Search This Blog

Saturday 5 November 2022

SAUTI YAKE MASIKIONI MWANGU - 2

 








Simulizi : Sauti Yake Masikioni Mwangu

Sehemu Ya Pili (2)







kuki alifikiria kidogo, akamtazama Maufeng machoni na kuona ni jinsi gani rafiki yake alikuwa na kiu ya kufanya kile wanachokizungumzia. Akarudi kwa upande wake, akashaurina na moyo wake kwa sekunde chache kabla ya kuja na jibu moja thabiti la ‘sawa, tutakwenda.’

*******************************

Kwenda kisiwani Jiaju ulikuwa ni mpango uliopangwa kutimia, hivyo mara bara baada ya Mkuki na Maufeng kuweka akiba ya fedha watakazokwenda kuzitumia kukodia boti walipanga siku ya kutoroka.

Ilikuwa ni Jumanne jioni, walifanya harakati hizo bila kugundulika na mtu yeyote. Walipanda boti ndogo iliyokuwa ikielekea huko Jiaju na walifika kesho yake asubuhi.

Fujo za soko la samaki kisiwani Jiaju liliwapa picha halisi ya jinsi eneo hilo linavyohitajii watu wachangamfu. Kila waliyemuona alikuwa ‘bize’ na mambo yake. Watu walipita huku na huko, mgongano ulikuwa ni mkubwa sana hata Mkuki alijikuta akifananisha eneo hilo na Kariakoo Mtaa wa Kongo .

Walichukua chumba katika nyumba moja ya kulala wageni kisiwani hapo ambayo ilikuwa ikihudumiwa na mwanamke mnene kweli kweli aitwaye Faye—na sasa wakaanza maisha mapya yenye matuamini makubwa ya kufanikiwa na kurejea nyumbani na pesa mzomzo; pesa nyingi kweli kweli.

Mpango wao nambari moja ilikuwa ni kutafuta mtumbwi wa kukodi ambao wangeutumia kwa kufanyia kazi kwa kipindi cha siku thelathini na kurejea nyumbani, waliamini kwa muda huo watakuwa wamehifadhi pesa nyingi kwa ajili ya kufanyia mambo mengine mbali na uvuvi pindi watakaporejea kijijini Chensua.

Ili kupata boti ya kukodi walihitaji dalali wa kuwasaidia kutafuta, na ili kumpata dalali walihitaji mtu wa kuwaunganisha kwa mmoja ambaye atawatafutia boti nzuri kwa ajili ya kazi, na ili kufanikisha hilo ilibidi wajenge ukaribu na Faye—yule mwanamke bonge muhudumu wa ‘gesti’ waliyofikia.

Ilikuwa rahisi zaidi kwa wao kuwa karibu na Faye kupitia Maufeng kwa sababu kwa pale kisiwani Mkuki alikuwa akionekana ni kama kitu cha ajabu na hilo lilijitokeza tangu siku ya kwanza walipowasili. Wathaiwan wengi hakuwahi kupata kumuona binadamu mwenye ngozi yenye rangi kama Mkuki, yeye alikuwa ni mtu mweusi wa kwanza kufika kisiwani Jiaju na wa kwanza kukumbana na ubaguzi wa rangi kisiwani hapo.

Basi Maufeng akaanzisha ukaribu na dada huyo. Alimfuata pale mapokezi, akamsalimu.

“Umechokaa kukaa ndani?” Aliuliza Faye baada ya salamu.

“Hapana. Ila nimependa kuja kukaa na wewe malaika.” Akasema Maufeng, hapa akijtahidi kutumia maneno mazuri ya kumvutia Faye.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Faye akacheka kabla ya kujibu. “Kumbe ni muongeaji.”

“Kwanini?”

“Basi tu. Sura yako inaonesha ni mkimya.” Akasema na kuongeza. “Utakaa hapa mpaka lini?”

“Bado sijajua. Wewe unapenda niondoke lini?”

Akacheka kidogo Faye na kujibu. “Usiondoke”

“Basi nitafanya hivyo.” Akasema Maufeng.

“Kwani umekuja kwa ajili gani? Kununua samaki?”

“Nimekuja kuvua. Lakini bado kuna mambo yananikwamisha.” Akajibu Maufeng lakini kabla hajaendelea akaingia mteja ndani, Faye akainuka na kwenda kumuhudumia kisha akarudi kuendelea na maongezi na Maufeng.

“Enhee. Umesema kuna mambo yanakukwamisha? Mambo gani?”

“Nataka mtumbwi wa kukodi.”

“Mbona iko mingi sana hapa, tena ya gharama tofauti. Naweza nikakuonganisha na dalali.” Akasema Faye bila kujua kwamba alikuwa akielekea kwenye hitaji lilimsogeza Maufeng karibu yake.

“Nitafurahi sana.”

“Basi usijali. Jioni nitakukutanisha naye.” Akasame Faye na mazungumzo mengine yakashika hatamu huku akipewa ofa ya kinywaji na Maufeng.

Jioni; mkuki na Maufeng walikuwa ndani, mlango wa chumba chao ulibishwa hodi, Maufeng akainuka kwenda kufungua. Alikuwa ni Faye, alikuja kwa lengo la kumuita Maufeng ili akutane na dalali wa mitumbwi.

“Sawa, tunakuja.”

“Mnakuja!? Wewe na nani? Na yule mwenzako mweusi.” Faye akahoji lakini kwa sauti ya kunong’ona ili Mkuki asisikie.

“Ndiyo. Kuna tatizo?”

“Hapana lakini.... Au sawa, njoo naye.” Akasema Faye kisha akarejea mapokezi ambapo dalali alikuwepo.

Maufeng akamchukua Mkuki na wakaongozana hadi mapokezi, hawakumuona mtu yeyote eneo hilo zaidi ya Faye mwenyewe.

“Yuko wapi?” Akauliza Maufeng.

“Yule pale,” Faye akaelekeza huku akimnyoshea kidole mwanaume mmoja aliyeketi kwenye viti vya baa ndogo iliyopo kwenye gesti hiyo. “Twendeni.” akaongeza kisha akazunguka kutoka mapokezi na kuongoza njia kuelekea alipokuwa ameketi mwanaume yule.

Wakamfikia.

“Taro?” Faye akamuita kwa jina mwanaume huyo. Taro akainua kichwa kuwatamaza.

Alikuwa ni mwaname wa mwenye asili ya Kijapani, mkubwa kiumri kwa  miaka kumi au zaidi ukimlinganisha na kina Mkuki. Mwanamume mnene kiasi, mwenye nywele nyingi nyeusi za kulazwa kwa nyuma na macho ya kuvimba ya Kijapani.

Alimtazama sana Mkuki kama mtu anayeshangaa muujiza fulani.

“Nini hiki?” Akauliza Taro.

“Ndo watu niliokwambia wanataka boti ya kukodi.” Akajibu Faye.

“Huyu na huyu?” Akahoji Taro.

“Ndiyo. Kwani vipi?” Akadakia Maufeng, aliamua kufanya  hivyo  kwa sababu aliona chembechembe za kibaguzi kwenye maswali ya Taro.

“Kwani vipi? Nashangaa. Sijawahi kuona mtu mwenye upendo kama wewe. Mtu anayefuga nyani na anamtanbulisha nyani wake kama mshirika mwenzake.” Akadhihaki Taro kisha akatoa cheko kubwa la kishenzi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Sawa. Naona ni vyema tungeendelea kuzungumzia sababu ya kuwa hapa.” Akasema Maufeng, wakati huo Mkuki akijitahidi kujituliza, kujizuia asikwazike na kejeli za aina ile.

Taro akaendelea kucheka. “Hatuwezi kuendelea. Inabidi kwanza unionyeshe kibali cha kumiliki mnyama pori, na kibali cha daktari kuthibitisha kwamba nyani wako hawezi kutusababishia madhara ya kiafya sisi binadamu.” Akasema lakini kabla hata hajamaliza Mkuki alimrukia, akamkwida, akamnyanyua kutoka kwenye kiti alichokuwa ameketi na kumpiga kichwa matata kwenye midomo hata akachanika, akatokwa damu.

Maufeng na Faye wakawa waamuzi, wakawatenganisha ili Mkuki asiendele kimuadhibu Taro.

“Nitakuua. Nitakuua.” Akasema kwa sauti ya juu Mkuki huku akiwa ni mwenye ghadhabu kwelikweli. Kwa bahati mbaya sauti ilitua kwenye masikio ya askari polisi watatu waliokuwa wakikatiza eneo hilo wakiongozwa na kamanda Su Lee—askari wa kike ambaye ni mmoja wa maaskari polisi viongozi wa kituo cha pekee cha polisi kilichopo kisiwani hapo.

Maaskari wakawasogelea na kitu cha kwanza kukiona ilikuwa ni Mkuki, na aliwashangaza kiasi kwamba badala ya Su Lee kuhoji kuhusu kilichowapelekea pale alianza kuuliza kuhusu Mkuki.

“Nini hiki?” Akahoji Afande Su Lee huku akinyoosha kifimbo chake cha kiaskari kumuelekea Mkuki.

“Ni mshenzi afande. Anataka kuniua. Amenijeruhi hapa.” Akasema Taro huku akionesha jeraha lake mdomi.

Afande Su Lee akamsogelea Mkuki—alikuwa ni mwanamke wa shoka, mwanamke asiyefanana na wanawake wengi. Alikuwa na mwili wa mazoezi kama mwanaume, mrefu tofauti na walivyo Wathaiwan wengi. Sura yake pia ilikuwa ni  ya ugwadu kweli kweli, ni kama mtu anayekunywa chai moto kwenye kikombe cha plastiki; kwa kifupi Afande Su  Lee hakuwa na haiba ya kike kabisa.

“Wewe ni nani?” Akahoji Afande huku akimuinamia Mkuki.

“Afande ulikuwa ni ugomvi wa kawaida tu, ugomvi wa kibiashara. Mimi na mwenzangu hapa tunataka kukodi boti kwa.....” akadakia Maufeng lakini Su Lee alimkatisha kabla hajamaliza.

“Kelele.”

Maufeng akapiga kimya, Su Lee akamgeukia Mkuki.

“Ni mgeni hapa? Mimi naitwa Inspekta Su Lee, na nina taarifa nyingi kuhusu nyani kama wewe. Leo nakupa nafasi ya upendeleo, lakini tukikutana siku nyingine katika tukio la namna sitakuacha.” Akasema, kisha bila kupoteza muda akachukua watu wake, wakaondoka na hiyo ilikuwa ni kama ‘zali la mentali’ kwa sababu hakuna mtu aliyewahi kuingia kwenye anga za Inspekta Su Lee  na akapona kirahisi namna ile—huenda lile lilitokea kwa sababu za msingi ambazo alizifahamu Inspekta mwenyewe.

Baada ya Inspekta Su Lee kutokomea na watu wake mazungumzo kuhusu  boti ya kukodi yakaendelea.

“Vipi? Tunapata boti au mpaka jeraha lipone?” Akauliza kwa kejeli Maufeng.

“Mnataka boti gani?” Akaukiza Taro na Maufeng akataja aina ya boti wanayoitaka.

“Kwa siku ngapi?” Akauliza.

“Siku thelathini.” Akajibu Maufeng.

“Zipo,” akasema Taro na kutaja bei ambayo ilikuwa ni sawa na kiasi ambacho kina Mkuki walikuaa nacho.

******************************

Kazi ilianza mara moja baada ya kupata boti, waliingia baharinii kila usiku na asubuhi walirudi na lundo la samaki kama ilivyo kwa wavuvi wengine. Waliuza samaki wote waliokuwa wakipata na pesa waalitumia kiasi kidogo na kilichobaki walihifadhi kwa ajili ya mpango wao.

Hata hivyo mfumo wa maisha pale kisiwani haukuwa rahisi kwa Mkuki, aliandamwa na ubaguzi wa daraja la juu sana ingawa mwenyewe aljitahidi kuwa mvunilivu. Alifanikiwa katika hiko kutokana na roho ya kutafuta akiyokuwa nayo. Alijua anachotafuta, alifahamu hitaji lake kwahiyo hakuwa na sababu ya kuziruhusu hisia za kibaguzi za watu wengine zimkwamishe.

Upande wa Maufeng mambo yalikuwa ni burudani, maisha ya pale kisiwani yalikuwa  murua sana kwake kiasi kwamba hadi alipata mpenzi. Alianzisha uhusiano na mrembo ‘kibonge’ Faye ingawa uhusiano wao  haukuwa na dalili ya kwamba ungefika mbali.

Sio tu uhusiano, pia Maufeng alitengeneza marafiki wengi wapya lakni ubaya ni kwamba hawakuwa marafiki wema, wengi walikuwa ni wavuvi wapenda pombe na uasherati mwingine uliojaa kisiwani pale na hii ilipelekea hata Maufeng naye akafunzwa ujinga huo; yaani nguvu ya marafiki hao ikamchukua kabisa Maufeng na sasa hata yeye akaanza kujaribu kutumia vileo na tamati akaja kuwa ni mlevi mbwa kiasi kwamba hata akawa kero kwa watu waliomfundisha.

Sasa pombe ikawa ni sehemu ya maisha yake, ikamuendesha barabara hata akafikia hatua ya kuomba kuwa kila wanapopata pesa yeye na Mkuki wagawane ‘pasu kwa pasu’, kila mmoja afe na chake jambo ambalo Mkuki alikataa katakata.

************************************







“Hapana. Utachukua pesa kidogo kwa ajili ya hizo pombe zako. Mpango wetu wa kuweka pesa uko pale pale.” Alieleza Mkuki kupinga suala la kugawana pesa, alijua kuwa baadae  lingemsababishia matatizo, angeonekana kamnyonya au kumdhulumu mshirika wake.



Hata hivyo tabia ya ulevi ilimzidi nguvu Maufeng kiasi kwamba sasa akawa hata kula hataki. Akafunga ndoa rasmi na pombe, yeye akawa pombe na pombe ikawa yeye.

Mkuki alijitahidi sana kumuonya, kumrudisha kwenye reli lakini hakufanikiwa—tayari walishakuwa sio watu wa kufanana tena, ulevi ulififsha urafiki wao kwa kiasi kikubwa mno.

********************************

Ni mwanaume gani pale kisiwani angethubutu kuwa na mwanamke wa aina ya Su Lee, mwanamke mwenye kila åkigezo cha kuitwa jike dume, kuanzia umbile, sura na hata tabia. Hivyo ndivyo ambavyo Su Lee alikosa wanaume. Mbali na kukosa wanaume alikuwa na siri kubwa moyoni, siri aliyoitengeneza mwenyewe kutokana na fikra ambazo zilizaliwa kupitia mitazamo ya watu mbalimbali aliyowahi kuisikia na kuifuatilia.

Aliwahi kuishi katika mapenzi, lakini kwa kipindi chote hicho hakuwahi kupata mwanaume aliyewahi kumridhisha katika tendo na hii ni kwa mujibu na nafsi yake mwenyewe.

Kwanini alikuwa haridhiki? Su Lee yeye alijijengea imani kwamba ili ufurahie tendo ni lazima ukutane na mwanaume mwenye uume mkubwa; ubaya katika hili ni kwamba, wanaume wengi wa Thaiwan walikuwa na maumbile madogo yenye kuwatosha watu wasio na mtazamo kama wake. Na hii ndiyo sababu hakutaka hata kumkamata Mkuki siku ile kwa kuwa  moja ya taarifa alizowahi kusikia kuhusu watu weusi ni kwamba wana madubwasha makubwa ndani ya suruali zao, hivyo aliamini siku moja Mkuki atamsaidia kukata kiu aliyonayo.

Basi mpango nambari moja wa Su Lee ulikuwa ni kumtafuta Mkuki na kumueleza ukweli ingawa hilo halikuwa jambo jepesi kwa kuwa alitaka lifanyike kwa siri. Akapanga mkakati, akajiahidi kwamba atamtafuta yule rafiki yake kwanza, yaani Maufeng, kisha kupitia huyo atajenga ukaribu na Mkuki na tangu hapo itakuwa rahisi kutimiziwa hitaji lake.

Usiku mmoja alitoka kwenda kwenye gesti wanamoishi kina Mkuki, hiyo ilikuwa ni sehemu ya kutimiza mpango wake. Alikuwa amevalia kiraia, sketi ndefu na blauzi. Alikwenda moja kwa moja hadi kaunta ambapo alimuulizia Maufeng.

“Hayupo afande. Amefanya kosa gani?” Alijibu na kuuliza Faye.

“Hakuna tatizo. Nilikuwa na shida na mmoja kati yao.”

“Hata yule mwenzake? Yule mweusi”

“Ndiyo.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Yule yupo ndani. Nimuite.”

“Sawa.”

“Nimwambiaje?”

“Kawaida tu. Mwambie namuhitaji.” Akaelekeza Inspekta Su Lee.

Basi Faye akazunguka na kutoka pale kaunta, akaelekea kwenye kordo ya vyumba na ndani ya sekunde sitini alirudi akiongozana na Mkuki.

“Habari yako?” ikamtoka sabahi Inspekta Su Lee huku akimpa mkono Mkuki na kutabasamu pia. Kile kilichokuwa kikiendelea ilikuwa ni kama ndoto kwa Faye ambaye alikuwa akimfahamu uzuri Inspekta, tangu amjue hakuwahi kumuona akitabasamu hata siku moja, ile ilikuwa ni kama uchuro.

Mkuki akampa mkono pia, wakashikana.

“Salama.” Akaitikia ile salamu na kuongeza. “Nimeambiwa unanitafuta?”

“Ndiyo. Ninashida na nyinyi, mwenzako yuko wapi?”

“Ametoka.”

“Basi hata wewe peke yako unaweza kunisaidia. Tunaweza kuondoka pamoja?” Akauilza Afande Su Lee.

Mkuki alifikiria kidogo. “Sasa hivi?” akauliza.

“Ndiyo.” Inspekta akajibu, basi Mkuki akakubali, kisha akaingia ndani kwenda kubadilisha nguo kwa sababu alikuwa amevalia isivyotakikana, na punde alikuja akiwa ndani ya fulana, suruali nyeusi na viatu vya wazi vya kufanana na malapa.

Baada ya pale wakaondoka pamoja, Inspekta Su Lee na Mkuki. Inpsekta alimuongoza Mkuki hadi ufukweni, eneo ambalo likikuwa tulivu sana  na sahihi kwa mazungumzo mazito ya namna ile. Wakiwa huko, alimueleza kila kitu tena kwa kujiamini, aliweka bayana shida yake na jinsi ambavyo angependa Mkuki amsaidie; alihitaji mtu wa kumkuna.

Sasa ukawa ni wasaa wa Mkuki kutoa majibu, ilikuwa ni nyakati ngumu kweli kweli. Yeye kama mwanaume alitakiwa atoe kauli moja thabiti ambayo ama ni ya kukataa au kukubali. Nafsini hakuwa na hitaji na Inspekta Su Lee, hii ni sawa  na kusema kwamba hata kama atakubali kuwa msaada kwa Inspekta itakuwa ni kwa sababu za nje ya upendo, si kwamba atakuwa amefanya hilo kwa matakwa yake.

Lakini hata hivyo Mkuki alikuwa na sifa moja kubwa, sifa ya kujiamini.  Yeye hakuwa mwoga-mwoga, alikuwa ni mtu mwenye msimamo hasa linapokuja suala zima la kusimamia mtazamo wake; yaani anapodhani kwamba jibu la jambo fulani ni hapana basi husimama katika hapana yake na kuiwekea msingi wa hoja ngumu na imara.

“Nimekuelewa Inspketa, lakini bahati mbaya mimi nimeoa. Ni mume wa mtu.” Alieleza Mkuki baada ya kufikiria kwa muda kidogo.

“Sio tatizo…..” alieleza Inspekta Su Lee. Alimbembeleza sana Mkuki lakini mwanamume aliendelea kusimama imara palepale kwenye ‘hapana’ yake bila kutetereka, bila kutetemeka na tamati ya mazungumzo ilikuwa ni kuondoka ilihali Inspekta akiwa ameshindwa kufanikiwa kutimiza azimio lake.

***************************

Mvutano mkubwa uliibuka kati Mkuki na Maufeng. Siku za kurejea nyumbani zilikuwa zimetimia, walitakiwa kesho ya siku hiyo waondoke lakini sasa Maufeng alikuja na wazo jipya lililokwenda kinyume na makubaliano yao. Yeye alitaka wagawane nusu kwa nusu ya pesa walizohifadhi kwa kipindi chote, kisha Mkuki aondoke mwenyewe na kumuacha Maufeng palepale kisiwani Jiaju.

”Haiwezekani Maufeng. Siwezi kukupa nusu ya pesa na nikakuacha hapa. Turudi nyumbani tukagawane huko kisha utarudi huku kama umepapenda.” Alipinga Mkuki.

Mvutano ulishika kasi kweli kweli, kelele za nataka ‘pesa zangu’ kutoka kwa Maufeng zilipaa hadi nje ya chumba kiasi kwamba ziliwakera hata wateja wengine.  Mkuki aliendelea kusimamia maamuzi yake hata mwishowe Maufeng akanyoosha mikono juu, akakubali; akaomba kiasi kidogo cha pesa kwa ajili ya kwenda baa usiku huo ili kesho asubuhi waondoke kurejea kijijini Chensua.

Basi alikwenda kuongezea ulevi kwenye baa moja ambayo si watu wengi walikuwa wakiipenda; ilikuwa karibu na ufukwe, eneo ambalo lilikuwa kimya sana ukilinganisha na maeneo mengine ya kisiwani hapo. Akafika na kuagiza ‘ulabu’, akaketi kwenye meza na kuanza taratibu kupata kinywaji.

Punde wakaingia wanaume watatu na wanawake wawili, wakaketi kwenye meza ya karibu na pale alipokuwa Maufeng, wakaagiza na kundelea kunywa huku wakipiga soga na kucheka kwa furaha, walionekana kuwa ni marafiki wa karibu sana na wale wanawake walikuwa ni wapenzi wao.

Baada ya chupa mbili za bia iliyochanganywa na pombe kali Maufeng alinyanyuka ghafla, akajinyoosha huku akipiga kelele kubwa kana  kwamba aliyepandwa na mashetani.  Punde akanyamaza, akaanza kucheza taratibu huku akiwasogelea wale watu watano waliongia pale baa  na kuketi karibu yake.

Akawafikia.

“Mbona mko na wanawake wazuri?” Akauliza Maufeng. Wale watu wakamtazama bila kumjibu, walimdharau ya kwamba alikuwa ni mlevi ambaye tayari pombe ilishamtawala kichwani mwake; lakini kumbe haikuwa hivyo; kilichomnyanyua Maufeng na kumsogeza pale hazikuwa pombe, bali ni lile tatizo lake la akili ambalo humtokea mara chache.

“Nawauliza mbona mnakuja na wanawake wazuri na wote mnakaa nao peke yenu?”

“Vipi kwani. Hebu jichunge, starehe yako isiwe kero kwetu.”

“Unasemaje. Nakukera? Sasa naondoka naye huyu.” Akasema Maufeng huku akimshika mkono mwanamke mmoja kati ya wale wawili na kuanza kumvuta.

Kitendo bila kuchelewa wale wanaume watatu wote wakasimama, mmoja akauachanisha mkono wa Maufeng na wa yule mwanamke kisha akamsukumia huko, Maufeng akaanguka chini kama kiroba cha viazi mbatata kilichoachiwa na mchuuzi.

Akasimama, akaanza kuwafuata tena, hapa akiwa amekunja ngumi kwa lengo moja tu, kupambana nao. Uwendazimu wake wa msimu ulikuwa ukimuendesha mno, na laiti kama wale watu wangefahamu tatizo lake wangeondoka na kumuacha.

Basi mmoja kati yale wanaume akata kumfundisha adabu, naye akakunja ngumi na kukaa mkao wa tayari kupigana.

Ghafla Maufeng akarusha teke huku akipepesuka kwa ulevi, jamaa akainama kukwepa, akajizungusha mara mbili na kutokea upande kushoto mwa Maufeng, akampiga ngumi konzi eneo la mbavuni, kisha akamchapa na ubapa wa kiganja cha mkono chini kidogo ya kichogo—hayo yalikiwa ni mapigo ya Kong-fu.

Basi Maufeng akapepesuka na kwenda kuangukia juu ya meza ya wale majamaa hata chupa zenye vinywaji zikapasuka na kumjeruhi.

Yule mwanaume akajiweka sawa akimsubiria aamke ili aendelee kumshushia kasheshe lakini ajabu ni kwamba zilipita sekunde kadhaa bila dalili yoyote ya Mauufeng kuamka.

“Vipi?” Wakaulizana wenyewe kwa wenyewe.

“Hebu muangalie.” Mwingine akashauri.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Basi mmoja akamsogelea na kumgeuza na papo hapo ndipo aligundua kuwa Maufeng amezimika. Akataka kujua kuwa alikuwa amepoteza fahamu au amekata roho kabisa, akamuwekea mkono shingoni kujua mwenendo wa mwili wake. Akagundua kitu, akawageukia wenzake kuwatazama. “Hamna kitu.” Akawapasha habari kisha akasimama haraka haraka. “Tuondokeni.” Akawaambia kisha kwa pamoja walitoka baa hapo mbio mbio na kuacha mwili wa Maufeng pale juu ya meza.

***************************





Asubuhi ya safari Mkuki aliamka, hakumuona Maufeng kurejea nyumbani lakini hakutaka hilo likwamishe safari yake. Alipanga kwamba atachukua pesa zote na kurejea nyumbani, lakini ataacha ujumbe na pesa kidogo kwa Faye ili kwamba mwenzake atakaporejea ajue kinachoendelea pamoja na kupata nauli ya kumuwezesha kurejea kijijini Chensua.

Basi baada ya kujiandaa akatia pesa zote katika begi lake la mgongoni, kisha juu ya pesa akaweka nguo chache alizokuwa nazo, Akafunga begi, akasimama na kuanza kuondoka.

Kabla hata hajafika mlangoni kuna mtu alibisha hodi. Mkuki akafungua huku akiomba Mungu mtu huyo awe ni Maufeng ili waondoke pamoja. Lakini mambo yalikwenda kinyume, badala ya kumuona rafiki yake macho yake yalikutana na sura ngumu ya Inspekta Su Lee pamoja na askari wengine watatu wa kiume.

“Inspekta!? Karibu.” Akasema Mkuki huku akitabasamu.

“Unaenda wapi?” Akauliza Inspekta huku akijitahidi kuifanya ile sura yake ya ugwadu kuwa chachu zaidi.

Akajiumauma kabla ya kujibu Mkuki. “Nyumbani.”

“Peke yako?” Akauliza Su Lee.

“Aaah! Hapa... Ndiyo.”

“Ni ndiyo au hapana?”

“Ndiyo. Naondoka peke yangu.”

“Mwenzako?”

“Atakuja yeye peke yake pia.”

“Yuko wapi? Kwanini aje peke yake.”

“Aliondoka jana usiku lakini....” hakumaliza Mkuki. Inspekta Su Lee akatoa agizo la kukamatwa kwa Mkuki mara moja.

“Tazama na begi lake kuthibitisha alichokisema Faye.” Akasema Inspekta Su Lee kuwambia askari wake, Mkuki alichanganyikiwa, hakuwelewa kilichokuwa kinaendelea.

Iko hivi; baada ya Maufeng kuuawa kule baa, wamiliki walitaka kukwepa dhahama kwa sababu hawakuwa wakiwafahamu wale wauaji, hivyo ili kufanikisha hilo waliuchukua mwili wa Maufeng na kwenda kuutupa ufukweni ambapo ulionekana asubuhi na watu wakatoa taarifa polisi.

Baada ya Inspekta Su Lee na watu wake kufuatilia walikwenda kwenye 'gesti' alipokuwa akiishi Maufeng, na walizungumza na Faye kwanza kama muhudumu ambaye pia alikuwa ni mpenzi wa Maufeng.  Walimueleza hali halisi kwamba Maufeng ameuawa, na wanamfikiria Mkuki kama mshukiwa nambari moja wa tukio hilo.

Hapo Faye alitiririka akiwathibitishia kwamba ni lazima Mkuki alihusika katika tukio lile.

“Jana usiku walikuwa wanagombania pesa. Itakuwa amemuua ili aondoke na pesa zote peke yake.” Faye aliwaeleza polisi namna hiyo, hapa akisimulia ugomvi uliotokea usiku wa jana kabla ya Maufeng hajachukua pesa kidogo na kwenda baa ambapo umauti ulimkuta.

Basi afande mmoja akachukua begi la Mkuki, akafungua na kuanza kutoa nguo moja baada nyingine na mwishoni, baada ya kutoa nguo  zote alikumbana na maburungutu ya pesa.

“Ni kweli. Kuna pesa.” Akataarifu askari huyo na hiyo ilitosha kuwa sababu kamili ya kuondoka na Mkuki kwa tuhuma za kwamba alimuu Maufeng ili atoroke na pesa zote.

Tayari kila kitu kilianza kuingia giza tangu hapo, ni wazi kwamba kwa jinsi hali ilivyokuwa ilikuwa ni ngumu sana kwa yeye kuchomoka katika hatari ile—ushahidi wa kimazingira ulimbana; lakini pia uhasama alioutengeneza dhidi ya Inspekta Su Lee, ile ya kumkatalia kuwa mwandani wake ilikuwa ni miongoni mwa mambo ambayo pengine yatamfanya akose kabisa msaada.

*****************************

Mlango wa selo ulifunguliwa, akaingia askari mmoja aliyekonda kweli kweli, mwenye sura nyembamba yenye kuchekesha kuitazama, yenye masharubu ya dharau yaliyokaa kama kuti la mnazi juu ya mdomo wake.

Alikuwa amemfuata Mkuki, akamchukua, na kumpeleka kwenye chumba cha mahojiano. Akamkalisha kwenye kiti, kisha askari akatoka nje na punde akaingia Inspekta Su Lee na kikombe kidogo cha udongo chenye kahawa.

Akaketi kwenye kiti kingine cha mbele ya pale alipiokuwa Mkuki, wakawa wanatazamana uso kwa uso.

Inspekta akapiga funda moja la kahawa moto, kisha akakiweka kikombe juu ya meza iliyokuwa katikati yao, akamtazama usoni Mkuki kisha yakamtoka maneno; “Giza sio zuri, lakini ni sehemu nzuri ya kuziona nyota.” Akasema Inspekta.

Akaendelea.

“Upo gizani, sio kwa sababu uteketee, bali ili uweze kuziona nyota, kuzijua, na kujiweka karibu nazo. Nahisi nimekujua vizuri kwa muda mfupi nilopata kukaa pamoja nawe, najua huwezi kumuua Maufeng, huwezi kumuua mtu yotote. Huna roho hiyo.”

Akanywa kahawa Inspekta na kuendelea.

“Lakini ni nani atakayekuwa tayari kukuamini? Na hata kama yupo, Je, atakuwa na nguvu ya kuiaminisha dunia kuwa hujamuua rafiki yako? Kama hakuna anayeweza basi hakuna cha kukuondoa gizani, lazima upotelee humu isipokuwa kama utaamua kubadilika, kama utaamua kubadilisha mawazo yako, kama utaacha kufikiria kutafuta njia ya kutoka gizani, badala yake ukaamua kuzitazama nyota na kujiweka karibu nazo.”

“Mimi ni nyota Mkuki, na unanihitaji utake usitake.” Akasema Inspekta kisha akasimama, akaendelea kuzungumza. “Sikia, kesho asubuhi tutakupeleka mahakamani, ni nje ya hapa kisiwani. Na kama utapandishwa kizimbani basi habari zako zote zitaishia hapo, utapotelea gerezani. Mtu pekee mwenye uwezo wa kukuokoa ni mimi, lakini ili nikusaidie inabidi ukubali na uhaidi kunipa kile nikichokuomba.”

Akamuinamia.

“Nadhani tumeelewana. Nakurudisha ndani, jioni nitakuja kwa ajili ya kusikikiza maamuzi yako ya mwisho. Kuishi gizani au karibu na Nyota.” Akasema Inspekta Su Lee na mazungumzo yakaishia hapo, akaondoka wakati Mkuki alichukuliwa kurejeshwa selo.

Aliingia selo akiwa na mawazo maradufu ya ilivyokuwa awali. Mwanzo, kabla hajazungumza na Inspekta Su Lee alikuwa akifikiria jinsi gani  atajikwamua katika dhahama hilo, lakini sasa alikuwa akifikiria jinsi atakavyokwakumuka na kwenda kuanza sekeseke jipya la kumuhudumia kingono Inspekta Su Lee.

Alikuwa katikati ya mtihani mzito lakini mwepesi, kwa sababu kwa upande wake kama mwanaume, suala la kuwa mtumwa wa ngono wa mwanamke halikuwa ni tatizo kubwa sana ukilinganisha na lile la kwenda kuozea jela.

Alitumia muda mwingi sana kujiuliza maswali lukuki ya msingi kwa ajili ya kuhakikisha anapata jawabu sahihi juu ya ule mtihani mzito anaoukabili. Nafsi yake ilimshauri kuwa asikubali kuozea jela wakati akili nayo ilimkumbusha kuwa hatopoteza chochote kuwa uraini hata kama atakuwa akitumikishwa na Su Lee. Maswali ya aina hii yalimsaidia kupata jibu moja lililosahihi kwa upande wake, kwamba atakubali kutimiza hitaji la Inspketa Su Lee ili tu aendelee kuwa uraini wakati akiendelea kupanga mipango mingine hata ya kutoroka kurejea kijijini Chensua kwa mzee Wong na Mei Lee.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Jioni Inspekta alikuja kama alivyoahidi, akaomba aletewe mtu wake kwa ajili ya mazungumzo. Mkuki alipokuja wala hawakuzungushana, mtoto wa kiume alitoa kauli iliyothabiti ya kwamba yuko tayari kufanya kama ambavyo Inspekta aliomba ilimardi tu asitupwe gerezani.

*******************************

Asubuhi watuhumiwa wengine walichukuliwa kwa ajili ya kupelekwa mjini, mahakani lakini si mkuki. Inspekta alifanya awezavyo na akaondoka naye nyumbani kwake anapoishi.

“Karibu.” Alimkaribisha ndani mara baada ya kufungua mlango. Mkuki akapita na kuketi kwenye kochi sebuleni.

Ilikuwa ni nyumba ya chumba na sebule ndogo; basi Inspekta Su Lee akaingia chumbani na alipotoka alikuwa amevalia kigauni kifupi na chepesi cha kulalia, lakini niamini mimi kwamba bado hakuwa akivutia hata kama aliacha wazi sehemu kubwa ya mwili wake.

“Naenda kuoga. Nakuja.” Akasema, kisha akatoka nje kuelekea bafuni.

Kuachwa peke yake kulisisimua lile wazo la kutoroka ambalo Mkuki alikuwa nalo tangu alipofanya maamuzi ya kukubali ombi la Inspekta. Palepale akapiga hesabu matata za kufanikisha zoezi hilo, lakini jambo lililomkwamisha ni wapi ambapo atakimbilia ikiwa kisiwa cha Jiaju kilikuwa ni kidogo sana na Inspekta Su Lee alikuwa na mkono mrefu wa kipolisi, kwamba kama ataamua kumtafuta haitokwisha hata siku moja atakuwa ameshamtia mikononi.

“Nenda tu. Hayo mengine yatajulikana mbele kwa mbele.” Nafsi yake ilimpa ushauri wa kijasiri namna hiyo. Akaupokea, akasimama, akanyata taratibu na kutoka nje, Akatazama hali ilivyo na alipoona kuna utulivu wa kutosha alitimua mbio barabara bila kutazama nyuma.

Alishika njia ya kuelekea lilipo soko, na ni kama alikuwa akiongozana na malaika wa mafanikio, alifika sokoni bila hata kuwa akifuatiliwa nyuma na Su Lee. Alijibanza sehemu moja pale sokoni, karibu na eneo ambalo boti nyingi kutoka China na sehemu nyinginezo zilikuwa zikipakia samaki. Aliona jinsi shughuli ilivyokuwa ikiendelea, aliona jinsi watu wanavyoingia na kutoka kwenye boti hizo wakipakia maboksi ya palastiki yaliyojaa samaki.

Haraka akapata wazo, akaona ili kumkimbia Su Lee, ni vyema akaingia kwenye moja ya boti hizo, na akaondoka nazo zinapoelekea, kisha akiwa huko akatafuta  njia ya kurejea kijijini Chensua kwa mzee Wong na Mei Lee.

JE MKUKI ATAFANIKIWA KATIKA MPANGO WAKE.

*****************************





Alifanya kama alivyofikiria; alinyata taratibu hadi kwenye boti moja wapo ya zile zinazopakia maboksi ya samaki, akaingia huku akiamini hakuna mtu yeyote yule aliyemuona, na huko akatafuta mahala pazuri pa kujificha na palipotulia zaidi.

Akiwa bado ndani ya boti ametulia, alimuona Inspekta Su Lee na kundi la maaskari takriban watano wakiingia pale sokoni. Akajibanza zaidi huku akichungulia na kuona jinsi waliyokuwa wakimtafuta kwa kumuulizia kwa watu huku wakiangaza huku na huko. Hapa sasa ndipo Mkuki alijikuta akigeuka kuwa mtumishi mzuri wa Mungu, alisali sala zote, aliomba na dua za kila namna ilimradi tu asiingie mikononi mwa Inspekta Su Lee kwa mara nyingine.

Lakini huenda Mungu aliyemuomba hakutaka Mkuki afanikiwe, kwani akiwa pale alimuona Inspekta Su Lee akizungumza na jamaa mmoja, bila shaka alikuwa akimuuliza kama amemuona Mkuki maeneo hayo na jamaa akaonekana akieleeza kwa mikono kuelekewa kule kule kwenye boti aliyokuwemo Mkuki.

Basi Inspekta Su Lee akaachana mtu huyo, kisha taratibu akaanza kuelekea kule kwenye boti. Moyo wa Mkuki ulidunda mara nane zaidi ya kawaida, ni kama ulifungwa turbo kwa ndani. Alihisi joto kali mtoto wa kiume, jasho jembamba lilimiminika hata akawa kama chupa ya bia iliyochomolewa katika friji yenye ubaridi wa kiasi cha kugandisha, alihisi haja pia, tena zote mbili, kubwa na ndogo, na hii kubwa ilikuwa ni ya uharo tu. Alijua kama endapo Inspekta Su Lee atamdaka kwa mara nyingine, kamwe hatopata muawana kutoka kwa mtu yeyote yule; atahukumiwa kwa kosa la mauaji, kosa la kuwatoroka polisi na makosa mengineyo ambayo Inspekta huyo ataamua kumpa.

Inspekta akakaribia kwenye boti, hapa sasa Mkuki akamsikia akizungumza na kiongozi aliyekuwa akisimamia upakiaji wa maboksi ya samaki katika boti hiyo, akamsikia akisema kwamba kuna mtu wanamtafuta, na ameonekana ameingia kwenye boti hiyo.

“Sawa. Unaweza kumtafuta.” Kiongozi akamjibu Inspekta, naye mwanamama akaingia huku akitazama kwa kupeleleza kona zote muhimu.

Mkuki alikuwa akitazama, alijituliza pale huku akitetemeka kwa uwoga. Basi Inspekta akasogea upande ule ule aliokuwamno Mkuki, akasimama mbele ya palepale alipojificha Mkuki, na ni kama alihisi kitu maeneo hayo. Akageuka, akatazama pale alipojilaza Mkuki, palikuwa na giza, ilikuwa si rahisi kuona bila ya kuinama na kuchungulia; basi naye Inspekta akaanza kuinama ili one vizuri.

“Inspekta?” ghafla alisikika mtu akiita kutoka nje ya boti, Inspekta Su Lee akaacha kutaka kuendelea kuchungulia ile sehemu, akasimama, akatazama kule alipoitwa, akamuona mmoja wa askari wake akimpungia mkono kwa ishara ya kwamba aende, kuna kitu wameona.

Inspekta akatoka ndani ya boti kwenda, huko kulikuwa na mvuvi mmoja waliyemkamata na madawa ya kulevya mengi kweli kweli hivyo ilibidi nguvu ihamie huko sasa ingawa Inspekta hakutaka kupoteza muda  mwingi katika hilo; alikuwa akimtaka Mkuki tu amfunze adabu.

Basi wakati wao wanaendelea kujadili, shughuli ya kupakia mizigo kwenye boti aliyokuwemo Mkuki ilifika tamati. Nahodha wa chombo hicho akapokea maagizo kutoka kwa kiongozi kwamba awashe mashine na safari ianze mara moja, na hivyo ndivyo ilivyokuwa.

Mkuki alishukuru sana pale boti ilipoanza kuacha soko la samaki la kiswani Jiaju na kutokomea baharini; hakuwa akifahamu boti inakwenda wapi lakini alichoshukuru ni kwamba alinusurika kuangamia.

Boti ilikuwa ikilekea China katika jiji kubwa na maarufu la Hong Kong. Ilikuwa ni safari ya takriban kilomita 2000 kutoka kisiwani Jiaju. Wakiwa wanakaribia Mkuki alianza kuona majengo marefu ya jiji hilo. Alihisi furaha kubwa moyoni kwa kila kitu, sura ya jiji la Hong Kong ilimfanya apate matumaini mapya ya maisha hata akajikuta anafutilia mbali wazo lake la kurejea kwenye nchi ndogo na maskini aliyotoka—hii ni sawa na kusema kwamba alifutilia mbali wazo la kurudi kwa kina Mei Lee.

Alidhamiria kuanzisha maisha hapo na kiu ya kuona hilo linafanikiwa ilimfanya hata akapata taswira ya jinsi mambo yatakayokwenda; alijiona jinsi akiomba ajira, anakubaliwa, anaanza kazi, anapata ujira wake, anatumia ujira kidogo na kiasi kinachobaki anahifadhi kwa ajili ya kwenda kukuza maisha pindi atakaporejea Tanzania kwao.

Boti aliyoipanda ilisogelea pwani ya mjini Hong Kong, ikaegeshwa kwenye eneo la bandari ndogo ambapo yalikuwepo magari kwa ajili ya kubeba samaki walioletwa na boti hiyo. Hapo Mkuki akachomoka bila kuonekana, ilikuwa ni kazi rahisi sana, na hakutaka kupoteza muda pale bandari, akaingia moja kwa moja mtaani.

Kwa mara ya kwanza kuwa China aligundua kitu; aling’amua kuwa hiyo ilikuwa ni ardhi ya fursa kwa jinsi ambavyo muingiliiano wa watu ulivyokuwa mkubwa. Aliona raia wakipishana huku na huko, kila mmoja akiwa na habari zake, na hakuonekana hata mmoja aliyekuwa akimjali yeye wala mwingine—hiii ikimpa imani ya kwamba labda hata ile kadhia ya ubaguzi itapungua.

Basi alijichanganya mtaani kama raia wengine wa kawaida, hakuna aliyegundua kwamba alikuwa ni mgeni ambaye hakuwa na kibali cha kuishi ndani ya China. Alizunguka akikatiza mitaa mbalimbali ya mji huo, ilipita mtaa wa Shengh ambao unaungana na barabara kubwa iitwayo Mao, huko akapitapita na kutokea kwenye barabara nyingine iitwayo Huan, ambayo ilimuongoza hadi kwenye chochoro moja ambayo iliundwa na majengo mawili kulia na kushoto; jengo moja likikiwa ni ofisi za kampuni iitwayo Huan Express inayomiliki boti za abiria, na jengo lilingine lilikuwa ni mgahawa mkubwa uitwao Chensee.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Jengo la mgahawa lilikuwa na mlango nyuma, kule kichochoroni ambako Mkuki alikuwa anapita. Basi karibu na hapo mlangoni aliwaona vijana sita wenye asili ya kiafrika, walikuwa wakibeba maboksi ya samaki kutoka kwenye gari na kuyaingiza ndani ya mgahawa.

Matumaini ya Mkuki yakaongezeka zaidi, akajiaminisha kwamba wale Waafirka wenzake ni lazima watampa msaada wa aina yoyote ile, ama kazi au mahala pa kulala.

Haraka akawafuata, alipokaribia wakamuona, walikuwa wamepumzika kubeba maboksi japo kwa dakika moja.

Akawafikia.

“Habari zenu?” Akawasilimu kwa lugha ya Kithaiwan, lugha ambayo ilikuwa ni sawa na Kichina tu.

Wakamuitikia kwa pamoja. Akaendelea. “Ndugu zangu nina shida, sijui naweza nikapata msaada kutoka kwenu?.”

“Ongea tu.” Mmoja akamjibu.

“Mimi naitwa Mkuki, nimeingia leo hapa China. Hizi mnavyoniona sina hata sehemu ya kulala, na sina ndugu wala simfahamu mtu yeyote hapa Hong Kong, naombeni mnisaidie hifadhi kwa siku mbili tatu.” Akajieleza lakini badala ya wale watu kumjibu walianza kuinuka mmoja baada ya mwingine na kuanza kubeba maboksi ya samaki na kuingiza ndani.

Mkuki alibaki ameduwaa, hakutegemea mapokeo ya aina ile kutoka kwa watu ambao alikuwa akifanana nao asili. Walimuacha peke yake kwa mtindo wa kumdharau sana kana kwamba aliongea pumba tupu.

Punde mmoja wa wao akarudi kwa ajili ga kuchukua boksi lingine, hakumsemehsa Mkuki kana kwamba hakuwa akimuona pale alilosimama.

“Ndugu yangu.” Mkuki akaamua kumuita, yule mwanaume akaacha kubeba boksi akamgeukia.

Mkuki akaendelea. “Naomba nisaidie Kaka. Sisi ni kitu kimoja.”

“Umetokea wapi?’ Akauliza.

“Nimetokea Thaiwan.”

“Kwahiyo wewe ni Mthaiwan?”

“Hapana. Yaani nilikuwa naishi huko, lakini mimi ni Mtanzania.” Akafafanua.

“Mtanzania? Sawa. Lakini sikia nikwambie, China kuna maisha magumu sana tofauti na unavyofikiria, sio rahisi kupata msaada kwa mtindo wako unaoutumia.  Labda cha kukusaidia nikuitie Mtanzania mwenzako ndo mnaweza mkaelewana, ila binafsi sina cha kukusaidia.”

“Wewe ni wapi kwani?” Akauliza Mkuki.

“Kwani unataka kugundua nini? Sioni faida ya wewe kujua asili yangu, cha msingi ni uniambie kama nikuitie Mtanzania mwenzako au niache.”

“Sawa. Niitie.” Akasema Mkuki,

Basi yule jamaa akabeba boksi la samaki, akaingia mgahawani akimuacha Mkuki akisubiri mrejesho wa kile alichoahidiwa.

Jamaa yeye alikuwa ni mtu kutoka Ghana; yeye pamoja na wale wenzake walikuwa ni vibarua wa kazi mbalimbali hapo mgahawani; walibeba maboksi, walioosha vyombo na kadhalka—walitoka kwenye ardhi za mama zao kwa ajili hiyo ya kutafuta maisha nchini China.

Basi punde yule jamaa akarejea akiwa mikono mitupu, alikujua kuchukua boksi moja ambalo liliasalia kwenge gari pamoja na kumpa mrejesho Mkuki juu ya kile walichokubaliana.

“Anakuja.” Akawambia Mkuki juu kwa juu, yaani hata hakusimama, alizungumza huku akienda kwenye gari, akachukua boksi la samaki ambalo lilikuwa la mwisho kwenye gari, akaingia nalo mgahawani akimuacha mkuki amesimama pale pale.

Sekunde sitini baadae ule mlango wa mgahawa ukafinguliwa, akatoka mwanaume mrefu, mnene, mweupe mwenye nywele zilizopunguzwa kawaida na hata ndevu pia. Alikuwa amevalia eproni jeupe kama wale waliokuwa wakibeba maboksi lakini la kwake liliuwa limechafuka zaidi.

Mkuki hakumuona sura na hata yule jamaa hakumuona Mkuki kwa sababu alitoka kinyumenyume akiwa anazungumza na mtu aliyekuwa ndani.

Mkuki akajiweka sawa, akajipanga barabara kwa ajili ya kuzunguma na Mtanzania mwenzake huku akimaini kwamba kwa hatua hiyo aliyofikia msaada utakuwa ni kiti cha lazima.

Yule jamaa akamaliza kuzungumza, akageuza uso wake alipokuwa Mkuki lakini ghafla aliacha kutembea, akamtazama Mkuki kwa kumtumbulia macho kana kwamba amemuona mtu waliyepotezana kitambo kirefu.

“Mkuki?” Jamaa akaita kwa sauti yenye mirindimo iliyoashiria kutoamini kile anachokiona.

“Meja!?” Mkuki naye akalipa mapigo kwa mtindo ule ule.

Basi hapo kilifanyika kitendo ambacho si cha kawaida; Meja alimkimbilia Mkuki na kumkumbatia huku akilia tena machozi kabisa kama mtoto mdogo na hata kwa Mkuki ilikuwa hivyo hivyo.

*****************************



http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Mkuki umepona ndugu yangu? Siamini, siamini kaka.” Alisema jamaa yule ambaye Mkuki alimuita kwa jina moja la Meja.

Mkuki alishindwa hata kuzungumza, aliendele kuangua kilio kama mtu aliyechanganyikia, akawa anamuachia kidogo Meja, anamtazama usoni kisha anamvuta wanakumbatiana tena.

Baadae waliachana, kila mmoja akjifuta machozi, Meja akamtaka Mkuki wasogee karibu na ile gari iliyokuwa na maboksi ya samaki, wakasimama hapo kwa kuigemea.

“Mkuki ujue siamini kama ni wewe? Uliponaje?”

“Ni stori ndefu Meja, nadhani tutapata muda nitakusimulia vizuri. Nashukuru Mungu nimepona.”

“Dah! Kwahiyo ulijuaje niko hapa?”

“Hata nilikuwa sifahamu kama nitakukuta hapa. Mi nilikuja natafuta kazi.”

“Kwahiyo unaishi maeneo gani?”

Akajichekesha kidogo Mkuki kabla ya kujibu. “Hata sijui nikujibu nini. Mimi sina hata pakulala Meja, ndo kwanza nimeingia leo hapa China.”

“Kwahiyo ulikuaa unaishi wapi sasa?” akauliza Meja, na yeye hupenda kutumia sana neno 'kwahiyo' kwenye mazungumzo yake.

“Nitakwambia tutapotulia. We unaishi wapi?”

“Niko hapo nyuma, panaitwa Huanzou. Nimepanga, naishi na mwanamke na tuna mtoto mmoja wa kiume anaitwa Jisu, nimeamua kumpa jina la muasisi wa hii safari yetu aisee.” Akaeleza Meja.

“Dah! Hongera. Na hapa ndo kazini?”

“Ndiyo. Naosha-osha vyombo bwana, lakini nashukuru Mungu mkono unaenda kinywani.” Akasema na kuongeza. “Sasa sikia Mkuki, inabidi mi nirudi ndani nikakimbize. Ngoja nikuletee kitu ukae hapa unisubiri, namaliza kazi muda si mrefu tunaondoka pamoja nyumbani.” Akasema Meja kisha akaingia ndani na punde akatoka akiwa na kreti tupu, akampa Mkuki akalie halafu yeye akarudi tena ndani.

Mkuki alikaa pale nje asiamini kilichotokea; aliona ni kama muujiza ama ngekewa, na alishindwa kabisa kujizua kumshukuru Mungu kwa kumuongoza hata kukutana na msaada wa uhakika namna ile.

Meja alikuwa ni rafiki yake, mshikaji wake na kaka yake wa hiari pia. Kiumri Mkuki alikuwa mdogo kwa Meja, alizidiwa miaka takriban sita ingawa alionekana ni mkubwa kutokana na maisha magumu aliyopitia.

Aliendelea kuwa pale huku akikumbuka jinsi ambavyo alipata kujuana na Meja; walivyokutana kwa mara ya kwanza na jinsi walivyokuza urafiki wao.

Aliikumbuka siku ile, ilikuwa ni Jumamosi jioni, alitoka nyumbani kuelekea kwenye Uwanja wa Mpira wa miguu wa Shule ya Msingi ya Tandale ‘A’ iliyopo huko Tandale ambapo wote wawili, Meja na Mkuki walizaliwa na kukulia. Alikwenda kutazama mechi iliyozikutanisha timu mbili kutoka Tandale; Mafisi FC kutoka Tandale Sokoni na Wakali wa Danta kutoka Tandale Bondeni.

Mkuki alifika na kusimama pembeni mwa uwanja akiegemea ukuta wa jengo moja la madarasa ya shule ya msingi Tandale. Pembeni yake kulikuwepo na kundi la vijana wapatao nane wakivuta bangi; ni kawaida kwenye viwanja vya mpira vya shule nyingi Tanzania, kila jioni vijana wa kihuni hujumuika huko na kuvuta bangi haswa zinapochezeka mechi za timu za mitaani namna hiyo.

Miongoni mwa lile kundi la vijana nane alikuwepo Meja, alikuwepo na Jisu pia ambaye yeye ndiye aliyekuwa ‘Pusha’, yaani aliyekuwa akiwauzia wenzie bangi.

Basi Mkuki alifanya kazi mbili akiwa pale aliposimama, macho yake yalitazama kabumbu wakati masikio yalisikiza mazungumzo ya wale wavuta bangi wa karibu yake.

Mada kubwa waliyokuwa wakiijadili ilikuwa ni kuzamia nchini Afrika ya Kusini kwenda kutafuta maisha, na Jisu alitawala mazungumzo yao; alionekana kuijua mno Afrika kusini kwa jinsi ambavyo aliielezea. Aliwasimulia wenzie jinsi ambavyo watu huzamia meli, wanavyoishi baada ya kufika Afrika Kusini, wanavyotafuta pesa na mambo mengine mengi.

Stori zile zilimvuti sana Mkuki hata akajikuta akihamisha akili yake yote upande ule badala ya kutazama kabumbu. Yeye alikuwa ni miongoni mwa vijana wengi wa Kitanzania wasiokuwa na kazi wala kibarua rasmi cha kuwaingiza kipato cha kuendesha maisha yao, kiasi kwamba nafsi zao ziliingiwa giza na imani mbovu ya kwamba ni rahisi sana kufanikiwa kimaisha kama utapata fursa ya kufanya kazi yoyote ile katika mataifa yaliyoendelea.

“Mimi nilikuwa naishi Pritoria, yaani kule ndo pesa nje nje. Ukiwa mjanja mjanja mbona shega tu, unapiga sana pesa.” Mkuki alimsikia Jisu akizungumza namna hiyo; hakuwa akimfahamu hata kwa jina lakini kwa yale mazungumzo yake aligundua kwamba jamaa huyo alishawahi kuishi Afrika Kusini.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Basi Mkuki aliendelea kuwasikiliza akiwa palepale huku nafsi ikimsukuma kutamani kupata nafasi japo mara moja ya kuishi Afrika kusini ili apate pesa zile alizokuwa akizisimulia Jisu, ili aweze kujikimu yeye sanjari na kuwasaidia wazazi wake ambao walikuwa wazee wasiokuwa na msaada licha ya kwamba walikuwa na watoto tisa kujumuisha na Mkuki.

Basi wakiwa bado palepale uwanjani, ghafla Mkuki aliona watu wakikimbia hovyo kuja upande aliokuwa amesimama yeye, kisha papo hapo akawaona wahuni nao wamesiamama na kuanza kutimua mbio huku wakipishana taarifa kwamba kulikuwa na kundi la maaskari polisi limevamia uwanjani hapo kwa ajili ya kuwakamata wavuta bangi.

Ni kweli, askari hao walikuja kwa lengo la kuwanasa wavuta bangi lakini kutokana na hali ilivyo hata waliokwenda kutazama mpira tu walikimbia kwa kuhofia kukamwatwa na kuchanganywa na kundi ambalo hawakuwa miongoni mwao—basi ikawa  ni patashika nguo kuchanika, watu walikimbia huku na huko na kutimua vumbi si kidogo.

Basi Mkuki alikuwa ni miongoni mwa wasiovuta bangi lakini wakakimbia kujiepusha na dhahama. Alitoka mbio kulelekea upande ambao haukuwa na polisi wengi na ni watu wachache tu waliopita huko. Mbele yake alimuona Meja akikimbia sambamba na Jisu, yule muuza bangi aliyekuwa akitoa simulizi nyingi kuhusu Afrika Kusini.

Mkononi Jisu alikuwa ameshikilia mfuko wa nailoni uliokuwa umejazwa bangi za biashara, alihakikisha ameukamatia kwa uhodari ili usije ukadondoka na akapata hasara kubwa. Lakini akiwa bado kwenye mbio ghafla kandambili yake aliyokuwa amevaa ikakatika, mkanda ukamnasisha na kupelekea anaanguke chini kama mzigo. Alibingilika huko Jisu, wakati mfuko wake wa bangi uliangukia mbali na yeye. Akajitahidi kuinuka mara moja, akatazama umbali wa zilipo bangi zake akilinganisha na umbali wa askari polisi, na kwa hesabu za haraka akagundua kuwa kama atathubutu kusema azifuate bangi hizo basi askari watamfikia na kumtia mbaroni.

Akapiga moyo konde, akaonelea ni vyema kama atajinusuru yeye kuliko kukamatwa na kutupwa selo ambako ili kutoka angetakiwa atoe rushwa ya kiasi kikubwa cha pesa ukilinganisha na thamani ya zile bangi zake.

Akakambia, akauacha mzigo.

Mkuki aliuona mfuko ule, alipoufukia akauokota, kisha akendelea na safari yake lakini kwa bahati mbaya askari polisi mmoja alimuona, hivyo akaanza kumfukuza yeye kama yeye.

Mkuki aligundua ugeni huo uliokuwa nyuma yake, na hapo sasa akanuwia kwamba atakimbia mpaka mwisho wa pumzi yake ili asinase mikononi mwa askari wale wachapakazi lakini wapendwa rushwa, kwani laiti kama watamkamata, hatotoka nyuma ya nondo hadi pale atakapotoa hongo ya kiasi kikubwa cha pesa.

Basi mbio za Mkuki na polisi zilihamia hadi mtaani, Mkuki alikatiza chochoro hizi na zile ili kumpoteza afande huyo lakini bado askari alikuwa nyuma yake, bila shaka hata yeye alinuwia kwamba ni lazima amkamate tu—ilikuwa ni mshikemshike.

Basi Mkuki alipita chochoro mbili tatu na alipotazama nyuma akagundua kuwa amempoteza kidogo yule askari. Hakuona sababu ya kuendelea kukimbia zaidi, hapo aliamua kuingia kwenye ua wa nyumba moja ili apate kujificha. Ubaya ni kwamba ua wa nyumba aliyoingia ulikuwa mtupu, haukuwa na sehemu ya kujificha. Akapiga hesabu za haraka, akagundua kwamba kama atathubutu kutoka nje na kuendelea kukimbia ni lazima yule afande atamkuta na kumtia mbaroni, hivyo ilikuwa ni lazima atafute pahala salama pa kujificha ndani ya nyumba ile ile.

Akapata wazo ndani ya sekunde chache; akaona itakuwa vyema na salama zaidi kwake kama ataingia kwenye choo cha nyumba hiyo na kujituliza kimya hadi pale atakapohakikisha hali imetulia.

Akafanya hivyo, akasogelea choo cha nyumba hiyo, akafunua pazia la kiroba lililokuwa likining’inia mlangoni, akaingia ndani, akajituliza tuli.

Akiwa huko alimsikia yule askari akipita, akasikia kama amekwenda mbele kisha akarejea, na akamsikia akimuuliza mtu kama alimuona kijana fulani akikimbia na mfuko, hakusikia jibu lakini punde kidogo baadae alisikia ukimya tu.

Mkuki alikaa mle chooni hadi alipojihakikishia kwa imani kwamba hali imetulia kabisa, akatoka akiwa na ule mfuko wenye bangi bila kuonekana na akashika njia ya nyumbani kwao moja kwa moja.

Alifika nyumbani, akaingia ndani kabisa na kujifungia chumbani, akauweka ule mfuko kitandani, akaufungua na kuzitamzama zile bangi. Zilikuwa ni nyingi sana hata akaingiwa na hesabu za haraka kuziuza na kupata kiasi kikubwa sana cha pesa.

Basi baada ya pale akafunga mfuko, akauficha uvunguni mwa kitanda na kutoka kwa ajili ya kwenda mtaani kutafuta mteja wa kununua zile bangi.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Lakini siku zote biashara chafu hufanywa na watu wazoefu, na hii ilipelekea Mkuki ashidwe kabisa kupata mteja wa kununua zile bangi kwa takriban siku saba kwa sababu hakuwa akifahamina na wateja na aliogopa kumuuliza kila mtu kwa sababu ile ilikuwa ni biashara haramu. Sasa akachoka na biashara hiyo isiyouzika, na wazo pekee alilokuwa nalo ni kuurejesha ule mzigo kwa mwenyewe.







ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog