Akamualika tena pale Hotelini kwake kwa ajili ya mazungumzo zaidi na kusaini mkataba wa hiyo deal. Wakiwa hapo hotelini watu wawili tu, Lustig pia akampa ombi maalumu bwana Andre Poisson kuwa amejitahidi sana kumpigia debe mpaka amepewa hiyo dili hivyo akamuomba 'asimsahau'.
Baada ya kusaini mkataba, Bw. Andre Poisson akalipia gharama ya kupewa hivyo vyuma (Eiffel Tower) pia akampa na asante Lustig. Yaani kwa maneno mengine akalipia gharama za kununua Eiffel Tower pia akatoa na rushwa kwa ajili ya kusaidiwa kununua mnara huo.
Baada ya kusaini na makabidhiano ya pesa kila mtu akaondoka na njia yake. Wiki kadhaa baadae ndipo ambapo Andre Poisson akang'amua kuwa ametapeliwa baada ya kutomuona tena Lustig na kukosa mawasilino naye.
Baada ya kugundua ametapeliwa Andre alijisikia aibu kubwa kiasi kwamba mpaka akashindwa kwenda polisi kwa kuhofia kuchekwa na jamii kwa kufanywa mjinga kiasi hicho kununua mnara wa serikali ambao ndio kama kitambulisho cha jiji la Paris. Ingelikuwa hapa Tanzania tungesema ni sawa sawa na mtu akuuzie ile sanamu ya askari pale posta. Ilikuwa ni aibu kubwa.
Mtikisiko wa mfumo wa Kibenki Marekani..
Baada ya pilika pilika za huku na huko na kukoswa koswa kukamatwa nchini Ufaransa kwani aliuza tena kwa mara ya pili Eiffel Tower na bwana huyu aliyemuuzia Mara ya pili alipogundua ametapeliwa hakukaa kimya kama Andre yeye akaenda polisi hivyo ikamlazimu Lustig akimbie Ufaransa kuhofia kukamatwa.
Baada ya kurudi marekani Lustig akaanza tena kuhangaika ili apate channel nyingine ya kujiingizia pesa kwa njia haramu.
Moja ya matukio aliyoyanya ilikuwa ni kumtapeli 'Baba wa wahuni' (Gangster's Godfather) wa kipindi hicho aliyeitwa Al Capone. Lustig alimfuata Capone na kumuomba amuazime dola elfu hamsini akafanyie 'dili'.. Capone akampa hiyo hela. Lustig akaenda kuiweka hiyo fedha benki bila kuifanyia chochote kwa muda wa miezi miwili kisha akaitoa na kumrudishia Capone akimlalamikia kuwa biashara aliyoifanya imefeli.
Capone akafurahishwa sana na 'uaminifu' wa Lustig kwamba licha ya kupata hasara kwenye biashara yake lakini amejitahidi kumrudishia fedha yake yote. Kuonyesha furaha yake na kumpoza Lustig kwa biashara kufeli akampatia dola elfu tano pasipo kujua kuwa hili ndio lilikuwa lengo hasa la Lustig toka siku alipokuja kumuomba hela.
Tukio lingine lilikuwa ni pale ambapo Lustig alimuuzia Sheriff kutoka Texas 'mashine ya kuprint hela'. Miezi kadhaa baadae Sheriff akafanikiwa kumkamata Lustig. Lustig akamuambia Sheriff kuwa kama atakubali wayamalize wenyewe bila kwenda kwenye vyombo vya sheria yeye yuko tayari kumlipa hela yake mara mbili zaidi. Sheriff akakubali na Lustig akamlipa hela yake mara mbili.
Kesho yake Sheriff alipopeleka hela benki kuzihifadhi akaambiwa kuwa zile pesa ni bandia.
Baada purukushani za huku na kule za kutafuta chaneli nyingine ya 'biashara' hatimaye Lustig akawakusanya mkemia aliyeitwa Tim Shaw, pamoja mtu maarufu wa kugushi aliyeitwa William Watts na wakaunda matandao hatari wa kutengeneza noti za kugushi za dola za marekani.
0 comments:
Post a Comment