalia kwa kupitia kwenye ile miwani mieusi aliyoivaa. Ni miwani iliyoonekana chini ya kofia kubwa ya pama aliyokuwa amevalia.

“Haya, nisikilize kwa makini...” akasisitiza Salum Zakwa.

“Sawa, mkuu...nakusikiliza…”

“Ni hivi, huyu Abdul Zengekala, anaishi katika nyumba yake iliyoko mtaa wa Undali, eneo la Upanga. Lakini sitaki mumfuatilie nyumbani kwake, bali mumtafute katika sehemu ile anayopenda kwenda kustarehe kila mara. Huwa anapendelea kwenda katika Hoteli ya Afriko, iliyoko mtaa wa Samora. Humo huwa anakwenda na kuingia ndani ya Casino, ambapo pia hucheza kamari, mchezo ambao huwa anaupendelea sana...” Salum Zakwa akanyamaza kidogo.

“Basi, hapo ndiyo itakuwa kituo chenu cha kwanza kumfuatilia. Baada ya kuingia ndani...” akaendelea kusema Zakwa. “Mtatukuta tumekaa naye katika meza moja tukicheza mchezo wa kamari. Hapo mimi nitawapa ishara zote wakati huo yeye akiwa amezamia katika uchezaji wa kamari, natumaini atakuwa anatoka mara kwa mara kwenda chooni kujisaidia kutokana na pombe anazokunywa. Sikufundishi kazi Vasco, nafikiri utakapopata nafasi ya kwenda kummaliza na kumwacha huko huko chooni, sijui umenipata?”

“Nimekupata bosi...” Vasco Nunda akaitikia kuashiria kuwa alikuwa amemuelewa boasi wake mpya, ambaye kwa muda ule alikuwa anataka kumpa mtihani wa kuweza kumuajiri awe mpambe wake.

“Haya, mimi sina zaidi, na kwa utaratibu wangu huwa sipendi kuongea mambo mengi sana. Ninachohitaji ni vitendo tu, hata Liston anajua hilo!” Salum Zakwa akaendelea kumwambia Vasco kwa msisitizo!

“Nimekuelewa bosi, natumanini na mimi ni mtu wa vitendo zaidi,” Vasco Nunda naye akasema.

“Sawa, mimi nikitoka hapa, naelekea Hotel Afriko, kukutana na wafanyabiashara wenzangu wawili, Alfred Kwega na Maiko Nilla, akiwemo yeye Abdul Zengekala. Haya, kazi kwako!”

Baada ya kupeana majukumu yale, Salum Zakwa aliondoka kwa mwendo wa taratibu kama kivuli, halafu akaliendea gari lake alilokuwa ameliacha mbali na pale. Vasco na Liston wakabaki wakimwangalia hadi alipopotea machoni mwao. Ni harufu ya moshi wa sigara aliyokuwa anavuta ndiyo ulioweza kusikia nyuma yao!

“Vasco,” Liston akasema.

“Niambide mtu wangu…” Vasco akaitikia.

“Kumekucha ndugu yangu…twen’zetu!”

“Na kweli!”

Vasco na Liston walijiondoa eneo lile la ufukweni mwa bahari na kulifuata gari lao lililokuwa katika sehemu ya maegesho. Wakapanda na kuondoka kuelekea Hotel Afriko, iliyoko katikati ya jiji la Dar es Salaam. Kwa muda wote Vasco alikuwa akiiwazia ile kazi aliyokuwa amepewa ikiwa ni kipimo chake cha kuajiriwa na Salum Zakwa. Ni kazi iliyombidi aifanye kwa ufanisi wa hali ya juu ili aweze kujenga uaminifu dhidi ya bosi wake mpya!

Msururu wa magari yaliyokuwa yanatokea Kigamboni haukuwa mkubwa sana mara walipofika katika kivuko, kwani waliunga foleni katika magari matatu yaliyotangulia, na kivuko kilipofika, gari lao liliingia na safari ya kuelekea ng’ambo ya pili ikaanza. Walipofika wakatoka ndani ya kivuko na kuendelea na safari yao huku wakiongea hili na lile katika kupeana moyo juu ya kazi ile waliyokuwa wanakwenda kuifanya, kumkabili Abdul Zengekala, aliyetekiwa kuwajibishwa haraka iwezekanavyo.

Hatimaye waliifuata Barabara ya Kivukoni hadi walipofika Posta ya zamani, ambapo walipinda kulia kuufuata mtaa wa Azikiwe hadi katika Sanamu ya Askari kwenye mzunguko wa makutano ya mtaa huo na mtaa wa Samora. Wakaufuata mtaa wa Samora hadi walipofika katika hoteli hiyo ya Afriko, iliyoko ndani ya jengo la ghorofa kumi. Ni jingo lililokuwa limepangishwa na ofisi za taasisi mbalimbali, huku hoteli ile ikiwa moja wapo. Hoteli hiyo ilichukua upande mmoja wa chini, ukifuatia na ghorofa ya kwanza, ya tatu na ya nne, ambapo pia palikuwa na kumbi mbili kubwa kwa ajili ya sherehe za harusi au hata kwa mikutano. Pia, katika ghorofa ya tatu, ndipo palipokuwa na Casino, iliyokuwa inahudumia wateja wa aina mbalimbali.

Liston alilipaki gari katika maegesho yaliyokuwa mbali kidogo upande wa pili wa Barabara ya Sokoine, ambapo palikuwa na magari mengine yamepaki. Halafu wakashuka na kuivuka barabara na kuelekea usawa wa lango kubwa la kuingilia mle hotelini na hatimaye wakaingia kama vile walikuwa wateja wa kawaida tu. Waliweza kuwapita walinzi wa kampuni ya ulinzi ya binafsi waliokuwa wanalinda pale, ambao hata hawakuwashtukia kama walikuwa ni watu waovu kwa jinsi walivyokuwa wamevalia nadhifu.

Baada ya kuingia ndani, Liston na Vasco walipandisha ngazi hadi katika ghorofa ya tatu, kwani hawakutaka kutumia lifti kwa sababu za kiusalama zaidi. Sehemu ile waliyofikia kulikuwa na ile Casino mashuhuri ambayo Abdul Zengekela anapenda kuingia na kuburudika. Mlangoni palikuwa na walinzi wengine ambao waliwapita na kwenda kwenye dirisha la kulipia kiingilio cha kuingia mle ndani ya Casino. Baada ya kulipia, wakaingia na kukuta wateja wakiwa wengi, wanaume kwa wanawake, ambao wengi wa wanawake wale, walikuwa wamevalia mavazi ya nusu uchi.

Taa za mle ndani zilikuwa zinawaka kwa mwanga hafifu ambao haukuwa kero kwa watu waliokuwa mle ndani. Vasco na Liston wakajichukulia sehemu ya kupumzika, ambayo ni nzuri kwa kuwaangalia watu waliokuwa wanaingia mle ndani na kutoka. Waliamua kuelekea sehemu ya kaunta, kwenye viti virefu vilivyokuwa vimeizunguka ile kaunta, ambapo pia kulikuwa na wateja wengine wamekaa. Walikaa pale na kuagiza vinywaji, ambapo waliendelea kunywa huku wakiwaangalia, Salum Zakwa na wafanyabiashara wenzake, Josia Kessy, mmiliki wa hoteli ile, Alfred Kwega, Maiko Nilla na mtu wao, Abdul Zengekala anayetakiwa kufungiwa kazi usiku ule!







*******

Kwa muda wote, Salum Zakwa na wafanyabiashara wenzake walikuwa wakicheza kamari, mchezo ambao walikuwa wanaupendelea sana, kwani walikuwa wakicheza kiushindani na atakayeshinda angeondoka na kitita kiubwa cha fedha. Mbali ya kucheza kamari, pia walikuwa wakinywa pombe za bei mbaya kudhihirisha utajiri wao, na mara vilikuwa vikisikika vicheko vilivyokuwa vikitokea tumboni huku pia matumbo yao yakitikisika. Hakika ni watu ambao kwa muda ule hawakuwa na wasiwasi wa maisha kwa ujumla, ukizingatia walikuwa wanamiliki kiasi kikubwa cha fedha, kiasi cha kufanya fedha nyingine wazichezee tu katika mchezo huo wa kamari.

Abdul Zengekala alikuwa amejumuika ma wafanyabiashara wale walioko katika daraja la juu. Yeye alikuwa akinywa ile pombe aina ya Jack Daniels kwa kasi, na pia akicheza kamari, mchezo ambao alikuwa anaumudu sana akiwa mchezaji mahiri. Na kwa kiasi fulani alikuwa akiwala wale watu watatu, wafanyabiashara aliokuwa nao. Kwa ujumla hakuwa mtu mwenye fedha hapo alipo, isipokuwa ni ukaribu wake na mmiliki wa hoteli hiyo, akiwa ni mteja wake wa siku zote, na pia mfanyabiashara wa dawa za kulevya, akizichukua kwa Salum Zakwa. Basi, huo ndiyo ukaribu uliowafanya wajumuike wote.

Muziki uliokuwa ukitumbuiza kwa sauti ambayo siyo ya maudhi iliendelea kusikia humo ndani. Kila mtu alikuwa katika kile kilichompeleka ndani ya Casino hiyo. Hayo mambo ya kucheza kamari hayakuwahusu Vasco na Liston, walioingia humo ndani, kwani walikuwa wanamsubiri mtu wao, Abdul Zengekala, wapate wasaa wa kummaliza. Kitu ambacho kingemfanya Vasco aifanye kazi yake kwa uhakika zaidi, ilimbidi amsubiri mpaka aelekee chooni, halafu ndipo amfutilie na kumfungia kazi humohumo bila mtu yeyote kufahamu.

Kwa muda wote waliokuwa wamekaa pale kaunta ya kuuzia vinywaji, macho yao yalikuwa yakielekea kwa mtu wao, na hawakutaka kumpoteza hata sekunde moja. Walikuwa wanakunywa pombe lakini mawazo yao yote yakiwa kwa windo lao ambalo lilikuwa umbali wa mita kumi tokea pale walipokuwa wamekaa wao. Na kwa upande wake, Abdul Zengekala ambaye alikuwa hajui kilichokuwa kinaendelea, aliendelea kucheza kamari huku akinywa kwa furaha kinywaji chake, kama ilivyo kawaida yake.

Wanyabiashara aliokuwa anacheza nao walikuwa makini kucheza huku wakishangaa jinsi Abdul alivyokuwa anawala fedha zao kila wanapoingia raundi kitu ambacho kilikuwa kinawauma sana. Hata hivyo, baada ya muda, aliwaaga wenzake, kisha akanyanyuka kuelekea chooni kwa kupitia mlango mdogo wa kioo, ambao ulikuwa ni wa kuusukuma. Macho ya Vasco na Liston yakamsindikiza hadi alipoishia ndani ya mlango ule!

“Mambo safi sasa, naona mtu wetu anaelekea chooni,” Liston akamwambia Vasco.

“Ndiyo, anakwenda chooni kujisaidia…” Vasco Nunda akadakia huku akili yake ikimtuma cha kufanya!

“Hii ndiyo nafasi nzuri Vasco,” Liston Kihongwe akamwambia na kuendelea. “Nenda kamfungie kazi mlemle hakuna kumlazia damu!”

“Poa, naona huu ni muda muafaka kwa kumfungia kazi!” Vasco Nunda akasema huku akijiondoa pale kaunta kwa mwendo wa taratibu.

Ndani ya ukumbi ule wa Casino kila mtu alikuwa akiendelea na mambo yake, na wala hakuna aliyeshtukia juu ya ule mchezo unaotakiwa kuchezwa na wale watu wawili waliokuwa makini kwa kila hatua wanayopiga. Vasco Nunda akaendelea kumfuata nyuma Abdul Zengekela kama na yeye alikuwa anaelekea chooni kujisaidia. Hakuna mtu mwingine aliyejua kilichokuwa kinaendelea, zaidi ya Salum Zakwa Mnube, aliyekuwa umbali mfupi tu kutoka pale walipokuwa wamekaa!

Kazi hiyo!



********

Vyoo vya Hotel Afriko ni nadhifu kama ilivyo hoteli yenyewe yenye hadhi ya kitalii. Vilisafishwa na kupuliziwa hewa nzuri ya manukato karibu kila baada ya saa mbili, hivyo viling’aa na kunukia wakati wote. Hata hivyo, vyoo vya upande wa Casino vilikuwa bora zaidi kuliko vyoo ya sehemu nyinginezo. Si tu vilikuwa vya marumaru safi inayomeremeta na yenye vioo vya kujiangalia mwili mzima, bali pia vilisafishwa baada ya kila saa moja. Walikuwepo wahudumu makini kwa ajili ya kazi hiyo, ambao walikuwa pale kwa muda wote wa kazi.

Kwa hilo la kuwepo kwa wahudumu muda wote, kwa Vasco Nunda hakulifahamu kabisa, au tuseme hakulifanyia utafiti kabla ya kufikiria kuifanya kazi ile ya kumuua Abdul Zengekala, kazi aliyokuwa amepewa na Salum Zakwa. Basi, muda huo ndiyo alikuwa akimfuatilia kwa makini baada ya kuingia mle chooni kujisaidia. Choo cha wanaume cha upande wa Casino, kina vyumba sita vya kujisaidia haja ndogo na mabeseni sita ya kuoshea mikono.

Vasco Nunda alipoingia humo ndani akiwa hatua tatu tu, nyuma ya Abdul Zengekala, akamuona anaingia kwenye chumba kimojawapo na kujifungia. Vasco akaangaza humo ndani mlionururishwa kwa taa kali za mianzi. Mlikuwa kimya kabisa, ukiachia mdundo wa muziki uliosikia kwa mbali. Hapakuwa na mtu yeyote kwenye mabeseni ya kuoshea mikono, ilielekea choo kilikuwa kitupu muda huo, isipokuwa wao wawili tu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Hata hivyo, Vasco aliamua kuhakikisha kwanza, ambapo aliufungua mlango na kuhakikisha katika vile vyumba vine na kuchungulia ndani. Alikuta vyumba vilikuwa vitupu, na alipokuwa anaangalia chumba cha tano, ndipo Abdul Zengekela alipotoka na kwenda kwenye beseni moja wapo na kuanza kunawa mikono. Vasco alikuwa na hatua sita tu za kumfikia, ambapo alinyanyua hatua ya kwanza huku akikitoa kisu chake kilikuwa kisu cha spiringi, hivyo akakibonyeza kiachizi kisu kikachomoza pamoja na mlio hafifu uliolia, “Pup!” Lakini, Abdul Zengekela, kwa sababu tatu, hakuweza kuusikia mlio huo!

Kwanza, alikuwa ameshaanza kulewa. Pili, bomba la maji alilifungulia sana, maji yalifanya kelele. Tatu, mle ndani kulikuwa na mvumo hafifu wa muziki uliotoka kwenye ukumbi wa Casino. Hivyo Vasco akamnyatia hatua tatu huku akikikamata vizuri kusu kile cha inchi sita chenye makali pande zote mbili. Kilikuwa ni kisu maalum kwa mauaji na siyo cha jikoni. Alipokuwa anavuta hatua ya nne, akasikia mlango unafunguliwa. Ilikuwa ni sauti ndogo, kama ya mtu anayepumua kwa nguvu, lakini Vasco alisikia!

“Pumbavu!” Vasco Nunda akajisemea kimoyomoyo, na kwa kasi ya ajabu akakifunga kisu na kukirudisha mfukoni. Halafu akaenda kwenye beseni moja, ambapo alifungua maji na kujifanya ananawa mikono, akiutazama mlango kwa pembe ya jicho. Mhudumu wa hoteli ile aliingia na ndoo na vifaa vinginevyo vya kufanyia usafi, ambapo aliiweka ile ndoo chini na kuanza kufanya usafi kwa brashi maalum la kufutia maji yaliyomwagika chini.

Abdul Zengekela alipomaliza kunawa mikono, usoni na kusukutua mdomo, akajifuta kwa taulo. Halafu akatoka nje bila kujua kilichokuwa kinaendelea nyuma yake, kwamba kulikuwa na mtu aliyetaka kuuondoa uhai wake. Vasco aliyekuwa akimwangalia kwa uchungu mwingi, akasema tena, “Pumbavu sana!” Safari hii kwa sauti ya chini sana. Hata yule msafisha vyoo hakuisikia!

Vasco Nunda alitoka kule chooni na kuelekea kaunta, alipokuwa amekaa mwenzake, Liston. Muda huo Abdul alikuwa mbele yake akijikokota kuelekea katika ile meza walipokuwa wamekaa akina Salum Zukwa na wafanyabiashara wenzake wakicheza kamari. Macho ya watu wawili, Salum na Liston yalimuangalia kwa pamoja baada ya kuacha kumwangalia Abul. Walikuwa wakijiuliza imekuwaje tena ameshindwa kumshughulikia mtu wao wakati walikuwa wameingia wote mle chooni? Hawakupata jibu lolote zaidi ya kumsubiri yeye mwenyewe, Vasco atakavyowaeleza.

Vasco Nunda aliendelea kutembea hadi alipofika pale kaunta alipokuwa amekaa Liston. Akakaa kwenye kiti chake huku akivuta pumzi kwa nguvu na kuzitoa kiasi cha tundu za pua yake kutoa mlio mdogo kama filimbi. Kwa sauti ya utulivu, kama vile alikuwa anazungumzia kufunga goli katika mchezo wa kandanda, akamwambia Liston:

“Bro, imeshindikana...”

“Imekuwaje tena?” Liston akamuuliza huku akiitazama meza ya katikati na kumuona Abdul Zengekala akiendelea na mchezo wa kamari!







*******

Akatikisa kichwa!

“We acha tu,” Vasco akasema huku akijiwashia sigara. Halafu akaendelea. “Katika dakika ya mwisho kabisa kukamilisha kitendo, mshenzi mmoja akaingia!”

“Mshenzi gani?”

“Msafisha vyoo. Ilikuwa bahati yangu nilimsikia akiingia, la sivyo ingenibidi niue watu wawili, au nitoke mkuku hadi nje kabisa. Yule mshenzi ni lazima angepiga kelele baada ya kuona nimeua mtu mle chooni, sijui ingekuwaje!” Vasco Nunda akaendelea kusema huku akisikitika!

“Nilijua kuwa chooni hapakuwa mahali pazuri kwa kazi hii. Lakini sikutaka kukwambia, nikitaka kuuona ujuzi wako!” Liston akamwambia huku akicheka kidogo.

“Aisee, kumbe ulikuwa unanitega?”

“Sina maana hiyo. Lakini ukweli ni kwamba mimi nisingethubutu kuifanya kazi hii chooni. Pangetokea utata kama uliokutokea, nisingeweza kukimbia!”

“Ungewashughulikia wote wawili, Abdul na yule mwosha vyoo?”

“Je, yule mwosha vyoo angekuwa mwepesi kuliko mimi?”

“Ingekuwa hatari upu!”

“Ok, hebu tupange cha kufanya sasa...”

“Hakuna kilichoharibika. Tumvizie nje mpaka atakapotoka, natumaini huko hakutakuwa na kiwingu sana hasa ukizingatia saa hizi ni usiku..”

“Poa, ni nje, Twende tukamsubiri garini...” Liston akasema huku akiitazama saa yake ya mkononi. Ilikuwa inakaribia kufika saa saba na nusu za usiku.

Liston na Vasco walimaliza vinywaji vyao vilivyokuwa vimebaki katika glasi zao, halafu wakajitoa pale kaunta na kutoka kwa mwendo wa taratibu tu kama walivyokuwa wateja wengine. Baada ya kufika kwenye korido, hawakutaka kushuka kwa ngazi tena kama waliovyopanda nayo, bali walipanda lifti iliyowateremsha hadi kule chini, mwanzo wa ghorofa. Baada ya kutoka ndani ya lifti, wakatoka hadi nje ya hoteli kwa kupitia mlango mkubwa uliokuwa unatazamana na mtaa wa Samora.

Usiku ule hali ya jiji la Dar es Salaam ilikuwa imetanda ukimya wa pekee, na ni magari ya kuhesabu tu yaliyoonekana yakipita katika mtaa ule uliokuwa unakatiza mbele yao. Upande wa mbele ya hoteli, sehemu ya maegesho, magari ya wateja yalikuwa yamepaki upande wa pili. Hivyo, Vasco na Liston walisimama kwa muda huku wakiangaza macho yao pande zote, na kuwaona walinzi wawili wa hoteli ile, waliokuwa ndani ya kibanda chao kilichokuwa upande wa kushoto, ambao walikuwa makini sana na ulinzi wakijaribu kuangalia kila kinachoendelea.

Lakini Liston na Vasco hawakuwa na shughuli nao, bali waliamua kuelekea sehemu ile walikopaki gari lao Toyota Mark 11 Grande, upande wa pili wa barabara. Wakavuka na kuliendea na baada ya kulifikia, wakafungua milango na kuingia ndani, halafu wakabaki mle wakimsubiri Abdul atoke mle hotelini. Kwa muda wote walikuwa wakiyakodoa macho yao kuelekea usawa wa mlango wa kutokea!



********

Ndani ya ukumbi wa Casino bado kulikuwa kumechangamka. Muziki ulikuwa unaendelea kurindima kwa sauti ya kiasi, pia waliweza kuonekana akina dada waliokuwa wakizunguka huku na kule huku wamevalia mavazi ya nusu uchi kama siyo uchi kabisa. Pia, walikuwepo watu wa mataifa mbalimbali, wazungu, wahindi, waarabu na wengineo. Kwenye pembe za chaki waliweza kuonekana watu wamegandana wakiliwazana kimapenzi. Hayo ndiyo mambo ya Casino!

Katika meza ile ya katikati, wale marafiki wanne, Josia Kessy, mmiliki wa hoteli ile ya Afriko, Salum Zakwa, Mkurugenzi wa Shirika la Utafiti wa Udongo, Alfred Kwega, mfanyabiashara na Maiko Nilla, waliokuwa wanacheza kamari, wote kwa pamoja waliamua kuwa imetosha kucheza kamari kwa usiku ule. Hivyo ulikuwa ni muda muafaka wa kwenda kupumzika hasa ukizingatia ulikuwa ni usiku mwingi.

Mmiliki wa hoteli ile, Josia Kessy, na Abdul Zengekala, ambaye alikuwa amelewa na aliyeibuka mshindi usiku ule, hawakuwa na la kusema. Na ile ni kwa sababu mchezo wa kamari kwenye Casino, hauna raha kuchezwa na watu wawili tu, ilibidi mchezo ukome. Kwa kawaida, mchezo ukiisha, mtu alikuwa na hiari, ama ahesabu fedha yake kutathmini faida na hasara au kuinuka na kuondoka.

Kwa vile siku ile mshindi alikuwa ni Abdul, jambo ambalo halikuwa la kawaida, na alikuwa akihesabu kibunda cha maana pamoja na kulewa kwake, kila mmoja akaamua kuhesabu fedha zake. Bila shaka walitegemea baada ya kuhesabu, Abdul angetangaza kuvuna kiasi gani cha fedha ili kuwakoga wenzake. Ili kumhamasisha Abdul atangaze kiasi alichopata, kila mmoja baada ya kuhesabu kibunda chake, alitangaza faida au hasara aliyoipata. Hakuna aliyechuma!

Mtu wa kwanza kutangaza mapato na hasra zake alikuwa ni mfanyabiashara, Alfred Kwega, ambaye alisema, “Nimeliwa shilingi milioni moja, laki mbili na hamsini elfu...ahaaa!”

“Mimi nina bahati,” Maiko Nilla akasema. “Mimi nimeliwa shilingi laki saba na arobaini alfu!”

“Mimi nina bahati kuliko wewe,” Josia Kessy mmiliki wa hoteli akasema na kuongeza. “Nimeliwa shilingi elfu themanini tu...”

“Niangalieni mimi. Nimechukuliwa shilingi milioni mbili na laki moja na thelathini!” Salum Zakwa akasema.

“Ahahahahaaaa!” Wote wakacheka kicheko cha kitajiri!

Kila mtu alicheka pale, isipokuwa Abdul Zengekala tu, aliyekuwa akiendelea kuhesabu fedha zake, kijasho kikimvuja usoni inawa mle ndani kulikuwa na kiyoyozi. Bila shaka hakuwa hata na habari ya matangazo ya wenzake waliyokuwa wanatangaza jinsi walipoliwa fedha zao. Ingawa walicheka, lakini Josia Kessy, Alfred Kwega na Maiko Nilla, na Salum Zakwa, hakuna walichopoteza, kila mmoja kilikuwa kama ni biskuti tu kwake. Walikuwa wakimsubiri Abdul amalize kuhesabu, kila mmoja akajilegeza kitini na kufanya hili na lile.

Aliyevuta sigara, aliwasha, aliyekunywa pombe, aliinua glasi yake, na aliyetumia vyote alifanya hivyo. Lakini Abdul hakuwa na haraka, kwani aliendelea kuhesabu noti taratibu, pia akivuta sigara mfululizo na na akiishambulia wiski yake ya thamani. Hatimaye alipomaliza kuhesabu, akaanza kuziweka noti zake mfukoni mwake.

“Vipi Abdul?” Alfred Kwega akamuuliza.

“Vipi kitu gani?” Abdul akauliza.

“Hutaki kutangaza?”

“Kutangaza?” Akauliza. “Kwani nyie mmetangaza?”

“Ndiyo, hukutusikia?”

“Hapana, sikuwasikia mimi!”

“Umetula wote!”

“Oh, bahati mbaya sana...” Abdul akasema na kuendelea. “Lakini ni kama mjuavyo. Kila mtu ana siku yake.”

“Kama vile siku ya kuzaliwa na siku ya kufa?” Josia akamuuliza.

“Ndiyo manaake!”

Kila mtu akainuka, isipokuwa Abdul tu, alikuwa bado akishindilia noti mifukoni na chupa yake ilikuwa bado ina pombe kidogo sana. Baada ya kumaliza kushindilia fedha zake katika mfuko wa suruali, akajiweka vizuri na kurekebisha suti yake aliyokuwa amevalia. Kisha akaichukua ile chupa iliyokuwa na pombe kidogo, halafu akaimimina kwenye glasi. Akainyanyua na kupiga mkupuo wa nguvu, huku pia akikunja sura yake kutokana na ukali wa pombe ile, na alipomaliza, akafuta mdomo wake kwa kiganja cha mkono wake wa kushoto.

Alipohakikisha kila kitu kiko sawa, Abdul Zengekala akaanza kunyanyua hatua mja baada ya nyingine kutoka pale katika ukumbi wa Casino. Miguu ilikuwa mizito kutokana na ulevi aliokuwa nao, hakika alikuwa anaona maruweruwe!

********

Zilikuwa zimebakia dakika chache tu kutimia saa nane za usiku. Kwa vile haikuwa mwisho wa wiki, mbele ya Hotel Afriko palikuwa na magari machache sana, kama kumi au kumi na tano, kwani mengine yalikuwa yameshaondolewa na wateja waliokuwa wamefika pale kujiburudisha. Mlinzi mmoja alionekana akizunguka katika kuimarisha hali ya ulinzi kwa ujumla, na pia akisubiri fadhila kutoka kwa wateja wanaotoka ndani ya hoteli, ambao wengi wao humwachia kitu kidogo, kutokana na kuwalindia magari yao.

Upande wa pili sehemu ya maegesho, kwenye lile gari aina ya Toyota Mark 11 Grade, walikuwepo vijana wawili, Vasco Nunda na Liston Kihongwe, waliokuwa wakiutazama mlango mkubwa wa kutokea kule hotelini kwa muda wote waliokuwa pale, wakimsubiri mtu wao, Abdul Zengekala. Ingawa moja ya kazi yao ni uvumilivu, lakini kile kitendo cha kutomuona Abdul akitoka, kiliwachosha sana hasa ukizingatia palikuwa panaanza kupambazuka!







*******

“Hivi ulisema Abdul hana gari sivyo?” Vasco Nunda akamuuliza Liston.

“Ndiyo, hana,” akajibu Liston aliyekuwa amekaa nyuma ya usukani.

“Ni wazi mwenyewe kalewa. Usiku mwingi huu, na yeye anaishi Upanga. Hivi haawezi kupewa lifti na mmojawapo kati ya wale wanne anaocheza nao Kamari!”

“Sidhani,” Liston akajibu huku akiwasha sigara.“Abdul hawezi kuwa na urafiki na yeyote kati yao. Wale wanne ni matajiri sana. Nashangaa kwa nini wanacheza naye kamari!”

“Abdul anatambia fedha aliyomzika bosi, Salum Zakwa!” Vasco akakumbushia.

“Ndiyo, lakini utajiri wake ni kama shilingi milioni thelathini, tutaita utajiri. Ni wa muda na uko ukingoni, kama bado haujaporomoka!”

“Leo bahati imemkubali sana. Anaweza kuondoka na milioni kumi!”

“Kama ni mimi, nikiwa katika hali hali aliyonayo, nisingeondoka hotelini,” Liston akasema na kuongeza. “Ningechukua chumba na kulala hapahapa!”

“Abdul anaweza akafanya hivyo?” Vasco akauliza. Ni dhahiri wazo hilo halikumpendeza.

“Sijui...” akajibu Liston. “Lakini sidhani, kwanza Abdul hana busara, mtu yeyote anayejaribu kumzunguka, hana busara. Na pili, pombe ya kukithiri haiongezi busara, bali hupunguza!”

Vasco Nunda akashusha pumzi ndefu, akayaangalia magari yaliyokuwa hapo. Palikuwa na teksi mbili au tatu, na zote zilikuwa mbali. Hivyo akaridhika kimoyomoyo, na muda huohuo simu ya Liston ikaita. Akaitoa kwenye mfuko wa koti, na kuiweka sikioni, halafu akasema:

“Liston?” Upande wa pili wa simu ukasema. Wlikuwa ni bosi wake, Salum Zakwa Mnube!

“Ndiyo, bosi...” Liston akaitikia.

“Mko wapi?”

“Tuko mbele ya hoteli, sehemu ya maegesho...”

“Vizuri,” Salum Zakwa akasema. “Abdul yuko Casino, natumaini mlimwona, na mchezo umekwisha. Anajiandaa kuondoka...”

“Mimi naVasco tulikuwa hapo Casino, na tulimuona akiwa na kibunda kizuri cha fedha na amelewa. Je, hawezi akaamua kuchukua chumba na kulala hapahapa?”

“Akifanya hivyo nitakufahamisha, na kazi hii itafanyika kesho. Lakini sidhani kama atafanya hivyo, Abdul akijaa fedha, huwa ana tabia ya kwenda Mzambarauni, kwa Mama Hidaya, na kuchukua msichana mrembo wa kwenda kustarehe naye. Hata kama ikiwa ni saa kumi za usiku!”

“Basi, vizuri...” Liston akasema.

“Kwa hiyo nataka mkimtia mkononi mumpeleke ‘Chumba Namba Moja,’ nina maongezi naye muhimu sana! Au unahitaji msaada wa kuongezewa nguvu?”

“Hapana...sihitaji...”

“Mtaweza wenyewe?”

“Bosi, unadhani mimi na Vasco itatushinda kazi hii?”

“Lakini Liston. Vasco bado kinda, sijawa na uhakika na utendaji wake. Nataka kazi hii itendeke kiuhakika, sitaki mnisumbue bure kwenda Chumba Namba Moja!”

“Basi, leo utaona utendaji wake...hatatusumbue bure...” Liston akamwambia Salum Zakwa.

“Ok, nitaona...mkimpata Abdul mnifahamishe...”

“Sawa bosi...”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Sasa kaeni chonjo...Abdul katoka ukumbi wa Casino...” upande wa pili wa simu ulisikika Salum Zakwa aliyekuwa kule juu hotelini akimwambia Liston.

“Sawa, bosi…” Liston akasema. Halafu simu ikakatwa!

Kwa vile wote wawili waliyasikiliza mazungumzo yale, macho yao yakaelekea kwenye mlango wa mbele wa Hotel Afriko. Hoteli hiyo kama hoteli zote nyingine kubwa, ilikuwa na mlango wa nyuma pia, lakini huo ulikuwa hautumiwi na wateja. Ulikuwa maalum kwa ajili ya shughuli za hapo hotelini, kama vile kuingiza vitu vya kupikwa jikoni na bidhaa nyinginezo na kutolea takataka.

Hata hivyo, halikuwa jambo geni mteja kutumia mlango huo kama anajuana na watumishi wanaohusika au atahonga kiasi cha kutosha. Lakini ilikuwa kosa kubwa ambalo lingemfukuzisha kazi mtumishi mhusika.

“Je akitokea mlango wa nyuma?” Vasco Nunda akauliza huku akiipapasa bastola yake!

“Kwa nini afanye hivyo!” Liston akashangaa. “Kwani leo ni siku ya kawaida kama siku yoyote nyingine. Isipokuwa kavuna vizuri tu!”

“Ana bastola?”

“Hakuna mtu anayejihusisha na bosi, asiyekuwa na bastola. Lakini jinsi alivyolewa, na kama angali anayo, na kama kaja nayo, sidhani kama atakuwa na uwezo wa kuitumia!”

“Aisee, basi kuna kazi...”

“Si ndogo...”



********

Vasco Nunda aliiangalia saa yake ya mkononi. Ilikuwa imetimu saa nane na dakika tatu za usiku, halafu akayarudisha macho yake kwenye mlango wa mbele wa hoteli ya Africo. Ni watu wachache sana waliokuwa wakiingia wakati ule, lakini wengi walitoka na kuelekea kwenye magari yao au teksi na kuondoka isipokuwa Abdul Zengekala, mtu wao waliokuwa wanamsubiri kwa hamu kubwa.

Hatimaye Vasco na Liston, wakawaona wale marafiki watatu, Salum zakwa, Maiko Nilla na Alfred Kwega, wakitoka. Kama walivyoongozana, wote watatu wakaingia ndani ya lile gari aina ya Ranger Rover Vogue, la Salum Zakwa, ambapo kwa muda ule alikuwa akiliendesha mwenyewe. Kwega alikaa mbele pamoja na Zakwa, ambapo Maiko alikaa ule upande wa nyuma peke yake.

Gari likatiwa moto na kuondolewa katika eneo lile la Hoteli Afriko, kwa mwendo wa taratibu hadi lilipoingia katika Barabara ya Samora na kuishia mbele ya macho yao. Vasco akaiangalia tena saa yake. Ilikuwa imetimu saa nane na dakika kumi. Akamwangalia Liston na kumwambia:

“Inawezekana bosi, amekosea...”

“Sijamuona akikosea hata siku moja, acha kabisa!” Liston akamwambia Vasco.

“Nasema hivyo kwa sababu, pengine Abdul si mpumbavu kama mnavyodhani. Pengine kachukua chumba kule hotelini...”

“Sikiliza Vasco,” akasema Liston na kuendelea. “Kwa nini usimpigie simu wewe na kuzungumza naye? Wewe ni mmoja wetu sasa. Itumie simu yako kwa mara ya kwanza!”

“Hakuna shaka...” akasema Vasco.

“Unaikumbuka namba yake?”

“Ndiyo, naikumbuka...”

Halafu akatoa simu yake na kubonyeza namba ya simu ya Salum Zakwa. Alipojibiwa:

“Ndiyo!”

“Vasco!” Akasema na kukata simu!

“Huo ndiyo uzuri wako...hukawii kujifunza!” Liston akamwambia.

“Ahsante mwalimu wangu...” Vasco akamwambia.

Baada ya dakika tatu, simu ya Vasco ikaita. Akaiweka sikioni na kusema:

“Ni mimi Vasco, bosi...”

“Unasemaje?”

“Naona kumekuwa kimya hapa hotelini. Hatumuoni mtu wetu akitoka. Je, inawezekana amechukua chumba ?”

“Hajachukua chumba. Akichukua utaarifiwa, na nilisahau kuwafahamisha kuwa yule jamaa akilewa huwa hatumii lifti. Hutapika sana, hivyo hutumia ngazi, na katika hali aliyokuwa nayo, atatumia muda kuteremka kutoka ghorofani. Na pengine aende chooni kujisaidia katika kila ghorofa, hivyo fanyeni subira...”

“Sawa bosi...”

“Una uhakika mtaiweza kazi hii peke yenu?”

“Usiwe na wasiwasi bosi...”

“Ok, mkimpata tu, mnitaarifu. Hata kama ikiwa saa kumi za usiku, sawa?”

“Bosi,” Vasco akasema. “Abdul ametoka! Kazi imeiva, tutawasiliana...”

“Hakuna shaka…”

Vasco na Liston wakamwona Abdul Zengekela akitokeza kwenye mlango wa mbele wa Hotel Afriko. Baada ya kutoka, akasimama kwa nukta mbili tatu kwenye ngazi akiyumba na pia akivuta hewa safi nje ya hoteli. Akaangaza macho huku na kule, akitafuta teksi iliyoko karibu, ambapo aliiona ikiwa kama hatua arobaini kutoka alipo. Abdul kaanza kuifuata kwa hatua za taratibu huku akiyumba kiasi kwa ulevi.

Vasco akatoka ndani ya gari na kumfuata Abdul kwa hatua ndefu. Akamfikia akiwa angali yuko mbali na teksi ile aliyokuwa anaiendea. Akamwita kwa jina lake,“Haloo Abdul...”

“Yeah!” Abdul akasema huku akiendelea kutembea akijikaza asiyumbe.

“Naomba nisubiri, bosi, Salum Zakwa anataka kuzungumza na wewe...” Vasco akamwambia kwa sauti ambayo aliweza kuisikia.

“Hapana...hapana. Siwezi kuzungumza naye usiku wa leo, nimelewa...” Abdul akamwambia Vasco. Na wakati huo alikuwa ameshamfikia karibu na kumkinga kwa mbele yake!

Abdul akabaki ameshangaa!

“Unasema huwezi kuonana naye?” Vasco akaendelea kumuuliza. Mkono wake ukazama nyuma ya mgongo wake kiunoni, ambapo alichomoa bastola!

“Siwezi...nimelewa!”

“Unakiona chuma hiki? Bila shaka unakitambua. Hakina mzaha, haya twende zetu!”

“Mh, ni kitu gani hiki?” Akauza Abdul!

Ina maana ni kutekwa nyara?”

“Unaweza kukiita chochote kile utakacho. Ukweli ni kwamba, kama ujuavyo, bosi hapaendi kuona amri yake haikutiiwa. Ok, twende zetu!” Vasco akamwambia. Halafu akamshika mkono na kumpeleka kwenye gari lile, Toyota Mark 11 Grande.

“Shit!” Abdul akasema huku akitembea bila kupenda!



*******

Huku wakitembea, Vasco akampapasa Abdul, ambapo aligundua alikuwa na bastola aliyoichimbia kiunoni. Akaichukua na kuichomeka kiunoni mwake kwa tahadhari kubwa.

“Huwezi kuichukua bastola yangu!” Abdul akamwambia!

“Sasa hivi huihitaji,” Vasco akamwambia na kuendelea. “Umelewa, unaweza kuipoteza. Au hata inaweza kukudhuru wewe mwenyewe!”

Walipolifikia gari, Vasco akaufungua mlango wa nyuma na kumsukumia Abdul ndani. Abul akabaki akilalamika, akijiinua kujiweka vizuri kitini. Baada ya kumwingiza, Vasco naye akaingia garini na kumwambia Liston:

“Twen’zetu, Liston...”

“Nyie ni akina nani? Mbona siwajui?” Abdul akawauliza huku akijaribu kuwaangalia!

Liston akalitia gari moto huku akicheka. Akawasha taa ya humo ndani ya gari, halafu akageuza kichwa na kuuliza:

“Hata mimi hunijui?”

“Mh, Liston, nini kinachoendelea?”

“Bosi anataka kukuona...” Liston akamwambia huku akizima ile taa.

“Kuniona? Usiku wote huu?”

“Unauliza hivyo kana kwamba hujui kwamba bosi, huwa hatangazi sera zake, pengine anataka kukupa mzigo. Kuna mzigo ulioingia jana!”

“Unasema kweli?” Abdul akauliza kwa jazba!

“Ni kweli...”

“Lakini kama ni hivyo, kwa nini asiniambie wakati tulikuwa wote tukicheza kamari kule Casino?”

“Sijui. Pengine kuna mazungumzo kati yenu, kabla hujakabidhiwa mzigo. Nasikia una deni kubwa la nyuma, kitu kama milioni kumi!”

“Oh, ndiyo!” Abdul akakubali. “Hapa nina milioni tano, sijui itakuwaje!”

“Bosi atafurahi sana,” Liston akasema na kuendelea. “Hiyo ni dalili ya uaminifu. Sasa pumzika na uwe huru!”

“Ooohps!” Abdul akapumua, halafu akajipweteka kwenye siti mororo ya nyuma na kukipunguza kitanzi cha tai yake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Kidogo akawa na matumaini!

Vasco Nunda akaitoa simu yake na kubonyeza namba za simu ya Salum Zakwa. Alipoitikiwa, akataja jina lake na kuikata kama ilivyo ada. Baada ya dakika mbili, simu ikaita, naye akaipokea:

“Vasco hapa, bosi...”

“Vipi?” Salum Zakwa akauliza.

“Tayari, Abdul tunaye garini. Tuko njiani...”

“Vizuri sana. Je, palitokea tatizo lolote?”

“Hapana...”

“Vizuri. Basi, mpelekeni ‘Chumba Namba Moja,’ nitakuwa nanyi baada ya dakika chache...”

“Sawa, bosi...ni utekelezaji!”



********







ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog