Search This Blog

Saturday, 5 November 2022

MPITA NJIA - 4

 








Simulizi : Mpita Njia

Sehemu Ya Nne (4)





Katika kituo cha polisi Buguruni, Tafu alikuwa amejenga urafiki sana na yule mtu aliempa simu mle mahabusu, kwani walikaa pamoja na kuzungumza mengi tu. Mara mlango wa Mahabusu ulifunguliwa, askari mmoja akamtaka Dereva wa Pikipiki, atoke nje. Tafu alichomoka nje akafungwa pingu za mikono kwa nyuma, kisha akaongozana na askari wawili hadi kwenye gari yao akapakiwa ndani ya gari ile, akapelekwa katika kituo cha Sitaki shari kwa mahojiano zaidi. Tafu akiwa ndani ya gari. Alikuwa mpole sana kiasi unaweza kudiriki kusema kuwa Tafu ameonewa, wala hashiriki vitendo vya kihalifu. Kumbe habithi kama yeye hakuna. Ama kweli siku za mwizi ni arubaini.

Tafu alifikishiwa Muembeni moja wa moja, akawakuta watu wa kazi wanamsubiri. Aliwekwa kwenye kiti wanaume wakamzunguka wakaanza nae mahojiano. “Tafu tuambie ukweli, wewe tunajua umetumwa tu kuwafatilia wale watu, kisha ungelipwa ujira wako, je huyo aliekutuma anafanya kazi gani?” Tafu alidanganywa akichotwa akili zake waone atapindisha maelezo au atakubaliana nao. “Wazee kwa kusema ukweli mie yule mtu, huwa ananitumia tu kama kunituma au kumpakia kumpeleka katika mihangaiko yake, ila anafanya kazi gani kwa kweli sijui kabisa.” Wale askari walitazamana tena kwa siku ile ikiwa ni mara ya tatu. Walitizamana hasa kwa kutambua Tafu, anapindisha maelezo yake. “Ohoo sawa bwana, je unamfahamu Nigga?” Mkuu wa upelelezi aliendelea kumchecheza kwa maswali, ili kutambua kama anaongea ukweli au anadanganya. “Nigga wazee, mie simtambui kwanza hilo jina kwangu geni ndiyo leo nalisikia masikioni mwangu.” Wale askari walipandwa na hasira wakataka kumshushia kipondo cha Mbwa mwizi, laini mkuu wa upelelezi aliwazuia kwa ishara kuwa bado mapema sana, watulie kwanza kisha yeye akaendelea kumuhoji yule dereva. “Umesema Nigga humjui, je mtu anaeitwa Baba Ubaya unamfahamu?” mkuu wa upelelezi alipomuuliza swali lile alimtazama usoni moja kwa moja. Nigga aliwajibu askari wale kuwa hamfahamu. “Kwa hiyo hata mkewe Nigga wewe humtambui?” Mkuu wa upelelezi alimsaili kwa utulivu hatua kwa hatua na alishamuona kuwa anawadanganya. “Sasa wazee kama mtu mwenyewe simtambui, nawezaje kumtambua mke wake?” Mkuu wa upelelezi aligeuka akamtazama askari aliekuwa yupo makini, akampa ishara ya kichwa, yule bwana akapiga saluti, akatoka pale kwenye mwembe, baada ya dakika kama nne hivi akarudi pale akiwa na mke wa Baba Ubaya. Mkuu wa upelelezi akamuuliza Tafu; “Unamfahamu huyu mwanamke?” Tafu alimtazama mwanamke yule kisha akamkataa kuwa hamfahamu. Mkuu wa upelelezi alimgeukia mke wa Baba Ubaya akamuuliza. “Wewe unamjua huyu?” Mke wa baba ubaya akajibu kwa uchungu huku machozi yanamtoa. “Ndiyo namjua huyo ndiyo Tafu wazee, yeye huyo ndiyo anajua silaha zilipo.” Tafu alihamaki akamtolea macho yule Mke wa Baba Ubaya. “Wewe unanifahamu mimi, au unanitafutia matatizo tu, waambie ukweli wazee siyo unataka kuongopa ili unipe mie matatizo yako.” Tafu aliendelea kumkataa mke wa Baba Ubaya kuwa hamfahamu, ilihali kila askari aliekua pale alikuwa akitambua kuwa wanafahamiana.“Tafu umeweza kutudanganya jana ila huwezi tena kutudanganya na leo. Mjinga pa kwenda tu, pakurudi anajua pabaya na pazuri. Jana ulifanikiwa kuwatorosha wahalifu wenzako, lakini tambua kuwa sisi ni Serikali, na siku zote serikali ina mkono mrefu. Leo utatuambia kila kitu wewe, au utaondoka hapa ukiwa maiti, kwani hatujawahi kuja na mtu hapa ambae tunauhakika kwa asilimia zote kuwa ni muhalifu, tukamuhoji hapa kisha akaendelea kukataa, ukifanikiwa kukaza hadi mwisho usiseme basi wewe utakuwa ndiyo mtu wa kwanza. Sasa utani tunaweka pembeni, tunataka bunduki zetu.” Mkuu wa upelelezi aliposema maneno yale, akaamrisha vijana wa kazi, kutoa kipondo kwa Tafu. Askari wale wakiwa na mafunzo maalum ya kumtesa mtu, waliweza kutoa dozi yao, ikawa ndani ya dakika tano, Tafu hatizamiki kachakaa sana. Ila bado alikuwa anaendelea kukaza tu, kwani aliona bora kifo kwake kuliko kuwataja wenzake kisha ikawa kesi ambyo yeye ndiyo atakuwa ameifanya inyooke. Akaona atakwenda kufia jela akiwa kwenye mateso makali. Hivyo aliendelea kukomaa kuwa hamjui mtu yoyote kati ya wale aliotajiwa, lakini pia alimkana hata mke wa Baba Ubaya ambae ameshakaa nae sana, akiwa anamfahamu kwa makoko na matandu.

***

Baba Ubaya alimwambia rafiki yake Sirengo ampeleke nyumbani kwake, kwani kuna vitu vingi sana ambavyo hana risiti navyo vya wizi, pamoja silaha anayoimiliki kinyume cha sheria, akavihamishe kwani anatambua kuwa askari wale baada ya mahojiano na mke wake, lazima watakwenda kupekua nyumbani kwake, hivyo akaona muda ule ambao kabla hawajafika utakuwa ndiyo muda muafaka wa kwenda kuhamisha ‘mazibo’ Sirengo akamshauri achukue gari kubwa ili ahamishe vitu vyote vya nyumba nzima, ili ahame kabisa katika nyumba ile, lakini Baba Ubaya akamwambia wakaondoshe ‘Mazibo’ yaani vile vitu visivyokuwa na risiti tu, kwani vinawezwa kupelekwa Mahakamani kisha vikawa vielelezo muhimu wakaitwa walioibiwa wakenda kuvitambua vitu vyao, hiyo itakuwa ni kesi iliyosimama isiyokua na chembe ya shaka kabisa ndani yake. Baba Ubaya alimpigia simu Nigga kumfahamisha lengo lake la kwenda kuchukua vitu vyake kwake, lakini Nigga alimshauri vinginevyo kwenye simu. “Baba Ubaya watafute watu wakahamishe vitu vyote usiende wewe mwenyewe, kwani huwezi kujua wangu, unaweza kufikiri askari watakuja usiku kisha wakaja mchana wakakukuta upo, utajuta majuto makubwa sana wangu, bora kama vipi tuma watu tu.” Baba Ubaya alisikiliza ule ushauri wa watu wawili wote wakimtaka kuhamisha vitu vyote, lakini akaamua kushuka ndani ya gari ya rafiki yake, ili akijifanya kutafuta roli la kwenda kupakia mizigo yote. Baba Ubaya badala yake alichukua Taxi akaamua akaondoshe vitu vya thamani kubwa ambavyo alivipata katika wizi. Lakini asingeweza kumuagiza mtu akondoshe silaha ya moto ambayo ni Bastola. Angekuwa anazidi kujipalia makaa kwa jamii, kuwa yeye ni muhalifu.

Baba Ubaya alikwenda na taxi hadi nyumbani kwake akafungua geti na kumtaka derevawa wa taxi kuiingiza ndani gari ile, kisha akafunga geti kwa ndani baada ya gari ile kuingizwa ndani, yeye aliingia ndani ya nyumba yake akaingia kila sehemu kulipokuwa na vitu vya wizi alivitoa akaviingiza katika gari ile kwa haraka haraka, ili kupoteza ushahidi wa vitu vile vya haramu. Akaenda chumbani kwake akainua sofa dogo chini yake akatoa Bastola aina ya Chinese inayobeba risasi nane, akaivaa kiunoni mwake. Pia akachukua na risasi zilizokuwa katika boxi lake dogo, akiwa katika haraka haraka mara box lile likaanguka risasi zikasambaa pale sebuleni. Akawa akiziokota huku akiona zinamchelewesha mara akasikia muungurumo wa gari ukielekea nyumbani kwake kwenye geti lake akaacha kuokota akapagawa mara mbili ya mwanzoni. Mapigo ya moyo yakawa yanamuenda mbio kama saa mbovu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

***

Tafu Guy alikuwa hoi bin taabani kwa kichapo, akawa amelewa asijue kitu gani sahihi afanye aidha awaambie ukweli wazee au laa. Uso wake ulikuwa umemvimba sana,damu zilikuwa zikimmwagika kinywani mwake. Mara akasikia sauti isiyokuwa ngeni masikioni mwake ikimwita kwa kejeli na kumwambia. “Tafu Guy huna kitu utakachokificha rafiki yangu, sana sana utaumia tu bure kwani kila kitu kipo wazi kabisa. Nyoosha maelezo hayo wangu huna pakutokea katika hili.” Tafu kwa macho yaliyovimba aliuinua uso wake kwa shida, akamuona mtu ambae sura yake pia haikuwa ngeni machoni mwake. Ila kilichomfanya akaze macho zaidi kumtazama kwa makini, ni pale alipomuona yule bwana aliemwambia maneno yale akiwa amevaa sare za jeshi la Polisi na mkononi mwake ana cheo cha Koplo.

Tafu Guy alimtazama vizuri mtu yule moyo wake ukaingia ganzi isiyosemeka, kwani alikuwa ni yule mtu aliempa simu wakiwa mahabusu kule kituo cha Polisi cha Buguruni.

Tafu Guy alifedheheka sana, alikuwa mdogo kama nukta. Uso wake aliuelekeza chini kwa aibu, akawa hana budi ila kukubali matokeo, akawa mtiifu katika ule msemo usemao, kubali yaishe. Tafu Guy akakubali matokeo, akanyoosha maelezo akiwa ameshaumia, kwani hakuwa tena na namna ya kukwepea. Ama kweli ujinga donga la kichwa mkaguzi mkono.

Mkuu wa upelelezi alishauri muda uleule waende nyumbani kwa Baba Ubaya, kwani katika Maelezo yake Tafu Guy, alimtupia mpira Baba Ubaya kuwa ndiyo mwenye silaha. Hivyo mkuu wa upelelezi akaamua haraka waende wakapekue kabla hakujahamishwa silaha ikiwa kweli zimo ndani ya nyumba ile. Hivyo dakika kumi baadae wakawa na kila kitu muhimu kilichohitajika katika safari ile, hati ya upekuzi, askari wa kazi, silaha na Mke wa Baba Ubaya wakawa nae njiani kuelekea nyumbani kwa Baba Ubaya. Wakiwa katika magari mawili ya Polisi yenye namba za Kiraia, Kwenda kupekua nyumbani kwa Baba Ubaya. Walipofika Tabata nyumbani kwa Baba Ubaya gari zilikwenda moja kwa moja hadi katika geti lakuingilia magari. Askari Polisi walishuka katika magari yao wakaizingira ile nyumba kila pembe wakawa wapo makini kwa kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Mkuu wa upelelezi na mke wa Baba Ubaya, walikwenda pamoja kwa mjumbewa shina wa mtaa ule,ili akawe shahidi katika upekuzi walioukusudia. Walipofika kwa mjumbe askari mkuu wa upelelezi, akajitambulisha kwa mjumbe yule dhumuni lao la kwenda pale, mjumbe akaongozana nao hadi katika nyumba ya Baba Ubaya, walipofika pale wakalikuta geti kubwa limefungwa huku alama za matairi ya gari zikionekana kwa wazi kabisa pale chini ya ardhi usawa wa geti lile.



Mkuu wa Upelelezi aliwaamuru vijana wake wa kazi, kufanya kazi. Naam ilikuwa kama watu waliokuwa wakisubiri amri tu. Askari watatu shupavu waliparamia ukuta wa numba ile kwa tahadhali kubwa. Walipofika juu ya ukuta wakaweka pozi pale juu, kisha kila mmoja alichomoa silaha yake kiunoni mwake. Tendo lakuchomoa silaha lilikuwa likifanyika pamoja na kimya kimya bila kuzungumza neno. Kisha mmoja wa askari wale alihesabu kwa vidole kuwaoneshea wenzake, moja, mbili, tatu. Askari wale waliruka kwa mtindo wa Sarakasi wakabimbilika walipofika chini, kisha kila mmoja akawa amepiga goti moja chini, Bastola zao zikiwa mbele mikononi mwao, wakizielekeza huku na kule, kwa namna ya kumtafuta adui alipo, lakini hakukuwa na rabsha yoyote. Askari wale mmoja alifungua Geti dogo kwa ndani, ili kuruhusu wenzao pamoja na Mke wa Baba Ubaya na Mjumbe, kuingia ndani mle kwa shughuli waliyoikusudia. Nao wakajichoma ndani mle pale uwani, askari wakaizunguka ile nyumba huku umakini ukichukua nafasi kubwa zaidi.

Nyumba ile ilikuwa ipo kimya sana, hakukuwa na dalili ya mtu ndani yake. Kwenye uwa ule mpana wa nyumba ile kulikuwa na gari moja ndogo aina ya Toyota Vitz, ikiwa Imeegeshwa. Askari wale baada yakuingia pale uwani, wakamuuliza Mke wa Baba Ubaya kama anao funguo ya kufungulia mlango mkubwa wakuingilia ndani ya nyumba ile. Mke wa baba Ubaya akasema hana funguo pale alipo, funguo zilikuwa kwenye pochi yake iliyokuwa imebaki polisi. Mkuu wa Upelelezi wa kituo cha Buguruni akawaamuru askari wale kuuvunja ule mlango. “Mjumbe sheria inaturuhusu kama nyumba tunaitilia mashaka kuwa ina vitu vya hatari, basi sheria inaturuhusu kuvunja mlango ili kutoa vitu hivyo, kwa hiyo humu ndani tunamashaka kuwa na vitu vwa hatari kwa maana ya silaha. Tunatimiza wajibu wetu tuliopewa na sheria.” Baada yakusema maneno yale mkuu wa upelelezi akawaamuru vijana wake wauvunje mlango wa nyumba ile ili waweze kuingia ndani kwa ukaguzi. Vijana walikwenda kwenye gari yao nje wakarudi na shoka mbili kwa ajili ya kufanyia kazi ile.

***

Baba Ubaya aliposikia mlio wa gari ukielekea katika geti lake, jasho lilimtoka, woga ulimtawala sana. Akasogea dirishani huku akiikoki Bastola yake ili kuitumia. Akachungulia nje kwenye geti lake, akaiona gari ya jirani yake ikigeuza karibu na geti lake. Moyo wake uliokuwa ukipiga kwa kasi ukapoa, akashusha pumnzi ndefu, kisha haraka haraka nguvu zikamrejea mwilini mwake, akazirejea zile Risasi akajitahidi kuziokota moja baada ya moja kwani zilikuwa zimesambaa chini pale sebuleni kwake. Akiwa anaziokota zile Risasi, nafsi yake ikawa inamuenda mbio huku akisikia nguvu nyingine asiyoifahamu ikimuongoza kuondoka haraka mahala pale. Baba Ubaya hakusubiri tena, kuendelea kupoteza muda kwa kuziokota zile Risasi, aliziacha zile Risasi pale chini alizokuwa hajaziokota, Bastola yake akaifunga usalama wake ili katika mashimbo na mitikisiko isiifyatue ile Risasi iliyokuwa tayari ameshaivuta chemba ikisubiri kutolewa kuelekezwa sehemu lengwa. Kisha akaisweka nyuma ya kiuno chake kisha shati lake akawa hakulichomekea ili kuzuia kuonekana kwa silaha ile na dereva wa taxi au mtu mwengine yeyote awae. Kisha akachomoka mbio hadi uwani. Akaufunga mlango mkubwa wa uwani kwa funguo akamwambia dereva awashe gari kisha yeye akalifungua geti lile, dereva Taxi akatoa gari nje ya geti lile. Baba Ubaya alilifunga lile geti kwa funguo kisha akaingia kwenye gari ile akamuamuru dereva wake aendeshe gari waelekee Tabata Segerea. Dereva akaiondosha gari ile kwa mwendo wa taratibu akaelekea Tabata Segerea. Wao wakiwa wamefika Tabata Bima wakipinda kulia kwenda Tabata Segerea wakitokea njia ya Tabata Mawenzi, askari wakafika nyumbani kwake wakiwa wapo kamili gado. Wakipishana kwa takribani dakika tato tu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

***

Shuwea Namjupa, alikuwa akimnywesha uji, mwanawe lakini donge lilikuwa limemjaa rohoni mwake kwa kiasi kikubwa sana. Msafiri Namjupa, alikuwa amejilaza kitini akitafakari kwa kina maisha yake na matukio yaliyomkuta. “Dada mie naonelea nirudi nyumbani Lindi, kwani kazi iliyonifanya niwe katika mji huu, imeshatimia. Nilikuja kukuhangaikia dada yangu ili utoke gerezani, nashukuru Mungu sasa hivi upo nje ukiwa huru. Hivyo inanibidi mie sasa kurejea nyumbani kisha nina mpango wa kwenda Tunduru kusaka bahati yangu, nafikiria kwenda kuchimba Madini. Pengine Mungu anaweza kunipa huko kwani mji huu, nitaishia kupata pesa ya kula.” Msafiri Namjupa alikuwa akimwambia dada yake aliekuwa amemuona hana raha tangu jana yake walipokuwa wakishindana juu ya Mbuya Fabiola. “Mdogo wangu unajitafutia matatizo tu ya bure, kwani bahati Mungu hakupi mara mbili, ameshakupa ya Mbuya umeipiga teke basi huko utakwenda kufa tu.” Shuwea alimjibu mdogo wake huku akiwa amenuna kwelikweli, kwani alimuona mdogo wake ni punguani kwa bahati aliyoipata kisha akaichezea akaukumbuka ule msemo usemao, asiekuwa na bahati, habahatiki. “Dada yangu mie sipo kama utakavyo wewe, najua umeninunia kwa mie kukataa kukubali matakwa ya Mbuya, lakini dada yangu kila likuepukalo basi lina kheri na wewe.” Msafiri alimwambia dada yake huku akiinuka pale kitini na kukaa kitako. “Kaka yangu tupo wawili tu, maisha yetu niya dhiki, mie nina mtoto mdogo siwezi kuishi na mtoto huyu peke yangu bila ya kazi wala msaada kutoka kwa mtu mwengine. Hivyo kama kaka yangu ungekuwa na Mbuya, hata kama ungekuwa huna mapenzi nae ya dhati, Ila ungezuga nae tu tukala pesa zake mambo yetu yakatunyookea, tungebadilika kimaisha kuliko udhalili huu tulionao. Kodi ya nyumba pia inatushinda, kula yetu ya mashaka, hivi asingekuwa Mbuya sie tungekuwa wageni wa nani katika mji huu?” Shuwea Namjupa alizungumza kwa uchungu mkubwa sana, akiangalia maisha halisi wanayoishi ni maisha ya kimasikini sana. Alivyokuwa jela japokuwa alikuwa ni Mfungwa, lakini kila siku ya Mungu alikuwa haumizi kichwa kuhusu kula, japokuwa chakula kile hakikuwa na ladha kama chakula cha uraiani, lakini alikuwa akikipata. Kwani lilikuwa ni jukumu la Serikali kuhakikisha wafungwa wanakula kila siku ya Mungu, ijapokuwa walikuwa wakila mlo mmoja tu kwa siku, hadi kesho yake baada ya asubuhi kunywa uji, lakini alikwisha yazowea maisha yale. Kwani miaka miwili inatosha kumfanya mtu kuyazowea mazingira aliyopo. Shuwea aliona maisha ya kujitafutia tena na mtoto mdogo ambae ana mahitaji anayoyataka, hakika yalimsumbua sana. Akamuomba Mungu awabadilishie maisha. Msafiri Namjupa aliinuka akenda kuchukua kopo la maji na mswaki wake mkononi, akatoka nje ili kukwepa maneno yaliyokuwa yakimuumiza sana moyo wake kutoka kwa dada yake. Hakika moyo wake ulikuwa umekufa ganzi kwa Mbuya Fabiola.

***

Mbuya Fabiola alikuwa amekaa akiwa na Iddy Teva, katika mgahawa mmoja ila hakuwa na raha moyoni mwake, afya na muonekano wa Iddy Teva hakuufurahia hata kidogo, alimtazama kwa makini kisha akamuuliza kwa utulivu. “Iddy nakuona siha yako haipo vizuri, kwani kabla hujenda jela hukuwa hivi, ulikuwa na siha njema lakini sasa nakuona upo dhaifu, vipele tele mwilini mwako, ngozi yako imejaa harara, nywele zako zimebadilika zinakuwa za shombe, vipi kulikoni?” Iddy Teva, alishushia funda la juice kinywani mwake kisha akashusha pumzi ndefu akamwambia. “Mbuya, nitakwambia ukweli wangu. Nikiwa jela nilikuwa nakula vyakula ambavyo havina virutubisho, hivyo afya yangu ikayumba sana, nilikuwa naumwaumwa mara kwa mara, jamaa wakanambia kuwa ni kwa sababu ya vyakula. Ila nilipokwenda kupima afya niligundulika nimeathirika naishi na virusi vya Ukimwi.” Mbuya Fabiola juice ilimpalia, akakohoa sana aliposikia maneno yale, mwili wake ukaanza kumtoka jasho jingi, presha ikaanza kumpanda. “Iddy umesema umefanyaje?!” Mbuya alimuuliza swali lile kama hakusikia namna Iddy Teva alivyoeleza awali. “Mbuya huu siyo wakati wakuficha maradhi, huu ni wakati wakujitambua. Usikubali kuendelea kukaa kigani njoo kwenye mwangaza uonekane ili usaidiwe. Mie nimepima virusi vya Ukimwi nimekutwa ni Muathirika, hivyo lazima nikwambie na wewe ukapime afya yako, pengine unaweza ukakutwa mzima.” Mbuya Fabiola alishusha pumzi nzito, kisha akashika mikono yake kichwani, midomo yake mate yalimkauka akawa anapitisha ulimi wake ili kuupa mate. Aliinua uso wake akamtazama Iddy Teva kama ndiyo anamuona mara ya kwanza siku ile. Hakika Mbuya alichanganyikiwa sana. Hakuwa na amani katika nafsi yake. Machozi yalimtoka bila kujitambua, alitingisha kichwa chake kushoto kulia kwa masikitiko makuu. Mbuya hakutaka kukaa tena pale, alichanganyikiwa sana aliinuka akaondoka sehemu ile huku akifuta machozi, akamuacha Iddy Teva amekaa ameshangaa. Iddy Teva aliinuka pale alipokuwa amekaa akamfata Mbuya, akawa anamwambia kwa upole. “Mbuya huna sababu yakulia njia nzima. Using’atwe na Mbwa ukatangaza kidonga. Twende tukapime ili ujitambue kwani kuishi kwa mashaka siyo vizuri, naweza mie nikawa nimeathirika wewe ukawa ni mzima, na ikiwa nawe utakutwa umeathirika, basi utakuwa umejitambua. Mie nisingekwenda jela nisingejua yote haya, lakini hakuna mtu aliejela akawa na Virusi kisha asijulikane kutokana na lishe duni inayopatikana kule. Hivyo nakushau….” Iddy Teva hakumalizia kauli yake Mbuya alimkatisha kwa ukali. “Niache usiniambie mambo yako, ushanipa Ukimwi mie unanihubiria nini, ushaniharibia ndoto za maisha yangu, nawezaje kumwambia baba yangu kuwa nimeathirika mie. Naomba kuanzia leo hii, usinifate tena endelea na maisha yako achana na mie kabisa, au nitakufanyia kitu mbaya!” Mbuya baada yakusema maneno yale, akasimamisha Bajaji iliyokuwa ikipita barabarani akaingia na kumuamrisha dereva ampeleke hospitali ya kulipia iliyokuwa na vipimo vizuri ili akacheki afya yake. Dereva aliigeuza bajaji yake akaelekea mjini. Iddy Teva akajilaumu, kwa nini amemwambia ukweli badala yake kumbe angemdanganya, lakini alikuwa keshasema ukweli. Ama kweli kweli inauma.

***

Wakili Neema Faraja alikwenda TRA, pale mkabala na ‘Strongroom’ akaingia ndani ya ofisi zile, akamkuta mdada mmoja akiwa anawahudumia wateja wenye shida mbalimbali, nae akasubiri hadi zamu yake ilipofika akaulizwa asaidiwe kitu gani katika ofisi ile. Wakili Neema faraja alitoa kitambulisho chake akajieleza kisha akasema haja yake kwa yule muhudumu. Yule dada aliandika kwenye karatasi namba aliyopewa na Waili Neema kisha akamuomba asubiri kidogo kisha yule dada akapanda juu ya jengo lile ili kufatilia ile namba aliyokuwa nayo mikononi mwake. Baada ya dakika zipatazo kumi hivi yule dada alirudi na jalada kubwa, akachukua karatasi akajaza vitu alivyokuwa akivitaka wakili Neema kisha akamkabidhi ile karatasi na yeye kulirejesha lile jalada pahala alipolitoa awali. Wakili Neema aliitazama ile karatasi kwa makini, kisha akaiingiza katika mkoba wake, akatoka katika ofisi zile akawa anaelekea katika gari yake alipoiegesha. Mara simu yake ikaanza kuita. Wakili Neema Faraja aliitazama ile namba ya simu akaiona ni namba ngeni, ila kwa kazi yake amekuwa akipigiwa simu na watu mara kwa mara, hivyo akaipokea simu ile akaiweka sikioni. Upande wa pili wa simu ile ulijitambulisha kwa ufupi ukaomba kukutana nae muda ule kwa kile kitu kilichoelezwa ni muhimu sana na cha dharula. Wakili Neema akakubaliana na yule mtu aende ofisini kwake ili wakazungumze, akamuelekeza mahali ofisi zake zilipokuwa na yule mtu akaahidi kwenda muda si mrefu. Wakili Neema alikata simu akaiweka mfukoni kwake akaifikia gari yake, akafungua mlango akazama ndani akaiwasha gari ile na kuondoka kuelekea ofisini kwake.

***

Mkuu wa upelelezi aliwaamuru askari wavunje mlango ule, mara walipofika pale na shoka zao. Askari wale wakaanza kupiga shoka katika kitasa cha mlango ule, na mara ule mlango ukaachia. Askari wale waliziweka shoka pembeni wakenda wale askari walioruka ukuta wakaesabu kwa mtindo uleule wa vidole bila kutoa sauti kisha waliusukuma ndani ule mlango kwa nguvu, na wao wakalala chini kifudifudi kwa pamoja kwa haraka. Walilala vile huku silaha zao zikiwa zimetazama mbele tayari kwa kushambuliana na adui. Walipoona kimya hakuna upinzani, kwa haraka wakasimama huku bastola zao zikiwa wamezishika kwa mikono miwili, zikiangalia juu zikiwa usawa wa masikio yao, wakagawana wawili wakawa kila mmoja anatembea na ukuta wake na yule mtu wa tatu yeye alikuwa ameelekeza silaha yake mbele, macho yake yakitazama mbele, kidole chake kikiwa kwenye Trigger tayari kwa kufyatua risasi mara moja. Walitembea na korido ile hadi wakatokezea sebuleni. Walipohakikisha pahala pale ni salama askari mmoja alitoka nje uwani akasema kuwa; “Mkuu huku ni showari kabisa, mtuhumiwa hayupo hivyo hakuna upinzani.” Baada ya askari yule kusema maneno yale kwa mkuu wake huku akipiga saluti wakati akimwambia maneno yale, Mkuu wa upelelezi aliingia ndani ya nyumba ile pamoja na Mjumbe, na Mke wa Baba Ubaya. Walifika sebuleni, asakri wale pamoja na Mke wa Baba Ubaya na Mjumbe, walipigwa na butwaa pale walipozishuhudia Risasi karibu Kumi na mbili zikiwa chini katika zulia sebuleni pale zimesambaa. “Mjumbe unaona, hizi ni Risasi za silaha aina ya Chines, tena ni mpya hizi inaonekana kuwa jirani yako anamiliki maboxi kwa maboxi ya risasi pamoja na silaha zake. Hivyo tunaomba uwe shahidi katika hili.” Mkuu wa Upelelezi alimwambia Mjumbe wa shina, kuhusu zile Risasi zilizokuwa pale chini. Kisha kupitia simu yake ya mkononi Mkuu wa Upelelezi alizipiga picha zile Risasi pale kwenye zulia, kisha akatoa glovu pamoja mfuko maalum mifukoni mwake akazivaa zile glovu. Akaziokota risasi zile na kuziweka katika ule mfuko maalumu wa plastiki mweupe alioutoa pamoja na glovu mfukoni mwake. Baada yakuziokota Risasi zote, walikagua sebule yote, kisha wakataka kuvunja mlango wa chumbani kwa Baba Ubaya baada yakuulizwa Mkewe chumba chao kipo wapi, na yeye akaonesha. Walipojaribu kuufungua mlango ulikuwa wazi haujafungwa, hivyo walimuingiza mjumbe kwanza ndani ya chumba kile kisha wakaingia wao na Mke wa Baba Ubaya, walipekuwa lakini hawakukuta kitu kingine cha maana kwao. Mkuu wa Upelelezi, alitoa simu ya Mke wa Baba Ubaya, akamwambia ampigie mumewe, amwambie ende pale nyumbani kwake kuwa kumetokea matatizo ya umeme, hivyo afike mara moja. Mke wa baba Ubaya aliichukua ile simu yake akabonyeza namba za simu za Baba Ubaya, kwenye mtandao wa Airtel simu yake ikawa inaita upande wa pili. “Halow”? Baba Ubaya aliipokea simu ya mkewe huku akihema sana. Ndipo Mkewe alipomwambia kama alivyoelekezwa na Polisi. Lakini baba Ubaya alisema maneno yaliyowafanya askari wale watizamane na kutingisha vichwa vyao.



“Nisikilize wewe mwanamke, hayo majanga yako uliyoyatafuta yamalize mwenyewe, hiyo ndiyo faida ya ubishi. Natambua kuwa upo na askari na kwa taarifa yako wakati unakamatwa na polisi pale Tabata Sheli, mie nilikuwa nipo jirani na wewe. Hivyo mchezo wote nimeuona. Kwa hiyo tafuta njia nyingine ya kunivuta siyo hiyo, mie sidanganyiki wala sivutiki kizembe hivyo. Ungenisikiliza nilivyokuasa uiache ile gari yote hayo yasingetokea, ila kwa sababu ya ubishi wako. Leo umeona faida ya ubishi malizana nao hao watu wako.” Baba Ubaya aliposema maneno yale, wale askari Polisi walitingisha vichwa vyao kwa masikitiko, hasa waliposikia kuwa Muhalifu wanaemtafuta alikuwepo katika eneo la tukio. Mkuu wa upelelezi aliikata simu ile, kisha akaiweka mfukoni mwake ikiwa ipo on. “Hebu naomba picha zote za mumeo tafadhali.” Mkuu wa upelelezi alimwambia mke wa Baba Ubaya. Mwanamke yule aliwaonesha albam zilipo pale chini ya meza, mkuu wa upelelezi aliinama akazichukua albam mbili zilizokuwa pale akaanza kuzipekua. Mara akakutana na picha iliyokuwa imepigwa Bar ikiwa inaonekana wanaume watatu wamekaa katika meza iliyochafuka chupa za bia na nyama choma. Mkuu wa upelelezi alimgeukia mke wa Baba Ubaya akamuuliza. “Unaweza kunitajia hawa ni kina nani?” mke wa baba Ubaya aliitazama ile picha kisha akaanza kutaja majina ya watu waliokuwa wakionekana kwenye picha ile. Huyu aliekuwa amekaa kati ndiyo mume wangu, huyo wa kushoto kwake ni Nigga, na huyo wa kulia kwake ni Carlos Boga,” mke wa Baba Ubaya alimjibu mkuu wa upelelezi, kama alivyoulizwa. Mkuu wa upelelezi aliibandua ile picha kutoka katika albam iliyokuwepo kisha akasema. “Nina kazi na picha hii, hivyo ninaichukua” Mke wa Baba Ubaya hakuwa na pingamizi alibaki kuwa mpole “Huyu ameona kweli wakati mkewe anakamatwa na ndiyo maana ameondoka humu, hivyo turudini kituoni tukajipange upya namna yakumkamata huyu na wenzake wote waliokuwa katika mtandao wa Kihalifu. Kwani kufukia sasa watu hawa watakuwa wameshapashana habari juu ya tukio hili la leo, hivyo watakuwa wanajiandaa kutoroka au wanakimbia kwenda mbali nje ya mkoa huu” Mkuu wa upelelezi aliwaambia wenzake, ikawa hakuna wakupinga. Mjumbe alishukuriwa akapewa namba za simu na mkuu wa upelelezi ili akimuona Baba Ubaya amekwenda pale nyumbani kwake, aweze kupiga simu Polisi. Kisha na wao wakachukua namba zake za simu wakamruhusu ende akaendelee na shughuli zake. Polisi wale waliondoka mahala pale akabakizwa askari mmoja aliekuwa amevaa nguo za kiraia. Awe katika maeneo ya jirani na nyumba ile bila kutambuliwa na watu kwamba yeye ni askari, ili atoe taarifa kama ataonekana Baba Ubaya eneo lile. Kisha wao wakashika njia kurejea kituoni sanjari wakiwa na mke wa Baba Ubaya.

***http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Mbuya Fabiola, alikuwa anatoka hospitali akiwa analia machozi yakim mwagika sana. Alikuwa ametaharuki vibaya mno. Macho yake yalimvimba kwa kulia. Aliingia katika Taxi akamwambia dereva ampeleke Mtoni Kijichi. Dereva Taxi aliwasha gari huku akimwambia bei abiria wake, ambae wala hakubisha pia hakutaka kulilia hali. Kwani alikuwa keshavurugwa. Mbuya alipofika nyumbani kwao, akamlipa pesa dereva wa Taxi ile aliyoitaja ambayo alijua ataombwa apunguze bei, lakini ikawa kinyume chake. Aliliendea geti akabonyeza kengele ya pale mlangoni nje ya nyumba yao, mlinzi akamfungulia mlango. Mbuya aliingia ndani kwao akiwa mnyonge sana na mwenye kilio kisichojificha. Alipoingia sebuleni alikutana na baba yake amekaa sebuleni akitazama Runinga. Kapteni Fabiola alipomuona mwanawe analia, akakaa vyema ili kujua kilichomsibu. Mbuya alimuamkia baba yake, kisha akataka kupitiliza ili aingie ndani lakini baba yake alimwita. “Wee Mbuya kuja hapa, unakuja na kilio namna hivyo umepatwa na nini?” Mbuya alisimama pale alipokuwa amefika kisha akageuka na kwenda pale alipokuwa baba yake akakaa pembeni yake, kilio kikubwa kikamtoka Mbuya Fabiola mbele ya baba yake. “Baba nakufa mie, nimetoka hospitali kupima afya yangu nimegundulika nina virusi vya Ukimwi.” Mbuya Fabiola alipofika sehemu hiyo akazidisha kilio sana. “Pole sana mwanangu, dah ama kweli Ukimwi umekuwa ni adui mkubwa katika familia yangu.” Mbuya alipomsikia baba yake anasema vile akamshangaa sana. Akanyamaza kulia akafuta machozi kisha akamuuliza. “Dady Ukimwi umekuwaje adui mkubwa katika familia yetu?!” Kapteni Fabiola aliinamisha kichwa chake chini kwa muda bila kusema kitu. Hali ile ilimpa wasiwasi Mbuya yakutaka kujua kulikoni, kwani haikuwa hali ya kawaida kwa baba yake, aulizwe jambo kisha ainame namna ile tena bila majibu. “Dady, hebu niambie vizuri, kuna mtu yeyote katika familia yetu aliekufa kwa Ukimwi?!” Kapteni Fabiola, alipoinua kichwa chake, uso wake ukaonekana umemjaa simanzi ya hali ya juu, japo hakuwa akitokwa na machozi, lakini dhahiri shahiri alionekana ni mtu mwenye huzuni isiyosemeka. “Mwanangu Mbuya, kwanza nisamehe sana mimi baba yako kwa kukuficha, muda mrefu kuwa wewe ni muathirika!” Kapteni Fabiola aliposema maneno yale, Mbuya akatoa macho, kama mjusi aliebanwa na mlango. “Dady unasema umenificha kuwa mie nimekuwa muathirika kivipi, mbona sikuelewi?” Mbuya alikuwa amechanganyikiwa kupita maelezo, kwani yeye alikuwa akilia sana wakati alipojitambua kuwa ameathirika. Tena lawama zote alikuwa akimtupia Iddy Teva kuwa amempa maambukizi, alimtupia yeye kwa sababu Iddy Teva ndiyo mwanamme wake wa kwanza maishani mwake, ndiyo mwanamme aliemtoa usichana wake, hivyo kwake Iddy Teva alikuwa ndiye mtu pekee aliebahatika kufanya nae mapenzi katika umri wa miaka kumi na minane aliyokuwa nayo. Hakuwa na mwanaume mwengine. Hivyo kuchanganyikiwa kwake alikuwa akijishauri pindi angeulizwa na baba yake mtu aliempa virusi, lakini badala yake anaambiwa yeye alikuwa ni muathirika wa VVU wa muda mrefu! “Mwanangu marehemu mama yako, alikuwa ni muathirika wa VVU. Nawe umeambukizwa virusi hivyo kutoka kwa marehemu mama yako. Kwani wakati tunagundua kuwa mama yako ameshaathirika, wewe ulikuwa ukinyonya mwanangu. Tulikwenda kukupima tukagundua kuwa nawe umeshaathirika. Maambukizi uliyoyapata kutoka kwa mama yako. Wakati ule wa mimba yako, miaka kumi na minane nyuma nchini kwetu Tanzania, wataalamu wa mambo ya afya walikuwa bado hawajagundua dawa za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Hivyo tulikuachisha ziwa la mama kunyonya, ukaanza kunyonya maziwa ya kopo, na tumetumia gharama kubwa sana za kipesa, ikiwamo kuwa unakula vyakula vyenye virutubisho, mboga za majani na matunda ili afya yako iimarike na kweli karika umri wa miaka uliyonayo, leo ndiyo umejitambua kuwa wewe ni muathirika wa VVU.” Mbuya alishusha pumzi ndefu sana, akamsikitikia Iddy Teva alikuwa amemlaumu kuwa amemuathiri kwa kumpa virusi, kumbe yeye atakuwa ndiyo aliemuambukiza mtoto wa watu. Mbuya aliinama pale alipokuwa amekaa, akainua uso wake kumtazama baba yake. Akamuona baba yake anaukwepesha uso wake wasikutane macho yao. “Mwanangu umerithi mali yote kutoka kwa mama yako, ni kwa sababu wewe ndiyo mtoto wetu wa pekee, kwani baada ya kuachishwa kunyonya, mama yako aliugua kwa muda mrefu, kiasi ya miaka mine hadi roho yake ilipoacha mwili wake. Hivyo ndivyo ilivyokuwa mwanangu, na ndiyo maana mie nilikuwa mkali zaidi kwa watoto wa kiume, kwani ukiwa ni muathirika unapofanya ngono, huongeza athari za kuzipunguza zaidi kinga zako za mwili. Na inaweza kukupelekea kufa haraka.” Kapteni Fabiola alimwambia mwanawe bila yakumtazama usoni. Alikuwa akimuonea huruma sana, kwani Mbuya bado alikuwa Ubwabwa wa shingo bado haujamtoka. “Samahani Dady, unataka kuniambia na wewe pia ni muathirika?!” Mbuya alimuuliza swali gumu baba yake huku akimtazama bila kupepesa macho. “Mwanangu unauliza makalio ya mbwa wakati mkia unauona? Mie pia nimeathirika ndiyo.” Mbuya alimtazama baba yake, roho yake ikamuuma sana, akamuuliza baba yake kwa uchungu. “Dady hebu niambie ukweli nani alieleta Ukimwi katika familia yetu?” Kapteni Fabiola alitikisa kichwa kama mtu aliekuwa akilisubiri swali lile. “Alieleta ukimwi katika familia yetu ni ajali mwanangu.” Mbuya hakumuelewa baba yake akamuuliza kwa mshangao. “Ajali?! Unamaanisha nini sijaelewa.” Mzee Fabiola alikohoa kidogo kisha, akamjibu mwanawe kwa utulivu. “Mama yako akiwa na mimba yako ya miezi miwili, walipata ajali ya gari iliyouwa watu wengi, na kuwajeruhi pia. Hivyo mama yako nae alikuwa ni miongoni mwa majeruhi wale, alichanika mguuni damu nyingi zikamtoka, lakini pia hakuweza kuzuia damu za majeruhi wengine kumgusa pale katika jeraha lake, na ndipo matatizo yalipoanzia hapo mwanangu.” Mbuya Fabiola alilia sana alipotambua kiini cha matatizo ya familia yao kuwa wameathirika kutokana na ajali, kasha yakazaliwa majanga yote yale kwao. Baba yake akambembeleza sana, na mara kuna kitu kikawasitua wote wawili wakawa katika mshangao.

***

Wakili Neema Faraja, aliegesha gari yake nje katika jengo la ofisi yake, akashuka ndani ya gari na kutaka kupiga hatua kuingia ndani ofisini mwake, mara akasikia jina lake likiitwa. “Wakili Neema” kisha Yule aliekuwa akimwita alimfata pale alipo akamsalimia na kumwambia. “Samahani nimekuja na mwanangu mtoto wa marehemu dada yangu, anamatatizo ya kisheria yamempata, hivyo alikuwa akiuhitaji msada wa kutetewa ndiyo nimekuja nae ili tuzungumze ikibidi tukulipe kabisa ili ufatilie jambo hilo.” Alizungumza Yule mgeni aliekuwa nae pale. “Ohoo sawa twendeni ndani ofisini tukazungumze, tusiongelee hapa.” Wakili Neema Faraja aliongoza njia wakaelekea ofisini kwake na wageni wale wawili. Walipofika ofisini wakili Neema alitoa funguo katika mkoba wake, akafungua mlango wa chumba cha ofisi akawakaribisha wageni wale. “Karibuni sana, kama nilivyowaelekeza hapa ndiyo ofisini kwangu. kisha sura yako siyo ngeni machoni kwangu, vile tulionana wapi hebu nikumbushe.” Wakili Neema Faraja alimwambia Yule mgeni wa kike alieongozana na kijana wa kiume. “Mmmm kweli sasa unaanza kuzeeka, mie tulikutana Mahakama ya Temeke, ulikuwa na kesi ya kijana mmoja Yule siku ile tulikuwa tukiongea mimi na wewe, hadi ikatokea tafrani.” Wakili Neema akamkumbuka Yule mama aliekuwa akiongea nae kisha ukatokea mtafaruku wa Msafiri kukamatwa na Polisi kituuteni. “Naam nishakukumbuka ndiyo maana nikasema sura yako siyo ngeni machoni mwangu, kwani siku ile tulizungumza na nikakupa cadi yangu ya namba za simu, ukanambia umependenda nilivyomtetea Yule kijana, hivyo ukaomba mawasiliano yangu. Leteni habari nawasikiliza” Yule mgeni akamgeukia Yule kijana akambonyeza kwa kumpa ishara ili azungumze. “Eee dada mie nimekuja nina http://deusdeditmahunda.blogspot.com/matatizo yamenipata hivyo nahitaji sana msaada wa kisheria. Mama mdogo amenambia umahiri wako, hivyo naomba sana unambie ujira wako ni kiasi gani ili nione kama ninaweza kukulipa ili unitetee kwani hali imekuwa tete sana kwa upande wangu dada yangu.” Yule kijana alimwambia Wakili Neema Faraja, huku akitazamana nae usoni. “Malipo inategemea na kesi ipoje, yaani kesi gani ipo wapi, kama ipo Polisi au Mahakamani, kisha baada yakujua hayo ndipo linapokuja suala la kesi hiyo itagharimu kiasi gani, hasa kutokana na wingi wa Mashahidi wa kesi husika, lakini pia imesimamaje. Kwa hivyo basi nieleze kama unakesi polisi, kesi yenyewe ni nini au kama una kesi iliyopo mahakamani basi unambie ipo mahakama ipi, na ni kesi gani.” Wakili Neema Faraja, alimwambia Yule mteja wake aliekuwa ofisini kwake. “Mie bado sijafikishwa Mahakamani, lakini pia bado sijakamatwa! Ila naona kama muda si mrefu naweza kupatikana ndiyo maana nimechukua nafasi hii kukuona ili unitetee.” Alimaliza Yule kijana maneno yake ambayo yalimuacha hoi wakili Neema. “sasa mtu ambae hujakamatwa wala hujafunguliwa kesi mie nakutetea vipi hapo?” Wakili Neema Faraja alimuuliza Yule kijana aliekuwa hodari wa kujieleza. “Ipo hivi, mie nikwambie ukweli ni mjanja wa mjini wa mambo yetu yakutafuta mkate wa kila siku, sasa kuna jambo linanipa tabu sana kwani natafutwa na Polisi, kwa tuhuma za ujambazi ambazo kweli mimi ni mshirika wa mambo hayo. Na ujambazi huo nimeushiriki mimi mwenyewe kwa kuupanga na kuucheza, sasa natafutwa na Polisi kwa Udi na Uvumba. Hivyo ninachotaka ikiwa tutakubaliana basi mie nikulipe pesa zako zote, kisha wewe unichukue na kunifikisha kituoni. Wale wakiona wakili ndiyo amenipeleka mwenyewe kwa maana yakujisalimisha, basi hawatanipiga ila nikiwa nipo peke yangu haki kwa upande wangu haitatendeka. Nitapata kibano sana naweza kupata ulemavu wa kudumu kama siyo kufa kabisa. Hiyo ndiyo shida yangu kubwa sana wakili.” Wakili Neema Faraja alimtazama vizuri Yule mtu, huku akiwa anachezea simu yake, kisha akamuuliza kwa utulivu mkubwa. “Umesema wewe bado hujakamatwa ila polisi wanakutafuta. Unataka mie nikuchukue nikupeleke Polisi ikiwa nimekusalimisha sawa, lakini ni vyema nikajua hilo tatizo linalokufanya utafutwe na Polisi, ili nijue namna gani naweza kukusaidia.” Yule kijana akafikiri kidogo kisha akaanza kufunguka. “Naitwa Joseph Kazi, ila jina maarufu naitwa Nigga. Takribani miaka miwili nyuma nilifanya tukio la uhalifu Upanga kwa wahindi, hivyo kabla ya uhalifu ule nilikuwa nimezoeana na kuanzisha mahusiano ya kimapenzi na dada wa kazi anaeitwa Shuwea Namjupa.” Nigga alisimama kuzungumza kwani alimuona wakili Neema macho yamemtoka pima.

Wakili Neema faraja moyo wake ulipiga sarakasi, aliposikia habari ile akafanya tendo la haraka!





Wakili Neema Faraja, alimwambia Nigga; “Samahani naomba nimtumie ujumbe mtu wa chakula asiniletee kwani sijisikii kula.” Nigga na mama yake mdogo wakakubaliana nae. Wakili Neema badala ya kutuma ujumbe kama alivyosema, kwa haraka akabonyeza simu yake hadi akafika sehemu ya kurekodia, akabonyeza kitufe cha record kisha akamwambia Nigga aendelee keshatuma ujumbe sehemu husika. “Mbona umeonekana kustuka nilipokutajia jina la Shuwea Namjupa, vipi unamfahamu?!” Nigga alimuuliza wakili Neema Faraja, huku akionesha mshangao usoni mwake. Wakili Neema alikuwa amesoma saikoloji hivyo alimgundua Nigga wasiwasi wake akamtuliza. “Kilichonifanya nishangae ni kwamba, tukio ulifanye miaka miwili nyuma, Polisi waje kukutafuta sasa hivi kulikoni?” Nigga alitulia akamjibu. “Polisi walikuwa wakitutafuta muda mrefu, ila walikosa kujua tulipo kwa sababu hawakuwa na mtu wakuwapa taarifa zetu, nami yule mwanamke hakuwa akipajua nyumbani kwangu, hivyo yule mwanamke Shuwea Namjupa sasa hivi ninavyoongea na wewe, ametoka Jela yupo nje. Tangu jana aonekane na rafiki yangu tuliocheza wote ule mchezo Baba Ubaya, watu watatu washakamatwa hivi wapo ndani.” Nigga alimueleza wakili Neema akiwa hana habari kabisa kuwa kutoka jela kwa Shuwea Namjupa ni kutokana na juhudi zake. “Ahaa kama nimekuelewa vyema, unahitaji msaada wangu kipindi hiki ambacho yule dada Shuwea ametoka jela na kwamba yeye anaweza kuwa shahidi wa Polisi ikawa matatizo kwenu si ndiyo?” Nigga alisogea pale kitini akiwa ni mtu alieguswa hasa akajibu. “Naam khaswaaaa, hapo yule mwanamke akiletwa kwenye gwaride la utambulisho atatutambua, pia atakwenda Mahakamani kutoa ushahidi kwani yeye alikuwapo katika eneo la tukio, hivyo ni shahidi muhimu sana, ni mtu pekee tunaemuhofia sijui utanisaidiaje juu ya hilo.” Wakili Neema Faraja, alimtazama kwa makini Nigga, akamgeukia mama yake mdogo kisha akamuuliza Nigga. “Yule mwanamke alikuwa ni mpenzi wako?” Nigga akamjibu huku uso wake ameuinamisha chini. “Alikuwa demu tu siyo kama nilikuwa na mapenzi nae hapana, ila nilianzisha mahusiano nae kwa vile alikuwa akifanya kazi za ndani kwa muhindi lengo langu hasa lilikuwa nikukaa nae karibu, niyasome mazingira ya mle ndani kisha nifanye dhumuni langu, jambo ambalo lilifanikiwa.” Wakili Neema alimsikiliza Nigga huku akiitupia macho simu yake kama inaendelea kurecord sawasawa. “Sasa naweza kukusaidia ila nisikilize kwa makini sana, kama utanielewa basi tambua kesi hii unayotafutwa kwayo haitakufunga, ila kama ukinipuuza basi hata kama nitakutetea Mahakamani kwa ushahidi uliopo hautakwepa kifungo.” Nigga alikuwa ametulia tuli amepoa kama maji ya mtungi, alikuwa hana pingamizi ila kumsikiliza wakili anachosema kwake. “Shuwea Namjupa unajua kama ulimpa Mimba na sasa hivi ana mtoto wako?” Nigga alimuangalia mama yake mdogo kwa mshangao kuwa huyu wakili amejuaje jambo hilo, lakini mama yake mdogo hakumtazama bali alikuwa ametoa macho kwa wakili tu. “Nakumbuka aliwahi kunambia kuwa ana mimba yangu ni kweli, lakini wewe umejuwaje hilo?!.” Nigga alimuuliza wakili Neema huku moyo wake ukimuenda mbio. “Sikia Nigga, nataka kukusaidia kwani mie kusaidia watu ndiyo kazi yangu inayonipa ugali wangu. Hivyo nikufahamishe tu kwamba Shuwea namjupa mie ndiye niliemtoa kwa rufaa akatoka Jela akiwa huru.” Wakili Neema alimwambia Nigga huku akimtazama usoni, alimuona Nigga amestuka sana kwa kauli ile woga ukiwa umemtawala sana. “Mimi ni wakili wa utetezi, sheria inaninyima kumtetea mrufani ambae ametoka akawa shahidi kisha nikakutetea na wewe mshitakiwa kwa maana kwamba nitakuwa nimeshajua ukweli mzima wa jambo lako, lakini pia sheria inaninyima kutoa siri za mteja wangu nje. Hivyo siwezi kuwa wakili wako, wala siwezi kuwa adui yako, ila naweza kukusaidia kama utakuwa unaniamini.” Wakili Neema alimwambia Nigga aliekuwa tayari mwili wake wote umelowa jasho kama mle ndani hakuna kiyoyozi. Nigga alitaka msaada kwa gharama yoyote, hivyo alimwambia wakili Neema amsaidie yupo tayari na anamuamini hana wasiwasi nae. Wakili Neema akamueleza mianya yakumfanya Nigga awe mbali mno na kifungo, lakini pia kama atatekeleza hilo jambo alilomwambia, ataishi bila mashaka yoyote. Nigga pamoja na mama yake mdogo waliwafikiana na maneno ya wakili Neema wakakubali kutekeleza maagizo yake wakakubaliana siku ileile kutimiza maelekezo yake. Baada yakuafikiana wakapeana mikono wakakubaliana siku ya pili yake waje kwa ajili ya kutimiza kila kitu walichokubaliana.

***

Kapteni Fabiola, akiwa na mwanawe pale Sebuleni, walishangazwa na mtu waliemuona ameingia pale sebuleni, Kapteni alikuwa hamfahamu yule mtu lakini Mbuya alikuwa akimfahamu vizuri sana. “Dada Shuwea, umepajuwaje nyumbani?” Mbuya Fabiola alimuuliza Shuwea Namjupa aliekuwa amesimama akiwa na mtoto wake mgongoni akiwa amelala. Kapteni Fabiola alimtazama mwanawe akamuuliza, “Nani huyu?” Mbuya akamjibu baba yake. “Huyu nimemfahamu nilipokuwa Jela, ndiyo alinipokea akanisaidia sana. Karibu Dada Shuwea, vipi unahabari gani?” Shuwea Namjupa aliinama akamuamkia Kapteni Fabiola, kisha akasema. “Mie sikuwa najua kama hapa ndiyo nyumbani kwenu ila mie nimeshapita nyumba nyingi huku Mtoni Kijichi, napita kuombaomba kazi kama za kufua, au za usafi wa nyumba ili nipate pesa yakula na mwanangu, kwani sina mtu wakunisaidia maisha haya na mtoto mchanga.” Shuwea Namjupa alimjibu Mbuya na baba yake akiwa bado amesimama pale alipokuwa. “Asante sana ila hapa tuna mashine za kufulia nguo, usafi yupo shamba boy anafanya, nenda kajaribu sehemu nyingine.” Kapteni Fabiola alimjibu Shuwea Namjupa huku akiwa hakufurahia kuingia hadi sebuleni, akapanga kumshughulikia mlinzi wake baadae. “Baba japokuwa hatuna kazi ya kuifanya yeye ili apate pesa nyumbani kwetu, basi naomba tumsaidie japo pesa kidogo tu, ili akajikimu na mtoto wake, hivi kama nyumba zote akijibiwa hivyo ataishije?” Mbuya alimuomba baba yake. Kapteni Fabiola alitoa noti ya shilingi elfu kumi akampa shuwea. “Asante sana nashukuru mzazi wangu, kwa msaada wako kwangu Mungu awazidishie.” Shuwea Namjupa alishukuru mungu akaaga na kuondoka mle ndani, akiwa ameshapata pesa yakununulia unga wa uji wa mwanawe. Mbuya alitoka nae nje mgeni yule, baba yake hakumzuwia kwani alikuwa akiitafuta namna yakumfanya mwanawe aishi kwa furaha kama awali, hivyo hakutaka kumkera kabisa. “Mbuya mbona macho yamekuvimba namna hiyo wifi yangu kama mtu uliekuwa ukilia?” Shuwea namjupa alimuuliza Mbuya kwa namna ya utani. “Wifi yako nitakuwa mie, unao mawifi zako ila siyo mie. Kuna matatizo kidogo yametokea nyumbani ndiyo nilikuwa nalia.” Shuwea alimtazama Mbuya kwa makini akamuona ni mtu aliekuwa akijilazimisha aonekane ni mwenye furaha ilihali hayupo vile. “Kuhusu Msafiri ondoa shaka, wewe lazima utakuwa wifi yangu tu, kwani nimezungumza na Msafiri kwa kina, anaonekana kunielewa na nakuhakikishia atakuoa wifi yangu, wewe niachie mie tu.” Shuwea Namjupa bado alikuwa aking’ang’aniza uhusiano wa Mbuya kwa kaka yake. Ama kweli umasikini mbaya sana. “Mie Msafiri haniwezi tena sasa hivi, wala mie sipo tayari kuwa nae.” Mbuya Fabiola alimjibu Shuwea Namjupa, mara simu ya Mbuya ikaanza kuita. Mbuya aliitazama ile namba ya simu iliyokuwa ikiita akaitambua. Akaiweka simu ile sikioni kwa haraka huku akiipokea. “Wakili Neema shikamoo, ehee, ndiyo tena kama bahati ninae hapa hapa ninavyoongea na wewe. Ahaa sawa nitamwambia, au nimpe simu, haya basi nitamwambia usijali.” Mbuya Fabiola aliikata ile simu akamgeukia Shuwea akamwambia; “Kesho saa mbili asubuhi wakili Neema ameniagiza nikupeleke ofisini kwake amesema ni muhimu sana usikose.” Shuwea akashangaa sana. “Kuna nini tena, au wale wahalifu wameshakamatwa?” Shuwea namjupa alimuuliza Mbuya, lakini hakuwa na jibu la swali lile. “Usiumize kichwa chako, kesho panapo majaaliwa tutafahamu tu mbichi na mbivu, shaka ondoa.” Baada ya mbuya kumjibu Shuwea maneno yale, wakaagana wakiwa wamekubaliana siku inayofata wakutane wapi ili waende kwa Wakili Neema.

***

Siku ya pili yake Mkuu wa Upelelezi wa kituo cha Polisi Buguruni, alikuwa ofisini kwake akiwa na magazeti matatu mbele ya meza yake, magazeti ya siku ile. Magazeti yale yalikuwa yamepambwa na picha kubwa za watu watatu, waliokuwa wamekaa kwa pamoja kwenye meza iliyokuwa imejaa chupa za bia na nyama choma. Pia zikaonekana picha za risasi zilizokuwa zimezagaa sebuleni kwa Baba Ubaya. Magazeti yale yalikuwa yamepambwa na vichwa vya habari tofauti, vilivyokuwa vikisomeka hivi; MAJAMBAZI HATARI WANATAFUTWA NA POLISI, ZAWADI NONO KWA WATAKAOFANIKISHA KUKAMATWA KWAO. Kisha chini ya kichwa kile kukafatiwa na maandishi yaliyoandikwa kwa herufi ndogo majina ya watu wale. Gazeti la pili lilikuwa na kichwa cha habari kilichosomeka hivi; MAJAMBAZI SUGU YANATAFUTWA NA POLISI. TOA TAARIFA POLISI UKIYAONA. BONGE LA ZAWADI LITATOLEWA. KWA YEYOTE ATAKAETOA TAARIFA ZA MAHALI WALIPO. Gazeti la tatu lilipambwa na kichwa cha habari kilichosomeka. SURA HIZI NI HATARI KATIKA JAMII, KAA MBALI NAZO NI MAJAMBAZI HATARI. TOA TAARIFA POLISI KATIKA NAMBA HIZO HAPO. Kisha zikawekwa namba za simu za mkuu wa upelelezi wa kituo chahttp://deusdeditmahunda.blogspot.com/ Polisi cha Buguruni pale mbele ya gazeti lile. Mkuu wa Upelelezi alitikisa kichwa kukubaliana na uandishi uliotumika, kwani baada ya siku ya jana alipotoka kwa Baba Ubaya na ile picha, aliweza kwenda kuonana na mkuu wake wa kituo, akamfahamisha safari yao kwa Baba Ubaya ilivyokuwa, Mkuu wa kituo akazungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi Ilala. Nae akaita vyombo vya habari akatoa taarifa ile huku akiwaomba raia kutoa ushirikiano kwa Polisi. Pia akawataka Polisi Jamii, ulinzi shirikishi nao wafanye kazi yao katika kufanikisha jambo lile, zawadi ya shilingi laki tano ikatangazwa kwa mtu atakaefanikisha kukamatwa kwa watu wale. Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi wa Ilala, aliwaonesha waandishi wa habari ile picha pamoja na majina ya wale wahalifu, pia akawapa picha alizopiga mkuu wa upelelezi kwa simu yake namna zile risasi zilivyokuwa zimezagaa pale chini. Mkuu wa upelelezi akiwa anatafakari atumie mbinu gani ili kufanikisha kukamatwa kwa wahalifu wale, mara simu yake ambayo namba zake zilikuwa zipo katika gazeti ikawa inaita nae akaipokea kwa haraka huku akiwa na kalamu yake mkononi, akiwa tayari kwa kuandika. Ndipo alipopewa taarifa iliyomfanya atoke nje ya ofisi yake haraka.

***

Baba ubaya alikuwa amelala kwa rafiki yake, asubuhi alikuwa akitazama Runinga ili kupata habari za kitu kilichojiri baada ya jana kuitwa na mkewe akiwa chini ya mikono ya Polisi. Akiwa katika kutazama taarifa ya habari asubuhi ile, hakukuwa na habari mbaya kwake, ila ilipofika kile kipindi cha YASEMAVYO MAGAZETI. Baba Ubaya aliiona sura yake, kwenye magazeti yale akiwa na Nigga, pamoja na rafiki yake Carlos Boga ambae usiku wa siku iliyopita ndipo alipokuwa amepitisha usingizi wake. Magazeti yale yalikuwa yakinadi kutafutwa kwao, pia zawadi iliyoahidiwa kutolewa kwa mtu atakae fanikisha kukamatwa kwake. Baba Ubaya aliinuka pale kitandani akakaa kitako. Mapigo ya moyo wake yakapoteza uelekeo. Hasa alipoona gazetini mle kupitia Runingani, sebule ya nyumbani kwake ikionekana vyema kabisa na jinsi Risasi zilivyozagaa pale chini. Baba Ubaya alichukua simu yake akampigia rafiki yake Carlos Boga, aliekuwa chumba kingine kuhusu habari ile. Rafiki yake nae akamjibu yupo macho anaitazama taarifa ile. Alipompigia simu Nigga, simu yake ikawa haipatikani. Aliipiga zaidi ya mara tano lakini bado simu ile ilikuwa haipatikani. Baba Ubaya akapagawa sana. Akamfahamisha Carlos Boga kutopatikana kwa simu ya Nigga, Carlos akatoka chumbani kwake akaenda katika chumba alichokuwa Baba Ubaya, akamgongea akafunguliwa mlango akaingia ndani wakakaa kujadili nini wafanye kwani hali imeshakuwa tete kwa upande wao. “Unajua siyo kawaida kwa Nigga kuzima simu yake, hivyo nina wasiwasi sana asije akawa nae keshakamatwa!” Baba Ubaya akamwambia rafiki yake. “Je ikiwa kweli amekamatwa, na hapa alishawahi kuja tulivyokuja kugawana ile pesa ya siku ilee, zile milioni tatutatu. yule anapafahamu sasa hapa itakuwaje, lakini pia sura zetu zishaanikwa katika magazeti sasa tunaishije, tunatembeaje, hawa majirani wanaotuzunguka kwa tama ya pesa watatuchoma tu wangu. Hapa pameshakuwa siyo chimbo tena.” Carlos Boga alimwambia Baba Ubaya, wakaingia katika mchecheto wa nafsi, ikawa moja haikai, mbili haiingii! Mara wakasikia gari imefunga breki nje ya geti la nyumba ile, na mlango wake ukaanza kugongwa kwa kwa fujo. Baba Ubaya na Carlos Boga walikuwa kama panya aliefungiwa na paka chumba kimoja kisichokuwa na shimo. Ile nyumba ilikuwa na dari juu, lakini walikuwa wakitafuta pakukimbilia. Chumba kilikuwa hakitoshi. Fadhaa iliwaingia sana. Wakiwa katika hali ile mara simu ya Baba Ubaya ikaanza kuita kwa sauti. Baba Ubaya kama Mkizi aliirukia ile simu yake huku akitetemeka, akaiziba sehemu ya sauti akaitizama simu ile, huku akihema kwa nguvu jasho jingi likimtoka!





Baba Ubaya alikuwa akichelea kupokea ile simu kwa sababu, hakuwa akijuwa mpigaji wa simu ile kama alikuwa salama au laa. Au kama alikuwa na askari au yupo peke yake. Hivyo aliikata simu ile. Kisha kama mtu aliezinduka kutoka katika gumbizi la usingizi mzito, alinyoosha mkono wake kwenye mto, akachukua Bastola yake aliyokuwa ameiweka pale, ili muda wowote ikihitajika kutumika basi iweze kutumika. Aliipandisha Risasi chemba, akawa ameielekeza Bastola ile kwenye mlango ili mtu akiingia kwa nguvu tu, lengo lake lilikuwa ni kumpiga Risasi kila aingiae mle kwa nia yakuwakamata kisha ajimalize na yeye mwenyewe. Baba Ubaya sura ya utu ilimbadilika akauvaa unyama wa nafsi. Yule mtu aliekuwa akigonga geti lile mfululizo akasema kwa sauti kule nje ya geti. “Oyaa watu wa humu ndani, toeni takataka hizo, siyo tunagonga mara nyingi nyie mmekaa kimya tu humo, gari ikiondoka siyo muanze kutusimamisha sie hatutasimama, maana mnaleta dharau.” Maneno yale ya yule mtu kule nje, yaliwafanya Baba Ubaya na Carlos Boga, watizamane huku wakiguna kwa pamoja “Mmmmh!” Mara wakasikia ile gari ikiondoka pale usawa wa geti lao, huku ile sauti ikisikika ikinadi kwa watu wengine wa pale mtaani kwa nguvu. “Toweni taka hizo, toweni taka hizo.” Mara wakasikikia sauti za wanawake wakiwa wanakimbilia gari ile wakipeleka takataka. Baba Ubaya na Carlos Boga, walishusha pumzi ndefu, kisha wakatikisa vichwa vyao kwa masikitiko. Carlos Boga alifungua mlango, akaenda pale kwenye geti, akachungulia nje akaona watu wakipakia takataka ndani ya gari ya kubebea takataka. Aliporudi ndani alikutana na Baba Ubaya, mlangoni nae akiwa anatoka nje ya chumba kile jasho jingi likiwa linamtoka mwilini mwake. “Mwanangu hapa chaka lishaungua, tufanye maarifa tusepe, kwani moyo wangu umekwenda mbio sana. Yaani hadi muda huu najihisi sipo vizuri.” Baba Ubaya alimwambia mwenyeji wake Carlos Boga. “Siyo mchezo hata mie nilipagawa sana, maana nilijua wajomba washaingia, Nigga keshawaleta. Kumbe presha yetu tu bure. Sema yule bwege wa kuchukua taka sasa ule ndiyo ugongaji gani kama wa wajomba.” Carlos Boga alimwambia rafiki yake, kisha wote wakatungua kicheko kikubwa kwa woga waliojivika nao, kumbe watu wa takataka! “Unajuwa mtu aliekuwa akinipigia simu ni Nigga?” Baba Ubaya alimuuliza rafiki yake. “Aaa bwana weee, hebu mpigie simu kisha mchekechee ujue yupo na wazee, au yupo peke yake. Isije wazee wamempa simu ili aongee kujua mahala tulipo, yule mtu huwa hazimi simu yake saa ishirini na nne. Ikiwa amekamatwa na polisi, hapa kweli chaka litakuwa lishaungua, hatuwezi kukaa tena kwani hapa Nigga anapafahamu vizuri.” Baba Ubaya aliiwasha simu yake, baada yakuwaka akampigia simu Nigga. Wakawa makini kumsikiliza wajue atapokeaje simu ile, mara simu ile ikajibu. ”Simu unayopiga kwa sasa haipatikani, tafadhali jaribu tena baadae.” Walitazamana tena kwa mara ya pili marafiki wale kwa siku ile. Carlos Boga alitoa simu yake, akaipiga namba ya Nigga, lakini hakupata jibu tofauti na mwenzake. Simu ile waliyokuwa wakiipiga ilikuwa haipatikani. Wanaume wale wakaitilia mashaka hali ile, wakajipanga haraka kwa kuondoka kwani hawakutaka kuifanya ajizi, kwani ukiifanya ajizi na mambo yanaajizika. Ajizi nyumba ya njaa. wasije kukutwa bure wakaokotwa kama kumbikumbi.



***

Nigga alikuwa ameamka nyumbani kwa mama yake mdogo. Simu yake ilikwisha chaji usiku na umeme ulizimika. Hivyo asubuhi uliporudi umeme akaiweka simu yake katika chaji. Alifungulia Runinga iliyokuwa chumbani mle, akawa akitazama magazeti yanasemaje. Mara kilipoanza kipindi cha magazeti, kwa macho yake aliyashuhudia magazeti yale, yakiwa yameweka picha yao katika kurasa za mbele kabisa. Moyo wake ulimuenda mbio sana, akaangalia kipindi kile akalisoma jina lake katika gazeti akiwa anatafutwa kwa ujambazi yeye pamoja na wenzake. Nigga aliona kimenuka, harakaharaka akaiwasha simu yake iliyokuwa kwenye umeme ikiingia chaji, akampigia simu Baba Ubaya, ili amueleze huko alipo atazame Runinga kuhusu picha zao na kutafutwa kwao. Aliisikia simu yake ikiita upande wa pili, mara ikakatwa simu yake. Nigga alishangaa sana kukatiwa simu na rafiki yake, akaamua ampigie tena lakini safari ile aliambiwa simu aliyoipigia haipatikani kwa maana imezimwa. Nigga hakutaka kufikiri mara mbili, akahisi Baba Ubaya keshakamatwa, hivyo akaamua kuizima na yeye simu yake ili asivutwe na Baba Ubaya. Hivyo aliinuka akenda kujiandaa kwa kwenda kwa wkili Neema. Baada yakuwa sawa akaingia katika gari ya mama yake mdogo, wakiwa pamoja wakaelekea kwa wakili Neema Faraja. Nigga alivaa kofia ya Kapelo, aliishusha kwenye uso wake kofia ile, ukawa huwezi kuiona sura yake hadi atoe kofia usoni mwake. ndiyo ungeweza kumtambua.

***

Wakili Neema Faraja, aliwahi kuingia ofisini kwake asubuhi ile, mkononi mwake alikuwa na magazeti mawili ambayo hupenda kuyasoma mara kwa mara. Alikaa katika kiti chake akayaweka magazeti yale mezani, kisha akatoa ile karatasi aliyotoka nayo TRA, akaitazama tena kwa umakini. Macho yake yalipolitazama gazeti lililokuwa juu, akaiona namba ya mkuu wa upelelezi wa kituo cha Polisi cha Buguruni ikiwa inasomeka kwa uwazi. Aliipiga namba ile ikawa inaita upande wa pili. Wakili Neema Faraja aliisubiri simu ile ambayo haikuita muda mrefu ikapokelewa. Wakili Neema Faraja, alijitambulisha kwa mwanausalama yule, kisha akasema jambo alilolikusudia kwake. “Halow kiongozi, nilikwambia siku ile muende TRA ili kufatilia taarifa za ile gari, je mlifanikiwa kwenda?” Mkuu wa Upelelezi akamjibu kuwa hawakufanikiwa kwenda ila tayari ile gari wanayo kituoni wameshaikamata. Wakili Neema faraja akatikisa kichwa juu chini kukubaliana na taarifa ile, lakini kwa upande mwengine akiwapongeza kwa kazi nzuri yakufanikiwa kulikamata gari lile. akamwambia mkuu wa upelelezi. “Mie kwa utashi wangu tu kama raia mwema, nimekwenda TRA, nimepata taarifa muhimu sana. Hebu kaangalie kwenye leseni ya barabara, (ROAD LICENCE) pamoja na bima ya gari hiyo, kama inasoma jina gani la mwenye gari hiyo, kwani TRA inamtambua mmiliki wa gari namba hiyo kuwa ni Gulamhussein Gondrap Shaha. Haijafanywa uhamisho wa jina la mtu mwengine tangu ilipowasili gari hiyo nchini mwaka 2012.” Wakili Neema alipomwambia lile jina lenye asili la bara la Asia, mkuu wa upelelezi alitoka haraka nje ya ofisi yake, akenda kwenye ile gari na kusoma jina la mmiliki wa gari ile linavyosomeka pale kwenye kioo, katika Leseni ya Barabara pamoja na Bima. Jina aliloliona likisomeka pale na jina aliloambiwa na wakili Neema Faraja yalikuwa ni majina mawili tofauti. “Huku jina la mmiliki wa gari hii linasomeka ni UBAYA MZUZURI” mkuu wa upelelezi alimwambia wakili Neema. “Basi hiyo gari itakuwa ni ya wizi, kwani namba hizo zinasomeka kama nilivyokueleza. Hebu andika cheses namba, hizi kisha ulinganishe na hizo hapo kwenye gari hiyo,” Wakili Neema Faraja alimsomea namba za cheses alizopewa kule TRA za gari halisi lenye namba zile. Mkuu wa upelelezi aliandika katika mkono wake kwa kalamu namba zile alizokuwa akitajiwa na wakili Neema. Kisha wakili Neema akamsomea na namba ya mashine ya gari halisi yenye namba zile kama alivyopewa TRA. Mkuu wa upelelezi alipotazama vitu hivyo akaviona vipo mbalimbali kama maji na mafuta. Mkuu wa upelelezi akajiridhisha kuwa ile gari, hakuna ubishi ni ya wizi, na namba zile zilizokuwa zimefungwa kwenye gari ile ni namba za bandia, yaani siyo halisi kwa gari ile. Hivyo aliiandika cheses namba ya gari ile, ili aipeleke TRA kupata namba halisi za gari ile. Wakakata simu na wakili Neema, mkuu wa upelelezi akatoka asubuhi ile akenda TRA, hakika aliyoyapata kule kwa namba zile za Cheses, zilimfanya aandae jalada lingine la kesi. Akashika njia kuelekea Sayansi pale kijitonyama kwa taarifa zaidi za kikazi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Wakili Neema alipokata simu ya mkuu wa upelelezi, mara aliwaona Mbuya Fabiola na Shuwea namjupa akiwa na mwanawe pamoja na Msafiri wakiingia katika chumba cha ofisi yake. “Karibuni sana, poleni kwa kuwasumbua asubuhi hii.” Wakili Neema aliwakaribisha wageni wake, kwa maneno ya bashasha. “Usijali Dada Neema, tumekaribia pole na wewe kwa kukuvamia, kwani bwana Msafiri dada yake alipomwambia kuwa umemwita nae akataka aje kusikia kulikoni?” Mbuya Fabiola alimwambia wakili Neema. Wakili Neema aliwakaribisha katika chumba cha pili kilichokuwa na viti vingi, wageni wake wakakaa kitako, akawauliza kama wameshapata chai, mbuya akasema bado ila watakunywa wakishatoka pale. “Ahaa sawa hakuna neno, Mbuya vipi shule kwani muda mrefu upo mtaani.” Wakili Neema Faraja alimuuliza mbuya Fabiola. “Jamani dada Neema shule tumefunga kwa wiki mbili, hadi ishe Pasaka ndiyo maana unaniona nipo mtaani.” Wakiwa katika kuzungumza haya na yale, wakili Neema alikuwa hajawaambia dhumuni la kuwaita pale asubuhi ile. Mara gari iliyokuwa ikiendeshwa na mwanamke, iliegeshwa jirani kabisa na ofisi ile ya wakili Neema. Watu wawili wa jinsia na umri tofauti walishuka kutoka ndani ya gari ile, wakabisha hodi katika ofisi ile. Wakili Neema Faraja alitoka katika chumba kile alichowaweka wakina Mbuya, akaenda katika chumba cha awali kinachoanza ambapo ndipo kuna mlango wa kuingilia katika ofisi yake, akawakaribisha wageni wale, nao wakakaribia lakini hakuwaweka katika chumba kile bali aliwapeleka katika chumba walipokuwapo kina Shuwea Namjupa. Wale wageni wakati wakipita katika ofisi ile kuelekea chumba cha pili, waliyaona magazeti mawili pale juu ya meza, yakawafanya watizamane. Wageni wale waliingia katika chumba cha pili wakafanya idadi ya watu waliokuwamo ndani ya chumba kile kufikia watu saba. Baada ya wageni wale kukaa vitini, Yule mgeni wa kiume aliitoa ile kofia yake usoni mwake, akaiweka juu ya meza. Shuwea Namjupa alipomtazama Yule mtu alievua kofia, moyo wake ukaenda mbio, alianza kutetemeka kijasho chembamba kilimtoka. Hakuwa na amani kabisa. Shuwea Namjupa akaanza kulia huku akimnyooshea kidole Yule bwana alievua kofia yake. “Huyu bwana ndiyo …..!” “…aliesababisha wewe wende jela.” Wakili Neema Faraja alimkata kauli Shuwea Namjupa, aliekuwa ameanza kupagawa. Mbuya Fabiola pamoja na Msafiri wote walimtumbulia macho mtu Yule, wakawa wakimtazama mtazamo tofauti kabisa.

“Shuwea huna sababu ya kupagawa, tulia na unisikilize kwa makini sana.” Wakili Neema faraja alimwambia Shuwea Namjupa, huku akimtazama moja kwa moja usoni mwake. Alimuona Shuwea ametulia kimya lakini anahema juujuu kama mama mjamzito wa miezi tisa. “Nigga kutana na Shuwea Namjupa. Na Shuwea kutana na Joseph Kazi au Nigga. Hamkukutana hapa kwangu kwa bahati mbaya laa hasha. Bali ni kwa makusudi mazima, ambayo kama mtanisikiliza kwa makini kila mmoja atafaidika na maneno yangu. Hasa kwa upande wako Shuwea Namjupa utanufaika zaidi kwenye hili, kwani Nigga nimeshaongea nae hana matatizo juu ya hilo.” Wakili Neema Faraja aliwaeleza wale watu huku akizungumza kwa utulivu mkubwa sana. Alipoona kuna utulivu akaendelea kuzungumza. “Shuwea wewe ni shahidi pekee uliobakia katika kesi ambayo ilikuweka Jela ukiwa ni Mfungwa. Mengi yamepita sitaki kuyarejea ila zingatia jambo moja tu kwamba, yaliopita si ndwele, tugange yaliyopo na yajayo.” Kwa mara nyingine wakili Neema alisimama kuzungumza akamtazama Shuwea Namjupa ambae mapigo yake ya moyo yalianza kurudi katika hali yake ya kawaida taratibu. Wakili Neema alimgeukia Shuwea Namjupa akaendelea kusema; “Kwa nini nimesema wewe ndiyo shahidi pekee mwenye nguvu uliyobakia? Aliekuwa muajiri wako kwa taarifa ya uhakika kabisa ambayo nimeithibitisha mimi mwenyewe, ameondoka nchini amehamia Canada huu mwaka mmoja sasa. Yule mama yake mzazi aliekuwa akiishi nae pale kwake Upanga amefariki mwaka mmoja uliopita. Mie jana nimefika kwenye nyumba ile kama ilivyokuwa ikionekana namba yake katika hati la shitaka. Majibu hayo nimepewa na watu wanaoishi sasa katika nyumba ile ya Msajili, uliokuwa ukifanya kazi za ndani wewe.” Wakili Neema aliposema maneno yale, Nigga alishusha pumzi ndefu, mama yake mdogo akaanza kutabasamu, Shuwea Namjupa alitoa macho ya kumsikitikia Yule mama wa muajiri wake, Mbuya na Msafiri walikuwa makini sana kumsikiliza wakili Neema dhumuni la kuwaita kwao. Faraja alikuwa amekaa mapajani kwa mama yake ananyonya kidole chake hana habari na mambo ya Dunia yanavyokwenda. Wakili Neema akaendelea kueleza habari ile muhimu sana. “Hivyo basi Polisi wakati ulipowaeleza ukweli kuwa humjui Nigga anapoishi wala mshenga feki wake, hawakutaka kukuelewa kabisa na walihakikisha wanaungaunga ushahidi na hatimae ukavaa nguo za Kifungwa ukawa mfungwa wa namba ndefu na kazi ngumu. Ajabu Polisi haohao waliohakikisha umefungwa, leo hii watakupamba nakukufanya uwe shahidi wao kwa vile wewe ulikuwapo na uliona tukio wakati wahalifu hawa walipofanya uhalifu wao. Haijalishi kuwa mtendewa wa tukio kuwa hayupo basi kukawa hakuna kesi, laa haipo hivyo. Kesi hii mlalamikaji ni jamhuri ambae ni Serikali, labda niwaulize Serikali inasafiri?” Wakili Neema alipofika hapo alinyamaza kimya kungoja majibu kwa watu aliokuwa akiwaeleza. Nigga na Shuwea wote walijikuta kwa pamoja wakimjibu kwa kichwa kuwa Serikali haijaondoka bado ipo. Wakili Neema Faraja akaendelea kuzungumza. “Sawa kwa hiyo Serikali itakufanya Shuwea Namjupa, kuwa ni shahidi namba moja. Mahakama ikikuletea Samansi kwa maana ya wito, huna namna yakukataa kuitika wito huo. Kwani kukataa ni kuidharau Mahakama, hivyo Mahakama inaweza kukufunga kwa kosa la kuidharau. Kasha bado ukaendelea kuwa shahidi hivyo ndivyo sheria inavyosema. Hivyo mie nimeonelea kwamba huna sababu yakuwa shahidi katika kesi ambayo ilishakufunga awali. Hebu fikiria vipi kama nisingekuwapo kukata rufaa kwa sababu nilizoziorozesha ukawa huru, huoni muda huu ungekuwa bado upo Jela ukitaabika?” Wakili Neema faraja alikuwa akimjenga kisaikolojia sana Shuwea Namjupa. “Hilo halina ubishi Wakili kwani mie nilihangaikia rufaa yake kwa miaka miwili lakini hakutoka jela hadi ulipokuja wewe hakumaliza hata mwezi mmoja akawa huru.” Msafiri Namjupa alisema akiongeza kuhusu suala lile.

Wakiwa katika mazungumzo yale, nje ya ofisi ya wakili Neema Faraja, Mkuu wa Upelelezi wa Kituo cha Polisi Buguruni aliegesha gari yake akashuka kuelekea katika ofisi ya wakili Neema Faraja!



Ndani ya ofisi ya Wakili Neema katika chumba walichokuwamo yeye na wageni wake, mazungumzo yao yalikuwa yanaendelea.

“Shuwea ukiwa upo hapa Dar es salaam, Mahakama itakuletea wito, ili uende ukatoe ushahidi. Hivyo nimeongea na Baba Faraja na yeye amekubaliana na mimi kuhusu hilo, kuwa akupe pesa kama kifuta jasho cha mtoto kumlea peke yako, kukuingiza katika matatizo, lakini pia iwe ya nauli unatakiwa leo hii, hii usafiri utoke nje ya Mkoa huu wende Mkoa mwengine, japo ukakae kwa miezi mitatu tu. Sasa kama utakwenda kwenu Nachingwea au popote utakapoona patakufaa ni sawa tu.” Wakili Neema alimwambia Shuwea Namjupa aliekuwa yupo makini sana kumsikiliza. “Hebu mpe ule mzigo tuliozungumza wa kumuondoa shahidi muhimu.” Wakili Neema Faraja alimwambia Nigga, atoe pesa walizokubaliana. Nigga alimtazama mama yake mdogo kumuashiria kuwa atoe mzigo, nae akafungua mkoba wake wa mkononi, akatoa bandari la noti za shilingi elfu kumi kumi tupu, akamkabidhi wakili Neema huku akimwambia. “Hizo ni Milioni tatu kama ulivyoagiza” Yule mama yake mdogo Nigga alimkabidhi wakili Neema fedha zile. Wakili Neema alizishika zile pesa akamuuliza Shuwea Namjupa. “Je nikupe hizi pesa ufanye kama nilivyokueleza, au nimrudishie mwenyewe ili uendelee na kutoa ushahidi?” Shuwea huku akinyoosha mkono wake wa kulia alisema. “Nipe noti hizo niende Nachingwea leo hii, nakaa hapa sina lolote lakufanya naomba omba tu, bora nikafanye biashara ili nipate kumlea mwanangu.” Wakili Neema alitabasamu akamkabidhi zile pesa.

Mara wakiwa katika kukabidhiana Mlungula, mlango wa ofisi ya Wakili Neema uligongwa, mtu aliekuwa akibisha hodi alikuwa amefungua ule mlango na kuingia ndani katika chumba kile cha kwanza cha ofisi ya Wakili Neema Faraja, akaketi kwenye kiti huku macho yake yakipiga katika meza iliyokuwa pale akayaona magazeti mawili yamewekwa pale juu, ambayo asubuhi ile alishayasoma ofisini kwake. Wakili Neema Faraja, aliisikia hodi iliyogongwa katika mlango wa ofisi yake, akawaomba radhi wageni wake ili akamsikilize mgeni. Wakili Neema alipofika katika chumba alichokuwapo mgeni, Yule bwana alitaka kusema kitu, lakini alimfanyia ishara ya kumzuwia asiseme neno, kwa kuweka kidole chake kidogo mdomoni mwake, kisha akamuashiria atoke nae nje ya ofisi yake. Yule mgeni alitii ishara ile huku akitikisa kichwa chake juu chini kuwa amemuelewa. Aliinuka akatoka nje kumfata wakili Neema aliekuwa ametangulia nje ya ofisi yake. “Najua kuja kwako ni kwa sababu ya ule ujumbe wangu niliokutumia, hivyo umekuja muda muafaka sana,” kisha wakili Neema alimpa mikakati yakufanikisha azma yao. Mkuu wa upelelezi aliitikia kwa kichwa, akampa tano Wakili Neema kisha akasema. http://deusdeditmahunda.blogspot.com/“Asante sana kwa ushirikiano mwema tupo pamoja sana.” wakili Neema akaagana na mkuu wa upelelezi akarudi ofisini kwake kuendelea na wageni wake. Mkuu wa upelelezi alitoa simu yake akapiga simu sehemu aliyoikusudia, kisha akatoa maelekezo muhimu.

Wakili Neema Faraja aliporudi chumbani mwake, alimuona Nigga amembeba Faraja anacheza nae. “Alaa mtoto yupo na baba yake eee?” wakili Neema aliwatania mle ndani wote wakaangua kicheko mle ndani kisha akachukua nafasi yake ya uenyekiti wa kikao kile akaendelea. “Nigga tumemaliza hatua moja kubwa ya kumuondoa shahidi muhimu katika kesi hii. Sasa hatua ya pili fanya kama vile tulivyozungumza ili nimpe jukumu hili mtu ambae namuamini, nimeshafanya kazi nae sana anajua kuchambua sheria ili kesho saa nne uje wende nae kituo cha Polisi na kila kitu nitazungumza nae ondoa shaka.” Wakili Neema liposema maneno yale akamtazama Nigga. Mama yake mdogo niga aliingiza mkono katika mkoba wake akatoka na kitita cha pesa tasilimu shilingi Milioni moja na nusu, akamkabidhi wakili Neema. “Huu mzigo wetu, Milioni moja na nusu kama ulivyotuagiza.” Mama yake mdogo Nigga alisema maneno yale kumwambia Wakili Neema. “Sawa nimepokea basi hakuna shida kesho saa nne tukijaaliwa mje hapa, ili mwende pamoja kituoni mkamalize mambo haya, amini hutoguswa hata kidogo, na kesi itakuwa haina ushahidi utarudi uraiani ukiwa huru.” Wakili Neema aliwaambia maneno yale huku akichukua ile pesa akaiweka kwenye droo la kabati lake. “Basi sie tunakushukuru sana kwa msaada wako, hivyo hatuna budi tuondoke kurudi nyumbani kwani huyu kutembea tembea kwa sasa siyo vyema, kwani wametolewa sura zao na zawadi zimetangazwa.” Mama yake mdogo Nigga alisema maneno yale huku wakiinuka. “Kweli kabisa umeona magazeti hayo, hivyo vumilia siku ya leo kwa kukaa ndani, ili kesho tutakuwa tumepata sababu nzuri kabisa za kisheria kwamba tumeona picha katika magazeti, mteja wetu kuwa anatafutwa na polisi kwa tuhuma za Ujambazi, hivyo tumemleta tunaomba twende Mahakamani ili Serikali ikathibitishe tuhuma hizo.” Wakili Neema aliwaambia watu wale ambao walimuamini kupita kiasi kuwa atawasaidia katika kesi inayowakabili. Nigga alitoa noti ya shilingi Elfu kumi, akampa Faraja, kisha akamrudisha kwa mama yake, wao wakaaga na kutoka nje ya ofisi ile. Wakili Neema Faraja aliwasindikiza hadi nje ya ofisi yake akaagana nao. Nigga alikuwa ameshaitupia kofia yake hadi usoni, akaagana na wakili Neema kwa kupeana mikono, kisha akaingia kwenye gari na mama yake mdogo akaingia upande wa dereva wakaondoka.

Wakili Neema Faraja alirudi ofisini kwake, kuzungumza na wageni wake. “Dada Neema sijui hata nikupe nini yaani sikuwa na mawazo kama katika maisha yangu, ningeweza kushika Milioni tatu ziwe zangu, yaani hapa leo hiihii naondoka sina chakuniweka tena.” Shuwea Namjupa alimwambia wakili Neema pale alipokuwa amerudi kuwasindikiza wageni akawa ameketi kitako kitini kwake. “Shuwea utaondoka ila siyo leo wala kesho, kwani unajukumu zito unalotakiwa kulifanya ambalo bado hujalitimiza.” Wakili Neema Faraja alimwambia Shuwea maneno yale huku, akimtazama usoni mwake kwa makini. “Jukumu gani hilo tena ?!” Shuwea alimuuliza wakili Neema kwa mshangao. “Lakusimama Mahakamani, kutoa ushahidi dhidi ya madhalimu Nigga na wenzake ambao leo hii, watakuwa kama siyo wote basi baadhi yao watakuwa mikononi mwa Polisi.” Wakili neema alimjibu Shuwea Namjupa kwa utulivu. Wageni wale wote kwa pamoja walipigwa na butwaa kubwa sana, wakawa hawamuelewi kabisa wakili Neema kwani muda mfupi uliopita walizungumza vingine na sasa anabadili habari na kueleza vingine. “Lakini si umenambia nimepewa pesa ili niondoke hapa nisiwe shahidi, sasa tena mbona sielewi?!” Shuwea Namjupa alimwambia wakili neema sura yake ikiwa katika mshangao mkubwa sana. “Mimi ndiyo najua ninachokifanya Shuwea, wewe ulikuwa ukihitaji pesa sana kwa wakati huu uliotoka katika matatizo. Lakini kumbuka wale ni wahalifu, hivyo tambua maishani mwako kuwa haki hainunuliwi. Hizo pesa fanyia mambo yako na kizimbani utapanda kuwa shahidi.” Wakili Neema alimwambia Shuwea Namjupa aliekuwa hoi bin taabani kwa kuchoka kwa kauli ile. “Dada Neema wale wakishinda kesi hawataniua mie kwa kuchukua pesa zao, kisha nikawasaliti?” Shuwea aliuliza kwa hofu. Wakili Neema Faraja ili kumtoa wasiwasi Shuwea Namjupa, alimuonesha kitu kilichowaacha midomo wazi wote waliokuwa mle ndani ya osifi ile kasoro Faraja Joseph Kazi Nigga.

***

Nigga na Mama yake mdogo, waliondoka katika jengo lile la Sayansi na Teknolojia, pale Kijitonyama kwenye ofisi ya Wakili Neema, wakashika njia ya kuelekea Tandale kwa Mtogole. Walikuwa wakipita njia za ndanindani wakichelea kupita barabara kuu kwa kuchelea maaskari. Mkuu wa upelelezi alikuwa ameziacha gari tatu kutoka katika gari aliyokuwa Nigga na mama yake mdogo, akiwafatilia ili afike nao mwisho wa safari yao, pengine anaweza kupata faida zaidi. Akiwa katika kuwafatilia wahalifu wale mara simu yake ya mkononi iliita akaipokea. “Afande tupo kamili, tunaomba uelekeo tafadhali umenisoma mpaka hapo?” Sauti iliyokuwa ikizungumza upande wa pili ilimwambia mkuu wa upelelezi. “Nipo Tandale nakata kulia naelekea Sinza, kipusa kinasafirishwa na gari namba, Tango kenda ziro kenda, Alfa, Blavo, Julieth. Nimesomeka?” (T = Tango, Kenda = 9, Ziro = Sifuri, Kenda= 9. Alfa = A, Blavo =B, Julieth =J) yaani alimaanisha T 909 ABJ. Mkuu wa upelelezi alijibu huku akipunguza mwendo gari yake akipanda tuta la Tandale Magharibi pale shule, wakielekea Sinza Uzuri. Upande wa pili wa simu ile ukajibu. “Nimekusoma Afande tupo Ubungo mataa, tunapinda kulia kukamata barabara ya Morogoro, tunakuja kuingia hapo Shekilango ili kuwa nanyi Sinza.” Upande wa pili ulizungumza kisha ikakatwa simu ile. Safari ile iliendelea hadi walipofika makutano ya Barabara ya Sinza Uzuri na Shekilango, gari aliyokuwa Nigga ikapinda kushoto, kuelekea barabara Shekilango Sinza Kumekucha. Gari mbili zilizokuwa mbele ya mkuu wa upelelezi, moja iliingia sheli pale kwenye makutano yale, na ya pili ilipinda kulia kuelekea Sinza Palestina. Mkuu wa upelelezi alipinda kushoto, mara Daladala lililokuwa likishusha abiria katika kituo cha Sinza Kijiweni likaingia barabarani, likakaa mbele ya gari ya mkuu wa upelelezi, na mbele yake ikiwa Toyota Noar ya rangi nyeupe ambamo ndimo alimokuwamo Nigga na mama yake mdogo. Mkuu wa upelelezi aliipigia ile simu aliyokuwa akiongea nayo awali akatoa maagizo.“Nipo Kamanyola hapa barabara ya Shekilango, mmefikia wapi?” Upande wa pili ukajibu. “Tupo Rombo hapa kiongozi, tukijia huko Sinza.” Mkuu wa upelelezi, akawaamuru wageuze gari kwani adui amekaribia maeneo yale, naam askari wanne waliokuwa katika Toyota Corola TI New Model, waligeuza gari ile kwa haraka na mara wakaiona gari aina ya Noar iliyokuwa na namba tajwa ikipita taratibu, ikiwa na vioo vya kiza, ikielekea Barabara ya Morogoro, na wao wakaiingiza barabarani gari ile wakiwa mbele ya mkuu wao wa upelelezi. Lile Daladala liliingia kituoni kupakia abiria. “Maelekezo kiongozi tunamaliza hapahapa au ipoje?” Simu ya upande wa pili iliuliza, mkuu wa upelelezi akamwambia wanawafatilia hadi mwisho wa safari yao, watamaliza huko kwani wanaweza kupata faida zaidi ikiwa watakwenda nao hadi mwisho. Kisha simu ile ikakatwa ikawa watu wapo makini zaidi na jambo lile.

Nigga akiwa ndani ya gari na mama yake mdogo, akaamua ampigie simu Carlos Boga ili kujua kama Baba Ubaya yupo salama au amekamatwa, simu ya Carlos Boga ikaanza kuita na hatimae ikapokelewa upande wa pili. “Halow?”Sauti ya Carlos Boga ilisikika kwenye simu ile ikiitika kwa mashaka. Nigga akamsalimia kisha akamuuliza. “Ebwana nimempigia simu leo asubuhi Baba Ubaya simu imeita kisha ikakatwa, nimempigia tena simu yake ikawa haipatikani, je kuna usalama huko au Tafu Guy keshamvuta maana nimeona kwenye magazeti yaani tumecharaziwa kinoma wangu?” Carlos Boga alimtazama baba ubaya, aliekuwa pembeni yake akalaoud spika ili na mwenzake asikie. “Baba Ubaya tangu jana mie sijawasiliana nae, wewe upo wapi saa hizi mbona nimekupigia simu ulikuwa hupatikani, au ndiyo upo na wazee unanichekecha?” Carlos Boga alimwambia Nigga, huku akiwa makini na sauti zingine kama zitatokeza kwani hawakuwa na imani nae walikuwa wanamuhisi ameshakamatwa. “Mie nipo na Mama mdogo tunatoka kwa wakili, yaani nimeshaharibu kesi yote wangu, kama huniamini wewe sauti ya mama mdogo, unaifahamu tushafanya mgao sana nyumbani kwake, hebu ongea nae akutoe wasiwasi kwanza.” Nigga baada yakuzungumza maneno yale, akampa simu mama yake mdogo akazungumza nae, akathibitisha kuwa kweli yupo nae na wapo salama. “Poa mama nimekuelewa mpe simu huyo.” Mama mdogo wake Nigga akampa simu mwanawe akaendelea kuzungumza na mwenzake. “Mwana mie mwenyewe nilikuwa najua Baba Ubaya keshamalizwa, kwani jana simu yangu ilikwisha chaji, na kule nilipokuwa chimbo, kwa mama mdogo jana kulikuwa hakuna umeme, hivyo umeme umerudishwa asubuhi ndiyo nikapata nafasi yakuchaji simu, sasa tunaonana wapi kwani nina habari muhimu sana kutoka kwa Wakili. Tena nimeonana na yule Demu aliekuwa beki tatu wa Muhindi, kule tulipopiga pesa ndefu, yaani nimemaliza kabisa hakuna kitu wangu, nanyi nataka niwaambie kitu kama vipi mtafute na Baba Ubaya, ili tuwe wote niwaambie nini cha kufanya.” Nigga alimwambia Carlos Boga ambae sasa alimuamini kuwa kweli hakuwa kwenye matatizo. “Baba Ubaya nipo nae hapa, kama vipi njoo Tabata Kisiwani, pitia hapo mwanachi relini, sie tutakuona tulipo kisha tutakupa maelekezo.” Carlos Boga alimwambia Nigga kwenye simu ile. “Poa nakuja na mama mdogo sasa hivi kwani tupo, Shekilango hapa tunaingia boda la kushoto huku Makaburini kutokea njia ya Ubungo maziwa. Tutatokea hapo Mama Land, kisha tutaingia barabara ya mandela hadi hapo Tabata mwananchi, tutaingia kulia kuwafata.” Nigga alizungumza na simu ile kisha akakata ile simu huku akiwa na shauku ya kukutana na wenziwe. Walitembea wakapita njia aliyoisema hatimae wakafika Tabata Mwanachi, wakaingia kulia relini huku zile gari za Polisi zikiiacha ile gari kwa mbali kidogo kisha nazo zikapinda kulia wakihakikisha hawawapotezi kabisa machoni mwao. “Oyaa tumeshaingia hapa Relini, mpo upande gani?” Nigga alimpigia simu Carlos Boga akamuuliza. “Ahaa mmeshapinda ee, mpo na gari aina gani?” Carlos Boga alimuuliza Nigga, kwani sehemu aliyokuwa amekaa alikuwa akiziona gari zote zilizokuwa zikiingia na kutoka. “Tupo na Noar ya Mama mdogo ile nyeupe, tuliofaulushia mzigo siku ile bwana.” Nigga alimjibu jamaa yake. “Sawa hapo ulipo shuka wewe peke yako, kisha rudi nyuma huku Relini utatukuta tunakusubiri.” Carlos Boga, alikuwa anamchekecha Nigga wajue kama yupo peke yake kweli au yeye na mama yake wote wametekwa kisha wanawavuta. Nigga alimwambia mama yake. “Hawa wezi bado hawaniamini hivyo wewe nenda kapaki mbele mie nakwenda kuonana nao kisha nitakuja nao.” Mama mdogo wa Nigga alisimamisha gari, Nigga akashuka akawa akitembea kwa miguu akielekea relini barabara kubwa ya Mandela.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Wale askari waliiona ile gari Toyota Noar ikisimama kule mbele, kisha Nigga akashuka akawa akitembea kwa mguu kurudi nyuma walipokuwa wao. Dereva wa Polisi alisimamisha gari yake, akavuta waya wa Boneti la gari yake haraka, kisha akatoka nje na kitambaa akalifungua boneti lile, akaufungua mfuniko wa Rejeta, moshi mwingi ukaonekana kutokana na Presha na joto la mashine ya gari ile, kila aliyoiona gari ile aliamini ilikuwa inachemsha asingetilia mashaka kusimama kwake katika hali ile. Mkuu wa upelelezi aliipita ile gari kama haijui, akawa anaifata Toyota Noar ilipokuwa inaelekea.akapisha na Nigga taratibu, bila kumtazama.

Nigga alikuwa ametembea hadi usawa wa gari ile iliyofunguliwa buti, akawa akiipita ile gari huku akizungumza na simu yake. “Oyaa sema mnazingua bwana, bado hamjaamini tu kuwa mie sipo na ugeni, sasa mmesimama wapi, naona mnanizeveza tu, kama hamniamini mie niende zangu bwana siyo tunauzishana sura tu!”







ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog