Simulizi : Sura Mbili
Sehemu Ya Pili (2)
Kufuatana na mpangilio wa Salum Zakwa Mnube, ‘Chumba Namba Moja,’ ni sehemu iliyokuwa tulivu iliyoko ufukweni mwa Bahari ya Hindi, eneo la Kunduchi, kilomita nzima kutoka barabara kuu iendayo Bagamoyo. Palikuwa pamezungukwa na miti ya minazi iliyokuwa imefungamana na pia kuzungukwa na vichaka vilivyofanya eneo lile lijifiche sana. Hapakuwa mahali pa kumkuta mtu au watu wakibarizi hapo usiku wa manane, na mchana ndiyo palikuwa sehemu nzuri ya kuogelea hata ukiwa uchi.
Vilevile palikuwa na njia ya kienyeji kutoka barabara kuu hadi pale katika sehemu husika. Liston ambaye hakuwa mgeni na eneo lile, akaitumia kupita na gari lile, hadi walipofika karibu na ufukweni, sehemu yenye mchanga laini na mweupe. Akalisimamisha gari umbali wa mita hamsini kutoka baharini.
“Tumefika,” Liston akasema huku akilizima gari, lakini akiziacha taa zikiwaka.
“Oh!” Abdul Zengekela akaishia kuguna!
“Abdul, naamini wewe si mgeni na mahali hapa...”
“Siyo mgeni hapa...”
“Na wewe Vasco?”
“Hii ndiyo mara yangu ya kwanza kufika hapa...” Vasco Nunda akasema na kuendelea. “Mmepagunduaje?”
“Ahahaha!” Liston akacheka na kusema. “Ni bosi ndiye aliyepagundua hapa. Hata mimi nilikuwa sipajui, na utashangaa sehemu anazozijua, twende tukakae ‘Chumba Namba Moja’ tukapumzike tumsubiri bosi...”
Wote watatu wakashuka garini na kwenda kukaa kwenye gogo la mti wa mnazi, lililokuwa limemulikwa na taa za gari. Ni gogo lililokuwa linatumiwa na watu wanaofika pale katika saa za mchana, wakiwa ni waogeleaji au wanaojihusisha na shughuli za uvuvi. Baada ya kufika pale, Liston na Abdul wakakaa, lakini Vasco akabaki amesimama. Haukuwa usiku wa joto wala baridi, lakini upepo mwanana ulipepea kutoka baharini. Wote wakawasha sigara na kuanza kuvuta.
“Hapa ndipo shughuli nyingi za bosi hutendeka. Au siyo Abdul?” Liston akasema.
“Ndiyo, ndiyo...” Abdul akajibu kinyonge!
“Sasa kama bosi angekupigia simu na kukwambia uje hapa kuchukua mzigo, ungekujaje na hali gari lako umeliuza? Kama nijuavyo, bosi, huwa hapendi maajenti wake au sisi Wapambe wake tutumie teksi katika shughuli hizi!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Gari langu sijaliuza,” Abdul Zengekala akasema kwa kuongopa. “Nimemwazima rafiki yangu Nurdin Balawi. Ningeweza kulipata, au ningeazima gari la mtu mwingine...”
“Usiku wote huu?”
“Ndiyo,” akajibu Abdul kikakamavu. Ulevi ulikuwa unampungua, pengine kwa sababu ya upepo, na pengine kwa sababu ya matumaini ya kukutana na Salum Zakwa, na kuupata ‘mzigo’.
“Aisee...” Liston akaishia kusema.
“Eti, Liston, nikimpa Salum Zakwa, shilingi milioni tano, hawezi kunipa mzigo mwingine wa thamani ya milioni kumi?” Abdul akamuuliza.
“Unazo hapa hapa hizo fedha?”
“Ndiyo, ninazo hapa.”
“Sioni kwa nini asikupe mzigo wa milioni ishirini, au hata hizo hujalipa?”
“Sijui, sikumbuki. Tatizo letu sisi maajenti ni kwamba hatuiuzi hii bidhaa huko mitaani sisi wenyewe. Ndiyo, tuna marafiki, tena ni watu wa uhakika, ambao tunawauzia, au tuseme tunawakopesha. ‘Mapusha’ ambao wanauza mitaani, ni wao wanaotuangusha!” Abdul Zengekala akamwambia Liston.
Baada ya maongezi mafupi, kimya kifupi kikatawala, wakakaa wakimsubiri Salum Zakwa afike pale. Wakati wakiwa kimya, mara mvumo wa sauti ya gari ukasikia kutoka mbali, kitu ambacho kilikuwa nadra kwa usiku ule wa manane. Liston akajitayarisha na kutoa bastola yake huku akisema:
“Nasikia mvumo wa gari...”
“Labda ni askari wa doria...” Vasco akasema huku akiyakodoa macho yake kule mlio wa gari ulipokuwa unatokea.
“Kama ni askari wa doria, wakileta za kuleta na kutuharibia mipango yetu, napambana nao!”
“Mimi simo!” Abdul Zengekela akasema. “Sitaki kesi ya kuua! Sitaki kesi ya aina yoyote!”
“Sidhani, askari wafuate nini huku saa tisa za usiku? Hizo doria za mjini zinawashinda, waje kufanya doria huku? Lazima watakuwa ni wanga wenzetu tu, kama siyo bosi!” Liston akauliza.
Mvumo wa gari ukazidi kuwasogelea katika eneo lile la ufukweni walipokuwa. Mara gari jeusi aina ya Ranger Rover Vogue, likaegeshwa kando ya Toyota Mark 11 Grande la Liston. Bila kuzima taa za gari hilo, Salum Zakwa alishuka, na muda huo sehemu ile kukawa kweupe kama vile mchana, kiasi kwamba, Liston, Vasco na Abdul wakafinya macho yao kwa kuumizwa na ule mwanga wa taa za magari mawili.
Kama kawaida yake, Salum Zakwa alikuwa amevalia nguo zilezile alizokuwa amevalia muda ule alipokuwa kule, Hotel Afriko Casino, na kwa vile taa za gari zilimpiga mgongoni, alionekana kama kivuli!
“Ndiyo, Abdul Zengekala....habari za mida...” Salum Zakwa akamwambia Abdul Zengekala.
“Habari nzuri, bosi...” Abdul akaitikia.
“Vizuri sana...naona unatesa tu! Pombe, kamari, wanawake...”
“Ah, hayo ni maisha tu. Nimepooza sana...”
“Nakubaliana na wewe. Na sina ugomvi na mtu anayetafuna fedha yake, lakini tatizo ni kwamba unatumia fedha zangu. Unakumbuka nakudai shilingi ngapi?”
“Ni milioni kumi, mzee, kama sikosei. Hapa nina milioni tano...”
“Zile ulizotula muda ule pale Casino?”
“Ndiyo, mzee. Ndiyo hizo...”
“Sijui kwa nini tunakubali kucheza na mtu asiyekuwa na kitu,” Salum Zakwa akamwambia na kuongeza. “Au kwa vile wakati mmoja ulijaa kishenzi kwa fedha zangu!”
Abdul Zengekala akabaki kimya. Hakusema kitu. Akahisi mambo hayakuwa mazuri hata kidogo kama alivyotazamia, akameza mate ya uchungu!
“Je, nikikwambia nakudai shilingi milioni thelathini, na siyo milioni kumi, utasemaje?” Salum Zakwa akamuuliza.
“Inawezekana mzee. Ni muda mrefu umepita, unaweza hata ukanidai na riba,” Abdul akajibu kinyonge na kuendelea. “Tatizo ni kwamba mambo hayakuniendea vizuri. ‘Mapusha’ wangu wengi hawajanilipa, na wengine wamekamatwa na polisi. Hawana uwezo wa kunilipa!”
“Uongo mtupu!” Salum Zakwa akabwata kwa ghadhabu!
“Kweli tupu. Natumaini hata wewe unaielewa biashara hii...” Abdul akazidi kujitetea.
“Nimefanya uchunguzi. Unadhani mimi fala kama wewe? Ni ‘pusha’ wako mmoja tu aliyekamatwa na polisi, na ulikuwa unamdai milioni mbili tu. Kiasi hicho mimi nisingejali, lakini milioni thelathini? Unadhani mimi nayaokota yale madubwana?”
“Nakuomba unisamehe mzee,” Abdul akasema huku akitetemeka. “Sitarudia tena. Na naahidi kukulipa milioni thelathini zako...”
*******
“Utazitoa wapi? Wewe umekwisha, hata gari lako umeliuza! Unadhani nitakupa mzigo mwingine? Nikupe wewe mcheza kamari, mzinzi, mlevi? Tena hutaki wanawake wa bei poa pale mtaa wa Ohio, unataka wa kule Mzambarauni kwa Mama Hidaya, ambao dau lao ni chini ya laki mbili au tatu. Hapana, Abdul wewe umekwisha, hujui kutafuta, unajua kutumia tu! Na hata ukipewa milioni hamsini utazimaliza ndani ya wiki moja!” Salum Zakwa akaendelea kumhabarisha Abdul Zengekala!
Abdul akabaki amenyamaza kimya!
Pombe ikamtoka kichwani haraka sana!
“Umenidhulumu Abdul!” Salum Zakwa akarudia kumwambia!
“Ndiyo...mzee...” Abdul akasema kwa kusita.
“Ok, utanilipa lini?”
Abdul akanyamaza kimya!
“Eti, utanilipa lini fedha zangu?”
Kimya!
“Umekuwa bubu?”
Kimya!
“Vasco!” Salum Zakwa akamwita!
“Bosi!” Vasco akaitikia!
“Naona rafiki yangu, Abdul, amekuwa bubu ghafla. Hebu mchangamshe apate akili!” Salum Zakwa akamwambia Vasco!
Huo ulikuwa ni mtihani kwa kwanza kwake!
“Sawa, bosi! Ngoja nimwadabishe” Vasco Nunda akasema huku akipeleka mkono wake mfukoni!
Kufumba na kufumbua kisu chake cha spiringi kilikuwa mkononi mwa Vasco, keshakibonyeza na kimeshachomoka! Sekunde hiyohiyo, Abdul akalia!
“Mamaaa! Sikio langu! Oooohps!”
“Sikio lako hili hapa!” Vasco Nunda akasema huku akimshindilia Abdul mdomoni mwake!
“Ptuu!” Abdul Zengekala akalitema sikio lake haraka! Kipande hicho cha sikio kikadondoka chini na damu nyingi ikaanza kutoka katika jerehe lile lililobaki kama kigutu cha sikio!
Salum Zakwa alivutiwa na kitendo cha Vasco kufanya shambulio la ghafla, ambalo kamwe hakutegemea! Hivyo akapiga makofi machache na kumwambia:
“Safi sana Vasco! Kazi nzuri!”
“Lakini tambua kuwa hunitendei haki mzee!”Abdul Zengekala akamwambia Zakwa kwa hasira, huku damu zikiendelea kumtoka kwa wingi pale katika jeraha sikioni na kulowanisha kiganja chake alichokuwa amejishika. Damu nyingine ikalowanisha suti yake ya rangi ya maziwa aliyokuwa amevalia na kuonyesha mabaka mekundu!
“Nani hakutendei haki?” Salum Zakwa akauliza huku akitabasamu!
Tabasamu la kifedhuli!
“Nakudai halafu unaleta za kuleta?” Akaendelea kumwambia Abdul huku ameikamata bastola yake mkono wa kulia, huku ameificha nmyuma ya mgongo wake.
“Najua kuwa unanidai mzee...lakini...” Abdul Zengekala akaendelea kusema.
“Lakini nini? Sina mzaha na fedha!” Salum Zakwa akamkatisha. Mara bastola yake ikalipuka mara mbili! Mkono ulishatoka nyuma ya mgongo na kumwelekea Abdul!
“Ooohpsi...Oohps!” Abdul Zengekala akapiga kelele huku akishikilia kifuani kwa mikono yake miwili. Ni sehemu ambako risasi mbili kutoka kwenye bastola ya Zakwa zilimpata na kufanya doa jekundu la damu lionekane!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Shenzi sana!” Salum Zakwa akamalizia kusema!
Baada ya Abdul Zengekala kusimama kwa muda huku akiyumba kugombana na uhai wake, akaanguka chali nyuma ya gogo la mnazi. Halafu Salum Zakwa akabaki akimwangalia takriban dakika moja hivi, na kimya kikatawala kwa muda. Hata wadudu wa vichakani wakaacha kulia!
“Ahahahaaaa!” Ghafla Salum Zakwa akacheka kitu ambacho kilikiwashangaza, Vasco na Liston!
“Mnajua nacheka nini?” Akawauliza!
“Hapana, bosi...” wote wakasema.
“Kazi hii ilitakiwa ifanywe na Vasco, siyo mimi. Hata hivyo umefaulu. Tangu sasa wewe ndiye mpambe wangu mkuu, na Liston atakuwa msaidiza wako. Lakini kazi mtasaidiana wote bila kubaguana, mpo?”
“Tupo bosi...” Vasco akasema.
“Sawa bosi...” Liston akasema ingawa kwa kiasi fulani hakufurahia uamuzi wa bosi wao, lakini hakuwa na la kufanya. Alijua fika kumkatalia ni sawa na kujihukumu adhabu ya kifo!
“Na msisahau kuwa huyo fala kajaa fedha, milioni tano. Hatazihitaji tena, ni zenu!” Salum Zakwa akawaambia Vasco na Liston waliokuwa bado wamesimama.
“Sawa, bosi…” wakasema kwa pamoja.
Baada ya kuwaambia vile, Salum Zakwa akajivuta kwa hatua za taratibu na kuingia ndani ya gari lake huku akiwa bado ameikamata bastola yake mkononi. Baada ya kupanda, akalitia moto na kuliondoa lile kwa mwendo wa kawaida.
Akapotea!
Salum Zakwa alipoondoka, Vasco na Liston, wakaiendea maiti ya Abdul, iliyokuwa imelala nyuma ya gogo la mnazi. Wakaanza kuipekuwa kwa makini ambapo walichukua zile fedha zilizokuwa mfukoni mwake. Vasco akazihesabu, kisha akamwambia Liston:
“Jamaa alikuwa amejaa, shilingi milioni tano na laki mbili. Je, nusu kwa nusu?”
“Ndiyo,” akajibu Liston. “Au unataka kunizidishia kwa vile mimi ni mkubwa?”
“Ni mkubwa kiumri, siyo wadhifa. Mimi ndiye ‘Mpambe Mkuu’ sasa...”
“Sawa mkuu...”
“Fedha zake tumezichukua. Je, hii bastola yake niliyoichukua mwanzo, tuifanyeje?” Vasco akamuuliza Liston.
“Bastola hiyo tutaitumia, wewe ulitaka tuifanyeje? Tuitupe?”
“Sina maana hiyo...”
“Basi, kuanzia sasa ni mali yetu!”
“Hakuna shaka...”
Baada ya kugawana fedha zile na kuhakikisha hakuna kinachoendelea zaidi, Vasco na Liston wakaisukuma maiti ya Abdul Zengekala hadi ndani ya vichaka vilivyojaa katika eneo lile, na walipohakikisha wameificha, wakaliendea gari lao na kupanda. Liston akalitia gari moto na kuliondoa katika eneo lile la Ufukweni Kunduchi. Hawakujali kile kilichotokea!
********
Alfajiri kulipambazuka vizuri bila kuwa na dalili za kunyesha mvua. Hali ya uchangamfu ikarudi katika hali yake ndani ya jiji la Dar es Salaam. Ni watembeao kwa miguu waliokuwa wanapita katika eneo lile la Kunduchi, ufukweni mwa Bahari ya Hindi, ndiyo walioiona maiti ya Abdul Zengekala, ikiwa imelala ndani ya kichaka kilichofungamana. Kama kawaida, eneo lile palikuwa na ile njia ndogo inayotokeza baharini, ambayo hutumiwa hata na wavuvi waliokuwa katika shughuli zao za uvuvi.
Asubuhi hiyo, vijana wawili walikuwa wakipita kuelekea baharini katika shughuli zao za uvuvi, na mmoja wapo alibanwa na haja ndogo. Akaamua kuchepuka kidogo na kuingia ndani ya kichaka ili kujisaidia. Lakini kabla hajaanza kujisaidia, alikuwa ameangalia mbele yake, ambapo aliona kitu kimelala katika majani katikati ya kichaka kile. Alipoangalia vizuri, ndipo alipoona ulikuwa ni mwili wa mtu uliokuwa umelala chali!
“Mh,” kijana yule akaguna na kutaka kurudi nyuma kidogo!
“Vipi mshikaji?” Mwenzake akamuuliza.
“Nini kile?”
“Kwani kuna nini?”
“Naona kama kuna mtu amelala ndani ya kichaka!”
“Unasema kuna mtu?”
“Ndiyo...njoo uone...”
Vijana wote wawili wakamsogelea maiti yule karibu kabisa, ndani ya kichaka kile kilichokuwa kimefungamana. Ndipo walipoweza kuiona vizuri maiti ya mtu aliyekuwa amelala chali, ametapakaa damu karibu nusu ya mwili wake. Maiti yule aliyeonekana kama mtu wa makamo kiasi, alikuwa bado amevaa nguo zake za gharama, suti ya rangi maziwa, shati jeupe, tai nyekundu. Miguuni alikuwa amevalia viatu vyeusi vya ngozi.
Kwa muda ule mifuko yake ya suruali ilikuwa imechomolewa nje, kuashiria kuwa alikuwa amepekuliwa na kuchukuliwa kila alichokuwa nacho! Simu yake ya mkononi, ya gharama, ilikuwa imeanguka kando yake na kuonyesha waliompora hawakuwa na shida nayo.
“Kweli ni mtu! Sasa tufanye nini?” Kijana akamuuliza mwenzake.
“Cha muhimu ni kuwajulisha polisi...” mwingine akamwambia.
“Hapana, haiwezi kuwa msala ndugu yangu?”
“Hapana, haiwezi kuwa msala. Yaani kuwataarifu polisi kuna kosa gani?”
“Basi, tufanye hivyo. Je, unazijua namba za dharura?”
“Nazijua, ngoja nipige...” kijana akasema, halafu akaanza kupiga namba za dharura, Kituo Kikuu cha Polisi.
Simu ile ikaanza kuita kwa muda kidogo, halafu upande wa pili ikapokelewa:
“Polisi Kituo cha Kati....nikusaidie...”
“Mimi msamaria mwema...”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndiyo msamaria...nikusaidie...”
“Napenda kutoa taarifa kuwa kuna maiti ya mtu, mwanaume, iko ndani ya kichaka eneo hili la Kunduchi...”
“Kunduchi sehemu gani?”
“Ni eneo hili la ufukweni, karibu na njia ya wavuvi...”
“Haya, tunashukuru...tunazifanyia kazi taarifa hiyo...”
“Haya...”
Walipomaliza kuwasiliana, simu ikakatwa, na vijana wale wakaendelea na safari yao waliyokuwa wanaelekea, na kuiacha ile maiti, ambayo kwa muda ule ilikuwa imeshaanza kuzungukwa na watu waliokuwa wanapita njia ile. Kila mmoja alikuwa akizungumza lake!
*******
Wiki moja iliyopita, ndani ya Jengo la makao Makuu ya Polisi,jijini Dar es Salaam, katika chumba maaluum cha mikutano, palifanyika kikao cha Wakuu wa Idara ya Upelelezi nchini, kutathmini hali ya uhalifu nchini kwa ujumla. Ni mkutano uliokuwa umeandaliwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), na ile ilitokana na hali kuwa mbaya, hasa baada ya kushamiri kwa biashara haramu ya dawa za kulevya.
Hali ilikuwa ni tete, na maofisa wa Jeshi la Polisi waliona kuwa kwa kiasi fulani walikuwa wamelegea na kuruhusu biashara ile ifanyike bila wasiwasi wowote. Walikuna vichwa vyao na lawama zikashushwa kwa baadhi ya wahusika hasa Mkuu wa kitengo cha kuzuia Dawa za kulevya, kwani hakuna aliyependa kubeba lawama kwa kadhia ile nzito.
Chumba cha mikutano kilikuwa na wajumbe wapatao ishirini hivi, kutoka katika vitengo mbalimbali kutoka katika idara ile ya upelelezi. Mkurugenzi wa Upelelezi alikohoa kidogo ili kusafisha koo lake, halafu akawaangalia wajumbe wote na kuanza kusema:
“Ndugu wajumbe, hii ni mara nyingine tena tumekutana hapa katika kikao chetu cha kujadili hali ya usalama kwa ujumla. Tunajadili kuhusu hili wimbi la wafanyabiashara wa dawa za kulevya lilivyoshamiri hapa nchini….” Akanyamaza kidogo huku akiwaangalia wajumbe.
“Ni kama mnavyoelewa, ni hivi karibuni tumefanikiwa kukamata shehena kubwa ya dawa za kulevya, ambazo zilikuwa zimetokea kisiwani Zanzibar kwa nia ya baharini. Hiyo inaonyesha ni jinsi gani watu hao walivyokuwa wamejiandaa kiasi kwamba pia walikuwa na silaha za moto katika kufanikisha biashara zao. Hivyo basi, kukutana kwetu hapa, ni juu ya kujadili namna ya kuweza kupanga operesheni maalum ya kuwadhibiti wafanyabiashara hao…”
“Kwa kuianza operesheni yetu, tumepanga kuianzia hapa nchini na hata kisiwani Zanzibar, ambapo kumekuwa kama kituo kikubwa cha kupitishia dawa hizo kwa kutumia njia za baharini na hata kwa ndege. Kwa mujibu wa upelelezi na mahojiano yaliyofanyika kwa watuhumiwa wale waliokamatwa, tumefanikiwa kupata majina ya wafanyabiashara kadhaa wa hao. Lakini huwezi kumkamata mtu bila kuwa na ushahidi kama anajihusisha na biashara hiyo.
Ndiyo maana tumekutana hapa ili kuchagua au kupendekeza makachero kuiendesha operesheni hii. Na kwa pendekezo langu, napendelea wateuliwe makachero wachache tu ambao ni mahiri. Hii inatokana na kuwa makachero wengi itasababisha kazi isifanyike kwa ufanisi, hivyo ifanyike kwa wachache tu!” Mkurugenzi akanyamaza tena na kuwaangalia wajumbe kama maneno yale yamewaingia.
“Mkuu wa kitengo, Kamishana Dickson Kweka,” Mkurugenzi akamwita.
“Afande,” Dickson Kweka akaitikia.
“Suala hili linakuhusu sana wewe…”
“Ni sawa, afande…”
“Wewe unawajua vizuri askari wako, hivyo basi, tunataka uteue jina la kachero ambaye unaona anafaa kwenda kuiendesha operesheni hii.”
“Sawa, sawa afande!”
“Haya, kazi kwako!”
Kamishna Msaidizi wa Polisi, Dickson Kweka akanyamaza kimya kwa muda huku akitafakari kwa kina, kwani alikuwa akiwaza na kuwazua jinsi ya kumpata kachero mahiri wa kwenda kuifanya kazi hiyo. Ukweli ni kwamba alikuwa na makachero wengi, lakini kati ya hao, kulikuwa na wale mahiri ambao aliwafahamu vizuri, hasa kiutendaji, kitabia na pia kujituma. Hivyo basi, alimpata kijana wake mahiri, Kachero Inspekta Raymond Gopi!
“Mkuu, ninapendekeza kijana wangu, Kachero Inspekta Raymond Gopi, huyu anaweza kutusaidia katika operesheni hii,” Dickson Kweka akamwambia Mkurugenzi wa Upelelezi.
“Ni vizuri. Natumaini wewe unamfahamu vizuri kijana wako, hivyo nauheshimu uteuzi wako. Cha muhimu ni kazi ifanyike kwa ufanisi…”
“Kazi itafanyika mkuu, hakuna tatizo.”
Hivyo basi, mara baada ya kukubaliana, kikao kile kilichoshirikisha wakuu wale wa upelelezi, kiliamua kukubaliana na kuteua askari mpelelezi kushiriki katika operesheni ile ya kuwasaka wafanyabiashara wa dawa za kulevya. Operesheni hiyo ilitakiwa ifanyike baada ya watuhumiwa, kadhaa waliokamatwa kuhojiwa na kutoa ushirikiano wa hali ya juu, jinsi biashara ile inavyofanyika.
Mkuu wa Kitengo cha kuzuia Dawa za Kulevya nchini, Kamishana Msaidizi wa Polisi Dickson Kweka, ndipo alipopendekeza jina la kijana wake mwaminifu na mchapa kazi, Kachero Inspekta Raymond Gopi, ili kushiriki katika operesheni ile kabambe. Baada ya kupewa jina lile, lilipita bila kupingwa na wakuu wale na kilichobaki ni kazi kufanyika.
Kachero Inspekta Raymond, ni mpelelezi mashuhuri kutoka katika kikosi cha kupambana na dawa za kulevya, akiwa ni mmoja wa wapelelezi waliofanikiwa kupata mafunzo hayo ndani na nje ya nchi ya Tanzania, juu ya taaluma ya upelelezi. Ndiyo tuseme alikuwa amefuzu haswa na jina lake kuwa katika faili maalum la makachero wanaotegemewa.
Yeye alikuwa bado ni kijana mbichi, akiwa na umri wa miaka 35 hivi ya kuzaliwa, mwenye urefu wa futi tano na nchi nane, akifuatiwa na umbile liliojengeka kikakamavu, ambalo halikuruhusu mhalifu yeyote alichezee. Kijana Raymond Gopi ni mweupe kiasi, mtanashati mwenye sura yenye mvuto, ambayo huwasumbua sana watoto wa kike, ambao hawakuacha kumgombania.
Hivyo basi, baada ya kikao kile, Kachero Inspekta Raymond aliitwa mbele ya Mkuu wake wa kazi, Kamishana Msaidizi wa Polisi, Dickson Kweka, ambaye alimweleza yote juu ya kuteuliwa kwake, kushiriki katika operesheni ile maalum ya kukata na shoka. Nim operesheni iliyotakiwa kufanya kimyakimya. Hivyo Kweka alimwangalia kwa makini, halafu akavuta pumzi ndefu na kusema kwa sauti ndogo:
“Raymond…”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Afande…” Kachero Inspekta Raymond akaitikia huku akimwangalia mkuu wake.
“Nimekuita hapa kuhusu operesheni maalum inayotakiwa kufanyika. Wewe unatakiwa kushiriki…” Dickson Kweka alimweleza yote juu ya kile kilichotakiwa kufanyika.
“Nimekuelewa, afande…” Kachero Inspekta Raymond Gopi alimwambia.
Baada ya kumaliza kupeana majukumu, waliagana, na Kachero Inspekta Raymond akaelekea ndani ya ofisi yake iliyokuwa katika ghorofa ya nane ndani ya jengo lile, tayari kwa kujiandaa kwa kazi ile. Akachukua baadhi ya vifaa vyake ambavyo aliona vingemsaidia katika upelelezi wake, ikiwemo bastola yake aliyokuwa anaruhusiwa kutembea nayo akiwa katika kazi kama zile za hatari! Ni silaha aliyokuwa anaihifadhi katika ghala ya silaha iliyokuwa mlemle jengoni kwa ajili ya kazi za dharura kama zile. Pia, alichukua na risasi za kutosha zilizokuwa ndani ya magazine za kuhifadhia risasi, ambazo aliziweka katika mkoba maalum.
Wakati Kachero Inspekta Raymond Gopi alipokuwa amepangiwa majukumu yale ya kushiriki katika operesheni hiyo, ndipo mkasa huu unaomhusisha salum zakwa ulipotokea na kujikuta yeye Raymond akishiriki!
********
Majira ya saa tatu za asubuhi hivi, gari la polisi, aina ya Toyota Land Cruiser, lilifika pale ufukweni mwa bahari, likiwa na askari polisi kumi wa kikosi maalum. Walikuwa wameongozana na mkuu wa msafara, aliyekuwa na cheo cha Sajini, ambao walishuka na kulizingira eneo lile la tukio kwa kuanza kufanya uchunguzi wa awali.
Uchunguzi wa muda walioufanya, waliweza kumjua mtu yule aliyekuwa ameuawa kwa kupigwa risasi, alikuwa ni Abdul Zengekala, mtu aliyekuwa anajulikana sana jijini, kama mfanyabiashara, na alikuwa anaishi mtaa wa Undali, Upanga.
Mbali ya kuwa mfanyabiashara, pia, mtu huyo alihisiwa kama anajishughukisha na biashara haramu ya dawa za kulevya, ingawa hakuwahi kukamatwa hata mara moja.
Kingine ambacho kilizidi kuwashangaza askari polisi wale, ni juu ya maiti yule kuwa amepekuliwa na mifuko, kitu ambacho kwa wao walihisi labda alitekwa nyara na majambazi waliokuwa na nia ya kumpora fedha.
Maiti ile ya Abdul Zengekala, ikachukuliwa kunako majira ya saa tano baada ya uchunguzi kukamilika. Ikapelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuhifadhiwa na kufanyiwa uchunguzi zaidi wa kitaalam, na kupata ripoti ya daktari.
*******
Kwa vile tukio lile lilihusiana na mfanyabiashara wa dawa za kulevya, na pia, ile operesheni maalum ya kupambana na wafanyabiashara wale ilikuwa inaendelea nchini, askari polisi wakaamua kumjulisha Kachero Inspekta Raymond Gopi, ili afuatilie, huwenda akapata fununu ya chanzo cha kifo kile. Kwa vyovyote walikihusisha kifo kile na wahusika wa mtandao wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya, si vinginevyo!
Kachero Inspekta Raymond, baada ya kupata taarifa ile kwa njia ya simu, hakuifanyia mzaha kabisa, kwani aliondoka kwenye kituo chake cha kasi, Kurasini, akiongozana na Kachero Benito, wakitumia gari aina ya Land Rover la kitengo, dereva akiwa ni Kachero Benito. Walipotoka pale kituoni, walielekea moja kwa moja hadi Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ambapo walipofika, waliingia hadi ndani ya chumba cha kuhifadhia maiti, na kuiona ile maiti ya Abdul Zengekala.
Wote wakaitambuamaiti ile kwa vile ni mtu waliyekuwa wanamfahamu sana, na pia sehemu alizokuwa anapendelea kutembelea katika matanuzi. Kati ya sehemu hizo, ni katika Casino, iliyoko ndani ya Hotel Afriko, ambapo hukutana na jamaa zake na kucheza mchezo wa kamari yenye madau makubwa ya fedha!
*******
Baada ya kutoka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Kachero Inspekta Raymond Gopi akamwambia Kachero Benito waelekea mtaa wa Undali, Upanga, nyumbani kwa Marehemu, Abdul Zengekala. Wakaelekea huko moja kwa moja hadi walipofika katika nyumba ile iliyokuwa imezungukwa na uzio wa ukuta, na upande wa mbele kukiwa na geti kubwa la chuma. Baada ya kulipaki gari kando ya barabara, wakashuka na kuiendea ile nyumba hadi walipofika getini. Hali ya ukimya ilikuwa imetawala eneo zima, labda ni sauti za ndege tu, ndizo zilizoweza kusikika kutoka juu ya miti iliyozuguka katika eneo lile tulivu.
Hata hivyo, pale getini, kando ya ukuta, palikuwa na kengele, ambayo Raymond aliibonyeza ikaanza kuvuma kule upande wa ndani. Haukupita muda mrefu, kijana mmoja mwenye umri kati ya mika ishirini hivi, alitokea na kulifungua geti. Akawaona Raymond na Benito wamesimama pale!
“Karibuni...” akawaambia huku akiwaangalia kwa hofu kidogo.
“Ahsante...sisi wageni wako...” Kachero Inspekta Raymond akamwambia.
“Karibuni ndani,” kijana yule akawaambia na kuwaruhusu waingie ndani ya geti lile.
Baada ya kuingia ndani, makachero hao wakaenda kukaa kwenye viti vilivyokuwa katika bustani nzuri iliyokuwa mbele ya nyumba ile. Na kwa muda ule kabla hawajafika pale, ilionyesha kuwa kijana yule alikuwa akiifanyia usafi bustani ile, kwani vitendea kazi vyake vilikuwa pale.
“Ndiyo kijana, hali yako...” Kachero Inspekta Raymond akamsalimia.
“Nzuri...”
“Vizuri, sisi ni Makachero, Inspekta Raymond na Benito, tumekuja hapa kwa mahojiano kidogo...”
“Sawa tu, na mimi naitwa Jumaa Kibwabwa...” kijana yule akajibu.
“Ahsante sana Jumaa, natumaini hapa ni nyumbani kwa Abdul Zengekala, sivyo?”
“Ndiyo, ni nyumbani kwake...”
“Je, kwa muda huu yuko wapi?”
“Huyu bwana tokea jana hajarudi nyumbani...”
“Kwa nini hajarudi?”
“Kwa hilo sijui. Lakini hiyo ni kawaida yake, mara nyingi huwa anashinda hukohuko, akisema yuko kwenye mishughuliko ya kibiashara.”
“Je, mara ya mwisho mmewasiliana lini?”
“Kwa mara ya mwisho tumewasiliana jana usiku, akaniambia yuko Hotel Afriko...”
“Baada ya hapo?”
“Sijawasiliana naye tena!”
“Wala hukumpigia simu?”
“Sikumpigia, kwa sababu siyo kawaida yetu. Yeye ndiyo huwa anapiga!”
“Je, mke wake yupo?
“Mke wake wameshaachana muda mrefu sana...”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sasa anaishi peke yake?”
“Ndiyo, shida zake zote huzimalizia kwa wanawake wa nje...”
“Basi, kuna taarifa nazotaka kukwambia. Ni kwamba, Abdul Zengekala ameuawa, na maiti yake imeokotwa kule Kunduchi, ufukweni mwa Bahari ya Hindi....”
“Ameuawa?” Kijana, Jumaa akashtuka!
“Ndiyo.”
“Na nani?”
“Mimi na wewe hatujui. Labda unaweza kutujulisha mtu aliyekuwa na uhasama naye, au wanadaiana.”
“Inawezekana ni wafanyabiashara wenzake...”
“Biashara gani?”
“Biashara ya unga. Nafikiri wamedhulumiana, kwani alikuwa ana madeni mengi sana, na walikuwa wakimtishia maisha, kiasi kwamba aliamua kuwa mlevi ili kupunguza mawazo!”
“Aisee, unaweza kuwakumbuka wafanyabiashara hao?”
“Mimi siwajui, kwani biashara yao huifanya kwa kificho sana...”
“Haya kijana, sisi tunashukuru, tunatoka, tukikuhitaji tutakuja tena.”
“Haya, karibuni...” kijana yule akasema huku akiwa na huzuni kubwa! Hakujua kiliochokuwa kinaendelea, akabaki akiwaangalia makachero wale mpaka walipoishia getini!
Makachero wale wakapanda garini, na Benito akaliondoa gari kuelekea katikati ya jiji la Dar es Salaam, ilipo Hotel Afriko, katika mtaa wa Samora. Baada ya kufika, Benito akalipaki gari sehemu ya maegesho nje ya hoteli ile, halafu wote wakashuka na kuingia ndani. Wakafikia katika eneo la mapokezi, ambapo alikuwepo mwanadada mmoja mrembo.
“Karibuni...” akawakaribisha.
“Ahsante sana...”
“Niwasaidie jamani,” mwanadada yule akawaambia.
“Namuulizia mmiliki wa hoteli hii, sijui yupo?”
“Bwana Josia Kessy sivyo?”
“Ndiyo.”
“Yupo ofisini...”
“Naomba kuonana naye.”
“Una miadi naye?”
“Hapana, sina miadi...”
“Basi, itakuwa ngumu...”
“Mwambie ni mimi Kachero Inspekta Raymond, kutoka...”
“Sawa,” mwanadada yule akasema. Halafu akapiga simu ya maungio ya ndani kwa ndani kwa kumpigia mmiliki wa hoteli ile. Akaongea naye kwa kumfahamisha ugeni ule.
“Unaweza kwenda...” mwanadada yule akamwambia.
“Ofisi yenyewe iko wapi?”
“Aisee, iko katika ghorofa ya nne, inapidi upande lifti...”
“Oh, kumbe iko juu?” Raymond akasema. Halafu akaiendea lifti, ambayo alipanda kuelekea juu. Akamwacha Kachero Benito akibaki pale mapokezi, kwani hawakuona sababu yoyote ya wao kwenda wote katika kumhoji mmiliki yule.
Baada ya lifti ile kufika katika ghorofa ya tano, Raymond akashuka na kuelekea katika ofisi ile iliyokuwa katika upande wa kushoto mwa korido. Akabisha hodi na kuingia ndani huku akiwazia namna atakavyopokelewa. Alipoingia, alimkuta Kessy amekaa katika meza yake akiendelea na majukumu ya kikazi. Ni ofisi iliyopendeza kutokana na mpangilio wake, ambapo kulikuwa na kila kitu kilichokuwa kinahitajika.
“Karibu ndugu yangu...” Kessy akamwambia.
“Ahsante sana...” Raymond akaitikia huku akiangaza macho yake haraka haraka ndani ya ofisi ile nadhifu.
“Mini ni Kachero Inspekta Raymond,” akaanza kujitambulisha na kuendelea. “Nimekuja hapa kwako kwa shida moja tu...”
“Shida gani?” Kessy akamuuliza.
“Sijui unamfahamu mtu anayeitwa Abdul Zengekala?”
“Ndiyo, namfahamu sana. Ni mmoja wa wateja wangu anayekuja hapa katika hoteli yangu...”
“Je, mara ya mwisho kuonana naye ni lini?”
“Mara ya mwisho ilikuwa jana usiku.”
“Baada ya kuonana naye?”
“Tulikaa wote, tukiwa pamoja na rafiki zangu, ambapo tulikunywa na hata kucheza kamari kule Casino...”
“Mlipomaliza kucheza kamari ikawaje?”
“Alitushinda wote, na kupata kiasi kikubwa cha fedha, na hatimaye akaaga na kuondoka zake.”
“Basi, kwa taarifa yako, Abdul Zengekala ameuawa!”
“Ameuawa?”
“Ndiyo, tena jana usiku...”
“Ameuawa na nani?”
“Hatujui, ndiyo maana nimekuja hapa kwako.”
“Ukweli hata mimi sijui, kwa vile hatuna uhasama naye...”
“Je, hakuna mtu mwingine unayemhisi kama ana uhasama naye?”
“Kwa kweli sijui. Lakini inawezekana ikawa ni majambazi...”
“Majambazi, kwa nini unasema hivyo?”
“Jana usiku, Abdul alikuwa na fedha nyingi sana!”
“Kiasi gani?”
“Kama milioni tano hivi.”
“Oh, basi, inawezekana, lakini hakuwa na gari?”
“Hakuwa na gari, kwani keshaliuza kitambo sana!”
“Kwa nini?”
“Unga ulikuwa unamharibu...anaendekekeza matumizi ya hali ya juu. Ameshaonywa sana, lakini imeshindikana!”
“Anatumia unga?”
“Hapana, yeye ni muuzaji!”
“Ah, hayo tuyaache, je, hapa kwenye hoteli yako si kuna walinzi?”
“Ndiyo, ninao walinzi sita, wanaopokezana zamu, na wanalinda kwa muda wote.”
“Basi, naomba kuongea nao...”
“Unaweza kuongea na mmoja wao, ambaye yuko sasa...”
“Haya, nashukuru,” Kachero Inspekta Raymond akasema. Halafu akanyanyuka kitini na kutoka pale katika ofisi ya Kessy, huku akisindikizwa naye hadi walipotoka na kufikia kwenye korido ndefu.
Hakika kwa Kessy, alijua kuwa limeshasanuka, na siyo mwingine aliyetekeleza mauaji yale, zaidi ya Salum Zakwa, ambaye ndiye aliyekuwa mshirika wake mkubwa kibiashara. Hata hivyo hakutaka kumshtua kuwa kachero wa polisi alikuwa amefika pale kufuatilia mauaji yale! Baada ya kufika kwenye korido, Kachero Inspekta Raymond na Kessy, wakapeana mikono na kuagana, na Raymond akaiendea lifti na kubonyeza batani. Ilipofunguka, akapanda na kushuka nayo hadi chini, mwanzo wa ghorofa.
*******
Kachero Inspekta Raymond alipotoka ndani ya lifti, alielekea sehemu ile walinzi wanayokaa, ambapo alimkuta mlinzi mmoja, ambaye alikuwa ameunganisha zamu kwa kumshika mwenzake aliyekuwa na matatizo ya kifamilia. Mlinzi yule alikuwa amevalia sare za ulinzi, shati la rangi nyeupe, suruali ya bluu, na kofia ya rangi ya bluu vilevile. Kwenye shati lake kulikuwa na na nembo iliyoandikwa jina la hoteli ile kumtambulisha kuwa ni mlinzi.
“Hali yako...” Kachero Inspekta Raymond akamsalimia huku akimwangalia kwa makini.
“Nzuri...”
“Mimi ni Kachero Inspekta Raymond, natokea...” akajitambulisha.
“Ndiyo, na mimi naitwa Shemdoe, nikusaidie...” mlinzi yule akajitambulisha.
“Naomba kufanya mahojiano na wewe.”
“Sawa tu, unaweza kufanya.”
“Wewe ni mlinzi wa hapa?”
“Ndiyo, mimi ni mlinzi.”
“Nasikia jana usiku ulikuwa zamu?”
“Ndiyo, nilikuwa zamu na mwenzangu.”
“Vizuri, je, unamfahamu Abdul Zengekala?”
“Ndiyo, namfahamu. Ni mteja mkubwa wa hapa hotelini...”
“Mara ya mwisho kumuona ni lini?”
“Mara ya mwisho ilikuwa jana usiku.”
“Usiku wa saa ngapi?”
“Usiku wa saa nane au tisa hivi...”
“Ulipomuona, alikuwa katika hali gani?”
“Alikuwa amelewa sana. Baada ya kutoka nje, akaanza kutafuta usafiri wa teksi, ambazo zilikuwa mbali na hapa hotelini. Lakini kabla hajaita teksi, nikamwona mtu mmoja aliyekuwa kwenye gari moja iliyokuwa imepaki pale, akishuka na kumfuata. Baada ya kumfikia, wakaongea mawili matatu, halafu akamchukua kama vile watu wanaofahamiana. Wakaingia ndani ya hilo gari, kisha wakaondoka...” mlinzi yule akamaliza kusema.
“Hukuwatilia mashaka?”
“Kwanza nilikuwa na wasiwasi nao, kwa vile walikuwa wamekaa muda mrefu ndani ya gari yao kama walikuwa wakimsubiri mtu.”
“Hukuwahoji?”
“Sikuwahoji, kwa vile nilidhani ni wateja wanaosubiri wanawake zao...”
“Walikuwa kwenye gari ya aina gani?”
“Ni gari dogo, kama sikosei ni Toyota Mark 11.”
“Ulizisoma namba zake?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hapana, sikuzisoama, kwa vile sikuwatilia mashaka.”
“Kwa taarifa yako, Abdul ameuawa!”
“Ameuawa?” Mlinzi yule akashtuka!
“Ndiyo, nafikiri watu hao waliomchukuwa, ndiyo waliomuua!”
“Mungu wangu!”
“Je, ukiwaona watu hao unaweza kuwatambua?”
“Hapana, siwezi kuwatambua...”
“Haya, nashukuru sana kwa ushirikiano wako. Mimi natoka, kama kuna la ziada, nitakuhitaji kwa mahojiano...”
“Sawa mkuu...”
Baada ya Kachero Inspekta Raymond kumaliza kuongea na yule mlinzi, akamuaga na kuondoka zake, huku akimwacha mlinzi huyo amechanganyikiwa kwa kutoamini kama Abdul Zengekala alikuwa ameuawa, na kwa sababu gani! Pia, kwa upande wa Raymond, alikuwa amechanganyikiwa, kwani hakuweza kujua muuaji ni nani, lakini akawatilia mashaka wafanyabiashara wale wa dawa za kulevya waliokuwa na mtandao mkubwa.
Kachero Inspekta Raymond akaliendea lile gari lililokuwa limepaki katika maegesho, ambapo Kachero Benito alikuwa ameshatangulia na kuingia upande wa dereva. Baada ya kuingia, Benito akalitia moto na kuliondoa kwa mwendo wa taratibu, kulitoka eneo lile la Hotel Africo.
“Benito,” akamwita.
“Afande...” akaitikia Benito.
“Bado tuna kazi nzito...”
“Kwa nini afande?”
“Tukio hili, linahusisha wafanyabiashara wa dawa za kulevya. Hivyo kazi bado inaendelea...”
“Sawa afande.”
“Twende moja kwa moja kituoni.”
Gari likaingia katika barabara kuu ya Samora.
********
Siku iliyofuata, baada ya kutekeleza mauaji ya mfanyabiashara mwenzo, Abdul Zengekala, Vasco Nunda na Liston Kihongwe, walikutana na Salum Zakwa. Kama kawaida, walikutana katika sehemu ya faragha, ambayo siyo rahisi kushtukiwa na wana-usalama, watu waliokuwa wanafuatilia nyendo zao. Kwa vyovyote alijua baada ya mauaji yale kutekelezwa, ni lazima watu wengi wangeshangaa hasa ukizingatia, Abdul alikuwa anajulikana na watu wengi jijini Dar es Salaam.
“Tumekutana tena baada ya kuachana jana usiku...” Salum Zakwa akawaambia.
“Ni kweli, bosi...” wote wakasema kwa pamoja.
“Nawapongeza kwa kazi nzuri mliyoifanya jana usiku, kwa kukiondoa kigogo kile. Ukweli ni kwamba kilikuwa kinaninyima usingizi, hatimaye sasa nitapata usingizi…” Salum Zakwa akaendelea kuwaambia Vasco na Liston kana kwamba alikuwa anaongelea jambo zuri!
Vasco na Liston wakatikisa vichwa vyao bila kuzungumza!
“Kuna mtu ana hoja?”
“Ndiyo, bosi...” Vasco akasema.
“Hoja gani?”
“Nauliza kwamba, baada ya kufanya mauaji yale, hatuwezi kushtukiwa?”
“Kwa nini unauliza hivyo?”
“Nauliza, kwa sababu jana usiku, tulimchukua Abdul, pale Hotelini, huku hata walinzi wa pale wakituona. Sasa huoni kwamba, kama watakuwa wamezisoma namba za gari, watakuwa wamegudua wauaji?”
“Ni kweli, umesema jambo la maana!” Salum Zakwa akasema na kuona kuwa jambo lile lilikuwa ni la msingi!
“Ina maana nje palikuwa na walinzi?” Akauliza tena.
“Ndiyo, walikuwepo walinzi wawili,” Vasco Nunda akasema.
“Waliwaona?”
“Nafikiri walituona, maana tulikuwa tumepaki gari leti pale kwenye maegesho...”
“Wakati wa kumchukua Abdul waliona pia?”
“Nafikiri waliona. Lakini sijui kama walitilia maanani, la sivyo wangetufuata kutuuliza!”
“Ah, kama ni hivyo, msijali. Kama mambo yataharibika, mimi nitasawazisha, kwani nina watu wangu!” Salum Zakwa akawambia kwa kujiamini sana.
“Sawa, bosi,” Vasco akasema.
“Hakuna shida, bosi...” naye Liston akasema.
“Sasa!” Salum Zakwa akaendelea kusema. “Napanga kazi rasmi!”
Vasco na Liston wakamsikiliza!
“Vasco!” Salum Zakwa akaita.
“Naam, bosi...”
“Kuanzia sasa, unaanza kazi rasmi kwenye himaya yangu. Utafanya kazi kwa maelekezo yangu, ukishirikiana na Liston. Lakini wewe ndiye kiongozi, na Liston msaidizi wako, mmenielewa?”
“Ndiyo, bosi!”
“Kama mmenielewa sawa. Imebaki kazi sasa, tunaweza kuagana kila mmoja na shughuli zinazomkabili!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Lakini wakati Salum Zakwa akitaka kuagana na vijana wake, simu yake ya mkononi iliita. Alipoiangalia simu yake, akaiona ni namba za Josia Kessy, mmiliki wa Hotel Afriko!
“Ah, Kessy!” Salum Zakwa akasema huku akiwaangalia, Vasco na Liston! Kisha akaipokea:
“Haloo...Kessy...Zakwa hapa…”
“Haloo...Zakwa...za saa hizi...”
“Ni nzuri...nipe habari...”
“Habari mbaya sana!”
“Kwa nini unasema mbaya?”
“Polisi wametoka hapa kwangu sasa hivi!”
“Polisi? Wamefuata nini?”
“Wanafuatilia kifo cha Abdul Zengekala. Je, una habari amekufa?”
“Kifo chake kinanihusu nini?” Salum Zakwa akasema.
“Usiseme hivyo! Kinakuhusu nini, wakati jana tulikuwa naye wote tukicheza kamari Casino, halafu akatutafuna vibaya?”
“Sasa kuwa naye jana, ndiyo kinihusu?”
“Si unajua mambo ya polisi? Upelelezi lazima uanzie kwetu, kama alivyoanzia mpelelezi huyo kufika hapa. Hebu naomba nieleze ni kipi kinachoendelea, kwa vile najua kuwa wewe na Abdul mlikuwa na migongano katika biashara zenu!”
“Ni kweli Kessy. Wewe ni ndugu yangu, siwezi kukuficha, Abdul nilikuwa namdai fedha nyingi sana, hivyo jana nilimchukua na kujaribu kufanya mazungumzo naye jinsi ya kunirudishia, lakini akaniletea za kuleta!”
“Hivyo ukamuua?”
“Ndiyo, nikamlipua!”
“Kumbe ni wewe?”
“Ndiyo, ni mimi. Kitu cha muhimu kwa sasa, ni wewe kunitunzia siri!”
“Aisee, itabidi ujihadhari sana, kwani polisi wanafuatilia...”
“Hawaniwezi, mimi ni mtu mzito!”
“Haya, kwa heri...”
Baada ya kumaliza kuongea na simu, Salum Zakwa akavuta pumzi ndefu na kupumua kwa nguvu. Halafu akawaangalia tena, Vasco na Liston, ambao walikuwa wakiyafuatilia maongezi yale kwa kina.
“Nilikuwa naongea na Kessy...” akawaambia.
“Ndiyo, bosi....” wote wakasema.
“Anasema eti askari polisi wamefika pale ofisini kwake, kuulizia kifo cha Abdul...”
“Kweli bosi?” Vasco Nunda akauliza kwa hamaki!
“Usihofu bwana mdogo, hizi ndizo hekaheka zetu!”
“Haiwezi kuwa soo?”
“Nakwambia ondoa wasiwasi, hawawezi kugundua chochote. Abdul atazikwa, na mambo yatakwisha! Tuendelee na shughuli zetu. Tunaufunga mjadala huo!” Salum Zakwa akawaambia!
“Sawa, bosi...” wote wakasema kwa pamoja.
Baada ya kupangiana majukumu, wote wakatawanyika!
*******
Habari za mauaji ya Abdul Zengekala zilitapakaa ndani ya jiji la Dar es Salaam. Vyombo vya habari vilitangaza habari hizo kwa kina huku vikilaani kitendo hicho ambacho kilishajukana ameuawa na watu wa mtandao wa wafanyabiashatra haramu ya dawa za kulevya. Jeshi la Polisi lilitakiwa kufanya upelelezi wa kina kufanikisha kupatikana kwa watuhumiwa hao. Hata hivyo hakuna mtu yeyote aliyekamatwa na muuaji, Salum Zakwa, aliendelea kutamba, akiendelea na shughuli zake. Maiti ya Abdul ikazikwa katika makaburi ya Kisutu na watu wa jamaa yake. Huo ndiyo ukawa mwisho wake!
Baada ya mauaji ya Abdul Zengekala, wiki hiyohiyo, Salum Zakwa alikutana na wafanyabiashara wenzake, Josia Kessy, mmiliki wa Hoteli ya Africo, Alfred Kwega na Maiko Nilla. Kama kawaida yao waliingia ndani ya Casino na kuendelea na starehe zao, wakinywa vinywaji vya bei mbaya na pia wakicheza mchezo wa kamari waliokuwa wanaupendelea. Lakini hali ya huzuni ilikuwa imetanda kwao, hasa ukizingatia kile kifo cha mwanachama mwenzao, Abdul Zengekala kilichokuwa kimetokea.
Ukweli ni kwamba, ingawa Abdul alikuwa ni mtu asiyekuwa na hadhi kwao, lofa tu, asiyekuwa na chochote, lakini alikuwa anachangamsha sana wanapokuwa katika mchezo ule wa kamari ambao alikuwa anaujulia sana na pia akiwala mara kwa mara!
“Vipi jamani, mnajua mimi siamini kama Abdul Zengekala amekufa?” Maiko Nilla akasema kwa mzaha baada ya ukimya kutawala muda mrefu.
“Kwa nini unasema hivyo?” Alfred Kwega akamuuliza.
“Ah, ni kama namwona vile, si unajua tulikuwa tumemzoea?” Maiko akasema.
“Ndiyo hivyo, tukubali kuwa, Abdul ameshakufa na amezikwa. Ni kumsahau kwa sasa!” Salum Zakwa akasema. Ukweli ni kwamba hakupendelea kabisa yale maongezi, hasa ukizingatia kuwa yeye ndiye mhusika mkuu wa mauaji yale!
“Ndiyo, lazima tumkumbuke kwa sababu ni jamaa yetu, na pia alikuwa akitupuna fedha zetu mara kwa mara!” Alfred Kwega alisema huku akasema.
“Eti nasikia aliuawa na wahuni waliomteka nyara?” Maiko Nilla akauliza.
“Inawezekana, maana siku ile Abdul alikuwa na fedha nyingi sana, ambazo nyingi alitula sisi,” Josia Kessy alisema huku akimtupia jicho la wizi Salum Zakwa, ambaye naye alimtupia jicho! Macho yao yalipokutana, salum akayakwepa!
“Inawezekana, kwani jiji hili limeshaharibika siku hizi!” Salum Zakwa naye akaunga mkono ili kupoteza lengo!
“Lakini damu yake itawalilia!” Maiko Nilla akaongeza kusema huku akisikitika kwa kutikisa kichwa chake.
Hakika huo ulikuwa ni msumari wa moto kwa Salum Zakwa, ambaye nafsi yake ilikuwa ikimsuta kwa kumuua mtu yule ambaye alikuwa na haki ya kuishi hapa duniani, lakini akaondolewa pasipo kupenda. Hata hivyo, kwa upande wa Josia Kessy aliyekuwa anaujua mpango mzima, na jinsi Abul Zengekala alivyouawa na Salum Zakwa, aliamua kuificha siri hiyo, kwa rafiki yake huyo, ambaye pia ni kigogo hapa nchini!
Maongezi yale yalimsumbua sana Salum Zakwa, ambapo alichukia sana na kuamua kuaga na kuondoka ndani ya ukumbi ule wa Casino, kurudi nyumbani kwake, Upanga. Aliondoka na kuwaacha, Josia Kessy, Maiko Nilla na Alfred Kwega wakiendelea kucheza kamari. Tokea siku hiyo ndiyo ukawa mwisho wake wa kwenda kwenye hoteli ile ya Africo kucheza mchezo huo wa kamari!
********
Vasco Nunda alianza kazi rasmi kumtumikia Salum Zakwa. Yeye na Liston Kihongwe wakawa wanampeleka bosi wao, katika sehemu mbalimbali za jiji kukutana na maajenti wake, ama kuwakabidhi bidhaa, au kupokea fedha, ama vyote, kukabidhi na kupokea. Na wakati huo pia, Kamba alikuwa akiwaonya maajenti waliokuwa wanachelewesha malipo.
Kazi hiyo ya hatari na ya roho mkononi, walikuwa wakiifanya saa za usiku tu. Na mara nyingi walitumia gari la Liston, ambaye ndiye aliyekuwa dereva kwa wakati huo, na Vasco alikuwa ndiye mpambe. Hata hivyo, waliambiwa kuwa endapo itatokea rabsha, hasa na polisi, wote watatu, Vasco, Liston na bosi wao, lazima watumie bastola. Ni kufa ama kupona, hakuna kukamatwa kirahisi na kupelekwa mahakamani. Lakini hapakutokea matatizo katika kazi hiyo!
Salum Zakwa alizidi kumwamini kijana, Vasco Nunda, siku hadi siku kwa kadri alivyokuwa anafanya kazi kwa ufanisi. Na baada ya mwezi mmoja, akampa fedha za kununua gari jipya, aina ya Toyota Land Cruiser GX. Hilo ni gari la gharama kubwa, ambalo lilikuwa linamilikiwa na watu wenye uwezo wa kifedha tu, na siyo mlalahoi. Hakika Vasco akawa ni mmoja wa vijana walioonekana matawi ya juu, na kila mmoja alimnyooshea kidole kutokana na mafanikio yale ya haraka haraka.
Baada ya miezi mingine miwili iliyofuata, Salum Zakwa alimpatia fedha ya kujenga nyumba ya kifahari eneo la Kinondoni Hananasif, katika kiwanja alichonunua kwa bei mbaya sana. Maisha yakawa yananyooka Vasco kwa upande wake, akiiona ile si ndiyo kazi aliyotakiwa kuifanya mtu kama yeye, mwanaume wa shoka!
Siku moja, Vasco na Liston walikuwa wamekaa sebuleni, katika nyumba mpya ya Vasco, aliyoijenga. Wakati huo walikuwa wakijiburudisha na vinywaji na pia wakiwa katika maongezi yanayohusu kazi zao kwa ujumla.
“Liston,” Vasco akamwita kwa sauti ndogo.
“Naam...” Liston akaitikia huku akimwangalia.
“Naomba kukuuliza kidogo mambo fulani…”
“Uliza tu ndugu yangu…”
“Hivi huyu bosi wetu, atakuwa anaingiza shilingi ngapi kwa mwezi? Mimi na wewe anatulipa milioni tatu kwa mwezi. Anatununulia magari, ametujengea nyumba, na ukiwa na shida ya laki mbili tatu anakupa kama vile anakupa peremende. Na watu wake wengine ambao hatufahamiani nao unafikiri anawalipa kiasi gani?”
“Anaingiza pesa nyingi sana,” Liston akamwambia na kuendelea. “Unajua kila baada ya miezi sita, huwa analetewa mzigo wa kilo mia moja, ambao ananunua kiasi cha shilingi milioni mia tano, lakini katika dola za Kimarekani au paundi za Kiingereza. Kisha yeye anauza kilo moja shilingi milioni ishirini. Je, unajua anatengeneza kiasi gani?”
“Hapana, sijui, mimi mahesabu yamenipiga chenga...”
“Anatengeneza milioni elfu mbili!”
“Mungu wangu!” Vasco akasema kwa mshangao. Akataka kusema neno, lakini simu yake ikaita. Akaichukua na kuiweka sikioni.
“Haloo...” akasema
“Vasco!” Ilikuwa ni sauti ya SalumZakwa!
“Bosi...” Vasco akaitikia.
“Nimepokea simu kutoka ng’ambo. Mzigo utaingia leo saa nane za usiku, nitawahitaji nyote. Unajua Liston yuko wapi?”
“Ninaye hapa...”
“Vizuri,” Salum Zakwa akasema. “Saa nane kamili za usiku, tukutane ‘Chumba Namba Moja.’ Tumieni gari moja tu, lako au lake...”
“Sawa, bosi. Ni utekelezaji...”
********
Walitumia gari la Vasco, Toyota Land Criser GX. Ni gari ambalo lingeweza kuhimili pilikapilika zile za usiku hata kwa kufukuzana na askari wa polisi watakaokuwa wamewashtukia. Hivyo walijiandaa harakaharaka huku pia wakichukua silaha zao, bastola za kuwalinda. Walipokuwa tayari, waliondoka pale Kinondoni kuelekea katika makutano yao ufukweni mwa bahari. Usiku huo magari hayakuwa na foleni kubwa sana, kitu ambacho kiliwafanya wafike katika eneo lile kabla ya saa nane kamili za usiku.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kufika eneo hilo la Kunduchi, waliwakuta vijana wengine watatu, mmoja wao akiwa dereva, aliyewafikisha kwa gari moja aina ya Toyota RAV 4J ya rangi iliyofifia, ambayo ilikuwa imepaki katikati ya kichaka chenye giza.
Kwa mtu wa kawaida angepita pale kwa usiku huo, ilikuwa siyo rahisi kuliona gari lile, hakika walikuwa wamejiandaa vya kutosha jinsi ya kujilinda. Dereva yule kijana, alijulikana kwa jina la Sudi Makapeti, na wale vijana walikuwa ni wapagazi maalum wa kupakua mizigo ya dawa za kulevya inayofikishwa kwa boti maalum kutoka katika moja ya meli zinazotia nanga baharini.
Wote walikuwa wamekaa katika yale magogo ya mnazi, wakiendelea na maongezi yao kwa sauti za chini. Hakika eneo hilo kwa usiku ule lilikuwa linatisha kwa vijana wote waliokuwa pale, hasa kwa Vasco, kwani eneo hilo ndilo alilouawa mfanyabiashara, Abdul Zengekala, kipindi kile walipokuwa wanadaiana fedha na bosi wao, Salum Zakwa!
*******
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment