Simulizi : Mpita Njia
Sehemu Ya Pili (2)
Siku ya jumatatu Mbuya Fabiola, alirudishwa shule na baba yake, akakabidhiwa kwa uongozi wa shule, akawekwa kitako akasemwa sana juu ya umuhimu wa elimu, kwani walimuona kama mtu aliekuwa katika kipindi cha ujinga. Hivyo walimpa taratibu za kuishi shuleni pale, na kama akikaidi basi atafukuzwa shule. Kupokelewa kwake tena shuleni pale, ni kwa sababu ya heshima ya mzazi wake shuleni pale, kwani katika shule ile, baba yake amepewa nafasi yakuwa mlezi. “Huyu kulikuwa na watu wakimdanganya, ila mie nimeshachukua hatua stahiki, na kesho mshtakiwa aliemrubuni mwanangu, atapelekwa mahakamani Temeke, kwani Polisi wa kituo cha Maturubai wamenipigia simu na kunipa taarifa asubuhi hii. Hivyo nadhani sasa mwanangu atasoma, naomba walimu mumpokee nakumpa ushirikiano unaostahiki.” Kapteni Fabiola aliwaambia walimu waliokuwa pamoja waliomketisha chini mwanawe Mbuya Fabiola kumuelimisha. Baada yakikao cha karibu saa nzima, Mbuya aliruhusiwa kuendelea na masomo, akaambiwa aende bwenini kwake ili akajiandae kwa kuingia darasani. Kapteni Fabiola aliagana na walimu akashika njia akenda zake kazini, akimuacha mwanawe pale shuleni alipokuwa akikaa pale pale. Mbuya Fabiola, aliinuka akaelekea Bwenini huku akiwa hana raha hata kidogo moyoni mwake. Alipofika Bwenini akatua begi yake ndogo akaifungua, akatoa simu ya mkononi akaiwasha, kisha baada yakuwaka simu ile, akabonyeza namba alizozikusudia, na simu ya upande wa pili ikaita. Mbuya alishusha pumzi nzito pale simu ile ilipopokelewa. Aliongea na simu ile haraka haraka huku akitazama huku na kule. Alitumia dakika kumi kuzungumza na simu ile, alipokuja kukata simu ile, Mbuya aliitazama ile simu kisha akatabasamu.
***
Msafiri tangu amelazwa akiwa hajitambui hadi amerejewa na fahamu zake, hakuweza kumuona rafiki yake yeyoye kwenda kumuangalia pale hospitalini. Hali yake ilikuwa mbaya kwa upande wa chakula, kwani hakuwa na ndugu wakumpelekea chakula, bahati ilioje kwake ilikuwa ni mgonjwa aliekuwa jirani yake, alieletewa chakula na ndugu zake, alikuwa amekatazwa kula chakula kwa vile alikuwa akienda kufanyiwa upasuaji wa ngiri, hivyo chakula kile akawaomba jamaa zake wampe Msafiri ale. Msafiri alipokea chakula kile akala kwa kutafuna kwa tabu, kwani taya zake zilikuwa zikimuuma sana. Baada yakumaliza kula, mara aliwaona watu watatu wakielekea katika kitanda chake. Mmoja wa watu wale alikuwa amevaa koti kubwa jeupe, na wale watu wengine wawili walikuwa wamevaa mavazi ya kawaida. Walipofika pale kitandani kwa Msafiri Namjupa,, mmoja wa watu wale alikuwa ameshika bahasha ya ukubwa wa A4, mikononi mwake. akaifungua ile bahasha akatoa karatasi nyeupe zilizokuwamo katika bahasha ile, akachomoa kalamu ya wino katika mfuko wake wa shati akamkabili Msafiri. “Naitwa Coplo Deo Mrema, natokea kituo cha polisi maturubai Mbagala, tumekuja hapa ili kuchukua maelezo yako. Yule mtu aliejitambulisha kuwa ni askari, akawa tayari kwa kuchukua maelezo ya Msafiri Namjupa. “Mtuhumiwa wewe unaitwa nani, kabila yako, dini yako, kazi yako, na mahali unapoishi?” Askari Coplo deo, alimsaili mtuhumiwa. Msafiri aliyajibu maswali yale akiwa katika utulivu mkubwa. Yule askari aliandika majibu ya Msafiri katika karatasi nyeupe, kisha akamuuliza tena. “Unakumbuka nini hadi ikapelekea Polisi wamekuja kukukamata?” Msafiri alieleza katika maelezo yake, tangu alipomdhamini Mbuya, akakaa nae nyumbani kwake akiwa hapajui nyumbani kwao, akaeleza namna alivyomwambia Mbuya ampeleke nyumbani kwao ili akapajue, akamueleza namna walivyofika kwao na matatizo yaliyomtokea, akamueleza alivyokimbia nakupigiwa kelele za wizi, akamueleza alivyoshambuliwa na raia hadi akajisalimisha katika nyumba ya Mjumbe, akamueleza ujio wa askari hadi yeye kupelekwa Polisi maturubai, na katika hali asiyoifahamu alipoteza fahamu, alipokuja kurejewa na fahamu zake akajikuta yupo pale hospitali, lakini hakujua alifikaje pale. Ikawa ndiyo mwisho wa maelezo yake. Yule askari aliyaandika maelezo yale, kisha akamtaka Msafiri ayasaini maelezo yake. Msafiri akasaini sehemu aliyooneshwa. Baada yakusaini maelezo yale, wale askari wakamwambia Yule mtu aliekuwa amevaa koti jeupe. “Asante dokta, sie tumemaliza kazi yetu, tunashukuru kwa ushirikiano wako.” Wale watu walisema maneno yale huku wakimpa mkono Yule Dokta, kisha wakatoka nje ya wadi ile. Msafiri alikaa akatafakari akaona muda wowote, anaweza kupelekwa mahakani, kwani kuchukuliwa maelezo ni kuitengeza kesi. Siku ile ilipita vibaya sana kwa Msafiri kwa kuwaza mengi sana kichwani kwake.
Siku ya jumanne, nyakati za asubuhi msafiri akiwa kitandani kwake ameketi, akitazama watu wanaoingia na kutoka katika wadi ile, mara uso wake ukamuona mtu aliemjia jana kumchukulia maelezo yake.Moyo wa Msafiri ulipiga kwa kasi sana. Alimuona mtu Yule akimfata Msafiri pale alipo, alipomfikia hakukuwa na salamu, bali akamuamuru anyooshe mikono yake. Msafiri akanyoosha mikono yake, Yule askari akatoa pingu na kumfunga pingu mikono yake kwa mbele, kisha akatoka nae nje ya wadi ile. Walipofika nje, Msafiri aliiona gari ya polisi ikiwa na Polisi ndani yake, ikisogezwa na kuwekwa vizuri mkao wa kutoka. Msafiri alipandishwa nyuma ya gari ile, akaamriwa kukaa kitako. Gari ya Polisi ikaondolewa ikaelekea wilaya ya temeke, ikapiga breki katika mahakama ya wilaya ya Temeke, msafiri akapelekwa moja kwa moja Mahakamani kwa hakimu. Alipofikishwa mahakamani kesi iliyokuwa ikiendelea kusikilizwa ilipokwisha, akasimamishwa Msafiri katika mahakama ile akasomewa mashitaka mawili na karani Yule. “Mshitakiwa unaitwa Msafiri Namjupa, una miaka ishirini na saba, dini yako ni Islam, kabila lako Mmakonde,kazi yako ni kufanya biashara za kutembeza, unaishi Mbagala Kizuiani, kweli si kweli?” Msafiri alijibu “Kweli” kwa karani Yule, na karani akaweka alama ya pata katika karatasi yake kisha akaendelea. “Katika kosa la kwanza mnamo tarehe saba, ya mwezi wa tatu,mwaka huu wa elfu mbili na kumi na nne, siku ya Ijumaa, Mshatikiwa ulimdhamini Mbuya Fabiola, kisha ukaishi nae nyumbani kwako kama mke na mume, huku ukitambua kuwa Mbuya ni mwanafunzi, je kweli si kweli?” Msafiri huku moyo wake ukimuenda mbio kama saa mbovu akajibu “Sikweli”. Karani aliweka alama ya kosa katika karatasi yake, katika sehemu ile, kisha akaendelea. “Mshitakiwa katika kosa la pili, unashitakiwa kwa kumbaka Mbuya Fabiola na kumsababishia maumivu makali, je kweli au si kweli?” Msafiri akajibu “Si kweli.” Karani wa mahakama aliweka alama ya kosa katika karatasi yake pale katika fungu lile, kisha akaketi chini. Mara kikatokea kitendo ambacho Msafiri hakukitarajia kutokea, wala wale askari Polisi waliompeleka pale,kitendo kile kikamuacha kinywa wazi kwa mshangao!
Baada ya karani wa Mahakama kuketi kitako, mara bila kutarajia aliingia mwanamke alievaa suti ya rangi nyeusi, kisha akainama kama ishara ya heshima kwa Hakimu na kwa picha iliyokuwa ukutani ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kisha akaketi katika lile benchi alilokalia muendesha mashitaka wa Serikali kwa pendeni yake. Muheshimiwa hakimu baada ya kuandika, alimtazama Yule muendesha mashtaka wakili wa Serikali kama ana lolote la ziada, na Yule wakili akasimama na kueleza. “Muheshimiwa shauri hili limekuja kwa kutajwa, upelelezi wake umeshakamilika hivyo tunaomba tarehe ili tuje kumsomea Facts Mshitakiwa.” Alipomaliza kusema maneno hayo wakili wa Serikali akaketi katika benchi, na mara Yule Dada alieingia mwenye suti ya rangi nyeusi alisimama akajitambulisha. “Niiependeze Mahakama yako Mheshimiwa, naitwa wakili Neema Faraja, namuwakilisha Mshtakiwa Msafiri Namjupa.” Wakili Neema alipojitambulisha vile, ikawa ni mshangao kwa askari Polisi, pia ikawa ni mshangao kwa Msafiri. Msafiri alibaki mdomo wazi akiwa hajui aseme nini, kwani hakutambua Yule wakili amewekwa na nani, ili amtetee pale mahakamani, kwani amekwenda kwa wakati muafaka. Wale askari Polisi wao walishangaa kwa wakili Yule kusimama Mahakamani kwani hawakuamini macho na masikio yao kwa maneno ya Wakili kumtetea Msafiri kwa vile muda wote Msafiri alipokuwa hospitali hakupata kutembelewa hata na mtu mmoja, kwani Polisi waliokuwa wakimlinda Msafiri bila ya yeye kutambua kama analindwa, tena walikuwa wakibadilishana zamu ili Msafiri asitoroke, walishangaa kwa vile walimuona Msafiri ni lofa hivyo angelipata wapi pesa yakumuweka wakili?!
Wakili Neema Faraja hakukaa kitako alipojitambulisha, bali alimtazama hakimu aliekuwa akiandika katika jalada lake, kisha akaendelea kusema. “Mheshimiwa mteja wangu amepigwa kama unavyomuona hapa alipo, kichwa chake kimejaa plasta, mdomo umemvimba, jicho limemvimba, basi bila shaka hata ndani ya mwili wake atakuwa amepata maumivu makali, kwa kuwa ndiyo ameletwa ‘fresh Case’ naiomba mahakama yako iingize katika kumbukumbu jambo hilo. Pia naiomba mahakama yako, iiamuru Polisi watupe PF3 ya mgonjwa ili tuone kama dakitari amejaza alichomtibia mteja wangu, na kwamba tuone kama ameeleza maumivu na vidonda hivi vimesababishwa na kitu gani. Pia kwa kuwa wakili wa Serikali ameifahamisha Mahakama yako tukufu kwamba upelelezi umeshakamilika, basi naomba watupatie maelezo ya mashahidi ili kuja kuwahoji, ni hayo tu mheshimiwa kwa sasa” Wakili Neema Faraja baada yakusema maneno yale aliketi chini katika bechi.
Msafiri alikuwa kama yupo katika ndoto, kwani yeye hakuwa akijua chochote kinachohusu sheria. Hivyo kwake ilikuwa ni Neema na Faraja kubwa kama jina la wakili wake.
Mheshimiwa Hakimu, aliandika katika jalada lake maelezo yale, kisha akamwambia muendesha mashitaka wa Serikali. “Je unayo PF3 ya mshitakiwa hapo ulipo?” Muendesha Mashtaka akatazama katika karatasi alizokuwa nazo za kesi ile hakuwa na PF3 mikononi mwake, hivyo alisimama akamwambia Hakimu. “Mheshimiwa bado haijanifikia hapa, katika jalada langu hivyo sina.” Wakili Neema faraja alisimama baada ya wakili wa serikali kuketi, akamwambia Mheshimiwa Hakimu. “Mheshimiwa mteja wangu ametolewa hospitali na ameletwa hapa katika mahakama yako. Hivyo hakuna dakitari anaeweza kumtibu mgonjwa aliekuwa katika hali kama ya mteja wangu bila ya Police Form Number 3 (PF3) hivyo askari waliomleta hapa kutoka hospitali wapo, na natambua hawawezi kumchukua mgonjwa kienyeji tu kutoka hospitali,lazima watakuwa wamefata taratibu. Hivyo naiomba Mahakama yako iwaamuru watukabidhi PF3, kwani hiyo ni haki ya mteja wangu na tuna hoja nyingi tutazojenga kutokana na hiyo PF3.” Wakili Neema Faraja alikuwa akiongea kwa kujiamini sana kisha akaketi. Hakimu akaamuru askari waliokwenda na mshtakiwa waingie Mahakamani pale. Kiongozi wa Askari polisi aliingia pale Mahakamani akapiga saluti mbele ya Mheshimiwa hakimu akawa mtiifu sana.
“Unayo PF3 ya mshtakiwa?” Hakimu alimtupia swali Yule askari aliekuwa mbele ya Mahakama. “Eee ndiyo ninayo Mheshimiwa.” Yule askari alisema maneno yale, akaitoa ile PF3 akamkabidhi karani wa Mahakama ili ampe Hakimu. Karani aliipokea na kutaka kuiwasilisha kwa hakimu, lakini hakimu akamwambia ampe wakili wa mshitakiwa. Wakili Neema Faraja alipoipokea Form ile, aliitazama kisha akasimama na kuieleza mahakama. “Mheshimiwa PF3 hii, haijajazwa na Dakitari kuonesha alichomtibu wala kilichosababisha majeraha na maumivu ya mteja wangu, hivyo naweza kuieleza mahakama yako kuwa mteja wangu hakupelekwa hospitali na Polisi. Kwa kuwa hakupelekwa hospitali maana yake amekosa haki yake ya kimsingi ya kutibiwa. Hivyo basi naiomba Mahakama yako impe dhamana mteja wangu ili tukamtibie mheshimiwa.” Baada yakusema maneno yale, Wakili Neema Faraja akaketi. Hakimu aliandika yale maelezo kisha akawageukia upande wa mashitaka akawauliza. “Kwa nini hiyo PF3 haikujazwa na dakitari, yaani alitibiwajwe bila PF3? Kwa kawaida mgonjwa wa namna ya Mshtakiwa anapotokea Polisi kwenda Hospitali hutakiwa kuwa na PF3, na dakitari ajaze alichotibu, na aeleze kilichomsibu mgonjwa. Hivi akifa huyo sasa hivi mtasema amekufa kwa sababu gani?” Hakimu aliwaeleza upande wa mashitaka waliokuwa kimya bila ya majibu. “Shauri hili naliahirisha hadi baada ya wiki mbili, dhamana ya Mshtakiwa ipo wazi, mdhamini mmoja wa kawaida je Mshtakiwa unae mdhamini?” Hakimu aliahirisha shauri lile, nakumuuliza Msafiri ambae alikuwa ametoa macho tu kwa mshangao. Wakili Neema Faraja alisimama akasema kuiambia mahakama.‘Tunae Mdhamini Mheshimiwa. Taratibu zikafanyika Msafiri akadhaminiwa. Wakili Neema Faraja akaenda nae hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa kutumia usafiri wa gari yake.
***
Shuwea katika siku ile ya jumatatu, aliendelea kumfahamisha wakili wake Neema Faraja, matukio yaliyomtokea hadi alipofikishwa mahakamani. Akamueleza ushahidi uliotolewa na hatimae ushahidi ukambana kwa kushindwa kuvunja hoja nzito za upande wa mashitaka. Siku ya hukumu ilipofika hakimu aliisoma hukumu ya kumtia hatiani Shuwea Namjupa. Katika kosa la kwanza mahakama ilimuona na hatia ya kupanga njama katika siku isiyojulikana, muda wala sehemu waliyokaa,ili kutenda kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha. Hakimu aliisherehesha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya kumi na sita inavyomtia hatiani Mshtakiwa katika kosa kama hilo. Ni lazima washtakiwa wawe wakifahamiana kabla ya kosa wanaloshitakiwa kwalo liwe halijatendeka. Na kwa kuwa Mshtakiwa Shuwea namjupa ameshindwa kukanusha mbele ya mahakama kuwa washitaiwa hawajawahi kufika pale alipokuwa akifanyia kazi ambapo ndipo tukio lilipofanyika. Lakini pia alishindwa kukanusha kuwa washitakiwa walipokwenda katika nyumba iliyofanyika tukio, yeye aliwatambulisha kama ndugu zake. Na kwa kuwa mmoja wa mshtakiwa ambae hakuwapo mbele ya mahakama ile wala mwenzake walioshiriki kutenda kosa, ilielezwa na upande wa mashitaka kuwa alishakwenda nyumbani kwao mara nyingi sana, na Shuwea ameshindwa kukanusha kama Mshtakiwa ambae bado hajapatikana kama hakuwahi kufika katika nyumba aliyokuwa akifanyia kazi, ambae pia yeye alimtambulisha kuwa ni nduguye.Mahakama ikakubaliana na hoja za upande wa mashitaka pasi na shaka yoyote kuwa Mshitakiwa alikuwa akifahamiana na wahalifu wale ambao bado hawajakamatwa. Na kwa kuwa hakuna tendo lolote la unyang’anyi linalofanyika bila ya kupangwa. Hivyo Mahakama ikamtia hatiani katika kosa hilo na kumuhukumu kifungo cha miaka saba jela. Na katika kosa la pili la unyang’anyi wa kutumia silaha, mshitakiwa kwa kuwa alishatiwa hatiani kuwa alikula njama ya kutenda kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha, mahakama pia ikamtia hatiani katika kutenda kosa hilo, hivyo ilimuhukumu adhabu ya kifungo cha miaka thalathini jela na kazi ngumu, adhabu zikaambatanishwa, hivyo Mshtakiwa akahukumiwa kifungo cha jumla cha miaka Thalathini. Huo ukawa ndiyo mwisho wa maelezo ya Shuwea Namjupa kwa Wakili neema Faraja. Baada yakuelezwa maneno yale pia yakiwa yamerekodiwa katika kifaa kile maalum,wakili Neema Faraja alikichukua kile kifaa akakizima, kisha akatoa shukurani kwa mkuu wa gereza lile, akamgeukia Shuwea Namjupa akamwambia. “Kuwa mvumilivu kesi hii, naikatia rufaa muda si mrefu nakwenda kujipanga niangalie namna gani naweza kukuchomoa hapa ulipo.” Baada yakusema maneno yale akaaga na kumshumu Mtoto wa Shuweakatika shavu lake kisha kama aliekumbuka jambo akamuuliza Shuwea “Mwanao anaitwa nani?” Shuwea aliinua uso wake uliokuwa umeanza kupata Faraja akamjibu. “Nimeamua nimwite Matatizo” Wakili Neema akamtazama Shuwea kisha akamwambia “Mie kuanzia leo nitakuwa namwita Faraja jina la baba yanguna siyo Matatizo tena.” Baada yakusema maneno yale Wakili Neema Faraja akaaga nakutoka akisindikizwa na yule askari aliekuwa yupo na mkuu wa gereza katika ofisi ile.
***
Mbuya Fabiola alikuwa darasani akisoma lakini akili yake yote haikuwa katika chumba cha darasa bali ilikwenda mbali sana. Alikuwa akiwaza mambo yanavyokwenda. Mwalimu aliekuwa darasani akifundisha kila alipokuwa akimtazama Mbuya, alimuona hayupo kabisa katika kipindi chake. Hivyo alimrushia chaki ikamstua na kumuondosha kutoka katika lindi la mawazo alilokuwa amezama. “Wewe haupo hapa darasani unawaza nini?” Mwalimu alimuuliza huku akiwa amemsogelea pale alipokuwa amekaa. “Mwalimu naumwa na tumbo sijisikii vizuri hata kidogo.” Mbuya Fabiola aliongopa wazi kabisahuku akijipinda na kujinyonganyonga. Mwalimu alimtazama akamwambia “Nenda bwenini kapumzike” Mbuya alijizoazoa na kutoka katika chumba cha darasa akaelekea katika Bweni. Alipokaribia Bwenini tu alichanganya mwendo hadi ndani ya Bweni. Akiwa yupo peke yake wenzake wakiwa darasani aliingiza mkono katika Ashaakum alipokuwa ameificha simu yake akiwa ameizima, akaiwasha huku akiwa na haraka. Baada ya simu ile kuwaka alitaka kubonyeza kupiga simu ili aongee na mtu aliemwita muhimu, mara katika simu yake ukaingia ujumbe. Mbuya alipouona ujumbe ule, akamtazama mtu aliemtumia ule ujumbe jina lake, lakini halikutoka jina bali ilitoka namba tu, hivyo akaharakisha kuufungua. “Mbuya mpenzi baba yako ameniweka jela, kwa ajili ya Mapenzi yako kwangu, hivyo nateseka huku wewe ukiwa umetulia nje. Jumatano nakwenda mahakamani kwa Mara ya sita tangu niwe huku jela. Masharti ya Dhamana yaliyowekwa ni magumu kwangu. Mie sina ndugu wala jamaa anaefanya kazi Serikalini, vinginevyo ningekuwa nimeshadhaminiwa. Lakini wadhamini wawili wote wawe wafanyakazi wa Serikali nimekosa kutimiza masharti ya dhamana, hivyo kuonesha unanijali naomba unitumie pesa katika namba hii ili niweze kujenga mazingira yakuishi vyema jela. Hiyo ni namba ya jamaa tu humu jela ambae ndiyo amefanikiwa kuingiza simu, siyo namba yangu, ni mimi nilietayari kufa kwa ajili yako Iddy Teva. Mbuya alipousoma ujumbe ule moyo wake ukaruka sarakasi! Ujumbe ule ulitoka katika gereza la keko jijini Dare s salaam. Ulitoka kwa mtu aliepelekwa Jela na Baba yake kwa kosa kama la Msafiri. Mbuya alitazama salio lake la M pesa, akamrushia pesa kiasi ili aweze kutengeneza mazingira yakuishi jela. Kisha huku wahaka wa moyo ukimkabili Mbuya Fabiola, alibonyeza nambari kadhaa, kisha akawa akisikiliza upande wa pili simu ile ipokelewe. Baada yakupokelewa alizungumza na mtu Yule harakaharaka huku akiwa yupo makini kwa kila sentensi aliyokuwa akiiongea Yule mtu wa upande wa pili. Mbuya alipewa habari iliyomfanya achangamke kwa Furaha.
***
Wakili Neema Faraja, alifika katika hospitali ya taifa Muhimbili, akashuka pamoja na Msafiri wakaongozana hadi kwa mganga mkuu wa hospitali ile. Alipomuona alijitambulisha kwake, kisha akatoa ile PF3 nakumuonesha akataka dakitari aliemtibu mteja wake, aijaze kadili alivyomtibu, na aandike sababu za maradhi yake ili aifanyie kazi katika kesi inayomkabili mteja wake. Mganga mkuu aliipokea ile PF3, akalitazama jina lililoandikwa katika fom ile, kisha akaangalia katika kumbukumbu zake pale hospitali, akatambua Msafiri Namjupa alikuwa ameruhusiwa asubuhi pale hospitalini kwake, na madaktari waliomtibu pia walikuwa bado wapo kazini wameingia asubuhi ile. Mganga Mkuu akainua simu yake ya mkononi akampigia mganga kiongozi aliekuwa akimtibia Msafiri akamwita katika ofisi yake. Alipofika paleofisini kwa mganga Mkuu, akamuona Msafiri na mtu mwengine asiemfahamu. Hivyo Mganga Mkuu alimtambulisha kwa Wakili Neema Faraja akamuleza nia na madhumuni ya kwenda kwake pale, kisha akaoneshwa na ile PF3 ya mgonjwa aliemtibia aliekuwa mbele yake. Yule daktari kiongozi aliekuwa akimtibia Msafiri, akaitazama ile Form ya Polisi aliyooneshwa, akatikisa kichwa kwa masikitiko. Kisha alieleza jambo ambalo hakika Wakili Neema Faraja, lilimfanya atoe macho kwa fadhaa!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kiongozi wangu nasikitika kukueleza kuwa, hiyo siyo PF3 niliyoletewa mie, au ziwe zimeletwa mbili ila hiyo sikupewa. Kwani niliyoletewa mie nimeijaza na kuisaini. Lakini hii inaonesha jina lake tu mgonjwa.” Yule dakitari aliekuwa akimtibia Msafiri alimwambia Mganga mkuu, ambae ni kiongozi wake. Wakili Neema Faraja alitoa macho, fadhaa ikampanda akamtazama yule daktari kama vile hakumsikia alichokuwa amesema. Akajiuliza katika nafsi yake, kama dakitari amejaza PF3 ya mgonjwa, inakuwaje inabadilishwa tena mbele ya mahakama, hakuna ubishi kuwa mahakama imedanganywa kitu ambacho ni kosa kwa mujibu wa Sheria kuidanganya Mahakama. “Sasa Dokta kama uliijaza hiyo PF3, na sie tumepewa hii ambayo haijajazwa unatuambiaje, tukuamini wewe au walietupa hii wakisema ndiyo iliyotoka hospitali?!” Wakili Neema Faraja alimtupia swali yule muuguzi kiongozi, ambae alimjibu kwa msisitizo. “Kwa kawaida namna ya ugonjwa aliokuwa amekuja nao kijana hapo, tusingeweza kumtibia kama isingekuwapo hiyo PF3, kwani kuna wahalifu wanaweza kutibiwa kwa namna hiyo, kisha tukaonekana tunawasaidia wahalifu. Ndiyo kuondosha utata huwa tunawapokea wagonjwa hao kwa PF3. Baada ya kuwatibu huwa upande wa pili wa karatasi hiyo ndiyo sie tunajaza kila tulichokiagua kwake, na sababu za maradhi yake kwa mujibu wa vipimo na utaalam tulionao, hivyo haiwezekani umtibie mtu wa aina hiyo kisha aruhusiwe bila kuijaza karatasi hiyo.” Maneno yale yalimuingia sana Wakili Neema Faraja, akatikisa kichwa chake kwa kuonesha amemuelewa Dakitari yule. “Sawa Dokta nimekuelewa je tunafanyaje sasa ikiwa mteja wangu hana PF3 ambayo ni utetezi kwake lakini ametibiwa na wewe?” Wakili Neema Faraja alimtupia swali yule Dakitari huku akimtazama moja kwa moja usoni mwake. “Ninachoweza kufanya nikuijaza hiyo iliyopo, ikiwa ya awali haipo hakuna njia nyingine.” Alijibu yule Dakitari na Wakili Neema Faraja alimpa ile PF3 ili ijazwe. Dakitari aliijaza PF3 ile kwa mujibu wa alichomtibu mgonjwa wake, akajaza sehemu zilizopata maumivu, michubuko, mipasuko, uvimbe, na sababu ya maradhi yake, kisha akaisaini na kumkabidhi wakili mikononi mwake. Yule Dokta akamuuliza wakili Neema Faraja, baada yakumkabidhi ile karatasi aliyoijaza. “Je? kuna tatizo lingine, kwani nina mgonjwa namuhudumia wodini.” Wakili Neema faraja akamjibu. “Hapana Dokta sina tena tatizo lingine, kwani nilichokitaka tayari nimeshakipata, tena mbele ya mganga mkuu, hivyo mie natoka sasa nawashukuru sana kwa ushirikiano wenu.” Mganga mkuu alisimama akapeana mikono na Wakili Neema wakaagana, na Wakili Neema akaondoka na Msafiri pamoja. “Samahani Wakili wangu, unajua napata tabu sana za kufikiri tangu nipo Mahakamani hadi sasa hivi, ninaswali naomba kukuuliza.” Msafiri alimwambia wakili Neema, na wakili nae akacheka kisha akamjibu. “Natambua swali unalotaka kuniuliza, bila shaka ni nani alieniweka na kunilipa ili kukutetea wewe. Lakini naomba nikufahamishe jambo moja ambalo pia hulijui. Jana siku ya jumatatu nilikuwa gereza la Segerea kuzungumza na dada yako Shuwea Namjupa, amenambia kila kitu kinachohusiana na kesi yake, hivi leo nakwenda kujenga hoja kisha nitaiwasilisha Mahakama ya rufaa ili apate tarehe aende akasikilize rufaa yake.” Msafiri Namjupa hakika alikuwa ameghumiwa sana kwa majibu ya wakili wake. “Sasa umenipa swali lingine la ziada. Nilidhani unanitetea mimi pekee kumbe na dada yangu pia? Ninashauku sana kufahamu nani aliekuweka ututetee mimi na dada yangu?!” Msafiri Namjupa alikuwa haelewi kabisa akili yake imechoka kwa wakili yule kuwa ni mtetezi wao, bila yakumtambua mfadhili aliemuweka. “Msafiri nikikataa kukutajia huyo mtu wewe utakataa kutetewa na mimi?” Wakili Neema Faraja alimtupia swali lile huku akiwa anafungua mlango wa gari yake. “Hapana sina ujanja wa kukataa wakili, kwani nitafungwa mie sijui sheria hata kidogo. Ila kesi ikionekana ina wakili huwa mshitaiwa huburutwi kwani wanajua yupo mtu anaemtetea ambae anaifahamu sheria.” Msafiri alimjibu Wakili wake huku akipanda ndani ya gari yake, na wakili Neema akaiondosha gari ile mahala pale kwa mwendo wa pole. “Nimekula kiapo na huyo bosi wangu alienipa kuwatetea wewe na dada yako kuwa nisimtaje hadi mnamaliza matatizo yenu yanayowakabili, na kwa kuwa bado hatujayamaliza matatizo hayo, basi kiapo changu nakiheshimu sitomtaja kabisa.” Wakili Neema alikuwa akiendesha gari yake, akiwa yupo katika geti lakutokea katika hospitali ya Muhimbili, alikabidhi kadi yao pale getini kisha akaingia mitaani.
***
Wiki moja baadae, wakili Neema alikwenda katika Mahakama ya rufaa akawasilisha hoja yake nzito ya kisheria, dhidi ya mteja wake Shuwea Namjupa. Msajili wa Mahakama aliipokea hoja ile akaiweka katika mpango wa kuipa tarehe ili kwenda kusikilizwa rufaa ile. Wakili Neema Namjupa alikuwa ameumiza kichwa chake kwa hoja nzito yenye nguvu ya kisheria, ili kuonesha kuwa mteja wake amefungwa kimakosa kwa mujibu wa sheria. Aliishawishi mahaka ya rufaa imuachie huru mteja wake, kwani sheria ilikiukwa wakati wa kutoa maamuzi. Akajenga hoja pana yenye mashiko ya kisheria, kisha akaichambua Mahakama kuwa ipo kwa ajili ya kutekeleza sheria na kanuni ya adhabu, hivyo kwa kuwa sheria imekiukwa basi mteja wake Shuwea Namjupa aachiwe huru. Wakili Neema alitumia Mifano ya kesi zilizopita ambazo Jaji wa Mahakama ya rufaa alitolea maamuzi. Mwisho akasisitiza kuwa mteja wake amekaa rumande muda mrefu, ameshatumikia kifungo kwa miaka miwili sasa, lakini pia ana mtoto mdogo anaenyonya ambae hana hatia lakini yupo ndani ya gereza akiwa na mama yake, hivyo akaiomba ofisi ya msajili impe kipau mbele Mrufani kwa sababu hizo alizozitaja na zile alizojengea hoja kupinga hukumu ya mteja wake.
***
Wiki mbili zilipita Msafiri akiwa yupo sawa ki afya alipanda Mahakamani ili kusomewa Facts, Muendesha mashtaka wa Serikali alisimama na kuifahamisha Mahakama. “Mheshimiwa shauri hili limekuja kwa ajili ya kumsomea Facts mshtakiwa, upelelezi wake umeshakamilika.” Baada yakusema maneno yale akaketi katika Benchi kumpa nafasi wakili wa utetezi kujitambulisha, ili kuingia katika kumbu kumbu za mahakama.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/ “Naitwa wakili Neema Faraja namuwakilisha mshitakiwa.” Nae baada yakusema maneno yale akaketi katika bechi. Mheshimiwa hakimu alimuamuru karani wa Mahakama, kumsomea Facts mshitakiwa. Karani alisimama akachukua karatasi ya hati ya shitaka (Facts) akaanza kumsomea Mshtakiwa. Facts ilisomeka kwa kuandika jina la mshitakiwa, umri wake,dini yake, kabila yake, kazi yake, na sehemu anayoishi, kisha karani akamuuliza mshitakiwa kama ni kweli au si kweli, Msafiri akajibu kweli. Karani akamsomea mshitakiwa mashitaka mawili ambayo yote aliyakana kuwa si kweli. Karani akasoma Facts kuwa upande wa mashitaka utaleta mashahidi wane katika kuthibitisha shitaka lile, pamoja na kielelezo kimoja ambacho ni maelezo ya kukiri kosa mshtakiwa. Baada ya kusoma Facts ile karani alimkabidhi Hakimu, na hakimu akamtazama muendesha mashitaka kama ana ziada, nae akasimama na kueleza. “Muheshimiwa tunaomba tarehe ili niwalete mashahidi wangu, tuongee kesi.” Baada yakusema maneno hayo akaketi kitako akasimama Wakili wa utetezi. “Mheshimiwa naomba nipatiwe maelezo yote ya mashahidi muhimu katika shitaka linalomkabili mteja wangu, na ninaomba kama ikiwezekana kwa kuwa mashahidi wane ni wachache basi katika tarehe itakayoridhiwa na mahakama yako, mashahidi hawa wangeletwa wote ili tumalize ushahidi siku hiyo. Kwani naamini inawezekana.” Wakili wa utetezi alipokwisha kusema hayo akaketi kitako. Hakimu alimwambia karani kumkabidhi hivyo vitu wakili wa utetezi pamoja na nakala ya facts, nae akafanya hivyo. “Kesi hii naiahirisha hadi baada ya siku tatu, upande wa mashitaka hakikisheni mnaleta mashahidi wengi kama siyo wote. Mshitakiwa Dhamana yako bado inaendelea.” Kesi iliahirishwa Msafiri na wakili wake wakaondoka pamoja.
Baada ya siku tatu, kesi iliendelea upande wa mashitaka ilileta mashahidi watatu kwa mpigo,na kielelezo cha maelezo ya kukiri kosa mshitakiwa. Shahidi wa kwanza kupanda kizimbani kutoa ushahidi alikuwa ni kapteni Fabiola. Aliapishwa na karani wa mahakama kwamba ushahidi atakaoutoa utakuwa ni wa kweli, akiwa chini ya kiapo ikabainika kuwa anatoa ushahidi wa uongo basi sheria itachukua mkondo wake. Kapteni Fabiola alisimama Mahakamani akiwa chini ya kiapo kutoa ushahidi wake kama atakavyoongozwa na muendesha mashitaka. Hakimu alimtaka Msafiri Kusimama kisha akamuuliza kapteni Fabiola ambae ndiye shahidi namba moja kwa sababu ameanza yeye kupanda kizimbani kutoa ushahidi. “Shahidi unamfahamu Mshitakiwa aliekuwa mbele yako?” Kapteni Fabiola alimtazama Msafiri kwa chuki pale alipokuwa akajibu kuwa anamfahamu. Hakimu akamuamuru Msafiri aketi chini, akamuachia muendesha mashitaka amuongoze shahidi wake. “Shahidi umeieleza Mahakama kuwa unamfahamu Mshitakiwa, hebu ifafanulie mahakama unamfahamu vipi, na unatoa ushahidi wa jambo gani dhidi yake?” Wakili wa upande wa mashitaka alikuwa akimuongoza shahidi wake mbele ya mahakama kama sheria inavyomruhusu kufanya hivyo. “Nakumbuka mnamo siku ya ijumaa majira ya mchana, Mshitakiwa alikuja nyumbani kwangu Mtoni kijichi, akiongozana na mwanangu ambae hayupo mahakamani, baada yakufika mwanangu alinieleza kuwa Mshitakiwa alimuweka kinyumba nyumbani kwake, pia alimdhamini mahakani na kufanya nae mapenzi kwa nguvu katika siku nne alizokaa nae nyumbani kwake, hivyo alipokuja nyumbani kwangu, mwanangu alinieleza hayo na kuongezea kuwa amemleta pale ili achukue nguo zake na kumtorosha, kama itakavyokuja kuthibitishwa na Mwanangu mwenyewe ambae ni shahidi katika kesi hii.” Kapteni Fabiola alikuwa akiongea huku povu la mdomo likimtoka kuashiria hasira na presha vikimtawala katika moyo wake. “Ehee baada ya kukueleza kuwa amekwenda nae pale ili kuchukua nguo zake ili akaishi nae huko kwake nini kilifuata?” Wakili wa utetezi aliendelea kumsaili shahidi wake. “Baada ya kunieleza hivyo, nikamuuliza mshitakiwa kama ni kweli anayosema mwanangu, akakataa kuwa hakumpeleka kuchukua nguo, ila nilipomuuliza kama alimdhamini mahakamani akakubali kuwa kweli yeye ndiyo aliemdhamini. Baada yakukubali kuwa ndiyo aliemdhamini, mimi nilimkaripia sana, kabla sijamshika akakimbia kutoka nyumbani kwangu, na raia baada yakumuona anakimbia mbio kutoka nyumbani kwangu walimsimamisha lakini mshitakiwa akakataa kusimama, ndipo walipompigia kelele za wizi, na hatimae akakimbilia katika nyumba ya mjumbe, baada yakupata taarifa kuwa yupo kwa mjumbe tukatoka kufatilia ndipo nilipomkuta Mshitakiwa akiwa mikononi mwa Polisi amekamatwa. Hivyo nikafungua kesi hii ninayoitolea ushahidi.” Kapteni Fabiola alitua katika nukta hiyo akipindisha kabisa kama alitaka kumuua Msafiri kwa mikono yake, kama alichukua sheria mikononi, kwa kumkaba na kumtoa alama za shingoni, lakini pia alimtishia kwa silaha ya moto. Baada yakufika mwisho wa ushahidi wake, Wakili wa Serikali alimueleza hakimu kuwa “Ni hayo tu Mheshimiwa.” Kisha akaketi mahala pake. Hakimu baada yakuandika akamtazama Wakili wa utetezi ambae alikuwa ameshasimama tayari kwa kuhoji. Hakimu akamruhusu wakili wa utetezi amhoji Shahidi wa upande wa Mashitaka. “Shahidi umeifahamisha mahakama kuwa umeelezwa na mwanao kuwa amewekwa kinyumba, amedhaminiwa mahakamani na mteja wangu, lakini pia amembaka, je unaithibitishia mahakama hii, kuwa ushahidi wako ni wa kuambiwa na mwanano na si wakuona?” Mzee fabiola akajibu “Ndiyo nimeambiwa na mwanangu na ni kweli amemfanyia hayo.” Bada ya Kapteni Fabiola kujibu vile, Wakili Neema Faraja akamgeukia Mheshimiwa hakimu na kumwambia. “Mheshimiwa shahidi amekili mbele ya mahakama yako tukufu kuwa ushahidi wake ni wa kuambiwa. Na kwa mujibu wa Sheria ya ushahidi kifungu cha sitini na mbili sheria ya mwaka elfu moja mia tisa na sitini na saba, (Setion No 62 TEA 1967) sheria imetamka wazi kuwa ushahidi wenye nguvu na unaokubalika mbele ya mahakama ni ushahidi wa kuona tukio na siyo ushahidi wa kuambiwa. Hivyo naomba uutupilie mbali ushahidi huo kwani unamapungufu kwa mujibu wa sheria, hivyo sina swali la ziada kwa shahidi kwani hata ushahidi alioutoa wa kumdhamini motto wake mahakamani, siyo kesi inayomkabili mteja wangu mbele ya mahakama yako hivyo hauna maana ushahidi huo katika kesi hii.” Wakili wa utetezi Neema Faraja alikaa kitako, hakimu akaandika maelezo ya wakili kisha palepale, akatoa hukumu ya hoja ya Wakili. Kisheria inasemwa ni kesi dhidi ya kesi, hakimu alichimba vitabuni, akatoa hukumu kwa jambo lile. “Hakika kwa mujibu wa sheria Section No. 62 The Evidence Act of 1967, inatamka wazi kuwa ushahidi wa kuelezwa jambo haukubaliki mbele ya mahakama, isipokuwa ushahidi wa kuona, hivyo ushahidi wa PW 1, (Procequetion Witness No. 1)kwa kuwa amekili wazi kuwa ushahidi wake ni wakuambiwa, basi ushahidi wake hauna maana katika shauri hili.” Baada yakusema maneno yale Kapteni Fabiola alitolewa nje ya Mahakama, akiwa amevimba kwa hasira, ushahidi wake ukiwa umekataliwa. “Shahidi mwingine?” Hakimu alimueleza wakili wa upande wa mashtaka, akaingia askari mchukua maelezo ya mshitakiwa, akapanda Kizimbani akaapishwa, kisha akaanza kutoa maelezo yake. “Mie ndiyo mpelelezi wa shauri hili, Mshitakiwa namfahamu kwani nimemchukulia maelezo yake ya kukili kosa kwa hiyari, nilimpa haki zake zote za kimsingi, nilimuuliza kama anataka kuwa nashahidi au ndugu au jamaa yeyote yule wakati wa kutoa maelezo yake akasema kuwa hana haja yakuwa na shahidi na kwamba atatoa maelezo yake yeye mwenyewe peke yake. Baada yakukubali kutoa maelezo akakili kuwa anamfahamu Mbuya Fabiola, alikuwa nae nyumbani kwake. Akimdhamini Mahakamani na kuishi nae kinyumba kwa muda wa siku nne kama mke na mume. Baada yakutoa maelezo yake nilimpa ayasome, akaridhika na maelezo niliyoyaandika akasaini.” Shahidi alikamilisha maelezo yake, Hakimu akaandika maelezo yale, kisha akamtazama wakili wa utetezi, akamuona muda tu ameshasimama akiwa damu yake inamchemka katika kushindana kisheria. Baada ya hakimu kumruhusu kumuhoji shahidi, Hakika kilitokea kitu kikaharibu kabisa kesi ile!
Hakimu baada ya kusomwa maelezo yale yakukili kosa mshtakiwa, akauliza upande wa utetezi kama wana pingamizi dhidi ya maelezo yale yasipokelewe kama kielelezo na Mahakama. Wakili Neema Faraja akasimama na kujibu kwamba wanalo pingamizi. “Mheshimiwa kwa mujibu wa maelezo hayo kama yalivyosomwa mbele ya Mahakama yako,muda wake yaliyochukuliwa yamepoteza sifa za kupokelewa kuwa kielelezo katika shauri hili. Nitatoa sababu tatu muhimu kwa nini yasipokelewe maelezo haya kama kielelezo. Katika CRIMINAL PROCEDURE ACT (CPA) OF 1985, SECTION NO 50 SUB SECTION 1, sheria imetamka wazi kwamba mshitakiwa anapokamatwa, anapaswa kuchukuliwa maelezo yake ndani ya saa nne toka kukamatwa kwake. Ingawa pia natambua kwamba kwa mujibu wa sheria hiyohiyo ya mwenendo wa makosa ya jinai kifungu namba 51, kinasema kuwa askari anaweza kuomba kibali kwa hakimu kuomba muda uongezwe kutoka saa nne hadi saa sita, lakini upande wa mashitaka hawana kibali hicho, wamemchukulia maelezo mteja wangu siku ya nne tangu kukamatwa kwake, hivyo ni kinyume na taratibu za kisheria kama nilivyosema hapo awali. Sababu ya pili kwa nini maelezo hayo yasipokelewe kama kielelezo, yamekosa sifa za kisheria kwani kwa mujibu wa sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai nchini CPA ya mwaka 1985, katika kifungu cha 10, kifungu kidogo cha 3, Kinatamka kwamba. Maelezo ya mtuhumiwa yanayochukuliwa na Polisi yanapaswa yawe na saini tatu, Pawepo na saini ya ndugu, au rafiki, au wakili akiwa ni shahidi wakati wakuchukuliwa maelezo mtuhumiwa. Pia iwepo saini ya mtoa maelezo, na iwepo saini ya mchukua maelezo. Lakini maelezo hayo yamekosa saini ya mtu wa tatu, ambae angeweza kuja mahakamani na kuithibitishia mahakama yako kwamba maelezo hayo yalichukuliwa kwa hiyari, hivyo naomba yasipokelewe kama kielelezo kwa kukiuka taratibu. Tatu mteja wangu alipokuja fresh case nilikuomba uweke katika kumbukumbu mheshimiwa kuwa amepigwa na kuumizwa. Naweza kusema hata hayo maelezo yanaweza kuwa yameandikwa huko na shahidi anapopajua mwenyewe kisha akamsainisha mteja wangu. Kwani kama waliweza kutoifikisha kwako PF3 ambayo dakitari aliijaza na kwako Mheshimiwa ukadanganywa kwa kupewa PF3 ambayo haijajazwa, imeonesha ndani yake kuna dharau na uongo mkubwa katika kuidanganya mahakama yako. Kitu ambacho kimekwenda kinyume na sheria namba 102 ya kanuni ya adhabu sura ya kumi na sita, inayotamka wazi kwamba. Shahidi akitoa maelezo ya uongo mbele ya Mahakama na huku anaelewa ni uongo (Forgery) basi anastahili kushitakiwa katika Mahakama aliyotolea ushahidi, wakati anapoutolea huo ushahidi. Hivyo naomba mahakama yako iliangalie hilo muheshimiwa ili iwe fundisho kwa mashahidi wengine wanaotoa ushahidi wa uongo”. Maneno hayo ya mwisho yalileta matatizo kwa upande wa mahakama na Polisi, kwani Hakimu alimtaka Polisi aliekuwa akitoa ushahidi ambae ndiyo alieonesha PF3 iliyokuwa haijajazwa na daktari, kujibu hoja kwamba aliidanganya mahakama? Shahidi alijibu kizembe mbele ya Hakimu.”Mheshimiwa PF3 ya mshtakiwa ilikuwa haijajazwa, ile niliyoionesha ndiyo ilivyotoka kwa dakitari.” Hakimu alimtazama shahidi kwa makini kisha akamwambia, ukimaliza kutoa ushahidi wako, utabaki hapa ili mahakama ikathibitishe kama daktari hakuijaza hiyo PF3, sasa ole wako iwe imejazwa kisha wewe unaiongepea mahakama, sheria itafata mkondo wake. Ehee shahidi muulize maswali shahidi kama unayo, maelezo haya sijayapokea hayakufata sheria.” Hakimu aliposema maneno yale yakumuweka shahidi chini ya uangalizi wa mahakama, yalimvuruga shahidi akawa hayupo makini akili yake yote ikawa ikibainika kwamba PF3 ilijazwa na yeye hakuiwasilisha mahakamani badala yake aliiwasilisha isiyokuwa ile, hakika kitendo kile kiliharibu kesi kwani shahidi alitoka katika kujiamini na kuwa akibabaika kujibu maswali ya shahidi na kutoa mwanya wa upande wa utetezi kuranda walivyotaka.
“Shahidi ukiwa ni askari ambae unafata taratibu za kisheria, huoni kuwa wewe hukustahiki kuwa mpelelezi wa shauri hili?” Wakili Neema Faraja alimtupia swali la kumuudhi shahidi ili achukie na kutoka nje ya kujipanga kwake. “Nastahili kuwamo ndiyo maana nimeaminiwa na nimepewa jukumu hilo.” Shahidi alipojibu hivyo bila kutambua kuwa Wakili alikuwa akimtega, akatupiwa swali lingine la fadhaa. “Shahidi umeifahamisha mahakama kuwa wewe ndiyo mpelelezi wa kesi hii,na kwamba mteja wangu umemfahamu pale ulipomchukulia maelezo si ndiyo?” Shahidi wa upande wa mashtaka akajibu kwa kifupi. “Ndiyo” wakili Neema akamtupia swali lingine. “Shahidi unatambua kwamba ukiwa ni mpelelezi wa shauri, hutakiwi kuwa ndiyo mchukua maelezo ya kukili kosa ya mshtakiwa?!” Shahidi alipotupiwa swali lile akakaa kimya pale kizimbani. “Jibu swali shahidi uliloulizwa” Hakimu alimwambia shahidi ajibu swali lile. “Naomba arejee swali mheshimiwa.” Hatimae shahidi akapata kauli. “Rudia swali lako hajasikia vizuri.” Hakimu alimwambia wakili Neema Faraja, arudie swali lake na wakili akauliza tena huku akiliendeleza swali lile. “Unatambua kwa mujibu wa sheria, mpelelezi wa kesi hatakiwi kuwa ndiyo mchukua maelezo ya ungamo?” shahidi alikaa kimya kisha akajibuhttp://deusdeditmahunda.blogspot.com/ kwa mkato.”Sikumbuki” Wakili Neema Faraja alimgeukia hakimu akamtazama kisha akamwambia. ”Mheshimiwa Kukili kwa Polisi mpelelezi kumchukulia maelezo ya ungamo mshitakiwa haikubaliki kisheria. Kwani katika kesi ya Isirael s/o Kamukolse na wenzake, dhidi ya jamhuri (V.R) 1956 E.A.C.A 52,ipo katika ukurasa wa 72 kitabu cha (141 LAW IN AFRICA) EVIDENCE IN EAST AFRICA, katika kesi tajwa ilielezwa kuwa kisheria haishauriki, na wala haikubaliki kwa anaepeleleza kosa kuchukua maelezo ya ungamo. Kwa kuwa shahidi amesema yeye ndiyo mpelelezi wa shauri hili, lakini pia amemchukulia maelezo ya ungamo mteja wangu, basi kwa mujibu wa sheria inamkataa, naomba aenguliwe kabisa kuwa shahidi katika shauri hili amepoteza sifa.” Baada ya kusema maelezo hayo marefu ya kisheria, wakili Neema Faraja aliketi chini akaiachia mahakama ifanye maamuzi dhidi ya shahidi yule. Hakimu aliandika maelezo yale, ikabidi aahirishe kesi ile kwa muda, ili ende chemba cort akapekue kitabu tajwa ili ajiridhishe na kutoa maamuzi. Watu walisimama hakimu akatoka katika chumba cha mahakama, akatumia kama nusu saa hivi aliporudi mahakamani baada yakuipitia sheria aliyoisema wakili Neema faraja, alitoa maamuzi ya jambo lile, shahidi akaambiwa hakustahili kwa mujibu wa sheria kuwa shahidi wa mambo mawili, aidha ingekubalika kama angepanda pale kama shahidi mpelelezi, angeeleza upelelezi wake aliyogundua dhidi ya Mshtakiwa. Au angepanda mahakamani kama shahidi mchukua maelezo tu. Baada yakuenguliwa kwa mujibu wa sheria, hakimu akawaambia wamlete shahidi mwingine. Upande wa mashitaka uliita shahidi wake wa tatu, lakini hakutokea mahakamani. “Mheshimiwa shahidi wangu wa tatu, alikuwapo nikamuandaa asubuhi ila nasikitika muda huu kila ninavyomwita haitiki, hivyo naomba tarehe ili niwalete mashahidi wawili waliosalia.” Hakimu aliandika katika jalada lake kisha akasema. “Mashahidi hawa wote wanapatikana mji huu, hivyo nawapa siku tatu mje na mashahidi wenu wote ili tumalize shauri hili. Ninaiahirisha kesi hii hadi siku tatu zijazo. Mshtakiwa dhamana yako inaendelea.” Hakim aliahirisha shitaka lile, Polisi aliezuiwa na Mahakama akawa moyo wake unamuenda mbio sana hakuwa na furaha kabisa, alikuwa amenyong’onyea akaishiwa pozi.
***
Katika gereza la wanawake la Segerea, Shuwea Namjupa aliitwa utawala na Odeli kwenda kusikiliza wito. Alipofika pale kama kawaida ya Mfungwa na Askari magereza, Shuwea alichuchumaa chini huku akiwa na shauku yakutaka kujua wito ule ulihusiana na nini. “Mfungwa hapa zimeletwa tarehe kutoka katika ofisi ya msajili. Hivyo unatakiwa kufika mahakani pale Mahakama ya Rufaa Sokoine drive, utakwenda kwa siku tatu mfululizo, bila shaka kusikilizwa kwa Rufaa yako” Askari Magereza anaeshughulika na masuala ya utawala, alimwambia Shuwea taarifa ile, kisha akamtajia tarehe zenyewe za kwenda Mahakamani. Hakika ilikuwa ni faraja kubwa sana kwa Shuwea kupata tarehe yakwenda kusikilizwa Rufaa yake. Tangu awe Mfungwa ikiwa imetimia miaka miwili kasoro siku kadhaa, hakuwahi kupata tarehe ya kuitwa kwenda kusikiliza rufaa yake, sasa ametokea wakili Neema Faraja, anaona mara moja amepata tarehe yakuitwa mahakama ya rufaa, ama kweli ikiwa mtu huna kitu, ni kama kinyama cha mwitu. Shuwea alirudi kwa wenzake akiwa na furaha tele moyoni mwake. Aliwakuta wenzake wakisukana nywele huku wakiwa na kiredio kidogo wakisikiliza kipindi cha muziki wa mwambao. Shuwea furaha yake alikatika viuno vya kufa mtu huku akifurahia kupata tarehe ya kusikilizwa Rufaa yake. Wenzake walimshangaa na kutaka kujua aliitiwa nini kule utawala, lakini yeye hakujibu alikuwa akiimba na kucheza tu. Wale wenzake waliizima redio iliyokuwa ikiimba, ili waelezwe kilichomfurahisha mwenzao, lakini Shuwea akaendelea kucheza yeye mwenyewe huku akijiimbia. “Wewe jela ishakuchanganya naona, manaake huna tofauti na mwehu kabisa. Tunakuuliza umefurahi nini wewe unademka tu hebu tuondolee uchizi wako hapa sie tushavurugwa usituzingue.” Mfungwa mmoja rafiki wa Shuwea alimwambia rafiki yake kwa utani huku wakicheka. “Ndugu zangu sina muda mrefu mungu akinijaalia narudi duniani. Nimepata tarehe yakuitwa na msajili Mahakama ya Rufaa, ili kusikilizwa rufaa yangu. Hivyo ninaanza kufurahi kabisa hapa.” Shuwea alivyosema vile shoga yake aliemuuliza swali lile akaangua kicheko kikubwa sana, hadi machozi yakamtoka. Shuwea alimshangaa rafiki yake anakicheka kitu gani namna ile? ”Sasa wewe mwizi unacheka nini hadi kinakutoa machozi namna hiyo?” Shuwea alimuuliza shoga yake kwa mshangao. Yule shoga yake aliekuwa akicheka alifuta machozi huku akiendelea kucheka akamjibu shoga yake. “Sikia mwizi, siyo kila aliekata rufaa ametoka litambue hilo. Wengi tunao na wengine wapo katika magereza mbalimbali duniani walikata rufaa kisha rufaa zao zikadunda. Hivyo usifurahie sasa kwani ukidunda rufaa yako utaumia sana, ingawa tunapaswa kuishi kwa matumaini kama tutatoka muda wowote humu gerezani. Subiri Jaji akwambie huna hatia upo huru, hapo hata ukitaka kugaragara fanya hivyo.” Maneno yale yaliingia katika moyo wa Shuwea kama mkuki wenye ncha kali, kwani alikuwa mnyonge ghafla hasa akizingatia kuwa ni kweli wapo watu waliokata rufaa kisha rufaa zao, hazikubadilisha matokeo yoyote, au waliongezewa vifungo. Shuwea alishuka matawi hadi akawa katika shina hatimae akakaa kitako akatoa titi lake nakumpa mwanawe anyonye, furaha yake ikatoweka akamuachia Mungu.
***
Mbuya Fabiola alikuwa Bwenini ameketi, mara akaja mwanafunzi mwenzake akamwita na kumpa maelekezo. “Mbuya unaitwa kwa ‘Head Master’, sijui umefanya nini wangu?” Mbuya Fabiola aliinuka akaenda ofisini kwa Mkuu wa shule kusikiliza wito. Alipofika alimuamkia kiongozi yule akasubiri maelekezo. “Mbuya imeletwa Samansi hapa kutoka katika mahakama ya Temeke kesho saa mbili asubuhi unahitajika katika mahakama hiyo kwani unatakiwa kwenda kutoa ushahidi. Hivyo nimekupa ruhusa leo hii wende nyumbani, ili kesho ufike mahakamani, na baada ya kesi hiyo kesho itakubidi urejee shule, uje kuniona sawa? Mkuu wa shule alimwambia Mbuya kisha akamaliza kwa swali na mbuya akaitikia kwa kichwa ile ndiyo yake. Mbuya aliondoka akarudi bwenini akakusanya baadhi ya vitu vyake muhimu akarejea nyumbani kwao. Alipofika kwao alimkuta baba yake akiwa ameketi hana amani. Mbuya alimuamkia baba yake, kisha akamwambia kuhusu kutakiwa kwake mahakamani. Baba yake alimweleza mwenendo wa kesi ulivyokwenda, na kwamba askari alieficha PF3 amepelekwa gerezani kwa muda wa wiki mbili kwa kosa la kuidanganya Mahakama. Hivyo Shahidi muhimu katika kesi iliyokuwa wakiitolea ushahidi ni mpangaji mwenzake yule kijana. Ila amesema leo asubuhi hii kuwa amefiwa hivyo amekwenda kwao kwenye msiba, hatoweza kwenda kutoa ushahidi Mahakamani. kwa hiyo amebakia mwanae kuwa ndiyo shahidi muhimu sana katika kesi ile hivyo akamtaka asimuangushe. Mbuya akamthibitishia baba yake, shaka aondoe kwani yeye atakomaa sana katika jambo lile na Msafiri lazima afungwe maisha. Kapteni Fabiola alimkumbatia mwanawe, kwa furaha akamuahidi kuwa kesho atakwenda nae mahakamani kumsindikiza.
***
Hauchi hauchi unakucha. Hatimae siku tatu zikafika Mahakama ikakaa ili kuendelea na kesi ile. Siku ile ya Ijumaa ilijaza watu wengi sana hadi wakawa wanakanyagana. Mzee Mbuya Fabiola alikuwa amekaa mbele katika mbao au Benchi la wasikilizaji, Mbuya Fabiola alikuwa katika chumba cha mwendesha Mashtaka akiandaliwa kwa ajili yakutoa ushahidi madhubuti. Kwani kesi ile ilionekana ushahidi wote umetupiliwa mbali na Mahakama hivyo walijipanga kisawasawa. Kesi ya tatu ikaitwa kesi inayomkabili Msafiri dhidi ya Jamhuri. Msafiri akapanda kizimbani, wakili wa Serikali alisimama nakujitambulisha kama ilivyo ada. “Muheshimiwa naitwa Christopher Shola, shauri hili limekuja kwa ajili ya kuzungumzwa, kwa leo nina shahidi mmoja muhimu mtendewa wa tukio, hivyo pia naomba kuifahamisha mahakama yako kuwa tutafunga ushahidi kwa shahidi huyo hatutaleta shahidi mwengine.” Baada yakusema maneno yale, wakili wa Serikali aliketi mahala pake, akasimama wakili wa utetezi kujitambulisha. “Naitwa wakili Neema Faraja namuwakilisha mshtakiwa, tupo tayari kuongea kesi mheshimiwa.” Wakili Neema nae baada yakusema hayo akaketi kitako mahala pake. Hakimu aliandika katika jalada lake, kisha akaamuru aitwe shahidi mbele ya mahakama. Mbuya Fabiola aliingia Mahakani akiwa amenuna, akaapishwa na karani kama ilivyo ada kisha akawa tayari kwa ajili ya kutoa ushahidi, ili kuthibitisha shitaka kwa mshitakiwa mbele ya Mahakama. Mahakama yote ilikuwa kimya kabisa, wakisikiliza ushahidi utakaotolewa. Mbuya Fabiola alimtazama Msafiri Namjupa, na Msafiri nae akawa akimtazama Mbuya Fabiola, wakawa wanatazamana.
“Shahidi unamfahamu Mshitakiwa aliepo mbele yako?” Hakimu alimsaili Mbuya Fabiola huku akimtazama moja kwa moja usoni mwake. “Naam namfahamu” Mbuya Fabiola alimjibu hakimu huku akitazama chini macho yake. “Unamfahamu kivipi?” Hakimu alimtupia swali lingine Mbuya Fabiola. “Namfahamu ni mdhamini wangu, amenidhamini katika Mahakama ya mwanzo Mbagala, na nikafika hadi nyumbani kwake na kukaa kwa siku nne.” Mbuya Fabiola alijibu swali lile, huku Msafiri akimtumbulia macho kwa fadhaa. Hakimu alimtazama mwendesha Mashtaka wa Serikali Wakili Christopher Shola, ili aendelee kumuongoza shahidi yake. Msafiri aliamriwa kuketi, wakili wa Serikali akasimama akaanza kumuongoza shahidi yake. “Shahidi umeifahamisha Mahakama kuwa unamfahamu mshitakiwa, na kwamba ulikuwa nyumbani kwake kwa siku nne, je ulikuwa mkilala vyumba tofauti au chumba kimoja?” http://deusdeditmahunda.blogspot.com/Mbuya Fabiola akajibu. “Tulikuwa tukilala chumba na kitanda kimoja.” Mbuya Fabiola alijibu huku akimtazama muendesha mashtaka. “Hebu ifahamishe Mahakama, ndani ya siku nne mlizokuwa mmelala pamoja je mlikuwa mkilalaje?” Wakili wa Serikali aliendelea kumuongoza shahidi wake. Msafiri alimtazama Mbuya huku akihema juu kwa juu kwa kihoro kwani hakutarajia kabisa ushahidi wa aina ile. “Tulikuwa tukilala kama mke na mume.” Mbuya alijibu swali lile huku akitazama chini. Wakili wa Serikali akamgeukia Hakimu akamwambia. “Mheshimiwa ni hayo tu, shahidi angu ameifahamisha mahakama yako kuwa alikuwa akiishi kama mke na mume. Hivyo naiomba Mahakama yako itambue tu kuwa Mke na Mume huwa wanafanya nini. Na kwakuwa shahidi wangu ni mwanafunzi hakuna ubishi kuwa mshitakiwa amemrubuni hadi kwenda nae nyumbani kwake na kumfanya kuwa mke wake wa muda, Ni hayo tu mheshimiwa.” Wakili wa Serikali alimaliza kumuongoza shahidi wake akaketi kitako. Hakimu aliandika katika jalada lake, kisha akainua uso wake kumtazama wakili wa utetezi, akamuona ameshasimama akiwa tayari kwa kumhoji shahidi. Hakimu alimpa ishara wakili wa utetezi, ili aendelee na wakili Neema alimkabili shahidi. “Shahidi unafahamu kesi uliyokuja kuitolea ushahidi katika mahakama hii?” Mbuya Fabiola akajibu. “Ndiyo naifahamu.” Wakili huku akiwa hamtazami akamtupia swali lingine la haraka. “Kesi gani?” Mbuya akajibu “Kubakwa na kurubuniwa.” Wakili Neema akamuuliza Mbuya huku akiwa anatembea katika Mahakama ile huku na kule. “Shahidi unao uthibitisho wowote kama wewe umebakwa na mteja wangu?” Mbuya Fabiola akakaa kimya. Msafiri alishusha pumzi ndefu pale alipokuwa. “Jibu swali shahidi.” Hakimu alimwambia Mbuya Fabiola aliekuwa amekaa kimya. “Sijaelewa swali!” Hatimae akafunguka kumwambia hakimu, na hakimu akamtaka wakili Neema kumuuliza tena. “Labda nikuulize namna hii, unao uthibitisho wowote unaoonesha wewe umebakwa na mteja wangu au huna?” Wakili Neema Faraja alimuuliza Mbuya Fabiola huku akiwa bado anatembea huku na kule katika mahakama ile. Mbuya akajibu kinyonge, “Sina uthibitisho” Wakili Neema Faraja alimsogelea Mbuya pale alipo kisha akamtupia swali lingine. “Ikiwa huna uthibitisho kama umebakwa na mteja wangu, mahakama itathibitishaje kama umebakwa?” Mbuya hakuwa najibu akapiga kimya. Wakili Neema akamtupia swali lingine. “Shahidi wewe una miaka mingapi?” Mbuya Fabiola akajibu kwa haraka; “Miaka kumi na nane.” Jibu lile lilimfanya wakili Neema Faraja kutabasamu, kisha akamtupia swali lingine. “Shahidi hebu ieleze Mahakama mteja wangu amekurubuni vipi ikiwa wewe siyo mtoto mdogo na nimsomi?” Mbuya Fabiola kwa mara nyingine tena akakaa kimya. “Unaulizwa umerubuniwa vp, jibu swali.” Hakimu alimuuliza Mbuya Fabiola huku akiwa amesimamisha kuandika akimtazama. Mbuya hakuwa na jibu la swali lile. Ama kweli panapo ukweli uongo hujitenga. Wakili Neema Faraja akamgeukia mheshimiwa Hakimu akamwambia. “Mheshimiwa mteja wangu anakabiliwa na mashtaka mawili katika Mahakama yako, kumrubuni mwanafunzi na kosa la pili kumbaka. Lakini hadi upande wa mashitaka leo walipofunga ushahidi wao, wameshindwa kuthibisha mashitaka hayo pasi na shaka. Upande wa mashtaka ulipaswa uwe na PF3, iliyojazwa na daktari kuthibitisha kuwa kweli Mbuya Fabiola alibabwa, lakini hawakuweza kuleta kielelezo hicho mbele ya mahakama yako. Hata ‘Victim’ Mbuya Fabiola ambae ni PW 3, katika shitaka hili pia ameithibitishia Mahakama yako tukufu kuwa hana uthibitisho wowote kuwa amebakwa. Lakini pia ameshindwa kuithibitishia Mahakama kuwa amerubuniwa. Hivyo naiomba mahakama yako itende haki kwa Mteja wangu, kwani hakuna ushahidi wowote uliotolewa mbele ya Mahakama yako uliothibitisha mashtaka yanayomkabili mteja wangu.” Wakili Neema Faraja baada yakusema maneno yale aliketi katika kiti chake, akiiachia Mahakama ifanye maamuzi.
Hakimu aliandika katika jalada lake kwa muda, kisha akainua kichwa chake akasema. Kesi hii naiahirisha hadi siku ya Jumatatu, ili kuja kwa maamuzi madogo(Ruling) Mshtakiwa Dhamana yako inaendelea. Baada yakusema vile hakimu alimuamuru karani kuita kesi nyingine. Msafiri aliondoka pale alipokuwa kizimbani, akamfata wakili wake. Mbuya Fabiola alimfata baba yake wakaondoka pamoja. Uma wa watu waliokwenda kusikiliza kesi ile, ulitawanyika kama vile Mahakama ilimaliza muda wake.
Siku ya Jumatatu, watu walikuwa wengi mara dufu, Kapteni Fabiola alikaa katika kikazi chake, lakini mwanawe hakuwapo Mahakamani. Msafiri alikuwa amekaa akiwa na mawazo tele kwani yeye hakuwa akijua sheria, lakini hali ilikuwa ni tofauti sana kwa wakili Neema Faraja ambae alikuwa akitabasamu muda wote.
Nje katika maegesho ya magari, ilikuja gari moja aina ya Toyota Noar, yenye rangi nyeusi iliyokuwa na vioo vya kiza, dereva wake akaiegesha sanjari na ilipokuwa gari ya wakili Neema Faraja. Watu wanne waliokuwa ndani ya gari ile hawakushuka, bali waliendelea kubakia ndani ya gari ile kiyoyozi tukihusika kuwapa hewa safi ya baridi mle ndani, gari ile ikiwa ipo katika muungurumo haikuzimwa.
Kesi ya Msafiri ilipoitwa, Msafiri alipanda kizimbani kama kawaida, mawakili walijitambulisha wote wawili wa upande wa mashtaka na wa utetezi, kisha wakili wa mashtaka akasimama baada ya Yule wa utetezi kuketi chini akasema. “Mheshimiwa shauri hili limekuja kwa Ruling, tupo tayari kwa kuendelea na hatua hiyo.” Hakimu aliandika katika jalada lake, kisha akaanza kusoma yale maamuzi aliyokuwa ameshayaandaa.
“Mshtakiwa Msafiri Namjupa, umeshtakiwa kwa makosa mawili, kosa la kwanza kumrubuni mwanafunzi, na kosa la pili kumbaka mwanafunzi huyo aitwae, Mbuya Fabiola. Upande wa mashitaka ulileta mashahidi watatu ili kuthibitisha mashitaka hayo, na kielelezo kimoja ‘Question Statement’ ya mshtakiwa. Upande wa utetezi walipinga maelezo hayo kwa mujibu wa sheria, na mahakama yangu ikakubaliana na hoja za upande wa utetezi. Lakini pia katika mashahidi hao wote watatu, akiwamo mtendewa wa tukio, wameshindwa kuithibitishia mahakama yangu kuwa Mbuya Fabiola alibakwa na Msafiri Namjupa, au Kurubuniwa nae. Mtendewa wa tukio ambae ndiyo chanzo cha kesi hii, na ndiyo anaeelezwa kufanyiwa vitendo hivyo, nilitarajia angekuwa na uthibitisho kutoka kwa dakitari kuthibitisha kweli amefanyiwa tukio hilo. Pia PW 3, Mbuya Fabiola ameshindwa kuishawishi Mahakama yangu imuone kweli amerubuniwa na Msafiri Namjupa. Hivyo kesi hii ushahidi wake uliotolewa unamashaka mengi sana kwa mujibu wa sheria, lakini pia unagubikwa na utata na kuacha maswali mengi sana. Vipi mtu alierubuniwa ashindwe kueleza namna alivyorubuniwa, vipi mtu aliebakwa asipelekwe hospitali kupimwa, na daktari akathibitisha kuwa kweli amebakwa, lakini pia kumpima afya yake. Hivyo kwa mujibu wa kifungu cha 114 cha sheria ya Ushahidi (TEA 1967) sheria hiyo imetamka wazi kwamba; Ni kazi ya upande wa mashitaka kuthibitisha ushahidi unaotolewa unakuwa hauna mashaka yoyote mbele ya Mahakama, ushahidi wa mashaka unamwacha huru mshitakiwa. Lakini pia katika sheria hiyohiyo ya ushahidi katika kifungu namba 113, kimeweka bayana kuwa; ushahidi utakaokuwa na nguvu kisheria utakaotolewa na upande wa mashtaka ni lazima uwe timilifu, usio na shaka ili kumtia hatiani mshitakiwa. Kwa kuwa ushahidi uliotolewa katika kesi hii, umeshindwa kuthibitisha mashtaka yanayomkabili mshitakiwa pasi na chembe ya shaka, Mahakama yangu kwa kutumia kifungu namba 230, cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (CPA) ya mwaka 1985, imemuona mshtakiwa Msafiri Namjupa hana kesi ya kujibu katika kesi inayomkabili, hivyo inamuachia huru kabisa.” Hakimu alimaliza kuipitia hukumu ile ndogo (Ruling) na kumuachia huru mshtakiwa Msafiri Namjupa. Ama kwa hakika Msafiri Namjupa alilia kwa furaha, akamshukuru Mungu kumvua na balaa lile la kifungo cha maisha jela. Akamshukuru sana wakili wake Neema Faraja kwa kumfanya awe huru. Machozi ya furaha yalimtoka bila yakujitambua. Ama kweli aliekuwamo hatoki, na asiekuwamo haingii. Au naweza kusema lililokuwa la kumkosa, halikuwa lakumpata.
Hali ilikuwa ni tofauti kwa Kapteni Fabiola kwani ilikuwa kama mtu aliegongelewa misumari, alishindwa kuinuka pale chini alipokuwa amebarizi. Alibaki amebung’aa macho yake yakimtazama Msafiri kwa hasira sana. Msafiri nae alimtazama Yule mzee Kapteni Fabiola akiwa amejaa hasira kali. Watu kama kawaida waliondoka mahakamani pale, huku wengine wakimpongeza Msafiri kwa kumpa mkono na hongera ya mdomo. Marafiki zake Msafiri tangu kesi ile ilipoanza hadi kufikia siku ile, walikuwa hawajatokea kabisa mahakamani kila mtu alikuwa akiendelea na hamsini zake.
Wakili Neema aliitwa na Mama mmoja aliekuwa amevalia ushungi, nje ya Mahaama ile akasogea nae pembeni wakawa wakizungumza. Msafiri alikuwa akiendelea kupeana mikono na watu waliokuwa wakimpa pongezi kwa kuachiwa huru.
Kapteni Fabiola alijizoazoa pale chini, moyo wake ukimuuma sana, hasira na chuki dhidi ya Msafiri zikimtawala sana, Alipofanikiwa kuondoka alielekea ule upande aliokuwapo Msafiri Namjupa. Kapteni Fabiola alipangua watu akawa akipiga hatua kumsogelea Msafiri Namjupa. Msafiri alikuwa amesimama pale akimsubiri wakili wake aliekuwa akiongea na mtu, hivyo asingeweza kuondoka peke yake, alikuwa amesimama pale nje kama unaelekea Uwanja wa Taifa.
Wakili Neema Namjupa aliongea na Yule mama karibu nusu saa hivi, kisha akaagana ya Yule mama akawa akielekea katika maegesho ya magari pale nje alipoegesha gari yake, akitarajia kukutana na Msafiri ili waondoke. Akiwa katika kutembea kulielekea gari lake, mara akasikia makelele watu wakipiga huku wakikimbia hovyo kule nje. Wakili Neema aliongeza mwendo ili kujua kulikoni, lakini hakwenda hata hatua kumi kutoka pale, kwani aliwaona watu watatu wakiwa wameshika bastola mikononi mwao, wakiwa wamemdhibiti Msafiri Namjupa barabara wanamuingiza katika gari aina ya Noar yenye rangi nyeusi, iliyokuwa na vioo vya kiza. Wakili Neema aliisoma namba ile gari akatoa Camera yake ndogo ya Digital aina ya Sony, akaipiga picha ile gari na wale watu waliokuwa wakimuingiza kwa nguvu Msafiri ndani ya gari ile. Wakili Neema haraka alirudi mbio ndani ya Mahakama kuita askari Polisi wampe msaada, lakini hata walipotoka na askari wale ile gari ilikuwa imeshatoweka mahala pale. Watu walikuwa wamepagawa hasa, kwani tukio lile liliwafadhaisha sana. Kila mtu alibaki akisema lake.
Kapteni Fabiola aliingia ndani ya gari yake akaiondosha taratibu sehemu ile, akakata upande wa kulia kuelekea temeke ilipokuwa barabara ya Mandela upande ambao ndipo ile Noar nyeusi ilipokata na kuelekea.
Wakili Neema Fabiola aliwapa ile namba ya gari wale maaskari, ili kutoa taarifa kwa njia ya simu ya upepo, ili askari wa usalama barabarani pamoja na askari wa doria waweze kuikamata gari ile. Askari waliichukua ile namba ya gari kutoka kwa wakili Neema Faraja, wakaitazama kisha wakamtazama wakili Neema wakamwambia, tutaifanyia kazi wewe endelea na kazi zako. Askari walikuwa na hasira sana na wakili Neema kwani amesababisha mwenzao, kwenda jela kwa wiki mbili, hivyo walimchukia sana. Hata wakili Neema alipoacha namba zake za simu ili gari ile ikikamatwa wamwambie, askari wale waliichukua namba ile, lakini wakili Neema alipowapa mgongo tu, waliichana karatasi iliyokuwa na namba yake ya simu! Mara simu ya wakili Neema faraja, iliita na yeye akaipokea. Ujumbe aliopewa kwenye simu ile, ulimpeleka mbio huku akiwa ametaharuki sana.
Wakili Neema haraka aliingia ndani ya gari yake, kwa mwendo wa haraka alielekea Mbagala huku moyo wake ukiwa unamdunda sana. Aliingia barabara ya uwanja wa Taifa, akapinda kulia hadi katika makutano ya Barabara ya Mandela na Uwanja wa Taifa, akapinda kushoto kama anaeelekea Bandari, akakanyaga mafuta kwa mgandamizo mkubwa, gari yake ikaongeza mwendo kwa kadiri ilivyokuwa ikiendeshwa. Alipofika katika taa za kuongozea magari umaarufu wa sehemu ile hujulikana kama machinjioni, kutokana na ajali za mara kwa mara zinazotokea eneo lile. Ni makutano ya Barabara ya Kilwa na Mandela, wakili Neema Faraja akakaa upande wa kulia kwake, taa ziliporuhusu magari kukata alipinda upande wa kulia, akaiacha Barabara ya Mandela na kuingia katika Barabara ya Kilwa. Alikanyaga pedeli ya mafuta garihttp://deusdeditmahunda.blogspot.com/ ile ikaongeza mwendo zaidi, akiwa yupo maeneo ya viwanja vya maonesho ya Biashara vya Sabasaba, simu yake ikaanza kuita. Wakili Neema Faraja aliitazama simu ile namba ya mtu aliekuwa akimpigia, mara moja aliitambua namba ile na ndiyo iliyomfanya akimbizane vile muda ule, pale alipompigia akiwa katika Mahakama ya Temeke. Wakili Neema Faraja aliipokea ile simu huku macho yake akiwa ameyakodoa mbele ya gari ile. “Halow nakusikia.” Wakili Neema Faraja aliipokea ile simu kwa wahaka mkubwa, na mtu wa upande wa pili akampa taarifa nyingine iliyomchanganya zaidi. Wakili Neema aliikata ile simu yake akaizima kisha akawa anaimiliki gari yake vyema katika kukimbilia kule aendapo. Alikuwa amefika katika Mzunguko wa Mtoni kwa Azizi Ally, akanyooka kuitafuta Mtoni Mtongani, katika wilaya ile ya Tekeme maarufu wakazi wa maeneo ya Wilaya ile wakipaita kwa mkato TMK. Wakili Neema akapandisha kimlima kidogo cha pale Madafu, akaifikia Mtoni Mtongani, akapunguza mwendo wa gari yake kwani watu wengi walikuwa wakivuka eneo lile. Alipolipita eneo lile lenye vurugu za magari, akateremsha kilima cha Mtoni Mtongani, pale eneo ambapo Juu kuna Barabara ya Treni, na chini kunapita magari. Wakili Neema alikuwa aiikimbiza gari yake huku akitazama saa yake kama anakwenda sawa na muda. Wakili Neema faraja aliongeza mwendo wa gari yake akawa anapandisha kilima cha KTM pale Mbagala. Akiwa katika kupandisha kilima kile akiendesha kwa upande wa kushoto mwa Barabara ile, mara aliiona Toyota Noar nyeusi, ikiwa upande kwa Kulia mwa Barabara ile ikitokea Mbagala ikiwa ipo kasi. Upana wa Barabara ile wakili Neema Faraja hakuweza kuona ndani ya gari ile watu waliokuwamo, kwani mbali ya upana mkubwa wa barabara ile lakini pia ile gari vioo vyake vilikuwa vya kiza, tena havikuwa wazi, bali vilikuwa vimefungwa. Wakili Neema Faraja hakutaka kurudi nyuma bali aliongeza mwendo wa gari yake, akiitafuta Mbagala Sabasaba, akaimaliza na kuishika Mbagala kwa Kipati hatimae akafika Mbagala Kizuiani, akaiacha ile barabara ya Kilwa, akapinda kulia kuelekea barabara inayokwenda katika Mahakama ya Mwanzo Mbagala Kizuiani. Alipoikaribia Mahakama ile akaiona gari ya Kapteni Fabiola imeegeshwa nje mwenyewe hakuwapo ndani ya gari yake. Wakili Neema Faraja aliegesha gari yake akashuka, na kuingia katika jengo la Mahakama. Alipoingia tu ndani ya Mahakama ile, akamuona Kapteni Fabiola akiwa ameketi katika Benchi huku miguu yake akiwa ameikunja katika umbo la namba nne. Wakili Neema Faraja, alikwenda akaketi mbele yake akamkazia uso wakawa wanatazamana. Kapteni Fabiola uso wake uliweka matuta madogo, akaiachanisha miguu yake kutoka katika ile namba nne aliyokuwa amekaa, na kukaa mkao wa kawaida.“Umefata nini huku wewe?” Kapteni Fabiola alimwambia wakili Neema Faraja huku akiwa amechukia vibaya sana. “Nimemfata mteja wangu Msafiri Namjupa. Sikia Kapteni Fabiola acha kabisa kucheza na Sheria, ninayo taarifa kamili kuwa umefanya mipango mteja wangu akamatwe kwa kuonekana kuwa mtu aliemdhamini amemtorosha ili umpeleke jela, kwa kumdhamini Mwanao na kisha kumtorosha mshitakiwa. Unafahamu tarehe ya kesi iliyokuwa itajwe katika Mahakama hii, mteja wangu alikuwa katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke, hivyo Mwanao alipaswa kufika Mahakamani lakini ulimzuia mwanao asifike Mahakani ili umpe matatizo mteja wangu, sasa nakwambia hivi hatokwenda jela huyu kama mimi nikiwa bado nipo hai, ila kama atapandishwa kizimbani kwa shitaka la kumtorosha mshitakiwa na wewe umekuja hapa ukiwa ndiyo mlalamikaji ulietukanwa basi umenoa kabisa kumfunga Msafiri. Wewe umefanikiwa kumuweka jela Iddy Teva, kwa kuwa hana uwezo wa kuweka wakili ndiyo maana hadi leo anasota jela. Lakini kwa Msafiri kamwe hatoburuzwa ikiwa wakili wake nipo. Tambua kwamba namjua mwanao shule anayosoma hivyo kama utampandisha Msafiri kwa kosa hilo, basi na mwanao nitampandisha mahakamani. Msafiri atakuwa kwa mahabusu wanaume, na Mbuya atakuwa kwa Mahabusu wanawake wote wakiwa gerezani upo?!” Wakili Neema Faraja alizungumza kwa kirefu akiwa haonekani kutania hata kidogo. “Wewe ni nani aliekwambia habari hizi?” Kapteni Fabiola alitaharuki sana kwa kuelezwa mambo yale ambayo kwa hakika ndivyo ilivyokuwa dhamiri yake. “Kapteni kumbuka mimi ni Wakili ambae nilikuwa upande wa Serikali, na sasa nimeamua kuwatetea watu badala yakuwakandamiza. Hivyo angalia na chunga sana. Usipokuwa makini unaweza kujikuta na wewe unakuwa gerezani kwa makosa ya kujaribu kumuua Msafiri. Kwani alama zako za vidole zilizobaki katika shingo ya Mteja wangu na kumsababishia maumivu makali, zimeonekana na dakitari lakini pia nimekwenda kwa mkemia Mkuu wa Serikali amezihifadhi zile alama katika compyuta yake. Hapa kama nikisema tu uchukuliwe alama za vidole, ili zikalinganishwe na zile zilizokuwapo kwa mkemia, amini utaozea jela Mzee, hivyo usitake kuyafanya mambo madogo kuwa makubwa, wewe ndiyo uliyemshitaki mwanao hapa, na wewe ndiye unaeweza kuifuta kesi hiyo hapa, vinginevyo tutaoneshana vyeo vyetu, wewe ukiwa Kapteni na mimi nikiwa Wakili. Wakili ambae nilishafanya kazi Serikalini na sasa nipo upande wa utetezi.” Wakili Neema Faraja alikuwa akimuelewesha Kapteni Fabiola vitu ambavyo hakuwa akivijua wala kuvizania kabisa.
Kapteni Fabiola alimtazama kwa makini Neema Faraja aliekuwa hana hata chembe ya woga machoni mwake, na aliekuwa hatanii hata kidogo. Wakili Neema Faraja aliingiza mkono wake katika mfuko wa suti yake ya kiwakili iliyokuwa imemkaa vyema mwilini mwake, kisha akatoka na karatasi iliyokuwa imeandikwa na kusainiwa na kugongwa mhuri akaikunjua na kumuonesha Kapteni Fabiola kisha akamwambia. “Hii ni PF3 ambayo sikuitumia katika kesi niliyotoka kushinda muda mfupi uliopita. Kwa kuwa natambua kielelezo kimoja hakiwezi kutumika mara mbili, katika Mahakama tofauti kwa mujibu wa sheria, hivyo sikuwa mjinga au msahaulifu nilipoacha kukitumia kielelezo hiki pale katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke, bali nilikuwa nimeshajipanga kuja kukitumia kielelezo hiki hapa, hivyo nakushauri futa kesi hii niondoke na Msafiri au tuendelee kushindana kisheria na mwisho wa mashindano yetu amini kwamba wewe na Mbuya nyote mtakwenda jela, na Msafiri atakuwa uraiani habari ndiyo hiyo.” Wakili Neema Faraja hakika alimkamata kisawasawa Kapteni Fabiola. Kwani alikuwa hana maneno yakupinga maelezo yale. Wakiwa katika kutazamana mara Karani wa Mahakama alitoka nje akaanza kuita. “Katika kesi ya jinai namba 63, Mshitakiwa Mbuya Fabiola.” Karani baada ya kuita jina la mshitakiwa na namba ya kesi akaingia katika chumba cha Mahakama ile. Kapteni Fabiola aliinuka, akaingia katika chumba cha Mahaka. Wakili Neema Faraja nae hakutaka kufanya ajizi bali aliinuka akaingia katika chumba cha Mahakama. Wakiwa ndani ya chumba kile kilichokuwa na hakimu, karani na wazee wa baraza watatu, mara aliletwa Msafiri Namjupa na Polisi, akiwa na Pingu mikononi mwake. Akafunguliwa pingu zile pale katika chumba cha Mahakama. Msafiri akashangaa sana kumuona Wakili Neema Faraja, kwani hakutarajia kabisa kumuona tena Wakili wake kwa siku ile, hasa akizingatia mazingira ya alivyokamatwa, kwani ilikuwa ni mithili ya utekaji. Moyo wake ukajaa faraja sana, machozi yakawa yakimlengalenga pale alipotazamana na Wakili wake, akaonesha sura ya Huruma iliyokuwa ikihitaji msaada. Wakili Neema Faraja aliketi kitako katika benchi lililokuwa ndani ya chumba kile. “Mdhamini Mshitakiwa yupo wapi, na kwa nini katika tarehe iliyopangwa hukutaka kuja nae kama nilivyokuagiza, hadi tumetoa waraka wa kukamatwa kwako?” Hakimu wa Mahakama ya mwanzo alimuuliza Msafiri huku akimtazama usoni moja kwa moja.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/ “Mheshimiwa naitwa Wakili Neema Faraja namuwakilisha mshitakiwa.”Wakili Neema Faraja alisimama kisha akajitambulisha mbele ya Mahakama ile. Hakimu aliandika katika jalada lake, alipomaliza kuandika alimuona mlalamikaji Kapteni Fabiola akiwa ameinua mkono juu akiomba nafasi yakuzungumza mbele ya Mahakama ile. Hakimu alimpa nafasi Mlalamikaji ili azungumze. “Mheshimiwa naiomba Mahakama yako iifute kesi hii, kwani nina majukumu mengi sana ya kikazi, lakini pia mwanangu ameniomba Msamaha kwa yaliyotokea hadi kupelekea kumfikisha hapa, na nimeshamsamehe. Hivyo naomba kuliondosha shauri hili Mahakamani.” Kapteni Fabiola aliposema maneno yale, ilikuwa ni ganzi na butwaa kutoka kwa Msafiri, hakutambua kwa nini Kapteni Fabiola ameamua kuliondosha suala lile mahakamani, aliinua uso wake kumtazama Wakili wake, alimuona akiwa makini sana akimtazama Kapteni Fabiola. Hakimu aliandika maneno yale, akawauliza wazee wa baraza. “Mnasemaje wazee mlalamikaji ameomba tuliondoshe shauri hili Mahakamani, je nini rai yenu katika hili?” Wazee wa Baraza walitazamana kwa muda kisha mzee mmoja, alitamka kwamba. “Kama mlalamikaji mwenyewe ameamua kuliondosha shauri hili Mahakani, bila ya kushawishiwa au kutishiwa na mtu mwengine, basi mimi rai yangu naona tuliondoshe shauri hili” Hakimu aliandika katika jalada lake kisha akamuuliza Mzee mwengine. “Mzee Omari Badi wewe unashaurije?” Mzee Omari Badi alijikohoza kidogo kisha akasema. “Mie sina Pingamizi juu ya hilo, kwani hakuna kesi isiyokuwa na mlalamikaji, sasa kama mlalamikaji mwenyewe ameamua aiondoshe kesi hii kwa maana yakuifuta basi hapana budi ila kuifuta, hayo ndiyo mawazo yangu.” Mzee Omari badi alitamka maneno yale huku akimtazama hakimu. “Haya Mzee Hugwe Zawose, nawe unamawazo tofauti na wazee wenzio?” Hakimu alimuuliza Mzee Hugwe Zawose aliekuwa kimya muda wote uso wake ukionekana upo katika tafakuli nzito. “Mmm mimi sina pingamizi, ila kijana ameletwa hapa baada ya Mahakama yako kuandika ‘Arest Warrant’ kwani hakumkabidhi mshitakiwa katika tarehe iliyopangwa, wala yeye hakutokea kueleza kama walikuwa na dharula yoyote, hivyo pamoja kama utaifuta kesi ya msingi, je na hili litatatuliwajwe?” Mzee wa baraza Hugwe Zawose, alimalizia kuzungumza akaendelea kuwa kimya kusikiliza mahakama nini itakachoamua, ila yeye mawazo yake ameshayawasilisha. Hakimu aliandika katika jalada lake kisha akampa nafasi wakili Neema Faraja azungumze. “Wakili unasemaje kwani mlalamikaji ameiomba Mahakama ilifute suala hili katika Mahakama hii je, una pingamizi na hilo?” Wakili Neema Faraja alisimama akaanza kwa kusema. “Mheshimiwa mchonga mwiko, amewania mkono wake usiungue. Hivyo kila muweka wakili anahitaji kutetewa. Furaha ya wakili ni kushinda kesi anayoisimamia, hivyo mie mawazo yangu nitayakita katika sheria zaidi kwa vile ni mwanasheria. Katika sheria ya mwenendo ya makosa ya jinai, ya mwaka 1985 kwenye kifungu cha 224 sheria hiyo inatamka bayana kwamba; Mlalamikaji anao uwezo wa kuondosha shauri Mahakamani ikiwa ni kosa dogo. Na kama ni kosa kubwa basi itabidi apate kibali kutoka kwa DPP, kabla kosa hilo halijafikishwa kwa hakimu. Sote tutakubaliana kuwa matusi ni kosa dogo, ukilinganisha na makosa mengine. Hivyo nampongeza Mlalamikaji kwa kuwa tayari kuliondosha shauri hili, na sheria pia inaruhusu hivyo naomba Mahakama yako iridhie maombi hayo.” Hakimu aliandika yale maneno ya wakili Neema Faraja, kisha akatoa maamuzi. “Kwa kuwa mlalamikaji ameridhia kuliondosha shauri hili Mahakamani, na kwa kuwa wazee wa baraza wote mmekubaliana na hili hamkupingana basi Mahakama yangu haina sababu yakuzuia kuliondosha. Mzee wa baraza Hugwe Zawose nikiiondosha kesi hii kwa kuifuta, basi hata kule kutokuja Mdhamini na Mtuhumiwa napo pia kutakuwa kumefutwa kwani hii ndiyo kesi ya msingi. Hivyo ninatamka kwamba nimeifuta kesi hii.” Baada ya hakimu kusema maneno yale, wakili Neema Faraja alikwenda kumpa mkono Kapteni Fabiola, na kumpongeza kwa kitendo kile cha kiungwana alichokifanya. Pia alimwita Msafiri akamwambia nae ampe mkono. Kapteni Fabiola aliinua mkono wake akamnyooshea Msafiri Namjupa ili washikane mikono kwa kuyamaliza, lakini Msafiri Namjupa aliupita ule mkono akaupotezea na kama hauoni, akamuacha Kapteni Fabiola akiwa amebaki amenyoosha mkono wake bila kupokelewa.
Wakili Neema Faraja akamwambia Msafiri Namjupa, “Mpe mkono tafadhali kwani hujui Mungu alipanga nini hadi haya kutokea. Jifunze kusamehe kwa aliekukosea epuka kufanya visasi kwa watu, hata kama amekukosea jambo kubwa kiasi gani muachie Mungu atakulipia usihukumu wewe.” Msafiri Namjupa alimtazama wakili wake, akamwambia kwa uchungu mkubwa. “Huyu mzee alipanga kuniua huyu, siyo mtu mzuri hata kidogo, hivi ningelikuwa marehemu ningempa mkono saa ngapi, lakini Mungu amejaalia sijafa bado alikusudia kunifunga, wakati ukweli sijamuingilia mwanawe wala sikuwa nimemrubuni, au kumfahamu kabla. Moyo wangu unaniuma sana nafikiri pengine kama siyo juhudi zako wakili wangu, hivi sasa mie ningekuwa naozea jela.” Msafiri alipofika hapo machozi yalikuwa yakimtiririka mashavuni mwake. “Msafiri yaliyopita si ndwele tugange yaliyopo na yajayo, nakuomba mimi mpe mkono tafadhali.” Wakili Neema Faraja bado alikuwa akiitafuta suluhu kwa mtu mwenye uchungu mkubwa sana. “Sikia wakili, kama hataki basi hakuna neno kwani mkono wake mie hautanipunguzia wala kunizidishia kitu.” Kapteni Fabiola alisema maneno yale kisha akageuka pale alipokuwa akashika njia kuelekea garini kwake. “Msafiri hukufanya kitendo cha busara hata kidogo, kumbuka haya ni maisha, na siku zote maisha ni mzunguko, basi amini asiefaa leo aweza kufaa kesho.” Wakili Neema Faraja alimwambia Msafiri, kisha akamwambia. “Sawa nashukuru umekuwa huru, kwani hiyo ndiyo kazi ambayo nilipewa kuifanya na Mungu amejaalia nimeitimiza. Mie kwako nilipewa kazi moja yakuhakikisha unatoka ukiwa pale mahakamani Temeke, ila huku nimeongezewa tenda nyingine na Bosi wangu alienipa kazi hii.” Msafiri alimtazama Wakili Neema Faraja, kisha akasema. “Samahani sana kwa yaliyotokea, ila siku yoyote nikikutana nae tena nitahakikisha nampa mkono kwa kumsalimia. Sasa naomba sana unieleze huyo Bosi wako aliekupa kazi hii ni nani, kwani nakumbuka mara ya mwisho ulisema hutonambia hadi niwe huru, nashukuru leo hii nipo huru, hivyo naomba unambie tafadhali.” Wakili Neema alipiga hatua hadi kwenye gari yake alipoegesha, akaiegemea na kumwambia Msafiri Namjupa. “Utamjua tu ila bado sijamaliza kazi yangu, Mungu akijaalia kutoka Dada yako, basi nitawaambia pamoja kwani hata dada yako nae anashauku ya kufahamu jambo hilo. Sasa Mie nakuacha, nakwenda kujipanga na mambo mengine, ila chukua kadi yangu ya biashara hii, humo kuna namba zangu za simu na ofisi yangu ilipo. Kwa tatizo lolote la kisheria unaweza kunitafuta kwa namba hizo.” Baada yakusema maneno yale, huku akimkabidhi kadi iliyokuwa na namba zake za mawasiliano, akataka namba za simu za msafiri, lakini Msafiri hakuwa na simu! Basi Wakili Neema akamwambia tarehe ambazo Shuwea atakwenda Mahakama Kuu, ili kusikiliza rufaa yake. Kisha wakaagana Wakili Neema akaingia ndani ya gari yake, akaiwasha simu yake na kuwasha gari akaondoka kuelekea mjini. Msafiri alisimama pale alipo akiishuhudia gari ile inavyoondoka hadi kuingia katika barabara ya lami na kupotea katika mboni za macho yake, nae akageuza akaelekea kwake jirani na pale Mahakamani.
***
Siku ya Jumapili, Msafiri alikwenda katika gereza la wanawake la Segerea kumtembelea dada yake, kwani tangu yalipompata matatizo, hakuwahi kwenda kutokana na hali yake. Aliandikisha jina la dada yake aliekwenda kumtembelea, akamnunulia sabuni, mswaki na dawa ya meno, pamoja na Biskuti za mpwa wake. Akaingia navyo pale ndani katika sehemu ile maalumu ya kuonana na mahabusu na wafungwa waliokuwa ndani ya gereza lile. Msafiri alikwenda mapema, hivyo watu hawakuwa wengi aliweza kuongea kwa nafasi bila bugudha ya kelele au kukatishwa mazungumzo yao. “Vipi mbona umekuja peke yako mjomba yupo wapi?” Msafiri alimuuliza dada yake aliekuja bila ya mwanawe. “Mpwa wako amelala nimekataa kumsumbua kwani usingizi wa jela ni mashaka matupu.” Msafiri baada yakujibiwa vile, alimueleza dada yake mkasa uliomsibu, akamwambia ubaya aliofanyiwa na Mbuya Fabiola, na ushahidi aliokwenda kuutoa mahakamani, dada yake alihuzunika sana, akafikiria wema aliomtendea akiwa nae gerezani, jinsi alivyokuwa akihakikisha anaoga, anakula vizuri na kumfanya asiwe na tabu ya ugeni wa jela. Akafikiri wema aliotendewa na kaka yake wa kumdhamini, amemlipa maovu. Ama kweli tenda wema wende zako usingoje shukurani. Shuwea akamuona Mbuya ni Mtu mbaya sana kama baba yake, akamchukia sana katika nafsi yake. Mwisho wa yote Shuwea akamwambia kaka yake. “Jumatano mie ndiyo nakwenda kuomba Mungu, nimepata tarehe ya Mahakama Kuu, hivyo niombee dua kaka yangu, asaa kheri Mungu ataniondosha katika matatizo haya, kwani yeye pekee ndiyo aujuae moyo wangu ulivyokuwa haujahusika kwa kesi hii, niliyofungwa kwayo.” Msafiri alimpa moyo dada yake akamwambia. “Muachie Mungu dada yangu, mie nilipokuwa uvunguni mwa kitanda nyumbani kwa Mjumbe jamaa wakitaka kunichoma moto, nilimuomba Mungu sana nashukuru Mungu amenisikia na nimeshinda kesi tena kesi iliyoendeshwa kwa haraka. Hivyo nawe omba Mungu utatoka, kwani wakili Neema ni Mahiri sana kwa sheria, kama yeye amekata rufaa maana yake ameona kuna sehemu ambazo zinaweza kukutoa ukaachiwa huru.” Mtu na dada yake walizungumza kwa kina hadi wakaishiwa maneno, askari akawaambia wamalize kwani wameshazungumza kwa muda mrefu. Msafiri alikwenda sehemu ya kukabidhiana vitu, akampa askari vile vitu alivyokwenda navyo vikakaguliwa kisha akapewa Shuwea, wakaagana na kaka yake, wakikubaliana siku ya jumatano wakutane Mahakama Kuu. Msafiri akatoka pale huku akiwa na fikira nyingi kuwa yeye alisota sana katika kufatilia rufaa ya dada yake, lakini hakuwahi kufanikiwa, maana yake kwamba kama siyo wakili Neema Faraja, basi dada yake angesubiri sana. Msafiri alishukuru sana alivyopatikana wakili akawa na matumaini ya kutoka kwa dada yake, kwani atakuwa na hoja nzito za kisheria, tofauti na sababu walizozitoa wao kuwa dada yake hakuiba tu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
***
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment