Search This Blog

Saturday, 5 November 2022

MPITA NJIA - 1

 




IMEANDIKWA NA : IBRAHIM M. GAMA



*********************************************************************************



Simulizi : Mpita Njia

Sehemu Ya Kwanza (1)





Kundi kubwa la watu lilikuwa limeizunguka nyumba moja iliyokuwa maeneo ya Mtoni Kijichi katika wilaya ya Temeke, mkoa wa Dar es salaam. Watu waliobeba silaha mbalimbali za kijadi walikuwa wamepandisha hasira sana, huku wakipiga kelele “Mtoeni huyo, mtoeni huyo, au tunachoma moto nyumba” mafuta ya petroli yalikuwa tayari yashakuwa mikononi mwa watu wale wenye hasira, viberiti vya gesi vikiwa mikononi mwao. Wapo waliotoka na Rungu, mapanga, sime, na visu vya kawaida pamoja na mikuki. Idadi kubwa ya watu wale walikuwa wamebeba mawe mikononi mwao, kwani kuna nyumba iliyokuwa jirani ilikuwa ikiendelea ujenzi wake, ndiyo iliyokuwa ikitoa takrima ya mawe. Watu makundi kwa makundi waliokota mawe yale kila mmoja na jiwe aliloweza kuliinua lakini pia kulirusha, alilitwaa na kuingia katika mkumbo. Madereva wa Bodaboda nao hawakubaki nyuma katika sekeseke lile, walikuwa wakizizimua pikipiki zao, kwa milio tofauti huku wakipiga misele, kwa furaha ya kutaka kuuliwa mtu! Kama hiyo haitoshi kwa umoja wao, kila pikipiki iliyokuwa pale katika pikipiki zile takribani hamsini zilitoa mafuta ya petroli kwa ajili ya kuchomwa mtu moto. “Toa mwizi huyoo, wewe mzee ndiyo unafuga wezi unakula nao eee, leo kama hujamtoa huyo mwizi basi tutamuua. Tena tutamuulia humohumo ndani ya nyumba yako kwa kuitia moto” Maneno yale hayakuweza kubadilisha msimamo wa mmiliki wa nyumba ile mzee mmoja wa makamo aliekuwa nje ya nyumba yake, akishikilia kuwa hayupo tayari kumtoa nje kijana yule aliekimbilia nyumbani kwake. Ila atafanya hivyo mara watakapowasili Polisi pahala pale, kwani yeye ni mjumbe wa nyumba kumi katika eneo lile, hivyo asingeweza kumsaliti mtu aliejisalimisha katika sehemu ya usalama, kisha yeye amtoe nje kuwakabidhi watu wanaochukua sheria mikononi mwao. Katu hakutaka kufanya hivyo, japo vitisho vilishamiri kila upande kutoka katika kundi lile la watu waliokuwa na hasira kali. “Mie nimepiga simu Polisi wanakuja, hivyo subirini Polisi nikishawakabidhi mtu wao kisha muwaambie wao wawape huyo mtu ili mmuue, kama wao watawapa basi watakuwa wao siyo mie niliesababisha kifo cha mtu.” Vijana wale walikuwa wakaidi kwelikweli hawakutaka kabisa kumuelewa yule mzee aliekuwa akitumia busara pahala ambapo hakuna hata mtu mmoja aliekuwa tayari kuifata. Mara wengine wakaanza kutupa mawe katika nyumba ile, mawe yalirushwa juu ya bati, mara wapige mawe katika madirisha, ilimradi katika nyumba ile kulikuwa kumetawaliwa na dhahama na hekaheka pamoja na taharuki kubwa. Wakazi waliokuwa ndani ya nyumba ile, walikuwa hawana amani hata kidogo kwani waliona wakihatarisha maisha yao, ikawa kila mwenye simu aliekuwa ndani ya nyumba ile, alipiga simu yake Polisi ili kupata salama ya maisha na mali zao, kwani kitu kinachoitwa amani kilikuwa kumetoweka na kusafiri mbali sana na nyumba ile.

Ndani ya nyumba ile, katika chumba kimoja chini ya uvungu wa kitanda alikuwa amelala kijana mmoja aliekuwa anakadiriwa kuwa na umri chini ya miaka thalathini, na juu ya miaka ishirini na tano. Alikuwa amevimba uso wake kwa kipigo kutoka kwa watu wenye hasira kali, alikuwa akivuja damu kichwani kwake, mavazi yake yalikuwa hayajulikani rangi yake sawasawa, kwa namna yalivyotapakaa damu. Miguu yake ilikuwa pekupeku ikiwa imejaa vumbi, wakati alipotoka nyumbani kwake alikuwa amevaa raba za kisasa za vijana. Alikuwa uvunguni amelala kifudifudi machozi yakimtoka mfululizo, alikuwa akijuta majuto ya Firauni. Hakika alijitambua tangu azaliwe hakuwahi kudokoa kitu cha mtu, lakini leo yupo katika nyumba asiyoifahamu,akiwa anashindana na nguvu ya mauti kutoka kwa watu waliomkimbiza kwa mwendo wa mita kama mia mbili hivi, urefu wa viwanja viwili vya mpira wa miguu. Alikuwa akilia kwa mengi sana, kwani katika mji huu wa Dar es salaam alikuwa hana ndugu mwengine zaidi ya dada yake ambae yupo gerezani akitumikia adhabu ya kifungo cha miaka thalathini na kazi ngumu, lakini hakika kosa alilofungwa kwalo hakulitenda! Dada yake ameingia gerezani akiwa na mimba changa ambayo imekulia jela na hatimae alipohukumiwa kifungo kirefu cha miaka thalathini, kutokana na mshtuko wa hukumu ambayo hakuitarajia akajifungua mtoto njiti, wakati huo mimba yake ilikuwa na miezi saba tu. Sasa anaishi Gerezani akitumikia adhabu akiwa na mwanawe mikononi, mtu pekee aliekuwa tegemeo la kumchukua mtoto wa dada yake ili amlee, hakuwa mwingine zaidi yake yeye ambae yupo chini ya uvungu wa kitanda akiyanusuru maisha yake. Ama kwa hakika alikuwa hajihurumii yeye hata kidogo, bali alimuhurumia sana dada yake, kwani yeye ndiyo anaehangaika kumkatia rufaa na taratibu bado zinaendelea akawaza vipi kama akiuwawa, nani atamshughulikia dada yake kutoka nje ya gereza akiwa huru, je mtoto mchanga anaeishi gerezani na mama yake kama mfungwa ambae hapati kucheza na watoto wenzake akiwa huru, hapati kusoma ikiwa ataendelea kuishi gerezani tofauti na watoto wenzake waliokuwa uraiani, hapati lishe bora, hapati malezi mazuri kila siku analala na kuamka akiwa ndani ya gereza amri na adhabu akizishuhudia hadi ameshafikisha miaka miwili kasoro mwezi mmoja, akikulia gerezani. Amekosa nini mtoto huyu? Hayo ndiyo yaliyomliza sana yule kijana pale uvunguni mwa kitanda. Kitu kilichomfanya awe ndani katika nyumba ile chini ya uvungu wa kitanda, ni kwa vile pumzi zilishamuishia wakati akikimbizwa na wale mazabania waliokuwa wakiitaka roho yake kwa gharama yoyote ile, akaona kama ataendelea kukimbia atafia mikononi kwa watu wale waliokuwa wakiongezeka katika kumkimbiza. Kwani mara mbili alipigwa ngwala akaanguka, akakutana na mateke na ngumi kali za uso, akajitahidi na kuweza kupambana akafanikiwa kusimama na kukimbia hadi alipofika mbele ya nyumba hii aliyopo sasa akaiona bendera ikipepea nje ya nyumba hiyo. Na kwa kuwa mlango wa kuingilia ndani ulikuwa wazi, ndipo nguvu za ajabu zilipomjia akapanda ngazi chache zilizokuwa nje ya nyumba ile akaingia ndani kwa kasi kubwa huku akihema juu juu, pumzi zilikuwa zimempaa sana macho yalimtoka pima kwa hofu ya kifo. Mdomo ulimpauka mate yakatoweka kinywani mwake. Alikuwa yumo ndani ya nyumba ya mjumbe wa nyumba kumi wa mtaa ule. Wale watu waliokuwa wakimkimbiza walimuona akipanda ngazi kuingia ndani ya nyumba ile, akiwa amewaacha nyuma kama mita kumi tu. Wale watu waliokuwa wakimkimbiza walirusha mawe kama mvua mengine yakimkosa na mengine yakimsindikiza katika mgongo wake. Yule kijana aliwapita mbio wenyeji waliokuwa wamekaa kitako wakipata mlo wa mchana, akajichoma katika chumba kimoja kilichokuwa wazi mlango wake, na hakikuwa na mtu ndani yake. Akajifungia kwa ndani akaingia chini ya uvungu wa kitanda kile akalala kifudifudi mwisho kabisa wa ukuta, huku macho yake yakimtoka kwa fadhaa, akiendelea kuhema kwa nguvu kama mtu alieshikwa na maradhi ya Pumu. Pale chini alikuwa akimuomba Mungu kila aina ya maombi, ili asiuwawe na raia wale wenye hasira kali kwani yeye hakuwa mwizi kabisa. Lakini pia ana adhma ambayo bado hajaitimiza, ana jambo katika kifua chake aliapa kabla hajafariki dunia alitimize jambo hilo hivyo ikiwa atauwawa mambo yote kwake yatakwenda kombo, na mipango ya ulezi wa mpwa wake na rufaa kuhusu dada yake pia yatakwenda halijojo hali itakuwa vipi kama siyo tete.

Mawe yaliokuwa yakirushwa na wale watu, moja lilimpata mwenye nyumba mkononi mwake aliekuwa ametulia usawa wa mlango kupata hewa safi, huku akipata chakula cha mchana nyumbani kwake akiwa na familia yake iliyokuwa futi kadhaa wakiwa wameizunguka sahani ya ugali na bakuli lililokuwa na mboga ya maharage, likiwa limezamishwa juu ya ugali ule wakipata mlo wa mchana. Hakika ilitokea taharuki kubwa sana kwa yule kijana kuingia kwa ghafla vile mle ndani akivuja damu, huku wingi wa mawe ukimiminika kama mvua kutoka nje, wale wana familia hawakuweza tena kuendelea kukaa kula ugali, kila mmoja aliitafuta njia yake wakiuwacha ugali uking’ong’wa na Inzi. Lakini katika kukimbia kwao hawakuweza kutoka nje kwani kule kulikuwa hakutokeki kwa wingi wa mawe, na ndani kulikuwa hakukaliki kwa yule mtu aliejifungia ndani akiwa amevururuka damu mwili mzima. Hivyo kila mmoja alikimbia mle ndani asijue aende wapi, hasa baada ya kusikika kelele kubwa kutoka nje. “mwizi huyoo. Mwizi huyooo, kamata huyooo, uwa huyoo!” Mwenye nyumba aliekuwa karibu na mlango, yeye alikimbilia pale mlangoni akachomoa funguo, akatoka nje kisha akaufunga ule mlango kwa funguo. Akiwa nje huku mawe kadhaa yakimshambulia katika mwili wake huku nae akiweka mikono yake kichwani kuziba kichwa chake kisiharibiwe na mawe. Mara kundi lile la watu likawa limefika mahala pale, lakini likiwa limesitisha kwa muda zoezi la kurusha mawe likimdai mtu wao ili wamalizane nae. Ama kwa hakika kuna maeneo akikimbizwa mwizi, basi huwa ni kitahanani.

Yule kijana akiwa chini ya uvungu wa kitanda alikuwa akitafakari, jambo lile lililompelekea hadi kuwa katika dhahama ile, alijuta ndani ya nafsi yake kwa maamuzi aliyokuwa ameyafanya, alijuta sana huku machozi yakizidi kumtoka kama maji, alijiona anakufa ilihali hakufanya kosa lile, kama akinusurika kufa kwa kifo kile cha aibu, atakwenda Polisi na hatimae gerezani ilihali hakufanya jambo lile, alilia akalia lakini hakuweza kubadilisha matokeo, kwani tukio lile kule nje liliwavuta wadaku wengi sana, watu walijaa ikawa hadi wanakanyagana, kiasi ikafikia hata hakuna nafasi ya kutema mate. Kwani mtu angetaka kutema mate basi angemtemea mwenzake. Ajabu hata watu waliokuwa wamefika wakati ule walipouliza kuna nini pale, na walipojibiwa kuna mwizi, basi wao walianza kushadadia “ Atolewe nje huyo ili apigwe na achomwe moto ili liwe fundisho kwa wezi wote!” Hii ni ajabu sana kwani vurugu zote zile hakuna mtu hata mmoja aliekuwa akidai kwamba yeye ndiye alieibiwa na yule aliekuwa amepigwa mawe kwa kosa linalosemekana kuwa ni la wizi. Watu wale walikuwa wapo tayari kutoa roho ya mtu ambae wala hakuna mtu anaesimama na kusema kwamba yeye ndiye alieibiwa kitu au pesa au chochote kile.

Kijana mmoja Mwanaharashi alipanda juu ya paa la nyumba ile akiwa na kidumu chake cha lita tano kilichokuwa na mafuta ya Petrol yaliyotolewa na watu wa Bodaboda, akaanza kuyamwaga mafuta yale juu ya bati, kitendo ambacho kilishangiliwa sana na watu waliokuwa nje ya nyumba ile waliokuwa wakishuhudia kitendo kile. Watu walipiga mbinja zikahanikiza eneo lile, macho ya watu wote yakawa yanatazama juu ya paa la nyumba ile kwa yule kijana aliekuwa akitaka kuchoma moto nyumba ya watu. Wale watu waliokuwa chini walikuwa wakimpamba kwa sifa za kijinga jinga, nae akapata kichwa akamwaga kila sehemu juu ya paa lile. “Ndiyo mwana haribu mtu wetu, tunakuaminia wewe ni nomaa choma mwana tupo nyuma yako!” Harufu ya mafuta ya Petrol ikasambaa katika eneo lile kwa kadiri upepo ulivyokuwa ukielekea. Mwenye nyumba alikuwa akishuhudia pasi yakuwa na kauli kwa kundi lile la watu waliokuwa wamepagawa, wakitaka kuitoa roho ya mtu tu huku wakishuhudia. Mapigo ya moyo yalimuenda mbio kama saa mbovu, kwani nyumba yenyewe ameipata baada ya kuuza nyumba yao ya urithi iliyokuwa magomeni mtaa wa Idirisa, walipogawana pesa na ndugu zake yeye ndiyo akanunua kiwanja pale Mtoni Kijichi, miaka kumi na mbili iliyopita akajenga nyumba ambayo hadi leo haijesha kwa asilimia mia moja. Leo nyumba yake ikichomwa moto atakuwa mgeni wa nani katika jiji hili?! Yule mwenye nyumba akiwa katika kuwaza, mara kikatokea kizaazaa kikubwa!

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Mara milio ya risasi ilisikika eneo lile, kikatokea kizaazaa kikubwa kwa umati wa watu uliokuwa umefurika eneo lile. Yule mtu aliekuwa juu ya paa akiwa sasa ameshatoa kiberiti ili awashe moto nyumba ya watu, kwa sababu tu amehifadhiwa mwizi! Alitafuta pa kukimbilia ili kukwepa kukamatwa na polisi waliokuwa wamefika na gari mbili huku wakirusha risasi za moto juu hewani pamoja na mabomu ya machozi ili kuwatawanya mamia ya raia wenye hasira kali, waliokuwa wamekusanyika pale. Raia wale walitawanyika kama makundi ya Nzige kwani walikimbia hovyo mahali pale, huku wakikanyagana na kulaliana huku kelele za woga na hofu zikiwatoka . Njia zote zilikuwa hazitoshi kwani watu walikuwa ni wengi na wote kila mmoja alikuwa akisalimisha roho yake, akiogopa risasi ambazo zilikuwa zikipigwa juu hewani. Lakini pia wakiogopa kukamatwa na kupelekwa kituoni kutokana na kadhia ile. Mabomu ya machozi yalianza kuwafukuta katika macho yao. Kizaazaa chake kilikuwa ni kikubwa sana. Ndani ya dakika zisizozidi tatu, palikuwa peupe mahala pale, baadi ya vitu vilivyodondoshwa na raia wale vilionekana kwa uwazi kabisa. Zikiwemo ndala, yeboyebo, kofia, Khanga na mitandio ilimradi kila mtu alitokomea zake alipopajua kusalimisha maisha yake. Moshi mwingi wa mabomu ulitanda mahala pale, na wale watu waliokuwa maeneo ya jirani ambao hawakuwa na habari ya mwizi, kwa upande wao hali ilikuwa tete zaidi. Kwani waliposikia milipuko ya mabomu ya machozi ikipigwa wao walikumbuka mabomu yalioripuka Mbagala, ambayo kule kwao pia yalifika na kufanya madhara makubwa, hivyo wakaona kumekucha mabomu yashaanza tena upya, hivyo walikimbia kunusurisha maisha yao huku wakiacha milango wazi, eneo lote la jirani ya pale watu walikimbia hovyo tu wakijua Dhahama ya mabomu imerudi. Ingawa wapo baadhi ya watu wabishi waliokuwa katika eneo la tukio wao walitoa leso zao wakajifunika pua na macho yao, wakawa wamesimama kwa umbali mrefu wakiendelea kushuhudia kadhia ile.

Polisi wakiwa na silaha za moto, walikuwa wameizunguka nyumba ile wakamuuliza mzee aliejitambulisha kwa jina la Onesmo Baharia, ambae alikuwa nje ya nyumba ile ambae pia ndiye mmiliki halali wa nyumba ile. Askari wale walimuuliza kama huyo mwizi aliejifungia ndani ya nyumba yake kama alikuwa na silaha au hakuwa na kitu, na kwamba ameingia chumba gani. Mzee Onesmo Baharia aliwajibu kuwa hakuwa na silaha wakati anaingia, labda kama aliificha katika nguo zake. Kisha akawaambia wale asakri kuwa yule mwizi amejifungia katika chumba cha watoto wake. Baada ya kujibu mzee Onesmo Baharia alifungua mlango akawaonesha chumba alichokuwa ameingia yule kijana anaesadikiwa kuwa ni Mwizi. Chumba ambacho hadi muda ule alipowaonesha askari wale, bado mlango wake ulikuwa umefungwa kwa ndani. Polisi walijipanga vyema wakamtaka Yule kijana aliekuwa ndani ya chumba kile, ajisalimishe kwa kutoka nje ya chumba kile, pia aisalimishe na silaha yake. Yule kijana aliekuwa ndani hakufanya ukaidi, kwani hata yeye alizisikia kwa masikio yake, sauti za risasi na mabomu kutoka kwa askari wale waliokuwa wamevaa maski katika nyuso zao ili kujikinga na moshi wa sumu wa kuwasha wa mabomu. Hivyo alifungua mlango akatoka nje ya chumba kile huku mikono yake akiwa ameiinua juu, kuashiria kujisalimisha mbele ya wale wanausalama wa kulinda raia na mali zao.

Alitoka nje akiwa amechakaa sana, damu zilikuwa zimeanza kuganda, uso wake umemvimba kwa kipigo, hakika ulikuwa huwezi kumtazama mara mbili kama wewe siyo shababi na jasiri. Kijana yule alinyoosha mikono yake juu akapiga hatua kadhaa lakini hakuwa na silaha mikononi mwake. Aliwaona askari watatu wakiwa wamepiga goti moja chini ya sakafu ya nyumba ile huku mitutu ya Bunduki aina ya SMG ikiwa imemuelekea tayari kwa mashambulizi, kama wataamrishwa na mkuu wao aliekuwa amesimama makini na tahadhari kubwa akiwa na redio call yake mkononi. “Piga magoti na nyoosha hivyo hivyo mikono yako juu” Amri ya mkuu wa askari wale ilimuamrisha yule kijana aliekuwa hoi kwa kuvuja damu nyingi. yule kijana alitii amri akapiga magoti, huku mikono yake akiwa ameinyoosha juu akitetemeka mwili wake wote kwa wingi wa hofu na woga uliomjaa moyoni mwake. Macho yake yalikuwa yanamvuja machozi siyo tu alikuwa akilia kwa kukamatwa na polisi laa, bali moshi wa mabomu ulimuingia machoni na puani na kumpa adha kubwa iliyokuwa ikimtoa machozi. Askari Polisi mmoja aliinuka pale alipokuwa amepiga goti moja, akamkabili yule kijana kwa kutoa pingu na kuifunga mikono yake kwa nyuma, kisha akamlaza kifudifudi huku akimpekua na kumtaka awape Bunduki yao. Wale askari wengine wawili waliingia ndani ya chumba kile, wakamtaka na mwenye nyumba nae aingie mle ndani ili wapekue na yeye akiwepo, ili aweze kuona kama kuna silaha yoyote itakayopatikana ikiwa imefichwa na Yule mwizi au kidhibiti chochote. Hivyo wakaingia mle ndani wakaanza kupekua kila sehemu mle katika chumba kile. Walichungulia chini ya uvungu wa kitanda ambapo kulikuwa kumechafuka kwa damu hawakufanikiwa kuona kitu, wakapekuwa katika matenga ya nguo, na kila walipopatilia shaka, katika chumba kile cha kulalia watoto wa yule mwenye nyumba, lakini hawakufanikiwa kupata silaha yoyote ile, hatimae wakatoka nje wakaongeza nguvu kwa yule kijana wakimtaka awatajie wezi wenziwe, na wapi ilipo silaha yao. “Jamani mie siyo mwizi hiyo Bunduki naipata wapi, mie siujui wizi tangu nimezaliwa!” alijitetea yule kijana huku akilia lakini haikuwa kinga kwake alikuwa kama mtu mwenye kutwanga maji kwenye kinu. Kwani ilikuwa ni tofauti na mawazo ya Polisi. Wao Polisi wameshawazoea wezi wengi wanapowakamata, huwa hawakubali kuwa wameiba hata kidogo, hivyo wakawa wakifikiri kuwa na huyu atakuwa ni mmoja wao. Hivyo alichezea makofi ya uso na masikio bila kujali damu na manundu ya uso yaliotokana na raia waliomkimbiza walivyokuwa wamemuumua sura yake, bali walimchapa makofi wakimdai Bunduki ambayo kwa hakika Yule kijana hakuwa nayo pale, wala alipotoka. Polisi wakamwambia akifika katika kiti moto atasema tu ilipo silaha yao. Walimuinua kituuteni wakatoka nae nje msobemsobe, wakamrusha nyuma ya gari yao, na askari mmoja aliekuwa amesimama katika gari ile akamuinua na kuifunga mikono yake kwa pingu na bomba la gari ile, aina ya Toyota Land Cruser iliyokuwa wazi, ikiwa imekunjwa turubai lake kwa juu. Askari wale walipanda ndani ya gari yao na muhalifu wao, yule mzee mwenye nyumba alitakiwa aende kituoni kutoa maelezo, kwa kadiri anavyofahamu kilichotokea, hivyo alipandishwa katika gari ya pili ya Polisi, na safari ikaanza kuelekea kituoni.

Mara ilitokea kwa kasi gari moja ndogo aina ya Hyundai ya rangi ya Fedha ikasimama mbele ya gari ya Polisi. Ndani ya gari ile mlikuwa na watu wawili mbele, msichana mrembo aliekuwa amekaa kiti cha pembeni cha mbele, na dereva mwanaume ambae umri wake ulikuwa ni mtu wa makamo. Yule dereva wa gari ile akashuka chini nje ya gari ile, akiwa amevalia sare za rangi ya kijani za jeshi la wanachi Tanzania (JWTZ), mabegani mwake akiwa ananyota tatu kila bega. Askari Polisi walipiga saluti kwa askari jeshi yule, kisha yule askari jeshi alipitiliza huku akiyatazama kwa makini magari yale ya Polisi, hadi nyuma ya gari ya pili akatazamana uso kwa uso na yule kijana anaesadikiwa kuwa ni mwizi, huku yule mzee akiwa amekasirika vibaya sana alimkazia macho yake yaliojaa shari akamnyooshea kidole cha hatari. Askari Polisi walishangazwa kwa kitendo kile wakawa makini kufatilia jambo lile. Mara Yule mwanajeshi akatoa msonyo mkubwa kisha kwa haraka akachomoa Bastola kiunoni mwake ili ampige risasi yule kijana. Askari waliokuwa nyuma ya gari ile wakamzinga yule kijana kwa pamoja huku mmoja wao, alipiga saluti huku akitamka kumwambia yule askari jeshi aliepandwa na hasira. “Hapana Afande usifanye hivyo, huyu tayari yupo chini ya mikono yetu akiwa chini ya ulinzi, hivyo kama wewe ndiye aliekuibia tunakuomba uje kituo cha Polisi Maturubai pale Mbagala uje ufungue jalada, kuliko kumuua mikononi mwetu utatupa sisi kesi, gari ya mbele tunae mjumbe anaekwenda kutoa maelezo yake, kwani huyu mwizi alikuwa amekimbilia nyumbani kwake, na tumemtoa akiwa mzima hivyo ukimuua hapa mbele ya mjumbe na raia wakiona kitendo hiki, utatupa matatizo sisi kwa hiyo samahani sana Afande hata kama amekuibia, haiwezekani kuuliwa tena kama raia walishindwa kufanya hivyo kabla sie hatujatokea” Yule askari alisema maneno yale huku akimtazama askari jeshi aliekuwa ameshika Bastola huku akitweta kwa hasira.

Yule kijana alikuwa akilia na kusali huku akilitaja jina la Mungu mara kwa mara ili kumpa nusura na lakadha tan maanani, lililokuwa limemsibu. Hakika siku yake ilikuwa mbaya kuliko neno mbaya lenyewe. Yule askari wa JWTZ alionekana kuelewa maneno ya askari Polisi hivyo akaishusha silaha yake chini, akageuka akaiendea gari yake akapanda akaizungusha na kutangulia yeye mbele huku msafara wa gari mbili za Polisi ukiwa nyuma, wakielekea kituo cha Polisi Maturubai pale Mbagala, wakitokea Mtoni kijichi karibu kabisa na Mbagala kongwe au jina maarufu siku hizi ikiitwa Mbagala kuu.

Wale Raia waliokuwa wamekimbia mabomu ya machozi walijisogeza eneo la tukio pale magari yale yalipoondoka mbele ya uso wao, ndipo na wao wakashika njia kuendelea na hamsini zao, kwani walivunjikiwa na mambo yao kwa kutaka kutoa roho ya mwenzao, bila kuwa na ushahidi wa wizi wake, lakini hata kama wangelikuwa na ushahidi bado vyombo vya sheria vipo siyo vyema kuchukua sheria mikononi, kwani wakati mwengine wamekuwa wakiuliwa watu pasi na hatia. Ni vyema kutii sheria bila ya shuruti.

Wale askari waliokuwa katika gari ya nyuma wakamsaili yule kijana huku gari ikiwa inatembea. “Wewe umemuibia nini Afande, yaani hukuona sehemu zote za kuiba hadi ukamuibie askari eee?!” Yule kijana jibu lake lilibaki kuwa lilelile wala halikubadilika. “Jamani mie siyo mwizi, wala wizi siujui!” kwa jibu lile liliwatia hasira askari Polisi kiasi wakamchapa vibao huku akiwa hana namna ya kujitetea, kwani mikono yake ilikuwa imefungwa kwa nyuma na pingu mbili, zikiwa zimefungwa katika Bomba ya gari ile hivyo alikuwa akiinamisha uso wake chini anapata makonzi ya kichwa, akiuinua uso wake, anakutana na vibao vikali vya mashavu na masikio hali ikawa vile hadi Yule kijana akasema kwa kuropoka “Kweli mimi ni mwizi, nimemuibia pesa yule mzee” Askari wale wakaacha kumpiga huku wakimcheka na kumwambia. ”Sasa ulikuwa ukikataa nini, watu kama nyie ilikuwa raia wamalize kabisa sisi tukija tukute maiti tu basi kwani mnakera sana. Nyie wezi ndiyo mnaotunyima usingizi usiku hatulali kwa ajili yenu, pumbavu kabisa wewe ulikuwa ukikataa kukubali ukweli, hivi yule Afande kawaacha watu wote kwa nini akufate wewe na siyo mtu mwingine” Askari wale walikuwa wakimtazama yule kijana aliekuwa hajiwezi kwa hali wala mali, kwani alikuwa yupo hohe hahe hana tofauti na Yakhe.

Gari zile zilichanja lami, hatimae zikawasili katika kituo cha Polisi Maturubai, Yule kijana alifunguliwa pingu akaingizwa ndani ya kituo kile, akaswekwa mahabusu ili kwanza kumsikiliza yule askari ambae sasa alikuwa ameteremka na yule msichana mrembo, aliekuwa ameongozana nae pale. “Ndiyo Afande pole sana kwa usumbufu, je kijana amekuibia pesa ngapi Afande?” Askari kiongozi ambae ndiye aliekuwa akionekana kuwa mkubwa kicheo kuliko askari wote waliokuwa katika msafara ule alimuuliza yule Mzee askari wa jeshi la wananchi wa Tanzania. Huku akimpa kiti akae ili apate kutoa maelezo yake kwa utulivu. Kwani askari waliokuwa nyuma ya gari ile wakiwa wanaelekea pale, walimdokeza kuwa kijana amekili kuwa ni mwizi, amemuibia pesa Afande.

“Asante Staf Sajent, ee yule kijana kwa kweli siyo mwizi. Na kama anayo tabia hiyo basi kwa wengine kwangu mie hajaniibia chochote!” Yule mzee askari wa jeshi la wananchi alipojibu swali lile, ilikuwa ni mshangao kwa mjumbe, aliekuwa pale pamoja na maaskari wale waliokuwa wakimpiga yule kijana hadi akakubali kuwa amemuibia pesa yule mzee. Wale askari waliompiga kijana yule nafsi zao zikawasuta sana kwa kumuhukumu mtu pasi na ushahidi. Hakika majibu yale yalibadilisha kabisa hali ya hewa, na kuleta jambo jingine kubwa zaidi!





“Yaani Yule kijana alinusurika kuchomwa moto kumbe siyo mwizi, amepigwa mawe na kundi la wananchi wenye hasira kali kumbe hakuwa mwizi? Nyumba yangu imenusurika kuchomwa moto kwa kukataa kumtoa nje yule kijana kwa wale watu waliokuwa na hasira kali kumbe siyo mwizi?, Laa haula walaa kuuwata ila billah!” Mjumbe alishindwa kulificha jakamoyo lake, ikabidi alitamke kwa sauti mbele ya wale askari.

“Sasa Afande kama Yule kijana siyo mwizi, iweje umtolee silaha na kutaka kumpiga?” Yule Staf Sajent mkuu wa msafara ule alimuuliza yule mwanajeshi huku mshangao wake bado ukiwa haujamtoka usoni mwake.

“Yule kijana amemrubuni binti yangu huyo hapo, amemdhamini mahakamani akamuweka kinyumba kwake wakati akijua kabisa kuwa anafanya makosa. Leo amekuja nae nyumbani bila shaka akijua kuwa mie sitakuwapo nyumbani, ili mwanangu achukue nguo zake apate kuondoka nae aende nae kwao. Walipokuja nyumbani kwa bahati nzuri kwangu na bahati mbaya kwa kijana wakanikuta nikiwa chumbani kwangu. Nilishangaa sana kusikia sauti ya binti yangu ikiniita kwa sauti, kwani mie natambua mwanangu hayupo uraiani bali yupo Gerezani. Baada yakutoka chumbani Binti yangu akanambia kuwa amekuja kunitaka radhi pia akaniambia dhamira ya huyo mwanaume na kwamba yeye hakukubaliana nayo, hivyo amekuja nyumbani kuniomba msamaha baba yake, anataka kurejea shuleni kusoma. Sasa mie nikamgadhibikia Yule kijana kwani mwanangu nilimpeleka mimi mwenyewe mahakamani, akapanda kizimbani nikiwepo, akasomewa shitaka la matusi ya nguoni akakana shitaka, kisha akaamriwa aende mahabusu katika gereza la Segerea hadi baada ya wiki mbili kwa kukosa dhamana. kwani alipoulizwa kama anae mdhamini, alisema hana na hakika hakuwa nae. Baada ya kushuka kizimbani ndipo mie nilipoondoka Ila yule kijana sijui alipotokea, wala amemdanganya nini mwanangu wala sijui. Na kwa nia ipi kama siyo mbaya hadi kumuharibia masomo yake. Yaani mwanangu hataki shule kwa kurubuniwa na kijana yule habithi mkubwa, mtoto niliepoteza pesa chungumzima kwa kumsomesha leo aje kutokea mjinga amrubuni mwanangu, hapana huyo kijana nitafika nae mbali sana hadi nihakikishe amefungwa maisha. Sasa nilipotaka kumshikisha adabu, akachoropoka mbio nje, ndipo mlinzi wangu alipomkimbiza kwa mita kadhaa huku akimpigia kelele za mwizi ili aweze kusimama lakini kijana ndiyo akaongeza mbio, basi walijitokeza raia wema wakamuunganishia na kelele huku mlinzi wangu akirudi nyumbani, akiwaacha raia wenye mbio zao wakiendelea kumkimbiza. Badaa ya muda walikuja vijana wa bodaboda ambao walimuona mlinzi wangu alipomkurupusha yule kijana, wakaja kunambia kuwa mtu wangu aliekimbia yupo katika nyumba ya Mjumbe. Ndipo nilipotoka na kuwakuta nyie mkiondoka nae.”

Yule mwanajeshi alipokuwa akisema maneno yale, wale askari polisi walitikisa vichwa vyao kwa masikitiko kuwa, raia wangeweza kumuua mtu asiekuwa na hatia yoyote ile, lakini pia yule kijana kumbe alikuwa akisema kweli kuwa siyo mwizi, hata alipokili kuwa ni mwizi kumbe alikuwa akitoa dudu mchuzini tu.

Mjumbe alikuwa amekasirika vibaya sana, kwani nyumba yake imepigwa mawe, imenusurika kuchomwa moto, ugali haukulika kwa tafrani ya mwizi, kumbe kijana yule hakuwa na hatia ya wizi. Ama kweli siri ya mtu ipo kifuani mwake.

“Kwa hiyo Afande Yule kijana alikuwa akiishi na mwanao kinyumba, na kwamba yeye amemdhamini mwanao ili kuwa nae kimapenzi, basi lazima atakuwa akimfahamu muda mrefu kwani huwezi kumdhamini mtu usiemjua. Sasa kama hivyo ndivyo basi hapa itabidi tufungue jalada la kumrubuni mwanafunzi, kumtorosha shule na kumbaka. Siyo tena shitaka la wizi, hili shitaka litakuwa ni kubwa zaidi ya wizi.” Askari aliekuwa akimsikiliza mwanajeshi alisema maneno yale huku akitoa karatasi tayari kwa kuandika maelezo yake.

“Sasa jamani mie sina tena maelezo yoyote hapa, kwani nilikuja kuthibitisha mwizi kukimbilia nyumbani kwangu, na wenyewe mmethibitishiwa kuwa Yule kijana siyo mwizi, basi mie nende zangu nyumbani nikale kwani njaa inaniuma hapa kama kidonda.” Mzee Onesmo Baharia, mjumbe wa nyumba kumi alikuwa akisema maneno yale huku akiwa ameshasimama kwa kuondoka.

Askari Polisi walimtazama yule mjumbe wakamwambia, “Bado mzee Onesmo unayo sababu ya kutoa maelezo,kwani mwanzo ilikuwa utoe maelezo ya mwizi kukimbilia nyumbani kwako, sasa utatoa maelezo kuwa Mgoni amekimbilia nyumbani kwako!” Mjumbe akakosa namna ya kukwepa ila ikabidi avute subira ili amalize jambo lile, kwani maji alishayavulia nguo, hakuwa nabudi ila kuyaoga. Pia akizingatia pale yupo Polisi, alichelea kama angekaidi amri yao asije kugeuziwa kibao kwa kutokutii amri halali ya polisi, likaja kutoka kwa Mjambaji, likenda kwa Mtema mate. Ikambidi awe mpole kama maji Mtungini.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Askari Polisi walimwita Yule msichana mrembo wakaanza kumuhoji, huku wakichukua maelezo yake kwa usahihi kadiri alivyokuwa akieleza yeye mwenyewe.

“Jina langu naitwa Mbuya Fabiola. Dini yangu ni Mkristo. Kabila yangu ni Mchaga wa Marangu Mtoni, Mkoa Kilimanjaro. Naishi Mtoni Kijichi, mimi ni mwanafunzi.” Alijieleza mtoto wa yule mzee mwanajeshi hadi mwisho wake akatakiwa kuyasoma yale maelezo kama yameandikwa sahihi kama alivyoyatoa. Mbuya Fabiola akayasoma maelezo yake kisha akayasaini kuwa yalikuwa sawa. Askari Polisi aliechukua maelezo yale, nae akaweka saini yake chini ya maelezo yale baada yakuandika kuwa ameyachukua maelezo yale kwa uaminifu, na chini ya kiapo kwa mujibu wa sheria.

Mjumbe nae akatoa maelezo yake mwanzo mwisho kisha akasaini, na askari aliechukua maelezo yale pia akasaini kisha akamruhusu mjumbe aende nyumbani baada yakuchukua namba zake za simu, akimueleza kuwa akihitajika kwenda kutoa ushahidi mahakamani ataitwa. Mjumbe akashika njia kwenda zake huku akilaani tukio lile moyoni mwake, kumpigia kelele za mwizi mtu asiehusika na wizi, ni jambo la hatari sana kwani linaweza kugharimu maisha ya mtu.

Baada ya mjumbe mzee Onesmo Baharia kuondoka, ikawa zamu ya Kapteni Fabiola kutoa maelezo yake.

***

Ilikuwa siku ya Ijumaa, katika maeneo ya Mbagala Kizuiani Mvua kubwa ilikuwa ikinyesha upepo mkali ulikuwa ukivuma kutoka mashariki kwenda Magharibi, ilikuwa mnamo majira ya saa tano za asubuhi, Msafiri Namjupa alikuwa akiisubiri mvua ikatike ili atoke aende katika mihangaiko yake ya kutafuta riziki, lakini mvua haikuonesha dalili za kukatika katika muda wa karibuni. Hivyo ilimuwajibikia kuingia barabarani huku akijibanza katika nyumba hii na ile, hadi akafika katika Mahakama ya mwanzo Mbagala, akajibanza mvua akiwa mpita njia kwenda mjini katika mihangaiko yake. Akiwa amejibanza Mvua katika Mahakama ile huku akitazama katika mahakama ile kama kuna askari magereza anaemfahamu, ili ampe salamu zifike kwa dada yake. Katika kutazama tazama kwake, mara uso wake uligota kwa msichana mmoja mrembo aliekuwa hamtambui, akimwita kwa ishara tena kwa msisitizo aende mahala pale alipo.

Msafiri Namjupa alimuuliza Yule msichana kwa ishara kama alikuwa akimwita yeye, kwani Msafiri Namjupa baada yakuiona ile ishara ya wito, aligeuka kutazama nyuma yake kama kulikuwa na mtu mwengine asiekuwa yeye aliekuwa akiitwa na msichana Yule asiemfahamu, lakini hakumuona mtu nyuma yake.

Yule msichana akamthibitishia kuwa anamwita yeye, hivyo akapiga hatua hadi pale karibu yake akamuona Askari Polisi mwanamke aliekuwa akimlinda msichana yule akiwa amempa mgongo. “Afande samahani huyu msichana ameniita, hivyo naomba ruhusa yakuzungumza nae.” Kabla yule askari Polisi wa Kike hajamjibu Msafiri Namjupa, Yule msichana akasema kumwambia yule askari. “Nina pesa zangu hapa naomba nimkabidhi huyu kaka ili anishughulikie dhamana yangu iliyokuwa wazi, kwani sina mtu mwengine wakumpa jukumu hili.” Baada ya kusema maneno yale Yule msichana alichomoa noti ya shilingi elfu kumi, akamkabidhi askari Polisi akanywe soda, na yule askari aliipokea pesa ile huku akimwambia yule mahabusu wake. “Hii usijekusema kuwa ni rushwa, umenipa mwenyewe wala sijakuomba mie.” Yule msichana alilazimisha tabasamu kwa askari yule huku akitikisa kichwa chake kukubaliana na maneno ya askari aliyoyatamka. “Haya ruksa muagize utakavyo, lakini unamfahamu wewe huyo mvulana, asije kuondoka na pesa zako asikufanyie hilo ulitakalo kwani watu wa siku hizi hawaaminiki kabisa.”

Yule Askari Polisi alisema maneno yale huku akiiweka pesa yake mfukoni. “ Hapana simfahamu huyu ni mpita njia tu, na hapa ninabahatisha tu kama akiwa muungwana basi atanisaidia kwani siwezi kuusemea moyo wa mtu vibaya kabla haujanitenda.” Yule msichana mshitakiwa alimjibu yule askari kisha akamgeukia yule mpita njia akamwambia. “Kaka yangu nakuomba sana, najua Mungu amekupitisha njia hii ili labda unisaidie. Mie nimepandishwa mahakamani kwa kushitakiwa kwa shitaka la Matusi ya nguoni, hivyo sina ndugu yangu wala jamaa yoyote anaejua jambo hili, na familia yangu ipo mbali na hapa. Kesi inayonikabili dhamana yake ipo wazi lakini sina mtu wa kunidhamini. Naomba sana kaka yangu nina pesa hapa shilingi laki moja, nimeambiwa jela pesa siruhusiwi kuingia nazo ndani, hivyo naomba nikupe wewe kisha unishughulikie suala la dhamana, kwa kupiga picha, barua kwa watendaji, nauli na kila kitakachohitajika, tumia pesa hii wala usiiogope ila hakikisha jumatatu naletewa ‘Remove oder’ ili uje kunidhamini, kwani mdhamini ni mmoja tu mtu wa kawaida, nakuomba sana kaka yangu nisaidie.” Yule mshitaiwa alimnyooshea pesa zote alizokuwa nazo mkoni mwake yule kijana asiemfahamu aliekuwa akipita njia ili kupata msaada kutoka kwake kwani alikuwa amehemewa, hakuwa na namna nyingine yakufanya. Ama kwa hakika lisilobudi hutendwa.

Msafiri Namjupa, alimtazama yule msichana mrembo anaekwenda jela, nafsi yake ikaingia imani sana, kwani nafsi yake ilikwenda mbali sana hadi kwa dada yake ambae yupo jela katika gereza la wanawake la Segerea, akitumikia adhabu ya kifungo cha miaka thalathini na kazi ngumu. Moyo wake ukafanya donda, imani na huruma ikamranda katika moyo wake akaipokea ile pesa huku machozi yakimlengalenga akamwambia. “Nitakusaidia usijali leo hii hii nitashughulikia jambo hili, jumapili nitakuja kukuona gerezani. Ila ukiingia gerezani muulize mfungwa anaitwa Shuwea Namjupa, yule ni dada yangu yeye yupo jela muda mrefu atakusaidia, mwambie kama mie nakudhamini na jumapili nitakuja kuwatembelea. Ukimwambia hivyo atakusaidia namna ya kuishi hizi siku tatu, jumatatu utarudi uraiani.” Yule mshitakiwa alimuandikia na kumpa jila lake kamili, jina la hakimu na kesi inayomkabili ili imrahisishie katika taratibu ya dhamana. Baada yakukamilisha mambo hayo akamuelekeza karani wake amuone ili kufanikisha jambo lile. Mara basi dogo la magereza liliwasili pahala pale, mahabusu wote wakaingia katika basi lile akiwemo yule ‘fresh case’ Mbuya Fabiola kisha askari magereza na askari polisi wakapanda nao gari ile ikaondoka mahala pale. Yule mshitakiwa machozi yalikuwa yakimtoka, kwa kwenda jela kwa mara ya kwanza maishani mwake. Ama kweli kila kitu kinataka mazowea.

Msafiri Namjupa hakuwa mgeni na mambo ya Mahakama, kwani kesi ya dada yake imemfanya azijue njia nyingi za taratibu za kisheria, hivyo alimuona karani wa Mahakama akazungumza nae kuhusu nia yake ya kumdhamini mshitakiwa, karani akamwambia hakimu mwenye shauri lile alikwisha ondoka hivyo isingekuwa rahisi kusaini ‘Remove Orde’ akamshauri akafatilie barua inayomtambulisha kutoka kwa mtendaji, kisha jumatatu mapema afike pale ili hakimu asaini kisha apatikane askari aipeleke magereza, au askari magereza waondoke nayo na siku ya jumanne mshitakiwa apelekwe mahakamani kwa kudhaminiwa. Msafiri akashika njia kushughulikia mambo aliyoelekezwa na karani, na kufikia saa tisa alasiri alikuwa amekamilisha taratibu zote za Barua ya udhamini.

***

Siku ya Jumapili Msafiri namjupa alikwenda katika gereza la segerea, akaandikisha majina ya watu wawili Mbuya Fabiola, na Shuwea Namjupa, mkononi mwake akiwa na zawadi alizowapelekea ili ziwafariji, kwa kuwa dada yake alikuwa ni Mfungwa hakuruhusiwa kula vyakula kutoka nje, hivyo kupitia Mbuya Fabiola, Msafiri Namjupa alimpa chakula alichonunua mgahawani ili waweze kula na dada yake, lakini mbuya akiwa ndiyo mpokeaji wa chakula, na Shuwea Namjupa yeye alipokea sabuni na mafuta ya Gel pamoja na Dawa ya meno. Msafiri Namjupa alimtazama mpwa wake aliekuwa mikononi mwa dada yake akiwa hana habari na dunia inavyokwenda, akiwa mwingi wa furaha wala wala asijue kinachomfurahisha, mtoto aliekuwa akiishi katika mazingira magumu sana. Machozi yalimbubujika Msafiri bila khiyari yake. Alitamani amchukue mtoto yule lakini bado alikuwa hajaachishwa ziwa, lakini pia dada yake kwa kuwa alikuwa akinyonyesha, ilimpa ahueni yakufanya kazi nzito hivyo kwa namna nyingine alimfanya mwanawe kuwa ni kinga yakufanya kazi, hivyo hakuwahi kupangiwa genge lolote lakufanya kazingumu, zaidi yakuwa ndani ya Gereza kila siku iendayo kwa mungu, akifanya kazi ndogondogo za kuokota mabakuli na vikombe walivyokula wafungwa na mahabusu waliokuwamo ndani ya gereza lile.

Msafiri alijikaja kiume akamweleza Mbuya hatua alizofikia kuwa jumatatu, itapelekwa Remove Order, na jumanne atakwenda Mahakamani kumdhamini. Baada ya kuzungumza kwa kituo na kuwakabidhi vitu vyao, Msafiri aliondoka huku donge likiwa limemshika rohoni mwake kwa namna mpwa na dada yake wanavyoteseka gerezani ilihali hawajatenda kosa lile. Msafiri alijisemea kimoyomoyo “Ama kweli si wote waliofungwa jela wana hatia!”

Siku ya Jumanne mapema asubuhi Mahabusu walipelekwa Mahakamani, Msafiri Namjupa alimdhamini Mbuya Fabiola, akatoka nae nje ya Mahakama, akiwa na wingi wa furaha.

“Kaka yangu nakushukuru sana kwa msaada wako, hakika umenionesha wewe ni muaminifu na mkweli. Hivyo naomba niende nyumbani kwako nikapafahamu unapoishi kwani sie tumeshakuwa ndugu. Nimekaa na dada yako Shuwea, hakika anahitaji msaada mkubwa kwani kwa namna alivyonihadithia, hajafanya kabisa kosa aliloshitakiwa nalo, nami nimeijua Jela nakuahidi tutakuwa bega kwa bega katika kuhakikisha Shuwea anatoka gerezani!”

Msafiri Namjupa aliipokea shukurani ile, akakubali kwenda na Mbuya Fabiola kumuonesha nyumbani kwake alipopanga, safari ambayo angeijua khatima yake asingeithubutu maisha yake lakini ndiyo hivyo, jambo usilolijua ni sawa na usiku wa kiza.







Msafiri Namjupa, aliongoza njia huku akizungumza haya na yale na Mbuya, hatimae wakatokezea katika nyumba aliyokuwa akiishi, chumba cha uani nyumba iliyokuwa na wakazi wake wenyeji wa mkoa wa kusini mwa Tanzania. Alipochomoza na Mbuya pale alipopanga, aliwakuta wapangaji wenzake wakiwa wamekaa uani wakipika chai asubuhi ile ya saa nne. Macho ya wapangaji wenziwe yalimtizama Mbuya, kisha wakamtizama Msafiri alivyo mwishowe wakatazamana wao kwa wao. Walitazamana kwa mshangao mkubwa wakiwa hawaamini macho yao, kwamba Msafiri anaweza kuwa na mwanamke mzuri kama yule. Macho yao na dhamira yao msafiri aliwang’amua hivyo akataka kuwaonesha wale wapangaji wenzake kuwa na yeye ni matawi ya juu. “Karibu nyumbani jisikie huru kabisa, hapa ndipo ninapoishi na hao hapo ni wapangaji wenzangu.” Msafiri alimwambia Mbuya kisha akatoa ufunguo mfukoni kwake akafungua kufuli lililokuwa limefungwa katika mlango ule wa chumba cha uani ambao haukuwa hata na kitasa. “Asante nimekaribia, na hao wapangaji wenzako nashukuru kuwafahamu.” Mbuya alimjibu Msafiri huku nae akiingia ndani katika chumba kile. “Halooow makubwa kipofu kaona mwezi leo!” Cheko la kebehi lilitoka kwa mpangaji aliekuwa akitoka kuoga katika choo kilichokuwa uwani, ambae alikuwa akitaniana sana na Msafiri. “Mbona hawa wapangaji wenzako wanakuwa waswahili sana?” Mbuya alimwambia Msafiri aliekuwa kimya, akitafakari maneno ya kejeli yaliokuwa yakisemwa kwa mafumbo pale uani. “Siyo wanakuwa hawa ni waswahili hasa kwa mkono, kwa sababu hawajawahi kuniona tangu nimehamia hapa mwaka mmoja uliopita, kuingiza mwanamke humu ndani ndiyo maana maneno yote hayo yanawatoka.”Msafiri alizungumza maneno yale huku akimtazama usoni Mbuya. Walipokutanisha macho yao kila mmoja akayakwepesha macho yake kwa mwenziwe. “Msafiri kwa mara nyingine tena nakushukuru sana kwa msaada wako ulioufanya kwangu, nami sina cha kukulipa mungu ndiye ajuae. Ila nina ombi kwako nilikuwa naomba nikae hapa hadi siku ya tarehe yangu ya kesi ili nisikupe mashaka. Kwani nisipoonekana mahakamani dhima hii utaibeba wewe, na kwa ukarimu na utu wako nisingependa kukupa usumbusu usiokuwa wa lazima!” Mbuya alimwambia Msafiri maneno yale, huku akitia huruma kwake. Msafiri alifikiri sana katika kichwa chake, akaona kama atamkatalia kisha akaondoka na tarehe ya Mahakama asipotokea hakika atampa yeye matatizo, kwani karatasi zote alizopeleka Mahakamani ni za ukweli kuanzia mjumbe hadi nyumba na mtaa aliojaza katika karatasi zile. Lakini pia moyo wake ukafika mbali sana akaona kuwa hawezi kukaa na waridi akaacha kunukia. Hivyo kwa kuwa hakuwa na mwanamke wa kustarehe nae, akaona hapo Mbuzi ameangukia kwa muuza supu. Hivyo hakuwa na namna ya kukataa ombi lile akaukumbuka ule msemo usemao Kufa kufaana hivyo akamkubalia kwa mikono miwili. “Mbuya nashindwa kukukatalia kuishi hapa kwangu, lakini mimi na wewe ni jinsia tofauti hivyo je huoni kwa kulala chumba kimoja kitanda kimoja, kitaniletea usumbufu wa mwili mwenzio?!” Msafiri alimwambia mbuya huku akiwa hamtazami usoni moja kwa moja, tamaa ya mwili ilimtawala hadi moyo wake ukashindwa kupiga vizuri kwa hatua zake. “Msafiri kwa ukarimu wako, na utu wako kwangu hakika utakacho kwangu radhi chukua, kwani ungechukua pesa zangu na kuondoka mie ningekupatia wapi? Ila ningekaa katika matatizo makubwa kwani siku nne nilizokaa Jela, nimeona kama nimekaa mwaka mzima. Hivyo kwa hilo shaka ondoa tutaishi pamoja hadi kesi hii itakapokwisha utaamua wewe khatima yangu.” Msafiri kwa majibu yale, akajiona ni mwenye bahati ya Mtende kumea Jangwani, hivyo hakutaka kuipiga teke ile aliyoiita riziki kitako. “Basi sawa hakuna shida kama ndiyo hivyo, wewe nenda kajimwagie maji uondoshe nuksi ya jela, mie nakwenda kufata vitafunwa ili tupate chai, na kuongea mengineyo” Msafiri alimwambia mbuya akamuonesha ndoo yakuogea, pamoja na sabuni na kilipo choo kisha yeye akatoka ili akanunue vitafunwa vya chai. Alipotoka pale nje aliwakuwa wale wapangaji wenzake wametandika mkeka nje wakinywa chai, huku macho yao yote yakiwa katika chumba cha Msafiri. “Hamuwashi, Hamzimi, mwaona donge la nini, kama mnaweza pandeni juu mkazibe, wanadamu,walimwengu kama yetu yawakera, mbona mtakereka sana, na mtakereka sanaaaa!” Msafiri aliporomosha wimbo huo wa mipasho alipokuwa akipita mbele ya wale wambea, walioacha kunywa chai vyumbani mwao, wakaamua wakae uwani kwa pamoja ili kupata umbea. Dongo lile walijikuta wakikaa kimya wakawa wadogo kama nukta, kwani walitahayari maana Msafiri alipokuwa akiimba wimbo huo huku akipita, haikuchukua muda mrefu Mbuya nae akatoka akiwa ndani ya taulo la Msafiri akienda kuoga.

Usiku wa siku ile ulikuwa mdogo sana kwa Msafiri kwani, alilala akiwa amemkumbatia mrembo Mbuya ambae hakika hakupata usingizi mzuri kwa siku nne alizokuwa Gerezani. Kwani alikutana na adha kubwa ya Kunguni na mbu, hivyo pale akiwa huru alilala kwa kujiachia akawa anakoroma kabisa. Msafiri alipokuwa akimtomasa ili kuivunja amri ya sita, mbuya alimwambia kuwa kutokana na msukosuko alioupata wa mahakamani na kwenda jela, amepatwa na Hedhi bila kutarajia, hivyo akamuomba Msafiri afanye subira kwani bado yupo kwake, hivyo atakula tunda hadi alikinai mwenyewe! Msafiri hakuwa na ubishi kabisa juu ya jambo lile aliona hana sababu ya kufanya pupa, kwani kila mwenye pupa hadiriki kula tamu. Hivyo alivumilia ingawa aliweza kupapasa hapa na pale katika maungo ya Mbuya, akajitesa maumbile yake sana kwani Mbuya alikuwa na joto ambalo lilimfanya msafiri kila muda ‘Mwamvuli’ wake kufunuliwa na upepo! Lakini ilikuwa ni tofauti kwa Mbuya, kwani yeye alilala raha mustarehe wala hakuwa na hata chembe ya kuhemkwa kutokana na uchovu aliokuwa nao.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Hali ile ya kulala pamoja bila Msafiri kuambua kitu, ilidumu kwa takribani siku tatu. Mbuya akiwa kwa Msafiri akipika na kupakuwa wakilala chumba na kitanda kimoja lakini kwa hakika hakukuliwa tunda kabisa ndani ya siku hizo tatu, kwa udhuru uliokuwapo. Msafiri hakutaka kuruka ukuta, bado alikuwa katika subira kubwa akiamini kuwa Mvumilivu hula mbivu.

Marafiki wa Msafiri walimshangaa sana rafiki yao kuwa hawamuoni mara kwa mara kijiweni nyakati za jioni kucheza Drafti, hivyo wakadhani labda anaumwa wakaamua waende kumjulia hali kwani siyo kawaida yake kutoonekana. Walipofika kwake wakamkuta Msafiri amejaa tele kama pishi ya mchele hana wasiwasi kabisa, ana kifaa siyo cha uswazi ni mtoto wa matawi ya juu. Wale marafiki zake walimsalimu kisha wakatoka nae nje rafiki yao ili kuzunumza nae. Walipokuwa nje wakamsifu kwa kuwa na msichana mrembo namna ile, wakamuuliza alipompata, Msafiri akawaeleza ukweli kila kitu, kuhusu kumpata kwake mwanamke yule. Hapo ndipo marafiki zake walipomshangaa rafiki yao na kumketisha chini, wakamwambia maneno ambayo yalimuingia barabara katika masikio yake akayazingatia kwa makini, na mwisho akawaahidi marafiki zake anakwenda yafanyia kazi. Msafiri akaagana na marafiki zake akarejea chumbani kwake akiwa mnyonge sana, kuliko alivyotoka ndani mle.

Mbuya Fabiola alimtazama kwa makini Msafiri usoni mwake, akamuona amebadilika sana, akamshangaa na kumuuliza. “Msafiri umepatwa na nini, kwani naona umebadilika sana huna furaha kulikoni, au marafiki zako wamekuudhi?” Msafiri alitikisa kichwa kuonesha kuwa hakuudhiwa na marafiki zake. “Sasa umepatwa na nini unaumwa?!” Mbuya akamtupia swali lingine, Msafiri akatikisa kichwa kuwa haumwi. “Sasa una nini hebu niambie basi kwani unavyokuwa hivyo unanitia mashaka mie.” Mbuya alimwambia maneno yale, kisha akainuka pale alipo na kumsogelea karibu ili amwambie kilichomsibu. “Mbuya, siwezi kuendelea kukaa na wewe humu, hadi kwanza twende kwenu nikapajue, niwaone wazazi wako, ndiyo tunaweza kuishi mimi na wewe humu. Unajua tunafanya hatari sana kuishi pamoja hivi bila mie kupajua kwenu, hivi ukianguka sasa hivi mie nakupeleka wapi? Kwa hiyo hata marafiki zangu wamenishauri, na mie nimeona ni kweli hivyo ninahitaji kwenda kwenu kupajua ndipo tutakaa pamoja.” Msafiri aliposema maneno yale, Mbuya alishusha pumzi ndefu kisha akakaa kimya kama dakika mbili hivi, akiwa anatafakari. Alipokuja kuinua uso wake akasema huku machozi yakimlengalenga machoni mwake. “Msafiri mie kwetu nikionekana tu, nitapata matatizo makubwa sana, kwani baba yangu ndiyo alienipeleka Mahakamani akanifungulia kesi ya matusi ya nguoni, lakini hakika mie sijui kutukana kabisa, bali baba alifanya vile ili kuniadhibu nikae jela labda nikitoka nitakuwa mtoto mtiifu, hivyo akiniona nakwenda nyumbani na yeye akijua mie sipo jela, Baba ataniuwa msafiri, naomba kama hutaki kukaa na mimi na wewe ndiyo ulienidhamini, basi nitafute mdhamini mwengine ili wewe ujivue dhima yakunidhamini, na mimi baada yakudhaminiwa na mtu mwengine, nitajua pa kwenda lakini kunipeleka nyumbani hapana nakuomba usifanye hivyo msafiri” Mbuya machozi yalimmwaika kama aliepigwa, lakini Msafiri akakaza uzi kuwa pale hakuna rai nyingine ila kwenda kupajua anapoishi ili awaone na wazazi wake. Mbuya aliomba hadi akapitiliza lakini mtoto wa kusini alikuwa haambiwi hivyo, aliendelea kukaza kamba kuwa ni lazima waende nyumbani kwao.

“Sawa nimekusikia Msafiri, ila wazazi wangu kwa sasa hata kama tutakwenda muda huu, hatuwezi kuwakuta ila kesho tukishaamka basi tutakwenda hakuna tabu, ila tambua kuwa unanipeleka katika matatizo makubwa.” Mbuya Fabiola alimwambia Msafiri huku akimtazama na kutia huruma, lakini haikuwa dawa hata kidogo kwani Msafiri aliendelea na msimamo wa kufata ushauri wa rafiki zake. Amesahau kuwa akili za kuambiwa, changanya na zako!

Siku ile usingizi haukuwapata watu wale, kwani Msafiri alichelea kama akilala asije kukimbiwa wakati yeye ni mdhamini katika kesi inayomkabili Mbuya, wakati Mbuya yeye alikuwa hana usingizi akiwaza kwenda kukutana na baba yake kwani anamjua mzee wake matata yake, lakini pia kuna jambo lingine kubwa ambalo hakumwambia Msafiri kwa nini hataki kurudi kwa baba yake.

Hakika hali haikuwa nzuri kabisa kwani Mbuya alipotaka kwenda chooni usiku ule, msafiri alimsindikiza na kurudi nae chumbani, yaani ilikuwa hakuna kuachana hata kidogo ilikuwa mithili ya Mbuyi Yondani ‘Vidic’ dhidi ya Hamisi Tambwe ‘Magoli’. Asubuhi kulipopambazuka Mbuya akamuuliza kama Msafiri bado ana nia ile ile, jibu alilolipata lilikuwa ndiyo bado nia ipo, ni lazima akapajue nyumbani kwao ndiyo waishi wote ili likitokea lakutokea ajue sehemu sahihi ya kumpeleka. Mbuya tofauti na usiku alivyokuwa mnyonge, baada ya kujua msimamo wa Msafiri alitabasamu akatikisa kichwa chake kwa masikitiko!

“Sawa mie wazazi wangu wanaishi Mtoni Kijichi hivyo tunaweza kwenda.” Baada yakunywa chai Mbuya alimwambia Msafiri yeye yupo tayari kwa safari, hiyo ikiwa ni majira ya saa tano asubuhi ikienda saa sita mchana. Msafiri akajipanga kwa kwenda kwa kina Mbuya akaulamba(Akavaa vizuri) kisha wakaongozana mguu kwa mguu hadi Mbagala Kizuiani, wakapanda gari za Kariakoo, wakashuka katika kituo cha KTM Mbagala, wakavuka barabara na ng’ambo ya barabara ile kulikuwapo magari yaliokuwa yakifanya safari za kwenda Mbagala kuu na Mtoni Kijichi, wakapanda gari pamoja na safari ya Mtoni Kijichi ikawadia, gari ilitembea hadi katika kituo ambacho Mbuya alishuka na Msafiri akashuka nae, yaani ilikuwa ni ng’adu kwa Ng’adu.

Mbuya alikuwa amenuna kupita maelezo, alikuwa ametangulia mbele na Msafiri akiwa kwa karibu nyuma yake hakuna maongezi baina yao yaliyozungumzwa. Mwendo wao ulifika tamati katika nyumba moja kubwa ya kifahari, iliyokuwa na geti mbele yake. Mbuya alibinya kengele na mlinzi alichungulia nje alipomuona mpigaji wa kengele ile ni Mbuya, aliufungua mlango kwa wahaka mkubwa, huku akionesha mshangao wa wazi machoni mwake. Mbuya aliingia ndani na Msafiri nae akaunga tela. Mbuya baada yakuingia ndani alimuuliza mlinzi kama baba yake yupo ndani, mlinzi akamjibu kuwa yupo sebuleni. Mbuya akamtaka msafiri aingie ndani sebuleni, na Msafiri hakuwa na ubishi akajitoma ndani. Walipoingia ndani ya Sebule ile, Kapteni Fabiola alikuwa amejaa tele akiwa anaangalia Runinga pale sebuleni. Kitendo cha kumuona mwanae Mbuya akiwa ameongozana na mtu kilimshangaza sana kwani hakutarajia kumuona mwanae nyumbani kwake. Mbuya alipiga magoti kwa baba yake akasema nae huku akilia mchozi wa nguvu. “Baba yangu nakuomba samahani sana, sasa nimejua kosa langu nataka kurudi shuleni. Huyu bwana niliekuja nae ndiyo aliekuwa akinizuzua nisiende shule, na hapa ameniagiza nije nichukue nguo ili niende kwao niondoke kabisa hapa mjini. Yule mwanaume aliekuwa gerezani keko, kwa kosa la kunirubuni kuacha masomo hakika yule siyo aliekuwa akinirubuni, ila huyu bwana niliekuja nae ndiyo anaenichanganya akili yangu, kwani hata uliponipeleka Jela yeye amekuja kunidhamini ili tuishi sote sasa nina siku ya nne nipo nyumbani kwake, nikipika nakupakuwa nimekosa baba yangu mie nimerejea nyumbani nataka kusoma, kwani Ng’ombe akivunjika mguu hurudi zizini, nimekosa mzazi wangu kumbuka Baba kuwa Mwenda Tezi na Omo, marejeo Ngamani.”

Msafiri alipigwa na Butwaa kubwa, akapata kigugumizi cha mwaka, kwani kilichotokea kilikuwa ni kitendo ambacho hakukitarajia hata kidogo, hivyo kulitokea mtafaruku wa hali ya juu uliomgharimu sana.





Kapteni Fabiola, alimtazama mwanawe akawa amekasirika vibaya sana, kisha akageuza uso wake kumuangalia Msafiri. Uso wake ulijenga makunyanzi pale alipomuona Msafiri akitabasamu huku akitikisa kichwa chache kwa masikitiko, na kukataa maneno ya Mbuya kuwa si kweli hata kidogo. Kitendo kile cha kutabasamu kwa Msafiri, kilimzidisha hasira na presha sana Kapteni Fabiola, hivyo alikurupuka pale alipokuwa akamvamia Msafiri kwa makofi mazito ya mashavu. “Yaani jambo la hatari wewe unachekelea siyo?” Msafiri alichanganyikiwa vibaya sana kwani, pale alipokuwa ameketi akicharazwa makofi, macho yake yaligota ukutani akaziona picha za Kapteni Fabiola akiwa amevaa sare za jeshi. Moyo wa Msafiri uliripuka ripu, akaiona hatari iliyokuwa mbele yake. “Hapana Mzazi wangu mie sicheki kwa mazuri, bali najisikitikia mimi mwenyewe wema wangu umeniponza, mwanao angesema ukweli kuliko huu uongo anaonizulia mbele yako, Mbuya usemayo ni kweli mie nimekurubuni usisome wewe? Ni kweli kuwa tumekuja hapa kwenu ili uchukue nguo zako nikutoroshe?, mie nina ujinga wapataje hata nije na wewe hadi hapa kwa kukutorosha mbona unanitafutia matatizo naomb…..” Msafiri hakumalizia kauli yake kwani Kapteni Fabiola alimnyamazisha kwa ukali. “Shat up! Unasema unasingiziwa huyu katokaje jela hukumdhamini au umemdhamini?” Msafiri huku woga ukichukua nafasi katika mwili wake, akamjibu yule mzee. “Ameniomba nimdhamini mzazi wangu ndiyo nikafanya hivyo, mie nilikuwa Mpita njia tu!” Kapteni Fabiola alimtandika kibao kikali cha uso Msafiri, akaona nyotanyota zikipita mbele yake. “Mpita njia anaweza kumdhamini mtu, asiemjua? Hebu usinifanye mie mtoto mwenzio. Huyu umemdhamini leo au ulikuwa nae nyumbani kwako?” Kapteni Fabiola alikuwa Mbogo kwelikweli. “Mmmm hapana sijamdhamini leo, ila…..!” Msafiri hakumalizia maneno yake kwani pale alipokili tu kuwa hakumdhamini siku ile, Kapteni Fabiola akathibitisha maneno ya mwanawe kuwa alimuweka kinyumba. Ghazabu zilimpanda hadi akawa anatetemeka akamtandika kibao cha Kelbu, Msafiri akatoa yowe kubwa la uchungu. “Pumbavu zako unasema wewe ulikuwa ni Mpita njia tu humjui mwanangu, ungeweza kukaa nae nyumbani kwako?! Unataka kumpa Ukimwi mwanangu? Leo utajua kilichomtoa Kanga manyoya!” Kapteni Fabiola baada yakusema maneno yale alimvamia kwa hasira Msafiri akaanza kumuadhibu kwa kipigo cha Mbwa mwizi. Mbuya alimtazama msafiri kwa muda anavyoadhibiwa, kisha huyoo akashika njia akaingia chumbani kwake, huku machozi yakimtiririka bila kujitambua, donge zito likiwa limemkaba rohoni mwake, alipoingia chumbani akajibwaga kitandani huku akilia kwa kwikwi. Aliikumbuka siku kama ile ya ijumaa alipokuwa mahakamani mara Msafiri akawa akipita njia pale nay eye akamuita, na kumuomba amdhamini. Machozi yalimzidi sana yakawa yameziba macho yake. Mara akasikia sauti ya Msafiri akilia kwa uchungu huku akiongea kwa sauti ya kukoroma. “Utaniuwa mzee wangu, mimi sijatembea na mwanao, mie nilikuwa Mpita njia tu sikuwa namfahamu kabla. Mbuya umenisaliti kwa mzazi wako unaniulisha mwenzio, nakufa dada Shuwea Buriani, nakufa Mpwa wangu sitokuona tena, nani atakulea Mpwa wangu, utakulia jela bila hatia, ooo mungu wangu nisaidie mja wako, wewe pekee ndiye unaojua ukweli wote, wema umeniponza mie, oooo mama yangu weeee!” Mbuya aliposikia maneno yale fikira zake zikenda mbali hadi gerezani, akamuona dada yake Msafiri, Shuwea Namjupa alivyomtendea wema katika siku nne alizokuwa amekaa gerezani, akakumbuka mkasa aliomuhadithia uliompelekea hadi kufungwa kifungo kirefu namna ile, akamkumbuka mtoto wake mdogo wa mikononi anaenyonya, akakumbuka kuwa Shuwea alimwambia kuwa kaka yake Msafiri ndiye anaemshughulikia kwa rufaa ili atoke Jela,na ndiye anaetarajia kumchukua mwanawe amlee mara atakapomuachisha ziwa. Kwani Rufaa inaweza kukubaliwa au kukataliwa.

Mbuya alikurupuka mbio hadi pale sebuleni akamkuta Msafiri akiwa amelazwa chini na baba yake amemkalia juu, mkono wake wenye nguvu ukiwa umeikaba shingo ya msafiri kwa nguvu. Mbuya huku akilia alimwita Baba yake huku akiwa anamvuta amuachie Msafiri huku akitamka kwa nguvu. “Baba utauwa basi imetosha baba msamehe.” Kapteni Fabiola hakusikia la Muadhini wala la Mnadi Swala, aliendelea kuukandamiza mkono wake uliokomaa kwa nguvu pale shingoni. Msafiri macho yalimtoka pima, pumzi zikampaa akaanza kuishiwa nguvu huku akikoroma, kwani ile kabali ilikuwa imemshika barabara. Mbuya hakutaka kusubiri tena, kwani huruma ilimwingia, nafsi yake ilimsuta kwa usaliti alioufanya akataka kujikosha kwa namna yoyote ile. Alimvamia baba yake akamsukuma pembeni huku akilia kwa kwikwi. Kapteni Fabiola alianguka pembeni akimuachia Msafiri akamgeukia mwanae akaanza kumchapa makofi ya uso. Msafiri baada ya kuachiwa alichukua pumzi kwa haraka, akajitutumua pale chini akijizoazoa akafanikiwa Kuinuka pale chini huku akipepesuka akatoka uani. Mlango mkubwa ulikuwa umefungwa hivyo akatimua mbio hadi pale mlangoni, akafungua geti kubwa ili atoke nje atokomee zake kusalimisha maisha yake, mara akamuona mlinzi wa Kapteni Fabiola akimfata mbio pale getini akitokea nyuma ya nyumba ile, kisha akasikia sauti ya Kapteni Fabiola ikimuamrisha yule mlinzi. “Kamata huyo shuwayni haraka sana.” Msafiri akafanikiwa kufungua mlango akatoka nje na kukimbia. Mlinzi wa Kapteni Fabiola alifungua mlango nakumuona Msafiri akikimbia. Ndipo nae alipoanza kumkimbiza lakini Msafiri kwa kuwa alikuwa akiinusuru roho yake alikuwa akikimbia kwa kasi zaidi. Watu walipomuona Msafiri akikimbia wakamshangaa sana, lakini yule mlinzi akaanza kuita kwa kelele “Mwizii huyooo, Mwizii huyooo, Mwizii huyooo.” Wale raia hawakutaka kualikwa, bali na wao walimuunganishia huku nao wakipiga mayowe ya “mwizii, Mwizii, Mwiziii” Kila mtu aliekuwa hana mbio, aliokota jiwe akarusha ilimradi mwizi apatikane, hakika mzahamzaha huwa kweli, baada ya muda kidogo tu, kundi kubwa la watu lilipatikana, likawa linakimbiza mwizi huku wakiazimia kumuua mwizi yule! Mara mbili watu waliokuwa mbele yake walimchota mitama wakampa ngumi za uso na mateke ya mbavu, nae akajitahidi kupambana akafanikiwa kusimama na kuendelea kukimbia, hadi pale alipofika katika nyumba ya Mjumbe Onesmo Baharia akajichoma ndani na kujifungia mle chumbani akaingia uvunguni akihema kwa nguvu. Na kundi la wale watu likawa nje likimdai mwizi wao wamuue, na kutaka kuchoma moto nyumba.

***http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Askari Polisi baada yakumchukulia melezo, Kapteni Fabiola wakamchukua Mbuya Fabiola wakamtaka awapeleke nyumbani kwa Msafiri ili kwenda kujiridhisha kuwa kweli alikuwa nae, ili kuandaa ushahidi mzuri wa kesi yake. Mbuya hakuwa na namna ya kukanusha, bali kwenda na askari wale ambao walimsihi Kapteni Fabiola aidha awasubiri au aende nyumbani akapumzike, kwani kesi ile imeshafika mikononi mwao, hivyo wanaishughulikia kikamilifu kwani nae alitaka kuongozana nao kwenda nyumbani kwa Msafiri. Kapteni Fabiola aliamua kusubiri pale ili aondoke na mwanawe.

Msafara ule uliongozwa na mbuya aliekuwa amewekwa mbele kati ya dereva na askari kiongozi aliekuwa kwenye msafara ule. Hatimae walifika Mbagala kizuiani katika nyumba aliyopanga Msafiri, askari wale wakajitoma ndani ya nyumba ile wakiwa na Mbuya, na kuwaita wenyeji wa nyumba ile ili kuwahoji. Baada yakutoka wenyeji wale askari walijitambulisha kwao, na mara moja walianza kazi yao. “Mnamfahamu huyu msichana?” Staf Sajent aliwatupia swali lile wale wenyeji huku akiwatizama usoni mwao kwa makini. “Huyu si mpenzi wake msafiri huyu? Ndiyo tunamjua alikuja hapa na msafiri chumba chao hicho hapo.” Dada mmoja alimjibu askari yule, kitendo kilichowafanya wale askari watizamane na kutikisa vichwa vyao kuwa kweli Msafiri alimuweka kinyumba mwanafunzi. “Huyo Msafiri yuwapi muda huu?” Yule askari kiongozi aliuliza swali gumu kwa wale wenyeji jibu lake akiwa analo, ila alikuwa na malengo maalumu yakutupia swali lile. “Mmmm sie hatujui kwani walitoka wote hapa na huyo mpenzi wake, labda huyo mpenzi wake atakuwa akifahamu alipo bwana wake, kwani amefanya nini?” Dada mmoja alieimbiwa mafumbo na Msafiri alijibu na kuuliza swali huku akiubibidua mdomo wake. “Je huyu binti alishawahi kulala humu na huyo bwana wake?” Staf Sajent alimuuliza yule dada ambae kisaikoloji alishamtambua kuwa hawendi vizuri na mpangaji mwenziwe, hivyo akautumia mwanya huo ili kupata ushahidi zaidi wa kesi ile. “Unauliza Embe Kibada? Ameshalala sana humu huyo, alikuwa akipika na kupakua na rusha roho tumeimbiwa kuwa sie tuna wivu, sasa sie tumuonee wivu Msafiri anaekaa chumba cha uani ana nini?!“ Yule dada alipouliza swali lile ana nini? Mara akatokea mwanamke mwengine aliekuwa pale akajibu kwa dharau. “Nashangaaa!” akikusudia kuwa anashangaa kwa lipi hadi amuonee wivu Msafiri. “Sawa sasa mpangaji mwenzenu yupo kituo cha Polisi Maturubai, anakabiliwa na mashitaka ya kumrubuni na kumtorosha mwanafunzi, hivyo tulikuja hapa kujiridhisha kama alikuwa amemficha hapa au wapi, lakini kwa mujibu wa majibu yenu hakuna shaka kuwa alikuwa nae hapa. Staf Sajenti aliwaambia wale wapangaji wenzake Msafiri. Askari walivuna taarifa muhimu kutoka kwa wale wapangaji wenzake Msafiri, hatimae wakapata ushahidi wa kutosha kuwa Msafiri ni hawara yake Mbuya, hivyo waliorodhesha majina ya mashahidi wale kisha wakachukua na namba zao za simu, wakawaambia kuwa wakihitajika kwenda kutoa ushahidi wa waliyoyaona wasisite kufanya hivyo. walirudi kituoni wakiwa na ushahidi huo wa watu waliowaona wanaokaa nyumba moja kuwa walikuwa wakiishi pamoja Msafiri na Mbuya.

Walipofika kituoni walimruhusu Mbuya aondoke na baba yake, na wao wakamtoa mahabusu Msafiri kwa ajili yakuchukua maelezo yake. Msafiri alipotoka mle mahabusu ya polisi alikuwa amevimba mara mbili ya mwanzoni, maumivu yalipanda katika mwili wake, michubuko iliyokuwa ikitoa damu ilikuwa imegandia na kufanya azidi kutisha, pia alikuwa akiugulia mbavu zake,kuwa zinamuuma sana, Jicho moja lilivimba akawa haoni vizuri, mdomo wa chini ulichanika kwa ngumi ya aliyopigwa mdomoni na raia wenye hasira kali, shingo yake alikuwa na alama za vidole za kukabwa, kichwa chake kilikuwa kimejaa manundu hakika alikuwa akihisi maumivu makali sana. Akawaomba wale askari wampeleke hospitali, kwani hali yake ilikuwa mbaya sana kwa maumivu. “Toa maelezo kwanza kisha tutakupeleka Hospitali, kwani hatuwezi kukaa na wewe bila yakuwa na maelezo yako.” Askari aliekuwa na cheo cha Koplo alimlazimisha Msafiri atoe maelezo yake katika hali ile aliyonayo.

Mara Mkuu wa kituo kile aliingia akamkuta Msafiri akiugulia maumivu huku akiwa ameshika mbavu zake. “Vipi huyu kafanya nini keshakwapua simu za watu?” Yule askari aliekuwa akimchukulia maelezo alisimama akapiga saluti kwa mkubwa wake kisha akamjibu. “Raia Afande wamefanya kazi yao” Msafiri pale alipoketishwa chini, alikuwa akisikia kizunguzungu kwani alimwaga damu nyingi sana, akajisikia kutaka kulala, Yule askari wa cheo cha Koplo, akamkaripia kuwa asilale pale. Mkuu wa kituo akauliza amepigwa kwa kosa lipi, akajibiwa kuwa aliitiwa kelele za wizi ndiyo raia wakamtengeneza vile. Mkuu wa kituo akatoa amri apelekwe hospitali kwani alimuona hali yake haikuwa njema kabisa. Polisi Yule alimjibu kiongozi wake “Sawa Afande tutampeleka ila gari muda huu imetoka ipo doria, mara itakaporudi tutampeleka.” Yule Mkuu wa kituo alitumia simu ya upepo kuita gari, na nusu saa baadae Msafiri akachukuliwa kupelekwa Temeke hospitali, lakini walipokuwa njiani kuelekea hospitali Msafiri alianza kuhangaika kama mtoto aliepatwa na ugonjwa wa degedege, akawa akikutua miguu na mikono huku macho yamemtoka, mithili ya mgonjwa wa kifafa, na baada ya muda akatulia tuli, wala asitingishike huku jasho jingi likimtoka mwilini mwake. Wale askari waliokuwa nyuma ya gari ile walimtazama namna alivyokuwa akihangaika bila msaada wowote, kwani wangefanya nini na wao siyo watabibu? Baada ya msafiri kutulia akiwa mwili wake unatoa jasho jingi askari mmoja akawaambia wenzake, “Humu hakuna Mtu!” Wale askari wakampa taarifa kiongozi wao alieuwa mbele ya gari ile, safari ikaendelea hadi katika Hospitali ya Serikali ya Temeke. Msafiri bado hakuweza kutikisika mwili wake, bali ulizidi kumwaga jasho jingi, ama kweli binaadamu kama hujafa bado hujaumbika.



.



Daktari wa Temeke Hospitali alimpokea Msafiri haraka, akamkagua mapigo ya moyo wake akampima mapafu yanavyopumua, akaamuru haraka apelekwe Muhimbili kwani hali yake ilikuwa mbaya sana iliyohitaji hospitali ya rufaa ambayo ina madaktari bingwa na wingi wa vifaa. Haraka haraka akapakiwa katika gari ya wagonjwa ya Hospitali ile, na dripu za maji zikaning’inizwa huku maji yale yakiingia katika mwili wa Msafiri. Gari ile ya wagonjwa iliwashwa taa zote na kuliza king’ora ili kutembea kwa haraka barabarani. Huku gari ya polisi ikiwa sanjari na gari ile aliyopakiwa Msafiri. Hali ya Msafiri bado ilikuwa haijabadilika hata kidogo kwani alikuwa hana kauli wala hatikisiki, kitaalam alikuwa yupo kwenye Koma. Unapokuwa katika hali hiyo unakuwa duniani haupo, Akhera wanakutafuta! Unakuwa humjui anaetoka wala anaeingia, yaani unakuwa nusu mfu. Hivyo mtu anapokuwa katika hatua hiyo inataka umahiri wa dakitari, na siku zako za kuishi zikiwa hazijesha ndiyo unaweza kurejea duniani, vinginevyo watu wengi wamebadilishwa majina yao nakuitwa Marehemu Fulani.

Gari ilikimbizwa kadiri dereva alivyopata njia, ingawa foleni za Dar es salaam, wakati mwengine husababisha hata namna yakuokoa wagonjwa na majanga ya moto, kushindikana kutokana na msongamano wa magari. Kwa kuwa Bahari kuu ndiyo ivukwayo, hatimae wakafanikiwa kufika katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili, taratibu zikafanywa za kukabidhiana mgonjwa, ikiwapo Police Form Number 3, (PF3) Msafiri alipokelewa na madakitari bingwa, akakimbizwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) mara moja huduma za kuokoa maisha ya mgonjwa yakafanyika, huku Msafiri akiwa chini ya ulinzi.

***

Mbuya Fabiola aliporudi nyumbani na baba yake, akaamriwa siku ya Jumatatu atapelekwa shule, hivyo akaingia ndani na kujifungia chumbani kwake, akakaa kitandani akiwa ameshika tama, ikawa akiwaza na kuwazua. Alimfikiria msafiri mateso aliyoyapata kwa ajili ya kumgeuka, akafikiri kuwa Msafiri angemuelewa yote yale yasingetokea, kwani wangeishi pale pamoja. Lakini ubishi wa msafiri umemgharimu sana. Mbuya alitumia mbinu ya kutoa mwiba wa makalio akae chini kisha ndiyo atoe mwiba wa mguu. Hivyo aliona ameshapokelewa nyumbani tayari, mambo mengine yatafata. Alikaa katika hali ile takribani saa nzima akiwaza na kuwazua, hatimae akawa amepata kitu cha kufanya, alipata njia ya kupita katika matatizo yake.

***http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Siku ya Jumatatu, katika Gereza la Segerea la wanawake, Odeli wa kifungwa alikuwa akiita jina la Mfungwa Shuwea Namjupa. (ODELI, NI MTUMISHI NDANI YA GEREZA) Hivyo Shuwea alikuwa amekaa anampa uji wa dona mtoto wake, katika majira ya saa tatu asubuhi. Uji ambao hunywa watu wazima, uji usiokuwa na kiwango bora kwa mtoto, wala kwa watu wazima. Lakini Shuwea angepata wapi uji wa lishe, angepata wapi maziwa ya kopo, hakuwa na namna ila kumpa uji aliokuwa akiupata. Shuwea Namjupa aliinuka na mtoto wake akaenda kumfata yule Odeli ili kujua kulikoni. “Unahitajika ofisini kwa Mkuu wa Gereza, kuna koti limekuja.” Shuwea alishangaa sana kusikia kauli ile, kwani alimuelewa vizuri sana yule Odeli pale aliposema Koti, alikuwa akimaanisha ni Wakili kwa lugha ya watu wa jela. Shuwea akaongozana na Odeli yule hadi kwa mkuu wa Gereza ambae ni mwanamke, akaingia ofisini kwake, akachuchumaa chini ikiwa ndiyo heshima ya Mfungwa anapokuwa mbele ya askari Magereza. “Kaa chini kwani utachuchumaa hadi saa ngapi?” Mkuu wa Gereza akiwa na askari mlinzi pembeni yake, alimwambia Shuwea kwani vile alivyokuwa amechuchumaa na mtoto begani, angeumia. “Kuna wakili huyu amekuja anahitaji kuzungumza na wewe, hivyo atajitambulisha kwako na utazungumza nae ili akusaidie.” Mkuu wa Gereza alimwambia Shuwea huku akimtazama yule wakili wa kike aliekuwa amevaa suti ya rangi nyeusi iliyokuwa imemkaa vyema kabisa. “Naitwa wakili Neema Faraja, natoka katika taasisi ya haki za binaadamu nchini, nimepewa taarifa zako siku ya Ijumaa hivyo nimeona nije nikusikilize ili nikusaidie, hivyo unahitajika kuwa wazi kwa kila kilichojiri ili niangalie namna gani naweza kukusaidia kisheria.” Yule wakili alijitambulisha na kumfahamisha Shuwea Namjupa anachotakiwa kufanya. Mshangao mkubwa ulimtawala Shuwea Namjupa, kwani alikuwa akifahamu fika kuwa hakuwa na pesa ya kumlipa wakili, wala kaka yake Msafiri hana pesa za kumlipa wakili, hivyo wakili huyu atamfanyaje? “Nani aliekuhadithia habari zangu?!” Shuwea alijikuta akimuuliza Yule wakili kwani alikuwa na wasiwasi asijekuwa siye wakili, halafu akaharibu mwenendo wa rufaa yake ambayo alikuwa ameshaanza kufatiliwa na kaka yake, ambae hadi kufikia siku ile ya jumatatu, Shuwea alikuwa hana raha kwani kaka yake hajamuona kumtembelea na siyo kawaida yake. “Shuwea huniamini kama mimi ni wakili? Vyema wasiwasi ndiyo akili naomba uangalie kitambulisho changu hicho hapo.” Wakili Neema Faraja alitoa kitambulisho akamuonesha Shuwea Namjupa usoni mwake ili akisome. “Nimekuja hapa Gereza la Segerea, kuna wafungwa wengi sana, lakini nimekuita wewe hivyo sidhani kama itakuwa na maana sana kumjua mtu alieniambia matatizo yako, ila zingatia tu kuwa huyo mtu alieniambia matatizo yako, pia ameshanilipa pesa niliyoitaka tayari ili kukusimamia katika matatizo yako, hivyo kama ukiwa huitaji msaada wangu, basi mie nitaondoka kwani sidai chochote.” Shuwea alitafakari kwa kina kisha akaamua kupiga moyo konde, akaamua kukisaliti kidole na jiwe liwalo kwake naliwe. “Sawa nimekuelewa na nipo tayari kupata msaada wako.” Shuwea alimwambia Yule wakili, huku akimuweka mtoto wake chini pale katika zulia jekundu la ofisi ile. “Kutokana na teknolojia ilivyo ninakupa kifaa hiki utakitumia kuongea kama kipaza sauti, kifaa hicho kitarekodi mazungumzo yako, kisha mimi nitakaa kusikiliza kila ulichokiongea kisha nitazame namna yakukusaidia.” Wakili Neema Faraja, alimwambia Shuwea maneno yale, kisha akampa kifaa kile kilichokuwa na ukubwa wa simu, akakiwasha na kumpa ili aeleze ni namna gani au mahakama gani, iliyomfunga na ilikuwaje.

“Mimi naitwa Shuwea namjupa, Mzaliwa wa Nachingwea Mkoa wa lindi. Nimehukumiwa kifungo cha miaka thalathini na kazi ngumu, na Mahakama ya Wilaya ya Ilala Mkoa wa Dar es salaam nime…..!” Shuwea kabla hajaendelea kuzungumza, Wakili Neema Faraja, aliingilia mazungumzo yake kwa wahaka mkubwa. “Umesema umehukumiwa kifungo cha miaka Thalathini na mahakama ya wilaya ya Ilala?!” Shuwea alimshangaa Yule wakili, kwani alichokiuliza ndicho alichokizungumza yeye. “Ndiyo nimehukumiwa kifungo cha Miaka Thalathini na kazi ngumu, kutokana na kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na mahakama ya Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es salaam.” Shuwea alirudia maelezo yake huku akiongeza kesi iliyomfunga huku akimtazama Yule wakili usoni mwake. Ila kitu kilichomshangaza Shuwea, alipokuwa akiitaja mahakama ya Wilaya ndiyo iliyomuhukumu adhabu ile, yeye alikuwa akitikisa kichwa chake juu chini huku akitabasamu! “Ehee ilikuwaje hadi ukahusishwa na shitaka hilo? Je ulitenda kweli hiyo kesi au umebambikiwa kesi na polisi?” Wakili Neema Faraja alimuuliza Shuwea huku akiwa makini sana. “Hapana mie sikutenda kosa hilo, ila nakumbuka miaka miwili nyuma, mie nilikuwa nikifanya kazi za ndani kwa mama mmoja wa kihindi Upanga jijini Dar es salaam. Nilikuwa nikikaa pale pale upanga mashariki. Utendaji kazi wangu ulikuwa ni mzuri tu, mie nilikuwa napika, kufanya usafi katika nyumba ile mali ya shirika la nyumba la taifa. Nikiwa ni mtu ninaelipwa pesa yangu ya mshahara nikawa nafurahia kazi yangu. Muajiri wangu alinipa simu ili kuwasiliana kama wakiwa wanakuja au kunipa maagizo haya na yale.” Shuwea alinyamaza kusema akamdhibiti mwanae aliekuwa ameinuka akitaka kumfata Yule wakili. Baada yakumdhibiti mtoto wake akaendelea kueleza. “Ile simu ilikuwa na uwezo wa kuunga mitandao ya kijamii, hivyo nilijiunga katika mitandao ya facebook, Whatsaap, Badoo, Telegram, Twoo, Viber, Tango na mengineyo ili kuwasiliana na watu mbalimbali duniani. Hivyo katika mitandao hiyo nilimpata mchumba humo tukawa tukiwasiliana mara kwa mara. Siku moja aliniuliza sehemu ninayoishi nikamwambia ukweli kuwa mie ninafanya kazi za ndani kwa wahindi, yeye akaifurahia kazi yangu, akaniambia kuwa kazi ni kazi bora mkono wende kinywani.” Shuwea alinyamaza kuzungumza akameza mate, kisha akaendelea. “Basi katika mazungumzo yetu, akaniambia anataka tuonane. Nikamwambia mie nafasi yakutoka ni ndogo sana kwani muajiri wangu ana mama yake mtu mzima, hivyo mie ndiyo nakaa nae, kwa hiyo siwezi kutoka kwenda hata sokoni, kwani kila kitu kipo ndani, na mboga mboga kuna watu maalumu huwa wakileta pale nyumbani. Yeye akaniambia kuwa ile ni kazi tu, kwamba leo ninayo itaweza kutokea siku nyingine nikawa sina, hivyo akaniambia tuonane ili ikibidi tuweze kuzungumza ana kwa ana hatimae tukikubaliana, aweze kunioa na kuwa mkewe. Mie nikamwambia nitatokaje katika mazingira kama yale, akanambia kwamba yeye atakuja nyumbani, mie niseme ni ndugu yake hivyo tutaweza kuongea mengi ya mimi na yeye. Basi mie nikaona sina namna ila niseme hivyo kwa muajiri wangu yeye atakapokuja pale nyumbani. Nikamwambia siku yakuja, nikamuelekeza nyumba namba, hatimae siku hiyo akaja nikaonana nae kwa mara ya kwanza kabisa. Kwa kweli alikuwa ni mvulana mzuri, mcheshi sana, Alikuwa Hb hasa, nikamtambulisha kama ndugu yangu kwa muajiri wangu. Basi mchana akawa akija pale nyumbani baada ya muajiri wangu kutoka kurudi dukani akisha kula, kwani mama yake wakati huo wa mchana huwa chumbani kwake amelala. Yule bwana tukawa tukifanya mapenzi kwa siri palepale nyumbani nyakati za mchana, na kwa kuwa mie sikuwa na uhuru wakutoka, basi nikawa natimiziwa mahitaji yangu ya mwili palepale nilipo, kwani mbuzi hula kwa urefu wa kamba yake. Mimi sikuwahi hata siku moja kutoka kwenda nyumbani kwake bwana Yule, wala sikuwahi kupajua hadi leo hii. Maisha yaliendelea hivyo hadi nikaona siku zangu zimegoma mwisho wa mwezi kutoka. Nilipomwambia Yule bwana hali hiyo, akaonesha kufurahi akanambia nisihofu atanioa na kulea mtoto wake kama kawaida kwani nae hakuwa na mtoto. Bwana Yule nilimpenda sana hadi nikawa natoa pesa zangu za mshahara nampa ili arekebishe mambo yake. Baada ya mahusiano ya namna ile kudumu kwa miezi mitatu, siku moja mchana alikuja yeye na rafiki yake mmoja ambae ndiyo mara yangu ya kwanza kumuona siku ile. Hivyo alipogonga kengele mie nilikwenda kumfungulia mlango kwani alishanipigia simu kuwa anakuja yeye na rafiki yake, akidai kuwa ni mshenga wake anakuja kuniona ili nimuelekeze amtume nyumbani kwetu kupeleka barua ya posa. Hivyo nilifurahi sana, hata baada yakuingia ndani nilikwenda nao kwa mama wa muajiri wangu kumuelekeza kuwa nimepata ndugu yangu mwingine leo amenitembelea, basi nikawaandalia chakula wageni, huku nikiwa na furaha tele moyoni mwangu, na mie Shuwea kuidiriki ndoa kuwa mke wa mtu. Basi baada ya kula wakanambia wao hawakai sana, bora niwaelekeze namna gani wanaweza kufika nyumbani kwetu. Mie nikamuelekeza Yule mgeni mpya, kijijini kwetu na mtu wa kumuona, hatimae akasema atakwenda siyo siku nyingi kutoka siku ile. Hivyo wakanambia wanataka kwenda kumuaga mama wa muajiri wangu, nami nikawapeleka hadi chumbani kwake, tulipofika chumbani kwa mama hakika sikutarajia wala sikuamini kitu kilichotokea. Nilihisi nipo katika usingizi mzito nikiota ndoto!”

***

Madaktari walikuwa wakijitahidi kwa kiasi kikubwa sana kuokoa maisha ya mgonjwa wao, mashine za gesi zilikuwa zimefungwa ili kusaidia mapafu kupumua vizuri, dripu za maji na damu zilikuwa katika mishipa ya mgonjwa Yule zikiingizwa kwa mwendo usiokuwa wa taratibu, sindano za kuzuia wadudu wa Tetenasi, na za kumpa nguvu mgonjwa, zote zilidungwa katika mwili wa mgonjwa Yule, huku Oxgen ikiwa imefunguliwa kwa wingi katika kifaa maalumu kilichokuwa, kimefungwa baina ya mdomo na pua yake. Madaktari wale walikuwa na vifaa maalum kama pasi ndogo ya umeme viwili, wakiviweka katika kifua chake, ili kuupa nguvu moyo wa Mgonjwa wao uweze kushituka na kupeleka mapigo ya moyo sawasawa. Hali ile iliendelea kwa dakika takribani ishirini, ndipo mashine inayopima mwenendo wa moyo na kuonesha mapigo ya moyo yanavyokwenda, ikatoa mlio mkali wale! madaktari watatu waliokuwa wakimshughulikia mgonjwa Msafiri pale kitandani kwake, wote wakageuka kuiangalia wakiwa na wahaka mkubwa!





Madaktari wale waliitazama ile mashine, iliyokuwa ikipiga kelele huku ikionesha mapigo ya moyo ya Msafiri yanavyosoma. Madatari wale walipongezana kwa kazi nzito na ngumu waliyoifanya hadi kufanikiwa kuokoa maisha ya mgonjwa wao. Ile mashine ilikuwa imepata mapigo yale na ndiyo maana ikawa inapiga kelele, Wale madaktari walikuwa hawajaamini kama mapigo yale yamepatikana vyema kwani hali ya mgonjwa ilikuwa tete. Ndiyo maana waliitazama mashine ile kuhakikisha ujuzi wao kama haujapoteza. Kwani wao kwa uzoefu wao, hutambua milio ya mashine ile inapopiga kwa mtu akiwa anapumua, lakini pia inapopiga kwa mtu akiwa hapumui yeye mwenyewe. Kwa mlio uliopiga pale ulikuwa ukiashiria kuwa, moyo wa mgonjwa umeamka na unapumua wenyewe. Madaktari wale waliendelea kumuachia mashine puani mwake ili kumsaidia kupumua kwa muda mrefu, kiasi cha nusu saa hivi wakaitoa puani kwa mgonjwa na kumuacha mgonjwa akiendelea kupumua vyema mwenyewe, na si kwa msaada wa mashine. Damu na maji yaliokuwa yakiingia kwa kasi katika mwili wa Msafiri, vimetoa matokeo mazuri sana. Msafiri alikuwa akipambana kupigania uhai wake, nafsi yake ilikuwa ikiugua sana kwani ilikuwa na majukumu ambayo haijayatenda bado. Baada ya siku moja akiwa pale katika chumba cha wagonjwa mahututi, Msafiri alihamishwa wadi ile akapelekwa katika wadi namba kumi na moja Kibasila, akawa akitibiwa majeraha ya vidonda na Nesi Hafsa Mwagala.

***http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Shuwea alipofika sehemu ile katika kuhadithia kwake, machozi yakamlengalenga machoni mwake. Alifuta machozi kwa sare yake yakifungwa ya rangi ya Njano iliyokuwa na maandishi meusi (MU) Magereza Urekebishaji aliyokuwa amevaa kisha akaendelea kueleza. “Yule niliemtambua kama mshenga, alijipinda ubavu wa kushoto ikawa kufumba na kufumbua, mikononi mwake alitoa Bastola ndogo nyeusi, akaikoki na kutuamrisha kuwa tutulie vilevile tusilete rabsha au atatuuwa kwa risasi. Kisha yule aliekuwa mpenzi wangu aliinama akapandisha suruali yake, akatoa gundi/plasta pana la plastiki jeupe linalotumika sana katika kufungia mizigo hasa ya box, akanigeukia mie tukawa tunatazamana uso kwa uso. Yule Mshenga alimwambia aliekuwa mchumba wangu, wape utamu hao. Nikawa sikuelewa lakini mara baada ya yule alieuwa mpenzi wangu kuelezwa wape utamu hao, akanifunga plasta ile pana ya plastiki mdomoni mwangu huku akiizungusha mikono yangu nyuma na kunifunga na gundi lile lenye nguvu yakunasa sana. Kisha akanilaza chini kifudifudi, uso wangu ukiwa umeelekea upande aliekuwa mama wa muajiri wangu. Nikafungwa miguu na plasta nikawa siwezi kuinuka, siwezi kuongea wala kushika chochote, kwa namna nilivyofungwa. Ila macho na masikio ndiyo yaliyokuwa yakifatilia tukio lile baya sana kwa upande wangu. Yule mama wa muajiri wangu yeye presha ilimpanda sana akawa akitetemeka huku akisema. Shuwea naleta mizi dani ya jumba yetu, veve nasema ni dugu yako kumbe naonesha mizi jumbani yetu. Yule mama alikuwa akiongea lugha ya kiswahili kibovu cha Kihindi. Mie nikalazwa chini kifudifudi pale nilipokuwa nimelala nikamsikia yule mshenga akimwambia yule mama wa muajiri wangu kuwa aoneshe pesa zilipo au anamuua kwa risasi. Yule mama alikuwa mgonjwa wa presha na muoga kupindukia, hivyo alikuwa hataki kufa kwa ajili yakusalimisha pesa, akawaambia wafungue kabati lililokuwa pale chumbani kwake katika mlango wa kati ndiyo kuna pesa za mwanawe alipokuwa akizihifadhi. Baada yakuambiwa hivyo na yule mama nae wakamfunga ile plasta waliyokuwa wakiita kwa jina la utamu, Katika mdomo wake, wakamfunga mikono na miguu yake pia. kisha kwa macho yangu pale nilipokuwa nimelala chini niliinua kichwa changu, nikashuhudia mabandari ya noti za dola za Kimarekani, na pesa za Kitanzania, zikihamishwa kutoka pale kabatini na kuingizwa katika mfuko. Hakika sijawahi hata siku moja kufikiri, wala kuona kama katika kabati lile kunaweza kuwa na pesa nyingi namna ile. Yule aliekuwa mchumba wangu akatoa mfuko mkubwa wa nylon mfukoni mwake, akazishindilia zile bandari za fedha katika mfuko ule, kisha wakachukua na simu yangu wakatokomea nisipopajua.” Shuwea alinyamaza kuzungumza, kwani sasa uchungu ulimuingia sana hasa baada yakuachwa na mimba, lakini pia kuuziwa kesi nzito namna ile iliyohusisha silaha ya moto. Baada yakufuta machozi akaendelea kumuelezea yule wakili, ili aokoke katika mazingira magumu ya ushahidi kama yale, kwani Mfa maji heshi kutapatapa, hivyo na yeye alikuwa akijiokoa na kifungo kirefu. “Ehee baada ya kuwa wewe umelazwa chini kifudi fudi ukiwa umefungwa, na mama wa muajiri wako nae pia amefungwa nini kiliendelea?” Wakili Neema Faraja alimsaili Shuwea huku akiwa na wahaka mkubwa sana wa kujua mwenendo wa kesi yake ulivyokwenda. “Baada ya Mchumba wangu na Mshenga kuchukua pesa nyingi sana, pesa zilizojaa kwenye mfuko mkubwa wa plastiki, wakatuacha pale na plasta zetu wao wakatoka na kutufungia mlango kwa nje wakatokomea zao. Tulikaa katika hali ile kwa takribani saa tatu nzima, ndipo alipokuja Muajiri wangu, huku akiita jina langu kwa nguvu. Nikafahamu kuwa bosi atakuwa amenipigia simu sana lakini hakunipata. Hata alipokuwa akiniita bado pia hakuweza kupata jibu langu, kwani nilikuwa najaribu kuitika lakini sauti haikuweza kutoka. Ndipo niliposikia mlango wa chumba tulipokuwapo chumba cha mama wa muajiri wangu ukifunguliwa, mara nikasikia sauti ya mwajiri wangu ikimwita mama yake huku akilia kwa uchungu! Nadhani kwa hali aliyoiona ya kabati languo mlango wa kati kuwa wazi, lakini pia sie kuwa katika kifungo cha plasta. Yule muajiri wangu alimuwahi mama yake akamfungua yale mapalasta. Baada yakufunguliwa yule mama akamwambia mwanawe kwa uchungu mkubwa, kuwa mie nimepeleka Majambazi nyumbani kwao, kwani watu niliokuwa nimewatambulisha pale kama ndugu zangu kwake, wamemtolea Bastola nakutufunga plasta wakaiba pesa zote za kabatini. Tena ikasemekana kama mie nilipanga mchongo ili wale wezi waje kuiba. wamejifanya na mie kunifunga plasta na kuchukua simu yangukama geresha tu, ili baadae nikapewe mgao wangu kitu ambacho si kweli hata kidogo. Yule bosi wangu hakuhangaika na mie kunifungua zile plasta, bali alipiga simu polisi na mie nikaja kuchukuliwa kituuteni nikapelekwa kituo cha polisi Msimbazi. Pale kituoni kwa kweli hakukuwa hata na askari mmoja aliekuwa amenielewa, pale nilipokuwa nikiwaeleza kuwa wale wezi sikuwa nawajua kabisa mahala wanapoishi. Japo pale kwa muajiri wangu, niliwatambulisha kuwa ni ndugu zangu. Kwa kweli kichapo na kibano nilikipata hasa kwani Polisi walikuwa wakizania kuwa ninajua kila kitu katika wizi ule, ila ninaficha ukweli. Kitu nilichoshukuru katika kupigwa kwangu kote, sikupigwa tumboni kwangu kwenye mimba yangu au mimba ingetoka.Lakini bora hata wangenipiga tumboni, ikatoka mimba ile kuliko adha anayoipata mwanangu kukaa gerezani bila hatia yoyote. Wale polisi walinilaghai kuwa nikubali kuwa ninawajua wale jamaa kuwa ni ndugu zangu, na kwamba wao hawatanipeleka mimi mahakamani bali watanifanya niwe shahidi wao! Mie nikabakia katika ukweli kuwa sikuwa nikiwajua wale wezi wanapoishi, ila kitu ambacho sikuweza kukikana, ambacho nilikili ni kule kuwatambulisha wale wezi kuwa ni ndugu zangu. Lakini ukweli wangu ulionekana ni uongo usiokubalika, kuwa watu niliowatambulisha kuwa ni ndugu zangu kisha niwe siwajui, na sifahamu wanapoishi. Hakika haikumuingia mtu yeyote akilini mwake lakini ndivyo ukweli ulivyokuwa, kuwa sikuwa nawatambua watu wale mahala wanapoishi.”

***





ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog