Search This Blog

Saturday, 5 November 2022

SURA MBILI - 5

  





    Simulizi : Sura Mbili

    Sehemu Ya Tano (5)





    ********

    “Sawa, chumba hicho ni namba 12. Naona hicho kinakufaa sana bosi wangu, maana kina kila kitu ndani. Nafikiri ukikiona utakifurahia,” mhudumu yule aliendelea kumwambia Vasco Nunda.

    “Poa, nipeleke…kitanifaa tu.”

    Masoud Kipengo akachukua kitabu kikubwa cha wageni na kuanza kupekua kurasa zake na kumuorodhesha kama mteje mpya aliyekuwa amefika pale siku hiyo. Akachukua kalamu na kuanza kuandika kwa kumuuliza:

    “Unaitwa nani?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Naitwa Pasco Memba…” Vasco Nunda akasema kwa kudanganya jina kama alivyobatizwa na Salum Zakwa!

    “Unatokea wapi?”

    “Natokea Magomeni…”

    “Namba za simu?”

    “Namba za simu ni 0655…” Vasco Nunda akaandika namba za uongo!

    Mhudumu Masoud Kipengo aliendelea kumwandika Vasco Nunda kumbukumbu zake katika kitabu hadi alipomaliza na kumwambia kuwa waelekee ndani ya chumba namba 12., ili wakakikague. Wakaondoka wote na kwenda kukiangalia kile chumba ambacho kilikuwa mwisho kabisa, sehemu iliyojificha. Baada ya Masoud kukifungua, Vasco akakiangalia na kuona kuwa kulikuwa na kitanda kikubwa cha futi sita kwa sita kilichotandikwa shuka nzuri, na juu yake kukiwa na mito miwili, kiti kimoja, meza, kabati la nguo lililokuwa ukutani, friji dogo, simu ya maungio ya ndani kwa ndani, na runinga ndogo pia.

    Juu darini palikuwa na pangaboi ambalo kwa muda ule lilikuwa linafanya kazi na kuifanya hali ya pale ipendendeze na kulifukuza joto lililokuwa linafukuta kule nje.Vilevile huduma za choo na bafu zilikuwa mlemle ndani. Vasco Nunda akaridhika nacho!

    “Ok, nimeridhika nacho…” Vasco Nunda akamwambia Masoud Kipengo aliyekuwa akimsubiri amwambie kama ameridhika nacho ama la.

    “Kama umeridhika sawa…” Masoud Kipengo akamwambia kisha akaondoka kurudi kule mapokezi na kumuacha mle chumbani.

    Vasco Nunda akakaa pale kwenye kiti na kuanza kuwaza juu ya yeye kuamriwa kuondoka nyumbani kwake, Kinondoni, na kukimbilia Bangaiza Gesti kujificha. Kwa vyovyote alifahamu kwamba bosi wake, Salum Zakwa, alikuwa na agenda ya siri kutokana na uamuzi wake wa kumtaka ahame nyumbani kwake, na kupanga gesti. Akiwa ni mtu hatari na Mafia, kwa vyoyote alitaka kumdhuru! Hata hivyo Vasco alijipa moyo kuwa kamwe asingemuweza, atamsubiri palepale, na akiwa ni mtoto wa mjini, asingemuweza! Akachukua simu yake na kumtafuta, ili amjulishe hatua aliyofikia.



    ********

    Askari polisi walifika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kukiwa kumeshapambazuka. Kama kawaida walikuwa wameongozana, wakiwepo wataalam wa alama za vile, picha na milipuko, na walifika wakiongozwa na Kachero Inspekta Raymond Gopi. Baada ya kufanya uchunguzi wao, waligundua kuwa muuaji alikuwa ni yuleyule aliyeua watun wawili na polisi walikuwa wakimsaka mtu huyo kwa udi na uvumba kutona na ukweli kwamba atakuwa na siri kubwa sana!

    Kachero Inspekta Raymond alimwita mmoja wa Madaktari waliovamiwa na mwuaji ndani ya chumba kile cha upasuaji aweze kumhoji kwa kina, kwani upelelezi wake aliamua kuuanzia palepale huwenda akapata fununu. Daktari yule aliyekuwa amevalia saer za kazi, alimwendea Raymond na kukaa katika benchi moja lililokuwa pale katika veranda.

    “Jina lako nani?” Inspekta Raymond alimuuliza.

    “Naitwa Dokta Jonas Msimbe…”

    “Vizuri Dokta Msimbe. Sijui unaweza kunielezea tukio zima lilivyokuwa?”

    “Ndiyo, mimi nakumbuka tulikuwa tunamhudumia yule majeruhi aliyepigwa risasi, lakini cha kushangaza ni kwamba tulivamiwa na mtu mmoja aliyekuwa na bastola, halafu akatupa amri ya kunyoosha mikono yetu juu!

    “Baada ya hapo…”

    “Ikatubidi sis tutii amri ile na kunyoosha mikono juu, huku tumegeukia ukutani. Halafu mtu yule akamsogelea yule majeruhi na kumpiga risasi kasha akatokomea zake!”

    “Alikuwa amevaa nguo gani?”

    “Alikuwa amevalia suti nyeusi…”

    “Ukimwona tene unaweza kumkumbuka?”

    “Kwa kweli sitoweza kumkumbuka kwa sababu alituingilia ghafla!”

    “Nashukuru sana…” Kachero Inspekta Raymond akaendelea kuwahoji wale wengine, ambao nao walieleza vilevile kama alivyoeleza Dokta Jonas Msimbe. Hakika hakupata cha maana zaidi, kwani alijua kuwa madaktari wale walipovamiwa walikuwa wameshachanganyikiwa na kushinwa kumtambua muuaji!

    Alipomaliza kuwahoji, Kachero Inspekta Raymond, aliwaaga madaktari wale na kuondoka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, na kuelekea kwenye kituo chake cha kazi, katika Kitengo cha Kupambana na Wafanyabiashara wa Dawa za Kulevya, Kurasini, jijini Dar es Salaam. Yeye Raymond alikuwa ameamua kuuanza upelelezi mara moja, katika sehemu zote yalipofanyika mauaji yale usiku wa kuamkia siku hiyo.

    Akiwa ni askari shupavu mwenye kuijali kazi yake, hakupenda kuzembea na ilikuwa ni kazi mtindo mmoja, kamwe hakuuthamini usingizi wakati watu walikuwa wanakufa ovyo. Na kuhusu mchumba wake, Maria, aliyekuwa na wivu wa kupindukia, alimuweka kando kwa muda. Alipanga kuwa wakati wa mapenzi ni mapenzi, na wakati wa kazi ni kazi! Huo ndiyo utaratibu aliojiwekea!

    Baada ya kufika ofisini kwake, Raymond aliwaita makachero, Benito, Dani, ambao alikuwa ameanza nao operesheni ile tokea mwanzo, na kachero mwingine, Maiko, ambaye ni dereva, tayari kwa kupanga mkakati wa kazi. Haikuchukua muda mrefu, makachero wale wakafika na kukaa katika viti, wakitazamana na Raymond, tayari kwa kupokea maelekezo.

    “Jamani, ndiyo hivyo,” Kachero Inspekta Raymond akaanza kuwaeleza. “Bado operesheni yetu inaendelea, kila mmoja awe tayari. Na inaanzia sehemu ile ya kwanza palipotokea mauaji, Magomeni Mapipa, mtaa wa Kisangilo…”

    “Ni sawa mkuu,” Benito, Dani na Maiko wakasema.

    “Ok, kuna mtu yeyote ana swali kabla ya kuuanza upelelezi wetu?”

    “Hakuna afande, sisi tuko tayari kwa kazi!” Benito akasema.

    “Kama mko tayari, haya twendeni!”

    Bila kupoteza muda, makachero wale wakatoka pale ofisini wakiwa na silaha zao vibindoni. Kwa hatua za haraka wakaliendea gari lililokuwa kule nje, sehemu ya maegesho katika uwanja mdogo uliokuwa mbele ya kituo. Ni gari aina ya Totota Land Cruiser Hard Top, lenye namba za kiraia, ambalo ni maalum kwa ajili ya kikosi kile. Nje, wingu zito la mvua lilikuwa bado limetanda angani huku pia manyunyu ya mvua yakishuka taratibu, lakini hali hiyo haikuwatisha makachero wale washindwe kuifanya kazi yao. Wakapanda gari na kuondoka, dereva akiwa ni Kachero Maiko, aliyekuwa mzoefu katika hekaheka zile, ambapo alilitia moto na kuelekea Magomeni Mapipa.



    ********

    Foleni ya magari barabarani ilikuwa imefungamana asubuhi hiyo. Mvua nayo ilikuwa inaonyesha ingeweza kuanyesha wakati wowote, kwani wingu zito jeusi lilikuwa limetanda juu ya anga la jiji la Dar es Salaam. Salum Zakwa alikuwa ndani ya gari lake aina ya Ranger Rover Vogue, katikati ya magari yaliyokuwa katika foleni ile, Barabara ya Bibi Titi Mohamed, akielekea ofisini kwake.

    Ingawa alitakiwa aendeshwe na dereva wa, akiwa ni Mkurugenzi, lakini hakufanya hivyo, kwa kuhofia asiweze kugundulika mipango yake aliyokuwa anaipanga kwa muda ule, hivyo akampumzisha dereva awe anafanya kazi za kiofisi tu, na yeye akatumia gari lake binafsi.

    Japokuwa foleni ile ilimpotezea muda mwingi sana, lakini Kamba hakujali, hasa kutokana na mawazo yaliyokuwa yanamuandama. Ni kuhusu ile operesheni yake aliyokuwa akiiendesha juu ya kuwaangamiza adui zake, kiasi kwamba haikwenda kama alivyotegemea. Ni hatari sana kwake, kama watu wale watakuwa hai, kwani mipango yake yote itakwenda mrama!

    Bosco Zambi alikuwa amefanikiwa kutoroka kabla hajauawa, na pia, naye Vasco Nunda anatakiwa auawe, kwani hakustahili kuishi, vilevile wao ndiyo wanaijua siri nzima kuhusika kwake na biashara ya dawa za kulevya. Wakati akiwa katika mawazo yale, mara simu yake ya mkononi ikaita, na alipoangalia namba za mpigaji, alikuwa ni Vasco!

    “Ohoo, Vasco…lete habari…” akamwambia.

    “Tayari nimeshamaliza kazi bosi…”

    “Tayari sivyo?”

    “Nimeshamlipua Liston!”

    “Nimeshazipata habari hizo…”

    “Na hapa naongelea Bangaiza Gesti.”

    “Ina maana sasa hivi unaongelea Bangaiza Gesti hapo Mwenge?”

    “Ndiyo..ninaongelea hapa…”

    “Safi sana…kazi nzuri. Lakini kuhusu Bosco tutampataje?”

    “Bosco kwa ajili ya nini bosi?”

    “Na yeye auawe, atatoa siri!”

    “Atakuwa ametoroka huyo!”

    “Ndiyo maana nakwambia atafutwe!”

    “Aisee?”

    “Ndiyo hivyo Vasco, hakuna jinsi.”

    “Oohps!” Upande wa pili Vasco Nunda alivuta pumzi ndefu na kuzishusha, kwa kuona bosi wao, Kamba, alikuwa analazimisha kitu fulani! Sasa angempata wapi Bosco Zambi wakati hajui sehemu alipokimbilia!

    “Tafadhali, Tekeleza hilo Vasco…kwaheri…” Salum Zakwa akamwambia. Halafu akakata simu baada ya kuona foleni ya magari inaendelea kusonga na magari yanatembea.

    Ukweli ni kwamba, Salum Zakwa aliona kuwa mipango yake inakwenda mrama, na muda siyo mrefu siri ile inaweza ikalipuka kuwa alikuwa anajihusisha na biashara ile haramu ya dawa za kulevya, wakati akiwa ni mtu mzito, kigogo, serikalini!

    “Ni lazima nimteketeze Vasco!” Salum Zakwa akajisemea moyoni. “Huyu anaweza kuja kutoa siri kwa polisi ambao watakuwa wananitafuta mimi. Nikishamuua, namsaka Bosco Zambi mimi mwenyewe ili kuuficha ukweli huu!”

    Ukweli ni kwamba Salum zambi alikuwa ameamua kuingia mwenyewe kazini ili kumsaka Bosco. Kwa vile alikuwa ni mwanajeshi, ambaye amepata mafunzo mbalimbali ya medani za kivita, namna ya kutumia silaha za aina mbalimbali na ujasiri. Hivyo kwa mtu kama Vasco Nunda asingemsumbua kichwa chake kabisa! Ni kumsambaratisha! Mara baada ya kumaliza kuongea na Vasco Nunda, Salum Zakwa akaendelea na safari yake ya kuelekea ofisini.



    ********

    Saa nne kasorobo za asubuhi, makachero, Inspekta Raymond, Dani, Benito, na dereva, Maiko, walikuwa wameshafika Magomeni Mapipa, mtaa wa Kisangilo. Huu ni mtaa mrefu unaoanzia upande wa kaskazini na kukatisha barabara ya Morogoro, kuelekea upande wa kusini, kuishia katika bonde la Jangwani. Gari likapaki pembeni, mwa mtaa ule, halafu wakashuka na kuiendea nyumba ya marehemu John Peka, aliyeuawa usiku.

    Asubuhi ile kulikuwa kumepambazuka bado kukiwa na mvua kidogo, isipokuwa ni wingu zito kutanda angani, na baadhi ya watu walidiriki kuvaa makoti. Mtaa mzima wa Kisangilo ulikuwa umepigwa na butwaa kwa wakazi wengi kupata taarifa za mauaji ya kijana, John Peka. Watu walikuwa wamekaa katika makundi wakijadili hili na lile, kila mmoja akisema lake kuhusiana na mauaji yale.

    Ni kijana aliyekuwa anafahamika sana kutokana na kuwa na nguvu za kiuchumi, na pia hakuwa na hiana ya kusaidia wale waliokuwa na shida, hususan vijana, hasa mateja yaliyokuwa yamejazana yakibwia unga. Pia, aliwasaidia wazee na watoto waliokuwa wanaishi katika mazingira hatarishi.

    Katika nyumba ya John Peka, palikuwa pamejaa watu wengi, kuonyesha kuwa palikuwa na msiba. Baada ya kuifikia nyumba ile, makachero wale wakatoa pole kwa wafiwa, halafu Raymond akaomba kuonana na Mary Mshanga, mke wa John Peka, aliyekuwa amekaa na baadhi ya ndugu na majirani wakimfariji pale sebuleni. Mary aliyekuwa na huzuni kubwa, alikuwa pia amejitanda khanga, hivyo baada ya kuombwa kuonana na Kachero Inspekta Raymond, alikubali halafu wakaendakukaa sehemu ya faragha, uani.

    “Kwanza kabisa, pole kwa msiba uliokupata…” Kachero Inspekta Raymond akamwambia.

    “Ahsante sana…” Mary Mshanga akasema huku machozi yakimtoka, naye akawa anayafuta kwa upande wa khanga.

    “Mimi ni Kachero Inspekta Raymond, nimekuja hapa kuhusiana na mauaji ya mume wako…”

    “Ni sawa…sijui nikusaidie nini…”

    “Kwanza kabisa unaweza kukumbuka tukio zima lilivyokuwa?”

    “Ndiyo, nakumbuka…”

    “Hebu nieleze…”

    “Kwanza kabisa kabla ya mume wangu hajauawa, tuliongea mengi sana. Jana usiku tulikuwa tumekaa sebuleni kama kawaida yetu baada ya kula chakula cha usiku. Lakini nikamwona hakuwa na raha kama kawaida yake, hivyo ikanibidi nimwulize kulikoni Akaniambia kuwa, kuna mzigo mmoja uliokuwa unatoka nje ya nchi, ambao umekamatwa uwanja wa ndege, pamoja na vijana waliokuja nao. Sasa wao ndiyo wanatuhumiwa kuwa walivujisha siri na mzigo huo ukakamatwa!”

    “Walikamatwa lini?” Kachero Inspekta Raymond akamuuliza Mary.

    “Walikamatwa juzi…”

    “Unafikiri ulikuwa ni mzigo gani huo?” Kachero Inspekta Raymond akamwuliza huku akianza kuuona mwanga kwa mbali juu ya upelelezi wake.

    “Kwa kweli sielewi,” Mary alisema huku akificha, kwani alifahamu fika yalikuwa ni dawa za kulevya, biashara aliyokuwa anaifanya mume wake!

    “Na huyo bosi wao ni nani?”

    “Simfahamu!”

    “Jina lake je?”

    “Anaitwa Zakwa…”

    “Jina la Zakwa tu?”

    “Nafikiri ni Zakwa …kama sikosei…simjui kivingine!”

    “Ni Zakwa yupi huyo?”

    “Ndiyo maana nikakwambia mimi simfahamu zaidi ya jina hilo!” Mary akasema kwa kusisitiza, na kweli Raymond akaona kwamba ni kweli alikuwa hamfahamu mtu huyo!

    Hata hivyo, Kachero Inspekta Raymond alikuwa anamfahamu Salum Zakwa, kwamba ni mmoja wa vigogo serikalini, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Udongo. Hata hivyo, Raymond hakumshtua zaidi, bali aliendelea kumhoji ili kupata ukweli wa sheshe lile!

    “Ndiyo mama…tuendelee…” Kachero Inspekta Raymond akamwambia Mary kwa sauti ya upole.

    “Baada ya marehemu kunieleza vile, nikamwacha amekaa pale sebuleni akiangalia runinga, akiwa pamoja na watoto wetu wawili. Nikaingia chumba cha watoto kuwatandikia vitanda ili wapate kulala. Wakati nikiwa kule chumbani, kumbe huku nyuma aliingiliwa na watu wawili waliokuwa na silaha, ambao walikuwa wamevalia miwani mieusi. Ndipo walipompiga risasi na kumwua!”

    “Oh, pole sana…kwa hivyo huwezi kuwatambua watu hao ukiwaona tena?”

    “Kwa kweli siwezi kuwatambua, kwani walikuwa wamevaa miwani mieusi, na pia nilikuwa na woga wa kuwaangalia.”

    “Ok,” Kachero Inspekta Raymond akasema huku akiandika kwenye kijitabu chake, halafu akamalizia kwa kusema. “Sasa sisi tunatoka, kama tutakuhitaji tena, basi tutakuja kwa mahojiano…”

    “Sawa, afande,” Mary akasema huku wakipeana mkono na Raymond.

    Alipomaliza kumhohji Mary, mke wa marehemu, John Peka, Kachero Inspekta Raymond alitoka mle ndani na kuwafuata, Benito, Maiko na Dani, waliokuwa wakimsubiri. Baada ya kuwafikia, akawaambia waelekee Kinondoni, mtaa wa Sekenke, nyumbani kwa kijana, David Osmond, ambaye naye alikuwa ameuawa jana yake. Wakapanda ndani ya gari, ambapo Kachero Maiko aliliondoa kuelekea Kinondoni, kwa kuifuata Barabara ya Kawawa, baada ya kuiacha ile ya Morogoro.

    Hatimaye wakafika Kinondoni, mtaa wa Sekanke, ambapo walivutiwa na watu wengi waliokuwa wamejaa kwenye nyumba ile ya David Osmond, na hata vilio viliweza kusikika kutoka kwa ndugu na jamaa. Kachero Inspekta Raymond akamwambia Maiko asimamishe gari kando ya barabara, hatua chache kutoka katika nyumba ile.

    Vilevile mbele ya nyumba ile, palikuwa na magari mengine ya jamaa za marehemu yaliyokuwa yamepaki kando ya mtaa huo mna kufanya msongamano kiasi. Wote wakashuka ndani ya gari na kuiendea nyumba hiyo, ambapo kama kawaida walitoa pole kwa wafiwa na kumhitaji mke wa marehemu, aliyejulikana kwa jina la Debora. Debora akatoka akiwa na huzuni kubwa ya kufiwa na mumewe, tena kwa kifo cha kinyama. Hivyo Raymond alimwita pembeni sehemu tulivu kwa ajili ya maongezi.

    “Pole sana kwa msiba,” Kachero Inspekta Raymond akasema huku akimwangalia Debora.

    “Oh, ahsante sana…” Debora akasema huku akilia kwa uchungu na kuongeza. “Wameniulia mume wangu…ooh!”

    “Pole sana.”

    “Ahsante.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Naomba nikuhoji kidogo. Mimi ni Kachero Inspekta Raymond na wale watatu tuliokuja nao ni wenzangu.”

    “Sawa…oh…oh!”

    “Hebu nieleze tukio zima…”

    Úsiku wa jana tulikuwa tumelala mimi na mume wangu. Lakini katikati ya usiku tukasikia mbwa wetu, Simba, akibweka ovyo. Ndipo mume wangu alipotoka nje kuangalia kuna kitu gani kinachomfanya mbwa apige kelele. Baada ya muda ndipo niliposikia vurugu za wale vurugu za watu waliokuwa wanapigana kule nje…” Halafu akaendelea kulia. “Ndipo nilipotoka nje,” akaendelea kusema Debora. “Kutoka tu, nikakuta mume wangu ameuawa kwa kupigwa risasi, pamoja na mbwa wetu…”

    “Je, ulifanikiwa kuwaona hao watu?”

    “Nilipotoka nje, niliwaona watu waili waliokuwa wamevalia nguo nyeusi, wakiruka uzio na kupotea kwa kutumia gari lao, ambalo walikuwa wamelipaki nje.”

    “Kwani marehemu alikuwa na ugomvi nao?”

    “Inawezekana…kwani mume wangu alikuwa na wasiwasi sana, akisema kuwa bosi wao amewatuhumu kwamba wamemgeuka kibiashara.”

    “Walikuwa wanafanya biashara gani?”

    “Kwa kweli sijui walikuwa wanafanya biashara gani…”

    “Je, unamfahamu huyo bosi wao?”

    “Nasikia ni mtu mkubwa serikalini.”

    “Jina lake je?”

    “Silifahamu…hiyo ilikuwa siri yake.”

    “Kwani walikuwa wanafanya biashara ya siri sana mpaka wajifiche kiasi hicho?”

    Kachero Inspekta Raymond alimwelewa Debora. Alifahamu fika kuwa wote walikuwa wakijihusisha na biashara ile haramu ya dawa za kulevya. Katika upelelezi wake alianza kupata mwanga na chanzo cha mauaji, ambayo yalikuwa ni kuwaziba mdomo wasije wakatoa siri pindi watakapokamatwa. Baada ya kumaliza kumhoji, Makachero Inspekta Raymond, Benito, Dani na Maiko, dereva, wakapanda gari na kuondoka katika eneo lile la Kinondoni. Waliamua kuelekea Barabara ya Morogoro, eneo lile alipookotwa Liston Kihongwe, baada ya kupigwa risasi na Bosco zambi, aliyekuwa anaishi katika maghorofa ya Shirika la Nyumba la Taifa, eneo la Faya. Baada ya kufika, Maiko akalipaki gari mbali kidogo na maghorofa yale, halafu wakashuka garini na kuelekea katika ghorofa lile, ambapo walipanda hadi juu ghorofa ya tatu, ambalo ni eneo alilokuwa anamiliki Bosco peke yake, na hakukuwa na mtu zaidi ya kuukuta mlango umefungwa.

    Katika ngazi, sakafuni, palikuwa na damu mbichi iliyoganda, ambayo ni ya Liston Kihongwe, aliyekuwa amepigwa risasi na Bosco Zambi usiku ule walipokuwa wamekwenda kumvamia. Hakika baada ya kufanya uchunguzi kidogo, hapakuwa na dalili zozote za kuwepo kwa mtu, wakajua kwamba alikuwa ametoroka kukimbilia sehemu isiyojulikana.

    Hivyo basi, Kachero Inspekta Raymond, akaomba msaada wa askari polisi wawili kutoka kituo Kikuu cha Polisi, kwa ajili ya kulinda eneo lile, ushahidi usiharibiwe. Baada ya askari wale kupatikana na kukabidhiwa lindo hilo, ndipo wao wakaondoka na kurudi ofisini kwao, Kurasini.

    Na ile ilikuwa ni kwa ajili ya kwenda kukaa kikao na kupanga mkakati, na kupanga makachero maalum wa kumfuatilia Salum Zakwa nyendo zake, na kila sehemu anapoelekea. Kwa vyovyote alikuwa ameshamshtukia na kumhusisha na matukio yale, ila isingewezekana kumkamata bila kuwa na ushahidi wowote!

    ********

    Hali ya mvua nyepesi za manyunyu, pamoja na baridi, vilikuwa vimetanda katika mji wa Morogoro. Upande wa kusini Mashariki, milima yote, ambayo ni kivutio kinachoijenga mandhari nzuri ya mji ule, ilikuwa imezungukwa na ukungu mweupe. Bosco na mpenzi wake, mwanadada mrembo, Marieta, walikuwa wameshafika mjini Morogoro tangia alfajiri ya siku ile, baada ya kukimbia kutoka jijini Dar es Salaam.

    Kitu cha kwanza baada ya kufika, Bosco alikwenda kulipaki gari lake, Nissan Murano, kwenye kituo cha mafuta, kilichoka eneo la Msamvu, ambapo pale anafahamika sana na mmiliki wa kituo kile. Na ile ilikuwa ni kwa ajili ya kulificha kwa usalama zaidi kama walikuwa wanamfuatilia. Baada ya kulihifadhi gari, ndipo walipokwenda kutafuta nyumba ya wageni, ijulikanayo kwa jina la Nyota Njema Gesti, iliyoko eneo lile la Msamvu, siyo mbali sana na Kituo cha Mabasi yanayotoka na kwenda Mikoani.

    Ni nyumba ambayo ilikuwa na hadhi kubwa, hasa kutokana na kutoa huduma nzuri na hali ya utulivu iliyokuwepo. Ni mara nyingi, Bosco alikuwa anafikia katika nyumba ile, hasa anapokuwa katika shughuli zake za kibiashara, hivyo ni sehemu aliyokuwa anafahamika sana. Walipatiwa chumba kizuri, kilichokuwa na kitanda kikubwa cha futi sita kwa sita, sofa moja lenye uwezo wa kukaliwa na watu watatu, na huduma zote, kama choo na bafu ndani, runinga, friji lenye vinywaji vya kila aina bila kusahau huduma za simu.

    Asubuhi hiyo baada ya kuoga, kupata kifungua kinywa na kupumzika vya kutosha, ndipo Marieta alipoanza kumdadisi Bosco juu ya wao kukimbilia pale Morogoro, wakitokea jijini Dar es Salaam, bila kupewa maelezo ya kina, zaidi ya kukimbia kama wakimbizi!

    Muda huo, Bosco alikuwa amekaa kwenye sofa, na Marieta alikuwa amekaa juu ya kitanda, amejfunga taulo kubwa, karibu nusu ya mwili, kwani hakuwa na nguo nyingine za kubadili, na pia hakutegemea kutoka nje ya chumba kile, kwani huduma zote walizipata mlemle. Muda wote Marieta alikuwa akimwangalia Bosco bila kummaliza, tuseme hakumwelewa!



    ********

    “Bosco mpenzi wangu…” Marieta akamwita kwa sauti ndogo.

    “Naam…” Bosco akamwitikia huku mawazo yake yakiwa mbali sana.

    “Nafikiri tumeshafika Morogoro…hebu naomba unieleze kinachoendelea, kwani unanitia wasiwasi sana…”

    “Wasiwasi wa nini Marieta?” Bosco akamuuliza.

    “Lazima niwe na wasiwasi…kwa nini tuje kujificha gesti?”

    “Ni kama nilivyokwambia mwanzo. Ni historia ndefu mpenzi…”

    “Historia ndefu? Kwani haielezeki?”

    “Inaelezeka!”

    “Haya, nielezee ili na mimi moyo wangu utulie ati!”

    “Ni kwamba, watu wale walikuwa wananitafuta mimi usiku ule, ili waniue!”

    “Unatafutwa uuawe?”

    “Ndiyo hivyo,” Bosco alisisitiza. “Ndiyo maana nikawawahi usiku wa jana kabla wao hawajaniwahi mimi!”

    “Mungu wangu! Mnagombania nini?”

    “Biashara tu, tena biashara ya ‘unga haramu!’ Bosi wetu ni ‘Zungu la unga’. Tena mtu hatari sana. Hasiti kuitoa roho ya mtu anayekatiza katika anga zake, kwa minajili ya kumharibia!” Bosco akaamua kutoboa!

    “Ina maana Bosco, una uhusiano na wauza dawa za kulevya? Basi wakitugundua tumejificha humu ndani, ujuen tumekwisha!” Marieta akasema huku akiwa na wasiwasi wingi.

    “Usiwe na wasiwasi, watu wale hawaniwezi kamwe!”

    “Hapana Bosco, mimi sitaki matatizo. Naomba nauli nirudi Dar es Salaam, wewe baki hapa Morogoro mpaka hali itakapopoa…” Marieta akataharuki!

    “Usiwe hivyo Marieta, ina maana na wewe unanisaliti? Au hunipendi? Si ndiyo maana yake?”

    “Mimi nakupenda Bosco,” Marieta akasema na kuongeza. “Na wewe unaelewa hilo kwa nakupenda, lakini kitendo cha kufukuzana na vyombo vya dola, siyo kitu kizuri. Cha muhimu wewe niruhusu niondoke nikaendelee na kazi zangu za Saluni!”

    “Marieta, utakuwa unanivunja moyo, kwani huu ni wakati muafaka wa wewe kunifariji. Isitoshe, kwani katika Saluni yako si kuna wafanyakazi wa kutosha. Pia, hapa nilipo nina fedha nyingi za kutosha, kama shilingi milioni sita hivi…”

    “Hata kama una mamilioni ya shilingi, sasa tutakuwa tunaishi humu ndani kama vile ni wakimbizi? Halafu pia, siwezi kuwaamini wafanyakazi wangu wa saluni, kwani ni lazima wasimamiwe! Nielewe Bosco!”

    “Mh,” Bosco akaguna bila kuongeza chochote.

    Halafu akanyanyuka na kusimama kama vile mtu aliyechanganyikiwa, kisha akaliendea dirisha lililokuwa upande wa kusini mwa chumba kile. Akalifungua pazia na kuchungulia nje, ambapo hakuona chochote zaidi ya uzio wa ukuta wa gesti ile, na mabati ya nyumba za jirani.

    Pia, aliwza kuiona ile safu ya milima mirefu, iliyokuwa na ukungu mweupe, ambayo iliyouzunguka mji wa Morogoro. Baada ya kuchungulia kwa muda kule nje, akalifunga kama lilivyokuwa mwanzo. Akarudi na kukaa kwenye sofa na kuendelea kumwangalia Marieta.

    “Mbona hueleweki Bosco? Hebu nijibu nilichokwambia!” Marieta akamwambia! Akazidi kumchanganya Bosco!

    “Sikiliza Marieta…” Bosco akamwambia huku akitetemeka kwa hasira zilizoonyesa wazi!

    “Nakusikiliza…” Marieta akamwambia huku akilirekebisha lile taulo kubwa alilokuwa amejifunga.

    “Unajua mpaka sasa unajifanya hunielewi nachosema! Nakubembeleza lakini naona unakataa, sasa ukileta mchezo nakumaliza sasa hivi! Unatakiwa kufuata amri yangu!” Bosco akasema huku akinyanyuka na kuuendea mkoba wake, ambapo alitoa bastola iliyokuwa ndani yake. Halafu akaikoki na kuingiza risasi chemba!

    “Mh!” Marieta akaguna na kumwangalia Bosco kwa hamaki!

    “Hii bastola ina sailensa… haitoi sauti.” Bosco akaendelea kumwambia marieta na kuongeza. “Hivyo mimi nitakumaliza humu ndani halafu naishia zangu!”

    “Umefika mbali Bosco. Wewe ni mpenzi wangu wa muda mrefu, na sasa inakuwaje leo unanitishia bastola?” Marieta akamwuliza huku akinyanyuka kutoka pale juu ya kitanda alipokuwa amekaa.

    “Unajua kuwa mimi nimeshachanganyikiwa, naomba utulie mpenzi wangu…” Bosco akamwambia Marieta huku akiwa amepunguza munkari. Halafu akamkalisha tena Marieta pale juu ya kitanda. Baada ya mabishano yale, Bosco na Marieta, walitulia kidogo kila mmoja akiwa na mawazo yake, Bosco akifikiria jinsi ya kujinasua katika janga lile na Marieta aliwaza mbinu za kumtoroka na kurudi jijini Dar es Salaam.

    Mchana ulipofika, kama kawaida, Bosco aliagiza chakula kutoka hotelini, na mhudumu akawapelekea. Wakaendelea kula huku wakishushia na vinywaji, Marieta akinywa mvinyo laini na Bosco akinywa bia aina ya Castle. Kwa muda wote walikuwa wamekaa sambamba, na ili kumlainisha Marieta asiweze kumtoroka, Bosco alianza kumpapasa na kumpiga mabusu mfululizo, na hata kula denda!

    Ni kitendo ambacho kilimlainisha Marieta, akiwa kama mwanamke, wakajikuta wakihamia kitandani wakiwa watupu, kwani hawakuwa na nguo, zaidi ya Marieta kujifunga taulo na Bosco halikadhalika. Akiwa ni mtaalam wa hali ya juu, Bosco alimpa mapenzi ya hali ya juu, yaliyomwacha Marieta akigugumia ovyo kwa kutoa kilio cha mahaba, na walipomaliza shughuli pevu, wakaelekea ndani ya bafu lililokuwa mle ndani na kujimwagia maji wakiwa wote, kwani Bosco hakutaka kumwachia mwanya! Alijua akifanya kosa tu, basi ataachwa kwenye mataa!

    Hatimaye baada ya kumaliza kuoga, wakarejea tena pale chumbani na kuendelea kunywa pombe, bia, ambazo zilikuwa mle ndani ya friji dogo. Ni pombe ambazo ziliwekwa kwa bili maalum ambayo mteja atakuwa ametoa, na kwa Bosco aliyekuwa mwenyeji ndani ya nyumba ile, alikuwa ameshatoa oda ya kuwekewa vinywaji anavyotumia.

    Kwa kipindi chote kile walichokuwa wamekaa ndani ya chumba kile, Bosco alijua kwamba Marieta asingekuwa na hamu ya kuondoka tena, bali wangebaki wakifarijiana kadri walivyokuwa wakijisikia. Kumbe haikuwa hivyo, wazo la Marieta lilikuwa ni moja tu, ni lazima amtoroke Bosco na kurejea Dar es Salaam kuendelea na shughuli zake!



    ********

    Majira ya saa nane za mchana, siku ile ya aina yake, iliyoambatana na mauaji ya kutisha ndani ya jiji la Dar es Salaam, Kachero Inspekta Raymond na wenzake, Benito, Dani na Maiko, walikuwa wamekaa ofisini wakipanga mikakati ya kazi. Na ile ni baada ya kutoka kufanya upelelezi kwa wahanga wote wa tukio lile, marehemu, John Peka, David Osmond na Bosco Zambi, aliyetoroka. Raymond aliwaangalia wote, halafu akavuta pumzi ndefu na kuuvunja ukimya uliokuwa umetanda na kusema:

    “Nimeona ni vizuri tukutane tena…” akawaambia na kuongeza. “Ili tuelezane kinachoendelea katika upelelezi nilioufanya kwa muda mfupi. Nimegundua kuwa mauaji yote yanayotokea, yamefanyawa na mhusika mkuu wa biashara ya dawa za kulevya, ambaye ni mmoja wa watu wazito serikalini. Pia, wale vijana watatu, Roki, Joe na Bomeza tuliowakamata Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, wakitokea nchini Pakistani na dawa za kulevya, wanahusiana na bosi huyo…” Raymond akanyamaza kidogo na kuendelea kuwaangalia kama walimwelewa.

    “Na mkubwa huyo,” akaendelea kusema Raymond. “Ndiye aliyeamuru John na David wauawe kwa kile alichosema walikuwa wamemchoma na kutoa taarifa kwetu ili wakamatwe. Sijui mmenielewa?”

    “Tumekuelewa afande…” Benito akasema.

    “Tupo wote afande,” Dani naye akasema.

    “Tunakuelewa afande,” Maiko naye akaongeza kusema.

    “Lakini afande, je, mtu huyo amefahamika kwa jina?” Benito akauliza.

    “Ndiyo, nimemfahamu, na hata nyie wote mnamfahamu. Ni mtu mzito kwa sasa, baada ya kustaafu Jeshi la Wananchi wa Tanazania, na baadaye kuingia serikalini. Ni mheshimiwa Salum Zakwa!” Kachero Inspekta Raymond akasema.

    “Mh, ni Salum Zakwa?” Benito akahoji.

    “Ndiye huyo!” Akasema Raymond na kuongeza. “Msishangae, ndiyo maana nimewaita hapa ukizingatia tuna kazi nzito mbele yetu. Kwa hivyo kuanzia kesho asubuhi wote watatu mtafanya kazi ya kumfuatilia mtu huyo nyendo zake, ambapo chochote mtakachokiona mtanijulisha kwa simu. Na hii tutafanya kama tulivyowafuatilia wahalifu wengine mpaka tulipowakamata katika ile operesheni ya pili, tokea operesheni hii maalum dhidi ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya ilipoanzishwa rasmi.”

    Kachero Inspekta Raymond akanyamaza kidogo, halafu akaongeza kusema, “Natumaini nyote mnafahamu anapoishi Salum Zakwa, au sivyo?”

    “Tunapafahamu, anaishi eneo la Sea View, Upanga, hakuna asiyepafahamu,” Maiko akasema.

    “Vizuri sana, sasa kwa vile mtatumia lile gari letu, Toyota Land Cruiser, lenye namba za kiraia, na dereva, Maiko, wasiliana na mtu wa kisima cha mafuta, uhakikishe limejazwa mafuta leo hii hii, na kesho ni kuamkia kumfuatilia tu bila kumuachia nafasi hata kidogo,” Kachero Inspekta Raymond akaendelea kusisitiza.

    “Sawa afande, nitafanya hivyo,” Kachero Maiko akasema.

    Baada ya kumaliza kupanga mipango ya kazi, wote waliagana na kila mmoja alielekea kwake. Cha muhimu kila mmoja alikuwa akiwazia kazi ile iliyokuwa inawakabili mbele yao, ya kupambana na, Salum Kamba, mtu mwenye taaluma kama yao. Alikuwa mwanajeshi!

    Hakika Kachero Inspekta Raymond, ambaye alikuwa ameivalia njuga opereresheni ile, alikuwa akijiuliza maswali kadhaa kichwani mwake, hasa kilichomuumiza kichwa ni juu ya kumpata Bosco Zambi aliyekuwa ametoroka na haijuliaki alipokimbilia baada ya kukoswa koswa kuuawa, na yeye kufanikiwa kujeruhi Liston kwa risasi. Kumbe kwa muda ule, alikuwa amejichimbia mjini Morogoro, akiwa na mpenzi wake, Marieta. Hata hivyo, alijua kuwa ni lazima atapatikana tu!

    ********

    Mpaka ilipotimu majira ya kumi za jioni, Bosco Zambi na Marieta walikuwa wamejichimbia ndani ya chumba chao walichopanga pale Nyota Njema Gesti. Walikuwa wakiendelea kunywa vinywaji taratibu. Kwa muda huo, Bosco alikuwa amepunguza wasiwasi kwamba, Marieta asingewea tena kumtoroka na kurudi Dar es Salaam, kama alivyokuwa amedhamiria. Alijua kuwa penzi alilokuwa amempa muda siyo mrefu, lilikuwa limemchanganya na kumfanya asahau kama kuna kutoroka!

    Kuhusu fedha za kutumia, Bosco hakuwa na wasiwasi kabisa, kwani alikuwa ametoroka na fedha nyingi tu, ambazo zingetosha kwa kufanyia matanuzi hata kwa mwezi mzima wakiwa pale mjini Morogoro. Pombe walizokuwa wanakunywa, ziliwafanya wawe wanatoka kwenda kujisaidia mara kwa mara katika choo kilichokuwa mlemle ndani ya chumba chao walichopanga. Sasa pale ndipo Marieta alipokuwa akipanga mpango wa kumtoroka Bosco, kwa kumvizia pindi atakapokwenda kujisaidia. Na kweli Bosco alipokwenda kujisaidia kwa mara nyingine, Marieta hakulaza damu, akaona ndiyo muda muafaka wa kumtoroka!

    Hivyo basi, Marieta akavalia nguo zake haraka haraka na kuuchukua mkoba wake uliokuwa na fedha, lakini aliviacha vile viatu virefu vya mchuchumio, halafu akaufungua mlango na kutoka ne ya chumba. Akaifuata veranda ndefu iliyotengenisha vyumba pande zote mbili na kuelekea sehemu ya mapokezi kwa tahadhari kubwa huku pia akiangalia nyuma. Pale mapokezi alimkuta mhudumu, mwanadada mmoja aliyekuwa akimhudumia mteje mmoja aliyekuwa amefika muda ule. Hakumsemesha zaidi ya kuendelea na safari yake huku akionekana mtu mwenye wasiwasi!

    “Vipi dada,” mhudumu yule akamuuliza.

    “Mimi naondoka anti…” Marieta akamwambia huku akiendelea kutoka nje!

    Mhudumu akamwacha na kuendelea kumhudumia mteja!

    Kumbe wakati Marieta alipokuwa akitoka nje, na ndiyo muda huo Bosco alikuwa akitoka chooni. Alipotupa macho yake pale kitandani, hakumwona Marieta, zaidi ya kuona viatu vyake tu vilivyokuwa sakafuni vimezagaa, hivyo akajua kuwa alikuwa ameteleza kama Kambale! Ni lazima m amemtoroka!

    Haraka, Bosco akavalia nguo zake, shati na suruali bila kuvaa viatu, ambavyo aliona vinampotezea muda tu. Na pia akaichukua bastola yake, ambayo aliichomeka nyuma kiunoni, upande wa mgongoni, kisha akutoka nje ya chumba na kuelekea sehemu ya mapokezi kwa mwendo wa kasi. Akamwona Marieta akiwa amesimama pale mapokezi akiongea na mhudumu wa sehemu hiyo, na alipojaribu kumwita, Marieta hakumwitikia zaidi ya kuanza kutoka nje kwa mwendo wa haraka huku akiwa pekupeku.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Naye Bosco akaamua kumfuata nyuma hadi alipotoka nje na kukimbilia kwenye uchochoro mmoja unaoingilia katikati ya nyumba zilizokuwa katika eneo lile la Msamvu. Wakati huo hali ya hewa ilikuwa shwari na ile mvua ilikuwa imekatika kwa muda ule. Hakika Bosco alikuwa amechanganyikiwa sana baada ya Marieta kufanikiwa kumtoroka.





    ********

    Marieta alipofika katika ule uchochoro, alianza kutimua mbio akiwa pekupeku bila kuvaa viatu, kwani hakuwa na muda wa kuvalia vile viatu virefu. Naye Bosco hakulaza damu, kwani alianza kumfuatilia nyuma akiapa kuwa angekuwa tayari hata kuitumia bastola yake iliyokuwa na kiwambo cha kuzuia mvumo, endapo asingesimama. Hatimaye wakatokeza katika mtaa mmoja uliokuwa na maduka na pilikapilika nyingi za watu.

    Watu wakashangaa kwa jinsi Bosco na Marieta walivyokuwa wanafukuzana, wengi wao wakidhani labda Marieta alikuwa amekula vya watu, sasa anatorokabila kutoa penzi kwa mtu husika! Marieta alikuwa anakimbia huku akipigana vikumbo na watu na hata pengine kujaribu kukwepa pikipiki za bodaboda zilizokuwa zikikatiza katika mtaa ule.

    Akaambulia matusi kwa baadhi ya madereva kwa kutaka kuwasababishia ajali isiyokuwa ya lazima! Hatimaye pumzi zikaanza kumwishia, akadondoka na kuanguka chini kwa kishindo! Bosco akamuwahi pale alipokuwa ameangukia na kumkusanya!

    “Shenzi sana!” Akamwambia kwa hasira!

    “Mama yangu!” Marieta akasema kwa hofu!

    “Marieta, tafadhali turudi gesti!”

    “Oh, mimi sirudi!” Marieta akasema!

    “Kwa nini hurudi?”

    “Mimi nakwenda Dar…oh!”

    “Haiwezekani!”

    Bosco akaanza kumvuta kwa nguvu ili warudi kule Nyota Gesti walipokuwa wamefikia. Lakini Marieta aliendelea kukaa chini, akikataa katakata kwa kugaragara ovyo. Wakati huo umati wa watu ulikuwa umewazunguka huku wakishangilia sakata lile na wengine walizomea kwa nguvu, wakisema:

    “Lipa vya watu!” Walisikika watu hao!

    “Mmezoea kuchuna mabuzi, haya sasa yamekutokea puani. Kakutana na mashine kubwa!”

    “Mabuzi mengine hayachuniki!”

    Watu waliongea mengi, lakini hawakujua kilichokuwa kinaendelea wala chanzo cha ugomvi ule. Katika purukushani ile na watu wengi kujaa, askari polisi wa doria walifika katika eneo lile mara moja. Askari wale walifika wakiwa katika gari lao aina ya Toyota Land Cruser, ambapo ndani yake walikuwepo askari sita waliokuwa na silaha. Askari polisi wawili wakashuka na kuwaendea Bosco na Marieta waliokuwa wakibiringishana pale chini, na Marieta akijitahidi kujiondoa mikononi mwa Bosco, aliyekuwa ameng’ang’ania nguo zake!

    “Jamani vipi?” Askari mmoja aliuliza!

    “Ah, huyu ni mpenzi wangu!” Bosco akamwambia yule askari.

    “Sasa mbona mnagombana na kuangushana? Nyie ni wapenzi kweli?” Askari wa pili akauliza.

    “Ndiyo, ni mpenzi wangu!”

    “Eti dada,” askari yule akamuuliza Marieta. “Huyu ni mpenzi wako?”

    “Ndiyo…ni wangu…”

    “Sasa mbona hivi? Mnatia aibu?”

    “Mimim nataka kurudi Dar, yeye ananizuia…”

    “Kwa nini anakuzuia?”

    “Ah….sijui…eer…” Marieta akasita kusema. Kitendo kile kikamtia wasiwasi yule askari!

    Ina maana nyie siyo wenyeji hapa Morogoro?”

    “Sisi tumetokea Dar es Salaam…” Marieta alijibu huku akionekana kusita na mwenye wasiwasi mwingi!

    “Aisee, hebu tuwapeleke kituoni hawa!” Askari polisi mmoja akamwambia mwenzake.

    “Na kweli, tena tumpekuwe kwanza huyu mwanaume!”

    “Njoo hapa!” Askari mmoja akamwambia Bosco. Bosco akasita kumwendea, kwani alikuwa na silaha, bastola kibindoni!

    Msala huo!

    “Nimefanya nini?” Bosco akauliza huku akirudi nyuma. Alifahamu wazi kwamba ni lazima angenaswa kwa vile pale alipo, alikuwa na bastola aliyokuwa anaimiliki isivyo halali!

    “Hutaki siyo?” Askari akamuuliza huku akimwendea na kumshika bega lake la kushoto. “Mikono juu!” Akamwambia!

    “Mikono ya nini juu? Kwani mimi mhalifu?” Bosco akaendelea kuuliza!

    “Lazima nikupekuwe!”

    “Huwezi!” Bosco akamwambia huku macho yake ameyatoa pima, tayari kwa kufanya lolote! Kisha akaupelekeka mkono wake mgongoni sehemu ilipokuwa ile bastola yake aliyoichomeka!

    Hakuwahi!

    Hata hivyo, askari polisi yule ambaye hakuwa na silaha, alimrukia Bosco ili ampokonye ile bastola! Wakapiga mweleka mzito na wote wakaanguka chini na kuanza kubiringishana na kulowana matope! Ule umati wa watu uliojazana ukaanza kushangaa na kupigwa na butwaa!

    Upande wa pili, wale askari polisi wengine, yule aliyekuwa naye na wale waliokuwa ndani ya gari wakaende na kusaidiana kumdhibiti Bosco. Wengine pia walimdhibiti Marieta asiweze kukimbia! Hakika kilikuwa ni kitimtim!

    Askari wale walifanikiwa kumdhibiti Bosco ingawa kwa taabu kwa ile naye alikuwa ni mtu wa mazoezi ya kujilinda. Pia, walifanikiwa kumpokonya ile bastola aliyokuwa nayo, ambayo risasi ilikuwa iko chemba tayari kwa kutumika! Wakawachukua wote na Marieta, wakawapakiza kwenye gari lao na kuelekea kule gesti walipokuwa wamepanga chumba ili kufanya upekuzi wa kina ndipo hatua nyingine zifuate!

    Walifika katika nyumba ile ya wageni ya Nyota Njema Gesti, ambapo mhudumu wa pale alitoa ushirikiano kwa polisi, ambapo walifanya upekuzi wa dharura ndani ya kile chumba walichokuwa wamefikia tokea alfajiri ya siku ile. Lakini hawakuambulia kitu kingine cha zida zaidi ya mkoba wa safari wa Bosco na baadhi ya vitu vingine kama viatu, simu za mkononi, ambazo hata hawakuwahi kuzichukuwa wakati wakiwa katika harakati za kukimbizana. Baada ya kukamilisha, wakawachukuwa na kuwapeleka kwenya Kituo Kikuu cha Kati cha Polisi, mjini Morogoro kwa hatua zaidi za kipolisi.

    Haikuchukua muda mrefu, baada ya kuhojiwa kwa kina na makachero waliokubuhu, iligundulika kuwa Bosco alikuwa ni mmoja wa wahusika wa matukio yale ya umwagaji damu na biashara haramu ya dawa za kulevya yaliyotokea jijini Dar es Salaam, na alikuwa akitafutwa na polisi kwa tuhuma zile. Na ile ilikuwa ni baada ya Marieta kueleza ukweli wote kuanzia mwanzo mpaka mwisho, jinsi walivyovamiwa na akina Liston na Vasco, walipokuwa ndani, na pia, Bosco alivyoweza kupambana nao na kuwashinda hatimaye kukimbilia pale Morogoro ili kujificha!

    Wote wawili, Bosco na Marieta wakawekwa chini ya ulinzi na kulazwa katika mahabusu za polisi, kila mmoja katika chumba chake, ndani ya kituo kikuu, wakisubiri kesho yake warudishwe jijini Dar es Salaam kwa usafiri maalum. Hakika kwa upande wa Bosco, alijiona kama mtu aliyekuwa ndotoni! Hakutegemea kukamatwa kikuku namna ile, kwani ni mtu aliyekuwa anajiamini sana, lakini ilikuwa ni sawa na Inzi kufia katika kidonda!



    ********

    Kachero Inspekta Raymond Gopi, alizipata taarifa za kukamatwa kwa kijana, Bosco, mjini Morogoro, kunako majira ya saa mbili za usiku. Alikuwa amejulishwa na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa huo, ambaye naye alikuwa ameshiriki katika mahojiano yale, kitu ambacho kilimpa faraja ya kuweza kuikamilisha operesheni ile mapema sana.

    Wakati huo alipokuwa amepewa ujumbe huo, ndiyo kwanza alikuwa amejipumzisha sebuleni, ikiwa ni baada ya kutoka katika kazi ile nzito ya usiku kucha, ya kuwasaka wauaji wale waliokuwa wakiendesha mauaji ndani ya jiji la Dar es Salaam.

    Kwanza kabisa, alikuwa amekaa na mchumba wake, Maria Mchome, anayesoma katika Chuo cha Diplomasia, Kurasini, ambaye alikuwa amemtembelea baada ya kutoka chuoni, ukiwa ni utaratibu wake kila mwisho wa wiki. Kwa muda wote walikuwa wakiongea mambo mengi tu, lakini cha muhimu ilikuwa ni juu ya harusi yao ambayo ilikuwa katika maandalizi ya mwisho.

    Ukweli ni kwamba, kwa Maria, aliona kuwa mchumba wake, Raymond alikuwa ametingwa sana na kazi za upelelezi, kiasi ambacho kingeweza kuiathiri harusi yao, kwa jinsi Raymond alivyokuwa bize na kazi, badala ya kushughulikia harusi yao. Huo ulikuwa ni mtazamo wake tu, lakini kwa upande wa Raymond, alikuwa anatimiza majukumu yake ya kazi kama inavyopaswa, hasa kwa kachero mahiri.

    “Vipi mpenzi, naona umepigiwa simu,” Maria alimuuliza baada ya Raymond kuipokea ile simu kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi Morogoro.

    “Ndiyo, nimepigiwa…” Raymond akamjibu huku akimuangalia kwa tabasamu. Alishamwelewa! Ni kitu wivu!

    “Kwa hivyo unaondoka sasa hivi, kama kawaida yako…”

    “Hapana, siondoki mpenzi…leo tuko wote mpaka majogoo yatakapowika…” Kachero Inspekta Raymond akamwambia,

    “Afadhali, nilifikiri tayari kumeshakucha kama kawaida yako,” Maria akasema na kuongeza. “Maana kila nikitokea mimi, ni lazima tukio litokee…”

    “Ndiyo hivyo mpenzi, leo halijatokea zaidi ya yale mengine ninayoyafuatilia…” Raymond akamwambia huku akimwangalia baada ya kumuona ni mtu aliyekuwa na wivu tu. Tuseme alishamzoea!

    “Poa, basi ni muda muafaka wa kulala sasa…” Maria akamwambia.

    “Ni kweli, tulale, kwani kesho Jumapili nategemea kuamka mapema sana…”

    “Ah, wewe tumeshakuzoea, naona cheo cha ukamishna hakitakukosa baada ya miaka minne mbele…”

    “Nashukuru kama unaniombea hivyo, kwani ni wengi wanaokililia lakini hawakipati…” Raymond akasema huku akiizima taa ya ndani iliyokuwa na mwanga mkali, na kuiwasha ile yenye mwanga hafifu, ambayo ilikuwa kando karibu na kitanda.

    Wote wakajitupa kitandani ili kuutafuta usingizi. Wakati huo, Kachero Inspekta Raymond alikuwa akiwaza kuwa ni kweli kuwa mwanamke akimpenda mwanaume, au wote wakipendana, ni lazima kuwe na wivu ili kudhihirisha upendo wao. Hata hivyo, Raymond akayaacha hayo na kuendelea kuiwazia ile kazi iliyokuwa inawakabili kesho yake! Kazi ya kuhakikisha kinara mkuu wa sakata lie, Salum Zakwa anapatikana!



    ********

    Jumapili kulipambazuka kukiwa na hali ya manyanyu ya mvua kiasi na kulifanya jiji la Dar es Salaam kuwa na ukimya wa aina yake. Ingawa habari za matukio ya mauaji zilikuwa zimesambaa katika vyombo vya habari, huku vingi, hasa magazeti, vikilaumu Jeshi la Polisi kushindwa kuzuia mauaji yale na kuruhusu wahusika kufanya watakavyo.

    Kwa upande wa Kachero Inspekta Raymond, siku ile aliamka asubuhi akiwa na mawazo juu ya operesheni waliyokuwa wanaiendesha, huvyo baada ya kujiswafi na kuvalia nadhifu, alimuaga mchumba wake, Maria, na kuelekea ofisini. Ilimchukua dakika chache tu kufika ofisini.

    Baada ya kuingia tu, akakaa kwenye kiti na kupanga la kufanya katika mpango kazi wake. Kwanza kabisa akachukua simu yake ya mkononi na kumpigia Kachero Benito, ili ajue yuko wapi kwa muda ule baada ya kuwapangia kazi ile ya kumfuatilia Salum Zakwa.

    Alipompata katika laini, Benito alimwambia kuwa kwa muda ule walikuwa wameshafika eneo husika wakiwa na gari, tayari kumfuatilia mhusika. Hivyo basi, Raymond akajua kuwa kazi ilikuwa inakwenda kama alivyopanga, akaridhika na kuendelea na kazi iliyompeleka ofisini asubuhi ile, ingawa ilikuwa ni siku ya jumapili.

    Kachero Inspekta Raymond akachukua lile faili la wafanyabiashara wa dawa za kulevya na kuanza kulishughulikia, kwani alitaka alikamilishe haraka sana, hasa ukizingatia saubuhi ile angepata misukosuko kutoka kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, ambaye angetaka apate taarifa za upelelezi unavyokwenda na hatua gani zilizochukuliwa.

    Na kweli baada ya kukaa mezani kwake, na kuanza kulishughulika faili hilo, simu ya mezani ikaita. Akaacha kuandika na kunyanyua kiwiko cha simu.



    ********

    “Kachero Inspekta Raymond…nikusaidie…” akasema.

    “Kweka hapa naongea…”

    “Naomba maelekezo yako afande…”

    Baada ya kujuliana hali ikiwa ndiyo utaratibu wa kawaida, ndipo alipomwambia, “Unasikia Raymond…”

    “Nakusikiliza afande…”

    “Hali ni ngumu.”

    “Hapa nilipo, ni kwamba kuanzia jana sijalala kabisa. Natumaini na wewe hali unaiona ukiwa ni mpelelezi wa matukio haya yanavyotokea hapa jijini, isitoshe Mkurugenzi wa Upelelezi anataka taarifa rasmi, ambapo anadai tumekaa tu huku watu wanauawa ovyo.

    Pili, kama ilivyokuwa mara ya kwanza, vyombo ya Habari, magazeti na televisheni, yameelezea habari hii kwa kina, ingawa juzi tuliwaita waandishi wa habari na kuwaonyesha wale watuhumiwa tuliowakamata na dawa za kulevya pale uwanja wa ndege…” akanyamaza kidogo huku akimmwangalia Raymond.

    “Wameshindwa kutusifia na kutuandikia vibaya. Sasa hii ni changamoto kwetu, ni kufanya juu chini wahusika wapatikane haraka iwezekanavyo! Mkurugenzi amesema kama kazi imetushinda, ataingia mwenyewe kazi ni na kutuonyesha jisi kazi ya upelelezi inavyofanyika! Sasa huoni kama hili ni tusi? Ina maana kazi imetushinda kweli? Eti Raymond…”

    “Kazi haijatushinda afande…” Kachero Inspekta Raymond akasema na kuongeza. “Na ufumbuzi wa sakata hili utapatikana leo hii, kwani mchawi wetu tumeshamtambua. Na mpaka muda huu ninapoongea na wewe, nimeshawatuma vijana wetu, Benito, Dani na Maiko, kufuatilia nyendo za mhusika wetu, ambapo watanijulisha kwa simu juu ya kazi inavyokwenda…”

    “Ni vizuri Raymond, endelea na kazi, lakini kumbuka kunijulisha kila hatua ya upelelezi ili na mimi niweze kuwajulisha wakubwa, ambao mpaka sasa ambao wanataka taarifa. Hivyo nakutakia kazi njema,” akamaliza Kweka.

    Baada ya kumaliza mazungumzo yao, Kachero Inspekta Raymond akabaki akilishughulikia lile faili. Hata hivyo, akachukuwa redio ya mawasiliano iliyokuwa pale juu ya meza, na kuanza kuwatafuta makachero wake, Benito, Maiko na Dani, waliokuwa wanafuatilia nyendo za mtuhumiwa wao, Salum Zakwa Mnube.

    “Redio namba kumi…ova!”

    “Nakupata…obva!” Benito akapokea.

    “Mko wapi sasa hivi…ova!”

    “Hapa tuko kituo cha Polisi Salender Bridge…ova!”

    “Endeleeni na kazi…hakikisheni mnamfuatilia kwa makinki…ova!”

    “Umesomeka afande…tunamfuatilia na kila hatua tutakujulisha…ova…”

    “Nimekusoma…ova and out…”

    Baada ya kumaliza kuwasiliana, ndipo Kachero Inspekta Raymond alipoendelea na kazi ile ya kuliandikia lile faili maalum la wafanyabiashara wa dawa za kulevya.



    ********

    Eneo la Upanga Sea View lilikuwa kimya kabisa asubuhi ile ya jumapili, hasa ukizingatia walikuwa wanaishi watu wenye kipato cha juu tofauti na uswahilini walipokuwa wanaishi watu wa kipato cha wastani. Kila mtu wa eneo lile alikuwa anaishi ndani ya himaya iliyodhibitiwa kwa geti. Pia, ile hali ya mvua za manyunyu ilikuwa imechangia kuwa na hali ya utulivu, huku pia magari machache yakionekana kupita katika barabara ile ya ufukoni.

    Wakati huo makachero, Beniti, Dani na Maiko walikuwa wameshafika eneo hilo kufuatilia nyendo za Salum Zakwa, ambaye kwa muda ule walijua kuwa alikuwa nyumbani kwake. Baada ya kufika, wakapitiliza na kwenda kulipaki lile gari aina ya Toyota Land Cruiser katika kituo cha Polisi Salender Bridge.

    Pale kituoni walikaa hadi ilipotimu saa mbili na robo za asubuhi, ndipo walipowasiliana na Kachero Inspekta Raymond aliyekluwa ofisini kwa muda ule, na kumjulisha hali inavyokwenda. Halafu wakaamua kujipangia kwa kujigawa, ambapo Benito na Dani walimwacha Maiko pale kwenye kituo cha polisi, akiwa na lile gari, halafu wao wakaamua kutembea kwa miguu kuifuata Barabara ya Sea View, wakitembea kama watu waliokuwa katika matembezi yao.

    Kwa ujumla, mtaa ule ulikuwa umetulia sana, huku upepo ukivuma kutoka baharini, ulizingatia kulikuwa na hali ya mvua za manyunyu. Nyumba ya Salum Zakwa, ilikuwa umbali wa mita 30 hivi kutoka katika barabara ya Ufukoni na ile ya Sea View, Upanga, pia haikuwa mbali na Hospitali ya Aga Khan. Hivyo, makachero, Benito na Dani walipofika karibu na lile Jumba la Utamaduni wa Urusi, wakasimama kando ya mti mmoja mkubwa Mkuyu, kama vile walikuwa wanamsubiri mtu, ingawa sehemu hiyo ilitulia sana.

    Pale waliposimama, waliweza kuliona vizuri lile jumba la Kamba, lililokuwa limezungukwa na uzio wa ukuta madhubuti, na mbele kukiwa na geti la chuma, na upande wa nyuma lilikuwa limepakana na Bahari ya Hindi iliyokuwa shwari kwa muda ule. Vilevile pale getini alionekana mlinzi wa kampuni ya binafsi ya ulinzi, akiwa ndani ya kibanda amekaa kujisitiri na yale manyunyu ya mvua.

    “Tumeshafika Dani, na jumba la mtu wetu ndiyo lile. Na muda huu inawezekana yuko ndani amelala, kama unavyojua watu wakubwa hawana presha kama sisi pangu pakavu tia mchuzi. Ulale saa hizi utaishije” Benito akamwambia Dani.

    “Ni kweli, mwahili ulale saa hizi? Thubutu! Sisi tusimame hapa kwa muda, huwenda tukaambulia chochote, kwani ni kweli mtu wetu hajatoka bado…” Dani akaongeza kusema.

    “Hata hivyo inabidi tuwe makini sana, kwani mtu mwenyewe ni mwanajeshi mstaafu na bado yuko makini kwa kila jambo analofanya, hivyo anaweza akawa naye amejiandaa!”

    “Hilo linawezekana. Mtu mwenyewe ni mafia, na anayejua anachokifanya ili kujilinda asikamatwe…ni muhimu kuwa macho kwa kila hatua tunayokwenda.”

    Makachero Benito na Dani wakaendelea kusubiri pale kwa muda wa saa nzima! Ni uvumilivu wa hali ya juu kumsubiri mtu ambaye hujui atatoka saa ngapi, kwani hawakuwa na ratiba yake!

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ********

    Wakati makachero Benito na Dani wakiwa wamesimama sehemu ya nje, barabara ya Sea View, Salum Zukwa, alikuwa ndani ya nyumba yake, ameshaamka muda mrefu sana. Siku hiyo ya jumapili alikuwa amekaa chumbani kwake akiwa na mawazo mengi sana juu ya mauaji yale aliyokuwa ameyaratibu yeye, ambapo hakujua polisi walikuwa wamefikia hatua gani, au wameshamgundua na kumwekea mtego gani.

    Tuseme hakujua kama alikuwa anaujua mwenendo mzima wa yeye kushiriki katika sakata lile! Muda wote, Salum alikuwa bize sana, kiasi kwamba hata familia yake ilimshangaa sana kumwona akiwa katika hali ile. Mke wake, Bi. Husna Binti Mbegu alipomuuliza kuhusu hali ile, alimjibu kuwa hali yake haikuwa nzuri tokea alipotoka safari ya nchini Uingereza, naye akamwamini.

    Hatua nyingine iliyofuata ni kwamba, Salum aliingia bafuni na kujiswafi na alipomaliza, alivalia nguo, suti ya kimichezo ya rangi ya bluu iliyoiva, raba nyeupe na kofia ya kapelo ya rangi nyeupe vilevile. Machoni alivalia miwani mieusi ingawa hakukuwa na jua. Ni mavazi ambayo huwa anapendelea sana kuyavaa wakati wa mwisho wa wiki kama anafanya mazoezi ya kutembea kwa miguu katika barabara ile ya Ufukoni, mpaka eneo la Feri na kurudi hadi nyumbani tena.

    Ni utaratibu ambao alikuwa amejiwekea, lakini kwa siku hiyo haikuwa hivyo, kwani alikuwa na mipango mingine. Alipomaliza kujiandaa, alichukua bastola yake aliyokuwa anaimiliki kihalali, na kuifanyia usafi. Baada ya kuifanyia usafi wa kutosha, akaijaza risasi kumi na mbili katika magazine yake iliyokuwa inatumia, halafu akaichomeka kiunoni kiasi kwamba ilikuwa haionekani kwa urahisi.

    Kwa mbali akajipongeza kwa hatua aliyokuwa amefikia. Alikuwa amepanga kwenda kule Bangaiza Gesti, Mwenge, kukutana na Vasco Nunda, lakini hakujua kama kwa nje kulikuwa na makachero wa Jeshi la Polisi waliokuwa wakimsubiri kwa hamu kubwa ili wamfuatilie kujua nyendo zake! Uvumilivu ni kitu muhimu sana, hasa kwa askari yeyote anapokuwa kazini au vitani. Makachero wale, Benito na Dani walikuwa wamemsubiri kwa hamu, kwa muda wa saa nne hivi mpaka watakapoelewa anataka kufanya nini!

    Ilipotimu saa sita za mchana, Salum Zakwa alitoka ndani akiwa amevalia ile suti ya kimichezo. Baada ya kutoka nje, akaelekea kwenye banda la gari, ambapo lilikuwepo lile gari lake, Ranger Rover Vogue. Hakupoteza muda, akapanda na kuliondoa kwa mwendo wa taratibu kutoka getini na hatimaye kuifuata Barabara ya Sea View, kuelekea usawa wa Kituo cha Polisi Salender Bridge.

    Alipofika kwenye taa za trafiki za makutano ya barabara ile na ya Ali Hassan Mwinyi, akalisimamisha gari kusubiri taa ya kijani iwake ili kuruhusu magari, kwani muda ule taa nyekundu ilikuwa inawaka. Taa iliporuhusu, Salum Zakwa, aliendelea na safari na kuifuata Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, kama anaelekea Oysterbay, akiwa hana wasiwasi wowote, wala kujua kama makachero wale, Benito na Dani, walikuwa wanamfuatilia nyendo zake!



    ********

    Alfajiri ya siku ile, Vasco Nunda aliamka kutoka usingizini. Akayafikicha macho yake na kuangaza pande zote ndani ya chumba alicholala, ambacho kilikuwa ni kigeni kwake. Ndiyo, alikuwa amelala gesti, kitu ambacho alikuwa hajakizoea, ukizingatia alikuwa ana makazi yake, ya maana tu eneo la Kinondoni. Pale alikuwa amelala kwa shinikizo la bosi wake, Salum Zakwa, kwa sababu alizozijua mwenyewe!

    Baada ya kuamka, Vasco alikaa juu ya kitanda kwa muda wa dakika kumi hivi, huku akiwaza na kuwazua juu ya kile kilichokuwa kinaendelea baada ya kutekeleza mauaji ya watu wale, John Peka, David Osmond na mwenzake Liston. Pia, alikuwa akijiuliza juu ya Bosco Zambi, alikuwa amekimbilia wapi, wakati bosi wao, Salum Zakwa anataka na yeye auawe? Je, atampata wapi?

    Baada ya kuwaza yale yote, Vasco alichukua taulo lilokuwa juu ya kiti, halafu akaelekea ndani ya bafu lililokuwa mle ndani kuoga. Alijikokota kama vile mgonjwa aliyekuwa ameugua zaidi ya wiki moja hadi aliopingia mle bafuni, na alipomaliza kuoga, akarudi tena chumbani na kuvalia nguo zake, ingawa hakuwa nadhifu. Alivalia bila kuchomeka shati na pia chini miguuni alivalia makubazi tu.

    Akiwa hana raha kabisa, Vasco aliamua kutoka nje ya gesti ile ili kunyoosha miguu na kusafisha macho yake. Hivyo alipotoka baada ya kumuaga mhudumu wa pale, alitembea taratibu kwa kuufuata mtaa uliokatiza vichochoroni, hadi alipofika katika mgahawa mmoja uliokuwa karibu na maduka yaliyokuwa katika eneo lile la Mwenge, ambapo aliingia ndani na kujipatia kifungua kinywa. Ni kifungua kinywa ambacho hakukila kwa raha hata kidogo. Alipomaliza kula, alijiondoa ndani ya mgahawa ule na kupitia kwa wauza magazeti waliokuwa wanauza katika eneo lile. Akaanza kuyapitia kwa macho magazeti ya siku ile Jumapili, huku akisoma vichwa vya habari vilivyomvutia.

    Vasco aliporidhika na magazeti yaliyomvutia, akayanunua magazeti matatu ya kiswahili na kuondoka nayo kurudi Bangaiza Gesti kwa hatua za kinyonge. Baada ya kufika, akaingia ndani na kujifungia. Akaanza kuyapitia magazeti yale moja baada ya nyingine na kukuta kumeandikwa habari za matukio yale ya mauaji ya kutisha jijini Dar es Salaam, na kwamba polisi walikuwa katika upelelezi wa kina ili kuwapata wauaji hao!

    Alipomaliza kuyapitia magazeti hayo, ambayo kwa kiasi yalimchefua, aliyatupa pale kitandani na kuiendea briefcase yake ambayo aliifungua na kutoa bastola yake ambayo ilikuwa imesafishwa vizuri na kujazwa risasi. Akaikoki na kuingiza risasi chemba, ikiwa ni tayari kwa kumlipua bosi wake, Salum Zakwa!

    Kwa muda wote alikuwa akiiangalia saa yake ya mkononi, na kuona muda ulikuwa unaendelea kwenda pasipo bosi wake huyo kumpigia hata simu! Akakaa kwa hali ya tahadhari!





    ********

    Makachero, Benito na Dani walimwona Salum Zakwa alivyokuwa anatoka na gari lake. Hivyo, Dani akampigia simu, Kachero Maiko, aliyekuwa kule Kituo cha Polisi, Salender Bridge, awafuate kwa gari lile, Toyota Land Cruiser. Naye hakukawia, akalitia moto na kuwafuata kwa mwendo wa wastani ili mhusika asiwagundue. Akawafikia na wao wakapanda garini, Benito akipanda mbele na Dani nyuma.

    “Vipi afande, ametoka?” Maiko akauliza.

    “Ndiyo, ametoka na gari, Ranger Rover, ya rangi nyeusi, tena hajafika mbali!”

    “Aisee, ndiyo ile iliyonipita muda siyo mrefu?”

    “Ndiyo yenyewe!”

    “Poa, sasa afande?”

    “Tumfuatilie!”

    “Sawa…” Maiko akasema. Halafu akaligeuza gari na kuanza kulifuatilia lile gari la Salum Zakwa.

    Baada ya kulifuatilia wakalikuta gari lile likiwa katika taa za trafiki, kwenye makutano ya barabara za Ali Hassan Mwinyi, Kenyatta na Kinondoni. Wakakaa nyuma ya gari lake, kwa kuyaacha magari matatu, na taa ziliporuhusu, wakaendelea na safari kumfuatilia Salum Zakwa. Benito aliyekuwa na redio ya mawasiliano, akaamua kumjulisha Kachero Inspekta Raymond, ambaye bado alikuwa ofisini, juu ya kinachoendelea. Benito akabonyeza batani na kuanza kuongea:

    “Radio namba nane…ova!”

    “Nakupata…lete taarifa…ova!” Kachero Inspekta Raymond akaipokea.

    “Mtu wetu tunae na tunamfuatilia…ova!”

    “Ametoka sivyo?’

    “Ametoka…ova!”

    “Anaelekea wapi? Ova!”

    “Hatujui anaelekea wapi…tuko katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi…ova!”

    “Mfuatilieni mpaka mwisho wake….halafu mnijulishe…ova!”

    “Tunamfuatilia…ova!”

    “Kazi njema…ova!”

    Ranger Rover iliendelea kusonga mbele na makachero wale wakaendelea kumfuatilia hadi walipofika Oysterbay, eneo la Morocco, kwenye taa za trafiki za makutano ya barabara za Rashid Kawawa na Ali Hassan Mwinyi. Kwa bahati nzuri taa za kijani ziliruhusu, hivyo wakapitiliza kuelekea Mwenge. Salum Zakwa aliyekuwa ndani ya gari lake, roho yake ilikuwa ikimdunda sana, inangawa hakujua kama alikuwa anafuatiliwa nyuma na makachero waliokuwa nan usongo naye! Akiwa kama askari, Mwanajeshi mstaafu, aliyefuzu katika medani ya kivita, aliamua kupoteza lengo baada ya kufika katika eneo la Makumbusho.

    Salum Zakwa aliamua kupinda upande wa kulia na kuifuata barabara ya udongo iliyokuwa inapita sambamba na uzio wa wa kijiji cha Makumbusho ya Kiutamaduni. Ni mchezo ambao uliwaacha makachero wale wakishangaa, lakini nao wakaendelea kumfuatilia tu mpaka wajue mwisho wake na kuambulia cha maana. Aliendesha gari mpaka alipotosheka, na muda wote alikuwa akiangalia kwenye kioo cha kuangalia nyuma, kiasi cha kuliona lile gari, Toyota Land Cruiser, lililokuwa linamfuatilia nyuma kama mkia!

    Akili yake ikafanya kazi haraka sana na kupanga la kufanya; hivyo akaamua kugeuza gari lake na kurudi kule alipotokea, ili kuchunguza kama ni kweli watu wale walikuwa wanamfuatilia yeye! Akapishana na gari la makachero wale, ambao walimwona akirudi kiasi cha kuwafanya washtuke! Wakampisha na kuwapita kwa mwendo wa kasi na kupotea!

    Alifaulu mchezo ule!

    Kachero Maiko akaligeuza gari lao haraka na kuanza kumfuatilia tena Salum Zakwa, kiasi kwamba walipofika katika barabara kuu ya Ali Hassan Mwinyi, hawakujua ameelekea upande gani, na magari yalikuwa ni mengi sana yukiwa katika foleni na mengine yakipita kwa kasi kutokea upande wa Mwenge.

    Hata hivyo, makachero wale wakaamua kurudi tena kwenye Kituo cha Polisi, Salender Bridge na kujipanga upya ili kujua Salum alikuwa ameelekea sehemu gani na pia wakifanya mawasiliano kwa njia ya redio ya mawasiliano, kwa askari wa doria kama walikuwa wameliona lile gari aina ya Ranger Rover, lakini hawakupata mafanikio, kwani kwa kila waliyemuuliza, hakuweza kulitambua kwa vile lilikuwa limeshapita kitambo!

    Kazi hiyo!

    Ni kitu ambacho makachero wale walikuwa hawajakijua, ni kwamba, Salum zakwa alikuwa ameshawashtukia muda mrefu, na baada ya kuhakikisha kwamba wanamfuatilia, ndipo alipowapiga chenga, akiifuata Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, kuelekea Mwenge, tena akipitia upande wa kulia kwa kulilazimisha na hatimaye kupata upenyo wa kulipenyeza na kuingia upande wa kushoto kuelekea Mwenge.

    Salum Zakwa akayapita magari kama sita hivi akiwa katika mwendo ule wa kasi na kujipongeza kwa kuwapotea watu wale ambao alikuwa bado hajawafahamu. Na pia, alijua kama walikuwa ni polisi, basi wangetumia mawasiliano ya redio za mawsiliano, na wamkamate kabla hajafika mbali. Hivyo akatumia mbinu za kupita juu kwa juu na kuwapotea! Breki ya mwisho ilikuwa ni baada ya kufika Mwenge, ambapo alilipenyeza gari lake na kwenda kulipaki ndani ya gereji bubu moja iliyokuwa ndani ya makazi ya watu, sehemu iliyojificha kidogo.

    Ni eneo ambalo alikuwa analifahamu na baadhi ya mafundi wa gereji hiyo pia aliwafahamu, na mara nyingi alikuwa akifanya hivyo anapofika katika eneo hilo kwa shughuli zake nyingine, ikiwa pia ni kukutana na wafanyabiashara wa dawa za kulevya, ambao alipenda sana kukutana nao ndani ya nyumba ile iliyojificha na siyo rahisi kwa maafisa wa polisi kuishtukia!

    Baada ya kukabidhi gari hilo, Salum Zakwa aliaga na kuondoka kwa kupoteza lengo, halafu akakatiza katika vichochoro kadha wa kadha vilivyomfikisha Bangaiza Gesti iliyokuwa mbali na pale. Akiwa amevalia ile suti ya kimichezo, ilikuwa siyo rahisi kumtambua, ambapo baada ya kufika, aliingia ndani ya gesti ile kwa kutumia mlago wa uani, ambao ndiyo mara nyingi hutumika kuingizia wake za watu kwenda kufanya ufuska ili wasionekane.

    Salum Zakwa hakupenda kupitia upande wa mapokezi, ambapo mhudumu yupo, wakati alishajua kwamba chumba alichokuwa amepanga Vasco Nunda, kilikuwa ni chumba namba 12 kilichokuwa upande wa kushoto kama unatokea mlango wa nyuma.



    *******

    Mlango wa chumba alichopanga Vasco Nunda uligongwa. Vasco akanyanyuka na kwenda kuufungua, huku akiwa na tahadhari ya hali ya juu, halafu akaufungua kwa ufunguo huku akichungulia kwenye tundu la ufunguo. Baada ya kuchungulia akaona ni Salum Zakwa, bosi wake, ambaye aliusukuma na kuingia ndani.

    “Karibu bosi…” Vasco akamwambia angali bado amesimama.

    “Oh, ahsante…” Salum Zakwa akasema huku akiingia na kuangalia sehemu ya kukaa.

    “Nilifikiri hutatokea bosi…” Vasco akamwambia huku akimwangalia kwa makini.

    “Unasemaje?” Salum Zakwa akamuuliza Vasco.

    “Nimesubiri sana…maana miadi tuliyowekeana inazidi kupita!”

    “Kwani nimechelewa?”

    “Ndiyo bosi…”

    “Hata hivyo nimejitahidi kwa kutumia akili ya ziada hadi ninafika hapa!”

    “Kivipi bosi?”

    “Nilipotoka nyumbani kwangu, Upanga, kuna watu waliokuwa wananifuatilia nyuma!”

    “Sasa ikawaje?”

    “Nilitumia ujuzi wangu wa medani ya kivita, nikafanikiwa kuwakwepa hadi nilipofika hapa Mwenge. Nahisi wale watakuwa ni makachero wa polisi!”

    “Mh! Hii si hatari jamani?”

    “Usijali, hawatuwezi!”

    “Sawa bosi!”

    “Ndiyo Vasco, sasa kazi tumemaliza?”

    “Naona tumemaliza bosi!” Vasco akamwambia!

    “Bado hatujamaliza!”

    “Kivipi bosi?”

    “Bado Bosco!” Salum Zakwa akasema na kuongeza. “Hatujui amekimbilia wapi! Hivyo ni lazima apatikane kabla ya polisi hawajamkamata!”

    “Sasa tutampata wapi bosi?”

    “Hayo siyo ya kuniuliza mimi Vasco! Kumbuka kuwa nimeshakulipa fedha zote, ambapo ilikuwa ni juu yako kumwua! Sasa unataka mimi niharibikiwe?”

    “Taratibu bosi!” Vasco akamwambia!

    “Hakuna taratibu Vasco! Hapa nilipo mimi nimechanganyikiwa! Ni hasara tupu, mzigo umekamatwa, polisi nao wananiandama!”

    “Mh!” Vasco akaguna. Halafu akainama chini huku akiwaza kwa muda.

    Lile wazo la kumtafuta Bosco alilitupilia mbali na haraka likamjia wazo la kupambana na Salum Zakwa kwanza, ambaye alionyesha dhahiri kuwa alifika pale kwa jambo moja tu, kummaliza yeye, na si vinginevyo!

    “Unaguna nini? Nipe jibu bwana!” Salum Zakwa akamwambia huku akimwangalia kwa hasira kali!

    “Sawa, mimi nitaifanya kazi hiyo ya kumtafuta Bosco popote pale alipo!” Vasco akamwambia huku akiendelea kujiweka katika hali ya tahadhari.

    “Ndiyo, fanya hivyo!” Salum Zakwa akamwambia na kumalizia. “Usipotekeleza tu…”

    “Mbona unanitisha bosi?” Vasco akamwuliza kwa hasira huku akimsogelea karibu kama mtu aliyetaka kupambana!

    “Unataka kufanya nini?” Salum akamuuliza Vasco huku akimwangalia kwa makini sana!

    Kwa kumshtukiza, Salum Zakwa akamrushia ngumi ya nguvu kumwelekea Vasco Nunda! Lakini Vasco aliiona na kuiepa kiasi cha kumfanya apitilize na kuangukia juu ya kitanda kile cha futi sita kwa sita, na Vasco akabaki anashangaa baada ya kukoswakoswa na ile ngumi nzito!

    “Umetangaza vita!” Vasco akamwambia huku akimwangalia Salum Zakwa aliyekuwa akijizoa na kunyanyuka kutoka pale kitandani alipoangukia.

    Na hata wakati ule alipoangukia pale kitandani, simu yake ya mkononi ilidondoka lakini hakuwa na habari nayo, zaidi ya kuwa na wazo moja tu, kuua!

    Kama umeme, Salum Zakwa alichomoa bastola na kumwelekezeaVasco. Halafu akamwambia kwa sauti kavu!

    “Shenzi sana kijana wewe! Hustahili kuishi!”

    “Na wewe hustahili kuishi!” Vasco naye akamwambia, kama umeme alichomoa bastola yake na kumnyooshea kumlenga! Ndiyo tuseme wote walikuwa wamelengana, na ni nani atakayemuanza mwenzake?

    Patamu hapo!

    Lakini kabla ya kufanya chochote, kitu cha ajabu kilitokea pale chumbani. Mlio wa kutisha ulitokea kutoka dirishani! Madirisha ya Bangaiza Gesti yalitengenezwa kwa mbao na nyavu, halafu kwa nje likatengenezwa dirisha jingine lililokuwa na vioo, ambalo hufunguka yote na kuruhusu upepo na hewa kuingia mle chumbani. Baada ya dirisha moja wapo lililokuwa wazi kujigonga kutokana na kusukumwa na upepo, ndiyo uliomfanya Vasco ageuke na kuangalia dirishani.

    Pale ndipo Vasco alipofanya kosa kubwa, Kwani Salum Zakwa alipata fursa nzuri ambapo alifyetua risasi kutoka kwenye bastola yake, na kumshindilia Vasco risasi mbili, ya shingoni na kifuani, ambazo zilimpata sawia, akaruka juu na kupiga yowe kubwa. Na alipotua chini alikuwa ameshakufa!

    Salum Zakwa akabaki akimwangalia alivyokuwa amelala pale sakafuni na damu nyingi zikimtoka, kiasi cha kumlowesha shati na nyingine kusambaa sakafuni! Baada ya kuhakikisha amemuua Vasco, akatoka mle chumbani kwa mwendo wa kawaida na kuishia kwa kupitia ule mlango wa uani!

    Akapotea!







    ********

    Awali, mhudumu wa mapokezi, katika nyumba ile ya wageni ya Bangaiza, Masoud Kimeo, alimwona Salum Zakwa wakati akiingia ndani kwa kupitia mlango wa uani badala ya ule aliouzoea. Kutokana na hali hiyo, alianza kumtilia mashaka akiwaza kwamba huenda mtu yule ni ‘shoga’ ama ‘basha’ aliyekuwa akimfuata mtu wake. Ukweli ni kwamba akiwa ni mtu mzoefu katika kazi ile ya uhudumu wa pale, aliweza kuwasoma hata wateja wake, wema na wabaya.

    Na kwa upande wa Salum Zakwa alikuwa anamfahamu muda mrefu, lakini kwa siku ile hakumfahamu kwa vile alifika kwa njia ya siri! Pia, isitoshe siku hiyo alikuwa amevalia suti ya kimichezo, miwani mieusi na kofia ya kapelo, ambavyo vyote vile vilimbadilisha kabisa. Basi, Masoud akaamua kumfuatilia baada ya kumwona akiingia ndani ya chumba namba 12, ambacho pia alikuwa amepanga mteja, Vasco Nunda.

    Kama kawaida, Masoud akanyemelea hadi katika mlango wa chumba kile na kusikiliza kilichokuwa kinaendelea baina ya watu wale wawili, ambapo baada ya muda akawasikia wakibishana kitu fulani kwa muda bila kupata muafaka. Ghafla ikatokea vurugu nzito baina ya watu hao waliokuwa wakigombania kitu ambacho kilimtia wasiwasi Masoud, hasa baada ya kusikia katika vyombo vya habari juu ya muuaji wa ajabu aliyezuka ndani ya jiji la Dar es Salaam na kumfanya awe na tahadhari kwa muda wote, na kwa wateja wanaopanga pale!

    Ndiyo maana Masoud akaamua kumfuatilia mtu yule kinyemela na hatimaye kuchungulia kwenye tundu la ufunguo ili kufahamu zaidi, lakini hakuona vizuri zaidi ya kufuatiwa na mlipuko wa risasi! Masoud akajitoa haraka pale mlangoni na kukimbia mbali kidogo akiwa na hofu kubwa, kwani hakujua kiliochokuwa kinaendelea ndani ya chumba namba 12! Ilikuwa ni hatari kubwa!

    Muda uleule wakati Masoud akishangaa, akamwona salum zakwa akiufungua mlango wa chumba na kutoka ndani ya chumba kile. Baada ya kutoka, akaangaza macho yake pande zote, na pia akamuangalia Masoud. Lakini hakumsemesha zaidi ya kunyanyua hatua na kuondoka kuptia mlango wa uani aliokuja nao na kupotea machoni mwake! Na mbaya zaidi hakuweza kumfahamu mtu huyo kutokana na mavazi yake na hofu iliyomtawala!

    Hiyo ndiyo hali aliyoiona Masoud, ambapo baada ya Salum Zakwa kuondoka, ndipo Masoud akiwa mhudumu, aliamua kuingia ndani ya chumba kile ili kujua kilichojiri. Baada ya kuufungua mlango tu, alichokiona mle ndani ilimbidi ashtuke sana kwa kushuhudia ule unyama wa hali ya juu uliofanywa ! Vasco Nunda alikuwa amelala chali sakafuni huku damu zikimvuja ovyo! Alikuwa ameuawa kwa kupigwa risasi!

    Masoud akachanganyikiwa baada ya kuiona maiti ya mtu aliyeuawa kinyama namna ile! Akatoka mbio na kuelekea sehemu ya mapokezi ambapo palikuwa na simu, ili akapige kuwajulisha polisi kuhusu mauaji yale yaliyotokea ndani ya chumba namba 12. Huku mikono ikimtetemeka, Masoud akaivamia simu na kuunyanyua mkonga, halafu akapiga simu kwa namba za dharura za polisi. Simu ikapokelewa, na yeye akajulisha hali halisi.

    Askari wa kitengo cha matukio na wale wa doria wakamjulisha kuwa wangefika muda siyo mrefu. Hakika zilikuwa ni taarifa za ajabu ambazo zilizidi kuwachanganya askari kwa jinsi muuaji yule alivyokuwa akiua kwa kutumia akili za hali ya juu, na jinsi alivyokuwa anakwepa mitego yao wanayoweka! Lazima mtu huyo ni Mafia! Waliwaza!

    Hata hivyo, baada ya muda habari za mauaji yale zikaanza kusambaa ndani ya jiji la Dar es Salaam, baada ya polisi kujulishana kwa njia ya redio ya mawasiliano.



    ********

    Makachero, Benito, Dani na Maiko, dereva, baada ya kumpoteza Salum Zakwa waliyekuwa wakimfuatilia, walibaki wamechanganyikiwa huku wakipanga cha kufanya. Walishindwa kumjulisha, Kachero Inspekta Raymond kuwa eti walikuwa wamempoteza mtu waliyekuwa wanamfuatilia, kwani ungeonekana ni uzembe wa hali ya juu.

    Hivyo basi, wakaamu kwenda kulisimamisha gari lao, sehemu iliyojificha kidogo, eneo la Victoria, kando kidogo ya Barabara ya Ali Hassan Mwinyi. Halafu wenyewe wakabaki ndani nya gari huku wakipanga cha kufanya kabla ya kumjulisha Inspekta Raymond.

    “Dani,” Benito akamwita.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nakusikiliza…” Dani akasema huku akimwangalia.

    “Unajua kuwa mtu wetu ametupotea?”

    “Ni kweli amepotea kimiujiza…” akasema Dani.

    “Na afande Ray anahitaji taarifa kutoka kwetu…unafikiri tutamwambiaje?”

    “Hilo ni kweli…hatuna la kumwambia…”

    “Sasa tufanyeje? Tupeane mawazo, na pia tambueni kuwa yule tuliyekuwa tunamfuatilia ni binadamu vilevile, na ana akili timamu!”

    “Tupange cha kufanya…” Benito akasema na kuongeza. “Tumfuatilie kuelekea Mwenge, sidhani kama atakuwa amerudi katikati ya jiji. Huenda tukaambulia chochote cha kutusaidia kuliko kukata tamaa!”

    “Ni kweli afande kama ulivyosema!” Kachero Maiko akaunga mkono ile hoja ya Benito.

    “Ok, Maiko, ondoa gari tuelekee Mwenge!”

    “Sawa, mkuu!” Kachero Maiko akasema. Halafu akapiga gari moto na kasha kuingiza gea, hatimaye kuliondoa kuelekea Mwenge kwa kuifuata barabara ndogo ya udongo.

    Hatimaye Maiko akaliingiza katika barabara ile ya Ali Hassan Mwinyi, ambayo ilikuwa na msongamano mkubwa wa magari. Baada ya kufika eneo la Bamaga, kwenye makutano ya barabara ile na ya Shekilango, Radio Call aliyokuwa nayo Benito, iliita katika wimbi lao, ambapo na Kachero Inspekta Raymond alikuwa anawatafuta ajue kuwa walikuwa wamefikia wapi katika kumfuatilia Salum Kamba!

    “Nakupata afande…ova!” Benito akaitikia.

    “Nipe taarifa…mmefikia wapi…ova!” Akauliza.

    “Tumelifuatilia windo letu…lakini limetupotea ghafla kama vile lilikuwa limeshtuka! Ova!”

    “Ni kweli liliwapotea…lakini kuna tukio la mauaji limetokea kule Mwenge, kwenye gesti ya Bangaiza….hivyo tukutane huko…ova!”

    “Nimekupata…nimekupata! Tunatekeleza…Ova!” Benito akasema.

    Baada ya kumaliza kuwasiliana, Benito akaiweka redio juu ya kiti cha gari, na kumwambia Maiko alielekeze gari kuelekea Bangaiza Gesti kama walivyoamriwa na Kachero Inspekta Raymond. Wakakatiza katikati ya vichochoro kadhaa, ambapo hawakuchukua muda mrefu sana, kwani walifika katika eneo la tukio na kukuta askari maalum wa kitengo cha matukio kutoka Makao Makuu ya Polisi, wapiga picha na wataalam wa milipuko, wameshafika katika eneo lile. Walikuwa wamezungushia utepe wa rangi ya njano, kwa ajili ya kulinda eneo lile lisikaribiwe na watu na kuharibu ushahidi.

    Kachero Inspekta Raymond alipofika, alijitambulisha na hatimaye kuanza kazi mara moja, ambapo aliingia ndani ya chumba kile namba 12, na kuishuhudia maiti ya Vasco Nunda ikiwa bado imelala palepale sakafuni. Uchunguzi ukaanza mara moja ndani ya chumba kile, kwa umakini wa hali ya juu. Lakini haikuchukua muda, kwani ile simu ya mkononi ya Salum Zakwa, ambayo alikuwa ameidondosha wakati wakipambana na Vasco kabla ya kumtwanga risasi.

    Pembeni ya mwili wa Vasco, palikuwa na simu yake ya mkononi pamoja na bastola iliyokuwa imedondoka kando ya maiti yake. Kwa muda wote huo, Masoud alikuwa sambamba na makachero weale ili kuwasaidia katika upelelezi, kwa kujibu maswali kadhaa ambayo ataulizwa.

    “Bila shaka kulitokea mzozo mkubwa ndani ya chumba hiki…” Kachero Inspekta Raymond akasema baada ya kukichunguza chumba kile kwa makini sana!

    “Ni kweli mkuu…” Masoud akasema huku akiwa bado ana wasiwasi!

    “Natumaini wewe ndiye mhusika mkuu wa hapa katika gesti hii, sivyo?” Raymond akamuuliza huku akimwangalia kwa makini ili kumjua kiundani zaidi.

    “Ndiyo, ni mimi…”

    “Hebu njoo hapa!”

    Masoud akamsogelea pale aliposimama.

    “Hebu niambie…huyu mpangaji wako alipanga lini hapa?”

    “Alipanga siku ya jana mkuu.”

    “Alikuwa peke yake alipokuja hapa?”

    “Ndiyo, alikuwa peke yake alipokuja kupanga… sikuona akiongozana na mtu mwingine. Na alilala hapa mpaka asubuhi ya leo bila kuwa na mtu…”

    “Jina lake ni nani?”

    “Kwenye kitabu cha wageni alikuwa ameandika jina la Pasco Memba, na anatokea Magomeni…”

    “Halafu ikawaje?”

    “Nikampatia chumba, ambapo alilala mpaka leo lilipotokea balaa hili!”

    “Baada ya kuja huyo mtu wa pili?”

    “Ndiyo manaake mkuu…hata sijui alitokea wapi…oh!”

    “Sasa huyo mtu wa pili unasema hujui alitokea wapi, je, aliingiaje?”

    “Mtu wa pili aliingia kwa kupitia mlango wa uani na, na baada ya kuingia tu, akagonga mlango katika chumba kile kwa siri, kama vile ni watu waliokuwa wanafahamiana. Akafunguliwa na kuingia ndani. Na cha ajabu ni kwamba hakupitia pale mapokezi kama ilivyotakiwa!” Masoud akasema kwa msisitizo.

    “Baada ya kuingia mle chumbani ulichukuwa hatua gani ukiwa kama mhudumu wa hapa?”

    “Ndiyo maana nikawafuatilia. Lakini wakati nikiendelea kuchunguza, ndipo nilipousikia mlipuko wa risasi ukitokea mle chumbani. Kabla sijaamua la kufanya, ndipo mtu yule alipotoka haraka na kupotea kwa kutokea mlango wa uani!”

    “Unaweza kumfahamu mtu huyo?”

    “Simfahamu, isipokuwa kimavazi tu aliyokuwa amevalia…”

    “Alivaaje?”

    “Alikuwa amevaa suti ya kimichezo, raba nyeupe na kofia ya kapelo. Kimambile alikuwa mnene kiasi…”

    “Lakini ukimwona tena unaweza kumfahamu?” Raymond akamwuliza.

    “Ndiyo, naweza kumfahamu!”

    “Vizuri sana, kama utaweza kumfahamu, tutakuja tena kwa mahojiano zaidi kama tutafanikiwa kumtia mbaroni. Ina maana utahitajika kuja kumtambua katika gwaride la utambnulisho.”

    “Niko tayari, akipatikana tu, nijulisheni.”

    “Hakuna shaka.”

    Baada ya mahojiano yale, Wataalam wale wa Idara ya Upelelezi waliendelea na kazi zao za uchunguzi taratibu mpaka walipomaliza na kuchukuwa vielelezo vyote. Ndipo Kachero Inspekta Raymond aliyekuwa na jukumu lile, aliporuhuruhusu maiti ile ya Vasco Nunda, ipelekwe katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kidaktari. Halafu wao wakaendelea na operesheni ya kumsaka Salum Zakwa popote pale atakapokuwa amejichimbia!

    Wote wanne walipanda gari lao, Toyota Land Cruiser, na kuondoka kwa mwendo wa kawaida, kurudi ofisini ili kupanga mkakati wa mwisho wa hitimisho wa kazi yao iliyokuwa inawakabili.

    “Jamani, kabla hatujahangaika sana kusumbua akili zetu, nafikiri muuaji tumeshamjua!” Kachero Inspekta Raymond kawaambia.

    “Bila shaka afande, muuaji atakuwa ni Salum Zakwa Mnube, ambaye alikuwa ametukwepa muda siyo mrefu wakati tulipokuwa tunamfuatilia! Alitutoroka na kuja kuyatekeleza mauaji haya!” Benito akasema.

    “Naam, ndiye yeye. Hata hii simu yake ya mkononi alikuwa ameidondosha kule chumbani wakati wakiwa katika mgogoro, nafikiri walikuwa wakipigana na mmoja wao akamzidi mwenzake maarifa!” Kachero Inspekta Raymond akawaambia na pia akiwaonyesha ile simu aina ya Nokia ya bei mbaya!

    “Hakika huu ni ushahidi tosha,” Maiko akaongeza kusema.

    “Ni kweli, ushahidi huu unatosha kumtia hatiani. Unafikiri atasema kitu gani kilichokuwa kimempeleka ndani ya chumba kile?” Dani naye akasema.

    “Lakini kabla ya kumkamata, ni lazima tuwasiliane kwanza na afande Kweka. Si mnajua kuwa yule ni mtu mzito serikalini, na yapaswa kufuata maagizo kwanza,” Raymond akawaambia.

    “Ni kitu cha muhimu, kwani kwa watu kama sisi, tunaweza kwenda kumkamata na hatimaye akatudharau tu. Si unajua tena vigogo? Siku zote wao hujiona kama nusu Miungu…” Maiko akaendelea kusema.

    “Maiko, tunaelekea ofisini moja kwa moja,” Kachero Inspekta Raymond akawambia.

    “Sawa afande,” Kachero Maiko akasema huku ameung’ang’ania usukani wa gari, macho yake kayaelekeza mita mia moja.

    Akipangua gea na kuongeza mwendo





    ********

    Salum Zakwa aliridhika baada ya kutelekeza mauaji yale dhidi ya Vasco Nunda. Hakika hakujua kama angeyatekeleza kwa ufanisi baada ya wote wawili kulengana kwa bastola, na kilichomsaidia akamzidi kete Vasco, ni baada ya dirisha kujigonga na kupiga kelele zilizomfanya adui yake ageuke kuangalia kilichojiri.

    Baada ya kufanikiwa kutoka ndani ya Bangaiza Gesti, akaliendea gari lake, Ranger Rover Vogue, alilokuwa amelipaki katika gereji bubu. Akapanda na kuondoka taratibu bila kushtukiwa na mtu yeyote. Alirudi nyumbani kwake, sea View, Upanga, kwa kuunganisha vichochoro kadhaa, baada ya kutoka pale Mwenge alipofanya mauaji, na alipofika nyumbani, aliliingiza gari na kulipaki gari katika sehemu ya maegesho, ambapo palikuwa na magari yake mengine.

    Salum Zakwa akashuka na kuelekea ndani ya nyumba yake na wala hakukumbuka kama alilifunga ama la. Hakika mawazo mengi yalikuwa yakimwandama kutokana na mauaji yale ya kijana Vasco! Tuseme yalikuwa yamemchefua na kwa muda wote alikuwa anakiona kivuli chake.

    Baada ya kuingia ndani, alielekea kwenye kabati maalum analotumia kuhifadhia baadhi ya pombe kali, halafu akauchukua mzinga mmoja wa wiski pamoja na glasi yenye shingo ndefu. Akatoka nao na kuelekea katika kibaraza za nyumba yake, kilichokuwa kinatazamana na barabara ya Sea View, upande wa mbele wa nyumba yake.

    Ilikuwa ni sehemu ya wazi, ambapo pia aliweza kuona mbali na hata magari yaliyokuwa yakipita mbele ya nyumba yake. Salum Zakwa aliamua kuwa ni vyema anywe pombe kali kwa muda ule, ili kupunguza mawazo yaliyokuwa yanamkabili.

    Na kwa mbali Salum alianza kuujutia uamuzi wake wa kujiingiza katika biashara ile haramu ya dawa za kulevya, ingawa alikuwa na kipato kikubwa tu, kilichomuwezesha yeye pamoja na familia yake kuishi. Ama kweli kumbe kuua mtu si jambo la mchezo, na kama polisi wangegundua kama ni yeye aliyefanya mauaji yale, basi amekwisha.

    Wakati akiendelea kupiga mafunda ya ile pombe kali, ndipo alipopata wazo la kuongea na mkubwa mwenzake, katika hali ya kujuliana hali. Akaingiza mkono katika mfuko wa suruali ile ya kimichezo aliyoivaa, lakini hakuikuta! Akaanza kuchanganyikiwa baada ya kugundua kuwa alikuwa ameidondosha ndani ya chumba namba 12 Bangaiza Gesti, alipokuwa anapambana na Vasco Nunda!

    “Mungu wangu! Kama nitakuwa nimeidondosha mle chumbani, nimekwisha, polisi wakiikuta nitakuwa sina utetezi kwa mimi kuhusika na mauaji!” Salum Zakwa akajisemea moyoni huku akiwa bado amesimama na mikono yake ameiweka kichwani!



    ********

    Makachero, Inspekta Raymond, Benito, Dani na Maiko, walirejea kwenye kituo cha kazi, ambapo walikutana na Mkuu wa Kikosi cha Kupambana na Wafanyabiashara wa Dawa za Kulevya, Dickson Kweka. Waliketi kwenye chumba maalum cha mikutano kwa ajili ya kupanga mkakati wa mwisho ya kuhitimisha kazi ya kumtia mbaroni ‘Kigogo’ yule Salum Zakwa Mnube, Kigogo huyo anayetuhumiwa kwa mauaji pamoja na kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya.

    Kutokana na tuhuma hizo, Dickson Kweka aliwasiliana na viongozi wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi, akiwemo, Inspekta Jenerali wa Polisi, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya JInai (DCI), Makamishna wa Polisi, bila kumsahau Waziri wa Mambo ya Ndani, ambaye yeye alijulishwa na ule uongozi wa juu. Kweka aliwaeleza hali ilivyo na wote wakaridhia kukamatwa kwa Salum Zakwa, kabla hajaharibu ushahidi.

    Baada ya ruhusa hiyo, Kikosi Maalum cha askari polisi kiliandaliwa kwa ajili ya kwenda kumkamata Salu Zakwa, huku Kweka mwenyewe akiwa kiongozi na kusaidiwa na makachero, Inspekta Raymond, Benito, Dani na dereva, Maiko. Baada ya kujiandaa vya kutosha, kikosi kazi kile kikaondoka na kuelekea eneo la Sea View, Upanga, nyumbani kwa Kamba, huku askari wakiwa wamejiandaa vya kutosha na kukabiliana na hatari inayoweza kujitokeza ama upinzani kama ukiwepo.

    Waliondoka wakiwa na magari mawili aina ya Toyota Land Cruiser, ambayo yalifika katika eneo hilo na kusimamishwa nje ya geti la nyumba ya Salum Zakwa. Mkuu wa msafara, Dickson Kweka, aliyekuwa kwenye gari la mbele akiwa na askari wanne, alishuka. Na pia, Makachero Inspekta Raymond, Benito, Dani na Maiko, waliokuwa kwenye gari la pili, nao wakashuka na kusubiri maelekezo mengine kutoka kwa mkuu huyuo wa msafara.

    Kabla ya kuamua la kufanya, wote wakaiangalia mandhari ya eneo lile kwa ujumla, ambapo waliweza kumwona yule mlinzi wa kampuni binafsi ya ulinzi, akiwa amesimama pale getini akiwaangalia baada ya kuona wamesimama pale. Dickson Kweka na timu yake wakamwendea mlinzi aliyekuwa pale mlangoni. Wakamwonyesha vitambulisho vyao na kutaka kuonana na Salum Zakwa, ambapo aliwaruhusu kuingia ndani huku akiwaangalia kwa hofu kubwa! Alijua kuwa limesanuka!

    Lakini kabla ya kuingia, makachero wale waligawana katika makundi, ambapo wengine walibaki kule nje wakiiziunguka nyumba kwa pande zote. Halafu upande wa ndani wakaingia Kweka, Raymond, Benito na Dani, tayari kukabiliana na Salum Zakwa, ndani ya himaya yake, ambayo kwa muda ule ilionekana kama himaya ya makaburini!



    ********

    Kama kawaida yake, Salum Zakwa alikuwa amekaa juu ya kibaraza cha nyumba yake akiendelea kunywa mfululizo, kinywaji chake, pombe kali, Jack Daniels. Alikuwa akiendelea kutafakari juu ya masahibu yaliyokuwa yanamkabili, pia akiangalia upande wa getini ilipokuwa inapita Barabara ya Sea View. Akaona magari mawili ya polisi, moja wapo likiwa ni lile aina ya Toyota Land Cruiser, lililokuwa linamfuatilia mchana ule alipokuwa anakwenda Mwenge, na yeye akafanikiwa kulikwepa. Moyo ukamlipuka kiasi cha kujisikia haja kubwa!

    Ni Polisi!Je, wamemfuata yeye? Akajiuliza!

    Lakini hakupata jibu!

    Akazidi kuwaangalia askari wale kwa hofu kubwa huku akijiona kama mtu aliyekuwa ndotoni. Magari yale yakasimama nje ya nyumba yake kwa umbali tofauti, halafu wakaanza kushuka watu hao, ambao alihisi ni askari polisi. Wakati akiendelea kuwaangalia, aliwaona wengine wakibaki upande wa nje kwa kuizunguka nyumba yake, na wengine wanne wakiingia ndani ya himaya yake baada ya kuteta machache na mlinzi wa getini..

    Baada ya kuingia ndani, wakaanza kupiga hatua kuelekea usawa wa mbele ya nyumba yake, wakati yeye akiwa amekaa juu ya kibaraza kilichokuwa juu ambapo alikuwa akiwaona kwa chini. Watu wale wanne waliokuwa wamevalia nadhifu, walitembea hadi walipofika mbele ya nyumba yake na kusimama karibu na bustani ya maua iliyokuwa na miti na maua yaliyofungamana. Ndiyo, yule mtu mmoja alimfahamu! Ni Mkuu wa Kitengo cha Kupambana Dawa za Kulevya nchini, Dickson Kweka! Mapigo ya moyo yakaongezeka mara dufu kiasi cha ule ujasiri wa kijeshi kumuishia ghafla!

    Walikuwa wameshamgundua?

    Amekwisha!

    “Mheshimiwa Salum Zakwa Mnube, habari za saa hizi…” Dickson Kweka akamsalimia.

    “Nzuri…” Salum Zakwa akajibu kimkato!

    “Sisi ni wageni wako…” Kweka akamwambia kwa sauti ya kawaida tu, ambayo siyo ya kukomandi!

    “Wageni wangu?” Salum Zakwa akawauliza.

    “Ndiyo mheshimiwa…tunakuhitaji…”

    “Mnanihitaji mimi?” Salum Zakwa akaendelea kuuliza kana kwamba hakuwaelewa!

    “Hebu ninakuomba ushuke hapo juu, halafu uje tuongee vizuri. Mbona unatuacha sisi tumesimama hapa chini. Fanya uungwana kidogo,”

    Dickson Kweka akaendelea kumwambia.

    “Sawa,” Salum Zakwa akasema huku akinyanyuka. Kisha akashuka akitumia ngazi iliyokuwa inatokeza upande wa nyuma, halafu akawafikia makachero wale waliokuwa wamefika pale.

    “Hamjambo lakini!” Salum Zakwa akawaambia.

    “Sisi hatujambo mheshimiwa…” Dickson Kweka akamjibu.

    “Haya, nimefika, sema shida!” Salum Zakwa alisema huku akijiamini na kujifanya kuuondoa ule woga aliokuwa nao tangia mwanzo.

    “Kwa ufahamisho, mimi ni Kamishna Msaidizi wa Polisi, Dickson Kweka, na hawa wengine ni makachero, Inspekta Raymond, Benito na Dani. Nafikiri tunafahamiana vizuri sana!”

    “Ndiyo, wewe nakufahamu vizuri sana…”

    “Hawa wengine je?”

    “Ah, mimi siwezi kuwafahamu watu wote!” Salum Zakwa akasema kwa dharau na kuongeza. “Jiji hili lina watu wengi sana, na mimi nikiwa mtu mkubwa, hufahamiana na watu wengi sana!”

    “Najua kuwa unakutana na watu wengi sana, lakini ninakuomba ujiandae na kuongozana wote kuelekea kwenye Kituo cha Kati cha Polisi…” Dickson Kweka akamwambia kwa sauti ya amri ya kipolisi!

    “Kwani nimefanya nini? Mbona mnanisumbua Jumapili yote hii?”

    “Ndiyo hivyo, tunakuhitaji kituoni, mambo yote yataongelewa huko. Wewe kama mheshimiwa tunakuomba utii amri hiyo, kumbuka Kutii Sheria bila Kushurutishwa!”

    “Ok, ngoja. Nisubirini hapo!” Salum Zakwa akasema, kisha akageuka na kuondoka kuelekea ndani ya nyumba yake. Makachero wale wakabaki wakimwangalia tu!

    Hawakumwelewa!

    “Ana maana gani?” Dickson Kweka akauliza huku akiwaangalia makachero wake!

    “Hatumwelewi afande!” Benito akasema.

    “Labda ana maana yake!” Dani akaongeza kusema.

    “Sasa tufanye nini afande?” Benito akamuuliza Dickson Kweka, mkuu wake wa kazi, ili awape amri cha kufanya dhidi ya Salum Zakwa!

    “Huyo lazima akamatwe, tujiandae kwa lolote!” Dickson Kweka akawaambia. Halafu makachero wale wakapeana ishara na kukaa tayari kwa kumkamata!

    Hazikupita dakika tano, kwani Salum Zakwa alitoka mle ndani kwake akiwa amekamata bunduki aina ya ‘Rifle Pump Action,’ huku amekunja sura yake! Akasimama pale barazani huku akiwaangalia makachero wale waliokuwa wakimsubiri kujua atafanya nini!

    “Ninajua kuwa nyie ni Maafisa wa Polisi…” Salum Zakwa akasema kwa sauti kubwa halafu akaendelea. “Naomba muondoke haraka sana kabla sijawajeruhi kwa risasi!”

    “Huyu mwendawazimu nini?” Dickson Kweka akasema huku akiwaangalia wenzake, Benito, na Dani. Kweli hakutegemea kitu kama kile, ukizingatia aliyaelewa madhara ya risasi! Huua mara moja!

    “Afande, huyu ni chizi!” Kachero Inspekta Raymond akasema!

    “Damu zimemdhuru!” Akadakia Dani!

    “Mtieni mbaroni!” Kweka akatoa amri!

    Lakini kabla makachero wale hawajapanga la kufanya, Salum Zakwa alifyetua risasi mbili kuwaelekezea pale walipokuwa wamesimama. Risasi zile zilichimba ardhi bila kuleta madhara yoyote! Wote wakaruka kiufundi, na kujibanza kwenye magari mawili yaliyokuwa yamepaki kwenye maegesho. Halafu wakachomoa bastola zao tayari kwa kukabiliana naye! Walijua kuwa yule alikuwa nui mwanajeshi na mbinu zote alizijua!

    Kosa moja, bao moja!

    Baada ya makachero wale kujificha katika magari, Salum Zakwa alijizatiti na kufyetua risasi ovyo, ambazo nyingine ziligonga kwenye vioo vya magari yale na kuvivunja. Ni hadi risasi zilipomuishia katika bunduki ile inayobebea risasi kumi tu. Purukushani ile iliifanya familia nzima itoke nje baada ya kusikia ile milo ya risasi, na hata majirani wa mitaa ya karibu walitoka wakijua labda walikuwa ni majambazi, hasa ukizingatia eneo lile la Upanga Mashariki walikuwa wanaishi watu wastaarabu na kulikuwa kumetulia.

    Mkewe, Bi. Husna, hakuvumilia baada ya kuona aliyokuwa anafanya mume wake. Yalikuwa ni mambo ya kutia aibu hasa ukizingatiaalikuwa ni mtu mkubwa serikalini, ambaye ni mfano bora kwa jamii. Hivyo Bi. Husna akanyanyua za haraka, huku umbile lake kubwa likimpa shida, na kumwendea pale aliposimama mume wake, aliyekuwa bado ameikamata ile bunduki ilioyokuwa inafuka moshi wa baruti!

    “Mume wangu unafanya nini? Umechanganyikiwa?” Bi. Husna akamuuliza!

    “Tafadhali!” Salum Zakwa akamwambia na kuongeza. “Niachie usinishike!”

    “Nikuache vipi wakati unapiga risasi ovyo mume wangu…oh!” Bi. Husna akaendelea kuuliza huku akiwa na wasiwasi!

    “Ngoja niwaonyeshe kazi hawa askri!” Salum Zakwa akasema huku akichomoa bastola kutoka nyuma ya mgongo wake kiunoni!

    “Achaaa!” mkewe akamsihi.

    “Toka hapa” Salum Zakwa akamwambia huku akimsukuma mke wake, ambaye alidondoka chini na kubaki akigaragara kutokana na umbile lake kubwa na uzito aliokuwa nao!

    “Mtumeee!” Akapiga kelele mkewe! Lakini yeye hakuwa na habari naye zaidi ya kutaka kupambana na makachero wale waliomwingilia katika himaya yake!

    Wakati wote huo, makachero wale, wakiongozwa na mkuu wa kitengo, Dickson Kweka, walikuwa bado wamejichimbia katika ubavu wa yale magari. Hata hivyo, Raymond akamwuliza mkuu wake:

    “Afande, tufanyaje sasa?”

    “Tusubiri kwanza. Si mnajua kuwa huyu ndiye mhusika mkuu, na hapaswi kuuawa?”

    “Hilo naelewa afande!”

    “Basi tuvute subira tutampata tu!” Kweka akasema. Halafu wakati huo Salum Zakwa alipokuwa akibishana na mke wake, yeye akatumia mwanya huo na kujisogeza kando jirani yake.

    “Tafadhali sana Kamba, jisalimishe!” Dickson Kweka akapaaza sauti.

    “Siwezi kujisalimisha mimi. Nyie ni watu wadogo sana!” Kamba akasema huku akitamba eneo zima kwa kiasi fulani alifurahia tukio lile kwa kuona makachero wale wa polisi, walivyokuwa wamejificha na kumwogopa!

    “Narudia tena…jisalimishe. Huko ni kutotii amri halali ya polisi!”

    “Siwezi kujisalimisha kamwe, labda ajisalimishe maiti yangu, na siyo zaidi ya hapo!” Salum Zakwa akaendelea kusema. Halafu kwa kitendo ambacho hakuna mtu aliyekitegemea, akajielekeza bastola kichwani mwake!

    “Unataka kufanya nini?” Dickson Kweka akamuuliza!

    “Mimi siyo mjinga! Najua adhabu ambayo inanikabili mbele yangu baada ya nyie kunikamata nikiwa hai. Hakika ni fedheha kubwa kwa mtu kama mimi mtumishi wa Serikali kukumbwa na kashfa hii, hivyo sipaswi kuishi katika ulimwengu huu!”

    “Ooohps!” Bi. Husna akapiga kelele kumwambia mume wake!

    “Mke wangu hilo halikuhusu kamwe! Cha muhimu wewe kutunza familia hii nitakayoiacha!”

    “Oh!” Bi. Husna hakuwa na la kufanya. Akabaki amesimama huku akiwaangalia makachero wale, ambao ndiyo alioona wangeweza kuyaokoa maisha ya mume wake!

    Hata hivyo, Kachero Inspekta Raymond, aliamua kutumia mbinu za kumnyatia Salum Zakwa kwa upande wa nyuma yake. Akazungukia sehemu iliyokuwa na bustani na maua yaliyofungamana, karibu na uzio. Baada ya kufika, akabanisha sehemu hiyo ambayo aliweza kumwona vizuri jinsi alivyokuwa akilumbana na mke wake, na pia kajiwekea bastola kichwani mwake tayari kwa kufyetua. Sehemu hiyo aliyobanisha, aliweza kuwaona wale makachero wawili, Benito na Dani, hivyo wakawa wanapeana ishara ya kitu gani cha kufanya ili waweze kumdhibiti na madhara yasitokee.

    Akili ya haraka ilimjia Dickson Kweka, ambaye alikuwa ameshauona mchezo mzima aliokuwa anaufanya Raymond, hivyo akatoa ishara fulani kwa Raymond, ambaye alinyanyua bastola yake na kufyetua risasi moja kuelekea kwenye pipa moja tupu lililokuwa jirani na Salum Zakwa. Baada ya pipa lile kupigwa risasi, lilitoa mlio fulani uliotokana na mlipuko wa baruti, ambao ulimshtua mtu huyo aliyekuwa na ndoto ya kujimaliza! Akashtuka kuacha!

    Kachero Inspekta Raymond aliyekuwa anamnyemelea, akamfikia kwa nyuma yake. Akaipiga teke ile bastola iliyokuwa mkononi mwake, na kuifanya iruke mbali! Salum Zakwa akachanganyikiwa na kutaka kurusha ngumi, lakini akawa amechelewa! Akakutana na mtutu wa bastola!

    “Usijiguse! Simama ulivyo!” Kachero Inspekta Raymond akatoa amri!

    “Ahahahaaa!” Salum Zakwa akacheka kidogo kicheko cha uchungu, na kuendelea. “Unastahili sifa kijana. Tena unastahili kuongezwa cheo!”

    “Sisi siyo wapumbavu! Tulijua kuwa ni lazima tukupate ukiwa hai, daima mbio za sakafuni huishia ukikongoni!”

    “Oohps! Na kweli!”

    “Lete mikono yako!” Kachero Inspekta Raymond akamwambia akiwa tayari kumfunga pingu!

    “Nimepatikana!” Salum Zakwa akasema. Hakutegemea yale yaliyotokea, lakini ndivyo iliovyokuwa!

    Hatimaye akafungwa pingu mikononi!

    Makachero, Benito na Dani, walibaki wakimpongeza Raymond kutokana na ule ujasiri aliopufanya, na kufanikiwa kumdhibiti Salum Zakwa Mnube aliyekuwa tayari kujitoa uhai wake baada ya kuona maji yalikuwa yamemfika shingoni. Bila kupoteza muda walimpakiza ndani ya gari alilokuwa anatumia Dickson Kweka, huku akiwa chini ya ulinzi, tayari kwa kupelekwa katika Kituo cha Polisi kwa hatua zaidi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Msafara wa kuelekea katika Kitu Kikuu cha Polisi ukaanza mara moja huku familia yake pamoja na majirani zake wakishangaa kwa kutojua kilichokuwa kinaendelea. Msafara huo ulifika kituoni na wakati Salum Zakwa anafikishwa, ni wakati huohuo kijana Bosco Zambi alikuwa anafikishwa akitokea mkoani Morogoro, alipokuwa amekimbilia baada ya kukurupushwa jijini Dar es Salaam usiku ule wa mauaji ya kutisha.

    Bosco alifikishwa pale kituoni akiwa chini ya ulinzi mkali wa askari polisi aliotoka nao huko. Salum Zakwa na Bosco Zambi walipotupiana macho na kuonana, kila mmoja alimshangaa mwenzake, hasa Zakwa akishangaa kwa polisi walikuwa wamemkamatia wapi Bosco, mtu ambaye naye alikuwa akimwinda ili ammalize! Wote wakatikisa vichwa na kutabasamu. Kwa vyovyote walijua kuna adhabu kubwa iliyokuwa inawakabili mbele yao!



    MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Blog