Search This Blog

Tuesday 20 December 2022

KWA AJILI YENU WANANGU, NITAMWAGA DAMU - 1

 



IMEANDIKWA NA SULTAN UWEZO


Simulizi: Kwa Ajili Yenu Wanangu, Nitamwaga Damu 

Sehemu Ya Kwanza (1)


Robinson aliamka asubuhi na mapema kuelekea shambani akiwaacha wazazi wake wakiwa bado wamelala, lengo likiwa kwenda kumalizia kieneo kidogo ambacho walikibakiza kulima kwenye shamba lao la mihogo.

Alichukua panga lake na jembe lake begani na kuianza safari ya Kuelekea shambani.

Kutoka nyumbani mpaka shambani kwao kulikuwa na kama kilometa kumi hivi na eneo hili lilionekana kuwa na rutuba kiasi chake na walilitegemea tofauti na eneo la upande wa milimani lilikuwa na kokoto nyingi sana hivyo halikuwa rafiki kwa kilimo.

Eneo la mzee Kaaya halikuwa kubwa sana ni kama viplot vitatu tu.

Alipofika shambani alianza moja kwa moja kulima eneo lile, ilipotimia saa nne asubuhi jua lilikuwa kali hivyo kumfanya aache kulima na Kuelekea bondeni ambako kulikuwa na kijito kidogo lakini kilichotiririsha maji mwaka mzima.

Alivua nguo zake na kuanza kuoga kwa kuogelea kwenye kisehemu ambacho maji hujikusanya na kuwa kama kibwawa hivi, aliogelea na alipomaliza alivaa nguo zake na kuondoka zake lakini akiwa njiani aliamua Kupitia kwenye migomba ili akatafute ndizi zilizoiva walau atulize njaa ambayo tayari ilikuwa imeanza kuchukua nafasi.

Aliizunguka migomba yote lakini hakukuwa na dalili yoyote ya uwepo hata wa chembe moja ya ndizi, alijilaumu sana.

"Ona sasa migomba yote hii inakosaje ndizi?"

Baada kujiridhisha kuwa hakukuwa na ndizi aliondoka zake kurudi shambani.

"Kwa njaa hii sijui nitafanikisha kumaliza eneo lililobaki." Alijisemea mwenyewe.

Mungu ni mwema alimaliza kulima kisehemu kile na kuchukua zana zake na kurejea nyumbani.


"Habari yako kaka!"


Ilikuwa ni salamu iliyomshtua Robinson akiwa njiani kurudi nyumbani. Aligeuka na kumuangalia aliyetoa salamu hiyo.

Alikutana na sura ya mtoto wa kike mrembo mwenye wingi wa tabasamu usoni.

Robinson aliangaza huku na kule kujua dada huyu katokea wapi na kama ni nyuma yake mbona alipokuwa anaingia kwenye barabara hiyo hakuona mtu.


"Kaka vipi nimekusalimia mbona hujibu?" Mrembo huyo aliuliza baada ya kuona Robinson hajibu salamu yake.

Na swali hili lilimtoa mawazoni.


"Salama dada, samahani kwa kuchelewa kujibu salamu yako nadhani ni uchovu tu." Alitetea.


"OK, naitwa Jackline." Mrembo huyu alijitambulisha.


"Naitwa Robinson."


"Nafurahi kukufahamu Robby."


"Siyo Robby, naitwa Robinson dada."


"Aah ok Robinson."


"Samahani Robinson naomba msaada wako, Gari langu limenizimia pale bondeni nimetoka mjini nilikuwa naelekea kijijini kwa mzee Fikirini na kabla sijafika mafuta yameniishia."


"Du pole sana, nakusaidiaje dada yangu?"


"Naomba msaada wa mafuta kijijini."


"Ni mbali sana kutoka hapa mpaka kijijini,lakini ngoja nijaribu."


"Asante sana kaka yangu, ngoja nikupe hela ila kidumu utaomba huko huko."


"Bila shaka, so wewe unabaki huku huku?"


"Inabidi nibaki mpaka utakaporudi ila utanikuta ndani ya gari."


"OK, basi ngoja niwahi."


Robinson alikimbia haraka kufuata mafuta ya gari la mgeni wake. Alishika vizuri panga na jembe ili visiweze kumkwaza kwa mbio zake. Aliwaza sana juu ya yule binti,


"Inakuwaje mrembo kama yule anatembea porini peke anajiamini nini? "


Ndani ya muda mfupi alikuwa nyumbani kwao akiweka zana zake za kazi na kisha kuingia kwenye kichumba cha kutunzia vyombo na kuchukua kidumu cha lita 5 na kutoka mbio.


"Robinson, Robinson." Mama yake aliita baada ya kumuona yuko juu juu na ghafla akitoka na kidumu. Lakini alikuwa kuchelewa kwani tayari alikuwa akikata kona ya mtaa wa tatu.


"Sijui anaharakia wapi mtoto huyu chakula chenyewe hajala." Aliwaza mama yake.


Alifika na kumuomba muuza petroli pale vibandani ampimie ya lita 5 kwani anaharaka sana.


"Samahani kaka nifanyie haraka niwahi ninasafari ya mbali." Aliongea Robinson.


"OK, dakika chache tu mdogo wangu."


Baada ya kulipa na kuridishiwa chenji yake alichukua dumu lile na kuanza kuondoka kwa kasi yake Kuelekea kule porini. Japo jua lilikuwa kali halikumzuia kutembea haraka ili kumuwahi mgeni wake akiamini binti kama yule kukaa porini kwa muda mrefu ni hatari.

Alifika na kumkuta Jackline akiwa kalala fofofo akiwa kalaza kiti cha mbele lakini kioo akiwa kakishusha.


"Jackline, Jackline, Jackline."

Alimuamsha kwa dakika kadhaa ndipo aliposhtuka kutoka usingizini.


"Niache Siyo mimi, siyo mimi."


"Siyo wewe nini Jackline?"


"Oogh sorry Robby, nilikuwa naota ndoto ya ajabu sana. Umeenda haraka sana ee mara hii au siyo mbali."

Jackline alijibu kwa swali.


"Sema njia yenyewe nimeizoea sana."


"Aisee, uko fasta sana Robinson."


Baada ya kuweka mafuta aliiwasha gari ikawaka, Jackline alifurahi sana kuona gari imekubali kusonga mbele.


"Robinson panda twende zetu hapa imepona."

Aliongea Jackline.


Robinson alipanda gari hiyo aina ya Honda na safari Kuelekea kijijini ilianza.


"Unatelemkia wapi Robinson." Aliuliza Jackline.


"Kwenye ile nyumba ya yenye bati kuu kuu."


"Ndo kwenu pale ee."


"Hapana, nyuma ya ile nyumba."


"Ok, nitafika nipafahamu."


"Karibu sana dada Jackline."


"Usijali."


Gari ilisogea taratibu kabisa na ikaacha Njia na kuelekea chini ya mti mkubwa wa mwarobaini uliokuwa nje ya nyumba yenye bati kuu kuu na kupaki. Jackline aliteremka kwa madaha na Kuelekea upande ule wa kushoto na kumfungulia Robinson mlango si unajua tena "MASHIKORO MAGHENI" kisha akalock milango na kumfuata Robinson.


"Twende zetu Robby." Aliongea Jackline.


"Njia ni huku kwenye hiki kiuchochoro."


"Ok."


Walitembea Kuelekea kwenye kiuchochoro hicho huku Robinson akiongoza njia.

Jackline aliwaacha watu wa mtaani hapo kuacha kazi zao na kumkodolea macho Robinson na mgeni wake huku wakimkazia macho zaidi Jackline kutokana na mavazi ambayo aliyavaa.


"We mama umemuona yule dada."


"Jamani jamani, sasa ndiyo nguo gani zile yaani suruwale imembana vile akitaka kuivua anafanyaje mwe." Aliongea mama huyu aliyepigwa butwaa.


"Hivi hata chooni anaendaga kweli maana kule nyuma nako kaaa!" Alichombeza mama mwingine aliyekuwa akitokea kuchota maji.


"We mama Joi hivi huyu binti ndiyo mke wa Robinson?" Aliuliza Mama muuza nyanya.


"Atambe na umaskini alionao atamuoa nani, mtoto wa mama Mashaka mwenyewe alimshinda kwenye uchumba tu baada ya kutajiwa ng'ombe watatu sembuse huyu mkanyaga lami?" Alijibu mama Joyce.


Robinson na mgeni wake walikata mtaa na hatimaye kufika nyumbani kwa kina Robinson.


" Karibu sana Jackline hapa ndo nyumbani."


"Ooh Asante Robinson ni pazuri." Alijibu Jackline.


Robinson aliingia ndani na kutoka na kiti kidogo cha miguu mitatu maarufu kama KIGODA na kumkabidhi mgeni wake, kisha kuingia tena ndani.


"Mama, mama!"


"Rabeka mwanangu, hivi ulikuwa unakimbilia wapi muda ule nakuita."


"Shikamoo mama."


"Marhaba, jibu swali langu kwanza."


"Mama nitakujibu tu lakini kwa muda huu njoo huku nje kuna mgeni."


"Katokea wapi?"


"Utajua hapo hapo nje."


Walitoka nje na kumkuta mgeni ambaye alionekana ni mgeni kijijini hapo.


"Mama Shikamoo." Alisalimia Jackline.


"Marahaba mwanangu, karibu kwetuu."


"Asante mama."


"Mama, huyu ni Jackline anatokea mjini kaja hapa kijijini kwetu na huyu ndie aliniomba nije huku kumnunulia mafuta ya petrol kwa ajili ya Gari lake ambalo liliishiwa."


"Aaa karibu sana mwanangu."


"Asante mama."


"Robinson au ndiye mkwe wangu nini maana nyinyi vijana mhh."


"Hapana mama nilikutana naye tu kule shambani."


Baada ya kutambulishana huko Jackline aliomba aende kwani bado anakasafari kidogo kwani alikuwa akielekea mwisho wa kijiji.


"Mama naomba mniruhusu niende, maana bado nina kasafari kidogo."


"Si usubiri baba yako aje umsalimie na umfahamu?"


"Wakati mwingine mama yangu nitamuona tu." Aliongea huku akiingiza mkono ndani ya pochi yake na kutoa noti tatu za elfu kumi. Na kumkabidhi mama Robinson.


"Asante Sana mwanangu Mungu akubaliki weweee."


"Kidogo mama."


"Karibu sana dada Jackline."


"Usijali Robinson."


Baada ya hapo walimsindikiza mgeni wao mpaka kwenye gari lake na kufungua mlango na kuingia ndani. Aliwasha gari na kulisogeza barabarani na kulipaki na kumwita Robinson.


"Hii ni namba yangu ya simu tusipoonana utanitafuta kwa mawasiliano. Na hii itakusaidia kwa mishe za hapa na pale."


"Asante sana nashukuru!"


Kisha gari liliondolewa kwa kasi na kutokomea. Huku nyuma Robinson hakuamini alichokiona mkononi mwake kwani alikuwa na kitita cha shillingi elfu sabini. Mama Robinson alimfuata mtoto wake na kumwambia kitu hiki.



Mzee Fikirini alifurahi sana kumuona binti yake Jackline tena ambaye waliachana kwa kipindi cha miaka ishirini na tano.

Jackline ni mtoto wa kaka yake mzee Fikirini ambaye alijulikana kwa jina la Joachim. Joachim na mke wake walifariki muda mrefu sana katika ajali ya gari ambayo ilitokea katika mlima Sekenke mkoani Singida walipokuwa katika ziara ya mapumziko katika kisiwa cha Ukerewe na katika ajali hiyo alinusurika binti yao wa pekee Jackline, ambaye baada ya taratibu zote kufuatwa alikabidhiwa mzee Fikirini kipindi hicho Jackline alikuwa na umri wa mwaka mmoja tu.

Kutokana na urafiki uliopitiliza baina ya mzee Joachim na mzee Jonathan Ubao. Ilibidi mzee Jonathan Ubao amuombe Jackline kutoka kwa mzee Fikirini ili akaishi naye nyumbani kwake mkoani Tabora ikiwa ni pamoja na kumpatia mahitaji yake ya muhimu kama vile Elimu kama asante yake kwa rafiki yake Joachim kwa msaada ambao alimsaidia kipindi alichokuwa amefirisika.

Mzee Joachim alimsaidia kiasi cha shilingi milioni nne ili imsaidie kumrudisha kwenye mstari, na hapo ndipo alipoamua kufanya biashara ya mazao hasa mchele ambapo alikuwa akinunua mpunga kutoka wilaya za Nzega na Igunga na kisha kukoboa na mchele kuusafirisha mpaka mkoani Singida ambako aliwauzia wafanyabiashara kutoka Arusha na Zanzibar kwa bei ya jumla. Biashara hii ilimfanya kuwa maarufu ndani ya miaka miwili, kwani kwa kipindi hicho cha miaka miwili tayari alikuwa na mtaji uliofikia milioni 30 kwa kipindi hicho na kumfanya kuwa na mashine yake ya kukoboa mpunga mkoani Singida.

Hii ilimrudisha kwa rafiki yake Joachim na kumshukuru kwa msaada wake na hakusita kumfahamisha maendeleo ya biashara zake.

Miaka kadhaa baadaye alisikitishwa na taarifa ambazo zilimfikia juu ya ajali mbaya ya rafiki yake. Ilimuuma sana Mr. Jonathan kutokana na maisha ambayo waliyapitia yeye na rafiki yake na mpaka kufikia hatua ya Kupokea msaada wa shilingi milioni nne kama mtaji na sasa alikuwa milionea.

Hivyo jukumu lake baada ya kukamilisha shughuli za mazishi ya mzee Joachim na mkewe ikabidi achukue jukumu la kumlea Jackline na kumsomesha mpaka pale atakapofikia. Na hilo ndilo alilifanya kwa Moyo wake wote.

Na leo hii binti huyu alikuwa kwenye ardhi ya baba yake mdogo mzee Fikirini pale kijijini Lupa Wilayani Chunya ambako mzee huyu alijishughulisha na kilimo cha mihogo, ndizi, mahindi pamoja na zao la Tumbaku ambalo kwa wakati huu wakulima walilazimika kutumia mtaji na hii iliwafanya wengi washindwe kulimudu zao hili na kuegemea kwenye mazao mengine na kuwaacha wakina Fikirini wakipambana na zao hilo kwa Kupitia migongo ya wakulima wakubwa pale kijijini.


"Hivi ni wewe mwanangu Jackline kweli?" Aliuliza mzee Fikirini.


"Baba ni mimi ndiye, kwani vipi?"

Alijibu Jackline.


"Yaani bado siamini kama ni wewe maana ni muda mrefu sana."


"Ni kweli kabisa baba lakini ramani uliyokuwa umenielekeza kuanzia pale madukani haikunisumbua sana japo nilipokuwa nimekaribia maeneo yale ya Kaea kwa chini kabla ya kuvuka daraja lile dogo mafuta yaliniishia, lakini nimshukuru sana yule kijana anaitwa Robinson alinisaidia sana."


"Aaa yule kijana nampenda sana kwa tabia yake, ni mtulivu, mwelewa, asiye na majivuno kama wenzake waliopo mtaani hapa. Kwanza bidii yake shambani wee acha tu mzee Kaaya kalamba dume."


Maneno yale ya mzee Fikirini yalipenya vilivyo masikioni mwa Jackline na kumfanya afikirie kuendelea kumfuatilia zaidi huyu Robinson. Mbali na hayo lakini Jackline alimsimulia baba yake safari nzima ya kimasomo pale Tabora mpaka mkoani Tanga na kisha nchini Afrika Kusini.

Kifupi baada ya kumaliza shule ya msingi alijiunga na Sekondari ya Nanga iliyoko Wilayani Igunga na baadaye kujiunga na Sekondari ya juu ya Umoja iliyo karibu kama kilometa kadhaa kutoka Kijiji cha Ndala-Nzega kwa elimu ya kidato cha tano na Sita.

Kwa kuwa shule ile ya Umoja ni ya kidini iliweza kuwadhamini wanafunzi ambao walifanya vizuri kwenye mitihani ya mwisho kidato cha Sita na Jackline akiwemo kwa elimu ya juu ya Chuo Kikuu na hapo ndipo Jackline alipata nafasi ya kuingia ndani ya Chuo Kikuu cha Soweto nchini Afrika ya Kusini.


"Kwa hiyo huko Afrika ya Kusini uliwahi kuonana na Mandela mwanangu." mzee Fikirini Aliuliza.


"Halafu na wewe baba bwana, kwani wewe mpaka umefika umri huo ni raisi gani wa Tanzania umewahi kuonana nae?"


"Mhh, tuachane na stori hizo za Mandela, maisha yalikuwaje kuanzia kwa mzee Jonathan mpaka Chuoni Afrika ya Kusini?"


"Kwanza kabla ya yote mama na wadogo zangu wako wapi baba, maana toka nimefika sijawaona."


"Mama yako yuko msibani sehemu moja umeipita inaitwa Bitimanyanga kuna rafiki yake alihamia huko miaka kadhaa nyuma ndo ambaye kafariki juzi baada ya kupigwa na radi akiwa shambani kwenye Matumbaku yetu haya, na mdogo wako Shamimu anasoma kidato cha tatu hapa hapa Lupa Sekondari na kaka yako Athuman anaishi jijini Mbeya akifanya biashara ya mitumba huko."


Wakati baba na mwana wakiendelea na mazungumzo baada ya kuachana kwa muda mrefu wakati huo wakiwa Wilayani Manyoni kabla ya mzee huyo kuhamishia makazi yake kijijini hapo. Alifika Shamimu kutoka shule na ndipo mzee Fikirini alipomtambulisha kwa Jackline na baada ya utambulisho huo Jackline na Shamimu walikumbatiana kwa furaha.


****


"Baba Robinson yaani Leo mwanetu katuletea neema hapa acha kabisa yaani toto tulizaaa."


"Mbona sikuelewi mke wangu kuna nini tena kuhusiana na hiyo neema?"


"Leo nikiwa nawaza hili na hili juu ya nini tutapika jioni hii, mara Robinson huyo kaongozana na mgeni wake, mgeni mwenyewe toto, toto kweli baba Robinson sijui walikitana wapi huko mimi nikajua ni mkwe wangu kumbe la hasha ni mtoto wa mzee wa kule juu uwanja wa ndege kwa mzee Fikirini."


"Mzee Fikirini, mtoto gani mbona huyu Shamimu bado anasoma hapa hapa Lupa ni nani huyo?"


"Mhh, we Robinson yule binti uliyekuja nae jina lake nani?"


"Anaitwa Jackline mama."


"Basi huyo ni mgeni wao tu kutoka mjini huko." Aliongea mzee Kaaya.


"Inawezekana lakini yote kwa yote mume wangu alichotufanyia yule binti acha tu mimi minoti, mwanao minoti yaani wiki hii ni mwendo wa kunikia msosi wa maana."


"Pendeni vya bure na mwanao angalieni mtaolewa ooh." Maneno ya mzee Kaaya.


"Yule si mwanamke? atatuoaje mimi na mwanangu labda mwanao Robinson. Na mwanangu ukifanikiwa kuwa na yule binti Hatareee tutanuka minoti na mihogo atabaki analima baba yako sisi wengine tunabadili magari tu."


"Wee nani alime mihogo peke yake na mimi si nitahama kutoka komoni mpaka bia."


Hizo zilikuwa ni tambo za Hawa wazazi wa Robinson iwapo angebahatika kuoana na Jackline na hatujui iwapo hilo litatokea kwenye hizi familia mbili.


****


Shamimu alikuwa na furaha kubwa wikendi hii baada ya dada yake kumbeba ndani ya gari yake na Kuelekea mjini Makongolosi kwa ajili ya kwenda kufanya manunuzi, wakiwa sheli ya mafuta wanajaza mafuta akatokea Robinson akiwa na rafiki yake kuja kununua petrol ya bodaboda ya rafiki huyo Awadh tayari kwa safari Kuelekea Mpirani Isangawana.


"Robby."


Robinson aligeuka kuangalia sauti ilitokea wapi lakini alipoangalia pembeni akawa ameifahamu ile gari, akakumbuka siku moja iliyopita gari ile aliipanda. Akiwa bado anaendelea kuishangaa ndipo mlango wa gari ile ulifunguliwa na msichana aliyechanua vilivyo akashuka na kuwafuata pale walipokuwa wamesimama.


"Mambo Robby!"


"Poa Jackline, hivi hapa nilikuwa naangalia anayeniita ni nani?"


"Ni mimi bwana."


"OK, kutana na rafiki yangu Awadh."


"Mambo Awadh, na ninafurahi kukufahamu."


"Awadh, huyu ni rafiki yangu anaitwa Jackline nimekutana naye jana kule Kaea baada ya gari yake kukata Wese."


"OK, Jackline karibu sana Lupa."


"Nishafika Awadh."


"Wapi sasa Jackline muda huu."


"Na ndo maana nimekufuata nilipokuona hapa, naelekea Makongolosi niko na mdogo wangu Shamimu lakini Njia yeye anadai haifahamu vizuri unaonaje ukaungana nasi kwenye hii safari utupe kampani!" Aliomba Jackline.


"Mbona sisi tun.......!"


"Mbona nini si umsindikize Jackline bwana kwani kule unakwenda kucheza wewe, mpira tuachie sisi Robby." Awadh alimkatisha Robinson.


Hakuwa na jinsi zaidi ya kumkubalia Jackline ombi lake lakini kwa sharti la kwenda kwanza nyumbani kwao akaombe ruhusa. Hilo halikuwa Shida sana kwa Jackline alikubali

na kuingia kwenye usukani na kugeuza gari Kuelekea maeneo ya misheni ya Lupa kwa nyuma ambako ndiyo nyumbani kwa kina Robinson.

Kutokana na hili Awadh Ilibidi aondoke peke yake Kuelekea mpirani.


"Sijaamini kama baba anaweza kuniruhusu kirahisi rahisi namna ile maana wazazi wangu ni watata balaa." Aliongea Robinson.


"Wanakupenda na ndiyo maana wanakuchunga sana, na hii imekufanya kuwa kivutio kwa kila mzazi pale kijijini."


"Kivutio namna gani Jack."


"Si ni upole na utulivu ulionao bwana. Kila mzazi anakusifia kwa hilo."


"Sasa ushaanza kuwa muongo, wewe umefika jana tu umeyajuaje haya?"


"Tukiwa njiani tukitokea nyumbani kuna sehemu ina kiduka tukiwa pale niliwasikia wazee fulani wakikujadili."


"Hata mimi niliwasikia dada, halafu wao wanadhani wewe dada ni mke wa Robinson." Aliongeza Shamimu.


"Mhhh." Robinson aliguna tu.


"Vipi Robby mbona unaguna kwani uongo mimi siyo mke wako?"


"Nitaanzia wapi mtoto wa mzee Kaaya na umaskini wetu."


"Usiseme hivyo Robby huwezi jua Mungu kaandaa nini mbele yako."


Safari iliendelea kuwa nzuri ndani ya hii gari ambayo tayari ilikuwa inaichungulia Makongolosi na safari ilikuwa fupi kutokana na utani wa hapa na pale na hapa ndipo Jackline alipogundua kuwa Robinson ni muongeaji sana.

Na kimoyomoyo akajisemea mwenyewe.


"Lazima nitampata tu Robinson."


Safari yao ikaishia nje ya geti la Hotel maarufu mjini Makongolosi inayojulikana kama PM HOTEL na kupaki gari nje ya hotel hiyo na kutelemka.

Waliposhuka aliwaongoza Robinson na Shamimu Kuelekea ndani ya hotel hiyo kutokana na ugeni uliokuwa umejionesha mbele yake. Wakaongoza mpaka kwenye moja ya mwamvuli na kukaa.

Mhudumu mmoja wa hotel hiyo aliwafuata wateja wake.


"Habari zenu, naitwa Magreth ni Mhudumu ndani ya hotel hii. Karibuni niwahudumie." Aliongea hayo na kuonesha kitambulisho chake kisha akawakabidhi menyu.


"Ok, tunashukuru kwa utambulisho wako ngoja tuipitie menyu hii kisha tutakuita dada eee." Jackline alimjibu.


Wakati hayo yote yakiendelea upande wa Robinson na Shamimu ilikuwa ni giza totoro hawakujua chochote kilichokuwa kikiendelea pale.


"Hii karatasi ina huduma zote zinazopatikana hapa kuanzia Chakula mpaka kulala, hivyo kila mmoja aangalie kinachomfaa kuweka tumboni."

Aliongea Jackline akimkabidhi Robinson ile menyu.


"Vitu vya wazungu hivi mimi sijavizoea hata kidogo, mimi naomba waniletee Wali maharage." Alijibu Robinson.


" Dada si uagize tu chochote kinachotufaa hapa badala ya haya makaratasi. "

Majibu ya Shamimu yaliwafanya wote waangue kicheko.


" Ni kweli kabisa Shamimu." Alijazia Robinson.


"Acheni hizo nyie chagueni vyakula ohh." Jackline aliongea akisimama na kumfuata Magreth.


Huku nyuma Shamimu na Robinson waliendelea kuchekana kutokana na kushindwa kuagiza vyakula walivyoambiwa waagize.


"Mbona hata wewe umechemka bwana usinishushue hapa." Shamimu alimwambia Robinson.


"Mimi hata Sekondari sijagusa ni kweli nina kaushamba, sasa wewe mwenzangu msomi kabisa." Alisema Robinson.


"Bwana ee kwenye misosi hakuna cha usomi wala nini, wote hollaaaaa."


"Ila dogo tumetia aibu balaa." Aliongea Robinson.


"Bwana eee." Maneno ya Shamimu.


"Halafu nimekumbuka, hebu weka namba yako ya simu hapa kwenye kimeo changu." Aliongea Robinson.


"Mambo ya namba yameanza hapa Mhhh usiharibu hali ya hewa Robby."


"Usihofu ni kwa ajili ya kuchati tu."


"Maana nikimuangalia dada ni kama tayari kakufia kifuani tayari."


"Acha hizo amekuambia?"


"Dalili zinaonekana tu."


Shamimu alirudisha simu haraka baada ya kumuona dada yake anarejea kuungana nao pale mezani.

Muda mfupi Magreth alifika akiwa na kuku watatu waliookwa vizuri na chupa kubwa ya soda aina ya koka kola. Hali ile iliwaacha macho kodo Robinson na Shamimu.


" Mbona mnashangaa si mlinipa kazi, kazi kwenu kuendeleza umafya kwenye hao kuku."

Aliongea Jackline.


"Kwa kweli, umetuweza na sisi ngoja tukuoneshe kazi ya mdomo." Aliweka utani Shamimu.


"Jamani baada ya kula tutaelekea kule madukani kila mmoja akang'ae kimjini mjini mnasemaje?"

Aliuliza Jackline.


"Si la kuuliza hilo dada." Alijibu Shamimu.


"Mimi mtanikuta hapa hapa naangalia televisheni." Aliongea Robinson.


"Kwa ajili ya nini, utanikwaza Robby.Hii safari tuko wangapi?"


"Robinson acha kumkwaza dada ndo nini sasa si ungebaki Lupa." Aliongea Shamimu kuonesha nae kutofurahishwa na kauli ya Robinson.


"Naombeni mnisamehe kama nimewakwaza jamani."


"Ok, ila siyo vizuri kujitenga tenga wakati tumekuja Pamoja."

Aliongea Jackline akionekana kukubali kumsamehe Robinson.


Waliendelea kukishambulia Chakula kile huku Robinson akiwa anawachekesha pale mezani.


"Niwe mkweli tu, toka kuzaliwa kwangu mwenzenu sikuwahi kula mkuku mzima kama leo da Asante sana mgeni kwa kuja."


Wote waliangua kicheko mpaka kupelekea Shamimu kupaliwa na soda iliyohama njia na kutokea puani.


"Robinson utasababisha Matatizo hapa bwana aaa." Aliongea Jackline.


"Hata yeye Shamimu kashindwa kuongea tu ni mwenzangu tu na ndiyo maana kakutwa na tukio hilo."

Aliongeza Robinson.


Kauli ile ya Robinson ilimkwaza sana Shamimu na kuondoka kwa hasira akitoka nje ya hotel.


"Unaona sasa maneno yako Robinson."


"Naomba mnisamehe jamani ilikuwa ni utani tu na sikujua kama nitamkwaza mtu." Alijitetea Robinson.


Aliinuka Robinson na kumfukuzia Shamimu kule nje na kumkuta akiwa katulia kwenye viunga vya nje. Alimsogelea na kumuomba msamaha.


*******


"Pole na yote mke wangu kuanzia msibani na njiani pia." Aliongea Mzee Fikirini


"Asante sana mume wangu, namshukuru Mungu tumesafiri salama mpaka kufika salama." Alijibu mama Shamimu.


"Ni jambo la kumshukuru Mungu mke wangu."


"Ni kweli kabisa."


Mzee Fikirini alimsimulia mke wake ujio wa mtoto wa marehemu kaka yake Jackline. Na kueleza namna alivyokuwa mkubwa.


"Unasema kweli mume wangu kuwa Jackline kaja??"


"Amini sasa kaja na mimi nilishikwa na mshangao kama wewe mke wangu."


"Kama ndoto Vile jamani."


"Kafika hapa na gari lake mizawadi kibao iko jikoni huko yaani ndani ya muda mfupi tumekuwa wengine kabisa."


"Kaja na gari?"


"Basi ana mihela huyo Jackline ee."


"Unashangaa gari wakati mwenzako alikuwa anaishi Afrika ya Kusini wee."


"Haa, ndio kile kipindi ulichokuwa humpati kwenye simu na kwanini mzee Jonathan alikuficha."


"Tuache hayo kikubwa amerudi nyumbani."


"Yuko wapi sasa."


"Wameelekea Makongolosi na mdogo wake kuna vitu amefuatilia huko sijui vitu gani hivyo."


"Waangalie wasijeibiwa gari lao."


"Hawawezi bwana."


Mama Shamimu aliingia jikoni kwa ajili ya maandalizi ya Chakula cha jioni. Alipofika huko jikoni vitu alivyokutana navyo hakuamini macho yake kwani baada ya kukuta mchele, Viazi, Ndizi, sukari, Chumvi, mafuta ya kupikia na vingine vingi.


" We baba Shamimu mavitu yooote haya si tutafungua duka sisi."


"Unashangaa hivyo njoo uchukue begi lako la manguo."


Alipokabidhiwa lile begi la nguo alipigwa na mshangao kwa alichokutana nacho ndani yake maana kulikuwa na kila aina ya nguo ya mwanamke kuanzia za ndani na hata nyingine nyingi kama Vile vitenge, kanga na Waksi za kutosha hakika ilikuwa furaha ndani ya nyumba hii.


Tukutane katika sehemu ifuatayo kujua kilichotokea.



"We baba Shamimu nakuomba huku ndani mara moja."


"Nakuja mke wangu ngoja niondoe gogo hili njiani."


"Utaliondoa tu mume si mazungumzo marefu sana bwana."


"Ok, nambie mke wangu."


"Mhhh, mzee Fikirini utasimameje mlangoni utafikiri unafukuzwa ingia bwana uketi kitako hapa kwenye kiti."


"Haya bwana nishaketi hivyo, lete nongwa."


"Wala si nongwa bwana bali ni mazungumzo juu ya huyu mtoto wetu wa kumlea Jackline."


"Enhee, kafanya nini tena Jackline?"


"Nisikilize basi mbona unamshawasha mapema hivyo."


"Haya endelea mke wangu."


"Kama unavyojua mume wangu maisha yetu yalivyo na umaskini huu...."


"Ndiyo najua mke wangu."


"Nikiangalia naona kabisa mwisho wa tabu umefika ni muda wa kuponda raha sasa, si unakumbuka dokomendi za Mali ya marehemu kaka yako mzee Joachim unazo wewe na zilikuwa zinamngoja mwanae Jackline akue ndipo umkabidhi nyaraka zote na utajiri uwe mikononi mwake na sisi kubaki mafukara wa kutupwa mume wangu."


Maneno ya mke wake yaligonga ngoma za masikio yake mzee wa watu lakini ni kama hakujua mke wake alimaanisha nini kwa kauli ile na kujikuta akimuuliza swali.


"Unamaana gani mke wangu kwa maelezo hayo."


"Nina maana gani tena mume wangu? Chemsha kichwa hicho wewe ni mwanaume hodari sana nakumbuka miaka ile ulipokuwa ukinitafuta uliamua kumwaga damu ya Hassan aliyekuwa akishindana nawe kunitafuta mrembo mimi. Nitashangaa kwenye hii vita ya kitoto kama itakushinda."


"Unamaanisha kuitoa roho ya Jackline ili tubaki na Mali zote mke wangu?"


"Kumbe nini sasa, unamuonea huruma umemzaa yule? Waliyemzaa wanamsubiri huko waliko."


"Mmhh, mke wangu Jambo ni kubwa hebu nipe muda wa kulifikiria mara mbili."


"Nakupa siku mbili tu kila kitu kiwe saaafi, nimemaliza unaweza kwenda mimi niendelee na mapishi."


"Sawa mke wangu."


Maneno yale yalimtoa jasho hasa ukizingatia hakutegemea kuyasikia maneno kutoka kwenye kinywa cha mke wake. Hii ilimfanya alipofika nje alijikuta jasho jembamba likimtembea Mwilini mwake. Aligeuka na kumwangalia mke wake aliyekuwa bize jikoni akiendelea kuandaa Chakula huku karoho kake kakiwa kwatuu.


"Hivi mke wangu karogwa au kalishwa maneno mazito kama haya. Eti nimuue Jackline eti kisa mali mmhh kweli mbele ya pesa hakuna mwenye roho safi." Alijisemea mzee Fikirini.


Mzee Fikirini aliondoka na Kuelekea kilabuni angalau akapumzike kwa kuungana na wazee wenzake kwenye unywaji wa pombe ya asali wenyewe wakiita WANZUKI, pombe iliyotengenezwa kwa kutumia asali ya nyuki wakubwa au Sukari na kwa wenyeji wa eneo hili la Lupa na viunga vyake wanaipenda sana pombe hii ambayo huhifadhiwa ndani ya chupa za soda.


******************


Baada ya kufanya manunuzi ya nguo zao ndani ya maduka ya nguo Makongolosi walirudi kwenye gari lao pale PM HOTEL na kuziweka ndani gari. Hakika hii ilikuwa ni siku nzuri sana kwa Robinson na Shamimu kwa shopping ya NGUVU waliyofanyiwa na Jackline ambaye muda wote alikuwa akichati na simu yake janja.

Watu waliokuwa wanawafuatilia walibaki kuwashangaa kwa namna walivyokuwa wakifanya matanuzi, na mbaya zaidi hawakujua hawa vijana wametokea wapi.


"Mengo umewaona watoto hao?" Alijikuta kijana mmoja akiropoka.


"Aise lile jamaa sijui linawamiliki hawa watoto? Kama ni wake zake daa mshikaji namuonea wivu sana maana warembo wameumbika Hatareee." Alijazia Mengo.


"Hebu mcheki yule twiga alivyofungasha, mtoto mkali yule daa mimi mpaka natamani niwateke wote." Aliongea yule kijana.


"Halafu mbona sura zao ni ngeni hapa mjini, wametokea wapi?" Aliuliza Mengo.


"Warembo wa taipu hizi hutokea sana Mkwajuni si unajua kule ni kiwanda cha kutengenezea watoto wazuri." Aliendelea kuwasifia yule kijana.


Walipohakikisha kila kitu kiko Sawa waliingia ndani ya gari tayari kwa kuianza safari ya Kuelekea Lupa. Jackline alikaa nyuma ya usukani na kuuzungusha na kuigeuza kwa kasi ikatimua vumbi jingi na kusimama kama mita tano mbele.


"Wee, weee fyuuuuuu bado hawajaona dada rudia tenaaaaaaa wakuoneeeee." Zilikuwa ni kelele na ndulu za Muosha magari pale nje ya hoteli.


"Huyu binti ni mwathirika nini? Vurugu gani hizi hajui haya ni mavyuma tu hayazoweleki." Aliongea bibi mmoja aliyekuwa akipita eneo na mzigo wake wa kuni kichwani.


"Bibiii hao ndo watoto wa mjini, enzi zenu mambo kama hayo hayakuwepo." Alimjibu kijana mmoja mshona viatu karibu na kontena la mtandao wa simu wa airtel.


Baada ya kulizungusha na kusababisha kelele na vumbi kubwa ajabu Jackline alishuka na kuelekea kwenye lile kontena na kupanda ngazi na kuzama ndani yake.


" Habari yako dada!"


"Safi, karibu dada."


"Asante, nipatie hizo Sumsung S 14 Naomba hiyo ya silver na hiyo nyeusi."


"OK, ngoja nikuchukulie huku stoo."


"Fanya haraka nina safari ndefu Ndugu yangu."


"Bila shaka."


Mhudumu aliingia kuzichukua zile simu stoo ambako huzihifadhi huko kwa kuhofia wizi, japo kuna nyepesi nyepesi zinasema hiyo ni njia ya kukwepa mapato.


"Hizi hapa dada."


"Kiasi gani kwa zote."


"Zikague kwanza ili kujiridhisha."


"Dada ee hujiamini, nikiona zimezingua si nitakurudishia?"


"Ilikuwa ni ushauri tu dada."


"Ondoa shaka."


"Kwa zote utanipa shilingi milioni moja kwa maana ya shilingi laki tano kwa kila moja dada."


Jackline anaonekana kutawaliwa na Uzungu zaidi, nafikiri kuishi kwa muda mrefu Afrika Kusini kumemfanya kuyaishi maisha ya WAZUNGU kwani kiasi alichotajiwa hakubisha hata kidogo zaidi ya kutoa kitita hicho kutoka kwenye pochi yake na kumlipa. Hapa angekuwa Mbongo ninayemfahamu mimi angelia kwenye bei na muuzaji mpaka wangeishia kwenye shilingi laki nane kwa zote. Kitendo hiki kilimfanya huyu dada muuzaji wa simu kutoamini Macho yake, kwani toka aajiriwe kwenye duka hilo miaka miwili iliyopita ndiyo mteja wa kwanza kutobishia bei.


"Kazi njema."


"Asante sana dada, karibu sana wakati mwingine."


"Nashukuru sana."


Alishuka ngazi haraka haraka na kuvuka barabara na kulifuata HONDA JET5 lake gari la kifahari ambalo ukiliangalia kwa juu juu waweza Sema ni gari la kawaida sana lakini huwezi amini thamani ya gari hili ni shilingi za kibongo milioni tisini na tano (95ml).

Gari ambalo Jackline alilinunua nchini Afrika Kusini wakati akiwa huko masomoni.


"Robinson, zawadi yako hii hapa nadhani kuhusu kuitumia unajua. Na wewe Shamimu ya kwako hii hapa, hapa ni mwendo wa kuchati kila mmoja."


"Ooough My God, Jackline umeninunulia simu ya gharama hivi! Nitakulipa nini kwa wema wako huu."


"Lazima uwaze hivyo Robinson, lakini kumbuka kuwa bila wewe siku ile ningeumbuka pale baada ya gari kuishiwa mafuta."


"Sina neno jingine zaidi ya asante. Nashukuru sana."


"Bila shaka Robinson."


"Dada Jack nashukuru kwa kuninunulia simu hili nadhani Shuleni watapata tabu sasa dude kama hili hakuna anayemiliki kuanzia Shuleni mpaka mtaani zaidi yetu sisi. Asante sana dada."


"Shamy wewe ni mdogo wangu ni wajibu wangu kukupa furaha."


"Shemeji tutawakimbiza pale Lupa kwa misimu hii mpaka waturoge." Shamimu alimnong'oneza Robinson aliyekaa kiti cha mbele na Jackline.


"Umeanza maneno yako Shamimu." Alimjibu huku akitabasamu, tabasamu hili nadhani lilikuwa linaashiria Jambo kuwa ikitokea zali analiachaje.


"Shamy unasemaje hapo?" Aliuliza Jackline aliyeshtukia mchezo.


"Hamna kitu dada."


"Mhh, haya bwana siwawezi kwa vituko vyenu."


Muda huu maongezi yanaendelea gari hili aina ya HONDA JET5 lenye muonekano maridhawa kama wa Harrier Mayai lilikuwa linahamisha vumbi kutoka barabarani na kulitupa nyuma na pembeni maeneo ya kijiji cha Upendo huku muziki ukiendelea kuburudisha ngoma zao za masikio na alikuwa si mwingine zaidi ya msanii wa nyimbo za Injili aitwaye Magreth Magenda akiimba wimbo wake wa NASHUKURU MUNGU.


"Dada nikwambie kitu."


"Niambie mdogo wangu mwenyewe."


"Na sisi siku moja moja uwe unatufundisha gari."


"Hilo tu, labda kama kuna jingine."


"Lingine lipo."


"Lipi hilo Shamimu."


"Natamani siku moja Robinson awe Shemeji yangu maana hapo mbele mmependeza sana."


"Jackline aligeuka akamtazama Robinson kisha Shamimu, akaishia kumtupia swali Robinson."


"Robinson unamsikia Shamimu anachokiwaza."


"Aaa nimemzoea kwa sasa Shamimu na maneno yake." Alijibu Robinson ambaye kiuhalisia kimoyo kilikuwa si chake.


"Mdogo wangu nakushukuru kwa ushauri wako lakini zingatia Masomo haya mengine waachie Wajuvi wa mambo." Alijibu Jackline ambaye kiuhalisia kwa Robinson katua anashindwa aanzie wapi hivyo kwa maneno ya mdogo wake anashukuru amepata pa kuanzia.


Mpaka muda huo miguu ya Jackline ilikuwa ikipishana kwenye peda za breki na moto maeneo ya Mamba 'A' kilometa chache kuikaribia Lupa.


Nini kitaendelea,

Tukutane sehemu ijayo




Honda jet5 lilitia nanga yake nyumbani kwa akina Robinson na wakashuka garini, wakati Robinson na Shamimu wakishusha mizigo garini yeye Jackline aliongoza mpaka kwa mama Robinson na kumkumbatia hali iliyosababisha mama huyu kushindwa la kufanya lakini ilibidi naye afanye hivyo hivyo japo kwa uoga, hebu fikiria kwa familia ya kimaskini na inayoishi kijijini kukumbana na mtoto kutoka kwenye familia ya kitajiri inakuwaje, na ndiyo maana walijaribu kumkanya mtoto wao Robinson kuacha kuambatana na binti huyo asije waletea Matatizo lakini mwisho wa siku binti huyo (Jackline) hakuacha kufika nyumbani hapo na kumuomba Robinson na tendo hilo huwafanya wazazi hawa kumkubalia tu kwa shingo upande.


"Mama samahani kwa kuchelewa kurudi ilitubidi tulale kutokana na giza lililotukuta tukiwa bado Makongolosi." Aliomba msamaha Jackline.


"Mwanangu ondoa shaka, japo tuliingia hofu juu ya hili lakini tukajipa Moyo kuwa ninyi ni watu wazima. Nimewasamehe kabisa." Unafikiri mama wa watu angejibu nini mbele ya binti Tajiri.


"Halafu mama naomba mnichukulie kama mwanenu na mimi, kwani najisikia faraja sana nikiwa na Robinson." Aliongeza Jackline.


"Mmhh, vipi kuhusu mzee Fikirini atatufikiriaje sisi kama lilivyo jina lake maana ni korofi yule mzee!!"


"Kuhusu wazazi wangu niachieni mimi nitashughulika nalo."


Wakati wakizungumza hayo tayari Shamimu alikuwa karibu na dada yake na alisikia kila kitu pale huku Robinson akiwa kaegemea mlango asijue ni nini kinaongelewa pale na moja kwa moja akajua Jackline anamchongea kwa mama yake juu ya mtafaruku ambao ulijitokeza kati yake na Shamimu kule Makongolosi.

Alitamani asogee pale ili akaombe msamaha lakini hakujua anatumia njia gani.


"Robinson siye tunakwenda, bye bye." Aliongea Jackline akimpungia Mkono.


"We mama si uwaandalie Chakula wageni mbona wanaondoka na njaa." Robinson alimwambia mama yake.


"Kweli wanangu, tupike kwanza mle ndiyo muondoke mnaharaka gani ilhali na Chuma mnacho?"


"Mama tunashukuru sana, siku nyingine tutakula itakuwa ni siku maalum ya kuja hapa."


"Karibuni sana lakini na leo pia mngekula wanangu jamani."


"Mama sisi hapa ni nyumbani muda wowote na wakati wowote tunakuja bila wasiwasi tunaomba uturuhusu tuende." Shamimu aliongea baada ya kuona ngonjera zimezidi.


"Karibuni sana japo mmekataa kula Chakula, ila mkifika nifikishieni salamu zangu kwa wazazi." Mama Robinson aliwaaga Jackline na Shamimu ambao waliingia garini na kuondoka.


"Wee mwanangu hebu njoo huku ndani hivi unajua hatukuelewi na hawa mabinti?"


"Kuhusu nini mama?"


"Kuhusu nini, hujui mmetoka wapi na toka lini mlipokwenda huko shauri yako si unamfahamu yule mzee Fikirini lakini."


"Mamaaa, unachofikiria walaaa sisi ni marafiki tu na kama ujuavyo mimi ndo mtu wa kwanza kufahamiana naye."


"Pamoja na hayo shauri yako, baba yako jana kawaka hapa balaa, nikakusaidia."


"Na mimi nilijua kuna jembe huku nyuma na ndiyo maana sikuwa na wasiwasi wowote ule, kwanza njoo uone vitu huku mama."


"Vitu gani hivyo, Umeona utumie gia zako kupoteza lengo, haya tuone hivyo vitu."


"Yaani mama mpaka nashindwa kumuelewa Jackline, kwanza pale alikuwa anakuambia nini?"


"Mambo ya wanawake wayatakia nini wewe mtoto wa kiume?"


"Mmhh, haya nimeacha. Angalia mambo aliyonifanyia Jackline, cheki simu hii ya bei mbaya Lupa nzima hakuna ni mimi na mdogo wake Shamy tu inauzwa laki tano mama, cheki hii saa umewahi iona wapi, hapo sijagusa pamba zenyewe humo Hatareee na lazima waturoge mwaka huu japo lambalamba walipita. Haya chukua mfuko huu una vitu vyenu na mume wako."


"Wee Robinson wewe utasababisha tufe kabla ya muda wetu. Simu ya laki tano kweli si ungemwambia akununulie ya shilingi elfu thelasini Halafu iyo nyingine ungetuletea tununulie mahindi hapa nyumbani."


"Mama chakupewa hakina maswali, wewe chukua weka mfukoni mengine yafuate."


"Ila mwanangu huyu mwanamke anakupenda si bure kabisa haiwezekani mavitu yote haya gharama yake shilingi ngapi?"


"Haiwezekani anipende mimi mtoto wa fukara mzee Kaaya."


"Na uzuri ni mzuri mwanangu unawakimbiza mtaani na ndiyo maana mtoto wa tajiri katua mwenyewe kwenye kidonda cha fukara, chezea kazi ambayo tuliifanya na baba yako?"


"Mara aah mara eeh familia gani choka mbaya ile, wana nini wale. Wananiita mpaka majina mabaya mimi eti Robinson Marapurapu. Sasa wataniita Robinson handsome chezea."


"Sasa mwanangu tuachane na hayo watajibeba wenyewe hawajui kila mchuma janga hula na wa kwao acha tule vitu vya Jackline siye ila angalia mwanangu utaolewa wewe."


"Mama, mimi kidume naolewa vipi kumbuka natokea bara si wa Mombasa mimi oohh."


Wakati wakiendelea na majigambo yao mara alifika jirani yao mama Kaundime na hii ni baada ya kuona lile gari likitokea pale na hiyo haikuwa mara moja kuliona.


"Jirani hodi, hodi."


"Karibu, karibu."


"Asante jamani, habari ya hapa."


"Robinson mbona hatuambizani kama umeoa?"


"Nimeoa toka lini mama yangu? Mbona unaniletea mikosi ya ajabu hivi."


"Mwanangu hajaoa, ila najua udenda umekutoka ulipoliona gari lile likitoka hapa, yule ni rafiki yake tu."


"Mhh makubwa marafiki wa jinsi mbili tofauti, inawezekana?"


Mambo ya kijijini wao hawaamini kuwa mtoto wa kike na wa kiume wanaweza kuwa marafiki zaidi ya kuwa na mahusiano. Ukaribu wa Robinson na Jackline uliendelea kuwa gumzo mtaani mpaka Watu wakaanza kumuonea wivu Robinson.


" Umetoa mimacho ya nini, wewe si ulisema huwezi kuolewa na mtu kama Robinson sasa nini?"


"Yaani mama we acha tu, Robinson kawa handsome utafikiri kazaliwa leo. Na nimeamini usimdharau mtu chini ya jua."


"Yamekushuka, shuuuuu mwanangu."


Yalikuwa ni mazungumzo kati ya Mwahija na Mama yake. Mwahija ni miongoni mwa wasichana ambao walimtolea maneno mbofu mbofu Robinson alipokuwa akitafuta fursa kwao.


************


Mzee Fikirini alijaa kwenye mawazo ya mke wake ambapo mwanzo alionekana kutoungana naye kwenye wazo lake la kupora Mali za marehemu shemeji yake ambazo kwa sasa walitakiwa kumkabidhi Jackline ambaye alikuwa amekuwa.

Mzee Fikirini aliamua kumuweka sawa Jackline ambaye usiku wa siku aliyotoka Makongolosi alimueleza kuwa nyaraka zote za usimamizi wa Mali za baba yake alikuwa nazo na alimkabidhi usiku ule ule, lakini akaenda mbali zaidi kwa kumwambia Jackline kuwa kutokana na ugeni wake kusimamia mali hizo ilibidi aombe msaada kwa rafiki wa marehemu Ndugu yake mzee Jonathan ambaye ni mlezi wa Jackline kwa kipindi chote hicho kuanzia utoto wake mpaka sasa.

Na suala ambalo lilikuwa mbele yake ilikuwa ni Kuelekea mjini Tabora kwa mzee Jonathan kwa ajili ya kumkabidhi rasmi ofisi Jackline ili azisimamie vizuri biashara zake.

Jackline aliwashukuru sana walezi wake kwa kulitambua hilo japo alionyesha masikitiko yake juu ya mlezi wake mzee Jonathan ambaye kwa kipindi chote hicho hakuwahi kumwambia kama mali alizonazo ndani yake zipo zao.

Akakumbuka siku aliyohitimu chuo alimweleza mzee huyo juu ya mipango yote ya safari yake itakavyokuwa.

Lakini cha ajabu anasema siku moja kabla ya safari yake mzee Jonathan alimpigia simu na kumweleza kuwa amepata dharura yeye na familia yake wanaelekea nchini China watakuwa huko kwa Muda wa miaka miwili.


"Unafikiri mali hizi tutazipata mzee wangu?"


"Mhh, kwa hiyo unataka kuniambia mzee Jonathan hayupo nchini kwa sasa?"


"Ndiyo baba."


"Hapa tunakazi kubwa ya kufanya, maana naona kengele ya kutapeliwa inanigonga."


"Jackline, unachoongea una uhakika nacho kweli?"

Aliuliza mama Shamimu, mama wa mipango ambaye taarifa hizi zilimchoma Moyo moja kwa moja japo hakuna aliyejua zaidi ya bwana yake mzee Fikirini.


"Mama ni kweli kabisa, na hata namba zao za simu hazipatikani. Mimi nilijua wameamua kunifukuza kisomi na ndiyo maana kwenye ujumbe wa mwisho ulikuwa na namba ya simu ya kwako baba na ndiyo tukawa tunawasiliana mpaka nilipofika hapa."


"Mhh mbona naona giza mbele mimi jamani." Aliongea mzee Fikirini.


"Giza la nini mume wangu haya yote uliyasababisha wewe kwanini ulichukua jukumu la kumuamini mtu na kumkabidhi utajiri mtu huku sisi tukiendelea kula mlenda?"


"Mke wangu leo unaniruka kabisa."


"We ee ishia hapo hapo nikuruke kwa lipi ambalo tulipanga Pamoja?"


"Sawa tu lakini kufikia asubuhi nitawapa jawabu la utata huu na kila mtu atalifurahia


naomba tukapumzike. Jackline tutaangalia asubuhi tufanye nini lakini suluhisho nitakuja nalo."


Jackline aliitikia kwa kichwa kwani muda huo wote alikuwa akilia tu asijue afanye nini? Na lililokuwa likimpa tabu kwanini mzee ambaye alimuamini kwa kila kitu tena rafiki mkubwa wa marehemu baba yake mzee Joachim, na aliyechukua jukumu la kumsomesha kumbe alisomeshwa kwa fedha halali za baba yake. Pia akamfikiria mzee Fikirini kwa nini alimuamini mzee Jonathan?

Lakini baadaye akapata jibu ilikuwa ni uoga wa kusimamia mali ambazo hajawahi kuwa nazo.

Mpaka anakwenda Kulala Macho yalikuwa mekundu.


"Nasema haiwezekani, haiwezekani nitakutafuta popote duniani mzee wangu Jonathan." Alijikuta akiropoka kwa Sauti ambayo ilipenya moja kwa moja mpaka chumbani kwa mzee Fikirini ambaye alisikia maneno hayo.


***************


Usiku ulikuwa mrefu kwa mzee Fikirini ambaye aliwaza sana juu ya alichosikia kwa Jackline kama kina ukweli ndani yake. Na pia akamfikiria mzee Jonathan alichokifanya kama ni kweli kwa nini aliamua kuwafanyia hivyo lakini. Alienda mbali zaidi na kufikiria jinsi ambavyo alimwambia ile siku alipokuwa akimkabidhi miradi na kufikia kumuahidi kuwa angezisimamia kama zake. Na sasa alikuwa nchini China sehemu ambayo hafahamu iko wapi na Watu wake wakoje na wanaishije. Hili lilimuumiza sana kichwa Akakumbuka namna ambavyo mke wake alimshawishi wamuue Jackline ili warithi mali zile. Akawaza mwisho wa siku jamii itakwenda kumtazama vipi kwenye hili si watajua ameshiriki kuhujumu mali za binti yao Jackline.


"Itabidi nifanye Jambo kabla ya asubuhi ili kujiweka mbali na hili." Aliwaza mzee Fikirini..


Katikati ya usiku mzee aliingia chooni akakikagua vizuri akauona mwamba uko imara. Akaurudisha mlango na kuchukua kamba ya katani ambayo ilikuwa nje kwenye mti aliyokuwa akiitumia kufungia nguruwe akaifunga vizuri kwenye mwamba wa Choo kisha akatengeneza kitanzi na kukivaa shingoni.



Kwanini mzee Jonathan katorokea nchini China, je ni kweli yuko huko?


Na mzee Fikirini anavaa kitanzi kwa lengo la kufanya nini??


Tukutane sehemu ijayo.






Hamza na mkewe Bi Aisha walizunguka huku na kule kumtafuta Bi Elizabeth ambaye mpaka mchana huo jasho likiwa linawatoka hawakuweza kumpata. Hali hii iliwachanganya sana wanandoa hawa kwani mpaka wanakwenda kulala hakukuwa na mgongano wowote na Bi Elizabeth sasa walishindwa kujua ni kipi kilimsibu mpaka kuamua kuondoka bila kuaga.


"Mume wangu hivi hili suala litakuwaje maana mpaka sasa hakuna dalili yoyote ya kumpata Bi Elizabeth na mimi nishajichokea tayari."

Bi Aisha alimuuliza mumewe walipokuwa wameketi chini ya mti wa mwembe.


"Yaani mpaka kichwa kinaniuma mke wangu, mtu mzima kama yule anaamuaje kufanya mambo kienyeji kiasi hiki sisi ndiyo wenyeji wake pamoja na mapungufu yake tuliamua kumsaidia hivyo hivyo kumbe yeye ana yake kichwani."

Hamza aliongea hayo huku akiangaza eneo lile labda anaweza kumuona au mtu yeyote aweze kumuuliza.


" Unaonaje tuachane naye mume wangu muda wa kufungua genge umeenda sana walau tukaokote chochote kile."

Bi Aisha alimshauri mume wake waweze kurudi nyumbani kuendelea na mengine.


"Ni kweli kabisa mke wangu huyu kaondoka ana yake kichwani sisi tuko bize kumtafuta huku yetu yakilala, twenzetu."

Hamza aliungana na mke wake kwenye hoja ya kuondoka hivyo alisimama na kumuinua Bi Aisha kisha wakaanza kutembea mdogo mdogo kurudi nyumbani kwao. Walitembea mpaka walipofika kwenye kiduka cha vinywaji ambapo Hamza aliona apitie kununua maji kutokana na jua kuwawakia sana na hivyo kuhitaji kitulizo cha baridi.


"Habari mkubwa!"

Hamza alimsalimu muuza duka.


"Salama kaka, karibu."


"Asante niombe maji makubwa mawili na yawe ya baridi ee."

Hamza alimwambia muuza duka huku akitoa waleti yake mfukoni.

Na baada ya kupewa aliondoka na kuungana na mke wake aliyekuwa akimsubiri pale barabarani. Walitembea taratibu mpaka walipofika nyumbani kwao lakini kitu ambacho kiliwashtua ni kukuta geti liko wazi wakati wao walilifunga.


"Ina maana hatukulifunga geti tulipokuwa tunatoka asubuhi?"

Hamza aliuliza huku akichungia ndani kuona kuna kipi kipya.


"Hata mimi nashangaa kwani wewe ndiye uliyelifunga wakati huo mimi nilikuwa naongea na simu pale."

Bi Aisha alimjibu mume wake huku naye akitaka kuingia ndani kujua kuna nini lakini mume wake alimzuia kwanza huku yeye ndiye akiingia ndani na kumuacha mke wake nje, Bi Aisha hakuwa mbishi alitii uamzi wa mume wake kwani alijua maana yake ni nini. Hamza aliingia mpaka ndani ambako baada ya kufika karibu na nyumba alianza kunyata huku akizunguka upande wa nyuma.


"Kijana wangu kuna nini tena mbona unanyata kama mwizi wakati nyumba ni yako?"

Sauti hiyo ilimfanya Hamza kushindwa kuendelea na nyato zake badala yake aligeuka kujiridhisha kama masikio yake hayajamdanganya kuwa huyo ni nani.


"Bi Elizabeth kwanini umetufanyia hivyo lakini?"

Hamza alimuuliza Bi Elizabeth baada ya kugeuka na kumuona ni yeye.


"Awali ya yote naomba msamaha kwa kitendo nilichokifanya asubuhi lakini sikuwa na jinsi na pili kwa kitendo cha kufungua mlango kwa njia isiyo sahihi wakati ninyi hamkuwepo."

Bi Elizabeth aliomba radhi kwa Hamza.


"Kama ulijua sisi si msaada kwako kwanini umerudi tena au ndiyo umerudi na mambo yako?"

Bi Aisha alimtupia swali baada ya kuingia na kukuta mazungumzo yakiendelea na kuingilia kati kabla mume wake hajamjibu.


"Najua nilichokifanya hakikuwa sahihi na ndiyo maana nikaona nirudi wanangu."

Bi Elizabeth aliwaeleza huku akienda chini kama ishara ya msisitizo wa ushawishi kwenye msamaha wake.


"Mama hebu inuka huna haja ya kutupigia magoti sisi kikubwa umejua kosa lako na kulikiri inatosha."

Hamza alimwambia huku akimuinua kitu ambacho hata Bi Aisha naye hakuwa tayari kukiona kikitokea kwa mtu kama Bi Elizabeth kuwapigia magoti hivyo naye alikazia kumtaka ainuke wameshamsamehe, aliinuka kisha wote waliingia ndani huku Hamza akirudi getini kulifunga.


****


"Jembe langu nipe taarifa ya ufukunyuku wako."

Jackline alimwambia Roberto baada ya kuipokea simu yake.


"Nimefuatilia kwa kina Dada Jackline na nilichokibaini ni kuwa Bi Elizabeth yuko uraiani na aliyehusika na huu mchezo wa kuhakikisha anatoka ni Tajiri mmoja kutoka Afrika ya Kusini anaitwa MackDone."


"MackDone? Ni nani huyu mpaka kufanya hivyo kwa Bi Elizabeth?"

Jackline alishtuka baada kulisikia jina ambalo hakulitarajia kabisa kwenye ishu ya Bi Elizabeth.


"Inavyosemekana huyu ni mchepuko wa Bi Elizabeth tokea ujanani kwao walitakaga kuoana lakini familia ya MackDone haikuwa tayari kumuona Bi Elizabeth kwenye ukoo wao kutokana na historia ya familia yao kwani kwenye familia ya akina Elizabeth alitokea kaka yao mmoja ambaye alikuwa ni mtekaji nyara maarufu nchini Afrika ya Kusini hivyo hawakutaka mbegu hiyo waipate."

Roberto alifafanua zaidi undani wa Bi Elizabeth na MackDone.


" Sasa Roberto kama iko hivyo iweje achukue uamzi wa kumtoa?"

Jackline bado alitaka kujua zaidi.


" Inasemekana MackDone alifanya kwa siri hata Bi Elizabeth mwenyewe mpaka sasa hana jibu kamili ni nani aliyemtoa jela na MackDone kafanya hivyo kwa mapenzi yake akiamini kuwa kwa sasa anaweza kuishi naye kwani mke wake waliachana miaka mingi iliyopita."


"Vizuri sana Roberto nimeipenda hii hivyo tayari tuna sehemu ya kuanzia zoezi letu."

Jackline alifurahishwa na maelezo ya Roberto.


"Kwa hiyo wewe tulia chora ramani yako kisha utanijulisha Dada yangu."

Roberto alimuachia kazi Jackline.


"Wala usijali mdogo wangu si unanijua nikipaniaga kitu huwa sirudi nyuma hata kidogo."

Jackline alimjibu Roberto kisha akaikata simu na kuirudisha mfukoni na alipogeuka alikutana na mume wake Daktari Abbas akimsubiri.


"Ni nani huyo?"

Daktari Abbas alimuuliza mke wake.


"Ni Opareta wangu Roberto alikuwa akinijulisha mtu aliyehusika kumtoa Bi Elizabeth."

Jackline alimjibu mume wake huku wakiondoka Makambi Hospital kwa rafiki yao Daktari Hans Murray ambaye walimtembelea siku hii.


"Ni nani aliyemsaidia?"

Mume wake alitaka kumjua mtu huyo.


"Kaniambia kuwa ni mchumba wake wa ujanani aitwaye MackDone mfanyabiashara kutoka Afrika ya Kusini."


"Namfahamu vizuri sana huyo jamaa ni maarufu sana Kusini mwa jangwa la Sahara."

Daktari Abbas alimjulisha mke wake kuwa anamfahamu vizuri mtu huyo.

Hivyo hapo hapo Jackline alimtumia ujumbe Jasmine alimjulisha walipofikia mpaka sasa.


"Ni kweli yuko nje na aliyehusika ni mchepuko wake wa nchini kwao Afrika ya Kusini."

Na baada ya muda mfupi ujumbe huo ulijibiwa na Jasmine.


"Tuanze kumchunguza huyu MackDone na watu wake wa karibu pamoja na Bi Elizabeth mwenyewe na wanaomzunguka Unaonaje?"


Jackline alitabasamu baada ya kuusoma ujumbe wa Jasmine kisha aliujibu kwa ufupi.


"Bila shaka."

Baada ya hapo aliiweka simu yake kwenye dashboard ya gari kisha akamuuliza mume wake.


"Kituo wapi?"


"Tuelekee St. Petro Schools kujua suala la watoto wetu limefikia wapi ili ikiwezekana wiki ijayo waanze masomo."

Daktari Abbas alimjulisha mkewe.


"Yes, nilishasahau mume wangu."

Hivyo Jackline alichukua tena simu kutaka kumpigia mtu lakini alisita kidogo akaiacha simu na kuangalia kwenye 'site mirror' kuiangalia Bajaj waliyoipita.


"Punguza mwendo kidogo baba Natalie."

Alimwambia mume wake huku macho yakiwa kwenye 'site mirror' Daktari Abbas hakutaka kuhoji kwani alishaona akili ya mkewe iko wapi alienda na kulipaki Harrier lao pembeni. Kisha Jackline alishusha kioo kidogo na muda si mrefu Bajaj ile iliwapita.


" Mume wangu unaweza kuamini kuwa Bi Elizabeth yuko kwenye hii Bajaj sijui anaelekea wapi?"

Jackline alimuuliza mume wake.


"Sijamuona vizuri lakini unaonaje tukaifuatilia kwa mbali Bajaj hiyo tujue anaelekea wapi?"

Mume wake alitoa wazo.


"Fanya hivyo."

Jackline alimjibu mume wake huku akibonyeza simu yake bila shaka ikiwa ni kuwataarifu wenzake juu ya alichokiona. Na mume wake naye alimpigia simu Mahmoud kumjulisha kitu.


"Wapi hapo fundi wangu?"

Alimuuliza baada ya kuipokea simu yake.


"Niko maeneo yangu ya kazi hapa mjini."

Mahmoud alimjibu.


"Usikae mbali na simu nitakupigia baada ya dakika kadhaa kuna issue' mpya."


"Bila shaka bosi wangu muda wowote na wakati wowote kwa ajili yako."

Mahmoud alimjibu Daktari Abbas.


"Pamoja."

Daktari Abbas alimjibu naye na kisha kukata simu na kuendelea kuifukuzia Bajaj ile kwa umbali ambao hawawezi kuwashtukia.




Safari ya kuelekea St. Petro Schools kufuatilia nafasi ya watoto wao mapacha Nathan na Natalie ikafia njiani badala yake ilizaliwa safari mpya ya kuifuatilia Bajaj ambayo ilimbeba Bi Elizabeth huku wakiiacha mita kadhaa mbele yao ili wasishtukiwe. Waliendelea kuifuatilia Bajaj ile mpaka ilipoacha barabara kuu na kuingia barabara ya vumbi ambapo nao wakaingia huko huko, ile Bajaj ilipofika nje ya lango la kuingia soko kuu la Windhoek ilisimama na abiria waliokuwa ndani kushuka. Kwenye kundi lile na Bi Elizabeth alikuwa miongoni mwao.


"Uko wapi Mahmoud?"

Daktari Abbas alimtumia ujumbe kijana wake Mahmoud akiwa anashuka ambapo alimzuia mke wake ambaye alitaka kuwafuata kule ndani.


"Usiwe na haraka mke wangu huwezi jua anaelekea wapi, ngoja aje kichaa wangu ndiye atamfuatilia bila kumtilia shaka yoyote."


"Yuko wapi sasa mume wangu huyo Mahmoud? Huyu mwanamke si wa kumuachia nafasi namna hii?"

Jackline aliumia moyo pale aliposhikwa mkono na mume wake Daktari Abbas.


"Uko wapi mkuu?"

Mahmoud aliona asipoteze muda akampigia simu.


"Njoo moja kwa moja hapa Kwenye lango kuu la kuingia sokoni utanikuta sasa hivi."

Daktari Abbas kuonesha msisitizo alikuwa akiongea kwa vitendo huku mke wake akiwa kavimba kwa hasira kaegemea gari macho yakiwa getini.


"Dakika sifuri mkuu siko mbali na hapo."

Mahmoud alimjibu Daktari Abbas na kukata simu. Na kweli muda si mrefu akawa amewasili na taxi yake na kuipaki karibu na wakina Jackline.


"Shemeji tutasalimiana baadaye kazi kwanza."

Mahmoud alimwambia Jackline huku akimfuata Daktari Abbas ambaye alikuwa kaketi mlangoni huku mlango wa gari ukiwa wazi.

Lakini Jackline hakuongea kitu zaidi kutoa tabasamu feki kwa Mahmoud.


"Ramani tafadhari."

Alimwambia bosi wake amuelekeze njia ya kuelekea.


"Nguo zake ni sketi nyeusi na t-shirt ya blue huku nje akiwa kajitanda mtandio mweupe, kaingia ndani ya hilo geti."

Baada ya kupata maelekezo hayo kutoka kwa Daktari Abbas hakutaka kupoteza muda alilifuata lango lile la soko. Alipoingia mle ndani alianza kuangaza huku na kule kwa muda na ndipo alipomuona kaketi kwenye banda fulani la matunda huku kukiwa na mwanaume na mwanamke wakihudumia wateja waliokuwa wameizunguka meza yao. Na yeye akautumia mwanya huo huo kuweza kufanikisha uchunguzi wake.


"Kaka naomba ndizi za shilingi elfu mbili na maembe ya mia saba, nifungie kisha papai moja lioshe na nikatie vipande."

Mahmoud aliagiza huku macho yake yakiwa pale alipoketi Bi Elizabeth.


"Mfuko huu hapa na mapapai haya hapa karibu."

Hamza akiwa hana alijualo alimkaribisha Mahmoud aliyekuwa akicheza na sms muda huo.


"Shukrani kaka mkubwa, karibuni nanyi hili papai kubwa sana."


"Usijali sisi vitu kama hivyo ni sawa na maji nyumbani."

Hamza alimjibu Mahmoud huku akiendelea kuhudumia wateja wengine. Akiwa anaendelea kula papai ndipo sikio lake moja liliponasa mazungumzo ya Bi Elizabeth na mke wa Hamza.


"Unajua nini mwanangu?"

Bi Elizabeth alianza akiwa anaiweka soda yake chini.


"Ndiyo mama nakusikiliza."

Bi Aisha alimjibu.


"Kesho natakiwa kuwaacha nimeikumbuka nyumba yangu."


"Mbona haraka kiasi hicho mama yangu hapa ni kwako kwani ndani ya muda mfupi tumeshakuzoea."


"Wala msijali hapa nimeshapata ndugu zangu tena naweza kuwaita wanangu kabisa hivyo lazima kuja kuwatembelea."

Bi Elizabeth alimjibu Bi Aisha.

Ni katika mazungumzo hayo Mahmoud alipata kile alichokikusudia kisha alitoa hela kulipia mazaga yake na kuondoka. Moja kwa moja aliwafuata wakina Jackline pale nje na kuwapa mchoro ulivyo.


"Kawasisitizia kuwa kesho lazima aondoke kwenda kwake."

Mahmoud aliwapa taarifa hiyo.


"Moja kwa moja hiyo ni Namport hakuna sehemu nyingine."

Jackline alijibu huku akifungua mlango wa gari na kuingia.


"Kwa hiyo huyo kijana ni nani kwake?"

Daktari Abbas aliuliza.


"Sijajua ni nani labda ni ndugu yake tu."

Mahmoud alimjibu.


"Kazi iliyobakia ni kujua huyo kijana anaishi wapi?"

Daktari Abbas alitoa kazi nyingine kisha akaingia kwenye gari akawasha na kuondoka zake huku akimuacha Mahmoud akitegua kiti na kujilaza kuwasubiri wakina Hamza kujua wataelekea wapi.

Kwa kuwa muda ulikuwa umeenda hawakuweza kuelekea shuleni badala yake walirejea nyumbani kwani tayari kigiza kilishaanza. Njia nzima hakuna aliyemsemesha mwenzake na hii ilikuwa ni kwa upande wa Jackline ambaye alichukia kuzuiwa kuwafuatilia wakina Elizabeth.


"Mbona nakuona kama umechukia hivi mke wangu? Au kukuzuia pale imekuwa tatizo?"

Daktari Abbas alimuuliza mke wake baada ya kushindwa kujizuia.


" Wala sijachukia mume wangu ni uchovu tu ndiyo maana niko hivi."

Jackline alijibu huku akiiwasha simu yake ambayo aliizima kusevu chaji ambayo ilikuwa inaelekea ukingoni.


" Sikiliza mke wangu, kwa sasa nakufahamu vizuri sana. Ukiwa umefurahi nakujua, ukiwa umenuna nakujua pia. Kikubwa elewa kwa sasa wewe ni mke wa mtu hujiongozi kama zamani kila utakacho kukifanya lazima tushirikishane."

Daktari Abbas alimwambia mke wake ambaye hakujibu chochote zaidi ya kushuka garini baada ya kuwasili nyumbani na kuingia moja kwa moja ndani bila hata kumsubiri mume wake kama ilivyo kawaida yao, Daktari Abbas alimtazama tu mke wake kisha akatikisa kichwa chake na kufunga milango ya gari na yeye akaingia ndani.

Alipofika ndani aliwafuata watoto wake wapendwa Nathan na Natalie waliokuwa wakijisomea kwa mtindo wa kuulizana maswali.


"Mmeshindaje wanangu?"

Aliwasalimu.


"Tumeshinda salama baba, pole na majukumu."

Natalie alimjibu.


"Baba hujatuletea zawadi yoyote?"

Nathan alimuuliza baba yake.


"Kwa leo nilisahau wanangu naombeni mnisamehe lakini kesho nitawanunulia zawadi kubwa."

Alimjibu huku akiwakumbatia kwa pamoja.


"Halafu wewe baba unasemaga hivyo hivyo na hiyo kesho ikifika utatuletea sababu mpya."

Natalie aliona amwambie baba yake ukweli.


"Hawezi kusahau, akisahau tu nitamkumbusha."

Jackline alikuja na kuingilia mazungumzo ya baba na watoto na kisha kumtetea. Wakati Jackline akifanya utetezi ule kwa watoto mara simu ya Daktari Abbas iliita akaitoa na kuiangalia alipomjua mpigaji alipokea na kutoka nje.


" Nipe ripoti Mahmoud."

Daktari Abbas alianza baada ya kupokea.


"Mkuu nimewafuatilia hawa Wazalendo mpaka kwao kabisa yaani huwezi amini wala si mbali sana."

Alimpa majibu ya maswali aliyokuwa akiyatarajia.


"Bi Elizabeth alikuwa nao?"

Daktari Abbas alimuulizia mtu ambaye ni muhimu kwake.


"Walikuwa pamoja na inavyoonekana ni kama ndugu hivi."


"Nipe mpango juu yao.


" Niachie usiku wa leo, kesho nakupa majibu ya kunyooka Mkuu wangu."

Mahmoud alimjibu Daktari Abbas.


" Kazi kwako."

Daktari Abbas aliongea na kuikata simu kisha akarejea ndani.

Upande wa Jackline naye akiwa jikoni kufanya maandalizi ya chakula mara simu yake iliingia ujumbe kutoka kwa Roberto.


" TAYARI NIMESHAFANYA MAMBO YANGU HIVYO KUNA DOGO YUKO HAPO NAMIBIA NIMEMPA KAZI ATAKAYOIANZA KESHO, HIVYO JIANDAE KIKAZI ZAIDI."

Baada ya kuusoma ujumbe ule Jackline alifurahi sana kisha alimjibu.


"SINA NENO NA WEWE MDOGO WANGU PIGA KAZI MAISHA YASONGE." Kisha aliendelea na mapishi yake. Daktari Abbas alimfuata mkewe jikoni na kumuaga kuwa kapata dharura kazini.


"Kwa hiyo ni mpaka kesho? Na chakula je?"

Jackline alimtupia maswali mawili mfululizo mume wake aliyeshindwa aanze na lipi kulijibu.


"Bila shaka, na chakula utanisamehe maana gari limeshafika kutoka Namport. Na kweli kabla hajamaliza kuongea honi ya gari ilipigwa nje ya geti na kumfanya kutoka mkuku mkuku akimuacha Jackline kamtolea macho.

Hapo hapo Jackline aliwaandalia chakula watoto wake kisha yeye akaichukua laptop yake na kumcheki Roberto whatsApp.


"Enhh ikoje ramani mdogo wangu?"

Jackline alimtumia ujumbe kupitia whatsApp.


"Baada ya kupekuapekua kwenye makabrasha yangu nikabaini kuwa Bi Elizabeth hajaondoka bado Windhoek na kumhusu Mackdone ni kweli anaishi Afrika ya Kusini ni mfanyabiashara mkubwa sana lakini nimepata mwanya wa kumuingia kwenye mishe zake na hii itanifanya nianze safari keshokutwa kuelekea huko."

Roberto alitoa maelezo yaliyomfurahisha sana Jackline na ambaye hapo hapo aliingia kwenye group lao la whatsApp liitwalo 'UNFORGETTABLE' na kuandika 'Makamanda' mambo yakawa kama hivi.


" Kamili mkuu."

Roberto alimjibu.


" Kuna nini jamani usiku huu? "

Jasmine alijibu kwa swali naye.


"Kamili gado Suka wetu lete mambo."

Jessica alijibu huku akiambatanisha na picha yake akiwa anajisomea.


" Ndiyo kusema Jessica? "

Roberto alimuuliza Jessica.


"Niache kwanza Roberto nina kesi na wewe kwanza tumsikilize Kamanda wetu analipi jipya."

Jessica alimjibu Roberto.


"Hana jipya huyo kwa sasa kashikwa mbavu na Dokota mchezo."

Jasmine aliingilia huku akiunganishia na viimoji vya kucheka mpaka machozi.


"Hamna jamani si hivyo, nilitingwa tu na vimajukumu vya hapa na pale ila kwa sasa kila kitu kiko sawa, ila kuna jipya ambalo baadhi yetu tunalijua na kwa wale ambao hamjui chochote naomba Roberto atupe taarifa rasmi."

Jackline alijitetea na kisha kwenda kwenye jambo ambalo lilimfanya aingie kundini ambako salamu yao huwa ni MAKAMANDA.


" Asante kiongozi, jamani vita yetu ni kama inakwenda kurudi tena au kuanza upya, na Safari hii inaonekana si ya kawaida kwani mtu ambaye tulikuwa tunamshuku tayari katoka gerezani kwa njia isiyojulikana kwani kifungo chake hakikuwa cha kutoka leo au kesho."


"Ni nani huyo au Bi Elizabeth?"

Jessica aliuliza.


"Jessica hakuna mwingine ni huyo huyo, hivyo kazi tuliyonayo kwa sasa ni kumfuatilia yeye na watu wake wa karibu kujua kuna nini wanataka kufanya."

Roberto alihitimisha maelezo yake.


"Na kwa kujazia tu aliyehusika kumtoa jela ni mtu mmoja anayeitwa Mackdone hivyo kila mmoja aanze kumfuatilia hasa wewe mama lenyewe Jessica, lakini Roberto kaanza kwa nafasi yake na anatarajia kuelekea Afrika ya Kusini kumfuatilia."

Jackline alifafanua.


"Haina haja kwa Roberto kuelekea huko kwa sasa nipeni siku nne nitawapa majibu juu ya huyo mtu na vipi kumhusu Bi Elizabeth?"

Jessica aliwatuliza na kutaka wampe nafasi.


"Bi Elizabeth hatuna mawasiliano yake labda tutumie utundu kupata ya kijana aliyempokea."

Jackline alimjibu.


"Limekwisha hilo jamani au kuna jingine kesho mapema tukutane hapa mwenzenu leo nimetingwa kidogo na kikazi fulani hivi."

Jasmine aliona akatishe mjadala ule kwa kuwa yeye suala lile alikuwa analijua. Baada ya kuagana Jackline aliizima laptop yake na kuiweka sehemu yake na kuelekea mezani kwa chakula lakini kabla ya kukaa akakumbuka kuwa hajawatengenezea neti watoto wake ambao muda huo walikuwa wameshaingia vyumbani mwao kulala.




Waliwasili nyumbani salama kabisa na kushuka kwenye Bajaj ambayo iliwaleta kisha Hamza kumlipa dereva Bajaj hela kisha naye kuingia ndani na kufunga geti,alipohakikisha kafunga vizuri aliondoka na kuelekea ndani.


"Mume wangu kuna kosa tumelifanya."

Bi Aisha alimwambia mume wake baada ya kuingia tu ndani.


"Kosa gani hilo mke wangu?"

Hamza alimuuliza mke wake.


"Si tumesahau kupitisha huu mfuko kwa rafiki yako Yusuf tukiwa tunarudi."


"Ni kweli aisee na si yameiva hayo hasa hasa maembe, itakuwaje sasa?"

Hamza alimuuliza mke wake nini kifanyike maana Yusuf alisisitiza sana juu ya kifurushi hicho cha matunda. Lakini kabla Bi Aisha hajajibu lolote Bi Elizabeth alitoa wazo.


"Mnaonaje kama mkimpigia simu huyo rafiki yenu kujua kama yuko nyumbani ili apelekewe mzigo wake maana si usiku sana."


"Haina haja mama ngoja niupeleke tu mara moja, narudi sasa hivi."

Hamza hakuona sababu ya kuanza kumpigia simu Yusuf kwa ajili ya uzembe wao hivyo akaona njia pekee ni kukimbia mara moja. Alitoka nje na kumuacha Bi Elizabeth na mke wake Bi Aisha wakiwa wanaendelea na shughuli za mle ndani. Lakini huko nje wakati Hamza anatoka hakuwa anajua chochote kile kama kuna mtu anawawinda hivyo baada ya kutoka nje na kulifunga geti na kuondoka zake naye Mahmoud akiyekuwa kwenye ukuta kajibana akiangalia namna ya kuingia ndani na baada ya kuona geti likifunguliwa alijificha na kwa kuwa aliyekuwa anatoka hakuwa na habari naye ilimpa nafasi nzuri Mahmoud kuanza kumfuatilia kwa nyuma kujua anaelekea wapi muda huo.


"Nisamehe sana rafiki yangu tulipitiliza nao lakini baada ya kubaini hilo nimeona nisipoteze hata sekunde nikuletee."

Hamza alikuwa akiongea na simu huku akiongeza mwendo na ni kama alikuwa anaongea na mwenye ule mzigo alioubeba.


"Nimekuelewa bwana na hapa niko nje ya geti la nyumba yako."

Hamza aliendelea kujieleza kwenye simu kuashiria kuwa mwenye mzigo ule hakufurahishwa na kile kilichofanywa na Hamza, baada ya sekunde chache geti lilifunguliwa na Yusuf alitoka nje.


"Naomba uzembe kama huu usijirudie tena kwa wakati mwingine na iwapo utajirudia sitaona sababu ya kukuacha na kumtafuta mtu mwingine ambaye atakuwa anaujali muda."

Yusuf aliongea hayo kisha akachukua mzigo wake na kurudi ndani na mlango ukafungwa bila kusubiri utetezi wa Hamza. Hamza alisimama kwa muda pale nje bila kujua nini afanye akili nyingine ikamwambia amgongee kengele Yusuf amuombe msamaha na akanyoosha mkono kwenye kwenye swichi ya kengele lakini akaahirisha na kuondoka zake. Baada ya kuondoka tu huku nyuma Mahmoud aliongoza moja kwa moja mpaka getini kwa Yusuf na kuipiga kengele kisha akasubiri mrejesho na baada ya muda mfupi mlango mdogo wa geti ulifunguliwa.


"Nani mwenzangu."

Yusuf aliuliza baada ya kufungua mlango na kumkuta mtu mbele yake.


"Samahani kaka naitwa Muddy."

Mahmoud alijitambulisha kwa Yusuf.


"Muddy, ndiyo naomba nikusaidie."

Yusuf alimwambia Mahmoud.


"Shida yangu ni ndogo tu ndugu yangu sijui unaweza kunisaidia kidumu chochote kile nikanunulie mafuta hapo mbele nimekatikiwa nikiwa hapo kilimani."

Mahmoud alidanganya.


"Kidumu? Mafuta? Kaka kote huko ulikopita umeona hapa ndiyo kuna stoo ya madumu ya mafuta?"

Yusuf alimuwakia Mahmoud baada ya kuisikia sababu aliyoitoa.


"Kaka samahani kama nimekukosea naomba nisamehe lakini halikuwa kusudio langu."

Mahmoud aliona aombe msamaha baada ya kuona mwenyeji wake si muelewa lakini Yusuf alishachelewa kwani wakati Mahmoud kamsogelea akiwa anamuomba msamaha alishamuwekea kifaa kidogo kwenye suruali yake ambacho kazi yake ni kufuatilia mazungumzo kati yake na yeyote anayemzunguka hasa Hamza.


"Achana na mimi weweee."

Yusuf aliongea hayo na kurudi nyuma mpaka ndani kisha kufunga mlango na kumuacha Mahmoud pale nje. Lakini kwa Mahmoud ilikuwa kama ni ushindi kwani baada ya kuachwa pale nje alitabasamu kwanza kisha aliondoka zake huku akiitoa simu yake na kuiwasha, ilipowaka kitu cha kwanza ilikuwa ni kukiunganisha kifaa kile na simu yake kisha akaondoka zake. Alirudi mpaka nje ya nyumba ya Hamza ambako aliitelekeza gari yake akaingia na kuiwasha kisha akaondoka zake. Baada ya kufika kwake akaichukua simu na kuanza utundu wake kuona kama anaweza kupata chochote kwa Yusuf.


"Shiiiit nini hii?"

Mahmoud alijiuliza swali la mshangao baada ya kushindwa kupata signo kutoka kwa Yusuf.


"Au ile device ina tatizo?"

Alizidi kujiuliza maswali ambayo hayakuwa na majibu, aliinuka na kutoka nje ambako alizunguka huku na kule kufikiria nini kimetokea kwa Yusuf. Katika kufikiria zaidi akaona aende kwenye gari lake ambako aliingia na kufungua kikasha fulani hivi.


" Ona sasa, nimefanya nini?"

Mahmoud alipigiza mikono kwenye usukani baada ya kuikuta device ambayo ndiyo ilikuwa tageti yake na ile ambayo ilikuwa na matatizo ndiyo aliichukua na kumuwekea Yusuf.


"Siyo mbaya, pa kuanzia nimepata."

Aliongea huku akishuka kwenye gari na kufunga mlango kisha akaingia ndani kwake.


****


Bi Elizabeth baada ya kuamka alijiandaa kwa safari yake, hivyo baada ya kuoga na kila kitu aliifuata meza ambayo alikuwa kaipamba kwa kifungua kinywa kabla ya kuingia kuoga. Alianza kupata kifungua kinywa huku wenyeji wake wakiwa bado wamelala na baada ya kumaliza aliondoa vyombo pale mezani ambavyo alikuwa kavitumia na kuacha vyenye chakula kisha akabonyeza alamu ya chumbani kwa Hamza na muda si mrefu Hamza na mkewe walitoka sebuleni.


"Mama mbona mapema hivyo?"

Bi Aisha alimuuliza Bi Elizabeth baada ya kumkuta akiwa tayari na mkoba wake anawasubiri.


"Kama ambavyo niliwaambia jana kuwa leo natakiwa kuondoka."

Bi Elizabeth alimjibu kwa ufupi.


"Tutakukumbuka sana mama yetu lakini ndiyo hivyo tena hatuna jinsi."

Hamza aliongea hayo akiwa anaketi kitini.


"Ni kweli kabisa mume wangu, kiukweli tutakumiss sana."

Bi Aisha naye aliungana na mume wake.


"Wanangu msiwe na wasiwasi ninyi tayari ni Wanangu na ndugu zangu hivyo kuondoka kwangu si kwamba ndiyo basi tena hapana hamuwezi jua inawezekana mkaniona hapa hata kesho."

Bi Elizabeth aliongea hivyo huku akimsogelea Bi Aisha na kumkumbatia mtu ambaye siku kadhaa nyuma alimchukia sana. Wakiwa wamekumbatiana Hamza aliinuka na kuingia chumbani ambako hakuchukua muda akawa amerejea tena.


" Basi mama tusiuchukue muda wako wa safari naomba tukutoe."

Hamza aliongea huku akimkabidhi hela mkononi ambazo zingemsaidia katika safari yake.


"Nawashukuru sana Wanangu sina cha kuwalipa ila Mwenyezi Mungu ndiye anajua."

Bi Elizabeth aliongea hayo huku machozi yakimtoka.


"Mama usilie basi."

Bi Aisha alimwambia huku akitoa kitambaa kidogo na kumkabidhi afutie machozi. Walitoka mpaka nje ambako walimsindikiza mpaka stendi kuu ya mabasi ya Windhoek ambako waliyakuta mabasi yakijiandaa kutoka hivyo akaingia kwenye basi la kampuni ya TIGER TOURS ambalo hufanya safari zake kati ya Windhoek na Namport na baada ya kuketi aliwapungia mkono wakina Hamza pale chini. Nao hawakuondoka pale mpaka waliposhuhudia likianza kuondoka nao ndiyo wakaondoka zao. Wao wakiwa wanarudi nyumbani mita kadhaa kulikuwa na Mark ll GX 100 na ndani yake kukiwa na Mahmoud tayari kwa safari ya kumfuatilia Bi Elizabeth huko Namport.


"Bi Elizabeth kuanzia sasa mimi ndiyo nitakuwa ndugu yako."

Mahmoud aliongea hayo na kuliondoa GX 100 lake eneo hilo. Akiwa nyuma ya usukani mara simu yake iliita na baada ya kuiangalia alikuwa ni Daktari Abbas.


"Mkuu una haraka sana aisee asubuhi yote hii?"

Mahmoud alijisemea na kuizima simu yake na hiyo ilikuwa ni kuonesha kuwa kwa muda huo hakutaka mawasiliano na mtu yeyote zaidi ya kuongea lugha ya vitendo na gari lake. Alilipita basi lile la Tiger Tours na kutangulia lengo likiwa ni kuwahi kufika Namport na kufanya maandalizi fulani kabla ya kuianza kazi yake inayompeleka huko Namport. Haikuwa Safari ya mchezo ilikuwa ni ndefu lakini kwa Mahmoud ilikuwa fupi sana kwani ndani ya masaa matatu alikuwa amewasili na moja kwa moja aliongoza mpaka zilipo ofisi za Tiger Tours na kuuliza muda wa kufika basi linalotokea Windhoek.


"Samahani dada naomba kuuliza."

Mahmoud alianza kwa mhudumu wa ofisi ya Tiger Tours.


"Bila shaka kaka yangu unaweza kuuliza tu."


"Basi lenu linalotokea Windhoek litafika hapa muda gani?"

Mahmoud alimuuliza.




"Basi letu linalotokea Windhoek litawasili hapa mida ya saa sita mchana kaka yangu."

Mhudumu alimjibu Mahmoud ambaye baada ya kupata majibu aliyokuwa anayahitaji aliiangalia saa yake na kubaini limesalia saa moja na robo. Alipumua kwa nguvu akaichukua simu yake na kuiwasha.


" Dada yangu nashukuru kwa msaada wako."


"Karibu tena."

Mhudumu alimjibu wakati Mahmoud akipiga simu hivyo kumpa ishara mhudumu huyo ya pamoja kisha akasogea pembeni ili aweze kuongea na simu.


"Mkuu sikutaka kuipokea simu yako muda ule nilikuwa kwenye mwendo mkali sana na pia nilikuwa nimepakia watu wengine garini."

Mahmoud alimtolea ufafanuzi Daktari Abbas.


"Enhh wapi hiyo mida hii?"

Daktari Abbas alimuuliza Mahmoud.


"Hapa ninapoongea na wewe mkuu niko ndani ya 'Namport Bus Terminal' nimewasili masaa machache yaliyopita tayari kwa kuanza mawindo yangu."


"Aisee uliwahi sana eeh?"

Daktari Abbas alimuuliza.


"Kawaida tu mkuu wangu kuna wazo nimelifikiria nitakujulisha iwapo litaleta matokeo ninayoyatarajia."

Mahmoud alimwambia mkuu wake wa kazi anachokwenda kukifanya pale Namport japo hakumuweka wazi mbinu anayotaka kuitumia.


"Nakutegemea sana Mahmoud kama ambavyo tuliongea jana."


"Na mimi siwezi kukuangusha kikubwa tuombeane tu uhai."


"Usihofu niko nyuma yako Mahmoud kwa lolote lile nijulishe ili kazi yetu isikwame."

Daktari Abbas alimpa moyo kijana wake.


"Sawa mkuu labda ungenifanyia mchakato wa muamala kwani kuna kila dalili ya kuwepo huku kwa siku kadhaa."

Mahmoud aliona atumie nafasi hiyo kumuomba hela Daktari Abbas.


"Nipe dakika sifuri hivi akaunti yako itakuwa tayari."

Daktari Abbas alimjibu na kisha Mahmoud alikata simu na kuangaza huku na kule kama kuna sehemu pale stendi anaweza kupata chakula na katika kuangaza angaza ndipo alimuona mrembo mmoja akiwa bize kuhudumia wateja na hapo ndipo Mahmoud akaona ndiyo sehemu muafaka kwake,hivyo akaenda pale na kutafuta kiti kilichotupu na kuketi kisha akampa ishara yule mhudumu aliyemvutia kwa ushapu wake wa kuhudumia wateja.


"Mambo mrembo.."

Mahmoud alimsabahi Mhudumu yule.


"Poa kaka yangu, karibu nikuhudumie."


"Asante sana mrembo, una ugali wa dona na samaki."


"Ugali wa dona utapata lakini upande wa samaki hapana hatuna tuna nyama ya ng'ombe, mbuzi na uyoga tu."


"Duu, naomba huo ugali na nyama choma ya mbuzi."


"Mara moja."

Mhudumu yule alimjibu na kutoka haraka pale nje na kuingia ndani kushughulikia odda ya Mahmoud. Huku nyuma Mahmoud macho yake yalikuwa kwenye saa yake kuona hachezi mbali muda. Chakula kililetwa na mhudumu akakiweka mezani kisha akampa ishara ya kumkaribisha.


"Sorry mrembo naitwa Muddy naomba uungane nami mezani kwa chakula hiki."

Mahmoud alijitambulisha na kumkaribisha mhudumu yule ambaye kiasi chake alimchota kiakili.


"Nashukuru kaka yangu."

Alishukuru huku akichukua kipande cha nyama kwa madaha na kukiweka mdomoni.


"Waoo waitwa nani vile?"

Mahmoud aliona atumie fursa hiyo kumuuliza jina.


"Wataka kunijua eee?"

Mhudumu alimuuliza Mahmoud huku akiishia zake pasipo kusubiri iwapo atajibiwa au la.

Mahmoud alimtazama mpaka alipoishia mlangoni kisha akatabasamu.


"Mimi ndiyo Mahmoud tageti yangu hujaijua bado mrembo."

Alijisemea kisha akakiangalia chakula chake mezani na kuanza kula lakini mara akaangalia saa yake na kugundua kuwa alikuwa na dakika chache akakifakamia chakula haraka haraka kabla hata hajamaliza aliinuka na kumfuata yule mhudumu akiwa kashika waleti.


" Sorry mrembo uliyekataa kunitajia jina lako naomba niondoke hela yako hii hapa na pia hii ni kadi yangu ukihitaji kuongea na mimi namba iko hapo."

Alimkabidhi kisha akawa anaondoka zake eneo hilo kuelekea alikokuwa kapaki gari lake.


"Kaka Muddy samahani."

Yule mhudumu alimfuata mbio huku akimwita Mahmoud.


"Kuna nini mrembo?"

Mahmoud aligeuka na kumuuliza.


"Umesahau chenji yako hii hapa."

Badala ya kuipokea ile hela Mahmoud alitabasamu na kumpa ishara ya kubaki nayo kisha yeye akaendelea na safari yake na kumuacha mhudumu yule ambaye alitamani aongee kitu lakini alishindwa kwani Mahmoud alishafika mbali na kulifikia gari lake na kuliegemea huku macho yakiwa kwenye lango la kuingilia mabasi. Mara Tiger Tours lilitokea na kuingia taratibu ndani ya stendi ile huku Mahmoud akiitazama saa yake kuhakiki muda alioambiwa na mhudumu wa kampuni hiyo kama alikuwa sahihi. Kisha aliingia ndani ya gari lake na kufuta kioo cha mbele ili aweze kuona vizuri mbele,ndipo alianza kufuatilia mmoja mmoja aliyekuwa akikanyaga ardhi ya pale stendi na kwa wale aliokuwa hana mpango nao aliachana nao yeye hamu yake ilikuwa ni kumuona Bi Elizabeth akishuka. Lakini mpaka mtu wa mwisho anaweka mguu chini Bi Elizabeth hakutokea hicho kilimstaajabisha sana Mahmoud.


"Whaaaaat.....? Mbona huyu mama hajashuka?"

Mahmoud hakuamini macho yake kwa kilichotokea hivyo akashuka haraka kwenye gari na kuwafuata wahudumu wa lile basi waliokuwa ndiyo wanajiandaa kutoka.


"He he samahani kidogo naomba kuuliza."


"Ndiyo kaka uliza tu."

Mhudumu mmoja aligeuka na kusimama kumsikiliza Mahmoud.


"Hili si ndiyo basi lililotokea Windhoek?"


"Ndiyo lenyewe kaka."

Mhudumu alimjibu.


"Mhh mbona kama sielewi hivi?"


"Huelewi nini tena?"


"Au njiani kuna abiria walishuka?"


"Mhh ni mmoja tu kashukia hapo juu kwenye kona ya kuelekea bandarini."


"Kona ya kuelekea bandarini?"

Mahmoud aliuliza kwa mshangao.


"Ndiyo kaka."


"Ni mwanamke au mwanaume?"

Mahmoud aliuliza.


"Kaka vipi mbona maswali mengi hivyo kama kuna abiria wako na hapa hujamuona si umtafute hewani?"

Aliingilia kijana mmoja ambaye alichukizwa na maswali ya Mahmoud akaona ampe makavu kisha akamshika mkono yule mhudumu wa kike na kuondoka zao na kumuacha Mahmoud akiwa anachezea funguo za gari huku hajui afanye nini? Baada ya kuwaza kwa muda kidogo akaona arudi kwenye gari.


"Haiwezekani huyu mwanamke anichezee mchezo hivi au kiini macho nini au huyu bibi mwangaaa?"

Mahmoud alijiuliza swali.


"Hujanikwepa bado Bi Elizabeth."

Aliwasha gari na kuondoka ndani ya stendi hiyo na safari ikawa mpaka pale mchepukoni akataka kuufuata ule mchepuko lakini akawa kama kakumbuka kitu hivi akaahirisha.


"Ngoja nielekee kwanza nyumbani nikafanye yangu kisha kwa huyu mwanamama hata kesho uzuri nyumba ilipo siwezi potea."

Alijisemesha mwenyewe kisha akaelekea kwake ambako ni mbali kidogo na kutoka eneo hilo alipo. Akiwa mdogo mdogo kuelekea kwake mara simu yake iliita tena na baada ya kuangalia mpigaji ni nani aliipokea.


" Ndiyo bosi."


"Wapi maeneo?"

Daktari Abbas alimuuliza.


"Kama ambavyo nilikueleza muda ule niko zangu Namport."


"Najua hilo Mahmoud, na ndiyo maana nakuuliza wapi maeneo kwani hata mimi niko hapa Namport toka jana usiku nilipata dharura hivyo nilikuja hapa na kazi ya leo ilikuwa ngumu sana hivi ndiyo napata muda wa kumua na ndiyo maana nikaona nikucheki ili ikiwezekana baadaye tuonane nikupe mkononi mzigo wako."


"Sawa tu bosi muda huu naelekea kwanza maskani kisha nitarudi tena huku kati."

Mahmoud alimweleza Daktari Abbas.


"Ukitoka kwako utapitia kwangu basi tuweke mambo sawa."


"Sawa mkuu."

Baada ya kukata simu Mahmoud aliongeza mwendo kwani alishapata uhakika wa maisha baada ya kuhakikishiwa kupata mkwanja usio na makato ya kodi.


****


Jackline aliwasiliana na mume wake ambaye mpaka muda huo wa alasiri alikuwa hajarejea nyumbani kutoka kazini akimuelezea kupokea simu kutoka shuleni St. Petro Schools na yale aliyoelekezwa kuyatekeleza.


"Walinipigia simu na kunieleza kuwa mfumo wao wa mawasiliano ulipata tatizo kwa siku mbili na kuwafanya kushindwa kutoa taarifa kwa wazazi wa watoto waliofanikiwa kupata nafasi shuleni kwao, wakaomba radhi. Lakini wanatutaka kuhakikisha tunawapeleka watoto ndani ya wikendi hii ili jumatatu waanze masomo hivyo nikaona kwa kuwa leo ni jumamosi niitumie kuwanunulia mahitaji muhimu ya shule na kisha kuwapeleka."

Huu ulikuwa ni ujumbe ambao Jackline alimtumia mumewe Daktari Abbas ambaye baada ya kuusoma aliona ampigie simu.


" Naam mke wangu."

Aliitika baada ya mke wake kupokea simu.


" Ndiyo hivyo mume baada ya kupokea maagizo yao niliona niingie 'shopping' kisha niwapeleke."

Alijibu Jackline.


"Kwa sasa uko wapi?"

Daktari Abbas alimuuliza mke wake.


"Tuko njiani kuelekea shuleni."


"Kila kitu kiko sawa? Na wanangu wanasemaje?"


"Wanao wamefurahi sana na hapa wanatamani kama vile turuke wafike haraka na kila kitu kiko sawa kabisa mume wangu."

Jackline alimjibu mume wake.


" Vizuri mke wangu wape simu niongee nao."

Jackline hakuwa na hiyana alimkabidhi Natalie simu.


" Shikamoo babaa... "

Natalie alianza kwa kumsalimia baba yake.


" Marahaba mwanangu, mnaendeleaje lakini?"

Daktari Abbas alimuuliza Natalie.


"Tumekususa baba hatukutaki tena kwetu si wewe umetusambo?"

Nathan alinyanganya kwa Natalie na kumjibu baba yake.


"Nathan punguza hasira mwanangu mwenyewe tena kidume pekee baba yako nilitingwa na majukumu huku kazini na ndiyo maana sikurejea."

Daktari Abbas alijieleza.


"Sitaki sitaki baba ili nikusamehe labda utuletee zawadi nzuri."

Nathan aliendelea kumgomea baba yake.


"Hilo tu wala msijali nikirudi tu nitakuwa na maboksi ya zawadi kwa ajili yenu wanangu nahangaika hivi usiku na mchana ni kwa ajili yenu ninyi na ninyi pia someni kwa bidii."


"Sawa baba, we love you."

Natalie alinyang'anya simu kwa Nathan na kumpa moyo baba yake.


"Nawapenda pia wanangu."

Daktari Abbas alimjibu mtoto wake kisha akaomba mama yao apewe simu.


"Mke wangu hakikisha unawafikisha salama na usisahau kuchukua mawasiliano ya mlezi wao."


"Wala usijali mume wangu na hapa ndiyo tuko kwenye viunga vya shule tayari."


"Okey nikuache basi kuna shughuli moja naimalizia ukikamilisha michakato hapo utanijulisha mke wangu."

Daktari Abbas alimwambia mke wake na kukata simu. Kisha alimtafuta Mahmoud kujua kafika wapi au bado hajaanza safari.


"Mkuu ndiyo nakaribia kwako hapa kwako."


"Vizuri sasa hapo nyumbani pitiliza huku Hospitali na uje moja kwa moja ofisini kwangu."

Daktari Abbas ambaye ndiye mmiliki wa King's Medicare Centre ya mjini Namport hapa ndipo palipowakutanisha Jackline na Daktari Abbas.


JE, NI NINI KITAENDELEA?






Baada ya kukamilisha taratibu zote za pale shuleni St. Petro Schools aliondoka kurudi nyumbani huku akiwa na matumaini makubwa ya kufanya shughuli zake kwa uhuru mara baada ya kuwapeleka shuleni watoto wake waliokuwa wanampa mawazo ya kubaki peke yao nyumbani bila mwangalizi zaidi ya mlinzi na ukizingatia mume wake muda mwingi huwa Namport kazini kwake. Alifungua na muziki ndani ya gari sasa akawa akitikisa kichwa kufuata mirindimo ya muziki huo tabasamu kubwa usoni.


"Sasa naweza kwenda popote pale kwani niko huru sasa na huyu anayetaka kunichunga masaa ishirini na manne mwache kwanza ipo siku nitamfungukia watoto isiwe pingu ya kunifungia nyumbani hata mimi nina mengi ya kufanya."

Aliendesha gari mpaka nyumbani kwake ambako alioga haraka haraka akabadili nguo zake na kuvalia mavazi ya kazi huku akitupia koti refu jeusi ambalo liliendana na jinsi ya blue na fulana nyeupe, akakifuata kioo akajitazama kwa muda akabaini kuna kitu kinamisi akaiendea miwani ikikaa sehemu yake na alipojiangalia tena akatikisa kichwa kuukubali muonekano huo kisha akachukua simu na kumpigia mume wake huku akivaa raba zake nyeupe za Adidas.


"Habari mke wangu."

Daktari Abbas alimsalimu baada ya kupokea simu.


"Salama mume wangu pole na majukumu."


"Mungu anasaidia bado naendelea kupambana japo nategemea baada ya siku nne zijazo nitakuwa hapo nyumbani."


"Sawa sawa mume wangu, ila mimi mwenyewe nataka kutoka mara moja jioni ya leo."

Jackline alimueleza mume wake.


"Safari ya wapi mke wangu? Au ndiyo unataka uanze mambo yako?"

Daktari Abbas alimuuliza Jackline kwa jazba kidogo ikihisi kuwa Jackline anataka kuanza kufanya vitu alivyomkataza.


"Siyo hivyo mume wangu kuna rafiki yangu mmoja kaja kutoka Tanzania kaniomba tukutane kwa chakula cha jioni."


"Rafiki yako? Ni nani huyo?"

Daktari Abbas alipata mashaka kidogo.


"Anaitwa Karen ni mfanyabiashara wa midoli na mapambo ya nyumbani."

Jackline alimfafanulia mume wake.


"Okey, kwamba anataka akufundishe na wewe biashara hiyo?"


"Sifahamu yeye kaniita tu si unajua tena mimi ndiye mwenyeji wake hapa Namibia."


"Basi sawa usisahau kumwambia mlinzi asiache lindo peke yake."


"Bila shaka mume wangu."

Jackline alimjibu mume wake na kisha kukata simu akamalizia kufunga kamba za viatu vyake akachukua kimkoba chake na kutoka zake mpaka lilipokuwa limepaki gari.


"Kamanda wa jengo."

Jackline alimtania mlinzi wake.


"Naam bosslady wangu."

Mlinzi alimjibu Jackline.


"Nifungulie geti mdogo wangu."

Alimwambia mlinzi kisha yeye akaingia garini na kuliwasha na baada ya geti kufunguliwa akalitoa gari nje na kusimama kisha akamwita mlinzi wake.


"Nitachelewa kurudi hivyo uwe makini na geti lako."


"Nitakuwa makini bosi si unanijua kijana wako."

Mlinzi alimjibu Jackline ambaye alitikisa kichwa kumkubalia na kisha kuondoka zake. Alishika njia kuelekea Namport kwa siri bila kutaka mume wake ajue hilo. Akiwa njiani alimpigia simu Jasmine kumjulisha safari yake hiyo.


" Shemeji anafahamu hilo?"

Jasmine alimuuliza Jackline.


"Nimwambie naumwa, nimemdanganya kuwa nakwenda kukutana na rafiki yangu Karen kutoka Tanzania hapa hapa Windhoek."


"Uongo wako huo utakutokea puani mwanamke wewe!!!"

Jasmine alimshambulia.


"Potelea mbali itakuwa ajali kazini mdogo wangu."

Jackline alimjibu.


"Sema ajali kazini hivyo hivyo unafikiri mazuri eeh, kwa mfano ikipatwa na majanga huko japo hatuombei yakukute?"

Jasmine alimuuliza.


"Acha kunichulia wewe huoni kama kausiku kameanza unataka nishindwi kuendelea na safari?"


"Hapana wala si hivyo."

Jasmine alimjibu.


"Nitakucheki nikifika huko na ujitahidi kuwa hewani muda wote."


"Bila shaka Kamanda wangu."

Jasmine alimjibu na kisha Jackline aliikata simu na kuiweka kwenye dashboard kisha akaukamata usukani na kukanyaga mafuta. Na baada ya masaa kadhaa akawa ameingia ndani ya Namport na moja kwa moja akaongoza mtaa ambao iko nyumba ya mzee Jerome Whistle aliyekuwa mume wa Bi Elizabeth ambaye kwa sasa ni marehemu. Na baada ya kulikaribia jengo hilo alisimama na kujifunga kitambaa kichwani ambacho alijua itakuwa ni ngumu kwa mtu kuweza kumtambua haraka kisha akachomoa bastola kwenye dashboard na kuikagua kama iko vizuri na baada ya kujiridhisha aliisogeza mafichoni gari kisha akashuka na kuanza kutembea kwa mguu kuifuata nyumba ya Bi Elizabeth. Alitembea mpaka alipoikaribia akajificha kwanza kwenye ukuta wa jengo lililo karibu na nyumba hiyo ambalo miaka takribani saba halikuwepo hapo,lengo likiwa kuangalia usalama kwanza.


"Nani wewe?"

Ilisikika sauti kutoka nyuma yake, alipogeuka aligindua kuwa ni mlinzi wa jengo hilo la ghorofa moja kutokana na mavazi yake ambayo alivalia na yeye Jackline kumuona vizuri kutokana na mwanga ambao ulimmulika.


"Ishakuwa nuksi hapa, sijui nifanye nini kujiokoa."

Jackline alijiwazia pale alipokuwa kachuchumaa.


"Nakuuliza wewe hapo au haunisikii?"

Mlinzi yule alimuuliza na safari hii akitumia tochi yake kummulika Jackline.

Baada ya kumulikwa Jackline akaona isiwe tabu aliinuka na kugeuka kumtazama mlinzi yule.


"Samahani kwa kukaa hapa kaka yangu nilikuwa nimejificha baada kufukuzwa na vijana fulani hapo mbele sikuwa na mpango muovu wowote ule."

Jackline alijitetea.


"Acha kunidanganya mrembo macho yako tu yanapishana na maneno yako, ongea ukweli haraka kabla sijakufyatua shingo yako."

Maneno ya mlinzi yule yalimfanya Jackline kuipapasa bastola yake kama iko sawa kisha akamuangalia mlinzi alivyosimama, kichwani kwake akifikiria namna ya kumtuliza.


" Kaka yangu naomba uniamini kwa niliyokueleza usinifikirie vibaya."

Jackline alijitetea huku akimsogelea mlinzi pale alipokuwa.


"Unakwenda wapi wewe sima....."

Kabla hajamalizia kauli yake Jackline alishainama kama upepo na kuzoa mchanga aliomrushia machoni mlinzi yule na kupotea zake.


"Macho yanguuuuu......."

Mlinzi alibakia kupiga kelele baada ya mchanga ule kumwingia machoni huku Jackline akiwa amelizunguka jengo lile kwa nyuma na kuifuata nyumba ya Bi Elizabeth kupitia nyuma. Aliusogelea ukuta na kuupanda kisha akatua ndani bastola mkononi akaufuata ukuta wa nyumba ambayo kwa ndani taa zilikuwa zinawaka.


"Mkuu yupo ndani anapika nifanyaje hapa?"

Ni sauti ambayo ilimshangaza Jackline, ilitokea kona nyingine ya nyumba hiyo.


"Ni nani huyu tena? Ina maana huyu mama anafuatiliwa na watu wengine tena?"

Jackline alijiuliza maswali hayo huku akimvizia huyo mtu aliyekuwa akiongea na simu, lakini akasita kuendelea kumsogelea mtu huyo aliyekuwa akiongea kwa sauti ya chini kidogo.


"Hapana sifahamu wako wangapi."

Jackline aliamua kugeuka kuurudia ukuta aondoke kabla hajaonwa na mtu huyo na kama bahati vile akafanikiwa kuuruka ukuta na kujificha kwenye kigiza ili aweze kumfahamu mtu huyo ni nani. Lakini akiwa katulia pale gizani akaona mwanga wa tochi ukimulika upande wake kama vile kuna mtu alikuwa anakuja akaona isiwe tabu haraka sana akauzunguka ukuta ule wa nyumba ya Bi Elizabeth na kukimbia.


"Shiiiit kabisa, wakina nani hawa walioingia kwenye lada zangu?"

Jackline alijiuliza mara baada ya kuingia kwenye gari. Au kundi la marehemu Nafiwe bado lipo nini na kama si wao hawa ni wakina nani sasa? "

Jackline aliendelea kujiuliza maswali ambayo hayakuwa na majibu.


****


Daktari Abbas alimfuata Mahmoud ambaye alikuwa ameshatoka mle ndani kwa Bi Elizabeth kupitia ukuta wa nyuma.


" Kwa hiyo tunafanyaje mkuu?"

Mahmoud alimuuliza Daktari Abbas.


" Hapa hatuondoi miguu yetu mpaka tumpate na kumpa zawadi yake."

Daktari Abbas alimwambia Mahmoud.


"Kwa hiyo unamaanisha turudi tena ndani?"

Mahmoud alimuuliza.


"Ndiyo maana yake Mahmoud tumeamua kuugeuza usiku kuwa mchana halafu turudi hivi hivi itakuwaje?"

Daktari Abbas alimuuliza Mahmoud ambaye alimuelewa bosi wake na kuupanda ukuta tena kwa mara ya pili na kumuacha pale chini.

Aliunyatia mlango wa mbele safari hii japo taa ilikuwa inawaka lakini yeye hakujali alijitoa mhanga. Aliufuata na kuibonyeza swichi ya kengele ambayo haikuwa mbali. Na baada ya dakika kadhaa mlango ulifunguliwa na mfunguaji kuchungulia nje kuna nini, kitendo hicho kilimgharimu kwani Mahmoud hakukosea alimvuta nje na kumpiga kabali ya shingo huku bastola ikiwa imeelekezwa sikioni mwa yule mtu.


"Samahani usiniue, niko tayari kufanya chochote kile unachokitaka."

Binti yule alijitetea baada ya kuona mdomo wa bastola unagusa sikio lake.


"Sikiliza wewe binti."

Mahmoud alimnyamazisha yule binti.


"Ndiyo nakusikia."


"Kwa usalama wa maisha yako naomba uniambie aliko Bi Elizabeth."

Mahmoud alimwambia yule binti huku akiitingisha bastola pale sikioni.


"Bi Elizabeth ndiyo nani?"

Binti yule aliuliza.


"Unasemaje wewe binti?"

Mahmoud alichukizwa na swali lile kutoka kwa binti yule kiasi cha kuanza kumvuta nyuma ya nyumba.


"Huyo Bi Elizabeth ndiyo nani nauliza?"


"Aaah kumbe wewe ni msanii siyo?"

Mahmoud alimuuliza.

Mara akiwa anamvuta kule nyuma ambako alipitia mara alisikia sauti kutoka ndani ikimwita yule binti.


"Wee Asteria umepatwa na nini mbona kimya?"

Ilikuwa ni sauti ya mwanamke ikiuliza kutoka ndani.


"Nisikilize sasa ukiinua kinywa chako tu ubongo wako ni halali yangu sawa?"

Mahmoud alimkanya Asteria aliyekuwa kambananisha kwenye kona.


"We Asteria, Asteria umeanza mambo yako siyo? Leo utalala huko huko kwa huyo hawala yako si unamthamini sana kuliko sisi ndugu zako."

Mama yule aliendelea kupiga kelele za vitisho huku akifungua mlango. Hapo ndipo Mahmoud alipomsukuma chini yule binti na kumuwahi yule mama kabla hajafanya chochote kile akamdaka na kumvuta pale alipokuwa yule binti.


" Unakwenda wapi wewe mtoto nitausambaza ubongo wako sasa hivi."

Mahmoud alimwambia yule binti aliyekuwa akitaka kukimbia huku bastola ikiwa imemuelekea huku akiwa kampiga kabali ya shingo mama yule aliyekuwa akipiga kelele ambaye ni kama mwenye mji huo.


HUYO MAMA NI NANI? ANA UNDUGU NA BI ELIZABETH?


NA VIPI KUHUSU JACKLINE KAKUTANA NA WAKINA NANI?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU YA KUMI NA MOJA YA KIGONGO HIKI.






Baada ya kuwathibiti mama na binti wake wa kazi Mahmoud aliwachukua tena mpaka ndani ya nyumba yao na kuwataka waongee ukweli juu ya Bi Elizabeth.


"Narudia tena, iwapo hamtaonesha ushirikiano kwangu jueni kuwa kifo kinawakaribisha sijui mmenielewa?"

Mahmoud aliwaambia huku akiwanyooshea bastola pale sebuleni kwao.


"Kijana wangu hakuna tunalokuficha hata moja,ni kweli kabisa sisi hatumfahamu huyo mwanamke wala hao wengine."

Mama huyu alimjibu huku akilia kwa kwikwi akiwa kamkumbatia binti yake pale chini.


"Acha kunidanganya wewe kama humfahamu mlianzaje kuishi kwenye nyumba yake?"

Mahmoud alimuuliza tena akiwa anayasaga meno yake kwa hasira huku dirisha likiwa limeegemewa na Daktari Abbas ambaye alikuwa ameshaingia ndani na kusalia pale dirishani akihofia kuionesha sura yake hivyo aliona asalie dirishani tu akichungulia na kusikiliza mazungumzo yale.


"Nyumba hii tulipangishwa na mtu mmoja aitwaye Thomas."


"Thomas? Ni nani huyu?"

Mahmoud alimuuliza kwa mshangao.


"Tuliunganishwa na dalali ambaye tulimpa kazi ya kututafutia nyumba."

Mama yule alimjibu Mahmoud.


"Sasa nimebaini unaendelea kunidanganya mama na ninachokiona ni kucheza na kifo jitafakari."

Mahmoud alimsogelea karibu zaidi mama huyo.


"Ukiutaka ukweli zaidi naomba nikupe mawasiliano yake huyo Thomas pamoja na dalali pia."

Mama mwenye nyumba alijitetea.


"Haraka nikabidhi mawasiliano hayo."

Mahmoud alimtaka mama huyo amkabidhi mawasiliano ya watu waliompangisha nyumba ile na ndipo yule mama alipoinuka ili aelekee chumbani kwake lakini Mahmoud alimzuia.


"Tulia wewe huwezi kwenda chumbani peke yako, uende peke yako ukafanye nini huko?"

Mahmoud alimwambia huku akimuinua na binti yake kisha kuwaongoza mpaka chumbani kwa yule mama ambaye alichukua kadi mbili na kumkabidhi Mahmoud.


"Naondoka ila mkijidanganya kucheza mchezo wowote wa kijinga mjue mtakuwa mmenikaribisha tena hapa kuchukua roho zenu."

Mahmoud aliongea na kutoka zake nje ambako alimkuta Daktari Abbas pale dirishani akiwa hajui afanye nini, waliruka ukuta na kuondoka zao.


" Tumechemka bosi, huyu Elizabeth hakufika huku."

Mahmoud alianzisha mazungumzo wakiwa kwenye gari.


" Usiseme hivyo kumbuka mkononi una namba za watu wanaoimilili hii nyumba hivyo watatuambia aliko Bi Elizabeth."

Daktari Abbas alimjaza matumaini Mahmoud.


" Kwa hiyo tufanyaje kwa sasa mkuu? "

Mahmoud alimuuliza Daktari Abbas.


"Muda huu ni usiku sana inabidi tuahirishe kazi hii ila tutaendelea nayo kesho kwa kuanza na hao wawili."


"Sawa mkuu."

Mahmoud alimjibu Daktari Abbas huku akiendelea kupambana na usukani. Lakini akiwa anaendesha mara aliiona gari ikija nyuma yao kwa mwendo wa kasi sana.


"Ni nani huyu?"

Mahmoud aliuliza akiwa ameleekeza macho yake kwenye 'site mirror'.


"Au tumeshachomewa utambi nini?"

Daktari Abbas aliuliza baada ya kuiona ile gari nyuma yao. Lakini wakiwa wanaendelea kujiuliza ni nani huyo anayewafuatilia mara lile gari liliwapita kama mshale.


"Mmnh huyo dereva anaonekana ni mwenyeji maeneo haya eeehh?"

Daktari Abbas aliuliza akimuangalia Mahmoud ambaye alisimamisha gari na kufungua mkanda.


***


"Habarini Wanajeshi wangu !!"

David Orlando aliwasalimu vijana wake.


"Kamili mkuu wetu."

Walijibu kwa pamoja.


"Nafurahi kusikia hivyo, sasa kama ambavyo niliwaambia jana kule mazoezini kuwa tutapata ugeni na sasa mgeni yuko mbele yenu hapa ni nani? Bila shaka atajitambulisha yeye mwenyewe, mama karibu ujitambulishe."

David Orlando aliwaelezea wenzake kisha akamkaribisha mgeni ajitambulishe kwa wenzake.


" Nafurahi kukutana nanyi vijana wangu najulikana kama Elizabeth ni mfungwa ambaye nimetoka kwa muda kwanza."

Maelezo hayo ya Bi Elizabeth yaliwafanya vijana wa David Orlando kutazamana usoni.


"Mfungwa uliyetoka jela kwa muda? Kivipi?"

Mmoja wa vijana aliuliza.


"Kuhusu hilo nitawaelezea mimi hapa."

David Orlando aliingilia kujibu swali hilo la kijana wake.


"Kama alivyojitambulisha yeye mwenyewe Bi Elizabeth ni kweli kabisa ni mfungwa ambaye yuko nje kwa muda baada ya kumwaga mahela kwa viongozi wa gereza ili tu wamuachie huru kwa muda aje kulipiza kisasi kwa wabaya wake waliomharibia maisha yake yeye pamoja na Familia yake ambayo yote iko ardhini. Hivyo kuanzia sasa Bi Elizabeth Mackey tutakuwa naye kwenye makazi yetu tukimpa mazoezi ikiwa ni pamoja na kushirikiana naye kwenye vita yake ya kisasi."

David Orlando alitoa maelezo kwa vijana wake.


" Ni kweli kabisa vijana wangu mama yenu nina matatizo makubwa sana ambayo kiongozi wenu nilishamueleza."

Bi Elizabeth alijieleza.


" Umeeleweka mama yetu tutakuwa bega kwa bega na wewe kwenye kila kitu ambacho unahitaji tukusaidie."

Kijana mmoja wapo alimpa majibu ya kumridhisha Bi Elizabeth.


" Nadhani umewasikia vijana wangu kazi kwa masikio yako mwenyewe mama yangu hivyo nafikiri ni muda wa kuianza programu yetu sasa."

David Orlando alimueleza Bi Elizabeth ambaye alikubaliana naye bila shaka yoyote ile.


"Natamani muda huu kabla ya majira ya magharibi tuelekee nyumbani kwangu nikakutane na kijana wangu ambaye nilimpa kazi ya kuitunza nyumba nafikiri ni muda muafaka wa shughuli zetu kuxiendeshea pale kwangu maana hapa ni pafinyu sana."

Bi Elizabeth alitoa pendekezo lake kwa David, kijana aliyejitolea kumsaidia mara baada ya yeye kusaidiwa na Bi Elizabeth akiwa gerezani.


" Ulisemalo ni sahihi kabisa mama yangu lakini kumbuka hapa ni maficho lakini kule kwako ni sehemu ya wazi na inayofahamika na wengi kwanini huyo kijana wako asiendelee kuishi pale mpaka mambo yako yatakapoenda vizuri?"

David Orlando alimshauri Bi Elizabeth.


" Nimekuelewa, lakini tunatakiwa kwenda nikaongee naye na pia kumjulisha kuwa nimerejea tayari."

Walikubaliana kwa pamoja kisha wakaondoka wote kuelekea nyumbani kwa Bi Elizabeth. Kutoka walipokuwa mpaka nyumbani kwa Bi Elizabeth kulikuwa na umbali kidogo hivyo iliwachukua kama saa moja na dakika kadhaa kufika. Walifika na moja kwa moja Bi Elizabeth Mackey akipiga kengele ya nje ya geti na baada ya kusubiri kwa muda mlango mdogo wa getini ulifunguliwa na kutoka mama ambaye alikuwa ni mgeni machoni pa Bi Elizabeth.


"Naitwa Bi Elizabeth Mackey ni mmiliki wa nyumba."


"Bi Elizabeth?"

Mama Asteria alishtuka kidogo baada ya kulisikia jina hilo la Bi Elizabeth.


"Vipi mbona umeshtuka kulisikia jina langu unanifahamu au umewahi kulisikia popote?"

Bi Elizabeth alimuuliza mama Asteria ambaye alikuwa bado kwenye mshangao.


"Haa..ha..hapana nilikuwa navuta picha kama nimewahi kulisikia popote pale lakini kumbukumbu zangu hazinipi majibu."

Mama Asteria alimjibu huku akiwaangalia vijana walioongozana na Bi Elizabeth kwa mashaka.


"Sijui mwenzangu ni nani hapa? Na pia unaweza kuniitia Thomas?"

Bi Elizabeth alimuuliza mama huyo.


"Mimi naitwa Diana Kaplan ni mke wa bwana Montenero ambaye ni mfanyabiashara wa mazao hapa Namport na hapa tumepanga."


"Mmepanga? Kivipi?"

Bi Elizabeth alimuuliza Diana Kaplan kwa mshangao.


"Ndiyo tulipangishwa na Thomas miaka miwili iliyopita na kwa kuwa tulimkeshi taslimu ya miaka mitatu hatujawahi onana naye."

Diana Kaplan alieleza.


"Thomas amekupangishia nyumba yangu kwa malipo ya miaka mitatu?"

Bi Elizabeth alimuuliza tena Diana Kaplan ambaye alimjibu kwa kutikisa kichwa.


"Mlimlipa kiasi gani kwa muda huo?"


"Makubaliano yalikuwa ni shilingi milioni sita kwa mwaka hivyo tulimkeshi shilingi milioni kumi na nane taslimu."

Jibu la Diana lilimnyong'esha zaidi Bi Elizabeth ambaye aligeuka kuwatazama wakina David huku akifuta machozi.


"Si mmesikia alichonifanyia Tom ina maana yeye akili yake alijua siwezi kutoka sasa si ndiyo?"

Bi Elizabeth aliuliza na kuanza kulia mbele ya Diana ambaye mp muda aliona kama anaota vile kwani usiku uliopita alivamiwa na Mahmoud ambaye alikuwa akimuulizia huyu huyu Bi Elizabeth jambo lililozidi kumchanganya na alitamani kama amsimulie mkasa wa usiku lakini akaona atulie tu.


"Jitulize mwanamke mwenzangu na kama huamini mimi nitakupa mawasiliano yake umuulize wewe mwenyewe."


"Utakuwa umefanya la maana dada yetu, tupe mawasiliano ya huyo Thomas na ikiwezekana na ya dalali aliyekuunganisha na Thomas."

David Orlando aliingilia kujibu baada ya Bi Elizabeth kubanwa na kwikwi. Basi ikabidi Diana aingie ndani kuzifuata namba hizo hitajika na kumpa Bi Elizabeth.


NINI KITAENDELEA?



Walipokabidhiwa zile namba waliaga na kuingia kwenye gari tayari kwa kuondoka. Lakini Bi Elizabeth Mackey alitoa pendekezo lake kwamba waelekee wapi, kuna kitu kilimuijia kichwani akaona itakuwa si vizuri iwapo hatafika mahali walipolala wapendwa wake wote hivyo safari ikaanza kuelekea mtaa kama nne kutoka nyumbani kwake hapo mpaka makaburini.


"Wanangu si mnaona magumu ninayopitia mama yenu? Na haya yote yasingetokea iwapo mume wangu asingewaokoa wale mbwa koko wa kike nyumbani kwangu, angalia sasa nimekaa jela miaka hiyo mingapi tayari nyumba yangu imepangishwa na vipi ningefia huko si ingeuzwa au kutaifishwa kabisa?"

Bi Elizabeth aliwaeleza wakina David huku upande wa mtandio ukiendelea kupita machoni kwake kufuta machozi yaliyokuwa yakitiririka bila breki.


" Unajua nini mama yangu? Kila binadamu ana mapito ya kuumiza na si kidogo lakini kuna muda wa kulitafakari mara moja moja kabla ya kulichukulia uamuzi."

David alimshauri Bi Elizabeth ambaye baada ya kuyasikia maneno hayo alimgeukia.


"Kwa hiyo unataka niachane na huu mchakato wa kisasi?"

Bi Elizabeth aliuliza.


"Ni ushauri wangu tu mama yangu ili kipindi hiki cha upweke ufanye mambo yako mengine ambayo yatakuinua upya kabisa."

David Orlando alimjibu tena Bi Elizabeth ambaye alitikisa kichwa kuonesha kutokukubaliana na ushauri wa wake.


"David wewe ni kijana shupavu sana na hata ile siku tulipokutana kwa mara ya kwanza nilipata nguvu mpya na ujasiri wa kuifanya kazi yangu kuwa nyepesi lakini kwa maneno yako unanikatisha tamaa sasa, lakini nashukuru kwa ushauri wako nitaufanyia kazi japo si kwa sasa."

Bi Elizabeth alimjibu David huku akishuka kwenye gari kwani muda huo tayari walikuwa wamewasili kwenye makazi ya kudumu ya watoto wake wawili Mustapha na Victor pamoja na mume wake mzee Jerome ambao wote walizikwa karibu. Na baada ya kuyaona makaburi yale ya wapendwa wake Bi Elizabeth alijikuta akiishiwa nguvu taratibu na kuanguka chini. David na kundi lake walipata kazi ya kufanya ambayo hawakuitarajia haraka sana walimchukua na kumrudisha kwenye gari kisha safari ya kurudi maskani kwao ikaanza mara moja.


"Tunaelekea hospitali?"

Dereva wao aliwauliza.


"Hapana tuelekee nyumbani mengine yatafahamika huko huko tukifika."

David alimjibu dereva wake. Na hapo safari ya kuelekea nyumbani kwao ilianza mara moja huku wakina David wakiendelea kumpatia huduma ya kwanza Bi Elizabeth. Mungu saidia wakiwa bado njiani alipata fahamu zake.


" Wapi tunaelekea? "

Alipozinduka aliuliza.


"Tunakupeleka Hospital mama."

David alimjibu.


"Hospitali? Kufanya nini huko kwani mimi ninaumwa?"

Aliuliza.


"Hapana ulipata mushtuko baada ya kuyakaribia makaburi."

David alimjibu Bi Elizabeth.


"Oohh my God, kwa hiyo sikuweza kuwakaribia?"

Bi Elizabeth aliuliza na kuanza kulia tena.


"Ndiyo mama."

Mmoja wa vijana alimjibu.


"Mume wangu naomba unisamehe kwa ambacho nilikufanyia kwa sasa nataabika sana naomba nisamehe sana na pia niombee msamaha kwa wanangu mume wangu."

Bi Elizabeth aliendelea kulia huku akiomba msamaha kwa mume wake kwa kitendo ambacho alimfanyia.


"Mama naomba turudi ukapumzike kwanza kisha tutarejea tena kwa wakati mwingine."

David Orlando aliona amtulize Bi Elizabeth ambaye alikuwa akitokwa machozi ya majuto.


"Nimewaelewa wanangu haina shida."

Alimjibu huku akifuta machozi yake, na cha ajabu alianza kucheka kitu kilichowashangaza wakina David.


"Ninyi mabinti nawahakikishia kutoka moyoni machozi yangu hayaendi bure lazima mtayalipia iwe au isiwe lazima."

Bi Elizabeth Mackey alikula kiapo hicho mara baada ya kuacha kucheka ghafla.


****


Jackline baada ya kupata kifungua kinywa pale Milan Inn Hotel alitoka na kuingia kwenye gari lake na mara baada ya kukaa kidogo alishuka tena kurudi mpaka chumbani kwake ambako alikumbuka kitu fulani. Aliichukua laptop yake na kuiwasha kisha akaenda moja kwa moja mpaka kwenye application ya whatsApp hapo alilifuata kundi lao la Makamanda na kuiweka salamu yao kama utambulisho.


"Makamanda."

Alianza Jackline.


"Niko hewani kamanda wangu."

Alijibu Jasmine.


"Nawachora tu kwa jicho la pembe."

Jessica naye aliibuka na viimoji vya kucheka.


"Kwamba mmewahi sana ee, mmechemka sana mimi kitambo sana nilikuwa hapa."

Roberto aliwajibu wakina Jackline.


"Au mlisahau kama mimi ndiyo afisa afya wa kundi? Kwa taarifa yenu mimi ndiye niliyefanya usafi wa ukumbi na kupangilia viti sasa sijajua kama ninyi mmewahi kabla yangu?"

Titiana aliibuka na komenti yake ambayo iliwaacha hoi wote mle kundini na pia ujio wake uliwafurahisha sana kwani alipotea hewani kwa muda.


" Titiana karibu bwana kitambo sana."

Jackline alimkaribisha Titiana.


" Mwambie Makamanda tumerudi."

Jasmine alichomekea.


"Mimi bado nina kesi na Roberto kwa kosa la kutufichia wifi yetu kipenzi."

Jessica alitania.


"Jamani mimi nafurahi sana kuwepo hapa kwa mara nyingine, niliadimika kwa muda kwa ajili ya masomo na mambo fulani fulani hivi na niwataarifu tu kuwa wifi yenu nimegraduate tayari kwa sasa ni mwendo wa kazi tu."

Titiana aliwajulisha kile ambacho walikuwa hawakijui wenzake.


" Ebwana ee hongera sana kwa hatua hiyo wifi yetu. Kwa niaba ya Makamanda niwape pongezi wote wawili wewe na mzee mzima Roberto kwa kuvumiliana kwa kila kitu."

Jasmine aliwawakilisha wenzake kuwapongeza Titiana na Roberto.


"Na mimi kwa niaba ya kipenda roho wangu, nawashukuru sana ndugu zangu kwa maombi yenu."

Roberto alishukuru kwa niaba ya mpenzi wake.


"Tunachokisubiri kwa sasa ni bonge la harusi tu, lakini yote kwa yote ndugu zangu jana usiku kidogo niishie mikononi mwa watu wasiojulikana lakini ile mbinu ya Roberto ya mchanga ilinisaidia sana nikasalimika pamoja na hilo kuna jingine nikakutana nalo ndani ya nyumba ya Bi Elizabeth."


"Usiturushe mioyo Jackline unataka kutuambia nini hapo?"

Jessica alichomekea.


"Baada ya kuruka ukuta na kuingia ndani ya nyumba wakati nanyata si nikamsikia mtu upande mwingine akiongea na simu akitoa maelekezo ya kinachoendelea ndani ya nyumba hiyo ikanipa hofu na kunipelekea kutimua mbio kabla hajaniona. Lakini swali langu ni wakina nani hao au 'The Black Eyez' hawakuisha? "

Jackline alihitimisha kwa swali.


"Kwanza nianze kwa kukupa pole kwanza na pili niulize kidogo huyo ambaye ulimchapa na mchanga ni tofauti na wa ndani?"

Roberto alimtupia swali mara baada ya kumpa pole.


"Ndugu zangu eneo lile limebadilika sana yaani hamuwezi amini kwa kipindi hiki cha miaka mingapi tulichokuwa nje ya Namport kumejengwa majengo ya maana na hata pale jirani na kwa mzee Jerome kuna jengo la ghorofa moja na hapo ndipo nilikuwa nimejificha si ndiyo akatokea mlinzi wa hilo jengo aaah si ndiyo nikamchapa nao? "

Jackline alifafanua zaidi.


" Kamanda shukuru Mungu umepona bwana kikubwa ni kujua ulimkuta Bi Elizabeth? "

Jasmine alimuuliza Jackline.


" Kiukweli ilikuwa ngumu kumpata baada ya kuondoka kuokoa maisha yangu baada ya kumkuta mbwa mwingine akinusa eneo lile."

Jackline alitoa maelezo tena, hivyo baada ya majadiliano ya muda mrefu ilibidi wakubaliane kutulia kwanza lakini kuendelea kumfuatilia Bi Elizabeth kwa kuwatumia watu wengine na iwapo watapata uhakika kuwa kaanza utukutu ndipo watakapochukua hatua. Baada ya kuagana ndipo Jackline alipozima laptop yake na kuamua kutoka nayo na kuingia garini tayari kwa safari ya kurudi nyumbani kwake Windhoek kabla mume wake hajarejea.


"Lakini kabla ya kuelekea nyumbani lazima nipate uhakika kwa kurudi tena nyumbani kwa Bi Elizabeth ikiwezekana nikajidai kama vile nimemtembelea."

Jackline alijisemesha huku akiondoa gari. Na baada ya mwendo kidogo aliwasili nyumbani kwa Bi Elizabeth Mackey na baada ya kushuka aliiendea swichi ya kengele na kuipiga. Na mara mlango mdogo wa geti ulifunguliwa na binti.


" Karibu mama mdogo."

Alikaribishwa Jackline.


"Asante mrembo."

Jackline alimjibu.


"Samahani mrembo sijui nimewakuta wenyeji?"

Jackline aliuliza.


"Wenyeji ndiyo sisi wenyewe mama mdogo."


"Kivipi mrembo?"


"Hapa tunaishi sisi yaani mama na baba."

Binti huyo alimjibu.


"Okey ina maana nyumba hii mmeinunua ninyi?"

Jackline alimuuliza tena.


"Hapana sisi hapa ni wapangaji tu wala si wanunuaji."

Alijibiwa.


"Ina maana yeye atakuwa wapi sasa?"

Jackline alijiuliza swali ambalo binti yule alilisikia.


"Unamuulizia nani mama mdogo?"

Binti yule alimuuliza.


" Mwenye nyumba hii aitwaye Bi Elizabeth."


"Bi Elizabeth?"


"Ndiyo mrembo unamfahamu?"


"Hapana simfahamu lakini najiuliza huyu mama ana nini maana jana tulivamiwa na mtu mmoja ambaye naye alikuwa anamhitaji mama huyo huyo, kwani kafanya nini?"

Binti huyo alimjibu huku akitoa maelekezo ya kilichotokea usiku wa jana. Maelezo hayo yalimshtua kidogo Jackline na ndipo alipovuta picha ya mtu aliyemsikia akiongea na simu.


" Nashukuru mrembo wangu ngoja mimi niondoke lakini iwapo lolote litatokea ambalo si la kawaida usisite kunijulisha mimi ni mtoto wa huyu Bi Elizabeth ninayemuulizia au kama atakuja utamwambia mwanao alikuja."

Jackline alimjulisha binti huyo aitwaye Asteria na kumkabidhi kadi yake kisha kuingia kwenye gari na kuondoka zake.


NINI KITATOKEA?




Ikiwa ni mida ya usiku wa saa nne Mahmoud alikuwa anaikaribia nyumba anayoishi dalali wa nyumba. Huyu ndiye dalali aliyetumiwa na Thomas kumpata mpangaji wa nyumba ya Bi Elizabeth ambaye ni Diana Kaplan. Kitu ambacho kilimshangaza Mahmoud ni kutopatikana kwa Thomas kwenye simu na mtu pekee ambaye alimtegemea muda huo kumpa taarifa za Thomas au za Bi Elizabeth alikuwa ni huyu dalali. Alifika eneo aliloelekezwa kwenye simu na kupaki gari lake, alishuka na kuiendea nyumba iliyokuwa mbele yake.


"Hodi humu ndani, hodi, wenyewe hodi....!"

Hakuna mtu aliyemuitikia hata mmoja hivyo akasogea mpaka dirishani na kuchungulia ndani ambako kulikuwa na mwanga wa umeme hakuona mtu lakini televisheni ilikuwa haikuzimwa hapo akapata matumaini kuwa mhusika hayupo mbali. Alitulia kwa muda kisha akarudi kwenye gari na kuzima taa akatulia kimya kumsubiri mwenyeji wake ambaye simu yake ilikuwa ikiita tu bila kupokewa muda huu.


"Atakuwa wapi au tayari wamepeana taarifa kuwa wanatafutwa nini? Lakini ngoja."

Mahmoud alijiuliza swali hilo ambalo hakuwa na uhakika nalo hivyo akaona arudi tena pale dirishani na baada ya kufika akaipiga tena ile namba.


"Okey hajaenda mbali huyu pimbi mbona simu iko mezani."

Alipata majibu ya swali lake mara baada ya kuisikia simu ikiita kutoka ndani. Akaona isiwe tabu akarudi kwenye gari kuendelea kumsubiri. Alisubiri kwa muda mrefu sana mpaka usingizi ukampitia pale pale kwenye gari na baada ya kuamka alienda pale dirishani na kukuta hali ni ile ile aliyokutana nayo awamu ya kwanza hivyo ikamlazimu kuukagua mlango.


"Mhh mbona mlango haujafungwa?"

Alijiuliza baada ya kuukuta mlango umeegeshwa tu. Akaangalia pande zote pale nje alipojiridhisha ni salama aliingia mpaka sebuleni, ambako alishtushwa kidogo na namna mazingira ya pale sebuleni yalivyokuwa.


"Si bure huyu kavamiwa mbona vitu vimesambazwa kiasi hiki? Na kwa namna vitu vilivyo inaonekana kulitokea ugomvi kwanza."

Mahmoud alijiuliza huku akiikagua ile sebule kwa umakini mkubwa. Na baada ya kujiridhisha kwa kile ambacho alikiona alitoka haraka na kuliendea gari lake ili aondoke eneo hilo lakini kabla hajafanikiwa kuufungua mlango wa gari alihisi kitu cha baridi kikimgusa kisogoni.


"Brother hivyo hivyo ulivyo ufungue mlango wa gari lako taratibu kabisa huku ukisikiliza maelekezo yangu."

Mahmoud alipumua kwa nguvu akiamini kuwa tayari kaingizwa mkenge. Hivyo hakuwa na namna alichokifanya ni kuwa mpole tu, akaingia ndani ya gari kisha yule mtekaji naye akafuata siti ya nyuma kilichomuacha mdomo wazi Mahmoud ni baada ya kukutana na mtu mwingine ndani ya gari akiwa kaketi siti mbele.


"Habari kiongozi, usishtuke sana sisi ni watu wema tu japo njia tuliyoitumia inaweza kukupa tafsiri tofauti lakini hatuko hivyo labda utulazimishe wewe mwenyewe kuwa wabaya."

Aliongea mtu huyo aliyemkuta kwenye gari akiwa anavuta sigara.


"Kwani mnataka niwasaidie nini?"

Mahmoud aliwauliza swali watu hao ambao idadi yao ilikuwa ni wawili.


"Vizuri sana mkubwa Mahmoud, dereva Taxi mkongwe ambaye una siri nyingi sana hapa mjini, sisi tunachotaka muda ni kutupeleka kwa bosi wako unayemtumikia tu hatuna kingine tunachokihitaji kutoka kwako."

Mahmoud alijibiwa.


"Mkuu mbona kama sikuelewi hivi,ni bosi gani mnayemtaka niwapeleke kwake?"

Mahmoud alijifanya kama vile hafahamu chochote juu ya kile wanachokihitaji lakini ukweli aliufahamu.


"Unasemaje wewe?"

Aliyekuwa nyuma na bastola alimuuliza huku akimsindikiza na ngumi nzito ya kichwa iliyomfanya Mahmoud kuona nyota nyota machoni na kabla hajafanya chochote walitoa kitambaa ambacho walimfunga usoni, hiki kitambaa ni kama kilikuwa na madawa ya usingizi hivi kwani baada ya kumfunga tu Mahmoud alipatiwa na usingizi mzito.


"Mhamishie siti ya nyuma huko kwisha jeuri yake huyo."

Aliyekuwa mbele alitoa maagizo hayo baada ya kufanikiwa kumlegeza Mahmoud. Alishushwa na kuhamishiwa siti ya nyuma ambako walimlaza na kisha kuondoka naye.


Walimchukua na kumpeleka moja kwa moja mpaka kwenye jengo moja chakavu na ambalo halijamalizika vizuri na kumuingiza mpaka kwenye chumba ambacho kilikuwa katikati ya jengo hilo na kumhifadhi.


"Mtaarifu bosi kuwa kazi yake tayari atuletee chetu abakie na mzigo wake."

Mtekaji ambaye muda wote alikuwa akitoa maagizo kwa mwenzake alimwambia tena afanye hivyo kwa bosi wao aliyewaagiza.


"Sawa kiongozi."

Alimjibu huku akimkagua Mahmoud mifukoni.


"Na vipi kuhusu hawa wengine?"

Alimuuliza kiongozi wake juu ya mateka wengine.


"Si bado hawajazinduka nao? Najua mpaka atakapofika mhitaji wao watakuwa wamekaribia kuzinduka au watakuwa wamezinduka."

Alimjibu.

Baada ya kumtoa kila kilichokuwa mifukoni mwa Mahmoud alitoa simu yake na kubofya namba ya aliyewatuma na kuipiga.


****


Jackline aliwasili salama kwake Windhoek na kumkuta mlinzi katulia lindoni kwake. Baada ya kupaki gari alimfuata mlinzi pale getini alipokuwa akilifunga geti vizuri.


"Nipe ripoti injinia wangu."

Jackline alimuuliza mlinzi wake kimafumbo kidogo huku akishika kidevu chake.


"Bado hajarudi."

Mlinzi alimjibu.


"Una uhakika kweli?"


"Mama huniamini kijana wako kweli?"

Mlinzi alimjibu kwa swali tena.


"Okey nimekuelewa bwana, ngoja nikajipumzimshe kidogo maana sijapata usingizi wa kutosha hizi siku mbili tatu."

Jackline alimwambia mlinzi huku akiondoka kuelekea ndani na kumuacha mlinzi akitabasamu tu. Akiwa ameingia tu chumbani simu yake iliita na baada ya kuiangalia alikuwa ni mume wake akaipokea.


" Mama Nathan sitaweza kurudi leo kuna tatizo kubwa limejitokeza."

Daktari Abbas alimtaarifu mke wake.


"Kuna tatizo kubwa? Ni tatizo gani hilo mume wangu?"

Jackline alimuuliza mume wake mara baada ya kupewa taarifa hiyo na pia kingine kilichomshtua Jackline ni namna ambavyo Daktari Abbas alikuwa akiongea.


"Nitakueleza baadaye mke wangu maana hapa mpaka nimechanganyikiwa sijui nifanye nini?"

Mume wake alimjibu na kisha kuikata simu kabisa. Jackline alichanganyikiwa kwani haijawahi kutokea hali kama hiyo kwa mume wake, akaona ampigie ajue kuna nini lakini simu ya Daktari Abbas haikuwa hewani. Alijaribu tena na tena lakini hali haikubadilika ilikuwa vile vile.


"Kapatwa na nini mume wangu?"

Jackline alijiuliza swali huku akiitupa simu kitandani na kutoa nguo.


"Haijawahi kutokea hali kama hii kwa mume wangu lazima kapatwa na jambo."

Jackline aliendelea kuwaza huku akielekea bafuni kuoga. Alioga na kutoka baada ya kila kitu hakuona hata sababu ya kuandaa chakula alijiandaa na kutoka. Baada ya kuingia kwenye gari alishuka tena na kurudi tena ndani ambako alisahau simu kitandani, aliichukua na kurudi kwenye gari ambako aliingia akaliwasha na kumpa ishara mlinzi afungue geti, lilipofunguliwa tu alitoka kama vile anafukuzwa kitu ambacho kilimshangaza mpaka mlinzi ambaye hajazoea kumuona bosi mama wake katika hali ile. Alitembea kwa umbali fulani hivi kisha akalisimamisha gari lake pembeni baada ya kukumbuka kitu, akaitoa simu na kumpigia Jasmine.


"Huu mwaka unaonekana kuniendea kombo tofauti na hii mingapi iliyopita."

Jackline alimwambia Jasmine baada ya kupokea simu.


"Una maana gani Jackline?"

Jasmine alimuuliza.


"Yaani huwezi amini ndugu yangu leo nimeingia Windhoek lakini sijafanikiwa kwa lolote kwani nimeigusa tu nyumba yangu Abbas ananipigia simu kuwa hatarudi kuna tatizo limempata na nilipojaribu kumdadisi ni tatizo gani hilo hakujibu akanikatia simu."


"Kwa hiyo unataka kusema nini sasa?"

Jasmine alimuuliza.


"Jasmine niseme nini hapo unafikiri? Niko njiani kurudi tena Namport nikajue ni tatizo gani limempata."

Jackline alimjibu Jasmine.


"Kwanini usingesubiri kwanza mpaka atakapokupa taarifa huwezi jua labda ni huko kwenye Hospitali yake?"


"Hata kama, mume wangu namfahamu vizuri sana ingekuwa ni kazini kwake asingenikatia simu na angenieleza moja kwa moja."


"Kumbe wewe nenda huko Namport lolote utakalo kutana nalo tujulishe mara moja tujue tunafanya nini?"

Jasmine aliona aungane naye tu pasipo kumkatisha tamaa Jackline.

Baada ya kukata simu alikaa sawa kwenye usukani na kuondoa gari.


"JACKLINE KUWA MAKINI NA NYENDO ZAKO TAYARI KUNA MTU ANAPITA KWENYE KILA HATUA YAKO."

Ujumbe uliingia kwenye simu yake Jackline alipunguza mwendo na kuichukua simu akaufungua ujumbe na kuusoma.


"Mhh ni nani huyu aliyenitumia ujumbe huu?"

Jackline alijiuliza baada ya kuusoma ujumbe huo ambao uliingia bila ya namba wala jina la mtumaji.


" Makubwa haya."

Sasa nitaujibu vipi ujumbe huu wakati hakuna namba ya mtumaji?"

Jackline alijiuliza swali hili huku akiwa kajishika kichwa kwa mkono kulia huku simu akiipigapiga kwenye usukani.


" Hebu ngoja kwanza."

Ni kama alikumbuka kitu aliifungua simu upande wa ujumbe na kumuandikia Jessica na Titiana.


" NAOMBA INGIA MTANDAONI NA UMTAFUTE MTU ALIYENITUMIA UJUMBE MUDA HUU USIO NA NAMBA."

Kisha akautuma kwa wote wawili waufanyie kazi na baada ya kuona umepiga tiki aliwasha gari ili kuendelea na safari.


"Mke wangu mambo yamekuwa magumu huku, Bi Elizabeth nahisi kaanza mambo yake japo sina uhakika. MAHMOUD KATEKWA NA WATEKAJI WANANITAKA MIMI NDANI YA SIKU MBILI NA NISIPOFANYA HIVYO TU WANAMUUA."


Ujumbe mwingine uliingia tena kwenye simu kabla hajaondoka na baada ya kuufungua na kuusoma ulimchanganya kabisa akajikuta anashuka kwenye gari.


" Haiwezekani, haiwezekani nasema haiwezekani Bi Elizabeth hawezi kufanya hivi kwa Mahmoud Mafia ambaye mimi mwenyewe alinishangaza kwa mbinu zake. Noooooo......"

Jackline alipiga kelele huku akilipiga teke tairi la gari. Alionekana kuchanganyikiwa baada ya kuupata ujumbe huu kutoka kwa mume wake Daktari Abbas.


NINI KINAKWENDA KUTOKEA?





Bi Elizabeth kwa kushirikiana na kundi la David Orlando walikuwa ndani ya nyumba moja ya kulala wageni ambayo si maarufu sana mjini Namport ikiwa nje kidogo ya mji wakiwa kwenye kikao cha kimkakati cha kuhakikisha kuwa wale wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine kuiangamiza familia yake wanapata kinachostahili.


"Vijana wangu naomba msinitupe katika mkakati huu lengo likiwa ni kulipa kisasi na baada ya hapo hata nikifa si kitu kwani nina faida gani ya kuendelea kuishi ilhali wapendwa wangu wote wamelala chini."

Alipofika hapo alianza kulia ikabidi David aanze kumtuliza na baada ya kutulia ilibidi waendelee na majadiliano kama ambavyo walikubaliana kufanya siku hiyo.


" Kwa hiyo mama ulikuwa unafikiriaje juu ya huu mchakato?"

David Orlando alimuuliza Bi Elizabeth.


"Ninachokifikiria kwa sasa ni kuwashughulikia kwanza wale vijana waliopangisha nyumba yangu bila ridhaa yangu hasa huyu Thomas pili ni huyu kijana ambaye amekuwa akinifuatilia toka Windhoek mpaka hapa tujue pia anamtumikia nani? Na uzuri tayari keshakamatwa toka jana usiku. Kisha tutatakiwa kumpa muda mpangaji wa kujiandaa kuondoka au kukubaliana na masharti mapya ya kuishi pale. Na mwisho mfumo tutakaoutumia kupambana na hiki kikosi hatari cha Jackline ni kwa kushtukiza tu na si vinginevyo wanangu."

Bi Elizabeth aliwafafanulia vijana wake mchakato utakavyokuwa kwa kipindi chote cha oparesheni yao.


" Kwa hiyo unataka kusema kuwa kazi hii tutaifanya kwa makundi makundi?"

David Orlando alimuuliza tena Bi Elizabeth.


" Ndiyo mwanangu, lakini itakuwa ni makundi mawili tu moja likiwa chini yangu na la pili litakuwa chini yako. Hapa naomba nifafanue kidogo, baada ya kuwashughulikia hawa tuliowakamata ninyi mtasalia hapa na mimi nitakuwa nje ya hapa hasa ambako nitabaini Jackline yupo."

Bi Elizabeth alifafanua, lakini kijana mmoja aliinuka na kutoa majibu ya kazi ambayo alipewa ya kupeleleza mahali anakoishi Jackline.


" Naomba nitoe majibu ya ni wapi anakoishi Jackline kwa sasa."

Alianza kijana huyo anayefahamika zaidi kwa jina la Makompyuta.


"Tujuze Makompyuta."

David alimpa nafasi ya kuelezea.


"Kwa muda wote ambao ulinipa kazi ambayo naweza kusema ilikuwa ngumu sana kwangu hatimaye imeweza kutoa majibu baada ya kuzama zaidi kwenye kompyuta zangu pale getoni kwa kushirikiana na rafiki zangu wa IT tukabaini kuwa Jackline ndani ya mwezi huu anaishi hapa hapa Namibia katika jiji la Windhoek na nzuri zaidi ni kwamba kaolewa na Daktari Mkuu na mmiliki wa Hospitali ya 'The King's Medicare Centre' aitwaye Daktari Abbas."

Makompyuta alitoa maelezo ambayo yalimfurahisha kila mmoja mle ndani hasa hasa Bi Elizabeth.


" Maajabu ya Mlokole kulilia pombe yaani huyu Daktari ninayemfahamu mimi ambaye aliwasaidia sana wakina Jackline wakiwa wagonjwa leo hii kamuoa?"

Bi Elizabeth aliuliza swali huku akijifuta machozi.


"Ndiyo Bi Elizabeth na tayari wamejaliwa kupata watoto mapacha wenye takribani ya miaka kama mitano au minne hivi."

Makompyuta aliendelea kudadavua kile ambacho alikuwa na uhakika nacho.


"Makompyuta unaongea nini tena hapa? Wakati unafahamu fika mama yako nahitaji kitu hapa? David mueleze Makompyuta."

Bi Elizabeth aling'aka japo alipewa taarifa nzuri.


"Nimekuelewa mama."

David Orlando alimjibu Bi Elizabeth. Na wakati mjadala ukiendelea mle ndani simu ya Bi Elizabeth iliingia ujumbe.


"KIPENZI NIAMBIE KIASI GANI UNAKIHITAJI KWENYE AKAUNTI YAKO MUDA HUU KWA SHUGHULI ZAKO?"

Ujumbe huu ulimfanya ainuke na kutoka nje huku akiendelea kuisoma ile meseji mara mbili mbili. Na baada ya kufika nje aliipiga ile namba.


"Wewe nani?"

Bi Elizabeth aliuliza baada ya simu kupokelewa upande wa pili.


"Ukiniita Mackie inatosha tu."

Upande wa pili ulijibu kwa ufupi tu.


"Mackie ndiyo nani? Na namba yangu umeipata wapi wakati namba yangu na simu yangu ni vipya na sina namba yoyote ile maana nimeanza kuitumia jana tu."

Bi Elizabeth alimuuliza huyu mtu aliyejitambulisha kwa jina la Mackie.


"Usipate hofu Bi Elizabeth juu yangu ni rahisi sana kwangu kupata chochote kile nikiamua hata wewe mwenyewe unalifahamu hilo. Naitwa Mackdone from South Africa una swali tena?"

Mackdone alijitambulisha zaidi.


"Kwa...kwa...kwa hiyo..."

Kabla Bi Elizabeth hajamalizia kauli yake Mackdone aliingilia kati.


"Acha kuichosha akili yako mpenzi kutaka kujua nini kimetokea mpaka nimekutafuta kifupi mimi ndiye niliyefanya mchakato wa wewe kuachiwa pale gerezani kwa kushirikiana na Wizara ya mambo ya ndani ya hapo kwenu."

Kauli hiyo ambayo Bi Elizabeth hakuitegemea kuisikia siku hiyo tena kutoka kwa mtu ambaye hakuwa akimuwazia kwenye oparesheni yake alipata mshtuko na kuanguka chini na kuzirai, hali hiyo iliwatoa ndani wakina David Orlando baada ya kusikia kishindo nje na kutoka. Walimchukua Bi Elizabeth na kumkimbiza Hospitali ya jirani ya Petromaria kwa matibabu huku David akiichukua simu ya Bi Elizabeth iliyokuwa imeanguka pembeni yake huku ikiwa bado haijazima na baada ya kuiangalia namba iliyokuwa bado inaflash ikabidi aikate na kumtumia ujumbe mtu huyo.


"UMEMSABABISHIA MSHTUKO MAMA YETU."


Baada ya kumtumia ujumbe huo David aliizima simu hiyo na kuiweka mfukoni. Walifika na kupokelewa na wauguzi wa hospitali hiyo ya Petromaria ambao walimuwahisha kwenye chumba cha wagonjwa wa dharura kwa matibabu.


"Nini kimemkuta mgonjwa wenu?"

Daktari alimuuliza David wakiwa ofisini kwa Daktari huyo.


"Sijui nini kilimtokea sababu alikuwa anaongea na simu lakini ghafla tukaona anakwenda chini hivyo hatujui alikumbana na taarifa gani kwenye simu."

David Orlando alimjibu Daktari kama ambavyo aliulizwa na Daktari huyo.


"Mmhh okay vizuri, naomba tusubirini hapo nje tupate kumshughulikia mara moja."

Daktari alimuelekeza David huku akiinuka kitini kutaka kutoka nje na kuelekea kwenye chumba alichoingizwa Bi Elizabeth.


****


"Hizo ni vurugu za Roberto dada Jackline ndiye aliyekutumia ujumbe huo."

Simu ya Jackline ilipokea ujumbe ambao baada ya kuufungua alibaini mtumaji ni Jessica na baada ya kuusoma alitabasamu tu kwani mpaka muda huo alikuwa kachoka akiwa hajui wanafanyaje juu ya Mahmoud ambaye hawakujua yuko wapi mpaka muda huo.


" Roberto wewe chizi kweli yaani ukaona unichezee akili yangu, haya bwana lakini ujumbe ulifika."

Jackline alijisemea mwenyewe akiwa nyuma ya usukani akielekea hospitalini kujadiliana na mume wake juu ya sakata la Mahmoud. Lakini akiwa bado hajaiweka simu pale kwenye 'phonestand' mara ujumbe mwingine ukaingia tena na hapo akaona hakuna jinsi zaidi ya kuliegesha gari pembezoni mwa barabara na kuifungua meseji ile.


"Wifi Jackline nimebaini ni nani aliyekutumia ujumbe usio na jina wala namba ni mdogo wako Roberto."

Alipoisoma meseji hii aliendelea kucheka Jackline.


"Wao kumbe kazi hii niliigawa kwa watu wawili?"

Jackline alijisemea mwenyewe na hapo hapo akaona ampigie simu Roberto.


"Niambie dada yangu."

Roberto alianza baada ya kuipokea simu.


"Ndiyo ukafanya nini sasa?"

Jackline alimuuliza Roberto.


"Ulishtuka ee, nilijua tu dada yangu lakini yote kwa yote sikuwa na baya lolote nilifanya hii kutokana na mtu anayenipa hizi taarifa kutoka hapo Namibia kunihakikishia hilo, hivyo sikuweza kukaa nalo."

Roberto alimweleza Jackline.


"Kwa hiyo unataka kunieleza nini mdogo wangu?"

Jackline alimuuliza Roberto.


"Ni kwamba kuna mtandao wa hatari umeibuka na uko mbioni kuanza shughuli zake za kumsaidia Bi Elizabeth kwa siri hatua kwa hatua na inavyoonekana mtandao huu uko chini ya Tajiri Mackdone. Na nina hofu hata utekwaji wa Mahmoud mtandao huo unahusika."

Roberto aliongea kitu ambacho kilimfanya Jackline kupata ubaridi na kusababisha vipele kumtoka mwili mzima.


" Mhh kwa hiyo unataka kuniambia kuwa Bi Elizabeth keshajipanga juu yetu?"

Jackline alimuuliza Roberto.


" Naweza kusema ndiyo au hapana kwani huu mtandao umeamua kufanya hivi kimya kimya kumsaidia huku naye Bi Elizabeth akiendelea na mikakati yake."

Jackline aliendelea kushikwa na ubaridi mwilini baada ya kupata taarifa za Bi Elizabeth kutoka kwa Roberto.


"Dada Jackline naomba jadiliana na shemeji yangu juu ya wajomba zangu Nathan na Natalie."

Roberto aliongeza.


"Una maana gani Roberto?"

Jackline alimuuliza.


"Leo hii katekwa Mahmoud unafikiri kesho ni nani? Hatujui hivyo tahadhari ni muhimu sana dada yangu tunachotakiwa kukifanya ni kuwahamishia Marekani au Uingereza kwa siri au hata huku Brazil waje kuishi na kusoma huku mpaka mambo yakiwa vizuri."

Roberto alimaliza kumshauri Jackline juu ya watoto wake kuhamishwa kutoka Namibia.


" Vipi mke wangu mbona haufiki tu hapa."

Ulikuwa ni ujumbe kutoka kwa Daktari Abbas kwenda kwa mkewe.


" Nashukuru sana Roberto kwa maono yako haya sidhani kama mume wangu atalipinga hili kama anahitaji kuendelea kuwaona watoto wake. Nitakucheki mdogo wangu naona shemeji yako ananicheki hapa."


"Bila shaka dada yangu, usilipuuze hili."


"Niamini mdogo wangu."

Jackline alimjibu na kukata simu kisha akafunga mkanda wake kisha akawasha gari lake na kuondoka zake kumuwahi mume wake ambaye alikuwa akimsubiri hospitalini kwake 'King's Medicare Centre' tayari kwa kuanza kuwafuatilia watu waliopewa kazi ya kumtafuta Mahmoud alipo.


JE, NI NINI KITAENDELEA?




Baada ya matibabu ya dharura Bi Elizabeth alipata fahamu zake na kuamsha matumaini ya kuendelea na mchakato wao japo Daktari aliwataka wamuache kwa muda mpaka siku inayofuata ili wamtazamie hali yake kwa masaa mengine zaidi. David aliomba kuongea na Daktari nje.


"Samahani Daktari nilikuwa naomba kuondoka na mgonjwa wangu kwa kuwa tayari kazinduka na anaendelea vizuri na iwapo itatokea hali yake kubadilika tutawasiliana."

David Orlando aliomba kuondoka na Bi Elizabeth japo Daktari aliendelea kushikiria msimamo wake wa awali.


" Nimekuelewa ndugu yangu, ila tu nielewe kwamba mgonjwa hataweza kuondoka hapa mpaka tukamilishe tiba yetu sisi kama wataalamu huwa hatuendeshwi na mihemko ya mtu bali huwa tunazingatia weledi zaidi."

Daktari alikazia msimamo wake ambao ulimfanya David awe mpole.


" David wala usijali kuhusu mimi ninyi rudini nyumbani mkaianze ile kazi ya kuyachambua yale magunia matatu kujua kama yatauzika ama la."

Bi Elizabeth alitumia lugha ya mafumbo kumfikishia ujumbe David ambaye alimuelewa vizuri akatikisa kichwa kuashiria kaelewa, hivyo aliwapa ishara vijana wake kuwa wanatakiwa kuondoka hivyo yeye alitoa simu mfukoni na kumkabidhi Bi Elizabeth ambaye aliipokea na kuiweka chini ya mto wa kulalia. David na kundi lake waliondoka na kumuacha Bi Elizabeth pale Petromaria.


"Oya ee sikilizeni safari yetu itatia nanga ya awali kule kwenye makazi ya kale."

David Orlando aliwapa maelekezo wenzake kisha wakaondoka kuelekea huko na baada ya masaa kadhaa waliwasili kwenye jengo hilo na kuwakuta watekaji wakiwasubiri kwa hamu sana.


" Karibuni, vipi mmekuja na mzigo wetu? "

Mmoja wa watekaji aliuliza baada ya David Orlando na kundi lake kuwasili pale jengoni.


"Kivipi?"

David aliuliza.


"Mhh inaonekana ninyi mmekuja kuja tu bila kujua ni kipi cha kufanya, mnaonaje iwapo kama mtaondoka hapa na kwenda kujipanga upya?"

Mtekaji alimjibu kisha akawataka waondoke.


"Lakini si mmeongea na mkubwa wetu? Na kitu kingine mnachotakiwa kukijua ni kuwa mkuu wetu alipata tatizo na yuko hospitali kwa matibabu."

David alijaribu kuwaelezea japo haikuwa rahisi.


"Nimesema ondokeni hapa mara moja mnafikiri sisi ni wafuasi wa ngonjera?"

Wale watekaji hawakuwa tayari kuwasikiliza wao walihitaji malipo yao tu na si kitu kingine.


"Ninyi pimbi hebu sikilizeni iwapo hamtafanikisha mzigo wetu mpaka kesho asubuhi mjue kuwa hawa nguruwe wenu tutawaachia wakale mahindi huko mashambani."

Jamaa aliwatisha wakina David ambao walikuwa wanaingia kwenye gari tayari kwa kuondoka eneo hilo ambapo walishindwa kuelewana. Lakini muda huo wakiwa kwenye kulumbana Mahmoud alikuwa akiwasikia vizuri sana hivyo haraka sana akaanza kukikagua kile chumba alichokuwa kafungiwa. Haraka sana Mahmoud akaanza kujifungua zile kamba alizokuwa kafungwa miguu na mikononi akianza na za mikononi kwa kuzisugua kwenye pembe za kiti alichokuwa kakalia.


"Washenzi hawa watajutia maamuzi yao."

Mahmoud aliongea hayo huku akiwa anaendelea kusugua kamba zile ambazo zilikatika na kuzifungua na za miguuni alipomaliza tu aliziegesha na kurudisha mikono nyuma kama ilivyokuwa awali. Mara mlango ulifunguliwa na wale watekaji waliingia mle chumbani.


" Wee nguruwe umezinduka tena siyo? Inavyoonesha wewe ni sugu wa haya madawa siyo?"

Mahmoud aliulizwa na watekaji.


"Wala sijui chochote kile, ninachowaomba ni kuniachia tu niondoke mahali hapa."

Mahmoud alijitetea.


"Unasemaje wewe?"

Aliulizwa na mmoja wa watekaji.


"Sikiliza Mahmoud kama ambavyo wewe ulivyoamua kuwa na kazi ya ziada ya kujiingizia kipato basi hata sisi tuliamua kuwafanya hivyo hivyo kama wewe kwa hiyo usifikiri utatoka bure bure hapa."

Yule mtekaji akiwa anatamba na sigara yake mdomoni huku mwenzake akiwa anawaandalia chakula wakina Mahmoud kwenye chumba kingine lilikuwa kosa kubwa sana kwani Mahmoud aliinuka na kumfuata yule mtekaji akiwa na ile kamba mikononi na kumvisha kisha akaanza kuivuta huku amemkandamizia ukutani.


"Aghh aghhh unan...unaniu....."

Jamaa alianza kutoa mlio wa maumivu huku Mahmoud akiwa kama vile hamsikii kwani aliendelea kuivuta kama ile mpaka alipoona kaishiwa nguvu kabisa ndipo akamuachia na kumlaza chini huku macho yakiwa mlango wa chumba ambacho alikuwepo mwenzake. Bila kupoteza muda Mahmoud alinyata kutoka nje. Yule mtekaji aliyekuwa akiandaa chakula kwa ajili ya Mahmoud na wenzake alitoka.


"Wee chizi pilipili umeweka wapi?"

Aliuliza akiwa ana uhakika anaongea na mwenzake lakini baada ya kuangalia mbele alipigwa na bumbuwazi.


"Whaaaat.....!" Alishikwa na butwaa haraka sana akamkimbilia mwenzake na kumuangalia.


"Baton, Baton, Batoniiiiiiiiiiiiiii..... Nooooooo acha utani basi."

Alipiga kelele akiwa amepiga magoti akiwa akamkamata kichwa. Na baada ya kuhakiki kuwa ameshakufa haraka sana aliinuka na kukimbilia kwenye chumba ambacho waliwahifadhi Thomas na dalali wa nyumba na baada ya kuingia kule hakuamini alichokutana nacho kwani kamba zilikuwa zikining'ia pale kwenye mbao za kenchi.


"Huyu Mahmoud huyu nikimkamataaaaaaa!!!!!!!! Atanitambua vizuri hanijui."

Alitoka mpaka nje na kuanza kukimbia huku na kule kuwatafuta walikoelekea. Lakini pamoja na kuhangaika kwenye maeneo karibu na pale hakuambulia chochote hivyo aliamua kurudi ndani na kuitoa simu iliyokuwa mfukoni mwa Baton na kumpigia Bi Elizabeth.


" Wewe mama huna akili kabisa na haujui biashara, unatupaje kazi wakati ukijua fika huna hata mia? Sasa nisikilize vizuri baada ya masaa mawili uwe umeingiza salio kwenye akaunti ambayo tulikupatia kinyume na hapo utatujua vizuri sisi."

Alimpiga mkwara Bi Elizabeth ambaye mpaka muda huo alikuwa bado hospitali.


" Kijana wangu punguza hasira tuweze kuongea kiungwana kupayuka si utamaduni wetu waafrika, nimewatuma vijana wangu hamkuwasikiliza mkawatimua mnajua walikujaje hapo? Okay siyo mbaya nisubirini dakika sifuri niwafanyie muamala wenu lakini itakuwa ni asilimia hamsini na inayobakia ni baada ya kutukabidhi mifugo yetu."

Bi Elizabeth alizungumza alimjibu kwenye simu.


" Acha ngonjera mama vitendo ndiyo vinamata hapa."

Alimjibu Bi Elizabeth na kumkatia simu na muda huo huo akiwa haelewi kipi kifanyike aliinuka na kuingia kule alikokuwa akiandaa chakula na kukimwaga kisha akatoka zake na kuuacha mwili wa mwenzake mle mle ndani.


" Pesa ikiingia tu breki ya kwanza ni Zambia kwa mjomba Salem, wakija watamkuta marehemu Baton ambaye ndiye atawakabidhi hiyo mifugo."

Alijisemea huku akitabasamu kuukaribia ushindi wa kupiga hela na kupotea zake, huku jasho linamtoka kwa hofu alivua shati lake na kuliweka begani hapo nje kulikuwa na baridi kali.


***


Mahmoud akiwa na Thomas pamoja na yule dalali ambaye alishirikiana na Thomas kuipangisha nyumba ya Bi Elizabeth. Na bila shaka ilikuwa ndiyo sababu ya Bi Elizabeth kuwakodia watu wawakate kwa lengo la kuwasulubisha mpaka waeleze lengo lao lilikuwa ni lipi kuipangisha nyumba ambayo siyo yao.


"Brother wewe ni nani mbona unatupelekesha tu tukiwa hatujui tunapelekwa wapi?"

Thomas aliuliza baada ya kuona Mahmoud akiwa anawapeleka tu bila kusema wanakoenda.


"Acha maswali wewe unachotakiwa kushukuru ni kuokolewa kutoka mikononi mwa watekaji."

Mahmoud alimwambia Thomas huku wakiwa ndani ya kimsitu ambacho kiko katikati ya mji ukiwa ni msitu wa kupandwa.


"Kaka hapo unatuzaja tu hakuna tulichokwepa kule na hapa ni yale yale, tulitekwa na sasa tumetekwa."

Dalali na yeye aliona aongee ya moyoni mwake.


"Hebu tulieni ninyi nitawabadilikia? Si mtu wa kawaida kama mnavyoniangalia kabla ya kuongea mengine hapa jiulizeni nimetokaje mle ndani? Kifupi mimi ndiye ambaye nilikupigia wewe masaa machache kabla ya kutekwa."

Ilibidi Mahmoud ajitambulishe kwao kitendo ambacho kiliwashangaza. Muda huo Mahmoud alikuwa akimtafuta Daktari Abbas ili amjulishe kinachoendelea.


" FANYA MPANGO UNIFUATE HAPA HORIZON FOREST NIMEFANYA YANGU TAYARI."

Mahmoud alimtumia ujumbe Daktari Abbas kumjulisha aliko. Kisha akairudisha mfukoni na kuwaongoza wenzake ndani ya msitu ule wa Horizon kwa lengo la kumsubiri Daktari Abbas.


"Samahani kaka naomba nikuulize swali kama hutojali lakini."

Dalali alimuomba Mahmoud.


"Uliza tu bila tatizo."

Mahmoud alimjibu.


"Kwanini ulinipigia? Na namba yangu uliipata wapi?"


"Wewe si ni dalali mtu wangu naikosaje namba yako?"

Mahmoud alimjibu kwa swali dalali.


"Kwa hiyo ulikuwa unahitaji nyumba?"

Wakati dalali akiuliza swali jingine mara gari iliwasili eneo lile japo ilikuwa tayari ni usiku. Na baada ya kushuka garini Jackline na Daktari Abbas walisogea mpaka pale walipokuwa wakina Mahmoud.


"Mahmoud poleni kwa janga lililowapata."

Jackline alianza kwa kuwapa pole wakina Mahmoud.


"Tunashukuru sana shemeji."

Mahmoud alijibu huku akiwa anawaongoza wakina Thomas kuingia kwenye gari.


"Mahmoud ilikuwaje mpaka ukaotewa?"

Daktari Abbas alimuuliza Mahmoud.


"Mkuu acha tu, hawa watu wanaonekana wana mtandao mkubwa sana sababu mimi nawasiliana na huyu dalali kumbe wao nao wanamvizia nimefika kwake nikakuta mlango uko wazi napiga simu yake inaita ndani narudi kwenye gari nikiwa na imani kuwa katoka kidogo si nikakutana na mdomo wa bastola?"

Mahmoud alitoa ufafanuzi.


" Pole sana, najua kwa sasa tutakuwa makini sana."

Daktari Abbas alimpa pole huku Jackline akiondoa gari mahali hapo kuelekea nyumbani kwao. Wakiwa wanaendelea na safari Jackline aliwaambia kile ambacho alikihisi.


" Nina wasiwasi kama kuna lolote mliongea na yule mama anayeishi pale kwa Bi Elizabeth atakuwa ndiye aliyetoa siri."


"Hilo liko wazi shemeji hakuna mtu mwingine zaidi yake lakini atajutia hilo."

Mahmoud alimjibu Jackline. Na wakati wanaendelea na mazungumzo mara ujumbe uliingia kwenye simu ya Jackline.


"UMEONA UNIONESHE NGUVU YAKO EEE, UMESHINDA LEO LAKINI JIANDAE KUILIPIA DAMU YA WANANGU."

Aliusoma ule ujumbe na kisha kumkabidhi simu mume wake ambaye aliusoma kisha akarudia tena kuusoma na safari hii alitoa na leso mfukoni akajifuta jasho usoni na shingoni kisha akamgeukia Mahmoud.


" Mchawi tayari kahisi kuwa Jackline ndiye aliyewatorosha mafichoni kwake."


"Huu ni mwanzo tu muache aendelee kuhisi hivyo hivyo moto utamuwakia tu."

Mahmoud alimjibu Daktari Abbas kwa kujiamini kabisa bila hofu yoyote ile. Kwa upande wa Daktari Abbas jasho liliendelea kumtoka bila shaka vitu kama hivi alikuwa akisimuliwa tu hakuwahi kuviona.


JE NI NINI KITAENDELEA?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA KIGONGO CHETU HIKI CHENYE KUSISIMUA ZAIDI.





Bi Elizabeth baada ya kutuma hela kwa yule Kijana mtekaji, aliondoka akiwa na timu nzima inayoongozwa na David Orlando kwa lengo la kwenda kuwachukua wakina Thomas na wenzake Mahmoud akiwa ni mmoja wao. Walifika kule porini ambako walihifadhiwa na baada ya kuwasili waliingia moja kwa moja mpaka ndani. Ukimya wa eneo hili uliwatisha wakina David.


"Hivi kuna watu kweli humu ndani mbona kimya hivi wakati tulipokuja sisi tulipokelewa nje?"

David aliuliza huku akiwa na Bi Elizabeth koridoni na watu wao wakikagua chumba kimoja baada ya kingine.


"Bosi kuna janga hapa."

Mmoja wao alitoa taarifa.


"Janga gani?"

Bi Elizabeth aliuliza.


"Kuna mtu kauliwa huku."

Majibu ya kijana wao yaliwafanya wote kuelekea kwenye chumba kile na baada ya kufika na kuukuta mwili pale walipigwa na butwaa.


"Kuna mtu katuotea hapa David."

Bi Elizabeth aliongea huku akimgusa puani marehemu Baton kuona kama anaweza kuwa hai.


"Ni mama nahisi na mimi lazima kuna watu wametuvizia hapa."

David Orlando alimjibu Bi Elizabeth.


"Hapana huyo si mwingine ni Jackline tu, mtoto Mafia sana yule lakini nitamuonesha mimi ni nani?"

Bi Elizabeth aliongea huku akiwapa ishara ya kuondoka eneo hilo lakini David alimkumbusha jambo.


"Na vipi kuhusu tuliyemtumia hela?"


"Hebu mpigie simu inawezekana katupiga huyo naye."

Alijibu huku akitoa simu na kumkabidhi David huku yeye akiliendea gari pale lilipokuwa limepaki. David alimpigia yule mtekaji waliyemtumia hela ambazo zilikuwa ni asilimia hamsini ya makubaliano simu yake ilikuwa ikiita tu lakini haipokelewi.


" Mama hapokei."

David alimjulisha Bi Elizabeth.


"Mtaarifu mtu wako wa IT amfuatilie huyo mpuuzi hawezi kwenda kokote na fedha yetu na huyo Jackline lazima tumuundie kikosi kazi cha kumfuatilia haiwezekani anipande kichwani."

Bi Elizabeth alitoa maagizo baada ya kupewa taarifa ya kutojibiwa simu yao. Hivyo waliondoka eneo hilo na moja kwa muda huo walielekea nyumbani kwa Bi Elizabeth kuongea na yule mama mpangaji na bahati nzuri walifika na kumkuta yupo anafua nguo zake. Aliwakaribisha baada ya kupiga kengele na kufunguliwa mlango mdogo wa geti.


"Karibuni."

Aliwakaribisha.


"Asante mwanangu."

Bi Elizabeth alijibu na kuingia ndani. Mwenyeji wao aliwakaribisha mpaka ndani.


"Bila shaka sura hizi hazijatoka kichwani kwako."

Bi Elizabeth alimuuliza mwenyeji wake.


"Nawakumbuka mama yangu."

Diana alimjibu.


"Vizuri kama unanikumbuka, sasa mwanangu ni hivi mtu aliyekupangishia nyumba yangu alikutapeli tu mimi ndiye mmiliki halali wa nyumba hii na kwa kukuhakikishia tu hilo unakiona chumba kile pale (akinyosha mkono) mle kuna kila kitu changu na ufunguo wa chumba kile nitakuonesha."

Bi Elizabeth alisimama na kuelekea kwenye ule mlango aliokuwa kauonesha alishika kitasa lakini akakumbuka kuwa ufunguo wake ameusahau hivyo akamwita David.


" Vunja kitasa hiki funguo sijui nimeiacha wapi? "

Bi Elizabeth alimpa maelekezo David.


" Sawa mama."

David alijibu na kuupiga teke mlango ambao uliitikia huku Bi Elizabeth akimtolea macho kwani yeye alimtaka avunje kitasa lakini yeye akaupiga teke ukafumuka japo haukuvunjika.


" Njoo mwanangu huku ndani sasa."

Bi Elizabeth alimwita Bi Diana kwenye kile chumba. Waliingia wote kwenye kile chumba na kuanza kupitia kitu kimoja baada ya kingine.


"Huyu hapa ndiye aliyekuwa mume wangu mzee Jerome aliyefariki miaka kadhaa nyuma, nisamehe mume wangu."

Alianza kulia huku akiipukuta ile picha iliyokuwa kwenye fremu yake.


"Na hawa hapa ndiyo wanangu Victor na Mustapha ambao nao wako sehemu moja na baba yao wamepumzika na kuniacha peke yangu."

Hapo alishindwa kujizuia aliiweka chini ile picha na kuanza kulia kwa nguvu hali hii ilimvuta Bi Diana na kujikuta akimfuata na kuanza kumtuliza Bi Elizabeth.


" Jitulize mama yangu najua ni maumivu kiasi gani unayoyapitia lakini nikwambie tu kwa uweza wa yule atutiaye nguvu siku zote hakika yatapita na utaanza mpya na familia mpya."

Maneno yale yalimfanya Bi Elizabeth kunyamaza na kumuangalia kwa muda Bi Diana kisha akaongea.


" Sikutegemea mwanangu kama unaweza kuwa na maneno mazuri kiasi hicho na ndiyo maana nilikuwa nimekuja kukufurumusha utoke kwenye nyumba yangu kutokana na kukiuka utaratibu lakini kwa uliyoniambia sina jinsi utasalia hapa kama muangalizi wa nyumba hii mpaka pale nitakapoleta utaratibu mwingine lakini hiki chumba usikiguse wala chochote kilicho ndani yake nitakachokuomba ni kumleta fundi aukarabati mlango huu"


"Nashukuru sana mama yangu kwa wema wako huu na mimi nakuhakikishia kuitunza vizuri nyumba yako kwa muda wote ambao nitakuwa hapa na vipi akija yule aliyetupangisha?"

Bi Elizabeth aliulizwa.


"Kuhusu huyo ondoa shaka tuko kwenye mchakato wa kumshughulikia japo kwa tahadhari chukua namba yangu."

Bi Elizabeth alimjibu huku akimkabidhi kadi yenye namba zake za mawasiliano. Na baada ya hapo Bi Elizabeth na kundi lake waliondoka kwenye nyumba hiyo na kumuacha mwenyeji wao akiendelea kuwasindikiza kwa macho kama haamini hivi kile alichokutana nacho siku hiyo. Wakiwa wanaingia kwenye gari simu ya Bi Elizabeth iliita na baada ya kutazama mpigaji ni nani hakuweza kuona zaidi ya namba tu hicho kikamfanya kujua ni namba ngeni.


"Halooo, nani mwenzangu?"

Bi Elizabeth alimuuliza baada ya kuipokea simu ile.



0 comments:

Post a Comment

Blog