Simulizi : Mpita Njia
Sehemu Ya Tano (5)
Kauli ile ya Nigga ilisikikwa vyema na wale askari waliokuwamo ndani ya gari ile, kiasi walitazamana mle ndani ya gari, kisha wakageuza sura zao kumtazama Nigga alipokuwa anaelekea, kule katika barabara kubwa. Wakiwa katika kumtazama vile, mara honi kubwa ililia na kila mtu akawa makini mle ndani kuona kwamba hawampotezi Nigga machoni mwao. Honi ile ilizidi kuwa kubwa kwa kadiri ilivokuwa ikisogea. Ilikuwa ni Treni ya abiria inayofanya safari zake Ubungo kwenda Relwe Station. Nigga alivuka Reli kwa haraka kabla ile Treni haijapita. Mara Treni ile ikawa inavuka makutano ya barabara ya Mandela kwa mwendo wa wastani kwani lilikuwa na kituo mbele pale Tabata Ami au Tabata Reli kwa jina maarufu.
Wale asakri walifungua mlango wa gari yao, wakashuka wakaanza kutembea kwa miguu wakielekea kule alipokwenda Nigga wakiwa wamegawanyika njia tofauti, wote wakiwa na ari kubwa yakuwakamata wahalifu wale. Asakri wale walitembea hadi pale katika Reli, wakasubiri treni ivuke ambayo ilikuwa imewakinga upande wa pili kutoona. Ilipopita Treni ile wakavuka Reli kuelekea upande wa pili wa Barabara ile huku kila mmoja akimtafuta Nigga kwa macho. Walikuwa wameishika rangi ya nguo zake alizovaa. Hivyo walipokuwa wakitazama huku na kule ili kuona nguo ile aliyokuwa amevaa, lakini Nigga alikuwa haonekani. Wale askari waliimaliza ile sehemu yote pale kuangalia, lakini Nigga hakuonekana machoni mwao. Wakiwa katika pande tofauti askari wale wakapeana taarifa kwa simu kwa njia ya ujumbe waangalie magari yaliyokuwa yameegeshwa maeneo yale kwani anaweza akawa amepanda kwenye gari anaongea na jamaa zake, hivyo askari wale wakawa makini zaidi na gari ndogo zilizokuwa zimeegeshwa katika maeneo yale hakuna gari ambayo ilikuwa maeneo yale ambayo haikutazamwa, kuanzia gari kubwa hadi gari ndogo.
Gari zilikuwa nyingi eneo lile, zilizoegeshwa na raia. Zipo ambazo madereva walikuwamo ndani ya magari yao, pia ziilikuwepo gari zilizokuwa tupu. Hivyo macho ya askari wale yalikuwa yakiitazama kila gari iliyokuwa karibu yao mbele ya macho yao.
Upande wa kulia kama ukitokea Ubungo, kwenye ofisi za gazeti la Mwananchi, ulikuwa na askari mmoja, upande ule wa pili kwenye kampuni maarufu ya AMI, napo kulikuwa na askari mwingine. Askari wa tatu yeye alikuwa akitembea baina ya osifi za Mwananchi hadi katika Sheli ya OILCOM iliyokuwa pale jirani lakini mote mle walipotazama hawakufanikiwa kumuona Nigga. Jasho liliwatoka askari wale, wakalilaumu sana lile Treni kupita muda ule, kwani liliwaziba wasiweze kuona kitu kilichokuwa kikiendelea upande wa pili. Asakri mmoja akatoa simu akampigia Mkuu wa upelelezi kumpa taarifa pia kumtaka ushauri, kwani mambo yalikuwa yanaonekana kuwapeleka halijojo. “Kiongozi, kupita kwa nyoka kuku amekimbia, kwani nyoka alikuwa amemziba mfugaji, kwa hiyo tunamtafuta ili apelekwe kwenye tenga lake.” Simu ile ilimchanganya sana Mkuu wa upelelezi. Haikumchanganya kwa maneno yake, hapana maneno yale alikwisha yafahamu kuwa, Nyoka ni Treni, Kuku ni Nigga, na Mfugaji ni askari. Alichokuwa amechanganyikiwa ni itakuwa vipi ikiwa Nigga watamkosa. “Ahaa kama haonekani barabarani, basi mtazameni katika majumba ya watu hapo jirani, au wasijekuwa wamemuiba wamemfungia kwenye gari, hebu kuweni makini kwani Kuku yule ni ghali sana ila namtaka akiwa mzima asipigwe manati” Mkuu wa upelelezi alimwambia yule askari aliekuwa akizungumza nae kwa simu. “Sawasawa nimekuelewa, najaribu kumtazama kwenye nyumba za watu, nadhani kuku wako atapatikana tu.”
***
Nigga alivuka ile Reli kwa haraka kupisha Treni iliyokuwa jirani, akiwa bado anaongea na simu alipewa maelekezo. “Acha kuongea sana wewe, unaiona hiyo gari iliyokuwa kulia kwako, ndiyo hiyo Taxi. Sasa iache hiyo Taxi, nyuma yake kuna GX 100 ingia humo ndipo tulipo tumeshakuona.” Nigga alipiga hatua hadi pale kwenye ile gari GX 100, akafungua mlango wa nyuma wa gari ile akapanda, kisha akaufunga mlango. Gari ile iliingia barabarani, ikaisubiri Treni ivuke dereva wake akaendesha kuelekea njia ya Ubungo. “Mwana usione kama tulikuwa tunakuzeveza laa, sie tunatakiwa tuwe makini sana kwa wakati huu, kwani sura zetu ni pesa kwa watu. Polisi washatufanya biashara ndiyo maana tunatakiwa kuongeza umakini sana.” Baba Ubaya alimwambia Nigga wakiwa wanatembea na gari iliyokuwa ikiendeshwa na Carlos Boba. “Sikia Nigga, sasa hivi kukaa Bar au sehemu kuzungumza kama ilivyokuwa tunafanya zamani, siyo dili tena yaani tutaisha sasa hivi wangu. Ila tutazungumza ndani ya gari kama hivi huku tunatembea hadi tukimaliza mazungumzo yetu, tunaachana tunaendelea na mambo yetu.” Carlos Boga alimwambia Nigga, maneno yale wakati huo wakiwa maeneo ya Gereji wakielekea Ubungo. “Nimewaelewa wanangu mwenyewe, sema nini kuna taarifa nzuri sana kwetu. Yule shahidi tuliotaka kumdondosha nishamnunua hatokuja tena mahakamani, hivi leo hii hii anaondoka Mkoa huu anakwenda kwao huko shamba. Pia yule Muhindi hayupo nchini amehamia Canada, yaani ameondoka kabisa hapa nchini kwa maana hiyo mna nini tena hapo ni Mpeto mtupu.” Taarifa ile iliwafurahisha sana wezi wale, wakawa wakipeana tano mle ndani, huku wakimpongeza Nigga kwa hatua aliyoichukua. “Mwana yule shahidi umeonana nae wapi, lakini pia umejuaje kuwa yule Mdosi kaondoka Bongo, usijekuwa unatupa imani kumbe ukawa muongo?” Baba Ubaya alimsaili rafiki yake. “Hapana mie yule mama yangu mdogo si mnajua kuwa ni mjanja, sasa aliniambia amechukua namba za wakili mmoja matata sana, yeye siku hiyo alikwenda pale Mahakama ya wilaya ya Temeke, alikwenda kumdhamini mtu, ndipo kwa muheshimiwa aliemfata akakutana na yule wakili akiwa anamtetea kijana mmoja. Unaambiwa yule wakili noma hadi kampeleka Polisi jela alivyokuwa ameruka nae. Yule dogo aliekuwa akimtetea akaachiwa, ndipo mama mdogo alipochukua namba zake, kisha akanipigia simu ili niende nionane nae, hasa baada yakumwambia kukamatwa kwa Tafu Guy na mke wako.” Nigga alimwambia Baba Ubaya, huku wenzake wakimsikiliza kwa makini sana. “Mama mdogo alimpigia simu akamuuliza kama anaweza kuonana nae wapi, ndipo yule wakili alipotuelekeza ofisi zake zilipo, basi tulipofika pale ikabidi nimchane wazi tu kuwa mie ni mjanja nikamueleza kuhusu ile Kesi na yule demu. Kumbe yule wakili ndiyo aliemchomoa Yule demu kwa rufaa!” Nigga aliendelea kuwaelezea wenzake kila kitu alichoongea na wakili Neema na hatimae, kuambiwa namna gani atakavyoweza kumsaidia, pia akawaeleza wenzake kuhusu kusafiri kwa Muhindi kuwa ameambiwa na wakili, na pia yeye mwenyewe amempa pesa Shuwea Namjupa na kuwa hatotokea tena Mahakamani. Taarifa ile iliwavutia sana, wakafurahi na kumpongeza sana wakili Neema faraja kwa taarifa yake. “Kwa hiyo mwana kesho utakuwa mikononi mwa Polisi, sasa kama ushahidi hakuna, mwenye mali hayupo wakili ushampa chake, si bora ukaushe tu usiende kusalimishwa kwa vile hakuna ushahidi, inamaana mambo yatakuwa doro hayana nguvu.” Carlos Boga alimwambia Nigga aliekuwa akizungumza kwa kujiamini sana.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
***
Wakili Neema Faraja, aliwaonesha kitambulisho chake wale waliokuwa wateja wake na aliekuwa bosi wake. Kitambulisho kile hakikuwa kile alichokiona Shuwea Namjupa kule Gerezani kuwa ni Wakili, bali kitambulisho cha sasa kilikuwa na nembo ambayo haiwezi kukaa katika vitambulisho vya kawaida hata iweje. Nembo ile ilikuwa ni ya Adamu na Hawa naweza kusema, lakini juu ya kitambulishp kile kulikuwa na maandishi makubwa yaliyosomeka; USALAMA WA TAIFA. Watu wale mle ndani ukimuondoa mtoto mdogo Faraja bin Nigga, wote walikuwa wameacha vinywa vyao wazi kwa mshangao. Hawakuamini kabisa kama wakili Neema pia nae ni askari tena siyo askari wa kawaida. “Ondoa shaka Shuwea Namjupa, hakuna mtu anaeweza kukuua wewe katika jambo hili.” Wakili Neema alisema maneno yale huku akikifunga na kukirudisha kitambulisho chake sehemu alipokitoa. “Tupo kwa ajili ya kutetea watu wasiokuwa na hatia, lakini hatupo kwa ajili yakutetea watu wezi wanaokili kabisa kuwa wamefanya jambo hilo, ndiyo maana nimeingia upande wa utetezi kukutana na watu hawa inakuwa rahisi kuliko ningebaki kuwa wakili wa Serikali, ningekuwa nao mbali sana watu wa namna hii, hivyo wapo ambao huatarisha amani ya taifa hili, nami nimekula kiapo kuwa nitailinda, nitaitetea na kwa vyovyote vile sitotoa siri ya Taifa langu, kwa hiyo siwezi kuwaacha Majambazi watambe, nami nikiwatetea siwezi abadani.” Wakili Neema Faraja alikuwa akisema maneno yale huku akiwa hana mdhaha hata kidogo. “Haya nimeelewa nipo tayari kutoa ushahidi popote pale, nikiwa chini yako dada Neema.” Shuwea Namjupa alimwambia wakili Neema Faraja. “Vyema, sasa fanya hivi, nakupa namba zangu za simu, pesa unazo leo hii nenda kanunue simu, iweke line kisha nipigie niipate namba yako, kwani ukiwa na simu mambo yanakuwa rahisi kuliko hivyo ulivyokuwa ukiishi kizamani. Wale watu hatari kwanza sasa hivi wanajificha wao, hivyo hawatakuwinda tena. Lakini pia Yule atawaeleza wenzake jambo hili hivyo hawatakuwa na maana na wewe tena” Wakili Neema alimgeukia Mbuya Fabiola akamuuliza swali la kizushi huku akiwa anatabasamu; “Mbuya ndoa yako na Msafiri tuitarajie lini?” Mbuya alipoulizwa swali lile badala yakucheka kama ambavyo wakili Neema alitarajia, badala yake alianza kulengwalengwa na machozi machoni mwake. Hali ile iliwashangaza sana Shuwea Namjupa na wakili Neema. Msafiri alikuwa hamuangalii Mbuya mawazo yake, alikuwa akifikiria kumuomba mtaji dada yake ili akanunue Balo la Mtumba auze nguo za mitumba kwani aliiona biashara ile inalipa sana kwa upande wake, na alishawahi kuifanya siku za nyuma.
Mbuya Fabiola aliinamisha kichwa chake chini kwa masikitiko, kisha akatikisa kichwa chake kuonesha hali ya kukataa lakini pia kukata tamaa. “Mie siwezi kuolewa tena siyo na Msafiri tu, bali hata na mwanaume mwingine yoyote kutokana na hali yangu!” Wakili Neema aliacha kule kutabasamu akamuuliza kwa mshangao. “Hali yako?! Hali gani hiyo?!” Mbuya Fabiola akajibu huku akilia kwa kwikwi. “Mie nimeathirika na VVU hivyo ndoto za maisha yangu zimeshaharibika kabisa.” “Baba yangu mzazi mzee Namjupa! Eee umeathirika?!” Shuwea Namjupa alishituka sana, Mbuya alipojibu vile alimfanya Msafiri ageuke kwa haraka kumtazama, huku akiwa haamini masikio yake kama amesikia sawasawa alichokisema Mbuya. ”Umeathirika?! Mbuya hebu acha utani huo!” Shuwea alimuuliza Mbuya kwa mshangao. “Shuwea kwani ajabu ipo wapi, mbona watu wengi tu wameathirika sembuse mie, nimeathirika ndiyo,” Mbuya alimjibu Shuwea Namjupa huku akimtazama usoni kwa macho yake yaliokuwa yamejaa machozi. “Mbuya pole sana mdogo wangu, hali hiyo umeitambua lini hivi karibuni au muda mrefu?” Wakili Neema Faraja, alimuuliza Mbuya Fabiola kwa utulivu. “Yaani nimetambua tatizo hilo siku ya jana tu, Shuwea ulivyokuja nyumbani jana ulitukuta na baba hatukuwa katika hali ya kawaida. Pale ndiyo nilikuwa nazungumza na Baba juu ya hilo.” Mbuya alisema kwa upole akiwa ameinamia chini. Msafiri alitikisa kichwa kwa masikitiko, akainua mikono yake juu akamshukuru Mungu, “Alhamdulillah.” Mbuya aliwaeleza kila kitu kilivyokuwa kama alivyoelezwa na Baba yake na hatimae akalia kilio cha kwikwi kwa uchungu mkubwa sana. Mbuya alibembelezwa kwa muda mrefu, lakini hakupoa haraka. Msafiri akamshika mabegani akamwambia; “Mbuya kuathirika na virusi, siyo mwisho wa maisha. Wala kuwa na virusi siyo kuwa ndiyo unaugua Ukimwi, wapo watu wengi wanaishi na virusi na mambo yao yanakwenda, hivyo umejitambua nakushauri kaangalie CD4 zako zimeshuka kadiri gani ili uanze dawa, kwani mara tu mtu anapojijuwa kuwa ameathirika, basi ndipo athari zinapoanza kwenye afya yake, lakini angekuwa hajijuwi pengine angekuwa sawa tu.” Mbuya alifuta machozi akanyamaza, kisha akaaga ili aondoke, wakili Neema akamzuwia asiondoke peke yake, akawaambia waondoke wote. Alitoa pesa ili awape pesa ya usafiri, lakini Mbuya na Shuwea wakaikataa wakasema pesa wanayo, hatimae wakaaga na kuondoka katika ofisi ile.
***
Wale askari walizunguka sehemu ile bila kuacha sehemu hata moja, wakizitazama gari zote zilizokuwa zimeegeshwa lakini hawakuambua kitu. Wakawasiliana na mkuu wa upelelezi hatua waliyofikia, ndipo mkuu wa upelelezi alipowaita na kuwapa mikakati kabambe yakufanya zikiwamo mbinu za medani. (MM)
***
Nigga akiwa na wenzake, mara simu yake ikaita. Alipoitazama ile simu aliiona namba ya simu ya mama yake mdogo, akaipokea. “Mwanangu mbona unaniweka hivyo, mie nina shughuli zangu za kufanya sasa unaponiweka hapa kama sina kitu cha kufanya unaniharibia mambo yangu.” Mama yake mdogo Nigga alimwambia mwanawe. “Samahani mama nipo na kina Baba Ubaya hapa, sasa fanya hivi njoo na gari huku Ubungo kibangu nyuma ya Riverside tumepaki gari tunaongea” Nigga alimjibu Mama yake. “Sawa nakuja sasa hivi, mpo na gari gani kwani mie kuzurulishwa sitaki.” Mama yake mdogo Niga alimuuliza Nigga. “Njoo utaiona gari GX 100, imeegeshwa hapa kwenye mti tunazungumza ili tuachane.” Nigga alimjibu mama yake huku akiendelea kuongea na wenzake. Kiasi ya dakika kama kumi na tano hivi, Toyota Noah Nyeupe iliyokuwa ikiendeshwa na mama yake mdogo Nigga ilikuwa imeegeshwa pale ilipo ile GX 100 waliyokuwamo Nigga na wenzake. Mara mlango wa pembeni wa ile Toyota Noah ulifunguliwa kwa haraka, wakatoka watu watatu wakiwa na bastola mikononi mwao. Mmoja wa watu wale aliiruka kwa samasoti ile GX 100 katikati akatua upande wa pili huku akiwa na Basotla yake mkoni akawaambia kwa sauti ya ukakamavu, “HATOKI MTU HAPA” wakaanza kuishambulia ile GX 100 katika matairi ya mbele huku wakiwaamrisha wale watu waliokuwamo ndani ya gari ile. “Tulia hivyohivyo humo ukitoka nje unakula Risasi.” Mara kioo cha mbele cha pembeni ya ile Toyota Noah kilichokuwa cha kiza kilishushwa chini, akaonekana mkuu wa upelelezi akiwa mle ndani amemuelekezea Bastola ya kichwa mama yake mdogo Nigga aliekuwa kwenye usukani huku machozi yakimtoka!
Milio ya Risasi ililindima eneo lile, ikawaogofya wakazi wa jirani wa eneo lile, wakaanza kukimbia hovyo. Wapo waliodhani kuwa ni majambazi wanafanya uhalifu, pia wapo waliodhani askari wanapambana na wahalifu. Eneo lile ilikuwa ni hekaheka kubwa sana.
Yule askari mtaalam wa mapambano ya mikono, aliufungua mlango wa mbele wa gari ile, akashindwa kwani gari ile ilikuwa imefungwa milango yake kwa lock. Hivyo akapiga ngumi moja takatifu, kioo cha GX 100 kikavunjika kikamwaga chenga ndani na nje ya gari. Baada ya kioo kuvunjika, uwazi wa dirisha la gari ile GX 100 uliruhusu kuonesha watu waliokuwamo ndani yake kwa viti vya mbele. Yule akari alipopeleka macho yake ndani ya gari ile atizame watu waliokuwamo, akakutana na mdomo wa Bastola ukimuangalia. Haraka akainua Bastola yake ili ashambulie lakini alichelewa, kwani Baba Ubaya alifyatua risasi mbili za haraka, zilizompata yule askari katika eneo la kifua na kumfanya adondoke kwa nyuma kichalichali huku akipiga ukelele “Aaaaaghhhhh.” Baba Ubaya akatoa lock za mlango ule wa mbele aliokuwapo akatoka nje ili apambane na hatimae atoroke. Lakini alipotokeza nje tu ya gari ile, alimshuhudia yule askari aliekuwa pale chini amelala akiwa amenyoosha silaha yake kwake huku akiwa bado amelala kichalichali akimtazama . Baba Ubaya akainua silaha yake ili ammalize kabisa lakini hakuwahi kidole chake, kufyatua Trigger kwani askari yule alifyatua risasi tatu mbili akipiga kifuani, na moja akapiga kwenye pagi la uso akauchangua ubongo katika kichwa chake. Damu na ubongo ulifumka ukarushwa kwa mita kadhaa. GX 100 ilichafuka damu ikawa huwezi kuiangalia mara mbili. Baba Ubaya alirushwa kama mzigo kwa ukali wa Risasi zile zilizopiga kwa karibu akadondokea juu ya boneti la GX 100 huku kidole chake kikiwa kimekandamizwa kwenye Trigger (Kifyatulio cha risasi) Risasi sita zikatoka mfululizo kutoka katika silaha ile Chines Automatic. Kwa kuwa mlalo aliokuwa amelazwa Baba Ubaya kwa mtupo wa risasi, mkono wake ulikuwa umeelekea ilipotazama ile GX 100, ambapo hakukuwa na watu jirani yake, au vinginevyo ingesababisha maafa au majeruhi makubwa yasiyosemeka. Yule askari baada ya shambulizi lile kwa Baba Ubaya, alibimbilika pale chini akapiga goti moja akawaoneshea silaha yake Nigga na Carlos Boga, iliyokuwa ikitoka moshi mbele kwenye mdomo wake. Nigga na Carlos Boga walikuwa wamechanganyikiwa sana. Kwani hawakukitarajia kabisa kitendo kile kutokea mbele ya macho yao. Kwani walimshuhudia swahiba wao Baba Ubaya akiwa hakuweza hata kuomba maji. Mara moja risasi zikambadilisha jina na kuwa marehemu Baba Ubaya. “Shuka chini wote mara moja mikono juu” Yule askari aliewaoneshea silaha yake aliwaamuru Nigga na Carlos Boga, kutelemka kutoka ndani ya gari ile kwa haraka.
Wale askari wawili waliokuwa upande mwingine, walikuwa wamelala chini baada ya mwenzao kurusha risasi kwa Baba Ubaya. Silaha zao zilikuwa zinatazama mbele kwenye milango ya gari ile ili mtu atakaejaribu kukimbia tu basi iwe ni halali yao. Waliposikia milio ya risasi imesimama haraka waliinuka wakaongeza nguvu kwa kuvunja kioo cha dirisha upande wa Dereva. Carlos Boga alipagawa zaidi kwani alikuwa anajizoazoa kutoka nje kwa upande wa pili, akageuza uso wake, upande ule iliolia kioo kuvunjika, Mara kufumba na kufumbua yule askari aliemshambulia Baba Ubaya alikuwa ameshazama ndani ya gari ile akawa ameweka mtutu wa batola kichwani kwa Nigga. Wakati Nigga amewekewa Bastola na askari aliepambana na Baba Ubaya, Carlos Boga alipogeuza shingo yake tu upande wake wa kulia kulipovunjwa kioo nae alitazamana na bastola nyingine kwa askari alievunja kioo kile.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Yule askari wa tatu hakuifanya ajizi, haraka alitoa pingu akazunguka na kupitisha mkono wake, kwenye Lock ya mlango akaibonyeza lock zile zikafunguka, akaufungua mlango wa nyuma wa gari ile, akawavesha pingu moja Nigga na Carlos Bogga. Mkono mmoja mmoja kisha akawavuta nje kwa nguvu akiwaamrisha watoke. Kwa kuwa Nigga na Carlos Boga, walikuwa viti tofauti iliwapa shida kidogo kupita sehemu moja, lakini ile amsha amsha za askari walijikuwa wametoka wote wawili kwa pamoja wapo nje ya gari ile. Wakaamriwa kulala chini. Yule askari aliewafunga pingu, alianza kuwapekua miilini mwao, lakini hawakuwa na kitu cha kuhatarisha amani. Askari yule baada yakuwapekuwa Nigga na mwenzake, aliuwendea mwili wa Marehemu Baba Ubaya akaipiga teke basola iliyokuwa kwa Marehemu Baba Ubaya mikononi mwake ikadondoka chini.
Yule askari aliepambana na Marehemu baba Ubaya, aliitazama fulana yake, akaiona imeweka mashimo mawili ya risasi kifuani mwake. Akaivua ile fulana, ndipo ilipoonekana BULET PROOF, aliyokuwa ameivaa kifuani mwake hadi tumboni. Aliibusu ile Bulet Proof kwa kuokoa maisha yake, akaona bila ya kifaa kile muda ule angekuwa tayari ni marehemu. Gari ya carlos Boga ilipekuliwa kwa haraka zikakutwa simu tatu, hakukuwa na kingine zaidi ya maganda mawili ya risasi ya bunduki aina ya Chines Automatic aliyoitumia Marehemu Baba Ubaya.
Mkuu wa upelelezi alimuamuru mama mdogo wa Nigga kushuka chini ya gari ile na yeye akashuka nae, akamvisha pingu mikononi mwake, kisha akamuweka katika viti vya Nyuma vya gari ile Toyota Noah. Mama Yule alikuwa hafai kupwa wala kulumagia, kwani alipoisikia milio ya risasi alikuwa akipiga kelele za woga sana hasa pale alipoushuhudia mwili wa Baba Ubaya ulivyoachana na roho yake.
Nigga na Carlos Boga waliinuliwa msobemsobe, wakapakiwa ndani ya ile Noah. Askari mmoja aliifata ile Bastola iliyokuwa chini, aliyokuwa nayo Marehemu baba Ubaya, akaichuua kwa Leso, akaizungushia kitambaa kile, ili asiishike kwa mikono yake. Mkuu wa upelelezi alikwenda katika ile gari GX 100, akaufungua mlango wa gari ile, akayatazama maganda mawili ya risasi yaliyokuwa ndani ya gari ile, akatikisa kichwa chake kwa kukubali kitu kilichokuwa kikipita katika akili yake. “Namba za maganda haya ya risasi, ni sawa kabisa na risasi tulizozikuta sebuleni kwa huyu mshenzi. Yaani huyu mtu ni hatari sana, hapa alitaka kutoroka.” Mkuu wa upelelezi alitamka maneno yale, huku akitoa redio ya upepo kutoka mfukoni mwake, akaongea na watu wa Breakdown waende pale katika eneo la tukio ili wakaivute, ile gari GX 100. Kisha akawasiliana na askari wa Doria Kenda, ili nao wafike pale kupakia maiti ya Marehemu Baba Ubaya. Akawaelekeza sehemu ile waliyopo na nusu saa baadae magari yale yalikuwa mahala pale yakiwajibishwa. Mwili wa Baba Ubaya ulipakiwa ndani ya gari Toyota Land Cruser pickup ya Doria Kenda, na GX 100 ikafungwa minyororo na gari aina ya Range Lover 109. ikainuliwa na ile gari yakuvutia magari yaliyopata ajali, Breackdown ikawa ikifungwa ili ivutwe.
Watu walikusanyika eneo lile, wakasimama mbali na tukio lile wakawa wanashuhudia kinachoendelea. Mara gari ya shirika la utangazaji la taifa TBC liliwasili eneo lile kwa kasi, wakashuka waandishi wake waliokuwa wamevalia vitambulisho shingoni mwao, wakaanza kuipiga picha za Runinga ile gari GX 100. Pia Camera zao zikamulika na ile maiti ya Baba Ubaya iliyokuwa imelazwa katika gari ya Polisi. Lakini walipotaka kuwapiga picha wahalifu, mkuu wa upelelezi alizuia wasifanye vile kwani wangeharibu upelelezi. Hivyo waliipiga picha ile Toyota Noah waliokuwamo watuhumiwa wakamulika kwenye namba za gari ile, kisha wakamuhoji mkuu wa upelelezi wa kituo cha buguruni kuhusiana na tukio lile, nae akazungumza nao. “Kwanza kabisa nachukua fursa hii, kuwapongeza sana watu wa habari, kwani leo asubuhi Runinga na Magazeti yalitangaza kuhusu wahalifu hawa, na hatimae sasa wote watatu, tumewatia mbaroni. Japo Jambazi moja lilipambana na Polisi lakini tumelishinda, kwani lilimtwanga risasi askari aliekuwa kazini kihalali, Mungu Bariki jeshi letu sasa lina vifaa vingi tunamshukuru kwa shukurani za kipekee IGP kwa kuboresha jeshi letu, kwa kutujazia vitendea kazi. Lakini kama ingekuwa askari wetu asingekuwa na kifaa kile cha kuzuwia risasi bila shaka angeuwawa na Jambazi leo. Tunatambua huu ni mtandao, hivyo tumejipanga vyema kuhakikisha tunatokomeza Ujambazi nchini. Napenda kutoa wito kwa raia wote nchini. Watoe taarifa kwetu mara wanapomuona mtu mtaani kwao haeleweki eleweki, na sisi mara moja tutafika eneo la tukio kwa wakati. Tunawaomba sana wanachi watuamini kwani jeshi lilipitia katika changamoto nyingi, na sasa tumejipanga kivingine kabisa. Wananchi nawaomba watii Sheria bila shuruti” Mkuu wa upelelezi alizungumza na watu wa habari.
Askari aliepambana na Marehemu baba Ubaya aliionesha Fulana yake, iliyokuwa na matundu ya risasi ambayo yalikuwa yapo mbele ya fulana yake, kuonesha kuwa alikuwa akipambana na adui ana kwa ana. Watu wa habari walichukuwa picha ile ili kuonesha yale matundu katika fulana ya askari yule. Kisha walihamia katika ile gari GX 100, wakawa wanaipiga picha zile kwani tayari gari lile lilianza kuvutwa kuondoshwa sehemu ile kupelekwa kituo cha Polisi buguruni kwa uchunguzi zaidi. Watu wa habari hawakuishia pale walimulika video yao kwa raia waliokuwa wamejaa kutazama tukio lile la hatari. “Hebu niambie wewe umeona nini hapa kimetokea?” Mwandishi habari alikuwa akimuhoji raia mmoja aliekuwa mbele kwenye kundi lile kubwa la watu, ili kupata taarifa ya shuhuda kunogesha habari yake. “Mie ninaishi Makoka, hivyo nilikuwa napita hapa natembea mdogomdogo kuelekea kwangu, mara nikasikia mikaa huku inalia!” “Mikaa au risasi?” Mwandishi habari alimuuliza yule raia wa jinsia ya kiume aliekuwa akizungumza kwa lugha ya mtaani zaidi. “Mikaa si ndiyo hizo Shaba, yaani ni noma sana zimelia shaba hakuna mtu aliebaki hapa kila mtu alilala mbele, hili kundi lote unaloliona hapa limeibuka mida hii mziki ulivyopoa.” Mwandishi habari alichoka choko, kwani lugha ya yule raia ilikuwa ni ile lugha ya watumia MAJANI. Au wenyewe wameubatiza jina wanauita MMEA. Wengine wanasema GANJA. Wapo wanaosema MARIJUANA Ila Kiswahili sanifu inaitwa BANGI. Kwani yule raia wakati akiongea maneno yale mwandishi ilibidi ahamishe Mike yake karibu na mdomo wa jamaa manaake, jamaa alikuwa na mdomo mweusi kama wa kunguru, uso ulikuwa umemvimba, alama za kichwani na usoni Tyson bondia kapitwa, yaani zilikuwa hazihesabiki, meno yake yalikuwa yamesalitiana na mswaki kwa muda mrefu tu nyuma. Rangi ya meno yake yalikuwa kama jezi ya timu ya mpira wa miguu ya vijana wa jangwani, au unaweza kusema ameweka Bizari kinywani mwake.
***
Mkuu wa upelelezi, mara alipopokea simu ya vijana wake kuwa Nigga haonekani eneo lile la Mwanachi pale relini, ndipo alipowaita wamfate mbele ya barabara ile walipoiacha gari yao, ikiwa imefunuliwa Boneti kama gari iliyochemsha. Hivyo wakaambizana kwa simu wote kwa pamoja wakarudi katika barabara ile ilipokuwa gari yao, lakini walipoifikia hawakupanda bali walimpa ishara dereva awafate kule mbele waendapo. Wao walipandisha ile njia ya gari mbele kulia kwenye kona upande wa kulia pale maarufu eneo lile wanapaita Tabata Kisiwani, wakaiona gari Toyota Noah ikiwa imeegeshwa ikitazama mbele walipokuwa wakielekea wao. Hivyo gari ile waliitazama kwa nyuma. Waliipita ile gari kama hawana habari nayo. Walisikia mziki wa rusha roho ukipigwa ndani ya gari ile. Mbele kama hatua hamsini hivi kutoka pale ilipokuwa ile Toyota Noah, waliiona gari ya mkuu wa Upelelezi ikiwa imeegeshwa. Hivyo walipoifikia wakafungua milango wakapanda ndani ya gari ile. “Sasa tunakwenda kwenye plan B Plus. Tunakamata yule mama pale, kisha yeye tutamlazimisha ampigie simu Nigga kwa simu yake, kisha sote tutapanda ndani ya gari ile. Ikiwa Nigga atakuja basi tutakamata yeye kwanza kisha atatupeleka kwa wenzake. Lakini ikiwa watakuja wote itakuwa tumepiga ndege wengi kwa jiwe moja sawa?” “Sawa Afande.” Askari wale watatu walijibu kwa pamoja. “Kwa kuwa tunakwenda kupambana na Majambazi ambao wanatumia silaha za moto kama sisi, risasi haitambui askari inauwa hata alieitengeneza. Je? mmevaa Bulet Proof wote?” askari wale kila mmoja akajibu “Ndiyo Afande tumevaa.” Baada yamajibu yale kutoka kwa askari wale shupavu vijana, ambao damu yao bado inachemka sawasawa kwa ujasiri na weledi. Mkuu wa upelelezi alimpigia simu yule dereva aliekuwa na gari aliyoifungua boneti akampa maelekezo. “Njoo haraka sasa hivi huku tulipo, utapinda kulia hapo mbele, utaiona ile gari iliyotuleta huku, piga pini nyuma na mie napiga mbele tunaanza na huyu. Kwani yule kuku wetu kesharuka barabara haonekani.” Baada yakusema maneno yale, mkuu wa upelelezi aliipindua gari yake akarudi alipotoka huku akiwa haoneshi kabisa kama anampango wowote na ile Toyota Noah iliyokuwa imeegeshwa upande wa kulia mwa barabara ile ya mtaa. Gari ya mkuu wa upelelezi iliposogea kidogo tu mbele, mara wakaiona ile gari yao nayo ikipinda ile njia ya kulia, ikiwa inakuja kwa kasi kiasi. Mkuu wa upelelezi aliongeza mwendo na yeye wakaipiga pini ya nyuma na mbele ile Toyota Noah.
Mama yake Mdogo Nigga, kabla hajatanabahi, Hamadi wanaume tayari walikuwa washabana mbele na nyuma, wamemuweka mtu kati. http://deusdeditmahunda.blogspot.com/Mama yake Mdogo Nigga akawa amepigwa na butwaa hakuwa na lakufanya kwa muwambo ule. Kabla hajajishauri kinachotokea mara askari watatu walishuka kutoka katika gari ya mkuu wa upelelezi, Bastola zikiwa mbele zinamlenga yeye. Askari mmoja aliufungua mlango wa mbele wa upande wa kushoto ambao ulikuwa wazi, akamtuliza atulie mama yake mdogo Nigga aliekuwa anatetemeka kwa hofu. “Askari, tulia hivyohivyo sikiliza maelekezo.” Yule askari alimwambia maneno yale huku mkono wake wa shoto akimuonesha kitambulisho chake, na mkono wa kulia akiwa ameshika silaha ile ya moto. Aina ya Revolver Six Round.
Askari mwengine aliimarisha ulinzi kwa raia akiwa amekamata Bastola Mkononi aliwatawanyisha raia waondoke mahala pale, kwani wakati wa kupiga simu kwa Nigga isije ikawapa taarifa wahusika. Raia waliokuwa nje ya nyumba zao, ambao waliliona tukio lile likifanyika, mara walipoona bastola tu zipo nje zinapungwa kwenye Noah na upande wao kila mmoja alitafuta sehemu yake yakukimbilia. Ilikuwa ni mbio kama walikuwa wakikamatwa wao. Watu waliminyana mlangoni wakigombea kuingia ndani. Hawakujali biashara zao zilizokuwa zimetelekezwa peke yao. Kila mtu alikuwa akijaribu kuyanusuru maisha yake. Katika nyumba nyingine mama mmoja alitoa kituko cha aina yake, kwani alikuwa siku zote hawezi kuinuka na kutembea kwa haraka. Ili ainuke ilimbidi aweke mikono yake kwanza chini ajizoezoe ndipo hatimae kwa kusimamia kitu ndiyo ainuke. Nyumba yake ilikuwa usawa wa ile Toyota Noah ilipoegeshwa, alikuwa akiuza mihogo yakukaanga, amejaza watu wadogo kwa wakubwa. Jina lake maarufu katika eneo lile akiitwa mama bonge kutokana na mwili mkubwa aliokuwa nao. Mara alipomuona Yule mwanaume amekamata bastola mkononi mwake akiwataka watu woye kuondoka haraka eneo lile, yule mama muuza muhogo alikuwa mwepesi kuliko vijana waliokuwa wakinunua mihogo yake. Kwani aliinuka kwa haraka akazitimua mbio ndani, huku nguo zake zikimtoka wala asisimame kuziokota, kifupi alikuwa hana habari kabisa kama nguo zilikuwa zikimdondoka akawahi kuingia ndani kisha akaufunga ule mlango akauegemea ili kuzuia wale watu waliokuwa na silaha wasiingie ndani ya nyumba yake. Dhana yake yote ilikuwa wale ni Majambazi tu, na sivinginevyo. Vijana waliokuwa nje walikuwa wakiusukuma ule mlango ili ufunguke waingie ndani, yule mama akawa akihisi wale watu wenye bunduki ndiyo waliokuwa wakiusukuma ule mlango. Hivyo alizidisha nguvu kubwa sana kuegemea mlango ule huku macho yakiwa yamemtoka kayakodoa, meno ameyakaza, anahema juu juu presha na pumzi zikiwa zimempaakwa tendo lile lakuutikisa mwili ule mkubwa kwa haraka. Ama kweli bunduki hutisha sana kwa asieizowea. Wale raia waliokuwa wakiugombania ule mlango ilibidi watafute nyumba nyingine za kujistiri lakini kwa pale, hawakuweza asilani kufua dafu.
Wale askari baada yakufanikiwa kumtuliza mama yake mdogo Nigga, mkuu wa upelelezi akatumia Mbinu za Medani, katika kumfanya mama yake mdogo Nigga atulie. “Tulia usiwe na wasiwasi, wala sie hatuna haja na wewe, ila wewe ni daraja tu ili kufanikiwa kumpata Baba Ubaya, hata Nigga tulikuwa tunamtaka ili atufikishe kwa Baba Ubaya tu, hivyo tulia shaka ondoa. Kama ukifanikiwa kutuvutia Nigga nae akatufikisha kwa Baba Ubaya, tunakuachia hatuna habari na wewe. Tulikuwa tupo nanyi tangu Kijitonyama tumetembea wote hadi hapa, shida yetu ingelikuwa ni nyinyi msingefika hadi huku, tungekuwa tumeshawakamata kulekule” Mama Nigga alishangaa sana maneno yale aliposikia walikuwa na askari wale tangu Kijitonyama. Maneno yale yalimuingia akaona kweli yeye siye anaetafutwa, kwani hata picha zake hazikuwekwa katika magazeti, jambo hilo likamtia moyo sana, bila kutarajia Mbinu za Medani zikamnasa mzima. “Mie Nigga ameniacha pale mbele, amesema anakwenda kuzungumza na wenzake nimsubiri hivyo sijui amekwenda wapi.” Mama Nigga alijibu kumwambia mkuu wa upelelezi . “Upo sahihi hujui alipokwenda Nigga hata sie tunalifahamu hilo. Lakini tunatambua kuwa hapa unamsubiri yeye. Pia tunafahamu kuwa muda huu, Nigga atakuwa na wenzake hivyo nataka umpigie simu, umwambie wewe umeshakaa sana mahala hapa, kama vipi akwambie alipo umfate au aje yeye. Kumbuka kuwa simu yako tunaloud spika sasa ukileta ujanja wowote wakumjulisha kuwa umekamatwa, basi tambua tutakujumuisha katika shitaka hili na wewe utakuwa ndiyo mshitakiwa namba moja. Hivyo fanya kama nilivyokwambia ili uwe huru.” Mama Niga ndipo ilipochukuliwa simu yake na askari yule, kisha akaambiwa yule mama ataje namba za Nigga akazitaja, na kwenye simu ile ilipopigwa namba ile likatoka jina Nigga Boy likiwa limehifadhiwa hivyo. Mkuu wa upelelezi aliipiga ile simu ilipoita akaweka spika ya nje kisha akaishika yeye ile simu, akamuwekea mdomoni mwanamama yule azungumze. Akiwa chini ya ulinzi wa Polisi, mama yake mdogo Nigga alizungumza na Nigga kwa simu, ndipo Nigga aliposema alikuwa na kina nani, wapo wapi na aina ya gari waliyokuwamo. Askari wale wanne wakaingia katika ile Toyota Noah, mkuu wa upelelezi akakaa mbele kwani itifaki ilikuwa ikimruhusu. Wale askari wengine watatu walipanda nyuma katika Noah ile, yule dereva aliebakia akapewa jukumu lakuita askari mwengine ili kuja kuiendesha gari ya mkuu wa upelelezi, kuipeleka kituoni. Akapewa ufunguo wa gari ile, pini zikatolewa za magari yale, mama yake mdogo Nigga akaendesha gari ile kuwafata kina Baba Ubaya sehemu walipokuwa.
***
Mwili wa Marehemu baba Ubaya, ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya taifa Muhimbili, taratibu za kuhifadhi maiti zikafatwa dakitari alipokea maiti ile ikawekwa katika chumba kilichokuwa na maiti wengi na baridi la kutosha Mochari. Ulihifadhiwa mwili wake katika jokofu maalum la kuhifadhia maiti. Baba Ubaya mara moja amehama katika dunia hii, amekuwa marehemu. Ama kweli binaadam tunadanganywa na pumzi tu, zikikata hatuna uhai tena. Baba Ubaya aliekuwa akipambana na askari, aliekuwa na nyendo nyingi tu, amelazwa katika jokofu hata Inzi hawezi kumfukuza mwilini mwake. Alikuwa amelazwa uso wake umeelekezwa juu.
Nigga, Carlos Boga pamoja na mama yao mdogo, moja kwa moja walifikishwa katika kituo cha Polisi cha Sitaki Shari. Kwa hatua zaidi. Watu wale hawakufikishwa Mahabusu (LOCKUP), bali wakaenda nao majumbani mwao kuwapekua kama wangeweza kupata silaha,au chochote ambacho kingekuwa ni hatari kwa raia kumiliki, lakini hawakupata kitu chochote cha hatari kwao ambacho kingewasaidia katika kesi. Wakarudi nao hadi katika mwembe maarufu katika kituo cha Sitaki Shari, ili kuwahoji kwa kina. “Haya tumefika hapa tunataka Kihusika chetu, leo mtatuambia Bunduki zilipo kwani Baba Ubaya yake tumeshaipata na tumeshamalizana nae, sasa bado nyie tunazitaka bunduki zenu, tuambieni haraka zipo wapi tukachukue, hata kama mmezifukia tutazifukua tu kwani majumbani kwenu hatukuzipata.” Mkuu wa upelelezi wa kituo cha Polisi Buguruni, aliwaambia wahalifu wale waliokuwa mbele ya macho yake. “Jamani samahani mie nina wakili wangu naomba nimjulishe kuwa nipo hapa ili aje.” Nigga alimwambia mkuu wa upelelezi huku akiwa amekata tamaa kabisa. “Huyo wakili wako atakuja tu, ila ukiwa hutaki Shari kama jina la kituo hiki, tupe mizigo yetu. Kama unadhani utaweza kukaza basi jaribu lakini mwenzako Tafu Guy, alikaza mwisho akiwa keshaumia ametuambia kila kitu hivyo bado nyie, kwani bado mpo vizuri hamjaharibika kabisa. Sasa nyie jifanyeni masugu muone mtakavyo chakaa.” Mkuu wa upelelezi alimwambia Nigga maneno yale akionesha hatanii hata kidogo. “Wazee mie sina Bunduki, mtaniuwa bure tu, Bunduki alikuwa nayo Baba Ubaya ndiyo tuliyokuwa tunaibia hiyo hiyo” Nigga alisema maneno yale, huku akitaharuki kwani aliwaona askari watatu waliojengeka kimazoezi wakijongea pale alipo huku wakinyoosha nyoosha viungo vyao. Askari wale walijongea sehemu ile kwa kazi moja tu, kuhakikisha mtuhumiwa anasema silaha zilipo. “Nyie mnampakazia Baba Ubaya kwa vile hayupo siyo? Basi bora ya mwenzenu aliekufa kuliko nyie mliokuwa hai, mbona cha moto mtakiona. Yaani mtaingia Gereji sasa hivi tuwatengeneze.” Mkuu wa upelelezi alikuwa amechachamaa sana hataki mchezo hata kidogo. “Wewe mama zipo wapi bunduki zetu tuambie au tunakuua sasa hivi” Yule mwanamke alipokuwa anajitayarisha kusema tu, alisikia kofi kubwa la uso limempata barabara usoni mwake, likamchonyota na kuona viruwe ruwe mbele yake. Mama yake mdogo Nigga akabadilika uso wake wote na kuwa mwekundu muda ule ule, kisha ukaanza kuumka alama ya vidole vikionekana wazi kabisa sehemu lilipotua lile pigo. “Sema ziwapi Bunduki zetu, wewe utakuwa unajua bunduki zilipo, tuambie zipo wapi?” Mama yake mdogo Nigga, alikuwa hana kumbukumbu katika maisha yake kwa umri aliokuwa nao kama aliwahi kupigwa kofi pambe kama lile maishani mwake. Wale askari waliokuwa wamejengeka kimazoezi walikuwa hawataki mchezo wala hawakuwa wakitazama uzuri wa mtu, kinyume chake wao walikuwa wapo kazini tu. “Baba zangu mie sijui wanapoweka ningewapeleka mkazichukue, lakini sijui lolote“ Mama yake mdogo Nigga wale askari waliokuwa pale, hakukuwa na askari hata mmoja aliekuwa na sifa ya kuwa baba zake, kwani yeye umri wake ulikuwa ni mkubwa kuliko wale askari aliokuwa akiwaita baba zake. Ama kweli kuchanganyikiwa kubaya. “Wewe Carlos Bogga nilikuwa nakutamani kweli, unanikumbuka mie wewe?” Carlos Boga aligeuka na kumtazama yule askari aliekuwa na nia yakumgeuza ili watazamane apate shabaha yake sawasawa. Kofi zito la nyuma ya kiganja, lilitua katika jicho na kwa kuwa sehemu ile ni laini, Carlos Boga alivimba muda uleule. Yule askari alikuwa na mikono migumu kama ubao! Hali ile ya kuguswa huyu na yule, iliendelea kwa muda lakini wahalifu wale walikuwa wamekaza kweliweli. Ndipo lilipoletwa kubwa lao ili kushikisha adabu watu. Lilikuwa ni Gongo gumu refu hatari, wengine waliliita Mpini wa mpingo, lakini watu wa kazi waliliita Mwana ukome. Ajabu wale askari walilipa jina la Fatuma. Nigga na Carlos Boga walipigwa katika maungio ya miili yao kwa gongo lile mpigaji akipiga kama anaua nyoka. Mpigaji alikuwa hapigi sehemu nyingine ila kwenye maungio tu. (JOINT) Dakika ishirini ya kichapo kile, Nigga akapopoteza fahamu akiwa katika kiti moto kituoni pale. Mwili wake ulimvimba mara dufu zaidi ya mwili wake. Lakini hadi anapoteza fahamu alibaki katika msimamo wake kuwa silaha alikuwa nayo Baba Ubaya yeye hana kitu hicho.
Mama yake mdogo Nigga hali ilikuwa tete kwa upande wake, kwani alifinywa ili aseme zilipo Bunduki, lakini kwa hakika kabisa alikuwa hajui zilipo, yaani angejua tu Bunduki zilipo basi muda uleule angeweza kuwapeleka sehemu zilipo. Hivyo alikuwa akiumia kwa jambo asilolifahamu. Polisi fikra zao walikuwa wakijua Mama yake Mdogo Nigga, akitingishwa sawasawa ataweza kuwaonesha silaha zilipo. Lakini mama yule alifinywa hadi haja ndogo zikamtoka, lakini kiliochake kikawa hajui zilipo silaha, lau kama angelijua angeenda kuwapa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Carlos Boga kichapo kilipokuwa kikubwa kwake akawaambia wale askari. “Wazee nasema ukweli msiniuwe, mie udereva ndiyo kitengo changu kwenye wizi sishiki silaha, silaha alikuwa nayo Baba Ubaya, ndiyo ile aliokuwa nayo kule.” Askari wale wakamuuliza Carlos Boga. “Haya kama wewe ndiyo dereva sasa tuambie matukio yepi mliyoyafanya, na mmefanya na nani au tunakumaliza kabisa. Na kama ikiwa utabahatika kutoka hapa, mwanamke utakuwa unamtazama macho tu katika umri wako wote uliobakia.” Carlos Boga akatambua kuwa kutaja matukio yote aliyoyafanya ni kujiongezea majalada yakwenda nayo mahakamani, hivyo akaona alitaje tukio la kesi ya Muhindi wa Shuwea pekee, kwani Nigga aliwaambia kuwa wale mashahidi muhimu wote hawakupo. Hivyo akalitaja tukio lile tu. “Haya tuambie mlioiba pale mlikuwa wewe na kina nani?” Carlos Boga akaweka mambo hadharani, ili kunusuru uhai wake, kwani siku ile amemuona Baba Ubaya akiaga Dunia, Nigga akizirai kwa kipigo, mama yake mdogo Nigga haja ndogo ikimtoka bila kujijua, akaona hapana asiumie zaidi. “Wazee pale tulikuwa watu watatu, mie nilibaki chini nje katika gari nikiwa dereva, Baba Ubaya ndiyo alikuwa Afsa aliyeshika silaha, na Nigga yeye alicheza uchale.” Lugha ile aliyokuwa akiizungumza Carlos Boga, askari walikuwa wakiifahamu sana. Aliposema Baba Ubaya alikuwa Afsa, alikuwa akimaanisha yeye ndiyo aliekuwa na amri kwa vile bunduki ilikuwa mikononi mwake hivyo hakukuwa na wakumpinga katika amri zake. Na aliposema Nigga alicheza Uchale, alikuwa amemaanisha, Nigga ndiyo alikuwa akikusanya vitu mle ndani, aidha kuwafunga Plasta, na mfano wa hayo. Kiasi kuwa Nigga alibeba pesa Baba Ubaya akawa akimlinda. Polisi waliendelea kumhoji Carlos Boga, lakini wezi wale wote walikuwa mambo mabaya yote walikuwa wakimsingizia Maiti Baba Ubaya ndiyo mwenye silaha, ndiyo alifanya vile ndiye aliefanya hivi, ili mradi walikuwa kila jambo kubwa ni Baba Ubaya.
Nigga alipopata fahamu alijikuta yupo hospitali Muhimbili akiwa na pingu mikononi mwake. Alitibiwa pale kwa siku kadhaa hadi alipopata nafuu alirudishwa kituoni.
***
Mkuu wa upelelezi aliandaa jalada lakuwafikisha Mahakamani watuhumiwa. Dada yake mke wa Baba Ubaya, aliachiwa pale kituoni kwa kuonekana hakuwa akijua lolote. Mke wa Baba Ubaya yeye alituhumiwa kwa kukutwa na gari ya wizi. kwani gari alilokamatwa nalo lilibainika ni mali halali ya Raia mwenye asili ya kiasia Gulamhussein Gondrap Shaha. Mama yake mdogo Nigga aliunganishwa katika shitaka na kina Nigga wizi wa kutumia silaha kwa Mhindi aliekuwa tajiri yake Shuwea Namjupa. Ambapo yeye alikuwa ameunganishwa katika shitaka lile kwenye chaji ya kula njama. Nigga na Carlos Boga, wao walifunguliwa mashitaka matatu. Shitaka la kwanza kukutwa na silaha kinyume cha sheria. Silaha iliyowekwa katika shitaka lililowakabili ni ile aliokuwa nayo Marehemu Baba Ubaya. Katika jalada lingine lilikuwa na mashitaka mawili, shitaka la kwanza kula njama yakutenda kosa la wizi wakutumia silaha, ambalo washitakiwa walikuwa watatu, kosa la pili kutenda kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha. Taratibu zikaandaliwa ili kufikishwa Mahakamani. Kabla hawajapelekwa Mahakamani, liliandaliwa gwaride la utambulisho ili kutambuliwa wahalifu waliofanya tukio lile la unyang’anyi wakutumia silaha. Wakiwa wamesimamishwa katika nafasi tofauti, kwenye mstari wa watu kumi, Nigga na Carlos Boga, waliulizwa kujipanga nafasi waliyoitaka, walipewa uhuru wakubadilisha mavazi kama wangetaka lakini wakasema wanekaa na nguo zao zilezile. Wakiwa wamepangwa katika mstari wa utambulisho ndipo Nigga alipoinua uso wake mbele akaona watu ambao hakuwatarajia kabisa kuwapo pale kwa tukio lile wakiongea na mkuu wa upelelezi. Nigga alipatwa na ganzi sana mwilini mwake, mapigo ya moyo yalimuenda mbio kuliko kawaida, jasho likaanza kumtoka huku vipele vya woga vikiota mwilini mwake. Alishangaa sana ‘Maiti’ kuwa pale Sitaki Shari!
Nigga akiwa amesimama uso wake aliuinamisha chini, alikuwa akihema kwa haraka presha ilimpanda hadi mwili wake ulikuwa ukitetemeka. Mara alimuona askari mmoja aliekuwa amevalia mavazi ya kiraia, akiwa na karatasi mkononi mwake pamoja na kalamu, akiwafata pale walipo. “Nigga na Carlos Boga, tumeandaa gwaride la utambulisho, hivyo mtambuzi atapita kuwatazama kwa mbele kisha atapita kuwatazama kwa nyuma, mtu akiguswa na shahidi basi huyo atakuwa ametambuliwa, na ikiwa mtu anaetambua akipita hakuwagusa basi itakuwa hajawatambua sawa?” Asakari mwenye cheo cha Inspekta, ambae ndie alikuwa msimamizi wa gwaride lile, aliwaeleza taratibu za gwaride la utambulisho linavyofanywa ili wafahamu. Nigga na Carlos Boga waliitikia kwa kichwa kuwa wameelewa. Yule askari msimamizi wa gwaride mwenye cheo cha Inspekta, alipaza sauti kuitwa mtu wa kuja kukagua, na mara moja akaitwa muhusika. Nigga alimtazama kwa wizi mama yule wa Kihindi alieelezwa na wakili Neema Faraja kuwa amefariki Dunia, akisogea katika eneo lile kwa tabu kutokana na afya yake kuzorota. Mama yule alikuwa amesimama kwa mbele ya mstari ule uliokuwa na watu kumi, akawatazama mmoja baada ya mmoja. Macho yake yalipofika kwa Nigga yakasita kuendelea yakasimama. Akamuangalia kwa makini, kisha akasogea hadi pale alipokuwa Nigga akamshika begani kuwa yule ndiye aliemfanyia uhalifu. Inspekta msimamizi wa Gwaride aliandika katika karatasi yake, kisha yule mama wa Kihindi akapita nyuma ya wahalifu wale, akamgusa tena Nigga begani mwake. Yule askari msimamizi wa gwaride lile aliandika tena katika karatasi yake. Baada ya pale yule mama wa kihindi alirudishwa ndani, mstari ule wa watuhumiwa ukabadilishwa, Nigga akabadilishwa nguo, akawekwa nafasi nyingine ya kusimama, akaitwa tena kwa mara ya pili yule mama wa Kihindi kwenda kukagua. Alipofika pale yule Mama hakumgusa mtu mwingine laa bali alimgusa tena Nigga mbele na nyuma katika nafasi nyingine aliyopangwa. Inspekta alifanya vile mara tatu, kama sheria inavyomuelekeza. Na katika mara zote tatu Nigga alitambuliwa peke yake. Carlos Boga yeye ingawa aliushiriki ule wizi, lakini kwa kuwa alikuwa ni dereva hakuuza sura yake kwa watu waliowafanyia unyanyang’anyi ule. Hivyo hakuonwa wakati wizi ukitendeka hivyo hakuguswa kabisa. Baada ya yule mama wa Kihindi kumtambua Nigga mara tatu, askari yule aliandika katika karatasi yake, kisha akamwambia Nigga bado mtu mwingine nae anakuja kufanya utambuzi, hivyo achague nafasi ya kukaa. Nigga alisimama katika msitari ule akibadilisha nafasi akajipanga katikati huku akiwa mnyonge kupita kiasi. Aliinamisha uso wake chini kwa mawazo, alikuwa akiiona jela ilee inamwita kwa haraka. Nigga aliinua uso wake mbele, pale Inspekta Missana John alipoamrisha aitwe shahidi mwingine kwenda kutambua mtu aliemuona kwa macho yake akiwafanyia uhalifu. Mara shahidi yule alijongea sehemu ile taratibu huku akitazama chini, hadi pale katika wahalifu wale kumi waliokuwa wamewekwa pamoja katika mstari mmoja. Shahidi yule alisimama mbele ya watu wale akawa akiwatizama nyuso zao kwa utulivu. Nigga aliinua uso wake macho yake yakakutana ana kwa ana na macho ya Shuwea Namjupa. Nigga alinyong’onyea akaishiwa mate mdomoni. Shuwea Namjupa alitembea hadi alipokuwa amesimama Nigga mzazi mwenzie, akamshika begani kuwa amemtambua kuwa ndiye aliekuwa amefanya uhalifu ule. Tendo lile la utambuzi lilifanyika mara tatu, akimtambua mbele na nyuma. Inspekta Missana John aliandika katika karatasi yake kisha akaamrisha wahalifu warudishwe rumande. Wakiwa wanatembea kuelekea Rumande Nigga alimuona wakili Neema akiwa ameegemea gari yake, mara moja akahisi kuwa ndiye aliemleta Shuwea Namjupa katika gwarie lile. Akajiuliza pesa zake alizotoa zimekwenda bure kumbe yule wakili alimdanganya. Kwani alisema yule mama wa Kihindi amefariki lakini pale amemuona. Akajiuliza mara mbili je Maiti anaweza kwenda kufanya utambuzi?! Ikiwa hiyo haitoshi anamuona na mtu aliempa pesa tasilimu Shilingi Milioni tatu, ambae ni mzazi mwenzie, amemgeuka amekwenda kumtambua, hivyo kama ameweza kwenda kituoni kumtambua basi hakuna shaka hata Mahakamani atakwenda pia. Kichwa kilimuuma sana Nigga akaiona siku yake imekuwa mbaya sana. Carlos Boga yeye aliona ushahidi utakaomsumbua mbele ya Mahakama utakuwa ni maelezo yake ya kukili kosa, lakini kwenye gwaride hakutambuliwa, hivyo akajiona hakuwa na kesi nzito kama kwa swahiba wake.
***
Dada yake Mke wa Marehemu Baba Ubaya alieachiwa huru, alipewa majukumu na mdogo wake kuwa akamtafutie wakili ili awasaidie kwenye kesi ile. Alipewa kadi ya benki iliyokuwa katika pochi yake, kiasi vitu vyake vyote aliwaambia askari wampe dada yake. Alimuandikia namba zake za siri za ATM ili aweze kutoa pesa zakumlipa wakili ili kumnusuru na janga lile. Dada mtu alipotoka aliuliza kwa ndugu jamaa na marafiki, akaelekezwa wakili mzuri akenda kuzungumza nae, wakaelewana wakafanya biashara.
Watuhumiwa walipelekwa mahakamani, katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu wakasomewa mashitaka yao, wote wakakana shitaka. Kutokana na makosa yaliyokuwa yakiwakabili, Nigga na Carlos Boga walikosa dhamana. Kwani unyang’anyi wa kutumia silaha umenyimwa dhamana yake. Sababu hasa ilikuwa ni kuchelea kuharibu ushahidi na mwenendo wa kesi pindi mshitakiwa akiwa nje kwa dhamana. Mke wa Marehemu Baba Ubaya, pamoja na mama yake mdogo Nigga walipata dhamamana kutokana na mashitaka yaliyowakabili wakadhaminiwa, wakaachiwa kwa dhamana. Nigga na Carlos Boga walipelekwa mahabusu katika gereza la Keko hadi baada ya wiki mbili kesi ile itakapotajwa tena.
***
Mbuya Fabiola, alikuwa amekaa katika mgahawa akipata chakula cha jioni kipindi kile cha likizo yake. alikuwa katika mgahawa ule kwa sababu maalum. Alikuwa mara kwa mara akiitazama saa yake, kama imeshawadia muda alioukusudia. Saa yake ilimuonesha kuwa ilishatimu saa kumi na mbili za jioni. Mara akiwa hajashusha mkono wake chini kutoka kutazama saa, alishikwa mkono wake kwa nyuma akashituka sana. Alipogeuka kwa haraka kumtazama aliemshika mkono, uso wake ukatahayari, mdomo wake ukatabasamu. “Karibu sana yaani nilikuwa natizama ifike saa kumi na mbili na dakika zake tu niondoke, kwani mie ahadi za kiswahili huwa sizitaki kabisa.”
Mbuya Fabiola alimwambia mpenzi wake Iddy Teva aliemwita katika mgahawa ule kuwa ana mazungumzo nae. “Mbuya mie ni mswahili wa kuzaliwa, ila sina tabia za kiswahili nina timiza ahadi. Naona leo umependeza sana kisha upo kwenye furaha kulikoni?” Iddy Teva alimuuliza mpenzi wake huku akivuta kiti akaketi kitako. “Hamna nipo kawaida tu ila siku hazifanani, ndiyo maana unaweza siku nyingine mtu ukawa na furaha, na siku nyingine mtu ukawa unahuzuni.” Mbuya Fabiola alimwambia maneno yale Iddy Teva, kisha akamshika mkono na kumpapasa kidogo. “Ehee Mbuya nambie mpenzi nimeona ujumbe wako kwenye Whatsapp wakunita eneo hili je kwema, kwani siku ile umeondoka tukiwa benibeni.” Iddy Teva alimwambia Mbuya Fabiola maneno yale huku nae akiupapasa ule mkono wake. “Iddy ni kwema tu ila ipo hivi, leo nimekuja kukwambia habari njema sana. Nimemshawishi Baba kuhusu wewe japo ilikuwa ni ngumu sana lakini kutokana na hali ya afya yangu, hatimae amekubali uwe mchumba wangu na nikimaliza masomo tuweze kufunga ndoa, hata kama ikiwa Bomani.” Mbuya Fabiola aliposema maneno yale, Iddy Teva alipatwa na mzubao mkubwa sana. “Vipi mbona umepatwa na mzubao wa namna hiyo, hupendi mie kuwa mkeo hebu niambie nijue nisije kupoteza muda wangu kwako bure.” Mbuya alimuuliza Iddy Teva kwa taharuki kubwa. “Mbuya siku tatu tu nyuma nimepeleka barua ya posa kwa mwanadada ambae tupo kituo kimoja cha kuchukua dawa za ARV, na kesho ndiyo tunafata majibu yetu.” Majibu yale yalimfanya Mbuya chakula alichokuwa anakula kimtumbukie nyongo. “Eeee ndiyo umeamua hivyo ee, kweli Iddy ulikuwa hunitaki kwani umeweza kufanya maamuzi hayo haraka sana wakati ulipaswa kunipa muda, inamaana ni jambo ambalo ulilipanga kabla ,ok sawa kwa hiyo unanambiaje sasa?” Mbuya alimuuliza Iddy akiwa ile furaha aliyokuwa nayo awali ikiwa imetoweka kabisa. “Mbuya unajua ile hali tuliyoachana nayo siku ile, uliniambia kabisa niachane na wewe, ukanituhumu kuwa nimekuambukiza Virusi vya Ukimwi, nikaona hakika hatutakuwa na mapenzi tena, ingawa nimekaa jela kwa sababu yako, lakini ikabidi nikubali matokeo ili nigange yajayo. Kwani sikuwa na hakika tena kama tungeweza kuendelea kuwa wapenzi. Ndiyo maana kukataa kuiambukiza jamii virusi, nikaona nitoe barua kwa muathirika mwenzangu na tumeshaahidiana kuwa hatutasalitiana kwani hata yeye aliambukizwa Virusi kwa sababu alikuwa ana Michepuko mingi, sasa tumeamua tunabadilika hatutaki tena michepuko.” Iddy Teva alipomwambia Mbuya maneno yale, alimuona Mbuya macho yake yanatokwa na machozi akilia. “Mbuya alilia kwa kwikwi, mara alikuja muhudumu pale katika meza yao akamuuliza Iddy Teva amuhudumie nini. Iddy kwa kuwa aliona bahari ilikuwa imechafuka ya mazungumzo yao, akakataa kuagiza chochote kwa wakati ule, akimwambia yule dada akijisikia atamwita kumuagiza kwanza anapumzika. Yule muhudumu akageuka na kuelekea kwa wateja wengine kutoa huduma. “Iddy nisamehe sana, nipo chini ya miguu yako. Wewe siye ulieniambukiza Virusi naomba utambue hilo, ila mie ndiye niliekuambikiza wewe.” Mbuya Fabiola alimwambia Iddy Teva aliekuwa makini kumsikiliza. “Sikwambii hivyo kwa sababu umeniambia unataka kuoa laa, ila nilikwita hapa ili nikwambie hilo na kukuomba radhi sana kwa kukuharibia maisha yako. Mie sikuwa natambua tangu awali kuwa ninaishi na virusi vya Ukimwi, ila baada yakupima kutokana na wewe ulivyoniambia umeonekana na virusi, nilirudi nyumbani nikiwa ninalia na mnyonge. Baba aliponiuliza kitu kinachoniliza nikamwambia nimepima afya yangu nimeonekana nimeathirika. Sikutarajia kutoka kwa baba maneno aliyonambia, kwani mie nilidhani nitachapwa nakufukuzwa nyumbani au hata kupelekwa Polisi, lakini kinyume chake amenambia niliathirika tangu nikiwa mdogo!” Iddy Teva macho yalimtoka pima, mdomo akauwachia wazi kwa habari ile. Akamuonea huruma sana. Mbuya alipofika sehemu ile akawa analia kwa sauti ya chini kilio kilichoambatana na mafua mepesi puani mwake. Iddy Teva alisogeza kiti chake, akapeleka mkono wake katika mabega ya Mbuya akamwambia kwa utulivu. “Mbuya pole sana, maisha yamekusaliti tangu mdogo kwa gonjwa hili hatari linaloisumbua Dunia nzima. Hakika hukuwa na hatia yakuwa muathirika, ila Mungu ametaka iwe hivyo kwako basi huna jinsi kwani Jitihada hazishindi kudura. Kadari ya Mungu imeshaamua hilo huwezi kulibadili tena, pole sana kwa matatizo yaliyokusibu. Tangu sasa nakufahamisha kuwa nitakuwa na wewe na ile barua ya posa nitamwambia mshenga wangu akabadilishe msimamo wetu, na uwamuzi wangu tangu leo hii ni wewe Mbuya Fabiola kuwa mchumba wangu na baadae uwe mke wangu wa ndoa mara tu utakapomaliza masomo yako.” Kauli ile ya Iddy ilimfanya Mbuya ageuke kumtazama Iddy usoni mwake. “Iddy unasema kweli mpenzi utakuwa pamoja na mimi?!” Mbuya alimuuliza Iddy Teva kwa kutokuamini kabisa. “Ni kweli mpenzi wangu, mie niliamua kuanzisha mahusiano mapya sehemu nyingine kwa sababu kuu tatu. Kwanza nilikuwa nimejisikia vibaya sana pale uliponambia kuwa mie nimekuambukiza virusi, nikaona kama ikiwa ni kweli utakuwa na visasi na mie hivyo tusingeweza kuishi kwa amani kwani imani yako ingekuonesha mie nimeyaharibu maisha na ndoto zako za baadae. Pili ni kwa sababu wewe mwenyewe ulinieleza siku ile niachane na wewe au ungenifanyia kitu mbaya, sikuwa na sababu yakulazimisha penzi pasipo na penzi. Tatu nilimuhofia sana Kapteni Fabiola, kwani alishanipeleka jela kwa ajili yako. Hivyo mambo hayo matatu yalinifanya mie nifikirie kuwa na mke sehemu nyingine. Ila kwa kuwa umenambia mzazi wako ambae ndie alikuwa ni changamoto kubwa katika mahusiano yetu amekubali uhusiano wetu. Pia umekili kuwa wewe ndiyo uliyeniambukiza mimi Virusi, lakini pia umeniomba msamaha basi na mie sina pingamizi kwako, nimekusamehe na nitaomba unifikishe kwa Kapteni Fabiola leo hii nikathibitishe hilo isiwe unanilaghai kumbe hali ikawa ni tofauti.” Iddy Teva na Mbuya Fabiola siku ile walikuwa kama ndiyo walikuwa wameonana kwa mara ya kwanza, mapenzi yao yaliibuka upya ikawa kiti mtekea, haba jana zaidi leo.
***
Kesi ya Nigga na wenzake, ilipokwenda tena katika mahakama ile, upande wa mashitaka wakaieleza mahakama kuwa ushahidi umekamilika, wakaiomba mahakama ipange tarehe fupi ili wapeleke Facts Mahakamani kuwasomea washitakiwa. Mahakama iliahirisha kesi ile hadi siku tatu baadae. Ilipokwenda tena pale Facts ilisomwa kwa washitakiwa wote. Ilionesha idadi ya mashahidi na vielelezo vinne, ambavyo kwa mujibu wa facts ile, kulikuwa na maelezo yakukili kosa washitakiwa wane. Pamoja na kielelezo cha silaha Bastola aina ya Chinise Automatic. Mashahidi waliosomeka kwenye facts ile walikuwa ni mashahidi watano. Alikuwapo Shuwea Namjupa, mama wa Kihindi tajiri yake Shuwea pamoja na tajiri yake mwenyewe aliewakuta wakiwa wamefungwa Plasta. Shahidi huyu Nigga alielezwa na wakili Neema Faraja kuwa amehama nchi hii amehamia Canada.
Kwa upande wa askari Polisi wao waliingiza mashahidi wawili muhimu. Alikuwapo Inspekta Missana John msimamizi wa gwaride la utambulisho, pia akakuwapo mkuu wa upelelezi wa kituo cha Polisi Buguruni ambae kesi ile yeye alikuwa ndiye mpelelezi wake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Facts ile ilikuwa imesomwa na Karani wa mahakama ile vifungu kwa vifungu. Katika kipengele cha kupanga njama yakutenda kosa, Mama yake mdogo Nigga alipoulizwa kuwa anawatambua washitakiwa wenziwe Nigga na Carlos Boga, alikili kuwa anawafahamu. Nigga ni mtoto wa dada yake na Carlos ni rafiki ya mwanawe. Hakujua katika kukili kule kwa kesi iliyokuwa inamkabili ya kula njama ya kutenda kosa alikuwa akijiingiza hatiani. Bahati mbaya sana sheria ya Kanuni ya adhabu katika SECTION NO 8 OF PENAL CODE CAP 16 inasema kwamba; Kutokujua Sheria siyo kinga yakutenda kosa la jinai. Isipokuwa itakuwa kinga tu kama sheria yenyewe itakuwa ndiyo kipengele cha kosa.
Mama yake mdogo Nigga akawaingiza matatani mwanawe na rafiki yake bila yakujua madhara yake. Kesi ile ikaendelea ikapangwa tarehe nyingine ambayo mashahidi waliitwa ili kwenda kutoa ushahidi. Ilipofika tarehe ya ushahidi Polisi ilipeleka mashahidi wote watano mahakamani pamoja na vielelezo vyao. Mashahidi walitoa ushahidi wao wote watano kila mmoja kwa muda wake, washitakiwa walipata fursa ya kuwahoji kutokana na ushahidi walioutoa. Kisha vidhibiti vikatolewa Mahakamani kama kielelezo wakianza na maelezo yakukili kosa washitakiwa. Washitakiwa walikosa namna ya kisheria ya kupinga maelezo yale yasipokelewe kama kielelezo, hatimae Mahakama ikayapokea kama kielelezo. Silaha ilipotolewa kama kielelezo washitakiwa waliipinga kwa nguvu kubwa wakidai hawakukamatwa nayo wao. Ushahidi ulioelezwa kuwa wamekutwa nayo wao wakaupinga sana. Walipoulizwa na Hakimu ilikuwa ni silaha ya nani, wakajibu ya Marehemu baba Ubaya. Walipoulizwa huyo marehemu wakati akiuwawa wao walikuwa nae wakakaa kimya hawakuweza kumkataa marehemu Baba Ubaya kuwa hawakuwa nae. Basi hakimu aliandika kila kilichotokea katika kesi ile. Baada yakukamilisha kutolewa ushahidi na vielelezo upande wa mashitaka ulifunga ushahidi wao. Mahakama ikapanga tarehe nyingine ambayo itatoa maamuzi madogo Ruling.
Tarehe iliyopangwa ilipowadia, Hakimu alitoa maamuzi madogo Ruling, washitakiwa wote watatu walipatikana na hatia wakatakiwa kujitetea ili kuieleza Mahakama kwanini wamehusishwa na shitaka lile. Washitakiwa wote kwa pamoja walijitetea, Mahakama ikawasikiliza kila mmoja, ikaandika utetezi wao kama walivyoutoa, hatimae wakamaliza Mahakama ikapanga tarehe ya kutoa hukumu.
***
Mke wa Marehemu Baba Ubaya, yeye alipelekwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala pale mtaa wa Lumumba na Barabara ya Morogoro. Alisomewa shitaka la kukutwa na gari la wizi. Wakili wake wa utetezi akasimama kujitambulisha kumtetea mshitakiwa. Kesi ilisomwa ikafikia siku ya ushahidi mmiliki wa gari ile alipopanda Mahakamani, aliieleza Mahakama kuwa yeye aliporwa gari yake na Mwanaume hakuwa Mwanamke. Pamoja na msaada wa wakili katika sheria, Mke wa Baba Ubaya ilipofika siku ya hukumu aliachiliwa huru na Mahakama ile, kwani ilionekana Mke wa Baba Ubaya alikuwa hakuiba wala kuwepo sehemu ya tukio, kwani hata mwenye mali hakumtambua. Hivyo Mahakama ikaamuru Gulamhussein Gondrap Shaha apewe mali yake. Mke wa Baba Ubaya wakati huo alikuwa ni kizuka yupo kwenye eda ya aliekuwa Mumewe wa ndoa. Pia alipotoka nje kwa dhamana kabla ya kesi kuanza kusikilizwa katika Mahakama iliyomuachia huru, aliweza kudai Maiti ya Mumewe Polisi ili akazike. Polisi hawakuwa na pingamizi walitoa kibali cha kuruhusu kumpa maiti ile. Hivyo aliichukuakua maiti ya aliekuwa mumewe, akajumuika na ndugu wa mume na wa kwake pamoja na jamaa wakamzika Mumewe kipenzi Baba Ubaya.
***
Shuwea Namjupa baada yakumaliza kutoa ushahidi Mahakamani, alikwenda nyumbani kwake akafungasha nguo zake pamoja na biashara za urembo alizozinunua. Shuwea katika fedha zake shilingi laki tano, alimpa kaka yake Msafiri ili afanye biashara. Walipokuwa wakifungasha kwa safari Msafiri Namjupa alikuwa amenunua Mabalo ya Mitumba, wakapakia katika gari mizigo yao wakapelekwa Mbagala Rangi Tatu katika kituo cha mabasi yanayokwenda kusini. Walipofika pale wakapakiza mizigo yao kwenye basi la Nachingwea wakasafiri kwenda kwao wakiwa wamedhamiria kufanya biashara. Chumba chao walikifunga ili watapokuja wakati mwingine kufunga mzigo, wawe na sehemu yakufikia. Wana ndugu wale waliamua kwa pamoja makazi yao yakudumu yawe ni sehemu yao walipozaliwa Nachingwea mjini. Kutokana na kadhia zilizowakumba waliamua warudi nyumbani kwani nyumbani ni nyumbani kukiwa kubaya au pazuri. Walikuwa wamejikosha kwa mavazi wakawa wanameremeta, furaha iliingia katika familia yao njaa waliipa mgongo shibe ikachukua nafasi. Ama kweli baada ya dhiki ni faraja.
***
Iddy Teva alifikishwa kwa Kapteni Fabiola akiwa hajiamini kabisa, lakini tafauti ya alivyotarajia alimkuta Kapteni Fabiola amepoa kama maji ya mtungi. Alimkaribisha vizuri akamwambia mbuya awapishe akatumia dakika takribani ishirini kumweleza kumruhusu kumuoa mwanawe baada ya kumaliza masomo. “Mie nimeridhika baada ya mwanangu kuniomba sana kuwa yeye ameshakuwa ni mtu mwenye kuelewa jema na baya, hivyo ili asome vizuri anakuhitaji uwe nae karibu ili umshauri mambo mema. Hivyo ulete barua ya posa mie sina ubishi kwani miezi michache ijayo Mbuya atafanya mitihani yakumaliza masomo yake. Hivyo unaweza kufunga nae ndoa. Kama ikitokea atachaguliwa kwenda chuo kikuu basi itakuwa haina tatizo, kwani chuo wanasoma watu wazima na maisha yao. Kamwe haitakuwa kiroja kwa mwanangu kusoma chuo huku akiwa ameolewa!” Kapteni Fabiola alizungumza sana na Mkwewe na Iddy Teva ukawa ndiyo mwanzo mwema ukawafanya wawe marafiki. Ama kweli wagombanao ndiyo wapatanao.
***
Siku ya hukumu ya kesi iliyokuwa ikiwakabili Nigga na mama yake mdogo pamoja na Swahiba wake Carlos Boga. Umati wa watu ulijaa sana katika Mahakama ya Hakimu mfawidhi Kisutu, hasa baada ya vyombo vya habari ikiwemo TBC kurusha mara kwa mara muendelezo wa kesi ile. Tangu TBC kuonesha lile tukio lililotokea kule Ubungo Kibangu nyuma ya Riverside katika wilaya ya kinondoni mkoa wa Dar es salaam, liliwavuta watu wengi sana kuhudhuria Mahakamani ili kupata muendelezo na khatima ya kesi ile. Waandishi habari walikuwa wamejazana sana katika chumba kile cha Mahakama, wanasheria kadhaa walikuwapo kwa ajili yakwenda kusikiliza kesi za wateja wao. Katika pembe moja ya Mahakama ile alikuwa amekaa Wakili Neema Faraja akiwa hayupo katika mavazi yake ya uwakili, akifatilia kesi ile iliyotarajiwa kutolewa hukumu.
Hakimu aliingia Mahakamani askari aliwainua watu katika lile tamko maarufu Mahakamani. “Coooooooooooooooooooort” Hakimu alipokaa katika kiti chake watu wengine nao waliketi kitako kusikiliza Mahakama ikifanya kazi yake. Kesi ya kwanza kuitwa ilikuwa ni ya kina Nigga na wenzake. Washitakiwa wote walikuwapo mahakamani, wakapanda juu ya kizimba. Wakili wa Serikali alisimama akaifahamisha Mahakama. “Muheshimiwa shauri hili limekuja kwa ajili ya kutolewa maamuzi, hivyo tupo tayari kwa hukumu.” Baada yakusema maneno yale wakili wa Serikali aliketi kitako. Hakimu aliwatizama washitakiwa kama walikuwa na udhuru wowote lakini hakukuwa na mshitakiwa alienyoosha mkono wake juu kuonesha ana tatizo. Hakimu akatambua kuwa washitakiwa nao pia walikuwa tayari kwa hukumu. Hivyo akalifungua jalada lake akaanza kuisoma hukumu iliyochokua saa nzima. Aliusoma mwenendo mzima wa kesi ulivyokuwa, ushahidi na vielelezo vilivyotolewa, utetezi wa washitakiwa na hatimae baada yakupitia pande zote mbili ya Mashitaka na Utetezi mwisho akatoa Maamuzi. “Mshitakiwa Halima Kibakaya,(HUYU ALIKUWA NI MAMA YAKE MDOGO NIGGA) Mahakama yangu imekuona una hatia ya kosa la kula njama la kutenda kosa. Kwani umeshindwa kukanusha mbele ya Mahakama yangu kuwa wewe na Washitakiwa hamfahamiani kabla ya shitaka hili. Hivyo ninakufunga kifungo cha miaka saba jela na kazi ngumu ili iwe fundisho kwa wengine. Mshitakiwa Joseph Kazi, au Nigga mahakama yangu katika kosa la kwanza lakula njama yakutenda kosa. Wewe pamoja na Mshitakiwa namba tatu Carlos Boga wote nimewatia hatiani, hivyo mtatumikia kifungo cha miaka saba jela na kazi ngumu. Katika kifungu cha pili, mahaka yangu imewaona mnahusika na silaha iliyoletwa na upande wa Mashitaka kwani mmeshindwa kujitetea kuwa marehemu aliekuwa pamoja nanyi hakuwa na silaha, hivyo kwa kuwa mmethibitisha kwamba silaha hiyo ni ya mtu alieuwawa na Polisi ambae nyie mlikuwa nae, ushahidi wa kimazingira unawatia hatiani kuwa mlikuwa nayo silaha hiyo kwa nia yakutenda kosa. Kwani Mtu mliedai kuwa na silaha hiyo upande wa utetezi mmeshindwa kuifahamisha Mahakama yangu kama alikuwa akiimiliki kihalali silaha hiyo. Hivyo kwa kosa hilo nawafunga kifungo cha Miaka mitano jela na kazi ngumu. Na katika kosa la tatu la unyang’anyi wa kutumia Silaha, ushahidi umeweza kuthibitisha shitaka pasi na chembe ya shaka kuwa washitakiwa mmetenda kosa hili. Kutokana na maelezo yakukili kosa mshitakiwa yaliyopokelewa kama kielelezo na Mahakama yangu mshitakiwa namba tatu Carlos Boga katika maelezo hayo umekili kwamba wewe ulikuwa ni Dereva mlipokuwa mkitenda kosa lile, Nigga alikuwa ni Chale kwa maana alikuwapo katika tukio. Lakini kwa ushahidi uliowasilishwa na Inspekta Missana john, ambae alikuwa amesimamia gwaride la utambulisho, mshitakiwa Nigga uliweza kutambuliwa kituoni na hata walipokuja hapa mashahidi wale waliweza kukutambua tena. Hivyo hakuna ubishi kuwa washitakiwa pamoja na mwenzenu ambae sasa ni Marehemu mmetenda kosa hili. Hivyo ninawaadhibu kifungo cha miaka thalathini jela na kazi ngumu. Adhabu zote hizo zitaambatana hivyo mtatumikia miaka Thalathini kwa ujumla wake. Ikiwa hamjaridhika na hukumu niliyoitoa mnaweza kukata Rufaa.” Hakimu alimaliza kuisoma hukumu ile iliyokuwa na karatasi sitini.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hukumu ile ilianzisha vilio na kusaga meno kwa wshitakiwa na familia zao, pamoja na ndugu jamaa na watu waliokwenda kusikiliza kesi ile wenye machozi mateke. Kwani Nigga na washitakiwa wenzake walikuwa wamepigwa Tatu bila!
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment