Simulizi : Sayari Ya Kifo
Sehemu Ya Tatu (3)
“Ha! Yaani mbona hapo ndio bado kabisa, we ulichokifanya uliona sawa eti? Sasa hapo mi ndio sijaanza ujue? Hapa najaribu tu mume, subiri action!” akasema akicheka na kuzunguka kuelekea alipo mumewe na kuanza kumfungua viatu, kisha shati na mwisho akamnyanyua kuelekea ndani.
Inspekta Kalindimya alikuwa kama zoba tu, hasira zote hata hakuelewa ni wapi zilipotelea, yale maswali yote aliyokuwa akijiuliza, sasa yalikosa majibu na hakuweza kuuliza.
Alikuwa kama Kondoo kwa mkewe, aliburutwa huyo hadi chumbani alipopelekwa kuogeshwa kabla ya kufikishwa mezani kwa ajili ya chakula cha usiku ambacho kilikuwa tayari kimeandaliwa.
Inspakta Jitu alikaa kituoni kwa dakika kama 7 ama nane hivi, kijana akaingizwa na kushangaa kumkuta mtu ambae anatafutwa yupo pale, kabla hajasema lolote, akasikia mmoja kati ya wale askari waliomkamata akimwambia Jitu kuwa wamempata.
“Safi sana, kazi nzuri vijana,” alisema huku akimpa mkono Yule kijana na kumkaribisha. Kijana alionekana kusitasita kidogo lakini baada ya sekunde kadhaa akaupokea mkono na kuketi pale ambapo Jitu alimuonesha.
Inspekta alipelekwa bafuni moja kwa moja na mkewe, wakaoga pamoja na baada ya kumaliza kuoga wakatoka kwa ajili ya kwenda kula, wakiwa mezani wanakula na kufurahia siku yao, simu ya mkononi ya Inspekta Kalindimya ikaita.
Jitu akiwa amekati ana kwa ana na kijana Yule aliemuagiza aletwe, akaanza kufanya mahojiano nae. Jambo la kwanza kumuuliza baada ya kumjua jina ni kumuuliza ni gari gani iliyomleta Yule marehemu pale uwanjani?
Kijana akasema kuwa aliiona aina Fulani hivi ya gari kama Land Cruiser, ilikuja na kupaki pale usawa wa mti, tena ikiwa na mwendo wa taratibu sana.
“Ni hali ya kutokuwa makini tu bro, ujue ile gari ilipofika pale walifungua milango kwanza ikawa wazi na jamaa wakawa kama vile wanapiga story milango ikiwa wazi, tena eneo hilo la jirani watu walikuwepo, lakini wala hatukushughulishwa na kufuatilia,” aliongea kwa kirefu kijana huyo baada ya kuaswa na Jitu kuwa yeye mwenyewe anajua pale alipo ni wapi, hivyo ujanja wake wowote utasababisha abaki pale hadi wakati ambao atakuwa tayari kusema ukweli.
Hicho ndio kilisababisha kijana awe mkweli, maana asili ya mateja ni kuliogopa gereza kuliko hata askari ambao ndio wamiliki wa gereza. Jitu akamuuliza;
“Je kuna pikipiki yeyote mliiona eneo la tukio?”
“Hapana, ila zilikuwa zinapitapita tu, lakini pale jirani na gari hapakuwa na pikipiki,” alifafanua na kisha akabaki akisubiria swali lingine.
Maswali yaliyofuatia, hayakuwa muhimu sana, ila baada ya kuridhika na kile alichokipata, Jitu akamtaka askari mmoja kwenda na kijana huyo hadi kwao ili aweze kupatafuta pindi ambacho watakuwa wakimuhitaji.
Inspekta Kalindimya akaipokea simu ile na kuongea nayo kwa dakika kadhaa, baada ya kumaliza maongezi yake akashusha pumzi kwa nguvu na kumtazama mkewe ambae nae alikuwa akimtazama yeye.
Alisita kumsemesha, maana alikuwa na hakika kabisa kwamba atakuwa amesikia kila kilicho zungumzwa, Zuwena akawa kimya tu akimtazama mumewe ambae muda huo akaegamia kiti na kushusha tena pumzi kwa nguvu.
Kila mtu alikuwa na akili tofuti na mwenzie, Inspekta alikuwa akiwaza jinsi ya kuaga kuondoka nyumbani, Zuwena nae alikuwa akifikiri ni hadi lini watakuwa na maisha ya aina hii? Mapumziko saa moja kazi masaa 23, alikasirika.
Hata kabla Inspekta hajafunua mdomo, Zuwena akanyanyuka kwa hasira na kuelekea ndani kwao, Inspekta nae akanyanyuka na kumfuata mkewe ambae alionekana kama amefura kwa hasira.
Alimkuta amejitupia kitandani, dalili ya mayonzi usoni, ishara kabisa macho yake yalikuwa yameanza kujaza machozi kwa ndani, ni neon moja tu lingeweza kupasua mirija ya machozi na kuanza kumwagika shavuni.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Zuwena alikuwa na dukuduku kubwa moyoni, Inspekta akawa tayari ameliona hilo, akataka kulidhibiti, lakini sasa anaanzaje hadi kulidhibiti? Akakosa jibu.
Pembeni ya kitanda, ndio aliketi Inspekta na kujishauri jinsi ya kumuaga mkewe, akainama na kumkiss shavuni, Zuwena akamzuia na kumwambia atoke aende.
“Si umeitwa kazini kwako huko? Yaani wewe nae unaitika tu kukubali, bila kuwaambia kuwa wewe nae kuna watu wanatakiwa wawe nawe muda wa mapumziko?” hapo ndio sasa kilio kikaanguka.
“Mke wangu, hii ni kazi, na hii kazi ndio ambayo ilitukutanisha mimi nawe, na sasa umesikia mwenyewe kuwa kuna uvamizi na mauaji, bila kulishughulikia tatizo hili mapema mke wangu, kesho inaweza kutukuta hata sisi, naomba niende mke wangu ukiwa radhi,” aliomba Inspekta kwa mapenzi makubwa.
“Ndio kwanza umeingia sasa hivi humu ndani, hata saa moja haijatimia, unaniomba mimi tena utoke, unaniomba mimi kama nani sasa?” alisema kwa sauti ya ghadhabu hasa.
“Zuwena wewe ni mke wangu kipenzi, napaswa kukujulisha kila kitu na ndio maana ninakuomba ili nitoke wewe ukiwa na ridhaa, kwani ridhaa yako ndio mafanikio yangu, Please my love, naomba uniruhusu niende,” aliomba Inspekta Kalindimya huku akimshika shika sehemu za usoni.
“Sasa nani amekuzuia wewe usiondoke? We unaweza kwenda tu, mi nimeanza kuzoea sasa, ila tambua kuwa maumivu yana mwisho,” akasema na kuvuta mto, akajilaza kwa kugeuka upande wa pili.
Inspekta alionesha kama hakujali vile, lakini moyoni ilimgusa, hasa pale aliposema
“Tambua kuwa maumivu yana mwisho,” hiyo ilikuwa ni kauli tata toka kwa Zuwena kwenda kwa Inspekta. Ila vivyo hivyo akanyanyuka na kuvaa, kisha akambusu mkewe na kutoka, akafunga mlango kwa nje na kuondoka.
Aliingia ndani ya gari huku akitafakari maneno ya mkewe,
“Hivi ina maana kuna siku atashindwa kunivumilia ama amemaanisha nini? Huenda ni hasira tu ambazo zimemfanya aropoke na maneno kama haya, lakini ukiangalia upande wa pili…”
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mawazo yake yalikatishwa na honi aliyokuwa anapigiwa na madereva wenzie waliokuwa nyuma yake kutokana na kwenda kwa mwendo mdogo mno ambao ulisababisha foleni.
*******
Saa mbili kasoro robo, Jitu alikuwa anawasili kituoni ili kuja kuweka rekodi juu ya kile alichokipata huko atokapo. Akiwa napaki pikipiki, akishangaa kuiona gari ya Inspekta Kalindimya ikiwa imepaki hapo.
Tayari waliagana kuwa watakutana sikuifuatayo, sasa imekuwaje tena awepo kazini usiku ule? Akahisi hali si shwari, ni lazima kuna tatizo tu lililomfanya mkuu wake awepo pale.
Akashuka na kuielelekea gari hiyo moja kwa moja kuikagua kama Inspekta yupo mle ama lah! Hakumkuta, akageuka pande hii na ile, lakini wala hakumuona pale nje, basi akaazimia kuelekea ndani.
Kule ndani alimkuta Inspekta akiwa amesimama na vijana wawili ikiwa inaonesha kama kuna habari nyeti wanampa, akamsalimia mkuu wake na kumwambia anamsubiri ofisini.
Inspekta akamwambia aende hapo kuungana nao asikilize mwenyewe kwani kuna tukio limejiri na amepigiwa simu haraka afike kituoni hapo.
“Ndio maana nimeshangaa kukukuta hapa saa hizi,” aliongeza Jitu huku akiwasogelea pale walipo Inspekta na askari wenzie.
“Inspekta Jitu, kwa kuwa wewe upo nyuma ya wakati ni kuwa, nimeitwa hapa kutokana na suala la Kelvin, unakumbuka jina hili?” alimuuliza akimtazama.
“Yeah! Nakumbuka jina hili, kwani ni jina la mtu ambae hadi sasa hatujui alipo na tunaamini tukimpata ndio tutapata muhusika mkuu wa kifo cha Allen,” alijibu kirefu.
“Ok! Kifupi ni kuwa, niliwapa kazi vijana hawa wawili wamtafute huyo Kelvin na pia niliwapa Plate namba za pikipiki kama ulivyonitajia hapo awali, ndio wamenijulisha kuwa wamepata mrejesho,” alijibu huku akiwatazama kwa zamu wale vijana.
Mwisho akarejesha macho yake kwa Jitu ambae alionesha kama kuwa na swali kwenye uso wake, Inspekta akaendelea
“Kutokana na uzembe wa kazi tulionao ndani ya jeshi letu na utendaji kazi mbovu, nasikitika kukujulisha kuwa mtu tunaemtafuta kwa zaidi ya siku moja, tunae mikononi mwetu na hatujui kama tunae hadi tuambiwe na watu wengine nje ya sisi,”
Inspekta Kalindimya akasema huku akitikisa kichwa na kuanza kuondoka taratibu akiwaacha wenzie wamesimama.
Jitu kama alieshikwa na mshangao hivi, ndio akamuuliza Inspekta kama mtu huyo anaemzungumzia ni Kelvin?
“Ndio yeye hasa, wamemkuta kituo cha Polisi Usalama Bunju, sehemu ambayo wewe pia ulikuwepo, tena amekutwa na Pikipiki ileile ambayo wewe ulinitajia namba zake, Inspekta Jitu, lawama za kwanza kwako, naomba uongeze umakini kwenye kazi yako, kwa hili unapaswa kulaumiwa, twende ofisini kwa maongezi zaidi,” taratibu akaanza kuondoka.
Alimbadilikia Jitu ambae nae sasa alijiona kama ni Zoba, Jitu nae akawaambia wale vijana waende kuendelea na kazi hadi watakapohitajika tena, wataitwa.
Nae kwa mwendo wa haraka akaanza kumfuata mkuu wake kuelekea ndani ambapo alimkuta akiwa ameketi kwenye kiti chake akitazama mlangoni kama mtu anaetegemea mtu muhimu kuingia.
Jitu alifika na kuketi mbele ya Inspekta ambae alimuuliza juu ya huko alipokuwa nae akamueleza alichokipata, Inspekta akamwambia kitu cha kufanya ni kumuagiza Kelvin aletwe pale Oysterbay haraka iwezekanavyo na ikiwezekana usiku uleule ili siku ifuatayo waweze kumuhoji wao wenyewe.
Jitu akanyanyuka muda huohuo na kutoka nje ambapo alienda Counter na hapo alikuta vijana wawili wakibishana na askari mmoja kuhusu kumuona Mkuu wa kituo cha Polisi muda uleule.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Jitu wala hakuwajali, bali alinyanyua simu na kupiga kituo kidogo cha Polisi Bunju na kutoa maelekezo kuwa mtuhumiwa mwenye jina la Kelvin anaijiwa muda huo na askari kutoka kituo cha Oysterbay.
Baada ya hapo akarejea ndani kwa wale vijana wawili na kuwaamuru wakamlete Kelvin na kumuhifadhi kwenye selo ndogo iliopo ndani ya ofisi ya Inspekta Kalindimya.
*****
Range Rover aina ya VG ya rangi ya Bluu Metallic ambayo sasa ilitaka kushabihiana na Nyeusi, ilionekana ikipaki pembeni ya geti la nyumba moja ghali mno kwenye Mtaa wa Makolokocho, Eneo la Uzunguni huko Mbezi.
Baada ya injini kuzimwa, kwa pamoja milango yote mine ikafunguliwa nusu, kama watu ambao walikuwa wamepanga, wakateremsha miguu yao kwa pamoja, hivyo miguu minne, mguu mmoja toka kwenye kila mlango ikaonekana imevalishwa kiatu cheusi, ambacho japo kilikuwa ni cha kudumkiza, lakini hakikuwa cha kamba.
Kisha tena kwa pamoja, milango yote sasa ikafunguliwa hadi mwisho na vijana wanne walio onekana kama ni mashababi hasa wakateremka. Walikuwa ni nadhifu hasa, kiasi ambacho walivutia na kuonekana kama ni wafanyabiashara wakubwa mno ama ni viongozi wa juu sana wa kiserikali ama Kitaifa.
Hiyo ilitokana na aina ya mavazi waliyovaa, walikuwa wamejivika mavazi ya suti ya Bluu ilioiva sana ambayo ilikuwa imeshabihiana na nyeusi kiasi ambacho kwa mtu yeyote alie mbali akiambiwa ni Bluu, basi ni lazima akatae.
Baada ya kushuka, wote walisimama na kutazama mbele huku wakigeuza vichwa vyao kila upande kama kwamba ni watu ambao wanatafuta kitu Fulani.
Waliporidhika juu ya kile walichokuwa wakikitazama, kwa wakati, kila mmoja akajitengeneza, walikuwa ni kama ‘Models’ huyu alijitengeneza ukosi wa shati lake, Yule alijiweka sawa kwa tai yake.
Wakati huyu mwingine akijirekebisha miwani na Yule wa mwisho alijiweka vizuri kwa kurekebisha, kifupi kila mmoja alijiweka vizuri, kisha wakafunga milango yao na Yule alieonekana kuwa ni dereva akabonyeza kitufe mkononi maalum (Remote) na kulock milango.
Kijana Raymond, ni mfanya biashara ndogo ndogo Jijini Dar Es Salaam, wakati huu alikuwa kwenye mishemishe zake kwenye viunga vya mitaa hii katika harakati za kusaka ugali wake wa kila siku.
Gari hiyo aina ya Range Rover ilikuwa imempita kwa mwendo wa taratibu kwenye mtaa huo tulivu, hivyo aliweza kuona kila kitu kilichokuwa kikiendelea hasa ukizingatia gari hiyo ilisimama mita 100 tu kutoka pale alipokuwa yeye akitembea kuelekea huko ambapo wao wamesimama.
Kutokana na kuwa na mambo mengi kabla hawajaanza kuteremka kuelekea lilipo geti, sasa Ray aliweza kuwa karibu yao hata kuwaona na kuwatambua watu hao ambao sasa walikuwa wamebakiza hatua chache kulifikia geti lililokuwa mbele yao.
Kama mtu ambae amefumbuliwa macho ghafla na kukutana na kitu ambacho alitamani kukiona, Ray alimtambua mmoja kati ya wale vijana wanne.
Akajikuta akiropoka na kuita kwa sauti ya juu, tena kwa mzuka kutokana na kumuona mtu ambae hakutegemea kumuona pale, tena akiwa kwenye hali ile.
“Brother chidii…” japo hakuwa mbali, Raymond alimuita kwa sauti ya juu sana ambayo iliwashitua wote na kumtazama kisha wakamtazama chidii wote kwa pamoja.
Walimuona chidii ameuma mdomo wa chini nakukunja uso kwa hasira,Dega akajishika kiunoni na kutaka kutoa bastola wakati huo Ray akisogea na tabasamu usoni Chidy akamzuia Dega na kurudisha jicho kwa Ray ambaye sasa alikuwa amefika.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Vipi Brother chidi?” hiyo ndio ilikuwa salamu yake huku akimpa mkono.
Chidy akatikisa kichwa bila ya kumpa mkono bali akaangalia huku na kule na kurudisha macho yake kwa Ray na kumuuliza yeye ni nani?
Ray sasa akiwa amepoteza kiasi katika kujiamini, akajitambulisha. Chidy bila ya kujionyesha kama amemuelewa ama lah, akamgeukia Dega na kumnyoshea mkono, ishara ya kupokea kitu.
Ray muda wote alikuwa akiutazama mkono wa Chidy, Dega akatoa bastola iliyokuwa na kiwambo cha kuzuia sauti na kumkabidhi bosi wake.
“Siku zote katika matembezi yako, ukikutana na mtu unaemfahamu kwa jina, usimuite kwa jina lake, muite kwa jina lolote unaloliona linafaa na halitomkwaza, kama naye anakujua, basi sauti yako itamfanya ageuke na kukutazama, sasa kwa kosa ulilonitendea leo nakupa adhabu ndogo, kwa kuwa ni kosa la kwanza, leo nitakupa onyo ili usije kurudia siku nyingine, kenge wewe, mschss,” akasonya Chidy na kumfanya Ray ajikute anaweka sufuria zake chini ili kupiga magoti kwa nia ya kuomba msamaha.
Mmoja kati ya wale vijana ambae alikuwa ni dereva akamsukuma chini kwa mguu wake wa kushoto aliomuwekea kifuani na Ray akaanguka chini kichalichali, Chidy akasogeza risasi kwenye Chemba na kumtwanga ya kwenye mguu wa kushoto huku akimzuia kupiga kelele kwa kuweka kidole chake cha shahada mdomoni.
Dega akapokea bastola toka kwa Chidy huku Ray akigalagala kwa maumivu kisha Chidy akamtazama Willy aliyekuwa pembeni yake na kumpa ishara Fulani ambayo hata Ray aliyekuwa amelala chini akilia kwa maumivu aliiona.
Baada ya Ray kuona ishara hiyo, ndio akazidisha kilio na kuomboleza na wakati huohuo watu watatu walianza safari ya kurejea garini wakimuacha Willy akiwa amesimama.
Unaweza kuendelea kutokea hapa sasa!
Kurudi kwao garini kulimanisha kuwa waghairi kile walichopanga kufanya, Willy aliebaki na Ray, akaingiza mkono juu ndani ya koti la suti aliovaa na huku gari ikisikika ikiwashwa.
Willy hakugeuka nyuma bali aliinama chini na kuchuchumaa Ray chozi lilizidi kumdondoka, alionesha kama ameyasahau maumivu ya risasi ya mguu na sasa alikuwa akilia kwa ajili ya maombolezo ya kunusuru maisha yake ambayo aliona kama yapo mikononi ya mtu huyu aliyebaki naye.
“Kilichokusaidia na kubaki hai hadi sasa hapa hakuna mtu hivyo hakuna aliye kusikia, lah sivyo ungetangulia kuzimu bwege we…” kisha akatoa mkono wake na hapo Ray akafumba macho huku akili yake ikimrejesha nyumbani kwao kwa kumkumbuka mama yake ambae alikuwa akimzuia kuja Jijini Dar.
“Mwanangu Dar kuna mengi, pambana hapahapa tu mbona unaweza tu kuchomoka kimaisha?” hayo ni mawazo yaliyopita kwenye mishipa yake ya fahamu kwa mwendo wa kasi ya upepo kwani aliamini ndio mwisho wa maisha yake.
Mkono wa Willy ulipochomoka kutoka kwenye koti lile, haukutoka na Bastola kama ambavyo Ray alidhania, bali ulitoka na kibunda cha noti kifuani huku akimpiga piga kwa mkono wake kwenye shavu kwa vikofi laini, akanyayuka na kumwambia
“Ole wako useme lolote kuhusu jambo hili, utakufa kimyakimya nyoko wewe,” akageuka na kumuacha Ray ambae alikuwa hajiamini kama ameachwa hai, kalala chini anatikisa kichwa kukubaliana na hilo.
Tayari gari ilikuwa imegeuza na sasa ilikuwa kwenye mwendo uleule wa taratibu mno na iliwakaribia pale walipo Willy na Ray, ikasimama na Willy akaingia garini na kuanza kutokomea kila mmoja kiwa na fikra zake kichwani.
Kabla hata hawajatoka eneo hilo, simu ya Chidy ikaita, aliitazama na kuipokea pasina kusema chochote, ila ilionekana kama upande wa pili ulikua ukiongea, kwani alisikika Chidy akiuliza ‘Wapi?’ kisha akasema ‘Tunakuja’ akakata simu na kusema neno moja tu kwa hasira kumwambia dereva ambae bado hakujua muelekeo wake, akasema Chidi;
“Tegeta, haraka.”
*****
Kaunta ya kituo cha Polisi cha Bunju, jalada limewekwa juu ya meza, Kelvin analetwa na kupewa mkanda avae, kisha sambamba na askari waliokuwa wakilikagua jalada, wakalifunga na kutoka.
Pingu ikiwa mikononi, akaingizwa ndani ya gari aina ya Land Rover Pick Up na kuondoka nae wakiwa askari wawili na dereva mmoja ambae nae pia ni askari.
Wakiwa kwenye mwendo mkali wanaliacha eneo la Bunju, wakiwa wanaikaribia njia panda ya kwenda kawe, gari moja aina ya Land Cruiser VG iliokuwa ikija kwa nyuma yao, ikawapita kwa mwendo wa kasi mno na ilipowavuka tu, ikakatisha ghafla na kuingia upande wao kwa mbele kidogo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Haikutoa ishara yoyote ya kuingia upande wao, kama si umahiri na umakini wa dereva wa gari ile ya Polisi, basi ingetokea ajali mbaya mno.
Upande wa pili, mtu aliekuwa akiendesha gari ile, hakuwa amekosea kile alichofanya na wala hakufanya kwa bahati mbaya, hapana, bali alikuwa amedhamiria kabisa juu ya kitendo hicho.
Kwani baada ya kunusurika tu kutokana na ajali hiyo, ingekuwa ni bahati mbaya angesimama ama hata angetoa ishara Fulani, lakini yeye haikuwa hivyo, bali aliongeza mwendo zaidi ya ule wa awali.
Ikamlazimu sasa dereva wa gari ya Polisi sasa nae aongeze kasi ili kumfikia mtu alie mbele yake. Dhamira hiyo haikuwa nzuri kwake, kwani ilikuwa ni kosa kubwa sana, maana ghafla tu ilitokea pikipiki aina ya Boxer na kutishia kuingia upande ule alipo yeye.
Ikabidi tena apunguze mwendo kwa kukanyaga breki kwa nguvu, gari ikasota kwenye barabara hiyo pana na bahati mzuri haikutoka nje ya barabara kutokana na kingo zilizokuwepo.
Hali hiyo ndio ikampa nafasi nzuri kabisa dereva wa pikipiki na sasa akaingia mzima mzima upande ilipo gari ya Polisi na kuanza kwenda mbele ya gari la Polisi kwa mwendo wa taratibu mno.
Kwa kuwa alikuwa yupo katikati ya barabara, aligeuka na kuwa ni kigingi cha kuzuia gari la Polisi kwenda kwa mwendo kasi, ikalazimika gari ya Polisi itembee mwendo autakao yeye dereva wa Bodaboda.
Jazba ikawapanda wale maaskari lakini mwenzao alikuwa amejipanga na alitambua ni nini anataka pale na pia alijua nini anafanya, sasa badala ya kwenda ule mwendo mdogomdogo aliokuwa akienda nao, ndio akasimama kabisa kama kwamba ameharibikiwa na pikipiki yake.
Ilikuwa ni jirani kabisa na kona ya Kawe, askari mmoja akashuka kwa ghadhabu na kumsogelea Yule bodaboda akiwa amejiandaa kumpiga hata makofi, maana alionesha ghadhabu mno usoni.
Lakini kabla hajamfikia, ilijitokeza ile Land Cruiser VG ya rangi ya Bluu na kupaki nyuma ya Pick Up kwa njia ya kuikatisha, hivyo gari ya Polisi ikawa imewekwa kati.
Mbele kulikuwa na Pikipiki ilioanguka barabarani na nyuma ndio hiyo gari ilizuia, kisha kwa mwendo wa kasi…
Wakashuka vijana watatu na kuivamia ile Pick Up ya Polisi, wakiwa na silaha nzito mkononi. Wakawateka kiurahisi sana askari waliokuwa ndani ya gari ambao walikuwa hawajajiandaa kwa lolote.
Pamoja na Kelvin ambae hakuwa akielewa lolote, aliwatazama tu waliokuja na suti kali na kuwataka watulie.
Askari aliekuwa chini, ndio kidogo alionesha uhai na hata kutaka kujaribu kupambana na wale walioshuka kutoka garini ambao wawili walikuwa wamempa mgongo na Yule wa tatu alionekana kama yupo na lengo Fulani tu garini.
Hakuonekana kuhangaishwa na mtu yeyote tofauti na akili yake kuwa imezama garini, huyo ndio askari wa chini aliona anafaa kuanza nae, hawa hawakuonesha tena kuwa ni wema.
Akampa mgongo na kuchomoa Bastola yake ili atakapo geuka afanye maangamizi, lakini kumbe alikosea, Yule aliedhani ni abiria yaani dereva wa pikipiki, kumbe alikuwa ni mwenzao.
Alikiona kitendo cha Askari Yule kuchomoa bastola, nae akaitoa ya kwake haraka na kumtandika risasi moja ya kifua, risasi iliyompeleka moja kwa moja chini huku wenzie wakishuhudia.
Wakati huo japo walikuwa na silaha, lakini walishindwa kujitetea kwani nao walikuwa wamewekekwa chini ya ulinzi. Yule jambazi mmoja akafungua mlango na kuchukua silaha zilizokuwepo ndani ya gari na kumnyanyua Kelvin.
Kilikuwa ni kitendo cha chini ya dakika tatu, gari ikapotea ikiwa imemteka Kelvin pia wakiwa wamepora silaha zote zilizokuwa ndani ya gari ya Polisi huku dereva wa bodaboda akiwa nae amepotea.
Hakuna aliemuona ameelekea wapi huku akiwa ameitelekeza ile pikipiki palepale barabarani.
Japo tayari ilikuwa usiku umeingia sana, lakini raia walikuwa wamefika kwa wingi huku wakiwa wanataka kuichoma moto ile pikipiki ya majambazi ambao wao waliamini kuwa watakuwa wanamkomesha mwenye pikipiki.
Hawakujua kuwa wakiichoma pikipiki watakuwa wamepoteza ushahidi, hivyo ikalazimika mmoja kati wa wale askari wawili apambane hasa na kuzuia tukio hilo kutokea kwa kupiga risasi juu ili kuwatawanya raia.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Dereva wa gari ya Polisi kwa kusaidiana na raia wema wakamnyanyua askari mwenzao aliepigwa risasi na kumuingiza garini ili kumuwahisha hospitali kujaribu kuokoa maisha yake iwapo itawezekana.
Watekaji waliondoka wakielekea Kawe kwa mwendo wa kasi mno na baada ya Mwili wa askari aliepigwa risasi kuingizwa ndani ya gari, nayo ikaondoka kwa mwendo wa kasi kubwa kuelekea Mwananyamala hospitali.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment