Simulizi : Mpita Njia
Sehemu Ya Tatu (3)
Upepo wa pwani, ulikuwa ukivuma kutoka kusini kwenda kaskazini, watu wa utabiri wa hali ya hewa waliuita upepo ule pepo za Kusi. Mji wa Dar es salaam ulikuwa na pilika zake lakini haukuwa na jua katika siku hiyo ya Jumatano. Hivyo joto lilipungua sana. Katika chumba cha mahabusu cha mahakama kuu, upande wa wanawake, miongoni mwa warufani waliokuwamo siku hiyo, alikuwamo na Shuwea Namjupa. Ambae siku hiyo alivua gwanda la kifungwa, akavaa nguo za kiraia. Ndivyo utaratibu ulivyo mrufani akiwa Mahakamani au mtu amefungwa, lakini bado akawa na kesi nyingine, basi siku yakwenda kusikiliza kesi yake Mahakamani, huruhusiwa kuvaa nguo za kiraia na siyo za Kifungwa. Mahakama ilikuwa bado haijaanza asubuhi ile, wakili wa Serikali walikuwa wamekaa na wakili wa utetezi Neema Faraja, wakizipitia sheria na sababu za rufaa alizokata wakili Neema Faraja kumkatia Mrufani Shuwea Namjupa, dhidi ya Mrufaniwa Jamhuri. Wakili Neema Faraja sababu zake nne zakukata rufaa zilikuwa zikisomeka hivi.
MAHAKAMA KUU YA TANZANIA, DAR ES SALAAM
Shauri la Rufani ya Jinai Na. 000 la 2014
(Kutoka Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni)
Kupinga Hukumu ya Mheshimiwa Hakimu NJASI MWAJASI)
Kati ya
SHUWEA NAMJUPA ......Mrufani
na
JAMHURI ......Mrufaniwa
HATI YA KUKATA RUFAA
SHUWEA NAMJUPA, mrufani, anakata rufaa kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania dhidi ya hukumu ya Hakimu wa Mahakama ya wilaya ya Kinondoni ambapo alionekana na hatia ya unyang’anyi wa kutumia silaha, akahukumiwa kifungo cha miaka thalathini, kwa sababu zifuatazo, yaani:
1. Hakukuwa na ushahidi wa kutosha uliotolewa ambao haukuwa na shaka, kwani hakuna shahidi hata mmoja alieieleza Mahakama akimuona Shuwea Namjupa akiwa ametowa silaha kwa muajiri wake, kisha akaiba.
2. Kwamba shahidi wa mashitaka ambae ndiye muajiri wa Shuwea Namjupa, hakuwapo wakati wa tukio, hivyo aliambiwa na mama yake, wakati huyo mama yake ambae alikuwapo wakati wa tukio hakuitwa Mahakamani kama shahidi muhimu. Badala yake shahidi akawa mwanawe ambae aliwakuta wakiwa wamefungwa kamba na pesa zikiwa zimeibiwa. Mtu anaeiba anawezaje kujifunga/kufungwa kamba na wenzake badala yakuondoka na hicho walichokwiba?
3. Kwamba Jamhuri haikuthibitisha mashitaka yake bila ya shaka ya maana dhidi yangu (mrufani).
4. Kwamba hakimu aliehukumu kwa adhabu alieitoa hakustahili kuadhibu adhabu kubwa hiyo kwa mamlaka yake. Kama alivyohukumu Jaji katika kesi ya MOHAMEDI RASHIDI na mwenzake dhidi ya Jamhuri. Ya 2005, washtakiwa walihukumiwa na hakimu wa mahakama ya wilaya Kinondoni, wakili wa mshitakiwa MOHAMEDI RASHIDI, alikata rufaa kwa sababu hakimu aliehukumu alikuwa ni hakimu wa Mahakama ya wilaya, hakuwa hakimu Mfawidhi, au Mkazi.ambao ndiyo wanaweza kumfunga mshitakiwa aliepatikana na hatia adhabu hiyo.
HIVYO BASI mrufani anaomba mahakama ibatilishe hukumu ya mahakama ya awali na kufuta adhabu iliyotolewa dhidi yake.
Sahihi
Mrufani
SHUWEA NAMJUPA
Gereza la Segerea
DAR ES SALAAM
Tarehe
Nakala kwa:
Mkurugenzi wa Mashitaka
Mawakili walizipitia hoja zile nzito za Wakili Msomi Neema Faraja, hadi muda ulipofika wakapanda Mahakamani, Mrufani Shuwea Namjupa akawa anaomba Mungu afanye miujiza ili aachiwe huru. Jaji aliipitia ile hati ya rufani kwa makini na sababu zilizoorodheshwa na wakili, kisha akamuuliza wakili wa Serikali kuhusiana na sababu zile za kisheria kama ana ubishi juu yake. “Mtukufu Jaji, sina ubishi juu ya sababu hizo za kisheria.” Wakili wa Serikali anaeiwakilisha Jamhuri alimwambia Jaji aliekuwa akiisikiliza rufani ile. Jaji aliandika katika jalada lake kwa muda, kisha akavua miwani na kumtazama mshitakiwa akasema. “Mrufani kutokana na sababu za wakili msomi zilizoorodheshwa hapa, mahakama yangu inakiri kwamba umefungwa kimakosa. Hivyo kama hati yako ya rufani inavyosema, nami naituta adhabu dhidi yako, kwa maana yakutengua maamuzi ya awali. Hivyo nawataka Serikali wawatafute wezi halisi waliohusika katika wizi huu, Shuwea Namjupa kuanzia sasa upo huru unaweza kwenda. Upande wa Jamhuri ikiwa hawakuridhika na maamuzi haya, wanaweza kukata rufaa ndani ya siku sitini kutoka leo”
Shuwea Namjupa, alikuwa haamini masikio yake, alikuwa akidhani yupo ndotoni. Msafiri namjupa aliekuwa katika sehemu ya wasikilizaji nae pia hakuamini masikio yake kama dada yake ameachiwa huru kwa siku ile ya kwanza tu aliyokwenda Mahakamani. Machozi ya furaha yalimtoka akawa anatingisha kichwa chake kushoto kulia akiwa haamini kabisa kile kilichotokea.
Shuwea alishuka kizimbani miguu, ikiwa mizito ganzi kubwa ikiwa imemtawala mwilini mwake, mtoto wake alikuwa amelala hana habari na mambo ya dunia yanavyokwenda. Askari Magereza tofauti na walivyokuja wakiwa wanamchunga na kumlinda Shuwea Namjupa, muda ule walimpisha njia pale katika mlango walipokuwa wamekaa ili atoke nje. Wakili Neema Faraja hakika amepeleka Neema na Faraja kubwa katika Familia ya Namjupa. Shuwea Namjupa alipofika nje ya Mahakama ile, akamuona kaka yake Msafiri akilia kilio cha furaha, Shuwea akaungana nae wakawa wote wanalia kwa pamoja huku wakiwa wamekumbatiana.
Wakili Neema Faraja alikuwa amesimama pembeni yao, akiwatazama ndugu wale, walivyokuwa wanalizana kwa furaha. Wakili Neema alitoa simu yake akabonyeza namba kadhaa, simu ya upande wa pili ikawa haipatikani, akaipiga tena kwa mara ya pili, bado simu ile ilikuwa haipatikani. Akaandika ujumbe na kuutuma ili akiwasha simu yake, aweze kukutana nao ujumbe ule. Baada yakutuma ujumbe ule aliwafata wale ndugu wa tumbo moja akawaambia; “Haya imetosha twendeni sehemu kwanza tukajipongeze, kisha tuagane kwani leo nimemaliza kazi yangu kwenu.” Baada yakusema maneno yale, Msafiri alimchukua mpwa wake ambae alikuwa ameamka kwa vile vilio. Shuwea alikwenda kumkumbatia wakili Neema Faraja kwa furaha akamwambia. “Asante sana dada Neema, Mungu atakulipa zaidi kwani bila wewe bado ningekuwa nipo Gerezani, kuna watu wengi wamefungwa Magerezani wakiwa hawana hatia na hawana watu wakuwasimamia na kuwafatilia, hivyo nakushukuru sana na tangu leo, kwa sababu ya kumbukumbu yako mwanangu namwita rasmi Faraja badala ya Matatizo kama ulivyonishauri nikiwa ofisini kwa mkuu wa Gereza.” Wakili Neema akafurahi kuona jina la baba yake likiwa limepata mtu. “Nashukuru sana kwa hilo, ila usinishukuru mimi bali mshukuruni alienipa kazi hii, nakunikutanisha nanyi. Nakuomba fanya yote ila mwanao Faraja hakikisha anasoma na akikuwa mkubwa basi asomee sheria, kwani sheria ndiyo muokozi wa duniani.” Baada ya wakili Neema kusema maneno yale mara simu yake iliingia ujumbe. Alipousoma ujumbe ule akaujibu kuwa anakwenda muda ule. Akawaomba wale waliokuwa wateja wake wapande ndani ya gari yake kuna sehemu kwanza wapite kisha awapeleke nyumbani kwao. Wakili Neema aliondosha gari na kuelekea maeneo ya Tabata shule pale Green Hotel. Wakili Neema Faraja alipofika pale aliiegesha gari yake, wakashuka kwa pamoja na kuelekea sehemu ya yakukaa. Walipofika katika viti alivyokuwa akiwaongoza wakili Neema kwenda kukaa, Msafiri na Shuwea mioyo yao iliwaripuka kwa fadhaa!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Shuwea alikuwa akivuta kiti ili akae, Wakili Neema Faraja akawaaga kuwa anakwenda msalani mara moja, kisha akaondoka kuelekea msalani. Shuwea alipokuwa anakaa mara macho yake yakatazama mbele meza ya tatu kutoka pale walipokuwa wamekaa, akamuona bwana mmoja akiwa anamtazama sana. Nae alipomuangalia kwa makini, moyo wake ulimripuka kwa fadhaa, akaachia mguno uliosikikwa na kaka yake Msafiri aliekuwa nae anaketi jirani yake. Msafiri alimtazama dada yake, akashawishika kudadisi kwa nini agune vile. Akamuona dada yake macho yake ameyakaza kutizama katika meza ya tatu. Msafiri nae akayahamisha macho yake kwa dada yake akayahamishia katika meza ile aliyokuwa akiitazama dada yake. Macho yake yalimuona Bwana mmoja mtanashati aliekuwa amevalia nadhifu, akiwa na mikufu mingi ya thamani shingoni mwake, akimfanyia dada yake ishara ya kukata shingo yake! Moyo wake ulimripuka sana kwani ishara ile aliiona kwa uwazi bila kificho mkono wa jamaa ukiiashiria kuikata shingo yake lakini akiwa anatoa ishara ile alikuwa akimtazama Shuwea. Msafiri akamgeukia dada yake akamuuliza mbona yule anakufanyia ishara ile, dada yake akamjibu.”Yule ndiyo katika watu walionifanya mimi nifungwe jela wao wakitumbua maisha kwa pesa za wizi, yule ndiyo aliekuwa mshenga wangu na ndiyo alietoa bastola siku ile alipokuja kwa muajiri wangu, na aliekuwa mchumba wangu akamtambulisha kuwa ni mshenga wake, akidaiwa kuja kuchukua maelezo kwangu ya namna yakumfikisha nyumbani kupeleka barua ya posa kumbe walikuja kwa nia ya kutenda ujambazi.” Msafiri alimuangalia tena yule jamaa, akawa hawezi kuamini kama yule anaweza kuwa jambazi, kwa namna alivyo kwani yupo njema sana, amevaa nguo na vitu vya thamani sana unaweza kumfananisha na Pedeshee fulani hivi. “Dada isijekuwa unamfananisha?!” Msafiri alimuuliza dada yake huku woga ukimuingia kwani kwa ishara aliyoiona na kama kweli yule mtu ndiye aliewahi kutoa Bastola akafanikisha wizi kutendeka, basi hawezi kushindwa kutoa Bastola pale alipo akawapiga na kufa kisha yeye kutokomea zake ili kuficha kukamatwa kwa tukio lile. “Sikumfananisha hata kidogo, ikiwa nimemfananisha kwa nini anifanyie ishara ile, anajua nimemfahamu na ndiyo maana amenitazama sana akiwa hayaamini macho yake kama mimi ndiye yule ambae yeye kwa ufahamu wake anajua nipo jela.” Shuwea alimjibu mdogo wake huku akiwa macho yake bado yamemkazia yule aliekuwa mshenga wake wa muda.
Wakili Neema alikuwa amekwenda chooni hivyo aliporudi pale katika meza waliyokuwa wale ndugu wawili, akawaona hawapo sawa kisaikologia, kwani wamekuwa wanyonge sana tofauti na walivyofika pale, akawauliza kulikoni? Kabla hawajajibu yule jamaa waliekuwa wakitazamana nae pale meza ya tatu, aliinuka na kutoka nje katika maegesho ya magari, wakamshuhudia akiingia katika gari moja la bei mbaya, akawasha gari yake akaondoka sehemu ile huku wakati akiondoka akairudia ile ishara yake kwa Shuwea. Kitendo kile kilionwa na Wakili Faraja akaitazama ile namba ya gari, haraka akaihifadhi kichwani mwake. Kisha akawauliza tena ndugu wale kwa pamoja. “Kwa nini yule jamaa aoneshee ishara ile kwenu, na nyie gafla mmekuwa hamna amani kulikoni?” Shuwea akamwambia wakili Neema kwamba yule jamaa ndiyo yule aliewatolea Bastola na kufanikisha wizi, akiwa na baba wa mtoto wake. Ni mtu hatari sana, ingawa sasa amenawiri na amependeza sana. Bila shaka ni zile pesa nyingi walizoiba zimewafanya watu wale wale raha, wakati yeye amekaa kwa kupata dhiki katika gereza. Shuwea alitikisa kichwa chake kwa masikitiko, akamwambia wakili Neema. “Naomba tuondoke mahala hapa haraka, kwani yule jamaa ni mtu mbaya sana, asije kuwatuma wenzake wakaja kuniua kisha wakaondoka ili kupoteza ushahidi. Mie sikubali kufa kabla sijahakikisha wanakamatwa na kwenda jela ili waonje uchungu ambao mie pia nimeupata, lakini pia ndiyo wanaostahili adhabu ya kifungo!” Shuwea Namjupa alikuwa akiongea huku akionesha woga na fadhaa kubwa katika maungo yake, hakuwa na amani hata kidogo. Mara alikuja muhudumu ili kuwahudumia, akawauliza; “Niwahudumie nini tafadhali?” Shuwea Namjupa kwa wahaka mkubwa akamjibu yule muhudumu. “Asante dada sie hatuhitaji kitu tunaondoka sasa hivi.” Wakili Neema alimtazama Shuwea akamuona vipele vya baridi vimemtoka mwilini mwake, akatambua kwamba woga umemjaa sana wasingeweza kukaa pale nakuongea chochote, wala kufanya tendo alilolikusudia kulifanya kwao, hivyo alitoa simu yake akatuma ujumbe sehemu aliyoikusudia, ikamrudia ripoti kuwa ujumbe wake umepokelewa ulipotumwa.
***
Yule jamaa aliekuwa amemfanyia Shuwea alama ya kifo, aliendesha gari yake hadi maeneo ya Tabata bima, akapinda kulia kama anaelekea Tabata Mawezi, alipofika mbele akapinda kulia hadi katika ukumbi na baa moja maarufu pale Tabata inayojulikana kwa jina la Madison Square, akaiegesha gari yake pembeni, huku mapigo ya moyo wake yakiwa yanamuenda mbio kama saa mbovu. Alichukua simu yake kutoka katika mfuko wa shati lake, akabonyeza namba kadhaa kisha akawa anasikiliza upande wa pili simu ile ikawa inaita, na mara ikapokelewa. “Halow , kuna kimeo siyo cha kawaida wangu, mie nilikwambia lakini siku ile tummalize yule demu, wewe ukaleta huruma zako za kijinga, sasa leo kwa macho yangu nimeonana nae hivi punde yupo huru uraiani, alikuwa amekaa na kijamaa kimoja kishamba tu, pale Green Hotel Tabata, yaani imenibidi niondoke haraka kwani amenitambua nikaona asije kunijazia watu ikawa Msala, kwani pale kituo cha Polisi kipo jirani. Hivyo wangu inabidi yule mwanamke auwawe haraka sana kama tunataka kuishi kwa amani, vinginevyo imekula kwetu.” Mshenga aliongea kumwambia rafiki yake waliokuwa wameshiriki kufanya uhalifu pamoja kazini kwa Shuwea, wakafanikiwa kuiba pesa nyingi sana ambazo sasa hivi zimewafanya kuwa matajiri wanaotajika mjini. Yule mtu wa upande wa pili alimweleza jamaa yake kwa kirefu, namna yakumshughulikia Shuwea Namjupa, ingawa katika nafsi zao walikuwa wamepagawa vibaya sana. Kwani hawakutarajia ndani ya miaka miwili yule mwanamke awe nje, wakati walishakuwa na taarifa kuwa amefungwa namba ndefu, jasho liliwatoka wanaume wale, kwa pamoja wakaazimia Lazima Shuwea Namjupa auwawe haraka sana, ikiwa wanataka kuishi kwa amani na furaha. Baada yakukubaliana maazimio yao, simu ilikatwa yule jamaa akabaki akiwa ndani ya gari ile kwa tafakuri nzito sana, kwani aliona maisha yake yapo hatarini, wakati yeye alishayatoa maisha keshayapatia. Moyoni mwake akaazimia kwa gharama zozote lazima Shuwea afe tena siyo muda mrefu.
Aliinamisha kichwa chake chini kwa muda akatafakari, alipoinua kichwa chake aliichukua tena simu yake, akabonyeza namba kadhaa, kisha akasikiliza simu ile masikioni mwake, simu yake ikaita upande wa pili kwa muda kisha ikapokelewa. “Upo viwanja gani wangu? Ahaa sasa fanya hivi hapo ulipo Dar West, nenda faster pale Green Hotel, kuna dada mmoja amevaa nguo za dukani za rangi rangi yupo na kijana mmoja mshamba mshamba hata kuvaa hajui, amekaa karibu na ukuta katika mwamvuli wa kwanza kutoka upande wa kushoto kama ukiingia pale mbele ya Hoteli ile. Nenda kawafatilie wanapokwenda wale watu hasa yule mwanamke alievaa nguo za dukani, rangi ya mwili wake ni maji yakunde, mfupi kwa kimo, amesuka nywele zake mtindo wa twende kilioni, mfatilie hadi mwisho wao, kisha nipe taarifa kwani huyo mwanamke anatakiwa kumalizwa haraka ni mtu mbaya sana kwetu, fanya hivyo wangu hakikisha upotezi rada!” Baada yakusema hivyo na upande wa pili kumkubalia agizo lake, alikata simu akabaki kwenye gari yake huku kijasho kikimtoka, wakati mle ndani ya gari kiyoyozi kilikuwa kikifanya kazi yake sawasawa!
Yule jamaa aliepigiwa simu akiwa pale Dar West Tabata, alitoka katika Bar ile haraka akaenda kwenye Pikipiki yake aina ya Boxer alipoiegesha nje ya ukumbi ule, akaipanda na kuiwasha akaelekea Green Hotel pale maeneo ya jirani na yeye alipokuwa. Kutoka Tabata Dar West hadi Green Hotel, ni baina ya pua na mdomo. Green Hotel ipo maeneo ya Tabata shule. Iliyopo katika wilaya ya Ilala Mkoa wa Dar es salaam.
Alipofika akaegesha Pikipiki nje ya Hoteli ile kisha akaingia ndani ya uzio wa Hoteli ile, ambapo kuna miamvuli kadhaa mikubwa kwa ajili ya wateja kupumzika na kupata vinywaji na chakula ikibidi. Yule bwana aliketi kitini akiipa mgongo barabara ya Tabata, macho yake yakawa yanatazama kule mbele ambapo watu wengi walikuwa wamekaa kujipumzisha, wakiwa wanapata vinywaji taratibu. Akamwita mhudumu akamuagiza bia aina ya Heineken, akawa anashushia taratibu huku akiwa yupo pale kwa kazi maalum. Kwani akiwa pale alihakikisha watu waliokuwa katika mwavuli wa Tatu hawapotezi hata kidogo, na pale alipokaa yeye na mwamvuli ule ulipo, kulikuwa hakuna kizuizi baina yao, hivyo akakaa kwa kutizama na kufatilia nyendo zao.
***
Wakili Neema Faraja, simu yake iliingia ujumbe, ikiwa ni majibu ya ujumbe alioutuma, akautazama ujumbe ule akausoma, kisha akawaambia ndugu wale huku akisimama na kuanza kuondoka. “Tunaweza kwenda twendeni.” Msafiri alikuwa katika kufikiri sana , ile alama ya mkono kukata shingo ilimjia sana akaona ni hatari kwa maisha ya dada yake, hivyo ni lazima afanye kitu, akaazimia kufanya ili kuokoa maisha ya dada yake. Waliinuka kwenye viti walivyokaa, wakaondoka kuelekea katika maegesho ya magari wakimfata wakili Neema Faraja kwa karibu. Yule mhudumu aliwatazama kisha akasonya msonyo hafifu, akapanga viti vyake vizuri vikiegemea meza.
Wakili Neema Faraja alipofika katika gari yake, alifungua milango ya gari yake kwa funguo, akitoa lock za milango kisha wakapanda. Akaiwasha gari ile na kuiondosha ile gari mahala pale, huku akili yake ikitafakali kwa nguvu nini afanye ili kufanikisha kuwatia hatiani wale wahalifu halisi wa Ujambazi waliomfanya Shuwea Namjupa, aende kifungoni kwa ajili yao. Alishika njia ya Tabata kuelekea Tabata Aroma akiitafuta Barabara ya Mandela, huku macho yake yakiwa makini kutazama vioo vya gari yake.
Yule mteja aliekuwa akinywa Bia aina ya Heineken, baada yakuona watu waliokuwa katika Mwamvuli ule wakiwa ni watatu na siyo wawili, alituma ujumbe sehemu ili kupata uhakika wa kazi yake, asije kuwafatilia watu ambao siyo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ujumbe uliporudi, ulimletea majibu kuwa ndiyo hao hao watu wake kutokana na maelekezo ya nguo alizokuwa amevaa yule kijana wa kiume, pamoja na nguo alizovaa mwanamke ambae ndiyo wanaomtaka kumuua ili kuondosha ushahidi, kwani hadi wakati ule walikuwa hawafahamu ametokaje jela, wakati alishavaa nguo za kifungwa na alihukumiwa namba ndefu. Kule kuonana nae mahala pale kulikuwa ni bahati mbaya kwao wote.
Pale alipokuwa ameketi akiwa na Pombe ndani ya Glasi na pombe nyingine ikiwa bado ipo kwenye chupa, yule bwana aliiacha ile Bia pale mezani, akamwita mhudumu akamlipa, akaifata pikipiki yake akaipanda. Akaiwasha huku macho yake yakiitazama ile gari waliyokuwa wamepanda Shuwea Namjupa na ndugu yake, ikiendeshwa na Wakili Neema Faraja ikiwa inavuka tuta la pale Dar West. Yule bwana aliiondosha ile pikipiki pale katika maegesho akaiweka barabarani, nae akaelekea Tabata Aroma akiifatilia ile gari iliyokuwa na hasimu wao.
Wakili Neema Faraja aliiendesha gari yake kwa mwendo wa wastani, akafika katika makutano ya barabara ya Mandela , na Tabata. Taa ziliporuhusu akapinda upande wa kulia kuelekea Buguruni, lakini macho yake muda wote yakiwa yanacheza na vioo vya gari yake.
Aliiendesha gari yake kwa mwendo wa kasi, kwani alipopita Tabata Matumbi, njia ilikuwa haina msongamano. Aliivuta ile gari hadi katika taa za kuongozea magari pale Buguruni Sheli. Alipokuwa akitizama nyuma aliiona pikipiki moja aina ya Boxer dereva wake akiwa hataki kabisa kukaa mbele ya gari yae. Kitendo kile kilimfanya afikiri mara mbili zaidi, kwani Pikipiki kadhaa pale kwenye taa za kuongozea magari, zilikuwa zipo mbee ya magari yote, kama ilivyo desturi yao madereva wa Pikipiki wanapofika katika taa za kuongozea magari., hupenda wao wawe mbele ya magari, kwani bodaboda siku zote huwa na haraka sana. Ila ajabu aliyoiona wakili Neema, ni kwa dereva Yule wa boxer kutokukaa mbele kama wenzake.
Taa zikaruhusu magari kutoka Tabata na Ubungo kupita, wakili Neema Faraja akazima gari yake makusudi kisha akavuta waya wa boneti, akashuka kufungua bonet la gari yake, akijifanya kama anatengeneza kitu vile. Ili Jambo lile alilolitilia mashaka alipatie ukweli wake. Wakati yeye akizima gari yake makusudi si Msafiri wala Shuwea Namjupa waliokuwa wakifahamu hatari iliyokuwa inawanyemelea. Ndiyo maana Wakili Neema alifanya vile makusudi mazima kuizima gari yake, ili kujiridhisha na dhana yake iliyokuwa ikimtuma kufanya vile. Magari yaliyokuwa nyuma ya gari ya wakili Neema Faraja, yalipiga honi kwa fujo kumtaka aondoe mkweche wake, wapo madereva waliokuwa wakimtukana matusi ya nguoni, kwa kuzimika kwa gari yake ikiwa mbele kwenye taa. Ama kweli asiekujua hakuthamini, kwani lau kama wangelifahamu kazi ya wakili Neema hakuna mtu hata mmoja ambae angemtukana, lakini wapi usilolijua litakusumbua tu.
Wakili Neema akiwa pale mbele ya gari yake , aliyashuhudia magari yakipinda pembeni kumkwepa ili kuepuka kukaa foleni, pia aliiona ile Pikipiki aina ya Boxer ikimpita pale mbele, dereva wake alitazamana nae uso kwa uso, kisha pikipiki ile aliishuhudia ikizivuka zile taa ikielekea Tazara, akapata nafasi yakuziona namba za pikipiki ile, akazishika namba zake kichwani mwake. Pikipiki ile baada yakuendelea na safari yake, badala yake ilipofika katika kituo cha Buguruni Chama dereva wake akaiegesha kushoto katika kituo kile. Wakili Neema Faraja alilishusha lile Boneti, akawasha gari yake kisha akaunganisha katika taa zile ambazo sasa zilikuwa zimetoka kijani zikawaka taa za njano. Alitembeza gari yake, akakipita kituo kile cha Buguruni chama. Kwa kioo chake cha ndani aliishuhudia pikipiki ile ikiingia barabarani ikiacha pengo la gari mbili tu nyuma ya gari yake. Wakili Neema alitabasamu kisha akaendelea kuiendesha gari yake kwa mwendo wa taratibu, akazivuka Reri za Buguruni, alipofika katika Taa zakuongozea magari za Tazara, pale katika makutano ya Barabara za viongozi mashuhuri, Barani Africa na duniani kwa ujumla, Barabara ya Nyerere na Mandela, wakili Neema Faraja akafanya kitu ambacho hakikutarajiwa kama kingefanyika!
Wakili Neema Faraja alipofika katika makutano ya barabara ile ya
Mandela na Nyerere, akiwa yupo gari ya tatu nyuma kutoka kuyafikia makutano yale, aliwaona askari Polisi wa Doria waliokuwa wapo pale kwenye mti, upande wa kushoto mwa Barabara ile inayotoka Buguruni Chama. Hivyo akaona lazima afanye kitu haraka sana. Alimtazama yule jamaa aliekuwa katika Pikipiki aina ya Boxer akamuona yupo gari ya tatu, nyuma yake akiwa hana mpango wa kukaa mbele. Wakili Neema alimuona askari Polisi mwenye silaha akipita kukagua magari yenye vioo vya kiza, lakini pia yale yalioonekana buti zao kubeba mizigo. Ndipo wakili Neema alipomwita kwa ishara ya kichwa, huku macho yake yakiwa yanamtazama yule mtu wa pikipiki kwenye vioo. Yule askari mwenye silaha akajongea katika gari ya wakili Neema huku akiwa na tahadhali kubwa sana. “Askari gari ya tatu nyuma kutoka kwenye gari yangu, kuna mtu na pikipiki aina ya Boxer amevaa suruali ya jinzi ya Blue na fulana nyeusi, namtilia mashaka kuwa siyo mtu mzuri kwani ananifatilia muda mrefu sana, hivyo naomba atiwe nguvuni tafadhali, mimi ni waliki na ningependa kujua kwa nini ananifatilia.” Wakili Neema alimwambia yule askari Polisi, na yule askari akatazama nyuma ya gari ya tatu kutoka pale alipo akaiona Pikipiki ile, dereva wake akiongea na simu. Yule askari aliifata Pikipiki ile kama hana habari nayo, lakini alipofika karibu akiwa bado gari moja tu aifikie, jamaa alikata simu akaiweka mfukoni akaiendesha Pikipiki ile kwa upande wa kushoto ili asikutane na yule askari, hivyo aliipitia kushoto ile gari lakini yule askari mwenye silaha akamuona haraka akakatisha mbele ya gari ile, akawa yupo mbele ya yule jamaa. Yule askari kwa kasi ya ajabu alipiga goti moja chini akamuelekezea mtutu wa bunduki aliyokuwa nayo mikononi mwake aina ya SMG, huku akimuamrisha asimame, au atamtwanga risasi kama atakaidi amri ile. Yule Dereva wa Boxer kwa wahaka mkubwa alikamata breki huku mapigo ya moyo wake yakimuenda mbio. Askari Polisi waliokuwa Doria pale kwenye mti, walipoona tukio lile haraka waliongeza nguvu. Walikimbilia pale wakaizima ile pikipiki, kisha wakachomoa funguo yake wakamshusha na kwenda nae pale kwenye mti walipokuwa wamekaa awali. Walipofika nae pale wakaanza kumpekua, hawakumkuta na kitu cha kuhatarisha amani, ila walimkuta na simu ambayo waliichukua simu yake ikawa ipo mikononi mwao.
Taa za Barabarani ziliruhusu magari yaliyokuwa yakitoka Buguruni kupita, lakini wakili Neema Faraja hakuondoka bali aliipindisha gari yake kushoto, akaiegesha kando ya gari ya polisi iliyokuwa pale kwenye mti, kisha akashuka chini kwenda alipokuwa yule jamaa na askari. Shuwea na Msafiri Namjupa mapigo ya mioyo yao, ilikuwa inapiga kwa kasi sana kwani waliona hatari kubwa sana inawakabili mbele yao. Hivyo walikaa kwenye gari ile ya wakili Neema wakiwa wanatetemeka kama wamemwagiwa maji ya baridi mwilini mwao. Tangu wakili Neema alipomueleza yule askari kama kuna mtu anawafatilia, wakatambua yule mtu mbaya aliemuoneshea Shuwea alama ya kuua atakuwa anawafatilia ili atimize azma yake.
Wakili Neema alipofika pale kwa wale askari, akatoa kitambulisho chake akawaonesha wale asakri, kisha akaelezea kuhusu yule bwana dereva wa Pikipiki namna alivyokuwa anahusika na watu wabaya kwa namna sehemu aliyotoka nae. Akaomba simu ya yule mtu ikaguliwe, na pia waende kituoni kwa mahojiano zaidi ikibidi, kwani lile suala ni kubwa kuliko wanavyolifikiria. Askari walimpandisha yule jamaa kwenye gari yao, Pikipiki yake ikaendeshwa na Askari wakaelekea kituo cha Polisi Buguruni, kwa maelezo zaidi. Wakili Neema aliifata gari yake akaongozana na gari ya polisi hadi katika kituo cha Polisi Buguruni. Walipofika pale kituoni wakaingia katika chumba cha mkuu wa upelelezi, kwa mahojiano. Wakili Neema akaeleza pale kituoni tangu kuhusu yule jamaa aliekuwa amefanya alama ya kuchinja, hadi kugundua kufatiliwa na yule bwana mwenye ile Pikipiki aina ya Boxer aliekuwa nae pale. Yule jamaa alikuwa akitatarika kama bisi kikaangoni, akijitetea kuwa hakuwa akimfatilia mtu yeyote Yule, yeye alikuwa katika safari zake binafsi.
Askari aliekuwa ameichukua simu ya yule jamaa dereva wa Boxer, aliiperuzi simu ile kwa haraka haraka mara akakutana na ujumbe uliomfanya amtazame mara mbili yule kijana dereva wa Pikipiki. “NDIYO HUYOHUYO, AMEVAA NGUO ZA DUKANI ZA RANGIRANGI, NI MAJI YA KUNDE RANGI YAKE, MFUPI KIMO CHAKE, YUPO NA JAMAA MWEMBAMBA MSHAMBA MSHAMBA, WAFATILIE HAO WATU, KWANI HUYO MWANAMKE NI LAZIMA AUWAWE HARAKA. WAFATILIE HADI MWISHO WAO, KISHA TUKISHAWAJUA WANAPOKAA TUTAKWENDA KUMALIZA KAZI, HUYO NI SHAHIDI MUHIMU SANA, KAMA AKIWA HAI ATATUHARIBIA KILA KITU CHETU MJI UTAKUWA HAUKALIKI HUU.” Ulisomeka ujumbe ule kwenye simu ya Yule jamaa katika sehemu ya ujumbe uliotumiwa simu ile katika siku ile muda si mrefu. Yule askari alipotazama sehemu ya kutuma ujumbe alikutana na ujumbe uliosomeka. “MBONA WAPO WATU WATATU, NA SIYO WAWILI KAMA ULIVYOSEMA, NISIJE KUWAFATILIA WATU SIYO?” Yule askari baada yakuzisoma zile jumbe alimuuliza Wakili Neema. “Upo na watu wengine katika gari yako?” Wakili Neema Faraja akamjibu , “Ndiyo.” Yule askari akamtaka akawaite wale watu wote waliokuwa nae. Wakili Neema alitoka nje akaenda pale alipokuwa ameiegesha gari yake, akawaita Shuwea na kaka yake, kisha akafunga gari yake nakuingia nao katika chumba cha wapelelezi. Yule askari alipowaona Shuwea na msafiri alimsogelea yule dereva wa Boxer, akamchapa kibao kikali cha shavu. “Mpumbavu mkubwa wewe, unakataa kuwa hukuwa ukiwafatilia, mbona humu kuna ujumbe uliotuma kujua watu unaowafatilia, na wewe umeelezwa namna ya watu unaotakiwa kuwafatilia?” Askari aliekuwa na simu ya yule kijana dereva wa Pikipiki aina ya Boxer, alimkaripia sana. “Nyie ni Majambazi eee, haya tunawataka hao wenzio sasa hivi.” Yule askari alimwambia yule bwana alieanza kutahayari mbele ya mikono ya polisi.
Wakili Neema Faraja, akawataka wale askari kumsikiliza Shuwea kuhusu kadhia ile, hivyo shuwea walimtoa uani, yule jamaa akaingizwa mahabusu.
Shuwea Namjupa, aliwaeleza wale askari alivyofika pale Green Hoteli alivyomuona yule muhalifu ambae amemfanya yeye akae jela kwa miaka miwili, akiwa na mwanae ambae baba yake ni katika hao wezi, akaeleza namna ilivyotokea tangu mawasiliano yao, hadi kufikia kufanya mapenzi na yule bwana,akaeleza namna alivyokwenda na mwenzake sehemu aliyokuwa akifanyia kazi, ambae ndiye aliemkuta pale Green Hotel, na hatimae kutolewa Bastola na kufungwa plasta pana, na kufanikiwa kuondoka na kiasi kikubwa sana cha pesa. Ambacho sasa kinawafanya wale bata kwa pesa zile, wakiendesha magari ya thamani kubwa.
Wale askari walichukua maelezo yake, chini ya wakili Neema. Wakiwa katika kuchukua maelezo mara ile simu ya yule jamaa aliyokuwa nayo askari aliekuwa akiandika maelezo ya Shuwea ilianza kuita. Yule askari aliitazama ile namba iliyokuwa ikiita akaliona jina lililokuwa likiipigia simu ile. Akatingisha kichwa kukubaliana na anachokiona. Simu ile ilikatika na yule askari akaiandikia ile namba iliyokuwa ikiipigia ile simu. “NILIKUWA NAENDESHA NIPO BARABARANI NITUMIE UJUMBE.” Kisha akautuma ule ujumbe kwenye ile simu iliyoipigia ambae aliliona jina lake, kisha akawa anasubiri kuona kama mtego wake utanasa au laa. Wakiwa bado katika kuchukua maelezo ya Shuwea mara simu ile ya dereva wa Pikipiki, ikaingia ujumbe. “UKITOKA KUWAFATILIA HAO, TUKUTANE UWANJANI ILI TUJADILI NAMNA YA KUMALIZANA NAE HUYO MWANAMKE HARAKA IWEZEKANAVYO.” Yule askari akamaliza kuchukua maelezo ya Shuwea, wakili Neema akaoneshwa zile jumbe zilizokuwa katika simu na askari yule, zikithibitisha kuwa kweli alikuwa akifatiliwa na yule jamaa, ingawa hakuwa akitakiwa yeye. Basi yule askari akatoa namba zake za simu kwa wakili Neema, na wakili Neema nae akafanya vile, kisha akaelezwa kuwa wao Polisi watahakikisha siku ile ile wanawatia mbaroni, kwani lazima wambane Yule mwenzao awambie uwanja wanaokutania na wahalifu wenzake, kasha watajenga mtego na hatimae kuwatia mbaroni kisha kuwafikisha katika vyombo husika. Wakili Neema Faraja aliagana na wale askari akatoka yeye na familia ya Mzee Namjupa, wakaendelea na safari yao. Wakiwaacha askari kufanya kazi yao ya kuchunguza, na kukamata na hatimae kufikisha katika vyombo vya sheria.
Wakili Neema Faraja, aliondoka na wateja wake, wakaiendea gari yake, wakaingia ndani ya gari. Kabla hajawasha gari, wakili Neema Faraja simu yake ikaingia ujumbe. Aliusoma ule ujumbe kwa makini, akatikisa kichwa chake kukubaliana na ujumbe ule, nae akaujibu ujumbe ule, kisha akawasha gari na kuingia Barabarani. Wakiwa ndani ya gari Faraja akaanza kulia njaa ilianza kumsumbua, uchovu wakuzunguka na magari, hakuwa amezoea. “Nashauri tutafuteni mgahawa ili tupate chakula, kwani huyo baba yangu tayari njaa inamsumbua.” Wakili Neema aliendesha gari hadi maeneo ya Temeke, wakatafuta Restaurant wakaingia wakaagiza chakula, wakala Faraja alikula kwa mikono miwili! Ama kweli njaa haijui mtoto wala mkubwa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kula, safari ya Mbagala iliendelea na hatimae wakafika Mbagala Kizuiani, na Wakili Neema akaombwa afike nyumbani kwao, ili aingie ndani kwani siku zote hakuwahi kufika hadi ndani. Hivyo hakuwa na pingamizi, aliiegesha gari yake nje wakashuka, na kuelekea ndai. Wapangaji waliokuwa wakiishi mle ndani ya nyumba ile, walikuwa wapo uwani wakamuona Shuwea, wote waliinuka na kumpa Pole Shuwea, wengine wakimpa hongera. Shuwea kabla yakwenda kufanya kazi kwa wahindi alikuwa amepanga katika nyumba ile, hivyo wale wapangaji alikuwa akiishi nao vizuri sana, ingawa tangu apate matatizo watu wale walikwenda kumtazama siku za awali tu, lakini tangu alipofungwa nao walikata tamaa, wakaona Shuwea atafia Jela. Hawakwenda tena kumtazama, kitendo kile cha kumpa pole, kilimtia uchungu kwani alikuwa amefika katika nyumba aliyoanzia maisha, kabla mdogo wake hajaja kutoka Nachingwea na kufikia hapo kwa dada yake. Shuwea alilia sana kwa furaha watu wakawa wakimbembeleza, na kumwambia mapito tu yale anyamaze, kwani dunia ndivyo ilivyo.
Wakili Neema Faraja alikuwa yupo kimya kabisa huku akitazama saa yake. Msafiri alifungua chumba akamkaribisha wakili Neema ndani. huku yeye akitangulia ndani ya chumba kile. Wakili Neema aliingia ndani ya chumba kile akayatembeza macho yake, chumbani mle akashuhudia kwa macho yake, namna ya umasikini ulivyokuwa umetawala chumba kile. Kwani chumba kilikuwa kama stoo kila kitu kilikuwa kipo hovyo, chumba kilikuwa kinanuka vumbi, vitu vilikuwa vipo shaghalabaghala. “Karibu sana wakili, hapa ndiyo kwetu, na haya ndiyo maisha yetu tunayoishi.” Msafiri alimwambia wakili Neema Faraja ambae nae alitikisa kichwa chake juu chini akiyakubali maisha yale. Shuwea Namjupa aliingia mle ndani ya chumba alichokiacha kwa muda mrefu, akamlaza kitandani mtoto wake aliekuwa keshashiba usingizi ukimnyemelea,naye akakaa kitandani, akawa anafuta machozi kwa huzuni, kwani roho yake ilifika mbali sana, aliwafikiria wenzake waliokuwa jela. Hakuwa akilia kwa sababu yakutaka kurudi Jela laa, bali aliwafikiria wenzake katika maisha aliyoyapitia kuwa bado wanaendelea kusota katika maisha magumu sana yasiyokuwa na thamani hata chembe, maisha ya udhalili, maisha mabovu kabisa.Ama kwa hakika Jela ni jumba la dharau. Ni heri ulale chini ukiwa huru, kuliko kulala juu ya godoro ukiwa Jela. Ama ni kheri ulale kwenye kiza kinene uraiani, kuliko kulala kwenye mwanga wa taa ukiwa Gerezani.
Wakiwa wamo chumbani wamekaa, wakili Neema Faraja simu yake iliingia ujumbe, nae akausoma ujumbe ule kisha akaujibu huku akitabasamu. Msafiri alimtazama wakili Neema, akawa na dukuduku kubwa lakutaka kumjua mtu aliewawekea wakili Yule. Hivyo alikaa vizuri pale katika kitanda ili amuulize swali lile. Kwani aliona umefika muda muafaka wa kulifahamu suala lile, kwa vile wote yeye na dada yake tayari walishakuwa wapo huru, hivyo alimkabili wakili Neema akamuuliza kwa shauku kubwa. “Wakili tunashukuru sana kwa jitihada zako, ulizozifanya za hali na mali hadi leo mie na dada yangu tupo huru. Lakini bado lile jambo linanisumbua sana katika moyo wangu, ni nani aliekupa kazi hii, hadi ukatufatilia na kutufanya leo hii tuwe ni familia tuliokuwa huru.” Msafiri alipomaliza kusema maneno yale kabla wakili Neema hajajibu kitu, Shuwea nae akadakia kwa msisitizo sana. “Hakika babisa jambo hilo niliwahi kukuuliza siku ya kwanza tu wakati, ulipokuja gerezani kwa ajili yakutaka kufahamu kesi yangu. Msafiri amekumbusha jambo ambalo lilikuwa lipo rohoni mwangu, kwani mtu huyo kwetu ni muhimu sana, na ni rafiki wa familia yetu, na tuna kila sababu ya kumpa shukurani zetu za dhati kwa kutufanyia wema huo, nakuomba sana dada Neema tuambie ili pia tukampe shukurani zetu, kwani huyo mtu ni zaidi ya ndugu.” Wakili Neema aliitazama saa yake, kisha akainua uso wake kuwatizama kwa zamu wana ndugu wale. Kabla kinywa chake hakijatamka lolote, mara walisikia mlango wa chumba kile uliokuwa umeegeshwa ukifunguliwa, na mara akaingia mtu ndani ya chumba kile akawa amesimama akiwaangalia. Wanandugu waliokuwamo mle ndani, miili yao ilikufa ganzi, wakataharuki sana kwa fadhaa. “Mbuya?! Umefata nini huku, mshenzi mkubwa wewe tokaaaaaaa!” Shuwea Namjupa alijikuta akitamka maneno yale, huku akisimama wima kwa hasira. Msafiri Namjupa alimkazia macho ya chuki, huku mapigo yake ya moyo yakimuenda mbio kupita mapigo yake ya kawaida akili yake ikawa inatafakari imfanye kitu gani mwanamke Yule mbaya sana hasidi wa roho yake.
Mbuya Fabiola alikuwa amekunja mikono yake kwa mbele kama mtu aliefunga swala, aliwatazama wanandugu wale walivyokuwa wamehamaki, kisha akasema kuwaambia. “Naomba mnipe nafasi na mimi niseme basi, najua nimekuja nyumbani kwenu bila taarifa, ila mngenisikiliza pengine msingenivesha huo ubaya mlionitwika nao.” Mbuya aliwaambia wale wana ndugu lakini, alikuwa akitwanga maji kwenye kinu. Kwani hakufanikiwa kuwatuliza. Shuwea Namjupa alichambia huku, na Msafiri Namjupa alisemea kule, ikawa ni tafrani moja kwa moja. Wakili Neema Faraja aliingilia kati akasema kuwaambia wale wana ndugu. “Naomba tusikilizane jamani, kwani kila mtu akiwa anazungumza tutakuwa hatuelewani humu ndani.” Shuwea Namjupa alikuwa akihema kwa nguvu, presha ilikuwa ipo juu imempanda, kwa namna alivyomchukia Mbuya kwa kitendo alichomfanyia kaka yake. Msafiri yeye alikuwa anatokwa na machozi ya hasira, kwa namna alivyokuwa akimtazama Mbuya aliekuwa mbele yake, alitamani kumvamia ampige vichwa amng’oe meno yake ya juu ili amalizane nae, lakini aliogopa kuchukua sheria mikononi, kwani jela hajafika ila Polisi ameijua. Hivyo alikuwa mpole hasira zake ziliishia kutoa machozi, huku moyo wake ukimdunda kwa kasi sana. “Naomba niwafahamishe kitu kimoja kuwa, mie ndiye niliemwita Mbuya mahala hapa, nimefanya hivi kwa sababu maalum, hivyo kama mtakuwa mmetulia na kunipa fursa ya kuwaeleza kwa nini nimemwita Mbuya hapa, basi nitawaambia sababu ya kumwita kwangu.” Wakili Neema Faraja alisema maneno yale huku akiwatizama ndugu wale usoni. Shuwea Namjupa alimtazama wakili Neema akakaa kimya kuashiria anamsikiliza. Msafiri nae kwa upande wake alikuwa kama dada yake, nae alikaa kimya. Mbuya Fabiola hakumsubiri wakili Neema kuzungumza, bali alitamka kumwambia wakili Neema. “Nakushukuru sana dada Neema kwa kazi yako nzuri sana, isiyomithilika kwa kufanikiwa kumtoa nje ya Gereza dada Shuwea na mwanawe. Lakini pia nikupongeze kwa kufanikiwa kushinda kesi ya Msafiri na kuwachiwa huru, hata pale nilipotambua mipango ya kukamatwa kwa Msafiri na kupelekwa Mahakama ya Mwanzo ili ionekane alinitorosha mimi Mahakamani, nilipokupigia simu kukufahamisha jambo hilo, uliweza kukimbia haraka hadi Mahakamani na kufanikiwa kumtoa. Kubwa zaidi nakupongeza kwa kuweza kunificha kwa Dada Shuwea na Msafiri kuwa mie ndiye niliekupa kazi hii, pale nilipokupigia simu siku ile ya Ijumaa na wewe ukakubali kuyashughulikia masuala haya kwa moyo wako wote. Asante sana, kwa kufanikisha suala hilo. Kwani sikuwa na ubaya kwa Msafiri hata kidogo, mie nilimwambia Msafiri kuhusu mzazi wangu lakini alikaidi kunisikia, akalazimisha niende nae nyumbani. Lakini sikuwa na namna ila ile niliyoifanya. Kitu ambacho sikukitarajia ni Msafiri kukimbizwa kama mwizi, kwa kweli iliniuma sana na ndiyo maana nikatumia pesa nyingi sana ili kuhakikisha Msafiri anakuwa nje, kwani Dada Shuwea nilishamuahidi kumshughulikia. Pesa alizoniachia marehemu Mama yangu ni nyingi sana, na nilifunguliwa akaunti na siulizwi nazitumiaje kwa vile ni haki yangu. Kwa kuwa siku hizi huduma za ki bank zimeunganishwa na mitandao ya simu, huniwia rahisi sana kutoa pesa kupitia simu. Na ndiyo maana hata uliponiambia malipo ya Dada Shuwea kumtoa ingeghalimu kiasi cha shilingi milioni mbili, sikuwa na ubishi nikakutumia yote bila deni. Hata ilipotokea tatizo la Msafiri nilipokupigia simu kukufahamisha jambo lile, ukataka milioni moja na nusu, nayo nikakupa yote bila ubishi. Mimi nilikwenda Mahakamani kutoa ushahidi kwa sababu ile ni Mahakama inapokwita ni lazima uwitike wito wake, lakini pia ilikuwa ni kumridhisha Mzazi wangu pekee anaenipenda kuliko kitu chochote. Ndiyo maana hata ushahidi wangu sikuongea kitu cha uongo kwa Msafiri Mahakamani, bali niliongea ukweli mtupu wala sikumkandamiza. Pia nikijua umahiri wako nikajua lazima utavunja hoja zile na hatimae Msafiri kuwa nje kama ambavyo iliyovyokuwa. Mie sikushindwa kuzua namna gani nilirubuniwa lakini Msafiri hakunirubuni bali mie ndiye niliemwita akiwa anapita njia tu” Mbuya Fabiola alisimama kusema maneno yale akenda kumkumbatia wakili Neema pale alipokuwa amekaa. Shuwea na Msafiri walitazamana kama watu waliokuwa wanaonana siku ile, walikuwa wamerowa chapachapa kwa jasho. Ukichanganya presha kubwa ya jambo lile na maneno ambayo hawakuyatarajia kuyasikia kwa mtu waliemuona ni adui mkubwa sana yaliwachanganya sana. “Sina shaka mmesikia maneno ya Bosi wangu kwenu, yeye ndiye alienipa kazi hii yakuwashughulikia hadi leo hii mpo nje mkiwa huru. Mbuya amenilipa pesa zangu zote milioni tatu na nusu simdai hata sent tano. Sasa sababu yakumwita hapa ilikuwa ni hii yakuwafahamisha nani alienipa kazi hii kwenu, nani alienihadithia matatizo yako Shuwea, nani alienijuza kukamatwa kwako tena Msafiri. Ndiyo maana nilikung’ang’ania sana kule mahakamani siku ile umpe mkono mzee Fabiola, lakini hukujua hekima yangu, kwani Mbuya ameniambia kutokana na mkasa uliokukumba bado hajalipa fadhila zake kwako. Hii kukutoa nje ya kesi ni kwakuwa yeye ndiye aliesababisha kesi ile, hivyo kukutoa ilikuwa ni jukumu lake, ila fadhila yake kwako anataka muwe wapenzi na hatimae kufunga pingu za maisha kwa moyo wako wa huruma uliomuonesha.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakili Neema faraja alipofika hapo akanyamaza akamtazama Msafiri, ambae jasho jingi lilikuwa likimmwagika mwilini mwake, kutokana na ufinyu wa hewa wa chumba kile, lakini pia hakutarajia pia maneno ambayo anayasikia. Moyo wake Msafiri ukaongeza mapigo yake kwa taarifa ile. Dada yake Shuwea alifanikiwa kusimama akamfata Mbuya akenda kumkumbatia huku akilia akamwambia. “Mbuya nisamehe mdogo wangu, sikuwa nayajua yote haya tangu mwanzo, nimekukaripia bure, nimekufukuza bure, kumbe mungu alikupa matatizo uje jela ili uwe sababu ya kunitoa, nakushukuru sana kwani wewe ni zaidi ya ndugu yangu. Wewew ni muhisani wetu, nakuomba msamehe Msafiri sana kwa kila kilichotokea ni ubinaadamu tu huo, nisamehe mdogo wangu ama kweli Zimwi likujualo halikuli likakwisha.” Shuwea Namjupa alimkumbatia Mbuya kwa muda huku akilia na kulombokeza kwa maneno yakumpongeza nakumuomba msamaha. Msafiri aliinama akafikiri sana kisha alipoinua macho yake kumtazama Mbuya, alikuwa akilia kwa huzuni. “Mbuya je kama ningekufa siku ile ingekuwaje, vipi kama ningechomwa moto nikafa kibudu huoni kuwa ungeidhulumu nafsi yangu, nakupongeza kwa kumtoa dada yangu, lakini nikimfikiria baba yako, sitaki tena kujiingiza katika matatizo kama yale, kwani nilikataa kumpa mkono siku ile, nae alikasirika sana kwa vile nilimfedhehesha hivyo atakuwa ameniwekea kinyongo sana katika nafsi yake, atakapotambua kama nina uhusiano na wewe, atanipiga risasi aniuwe, japo kuwa sina mpenzi katika Mkoa huu, lakini bado nataka kuishi kwa amani.”
***
Katika kituo cha polisi Buguruni, yule dereva wa Boxer alikuwa mahabusu akihaha kutafuta namna yakutoa taarifa kwa wenzake, aliwauliza mahabusu waliokuwamo mle ndani kama wana simu, lakini wote walikataa kuwa hawana simu mle ndani. Alikuwa akizunguka huku na kule mle ndani, pombe aliyokunywa ilimtoka yote akaona muda si mrefu jela inamwita. Akiwa katika kutafakari mara mlango wa mahabusu ulifunguliwa na asakri, akaitwa jina lake kisha akatolewa mle mahabusu, akapelekwa katika chumba cha upelelezi kwa kuhojiwa. “Wewe tuambie ukweli kabla hatujakuumiza, ushaiba wapi na wapi na ututajie wenzako uliokuwa ukiiba nao kama unataka salama yako.” Askari walikuwa wamezunguka wakiwa wapo tayari kwa kupata taarifa za uhalifu. Yule jamaa kabla hajajibu alisikia mikono yenye nguvu ikitua kwa nguvu kasikioni mwake, iliyopigwa pamoja ikamsababishia kusikia maumivu makali. “Sema wewe hatukubembelezi sie, wapo wapi hao wenzio tunawataka sasa hivi, yaani sie tubebe bunduki na nyie mbebe bunduki nani askari hapo kati yenu na sie?!” yule askari aliempiga makofi ya masikio alimuuliza kwa hasira. Yule kijana aligeuka nyuma ili amuone aliempiga, akachezea kibao chengine cha shavu kikamrejesha katika alivyokuwa amekaa awali. “Msiniumize wazee nipeni simu nimpigie ili nizungumze nae nimvute atakuja nanyi mtamkamata.” Aliongea yule kijana huku uso wake ndani ya dakika chache ulikuwa tayari umeshalulumka kwa kuvimba. “Sasa maneno si hayo, ulikuwa unataka kukaza nini fala wewe tutakuumiza.” Askari alimwambia huku akitoa simu ya yule jamaa akaitafuta ile namba iliyotuma ujumbe, akamwambia yule kijana wana ‘loud speker’ hivyo amwite aje buguruni Sheli muda ule, ili wamalizane nae. Kisha akaipiga ile simu akaiweka spika ya nje akampa yule jamaa azungumze nayo. “Halow niambie umepajua walipoishia wale walugaluga?” Sauti ya mtu wa upande wa pili ilisikika kwa wote waliokuwamo mle ndani. “Ndiyo nimefanikiwa, sema nini njoo haraka tukutane hapo Buguruni sheli, sasa hivikuna mambo yakuongea na kupanga!” Yule dereva wa Bodaboda alimwambia mwenzake. Wale askari walitikisa kichwa kukubaliana na wito ule, pia wakawa makini kumsikiliza atajibu nini. Yule mtu wa upande wa pili kwa pupa akamuuliza mwenzake. “Nije haraka au nisije haraka?” Dereva wa Boxer akamsisitiza, “Njoo haraka, yaani haraka bila kukosa wangu!” Yule mtu wa upande wa pili akamjibu. “Poa nimekusoma nakuja haraka sasa hivi hapo.” Baada yakusema maneno yale simu ilikatwa na askari akaichukua ile simu, wakajipongeza kuwa siyo muda mrefu wanamtia mtu mikononi mwao. Hivyo bila kupoteza muda walimchukua yule dereva wa Boxer, wakamuingiza katika gari ya kiraia iliyokuwa na vioo vya kiza, akawekwa kati katika siti ya nyuma akavishwa pingu za mikono, wakaenda kuweka mtego pale Buguruni sheli. Yule dereva tofauti na alivyokuwa awali, baada ya simu ile alikuwa ni mtu aliekuwa ametulia sana.
Askari waliokuwa na silaha ndogo Bastola, wawili walikuwa wameshuka eneo lile, askari watatu walibaki katika gari, na mtuhumiwa, wakawa wanamtazama kila mtu mwanaume anaepita eneo lile, ili dereva wa Boxer aelekeze mtu wanaemtaka ili wapate kumkamata, lakini dakika ziliyoyoma hakuna mtu aliekuwa ameonekana. Wale askari walisubiri sana lakini matokeo yalikuwa bado hayajabadilika, ilipita saa mbili nzima bila kuonekana mlengwa, askari akamwambia yule dereva wa Boxer. ”Mpigie tena muulize yupo wapi ili tujue kama vipi tumfate hukohuko alipo, kulipo kupoteza muda.” Ilipigwa ile namba kwa mara nyingine, lakini askari wale hawakuyaamini masikio yao kutoka katika simu ile ilivyokuwa ikisema. “Simu unayopiga haipatikani kwa sasa tafadhali jaribu tena baadae “ wale askari walitazamana wakaijaribu tena na tena kuipigia lakini majibu yalikuwa ni yaleyale, simu haipatikani. “Inaweza ikawa chaji imekwisha kwenye simu yake, ila tumsubirini tu atakuja.” Aliongea yule dereva wa Pikipiki kuwaeleza wale askari, nao wakamsikiliza wakaendelea kukaa pale. Waliganda hadi wakakamilisha saa sita za kuwapo pale lakini simu ya jamaa haikupatikana, hata mwenye simu hakupatikana, wale askari wakashauriana wamrudishe mahabusu yule bwana wabakie na simu yake wawe wakiijaribisha ili ikiita tu, basi wamvute wamalizane nae, Jamaa akarudishwa Mahabusu, wao wakakaa na simu ile wakiiweka kwenye chaji ili isizimike, lakini hadi kinaingia kiza simu ya jamaa bado ilikuwa haipatikani tu.
Yule jamaa aliepigiwa simu akiambiwa aende Buguruni Sheli haraka, baada yakupokea ujumbe ule, kwao ulikuwa na maana kubwa sana. Ndiyo maana ili kuthibitisha maana halisi ya jambo lile, alimuuliza mwenzake kuwa aende haraka au asiende haraka? Lakini mwenzake akamsisitizia aende haraka haraka, ndipo nae alipothibitisha kuwa mwenzao ameshakamatwa! Katika utendaji wa kazi zao, wanafahamu kuwa askari akimkamata mmoja wa muhalifu, basi hutumika kuitwa muhalifu mwengine kwa simu yake ili kumkamata. Kwa kufanya hivyo kumewezesha kukamatwa kwa wahalifu wengi sana, hadi kupelekea wengine kupeleka mpira, kwa wenzao na kuwakamatisha. Ndipo wao walipoanzisha mbinu hiyo kuwa ikiwa mtu amekamatwa na Polisi, na akatakiwa awavute wenzake, basi asikatae kwani kukataa kuwa huwajui tu, utachezea kipigo kikubwa sana, lakini ukikubali kupiga simu utakuwa umeepusha kipigo hicho, kwa vile Polisi watajua unawapa ushirikiano. Hivyo utakapompigia mmoja wa jamaa anaetakiwa na polisi, basi kumtambulisha kwako kuwa umekamatwa na Polisi, ni neno “Njoo haraka” pahala fulani, mwenzako ili kuthibitisha kama amekuelewa, atakuuliza aje haraka au asije haraka, nawe ukiwa kweli upo mikononi mwa Polisi basi utathibisha kuwa ende haraka, lakini akiwa hayupo na Polisi yaani hajakamatwa atamwambia asiende haraka. Kwa kusema hivyo atakuwa amempa taarifa kuwa yupo salama kabisa. Hivyo yule bwana baada ya kuthibitishiwa ende haraka akatambua mwenzao keshakamatwa, alichofanya baada yakukata simu yake, akawapigia simu wenzake wote kuwajulisha kuwa mwenzao keshakamatwa hivyo wasikubali kuvutwa ikitokea kupigiwa simu nae, kisha yeye akaichomoa ile line na kuivunja akabadilisha line ya mtandao mwengine, pia akaondoka nyumbani kwake japo kuwa wenzake hakuwahi kuwapeleka hata siku moja kupajua anapoishi.
***
Wakili Neema Faraja, alimtazama Msafiri kwa macho ya mshangao sana. Kwani wanaume wachache sana wanapoipata bahati kama ile, huwa wanajipindua ila wengi wao huwa hawaichezei hata kidogo. Wakiwa bado chumbani wakizungumza, mara mlango wa chumba kile ulifunguliwa, akaingia mtu aliesababisha kizaa zaa kikubwa sana!
Mama mmoja mtu mzima, aliingia katika chumba kile, akiwa amekasirika vibaya sana akidai kodi yake ya nyumba akaanza kutoa baadhi ya vitu nje ili afunge chumba kile. “Nimevumilia sana nishachoka, mie mjane kodi ya nyumba ndiyo inayonifanya niendeshe maisha yangu, huu ni mwezi wa sita sasa bado sijalipwa kodi yangu. Basi imetosha hameni humu ndani nipangishe mtu mwengine kwani nyumba hii ishawashinda.” Mama mwenye nyumba hakutaka kumuuliza mtu hali wala kumpa pole Shuwea ambae alikuwa na taarifa ya matatizo aliyoyapata lakini yeye aling’ang’ania kodi yake imekaa siku nyingi anataka chumba chake. Ilikuwa ni kizaazaa kikubwa sana, kwani wanandugu wale hawakuwa na pesa hata kidogo, Shuwea alimuomba yule mama mwenye nyumba, ampe muda japo wa mwezi mmoja ili ajipange alipe lakini hakueleweka. Ikawa mama anatoa chombo na Shuwea anakirudisha ndani. Tukio lile lilijaza wapangaji wa mle ndani na watu wa jirani. Watu ambao wote wakawa wamekaa kimya tu wasiweze kutoa msaada wowote kwa familia ile. Msafiri alimuomba yule mama aje kesho ili watafute kitu cha kuweka Rehani, wamlipe kodi yake anayowadai ila Bi Mkubwa akawa amekaza uso wa mbuzi, hasikii la mtu yeyote zaidi ya pesa yake. Yule Mama alikuwa na alama ya kumi na moja pembeni ya uso wake, akiwa ni mwenyeji wa Rufiji.
Wakili Neema kwa upole akamuuliza yule mama, “Kwani mama yangu unawadai shilingi ngapi hadi unawaadhiri kiasi hiki?” Yule mama akamtazama kwa jeuri kisha akamjibu. “Siyo nawaadhiri bali nimechoshwa kusumbuliwa kwa kufatilia haki yangu, nawadai kodi kwa miezi sita wamekaa humu hawajalipa, hivyo wanilipe kodi yangu ya miezi sita ninayowadai, kisha watoe kodi ya miezi sita mingine ili tusisumbuane tena.” Yule mama alizungumza kwa Lafudhi ya Kindengeleko huku akimtazama wakili Neema ambae wala hakuwa akifahamu kama anaongea na wakili. Mbuya alikuwa amekaa kimya muda wote, akishuhudia lile timbwili la mama wa Kindengeleko, mara simu yake ikaanza kuita. Aliitazama simu ile namba iliyokuwa ikipiga simu ile ni ngeni, akaamua kuipokea. “Halow?” mtu wa upande wa pili akamjibu. “Halow Mbuya, Iddy Teva hapa, nimeazima simu ya jamaa amekuja mahakamani kuwafatilia ndugu zake, mie leo hatimae nimeachiwa kwa upepelezi kutokamilika zaidi ya siku sitini hivyo naomba tuonane mpenzi wangu, ili uniliwaze kwani nimekaa jela kwa sababu yako.” Mbuya Fabiola alipatwa na kigugumizi sana kwani huku kuna kizaazaa, kule anaitiwa mapenzi. Sikia Iddy, mie kwa sasa sina nafasi ila kapumzike nitakutafuta pole sana.” Baada yakusema maneno yale Mbuya akakata simu huku mkono wake akashika kichwa chake kwa tafakuri. “Kodi yako kwa mwezi ni shilingi ngapi mama?” Wakili Neema Faraja alimuuliza yule mama mwenye nyumba aliewajazia watu. “Hao waliopanga humu wanajua bei yake, waulize usinichoshe na maswali, mie nimetoka Bungu nimefata pesa yangu hapa, au chumba changu sikuja kujibu maswali lukuki hapa.” Mama mwenye nyumba alikuwa ni jeuri kama chokaa mbichi.
Wakili Neema akamuuliza Shuwea, “Kodi ni shilingi ngapi hapa mnalipa?” Shuwea akajibu “Elfu kumi na tano kwa hivi vyumba vya uani. Vile vya ndani kodi yake ni shilingi elfu ishirini na tano.” Wakili Neema Faraja akatikisa kichwa kuwa ameelewa. “Keshakwambia bei ya kodi unamlipia au ulitaka kujua tu?” Yule mama alimuuliza wakili neema kwa jeuri. “Hiyo siyo pesa nyingi kwetu, tunakulipa hapahapa tulipo, ila rudisha vyombo ulivyovitoa nje.” Mbuya Fabiola alimjibu yule mama kwani wakili Neema hakuwa na muda wakujibizana nae alishamuona ni mjinga. “Haya mlipieni tena huyo masikini, mkaa bure nyumba za watu” yule mama alimwambia Mbuya pamoja na wakili Neema Faraja kwa lengo lakupata fedha zake. http://deusdeditmahunda.blogspot.com/Wakili Neema aliingiza mkono mfukoni mwake, ili atoe pesa, lakini Mbuya alimzuia.”Hapana dada Neema mimi nitatoa, msaada ulionipa ni mkubwa sana hadi sasa hivyo sitaki nikupe mzigo mwengine.” Mbuya alisema maneno yale akaingiza mkono katika mfuko wa sketi yake akatoa kitita cha pesa, akazihesabu noti za shilingi elfu kumikumi kumi na nane akamkabidhi yule mama na kumwambia. “Hizo ni laki moja na elfu thamanini, kodi yako ya miezi sita iliyopita na miezi sita ijayo je kuna shida nyingine?” Yule mama alichukua zile pesa akazihesabu huku akitia mate kidole chake, hadi akathibitisha kuwa zimetimia. “Shida nyingine hakuna, poleni sana kwa matatizo wanangu vipi yameishaje?” Watu waliacha uchungu wakacheka, yaani kumbe anafahamu kuwa watu wamepata matatizo ila alikuwa akidai kodi yake kwa namna isiyopendeza vile, ama kweli mtu chake. Yule mama alisema maneno yale uso mkavu kama hakuanzisha kizaaaa muda mfupi uliopita.Kisha alipoona hajibiwi akashika njia akenda zake.
“Jamani sasa mie nakwenda zangu, kesho nitapita Polisi ili kujua walipofikia kama wameweza kuwakamata wale wahalifu ama laa, hivyo mie nawaaga. Ila ninachowashauri hasa Shuwea, kuwa makini sana matembezi yako, kwani unawindwa na watu wanaokujua hivyo ni hatari sana kwa maisha yako chukua tahadhali wakati huu, hadi wale wahusika wote wakishatiwa mbaroni ndiyo utakuwa huru zaidi.” Wakili Neema Faraja alimwambia Shuwea namjupa, maneno yale kisha akainuka na kutaka kuondoka, ila Shuwea akamzuia na kumuomba akae kidogo, nae hakuwa na ubishi akafanya hivyo. “Dada Neema asante sana, wewe pamoja na Mbuya kwani Mungu hufanya vitu kwa maarifa. Mbuya kuja kwake Gerezani, kumesababisha mie kuwa huru na kifungo, lakini pia kuja nyumbani kumesababisha nilipiwe kodi, hapa ninapoishi nawashukuruni sana kwa misaada yenu kwetu. Huyu kaka yangu nadhani amepigwa sana kichwani ameumia kichwa chake kwa ndani ndiyo maana anashindwa kupambanua mambo. Ikiwa anamkataa Mbuya anataka aishi na mwanamke yupi? Hana akili sawasawa huyu. Hiki chumba alikuwa akiishi humu kwa vile mie nilikuwa Gerezani, hawazi kuwa hatutoweza kuishi sote tena lazima atafute chumba chake, na hicho chumba atakitafuta kwa pesa zipi kwa kazi ambayo hata kodi ya miezi sita kulipa imemshinda hapa. Ndiyo mana nasema hana akili huyu, Mbuya niachie nikae nae mie, nitazungumza nae naamini atakubali muwe pamoja.” Mbuya alitabasamu kisha akasema. “Dada Shuwea, wala huna sababu yakuzungumza nae, kwani siyo mtoto mdogo, na kama angekuwa ameumia kama ulivyodai, basi naamini asingekuwa na misimamo ambayo imetufikisha hapa tulipo, huyu ana asili ya ubishi tu, kwani yeye mwenyewe kwa kuambiwa na wanzeke, akang’ang’ania vitu ambavyo havikuwa na lazima. Sasa nasema hivi nimeshafanya mengi kwenu, kama fadhila nimeshalipa basi imetosha. Natambua kuwa Mzowea vya kunyonga, vya kuchinja haviwezi, au niseme Mzowea udalali, hawezi kazi ya duka. Mie nakwenda zangu akinihitaji atanitafuta. Asanteni sana na samahani kama nimewakwaza.” Baada yakusema maneno yale Mbuya akasimama akawa yupo tayari kwa kuondoka. “Msafiri kaka yangu, m bembeleze Mbuya asiondoke muyamalize, bahati inaondoka hiyo mdogo wangu, tambua kuwa bahati haiji mara mbili?” Msafiri Namjupa, alimtazama dada yake kwa mshangao kisha akasema kumwambia dada yake. “Dada yangu kama nimeandikiwa niwe masikini, daima siwezi kuwa tajiri. Na kama nimeandikiwa niwe tajiri, naamini nitapata tu. Mie nimekinai umasikini wangu. Pesa zake, mie nitabaki na utu wangu. Mwache ende sina haja nae.” Maneno yale yalimuudhi sana Mbuya akatoka akaenda zake, akaamua amtafute Iddy Teva ili akapumzishe akili yake. Wakili Neema aliaga akenda zake wakabaki wanandugu wawili tu chumbani mle.
“Kaka yangu umerogwa eee? Bahati unaipiga teke hivihivi, Mungu akupe nini kaka yangu, umeniudhi ungekuwa siyo ndugu yangu ningekuwa nishakutimua hapa kwangu, lakini ndiyo hivyo sina jinsi lakini wewe si bure kuna namna.” Msafiri alimshangaa sana dada yake, akamjibu kwa uchungu. “Dada Shuwea, mie nimepigiwa kelele za wizi nyumbani kwao hawa, hivi zingekuwa siku zangu zimefika wale watu wangeniuwa mimi bila hatia, je Mbuya angeishi na mimi, lakini pili Mbuya dini yake na yangu ni tofauti unadhani si ndiyo mambo yakubadilishana dini hayo, yeye na uwezo wao angekubali kubadili dini yake, baba yake tuna uhasama asingekubali lofa mie, tena niliemshinda Mahakamani niwe mkwe wake, tatizo dada yangu hutazami mbali, wewe unatazama hapahapa tu, Mbuya kama nitamshiriki ni matatizo makubwa acha nibaki na umasikini wangu.” Maelezo yale marefu ya Msafiri yalimfanya Dada yake amshangae sana. Walibaki katika hali ile hadi kiza kilipoingia, Shuwea alimuandalia mwanae chakula cha jioni, ugali laini akala, wakalala dada mtu akilala kitandani, na Msafiri akilala kitini, wote wakilala na nguo zao.
***
Wakili Neema asubuhi alikwenda katika kituo cha Polisi Buguruni, ili kufahamu Polisi wamefikia wapi kuhusu wale jamaa, akaonana na mkuu wa Upelelezi pale kituoni, akaambiwa mambo bado, jana waliweka mtego lakini hawakufanikiwa na isitoshe tangu yule mtu jana walipompata katika simu mwenzake akamwita Buguruni Sheli, simu yake hadi muda ule haijapatikana tena. Wakili Neema alifikiri kwa muda kisha akamwambia yule askari Mpelelezi. “Mie niliishika namba ya gari aliyokuwa akiiendesha yule mtu niliemuona akioneshea alama ya kumuua Shuwea namjupa, hivyo ninachoshauri kwa jeshi la Polisi, nisamehe kama nitakuwa ninaingilia kazi zenu. Ninaonelea kwa kuwa namba ya simu mnayo iliyowasiliana na huyu Dereva wa Bodaboda, lakini pia namba ya gari ipo hapo nikutizama namba ya simu imesajiliwa kwa jina gani, lakini pia kupata Print out kutoka katika kampuni ya simu ya laini hiyo, hapo kutawezesha kufahamu kwa kina namba za simu zilizokuwa zikiwasiliana na simu ile mara kwa mara, hasa muda ule baada ya nyie kumpigia simu yule jamaa, kwani kama atakuwa ametambua kwa namna moja au nyingine kukamatwa kwa jamaa yao, lazima watakuwa wamepashana habari, hivyo watu hao aliowasiliana nao muda mfupi baada ya kumpigia simu ndiyo mtahangaika nao, wanaweza kuwafikisha katika mafanikio. Pili kuhusu namba za gari inabidi mwende TRA ili kuangalia mmiliki wa gari namba hiyo ni nani, pia mtapata mawasiliano yake pale, na mtalinganisha jina la mmiliki wa gari na namba ya simu lengwa, mkifikia hapo mtakuwa mmepiga hatua kubwa kabisa na lazima wahalifu wote watiwe mbaroni.” Wakili Neema alikuwa akimshauri Polisi vitu ambavyo ni vya wajibu wa Polisi kuvifanya wakati wakitafuta kuwakamata wahalifu. “Sawa naomba utupatie hiyo namba ya gari ili tuifanyie kazi, pia hiyo gari itabidi isakwe barabarani mote ili nayo ikamatwe kwa upelelezi zaidi.” Mkuu wa Upepelezi wa kituo cha Polisi Buguruni alimwambia Wakili Neema kwa hamasa kubwa. Wakili Neema alichukua kikaratasi kidogo akaiandika ile namba ya gari na kumkabidhi. Wakili Neema faraja aliaga akaondoka akiahidi kupita au kupiga simu jioni kujua kitu kilichoendelea. Kisha akashika njia akenda zake.
Mlango wa Mahabusu ulifunguliwa, akaitwa mahabusu alieingizwa usiku ule jina lake, akatakiwa atoke nje ya lango lile kwani ndugu zake wamekuja kumuwekea dhamana. “Wewe Mahabusu uliefanya fujo kwenye Pool, toka humo ndugu zako wamekuja kukuwekea dhamana, sasa ukafanye tena fujo kisha uletwe tena hapa, lazima tukupeleke jela.” Yule Mahabusu aliitwa katika ofisi za Mkuu wa Upelelezi, akatoka huku akiwa anajinyoosha, akavaa shati lake mwilini mwake, akaongozana na yule askari aliemwita, alipofika ofisini kwa Mkuu wa upelelezi, akapewa chai iliyo kamili akanywa kwa utuo. Kisha baada ya chai ile akaangua kicheko cha taratibu huku akisema. “Daa Mbu wamenikomesha sana, siyo mchezo ila nimefanikiwa kumchunguza yule jamaa kama kawaida, kwani aliniamini kweli kuwa mimi ni mahabusu mwenzake, niliepelekwa mle kwa kufanya fujo kwenye mchezo wa Pool. Hivyo aliniuliza ninapokaa nikamwambia nakaa Tabata, basi yule bwana amenipa namba za simu za jamaa zake ili nikitoka niwajulishe kuwa yeye yupo Polisi na kama alivyomfahamisha jana mwenzao kuwa aje haraka, ikiwa ni ishara ya kukamatwa kwake, sasa amenisisitiza niwasiliane nao hao watu ili wahamishe mizigo. Hii maana yake ni Silaha wanazofanyia uhalifu.” Alisema yule askari alieingizwa mle mahabusu akiambiwa kuwa amefanya fujo lakini kumbe aliingizwa mle kwa kazi maalumu ambayo ameifanya ipasavyo. “Kazi nzuri Koplo, sasa bado utatakiwa urudishwe tena ndani mahabusu, tena ukiwa na simu ambayo tutai divert hiyo namba ili uhakikishe unampa yule jamaa awasiliane na hao jamaa zake, kisha sie tutazitrack namba zote atakazokuwa amewasiliana nazo, na hatimae tutakuwa tumeuwa Tembo kwa ubua. Hizo ndizo mbinu za medali (MM) Baada yakupanga mipango kila kitu kiliwekwa sawa, simu ikawekwa kwenye mfumo wa Divert, akapewa yule bwana akaiweka katika Ashaakum akafunguliwa lile lango la mahabusu akarudishwa ndani mle na mbilinge mbilinge kubwa. “Wewe unataka kutoroka eee, umeambiwa ndugu zako barua haijakamilika hawawezi kuja na barua ya Mjumbe kumdhamini mtu, wanatakiwa barua ya afisa mtendaji kata, sasa wewe unabisha nini?” Askari alimuingiza na makofi yule jamaa ambae ni mwenzao. Mahabusu wote waliokuwa mle ndani walimuhurumia sana kwa zile mbata alizopata. ”Wewe watakuua hao siyo watu wazuri, usibishane nao hao, wewe kuwa mpole tu ndugu yangu, utatoka na ulemavu bure humu.” Mahabusu mmoja aliekuwa amelala katika sakafu ya vigae ya mle mahabusu alimwambia yule mtu alieingizwa mle kituuteeni. “Nimerudi Mshikaji wangu, dhamana yangu imedunda barua wameikosea. Sema imekuwa kheri kwani nimempa askari mmoja pesa hapo, amekubali ndugu yangu anipe simu kwa vile anajua leo hii natoka, na mie nimeichukua simu hii ili kuwasiliana na jamaa wafanye haraka kunitoa, kwa hiyo chonga na wanao basi uwaeleze kila kitu kama wewe upo katika jumba hili, ili waweke sawa mambo kwani siunajua wangu, hii ni kesi usije ukapotea, na unaweza usiipate nafasi hii tena kwani mie jamaa wakirekebisha barua tu nakwenda nje, sina kesi mie nina mashauri tu.” Yule maabusu askari alimwambia yule dereva wa Bodaboda akimchota akili, nae akamshukuru sana yule mahabusu mwenzake kwa kufanikiwa kuingia na simu mle Mahabusu, hivyo aliichukua ile simu akabonyeza namba alizozikusudia, akaipiga ile simu na kuongea na jamaa zake, ndipo alipoingia mazima!
“Oyaaa Nigga, Tafu hapa. Nimefanikiwa kupata simu kutoka kwa mshikaji humu Mahabusu, hii simu ya jamaa yake ameiingiza. Sema nini mie nishalosti wangu, sema jamaa hawajanikamata na chochote zaidi ya simu tu, ikiwa na ujumbe wa Baba Ubaya, aliokuwa akinielekeza kuhusu yule demu wako uliezaa nae kule kwa Mdosi, hivyo wekeni mbali Mizigo kipindi hiki. Mie nakomaa nao najua nikikata nao wiki hakuna kitu, watakuwa tayari tuzungumze biashara basi nitamalizana nao tu. Najua wanakaza wanataka pesa.” Dereva wa Pikipiki aliejitambulisha kwa jina la Tafu, alikuwa akizungumza na Baba yake Faraja, mzazi mwenziwe Shuwea Namjupa. “Dah pole sana mwana nimekuelewa, sasa upo kituo gani?” Niga alimuuliza Tafu. “Nipo kituo cha Buguruni nakomaa nao, walishaniweka kiti moto, wakitaka niwataje nyie na niwalete mlipo, ndipo nilipowaambia nipige simu. Waliponipa simu yangu ili nipige tu nikamwambia Baba Ubaya, ile salamu yetu mtu akiwa kamalizwa.” “Hahahahahahaaaa naona uliwachomesha Mahindi kishenzi, wacha wagande wanamsubiri Baba Ubaya. Sasa baada ya wewe kumwita Baba Ubaya haraka tu, basi alipokujibu kuwa anakuja haraka, akatupigia simu sisi wote hivi sasa keshabadilika katoka kwenye Tigo, kahamia Airtel, kwa hiyo hiyo namba wataitafuta sana wajinga hao.” Nigga alifurahi sana kwa Polisi walivyodanganywa. “Sasa simu yangu wanayo wao, hivyo ujumbe wowote au simu mkiipata kutoka kwenye simu yangu, basi mjue ni wazee hao, mie sitowapigia hadi nikimaliza matatizo nitawajulisha na nyie mtanichekecha mtajua ukweli kama nimetoka, au nawavuta tu.” “Tafu guy, nakuamini mwana shaka hakuna wewe wakazie, kama wakiongea Biashara nambie nitume pesa kwa wakala ili umalizane nao, huna kesi hapo hujakamatwa na kitu chochote hao wanakulegeza tu, utoe pesa nyingi komaa nao mwana.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tafu Guy, alizungumza kwa kirefu na mtu aliekuwa akizungumza nae, ambaye ndiye aliekuwa Baba wa mtoto wa Shuwea. Kitu ambacho walikuwa hawakijui simu ile ilikuwa imewekwa katika Divert kwenye simu ya mkuu wa upelelezi pale kituoni, na mazungumzo yale yalikuwa yakirekodiwa moja kwa moja. Lakini hata baada ya wao kumaliza kuzungumza, simu ya Mkuu wa Upepelezi aina ya Samsung Galax Smartphone kupitia Program ya Mobile Locator, iliweza kuonesha mtu aliekuwa akiongea upande wa pili, alikuwa akizungumzia mahala gani. Hivyo Polisi walijipanga harakaharaka wakabeba zana zao, askari watano wakachukua gari yenye namba za kiraia, wakaingia barabarani kuelekea Tabata Mawezi kwa Nigga, ambapo ndipo aliposomwa kuwa yupo. Walipofika maeneo ya ALHAMZA Buguruni wakiitafuta Tadata Matumbi kulikuwa na foleni ya magari makubwa yaliyokuwa yamejazana katika barabara ile ya Mandela. Hali ile ilipelekea kuchelewesha mwendo kasi ambao walikuwa wakiuhitaji kuwafikisha haraka kwa Niga. “Hii miundo mbinu yetu mibovu sana, sasa foleni hizi hapa kama gari yakuzimia moto imeitwa kwa mfano Tabata Bima, si wataikuta hiyo nyumba imeshateketea yote!” “Wewe unasema gari yakuzimia moto tu, sie tunataka kumuwahi Muhalifu sasa hivi, foleni ndiyo hii, huoni kwamba anaweza kubadilika kutoka eneo moja kwenda eneo linguine tukamkosa? Kwa hiyo Miundo mbinu ni changamoto sana kwa nchi yetu, hasa hii Tabata. Pamoja bado serikali imejitahidi sana kujenga Barabara kwa wiwango cha lami, lakini suluhisho la kudumu kwa Tabata, napo pia kungejengwa njia mbili badala ya moja iliyopo.” Askari Polisi waliokuwa njiani katika Foleni walikuwa wakizungumza kubadilishana mawazo.
Nigga baada ya kukata simu ya Tafu Guy, aliwapigia jamaa zake, kuwafahamisha kuwa ameongea na Tafu, akawaeleza kila kitu walichoongea nae, wakafurahi sana kwa mwenzao kukaza kuwa hadi muda ule alikuwa bado hajawataja. Hivyo wakasema wamsaidie wamchangie pesa ili wakamchomoe katika matatizo yale. Hivyo wakaagana wakutane jioni ile maeneo ya Tabata Segerea chama, katika Bar maarufu inayojaza watu kama wanapewa vinywaji bure, iitwayo kwa Mfojo. Ili wapange na kujadili mambo yao kwa upana.
Wale askari walisogea taratibu, katika foleni ile walipolivuka daraja la Matumbi, dereva wake akaipandisha gari yao katika kituta kinachotenganisha Barabara ile ya magari na ya watembea kwa miguu. Akawa akiiendesha gari ile katika njia ile ya wendao kwa miguu. Kupita kule kuliwasaidia kutembea kwa haraka, walipofika katika kona ya Tabata pale Tabata Dampo, au Tabata Sheli, askari wa usalama barabarani, alisimama mbele yao ili aisimamishe ile gari kwa kupita sehemu isiyoruhusiwa, mara alipoinua mkono wake juu kuisimamisha, Mkuu wa Upelelezi alitoa shingo yake dirishani ili kutaka kumwambia kitu, na yule askari wa usalama barabarani alipomuona Mkuu wa upelelezi, akaushusha mkono wake chini, akawaashiria kupita huku akitabasamu. Wale askari Polisi kitengo cha kupambana na uhalifu wa kutumia silaha, walimsalimia yule Traffic kisha wakaendelea na safari yao. Walipinda kushoto kuelekea Tabata wakiiacha ile Barabara ya Mandela. Walipofika pale katika mzunguko baada ya kuivuka reli, wakapinda kulia wakielekea katika barabara ya chuo cha ualimu cha St Marry, wakiiacha ile barabara yakuelekea Tabata Aroma ambapo kulikuwa na msongamano sana wa magari. Barabara ile walitembea kwa haraka kabla hawajakifikia chuo cha walimu cha St Marry, wakapinda kushoto, walipita eneo maarufu pale Tabata linalojulikana Ubaya ubaya, wakiitafuta barabara ya Tabata Mawenzi. Mara Mkuu wa upelelezi alistuka pale alipokuwapo, hadi wenzake wakamshangaa. Mkuu wa upelelezi haraka aliingiza mkono wake mfukoni akatoa kikaratasi alichopewa na wakili Neema Faraja ofisini kwake, akakiangalia kwa haraka kisha akaigeuza shingo yake nyuma kuitazama gari waliyopishana nayo, kisha kwa haraka akatoa amri kwa dereva. “Geuza gari haraka ifate hiyo gari Tuliyopishana nayo sasa hivi.” “Afande unamtambua kwani huyo muhalifu tunaemfata?” Dedeva wa gari ile alimuuliza kiongozi wake huku akikanyaga breki akaigeuza ile gari nakuanza kuifatilia ile gari iliyokuwa hatua kidogo na pale walipokuwa, lakini ikiwa mbele yao. “Namba za hiyo gari ndiyo mtu aliesababisha safari yetu, huyo ninaamini kuwa ndiyo aliemtuma yule dereva wa Pikipiki amfatilie yule mwanamke huyo ni jambazi na ndiye tuliekuwa tukimsubiri jana pale Buguruni Sheli.” Yule Dereva alivyosikia maneno yale, akaongeza mgandamizo wa kukanyaga mafuta, gari ile ikaongeza kasi kuifata ile gari iliyokuwa mbele yao aina ya Toyota Alteza. “Tunajipanga kwa ambushi, hivyo hiyo gari milango yake itakuwa ipo kwenye Lock hivyo tunamuamrisha afungue mlango, kama akikaidi tunapiga risasi au mzee wa karateka kitengo chako hicho sawa?” “Ndiyo Afande” Askari watatu waliokuwa wamekaa nyuma wakajibu kumwambia kiongozi wao kuwa wamemuelewa. Dereva aliongeza mwendo hadi akawa ameikaribia kabisa gari ile lakini hakuipita, alikuwa akitafuta sehemu nzuri ili aibane nakuwakamata watu wote waliokuwamo mle ndani. Ile gari Toyota Alteza ya rangi ya Zambarau, iliyokuwa na mziki mkubwa , vioo vilivyowekwa kiza chepesi mbele na vioo vya kiza kizito katika vioo vya nyuma, mziki wake ulikuwa umefunguliwa mle ndani. Gari ile ilikuwa imeshafika pale katika makutano ya mzunguko wa Barabara ya kwenda Tabata Aroma na ile walipotokea wao. Ile gari Toyota Alteza ikaelekea Barabara ya Mandela ikiwa imewasha taa ya kuashiria kupinda kushoto kwenda Ubungo. Basi la abiria linalokwenda Tabata Kimanga/ Ubungo lilikuwa limewaziba lipo mbele yao, likisubiri gari kutoka Buguruni zilizokuwa zimeruhusiwa kupita zisimamishwe na askari wa usalama bararani, ili ipinde kuelekea Ubungo. “Hapo kabla hajapinda mpige pini huyo tumalizane nae hapahapa” Mkuu wa Upepelezi alimuamrisha dereva wao huku akijipinda ubavu na kuchomoa bastola kiunoni mwake, akaikoki kabisa kupandisha risasi chemba ili kuwa tayari kwa matumizi. Wale askari waliokuwa nyuma wawili waliinua Bunduki za kivita aina ya SMG wakazikoki huku wakiwa wamezielekeza juu silaha zao. Yule askari mmoja aliekuwa nyuma kati ya wale watatu yeye hakuwa na kitu, kwani yeye alikuwa ni mtu wa mapambano ya mikono aliekuwa na mkanda mweusi katika sanaa ya mapigano ya KARATE kwa jeshi la Polisi. Dereva wa ile gari ndogo ya Polisi aliingiza ile gari yao Sheli kama anaetaka kuweka mafuta, akaizungusha ile gari hadi karibu na ile Toyota Alteza iliyokuwa imeacha mwanya mkubwa akaichomekea kwa pini ambayo dereva wake asingeweza kuchomoa hata kidogo. Yule dereva wa ile gari aliekuwa akijiandaa kuendesha alisimama gafla huku akitukana kwa kupigwa pini ile, lakini kabla hata ajajishauri mara mbili aliona milango mitatu ya gari ile ikifunguliwa na Bunduki kubwa mbili zikitokea milango ya nyuma ya gari ile na bunduki ndogo moja ikitokea mlango wa mbele wa gari ile. Mara zile bunduki kubwa zikakohoa juu hewani, huku yule mtu wa Karate, alikuwa keshafika usawa wa Mlango wa dereva wa gari ile, kwa mkono mmoja tu aliachia pigo moja takatifu kwa kiganja cha mkono wake wa kulia katika kioo cha ubavuni kwa dereva, kioo cha Alteza kikamwaga chenga tupu pale mlangoni na kumwagika chini. Yule askari liingiza mkono akachomoa lock za gari ile, wakafanikiwa kuwadhibiti watu waliokuwa ndani ya gari ile, lakini kwa mshangao mkubwa watu waliokuwamo ndani ya gari ile, walikuwa ni wanawake wawili warembo.
Milio ile ya risasi katika mkusanyiko ule wa watu wengi, pamoja na magari yaliokuwa yapo kwenye foleni, kulisababisha taharuki kubwa kwa watu waliokuwa maeneo yale. Watu walikimbizana hovyo, wakijua Majambazi wanapora Barabarani kweupe. Kwani askari Polisi wale wote walikuwa wamevaa nguo za kiraia, hivyo ilikuwa ni vigumu sana kwa raia kupambanua kama wale ni askari wa ukweli au ndiyo walewale majambalika!
Raia wenye roho ngumu, walianza kurusha mawe kwa wale askari Polisi wakiwadhani ni Majambazi huku wakipiga kelele za wizi, ndipo wale askari wakaanza kuwakimbiza kwa kufyatua risasi juu huku wakiwafata, mchezo huo ulikuwa ukichezwa na wale askari wenye Bunduki aina ya SMG. Askari waliokuwa doria pale kwenye kibanda chao, waliwaona askari wenzao ambao wanawafahamu, hivyo nao haraka wakaongeza nguvu kwa kufyatua risasi hewani sehemu ile, hivyo kufanya eneo lile kuwa la hatari zaidi kwa muda ule. “Tulia hivyohivyo shuka chini mikono juu. Wote shukia mlango huu haraka.” Mkuu wa upelelezi alikuwa yupo kazini mwenyewe hakusubiri taarifa ofisini, aliwaamrisha wale watu waliokuwa mle ndani kwenye ile gari Toyota Alteza. Wale wanawake wawili walishuka chini huku wakiwa wanatetemeka sana kwani, kitendo kile kiliwashitua sana, presha ikawapanda woga ukawashika wakashuka kwa haraka huku wenyewe kabla hawajaambiwa kukaa chini, walikaa kitako kwani hawakuwa na nguvu za kusimama pozi ziliwaishia kabisa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wale askari wenye SMG walifanikiwa kuwakimbiza watu, utulivu ukapatikana hasa baada ya raia kuwaona askari watatu waliokuwa wamevaa sare za Polisi waliokuwa doria pale kwenye kona ile muhimu, wakiwa sanjari na wenzao katika kuwadhibiti watu waliokuwamo kwenye gari ile. Hakika ilitumika nguvu kubwa sana kuliko hata uwezo wa watu waliotarajia kupambana nao. Ile gari ya polisi ilikuwa bado imekaa vilevile ikiwa imeibana ile Toyota Alteza. “Ingia mle haraka tunakwenda kituoni.” Mkuu wa upelelezi aliwaamrisha wale wanawake wawili waliokuwa kwenye gari ile, nao kwa woga mkubwa waliingia katika gari ile ya Polisi yenye namba za kiraia iliyokuwa bado milango yake ipo wazi. Mkuu wa Upelelezi alilipekua lile gari, kwa haraka akapekua na begi ndogo za mikononi za wale wadada, akaziona simu mbili tofauti akazichukua na kukaa nazo mfukoni kwake. Zile ‘hand bag’ alizichukua akawarushia wenyewe mle kwenye gari waliyokuwepo kisha akawaambia. “Simu zenu ninazo nitawapa baada ya upelelezi.” Baada yakusema maneno yale, akawaita askari wale wawili waliokuwa na bunduki kubwa mikononi mwao, ili waondoke eneo lile, kwani wanakazi yakufanya kituoni muda ule na wale watu. Askari wale walipanda mmoja mbele na mwengine nyuma, kisha mkuu wa Upelelezi alipanda katika Toyota Alteza, na yule mzee ka karateka akakaa katika usukani wa gari ile Alteza safari ya kwenda kituoni ilianza. “Hawa tunakwenda nao Sitaki shari moja kwa moja tusiende nao Buguruni.” Mkuu wa Upelelezi aliwaambia wale askari waliokuwa mbele, gari ile ikawekwa sawa kutoka katika ule mkao wa kuibana ile Alteza, Traffic akayazuia magari mengine akaziruhusu zile gari kuingia katika barabara ile ya Mandela. Ikashika njia kuelekea kituo cha polisi Sitaki Shari.
Baada ya muda hali ya amani ikarejea katika eneo lile, shughuli zikaendelea kama kawaida, kama hakukutokea tukio lolote. Ingawa mabaki ya vioo vilivyokuwa chenga chenga vilizagaa pale chini ilipokuwa ile Toyota Alteza awali.
***
Baba Ubaya wakati tukio la kukamatwa mke wake akiwa na gari yake linatokea, yeye alikuwa yupo katika gari nyingine ya rafiki yake, Tabata Sheli wakiweka mafuta. Hivyo waliposikia milio ya risasi walihisi wao ndiyo waliolengwa hivyo waligeuka nyuma kutazama kule waliposikia milio ya risasi ikitokea, akaishuhudia gari yake, ikiwa imebanwa na gari nyingine ndogo, na watu wenye silaha wakiwa wameizingira gari ile. Wao walidhani labda ni Majambazi wanataka kuiba gari ile, walipowatazama vyema wakagundua kuwa ni askari Polisi, hasa baada yakuwaona askari wenye sare wakiwa wameongeza nguvu eneo lile. Walinzi wa kituo cha mafuta walikuwa wameshasimama na Bunduki zao wakidhani wamevamiwa na majambazi. Ili mradi kila muhusika pale alikuwa amerushwa roho yake kwa risasi zile. Muweka mafuta alipomaliza kuwawekea mafuta, alilipwa pesa yake haraka hawakusubiri chenji, waliiondoa gari yao eneo lile wakashika Barabara ya Mandela kuelekea Ubungo. Baba Ubaya alikuwa amechanganyikiwa sana alitoa simu yake akaanza kuwapa taarifa wenzake. “Oya Nigga mke wangu kamalizwa na wazee mbele ya macho yangu mshikaji wangu. Yaani yule demu mbishi sijapata kuona mie nilimkataza kabisa kuendesha ile gari siku mbili tatu hizi, nikamwambia atumie ile Vitz yake lakini wapi mshikaji wangu. Yaani kanisubiri mie nimetoka na Sirengo na gari yake, yeye kaichukua ile gari kampitia dada yake sijui walikuwa wanakwenda wapi, yaani kayazua Majanga kwa ubishi wake. Sasa kuweni makini sana kwani akichapwa makofi mawili tu yule, analeta mpira. Yaani dah kazingua sana yaani amenifanya nipagawe sana.” Baba ubaya alikuwa akiongea kwa hasira na uchungu mkubwa sana. “Daah?! Pole sana mtu wangu, ama kweli mkeo kayazua mshikaji wangu du? Yaani hatujamaliza la Tafu tayari lishakuja lingine, au Tafu ameshindwa kukaza, kaamua alengeshe?” Nigga alimuuliza rafiki yake Baba ubaya, akiwa amechanganyikiwa vibaya sana. “Hamna Tafu angekuwepo ningemuona kwani nakwambia picha limechezeka mbele ya macho yangu, yule demu alivyokuwa na mapepe kama angetazama macho yake, kwenye kituo cha mafuta mbona angenilengesha? Sema kama zali tu Mungu kamfumba macho yake hakutazama kule nilipokuwa. Tafu hakuwapo kabisa naona wale walikuwa na namba ya gari, wakawa wametega pale Tabata.” Baba ubaya alizidi kumuwasha rafiki yake.
***
Katika kituo cha Polisi Sitaki Shari, Mke wa Baba Ubaya na dada yake walibanwa kisawasawa na askari wale, waliochanganyika na wa kituo kile cha Sitaki Shari, katika ile kufinya ili kujua ukweli kwa mtuhumiwa kama anajua au laa. wanawake wale walikuwa hawana kaba. Lakini pia kifinyo kilikuwa si chakawaida kwao, wakashindwa kustahamili. Mke wa Baba Ubaya alianza kutapika maneno yaliyowafanya wale askari watizamane!
“Msiniuwe jamani, nitasema kweli kila ninachokijua.” Mke wa Baba Ubaya alikuwa yupo hoi sana machozi, na mafua mepesi vyote vilikuwa vikimtoka kwa pamoja. Urembo wake ulifubaa, uso ulimuwiva sana nywele zake zilitimka kwani nazo zilitumika katika kumfanya atoe ushirikiano. “Sasa ulikuwa unakaidi nini, wewe kubali tu mambo yashaharibika kubali yaishe. Haya sasa tuambie unajua kwamba mumeo ni Jambazi?” Askari Mkuu wa upelelezi wa kituo cha Buguruni alimuhoji Mke wa Baba Ubaya. “Mie sikuwa najua kama Jambazi, ila sasa nishajua kwani mara kwa mara huja na wenzake kuja kugawania pesa zao nyumbani, huwa ni pesa nyingi sana.” Majibu yale yaliwafanya askari wale watizamane, huku wakitikisa vichwa vyao kukubaliana kuwa sawa sawa. “Wanapogawana hizo pesa hapo kwako, huwa wanakwambia wapi walipozipata, au kazi waliyoifanya hadi kupewa mamilioni ya fedha?!” Mkuu wa kituo alikuwa akihoji, askari wawili walikuwa wakiandika mahojiano yale. Kitu ambacho mke wa Baba Ubaya alikuwa akifahamu ni kwamba maelezo yake yalikuwa yakirekodiwa moja kwa moja, kwa ajili ya ushahidi na utendaji wa kazi zaidi. “Wanapokuja na pesa zao, mie huwa hawaniruhusu kukaa nao, bali huingia chumbani au nikawa jikoni kisha wakishamaliza mgao, ndiyo mume wangu hunita na kunikabidhi pesa niweke. Siku moja alinipa pesa nyingi sana hadi Dola za Kimarekani nikamuuliza alipozipata, akanijibu mjini watu wanaishi kwa mipango.” Baada yakujibu swali na kueleza mke wa Baba Ubaya, alitupiwa swali lingine la haraka. “Hizo Dola na pesa nyingi alizokuja nazo, ilikuwa ni siku za hivi karibuni?” Mke wa Baba Ubaya alikaa vizuri kisha akasema. “Pesa zile ilikuwa ni kama miaka miwili iliyopita, kisha kwa vile hawakuwa wengi kama siku zingine wanavyokuwa, siku ile kila mmoja alipata mgao wa pesa za Tanzania Milioni thamanini tasilimu, na dola elfu Arubaini kila mmoja. Lakini hakuna tena mgao mkubwa zaidi ya ule kwa siku za karibuni kwani huja wakagawana milioni tatutatu, wakizidi sana Milioni nne” Askari mmoja aliandika kikaratasi kisha akampa Mkuu wa Upelelezi wa kituo cha Buguruni. Nae alikisoma kikaratasi kile kisha akamkabili mke wa Baba Ubaya akamuuliza. “Kama ulikuwa ukipewa pesa uweke, tunayo taarifa pia kuwa na Bunduki ulikuwa ukiweka wewe nyumbani kwako si ndiyo?” Mke wa Baba Ubaya, akajibu kwa sauti ya chini kidogo. “Mie huwa naweka ile ndogo ya mume wangu, zile kubwa huwa wakiondoka nazo wenyewe, anakuwa nazo Nigga.” Mkuu wa upelelezi wa kituo cha buguruni akamtupia swali lingine.“Wewe kwa Nigga unapajua?” mke wa Baba Ubaya alimeza mate ya uchungu kisha akajibu. “Mimi sipajui kwa Nigga, ila Tafu na mume wangu wanaweza kuwa wanapajua.” Jina Tafu, lilim rudisha nyuma mkuu wa upelelezi wa kituo cha Buguruni, akamuuliza mke wa Baba Ubaya kwa shauku kubwa. “Wewe unajua Tafu sasa hivi yupo wapi?” Mke wa Baba Ubaya akamjibu kwa kichwa kuashiria kuwa anajua, akaulizwa aseme alipo, nae akajibu. “Tafu tangu jana amekamatwa na yupo kituo cha Polisi Buguruni.” Wale askari waliokuwapo pale chini ya Muembe Sitaki Shari, walitazamana kwa mara nyingine tena. Askari mmoja aliandika kikaratasi kingine haraka akampa kiongozi wao, nae akakisoma kisha akamuuliza mke wa Baba Ubaya. “Wewe umejuaje kama amekamatwa, na yupo kituo cha Buguruni?” Mke wa baba Ubaya alichoshwa na maswali lakini hakuwa na jinsi kwani pale alikuwa chini ya ulinzi halali wa Polisi na ushirikiano ndiyo uliokuwa ukihitajika, na si vinginevyo. “Mie amenambia mume wangu, kuwa ameongea nae kwa simu akiwa na Polisi, kwa ishara zao wanazozijua, amemtambulisha kuwa amekamatwa, kuhusu kuwa kituo cha Polisi Buguruni, leo ameongea na simu akiwa yupo Mahabusu amezungumza na Nigga, akamfahamisha kuwa yupo Buguruni, Nigga baada yakuzungumza nae, ndiyo akampigia mume wangu kumwambia, na mume wangu akaniambia kuwa mwenzao yupo Buguruni.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Askari wale walimuhoji kwa muda mrefu sana, akatoa faida nyingi sana kwao, wakawa wamepata mambo mengi hata ambayo hawakuyatarajia. Kwani mke wa Baba Ubaya, aliropokwa kama kanywa maji ya chooni. Aliwataja kwa majina, watu wote aliokuwa akiwaona wakishirikiana na mumewe katika kufanya uhalifu, alieleza sehemu walizoiba kama alivyoelezwa na mume wake, na wapi zilipo silaha. Askari wale wakaona hawana jipya kutoka kwa mwanamke yule, kwani keshatoa faida nyingi sana, hivyo nguvu zikahamishiwa kwa Tafu. Yeye akapelekwa mahabusu pamoja na dada yake ambae hakuwa akijua chochote katika kadhia ile. Askari waliagizwa na mkuu wa upelelezi wampeleke Tafu pale Muembeni ili akae kwenye kiti moto, ili wavune taarifa ambazo zitawapelekea kuuvunja mtandao wote ule wa wizi. Hivyo askari wawili walitoka na gari wakaelekea kituo cha Polisi cha Buguruni kumfata Tafu Guy.
***
ITAENDELEA
Simulizi : Mpita Njia
Sehemu Ya Nne (4)
Katika kituo cha polisi Buguruni, Tafu alikuwa amejenga urafiki sana na yule mtu aliempa simu mle mahabusu, kwani walikaa pamoja na kuzungumza mengi tu. Mara mlango wa Mahabusu ulifunguliwa, askari mmoja akamtaka Dereva wa Pikipiki, atoke nje. Tafu alichomoka nje akafungwa pingu za mikono kwa nyuma, kisha akaongozana na askari wawili hadi kwenye gari yao akapakiwa ndani ya gari ile, akapelekwa katika kituo cha Sitaki shari kwa mahojiano zaidi. Tafu akiwa ndani ya gari. Alikuwa mpole sana kiasi unaweza kudiriki kusema kuwa Tafu ameonewa, wala hashiriki vitendo vya kihalifu. Kumbe habithi kama yeye hakuna. Ama kweli siku za mwizi ni arubaini.
Tafu alifikishiwa Muembeni moja wa moja, akawakuta watu wa kazi wanamsubiri. Aliwekwa kwenye kiti wanaume wakamzunguka wakaanza nae mahojiano. “Tafu tuambie ukweli, wewe tunajua umetumwa tu kuwafatilia wale watu, kisha ungelipwa ujira wako, je huyo aliekutuma anafanya kazi gani?” Tafu alidanganywa akichotwa akili zake waone atapindisha maelezo au atakubaliana nao. “Wazee kwa kusema ukweli mie yule mtu, huwa ananitumia tu kama kunituma au kumpakia kumpeleka katika mihangaiko yake, ila anafanya kazi gani kwa kweli sijui kabisa.” Wale askari walitazamana tena kwa siku ile ikiwa ni mara ya tatu. Walitizamana hasa kwa kutambua Tafu, anapindisha maelezo yake. “Ohoo sawa bwana, je unamfahamu Nigga?” Mkuu wa upelelezi aliendelea kumchecheza kwa maswali, ili kutambua kama anaongea ukweli au anadanganya. “Nigga wazee, mie simtambui kwanza hilo jina kwangu geni ndiyo leo nalisikia masikioni mwangu.” Wale askari walipandwa na hasira wakataka kumshushia kipondo cha Mbwa mwizi, laini mkuu wa upelelezi aliwazuia kwa ishara kuwa bado mapema sana, watulie kwanza kisha yeye akaendelea kumuhoji yule dereva. “Umesema Nigga humjui, je mtu anaeitwa Baba Ubaya unamfahamu?” mkuu wa upelelezi alipomuuliza swali lile alimtazama usoni moja kwa moja. Nigga aliwajibu askari wale kuwa hamfahamu. “Kwa hiyo hata mkewe Nigga wewe humtambui?” Mkuu wa upelelezi alimsaili kwa utulivu hatua kwa hatua na alishamuona kuwa anawadanganya. “Sasa wazee kama mtu mwenyewe simtambui, nawezaje kumtambua mke wake?” Mkuu wa upelelezi aligeuka akamtazama askari aliekuwa yupo makini, akampa ishara ya kichwa, yule bwana akapiga saluti, akatoka pale kwenye mwembe, baada ya dakika kama nne hivi akarudi pale akiwa na mke wa Baba Ubaya. Mkuu wa upelelezi akamuuliza Tafu; “Unamfahamu huyu mwanamke?” Tafu alimtazama mwanamke yule kisha akamkataa kuwa hamfahamu. Mkuu wa upelelezi alimgeukia mke wa Baba Ubaya akamuuliza. “Wewe unamjua huyu?” Mke wa baba ubaya akajibu kwa uchungu huku machozi yanamtoa. “Ndiyo namjua huyo ndiyo Tafu wazee, yeye huyo ndiyo anajua silaha zilipo.” Tafu alihamaki akamtolea macho yule Mke wa Baba Ubaya. “Wewe unanifahamu mimi, au unanitafutia matatizo tu, waambie ukweli wazee siyo unataka kuongopa ili unipe mie matatizo yako.” Tafu aliendelea kumkataa mke wa Baba Ubaya kuwa hamfahamu, ilihali kila askari aliekua pale alikuwa akitambua kuwa wanafahamiana.“Tafu umeweza kutudanganya jana ila huwezi tena kutudanganya na leo. Mjinga pa kwenda tu, pakurudi anajua pabaya na pazuri. Jana ulifanikiwa kuwatorosha wahalifu wenzako, lakini tambua kuwa sisi ni Serikali, na siku zote serikali ina mkono mrefu. Leo utatuambia kila kitu wewe, au utaondoka hapa ukiwa maiti, kwani hatujawahi kuja na mtu hapa ambae tunauhakika kwa asilimia zote kuwa ni muhalifu, tukamuhoji hapa kisha akaendelea kukataa, ukifanikiwa kukaza hadi mwisho usiseme basi wewe utakuwa ndiyo mtu wa kwanza. Sasa utani tunaweka pembeni, tunataka bunduki zetu.” Mkuu wa upelelezi aliposema maneno yale, akaamrisha vijana wa kazi, kutoa kipondo kwa Tafu. Askari wale wakiwa na mafunzo maalum ya kumtesa mtu, waliweza kutoa dozi yao, ikawa ndani ya dakika tano, Tafu hatizamiki kachakaa sana. Ila bado alikuwa anaendelea kukaza tu, kwani aliona bora kifo kwake kuliko kuwataja wenzake kisha ikawa kesi ambyo yeye ndiyo atakuwa ameifanya inyooke. Akaona atakwenda kufia jela akiwa kwenye mateso makali. Hivyo aliendelea kukomaa kuwa hamjui mtu yoyote kati ya wale aliotajiwa, lakini pia alimkana hata mke wa Baba Ubaya ambae ameshakaa nae sana, akiwa anamfahamu kwa makoko na matandu.
***
Baba Ubaya alimwambia rafiki yake Sirengo ampeleke nyumbani kwake, kwani kuna vitu vingi sana ambavyo hana risiti navyo vya wizi, pamoja silaha anayoimiliki kinyume cha sheria, akavihamishe kwani anatambua kuwa askari wale baada ya mahojiano na mke wake, lazima watakwenda kupekua nyumbani kwake, hivyo akaona muda ule ambao kabla hawajafika utakuwa ndiyo muda muafaka wa kwenda kuhamisha ‘mazibo’ Sirengo akamshauri achukue gari kubwa ili ahamishe vitu vyote vya nyumba nzima, ili ahame kabisa katika nyumba ile, lakini Baba Ubaya akamwambia wakaondoshe ‘Mazibo’ yaani vile vitu visivyokuwa na risiti tu, kwani vinawezwa kupelekwa Mahakamani kisha vikawa vielelezo muhimu wakaitwa walioibiwa wakenda kuvitambua vitu vyao, hiyo itakuwa ni kesi iliyosimama isiyokua na chembe ya shaka kabisa ndani yake. Baba Ubaya alimpigia simu Nigga kumfahamisha lengo lake la kwenda kuchukua vitu vyake kwake, lakini Nigga alimshauri vinginevyo kwenye simu. “Baba Ubaya watafute watu wakahamishe vitu vyote usiende wewe mwenyewe, kwani huwezi kujua wangu, unaweza kufikiri askari watakuja usiku kisha wakaja mchana wakakukuta upo, utajuta majuto makubwa sana wangu, bora kama vipi tuma watu tu.” Baba Ubaya alisikiliza ule ushauri wa watu wawili wote wakimtaka kuhamisha vitu vyote, lakini akaamua kushuka ndani ya gari ya rafiki yake, ili akijifanya kutafuta roli la kwenda kupakia mizigo yote. Baba Ubaya badala yake alichukua Taxi akaamua akaondoshe vitu vya thamani kubwa ambavyo alivipata katika wizi. Lakini asingeweza kumuagiza mtu akondoshe silaha ya moto ambayo ni Bastola. Angekuwa anazidi kujipalia makaa kwa jamii, kuwa yeye ni muhalifu.
Baba Ubaya alikwenda na taxi hadi nyumbani kwake akafungua geti na kumtaka derevawa wa taxi kuiingiza ndani gari ile, kisha akafunga geti kwa ndani baada ya gari ile kuingizwa ndani, yeye aliingia ndani ya nyumba yake akaingia kila sehemu kulipokuwa na vitu vya wizi alivitoa akaviingiza katika gari ile kwa haraka haraka, ili kupoteza ushahidi wa vitu vile vya haramu. Akaenda chumbani kwake akainua sofa dogo chini yake akatoa Bastola aina ya Chinese inayobeba risasi nane, akaivaa kiunoni mwake. Pia akachukua na risasi zilizokuwa katika boxi lake dogo, akiwa katika haraka haraka mara box lile likaanguka risasi zikasambaa pale sebuleni. Akawa akiziokota huku akiona zinamchelewesha mara akasikia muungurumo wa gari ukielekea nyumbani kwake kwenye geti lake akaacha kuokota akapagawa mara mbili ya mwanzoni. Mapigo ya moyo yakawa yanamuenda mbio kama saa mbovu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
***
Tafu Guy alikuwa hoi bin taabani kwa kichapo, akawa amelewa asijue kitu gani sahihi afanye aidha awaambie ukweli wazee au laa. Uso wake ulikuwa umemvimba sana,damu zilikuwa zikimmwagika kinywani mwake. Mara akasikia sauti isiyokuwa ngeni masikioni mwake ikimwita kwa kejeli na kumwambia. “Tafu Guy huna kitu utakachokificha rafiki yangu, sana sana utaumia tu bure kwani kila kitu kipo wazi kabisa. Nyoosha maelezo hayo wangu huna pakutokea katika hili.” Tafu kwa macho yaliyovimba aliuinua uso wake kwa shida, akamuona mtu ambae sura yake pia haikuwa ngeni machoni mwake. Ila kilichomfanya akaze macho zaidi kumtazama kwa makini, ni pale alipomuona yule bwana aliemwambia maneno yale akiwa amevaa sare za jeshi la Polisi na mkononi mwake ana cheo cha Koplo.
Tafu Guy alimtazama vizuri mtu yule moyo wake ukaingia ganzi isiyosemeka, kwani alikuwa ni yule mtu aliempa simu wakiwa mahabusu kule kituo cha Polisi cha Buguruni.
Tafu Guy alifedheheka sana, alikuwa mdogo kama nukta. Uso wake aliuelekeza chini kwa aibu, akawa hana budi ila kukubali matokeo, akawa mtiifu katika ule msemo usemao, kubali yaishe. Tafu Guy akakubali matokeo, akanyoosha maelezo akiwa ameshaumia, kwani hakuwa tena na namna ya kukwepea. Ama kweli ujinga donga la kichwa mkaguzi mkono.
Mkuu wa upelelezi alishauri muda uleule waende nyumbani kwa Baba Ubaya, kwani katika Maelezo yake Tafu Guy, alimtupia mpira Baba Ubaya kuwa ndiyo mwenye silaha. Hivyo mkuu wa upelelezi akaamua haraka waende wakapekue kabla hakujahamishwa silaha ikiwa kweli zimo ndani ya nyumba ile. Hivyo dakika kumi baadae wakawa na kila kitu muhimu kilichohitajika katika safari ile, hati ya upekuzi, askari wa kazi, silaha na Mke wa Baba Ubaya wakawa nae njiani kuelekea nyumbani kwa Baba Ubaya. Wakiwa katika magari mawili ya Polisi yenye namba za Kiraia, Kwenda kupekua nyumbani kwa Baba Ubaya. Walipofika Tabata nyumbani kwa Baba Ubaya gari zilikwenda moja kwa moja hadi katika geti lakuingilia magari. Askari Polisi walishuka katika magari yao wakaizingira ile nyumba kila pembe wakawa wapo makini kwa kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Mkuu wa upelelezi na mke wa Baba Ubaya, walikwenda pamoja kwa mjumbewa shina wa mtaa ule,ili akawe shahidi katika upekuzi walioukusudia. Walipofika kwa mjumbe askari mkuu wa upelelezi, akajitambulisha kwa mjumbe yule dhumuni lao la kwenda pale, mjumbe akaongozana nao hadi katika nyumba ya Baba Ubaya, walipofika pale wakalikuta geti kubwa limefungwa huku alama za matairi ya gari zikionekana kwa wazi kabisa pale chini ya ardhi usawa wa geti lile.
Mkuu wa Upelelezi aliwaamuru vijana wake wa kazi, kufanya kazi. Naam ilikuwa kama watu waliokuwa wakisubiri amri tu. Askari watatu shupavu waliparamia ukuta wa numba ile kwa tahadhali kubwa. Walipofika juu ya ukuta wakaweka pozi pale juu, kisha kila mmoja alichomoa silaha yake kiunoni mwake. Tendo lakuchomoa silaha lilikuwa likifanyika pamoja na kimya kimya bila kuzungumza neno. Kisha mmoja wa askari wale alihesabu kwa vidole kuwaoneshea wenzake, moja, mbili, tatu. Askari wale waliruka kwa mtindo wa Sarakasi wakabimbilika walipofika chini, kisha kila mmoja akawa amepiga goti moja chini, Bastola zao zikiwa mbele mikononi mwao, wakizielekeza huku na kule, kwa namna ya kumtafuta adui alipo, lakini hakukuwa na rabsha yoyote. Askari wale mmoja alifungua Geti dogo kwa ndani, ili kuruhusu wenzao pamoja na Mke wa Baba Ubaya na Mjumbe, kuingia ndani mle kwa shughuli waliyoikusudia. Nao wakajichoma ndani mle pale uwani, askari wakaizunguka ile nyumba huku umakini ukichukua nafasi kubwa zaidi.
Nyumba ile ilikuwa ipo kimya sana, hakukuwa na dalili ya mtu ndani yake. Kwenye uwa ule mpana wa nyumba ile kulikuwa na gari moja ndogo aina ya Toyota Vitz, ikiwa Imeegeshwa. Askari wale baada yakuingia pale uwani, wakamuuliza Mke wa Baba Ubaya kama anao funguo ya kufungulia mlango mkubwa wakuingilia ndani ya nyumba ile. Mke wa baba Ubaya akasema hana funguo pale alipo, funguo zilikuwa kwenye pochi yake iliyokuwa imebaki polisi. Mkuu wa Upelelezi wa kituo cha Buguruni akawaamuru askari wale kuuvunja ule mlango. “Mjumbe sheria inaturuhusu kama nyumba tunaitilia mashaka kuwa ina vitu vya hatari, basi sheria inaturuhusu kuvunja mlango ili kutoa vitu hivyo, kwa hiyo humu ndani tunamashaka kuwa na vitu vwa hatari kwa maana ya silaha. Tunatimiza wajibu wetu tuliopewa na sheria.” Baada yakusema maneno yale mkuu wa upelelezi akawaamuru vijana wake wauvunje mlango wa nyumba ile ili waweze kuingia ndani kwa ukaguzi. Vijana walikwenda kwenye gari yao nje wakarudi na shoka mbili kwa ajili ya kufanyia kazi ile.
***
Baba Ubaya aliposikia mlio wa gari ukielekea katika geti lake, jasho lilimtoka, woga ulimtawala sana. Akasogea dirishani huku akiikoki Bastola yake ili kuitumia. Akachungulia nje kwenye geti lake, akaiona gari ya jirani yake ikigeuza karibu na geti lake. Moyo wake uliokuwa ukipiga kwa kasi ukapoa, akashusha pumnzi ndefu, kisha haraka haraka nguvu zikamrejea mwilini mwake, akazirejea zile Risasi akajitahidi kuziokota moja baada ya moja kwani zilikuwa zimesambaa chini pale sebuleni kwake. Akiwa anaziokota zile Risasi, nafsi yake ikawa inamuenda mbio huku akisikia nguvu nyingine asiyoifahamu ikimuongoza kuondoka haraka mahala pale. Baba Ubaya hakusubiri tena, kuendelea kupoteza muda kwa kuziokota zile Risasi, aliziacha zile Risasi pale chini alizokuwa hajaziokota, Bastola yake akaifunga usalama wake ili katika mashimbo na mitikisiko isiifyatue ile Risasi iliyokuwa tayari ameshaivuta chemba ikisubiri kutolewa kuelekezwa sehemu lengwa. Kisha akaisweka nyuma ya kiuno chake kisha shati lake akawa hakulichomekea ili kuzuia kuonekana kwa silaha ile na dereva wa taxi au mtu mwengine yeyote awae. Kisha akachomoka mbio hadi uwani. Akaufunga mlango mkubwa wa uwani kwa funguo akamwambia dereva awashe gari kisha yeye akalifungua geti lile, dereva Taxi akatoa gari nje ya geti lile. Baba Ubaya alilifunga lile geti kwa funguo kisha akaingia kwenye gari ile akamuamuru dereva wake aendeshe gari waelekee Tabata Segerea. Dereva akaiondosha gari ile kwa mwendo wa taratibu akaelekea Tabata Segerea. Wao wakiwa wamefika Tabata Bima wakipinda kulia kwenda Tabata Segerea wakitokea njia ya Tabata Mawenzi, askari wakafika nyumbani kwake wakiwa wapo kamili gado. Wakipishana kwa takribani dakika tato tu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
***
Shuwea Namjupa, alikuwa akimnywesha uji, mwanawe lakini donge lilikuwa limemjaa rohoni mwake kwa kiasi kikubwa sana. Msafiri Namjupa, alikuwa amejilaza kitini akitafakari kwa kina maisha yake na matukio yaliyomkuta. “Dada mie naonelea nirudi nyumbani Lindi, kwani kazi iliyonifanya niwe katika mji huu, imeshatimia. Nilikuja kukuhangaikia dada yangu ili utoke gerezani, nashukuru Mungu sasa hivi upo nje ukiwa huru. Hivyo inanibidi mie sasa kurejea nyumbani kisha nina mpango wa kwenda Tunduru kusaka bahati yangu, nafikiria kwenda kuchimba Madini. Pengine Mungu anaweza kunipa huko kwani mji huu, nitaishia kupata pesa ya kula.” Msafiri Namjupa alikuwa akimwambia dada yake aliekuwa amemuona hana raha tangu jana yake walipokuwa wakishindana juu ya Mbuya Fabiola. “Mdogo wangu unajitafutia matatizo tu ya bure, kwani bahati Mungu hakupi mara mbili, ameshakupa ya Mbuya umeipiga teke basi huko utakwenda kufa tu.” Shuwea alimjibu mdogo wake huku akiwa amenuna kwelikweli, kwani alimuona mdogo wake ni punguani kwa bahati aliyoipata kisha akaichezea akaukumbuka ule msemo usemao, asiekuwa na bahati, habahatiki. “Dada yangu mie sipo kama utakavyo wewe, najua umeninunia kwa mie kukataa kukubali matakwa ya Mbuya, lakini dada yangu kila likuepukalo basi lina kheri na wewe.” Msafiri alimwambia dada yake huku akiinuka pale kitini na kukaa kitako. “Kaka yangu tupo wawili tu, maisha yetu niya dhiki, mie nina mtoto mdogo siwezi kuishi na mtoto huyu peke yangu bila ya kazi wala msaada kutoka kwa mtu mwengine. Hivyo kama kaka yangu ungekuwa na Mbuya, hata kama ungekuwa huna mapenzi nae ya dhati, Ila ungezuga nae tu tukala pesa zake mambo yetu yakatunyookea, tungebadilika kimaisha kuliko udhalili huu tulionao. Kodi ya nyumba pia inatushinda, kula yetu ya mashaka, hivi asingekuwa Mbuya sie tungekuwa wageni wa nani katika mji huu?” Shuwea Namjupa alizungumza kwa uchungu mkubwa sana, akiangalia maisha halisi wanayoishi ni maisha ya kimasikini sana. Alivyokuwa jela japokuwa alikuwa ni Mfungwa, lakini kila siku ya Mungu alikuwa haumizi kichwa kuhusu kula, japokuwa chakula kile hakikuwa na ladha kama chakula cha uraiani, lakini alikuwa akikipata. Kwani lilikuwa ni jukumu la Serikali kuhakikisha wafungwa wanakula kila siku ya Mungu, ijapokuwa walikuwa wakila mlo mmoja tu kwa siku, hadi kesho yake baada ya asubuhi kunywa uji, lakini alikwisha yazowea maisha yale. Kwani miaka miwili inatosha kumfanya mtu kuyazowea mazingira aliyopo. Shuwea aliona maisha ya kujitafutia tena na mtoto mdogo ambae ana mahitaji anayoyataka, hakika yalimsumbua sana. Akamuomba Mungu awabadilishie maisha. Msafiri Namjupa aliinuka akenda kuchukua kopo la maji na mswaki wake mkononi, akatoka nje ili kukwepa maneno yaliyokuwa yakimuumiza sana moyo wake kutoka kwa dada yake. Hakika moyo wake ulikuwa umekufa ganzi kwa Mbuya Fabiola.
***
Mbuya Fabiola alikuwa amekaa akiwa na Iddy Teva, katika mgahawa mmoja ila hakuwa na raha moyoni mwake, afya na muonekano wa Iddy Teva hakuufurahia hata kidogo, alimtazama kwa makini kisha akamuuliza kwa utulivu. “Iddy nakuona siha yako haipo vizuri, kwani kabla hujenda jela hukuwa hivi, ulikuwa na siha njema lakini sasa nakuona upo dhaifu, vipele tele mwilini mwako, ngozi yako imejaa harara, nywele zako zimebadilika zinakuwa za shombe, vipi kulikoni?” Iddy Teva, alishushia funda la juice kinywani mwake kisha akashusha pumzi ndefu akamwambia. “Mbuya, nitakwambia ukweli wangu. Nikiwa jela nilikuwa nakula vyakula ambavyo havina virutubisho, hivyo afya yangu ikayumba sana, nilikuwa naumwaumwa mara kwa mara, jamaa wakanambia kuwa ni kwa sababu ya vyakula. Ila nilipokwenda kupima afya niligundulika nimeathirika naishi na virusi vya Ukimwi.” Mbuya Fabiola juice ilimpalia, akakohoa sana aliposikia maneno yale, mwili wake ukaanza kumtoka jasho jingi, presha ikaanza kumpanda. “Iddy umesema umefanyaje?!” Mbuya alimuuliza swali lile kama hakusikia namna Iddy Teva alivyoeleza awali. “Mbuya huu siyo wakati wakuficha maradhi, huu ni wakati wakujitambua. Usikubali kuendelea kukaa kigani njoo kwenye mwangaza uonekane ili usaidiwe. Mie nimepima virusi vya Ukimwi nimekutwa ni Muathirika, hivyo lazima nikwambie na wewe ukapime afya yako, pengine unaweza ukakutwa mzima.” Mbuya Fabiola alishusha pumzi nzito, kisha akashika mikono yake kichwani, midomo yake mate yalimkauka akawa anapitisha ulimi wake ili kuupa mate. Aliinua uso wake akamtazama Iddy Teva kama ndiyo anamuona mara ya kwanza siku ile. Hakika Mbuya alichanganyikiwa sana. Hakuwa na amani katika nafsi yake. Machozi yalimtoka bila kujitambua, alitingisha kichwa chake kushoto kulia kwa masikitiko makuu. Mbuya hakutaka kukaa tena pale, alichanganyikiwa sana aliinuka akaondoka sehemu ile huku akifuta machozi, akamuacha Iddy Teva amekaa ameshangaa. Iddy Teva aliinuka pale alipokuwa amekaa akamfata Mbuya, akawa anamwambia kwa upole. “Mbuya huna sababu yakulia njia nzima. Using’atwe na Mbwa ukatangaza kidonga. Twende tukapime ili ujitambue kwani kuishi kwa mashaka siyo vizuri, naweza mie nikawa nimeathirika wewe ukawa ni mzima, na ikiwa nawe utakutwa umeathirika, basi utakuwa umejitambua. Mie nisingekwenda jela nisingejua yote haya, lakini hakuna mtu aliejela akawa na Virusi kisha asijulikane kutokana na lishe duni inayopatikana kule. Hivyo nakushau….” Iddy Teva hakumalizia kauli yake Mbuya alimkatisha kwa ukali. “Niache usiniambie mambo yako, ushanipa Ukimwi mie unanihubiria nini, ushaniharibia ndoto za maisha yangu, nawezaje kumwambia baba yangu kuwa nimeathirika mie. Naomba kuanzia leo hii, usinifate tena endelea na maisha yako achana na mie kabisa, au nitakufanyia kitu mbaya!” Mbuya baada yakusema maneno yale, akasimamisha Bajaji iliyokuwa ikipita barabarani akaingia na kumuamrisha dereva ampeleke hospitali ya kulipia iliyokuwa na vipimo vizuri ili akacheki afya yake. Dereva aliigeuza bajaji yake akaelekea mjini. Iddy Teva akajilaumu, kwa nini amemwambia ukweli badala yake kumbe angemdanganya, lakini alikuwa keshasema ukweli. Ama kweli kweli inauma.
***
Wakili Neema Faraja alikwenda TRA, pale mkabala na ‘Strongroom’ akaingia ndani ya ofisi zile, akamkuta mdada mmoja akiwa anawahudumia wateja wenye shida mbalimbali, nae akasubiri hadi zamu yake ilipofika akaulizwa asaidiwe kitu gani katika ofisi ile. Wakili Neema faraja alitoa kitambulisho chake akajieleza kisha akasema haja yake kwa yule muhudumu. Yule dada aliandika kwenye karatasi namba aliyopewa na Waili Neema kisha akamuomba asubiri kidogo kisha yule dada akapanda juu ya jengo lile ili kufatilia ile namba aliyokuwa nayo mikononi mwake. Baada ya dakika zipatazo kumi hivi yule dada alirudi na jalada kubwa, akachukua karatasi akajaza vitu alivyokuwa akivitaka wakili Neema kisha akamkabidhi ile karatasi na yeye kulirejesha lile jalada pahala alipolitoa awali. Wakili Neema aliitazama ile karatasi kwa makini, kisha akaiingiza katika mkoba wake, akatoka katika ofisi zile akawa anaelekea katika gari yake alipoiegesha. Mara simu yake ikaanza kuita. Wakili Neema Faraja aliitazama ile namba ya simu akaiona ni namba ngeni, ila kwa kazi yake amekuwa akipigiwa simu na watu mara kwa mara, hivyo akaipokea simu ile akaiweka sikioni. Upande wa pili wa simu ile ulijitambulisha kwa ufupi ukaomba kukutana nae muda ule kwa kile kitu kilichoelezwa ni muhimu sana na cha dharula. Wakili Neema akakubaliana na yule mtu aende ofisini kwake ili wakazungumze, akamuelekeza mahali ofisi zake zilipokuwa na yule mtu akaahidi kwenda muda si mrefu. Wakili Neema alikata simu akaiweka mfukoni kwake akaifikia gari yake, akafungua mlango akazama ndani akaiwasha gari ile na kuondoka kuelekea ofisini kwake.
***
Mkuu wa upelelezi aliwaamuru askari wavunje mlango ule, mara walipofika pale na shoka zao. Askari wale wakaanza kupiga shoka katika kitasa cha mlango ule, na mara ule mlango ukaachia. Askari wale waliziweka shoka pembeni wakenda wale askari walioruka ukuta wakaesabu kwa mtindo uleule wa vidole bila kutoa sauti kisha waliusukuma ndani ule mlango kwa nguvu, na wao wakalala chini kifudifudi kwa pamoja kwa haraka. Walilala vile huku silaha zao zikiwa zimetazama mbele tayari kwa kushambuliana na adui. Walipoona kimya hakuna upinzani, kwa haraka wakasimama huku bastola zao zikiwa wamezishika kwa mikono miwili, zikiangalia juu zikiwa usawa wa masikio yao, wakagawana wawili wakawa kila mmoja anatembea na ukuta wake na yule mtu wa tatu yeye alikuwa ameelekeza silaha yake mbele, macho yake yakitazama mbele, kidole chake kikiwa kwenye Trigger tayari kwa kufyatua risasi mara moja. Walitembea na korido ile hadi wakatokezea sebuleni. Walipohakikisha pahala pale ni salama askari mmoja alitoka nje uwani akasema kuwa; “Mkuu huku ni showari kabisa, mtuhumiwa hayupo hivyo hakuna upinzani.” Baada ya askari yule kusema maneno yale kwa mkuu wake huku akipiga saluti wakati akimwambia maneno yale, Mkuu wa upelelezi aliingia ndani ya nyumba ile pamoja na Mjumbe, na Mke wa Baba Ubaya. Walifika sebuleni, asakri wale pamoja na Mke wa Baba Ubaya na Mjumbe, walipigwa na butwaa pale walipozishuhudia Risasi karibu Kumi na mbili zikiwa chini katika zulia sebuleni pale zimesambaa. “Mjumbe unaona, hizi ni Risasi za silaha aina ya Chines, tena ni mpya hizi inaonekana kuwa jirani yako anamiliki maboxi kwa maboxi ya risasi pamoja na silaha zake. Hivyo tunaomba uwe shahidi katika hili.” Mkuu wa Upelelezi alimwambia Mjumbe wa shina, kuhusu zile Risasi zilizokuwa pale chini. Kisha kupitia simu yake ya mkononi Mkuu wa Upelelezi alizipiga picha zile Risasi pale kwenye zulia, kisha akatoa glovu pamoja mfuko maalum mifukoni mwake akazivaa zile glovu. Akaziokota risasi zile na kuziweka katika ule mfuko maalumu wa plastiki mweupe alioutoa pamoja na glovu mfukoni mwake. Baada yakuziokota Risasi zote, walikagua sebule yote, kisha wakataka kuvunja mlango wa chumbani kwa Baba Ubaya baada yakuulizwa Mkewe chumba chao kipo wapi, na yeye akaonesha. Walipojaribu kuufungua mlango ulikuwa wazi haujafungwa, hivyo walimuingiza mjumbe kwanza ndani ya chumba kile kisha wakaingia wao na Mke wa Baba Ubaya, walipekuwa lakini hawakukuta kitu kingine cha maana kwao. Mkuu wa Upelelezi, alitoa simu ya Mke wa Baba Ubaya, akamwambia ampigie mumewe, amwambie ende pale nyumbani kwake kuwa kumetokea matatizo ya umeme, hivyo afike mara moja. Mke wa baba Ubaya aliichukua ile simu yake akabonyeza namba za simu za Baba Ubaya, kwenye mtandao wa Airtel simu yake ikawa inaita upande wa pili. “Halow”? Baba Ubaya aliipokea simu ya mkewe huku akihema sana. Ndipo Mkewe alipomwambia kama alivyoelekezwa na Polisi. Lakini baba Ubaya alisema maneno yaliyowafanya askari wale watizamane na kutingisha vichwa vyao.
“Nisikilize wewe mwanamke, hayo majanga yako uliyoyatafuta yamalize mwenyewe, hiyo ndiyo faida ya ubishi. Natambua kuwa upo na askari na kwa taarifa yako wakati unakamatwa na polisi pale Tabata Sheli, mie nilikuwa nipo jirani na wewe. Hivyo mchezo wote nimeuona. Kwa hiyo tafuta njia nyingine ya kunivuta siyo hiyo, mie sidanganyiki wala sivutiki kizembe hivyo. Ungenisikiliza nilivyokuasa uiache ile gari yote hayo yasingetokea, ila kwa sababu ya ubishi wako. Leo umeona faida ya ubishi malizana nao hao watu wako.” Baba Ubaya aliposema maneno yale, wale askari Polisi walitingisha vichwa vyao kwa masikitiko, hasa waliposikia kuwa Muhalifu wanaemtafuta alikuwepo katika eneo la tukio. Mkuu wa upelelezi aliikata simu ile, kisha akaiweka mfukoni mwake ikiwa ipo on. “Hebu naomba picha zote za mumeo tafadhali.” Mkuu wa upelelezi alimwambia mke wa Baba Ubaya. Mwanamke yule aliwaonesha albam zilipo pale chini ya meza, mkuu wa upelelezi aliinama akazichukua albam mbili zilizokuwa pale akaanza kuzipekua. Mara akakutana na picha iliyokuwa imepigwa Bar ikiwa inaonekana wanaume watatu wamekaa katika meza iliyochafuka chupa za bia na nyama choma. Mkuu wa upelelezi alimgeukia mke wa Baba Ubaya akamuuliza. “Unaweza kunitajia hawa ni kina nani?” mke wa baba Ubaya aliitazama ile picha kisha akaanza kutaja majina ya watu waliokuwa wakionekana kwenye picha ile. Huyu aliekuwa amekaa kati ndiyo mume wangu, huyo wa kushoto kwake ni Nigga, na huyo wa kulia kwake ni Carlos Boga,” mke wa Baba Ubaya alimjibu mkuu wa upelelezi, kama alivyoulizwa. Mkuu wa upelelezi aliibandua ile picha kutoka katika albam iliyokuwepo kisha akasema. “Nina kazi na picha hii, hivyo ninaichukua” Mke wa Baba Ubaya hakuwa na pingamizi alibaki kuwa mpole “Huyu ameona kweli wakati mkewe anakamatwa na ndiyo maana ameondoka humu, hivyo turudini kituoni tukajipange upya namna yakumkamata huyu na wenzake wote waliokuwa katika mtandao wa Kihalifu. Kwani kufukia sasa watu hawa watakuwa wameshapashana habari juu ya tukio hili la leo, hivyo watakuwa wanajiandaa kutoroka au wanakimbia kwenda mbali nje ya mkoa huu” Mkuu wa upelelezi aliwaambia wenzake, ikawa hakuna wakupinga. Mjumbe alishukuriwa akapewa namba za simu na mkuu wa upelelezi ili akimuona Baba Ubaya amekwenda pale nyumbani kwake, aweze kupiga simu Polisi. Kisha na wao wakachukua namba zake za simu wakamruhusu ende akaendelee na shughuli zake. Polisi wale waliondoka mahala pale akabakizwa askari mmoja aliekuwa amevaa nguo za kiraia. Awe katika maeneo ya jirani na nyumba ile bila kutambuliwa na watu kwamba yeye ni askari, ili atoe taarifa kama ataonekana Baba Ubaya eneo lile. Kisha wao wakashika njia kurejea kituoni sanjari wakiwa na mke wa Baba Ubaya.
***http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mbuya Fabiola, alikuwa anatoka hospitali akiwa analia machozi yakim mwagika sana. Alikuwa ametaharuki vibaya mno. Macho yake yalimvimba kwa kulia. Aliingia katika Taxi akamwambia dereva ampeleke Mtoni Kijichi. Dereva Taxi aliwasha gari huku akimwambia bei abiria wake, ambae wala hakubisha pia hakutaka kulilia hali. Kwani alikuwa keshavurugwa. Mbuya alipofika nyumbani kwao, akamlipa pesa dereva wa Taxi ile aliyoitaja ambayo alijua ataombwa apunguze bei, lakini ikawa kinyume chake. Aliliendea geti akabonyeza kengele ya pale mlangoni nje ya nyumba yao, mlinzi akamfungulia mlango. Mbuya aliingia ndani kwao akiwa mnyonge sana na mwenye kilio kisichojificha. Alipoingia sebuleni alikutana na baba yake amekaa sebuleni akitazama Runinga. Kapteni Fabiola alipomuona mwanawe analia, akakaa vyema ili kujua kilichomsibu. Mbuya alimuamkia baba yake, kisha akataka kupitiliza ili aingie ndani lakini baba yake alimwita. “Wee Mbuya kuja hapa, unakuja na kilio namna hivyo umepatwa na nini?” Mbuya alisimama pale alipokuwa amefika kisha akageuka na kwenda pale alipokuwa baba yake akakaa pembeni yake, kilio kikubwa kikamtoka Mbuya Fabiola mbele ya baba yake. “Baba nakufa mie, nimetoka hospitali kupima afya yangu nimegundulika nina virusi vya Ukimwi.” Mbuya Fabiola alipofika sehemu hiyo akazidisha kilio sana. “Pole sana mwanangu, dah ama kweli Ukimwi umekuwa ni adui mkubwa katika familia yangu.” Mbuya alipomsikia baba yake anasema vile akamshangaa sana. Akanyamaza kulia akafuta machozi kisha akamuuliza. “Dady Ukimwi umekuwaje adui mkubwa katika familia yetu?!” Kapteni Fabiola aliinamisha kichwa chake chini kwa muda bila kusema kitu. Hali ile ilimpa wasiwasi Mbuya yakutaka kujua kulikoni, kwani haikuwa hali ya kawaida kwa baba yake, aulizwe jambo kisha ainame namna ile tena bila majibu. “Dady, hebu niambie vizuri, kuna mtu yeyote katika familia yetu aliekufa kwa Ukimwi?!” Kapteni Fabiola, alipoinua kichwa chake, uso wake ukaonekana umemjaa simanzi ya hali ya juu, japo hakuwa akitokwa na machozi, lakini dhahiri shahiri alionekana ni mtu mwenye huzuni isiyosemeka. “Mwanangu Mbuya, kwanza nisamehe sana mimi baba yako kwa kukuficha, muda mrefu kuwa wewe ni muathirika!” Kapteni Fabiola aliposema maneno yale, Mbuya akatoa macho, kama mjusi aliebanwa na mlango. “Dady unasema umenificha kuwa mie nimekuwa muathirika kivipi, mbona sikuelewi?” Mbuya alikuwa amechanganyikiwa kupita maelezo, kwani yeye alikuwa akilia sana wakati alipojitambua kuwa ameathirika. Tena lawama zote alikuwa akimtupia Iddy Teva kuwa amempa maambukizi, alimtupia yeye kwa sababu Iddy Teva ndiyo mwanamme wake wa kwanza maishani mwake, ndiyo mwanamme aliemtoa usichana wake, hivyo kwake Iddy Teva alikuwa ndiye mtu pekee aliebahatika kufanya nae mapenzi katika umri wa miaka kumi na minane aliyokuwa nayo. Hakuwa na mwanaume mwengine. Hivyo kuchanganyikiwa kwake alikuwa akijishauri pindi angeulizwa na baba yake mtu aliempa virusi, lakini badala yake anaambiwa yeye alikuwa ni muathirika wa VVU wa muda mrefu! “Mwanangu marehemu mama yako, alikuwa ni muathirika wa VVU. Nawe umeambukizwa virusi hivyo kutoka kwa marehemu mama yako. Kwani wakati tunagundua kuwa mama yako ameshaathirika, wewe ulikuwa ukinyonya mwanangu. Tulikwenda kukupima tukagundua kuwa nawe umeshaathirika. Maambukizi uliyoyapata kutoka kwa mama yako. Wakati ule wa mimba yako, miaka kumi na minane nyuma nchini kwetu Tanzania, wataalamu wa mambo ya afya walikuwa bado hawajagundua dawa za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Hivyo tulikuachisha ziwa la mama kunyonya, ukaanza kunyonya maziwa ya kopo, na tumetumia gharama kubwa sana za kipesa, ikiwamo kuwa unakula vyakula vyenye virutubisho, mboga za majani na matunda ili afya yako iimarike na kweli karika umri wa miaka uliyonayo, leo ndiyo umejitambua kuwa wewe ni muathirika wa VVU.” Mbuya alishusha pumzi ndefu sana, akamsikitikia Iddy Teva alikuwa amemlaumu kuwa amemuathiri kwa kumpa virusi, kumbe yeye atakuwa ndiyo aliemuambukiza mtoto wa watu. Mbuya aliinama pale alipokuwa amekaa, akainua uso wake kumtazama baba yake. Akamuona baba yake anaukwepesha uso wake wasikutane macho yao. “Mwanangu umerithi mali yote kutoka kwa mama yako, ni kwa sababu wewe ndiyo mtoto wetu wa pekee, kwani baada ya kuachishwa kunyonya, mama yako aliugua kwa muda mrefu, kiasi ya miaka mine hadi roho yake ilipoacha mwili wake. Hivyo ndivyo ilivyokuwa mwanangu, na ndiyo maana mie nilikuwa mkali zaidi kwa watoto wa kiume, kwani ukiwa ni muathirika unapofanya ngono, huongeza athari za kuzipunguza zaidi kinga zako za mwili. Na inaweza kukupelekea kufa haraka.” Kapteni Fabiola alimwambia mwanawe bila yakumtazama usoni. Alikuwa akimuonea huruma sana, kwani Mbuya bado alikuwa Ubwabwa wa shingo bado haujamtoka. “Samahani Dady, unataka kuniambia na wewe pia ni muathirika?!” Mbuya alimuuliza swali gumu baba yake huku akimtazama bila kupepesa macho. “Mwanangu unauliza makalio ya mbwa wakati mkia unauona? Mie pia nimeathirika ndiyo.” Mbuya alimtazama baba yake, roho yake ikamuuma sana, akamuuliza baba yake kwa uchungu. “Dady hebu niambie ukweli nani alieleta Ukimwi katika familia yetu?” Kapteni Fabiola alitikisa kichwa kama mtu aliekuwa akilisubiri swali lile. “Alieleta ukimwi katika familia yetu ni ajali mwanangu.” Mbuya hakumuelewa baba yake akamuuliza kwa mshangao. “Ajali?! Unamaanisha nini sijaelewa.” Mzee Fabiola alikohoa kidogo kisha, akamjibu mwanawe kwa utulivu. “Mama yako akiwa na mimba yako ya miezi miwili, walipata ajali ya gari iliyouwa watu wengi, na kuwajeruhi pia. Hivyo mama yako nae alikuwa ni miongoni mwa majeruhi wale, alichanika mguuni damu nyingi zikamtoka, lakini pia hakuweza kuzuia damu za majeruhi wengine kumgusa pale katika jeraha lake, na ndipo matatizo yalipoanzia hapo mwanangu.” Mbuya Fabiola alilia sana alipotambua kiini cha matatizo ya familia yao kuwa wameathirika kutokana na ajali, kasha yakazaliwa majanga yote yale kwao. Baba yake akambembeleza sana, na mara kuna kitu kikawasitua wote wawili wakawa katika mshangao.
***
Wakili Neema Faraja, aliegesha gari yake nje katika jengo la ofisi yake, akashuka ndani ya gari na kutaka kupiga hatua kuingia ndani ofisini mwake, mara akasikia jina lake likiitwa. “Wakili Neema” kisha Yule aliekuwa akimwita alimfata pale alipo akamsalimia na kumwambia. “Samahani nimekuja na mwanangu mtoto wa marehemu dada yangu, anamatatizo ya kisheria yamempata, hivyo alikuwa akiuhitaji msada wa kutetewa ndiyo nimekuja nae ili tuzungumze ikibidi tukulipe kabisa ili ufatilie jambo hilo.” Alizungumza Yule mgeni aliekuwa nae pale. “Ohoo sawa twendeni ndani ofisini tukazungumze, tusiongelee hapa.” Wakili Neema Faraja aliongoza njia wakaelekea ofisini kwake na wageni wale wawili. Walipofika ofisini wakili Neema alitoa funguo katika mkoba wake, akafungua mlango wa chumba cha ofisi akawakaribisha wageni wale. “Karibuni sana, kama nilivyowaelekeza hapa ndiyo ofisini kwangu. kisha sura yako siyo ngeni machoni kwangu, vile tulionana wapi hebu nikumbushe.” Wakili Neema Faraja alimwambia Yule mgeni wa kike alieongozana na kijana wa kiume. “Mmmm kweli sasa unaanza kuzeeka, mie tulikutana Mahakama ya Temeke, ulikuwa na kesi ya kijana mmoja Yule siku ile tulikuwa tukiongea mimi na wewe, hadi ikatokea tafrani.” Wakili Neema akamkumbuka Yule mama aliekuwa akiongea nae kisha ukatokea mtafaruku wa Msafiri kukamatwa na Polisi kituuteni. “Naam nishakukumbuka ndiyo maana nikasema sura yako siyo ngeni machoni mwangu, kwani siku ile tulizungumza na nikakupa cadi yangu ya namba za simu, ukanambia umependenda nilivyomtetea Yule kijana, hivyo ukaomba mawasiliano yangu. Leteni habari nawasikiliza” Yule mgeni akamgeukia Yule kijana akambonyeza kwa kumpa ishara ili azungumze. “Eee dada mie nimekuja nina http://deusdeditmahunda.blogspot.com/matatizo yamenipata hivyo nahitaji sana msaada wa kisheria. Mama mdogo amenambia umahiri wako, hivyo naomba sana unambie ujira wako ni kiasi gani ili nione kama ninaweza kukulipa ili unitetee kwani hali imekuwa tete sana kwa upande wangu dada yangu.” Yule kijana alimwambia Wakili Neema Faraja, huku akitazamana nae usoni. “Malipo inategemea na kesi ipoje, yaani kesi gani ipo wapi, kama ipo Polisi au Mahakamani, kisha baada yakujua hayo ndipo linapokuja suala la kesi hiyo itagharimu kiasi gani, hasa kutokana na wingi wa Mashahidi wa kesi husika, lakini pia imesimamaje. Kwa hivyo basi nieleze kama unakesi polisi, kesi yenyewe ni nini au kama una kesi iliyopo mahakamani basi unambie ipo mahakama ipi, na ni kesi gani.” Wakili Neema Faraja, alimwambia Yule mteja wake aliekuwa ofisini kwake. “Mie bado sijafikishwa Mahakamani, lakini pia bado sijakamatwa! Ila naona kama muda si mrefu naweza kupatikana ndiyo maana nimechukua nafasi hii kukuona ili unitetee.” Alimaliza Yule kijana maneno yake ambayo yalimuacha hoi wakili Neema. “sasa mtu ambae hujakamatwa wala hujafunguliwa kesi mie nakutetea vipi hapo?” Wakili Neema Faraja alimuuliza Yule kijana aliekuwa hodari wa kujieleza. “Ipo hivi, mie nikwambie ukweli ni mjanja wa mjini wa mambo yetu yakutafuta mkate wa kila siku, sasa kuna jambo linanipa tabu sana kwani natafutwa na Polisi, kwa tuhuma za ujambazi ambazo kweli mimi ni mshirika wa mambo hayo. Na ujambazi huo nimeushiriki mimi mwenyewe kwa kuupanga na kuucheza, sasa natafutwa na Polisi kwa Udi na Uvumba. Hivyo ninachotaka ikiwa tutakubaliana basi mie nikulipe pesa zako zote, kisha wewe unichukue na kunifikisha kituoni. Wale wakiona wakili ndiyo amenipeleka mwenyewe kwa maana yakujisalimisha, basi hawatanipiga ila nikiwa nipo peke yangu haki kwa upande wangu haitatendeka. Nitapata kibano sana naweza kupata ulemavu wa kudumu kama siyo kufa kabisa. Hiyo ndiyo shida yangu kubwa sana wakili.” Wakili Neema Faraja alimtazama vizuri Yule mtu, huku akiwa anachezea simu yake, kisha akamuuliza kwa utulivu mkubwa. “Umesema wewe bado hujakamatwa ila polisi wanakutafuta. Unataka mie nikuchukue nikupeleke Polisi ikiwa nimekusalimisha sawa, lakini ni vyema nikajua hilo tatizo linalokufanya utafutwe na Polisi, ili nijue namna gani naweza kukusaidia.” Yule kijana akafikiri kidogo kisha akaanza kufunguka. “Naitwa Joseph Kazi, ila jina maarufu naitwa Nigga. Takribani miaka miwili nyuma nilifanya tukio la uhalifu Upanga kwa wahindi, hivyo kabla ya uhalifu ule nilikuwa nimezoeana na kuanzisha mahusiano ya kimapenzi na dada wa kazi anaeitwa Shuwea Namjupa.” Nigga alisimama kuzungumza kwani alimuona wakili Neema macho yamemtoka pima.
Wakili Neema faraja moyo wake ulipiga sarakasi, aliposikia habari ile akafanya tendo la haraka!
Wakili Neema Faraja, alimwambia Nigga; “Samahani naomba nimtumie ujumbe mtu wa chakula asiniletee kwani sijisikii kula.” Nigga na mama yake mdogo wakakubaliana nae. Wakili Neema badala ya kutuma ujumbe kama alivyosema, kwa haraka akabonyeza simu yake hadi akafika sehemu ya kurekodia, akabonyeza kitufe cha record kisha akamwambia Nigga aendelee keshatuma ujumbe sehemu husika. “Mbona umeonekana kustuka nilipokutajia jina la Shuwea Namjupa, vipi unamfahamu?!” Nigga alimuuliza wakili Neema Faraja, huku akionesha mshangao usoni mwake. Wakili Neema alikuwa amesoma saikoloji hivyo alimgundua Nigga wasiwasi wake akamtuliza. “Kilichonifanya nishangae ni kwamba, tukio ulifanye miaka miwili nyuma, Polisi waje kukutafuta sasa hivi kulikoni?” Nigga alitulia akamjibu. “Polisi walikuwa wakitutafuta muda mrefu, ila walikosa kujua tulipo kwa sababu hawakuwa na mtu wakuwapa taarifa zetu, nami yule mwanamke hakuwa akipajua nyumbani kwangu, hivyo yule mwanamke Shuwea Namjupa sasa hivi ninavyoongea na wewe, ametoka Jela yupo nje. Tangu jana aonekane na rafiki yangu tuliocheza wote ule mchezo Baba Ubaya, watu watatu washakamatwa hivi wapo ndani.” Nigga alimueleza wakili Neema akiwa hana habari kabisa kuwa kutoka jela kwa Shuwea Namjupa ni kutokana na juhudi zake. “Ahaa kama nimekuelewa vyema, unahitaji msaada wangu kipindi hiki ambacho yule dada Shuwea ametoka jela na kwamba yeye anaweza kuwa shahidi wa Polisi ikawa matatizo kwenu si ndiyo?” Nigga alisogea pale kitini akiwa ni mtu alieguswa hasa akajibu. “Naam khaswaaaa, hapo yule mwanamke akiletwa kwenye gwaride la utambulisho atatutambua, pia atakwenda Mahakamani kutoa ushahidi kwani yeye alikuwapo katika eneo la tukio, hivyo ni shahidi muhimu sana, ni mtu pekee tunaemuhofia sijui utanisaidiaje juu ya hilo.” Wakili Neema Faraja, alimtazama kwa makini Nigga, akamgeukia mama yake mdogo kisha akamuuliza Nigga. “Yule mwanamke alikuwa ni mpenzi wako?” Nigga akamjibu huku uso wake ameuinamisha chini. “Alikuwa demu tu siyo kama nilikuwa na mapenzi nae hapana, ila nilianzisha mahusiano nae kwa vile alikuwa akifanya kazi za ndani kwa muhindi lengo langu hasa lilikuwa nikukaa nae karibu, niyasome mazingira ya mle ndani kisha nifanye dhumuni langu, jambo ambalo lilifanikiwa.” Wakili Neema alimsikiliza Nigga huku akiitupia macho simu yake kama inaendelea kurecord sawasawa. “Sasa naweza kukusaidia ila nisikilize kwa makini sana, kama utanielewa basi tambua kesi hii unayotafutwa kwayo haitakufunga, ila kama ukinipuuza basi hata kama nitakutetea Mahakamani kwa ushahidi uliopo hautakwepa kifungo.” Nigga alikuwa ametulia tuli amepoa kama maji ya mtungi, alikuwa hana pingamizi ila kumsikiliza wakili anachosema kwake. “Shuwea Namjupa unajua kama ulimpa Mimba na sasa hivi ana mtoto wako?” Nigga alimuangalia mama yake mdogo kwa mshangao kuwa huyu wakili amejuaje jambo hilo, lakini mama yake mdogo hakumtazama bali alikuwa ametoa macho kwa wakili tu. “Nakumbuka aliwahi kunambia kuwa ana mimba yangu ni kweli, lakini wewe umejuwaje hilo?!.” Nigga alimuuliza wakili Neema huku moyo wake ukimuenda mbio. “Sikia Nigga, nataka kukusaidia kwani mie kusaidia watu ndiyo kazi yangu inayonipa ugali wangu. Hivyo nikufahamishe tu kwamba Shuwea namjupa mie ndiye niliemtoa kwa rufaa akatoka Jela akiwa huru.” Wakili Neema alimwambia Nigga huku akimtazama usoni, alimuona Nigga amestuka sana kwa kauli ile woga ukiwa umemtawala sana. “Mimi ni wakili wa utetezi, sheria inaninyima kumtetea mrufani ambae ametoka akawa shahidi kisha nikakutetea na wewe mshitakiwa kwa maana kwamba nitakuwa nimeshajua ukweli mzima wa jambo lako, lakini pia sheria inaninyima kutoa siri za mteja wangu nje. Hivyo siwezi kuwa wakili wako, wala siwezi kuwa adui yako, ila naweza kukusaidia kama utakuwa unaniamini.” Wakili Neema alimwambia Nigga aliekuwa tayari mwili wake wote umelowa jasho kama mle ndani hakuna kiyoyozi. Nigga alitaka msaada kwa gharama yoyote, hivyo alimwambia wakili Neema amsaidie yupo tayari na anamuamini hana wasiwasi nae. Wakili Neema akamueleza mianya yakumfanya Nigga awe mbali mno na kifungo, lakini pia kama atatekeleza hilo jambo alilomwambia, ataishi bila mashaka yoyote. Nigga pamoja na mama yake mdogo waliwafikiana na maneno ya wakili Neema wakakubali kutekeleza maagizo yake wakakubaliana siku ileile kutimiza maelekezo yake. Baada yakuafikiana wakapeana mikono wakakubaliana siku ya pili yake waje kwa ajili ya kutimiza kila kitu walichokubaliana.
***
Kapteni Fabiola, akiwa na mwanawe pale Sebuleni, walishangazwa na mtu waliemuona ameingia pale sebuleni, Kapteni alikuwa hamfahamu yule mtu lakini Mbuya alikuwa akimfahamu vizuri sana. “Dada Shuwea, umepajuwaje nyumbani?” Mbuya Fabiola alimuuliza Shuwea Namjupa aliekuwa amesimama akiwa na mtoto wake mgongoni akiwa amelala. Kapteni Fabiola alimtazama mwanawe akamuuliza, “Nani huyu?” Mbuya akamjibu baba yake. “Huyu nimemfahamu nilipokuwa Jela, ndiyo alinipokea akanisaidia sana. Karibu Dada Shuwea, vipi unahabari gani?” Shuwea Namjupa aliinama akamuamkia Kapteni Fabiola, kisha akasema. “Mie sikuwa najua kama hapa ndiyo nyumbani kwenu ila mie nimeshapita nyumba nyingi huku Mtoni Kijichi, napita kuombaomba kazi kama za kufua, au za usafi wa nyumba ili nipate pesa yakula na mwanangu, kwani sina mtu wakunisaidia maisha haya na mtoto mchanga.” Shuwea Namjupa alimjibu Mbuya na baba yake akiwa bado amesimama pale alipokuwa. “Asante sana ila hapa tuna mashine za kufulia nguo, usafi yupo shamba boy anafanya, nenda kajaribu sehemu nyingine.” Kapteni Fabiola alimjibu Shuwea Namjupa huku akiwa hakufurahia kuingia hadi sebuleni, akapanga kumshughulikia mlinzi wake baadae. “Baba japokuwa hatuna kazi ya kuifanya yeye ili apate pesa nyumbani kwetu, basi naomba tumsaidie japo pesa kidogo tu, ili akajikimu na mtoto wake, hivi kama nyumba zote akijibiwa hivyo ataishije?” Mbuya alimuomba baba yake. Kapteni Fabiola alitoa noti ya shilingi elfu kumi akampa shuwea. “Asante sana nashukuru mzazi wangu, kwa msaada wako kwangu Mungu awazidishie.” Shuwea Namjupa alishukuru mungu akaaga na kuondoka mle ndani, akiwa ameshapata pesa yakununulia unga wa uji wa mwanawe. Mbuya alitoka nae nje mgeni yule, baba yake hakumzuwia kwani alikuwa akiitafuta namna yakumfanya mwanawe aishi kwa furaha kama awali, hivyo hakutaka kumkera kabisa. “Mbuya mbona macho yamekuvimba namna hiyo wifi yangu kama mtu uliekuwa ukilia?” Shuwea namjupa alimuuliza Mbuya kwa namna ya utani. “Wifi yako nitakuwa mie, unao mawifi zako ila siyo mie. Kuna matatizo kidogo yametokea nyumbani ndiyo nilikuwa nalia.” Shuwea alimtazama Mbuya kwa makini akamuona ni mtu aliekuwa akijilazimisha aonekane ni mwenye furaha ilihali hayupo vile. “Kuhusu Msafiri ondoa shaka, wewe lazima utakuwa wifi yangu tu, kwani nimezungumza na Msafiri kwa kina, anaonekana kunielewa na nakuhakikishia atakuoa wifi yangu, wewe niachie mie tu.” Shuwea Namjupa bado alikuwa aking’ang’aniza uhusiano wa Mbuya kwa kaka yake. Ama kweli umasikini mbaya sana. “Mie Msafiri haniwezi tena sasa hivi, wala mie sipo tayari kuwa nae.” Mbuya Fabiola alimjibu Shuwea Namjupa, mara simu ya Mbuya ikaanza kuita. Mbuya aliitazama ile namba ya simu iliyokuwa ikiita akaitambua. Akaiweka simu ile sikioni kwa haraka huku akiipokea. “Wakili Neema shikamoo, ehee, ndiyo tena kama bahati ninae hapa hapa ninavyoongea na wewe. Ahaa sawa nitamwambia, au nimpe simu, haya basi nitamwambia usijali.” Mbuya Fabiola aliikata ile simu akamgeukia Shuwea akamwambia; “Kesho saa mbili asubuhi wakili Neema ameniagiza nikupeleke ofisini kwake amesema ni muhimu sana usikose.” Shuwea akashangaa sana. “Kuna nini tena, au wale wahalifu wameshakamatwa?” Shuwea namjupa alimuuliza Mbuya, lakini hakuwa na jibu la swali lile. “Usiumize kichwa chako, kesho panapo majaaliwa tutafahamu tu mbichi na mbivu, shaka ondoa.” Baada ya mbuya kumjibu Shuwea maneno yale, wakaagana wakiwa wamekubaliana siku inayofata wakutane wapi ili waende kwa Wakili Neema.
***
Siku ya pili yake Mkuu wa Upelelezi wa kituo cha Polisi Buguruni, alikuwa ofisini kwake akiwa na magazeti matatu mbele ya meza yake, magazeti ya siku ile. Magazeti yale yalikuwa yamepambwa na picha kubwa za watu watatu, waliokuwa wamekaa kwa pamoja kwenye meza iliyokuwa imejaa chupa za bia na nyama choma. Pia zikaonekana picha za risasi zilizokuwa zimezagaa sebuleni kwa Baba Ubaya. Magazeti yale yalikuwa yamepambwa na vichwa vya habari tofauti, vilivyokuwa vikisomeka hivi; MAJAMBAZI HATARI WANATAFUTWA NA POLISI, ZAWADI NONO KWA WATAKAOFANIKISHA KUKAMATWA KWAO. Kisha chini ya kichwa kile kukafatiwa na maandishi yaliyoandikwa kwa herufi ndogo majina ya watu wale. Gazeti la pili lilikuwa na kichwa cha habari kilichosomeka hivi; MAJAMBAZI SUGU YANATAFUTWA NA POLISI. TOA TAARIFA POLISI UKIYAONA. BONGE LA ZAWADI LITATOLEWA. KWA YEYOTE ATAKAETOA TAARIFA ZA MAHALI WALIPO. Gazeti la tatu lilipambwa na kichwa cha habari kilichosomeka. SURA HIZI NI HATARI KATIKA JAMII, KAA MBALI NAZO NI MAJAMBAZI HATARI. TOA TAARIFA POLISI KATIKA NAMBA HIZO HAPO. Kisha zikawekwa namba za simu za mkuu wa upelelezi wa kituo chahttp://deusdeditmahunda.blogspot.com/ Polisi cha Buguruni pale mbele ya gazeti lile. Mkuu wa Upelelezi alitikisa kichwa kukubaliana na uandishi uliotumika, kwani baada ya siku ya jana alipotoka kwa Baba Ubaya na ile picha, aliweza kwenda kuonana na mkuu wake wa kituo, akamfahamisha safari yao kwa Baba Ubaya ilivyokuwa, Mkuu wa kituo akazungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi Ilala. Nae akaita vyombo vya habari akatoa taarifa ile huku akiwaomba raia kutoa ushirikiano kwa Polisi. Pia akawataka Polisi Jamii, ulinzi shirikishi nao wafanye kazi yao katika kufanikisha jambo lile, zawadi ya shilingi laki tano ikatangazwa kwa mtu atakaefanikisha kukamatwa kwa watu wale. Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi wa Ilala, aliwaonesha waandishi wa habari ile picha pamoja na majina ya wale wahalifu, pia akawapa picha alizopiga mkuu wa upelelezi kwa simu yake namna zile risasi zilivyokuwa zimezagaa pale chini. Mkuu wa upelelezi akiwa anatafakari atumie mbinu gani ili kufanikisha kukamatwa kwa wahalifu wale, mara simu yake ambayo namba zake zilikuwa zipo katika gazeti ikawa inaita nae akaipokea kwa haraka huku akiwa na kalamu yake mkononi, akiwa tayari kwa kuandika. Ndipo alipopewa taarifa iliyomfanya atoke nje ya ofisi yake haraka.
***
Baba ubaya alikuwa amelala kwa rafiki yake, asubuhi alikuwa akitazama Runinga ili kupata habari za kitu kilichojiri baada ya jana kuitwa na mkewe akiwa chini ya mikono ya Polisi. Akiwa katika kutazama taarifa ya habari asubuhi ile, hakukuwa na habari mbaya kwake, ila ilipofika kile kipindi cha YASEMAVYO MAGAZETI. Baba Ubaya aliiona sura yake, kwenye magazeti yale akiwa na Nigga, pamoja na rafiki yake Carlos Boga ambae usiku wa siku iliyopita ndipo alipokuwa amepitisha usingizi wake. Magazeti yale yalikuwa yakinadi kutafutwa kwao, pia zawadi iliyoahidiwa kutolewa kwa mtu atakae fanikisha kukamatwa kwake. Baba Ubaya aliinuka pale kitandani akakaa kitako. Mapigo ya moyo wake yakapoteza uelekeo. Hasa alipoona gazetini mle kupitia Runingani, sebule ya nyumbani kwake ikionekana vyema kabisa na jinsi Risasi zilivyozagaa pale chini. Baba Ubaya alichukua simu yake akampigia rafiki yake Carlos Boga, aliekuwa chumba kingine kuhusu habari ile. Rafiki yake nae akamjibu yupo macho anaitazama taarifa ile. Alipompigia simu Nigga, simu yake ikawa haipatikani. Aliipiga zaidi ya mara tano lakini bado simu ile ilikuwa haipatikani. Baba Ubaya akapagawa sana. Akamfahamisha Carlos Boga kutopatikana kwa simu ya Nigga, Carlos akatoka chumbani kwake akaenda katika chumba alichokuwa Baba Ubaya, akamgongea akafunguliwa mlango akaingia ndani wakakaa kujadili nini wafanye kwani hali imeshakuwa tete kwa upande wao. “Unajua siyo kawaida kwa Nigga kuzima simu yake, hivyo nina wasiwasi sana asije akawa nae keshakamatwa!” Baba Ubaya akamwambia rafiki yake. “Je ikiwa kweli amekamatwa, na hapa alishawahi kuja tulivyokuja kugawana ile pesa ya siku ilee, zile milioni tatutatu. yule anapafahamu sasa hapa itakuwaje, lakini pia sura zetu zishaanikwa katika magazeti sasa tunaishije, tunatembeaje, hawa majirani wanaotuzunguka kwa tama ya pesa watatuchoma tu wangu. Hapa pameshakuwa siyo chimbo tena.” Carlos Boga alimwambia Baba Ubaya, wakaingia katika mchecheto wa nafsi, ikawa moja haikai, mbili haiingii! Mara wakasikia gari imefunga breki nje ya geti la nyumba ile, na mlango wake ukaanza kugongwa kwa kwa fujo. Baba Ubaya na Carlos Boga walikuwa kama panya aliefungiwa na paka chumba kimoja kisichokuwa na shimo. Ile nyumba ilikuwa na dari juu, lakini walikuwa wakitafuta pakukimbilia. Chumba kilikuwa hakitoshi. Fadhaa iliwaingia sana. Wakiwa katika hali ile mara simu ya Baba Ubaya ikaanza kuita kwa sauti. Baba Ubaya kama Mkizi aliirukia ile simu yake huku akitetemeka, akaiziba sehemu ya sauti akaitizama simu ile, huku akihema kwa nguvu jasho jingi likimtoka!
Baba Ubaya alikuwa akichelea kupokea ile simu kwa sababu, hakuwa akijuwa mpigaji wa simu ile kama alikuwa salama au laa. Au kama alikuwa na askari au yupo peke yake. Hivyo aliikata simu ile. Kisha kama mtu aliezinduka kutoka katika gumbizi la usingizi mzito, alinyoosha mkono wake kwenye mto, akachukua Bastola yake aliyokuwa ameiweka pale, ili muda wowote ikihitajika kutumika basi iweze kutumika. Aliipandisha Risasi chemba, akawa ameielekeza Bastola ile kwenye mlango ili mtu akiingia kwa nguvu tu, lengo lake lilikuwa ni kumpiga Risasi kila aingiae mle kwa nia yakuwakamata kisha ajimalize na yeye mwenyewe. Baba Ubaya sura ya utu ilimbadilika akauvaa unyama wa nafsi. Yule mtu aliekuwa akigonga geti lile mfululizo akasema kwa sauti kule nje ya geti. “Oyaa watu wa humu ndani, toeni takataka hizo, siyo tunagonga mara nyingi nyie mmekaa kimya tu humo, gari ikiondoka siyo muanze kutusimamisha sie hatutasimama, maana mnaleta dharau.” Maneno yale ya yule mtu kule nje, yaliwafanya Baba Ubaya na Carlos Boga, watizamane huku wakiguna kwa pamoja “Mmmmh!” Mara wakasikia ile gari ikiondoka pale usawa wa geti lao, huku ile sauti ikisikika ikinadi kwa watu wengine wa pale mtaani kwa nguvu. “Toweni taka hizo, toweni taka hizo.” Mara wakasikikia sauti za wanawake wakiwa wanakimbilia gari ile wakipeleka takataka. Baba Ubaya na Carlos Boga, walishusha pumzi ndefu, kisha wakatikisa vichwa vyao kwa masikitiko. Carlos Boga alifungua mlango, akaenda pale kwenye geti, akachungulia nje akaona watu wakipakia takataka ndani ya gari ya kubebea takataka. Aliporudi ndani alikutana na Baba Ubaya, mlangoni nae akiwa anatoka nje ya chumba kile jasho jingi likiwa linamtoka mwilini mwake. “Mwanangu hapa chaka lishaungua, tufanye maarifa tusepe, kwani moyo wangu umekwenda mbio sana. Yaani hadi muda huu najihisi sipo vizuri.” Baba Ubaya alimwambia mwenyeji wake Carlos Boga. “Siyo mchezo hata mie nilipagawa sana, maana nilijua wajomba washaingia, Nigga keshawaleta. Kumbe presha yetu tu bure. Sema yule bwege wa kuchukua taka sasa ule ndiyo ugongaji gani kama wa wajomba.” Carlos Boga alimwambia rafiki yake, kisha wote wakatungua kicheko kikubwa kwa woga waliojivika nao, kumbe watu wa takataka! “Unajuwa mtu aliekuwa akinipigia simu ni Nigga?” Baba Ubaya alimuuliza rafiki yake. “Aaa bwana weee, hebu mpigie simu kisha mchekechee ujue yupo na wazee, au yupo peke yake. Isije wazee wamempa simu ili aongee kujua mahala tulipo, yule mtu huwa hazimi simu yake saa ishirini na nne. Ikiwa amekamatwa na polisi, hapa kweli chaka litakuwa lishaungua, hatuwezi kukaa tena kwani hapa Nigga anapafahamu vizuri.” Baba Ubaya aliiwasha simu yake, baada yakuwaka akampigia simu Nigga. Wakawa makini kumsikiliza wajue atapokeaje simu ile, mara simu ile ikajibu. ”Simu unayopiga kwa sasa haipatikani, tafadhali jaribu tena baadae.” Walitazamana tena kwa mara ya pili marafiki wale kwa siku ile. Carlos Boga alitoa simu yake, akaipiga namba ya Nigga, lakini hakupata jibu tofauti na mwenzake. Simu ile waliyokuwa wakiipiga ilikuwa haipatikani. Wanaume wale wakaitilia mashaka hali ile, wakajipanga haraka kwa kuondoka kwani hawakutaka kuifanya ajizi, kwani ukiifanya ajizi na mambo yanaajizika. Ajizi nyumba ya njaa. wasije kukutwa bure wakaokotwa kama kumbikumbi.
***
Nigga alikuwa ameamka nyumbani kwa mama yake mdogo. Simu yake ilikwisha chaji usiku na umeme ulizimika. Hivyo asubuhi uliporudi umeme akaiweka simu yake katika chaji. Alifungulia Runinga iliyokuwa chumbani mle, akawa akitazama magazeti yanasemaje. Mara kilipoanza kipindi cha magazeti, kwa macho yake aliyashuhudia magazeti yale, yakiwa yameweka picha yao katika kurasa za mbele kabisa. Moyo wake ulimuenda mbio sana, akaangalia kipindi kile akalisoma jina lake katika gazeti akiwa anatafutwa kwa ujambazi yeye pamoja na wenzake. Nigga aliona kimenuka, harakaharaka akaiwasha simu yake iliyokuwa kwenye umeme ikiingia chaji, akampigia simu Baba Ubaya, ili amueleze huko alipo atazame Runinga kuhusu picha zao na kutafutwa kwao. Aliisikia simu yake ikiita upande wa pili, mara ikakatwa simu yake. Nigga alishangaa sana kukatiwa simu na rafiki yake, akaamua ampigie tena lakini safari ile aliambiwa simu aliyoipigia haipatikani kwa maana imezimwa. Nigga hakutaka kufikiri mara mbili, akahisi Baba Ubaya keshakamatwa, hivyo akaamua kuizima na yeye simu yake ili asivutwe na Baba Ubaya. Hivyo aliinuka akenda kujiandaa kwa kwenda kwa wkili Neema. Baada yakuwa sawa akaingia katika gari ya mama yake mdogo, wakiwa pamoja wakaelekea kwa wakili Neema Faraja. Nigga alivaa kofia ya Kapelo, aliishusha kwenye uso wake kofia ile, ukawa huwezi kuiona sura yake hadi atoe kofia usoni mwake. ndiyo ungeweza kumtambua.
***
Wakili Neema Faraja, aliwahi kuingia ofisini kwake asubuhi ile, mkononi mwake alikuwa na magazeti mawili ambayo hupenda kuyasoma mara kwa mara. Alikaa katika kiti chake akayaweka magazeti yale mezani, kisha akatoa ile karatasi aliyotoka nayo TRA, akaitazama tena kwa umakini. Macho yake yalipolitazama gazeti lililokuwa juu, akaiona namba ya mkuu wa upelelezi wa kituo cha Polisi cha Buguruni ikiwa inasomeka kwa uwazi. Aliipiga namba ile ikawa inaita upande wa pili. Wakili Neema Faraja aliisubiri simu ile ambayo haikuita muda mrefu ikapokelewa. Wakili Neema Faraja, alijitambulisha kwa mwanausalama yule, kisha akasema jambo alilolikusudia kwake. “Halow kiongozi, nilikwambia siku ile muende TRA ili kufatilia taarifa za ile gari, je mlifanikiwa kwenda?” Mkuu wa Upelelezi akamjibu kuwa hawakufanikiwa kwenda ila tayari ile gari wanayo kituoni wameshaikamata. Wakili Neema faraja akatikisa kichwa juu chini kukubaliana na taarifa ile, lakini kwa upande mwengine akiwapongeza kwa kazi nzuri yakufanikiwa kulikamata gari lile. akamwambia mkuu wa upelelezi. “Mie kwa utashi wangu tu kama raia mwema, nimekwenda TRA, nimepata taarifa muhimu sana. Hebu kaangalie kwenye leseni ya barabara, (ROAD LICENCE) pamoja na bima ya gari hiyo, kama inasoma jina gani la mwenye gari hiyo, kwani TRA inamtambua mmiliki wa gari namba hiyo kuwa ni Gulamhussein Gondrap Shaha. Haijafanywa uhamisho wa jina la mtu mwengine tangu ilipowasili gari hiyo nchini mwaka 2012.” Wakili Neema alipomwambia lile jina lenye asili la bara la Asia, mkuu wa upelelezi alitoka haraka nje ya ofisi yake, akenda kwenye ile gari na kusoma jina la mmiliki wa gari ile linavyosomeka pale kwenye kioo, katika Leseni ya Barabara pamoja na Bima. Jina aliloliona likisomeka pale na jina aliloambiwa na wakili Neema Faraja yalikuwa ni majina mawili tofauti. “Huku jina la mmiliki wa gari hii linasomeka ni UBAYA MZUZURI” mkuu wa upelelezi alimwambia wakili Neema. “Basi hiyo gari itakuwa ni ya wizi, kwani namba hizo zinasomeka kama nilivyokueleza. Hebu andika cheses namba, hizi kisha ulinganishe na hizo hapo kwenye gari hiyo,” Wakili Neema Faraja alimsomea namba za cheses alizopewa kule TRA za gari halisi lenye namba zile. Mkuu wa upelelezi aliandika katika mkono wake kwa kalamu namba zile alizokuwa akitajiwa na wakili Neema. Kisha wakili Neema akamsomea na namba ya mashine ya gari halisi yenye namba zile kama alivyopewa TRA. Mkuu wa upelelezi alipotazama vitu hivyo akaviona vipo mbalimbali kama maji na mafuta. Mkuu wa upelelezi akajiridhisha kuwa ile gari, hakuna ubishi ni ya wizi, na namba zile zilizokuwa zimefungwa kwenye gari ile ni namba za bandia, yaani siyo halisi kwa gari ile. Hivyo aliiandika cheses namba ya gari ile, ili aipeleke TRA kupata namba halisi za gari ile. Wakakata simu na wakili Neema, mkuu wa upelelezi akatoka asubuhi ile akenda TRA, hakika aliyoyapata kule kwa namba zile za Cheses, zilimfanya aandae jalada lingine la kesi. Akashika njia kuelekea Sayansi pale kijitonyama kwa taarifa zaidi za kikazi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakili Neema alipokata simu ya mkuu wa upelelezi, mara aliwaona Mbuya Fabiola na Shuwea namjupa akiwa na mwanawe pamoja na Msafiri wakiingia katika chumba cha ofisi yake. “Karibuni sana, poleni kwa kuwasumbua asubuhi hii.” Wakili Neema aliwakaribisha wageni wake, kwa maneno ya bashasha. “Usijali Dada Neema, tumekaribia pole na wewe kwa kukuvamia, kwani bwana Msafiri dada yake alipomwambia kuwa umemwita nae akataka aje kusikia kulikoni?” Mbuya Fabiola alimwambia wakili Neema. Wakili Neema aliwakaribisha katika chumba cha pili kilichokuwa na viti vingi, wageni wake wakakaa kitako, akawauliza kama wameshapata chai, mbuya akasema bado ila watakunywa wakishatoka pale. “Ahaa sawa hakuna neno, Mbuya vipi shule kwani muda mrefu upo mtaani.” Wakili Neema Faraja alimuuliza mbuya Fabiola. “Jamani dada Neema shule tumefunga kwa wiki mbili, hadi ishe Pasaka ndiyo maana unaniona nipo mtaani.” Wakiwa katika kuzungumza haya na yale, wakili Neema alikuwa hajawaambia dhumuni la kuwaita pale asubuhi ile. Mara gari iliyokuwa ikiendeshwa na mwanamke, iliegeshwa jirani kabisa na ofisi ile ya wakili Neema. Watu wawili wa jinsia na umri tofauti walishuka kutoka ndani ya gari ile, wakabisha hodi katika ofisi ile. Wakili Neema Faraja alitoka katika chumba kile alichowaweka wakina Mbuya, akaenda katika chumba cha awali kinachoanza ambapo ndipo kuna mlango wa kuingilia katika ofisi yake, akawakaribisha wageni wale, nao wakakaribia lakini hakuwaweka katika chumba kile bali aliwapeleka katika chumba walipokuwapo kina Shuwea Namjupa. Wale wageni wakati wakipita katika ofisi ile kuelekea chumba cha pili, waliyaona magazeti mawili pale juu ya meza, yakawafanya watizamane. Wageni wale waliingia katika chumba cha pili wakafanya idadi ya watu waliokuwamo ndani ya chumba kile kufikia watu saba. Baada ya wageni wale kukaa vitini, Yule mgeni wa kiume aliitoa ile kofia yake usoni mwake, akaiweka juu ya meza. Shuwea Namjupa alipomtazama Yule mtu alievua kofia, moyo wake ukaenda mbio, alianza kutetemeka kijasho chembamba kilimtoka. Hakuwa na amani kabisa. Shuwea Namjupa akaanza kulia huku akimnyooshea kidole Yule bwana alievua kofia yake. “Huyu bwana ndiyo …..!” “…aliesababisha wewe wende jela.” Wakili Neema Faraja alimkata kauli Shuwea Namjupa, aliekuwa ameanza kupagawa. Mbuya Fabiola pamoja na Msafiri wote walimtumbulia macho mtu Yule, wakawa wakimtazama mtazamo tofauti kabisa.
“Shuwea huna sababu ya kupagawa, tulia na unisikilize kwa makini sana.” Wakili Neema faraja alimwambia Shuwea Namjupa, huku akimtazama moja kwa moja usoni mwake. Alimuona Shuwea ametulia kimya lakini anahema juujuu kama mama mjamzito wa miezi tisa. “Nigga kutana na Shuwea Namjupa. Na Shuwea kutana na Joseph Kazi au Nigga. Hamkukutana hapa kwangu kwa bahati mbaya laa hasha. Bali ni kwa makusudi mazima, ambayo kama mtanisikiliza kwa makini kila mmoja atafaidika na maneno yangu. Hasa kwa upande wako Shuwea Namjupa utanufaika zaidi kwenye hili, kwani Nigga nimeshaongea nae hana matatizo juu ya hilo.” Wakili Neema Faraja aliwaeleza wale watu huku akizungumza kwa utulivu mkubwa sana. Alipoona kuna utulivu akaendelea kuzungumza. “Shuwea wewe ni shahidi pekee uliobakia katika kesi ambayo ilikuweka Jela ukiwa ni Mfungwa. Mengi yamepita sitaki kuyarejea ila zingatia jambo moja tu kwamba, yaliopita si ndwele, tugange yaliyopo na yajayo.” Kwa mara nyingine wakili Neema alisimama kuzungumza akamtazama Shuwea Namjupa ambae mapigo yake ya moyo yalianza kurudi katika hali yake ya kawaida taratibu. Wakili Neema alimgeukia Shuwea Namjupa akaendelea kusema; “Kwa nini nimesema wewe ndiyo shahidi pekee mwenye nguvu uliyobakia? Aliekuwa muajiri wako kwa taarifa ya uhakika kabisa ambayo nimeithibitisha mimi mwenyewe, ameondoka nchini amehamia Canada huu mwaka mmoja sasa. Yule mama yake mzazi aliekuwa akiishi nae pale kwake Upanga amefariki mwaka mmoja uliopita. Mie jana nimefika kwenye nyumba ile kama ilivyokuwa ikionekana namba yake katika hati la shitaka. Majibu hayo nimepewa na watu wanaoishi sasa katika nyumba ile ya Msajili, uliokuwa ukifanya kazi za ndani wewe.” Wakili Neema aliposema maneno yale, Nigga alishusha pumzi ndefu, mama yake mdogo akaanza kutabasamu, Shuwea Namjupa alitoa macho ya kumsikitikia Yule mama wa muajiri wake, Mbuya na Msafiri walikuwa makini sana kumsikiliza wakili Neema dhumuni la kuwaita kwao. Faraja alikuwa amekaa mapajani kwa mama yake ananyonya kidole chake hana habari na mambo ya Dunia yanavyokwenda. Wakili Neema akaendelea kueleza habari ile muhimu sana. “Hivyo basi Polisi wakati ulipowaeleza ukweli kuwa humjui Nigga anapoishi wala mshenga feki wake, hawakutaka kukuelewa kabisa na walihakikisha wanaungaunga ushahidi na hatimae ukavaa nguo za Kifungwa ukawa mfungwa wa namba ndefu na kazi ngumu. Ajabu Polisi haohao waliohakikisha umefungwa, leo hii watakupamba nakukufanya uwe shahidi wao kwa vile wewe ulikuwapo na uliona tukio wakati wahalifu hawa walipofanya uhalifu wao. Haijalishi kuwa mtendewa wa tukio kuwa hayupo basi kukawa hakuna kesi, laa haipo hivyo. Kesi hii mlalamikaji ni jamhuri ambae ni Serikali, labda niwaulize Serikali inasafiri?” Wakili Neema alipofika hapo alinyamaza kimya kungoja majibu kwa watu aliokuwa akiwaeleza. Nigga na Shuwea wote walijikuta kwa pamoja wakimjibu kwa kichwa kuwa Serikali haijaondoka bado ipo. Wakili Neema Faraja akaendelea kuzungumza. “Sawa kwa hiyo Serikali itakufanya Shuwea Namjupa, kuwa ni shahidi namba moja. Mahakama ikikuletea Samansi kwa maana ya wito, huna namna yakukataa kuitika wito huo. Kwani kukataa ni kuidharau Mahakama, hivyo Mahakama inaweza kukufunga kwa kosa la kuidharau. Kasha bado ukaendelea kuwa shahidi hivyo ndivyo sheria inavyosema. Hivyo mie nimeonelea kwamba huna sababu yakuwa shahidi katika kesi ambayo ilishakufunga awali. Hebu fikiria vipi kama nisingekuwapo kukata rufaa kwa sababu nilizoziorozesha ukawa huru, huoni muda huu ungekuwa bado upo Jela ukitaabika?” Wakili Neema faraja alikuwa akimjenga kisaikolojia sana Shuwea Namjupa. “Hilo halina ubishi Wakili kwani mie nilihangaikia rufaa yake kwa miaka miwili lakini hakutoka jela hadi ulipokuja wewe hakumaliza hata mwezi mmoja akawa huru.” Msafiri Namjupa alisema akiongeza kuhusu suala lile.
Wakiwa katika mazungumzo yale, nje ya ofisi ya wakili Neema Faraja, Mkuu wa Upelelezi wa Kituo cha Polisi Buguruni aliegesha gari yake akashuka kuelekea katika ofisi ya wakili Neema Faraja!
Ndani ya ofisi ya Wakili Neema katika chumba walichokuwamo yeye na wageni wake, mazungumzo yao yalikuwa yanaendelea.
“Shuwea ukiwa upo hapa Dar es salaam, Mahakama itakuletea wito, ili uende ukatoe ushahidi. Hivyo nimeongea na Baba Faraja na yeye amekubaliana na mimi kuhusu hilo, kuwa akupe pesa kama kifuta jasho cha mtoto kumlea peke yako, kukuingiza katika matatizo, lakini pia iwe ya nauli unatakiwa leo hii, hii usafiri utoke nje ya Mkoa huu wende Mkoa mwengine, japo ukakae kwa miezi mitatu tu. Sasa kama utakwenda kwenu Nachingwea au popote utakapoona patakufaa ni sawa tu.” Wakili Neema alimwambia Shuwea Namjupa aliekuwa yupo makini sana kumsikiliza. “Hebu mpe ule mzigo tuliozungumza wa kumuondoa shahidi muhimu.” Wakili Neema Faraja alimwambia Nigga, atoe pesa walizokubaliana. Nigga alimtazama mama yake mdogo kumuashiria kuwa atoe mzigo, nae akafungua mkoba wake wa mkononi, akatoa bandari la noti za shilingi elfu kumi kumi tupu, akamkabidhi wakili Neema huku akimwambia. “Hizo ni Milioni tatu kama ulivyoagiza” Yule mama yake mdogo Nigga alimkabidhi wakili Neema fedha zile. Wakili Neema alizishika zile pesa akamuuliza Shuwea Namjupa. “Je nikupe hizi pesa ufanye kama nilivyokueleza, au nimrudishie mwenyewe ili uendelee na kutoa ushahidi?” Shuwea huku akinyoosha mkono wake wa kulia alisema. “Nipe noti hizo niende Nachingwea leo hii, nakaa hapa sina lolote lakufanya naomba omba tu, bora nikafanye biashara ili nipate kumlea mwanangu.” Wakili Neema alitabasamu akamkabidhi zile pesa.
Mara wakiwa katika kukabidhiana Mlungula, mlango wa ofisi ya Wakili Neema uligongwa, mtu aliekuwa akibisha hodi alikuwa amefungua ule mlango na kuingia ndani katika chumba kile cha kwanza cha ofisi ya Wakili Neema Faraja, akaketi kwenye kiti huku macho yake yakipiga katika meza iliyokuwa pale akayaona magazeti mawili yamewekwa pale juu, ambayo asubuhi ile alishayasoma ofisini kwake. Wakili Neema Faraja, aliisikia hodi iliyogongwa katika mlango wa ofisi yake, akawaomba radhi wageni wake ili akamsikilize mgeni. Wakili Neema alipofika katika chumba alichokuwapo mgeni, Yule bwana alitaka kusema kitu, lakini alimfanyia ishara ya kumzuwia asiseme neno, kwa kuweka kidole chake kidogo mdomoni mwake, kisha akamuashiria atoke nae nje ya ofisi yake. Yule mgeni alitii ishara ile huku akitikisa kichwa chake juu chini kuwa amemuelewa. Aliinuka akatoka nje kumfata wakili Neema aliekuwa ametangulia nje ya ofisi yake. “Najua kuja kwako ni kwa sababu ya ule ujumbe wangu niliokutumia, hivyo umekuja muda muafaka sana,” kisha wakili Neema alimpa mikakati yakufanikisha azma yao. Mkuu wa upelelezi aliitikia kwa kichwa, akampa tano Wakili Neema kisha akasema. http://deusdeditmahunda.blogspot.com/“Asante sana kwa ushirikiano mwema tupo pamoja sana.” wakili Neema akaagana na mkuu wa upelelezi akarudi ofisini kwake kuendelea na wageni wake. Mkuu wa upelelezi alitoa simu yake akapiga simu sehemu aliyoikusudia, kisha akatoa maelekezo muhimu.
Wakili Neema Faraja aliporudi chumbani mwake, alimuona Nigga amembeba Faraja anacheza nae. “Alaa mtoto yupo na baba yake eee?” wakili Neema aliwatania mle ndani wote wakaangua kicheko mle ndani kisha akachukua nafasi yake ya uenyekiti wa kikao kile akaendelea. “Nigga tumemaliza hatua moja kubwa ya kumuondoa shahidi muhimu katika kesi hii. Sasa hatua ya pili fanya kama vile tulivyozungumza ili nimpe jukumu hili mtu ambae namuamini, nimeshafanya kazi nae sana anajua kuchambua sheria ili kesho saa nne uje wende nae kituo cha Polisi na kila kitu nitazungumza nae ondoa shaka.” Wakili Neema liposema maneno yale akamtazama Nigga. Mama yake mdogo niga aliingiza mkono katika mkoba wake akatoka na kitita cha pesa tasilimu shilingi Milioni moja na nusu, akamkabidhi wakili Neema. “Huu mzigo wetu, Milioni moja na nusu kama ulivyotuagiza.” Mama yake mdogo Nigga alisema maneno yale kumwambia Wakili Neema. “Sawa nimepokea basi hakuna shida kesho saa nne tukijaaliwa mje hapa, ili mwende pamoja kituoni mkamalize mambo haya, amini hutoguswa hata kidogo, na kesi itakuwa haina ushahidi utarudi uraiani ukiwa huru.” Wakili Neema aliwaambia maneno yale huku akichukua ile pesa akaiweka kwenye droo la kabati lake. “Basi sie tunakushukuru sana kwa msaada wako, hivyo hatuna budi tuondoke kurudi nyumbani kwani huyu kutembea tembea kwa sasa siyo vyema, kwani wametolewa sura zao na zawadi zimetangazwa.” Mama yake mdogo Nigga alisema maneno yale huku wakiinuka. “Kweli kabisa umeona magazeti hayo, hivyo vumilia siku ya leo kwa kukaa ndani, ili kesho tutakuwa tumepata sababu nzuri kabisa za kisheria kwamba tumeona picha katika magazeti, mteja wetu kuwa anatafutwa na polisi kwa tuhuma za Ujambazi, hivyo tumemleta tunaomba twende Mahakamani ili Serikali ikathibitishe tuhuma hizo.” Wakili Neema aliwaambia watu wale ambao walimuamini kupita kiasi kuwa atawasaidia katika kesi inayowakabili. Nigga alitoa noti ya shilingi Elfu kumi, akampa Faraja, kisha akamrudisha kwa mama yake, wao wakaaga na kutoka nje ya ofisi ile. Wakili Neema Faraja aliwasindikiza hadi nje ya ofisi yake akaagana nao. Nigga alikuwa ameshaitupia kofia yake hadi usoni, akaagana na wakili Neema kwa kupeana mikono, kisha akaingia kwenye gari na mama yake mdogo akaingia upande wa dereva wakaondoka.
Wakili Neema Faraja alirudi ofisini kwake, kuzungumza na wageni wake. “Dada Neema sijui hata nikupe nini yaani sikuwa na mawazo kama katika maisha yangu, ningeweza kushika Milioni tatu ziwe zangu, yaani hapa leo hiihii naondoka sina chakuniweka tena.” Shuwea Namjupa alimwambia wakili Neema pale alipokuwa amerudi kuwasindikiza wageni akawa ameketi kitako kitini kwake. “Shuwea utaondoka ila siyo leo wala kesho, kwani unajukumu zito unalotakiwa kulifanya ambalo bado hujalitimiza.” Wakili Neema Faraja alimwambia Shuwea maneno yale huku, akimtazama usoni mwake kwa makini. “Jukumu gani hilo tena ?!” Shuwea alimuuliza wakili Neema kwa mshangao. “Lakusimama Mahakamani, kutoa ushahidi dhidi ya madhalimu Nigga na wenzake ambao leo hii, watakuwa kama siyo wote basi baadhi yao watakuwa mikononi mwa Polisi.” Wakili neema alimjibu Shuwea Namjupa kwa utulivu. Wageni wale wote kwa pamoja walipigwa na butwaa kubwa sana, wakawa hawamuelewi kabisa wakili Neema kwani muda mfupi uliopita walizungumza vingine na sasa anabadili habari na kueleza vingine. “Lakini si umenambia nimepewa pesa ili niondoke hapa nisiwe shahidi, sasa tena mbona sielewi?!” Shuwea Namjupa alimwambia wakili neema sura yake ikiwa katika mshangao mkubwa sana. “Mimi ndiyo najua ninachokifanya Shuwea, wewe ulikuwa ukihitaji pesa sana kwa wakati huu uliotoka katika matatizo. Lakini kumbuka wale ni wahalifu, hivyo tambua maishani mwako kuwa haki hainunuliwi. Hizo pesa fanyia mambo yako na kizimbani utapanda kuwa shahidi.” Wakili Neema alimwambia Shuwea Namjupa aliekuwa hoi bin taabani kwa kuchoka kwa kauli ile. “Dada Neema wale wakishinda kesi hawataniua mie kwa kuchukua pesa zao, kisha nikawasaliti?” Shuwea aliuliza kwa hofu. Wakili Neema Faraja ili kumtoa wasiwasi Shuwea Namjupa, alimuonesha kitu kilichowaacha midomo wazi wote waliokuwa mle ndani ya osifi ile kasoro Faraja Joseph Kazi Nigga.
***
Nigga na Mama yake mdogo, waliondoka katika jengo lile la Sayansi na Teknolojia, pale Kijitonyama kwenye ofisi ya Wakili Neema, wakashika njia ya kuelekea Tandale kwa Mtogole. Walikuwa wakipita njia za ndanindani wakichelea kupita barabara kuu kwa kuchelea maaskari. Mkuu wa upelelezi alikuwa ameziacha gari tatu kutoka katika gari aliyokuwa Nigga na mama yake mdogo, akiwafatilia ili afike nao mwisho wa safari yao, pengine anaweza kupata faida zaidi. Akiwa katika kuwafatilia wahalifu wale mara simu yake ya mkononi iliita akaipokea. “Afande tupo kamili, tunaomba uelekeo tafadhali umenisoma mpaka hapo?” Sauti iliyokuwa ikizungumza upande wa pili ilimwambia mkuu wa upelelezi. “Nipo Tandale nakata kulia naelekea Sinza, kipusa kinasafirishwa na gari namba, Tango kenda ziro kenda, Alfa, Blavo, Julieth. Nimesomeka?” (T = Tango, Kenda = 9, Ziro = Sifuri, Kenda= 9. Alfa = A, Blavo =B, Julieth =J) yaani alimaanisha T 909 ABJ. Mkuu wa upelelezi alijibu huku akipunguza mwendo gari yake akipanda tuta la Tandale Magharibi pale shule, wakielekea Sinza Uzuri. Upande wa pili wa simu ile ukajibu. “Nimekusoma Afande tupo Ubungo mataa, tunapinda kulia kukamata barabara ya Morogoro, tunakuja kuingia hapo Shekilango ili kuwa nanyi Sinza.” Upande wa pili ulizungumza kisha ikakatwa simu ile. Safari ile iliendelea hadi walipofika makutano ya Barabara ya Sinza Uzuri na Shekilango, gari aliyokuwa Nigga ikapinda kushoto, kuelekea barabara Shekilango Sinza Kumekucha. Gari mbili zilizokuwa mbele ya mkuu wa upelelezi, moja iliingia sheli pale kwenye makutano yale, na ya pili ilipinda kulia kuelekea Sinza Palestina. Mkuu wa upelelezi alipinda kushoto, mara Daladala lililokuwa likishusha abiria katika kituo cha Sinza Kijiweni likaingia barabarani, likakaa mbele ya gari ya mkuu wa upelelezi, na mbele yake ikiwa Toyota Noar ya rangi nyeupe ambamo ndimo alimokuwamo Nigga na mama yake mdogo. Mkuu wa upelelezi aliipigia ile simu aliyokuwa akiongea nayo awali akatoa maagizo.“Nipo Kamanyola hapa barabara ya Shekilango, mmefikia wapi?” Upande wa pili ukajibu. “Tupo Rombo hapa kiongozi, tukijia huko Sinza.” Mkuu wa upelelezi, akawaamuru wageuze gari kwani adui amekaribia maeneo yale, naam askari wanne waliokuwa katika Toyota Corola TI New Model, waligeuza gari ile kwa haraka na mara wakaiona gari aina ya Noar iliyokuwa na namba tajwa ikipita taratibu, ikiwa na vioo vya kiza, ikielekea Barabara ya Morogoro, na wao wakaiingiza barabarani gari ile wakiwa mbele ya mkuu wao wa upelelezi. Lile Daladala liliingia kituoni kupakia abiria. “Maelekezo kiongozi tunamaliza hapahapa au ipoje?” Simu ya upande wa pili iliuliza, mkuu wa upelelezi akamwambia wanawafatilia hadi mwisho wa safari yao, watamaliza huko kwani wanaweza kupata faida zaidi ikiwa watakwenda nao hadi mwisho. Kisha simu ile ikakatwa ikawa watu wapo makini zaidi na jambo lile.
Nigga akiwa ndani ya gari na mama yake mdogo, akaamua ampigie simu Carlos Boga ili kujua kama Baba Ubaya yupo salama au amekamatwa, simu ya Carlos Boga ikaanza kuita na hatimae ikapokelewa upande wa pili. “Halow?”Sauti ya Carlos Boga ilisikika kwenye simu ile ikiitika kwa mashaka. Nigga akamsalimia kisha akamuuliza. “Ebwana nimempigia simu leo asubuhi Baba Ubaya simu imeita kisha ikakatwa, nimempigia tena simu yake ikawa haipatikani, je kuna usalama huko au Tafu Guy keshamvuta maana nimeona kwenye magazeti yaani tumecharaziwa kinoma wangu?” Carlos Boga alimtazama baba ubaya, aliekuwa pembeni yake akalaoud spika ili na mwenzake asikie. “Baba Ubaya tangu jana mie sijawasiliana nae, wewe upo wapi saa hizi mbona nimekupigia simu ulikuwa hupatikani, au ndiyo upo na wazee unanichekecha?” Carlos Boga alimwambia Nigga, huku akiwa makini na sauti zingine kama zitatokeza kwani hawakuwa na imani nae walikuwa wanamuhisi ameshakamatwa. “Mie nipo na Mama mdogo tunatoka kwa wakili, yaani nimeshaharibu kesi yote wangu, kama huniamini wewe sauti ya mama mdogo, unaifahamu tushafanya mgao sana nyumbani kwake, hebu ongea nae akutoe wasiwasi kwanza.” Nigga baada yakuzungumza maneno yale, akampa simu mama yake mdogo akazungumza nae, akathibitisha kuwa kweli yupo nae na wapo salama. “Poa mama nimekuelewa mpe simu huyo.” Mama mdogo wake Nigga akampa simu mwanawe akaendelea kuzungumza na mwenzake. “Mwana mie mwenyewe nilikuwa najua Baba Ubaya keshamalizwa, kwani jana simu yangu ilikwisha chaji, na kule nilipokuwa chimbo, kwa mama mdogo jana kulikuwa hakuna umeme, hivyo umeme umerudishwa asubuhi ndiyo nikapata nafasi yakuchaji simu, sasa tunaonana wapi kwani nina habari muhimu sana kutoka kwa Wakili. Tena nimeonana na yule Demu aliekuwa beki tatu wa Muhindi, kule tulipopiga pesa ndefu, yaani nimemaliza kabisa hakuna kitu wangu, nanyi nataka niwaambie kitu kama vipi mtafute na Baba Ubaya, ili tuwe wote niwaambie nini cha kufanya.” Nigga alimwambia Carlos Boga ambae sasa alimuamini kuwa kweli hakuwa kwenye matatizo. “Baba Ubaya nipo nae hapa, kama vipi njoo Tabata Kisiwani, pitia hapo mwanachi relini, sie tutakuona tulipo kisha tutakupa maelekezo.” Carlos Boga alimwambia Nigga kwenye simu ile. “Poa nakuja na mama mdogo sasa hivi kwani tupo, Shekilango hapa tunaingia boda la kushoto huku Makaburini kutokea njia ya Ubungo maziwa. Tutatokea hapo Mama Land, kisha tutaingia barabara ya mandela hadi hapo Tabata mwananchi, tutaingia kulia kuwafata.” Nigga alizungumza na simu ile kisha akakata ile simu huku akiwa na shauku ya kukutana na wenziwe. Walitembea wakapita njia aliyoisema hatimae wakafika Tabata Mwanachi, wakaingia kulia relini huku zile gari za Polisi zikiiacha ile gari kwa mbali kidogo kisha nazo zikapinda kulia wakihakikisha hawawapotezi kabisa machoni mwao. “Oyaa tumeshaingia hapa Relini, mpo upande gani?” Nigga alimpigia simu Carlos Boga akamuuliza. “Ahaa mmeshapinda ee, mpo na gari aina gani?” Carlos Boga alimuuliza Nigga, kwani sehemu aliyokuwa amekaa alikuwa akiziona gari zote zilizokuwa zikiingia na kutoka. “Tupo na Noar ya Mama mdogo ile nyeupe, tuliofaulushia mzigo siku ile bwana.” Nigga alimjibu jamaa yake. “Sawa hapo ulipo shuka wewe peke yako, kisha rudi nyuma huku Relini utatukuta tunakusubiri.” Carlos Boga, alikuwa anamchekecha Nigga wajue kama yupo peke yake kweli au yeye na mama yake wote wametekwa kisha wanawavuta. Nigga alimwambia mama yake. “Hawa wezi bado hawaniamini hivyo wewe nenda kapaki mbele mie nakwenda kuonana nao kisha nitakuja nao.” Mama mdogo wa Nigga alisimamisha gari, Nigga akashuka akawa akitembea kwa miguu akielekea relini barabara kubwa ya Mandela.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wale askari waliiona ile gari Toyota Noar ikisimama kule mbele, kisha Nigga akashuka akawa akitembea kwa mguu kurudi nyuma walipokuwa wao. Dereva wa Polisi alisimamisha gari yake, akavuta waya wa Boneti la gari yake haraka, kisha akatoka nje na kitambaa akalifungua boneti lile, akaufungua mfuniko wa Rejeta, moshi mwingi ukaonekana kutokana na Presha na joto la mashine ya gari ile, kila aliyoiona gari ile aliamini ilikuwa inachemsha asingetilia mashaka kusimama kwake katika hali ile. Mkuu wa upelelezi aliipita ile gari kama haijui, akawa anaifata Toyota Noar ilipokuwa inaelekea.akapisha na Nigga taratibu, bila kumtazama.
Nigga alikuwa ametembea hadi usawa wa gari ile iliyofunguliwa buti, akawa akiipita ile gari huku akizungumza na simu yake. “Oyaa sema mnazingua bwana, bado hamjaamini tu kuwa mie sipo na ugeni, sasa mmesimama wapi, naona mnanizeveza tu, kama hamniamini mie niende zangu bwana siyo tunauzishana sura tu!”
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment