Search This Blog

Saturday 5 November 2022

SURA MBILI - 4

 






Simulizi : Sura Mbili

Sehemu Ya Nne (4)





Ni Vasco Nunda na Liston Kihongwe! Hawa ni watu aliokuwa amewaajiri kama walinzi wake wa siri, ambao waliweza kumlinda pasipo mtu yeyote kujua, na hata kutelekeleza mauaji ya siri pia pale atakapoamua. Pia, ni watu aliokuwa amewaajiri kwa kuwalipa vizuri sana kutokana umakini wao wa kazi ulivyokuwa, kwani walikuwa wakitekeleza kazi yao kwa mtindo wa Mafia, bila kuacha ushahidi kitu ambacho kiliwafanya wadumu naye kwa muda mrefu sasa. Tuseme walikuwa wako tayari kufanya kazi yoyote hata kuua, ili mradi walipwe kitu kinachoitwa fedha!

Hivyo basi, Salum Zakwa aliwapigia simu Vasco na Liston. Akawaambia wafike pale nyumbani kwake, Sea View, Upanga, haraka sana, kwani kulikuwa na maagizo muhimu. Wakiwa ni watu wa kazi, wakamjulisha kuwa walikuwa njiani kuelekea pale nyumbani, na yeye Kamba akabaki akiwasubiri palepale katika bustani nzuri iliyokuwa inafikiwa na upepo mwanana uliokuwa unatokea katika Bahari ya Hindi, na kumpatia burudani ya pekee. Pamoja na hayo, mawazo mengi yalikuwa yamemjaa akiwazia ule mkasa uliompata!

Kupoteza mzigo wa fedha nyingi!

Wakati Salum Zakwa akiendelea kuwaza na kuwazua, aliweza kuliona lile gari aina ya Toyota Land Criuser GX likipunguza mwendo kwenye barabara ile ya Sea View, kisha likakata kona kuelekea usawa wa lango kuu la nyumba yake. Aliweza kuliona gari hilo kwa kupitia kwenye uzio wa waya na michongoma uliokuwa umezunguka nyumba ile iliyokuwa imepakana na ufukwe wa Bahari ya Hindi kwa upande wa nyuma. Hatimaye gari hilo likafika langoni, ambapo mlinzi alifungua lango na gari likaingizwa hadi ndani na likapaki sehemu ya maegesho yanakopaki magari mengine.

Baada ya gari lile kupaki, vijana, Vasco na Liston wakashuka na kuelekea kule alikokaa Salum Zakwa, wakitembea kwa mwendo wa madaha. Vasco alikuwa amevalia suti nyeusi iliyomkaa vizuri, viatu vyeusi vya ngozi, pamoja na miwani mieusi ya jua huku ndevu zake amezinyoa kwa mtindo wa ‘O’. Kwa upande wa Liston alikuwa amevalia jaketi la ngozi na suruali ya jeans, huku chini akivalia viatu aina ya buti. Hakika walipendeza kiasi ambacho mtu yeyote asingewagundua kuwa walikuwa ni watu hatari sana.

“Karibuni vijana…” Salum Zakwa akawaambia huku akiwaangalia kwa zamu kana kwamba alikuwa anawakagua.

“Tumekaribia, bosi…” Vasco Nunda akasema huku akinyoosha mkono na kumpa Salum Zakwa.

“Ahsante sana…” Liston naye akasema huku akimpa mkono.

Walipomaliza kusalimiana, Vasco na Liston wakavuta viti na kukaa.

“Habari za tokea jana,” Salum Zakwa akasema.

“Habari ni nzuri…sijui wewe bosi,” Vasco akasema huku akimwangalia kwa macho yake makali.

“Habari siyo nzuri!” Salum Zakwa akasema.

“Imekuwaje tena” Ni kipi kilichojiri?”

Salum Zakwa akavuta pumzi ndefu na kuzishusha. Kisha akasema kwa sauti ndogo na ya mkwaruzo kama Chura, “Lazima niwaambie ukweli. Nimewaita nyote wawili kwa kazi!”

“Tunakusikiliza bosi.”

“Kuna kazi ya kuwalipua watu fulani, na kuhakikisha wanafutika katika uso wa dunia!” Salum Zakwa akawaambia kwa msisitizo huku amekunja ngumi! Halafu akaendelea kusema. “Kuna watu watatu nataka wafe mara moja, hivyo ni vyema niwape picha kamili.”

“Hebu tupe picha kamili…” Vasco Nunda akamwambia.

“Sina haja ya kurudia maneno. Ninajua wote wawili mnafahamu, na hivi karibuni wale vijana wenzetu watatu, Roki, Joel na Bomeza, walikuwa nchini Pakistani kwa kazi ya kuuchukua mzigo wangu wa mamilioni ya shilingi, baada ya mimi kutokea huko na kuandaa kila kitu, ikiwemo hata kusafisha njia katika kila idara. Nilimwaga fedha chafu kwa wahusika wote wanaohusika na ulinzi pale uwanja wa ndege, mpaka hata wafagiaji kama mnavyojua kawaida yangu!” Akanyamaza kidogo huku akiwaangalia kama maneno yale yalikuwa yanawainia.

“Sasa…” Salum Zakwa akaendelea. “Baada ya kuhakikisha mambo ni shwari, ndipo nikawapa kazi wenzenu, David, Bosco na John. Ilikuwa ni kazi ya kuwapokea na kuhakikisha mzigo huo unafika salama hapa nyumbani. Lakini cha ajabu baada ya vijana wale kufika kwa ndege leo asubuhi, wamekamatwa na polisi, na mzigo wote umepotea!”

“Unasema wamekamatwa?” Vasco Nunda akauliza.

“Ndiyo manaake! Na mzigo umepotea!” Salum Zakwa akasisitiza!

“Sasa una maana kuna mtu unayehisi amekuchoma?”

“Ndiyo, nina wasiwasi!”

“Una wasiwasi na nani?”

“Nina wasiwasi na wale vijana wangu, David, Bosco na John…”

“Kwa nini uwe na wasiwasi nao, wakati umefanya nao kazi hii muda mrefu?”

“Ninahisi hivyo, kwa vile kipindi cha nyuma niliwazika fedha nyingi. Na ndiyo maana tokea mwanzoni nilikuwa najaribu kuwaonya sana wasijaribu kunigeuka. Lakini ndiyo hilo wamefanya sasa…oh!” Salum Zakwa alisema huku akisikitika!

“Aisee, kwa hivyo unatakaje bosi?”

“Ndiyo maana nikawaita. Nataka niwape kazi, jamaa wote wafe! Najua wameshaniharibia kila kitu, ikiwa ni pamoja na kujulikana siri yangu kuwa ninafanya biashara hii haramu!”

“Kumbe unataka wauawe…” Vasco Nunda akasema kwa sauti ndogo kama vile kuua mtu lilikuwa ni jambo dogo sana!

“Nataka wauawe haraka sana kabla hawajakamatwa na kuzidi kuanikasiri zangu!”

“Sawa, bosi, tupange biashara. Nafikiri unajua kuwa hii ni nje ya mapatano yetu ya kazi ya kukulinda…”

“Hilo naelewa sana!”

“Nakuhakikishia tutaifanya kazi hiyo vizuri sana na wewe utaridhika!”

“Ok, tusipoteze muda, mnataka kiasi gani cha fedha kwa kazi hiyo?”

“Bila kuzungusha bosi, tunakupangia kuwa kila kichwa cha mtu tutahitaji shilingi milioni tatu. Hivyo vichwa vyote vitatu ni shilingi tisa, tunakuachia moja…” Vasco Nunda akamwambia huku amemkazia macho! Tena hakuwa na wasiwasi utafikiri ilikuwa fedha ndogo sana!

“Milioni tisa?” Salum Zakwa akauliza!

“Ndiyo bosi, au nyingi sana? Tambua tunamwaga damu za watu!” Vasco Nunda akasema kwa msisitizo.

“Hapana, siwazii hiyo fedha!” Salum Zakwa akasema na kuongeza. “Hiyo ni fedha ndogo sana ambayo hutumia kuhonga na kunywea pombe kwa siku moja!”

“Vizuri bosi, basi changamkia sisi tuingie kazini mara moja!”

“Sina tatizo, ili mradi kazi yangu ifanyike. Ngoja nikawachukulie…” Salum Zakwa akasema huku akinyanyuka na kuelekea ndani ya nyumba yake kwa kupitia mlango wa nyuma, ambao huwa hautumiki sana na familia yake. Akawaacha Vasco Nunda na Liston Kihongwe wamekaa pale bustanini wakimsubiri kwa hamu, na pengine wakiifurahia tenda ile iliyokuwa na malipo mazuri sana!



********

Baada ya kuingia ndani, Salum Zakwa hakukawia sana, kwani baada ya dakika zipatazo tano, alirudi akiwa ameshika mkoba wa ngozi mkononi. Akaufikishia juu ya meza na kuufungua taratibu, ambapo ndani yake paliweza kuonekana mabunda ya noti nyekundu za shilingi elfu kumi zilizopangana. Na fedha zote zilikuwa mpya kabisa na hata harufu yake iliweza kusikika katika tundu za pua! Harufu ya fedha haramu!

“Nimelete fedha hizi,” Salum Zakwa akawaambia.

“Tunaziona bosi.” Vasco akasema.

“Lakini sitowapa zote,” akasema na kuongeza. “Nitawapa shilingi milioni sita kwanza, na baada ya kumaliza kazi nawamalizia milioni tatu, na hata ikiwezekana nawapa nne kabisa, iwe kumi. Hiyo inategemea na ufanisi wa kazi, ambapo najua hamtaniangusha!”

“Hakuna tatizo bosi, mpaka sasa hesabu kuwa kazi imefanyika!”

“Haya, ngoja tuhesabiane…” Salum Zakwa akawaambia halafu akaanza kuzihesabu zile fedha hadi ilipofikia idadi waliyoitaka wao kwa kuanzia.

Salum Zakwa alipomaliza kuzihesabu, akawaambia, “Haya, Vasco, wewe ndiye kiongozi. Hivyo ninakukabidhi fedha hizi na kazi yangu ifanyike ipasavyo!”

“Usitie shaka bosi, kazi itafanyika. Lakini cha muhimu kwa sasa, hebu tupe ramani ya sehemu wanapoishi watu hao ndani ya jiji la Dar es Salaam.”

“Ni kweli, ni jambo la maana sana. Kijana wa kwanza, John Peka, anaishi Magomeni Mapipa, mtaa wa Kisangilo, nyumba namba…ambayo ameijenga mwenyewe, baada ya kununua nyumba ya kizamani iliyokuwa katika mtaa huo, halafu akaivunja na kujenga hiyo ya kisasa, hamuwezi kuipotea,” Salum Zakwa akasema.

“Ah, nyumba hiyo hata mimi naifahamu sana,” Liston Kihongwe ambaye alikuwa amenyamaza kimya muda mrefu akasema.

“Hata mimi naifahamu sana, kwani jirani na nyumba ile, palikuwa na demu wangu siku za nyuma. Kwa hilo ondoa shaka bosi…” Vasco Nunda naye akasema.

“Kama mmepafahamu, ni vizuri. Mtu wa pili ni kijana, David Osmond, ambaye anaishi Kinondoni, mtaa wa Sekenke, nyumba namba…ambayo nayo ni ya kwake mwenyewe. Nyumba hiyo imezungushiwa uzio na geti imara, hivyo mtajua namna ya kumpata…nafikiri mnanipata!”

“Tunakupata bosi!” Wakasema wote.

“Mtu wa mwisho ni kijana Bosco Zambi. Huyu anaishi katika maghofa ya Shirika la Nyumba la Taifa, eneo la Faya, Barabara ya Morogoro. Siyo mbali sana na kituo cha Mafuta, na anakaa katika ghorofa ya tatu, upande wa kulia, ambapo linatazamana na Barabara ya Morogoro kama unaelekea Ubungo. Ni matumaini yangu kuwa na hapo hamuwezi kupotea, kwani nyie ni watoto wa mjini…”

“Hilo pigia mstari, bosi, tumeshapafahamu. Sisi ni watu wa kazi, na hata ukitupa kazi ya kumfuata mtu ahera, tutakwenda tu, ili mradi tulipwe chetu!” Liston Nunda akasema kwa kuweka utani kwa kudhihirisha kuwa ni watu wa kazi!

“Hauna taabu, naona tumeshamalizana. Nategemea kazi itaanza muda wowote…mimi siwafundishi!” Salum Zakwa akamaliza kusema.

“Tegemea kazi nzuri, mimi nina Liston, ambaye ni mtu wa kazi,” Vasco Nunda akasema huku wakinyanyuka tayari kwa kumuaga Salum Zakwa.

Hawakupoteza muda, baada ya kukabidhiana zile fedha, Vasco Nunda na Liston Kihongwe wakaaga na kuondoka kwa mwendo wa taratibu na kuliendea gari lao. Wakapanda na kuondoka nalo, Vasco akiwa ndiye dereva, ambaye aliliondoa kwa mwendo wa taratibu na kulitoka eneo lile la Upanga Sea View. Salum Kamba, akabaki amekaa pale kwenye bustani akiliangalia jinsi lile gari lilivyokuwa linaishia langoni na mlinzi akiulifunga kama lilivyokuwa mwanzo. Kwa kiasi fulani alikuwa na matumaini kuwa Vasco atafanikiwa kuwaangamiza akina, David Osmond, John Peka na Bosco Zambi!

Ama kweli ni hatari!



********

Habari za kukamatwa kwa vijana watatu, Joe Besha, Bomeza Jadu na Roki Sekulu, zilitangazwa kesho yake baada ya waandishi wa habari kufahamishwa. Salum Zakwa naye alizipata habari zile mchana wa siku ile, ukizingatia yeye alikuwa ni kigogo serikalini. Ingawa alikuwa ni mhusika mkuu, lakini alishukuru sana kwa vile hakutajwa kama anahusika. Kwa kawaida, ‘Mzungu wa unga’ hatakiwai kujulikan kabisa na mbebaji anayemtuma ule mzigo kutoka nje ya nchi.

Ingawa Salum Zakwa alikuwa amenusurika kutajwa, wasiwasi mkubwa ulikuwa bado umemjaa kutokana na kubaki na wale vijana wake wengine, John Peka, David Osmond na Bosco Zambi waliokuwa bado hai. Kwa vyovyote alijua kukamatwa kwao kungesabaisha wamtaje kwa polisi kuwa na yeye ni mmoja wao, na kumfanya aunganishwe na watuhumiwa wengine wa biashara ile ambao wameshakamatwa katika ile operesheni kubwa inayoendeshwa nchini.

Hivyo basi, mkutano ule wa waandishi wa Habari uliohitishwa na Dickson Kweka, Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Wafanyabiashara wa Dawa za Kulevya nchini, yeye Salum Zakwa aliufuatilia kwa kina, ambapo mkuu yule alielezea jinsi walivyokamatwa pale uwanjani, na kwenda kutolewa dawa zile zilizokuwa na thamani kubwa sana, ambayo hakuitaja wazi kutokana na kile walichosema kuwa inavutia watu wengi kuifanya biashara hiyo kutokana na kuwa ina kipato kikubwa sana.

Pia, vingi ya vyombo vya habari, vikiwemo magazeti na televisheni, viliendelea kulipongeza Jeshi la Polisi nchini kwa kuianzisha operesheni ile, lakini wasiishie kukamata wafanyabiashara wadogo, watumiaji na wabebaji, huku wakiwaacha wafanyabiashara wakubwa, ambao ndiyo wahusika wakuu. Na hilo aliona ni kweli, kwani lilikuwa linamhusu yeye mwenyewe, ambaye ni mtu mzito serikalini, lakini anajihusisha na biashara ile haramu.

Hata hivyo siku hiyo ilipita na yeye akabaki akisubiri taarifa nyingine juu ya ile kazi aliyowapa, Vasco Nunda na Liston Kihongwe, kuhakikisha wanawamaliza, David, John na Bosco!



********http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Mtaa wa Kisangilo, Magomeni Mapipa, ulikuwa umepooza usiku ule, kutokana na mvua za masika zilizokuwa zinaendelea kunyesha, na kufanya pilikapilika za watu kupungua. Hakuna mtu ambaye angekubali kujitosa ndani ya mvua ile kama hakuwa na sababu ya maana, na hata wale waliokuwa wanaelekea katika sehemu za starehe, waliamua kuchukuwa usafiri wa teksi.

Kwa kawaida, mtaa ule, ambao ulikuwa na maduka mengi pamoja na grosari za vinywaji, huwa unapitisha watu wengi sana, ukiachilia mbali magari yanayokatiza kutokea mwanzo wa mtaa au hata katika kila kona inayokatiza katika mtaa huo maarufu tokea zamani.

Katika mtaa ule, nyumba ya kijana, John Peka, mfanyakazi wa Salum Zakwa, ilikuwa ni ya tano kutoka mwisho wa mtaa, na muda huo taa ya nje ilikuwa inawaka na kuangaza sehemu kubwa katika barabara inayokatiza mbele yake. Usiku huo wa saa tatu kasorobo, John alikuwa amejipumzisha sebuleni katika sofa, akiangalia runinga iliyokuwa ikiendelea ni vipindi vyake. Kando yake walikuwepo, mke wake, Mary Mshanga na wanawe wawili, Toni na Monica, waliojumuika wote wakiangalia runinga.

Pia, familia nzima, walikuwa wakiburudika na vinywaji baridi, juisi, ikiwa ni baada ya kumaliza kula chakula cha usiku. Huko nje, mvua ilikuwa bado inanyesha na kutoa kelele zilizokuwa zinagonga juu ya bati na maji yakitiririka na kelekea katika mifereji iliyotengeneza vijito visivyo rasmi. Kwa muda wote, John alikuwa akimwangalia mke wake, Mary Mshanga, ambaye alikuwa bado mrembo, na wala hakuonyesha dalili za kuchakaa, tangu alipomuoa mika sita iliyopita.

Kwa muda wote alioishi na mke wake, alikuwa akijishughulisha na biashara ile haramu ya dawa za kulevya chini ya bosi wake, Salum Zakwa. Ni biashara ambazo zilikuwa zinamuweka hatarini kila mara, na kipindi chote hicho, mke wake alikuwa akimpa moyo bila kujua ni biashara gani aliyokuwa anafanya zaidi ya kuona maisha yao yakiwa mazuri na kuzisahau shida ndogondogo!

“Baba Monica…” Mary, mkewe alimwita.

“Naam, mama Monica…” John Peka aliitikia huku akimwangalia mkewe.

“Vipi, mbona leo uko hivi?” Mary alimuuliza baada ya kumuaona akiwa amezama katika lindi zito la mawazo kuliko kawaida yake.

“Kwani nikoje?” John Peka akamuuliza!

“Hauko katika hali ya kawaida tuliyokuzoea. Je, unaumwa?”

“Hapana, siumwi. Usiwe na wasiwasi…”

“Lazima niwe na wasiwasi…maana umepooza sana. Nimekuzoea, lakini furaha yako imepungua, wewe siyo mtu wa kunyamaza muda wote. Wala huonei na mimi, na hata watoto…hapana kuna jambo!”

“Oohps!” John Peka akaguna huku akivuta pumzi ndefu. Ukweli ni kwamba alikuwa anamatatiza, tena makubwa sana!

Maneno aliyoambiwa na mke wake yalimwingia barabara, hivyo alihitaji kuonyesha furaha kwa mke wake mpenzi. Lakini kuna kitu kimoja aliona kuna haja ya kumwambia mke wake, juu ya tatizo lile linalomkabili, ingawa pengine mke wake asingeweza kuzuia kinachotarajiwa kutokea, lakini kujua lilikuwa jambo muhimu! Hivyo basi, John Peka akavuta pumzi ndefu na kuendelea kumuangalia mke wake, kisha akamwambia kwa sauti ndogo:

“Mama Monica mke wangu…”

“Bee…” Mary akaitikia huku pia akimwangalia.

“Ni kweli kuwa hali yangu kwa leo siyo nzuri…”

“Kwa nini siyo nzuri?”

“Kuna jambo moja limenisibu, lakini sina jinsi zaidi ya kukuelezea. Siyo kubwa sana, lakini sipendi niliache bila kukuambia…” John Peka alisema halafu akanyamaza kidogo huku akimwangalia mke wake alivyokuwa akimwangalia kwa makini. “…Najua kuwa una akili timamu,” akaendelea kusema John na kuongeza.

“Na unafahamu kwamba kwenye maisha ya binadamu na biashara kama yangu ya dawa za kulevya, matatizo ni ya kawaida kabisa na mambo mabaya nayo yanatarajiwa…”

“Mbona sikuelewi baba Monica?” Mary akamuuliza.



********



“Utanielewa mke wangu…”

“Nieleze nikuelewe…oh!”

“Katika biashara zangu kwa siku mbili tatu hizi si nzuri, na ningekaa kimya bila kukueleza chochote, lakini kwa jinsi mwelekeo ulivyo na hatua ambayo inaendelea leo, ukiwa kama mke wangu haifai kukuficha zaidi. Ni lazima ufahamu, na utambue kuwa mpaka muda huu, sielewani na bosi wangu, Salum Zakwa!”

“Ni kwa nini hamuelewani?”

“Wewe acha tu…” John Peka akasema. Swali la mke wake alilisikia, hivyo akijitahidi kuonyesha furaha kwa mke wake kipenzi. “Ni kwamba kuna wafanyakazi wenzetu watatu, ambao walikuwa wamerudi na mzigo kutoka nchini Pakistani, lakini wamekamatwa uwanja wa ndege jana. Hakuna mtu anayejua juu ya aliyevujisha taarifa hiyo ya kuja kwao kwa polisi, ambao waliwakamata punde tu waliposhuka katika ndege…unanipata mke wangu?”

“Nakupata…aisee?”

“Na kitu kibaya kilichotokea, ni kwamba mimi na wenzangu wawili, Bosco Zambi na David Osmond, tulipewa dhamana ya kuhakikisha ulinzi na mzigo huo unafika salama. Sasa umekamatwa, na bosi anatuambia tujieleze kwa nini umekamatwa, na ni nani aliyetoa siri hiyo?”

“Unafikiri ni kwa nini wawashutumu nyie watu watatu? Na wakati huo polisi wanawakamata nyie mlikuwa wapi?”

“Siyo kwamba tulikuwa wapi. Sababu kuu ni ile niliyokwambia kwamba anadai huwenda tulijua mpango mzima wa kukamatwa kwa mzigo. Na hata mazingira ya jamaa waliokamatwa yalikuwa ni dhahiri kwamba kuna mtu katoa siri. Halafu mbaya zaidi kazi ya kulinda usalama wa wale vijana tulipewa sisi watatu!”

“Lakini kwa upande wako umeliona tatizo hilo ni kubwa kiasi cha kukutia wasiwasi?” Mary akaendelea kumuuliza John.

“Siwezi kusema ni kubwa. Lakini ni kubwa kwa jinsi mazingira yalivyotokea, bosi hatuelewi, na amechanganyikiwa kama nilivyochanganyikiwa mimi!”

“Ina maana umeshindikana mpango wa kuweza kuukomboa huo mzigo ulipokamatwa na polisi?”

“Ni kitu ambacho hakiwezekani kamwe. Ndiyo maana bosi amechachamaa kwa vile suala limekuwa gumu kuliko yote yaliyopita kutokea. Hata wale askari tuliowategemea kufuatilia matatizo kama haya, wameonekene kushindwa kazi. Hakika ni kesi nzito sana. Ambapo mkuu wa upelelezi ameagiza ni lazima watu hao washughulikiwe kikamilifu!”

“Basi ni kazi kweli…” akasema Mary.

“Ni kazi kweli! Na pamoja na kutafutwa na polisi, lakini sidhani kama bosi, Kamba atatuacha hai, kwa jinsi ninavyomjua mimi! Kwani hapendi siri zake ziwe zinatoka nje, wala ajuliakane! Ukweli ndiyo huo!”

“Oh, umefika mbali sana. Hawezi kukufanya lolote…” Mary akasema kwa kumpa moyo mumewe, kwa sababu alifahamu yeye ndiye mwenye jukumu kubwa la kufanya hivyo kwa mumewe na si mtu mwingine. Ni yeye tu, ambaye maneno yake matamu, viganja laini na mabusu ya hapa na pale yangeweza kumfariji mumewe, na akili ikatulia kiasi cha kufikiri namna ya kupata muafaka wa suala zima.

Pamoja na kupewa moyo na Mary, moyo wa John ulikuwa mzito sana. Hali ya hatari aliiona ikimkabili, tuseme alisikia harufu ya kifo! Kimya kifupi kikatawala huku kila mmoja akiwaza lake kichwani, na hata baada ya muda, watoto, Toni na Monica, walikuwa wameshaanza kusinzia, hivyo mama yao, Mary, akawaambia wasubiri pale kando ya baba yao, halafu yeye aende akawatandikie vitanda.

Akanyanyuka na kuelekea katika chumba cha watoto na kumwacha mume wake, John Peka akiendelea kuangalia runinga, pamoja na watoto, ambapo hata hakujua kilichokuwa kinaendelea katika vipindi vyake. Muda wote alimwazia bosi wake, Salum Zakwa, mtu katili, mwenye itikadi za Kimafia!

Atachukua hatua gani!



********

Mvua bado ilikuwa inanyesha kule nje, ingawa ilikuwa imepungua kiasi. Gari aina ya Toyota Land Cruiser GX ilisimamishwa kando, karibu na duka la Mpemba, katika mtaa wa Kisangilo, eneo hilo la Magomeni Mapipa. Baada ya gari lile kusimama, milango miwili ya mbele, kulia na kushoto ikafunguliwa, halafu wakashuka watu wawili waliokuwa wamevalia makoti marefu na miwani mieusi, ambapo hakuna aliyeongea chochote.

Baada ya kushuka, wakasimama kwa muda huku wakiongea kwa sauti ndogo kana kwamba hawakutaka kusikika na mtu, na muda wote walikuwa wanaiangalia nyumba ya John Peka iliyoonekana kwa uwazi. Walipomaliza kuongea mawili matatu, wakaanza kuijongelea nyumba hiyo, kwa mwendo ambao hata watu hawakuhisi kama watu wale walikuwa na nia mbaya.

Watu wale hawakuwa watu wengine, ni Vasco Nunda na Liston Kihongwe, ambao walikuwa wamefika pale kwa kazi maalum waliyokuwa wametumwa na Salum Zakwa, ambayo waliamua operesheni ile waiendeshe kwa usiku ule kwa jinsi walivyokuwa wamejipanga. Kwa uzoefu waliokuwa nao, walijua kuwa ili kazi ile ifanikiwe kirahisi, ni vyema kuifanya usiku, ambapo watu wengi wanakuwa wamelala, na vua ile iliyokuwa inayesha pia, ingeweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa sana!

Nyumba ya John Peka ilikuwa imejengwa kama mita ishirini kutoka katika barabara ya mtaa, na ilikuwa imezungushiwa vizuizi vya vyuma vya nondo pande zote hata milangoni na madirisha. Na ile ilikuwa ni katika hali ya kujilinda na wezi, au watu wenye nia mbaya dhidi yake. Hivyo basi, hali ile walikuwa wameshaigundua, Vasco Nunda na Liston Kihongwe, kuwa kuingia mle ndani ni vigumu sana kwa usiku ule, lakini wakajipanga kumuingilia kwa vile mchana mzima walipojaribu kumtafuta, walishindwa kumpata na muda waliopewa kutekeleza kazi ile ulikuwa unakwisha!

Upande wa mbele wa nyumba ile hapakufaa kuingilia, hivyo wakalifuata geti dogo lililokuwa kando kidogo. Ni geti ambalo lilikuwa linatokeza sehemu ya nyuma ya nyumba, ambapo pia kuna sehemu ya kupaki gari, na vilevile ndiyo sebule ilipo.Vasco na Liston, walipanga wamwingilie John kwa kupitia upande ule nyuma ya nyumba. Basi, wakajisogeza hadi katika lile geti, na Vasco akalifungua taratibu kwa kutumia ufunguo malaya alizokuwa nazo nyingi tu, kisha wakaingia taratibu bila kushtukiwa na mtu yeyote. Baada ya kuingia, wakalirudishia tena geti, na safari ya kuuendea mlango wa kuingilia ndani ikaanza.

Vasco na Liston hawakupata shida, waliuona na kwenda kusimama jirani na mlango huo. Pale waliweza kuwaona watu waliokuwa ndani kwa kupitia katika dirisha, ambalo pazia lake lilikuwa halijafungwa vizuri, wakasubiri kwa muda huku wakiwa kimya kabisa, hadi walipoona mke wa John Peka, Mary Mshanga, alipoelekea chumbani na kumwacha John akiwa na watoto. Ndipo Vasco alipoufungua ule mlango kwa ufunguo malaya, halafu wakaufungua, na wote kuingia ndani kama vile walikuwa wenyeji, bila hata kubisha hodi! Hakika hawakutofautiana na mizimu kwa usiku ule!

“Mama yangu!” John Peka akasema huku amekumbwa na hofu kuu! Kidogo roho imtoke! Hakujua watu wale walikuwa wameingiaje mle ndani, kwani mawazo yake yalikuwa mbali sana! Na alipogeuka nyuma kumwangalia mke wake, Mary, hakumwona. Ni muda ule alipokuwa ameelekea chumbani! Kuwatandikia watoto tayari kwa kulala.

“Mamaa…eh!” Mtoto Toni akapiga kelele akimkumbatia baba yake!

“Mama..oh!” Monica naye akapiga kelele huku naye akimkimbilia baba yake!

Bila kusema kitu wala kukaribishwa, Vasco Nunda na Liston Kihongwe wakaingia kijivumi, huku mmoja wao akiurudishia mlango taratibu kama ulivyokuwa mwanzo. Wote wawili walikuwa wamekamata bastola mikononi mwao, wakajikaribisha kwenye masofa mawili madogo yaliyokuwa pale sebuleni huku wakiwa wamelowa kutokana na mvua zilizokuwa zinanyesha kule nje.

“Oh! Nyie akina nani?” John Peka akawauliza huku wasiwasi mwingi umemshika!

“Ahahahahaaaaa…hakuna haja ya kutujua!” Liston Kihongwe akasema kwa sauti nzito ambayo haikusikika mbali na hata mke wake, Mary aliyekuwa ndani chumbani hakuweza kujua kama kuna watu waliokuwa wameingia mle ndani!

“Hakuna haja ya kutujua braza!” Vasco Nunda naye akasema huku akiirusha rusha bastola yake mkononi. Akaunda tabasamu la uongo angali macho yake hayaonekani kutokana na ile miwani mieusi aliyokuwa amevaa!

“Mbona siwaelewi?” John Peka akaendelea kuuliza huku nusu akitaka kunyanyuka. Watoto nao wakawa wamemng’ang’ania!

“Usinyanyuke tafadhali! Kaa chini!” Vasco Nunda akamwambia!

John akarudi na kukaa kitako kwenye sofa huku akiendelea kutetemeka! Vasco na Liston wakamfikia karibu kama hatua tano tu hivi.

“Unasikia braza…” Vasco Nunda akaendelea kumwambia. “Tumetumwa kuja kwako, upo?”

“Mmetumwa na nani?”

“Vizuri sana. Tumetumwa na bosi, ambaye hata wewe unamfahamu…ni Salum Zakwa Mnube!” Vasco Nunda akaendelea kumwambia!

“Sasa amewatuma nini kwangu?”

“Sikiliza braza…tulichofuata ni kitu kimoja tu. Tunataka utueleze ukweli kuhusu kuvuja kwa siri ya mzigo ule uliokamatwa uwanja wa ndege juzi. Je, ni nani kati yenu watatu aliyeivujisha kwa polisi?”

“Oohpsi” John Peka akapumua kwa nguvu huku akigwaya, kwani Vasco na Liston walionekana dhahiri kwamba wamekuja kikazi, kwa kazi moja tu ya kutekeleza kile walichotumwa. Na kibaya zaidi ni kwamba alimjua bosi wao, Salum Zakwa alivyo!

Ukweli ni kwamba, yanapotokea makosa makubwa kama yale yaliyotokea, ni lazima madhara makubwa pia yatokee, yakiwemo mauaji! Sasa ndiyo pale alikuwa amechungulia mdomo wa bastola pasipo kujiandaa. Ni hatari sana!

“Aisee, bosi amewatuma sivyo…” John Peka akaendelea kuwauliza kana kwamba alikuwa hajawaelewa!

“Usitupotezee muda! Tumeambiwa ujieleze ipasavyo jinsi mlivyotoa siri, vinginevyo tunakuua!” Vasco Nunda akamwambia kwa hasira!

“Mh!” John Peka akaguna huku akitikisa kichwa chake. Hakujibu kitu, akabaki akiyazungusha macho yake ndani ya sebule ile, na pia akiwaangalia Vasco na Liston, waliokuwa wakimwangalia kwa makini mno kama wanamchunga asifanye jambo lolote. Mke wake, Mary, alikuwa chumbani, na watoto walikuwa wamejikunyata kwake, wakishangaa ujio wa watu wale waliokuwa wamevalia makoti marefu meusi, miwani mieusi na wamelowa maji kutokana na mvua ile iliyokuwa inanyesha kule nje!

“Sina cha kusema kwa vile bosi anaujua ukweli. Sisi hatukutoa siri yoyote, tunajua bosi anafanya hivyo kutukomoa, na kutaka kutuharibuia maisha sis au familia zetu! Huo ndiyo ukweli wenyewe!” John Peka aliendelea kuwaambia.



*******

“Unatupotezea muda bro!” Liston Kihongwe akasema huku akinyanyuka. Halafu akamwendea John na kumnyanyua kwa nguvu kutoka pale kwenye sofa. Baada ya kumnyanyua, akamkamata mikono yake na kuizungusha kwa nyuma na kuikusanya! Watoto, Toni na Monica wakasukumwa kando na kuonyeshwa ishara ya kufunga mdomo na vasco!

Wakanyamaza!

“Vipi jamani?” John Peka akabaki aliwauliza huku akiyatoa macho yake pima! Hakuweza kupata msaada wowote, watoto walikuwa nao wameshangaa! Mkewe naye alikuwa chumbani, hakujua kilichokuwa kinaendelea!

“Ngoja nikupe dawa!” Vasco Nunda akasema huku akikunja mikono ya koti lake. Halafu akampiga John ngumi mibili tumboni!

“Oh, Mungu wangu! Mtaniuaa!” John Peka akasema huku akisikia maumivu makali!

“Na kweli tunakuua!” Vasco Nunda akamwambia huku akiendelea kutoa kipigo cha kumlegeza John!

Watoto Toni na Monica waliokuwa wakishuhudia baba yao akipata kipigo kikali, hawakuvumilia, wakaanza kupiga kelele huku wakirukaruka! Pale ndipo Vasco na Liston walipoangaliana na kuona kuwa walikuwa wanapoteza muda bila kutekeleza walichokuwa wametumwa, mambo yataharibika kutokana na vilio vile vya watoto!

“Tunapoteza muda!” Liston Kihongwe akamwambia Vasco Nunda.

“Sasa?” Vasco Nunda akauliza!

“Tumlipue!” Liston akamwambia!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Poa,” Vasco akasema huku akikamata bastola yake imara na kubonyeza kifyatulio cha risasi huku akimlenga John Peka, ambapo alifyetua risasi mbili kuelekea kwake. John akajitahidi kutaka kutumia nguvu ili ajinusuru, lakini risasi zile mbili zilimpata kidevuni na kufumua taya lake!

“Ooh!” John Pekaaliguna na kupiga kelele. Hakuanguka chini, bali alibaki akipepesuka kama mlevi huku amekamatia taya lake lililokuwa linavuja damu! Macho yake aliyatoa akiwaangalia wauaji wale!

“Mmalizie!” Liston akasema baada ya kuona John hajaanguka!

“Mnaniua bure…ooh!” John Peka akasema huku akitaka kuwaendea watoto wake awakumbatie…akachelewa!

Risasi nyingine mbili alizopigwa na Vasco Nunda ndizo zilizoukatisha uhai wake. Akaanguka chini na kuanza kutapatapa kiasi kwamba asingemudu kusimama tena! Ilikuwa ni safari ya kuzimu! Ama kweli alikufa kifo kibaya sana bila hata ya kujitetea, ingawa na yeye alikuwa na bastola yake aliyokuwa ameichimbia sehemu. Lakini Vasco na Liston walimshtukiza ingawa alikuwa na wazo la kuwa nayo kutokana na hali ilivyokuwa imeharibika.

Baada ya kuhakikisha wamemmaliza John Peka, Vasco na Liston wakabaki wamesimama huku wakiiangalia maiti ya John. Watoto walikuwa bado wanapiga makelele, ambayo pia yalimshtua mama yao aliyekuwa chumbani akiwatandikia vitanda. Kwa muda wote alikuwa hajui kilichokuwa kinaendelea kule sebuleni hasa ukizingatia nyumba ile ilikuwa haina uwezo wa kuingiza sauti ndani kwa jinsi ilivyokuwa imejengwa mjengo wa kisasa. Lakini hizi kelele za mara ya pili, aliweza kuzisikia na kumfanya atoke haraka sana na kufikia sebuleni!

Hamad! Akakutana na mambo ya ajabu!

Ni sura mbili za watu asiowafahamu wakiwa wamekamata bastola mikononi mwao! Mumewe amelala chini huku damu zikimtoka kwa wingi! Watoto walikuwa bado wanalia! Akachanganyikiwa! Ni nini kinachoendelea?

Hakujua!

Kwa mstuko na fadhaa, Mary Mshanga akajikuta ameshafika pale alipokuwa amelala mume wake, John Peka, na akaanza kumtingisha kwa nguvu, ingawa alimwona akvuja damu nyingi kutoka kwenye majeraha yale ya risasi! Alipojaribu kumgeuza, akakuta ameshakata roho! Akageuza sura yake kuwaangalia Vasco na Liston, ambao walikuwa wakimwangalia huku wakiwa wamevalia miwani ile mieusi kiasi cha kutoweza kuwatambua! Hakika alikuwa katika hali ya kuchanganyikiwa na kutoekewa chochote!

Vasco na Liston wakapeana ishara, halafu wakatoka nje kama walivyokuja na kuurudishia mlango. Wakaondoka katika eneo lile huku wakiacha makelele yaliyokuwa yakipigwa na Mary, pamoja na watoto wake, Toni na Monica. Baada ya kulifikia gari lao, wakapanda na kuondoka katika mtaa ule wa Kisangilo, Magomeni Mapipa. Waliamua kuendelea na operesheni yao ya usiku kucha, wakiwa wameamua jambo moja tu, kuwaangamiza wote kabla hapajapambazuka! Na walikuwa wamebakia watu wawili tu! Ni David Osmond na Bosco Zambi!



********

Mpango wao ulionyesha kuwa mtu wa pili kuuawa usiku ule, alikuwa ni kijana David Osmond. Hivyo baada ya kutoka eneo lile la Magomeni, walielekea Kinondoni nyumbani kwake. Wakati wote ule, mvua bado ilikuwa inaendelea kunyesha, ingawa haikuwa kubwa sana. Wakaifuata Barabara ya Morogoro hadi kwenye makutano ya barabara ile na ya Rashid Kawawa, kwenye taa za trafiki. Pale Vasco alipinda kulia na kuifuata Barabara ya Kawawa moja kwa moja kuelekea Kinondoni.

Hakika walikuwa wameamua kuyafanya mauaji ya vijana wale kwa usiku mmoja ili wafunge kazi kabisa, na kwa vile kwa usiku ule magari yalikuwa machache sana barabarani, hawakukawia kufika nyumbani kwa David Osmond, mtaa wa Sekenke. Nyumba hiyo iliyokuwa kama mita zipatazo hamsini hivi kutoka katika barabara kuu, ilikuwa imejengwa mjengo wa kisasa na upande wa mbele kukiwa na geti la chuma, na pia imezungukwa na ukuta wa matofali.

Kwa muda ule, taa ya nje ilikuwa inawaka mwanga mkali kama zilivyokuwa nyumba nyingine za mtaa ule, ambao kwa usiku ule ulikuwa kimya kabisa. Baada ya kulipaki gari lao, wakashuka na kusimama kando ya gari na kuanza kupanga cha kufanya na kuongea kama watu waliokuwa wakibishania kitu, halafu baada ya kuafikiana, wakaondoka kwa hatua za taratibu na kuuendea ukuta wa uzio wa nyumba ile, sehemu ambayo palikuwa na mti mmoja mkubwa wa mwembe, uliokuwa sambamba na ukuta, matawi yake yakiwa yameenea mpaka ndani.

Sehemu hiyo ilikuwa na giza kiasi iliyosababishwa na ule mti, hvyo wakaukwea ule ukuta kiufundi na kutua ndani bila kutoa kishindo, kila mmoja akiwa na bastola yake mkononi. Ni kitu ambacho hawakujua, kumbe mle ndani ya nyumba ya David Osmond, palikuwa na mbwa mmoja mkubwa mithili ya beberu la mbuzi, ambaye kwa usiku ule alikuwa amefunguliwa kwa ajili ya ulinzi wa usiku. Hivyo basi, baada ya wao kutua ndani, mbwa yule akaanza kubweka kwa hasira na kuwaendea kwa kasi!

Wakashtuka!

“Mh, hii nuksi sasa!” Liston Kihongwe alisema kwa sauti ndogo huku ameinama usawa wa miti ya maua iliyokuwa imepandwa mle ndani!

“Katoka wapi huyu mbwa?” Vasco Nunda naye alisema huku ameuma meno!

“Tumlipue asituharibie kazi!”

“Alipuliwe!”

Akiwa katika kasi ya kuwaendea pale walipojichimbia, na kutaka kumvamia Vasco Nunda, hakufua dafu, kwani Vasco alimchapa risasi moja ya kinywani, ambayo iliyomrusha juu, na alipotua chini akatulia kimya! Kelele za mbwa zikaisha! Wanaume wakasonga mbele, na kuendelea kunyata kwa mwendo wa kichinichini na kwenda kubaisha kwenye kona ya ukuta.

Kumbe kule ndani ya nyumba, David Osmond alizisikia sauti za kelele za mbwa akibweka wakati alikuwa ameshalala usingizi, na baadaye kukawa kimya. Hivyo basi, akaamua kuamka na kuichukuwa bastola yake ili kujihami, kwa vyovyote hali ya hatari ilinukia! Halafu akatoka nje ili kuangalia ni kitu gani kilichomsibu. Akaufungua mlango wa nje na kuchungulia kwa hofu kidogo!

Vasco na Liston walimsikia akiamka. Wakamsubiri huku wamejificha kwenye kona ile ya nyumba, na alipochungulia tu, kitu cha kwanza kukiona, ni yule mbwa wake. ‘Simba,’ aliyekuwa amelala chini huku damu nyingi zikimtoka, na alikuwa amekufa! Akajiuliza ni kitu gani kilichokuwa kimemsibu, kisha akaamua kuvuta hatua kwenda kumuangalia pale alipolala huku akiwa ameikamata bastola yake imara mkononi.

Alipomfikia ndipo alipomwona amefumuliwa kinywa chake kwa risasi na ulimi umemtoka nje! David akashtuka na kutaka kurudi ndani haraka sana, ili aende kujipanga vizuri, ndipo akaanza kurudi kinyumenyume na bastola kaielekeza mbele na nyuma kadri alivyokuwa anarudi nyuma kwa kuuendea mlango mkubwa. Vasco na Liston walimwona vizuri sana, hivyo hawakumpa nafasi, wakamvamia mithili ya mnyama Chui aliyekuwa mawindoni. Wakamtia mikononi tayari kuikamilisha kazi yao waliyopewa na bosi wao, Salum Kamba!

“Tulia kenge wee!” Vasco Nunda akamwambia!”

“Tupa bastola yako chini!” Liston Kihongwe akadakia!

“Vipi jamani?” David Osmond aliuliza huku akiwashangaa wale watu waliomvamia!

Usoni walikuwa wamevaa miwani mieusi ya jua!

Woga ukamjaa, na harufu ya hatari ikanukia!

Ilikuwa kazi kweli!

“Hatuna muda wa kupoteza!” Vasco Nunda akamwambia na kuongeza. “Tumetumwa roho yako!”

“Mmetumwa roho yangu?” David Osmond akaendelea kuuliza!

“Ndiyo, tunaitaka!” Liston Kihongwe akaongeza kusema!

“Tumetumwa na bosi wako! Anadai kuwa mmemuuza!”

“Mama yangu! Hatujamuuza!”

“Sisi hatujui, tunatekeleza wajibu wajibu!” Liston Kihongwe akasema huku akiwa ameikamata bastola yake imara mkononi!

“Mh!” David Osmond akaguna huku akiona kuwamkifo kilikuwa kinamnyemelea! Na yeye hakupenda kufa kikuku bila kujitetea!

Kama umeme, David akaruka na kujigeuza angani, huku akitoa vipigo vya ghafla vilivyomfanya Vasco na Liston waanguke mbali kidogo na pale alipokuwa amesimama! Lilikuwa ni pigo la kushtukiza!

Baada ya kutoa vipigo vile vya ghafla, David Osmond ahakupoteza muda, akaiendea bastola yake aliyokuwa ameitupa chini tayari kwa mapambano! Kumbe huku nyuma, Vasco na Liston waliokuwa wameanguka chini, walikuwa hawajadondosha bastola zao, zilibaki mikononi mwao, na David alipoinama tu, Vasco alimwahi na kumfyetulia risasi moja iliyompata katika paji la uso. Akatoa yowe, kubwa na kuanguka chini huku akitapatapa! Alishakuwa maiti! Hakika ilitisha sana, kwani risasi ile ilifumua kichwa cha David kiasi kwamba ubongo wake ulitapakaa na kutawanyika! Walipomaliza kutekeleza mauaji yale, Vasco na Liston, walitoka ndani ya uzio wa nyumba ya David kwa kuruka kama walivyoingia mwanzo.

Debora Thomas, mke wa David Osmond alikurupuka kitandani akiwa na gauni la kulalia baada ya kusikia ile purukushani iliyokuwa inatokea kule nje, kama watu waliokuwa wanagombana. Kwanza kabisa hakutaka kuamka baada ya mume wake kutoka nje, lakini kilichomfanya atoke, ni baada ya kusikia vishindo ile, na kishindo cha mtu kuanguka na kutoa yowe kubwa! Na sauti hiyo ilikuwa ya mume wake! Baada ya kutoka nje, ndipo aliposhuhudia mauaji yale ya kuisha!

Mumewe David alikuwa ameuawa!

Debora alipoyatupa macho yake kule kwenye uzio, aliwaona watu wawili waliokuwa kama vivuli, wakiuruka ukuta na kutua nje. Ni Vasco na Liston, ambao waliliendea gari lao na kupanda harakaharaka, na Vasco akaliondoa kwa mwendo wa kasi kuutoka mtaa ule wa Sekenke. Pia, walikuiwa wakijipongeza kwa kuwamaliza watu wawili, David Osmond na John Peka, kama walivyotumwa na Salum Peka!

Gari lile lilipoondoka tu, ndipo Debora, mke wa David alipiga yowe kubwa lililowafanya majirani waamke haraka sana, lakini yeye akapoteza fahamu. Baadhi ya majirani waliofika na kuingia ndani ya uzio wa nyumba ya David, tena kwa kuuruka ukuta, waliikuta hali ile. Wakaanza kumpa huduma ya kwanza na mwingine akapiga simu polisi haraka!



Hakika ulikuwa ni usiku wa aina yake kwa askari polisi wale wa kitengo cha matukio cha waliokuwa zamu usiku ule. Walishangaa baada ya kupigiwa tena simu na kuambiwa kuwa yametokea mauaji ya mtu wa pili kwa kupigwa risasi na watu wasiofahamika. Kwani mwanzo kabisa, pia walipigiwa simu na kupewa taarifa za mtu mmoja kuuawa katika mtaa wa Kisangilo, Magomeni Mapipa, wakaenda na kumkta mtu yule aliyeuawa, na wakalipata jina lake kuwa anaitwa John Peka.

Baada ya kufanya shughuli zao za uchunguzi ikiwa ni pia ni kuchukua alama za vidole na maganda ya risasi, wakaichukuwa maiti na kuipeleka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa uchunguzi zaidi. Wakaahidi kurudi kesho yake asubuhi kwa ajili ya mahojiano zaidi na tukio zima lilivyotokea kama watawatambua wauaji!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Lakini sasa ndiyo hilo tukio la pili walipopigiwa simu tena! Hawakuelewa wauaji walikuwa na maana gani, ukizingatia walikuwa hawajapumzika tokea walipotoka katika tukio la kwanza Magomeni Mapipa, sasa ni Kinondoni! Makubwa!

Askari polisi wakafika katika eneo lile wakiwa na gari lao la matukio aina ya Toyota Land Cruiser. Wakashuka na kuanza kufanya uchunguzi katika eneo zima la kuizunguka nyumba ya David Osmond. Katika timu hiyo ya upelelezi, kama ilivyokuwa mwanzo, walikuwemo wapiga picha, wataalamu wa alama za vidole, na wa milipuko ya risasi.

Baada ya uchunguzi wao wa muda, waligundua kuwa ganda la riasi lililotumika katika mauaji ya John Peka, ndiyo hilohilo lililotumika katika mauaji ya David Osmond muda siyo mrefu sana. Hivyo ilimaanisha wauaji walikuwa ni walewale! Polisi wakaichukua maiti ya David na kuipeleka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Hata hivyo, Kachero Inspekta Raymond Gopi ambaye alikuwa akifuatilia matukio yale kwa usiku ule, alihisi kuwa lazima kutakuwa na jambo! Tena siyo dogo, hivyo akaamua kuingia katika upelelezi mara moja kutokana na mauaji yale yaliyomsisimua na kuwahusisha wafanyabiashara ile haramum na si vinginevyo! Aliamua kazi ile aianze kesho yake asubuhi.



*******

Ni katika usiku ule wa hekaheka uliokuwa unaendelea, na mauaji ya kutisha yakifanyika, kijana, Bosco Zambi, alikuwa amelala chumbani, nyumbani kwake, Maghorofani, eneo la Faya. Upande wake wa pili alikuwa amelala, mwanadada mrembo, Marieta Ngonyani, ambaye alitegemea kuja kuwa mke wake baadaye. Ndani ya chumba kile, taa ya rangi ya kijani hafifu ilikuwa inawaka na kuufanya mwili mwororo wa Marieta upendeze kutokana na rangi yake.

Kwa muda wote, Bosco Zambi alikuwa akimuangalia mpenzi wake kwa matamanio ikiwa ni baada ya kumaliza mechi pevu ya kwanza, na sasa alikuwa akijaribu kupasha ili aianze mechi ya pili. Ingawa Bosco alikuwa macho muda ule wa saa saba, lakini roho yake ilikuwa ikienda kasi sana kuashiria hali ya hatari.

Kusema kweli hali ile ilimnyima rah asana, ukizingatia ilikuwa haijawahi kumtokea hata mara moja, hivyo akaichukuwa simu yake iliyokuwa juu ya kijimeza kando ya kitanda. Alikuwa ameamua kuwapigia wenzake, John Peka na David Osmond na kuwaeleza jinsi hali ile ilivyo, labda wangeweza kumpa ushauri. Akapiga namba ya simu ya John Peka, ambapo iliita kwa muda kidogo, halafu ikapokelewa kwa sauti ngeni, haikuwa ya John!

“Haloo…nani?”

“Mimi Bosco…wewe nani?” Bosco Zambi akauliza.

“Mimi ni jirani yake…nikusaidie…”

“Nina shida na John tafadhali…”

“Oh, John ni nani kwako?”

“Ni rafiki yangu…”

“Aisee…kama ni rafiki yake, nakuomba uje huku nyumbani kwake, Magomeni…amepata matatizo…” sauti ile ikamwambia.

“Matatizo gani?”

“Kuna msiba umetokea usiku huu…”

“Msiba wa nani?”

“Ni kwamba John ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana usiku huu…”

“Mungu wangu! John ameuawa?”

“Ndiyo…”

“Ok, nakuja..”

“Jambo la maana…bai…” sauti ya mtu huyo ikamwambia na kukata simu!

Bosco Zambi akamaliza kusema na kubaki amechanganyikiwa baada ya kusikia John Peka ameuawa. Kwa vyovyote alijua kuwa aliyefanya mauaji yale hakuwa mwingine zaidi ya bosi wao, Salum Zakwa! Ni yeye alikuwa amewatuhumu kuwa walikuwa wamemsaliti na kumchoma kwa polisi na kusababisha vijana wake, kukamatwa na dawa za kulevya walipokuwa wanarejea nchini kutokea nchini Pakistani.

Akiwa bado amechanganyikiwa, Bosco Zambi akapiga namba za David Osmond, ili amjulishe na kumwambia kuwa ajihadhari kwa kile kilichomkuta mwenzao, John Peka. Simu ile ikaita kwa muda, halafu ikapokewa na mtu mwingine. Bosco Zambi akazidi kuchanganyikiwa si mchezo!

“Haloo…nikusaidie…” mtu yule akamwambia.

“Nani mwenzangu?” Bosco Zambi akamuuliza.

“Kwani wewe nani?” Mtu yule wa upande wa pili akamuuliza!

“Mimi ni rafiki yake…nina shida naye…” Bosco Zambi akasema huku akiwa na wasiwasi.

“Mimi ni jirani yake hapa Kinondoni…”

“Je, yeye yupo?”

“Nasikitika sana…hapa ninapoongea na wewe, ni kwamba rafiki yako David ameuawa usiku huu, sijui ni majambazi au vipi…”

“Mungu wangu!” Bosco Zambi akasema huku akizidi kuchanganyikiwa!

“Hivyo basi, nakusihi njoo tujumuike na kuchangia mawazo katika msiba. Ukweli ni kwamba hali hapa ni ya kusikitisha sana…” mtu yule alimwambia.

“Haya, nakuja muda siyo mrefu…” Bosco Zambi akasema na kuikata ile simu!

Bosco Zambi akageuka na kumwangalia Marieta, aliyekuwa bnado usingizini. Akanyanyuka kutoka pale kitandani ili kujiandaa kwa kitakachotokea! Kwa vyovyote alijua kuwa aliyebakia ni yeye tu, kwani wenzake John Peka na david Osmond walishauawa usiku ule, na ni lazima wauaji wale wangekuwa njiani kwenda kummaliza, kitu ambacho kilikuwa kimepangwa kutekelezwa kwa usiku huo!

Baada ya kunyanyuka, akaliendea kabati la nguo na kutoa nguo zake maalum, shati na suruali za kadeti, na kuvalia haraka. Kisha akaichukua bastola yake aina ya Grinner, na kuipachika kiwambo cha kuzuia mvumo. Ni bastola ambayo alikuwa ameinunua kutoka kwa wakimbizi wa Rwanda, miaka ya nyuma kule mkoani Kigoma. Akaipachika kiunoni, kwani aliamua kujiandaa kwa vita dhidi ya washenzi wale!

Bosco zambi hakumwamsha Marieta, isipokuwa aliufungua mlango wa chumbani na kutoka hadi sebuleni kwa hatua za kunyata ili asimshtue mpenzi wake. Hakuwasha taa ya ndani, isipokuwa alienda kubanisha kwenye pembe ya ukuta kwa kukaa juu ya meza ndogo ya kahawa. Akalisogeza pazia kidogo kiasi ambacho aliweza kuona mpaka kule nje, kuanzia chini kabisa inapopita Barabara ya Morogoro mpaka ngazi za kupandisha juu kuelekea katika nyumba yake. Kwa vyovyote Bosco aliutegemea ugeni wa Vasco Nunda na Liston Kihongwe! Kule nje mvua ilikuwa bado inanyesha!



********

Vasco Nunda na Liston Kihongwe waliondoka pale mtaa wa Sekenke, Kinondoni bila kushtukiwa baada ya kufanya mauaji ya kijana, David Osmond. Kwa muda wote wakiwa ndani ya gari, walikuwa wakijipongeza kwa hilo na kupanga kwenda kummaliza Bosco Zambi aliyekuwa katika orodha ile ya kufa! Walipotoka pale Kinondoni, waliifuata Barabara ya Kawawa, kisha ya Kinondoni hadi katika makutano na Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, ufukweni mwa Baharin ya Hindi.

Taa nyekundu ya trafiki ilikuwa inawaka, lakini Vasco hakusimamisha gari, bali alipitiliza na kuifuata barabara ya ile kuelekea daraja la Salender. Kisha mbele yake wakapinda na kuifuata Barabara ya Umoja wa Mataifa. Kupita kote kule, ilikuwa ni kupoteza lengo kama kuna watu walikuwa wakiwafuatilia wasijulikane kwa urahisi. Wakati huo ile mvua ilikuwa imekatika na kufanya jiji la Dar es Salaam kuwa kimya kwa usiku ule, na magari kutokuwa barabarani.

Hatimaye gari lao lilifika eneo la Faya, kwenye taa za trafiki, katika makutano ya Barabara ile ya Umoja wa Mataifa na ya Morogoro. Vasco Nunda akalipaki akalipaki gari karibu na kituo cha daladala, halafu wakashuka na kuanza kujadiliana kama vile ni watu wa kawaida waliokuwa wametoka katika starehe zao, ukizingatia jiji la Dar es Salaam kulikuwa hakuna kuulizana umetika wapi!

“Tumeshafika mwanangu…” Liston Kihongwe akamwambia Vasco Nunda.

“Ni kweli, ghorofa lenyewe ni lile pale lenye namba ‘C,’ Vasco Nunda akasema huku akiliangalia ghorofa lile.

“Ndiyo lenyewe, twe’nzetu…” Liston Kihongwe akasema.

“Lakini naona tubadilike kidogo…” Vasco Nunda akamwambia Liston.

“Tubadilike nini?” Liston akauliza.

“Tuvue haya makoti, watu wasije wakatushtukia…”

“Ni kweli…”

Wote wakayavua yale makoti na kuyaacha ndani ya gari, na kubakiwa na nguo zao za kawaida tu na kuonekana ni vijana watanashati. Kamwe hakuna mtu yeyote ambaye angeweza kuwashtukia kama walikuwa na nia mbaya, halafu wote wakashuka kutoka ndani ya gari, huku wakiwa wameyavua yale makoti yao na pia miwani mieusi waliyokuwa wamevalia.

Kwa kujihadhari, gari waliliacha likiwa katika muungurumo mdogo na milango ya gari hawakuifunga, bali waliiacha wazi ili kama wakikurupushwa waweze kuingia ndani ya gari kwa urahisi. Hiyo ni mbinu ambayo huwa wanaitumia mara nyingi sana na kuonyesha kufanikiwa.

“Bosi alisema anaishi ghorofa ya ngapi vile?” Liston Kihongwe akauliza kwa sauti ya chini.

“Usiwe mjinga Liston, bosi alisema ni ghorofa ya tatu…” Vasco Nunda akamwambia kwa hasira kidogo!

“Poa, twende nimeshakumbuka,” Liston akasema, kisha wakaondoka na kuufuata uchochoro mmoja uliokuwa pale na kutokeza katika ghorofa lile.

Taa ya nje ilikuwa inawaka na kuweza kuona ngazi zilizokuwa zinaelekea juu. Vasco na Liston wakaanza kuzikwea taratibu kuelekea ghorofa ya tatu alipokuwa anaishi Bosco Zambi. Wakauona ule mlango mkubwa wa kuingilia ndani na kutokezea sebuleni, ambapo ndani palikuwa na giza baada ya kuangalia pale dirishani. Sehemu yote ilikuwa kimya kabisa pale ghorofani, ambapo taa ya nje ilikuwa inawaka na kuwarahishia kuona vizuri, hivyo wakausogelea ule mlango na kuanza kubonyeza kengele!





********

Bosco Zambi alikuwa bado amekaa juu ya meza pale sebuleni. Kwa muda wote alikuwa akiyatupa macho yake kuelekea kule nje. Aliweza kuwaona Vasco Nunda na Liston Kihongwe walivyofika na kuliacha gari lao kule chini. Baada ya kushuka wakaanza kujadiliana na kupandisha ngazi hadi katika mlango wake kabla ya kubonyeza kengele.

Na hata kengele ilipobonyezwa, Bosco Zambi hakuufungua mlango, isipokuwa alizidi kuwachungulia lakini hakuweza kuwafahamu watu hao kwa sura. Mikononi mwa Vasco na Liston, walikuwa wamekamata bastola zao imara, na kuonyesha kuwa walikuwa wamefika pale kwa kazi moja tu, kuua! Alichofanya Bosco, ni kwamba aliwaangalia kwa makini, halafu akainyanyua bastola yake na kulenga shabaha kuelekea pale walipokuwa wamesimama!

Bosco Zambi alibana pumzi na kufyetua risasi mbili, ambapo risasi ya kwanza iligota ukutani na risasi ya pili ilimpata Liston katika bega la kushoto, ambapo aliguna kwa maumivu na kuanza kuyumba kama mlevi! Lakini Vasco alijizungusha hewani na kuelekeza risasi tatu kuelekea pale dirishani alipokuwa amesimama Bosco, lakini Bosco alikuwa ameshachuchumaa na risasi zile kumkosa!

“Mshenzi huyu!” Vasco Nunda akasema huku akiendelea kuangalia pale dirishani alipopiga zile risasi!

“Oooh! Vasco, nimeumia…turudi…” Liston Kihongwe alisema huku ameshika bega lake lililokuwa limejeruhiwa vibaya kwa risasi!

“Na kweli, tukajiandae!” Vasco Nunda alisema huku akirudi kinyumenyume kujihami. Ukweli ni kwamba hawakuujua uwezo wa adui jinsi alivyokuwa amejiandaa!

Kitendo kile kilimpa mwanya Bosco Zambikufyetua risasi nyingine zilizompata tena Liston Kihongwe katika bega la kulia, akapiga yowe kubwa na kuanguka chini! Akaanguka na kubiringika katika ngazi kuelekea chini huku akifuatiwa nyuma na Vasco!

“Mh, vipi Liston?” Vasco Nunda akamuuliza huku akimwangalia!

“Nimepigwa risasi nyingine…ooh! Vasco nibebe…” Liston akasema huku akisikia maumivu makali.

“Poa, lazima niondoke na wewe!” Vasco akamwambia huku akimbeba Liston ili aondoke naye.

Hata hivyo Vasco Nunda hakufika mbali, kwani wakati akikimbia na Liston aliyembeba begani, Bosco alitoka na kufyetua risasi nyingine ambazo zilimkosakosa Vasco na kupiga nguzo ya chuma ya umeme, ambayo ilitoa mlio na cheche za moto!

“Mungu wangu!” Vasco Nunda alisema huku akiwa hana la kufanya!

“Oh, vipi Vasco?” Liston Kihongwe akamuuliza Vasco Nunda huku akiuma meno yake kwa maumivu!

“Hatari tupu!” Vasco Nunda akasema huku akimbwaga chini Liston ili apate kujiokoa baada ya kuona mambo magumu!

“Unaniacha Vasco?” Liston akamuuliza Vasco!

“Ndiyo, nakuacha…”

“Kwa nini?”

“Sina jinsi Liston, hatuwezi kukamatwa wote!” Vasco Nunda akamwambia Liston, huku pia akiichukua ile bastola aliyokuwa nayo kibindoni mwake, ikiwa ni kwa ajili ya usalama zaidi. Baada ya hapo akalikimbilia gari lake lililokuwa mbali na pale.

“Nimekwisha! Tena mwisho mbaya sana!” Liston Kihongwe akajisemea huku akimwangalia jinsi Vasco Nunda alivyokuwa anaondoka!

Baada ya kulifikia gari, ambalo lilikuwa bado likinguruma kwa moto mdogo, Vasco Nunda akaingia ndani na kuliondoa kwa mwendo wa kasi huku magurudumu yakisugua lami na kutoa mlio mkali! Akaliingiza katika barabara kuu ya Morogoro, na kumwacha Liston aliyekuwa amejeruhiwa, akihofia kukamatwa na wananchi wenye hasira kali, au askari polisi wa doria wanaozungika jiji zima la Dar es Salaam kudhibiti uhalifu.

Vasco Nunda aliamua kukimbia na kumwacha Liston, kwani aliamua jambo moja tu, ni kwenda nyumbani kwake, Kinondoni, alipokuwa anaishi, ili akajipange upya! Kwa pale alikuwa amenyanyua mikono!



*******http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Bosco Zambi alirudi chumbani baada ya purukushani ile, na bastola yake alikuwa bado ameikamata mkononi ikifuka moshi wa baruti. Halafu akamwendea Marieta aliyekuwa bado amelala usingizi, na wakati huo hakujua kilichokuwa kinaendelea baina ya Bosco na watu wale!

“Haloo…Marieta…” Bosco Zambi akamwita huku akimtingisha.

“Beee…” Marieta akaitikia kivivu, kwani alikuwa katika usingizi muda ule, ambao ni usiku mwingi.

“Amka haraka Marieta!” Bosco akaendelea kusema.

“Oh, kuna nini?” Marieta aliendelea kuuliza huku akiwa na uchovu wa usiku ule. Halafu akaendelea kulala badala ya kuamka, kiasi ambacho kilimfanya Bosco azidi kuchanganyikiwa!

“Hivi unasikia?Amka Marieta?”

“Tunakwenda wapi usiku wote huu?”

“Wewe jiandae tu, usiulize!” Bosco Zambi akaendelea kumwambia huku akiahangaika kuchungulia dirishani.

Kule chini watu walikuwa wameanza kukusanyika!

Kwa bahati nzuri gari la polisi wa doria aina ya Toyota Land Cruiser lilipita katika barabara ile ya Morogoro, na kuukuta ule umati wa watu uliokuwa umemzunguka Liston Kihongwe. Wakaelekea pale na kuanza kuwahoji watu wale ambao nao hawakujua kilichokuwa kinaendelea na kufanya mpango wa kumsaidia majeruhi yule kumpeleka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Ulikuwa ni usiku wa aina yake kwa Jeshi la Polisi, jijini Dar es Salaam, kwa kukumbana na mauaji yale na majeruhi, yaliyokuwa yakiendeshwa na watu wasiojulikana!

Marieta aliamka na kuvalia nguo zake kama alivyoamriwa na Bosco Zambi. Baada ya kumaliza kuvaa, akachukua mkoba wake, halafu wakatoka nje huku Bosco akiufunga mlango wa nyumba yake, kwani hakutegemea kurudi mapema katika eneo lile, palikuwa pameshaharibika na polisi nao walikuwa wameshafika na kuanza kufanya mahojiano na watu. Nje katika ngazi, palikuwa pametapakaa damu mbichi iliyomshtia sana Marieta punde tu alipoiona!

Mwili ukamsisimka!

“He, hiki nini tena?” Marieta aliuliza!

“Ni damu hii!”

“Damu ya nani?”

“Ni maelezo marefu, twen’zetu…”

“Haya…” Marieta akasema huku akiwa haelewi ni kipi kinachoendelea!

Walipofika chini, wakakuta wale askari polisi wa doria wakiwa wanambeba Liston Kihongwe wakisaidiana na wananchi, kumuingiza ndani ya gari la polisi. Hata hivyo, Bosco Zambi hakujali wala kwenda kuangalia kilichojiri, kwani walitembea kwa mwendo wa haraka kuliendea gari. Na hata wale askari hawakuweza kumshtukia Bosco kama ni yeye aliyempiga risasi Liston, bali walijua ni watu waliokuwa wakiondoka kuelekea kwenye shughuli zao.

Kila aliyekuwa pale alikuwa akiongea lake!

“Hili ni jambazi!”

“Limepigwa risasi!”

“Mwenzake katoroka!”

“Ni nani kampiga risasi?”

Bosco Zambi hakuwajali wale watu, bali akiongozana na Marieta, walikwenda kupanda gari lile gari aina ya Nissan Murano, lililokuwa katikati ya magari mengine yaliyoko nje ya maghorofa yale. Akalitia moto na kuliondoa kwa mwendo wa kasi kuifuata barabara ya Morogoro, akiacha umati ule wa watu ukishangaa. Akaifuata barabara ya Morogoro, kuelekea Ubungo na magari yalikuwa machache sana usiku ule kiasi ambacho kilimfanya aliendeshe gari lile kwa mwendo wa kasi.

“Bosco…” Marieta akamwita.

“Naam,” Bosco akaitika.

“Hebu niambie…tunakwenda wapi?”

“Tunakwenda Morogoro!”

“Saa hizi?”

“Ndiyo, mambo yameharibika!”

“Yameharibika kivipi?”

“Hukumuona yule mtu aliyezungukwa na watu pamja na polisi?”

“Nimemuona…ni wewe uliyempiga risasi?”

“Ndiyo, ni mimi,” Bosco Zambi akasema na kuongeza. “We twen’zetu, mengi tutaongea huko mbele ya safari. Ni historia ndefu!”

“Mh, mambo makubwa!”

“Makubwa si mchezo!”

Bosco Zambi akaendelea kupangua gea na kuongeza mwendo, kuifuata barabara ya Morogoro, na hakuzungumza chochote na Marieta. Marieta alikuwa naye amenyamaza kimya huku mawazo yake yakiwa mbali sana baada ya kuchukuliwa kwa safari ambayo alikuwa hajaipangilia kamwe, zaidi ya kuchukuliwa kama mzigo!

********

Usiku ule wa saa nane, Vasco Nunda alisimamisha gari lake mbele ya lango la nyumba yake ya kifahari, eneo la Kinondoni Hananasif, alipokuwa anaishi, mara baada ya kukurupushwa na Bosco Zambi! Ni eneo tulivu ambalo alikuwa anakaa na hakuna mtu aliyekuwa anajua anafanya kazi gani zaidi ya kuona ni kijana aliyeukata kimaisha na kujenga nyumba yake ile ya kifahari iliyozungukwa na ukuta madhubuti.

Vasco Nunda akapiga honi mara tatu, la lango likafunguliwa na kijana wa kimasai aliyekuwa analinda katika himaya hiyo. Baada ya lango kufunguliwa, Vasco akaliingiza gari hadi katika uwanja mdogo, halafu akashuka haraka bila hata kmsemesha yule mlinzi, na kuingia ndani, ambapo alifikia sebuleni na kukalia sofa. Bila kupoteza muda, akachukuwa simu yake na kuanza kuwasiliana na Salum Zakwa Mnube, ili kumjulisha hali halisi ilivyokuwa!

“Zakwa hapa…” Salum Zakwa alisema upande wa pili.

“Mimi Vasco bosi…”

“Ndiyo…lete habari!”

“Bosi, tumeshamaliza nusu ya kazi!”

“Nusu ya kazi?”

“Ndiyo bosi…”

“Kivipi? Sikuelewi!”

“Tumewamaliza wawili…bado mmoja!”

“Bado mmoja kwa nini?”

“Baada ya kuwamaliza wale wawili, John Peka na David Osmond, tulikwenda nyumbani kwa Bosco Zambi kumshughulikia. Lakini tulipofika tu, tukakuta naye ameshajiandaa. Akaanza kufurumusha risasi kutoka ndani!”

“Halafu ikawaje?”

“Tukazidiwa bosi!” Vasco Nunda alisema kwa msisitizo, halafu akaendelea. “Na hapa ninapoongea nimemwacha Liston!”

“Umemwacha wapi?”

“Nilimbwaga barabarani baada ya kuwa nimembeba niondoke naye, baada ya kujeruhiwa kwa risasi. Hapo ndipo nilipozidiwa, kwani Bosco aliendelea kufurumusha risasi mithili ya mvua! Alikuwa amejiandaa!”

“Mama yangu!” Salum Zakwa akasema. “Sasa mambo yameharibika. Je, alikuwa na silaha?”

“Ndiyo, alikuwa na bastola, lakini niliwahi kuichukuwa!”

“Oh, umefanya vizuri…lakini pamoja na hayo, mambo siyo shwari. Isije akahojiwa halafu akavujisha siri! Hivyo dawa yake ni kummaliza kabisa!”

“Nakusikiliza bosi!”

“Changamka kabla hapajapambazuka, msake muda huu huu na inawezekana keshapelekwa Muhimbili kwa matibabu!”

“Nitafanya hivyo bosi…”

“Halafu kitu kingine cha muhimu inabidi uhame hapo nyumbani kwako kwa muda huu!” Salum Kamba akamwambia!

“Unasema nihame hapa nyumbani?”

“Ndiyo. Inabidi uhame hapo kwako ili polisi wasije wakakukamata punde watakapokushtukia kuwa ndiye muuaji!”

“Sasa nihamie wapi?”

“Utahamia gesti kwa muda. Natumaini unaifahamu Bangaiza Gesti, iliyoko Mwenge?”

“Ndiyo, naifahamu, si ile iliyoko mafichoni, maarufu kwa ufuska?”

“Ndiyo yenyewe. Basi, ukifika hapo atakuta nimeshawataarifu na huduma zote utapata kwa gharama yangu, upo?”

“Nakupata bosi…”

“Na pale ndiyo sehemu tutakayokutana na kupanga mipango yetu. Ukifika jitambulishe kwa jina la Pascal Memba. Ndivyo nilivyomwambia mhudumu wa pale!”

“Hakuna taabu bosi…nitafanya hivyo.”

“Basi, endelea na kazi!”



********

Baada ya kumaliza kuwasiliana, Vasco Nunda hakulala, alibadili nguo alizokuwa amevaa mwanzo, na kuvalia suti nadhifu ya rangi nyeusi iliyompendeza, bila kusahau bastola yake, ambayo ilikuwa imesheheni risasi. Alipomaliza kujiandaa, akatoka nje na kupanda gari lake, wakati huo ikiwa imetimu saa kumi na robo za usiku. Akalitia moto na kuondoka huku akimuaga yule mlinzi wa kimasai, ambaye alilifunga tene geti kama lilivyokuwa mwanzo.

Vasco Nunda alifika katika Hospiotali ya Taifa ya Muhimbili na kulipaki gari sehemu ya maegesho, ambapo kwa usiku ule yalikuwa ni mengi tu. Palikuwa na pilikapilika nyingi tu za watu pamoja na magari yaliyokuwa yanawaleta waathirika wa ajali za aina mbalimbali zilizotokea jiji. Hivyo, akionekana mtu nadhifu, Vasco Nunda alielekea sehemu ya Mapokezi na kuuliza kwa wauguzi wawili watatu hivi ambao walimwambia kwamba Liston Kihongwe alikuwa amepelekwa katika chumba cha uchunguzi, akifanyiwa upasuaji baada ya kufikishwa akitokea katika kituo cha Polisi cha Salender Bridge.

Hakikawia, Vasco Nunda akaelekea sehemu ile na kukaa katika kiti kimojawapo kati ya viti vilivyokuwa pale kwa ajili ya watu waliokwenda kuwajulia hali wagonjwa. Ni karibu na mlango wa kioo kisichoonyesha ndani, wa kuingia ndani ya chumba kile kilichokuwa na maandishi, ‘CHUMBA CHA UPASUAJI.’Na kwa ujumla eneo lote lilikuwa kimya kutokana na pilika kuwa siyo nyingi kwa wagonjwa wanaohitaji kufanyiwa upasuaji, na pia hakuna watu waliokuwa wanapitapita. Hiyo ndiyo hali aliyokuwa anaitaka Vasco, hasa ukizingatia alikuwa amekwenda pale kwa kazi moja tu, kumaliza Liston Kihongwe!

Vasco Nunda akajivuta hadi katika chumba kile na kusikiliza, ambapo alisikia madaktari wakiongea mle ndani, kuonyesha kwamba walikuwa wakimhudumia Liston, basi kitendo bila kuchelewa, Vasco akaufungua ule mlango wa kioo na kuingia ndani kama vile alikuwa ni mwenyeji, na mle akakuta madaktari waliokuwa wakimshughulikia Liston, kujaribu kuyaokoa maisha yake! Alikuwa amelazwa juu ya kitanda maalum, na kuzungukwa na madakrai wale pande zote, na sauti za mikasi tu zilizoweza kusikika. Hata Vasco Nunda alipoingia mle ndani, madaktari wale hawakushtuka sana zaidi ya kumuangalia na kumshangaa kwa vile hawakuruhusiwa watu kuingia ndani ya chumba kile!

Taratibu Vasco Nunda akachomoa bastola yake na kuiweka nyuma ya mgongo wake kama vile alikuwa ameiweka mikono nyuma. Baada ya kuwafika karibu, ndipo alipowaonyesha ile bastola na kuwaweka chini ya ulinzi madaktari wale waliokuwa bado wanamshangaa kwa yeye kuwaingilia na silaha. Hakuna asiyeujua uchungu wa kifo, kwani madakrai wote walinyoosha mikono yao juu, kiasi kwamba hata kelele za mikasi iliyokuwa ikidondoka ilisikia.

Vasco Nunda akatoa amri ya kurudi nyuma na kugeukia ukutani, na madaktari wale wakafuata amri hiyo kwa kumuacha Liston aliyekuwa amelala pale kitandani na kugeukia ukutani. Ukweli ni kwamba hawakumwelewa mtu yule, ambaye alijisogeza hadi katika kile kitanda alicholalia Liston na kumwambia, “Kwa heri rafiki yangu, sina budi kukumaliza usije ukatoa siri. Hiki ndiyo kiapo chetu, tutakutana kuzimu!”

Baada ya kusema vile, Vasco Nunda alifyetua risasi mbili kwa Liston, ambazo zote zilimpata kifuani. Hata hivyo, Liston hakusikia maumivu yoyote, kwani alikufa kimyakimya ukizingatia alikuwa amepoteza fahamu kwa muda wote, na alipomaliza kazi ile iliyompelekea pale, akarudi kinyumenyume na kuufungua mlango kisha akatokomea zake bila kushtukiwa na mtu yeyote. Wale madaktari waliokuwa bado wameuangalia ukuta, hatimaye mmoja wao akageuka nyuma na kuona mtu yule ameshaondoka!

“Jamani keshaondoka!” Akawaambia wenzake!

“Nini kinachoendelea?” wingine akauliza!

“Ni jambazi!”

“Amemuua!”

“Oh, tuwajulishe polisi!”

“Ni hatari sana…oh!”

Daktari mmoja akaiendea simu iliyokuwa mle chumbani, halafu akabonyeza namba za dharura za polisi. Baada ya kupiga, upande wa pili ukaasema:

“Polisi matukio hapa tukusaidie…”

“Hapa ni Hospitali ya Taifa ya Muhimbili…”

“Ndiyo, tukusaidie…”

“Yametokea mauaji!”

“Mauaji?” Alihoji yule askari!

“Ndiyo…kuna yule majeruhi aliyepigwa risasi na kuletwa hapa Muhimbili na polisimuda siyo mrefu, naye ameuawa kwa risasi na mtu mmoja aliyekuwa na bastola…”

“Oh! Leo ni kazi tu, mauaji mtindo mmoja, kuna nini? Ok, tunakuja…” askari polisi yule akasema upande wa pili wa simu ile ya dharura.

Daktari akaikata na kuweka kiwiko sehemu yake na kubaki ameshangaa, nusu akiwaangalia wenzake na nusu akiiangalia maiti ya Liston Kihongwe iliyokuwa imelala kifudifudi juu ya kitanda! Hakika ni mkasa ambao ulikuwa umewachanganya sana kwa jinsi mauaji yale yalivyokuwa yakiendeshwa kimpangilio na kudhihirisha kwamba muuaji alikuwa ni mtu mzoefu katika kazi ile, yaani mafia!

Lakini chanzo ndicho hakikujulikana!



********

Vasco Nunda alitembea kwa mwendo wa kasi kidogo punde alipotoka mle chumbani. Alipofika nje, akapanda gari lake na kuondoka kurudi nyumbani kwake akiwa na matumaini kwa kuhitimisha kazi ile ya mauaji ya usiku kucha! Alifika nyumbani kukiwa kumeshapambazuka, akaliingiza gari ndani la kama kawaida na kulipaki sehemu ya maegesho. Akashuka na kuingia ndani akiwa amechoka haswa kutokana na zile pilikapilika za usiku kucha, akatamani angalau kupumzika ili auondoe uchovu ule kwa kulala kidogo japo masaa mawili.

Lakini hakuwa na muda huo kabisa, ratiba ilikuwa imembana sana, kwani hakutakiwa kabisa kukaa pale nyumbani zaidi ya saa mbili kama alivyotahadharishwa na Salum Zakwa. Hivyo alichofanya ni kuuchukuwa mkoba wake mkubwa wa ngozi, ambapo aliweka nguo chache za kubadili, bastola yake na risasi za akiba, tayari Alipomaliza kujiandaa, Vasco Nunda alitoka na kumuaga yule mlinzi kwa kumwambia kuwa alikuwa na safari ya ghafla na kumpa maagizo kuwa awe macho na ulinzi wa pale nyumbani.

Mlinzi yule akamkubalia huku akijua ni kweli alikuwa anasafiri, kumbe alikuwa anakwenda Bangaiza Gesti, Mwenge, kujificha ili asikamatwe na poliosi watakaokuwa wana kiu ya kumkamata muuji yule aliyekuwa anaendesha mauaji usiku kucha!

Vasco Nunda alipatoka pale nyumbani kwake, Kinondoni Hananasif, akitembea kwa miguu kitu ambacho alikuwa hajazoea, kwani mara nyingi alikuwa akitumia usafiri wa gari lake. Lakini kwa siku ile ilikuwa ni kitu cha ajabu kidogo, kitu ambacho hata majirani wawili watatu walishangaa, lakini hawakumuuliza. Ni hadi alipofika katika barabara kuu, kwenye kituo cha teksi. Pale aliiendea teksi moja, ambapo dereva wake alikuwa amesimama nje yake, na alipomuaona akiiendea, akamwambia:

“Karibu bosi…”

“Ahsante…” Vasco Nunda akasema huku akiufungua mlango wa nyuma na kuingia ndani ya teksi. Hakupenda kupoteza muda katika sehemu ile.

“Unaelekea wapi bosi?” Dereva yule akamuuliza.

“Naelekea Mwenge…”

“Mwenge sehemu gani?”

“Ninafika jirani na Bangaiza Gesti, unaifahamu?”

“Kuna mtu asiyeifahamu gesti ile? Si ile inayosifika kwa watu kufanya ufuska muda wote? Hasa wezi wa wake za watu!” Dereva teksi yule akamwambia huku akiiondoa teksi.

“Ah, hayo mimi siyajui. Ninachotaka ni kufika jirani na pale, mambo ya ufuska siyajui kabisa. Sisi watu waungwana bwana!” Vasco Nunda akamwambia dereva yule, kumbe ni zuga tu, alikuwa anapafahamu fika.

“Na kweli, wewe hufananii kabisa na mtu wa kuingia ndani ya gesti hiyo inayonuka uvundo wa ufuska! Kama kweli kuna gonjwa la Ukimwi, basi litatumaliza!” Dereva yule akaendelea kusema lakini Vasco hakumjibu. Na wala hakupenda kuzungumzia suala lile, aliona kama vile anapoteza muda hasa kwa yale yanayomkabili!

Teksi ilifuata Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, ambapo palikuwa na foleni kubwa ya magari katika barabara ile. Ulikuwa ni usumbufu mkubwa lakini hawakuwa na la kufanya, hadi walipofika. Bangaiza gesti ilikuwa imejificha katikati ya nyumba nyingine, eneo la Mwenge, ikiwa imezungushiwa uzio, ambao kwa mtu aliyekuwa nje siyo rahisi kuona ndani. Hivyo teksi ilipofika jirani na pale, Vasco akamwambia dereva:

“Haloo, dereva, hapa panatosha…”

“Sawa bosi,” dereva akasema huku akipunguza mwendo tayari kwa kulisimamisha gari.

“Poa,” Vasco Nunda akasema huku akitoa pochi yake iliyotuna. Akachomoa fedha mna kumlipa dereva, kisha akashuka chini na kuelekea kule iliko Bangaiza Gesti. Alipoondoka tu, na teksi ile ikaondoka kwa kurudia na njia waliojia, na wala dereva yule hakujua kilichokuwa kinaendelea kuwa alikuwa amebeba mtu wa hatari, aliyekuwa ananuka damu za watu kwa mauaji aliyoyatekeleza usiku kucha!

Ili kupoteza lengo, Vasco Nunda aliamua kuingia ndani ya gesti ile kwa kupitia mlango wa nyuma, ambao unapitia katika geti dogo, halafu akatokeze mapokezi. Akaongeza hatua za haraka huku ameukamata ule mkoba wake vizuri kwa kuupachika begani hadi alipoingia ndani ya gesti ile kwa kupitia nyuma.

Baada ya kuingia, akaelekea hadi mapokezi, ambapo alimkuta kijana mmoja, mhudumu wa pale, aliyejulikana kwa jina la Masoud Kipengo, ambaye ni mzoefu sana wa biashara ile baada ya kuifanya kwa muda mrefu sasa. Kwa ujumla hali ya pale palikuwa kimya kabisa kana kwamba hakukuwa na mtu mle ndani.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Karibu bosi…” Masoud Kipengo akamkaribisha.

“Ahsante sana,” Vasco Nunda akasema huku akiikagua kwa macho mandhari ya eneo lile.

“Karibu sana…” aliendelea kusema Masoud Kipengo huku akimwangalia kwa makini Vasco Nunda. Alionekana ni mtu mwenye uwezo kwa jinsi alivyokuwa amevalia suti na umbile lake kwa ujumla.

“Mimi ninaitwa Pascal Memba,” Vasco Nunda alimwambia mhudumu yule kwa kumdanganya.

“Karibu sana ndugu Pascal…natumaini chumba chako kimeshaandaliwa. Ni oda iliyotolewa na mzee salum Zakwa” mhudumu yule akamwambia Vasco. Ni kweli kwamba alikuwa ameshawekewa chumba kama alivyojulishwa kwenye simu.

“Ahsante sana,” Vasco akasema huku akiona kuwa ile ilikuwa ni kulazimishwa kukaa sehemu ile bila ridhaa yake! Lakini hakuwa na la kufanya zaidi ya kukubali!











ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog