Search This Blog

Saturday, 5 November 2022

SURA MBILI - 3

 






Simulizi : Sura Mbili

Sehemu Ya Tatu (3)





“Habari za hapa jamani,” Liston akawasalimia.

“Poa,” wakajibu kivivu.

“Za kutangulia...”

“Shwari...”

“Haya, tupo wote!”

“Poa, karibu…”

Wote wakakaa kumsubiri bosi wao, Salum Zakwa.

Saa nane kamili, mvumo wa gari uliweza kusikia. Salum Zakwa akawasili pale na kulisimamisha gari, kisha akashuka akiwa na briefcace nyeusi mkononi mwake. Pia, alikuwa amevalia mavazi ya rangi nyeusi, yaliyomfanya asionekane vizuri kutokana na lile giza lililokuwa limetanda kote. Kama kawaida akawasalimia wapambe wake, ambao nao waliitikia kwa pamoja, na alipomaliza kuwasalimia, akachukua simu yake ya mkononi, na kuanza kuwasiliana na mtu, ambaye kwa muda ule hawakumfahamu zaidi ya yeye mweyewe!

Baada ya kumaliza kuwasiliana kwa simu, ndipo Salum Zakwa akajiegemeza katika ubavu wa gari lake kama alikuwa akisubiri kitu, na hakuwa akiongea chochote. Halafu punde tu, sauti ya mumo wa boti ikasikika ikitokea upande wa baharini. Ni boti ya ukubwa wa wastani, ambayo iliwasili pale ufukweni kimyakimya, ambapo ndani yake kulikuwa na watu wawili, ambao hawakuwa wabantu, walikuwa na asili ya Bara la Asia.

Baada ya boti kufika ufukweni, mmoja wao aliyeonekana kiongozi, aliteremka na kwenda hadi kwenye gogo la mnazi, ambapo Salum Zakwa alikuwa amekaa. Walionekana kama ni watu waliokuwa wanafahamiana sana katika kazi zao za kibiashara hiyo waliyokuwa wanaifanya, kwani alipomfikia Salum, alianza kuongea naye mawili matatu kwa lugha ya kiingereza.

“Mzigo tumeshakuja nao…” mtu huyo akamwambia huku akimwashiria kwa mkono kule ilipo boti.

“Kama mmekuja nao kinachofuata ni biashara,” Salum Zakwa akamwambia mtu huyo.

“Hebu nionyeshe kwanza fedha, hakuna kuaminiana siku hizi!” Mtu huyo akasisitiza!

“Hakuna shaka,” Salum akamwambia.

Briefcase ikafunguliwa na Salu Zakwa. Ndani yake ilikuwa imejaa fedha, noti, dola za Kimarekani, ambazo zilimfanya yule mtu mwenye asili ya asia, aridhike na kumfanyia ishara mwenzake ambaye alikuwa amebakia ndani ya ile boti iliyokuwa imetia nanga pale ufukweni. Akateremka na katoni moja la majani ya chai ambalo aliliweka juu ya gogo la mnazi baada ya kuwafikia. Halafu Salum akalifungua, na ndani yake kulikuwa na pakiti za kilo moja moja zilizokuwa zimefungwa kiufundi katika vifuko vya nailoni.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Salum Zakwa akaifungua pakiti moja, ambapo hakukuwa na majani ya chai ndani yake, bali kulikuwa na kete za unga wa dawa za kulevya, kila kete ilikuwa na gramu hamsini. Kete moja ikatobolewa na Zakwa, halafu akampa kijana mmoja, mpagazi, ambaye aliionja kwa ncha ya ulimi wake. Akaridhika na kukubali kwa kichwa kuwa kweli ilikuwa ni mali ya uhakika. Kazi ya kupakua ikaanza mara moja kutoka ndani ya boti ile, ambapo walipakuwa maboksi kadhaa yaliyokuwa yamesheheni dawa za kulevya zenye dhamani ya mamilioni ya fedha, ukiwa ni mzigo uliotoka nchi za Asia, kwa kutumia meli maalum ya uvuvi, ikitokea katika nchi ya Iran. Pia, ni meli ambayo iliingia kinyemela bila kushtukiwa ukiwa ndiyo utaratibu wao waliokuwa wameuzoea.

Baada ya kukabidhiwa fedha zao, watu wale walielekea ndani ya boti yao. Ikawashwa na kuondoka kwa mwendo wa kasi kuelekea kule baharini meli yao ilipokuwa imepaki. Kazi ile ya kupakua mzigo iliendelea kufanywa na wale vijana wawili, lakini, Salum Zakwa, Vasco na Liston walibaki wamesimama wakiangalia upakuaji ule ulivyokuwa unaendelea. Jumla zilikuwa katoni tano, kila katoni ilikuwa na uzito wa kilo ishirini. Hivyo vijana hao wakapakua mizigo hiyo kutoka kwenye boti na kupakia kwenye gari la Salum Zakwa ambalo liliweza kuhimili kubeba mzigo wote. Walipomaliza kupakia mzigo wote, Salum Zakwa akasema:

“Vasco Nunda kwenye gari langu, dereva na wapagazi mtatangulia, Liston utakuja nyuma yangu. Ni hadi tutakapofika Mzambarauni, ambapo tutaachana. Ikitokea patashika yoyote, ni mtutu na mkuku, sawa?”

“Sawa bosi!” Wote wakaitikia.

Dereva, Sudi na vijana wake, wakaingia ndani ya gari lile, Toyota RAV 4, na kuongoza msafara wa kurudi katikati ya jiji. Salum Zakwa akafuatia na Liston akamalizia, ambapo magari yote matatu yalikuwa yakienda kwa mwendo wa kasi sana kana kama vile magari yaliyokuwa katika msafara wa kiongozi mashuhuri!

“Vasco,” Salum Zakwa akamwita mpambe wake mkuu aliyekuwa amekaa naye mbele.

“Naam, bosi...” Vasco akaitikia huku akimwangalia.

“Unadhani ni kitu gani cha maana sana hapa duniani?”

“Nadhani kitu cha muhimu sana kwa binadamu, ni afya nzuri,” Vasco akamjibu na kuendelea. “Afya na ujasiri. Kwa sababu mtu mgonjwa na goigoi hawezi kufanya chochote cha maana!”

“Kama afya na ujasiri vingekuwa ni vitu vya maana sana, wewe usingekuwa kibarua wangu, kwani vyote hivyo unavyo!” Salum Zakwa akamwambia.

“Kumbe ni akili?” Vasco akaendelea kumuuliza.

“Hapana, si akili. Kuna watu wenye akili ajabu, lakini wanaishi maisha ya kawaida ya kawaida kabisa, kama wewe na Liston. Na wengine wanaishi maisha duni kuliko ninyi!

“Unataka kuniambia kitu muhimu duniani ni pesa?”

“Ndiyo, ni pesa. Kama huna pesa, hata malaria tu yanaweza kukuua, pamoja na mibavu yako na akili zako. Lakini kama una pesa, karibu maradhi yoyote yale unaweza kutibiwa kama si hapa nchini, ni nje ya nchi!”

“Lakini bosi, kama huna afya na akili utapataje hizo pesa? Ukirithi na hali huna ubongo utazipoteza...”

“Tunazungumzia mtu wa wastani, mwenye akili ya kawaida, kama mimi na wewe. Mtu kama huyo anahitaji ujanja tu, ili atajirike!”

“Aisee,” Vasco akasema.

“Na ingawa kila mtu anaogopa kusema waziwazi, ukweli ni kwamba hakuna anayejali umeupataje utajiri. Wazazi wako, mkeo, nduguzo, jamaa na marafiki hawajali kama ameiba, umethulumu au umefanya biashara mbovu kama hii yangu. Mradi tu usishikwe. Ukinusurika na kutajirika kila mtu atakuheshimu, atakuthamini na kukupenda. Lakini kama huna chochote, wewe ni takataka tu!” Salum Zakwa akaendelea kumwambia Vasco!

“Nakubaliana na wewe,” Vasco akakubali kwa kutikisa kichwa, kwani alikumbuka jinsi ndugu wa mama yake, walivyojitokeza ghafla baada ya yeye kuanza kupata fedha.

“Ndiyo, lazima ukubaliane na mimi!”

“Nimekubali...” Vasco akasema. Halafu bila kutegemea, akajikuta akimuuliza. “Samahani bosi, eti ile boti ilikuwa imetokea wapi?”

“Hilo ni kosa Vasco! Usipende kujua mambo yasiyokuhusu!” Salum zakwa akamwambia!

“Samahani bosi...”

“Ok, utajifunza. Hebu niambie jambo moja, unatumia unga?”

“Ndiyo, lakini si mtumiaji wa maana. Nautumia siku moja moja, hasa ninapokuwa na marafiki zangu wanaotumia.”

“Huo ndiyo mwanzo wake. Angalia, usiache ukutawale, kwani utaharibika...”

“Nafahamu,” akajibu Vasco. “Sidhani kama utanitawala kama unavyowatawala watu wengine!”

“Vizuri, nitakupa kete moja tutakapofika Mzambarauni, ambapo utakuwa unapata kete moja kila wakati mzigo utakapowasili. Mzigo huwasili kila baada ya miezi sita.”

“Sawa bosi...”

“Unajua kete moja ya gramu hamsini inauzwa kiasi gani?”

“Shilingi milioni moja...”

“Hiyo ndiyo bei ninayowauzia maajenti wangu....” Salum Zakwa akamwambia Vasco na kuendelea. “Maajenti nao hutengeneza kete zao za gramu kumi na kuwauzia wateja wao kwa laki tano kwa kete. Hivyo hupata milioni mbili na nusu. Na hao wateja wa maajenti wangu hutengeneza kete zao za gramu moja moja ambazo huwauzia wauzaji wa mitaani, mapusha, kete moja kwa laki moja. Hivyo nao hupata milioni moja katika hizo gramu kumi. Kama mteja wa ajenti akiuza gramu hamsini atapata milioni tano. Na hao mapusha huuza kidogo kwa mia tano hadi elfu moja, na kama pusha ataweza kuuza gramu kumi, atapata milioni kumi!”

“Ahahaa...” Vasco akacheka na kusema, “Kuna pusha mmoja anatumia ukucha wa kidole chake kidogo kama kipimo. Anauza ukucha elfu moja, na wala siyo ukucha mrefu. Sijui akiuza gramu moja atapata kiasi gani?”

“Ukipiga mahesabu ya pupa, utasasema mapusha ndiyo wanaopata faida kubwa kuliko mimi, kuliko maajenti wangu, kuliko wateja wangu. Kwa sababu kama pusha kete yangu moja ya gramu hamsini, ambayo ninauza kwa milioni moja yeye atapata milioni hamsini! Lakini hivyo sivyo mambo yalivyo. Wao, mapusha ndiyo wanapata faida ya chini kabisa na ndoyo wenye hali duni!”

“Kwa nini?”







*******

“Kwanza,” Salum Zakwa akasema. “Hakuna pusha anayeweza kuuza gramu mbili au tatu kwa siku. Wengine hata hiyo gramu moja huwasumbua wiki nzima. Pili, karibu mapusha wote wanatumia unga, wao na marafiki zao, ambao huwapa bure. Tatu, mapusha ndiyo wanaokamatwa mara kwa mara, siyo maajenti wangu wala wateja wa maajenti wangu. Hivyo wao hutoa pesa nyingi kwa askari polisi au mahakimu njaa, na nne, wanachezea pesa vibaya, hasa katika pombe na wanawake!”

Hatimaye msafara wao ulifika Mzambarauni, mtaa wa Kipata. Magari yakasimama kwa muda kando ya mtaa huo ambao kwa usiku huo bado kulikuwa na pilikapilika za watu wachache waliokuwa labda wanatoka katika starehe. Wengine walikuwa wanakula chipsi pembezoni mwa vibaraza. Hivyo hali ile haikuwatia wasiwasi wa kukamatwa na askari polisi wa doria ambao walikuwa wakizunguka usiku ule katika kuimarisha kazi za doria ndani ya jiji la Dar es Salaam.

Salum Zakwa aliongea mawili matatu na Vasco aliyekuwa naye ndani ya gari lake, halafu akampatia kipaketi kimoja cha dawa za kulevya kama alivyomhaidi. Hakukuwa na cha zaidi, Vasco na Liston walishuka, ambapo waliachana naye, ambaye yeye alijua alipokuwa anaupeleka ule mzigo wa dawa za kulevya. Ni sehemu ambayo kamwe hakupenda mtu mwingine ajue zaidi yake mwenyewe.

Dereva Sudi, aliyekuwa na lile gari jingine pamoja na vijana wake wawili, nao wakaondoka, kuelekea makwao. Kazi yao ilikuwa imekwisha kwa siku ile. Kama kawaida yao,Vasco na Liston, wakiwa ni watu wa kupenda starehe, wakaingia ndani ya nyumba ya Mama Hidaya. Ingawa ilikuwa ni saa tisa za usiku, lakini mlango ulikuwa wazi na pilikapilika ziliendelea usiku kucha. Baada ya kuingia humo ndani, walijipatia huduma ya vinywaji na hata wanawake warembo wa bei mbaya, ambayo ndiyo starehe waliyoipendelea.

Mambo ya fedha!



*********

Mara baada ya Salum Zakwa kuachana na Vasco Nunda pale Mzambarauni kwa Mama Hidaya usiku ule, yeye aliendelea na safari yake. Kwa muda ule hakuhitaji tena mpambe wa kumsindikiza hasa ukizingatia alikuwa anaupeleka mzigo wake sehemu ambayo hakupenda mtu yeyote apafahamu, hata hao wapambe wake. Ni kwamba hakuwaamni kwa asilimia mia moja, wanaweza kumgeuka mara moja!

Utaratibu wake aliokuwa amejiwekea, ulikuwa kwamba, baada ya kuupata mzigo kutoka nchi za nje, hasa unapokuwa katika idadi kubwa kama ule aliouchukua siku hiyo, huwa anaupeleka katika sehemu hiyo ya siri, ambayo pia wanunuzi wake hufika pale na kuununua mara moja ili kupoteza ushahidi. Wanunuzi wengi huwa wanaupeleka mikoani na hata nje ya nchi kama za Malawi, Zambia na hata Afrika Ya Kusini kwa kutumia usafiri wa barabara.

Maficho yake aliyokuwa anatumia mkuhifadhia mzigo huo haramu, yalikuwa eneo la Ubungo. Hivyo Salum Zakwa aliifuata Barabara ya Nelson Mandela, ambapo kwa usiku huo magari yalikuwa ni machache sana barabarani kitu ambacho kilimfanya aendeshe gari kwa mwendo wa kasi, hadi alipofika External, ambapo alipinda kulia na kuifuata barabara inayoelekea katika kiwanda cha maziwa. Hili ni eneo ambalo lina viwanda na mabohari mengi, vilevile reli ya treni ya mizigo ilikuwa inakatiza kuelekea huko viwandani. Kwa mbele yake kuna uchochoro mmoja ambao aliufuata na kutokeza kwenye moja ya mabohari yanayotumika kuhifadhia mizigo.

Getini palikuwa na walinzi wawili wa mgambo waliokuwa wanalinda bohari hilo. Vilevile bohari hilo lilikuwa linatumika na Shirika la Utafiti wa Udongo, ambapo baadhi ya mizigo yao ya sampuli za udongo na madawa huwa vinahifadhiwa hapo. Walinzi hao walikuwa wanamfahamu kama bosi wao, hivyo mlinzi mmoja alimfungulia mara moja, na gari la Salum akaliingiza gari ndani na kwenda kulisimamisha karibi na mlango mmoja wa kuingilia mle ndani ya bohari.

Salum Zakwa alishuka na kuongea mawili matatu na hao walinzi ambao naa walikuwa hajui kilichokuwa ndani ya gari, bali walimsaidia kuishusha kwa malipo maalum kamaalivyozoea kuwapa.

walinzi wale waliyekuwa wamekenua meno yao kwa furaha, walianza kushusha mzigo mmoja baada ya mwingine na kuiingiza ndani ya chumba kimoja kilichoko ndani ya bohari hadi alipomaliza yote. Ilikuwa ni kazi ya kukata na shoka, lakini kwa njaa aliyokuwa nayo walinzi hao, walihimili kuimaliza mizigo yote, halafu wakakatiwa kitita kikubwa cha fedha.

Mzigo ulipohifadhiwa katika sehemu salama, Salum Zakwa aliwaaga wale walinzi, halafu akaondoka kurudi nyumbani kwake, Sea View, Upanga, akiwa na matumaini. Akiwa ndani ya gari, alikuwa akiwasiliana na watu wa aina mbalimbali, wakiwemo wafanyabiashara ile ya dawa za kulevya, ambao alikuwa akiwafahamisha kuwa mzigo ulikuwa umeshaingia. Ni tayari kwa mauziano ili kuuondoa ushahidi ule! Kesho yake mzigo wote ulichukuliwa!

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

*********

Operesheni kali ya Jeshi la Polisi nchini, ilikuwa inaendelea kupambana na wale wafanyabiashara wa dawa za kulevya. Ingawa Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Wafanyabiashara wa Dawa za Kulevya nchini, Dickson Kweka, na jopo lake la makachero mahiri, Inspekta Raymond Gopi, Benito na Daniel kujipanga vizuri, hawakuweza kumgundua mara moja, Salum Zakwa, kwa vile alikuwa akiifanya biashara ile kwa kificho sana, na pia akiwa mtu mzito anayeheshimika mbele ya jamii.

Baada ya kuona kuwa hajashtukiwa, ndipo Salum Zakwa alipoendelea na biashara yake ambayo ilimuingizia kiasi kikubwa cha fedha, na kwamba aliamua kuitanua zaidi biashara hiyo, ukizingatia alikuwa ametegesha katika maeneo mbalimbali, hasa kwa kutumia wafanyabiashara wa kigeni, wanaomletea kwa meli, na pia kwa kuwatumia vijana wake maalum, Roki, Joel na Bomeza, ambao husafiri mpaka nchini Pakistan.

Vijana hao huwa wanarudi na unga, kwa kutumia mtindo wa kuzihifadhi kete tumboni na kuja nazo hapa nchini bila kushtukiwa, huku Salum Zakwa akiwa ameshasafisha njia kwa wote wanaohusika katika Viwanja wa Ndege vya Kilimanjaro, Mwanza, Dar es Salaam, Zanzibar, na hata Nairobi, nchini Kenya. Hivyo basi, baada ya ule mzigo wa kwanza kuingia na kufanikiwa kuusambaza wote, ndipo alipokaa na kupanga jinsi ya kuwatumia vijana wale.

Ukweli ni kwamba, vijana hao waliokuwa wanatumwa nje ya nchi, walikuwa hawafahamiani na lile kundi la kwanza, yaani wapambe wa Salum Zakwa, Vasco Nunda na Liston Kihongwe. Kila mmoja alikuwa akifanyakazi kivyake ili wasitambuane kwa kile Zakwa alichokiita kujilinda kiusalama ili wasichomane, Kwa kiasi fulani alifanikiwa kwa hilo. Tuseme, kwa jinsi alivyokuwa amejipanga, ni kwamba alikuwa na makundi matatu aliyokuwa amejizatiti nayo.

Kundi la kwanza ni la wapambe wake, Vasco Nunda na Liston Kihongwe. Hawa walitumika kwa kazi maalum ya kumlinda yeye na pia kuhakikisha hawezi kudhulumiwa mali zake. Ni ikitokea hivyo, ni kupambana na kuwamaliza wote! Kundi la pili ni la akina, David Osmond, dereva wake anayemtumia mara chache, Bosco Zambi na John Peka, wanaomsaidia katika shughuli za usambazaji kwa wateja wa mikoani.

Kundi la tatu ndiyo hilo la akina, Roki Sekulu, Joel Besha na Bomeza Jadu , ambao husafiri nchi za nje kuchukua mzigo kwa mtindo kwa kumeza tumboni. Hao ni vijana waliokuwa wanasafiri katika mazingira magumu sana huku wakihatarisha maisha yao kwa kumeza dawa zile matumboni mwao. Kulikuwa na hatari kubwa ya kuweza hata kupasukia tumboni na kusababisha mauti yao.

Wiki moja ilipita huku operesheni ikiwa bado inaendelea nchini dhidi ya wafanya biashara hao wa dawa za kulevya waliotapakaa sehemu mbalimbali. Hata hivyo Salum Zakwa hakutishika kabisa, kwani alikuwa akiendelea na utaratibu wa kazi zake zilizokuwa zinamkabili kwa kutumia kile kivuli chake cha ukurugenzi wa Shirika la Utafiti wa Udongo. Hakika alikuwa akijipanga ipasavyo kuweza kukwepa mitego yote ukizingatia aliweza kuiratibu kazi ile kwa kutumia watu wachache ambao hawakuweza kumjua kiundani zaidi.

Siku hiyo ya Jumamosi, ambayo ni siku ya mwisho wa wiki, nay a kimatanuzi aliyoipangilia, Salum Zakwa aliamua kukutana na vijana wakwe, Roki Sekulu, Joel Besha na Bomeza Jadu, ili kupanga mikakati yao ya kuwasafirisha kwenda nchini Pakistan, kuufuata mazigo wa dawa za kulevya. Kama kawaida walikutana kule katika ufukwe wa Hoteli ya Mikambo Beach, Kigamboni, ambayo ndiyo sehemu nzuri tulivu waliyokuwa wanakutana mara kwa mara ili kukwepa macho ya watu wanaowafahamu. Vijana wale ndiyo walikuwa wa kwanza kufika na kuelekea ufukweni mwa bahari ya Hindi, kumsubiri Salum Zakwa.



DAR ES SALAAM



*******

Walikaa sehemu ile ile palipokuwa na viti vya zege chini ya miti ya minazi iliyopandwa kisafu, na wakati huo giza lilikuwa limeshaingia na kufanya eneo hilo kuwe na giza kiasi na mwanga hafififu uliokuwa unatokea kwenye taa iliyokuwa umbali wa mita ishirini kutoka pale walipokaa. Baada ya kukaa kwa muda, ndipo walipomwona Salum Zakwa akiingia pale mithili ya kivuli, huku amevalia suti nyeusi kama kawaida yake. Mkononi mwake alikuwa ameubeba mkoba wake wa ngozi anaopenda kutembea nao mara kwa mra, vilevile alikuwa akitembea kwa mwendo wa kunyata hadi alipowafikia pale walipokaa, na yeye akajichukulia sehemu na kukaa karibu yao. Mkoba wake akauweka katikati ya miguu yake kwa kuukumbatia.

“Natumaini hamjambo vijana,” Salum Zakwa akawaambia.

“Hatujambo, bosi,” wote wakajibu kwa pamoja.

“Ni vizuri tupate vinywaji huku tukipanga mikakati yetu,” Salum Zakwa akawaambia.

Vinywaji vikaagizwa kwa kila mtu anachopendelea.

“Ndiyo vijana wangu,” Salum Zakwa akasema na kuendelea. “Nimewaita tena kwa ajili ya kupanga safari yetu ya kwenda nchini Pakistan. Ni kwamba mipango imeshakamilika kwa asilimia mia moja, nimeshakata tiketi na mtaondoka kwa ndege ya Shirika la Ndege la Emirates, ambayo huwa mnaitumia mara kwa mara, sijiu mnanipata?”

“Tunakupata, bosi,” Roki Sekulu akasema.

“Tupo wote, bosi,” Joel Besha naye akasema.

“Tupo pamoja, bosi…” Bomeza Jadu akaongeza.

“Vizuri kama mmenielewa vijana wangu. Kumbukeni kuwa nimeshasafisha njia kwa wahusika wote, hivyo jiandaeni kwa safari, mtaondoka kesho kutwa Jumatatu, majira ya saa mbili za usiku. Dereva, David Osmond atawachukua kuwapeleka uwanja wa ndege kama kawaida, halafu baada ya nyie kuondoka, na mimi nitakuja huko baada ya siku moja, ili kutafuta mzigo na kuulipia kabiasa. Sijui kuna mtu ana swali lolote?” Salum Zawa akawauliza huku akiwaangalia.

“Hauna swali lolote, kwani sote tuko tayari kwa safari,” Bomeza Jadu akasema.

“Haya, kama mko tayari, chukueni tiketi zenu hizi hapa,” Salum Zakwa akawaambia huku akitoa tiketi ndani ya mkoba wake aliokuwa ameufungua.

Vijana wale wakachukua kila mmoja tiketi yake.

“Pia, tumalizane kabisa kuhusu fedha za kujikimu,” Salum Zakwa akawaambia. “Ninawapa fedha ambayo imeshabadilishwa katika dola za kimarekani ili msipate usumbufu wa kubadilisha pale uwanjani, kwa ni itakuwa ni kupoteza muda tu!”

“Sawa, bosi…” wote wakaitikia huku sura zao zikioyesha furaha ilioje! Mambo ya fedha hayo!

Salum Zakwa alimpa kila mmoja kiasi chake cha fedha, ambacho kingemtosha kimatumizi. Baada ya kumaliza kuwapa fedha, ndipo walipoangana, Salum akatangulia kuondoka kuelekea sehemu alipokuwa ameliacha gari lake. Akawaacha vijana wale wakiendelea kunywa vinywaji vyao, kwani walishapata fedha za kutakata, ni kujirusha tu!



********

Siku ya Jumatatu, Salum Zakwa aliamka salama, ambapo alijiandaa tayari kuelekea ofisini. Baada ya kujiswafi, alivalia suti ya rangi ya kijivu iliyompendeza, na alipomaliza kuvaa, alimuaga mke wake na kuondoka. Alishuka ngazi kulifuata gari lake aina ya Ranger Rover Vogue, ambalo alikuwa anapenda kujiendesha mwenyewe, kwani hakupenda kutumia dereva kwa kile alichokuwa anakwepa kujulikana kwa siri yake. Na kama alipenda kutumia dereva, basi aliamu kumtumia kijana, David Osmond, ambaye ni mshirika wake.

Baada ya kulifikia gari lake, aliufungua mlango na kuiingia. Kisha akalitia moto na kuliondoa kuelekea katikati ya jiji, mtaa wa Azikiwe, ilipo ofisi ya Shirika la Utafiti wa Udongo. Muda huo wa saa mbili kasorobo za asubuhi, foleni ilikuwa ni kubwa sana katika Barabara ile ya Ali Hassan Mwinyi, kwa magari yaliyokuwa yanaelekea katikati ya jiji, lakini alifanikiwa kufika ofisini kunako majira ya saa mbili na nusu hivi, ambapo alilipaki gari nje ya Jengo la Benjamini William Mkapa, sehemu ya maegesho, kando ya Barabara ya Mnamdi Azikiwe ofisi ile ilipo.

Salum Zakwa alishuka ndani ya gari huku ameushika mkoba wake mkononi, halafu akaelekea ndani ya jengo hilo kwa hatua fupifupi. Alipofika kwenye lifti, alipanda na kuelekea juu katika ghorofa ya nne ilipo ofisi yao, ambayo ilikuwa kwenye korido ndefu iliyokuwa na ofisi nyingine za makapuni na mashirika mengine yaliyokuwa yamepanga katika jengo hilo. Ni ofisi iliyokuwa na wafanyakazi wapatao ishirini hivi, ambao wote walikuwa wakifuata amri yake akiwa kama mkurugenzi.

Kisha Salum Zakwa akaingia ofisini kwake mara baada ya kusalimiana na katibu Muhtasi wake, Bi. Grace Chambo, aliyekuwa amekaa ndani ya ofisi yake iliyoko jirani na ya kwake. Kitu cha kwanza baada ya kukaa, alichukua simu yake ya mkononi na kumpigia, David Osmond, dereva, ambaye alimsisitiza kuwa awe makini sana wakati atakapowapeleka vijana, Roko, Joel na Bomeza, uwanja wa ndege, tayari kwa safari ya kwenda nchini Pakistani.

Mara baada ya kuwapeleka uwanjani na kuhakikisha wameondoka salama, wakati wa kurudi, wakutane nyumbani kwake, Sea View, Upanga, kwa ajili ya maongezi mengine zaidi, kwa vile siyo maongezi yote wanayoweza kuyaongelea kwenye simu, kuhofia maongezi yao kunaswa. Kitu hicho alikuwa anakiheshimu sana! Baada ya kumfahamisha, ndipo alipoendelea na utaratibu wa kazi za siku ile zilizokuwa zinamkabili.



********

Majira ya saa moja kasorobo za usiku, vijana, Roki Sekulu, Joel Besha na Bomeza Jadu walikuwa wameshajiandaa kwa safari ya kwenda nchini Pakistan. Vijana wale ambao walikuwa wanaishi maeneo ya Kinondoni, mtaa wa Wema, walipitiwa na dereva, David Osmond, ambaye aliwapeleka uwanja wa ndege kunako majira ya saa moja za usiku hivi.

Hatimaye walifika katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, kunako majira ya saa mbili hivi, na moja kwa moja baada ya kushuka garini, walielekea katika jingo la kluondokea abiria. Walipomaliza taratibu zote za pale uwanjani, ndipo walipopanda ndanin ya ndege ile ya Shirika la Ndege la Emirates, ambayo iliruka na kuondoka kuelekea Pakistan.

David Osmond alipohakikisha vijana wale wameondoka, na yeye akaondoka pale uwanjani kurudi katikati ya jiji, na kuelekea nyumbani kwa Salum Zakwa, Sea View, Upanga. Baada ya kufika, alifunguliwa geti na mlinzi wa kampuni ya ulinzi ya binafsi, halafu akaliingiza gari hadi ndani, sehemu ya maegesho. Akashuka na kuelekea upande wa kibarazani, ambapo alimkuta bosi wake huyo amekaa kwenye kibaraza cha nyumba yake, sehemu aliyokuwa anapendelea kukaa mara kwa mara. Wakakaa na kuanza kuongea yao ya kibiashara yaliyokuwa yanawakabili.

“Vipi, umewafikisha salama,” Salum Zakwa alimuuliza David.

“Ndiyo bosi, nimewafikisha salama,” David Osmond akamjibu.

“Una uhakika hakuna mtu yeyote aliyekuwa anawafuatilia nyuma?”

“Hakuna bosi. Sidhani kama kuna mtu aliyetuungia mkia, kwani muda wote huwa makini sana kwa kila jambo.”

“Basi, vizuri. Sasa Mimi nilichokuitia ni kwamba na mimi nategemea kusafiri kesho kutwa kuelekea nchini Pakistan, katika shughuli zangu za kibiashara. Baada ya kufika huko Pakistan, nitakutana na wafanyabiashara wanaotutafutia mzigo huko Lahore, na kuhakikisha mzigo umefungwa vizuri katika mfumo wa ‘pipi,’ tayari kwa kubebwa katika matumbo ya vijana wetu. Pia, nitawakamilishia fedha zao kabisa ili tumalizane nao kabisa….” Salum Zakwa aliendelea kumwambia David Osmond.

“Vilevile,” Salum akaendelea kusema. “Nitawatembelea vijana wangu, ambao huwa wanafikia katika nyumba moja maalum iliyojificha sana kwenye milima yenye miinuko mikubwa, kiasi kwamba hakuna mtu yeyote anayewashtukia. Baada ya kumaliza kuwalipa fedha zao, ndipo na mimi nitaelekea nchini Uingereza kupoteza lengo, na hatimaye kurudi hapa nchini. Hivyo basi, dereva atakayenipeleka uwanja wa ndege wewe,” Salum Zakwa akaendelea kumwambia David Osmond.

“Sawa, bosi,” David akaitikia.

“Nakuonya kuwa, usiraibu kumwambia mtu mwingine, kwani wanaweza kuvujisha siri na hatimaye kuwekewa mtego. Kama kawaida yangu mimi nimeaga kuwa nakwenda nje ya nchi kuangaliwa afya yangu,”” Salum Zakwa akaendelea kumpa onyo David.

“Siwezi kumwambia mtu yeyote bosi,” David akamwambia.







******



“Haya, mimi ni hilo tu, unaweza kwenda,” Salum Zakwa akamwambia David.

“Nashukuru, bosi,” David akasema. Halafu akanyanyuka na kuondoka kwa hatua fupi kuelekea sehemu alipokuwa amepaki gari lake.

David Osmond aliondoka pale nyumbani kwa bosi wake, alimwacha amekaa pale juu ya kibaraza cha nyumba yake, akiendelea kunywa kinywaji chake taratibu huku kichwa chake kikipanga na kupangua mambo ya kufanya. Ukweli ni kwamba alikuwa na mipango mingi sana ya kuiratibu, yakiwemo ya ofisini kwake na yale ya biashara zake haramu!

Mara alipohakikisha David Osmiond ameondoka, ndipo aliamua kumpigia simu mtu mmoja muhimu sana. Ni Benard Ramson au Ben Ramson, ambaye ni Afisa Usalama katika Uwanja wa Ndege wea Julius Nyerere, ambaye walikuwa wanamtumia mara nyingi katik akusafisha njia, ili vijana wake wasiweze kukamatwa wanapotoka nje ya nchi wakiwa na zile dawa za kulevya. Baada ya kumpigia simui, upande wa pili ulisema:

“Haloo…mkuu…”

“Habari za saa hizi…” Salum Zakwa akamwambia.

“Hali ni nziri mkuu…” Ben Ramson akasema upande wa pili.

“Nina habari muhimu sana kwako…”

“Nipashe habari hiyo mkuu, si unajua nyie ni watu wakubwa?”

“Vijana wangu wamesfiri kwenda shamba kufuata mzigo…” Salum akamwambia.

“Ndiyo, nimewaona muda siyo mrefu, wameshaondoka kwenda shamba…” Ben akasema. Ni kweli kwamba alikuwa amewaona, Roki, Joel na Bomeza wakati walipokuwa katika harakati za kupanda ndege muda ule pale uwanja wa ndege.

“Basi ujumbe wangu ndiyo huo. Nakuomba uwasafishie njia na kuondoa magugu yasiwazuie mara wanaporudi kutoka shamba…” Salum Zakwa akamwambia.

“Hakuna shaka mkuu…tutafanya hivyo, kwani wanarudi lini?”

“Natumaini ni baada ya wiki moja hivi, kwani na mimi nategemea kuondoka kesho kutwa kuelekea hukohuko shamba. Lakini nitakapotoka shamba, nitapitia London, Uingereza, ndipo nitarudi hapa kabla wao hawajarudi, hivyo mengi tutawasiliana zaidi…”

“Sawa, mkuu, wakiwa tayari nijulishe tu, nitarekebisha mkuu, mambo yatakuwa safi…”

“Si kama kawaida yenu, mko watu kumi?”

“Ndiyo, tupo kumi, mkuu…”

“Basi, nitaweka fedha kwenye akaunti zenu kama kawaida…”

“Nitashukuru mkuu…”

Salum Zakwa na Ben Ramson wakamaliza mazungumzo yao.



********

Taarifa za kusafiri kwa vijana, Roki Sekulu, Joel Besha na Jadu, kuelekea nchini Pakistan, kuufuata mzigo wa dawa za kulevya, zilivuja na kumfikia kijana mmoja aliyejulikana kwa jina la Bruno Maliyatabu. Bruno ambaye mwanzo alikuwa ni mlinzi katika kampuni moja ya Upokeaji na Usafirishaji wa Mizigo, iliyokuwa inamilikiwa na mfanyabiashara mmoja wa kiarabu, Hasun Awadhi, ambaye alikuwa ameshakamatwa kutokana na tuhuma zile za kufanya biashara ya dawa za kulevya hapa nchini.

Kwa mara ya kwanza kabisa, kijana Bruno Maliyatabu alijisikia kuwa huru kulisaidia Jeshi la Polisi kwa kuwapa taarifa muhimu juu ya mtandao wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya, akiwa ameshajitoa katika kazi ile ya ulinzi katika kampuni iliyokuwa inamilikiwa na mfanyabiashara huyo. Hivyo aliamua kuwa msamaria mwema, na msiri, huku akitumia jina la siri, alilojulikana kama, ‘Boga Pevu,’ ili watu wasiweze kumgundua, hasa mtandao wa wauza unga, ambao wangeweza kummaliza mara moja kwa kuwaharibia biashara yao iliyokuwa inawapatia mafanikio makubwa.

Kwa vile Bruno alikuwa anafahamiana na wafanyabiashara wengi wa dawa za kulevya waliotapakaa katika pembe za mitaa ya jiji la Dar es Salaam, aliweza kupata fununu zile za vijana hao watatu, kwamba walikuwa wamekwenda nchini Pakistan, na walikuwa mbioni kurudi wakiwa na mzigo wa dawa za kulevya.

Siku hiyo alikuwa amekaa kwenye kijiwe cha vijana wanaojihusisha na biashara hiyo, sehemu za Kinondoni, mtaa wa Wema. Ndipo vijana hao walipoanza kuzungumzia juu ya vijana wale kurudi. Vijana hao waliochoka kimaisha na wabwia unga, walikuwa wakiwasifia vijana wenzao jinsi walivyokuwa wakipambana na maisha, kwa kuhatarisha hata maisha yao kwa ajili ya biashara ile ya unga.

Waliongelea mengi kwa kirefu sana, huku Bruno akiwapeleleza kwa makini, ambapo pia alijua ile siku ya wao kurudi, na watatumia ndege ya Shirika la Ndege la Emirates. Vijana hao waliokuwa wanaongelea habari hizo, hawakumtilia mashaka, wakijua kuwa ni mmoja wao, na asiyekuwa na mpango wowote! Kumbe walikuwa wakimwaga siri hadharani, ndipo Bruno, au Boga Pevu, alipoamua kuzifikisha taarifa zile kwa Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Wafanyabiashara wa Dawa za Kulevya nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi, Dickson Kweka, ili azifanyie kazi mara moja!



********

Ni siku nyingine ya asubuhi. Wingu zito lilikuwa limetanda angani na kuonyesha dalili za mvua kunyesha wakati wowote, ukizingatia ndiyo msimu wa mvua za masika ulikuwa umeanza. Kwa ujumla hali ya hewa ilikuwa ni nzuri kiasi cha kulifukuza joto lililokuwa likijikita ndani ya jiji la Dar es Salaam lenye pilikapilika nyingi.

Foleni ya magari barabarani haikupungua katika barabara kadhaa za jiji, zaidi ya kuongezeka na kufanya msongamano mkubwa wa magari ulioleta kero kwa waliokuwa wanatumia usafiri asubuhi ile, hususan kwa waliokuwa wanawahi makazini. Kwa ujumla matatizo yote yalisababishwa na msongamano wa magari.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Asubuhi ile kwenye taa za trafiki, katika makutano ya Barabara za Ali Hassan Mwinyi na Barabara ya Kenyatta, eneo la Upanga, gari moja aina ya Toyota Land Cruiser Prado, ilikuwa ni moja kati ya magari yaliyokuwa katika foleni ile. Ndani ya gari hilo, alikuwepo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi, Dickson Kweka, aliyekuwa akiendesha, ili kuwahi kazini asubuhi ile. Kwa muda wote alikuwa akiiangalia saa yake ya mkononi na kutikisa kichwa chake kutokana na msururu ule wa magari kwenda taratibu kutokana na taa, ingawa askari mwongozaji alikuwepo.

Wakati Dickson Kweka akiendelea kuwazia foleni ile, simu yake ya mkononi iliita. Akaichukua na kuangalia namba ya mpigaji, ambapo alimtambua; alikuwa ni kijana, Bruno Maliyatabu, au ‘Boga Pevu,’ mtu ambaye amejitolea kuwa msiri wa Jeshi la Polisi, kwa kuwafuatilia shughuli za wafanyabiashara wa dawa za kulevya!

“Haloo…Boga Pevu…lete habari…” Dickson Kweka akaipokea simu ile.

“Haloo…mzee…” Boga Pevu akasema upande wa pili.

“Habari za asubuhi…”

“Nzuri mzee…” Boga akasema na kuendelea. “Nimepiga simu ya ofisini lakini sijakupata, hivyo nikaamua kukupigia ya mkononi…”

“Ndiyo, leo nimechelewa kidogo, kwani mwanangu anaumwa.”

“Pole sana mzee…”

“Ahsante sana Boga…sijui una mpya gani?”

“Ndiyo mzee, kama kawaida yetu, na majukumu mliyonipa, kuna habari nyeti ambazo nataka kukumegea kuhusu watu wetu…”

“Ok, unaweza kunieleza baada ya kufika kazini. Naomba sana tukutane asubuhi hii!”

“Sawa mzee, utakuta nimeshafika.”

“Hakuna shaka, nitegemee baada ya saa moja.”

Baada ya kumaliza kuwasiliana, Dickson Kweka akaendelea na safari baada ya taa za trafiki kuruhusu magari. Akaifuata Barabara ile ya Ali Hassan Mwinyi hadi katikati ya jiji, na hatimaye akafika Kurasini. Hakika muda wote alikuwa na furaha baada ya kukamilisha kazi yao ya kwanza iliyokuwa inawakabili kwa kulisambaratisha genge la wauza dawa za kulevya lililokuwa linaongozwa na mfanyabiashara maarufu, Hasun Awadhi. Ni kazi ambayo ilikuwa imefanyika kama wiki mbili zilizopita na kukipatia sifa kubwa kitengo kile alichokuwa anakiongoza.

Kwa upande wake ilikuwa ni mwanzo mzuri operesheni iliyoanzishwa.

Dickson Kweka alifika ofisini baada ya robo saa, halafu akalipaki gari sehemu ya maegesho, ambapo palikuwa na magari mengine, mbele ya jengo la kituo. Hakupoteza muda, akashuka na kuingia ofisini huku ameshika

mkoba wake mkononi. Wakati huo, Boga alikuwa ameshafika na kukaa sehemu ya mapokezi akimsubiri, ambapo kwa asubuhi ile alionekana ni kijana mtanashati, mrefu na aliyevaa vizuri. Mkononi mwake alikuwa ameshika simu akibonyeza bonyeza namba mpaka alipomuona Kweka akiingia ofisini kwake.

Hata hivyo, Boga alisubiri pale nje kama dakika tano hivi, halafu akamfuata Dickson Kweka ofisini kwake. Baada ya kuingia akamkuta Katibu Muhtasi wake, ambaye alimruhusu kuingia ndani ya ofisi ile nadhifu, ambayo siyo mara yake ya kwanza kuingia. Akamkuta Kweka amekaa kwenye kiti chake cha mzunguko, na mbele yake kwenye meza palikuwa na mafaili kadhaa ambayo alikuwa anajiandaa kuyapitia, na alipomuona Boga, akatabasamu kidogo na kusema:

“Karibu Boga…”

“Ahsante sana…” Boga alisema. Halafu akavuta kiti kimoja na kukaa huku wakitazamana.

“Ndiyo Boga, lete habari…” Kweka akamwambia.

“Mzee kumekucha…” Boga akamwambia.

“Kumekucha sivyo?”

“Ndiyo mzee, kama kawaida yetu. Kuna habari nyeti nimezipata dhidi ya watu wetu tunaowafuatilia…”

“Hebu nipashe…” Kweka akamwambia huku akivuta karatasi moja tupu na kalamu tayari kwa kuandika chochote atakachoona kinafaa kuandikwa.

“Ni kama mlivyonipa kazi hii ya kuwafuatilia wafanyabiashara wa dawa za kulevya, ni kwamba kuna vijana watatu wa hapa jijini, ambao walikuwa wamesafiri nje ya nchi, wanategemea kurudi hapa nchini kesho kutwa, wakitokea nchini Pakistan, wakiwa na dawa za kulevya. Ni dawa ambazo hutumwa na ‘Bosi’ wao, ‘Zungu la Unga’ na‘Kigogo’ serikalini, ambaye pia ana marafiki wengi katika nchi za India na Pakistani…” Boga alisema halafu akanyamaza kidogo kupisha maelezo yale yamwingie Kweka.

“Je, unawafahamu vijana hao?” Dickson Kweka akamuuliza.

“Ndiyo, nawafahamu kwa sura na majina. Ni wakazi wa Kinondoni, ambao hiyo ndiyo kazi yao kubwa, wakitumiwa kama wasafirishaji kwa kutumia matumbo yao, kwa kumeza ‘pipi’ zilizofungwa, na kuweza kuja nazo hapa nchini. Tuseme ni watu wazoefu.”

“Vizuri sana, sasa naomba unitajie majina ya hao vijana…”



Vijana hao wanajulikana kwa majina ya, Roki Sekulu, Bomeza Jadu na Joel Besha. Ni vijana ambao kwa kiasi fulani wameshahathirika na dawa za kulevya, kwani nao huwa wanayatumia, na pengine ndiyo hao hao wanyonyaji wanaohakikisha ubora wa kiwango cha mzigo wanaotaka kuusafirisha,” Boga aliendelea kusema.

“Umsema kuwa huwa wanatumwa na bosi wao, je, huwa wataongozana wote?”

“Sidhani kama watarudi wote, kwani mara zote yeye huwa anarudi na ndege tofauti na vijana wake.”

“Wenyewe watarudi na ndege ya shirika gani?”

“Watarudi na ndege ya Shirika la Ndege la Emirates.”

“Vizuri, sasa turudi kwa bosi wao, unamfahamu?”

“Ndiyo, namfahamu…”

“Naomba unitajie jina lake na anapoishi, kwani vizuri kumfahamu Samaki mkubwa, siyo kuwafahamu wadogo tu,” Kweka akamwambia Boga.

“Ni kweli mzee, ni vyema kumfahamu papa, na siyo kambale…” Boga akaongeza kusema. Halafu wote wakacheka!

“Ok, mmwage hadharani huyo mtu!”

“Ni Mheshimiwa, Salum Zakwa, Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti wa Udongo…natumaini unamfahamu mzee…”

“Aisee, namfahamu sana, lakini sikujua kama anajihusisha na biashara hiyo haramu. Na hata nyumbani kwake napafahamu, anaishi eneo la Sea View, Upanga...”

“Basi, elewa kuanzia sasa kuwa anajihusisha na biashara hiyo. Ni mtu mzito sana Serikalini, lakini ni muhimu mkamate mzigo kwanza, kwani yeye anaweza kupatikana tu…”

“Vizuri sana Boga, maadam umenipa taarifa hizi, tutazifanyia kazi…” Kweka akamwambia Boga.

Baada ya kumaliza kupeana habari zile, Boga akamuaga Kweka, halafu akaondoka na kumuacha pale ofisini akinoa bongo na kupanga jinsi ya kuifanya kazi ile ukizingatia ndiyo kwanza walikuwa katika operesheni ile ya kupambana na wafanyabiashara wa dawa za kulevya, na mafaniko ndiyo yale yaliyokuwa yameonekana kwa kuwatia mbaroni vinara wengine, ambao wamepelekwa mahakamani.

Ili kuhakikisha zaidi kama Salum Zakwa alikuwa ni zungu la unga, Kweka akachukua lile faili lililokuwa na taarifa za wafanyabiashara wa dawa za kulevya. Akaanza kuyapitia yale majina kama yalivyokuwa yameorodheshwa na Kachero Inspekta Raymond. Hata hivyo, jina la Salum Zakwa halikuonekana, ina maana yeye alikuwa ni mtu anayejishughulisha na biashara ile kwa siri sana. Hivyo basi, akaliongezea jina lile kwa kalamu ili iwe kumbukumbu.

“Salum Zakwa!” Dikson Kweka akajisemea kwa sauti ndogo, ambayo aliweza kuisikia mwenyewe. Huyu ni mtu aliyemfahamu vilivyo, akiwa ni Mkurugenzi wa Idara ua Utafiti wa Udongo, na pia kabla ya kuteuliwa na Mtukufu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pia alikuwa kuwa Afisa wa Jeshi la Wananchi, aliyefikia cheo cha Kanali. Kiumri alikuwa na umri wa miaka 55 hivi, akiwa mwenye afya njema iliyomfanya aonekane mdogo kuliko umri wake.

Ni mtu ambaye walikuwa wanakutana katika maeneo mbalimbali katika shughuli za ujenzi wa Taifa, na hata katika sehemu za starehe. Ukweli ni kwamba alikuwa amefanikiwa kimaisha. Sasa hilo la kuhusika na biashara haramu ya dawa za kulevya, ukweli ni kwamba ilimchanganya Dickson Kweka. Hata hivyo Kweka alipanga kufuatilia habari zake kwa undani zaidi, akimshirikisha Kachero Inspekta Raymond, ambaye alimwita na kumwelezea juu ya kile alichoelezwa na mtoa siri wao, Boga Pevu! Wakapanga namna ya kumfuatilia!



********

Hali ya hewa ilikuwa bado ni ya mawingu mazito ya mvua za masika. Ndani ya eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, gari moja aina ya Toyota Land Cruiser ya rangi nyeusi ilionekana ikipaki katika eneo la maegesho ya magari. Baada ya kupaki, David Osmond alishuka na kuufunga mlango huku akihakikisha kama ameufunga vizuri. Aliporidhika, akanyanyua hatua kuliendea lile jengo la uwanja wa ndege, huku mkononi amekamata ufunguo wa gari.

David Osmond alikuwa amefika pale uwanjani kumpokea Salum Zakwa, aliyekuwa anatokea nje ya nchi, baada ya kusafri wiki moja iliyopita, katika mishughuliko yake ya kibiashara. Akiwa anajua anachokifanya, Zakwa alikuwa ameshawasiliana na walinzi wake, Vasco Nunda na Liston Kihongwe, ambao aliwapangia kazi maalum ya kumlinda kwa kumfuatilia nyuma bila mtu yeyote kufahamu, ukiwa ni utaratibu mpya alioupanga katika kukwepa vyombo vya dola.

Hivyo basi, katika ile kazi ya kwenda kumpokea uwanjani pale siku hiyo, alimtumia kijana, David Osmond, ambaye naye hakuwa anajua kama kuna walinzi wengine waliokuwa wamepangwa, tuseme walikuwa hawafahamiani kabisa. Siku zote alikuwa akiwajua washirika wake wawili tu, John Peka na Bosco Zambi, ambao kazi yao ni moja, huwa wanafanya pamoja.

Salum Zakwa, ‘zungu la unga,’ ambaye serikali ilikuwa haijamshtukia, alikuwa anatokea nchini Uingereza alikopitia kwa muda na kukaa siku mbili tu, akijifanya amekwenda kuangaliwa afya yake. Kabla ya hapo, alikuwa amekwenda nchini Pakistani, alikokwenda kukamilisha mipango yake ya biashara ya dawa za kulevya, ili wale vijana wake watatu, waweze kusafiri nayo hadi nchini kama alivyokuwa anafanya siku zote. Na hata mara nyingine huwa anasafiri na dawa hizo yeye mwenyewe, baada ya kufanikiwa kusafisha njia!

Mawazo ya David Osmond, alikuwa anajua kwamba bosi wake, Salum Zakwa, alikuwa anarudi akiwa na mzigo wa unga kama kawaida yake, ambapo mara nyingine huwa anapitia katika mlango wa wageni maalum ambao huwa wanapitia viongozi mbalimbali ambao hawakaguliwi. Hivyo hakutulia kabisa, kila mara alijenga wasiwasi, akihisi labda kuna watu waliokuwa wakimfuatilia yeye baada ya kuwagundua wakati akipokuwa anakwenda pale uwanja wa ndege. Kuna gari moja aina ya Toyota Land Cruiser GX ya rangi nyekundu ilikuwa ikimfuatilia nyuma, na hata sura ya waliokuwa ndani yake hakuwaona kabisa.

Lakini wakati alipokuwa anakata kona kuingia uwanja wa ndege wa Terminal II ndipo alipopoteza nao, hakukumbuka kama nao waliingia ama la, maana nyuma yake yaliingia magari kama matano kwa wakati mmoja na kumziba. Hivyo David alichukua tahadhari kubwa akijaribu kusoma kila sura ya kila mtu pale uwanjani, kusema kweli hakumwamini mtu kwa wakati ile, kila mmoja alimwona ni kachero wa Jeshi la Polisi! Ni hadi bosi wake, Salum Zakwa alipowasili. Hata hivyo kwa David hakuona na sababu ya kutojiamini, kwa vile si mara yake ya kwanza kumpokea, akiwa ni mtu mzito serikalini anayeheshimka!

Ndege kubwa aina ya Boeing 747 ya Shirika la Ndege la Uingereza, ilitua salama kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Abiria wote walishuka huku Salum Zakwa akiwa ni mmoja wao, ambapo muda huo alikuwa amevalia suti nyeusi iliyompendeza, na mkononi mwake alikuwa ameshika mkoba wa ngozi. Baada ya kukamilisha shughuli zote za pale uwanjani, alitoka nje na kumkuta David Osmond akimsubiri sehemu ile ya kusubiri abiria wanaotoka nje ya nchi.

Walipokutana, hakuna aliyetaka kuongea zaidi baada ya salamu fupi. Kisha David akampokea ule mkoba halafu wakaelekea pale alipokuwa amepaki gari. Walipofika kwenye gari, wakafungua milango na kuingia, ambapo Salum Zakwa alikaa upande wa kushoto. David akalitia moto na kuliondoa eneo lile la uwanja wa ndege kwa kuifuata barabara kwa mwendo wa taratibu. Ni hapo David alipoamua kumwambia juu ya mkasa uliompata kwa kufuatiliwa nyuma na watu asiowafahamu!

“Bosi…” David Osmond akasema.

“Sema, David…” Salum Zakwa akasema huku akimwangalia.

“Nilikuwa na wasiwasi sana, punde tu baada ya kufika hapa uwanja wa ndege...” David alimwambia huku macho yake kayaelekeza mbele.

“Kwa nini uwe na wasiwasi?” Salum Zakwa akamuuliza huku akitabasamu.

“Usalama wako,bosi!

“Ulifikiri nitakamatwa na unga?”

“Hapana…ila nilikuwa namchunguza kila mtu ili kuhakikisha usalama wako, pamoja na ‘mzigo.’ Hivyo kila sura ya mtu niliitilia mashaka ukizingatia kuna operesheni kali inayoendeshwa na Jeshi la Polisi kwa sasa, ambapo wenzetu wameshatiwa mbaroni, hivyo ni lazima niwe macho!” David Osmond aliendelea kusema.

“Usijali sana David,” Salum Zakwa akasema na kuongeza. “Mimi ninajua ninachokifanya na isitoshe ni mtu mkubwa sana serikalini. Hakuna wa kunisumbua!”

“Hilo naelewa bosi…”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Basi, usihofu…kaza buti!”

Walipotoka eneo la uwanja wa ndege, na kuingia katika Barabara ya Nyerere, kuelekea katikati ya jiji, ndipo David Osmond alipoanza kupata wasiwasi tena. Akageuka na kumwangalia bosi wake, kutaka kumwambia kuhusu lile gari lililokuwa linawafuata nyuma. Pia, alitaka kumwambia kuwa tokea mwanzo alipokuwa anakuja, kuna watu wawili walikuwa wakimfuata nyuma ya gari lao, na ndiyo hao walikuwa wanawafuatilia kwa sasa!

Kwa mtu yeyote, hasa akiwa kama dereva na mlinzi wa bosi, alitakiwa kuwa na uhakika wa kazi yake na kile anachokisema. Hakujua kama angeweza kuwadhibiti watu wale peke yake, ambapo alifikiri ni makachero wa Jeshi la Polisi walikuwa katika operesheni ile!





*******

Kwa mtu yeyote, hasa akiwa kama dereva na mlinzi wa bosi, alitakiwa kuwa na uhakika wa kazi yake na kile anachokisema. Hakujua kama angeweza kuwadhibiti watu wale peke yake, ambapo alifikiri ni makachero wa Jeshi la Polisi walikuwa katika operesheni ile!

“Najua unachowaza David…” Salum Zakwa akamwambia huku akimuangalia.

“Unasemaje bosi?” David akamuuliza!

“Ninasema kuwa najua unachowaza!” Salum akasema na kuongeza. “Ni kuhusu ile gari inayotufuatilia nyuma, au sivyo?”

“Ni kweli bosi, umejuaje?”

“Nadhani unajua kuwa mimi ni mtu wa aina gani katika nchi hii. Hakuna wa kunibabaisha!”

“Ah, bosi nakufahamu sana, wewe ni mtu mzito!”

Ni kweli David Osmond alimfahamu sana Salum Zakwa ipasavyo. Ni kati ya watu wenye akili sana na waangalifu wakubwa. Ni vigumu kumfuata kwa namna yoyote asigundue, tuseme alikuwa anajiamini sana ukizingaia aliwahi kuwa Afisa katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania, kabla ya kupatiwa wadhifa wa Mkurugenzi wa Kitengo cha Utafiti wa Udongo.

“Wameanza kukufuatilia saa ngapi?” David Osmond akamuuliza.

“Muda mrefu tokea nilipokuwa naelekea uwanja wa ndege,” David akamwambia.

“Tokea wapi?”

“Tokea nilipofika eneo la Vingunguti. Sijui kama walianzia hapo au nilitoka nao mbali…”

“Unasikia David…” Salum Zakwa akamwambia.

“Ndiyo, bosi…”

“Inakupasa uwe makini, kwani siku nyingine unaweza kunasa kwenye mdomo wa makachero wa polisi!”

“Siku nyingine?” David akauliza huku akimwangalia na kuendelea. “Kwani huoni ndiyo hao wanatufuatilia nyuma leo, wakiwa na gari lile, Toyota Land Cruiser?”

“Leo hakuna kitu kama hicho, wale ni watu wangu. Tuseme ni walinzi niliowatuma watuchunge sisi, na huwezi kuwafahamu.”

“Unasema ni walinzi?”

“Ndiyo, wanaitwa Vasco Nunda na Liston Kihongwe!”

“Aisee?” David akasema huku akishangaa kuwa kumbe walikuwa wengi lakini hawafahamiani!

“Ndiyo uelewe mpaka sasa!” Akaongeza!

“Mbona hukuniambia kama kuna watu maalum wa kutufuatilia?”

“Unasikia David, hii ni kazi ngumu. Na siyo kila kitu lazima ukijue. Hawa watu huwajui, na nimewaleta makusudi kwa vile nilijua hapa ‘Bongo’ kumeharibika kiasi kwamba watu kukugeuka ukiwa peke yako!” Salum Zakwa akamwambia.

“Hilo ni kweli bosi…”

“Halafu ujue kwamba hapa nilipo sikuja na mzigo…”

“Kwa nini hukuja nao?”

“Mzigo wanakuja nao vijana wetu, Roki, Joel na Bomeza, ambao wanatokea nchini Pakistan moja kwa moja baada ya mimi kuwasawazishia mambo yote. Watakuja na ndege ya Shirika la Ndege la Emirates, kunako majira ya saa mbili na nusu za asubuhi. Baada ya kusawazisha mambo yote ya mzigo huo, ndipo nilipopitia nchini Uingereza ili kupoteza lengo kama kuna watu waliokuwa wananifuatilia kunichunguza.”

“Ni jambo la busara bosi…”

“Hivyo basi, leo baada ya kunirudisha mimi nyumbani, wewe utarudi ili mkakae kikao na wenzako, Bosco na John, katika kupanga jinsi ya kwenda kuwapokea vijana wetu siku hiyo wanapokuja na ule mzigo kutoka nchini Pakistan. Si unajua tena shughuli za kuwapokea ni ngumu sana hasa kama ule mgao tunaotoa wa kusafisha njia, haujawafikia walengwa wote? Wanaweza kutugeuka mara moja, askari siyo watu kabisa! Baada ya kupanga na kukamuilisha, mnijulishe, sijui umenipata?”

“Nimekupata bosi, nitafanya hivyo.”

“Ninakuamini sana, hasa wewe ukiwa kama kiongozi wa wenzako. Safari nitakuwa macho sana, hasa kwa mtu atakayejaribu kutusaliti! Nitakuwa mkali na tusije tukalaumiana!” Salum Zakwa akasema kwa kutoa kitisho! Umafia!

“Hatuwezi kukugeukia bosi, si unajua kazi hii inatusaidia wote?”

“Ndiyo, muelewe hivyo! Sitaki mchezo, hali imeshakuwa mbaya sana! Si umesikia jinsi wenzetu walivyokamatwa katika operesheni ya Jeshi la Polisi inayoendelea?”

“Yote naelewa bosi…”

“Kuwa makini!”

Waliendelea na safari yao kuifuata Barabara ya Nyerere hadi walipoingia katikati ya jiji. Msongamano wa magari barabarani ulikuwa ni mkubwa, lakini walikwenda hivyohivyo kwani hiyo ni hali ya kawaida katika jiji la Dar es Salaam. Wakaingia katika Barabara ya Bibi Titi Mohamed ambayo waliifuata hadi walipokutana na Barabara ya Ali Hassan Mwinyi. Wakaifuata Baada hiyo hadi walipofika nyumbani kwa Salum Zakwa eneo tulivu la Sea View, Upanga.

Geti likafunguliwa na mlinzi mmoja wa kampuni binafsi ya ulinzi, na gari likaingizwa hadi ndani ya jumba lake lililokuwa ufukweni mwa Bahari ya Hindi. Ni jumba ambalo halikutofautiana na Kasri la Mfalme, hivyo gari ikasimamishwa nje ya baraza, na Salum Zakwa akashuka na kuingia ndani huku akiwa na ule mkoba wake wa safari ambao ndiyo mzigo wake wa pekee aliokuwa nao.

David Osmond alipohakikisha bosi wake ameshaingia ndani, akaliondoa gari na kuondoka katika eneo lile. Akiwa njiani, alikuwa akifanya mawasiliano na wenzake, Bosco Zambi na John Peka, na kupanga sehemu ya kukutana ili kupanga ule mkakati wa kuwapokea wenzao wanaorudi na ule mzigo wa dawa za kulevya. Baada ya kuwasiliana kwa simu, ndipo walipokubaliana kukutana Kinondoni ili wakapange mipango yao, na kama kawaida huwa wanakutana katika sehemu ya faragha, kwenye grosari ya Dada Enjo, iliyoko Barabara ya Kinondoni ikiwa hatua chache kutoka barabarani. Walipanga wakutane kunako majira ya saa kumi na mbili za jioni.

********

Eneo lote la Kinondoni, lilikuwa limechangamka vilivyo jioni hiyo. Watu wengi walikuwa katika mihangaiko yao, wengine wakielekea majumbani kutoka makazini, na wengine walikuwa wakijiandaa kuelekea katika starehe. Umbali wa mita ishirini kutoka katika barabara kuu ya Kinondoni, katika grosari ya Dada Enjo, vijana watatu, David Osmond, Bosco Zambi na John Peka, walikuwa wamekaa katika meza yao iliyokuwa chini ya mti wa muarobaini.

Hili ni eneo ambalo walikuwa wamezoea sana kulitembelea, hasa kutokana na mmiliki wa grosari hiyo kuwa ni mtu mcheshi sana na pia ana uhusiano wa kimapenzi na kijana David, akiwa ni kimada wake wa nje ya ndoa! Alikuwa ni mwanadada wa nguvu, aliyekuwa amejazia na kukamilika katika idara, kuanzia umbile la mwili wake, mweusi, miguu ya bia, amejazia makalio. Ni mrembo tosha asiyepitwa na mwanaume yeote bi akugeuka nyuma!

Vijana hao walikaa mbali kidogo na wateja wengine, kwani walikuwa na mazungumzo yao nyeti, ambayo hawakutaka watu wasiohusika wayasikie. Pale walikuwa wakinywa vinywaji, bia, na pia wakila nyama choma. Kamwe hawakupenda kukaa na mtu mwingine zaidi ya wao wenyewe, na hata dada Enjo mwenyewe hawakumtaka! Walikuwa wakiongea mazungumzo ya kawaida hadi walipofikia pale katika mazungumzo ya kikazi waliyopangiwa na bosi wao, Salum Zakwa! David alivuta pumzi ndefu na kuzishusha, halafu akasema:

“Ndiyo ndugu zangu, tumekutana tena katika majukumu yetu ya kazi…”

“Ni kweli, tufanye hivyo, maana ndiyo kazi inayotuweka hapa mjini…” akasema Bosco.

“Tupange mkakati…” naye John akasema.

“Kama kawaida leo nilikwenda kumpokea bosi, uwanja wa ndege. Niliondoka hapa mjini na kuelekea uwanjani taratibu bila kuwa na wasiwasi wowote. Lakini cha ajabu wakati nikiwa barabarani kuelekea uwanja wa ndege, nikawa nafuatiliwa nyuma na gari moja aina ya Toyota Land Cruiser ya rangi nyekundu, hadi nilipofika uwanjani. Na hata wakati wa kurudi, halikadhalika gari ile ilikuwa inanifuatilia na ndani yake kukiwa na watu wawili…” David akanyamaza kidogo huku akiwaangalia.

“Mimi nilifikiri labda ni makachero wa polisi wananifuatilia kiasi cha kunifanya, niwe na wasiwasi. Lakini bosi akanitoa wasiwasi na kuniambia kuwa wale walikuwa ni wenzetu, yaani walinzi ambao hata sisi hatuwafahamu!”

“Walinzi?” Bosco akauliza!

“Ndiyo, walinzi. Ina maana tuna walinzi ndani ya walinzi!”

“Ikawaje baada ya hapo?”

“Baada ya kumfikisha bosi, nao wakapotea! Sikujua walikoelekea!”

“Je, anawafahamu?” John akauliza.

“Siwafahamu, lakini alinitajia majina, ni Liston Kihongwe na Vasco Nunda. Ni watu ambao ni wageni kwetu!”

“Na majina yenyewe yanatisha!” Akasema Bosco, na wote wakacheka!

“Ok, tuyaache hayo. Cha muhimu amehimiza tupange jinsi ya kuwapokea wenzetu…” David akaendelea kusema.

“Hakuna jipya,” Bosco akasema na kuongeza. “Tutatumia njia tunazotumia siku zote kwa kwenda pale uwanjani kila mmoja akiwa na gari lake. Halafu baada ya kufika, tutayapaki sehemu tofauti na sisi kujigawa kila kona za eneo lile la uwanja, ili kujihami kwa lolote linaloweza kutokea.”

“Ni kweli tutatumia mtindo huohuo…” John akasema na kuelezea mipango yao kwa kirefu na kumalizia. “…na baada ya kufanikiwa, tutawapakiza katika magari yetu matatu na kuelekea nyumbani kwa bosi…”

“Sawa kabisa,” David akasema na kuongeza. “Lakini bosi ametoa angalizo. Ameseme kuwa tusifanya makosa yoyote yatakayosababisha mzigo wake kukamatwa! La sivyo tutamwelewa vibaya!”

“Mh, mbona anatoa vitisho?” Bosco akauliza.

“Ni kweli, anatutisha sasa! Kama ukikamatwa si bahati mbaya? Anatuletea uchuro sasa!” John akasema.

“Kweli ni uchuro. Lazima tuwe macho!” Akasisitiza David.

“Ok, tuombe Mungu ufike salama…” John akasema.

Baada ya kumaliza kupanga mipango yao, waliendelea na vinywaji vyao huku wakiongea mambo mengine mbali na ya kibiashara. Ni hadi ilipotimu saa tatu za usiku, wakawa wametosheka na kuondoka kurudi majumbani kwao, ambapo David alielekea nyumbani kwale, mtaa wa Kisangilo, Magomeni Mapipa, Bosco akaelekea nyumbani kwake, eneo la maghorofa ya Faya, na John akaelekea nyumbani kwake, Kinondoni, mtaa wa Sekenke. Wote walikuwa wamejiandaa vilivyo kwa kazi hiyo ya kesho yake asubuhi.



***************

Mvua za masika zilikuwa zinaendelea kunyesha mfululizo na kuwafanya baadhi ya watembea kwa miguu wajisitiri katika vibaraza vya majengo mbalimbali. Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Makachero wa Kitengo maalum cha kupambana na Wafanyabiashara wa Dawa za Kulevya, wakiongozwa na Kachero Inspekta Raymond Gopi, walikuwa wamejipanga vilivyo katika sehemu zao.

Walikuwa wakiisubiri ndege inayowaleta vijana wale, Joe Besha, Bomeza Jaduna Roki Sekulu, waliokuwa wanatokea nchini Pakistan wakiwa na dawa za kulevya! Hakika walikuwa wamejiandaa! Kachero Inspekta Raymond akiwa ni msimamiaji wa operesheni ile, alikuwa akiwasiliana kwa simu na mkuu wake wa kazi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi, Dickson Kweka, jinsi utaratibu ulivyokuwa unakwenda wakiwa na uhakika wa kuwanasa vijana wale ukizingatia mipango ilikuwa imeshakamilika. Na iwapo watafanikiwa, itakuwa ni kazi nyingine nzuri baada ya kufanikiwa kwa kazi ile ya kwanza ya kuwanasa wafanyabiashara wengine wa jijini Dar es Salaam.

Upande wa pili, vijana, David Osmond, John Pekana Bosco zambi walikuwa wameshafika pale uwanja wa ndege, wakiwa na magari matatu, kila mmoja akiendesha la kwake, tayari kuwapokea wenzao. Kama walivyokuwa wamejipanga jana yake, waliyapaki magari yao katika sehemu tofauti eneo lile la maegesho. Muda wote nao walikuwa wakiwasiliana kwa simu na bosi wao, Salum Zakwa, ambaye naye alikuwa akiwasisitiza kuwa macho na kuhakikisha mzigo huo unafika salama!

Lakini pia, vijana hao hawakuwa na wasiwasi wala kujua kama kulikuwa na mtego kabambe uliokuwa umewekwa na polisi, baada ya kupewa taarifa na kijana, Bruno Maliyatabu, au ‘Boga Pevu,’ ambaye alikuwa ameamua kuwa msiri wa Jeshi la Polisi kwa kuwataja wafanyabiashara wale, ambao wengi wao alikuwa anawafahamu baada ya kufanya nao kazi kwa muda mrefu.

Kwa ujumla, wote waliokuwa pale uwanjani, siyo makachero wale, wala David na wenzake, John na Bosco, ambao hawakuacha kuangalia saa zao za mkononi, ili kujua muda wa kuwasili kwa ndege ile ambayo hufanya safari zake za kufika Dar es Salaam mara kwa mara. Hali ya mvua ilionyesha kupunguza kasi yake na kuwa ya manyunyu, na muungurumo wa ndege ukasikika kutoka angani, ambapo ndege ile kubwa aina ya Air Bus, ilikuwa ikizunguka angani ili ipewe ruhusa ya kutua na waongoza ndege waliokuwa katika mnara wa kuongozea.

Kunako majira ya saa mbili na nusu za asubuhi, ndege ile ya Shirika la Ndege la Emirates, ilitua salama katika Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, na wakati huo mvua ilikuwa imeshakatika kiasi cha kufanya hali iwe nzuri. Ndege ile baada ya kutua, ikasogezwa na kusimama sambamba na jengo la uwanja tayari kwa abiria kushuka kwa kutumia mlango maalum unaopita juu kwa juu, na abiria wakaanza kushuka mmoja baada ya mwingine, na kupitia katika sehemu za ukaguzi kwa wale abiria watokao nchi za nje. Pia, mizigo iliyokuwa katika ndege, ilikuwa ikishushwa kwa kutumia nyenzo maalum, na kuingizwa kwa kufuata mkanda unaotembea.

Ndani ya chumba hicho, ambacho kilikuwa na utulivu wa kipekee, abiria walikuwa wakipita kwa zamu wakikaguliwa na mitambo maalum ili kubaini chochote kibaya. Katika sehemu ile ya ukaguzi, walikuwepo makachero wa Jeshi la Polisi, waliokuwa na mbwa wenye uwezo wa kunusa dawa za kulevya, na vitu vinginevyo. Pia, walikuwepo Maafisa wa Idara ya Uhamiaji na Ushuru wa Forodha, waliokuwa na hamu ya kuwanasa vijana wale, kwani walikuwa wameshapewa taarifa ya kuwasili kwao!

Kama kawaida, vijana, Roki Sekuli, Bomeza Jadu na Joe Besha, waliofika na ndege ile, walishuka huku kila mmoja akiwa kivyake, na kuacha watu kama kumi hivi au zaidi, kana kwamba hawakuwa katika safari moja. Hiyo ni mbinu walizokuwa wanatumia mara nyingi sana wanapokuwa katika safari zao za kusafirisha dawa za kulevya. Kwanza kabisa mbinu walizokuwa wanatumia, ni kuwa watu wa mwisho mwisho kabisa, ili kuwapumbaza wakaguzi, ambao mara nyingi huwa wanajua kinachoendelea, hasa Salum Zakwa anapokuwa ameshasafisha njia.

Ukweli ni kwamba walikuwa na uhakika wa kupita salama siku hiyo, wakiwa ni watu wazoefu katika biashara ile. Lakini cha ajabu baada ya kuika kwenye kizuizi cha ukaguzi, wote walijikuta wakiwekwa kando kwa nyakati tofauti, tena wakiwa chini ya ulinzi wa polisi. Wakachanganyikiwa kwa vile madawa yale walikuwa wameyahifadhi tumboni. Mara moja wakachukuliwa na kupelekwa kwenye kituo cha Polisi cha Uwanja wa Ndege kwa hatua zaidi za kiuchunguzi!

Kachero Inspekta Raymond, akiwa na makachero wezake, Daniel na Benito, waliondoka na vijana wale hadi katika kituo cha polisi, ambapo ungefanyika utaratibu wa kupewa dawa maalum ya kuweza kutoa zile pipi zilizokuwa na dawa za kulevya kwa njia ya haja kubwa, na kama ikishindikana kabisa, basi unafanyika utaratibu wa kupelekwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, yaweze kutolewa!

Na baada ya dawa hizo kutolewa, ndipo wafanyiwe mahojiano na waeleze kuwa ni mtu gani aliyekuwa anawatuma, kwani wao walikuwa ni wabebaji tu! Hakika walijiona kama watu waliokuwa ndotoni, hasa ukizingatia hawakutegemea kukamatwa kirahisi namna ile, na haikuwa mara yao ya kwanza kupita na mizigo ya hatari. Kwa vyovyote walijua kuwa kuna mtu aliyekuwa amewachoma, na alikuwa akifuatilia nyendo zao kwa muda mrefu sana.

Njia ya wokovu waliiona ni finyu sana, kwani pia walishindwa kuwasiliana na bosi wao, Salum Zakwa! Na pia hawakuweza kuwasiliana na wenzao, David Osmond, John Peka na Bosco Zambi, waliokuwa wanawasubiri kule nje ya uwanja sehemu ya kusubiria wageni wanaowasili.

Hali ilikuwa inatisha si mchezo!



********http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Saa nzima ilikuwa imepita baada ya ndege ile kutua. David Osmond, Bosco Zambi na John Peka walikuwa bado wakisubiri watu wao waliofika kuwapokea kutokea nchini Pakistani. Hata hivyo hawakuwaona baada ya kubonyezwa na mmoja wa watu wao wa siri anayesaidia uingizaji wao, kwamba walikuwa wamezuiliwa na maafisa wa usalama, baada ya kuhisiwa walikuwa na dawa za kulevya walizopaki matumboni mwao.

Ni mpaka muda ule walipochukuliwa na kupelekwa kwenye Kituo cha Polisi cha Uwanja wa Ndege, kilichokuwa eneo lile lile. Hakika wote walibaki wamechanganyikiwa sana. Na bila kupoteza muda, wakaamua kuondoka katika eneo lile la uwanja kila mmoja kivyake, ili wasije wakashtukiwa na kutiwa mbaroni na makachero wa polisi waliokuwa wamejazana karibu kila kona. Wote wakaondoka na magari yao na kuelekea katikati ya jiji huku wakiwasiliana kwa simu zao muda wote, na kabla ya kuamua la kufanya, wakaamua wakutane katika sehemu ya faragha kwanza na kupanga jinsi watakavyokwenda kumwambia bosi wao, Salum Zakwa!

Wakakubaliana kukutana katika hoteli ya Holiday Inn, iliyoko katikati ya jiji. Wakaelekea huko huku bado kila mmoja akipita njia yake hadi walipofika na kupaki magari katika sehemu tofauti. Hoteli ya Holiday Inn iko katika makutano ya mitaa barabara za Maktaba na Ali Hassan Mwinyi, ambayo ina hadhi ya kitalii. Hivyo basi, baada ya kushuka katika magari yao, wakakutana katika sehemu ya baa, iliyoko katika ghorofa ya kwanza, ambapo walikaa na kuagiza vinywaji laini aina ya mvinyo, na kuendelea kunywa huku wakitafakari namna ya kumuingia Salum Zakwa!

“Tumekutana tena jamani…” David Osmond akawaambia.

“Ni kweli tumekutana…maji mazito!” Bosco Zambi akasema,

“Ni nuksi tupu!” John Peka akasema na kuongeza. “Hakuna jinsi…twendeni tukamwambie hali halisi. Inawezekana dili hili lilishajulikana tokea mwanzo, siyo bure!”

“Hata mimi naona ni hivyo, kama alikuwa ameshasafisha njia, imekuwaje? Ina maana hata wale watu wetu wamemgeuka? Siamini!” David Osmond akasema kwa sauti ya masikitiko kidogo.

“Dili hili limeuzwa, huo ndiyo ukweli. Cha muhimu twendeni tukamweleze. Atajua cha kufanya!” Bosco Zambi akasema huku akitaka kunyanyuka.

“Poa, twendeni!” David Osmond akawaambia wenzake na kuongeza. “Tutamweleza hali halisi, ingawa najua kuwa hatatuelewa, ukizingatia bosi anachojua ni kupata tu, na siyo kukosa. Na pia ameshatumia fedha nyingi kwa Maafisa wa Usalama wa pale uwanjani hasa wa zamu ya leo. Sasa kitendo cha kumwambia umekamatwa, ni sawa na kutangaza vita!”

“Usihofu David, kama ni vita atangaze tu, hatujamsaliti sisi!” Basco Zambi akamwambia! Kwa kiasi fulani alijiamini sana!

Wote watatu wakanyanyuka na kuondoka huku wakiacha vile vinywaji vyao mezani kiasi cha kuwashangaza hata wateja wengine waliokuwa katika eneo hilo. Lakini kwa vile walikuwa wameshalipa, hakuna aliyewauliza. Wakashuka ngazi hadi chini, ambapo waliamua kupanda gari moja tu, la David Osmond, na kuondoka kuelekea kwa bosi wao, Salum Zakwa, eneo la Sea View, Upanga, ambapo hapakuwa mbali sana na eneo ilipo hoteli ya Holiday Inn.

Kwa muda ule hawakupenda kutumia magari kila mmoja na lake. Wakaifuata Barabara ya Ali Hassan Mwinyi hadi walipotokeza ufukweni mwa Bahari ya Hindi, na kuambaa na barabara ile hadi walipofika katika lango kuu la kuingilia ndani ya himaya ya Salum Zakwa! Mlinzi wa kampuni binafsi ya ulinzi alikuwa amesimama pale mlangoni akiendelea na kazi za ulinzi kama kawaida yake. Baada ya kuona gari lile limesimama pale langoni, akalifungua lango na kuliruhusu gari kuingia ndani.



*******

David akaliingiza gari na kwenda kulipaki katika sehemu ya maegesho, ambapo magari mengine matatu yanayomilikiwa na Salum Zakwa yalikuwepo. Muda wote huo alikuwepo akiwa amekaa kwenye meza moja iliyokuwa imezungukwa na viti vipatavyo viwili kila upande, ndani ya bustani hiyo iliyokuwa na kivuli cha kutosha na pia iliyozungukwa na miti ya kila aina. Vilevile palikuwa na maua yaliyopandwa kiufundi na mtunza bustani mahiri katika bustani hiyo iliyoko kando ya jumba lake la kifahari.

Meza ile ambayo pia ilikuwa ina mwamvuli, ilikuwa imajaa vinywaji baridi huku akikata kiu taratibu. Hapo alikuwa akiwasubiri vijana wake, David, Bosco na John, ambao walikwenda kuwapokea wenzao waliofika na mzigo ule wa dawa za kulevya kama walivyokuwa wanafanya siku zote.

Na kama iliyokuwa kawaida ya Salum Zakwa, alikuwa hafanyi mawasilano yoyote ya simu na vijana wake hasa wanapokuwa na mzigo hatari, mpaka ahakikishe mzigo unafika salama, akihofia kunaswa mawasilano yake na vyombo vya usalama, kama wangekuwa wanamfuatilia nyendo zake. Hivyo basi, huwa wanawasiliana punde wanapofika pale nyumbani kwake na si vinginevyo!

Sasa cha ajabu salum Zakwa alishangaa baada ya kuona vijana wake, David, Bosco na John, wakishuka kutoka ndani ya gari la David, bila kuwaona wale wengine, Roki, Joe na Bomeza! Macho yakamtoka pima na huku akiwaangalia kwa hamaki! Hali hiyo waliiona vijana wale, lakini wakaendelea kuijongelea meza yake kwa mwendo wa taratibu na pengine wakiwa wameinamisha nyuso zao chini kuyakwepa macho yake! Yalitisha si mchezo!

“Karibuni…” Salum Zakwa akawaambia huku akiyafikicha macho yake!

“Ahsante bosi…” David Osmond akasema huku Bosco Zambi na John Peka wakiwa wamenyamaza kimya. Halafu wakavuta viti vitatu na kukaa huku wametazamana na Kamba.

“Karibuni vinywaji mnavyopendelea…hapa kuna wiski, Konyagi, mvinyo, bia…chagueni mnachopendelea…” Salum Zakwa akawaambia huku akiunda tabasamu la kujilazimisha.

“Ahsante bosi…mimi nimetosheka…” David Osmond akasema.

“Nashukuru bosi…” Bosco Zambi naye akasema.

“Ahsante sana…” akaongeza John Peka.

“Mmegoma?” Salum Zakwa akauliza na kuendelea. “Haidhuru, David…nipe habari. Mbona hivi? Wenzenu wako wapi?”

“Hali mbaya bosi…” Bosco Zambi akamwambia.

“Mbaya kivipi…sijakuelewa…” Salum Zakwa akauliza huku akimwangalia kwa makini.

“Ni kwamba watu wetu wamekamatwa!”

“Msiniambie kuwa wamekamatwa!” Salum Zakwa akasema huku midomo yake ikimcheza na macho kumtoka!

“Ukweli ndiyo huo bosi, wamekamatiwa ndani wakati wakipekuliwa!”

“Shenzi sana, watakamatwa vipi wakati nimeshatoa fedha nyingi pale uwanjani? Ni lazima kutakuwa na mtu ametuchoma!”

“Inawezekana ikawa hivyo bosi…” Bosco Zambi akasema kwa kuunga mkono ile kauli ya bosi wake, Salum Zambi.

“Hata mimi naona. Nafikiri alifuatilia nyendo zetu na kugundua mpango wetu,” John Peka akasema.

“Hakika hii ni balaa bosi!” David Osmond akaendelea kusema.

“Unajua mpaka sasa mimi sijawaelewa?” Salum Zakwa akaendelea kusema kwa hasira. “Lazima kuna mmoja wetu ametusaliti, au nyie nyote mmeamua kuniangamiza kwa sababu mnazojua wenyewe!”

“Mh,” David Osmond akaguna na kuendelea. “Ukweli ni kwamba hatuwezi kufanya kitu kama hicho bosi, ukizingatia wote tunategemea biashara hiyo…”

“Hapana…lazima mjieleze halafu tuwekane sawa,” salum Zakwa akaendelea kusema huku mwili mzima ukimtetemeka! Hakuamini kile alichoelezwa na wale vijana wake!

“Sasa bosi…” David Osmond akasema.

“Sitaki maneno mengi!” Salum Zakwa akamkatisha na kuendelea. “Ondokeni hapa! Mkapumzike majumbani kwenu halafu tuonane baada ya siku mbili nitakapowaita tena mnipe jibu. Ukweli ni kwamba nimechanganyikiwa!”

Wote watatu wakanyanyuka. Waliitambua hali ile, hivyo hawakuona sababu yoyote ya kuendelea kukaa tena, kwani mwenye himaya alikuwa ameshawaamuru kuondoka haraka. Hivyo basi, wakaondoka kwa mwendo wa taratibu hadi walipolifikia gari la David. Wakapanda na kuondoka huku wakijua kuwa kutakuwa na vita kubwa sana kati yao na bosi wao, kitu ambacho walitakiwa wajihadhari nacho.

Kwa ujumla wote walikuwa wamenyamaza kimya ndani ya gari, kiasi kwamba hakuna aliyekuwa anaongea kutokana na mawazo yaliyokuwa yanawaandama. Hata hivyo, baada ya gari kulitoka eneo la himaya ya Salum Zakwa, David aliyekuwa anaendesha gari, akakata ukimya na kusema: “Jamani, hali ndiyo kama mlivyoiona kwa bosi!”

“Ni kweli hali ni mbaya, hata mimi nimeiona. Bosi amechukia sana, na cha muhimu ni sisi kujiahadhari naye kuanzia sasa!” Bosco Zambi akasema.

“Nyie mnafikiri tutajihadhari vipi” Unafikiri kuna mtu wa kuweza kumkwepa bosi? Ana mtandao mkubwa!” John Peka akasema.

“Sasa kama ana mtandao mkubwa, kwani sisi ndiyo tulioharibu?” David Osmond akaendelea kusema. “Hata hivyo ni kweli tujitahidi kujilinda, la sivyo tutegemee mabaya kwa upande wetu!”

“Basi, cha muhimu tuwe macho!”

“Hilo neno!”

Gari likachanja mbuga kuelekea katikati ya jiji.



********

Kituo cha Polisi Uwanja wa Ndege kiko katika eneo la uwanja wa zamani, Terminal 1. Ni umbali mfupi tu kutoka lilipo jengo kuu la uwanja, ambapo vijana wale walikamatiwa. Hivyo basi, watuhumiwa wale watatu, Roki Sekulu, Joel Besha na Bomeza Jadu, baada ya kukamatwa, walipelekwa pale kwa gari, wakiwa chini ya ulinzi.

Hakika walikuwa bado hawaamini kilichokuwa kinaendelea hasa ukizingatia ndiyo mara yao ya kwanza kukamatwa, inangawa walishasafirisha madawa yale mara nyingi kwa mtindo huo walioutumia. Walikumbuka kuwa walikuwa wamesafiri si chini ya saa zaidi ya nne, wakiwa na dawa zile walizozihifadhi matumboni mwao, na walikuwa hawajala chakula zaidi ya vitu vyepesi, kama soda, biscuti, ama juisi.

Pia, Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Dickson Kweka, alikuwa amefika kushuhudia wale vijana watatu waliokamatwa na makachero wake, Inspekta Raymond Gopi, Benito na Dani, wakiwa na dawa za kulevya wakitokea nchini Pakistani.

Baada ya kufika, akaingia ndani ya chumba maalum cha upelelezi, ambapo walikuwepo makachero wengine. Vijana wale wakaingizwa na kuwekwa tayari kwa kufanyiwa upekuzi wa awali ili kuwabaini kama walikuwa na zile dawa za kulevya matumboni mwao!

“Haya, atakuja mtu mmoja mmoja hapa…” Wakaambiwa wale vijana na Afisa mmoja wa polisi aliyekuwa amebeba vifaa fulani, kama beseni kubwa la plastiki, pamoja na chupa ya chai,iliyokuwa na chai ya moto ndani yake. Na ile ilikuwa ni muhimu sana kwa kusaidia watuhumiwa wale waweze kuzitoa dawa zile haraka!

Kijana Roki, aliyekuwa amekaa katika kiti kimojawapo, sambamba na wenzake, Joel na Bomeza, kwa muda wote alikuwa na wasiwasi, na hali ilikuwa ni mbaya sana, kwani muda wa kukaa na zile dawa tumboni mwake, ulikuwa umepita, hivyo kulikuwa na hatari ya kumpasukia tumboni na kusabaisha kifo. Hivyo alipoitwa, akanyanyuka na kumfuata Afisa yule wa polisi aliyemwita.

“Simama hapo…” akaendelea kuambiwa.

“Sawa,” akaitikia huku amesimama.

“Sasa nakuuliza, je, una dawa tumboni mwako?”

“Ndiyo, ninayo…” Roki akasema kwani hakuona sababu yoyote ya kubisha.

“Haya, vua nguo zako, suruali na nguo nyinginezo…”

Roki akavua nguo, akianzia suruali, bukta, chupi na kubaki alivyo!

“Haya, kunywa hii chai…” afisa wa polisi akamwambia.

Roki akapewa ile chai ya moto iliyokuwa ndani ya chupa, ambayo ilimiminwa kwenye kikombe cha udongo. Akaipokea ile chai na kuanza kuinywa mafunda kadhaa huku akiisikilizia ilivyokuwa inashuka tumboni mwake, na kwa mbali akawa anakunja sura yake. Alijua madhara mabayo yangetokea muda siyo mrefu, ambapo baada ya sekunde kadhaa, alichuchumaa katika lile beseni la plastiki na kuanza kuzitoa zile dawa kwa njia ya haja kubwa hadi alipomaliza zote. Zilikuwa zimefungwa kwa mtindo wa pipi, katika mafungu mbalimbali. Akabaki akipumua kwa nguvu kwa hali ile iliyomkuta, kukaa na dawa za kulevya tumboni siyo mchezo!

Jasho lilimtoka mwili mzima!

Halikadhalika zoezi lile liliendelea kwa vijana wale wawili, Bomeza na Joe, ambao nao wazitoa zile pipi zote za dawa, na kuonekana kilikuwa ni kiasi kikubwa cha dawa ambacho kina thamani ya shilingi milioni mia tatu mpaka nne hivi kwa hesabu za harakaharaka. Zilipomalizika zote, dawa zile zikahifadhiwa katika mifuko maalum ya nailoni. Na hatua nyingine iliyofuata ilikuwa ni kuwachukua watuhumiwa wale mpaka Makao Makuu ya Kitengo cha Kupambana na Wafanyabiashara wa Dawa za Kulevya kwa ajili ya mahojiano zaidi.

Hata baada ya kufikishwa kule na kuhojiwa kwa kina, walisema kwamba hawamfahamu hata mfanyabiashara mmoja wa dawa zile, zaidi ya wao kuwa wabebaji tu wanaotumwa nchi za nje kwa malipo makubwa. Ndiyo tuseme hata bosi wao, Salum Zakwa hawakumfahamu, kwa vile walikuwa wanawasiliana kwa njia ya simu tu na kupokea maelekezo, au hata kupokewa na wapambe wake, ambao nao hawakutakiwa kuzoeana nao!

Na ukweli ni kwamba, Salum Zakwa, alikuwa ni mtu anayejificha sana, ukizingatia alikuwa ni kigogo serikalini, hivyo mambo yake alikuwa anayafanya kwa usiri mkubwa sana. Mkuu wa kitengo, Dickson Kweka, alielekeza vijana wale wakae mahabusu, na kusubiri mpaka kesho yake, ili aweze kuwatambulisha kwa wananchi kwa kupitia vyombo vya Habari, ukiwa ndiyo utaratibu waliojiwekea katika vita ile kali inayoendelea nchi nzima! Ni kuwatokomeza wafanyabiashara wale!





********

David Osmond, John Peka na Bosco zambi, walipoondoka nyumbani kwa Salum Zakwa, Sea View, Upanga, mchana ule, yeye Zakwa alibaki amechanganyikiwa haswa. Ukweli ni kwamba hakujua mtu aliyekuwa amemchoma, hasa ukizingatia hakuweza kuwashirikisha watu wengi katika kuwauliza, kwani alikuwa amejijengea himaya ya pekeke, na kufanya aogopewe kama Mungu- Mtu. Hata famili ayke, mke na watoto walimwogopa na kutokaa karibu naye kabisa!

Basi, kwa muda ule, ndiyo aliuona umuhimu wa kumshirikisha mke wake katika mipango yake ya kibiashara, kwani kwa muda ule angeweza hata kumpa ushauri wa kumliwaza. Hasa, alichohofia zaidi, ni juu ya siri yake kuvuja, endapo vijana wale watahojiwa na polisi, juu ya mtu aliyewatuma mzigo ule, maana wakifinywa kidogo, wasingesita kumtaja! Lakini kwa hilo pia, akalipinga mawazoni mwake, kwani kwa namna moja ama nyingine aliwaamini vijana hao!

Wasingemtaja!

Hata hivyo, ili kujua kilichoendelea, Sa lum Zakwa alichukua simu yake, na kuamua kumpigia mtu muhimu sana, ambaye alikuwa kule uwanja wa ndege, ambaye kwa vyovyote alitegemewa kuwalinda vijana wale ili wasikamatwe. Mtu huyo hakuwa mwingine zaidi ya Ramson Kibenzi, aliyekuwa mfanyakazi katika kitengcha ukaguzi, ndani ya Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere. Yeye pia, ni mmoja wa mtandao wa wanaomsaidia sana Kamba, katika kupitisha vijana wake, wakiwa na dawa za kulevya walizomeza matumboni mwao.

Ingawa walikuwa wamewekeana masharti ya kutopigiana simu mara kwa mara kwa kuhofia kujulikana, lakini kutokana na kuchanganyikiwa, akaamua kumpigia ili aujue ukweli! Simu ilipopigwa iliita kwa muda bila kupokelewa, halafu ndipo sauti nzito iliposikia upande wa pili!

“Haloo…Zakwa…”

“Ndiyo Ramson…habari za huko…”

“Aisee, nafikiri vijana wako wamekueleza. Hali imekuwa mbaya sana, ni kitu ambacho hatukutegemea…vijana wamekamatwa!”

“Ndiyo, wamenieleza…lakini imekuwaje tena wakati nilishasafisha njia?”

“Ni kweli ulishasafisha njia…” Ramson akamwambia.

“Sasa kama nilishasafisha imekuwaje tena?”

“Tatizo limetokea baada ya mtu mmoja, bila shaka miongoni mwenu, aliyewatonya polisi juu ya wale vijana kurudi leo wakiwa na mzigo. Hivyo naomba mtambue hilo…hakuna jinsi…” Ramson akamwambia na kumzidishia hasira Salum Zakwa!

“Shenzi sana!” Salum Zakwa akatukana kwa hasira!

“Pole sana…”

“Haisaidii kitu!”

“Halafu naomba tukatishe mazungumzo wasije wakatushtukie…” Ramson akamwambia baada ya kuona akiongea kwa hasira!

“Haya bwana…” Salum Zakwa akasema kinyonge huku akiiangalia simu ambayo ilishakata mawasiliano!

Salum Zakwa akagonga ngumi juu ya meza huku akiendelea kuwaza. Ni kwamba ule ulikuwa ni mzigo mkubwa sana uliokuwa na thamani ya fedha zisizopungua shilingi milioni mia tatu za kitanzania. Ni mzigo ambao alikuwa ameufukuzia kwa muda mrefu sana, akiwapa kazi ya kuukusanya na pia kuufunga katika hali ya usalama ili uweze kubebeka kirahisi katika matumbo ya binadamu, kutokea nchini Pakistani hadi hapa nchini Tanzania.

Hivyo basi, Salum Zakwa aliamua kutangaza vita dhidi ya mtu yeyote aliyemsaliti, akianzia kwa vijana, David Osmond, Bosco Zambi na John Peka, akifahamu kuwa wao ndiyo waliomchoma baada ya yeye kuwahi kuwadhulumu kiasi fulani cha fedha. Hata hivyo haikuwa kweli, yalikuwa ni mawazo yake tu, aliyewachoma alikuwa ni kijana, Bruno Maliyatabu, au ‘Boga Pevu,’ ambaye aliwahi kuwa mlinzi na mshiriki katika biashara ile, lakini akaamua kuacha na kuwa msiri wa Jeshi la Polisi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Huyo Boga, ni mtu ambaye hakuwa mawazoni mwake kabisa, kwa sababu hakuwahi kufanya naye kazi na hata kumfahamu, ukizingatia yeye alikuwa hajihusishi na watu wadogo, walala hoi wasiokuwa na msaada kwake! Aliyemfahamu ni kijana, mwarabu, Hasun Awadh, waliyekuwa wanakutana mara kwa mara, kwa vile wako katika mtandao mmoja, na ambaye ndiye aliyekuwa bosi wa Boga, na kwa wakati ule alikuwa ameshakamatwa na dawa za kulevya.

Kwa hivyo Salum Zakwa akabaki akiwahisi watu wake ndiyo waliomchoma kwa polisi, bila kumhisi mtu mwingine yeyote aliyekuwa nje yake! Hivyo ni lazima awashughulikie ipasavyo! Kamwe hatakuwa na huruma kwa mtu aliyetaka kumuangamiza kwa kumtilia kitumbua chake mchanga! Alishaapa kuwa akuanzae mmalize!

Je, afanyeje? Akajiuliza! Akapanga awatafute watu maalum, wataalam wa kuua!



********







ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog